Alhamisi, 21 Julai 2016

Ujumbe: Kustahimili Mapingamizi makuu


Waebrania 12:3
Maana mtafakarini sana yeye aliyeyastahimili mapingamizi makuu namna hii ya watendao dhambi juu ya nafsi zao, msije mkachoka, mkizimia mioyoni mwenu”.

Ulimwengu huu ni ulimwengu wa mapingamizi, ni ulimwengu ambao kadiri kunavyokucha vipingamizi vya aina mbalimbali, Yesu aliweza kuyashinda mapingamizi nyote na ndio maana mwandishi wa kitabu cha Waebrania anataka tumtafakari sana Yesu ambaye alishinda mapingamizi makuu sana 

 "Dhoruba Katika Maisha zisikubabaishe na kukusumbua Yesu alizishinda mtafakari yeye"

Ulimwengu huu tulionao ni ulimwengu ambao unazidi kuwa wenye kutisha siku hadi siku na watu wanapoteza matumaini kabisa  Jonathan Park alitunga shairi hili kuuzungumzia ulimwengu huu na kusema 

·         Ni ulimwengu ambao mtu Fulani mahali Fulani amepoteza tumaini
·         Ni ulimwengu ambao mtu fulani mahali Fulani Ndugu kwa ndigu wanauana
·         Ni ulimwengu ambao mtu Fulani mahali Fulani anauawa kwaajili ya ngozi ya ragi yake
·         Ni ulimwengu ambao mtu Fulani mahali fulanmi anaona Fedha ni za muhimu kuliko imani, familia na marafiki
·         Ni ulimwengu ambao mahali Fulani serikali inatumia nguvu zake kuwatendea mabaya raia wake
·         Ni ulimwengu ambao mahali Fulani hawaruhusiwi hawaruhusiwi kuabudu Mungu au imani uitakayo
·         Ni ulimwengu ambao mahali Fulani mtu Fulani anamuua mwingine kwa jina la Allah
·         Ni ulimwengu ambao mahali Fulani mtu Fulani anamuua mwingine kwa jila la Mungu
·         Ni ulimwengu ambao mahali Fulani sehemu Fulani huwezi kutembea bila milio ya risasi kusikika
·         Ni ulimwengu ambao mahali Fulani mtu Fulani anakimbia nchi yake kutafuta maisha
·         Ni ulimwengu ambao mahali Fulani mtu Fulani anakimbia nchi yake na anakumbana na kifo
·         Ni ulimwengu ambao mahali Fulani baba anamtandika mtoto wake mpaka hawezi kutembea
·         Ni ulimwengu ambao mahali Fulani mama anamtupa mtoto wake wa kuzaa kwa vile eti hawezi kumtunza
·         Ni ulimwengu ambao maneno ya mtu au ahadi za mtu zimekuwa sio za muhimu tena
·         Ni ulimwengu ambao mwalimu anamwambia mwanafunzi huwezi kitu kabisa
·         Ni ulimwengu ambao watu wanasalitiana na marafiki wanakuwa maadui
·         Ni ulimwengu ambao vijana wanakata tamaa na kujiua
·         Ni ulimwengu ambao unakimbilia polisi au mahakamani upate haki unaishia kudhulumiwa
·         Ni ulimwengu ambao mtu Fulani anapatwa na mabaya wengine wanafurahi
·         Ni ulimwengu ambao unamwahisha mgonjwa hospitali ili kuokoa maisha yake anakufa kwa kukosa huduma za wahudumu wasio na haraka
·         Ni ulimwengu ambao mjomba anamuharibu mtoto wa dada yake mwenyewe kwa ulawiti
·         Ni ulimwengu ambao wanaume kwa wanaume wanaoana na wana wake kwa wanawake
·         Ni ulimwengu ambao watu hawaaminiani tena 

Hi jinsi gani tunaweza kustahimili hali hizi zote zenye kukatisha tamaa? 2 Timotheo 2:3, 8 Biblia inasema hivi “Ushiriki taabu pamoja name kama aksari mwema wa Kristo Yesu; Mkumbuke Yesu Kristo, aliyefufuka katika wafu, wa uzao wa Daudi kama inenavyo injili yangu”

