Alhamisi, 4 Februari 2016

Kujaribiwa Kwa Imani ya Mtu aliyeokoka !



Mstari wa Msingi  1Petro 1;6-7 “Mnafurahi sana wakati huo ijapokuwa kwa kitambo kidogo ikiwa ni lazima mmehuzunishwa kwa majaribu ya namna mbalimbali ili kwamba kujaribiwa kwa imani yenu ambayo ina thamani  kuu kuliko dhahabu ipoteayo ijapokuwa hiyo hujaribiwa kwa moto kuonekane kuwa kwenye sifa  na utukufu na heshima katika kufunuliwa kwake Yesu Kristo”


                                                    Mateso ya Wakristo nyakati za Karne ya Kwanza

Imani ya mtu aliyeokoka ni ya thamani kuu kuliko dhahabu. ili kuijaribu dhahabu na kuithibitisha kuwa ni dhahabu safi hupitishwa katika moto, dhahabu safi inapopitishwa katika moto mkali hutoka ikiwa inang’aa zaidi, Vivyo hivyo kwa wokovu ili kuijaribu imani ya mtu aliyeokoka na kuithibitisha kuwa ni imani safi  imani hiyo hujaribiwa katika maudhi na mateso  mtu anayestahimili na kushinda kwa kuvumilia maudhi na mateso  yoyote yakayoletwa kwake kwa sababu ya wokovu ndiye atakayeonekana mwenye sifa na utukufu na heshima wakati wa kuja kwake Yesu Kristo, Maudhi haya na mateso ni ya kawaida kwa kila mtu aliyezaliwa kiroho au aliyezaliwa mara ya pili  yaani kuokoka na hivyo hatupaswi kufikiria kuwa ni kitu kigeni Soma 1Petro 4;12 kimsingi majaribu haya hutoka kwa Yule mwovu shetani ambaye yeye anajua sana uzuri wa mbinguni kule tunako kwenda na kwa sababu hiyo anajaribu kuleta vikwazo ili tukate tamaa na kushindwa kwenda mbinguni ambako yeye alifukuzwa kutokana na wivu alio nao  hufanya juu chini ili kuhakikisha kuwa  hatuendelei na wokovu na kujiunga naye kule anakokwenda yaani motoni Mathayo 25;41, Mbinu kubwa anayoitumia ni kuleta makwazo na mateso na maudhi  ili tuvunjike moyo na hapo ndipo anapo furahia, ni muhimu kufahamu kuwa tunapaswa kuhakikisha kuwa tunasonga mbele  bila kujali ni vikwazo vya namna gani shetani anatuletea tukisimama imara namna hii mbele za Mungu tutakuwa tunang’aa kama dhahabu iliyopitishwa katika moto.

Waliozaliwa kwa mwili huwaudhi wale waliozaliwa kwa Roho.
Tangu zamani hata sasa watu waliozaliwa kwa mwili yaani watu ambao hawajaokoka huwaudhi na kuwatesa na kuwanenea mabaya watu waliozaliwa kwa roho yaani waliookoka hivyo sio kitu kigeni mambo haya yakimpata mtu aliyeokolewa katika nyakati hizi Wagalatia 4;29 “Lakini kama vile siku zile Yule aliyezaliwa kwa mwili alivyomuudhi Yule aliyezaliwa kwa Roho ndivyo ilivyo na sasa”

Yesu Kristo alichukiwa aliudhiwa, alinenewa mabaya tena aliteswa.
Kiongozi mkuu wa wokovu wetu Yesu Kristo alikamilishwa kwa njia ya mateso Waebrania 2;10
·         Aliudhiwa Yohana 5;16
·         Walimuita ana Pepo Yohana 8;48 Yohana 7;20
·         Ulimwengu yaani watu ambao hawajaokoka walimchukia  na kutafuta njia ya kumuua Yohana 7;19 Yohana 8;37,Yohana 7;1,7.
·         Yesu alichukiwa bure yaani bila ya sababu yoyote Yohana 15;24-25
·         Walimuita maerukwa na akili Marko 3;21
Vivyo hivyo katika nyakati zetu sio jambo la kushangaza kuona tukichukiwa kwaajili ya wokovu, mtu aliyeokoka atachukiwa ataudhiwa na kuteswa na watu wasiookoka na kupewa kila aina ya majina ya dhihaka Yesu alitujulisha mambo hayo mapema Yohana 15;18-21 .

Watakatifu waliotutangulia waliudhiwa kudhihakiwa na kuteswa.
Tangu zamani watu wa Mungu walipitia maudhi na mateso
-           Yusufu aliudhiwa na kutendwa machungu Mwanzo 49;22-23
-          Musa alishutumiwa na kuteswa Waebrania 11;24-25 watakatifu wengi waliumizwa vibaya , hata kupigwa mawe na kukatwa na misumeno Waebrania 11;32-38
-          Ayubu aliyekuwa mwenye haki  na mtimilifu alichekwa sana na majirani zake na kufanywa kicheko Ayubu 12;4 alikuwa machukizo kwa ndugu zake na hata wadogo walimdharau na kumdhihaki Ayubu 19;13-19,30;9-10
-          Watakatifu nyakati za kanisa la kwanza walifanywa kuwa takataka ya Dunia 1Wakoritho 6;4-10 Mtume Paulo alipitia kila aina ya mateso na maudhi na kuendelea  katika imani 2Wakoritho 11;23-27.

Wafuasi wa Bwana Yesu ni wale wanaoendelea kulishika neno katika dhiki.
Mtu aliyeokoka ambaye ataamua kuacha wokovu kutokana na kukwepa dhiki au udhia Yesu anamuita mtu aliyepandwa  penye miamba  na hamfurahishi Mungu kabisa Mathayo 13;20-21 wafuasi halisi wa Bwana Yesu ni wale ambao watatendelea katika wokovu pamoja  na dhiki wanazokutana nazo 1Wathesalonike 1;6 “ Imetupasa kuingia mbinguni kwa njia ya dhiki nyingi” Matendo 14;21-22

Kutakuwa na maudhi toka kwa wazazi, ndugu au mume
Kama tulivyoona kutoka kwa Bwana Yesu na watakatifu waliotutangulia sisi sote hatuna Budi kuudhiwa kwaajili ya imani ya wokovu, wakati mwingine ni kawaidia kuona ndugu wazazi hata mume akichukizwa kwaajili ya wokovu, utaitwa kila aina ya majina uliyechanganyikiwa au umerukwa na akili n.k haya yasikufadhaishe ikiwa tunaitwa tumerukwa na akili ni kwaajili ya Mungu  kumbuka hata watu wa nyakati za kanisa la kwanza walipewa majina hayo 2Wakoritho 5;13, Unaweza kupigwa makofi na mumeo na fimbo kwa ajili ya wokovu au kusingiziwa mambo mengi ili kusudi uache wokovu haya yasikufanye uache wokovu ukiteswa kwa ajili ya mema huu ndio wema hasa mbele za Mungu 1Petro 2;19-21 unaweza ukapigwa pia  na ndugu au wazazi, kunyimwa fedha za ada, chakula  au fedha za matumizi kutoka kwa mumeo, na kukatishwa tamaa kwa kila namna  vumilia kwaajili ya Mungu kwani itakusaidia nini kuupata ulimwengu wote na kupata hasara ya nafsi yako ukatupwa katika ziwa la moto? Marko 8;36 unaweza kuwekwa vikao ukaambiwa unavuruga ukoo au kutishiwa kutengwa na ndugu kwaajili ya imani mpya ya wokovu uliyoipokea haya yote yatoka kwa Yule muovu ili uiache imani Yesu alikuwa wa kwanza kuokoka katika familia yake  na nduguze walikuwa bado soma Yohana 7;2-5 Baadaye nduguze nao walipofahamu siri ya wokovu waliokoka na miongoni mwao alikuwa Yakobo aliyekuwa mtume Wagalatia 1;19  Mungu amekupa wewe neema ya kuwa wa kwanza na wengine watakufuata , ni jambo la kushangaza akiwa mtu ni wa kwanza kwenda chuo kikuu katika ukoo wao asisumbuliwe lakini aliyeokoka anasumbuliwa jipe moyo ulimwenguni tunayo dhiki lakini kama Bwana Yesu alivyoshinda sisi nasi tutashinda Yohana 16;33.