Kwa nini maandiko yanatutaka tumtafakari Yesu tunapopitia mambo magumu  ni kwa sababu sehemu Fulani hapa ulimwenguni kuna tumaini tumaini hilo linapatikana kwa Yesu, kama sehemu moja ya ulimwengu ni Gisa sehemu ya pili kuna Nuru Yesu ni Nuru ya Ulimwengu  Yohana 1:5 “ Nayo Nuru yang’aa Gizani, wala giza halikuiweza, Yohana 12:46 “ Mimi nimekuja ili niwe Nuru ya ulimwengu, ili kila aniaminiye mimi asikae gizani”

Tukiyafikiria haya tunaweza kuzimia mioyoni mwetu, yaani tunaweza kukata tamaa na kuona kuwa ulimwengu umekuwa sio mahali salama tena pa kukalika lakini tukimtafakari sana Yesu ambaye alishindamap[ingamizi makuu namna hii, Hatutachoka wala kukata tamaa wala kuzimia moyo.

Jumatatu, 18 Julai 2016

Ujumbe: “Si kwa Uwezo, wala si kwa nguvu bali ni kwa Roho yangu”


Kiini: Umuhimu wa Kumuachia Roho wa Mungu atawale

Andiko la Msingi: Zekaria 4:6-10

.6. Akajibu akaniambia, akisema, Hili ndilo neno la Bwana kwa Zerubabeli, kusema, Si kwa uwezo, wala si kwa nguvu, bali ni kwa roho yangu, asema Bwana wa majeshi. 7.Nani wewe, Ee mlima mkubwa? Mbele ya Zerubabeli utakuwa nchi tambarare; naye atalileta lile jiwe la kuwekwa juu kabisa pamoja na vigelegele vya, Neema, neema, ilikalie. 8. Tena neno la Bwana likanijia, kusema, 9. Mikono yake Zerubabeli imeiweka misingi ya nyumba hii, na mikono yake ndiyo itakayoimaliza; nawe utajua ya kuwa Bwana wa majeshi amenituma kwenu. 10. Maana ni nani aliyeidharau siku ya mambo madogo? Kwa kuwa watafurahi, nao wataiona timazi katika mkono wa Zerubabeli; naam, hizi saba ndizo macho ya Bwana; yapiga mbio huko na huko duniani mwote. ”


Utangulizi:

Zerubabel alikuwa ni Liwali wa Jiji la Yerusalem baada ya Wayahudi kurudi kutoka Uhamishoni, Jina Zerubabel ni muungano wa Maneno mawili ya Kiibrania Zeri na Babilon ambalo maana yake ni Mzizi au Chipukizi kutoka Babeli, aliteuliwa kuwa liwali wa Yuda na Mfalme Artashasta, liwali huyu alikuwa anakabiliwa na kazi ngumu ya Ujenzi wa Hekalu, Kazi hii ilikuwa ni Mapenzi ya Mungu kabisa na Mungu alikuwa ameweka moyoni mwake  Mzigo wa kulijenga Hekalu, wakati huu kazi ya Ujenzi ilikuwa ngumu sana kuliko wakati wa Suleimani ni muhimu kufahamu kuwa ni kazi rahisi sana kujenga kitu mara moja lakini ni kazi ngumu sana kukirudia, Kazi ilikuwa ngumu na yenye upinzani mwingi sana, Kama ilivyokuwa kwa Nehemia Mungu alipoweka Moyoni mwake kuujenga ukuta wa Yerusalem kulikuwa na upinzani mkubwa sana, Zerubabel hali kadhalika alikutana na upinzani mkali wakati wa kulijenga Hekalu.

Hali halisi ya upinzani ilikuwa Hivi:-

1.      Watu waliokuwa wakiuzunguka mji walijaribu kuwakatisha tamaa, waliwatisha, waliiba baadhi ya vifaa vya ujenzi,
2.      Kila mara tunapojihusisha na kazi yoyote ya Mungu ni lazima shetani atatumia kila mbinu na hila kuharibu kabisa mikakati na mipango ya kimungu na kutukatisha tamaa.
3.      Shetani anaelewa wazi nini kinatokea watu wanapokuwa wamekata tamaa na kujichokea
4.      Watu wanapokata tamaa kumuamini Mungu kunapungua, Mambo yoyote yale yakifanyika katika hali ya hofu na kutokumcha Mungu mafanikio huwa ni madogo sana, Biblia inasema Mungu hakutupa Roho ya woga “2Timoth 1:7” watu waliokata tamaa hudumaa, hawawezi kufanya jambo lolote lile Duniani, ukiwa na jeshi la wanajeshi waliokata tamaa hata uwe na vifaa vya kisasa vya aina yoyoteile ushindi unaweza kuwa ni hadithi ya kusikiliza tu

5.      Shetani licha ya kututishia bali pia atashambulia na kuiba furaha tuliyonayo
6.      Watu walimuacha Zerubabeli peke yake na kila mtu akaanza kuangalia mambo yake na kujenga nyumba yeke mwenyewe na unjezi wa hekalu ukawa umesimama watu walikufa moyo “Mathayo 6:33” Kumbuka jinsi Israel walivyokufa moyo baada ya wapelelezi kuleta habari mbaya ya kuvunja Moyo, walisahahu kabisa kuwa Mungu yuko Pamoja nao, walianza kutumia akili
7.      Zerubabel alikata tamaa kwa sababu alikuwa haoni njia tena maono yake yalianza kufifia na moyo wake ulianza kupoteza matumaini jaribu lilionekana ni kubwa na tayari ujenzi wa Hekalu ulionekana kuwa mzigo na mlima mkubwa ambao sio rahisi kuusawazisha

Ndipo Mungu alipomuinua Nabii Zekaria kwaajili ya kumtia moyo Zerubabel  Na nabii Hagai kwaajili ya kuwatia Moyo wayahudi, Nabii Zekaria alimueleza wazi Zerubabel ujumbe kutoka kwa Mungu kwamba si kwa nguvu si kwa uweza Bali kwa Roho yangu asema Bwana, Mungu aliukemea mlima uliokuwa unamkabili Zerubabel na kuutabiria kuwa utakuwa Tambarare Mungu alimuahidi kuwa macho yake yanazunguka kuangalia duniani kote ni nani anamtumaini yeye na kila anayemtumaini yeye hatata tahayarika

Inawezekana hali kama ya Zerubabel inajitokeza katika Maisha yako, umeanza kukata tamaa,umeshambuliwa na kukosa msaada umeanza kutumia akili zako katikakutatua majaribio yako lakini wiki hii ninazo habari njema kwako kuwa Bwana amenituma nikuambie umtegemee yeye Machjo yake yanaangalia ni nani anamtegemea naye atamruhusu Roho wake mtakatifu kukutia nguvu na kukuwezesha atalikemea kila tatizo linaloonekana kuwa gumu katika maisha yako na litakuwa tambarare, Bwana akubariki na kukuongeza kwa utukufu wake katika Jina la Yesu amen

Ujumbe Na mkuu wa wajenzi mwenye Hekima
Rev. Innocent Kamote.

Ijumaa, 15 Julai 2016

Mwana wa faraja!



Andiko: Matendo 4:36. “Na Yusufu, aliyeitwa na mitume Barnaba, (maana yake, Mwana wa faraja), Mlawi, asili yake ni mtu wa Kipro,”

 "Ndani ya Yesu Kristo kulikuwa na huduma ya Faraja, watu walifurahi kumsikia kumgusa na kumuona, ilikuwa Huzuni kwa wanafunzi wake alipowaambia kuwa ataondoka, lakini aliwaahidi kuwaletea mfariji yaani Roho Mtakatifu, ambaye hufanya kazi ya kuwahudumia watu waliomuamini"

UTANGULIZI:

Kufariji maana yake ni tendo endelevu la kuendelea kutia moyo, kutia matumaini, kutia nguvu, kila mtu duniani anahitaji kutiwa moyo, kuishi kwa matumaini, na kutokukata tamaa katika maisha yetu ya kila siku, Tunaishi katika ulimwengu wenye changamoto nyingi sana na bila huduma ya kutiana moyo ulimwengu hauwezi kuwa mahali pa kupendeza sana kuishi, Tunahitaji watu wenye huduma ya kutia moyo wawepo kila mahali, Nyakati za Kanisa la Kwanza Mungu alilipa Kanisa zawadi ya mtu mwenye karama ya kutia moyo wengine, Mtu huyu alijulikana kama Yusuphu Mlawi mzaliwa wa Cyprus.

·         Mitume walimuita mtu huyu “Barnabas” kuonyesha umuhimu wa huduma hii ya faraja
·         Tunawezaje kutiana moyo kila mmoja na mwingine? Ni kwa kujifunza kutoka kwa “Barnaba” na kuangalia kila alichokifanya:-

Huduma ya Barnaba.
I.       Alitia moyo kanisa kwa kuonyesha mfano wa matendo yake.
·         Aliuza shamba lake  na kutoa fedha Matendo 4:37 alionyesha mfano katika kanisa, Kutoa kwake ulikuwa ni moyo wenye kuonyesha kuwa anawajali wengine, lilikuwa ni jambo gumu sana kuuza shamba Yerusalem kwa ajili ya umuhimu wa kumiliki ardhi katika jiji hilo lakini Barnaba alifanya akionyesha kujali wengine.
·         Aliwatia moyo waliokataliwa katika jamii na kanisa Matendo 9:26-30, Paulo mtume ambaye ndiye Sauli alipookoka na kujiunga na wanafunzi pale Yerusalem watu walikuwa na mashaka naye Lakini Barnaba alikuwa na ujasiri wa ajabu alimchukua Sauli na kumtambulisha kwa mitume, Je tufanyeje kwaajili ya watu wanaokataliwa katika jamii au kanisani lazima wawepo wenye huduma ya kufariji na kutia moyo kama Barnaba.
·         Aliwatia moyo washirika kukaa katika kweli kwa Bwana Matendo 11:22-24, kudumu kwetu katika wokovu pia kunahitaji watu wa kukujenga na kukutia Moyo Barnaba alikuwa mtu wa namna hiyo alilitoia moyo kanisa la Antiokia kudumu katika imani
·         Alimtia moyo Muhubiri mwenye kipawa na kuhudumu naye Matendo 11:25-26, wakati jamii inawapiga vita watu wenye vipawa the talented people na wakati mwingine kuwachukia ni rahisi kuwapoteza watu wa aina hii kama hakuna huduma ya kutia moyo Paulo mtume alikuja kuwa muhubiri mkubwa sana na mwenye huduma kubwa sana lakini ilifanyiwa malezi na kutiwa moyo na Mchungaji Barnaba, watumishi wengi wa Mungu wameshindwa kulea watu wenye vipawa kwa kuhofia kuwa watameza huduma zao, au wameshindwa kuwasaidia waimbaji kwa kufikiri kuwa ni watu wasiochungika, kama tukiwaelewa na kuwatia moyo na kuwajenga watakuwa wenye kufaa sana katika kazi na ujenzi wa ufalme wa Mungu
·         Alitumika kuyatia moyo makanisa yaliyopata shida kwa kupeleka zawadi Matendo 11;27-30, Wakati kanisa la Uyahudi linapitia shida Kanisa la Antiokia lilimtuma Barnaba kupeleka msaada na kanisa likafarijiwa kwa nini Barnaba kwa sababu alikuwa na moyo wa kweli wa kujali na kuwajenga wengine.
·         Alilitia moyo Kanisa kwa ibada za kufunga na kuomba pamoja na mafundisho Matendo 13:1-3,  Namna nyingine ya kulitia moyo kanisa ni kukaa katika maombi, kufunga na kuabudu na kufundisha Barnaba alikuwa mstari wa mbele kufanya hayo mimi naamimi kwa vyovyote vile aliutafuta uso wa Bwana na kuwaombea wengine, alitumiwa na Mungu pia kwa ishara na miujiza maana yake aliwaponya watu wengine na pia kujitoa katika kazi ngumu sana ya umisheni.
II.       Alilitia moyo kanisa kwa kutumia neno la Mungu
·         Alilitia moyo waamini kukaa katika imani bila kujali dhiki Matendo 14:21-22 Barnaba na Paulo walilikumbusha kanisa kuwa imetupasa kuingia katika ufalme wa Mungu kwa njia ya dhiki nyingi, waliwakumbusha kuvumilia na kuwatia moyo, fikiria kama unapitia majaribu ya aina mbalimbali na hakuna wa kukutia moyo, je ungedumu katika imani?
·         Alilitia moyo kanisa kwa kutafuta suluhu ya kanisa la mataifa kuhusu tohara Matendo 15:1-2 Injili mbaya ya kutahiriwa kwanza ndipo uokoke ilipolivamia kanisa Barnaba akiwa na Paulo walibishana na waalimu hao wa uongo, lakini pia walikwenda Yerusalem kwaajili ya kutafuta suluhu ili kanisa liweze kufarijika
·         Alilitia moyo kanisa kupitia shuhuda za matendo makuu ya Mungu Matendo 15:12
·         Alilitia moyo kanisa kupitia waraka na maneno Matendo 15:31-32 baada ya maamuzi ya mitume waliyarudia makanisa yaliyosumbuliwa na fundisho baya na kuyaimarisha kwa misimamo ya mafundisho sahii na maamuzi ya kanisa kutoka mkutano wa Yerusalem
III. Alilitia moyo kanisa kupitia kuwepo kwake
·         Ulimwengu huu ni ulimwengu wa changamoto mbalimbali una dhiki nyingi Yohana 16:33
·         Ayubu ni moja ya mfano wa watu waliokutana na mambo magumu sana kiasi ambacho hata waliokuja kumfariji walikaa kimya kwa siku saba Ayubu 1;13-19,2;7-11-13
·         Kuwa na watu kama kina Barnabas ni kwa muhimu sana kwa sababu ziko nyakati ambazo kama wanadamu tunahitaji faraja kwani yako mambo yanatuelemea Majukumu ya kifamilia, watoto wasiosikia na kutii, mikwaruzo katika ndoa, Hofu za kupoteza ajira, mishahara isiyotosheleza mahitaji yetu, hasara za kibiashara, kazi nyingi nyumbani, upweke, kuvunjika kwa uchumba, lawama kutoka kwa ndugu, lawama kazini, lawama kwa bosi, mahitaji ya ada za wanafunzi, Bili za umeme, bili za maji, kodi ya mwenye nyumba mahitaji ya wazee kijijini, mahitaji ya palizi au maandalizi ya mashamba kupanda kwa bei ya vyakula, nguo za watoto, kusengenywa, mafarakano, visa vya majirani, mashambulizi ya wachawi, kuuguliwa, madeni ya vikundi vya mikopo saccos, kupigwa nyundo Kanisani, shida za washirika na wachungaji hali kama hizi na nyinginezo nyingi ndizo zinazopelekea Kuweko na hitaji la kufarijiwa au kutiwa moyo hili ni jambo muhimu sana na linahitajika sana katika wakati huu tulionao kuliko nyakati nyingine zozote, Huduma za watumishi kama Barnaba zinahitajika sana wakati wa maswala mzito kama hayo.

Hitimisho:                
Tafadhali kuwa mtu mwenye kutia moyo wengine na kuwafariji, usiwe mtu wa kuwaponda tu na kuwasema wengine vibaya utakuwa mwana wa uharibifu, Mungu anataka kina barnaba wawepo kila mahali , katika taifa, familia, mashuleni, majumbani na katika taasisi mbalimbali
Jihadhari kuwa mkosoaji na mvunjaji moyo watu yako maswala mazuri ambayo wanadamu wanayo hayo ndio vema yakajadiliwa kwa mujibu wa fundisho la kibiblia “Wafilipi 4:8
Uwepo wetu uwe na thamani kwa sababu kupitia kuwatia moyo wengine na kuwafariji dunia itakua mahali pazuri pa kukaa salama, utakumbukwa duniani kutokana na mchango wako mkubwa kwa jamii na dunia itaona ni afadhali umeondoka endapo utakuwa mtu mwenye kuharibu wengine

·         Barnaba alikuwa mwenye kujali wengine Caring
·         Barnaba alikuwa mwenye kutia matumaini wengine wasikate tamaa Consoler
·         Barnaba alikuwa ni mwenye kuwahurumia wengine Compassionate
·         Barnaba hakuwa mtu wa kubadilika badilika katika huduma aliyokuwa nayo Consistent
·      Alikuwa jasiri katika kile alichokiamini kuwajenga wengine na kuwatetea kwa gharama yoyote ile Convictions

Katika kuhudumia kwangu kanisa la Mungu mtu anayefanana na Barnaba ambaye mimi nimewahi kumuona ni rafiki yangu mmoja anaitwa Raphael Sallu Yeye ni Mchungaji wa TAG Mkanyageni huko Muheza huyu jamaa ni kama Barnaba siongei kumtetea kwa sababu ni rafiki yangu hapana lakini ndivyo alivyo.

Na Mkuu wa wajenzi mwenye Hekima

Rev. Innocent Kamote.