Watatuita tumepotea
Baada ya kuokoka itatulazimu kuyaacha mafundisho manyonge tuliyokuwa tunayatumikia katika madhehebu yetu ya mwanzoni yasiyohubiri wokovu Wagalatia 4;9 hatuwezi kuendelea kuabudu na sanamu na kushiriki divai inayolevya katika meza ya bwana .n.k. ni kwasababu hizi na nyinginezo nyingi inatulazimu kuachana na madhehebu hayo amabayo watu wake wanapinga wokovu na kushindwa kulisimamia neno la Mungu Wagalatia 1;14-16, Tunapofanya hivyo huko sio kutangatanga kwani mitume pia walifanya hivyo ,Yesu alitufundisha kuwa kama mfanya biashara anayetafuta luliu nzuri  akiiona huuza kila alicho nacho na kuinunua Mathayo 13;45-46 dhehebu lolote ambalo sio lulu nzuri halituwezeshi kujifunza neno la Mungu hilo sio lulu nzuri , wako watu wengie wanashindwa kuyaacha kwa sababu tu ya kutafuta utukufu kwa wanadamu Yohana 12;42-43 Luka 14;33  ili tuweze kushinda katika jaribu hili la imani  tunapaswa kutambua kuwa hatujapotea  bali tumetoka upotevuni  na tunaingia uzimani yaani katika njia halisi ya kwenda mbinguni kwao wanaotuita tumepotea ni ishara ya kupotea bali kwetu sisi ni ishara ya wokovu wafilipi 1;27-28.

Tafasiri za kibiblia za maana ya mtu aliyepotea
·         Mtu awaye yote anayesitasita katika mawazo mawili kumtumikia Bwana Yesu au Kumtumikia shetani au ulimwengu huyo amepotea Waebrania 10; 37-39, 1Wafalme 18;21.
·         Mtu awaye yote asiyeijua njia ya Mungu bali anafuata mapokeo ya wanadamu Zaburi 95; 10; Marko 7;6-8.
·         Watu waliokwenda mbali na maagizo ya Mungu siyo maagizo ya wanadamu  yaani maagizo yoyote yaliyo kinyume na Neno la Mungu zaburi 119;21
·         Watu wasiyoyajua maandiko hivyo kuyapotosha  na kuyatafasiri visivyo Mathayo22;29
·         Watu waliokwenda mbali na kweli ya neno la Mungu Yakobo 5;19
·         Watu wanaotetea divai na kumsingizia Mungu kuwa amehalalisha  wakati mbele za Mungu ni matapiko na uchafu Isaya 28;7-8
·         Watu wanaoacha kulisikia na kulifuata Neno la Mungu  linalofundishwa na watumishi wanaoisimamia kweli yote ya injili 1Yohana 4;6
·         Watu ambao injili imesitirika kwao yaani imefichwa na Ibilisi ambaye ndiye mungu wa dunia hii anayefanya kazi ndani yao wakimtumikia na kusema kuwa hakuna wokovu 2Koritho 4;3-4
·         Watu wasiopata maonyo yaliyo katika neno la Mungu bali hutafuta kufarijiwa  hata kama maisha yao hayaendani sawa na injili Mithali 5;23
·         Watu wanaoiacha njia iliyonyooka yaani Neno la Mungu na kufuata njia zao wenyewe 2Petro 2;15.
·         Watu wanaofuata vinyago vyao yaani dhehebu Fulani au mwinjilisti fulani badala ya neno la Mungu Ezekiel 44;10.

Watatuambia kwamba tumedanganywa na manabii wa uongo;
Baada ya kuchukua uamuzi wa kuifuata kweli ya injili  na hatimaye kuamua kuokoka  na vilevile kukutana na nguvu za Mungu zilizobadilisha maisha yetu kabisa  baada ya kufanyiwa maombezi na watumishi wa Mungu  walio tofauti na viongozi wetu wa kidini wa zamani  tuliokuwa tumewazoea ndipo sa utasikia maneno ya kukukatisha tamaa  kuwa hizi ni nyakati za mwisho na manabii wengi wa uongo watatokea  na kudanganya watu wengi Mathayo 24;11 ikiwa hatufahamu maana ya manabii wa uongo ni rahisi  kuanza kubabaika na kuwa na mashaka kwa msingi huo ni muhimu kufahamu  maana ya manabii wa uongo  tangu mapema katika hatua za mwanzoni kabisa za wokovu wetu.

Neno nabii maana yake ni nini? Ni muhimu kufahamu kwanza kuwa Biblia ililetwa kwetu katika lugha kuu mbili Kiebrania na kiyunani na sehemu chache kiaramu  kwa msingi huo Neno nabii katika Kiswahili limetokana na neno la kiebrania Nabiy ambalo maana yake ni Yeye anenaye maneno ya mwingine kwa kuongozwa na Roho wake huyo aliyemtuma  kutokana na maana hiyo sasa tunapata maneno nabii wa kweli na nabii wa uongo nabii wa kweli wa Mungu huyanena maneno ya Mungu siyo maneno yao wenyewe hawazungumzi kwa mapenzi yao  wenyewe  2Petro 1;21 hunena maneno kutokana na uongozi wa Roho matakatifu ambaye Yesu alisema atatutia katika kweli nyote Yohana 16;13 Kweli ni nini? Kweli ni neno la Mungu Yohana 17;17 kwa maana hiyo nabii wa kweli huubiri neno la Mungu kila wanalolifundisha huthibitishwa kwa neno la Mungu  kwa kusema kama yanenavyo maandiko 1Wakoritho 15;3-4 wao watahubiri wokovu na kuonyesha wazi kuwa Mungu anataka tuishi maisha matakatifu hapa duniani Zaburi 16;3 manabii wa uongo watadai kuwa hakuna kuokoka duniani watasema haiwezekani kuishi maisha matakatifui ukiwa duniani  tofauti na Biblia inavyotufundisha kuhusu wokovu ona Tito 2;11-12, manabii wa uongo watafundisha watu kuwa Mariamu ni mama wa Mungu wakati neno linasema ni majakazi yaani mtumwa wa kike Luka 1;38 hawa ndio manabii wa uongo watafundisha watu kusali kwa kutumia Rozari wakati biblia haifundishi aina hiyo ya maombi, watafundisha kuwa mtu akifa anakwenda pugatori au toharani. Watafundisha kuomba wafu au kuwaombea wafu na kutumia mvinyo au divai katika meza ya bwana haya ndiyo mafundisho ya manabiiwa uongo watazuia watu wasioe au kuolewa na kuacha kula aina Fulani za chakula hawa ndio wanaofundisha uongo kinyume na Biblia.

Wajibu wetu tunapoudhiwa au kuteswa na kudhihakiwa kwaajili ya wokovu.
·         Kuendelea na wokovu na kuwaacha waseme huku sisi tukikaa kimya Ayubu 21;3
·         Hatupaswi kurudishia matukano au kulipiza  kisasi bali tujikabidhi kwa Mungu katika maombi yanapotukuta hayo 1Petro 2;23,Warumi 12;18-19 Inatupasa kuushinda ubaya kwa wema warumi 12;20-21
·         Inatupasa kuwapenda na kuwaombea wanaotuudhi na kututesa Mathayo 5;44-45
·         Hatupaswi kuwaogopa wauao mwili kisha wasiwezi kuiua roho inatupasa kumuogopa Mungu awezaye kuangamiza mwili na roho pia katika jehanamu Mathayo 10;28,1Petro 3;14
·         Kamwe tusijaribu kutafuta amani kwa  kwa kuamua kuacha wokovu na kufuata masharti yao  huko ni kumkana Yesu Mathayo 10;33-39 wakiona tumesimama imara baada ya mateso yao mwishoni hawataendelea kutuonea na tutawavuta  katika wokovu.
·         Hatupaswi kumtii mzazi au mume  wanapotuelekeza kufanya mambo yaliyokinyume na wokovu au neno la Mungu  kama kuacha kuomba kusali na kuacha wokovu, laki tuyatii yale yote yalio sawa na neno la Mungu  Tito 3;1;Waefeso 6;1 Mke anapaswa kumtii mume sawasawa na maagizo ya Neno la Mungu  Waefeso 5;24 hata hivyo tunahitaji sana kumuomba Mungu hekima katika wakati kama huu wengi wamepoteza ndoa zao kwa sababu ya kukosa hekima na kujikuta wakiachika huu sio mpango wa Mungu  Biblia inatuagiza kuwajibu kwa upole na kwa hofu soma 1Petro 3;15 “ Mwe tayari siku zote kumjibu kila mtu awaulizaye habari ya tumaini lililo ndani yenu lakini kwa upole na kwa hofu, ni jawabu la upole linaloweza kugeuza hasira  na sio neno liumizalo au linalochochea Mithali 15;1
·          Inatupasa kuamini kwamba hatimaye Mungu atatuepusha na maudhi hayo kwani kwa kila jaribu kuna mlango wa kutokea, Mateso ya mwenye haki ni mengi lakini Bwana humponya nayo yote inatupasa kudumu katika maombi bila kukoma 1Wakoritho 10;13, Zaburi 34;19 1Petro 5;10-11 1Wathesalonike 5;17-18.

Dhehebu linalosimamia Neno la Mungu vema hunenwa vibaya.
Kumbuka kuwa dhehebu linalosimamia kweli ya wokovu hunenwa vibaya kila mahali hivyo hatupaswi kubabaika tunapoona pale tunapohamia pananenwa vibaya kila mahali na kuzushiwa kila aina ya uongo hii ni kawaida hata kanisa la kwanza lilinenwa vibaya kila mahali Matendo Matendo 28;22. 

Aina nyingine ya kujaribiwa kwa imani
Wakati mwingine mara baada ya kuokoka kunaweza kutokea hali mbaya ya kibiashara, kiasi cha fedha kupungua namaisha kuwa magumu unaweza pia kufukuzwa kazi, kuibiwa au kuandamwa na hali ambazo ni nzito na sio za kawaida hii ni kwa sababu ya Shetani kujaribu kufanya kila namna ili uiache imani hii yote ni kujaribiwa kwa imani yako 2Wakoritho 4;8-11 ni mitihani tu lakini tunapoendelea kushikilia misimamo Mungu hufurahishwa nasi na mambo huwa shwari

Thawabu kubwa kwa wote washindao baada ya kujaribiwa kwa imani yao
Kuna thawabu kubwa kwa kila mtu ambaye ataendelea na wokovu pamoja na kujaribiwa kwa imani yake huko ndiko kweli kumpenda Mungu Yeye akupendaye wakati wa dhiki ndiye rafiki Mathayo 5;10-12, 1Petro 4;12-14 jambo la kuangalia ni kwamba siyo sahii kuudhiwa na kuteswa kwa sababu ya kufanya dhambi huko siyo kujaribiwa kwa imani 1Petro 4;15-16.

Hakuna maoni: