Alhamisi, 6 Oktoba 2016

Nabii Obadiah


OBADIA MTUMISHI WA MUNGU NABII WA HAKI

Mwandishi wa kitabu cha Obadia.

A.     MWANDISHI NI NABII OBADIA MWENYEWE

-          Jina lake maana yake ni mtumishi wa Mungu sawa na “Abdullah” la kiarabu
-          Ni maarufu kama nabii wa haki
-          Kitabu chake hakina nukuu yoyote kuhusu yeye kazi yake  na wito wake
-          Tunajua kuwa alikuwa ni Nabii aliyetumwa huko Edomu kusini mashariki ya Yordani
-          Kitabu chake ndio kifupi kuliko vyote katika agano la kale
-          Tareha ya uandishi inakadiriwa kuwa mwaka wa 586 k.k.
-     Obadia haelezi ni lini alipata maono  na ingawaje ni kutokana na yale anayoelezea unaweza  kuhisi kuwa huenda ni baada ya anguko la Yerusalem

B.     UPEKEE WA KITABU CHA OBADIA 

-          Ni kitabu cha pekee katika ujumbe wake na urefu wake
-          Ni kifupi kuliko vyote katika Agano la kale na kinabeba Tangazo na hukumu nzito kuhusu dhambi
-          Ujumbe wa Obadia kimsingi uliihusu Edomu wana wa Esau  ingawa aligusia na kurejezwa tena kwa Wayahudi ambako kutatimia kwa ukamilifu atakapokuwa anarudi Kristo baada ya dhiki ile kuu

C.     HISTORIA YA MATUKIO KATIKA KITABU CHA OBADIA

-          Mwanzo 25;21-34,27;32-33 Hesabu 20;14-21, 2samuel 8;11-14-14, 2Nyakati 20;1-24,21;8-16
-          Ili kukifahamu kitabu cha Obadia Vizuri msomaji anapaswa kurudi nyuma na kuangalia maisha ya Mapacha wa Isaka yaani Yakobo na Esau
-          Mashindano yao yalianza tangu tumboni mwa mama yao na yaliendelea kwa karne nyingi katika ya vizazi vyao Mwanzo 25;21-34 watoto wote walikuwa na wazazi wacha Mungu na haki sawa ingawaje Esau alikuwa na shauku kwa mambo ya mwilini zaidi wakati Yakobo alikuwa na shauku ya mambo ya kiroho licha ya kuwa mwenye dhambi alikuwa na shauku katika Mungu na ahadi zake Waebrania 12;16 inasema Esau hakuwa mcha Mungu
-          Mungu aliona tabia zao hata kabla ya Kuzaliwa Mwanzo 25;23 Tabia tofauti na mitazamo Tofauti iliwapelekea vijana hao katika muelekeo Tofauti kidini, kiuchumi, na kimafanikio.
-          Upendeleo ulionyeshwa na kila mzazi ulichangia katika kuelekea kwenye migogoro wao
-          Baraka ambazo Isaka baba yao alikusudia kumpa Esau na zikaibiwa na Yakobo zilipelekea Chuki kubwa ya Esau dhidi ya Nduguye, Esau aliapa kuwa atamuua Yakobo na hii ilipelekea Yakobo kukimbia mpaka Padan- aram kwa mjomba wake Labani
-          Esau alitunza kisasi hicho kwa miaka 20 hivi mpaka wakati Yakobo  alipokuwa anarudi na Esau alituma kikosi cha askari 400 kumuua Lakini kwa neema ya Mungu, Mungu aliingilia kati na  wakapatana
-          Ingawa Esau na kizazi chake chote hawakuweza kuushinda uchungu waliokuwa nao dhidi ya Yakobo na kizazi chake
-          Miaka 300 baadaye kwa ajili ya uchungu na chuki Edomu haikuwaruhusu Israel kupita katikati yao walipokuwa wakitoka Misri Hesabu 20;14-21.
-          Mwaka 1042 k.k yaani kama miaka 700 hivi baadaye Daudi alizipiga nchi jirani na kupanua mipaka ya Israel na kuwafanya wana wa Esau yaani Edomu kulipa kodi yaani kutimiza unabii kuwa Esau angemtumikia Yakobo.
-          Wakati wa utawala wa Yehoramu Edomu waliasi 2Falme 8;20-22 na miaka 146 ilipita ndipo Edomu wakiungana na Waamoni na Wamoabu waliivamia Yuda wakati wa utawala wa Yehoshafati lakini Mungu alimpa Yuda ushindi.
-          Mwaka wa 586 k.k Edomu walifurahia ilipoanguka Yerusalem Zaburi 137;7 Ezekiel 35;15
-          Inaonekana kuwa baada ya Waedomu kushirikiana na Wakaldayo waliruhusiwa kukaa kusini mwa Israel baada ya wayahudi kuchukuliwa mateka huko Babeli
-          Walifanikiwa sana, lakini Makabayo baadae aliwashinda na kuwalazimisha kushika sheria za kiyahudi na baadaye wayunani na Warumi walipotawala waliliita eneo hilo Idumeya
-          Inasemekana kwamba Mfalme Herode mkuu anatokea katika jamii hiyo na eneo hilo
-          Baada ya mwaka wa 70 B.K Waedomu walimezwa na waarabu na wametoweka leo hawako kama Taifa au kabila.

D.     MISTARI YA MUHIMU

-          Msatari wa 3-4
-          15
-          17
-          21

E.     MIGAWANYO YA KITABU CHA OBADIA

-          Kuanguka kwa Edomu Mstari wa 1-16
-          Kuhuishwa kwa Israel Mstari wa 17-21

F.      UCHAMBUZI
*      Hukumu ya Mungu dhidi ya Edomu mstari wa 1-14.
-          Unabii unahusu kuanguka kwa Edomu  mstari wa kwanza unaonyesha kuwa kile Mwandishi aliandika sio mawazo yake lakini Mungu alikuwa amemfunulia “Tumesikia ujumbe kutoka kwa Bwana” hii inaweza kuhusu  Obadia kusikia kutoka kwa Mungu kabla ya kuandika na huenda Yeremia na Ezekiel pia walipokea ujumbe kama huo.
-          Mjumbe aliyetumwa inaweza kuwa Malaika au Roho wa Bwana aliyetumwa kuyachochea mataifa  kuinuka dhidi ya Edom


G.    HALI YA EDOMU
-          Walikuwa na kiburi Mstari wa 2-4 walijiinua kwa sababu walikuwa na eneo lisiloweza kuvamiwa na mafanikio ya kijeshi na kisiasa waliyokuwa nayo iliwapelekea Kujiamini na kuacha kumtumaini Mungu Zaburi 127;1 Bwana asipoulinda mji aulindaye akesha bure.


                 
Mabaki ya mji wa wa Petra ambao ulikuwa chini ya serikali ya Edomu kama ngome zake zinavyoonekana leo Picha na maelezo kwa hisani ya Maktaba ya Mchungaji Innocent Kamote.

-          Ingawa mji wao ulikuwa jangwani lakini mataifa mengi yaliionea wivu Edomu kwani walikuwa matajiri  wa visima vya maji na mabonde mazuri
-          Walikuwa na madini ya chuma na shaba na njia kuu za kibiashara  hata kwa njia ya bahari  hivyo utajiri wao pia ulichangia kiburi walichokuwa nacho Mstari wa 5,-6.
-          Edomu waliifanya biashara na Syria, Ashuru, India, Misri, Arabuni na Afrika
-          Mstari wa 5-6 unaonekana katika maono ya Obadia  kwamba wangepoteza utajiri wao moja ya mji wao mzuri ungetekwa  na huu ni mji wa Petra kiyunani au Sela kiibrania ambalo jina hilo maana yake ni mwamba,
-          Ilikuwa ni ngome kabambe isiyoweza kuanguka, tajiri na yenye kuzungukwa na mawe kila upande Linganisha Edom na ushauri unaotolewa katika 1Timotheo 6;1-19 hasa 17.
-          Kumbuka maagizo ya Mungu kwa Israel walipokuwa wakitoka Misri katika Kumbukumbu 2;4-5 na 23;7 na kitendo cha Waedom Hesabu 20;14-21 lakini pamoja na hayo chuki yao iliendelea Zaburi 137;7 na kulingana na  Ezekiel 35;1-11 Kitendo cha Edomu kilitokana na chuki na wivu wa kale  Galatia 6;7wenye uchungu.
-          Kumbuka!
           Mungu atayahukumu au huukumu mataifa kulingana na jinsi yanavyoshughulika na watu wengine na hususani watu wake aliowachagua Edomu walihukumiwa kutokana na tendo lao la kuwa kinyume na wanaoteseka katika Mathayo 25;31-46 Yesu alifundisha kuwa tuwasaidie wale wanaoteseka au wenye uhitaji kama wakimbizi, wathirika, masikini na wenye vita sasa ukilinganisha Matendo ya Edomu na Mathayo 5;43-45 na 1Yohana 3;15-18 tunajifunza kanuni za kuwapenda maadui zetu na chuki zinatufanya kuwa wauaji mbele ya macho ya Mungu kama hatia iliyowapata Edomu.

H.    SIKU YA BWANA MSTARI WA 15-17. 

Kwa ujumla hii inazungumzia swala la siku ya hukumu ya Mungu dhidi ya Maadui zake, Pia hutumiwa na Manabii kuelezea matukio ya mwisho wa dunia ambayo hujumuisha
·         Kunyakuliwa kwa kanisa
·         Dhiki kuu
·         Vita vya Armageddon
·         Kurudi kwa Yesu mara ya pili katika utukufu
·         Kuokolewa kwa Israel
·         Hukumu ya mataifa
·         Utawala wa Yesu Kristo wa miaka 1000 duniani
              Kwa ajili ya Edomu siku ya Bwana ilimaanisha siku ya hukumu ya Edomu kwa ajili ya uchungu dhidi ya Ndugu zao
-          Kiburi kingine cha Edomu ilikuwa ni rafiki zao Mstari wa 7 Waarabu walikuwa ndio rafiki wa karibu wa Waedomu  na walijiunga nao katika kuishambulia Yuda Zaburi 83;5-6 pia rafiki zao Waamini, Wamoabu, na wengine waliifanya biashara nao hawa waliwageuka
-          Kiburi cha kisiasa Mstari wa 8-9 Waliwategemea wenye Hekima, Viongozi wao wa kisiasa washauri na majeshi wataalamu wa Vita wa mlima Seiri  walijulikana sana kwa Hekima na maarifa ya ulimwengu inasemekana watu Rafiki wa karibu wa Ayubu mwenye Hekima Elifazi Mtemani alitokea Temani  ambazo ni sehemu za Edomu Linganisha msatari wa 9 na  Ayubu 2;11. Hekima ya kibinadamu inaweza kutumiwa kwa ajili ya Mungu na kwa utukufu wake kuufanya ulimwengu kuwa mahali pa salama Yakobo 1;5 Ingawaje maarifa na Hekima pasipo Mungu  haiwezi kusaidia katika kuikwepa hukumu yake.
-          Kiburi kilichotokana na nguvu za kijeshi mstari wa 9; na kuwa na makomandoo wa kivita  mashujaa watemani vilitilia hofu mataifa mengine Yeremia 49;16 walijitumainia katika hali hiyo lakini ilitabiriwa kuwa askari wake wangechinjwa na watu wangeachwa bila ya ulinzi
-          Sababu kuu za Maangamizi ya Edomu ni Mstari wa 10-14.

*      Uasi dhidi ya Ndugu zao
*      Kusimama peke yao kujitenga kiburi cha Kujiamini
*      Kufurahia maangamizi ya ndugu zao
*      Kuwadharau ndugu zao na kuwasengenya siku ya taabu zao
*      Kufurahia utajiri na mali za ndugu zao na Kuwashambuilia mateka waliosalia.

Uhusiano wa Kanisa na Israel


Wakristo wengi hawaelewi uhusiano ulioko kati ya Kanisa na Taifa la Israel Ni muhimu kufgahamu kuwa hatuwezi kuepuka nlabda kwa shingo ngumu kuwa kwa namna yoyote ile uhusiano ulioko kati ya kanisa yaani wakristo na wana wa Israel kuwa tuna uhusiano katika ilimwengu wa Roho ingawa tunaweza tusiwe na uhusiano wa kitaifa au kibalozi lakini katika Mungu Israel wanaungwa mojakwa moja na Kanisa Tutajifunza somo hili kwa kuzingatia vipengele  vitatu vifuatavyo;- 

  • ·         Israel imewekwa wakfu
  • ·         Kwa nini niipende Israel
  • ·         Uhusiano wa Kanisa na Isarel

Israel imewekwa wakfu.

Neno wakfu au kuwekwa wakfu maana yake ni kutenga kitu au watu au kutakasa kitu au mtu ili atumike kwa utukufu wa Mungu na si vinginevyo au kulaani kisitumike kwa namna nyingine isipokuwa Mungu tu na kwa sababu hiyoi kitu au mtu anapokuwa amewekwa wakfu anafanyika kuwa mali ya Mungu Kutoka 13;2, 29;1

     Katika maana hiyo basi ni muhimu kufahamu kuwa Israel ni Taifa au kabila na jamaa ambayo imewekwa wakfu, imeteuliwa  na kutengwa  kwa kusudi maalumu hivyo wao ni mali ya Mungu Kumbukumbu 14;2,4;20,Zaburi 135;4. Israel ni Taifa la Mungu na Yerusalem  ni mji wake mtakatifu na kamwe Mungu hawezi kuwasahahu mji hu na inchi hii na watu wake Zaburi 137;5-6, Mungu wa Israel ndiye Mungu tunayemuabudu  wokovu tulio nao umetoka kwa wayahudi, Masihi tunayemwadhimisha alikuwa myahudi na ametoka kwa wayahudi, hata mifumo ya ibada zetu tumerithi kwa wayahudi na Biblia tuliyo nayo kwa sehemu kubwa imeandikwa na wayahudi na manabii wote tunaowaamini ni wa jamii ya kiytahudi  kwa msingi huo kanisa linapaswa kuwa na uzalendo wa kisayuni kwa wana wa Israel na kuonyesha kuwapewnda na kuwajali na kuwa wanatuhusu, Leo hii vyomboi vya habari  na jamii ya watu wengine wa kisiasa na ulimwengu wa Kiislamu wamekuwa na mtazamo duni na hafifu dhidi ya Israel  na hivyo kuichukia na wakati mwingine kuilaani katika vitendo kadhaa jambo hili linapaswa kuchukuliwa kwa umakini na watu wanayoyajua maandiko Hili ni taifa masihi na ni taifa la Mungu  ardhi hii aliyopewa Ibrahimu alipewa na Mungu kwa hiyo kila mkristo anapaswa kuielewa siri hii na kuipenda Israel

Kwanini niipende Israel

1.       Kuipenda Israel ni kumpenda Mungu

Amri iliyo kuu kuliko zote ni kumpenda Bwana Mungu Kumbukumbu 6;5, kama tunampenda Mungu kwa dhati , bila hska pia tutapenda kile anachokipenda  na kuchukia anacho kichukia , Maandiko yanaonyesha kuwa Mungu anaipedna Israel na mji wake Yerusalem Zaburi 87;1-2 Labda mtu atasema sisi wenyeji wetu uko mbinguni na kama Abrahamu tunautazamia mji wenye misingi ambao mwenye kuubuni na kuujenga ni Mungu  Waebrania 11;10, Wafilipi 3;20,Wagalatia 4;26 dhana hiyo ni kweli kabisa  kila mkristo anajua kuwa kuna mji Yerusalemu ya mbinguni na Yesu alisema Yerusalemu huu wa sasa hatuwezi kukwea na kwenda kuabudu Yohana 4;21-24 Lakini Maneno ya Bwana yesu yanshitua zaidi unaposoma katika Mathayo 5;34-35 kluwa usiape kwa Yerusalem nmaana ndio mji wa mfalme mkuu (Yaani Mungu) na Yesu alisema kuwa mji huu utakanyagwa na mataifa kwa wakati tu Luka 21;24 uko wakati ambapo Heshima na utukufu wa Mungu utarudi na Mungu mwenyewe ataiatawala Dunia  nzima kuanzia hapa Israel Zekaria 14;4,9.


Pichani ni jiji la Yerusalem ambalo wayahudi wameapa hautagawanywa milele ,Upande wa kushoto ni Msikiti (The Dome of Rock) ukiwa umejengwa mahali ambapo palikuwa ni Hekalu la Wayahudi, hapo ni mahali makini wayahudi hawajapagusa bado,Waislamu huamini ndipo alipopaa Muhamad kwenda mbinguni (Uongo mtupu),na ni kibla ya kwanza kabla ya Makka.Ukouwezekano kwa wayahudi wenye msimamo mkali wa kidini kulijenga tena hekalu hilo mahali hapa 
(Picha kwa hisani ya maktaba ya Mwandishi wa somo Innocent Samuel Kamote.)

2.       Kuipenda Israel ni ufunguo wa mafanikio

Mungu amekuwa mwema kwa Israel kwa karibu miaka 1720 hivi Waisrael hawakuweko katika inchi yao mpaka mwaka wa 1948 waliporudi ambapo mji wao mkuu kwa wati huo ulikuwa ni Tel-aviv-Jafa ambao una bandari na wakati huo Yerusalemu haukuwa mikononi mwao Leo mji huu uko mikononi mwao Mungu ameanza kuirehemu Israel sawa na Zaburi ya 102;13-14 katika wakati huu ambapo Israel inazungukwa na mataifa adui wasio watakia mema hata kidogo ni muhimu kuipenda Israel na kuwaombea amani  kwani kwa kufanya hivi tunaruhusu Baraka biunafsi na za taifa letu kwa ujumla Zaburi 122;1-9

3.       Kwa sababu kanisa ni tawi na Israel ni shina yaani (asili).

Mkristo awaye tyote na mchungaji au kikundichochote cha faragha wanapaswa kutambua kuwa Israel ndio shina la wokovu wetu  au ni sawa na tawi lililopandikizwa katika shina ambalo ka asili ni Israel Warumi 11;11-21  Mungu anatuionya kanisa kuwa sisi ni tawi tu lililopandikizwa na Israel ndio shina halisi, kutokutii kwao na kumkatraa maishi kumeleta wokovu mkubwa kwa amataifa mengine kluweza kufurahia neema hii ya wokovu na baraka zitakuwa kubwa zaidi kama wakitii, kwa msingi huo kutokuipenda Israel ni kuchukia asili huku sisi tukiwa ni tawi tu lililopandikizwa Yesu alionyesha dhahiri kuwa wokovu wetu asili yake unatoka kwa wayahudi Yohana 4;22  Biblia yote kuanzia Mwanzo mpaka Malaki ambayo tunaiita Agano la kale  ni kitabu cha Mungu kwetu lakini kwa asili ni Biblia ya waebrania yaani wayahudi kwa msingi huo huwezi kamwe kumteganisha Mkristo na Myahudi adui wa wayahudi lazimam pia anakuwa ni adui wa wakristo anayetaka kuifuta Israel Bila shaka pia atataka kuufutilia mbali ukristo kwa msingi hio kila mkristo anawajibika kuikumbuka Israel

4.       Kuilaani Israel ni kujilaani na kuibariki Israel ni kujibariki

Tangu mwanzo Mungu alipomuita Ibrahimu ambaye ndiye baba wa Taifa hili alimtamkia Baraka zitakazoambatana na wale watakaombariki lakini pia Mungu aliweka laana kwa wale watakaomlaani Ibrahimu Mwanzo 12;1-3,26;1-6,28;10-15 Baraka hizio na matamko haya yanawahusu Israel hata leo kwa msingi huo kila mtu anapaswa kufahamu kuwa Mungu yuko nyuma ya maswala yote ya Israel tangu wakati wa Ibarahimu na uzao wake  wale watakaomnenea mema watabarikiwa na wale wanaomnenea vibaya watalaaniwa. Tafuta ukaone katika historia wale wote waliowahi kuitishia Israel waliishia wapi na Historia itakuambia kuilaani Israel ni kujiweka katika hatari

Uhusiano wa Kanisa na Israel.

Tumeona kwa namna Fulani uhusiano ulioko katia ya Israel na kanisa mwanzoni tulipokuwa tunazungumzia kwanini niipende Israel, Kanisa linapaswa kuelewa kuwa Mungu yuko pamoja na Israel na kuwa tunauhusiano mmoja kama tulivyoona sisi nasi tunapaswa kuhakikisha kuwa katika shughuli zetu za kimisheni pia tunawalenga wayahudi ili nao waokolewe Paulo mtume alikuwa na huruma sana dhidi ya ndugu zake hawa yaani wayahudi ambao sisi pia ni ndugu zetu  kwamba waokolewe na alikuwa akiwaombea sana Soma warumi 10;1 sisi nasi tunapaswa kuhakikisha kuwa tunawahubiria wokovu kwa kawaida kunakuwa na kitu cha ziada sana myahudi anapookoka wengi waliookolewa wametumiwa sana na Mungu aktika kuupanua Ufalme wake akiwemo Muhubiri maarufu Mourice Cerrulo na Benny Hinny Mungu na alisaidie kanisa kukumbuka kuwa na mkakati maalumu kuomba na kuhakikisha kuwa injili inawafikia wao pia aidha ni muhimu kanisa kuwaombea viongozi wetu wa kitaifa kuwa makini na kauli zao za kisiasa wanazozitamka dhidi ya Utendaji wowote wa kisiasa wa Israel, Wamarekani wengi wanaifahamu siri hiyo, kama unailaani Israel kasha unakwenda Marekani kuomba misaada ambao wao kuybarikiwa kwao kunatokana na kuwafanyia mema wayahudi je unadhani utafaidika au umasikini utaendelea kutufunika tu, wayahudi ni Ndugu zetu, Mungu wao ni Mungu wetu, manabii wao ni manbabii wetu, Mwokozi wao ni mwokozi wetu Biblia yao ni Biblia yetu, tumaini lao ni tumaini letu, mji wao ni mji wetu nukombozi wao ni ukombozi wetu tunauhusiano wa kudumu na Israel

somo limeandaliwa na 

Rev. Innocent Kamote
Mkuu wa wajenzi mwenye Hekima

Jumamosi, 24 Septemba 2016

Umuhimu wa maombi wakati wa mambo magumu!



Andiko la msingi: Zaburi 46:1-2Mungu kwetu sisi ni kimbilio na Nguvu, Msaada utakaoonekana tele wakati wa mateso, kwa hiyo hatutaogopa ijapobadilika nchi, Ijapotetemeka milima moyoni mwa Bahari

              Gereza ambalo Paulo na Sila walifungwa wakaomba na vifungo vikaachia huko Philipi


Utangulizi.
Kwa mujibu wa Mafundisho ya kibiblia kuhusu Maombi, Biblia inatoa maelekezo kwamba imetupasa kumuomba Mungu siku zote bila kukata tamaa Luka 18:1Akawaambia mfano ya kwamba imewapasa kumwomba Mungu siku zote , wala wasikate tamaa” kwa lugha nyingine imetupasa kumuomba Mungu siku zote bila kukoma 1Wathesalonike 5:17Ombeni bila kukoma” ni wazi kuwa  Biblia inatia moyo kuwa waombaji na kila siku kumuomba Mungu na kushukuru, ni katika hali zote na kwa namna yoyote imetupasa kuomba Maombi ni muhimu sana katika maisha yetu, na katika kudumisha uhusiano wetu na Mungu, Yesu alikuwa Muombaji, hatuna budi kuunganisha ucha Mungu wetu na maombi, kuacha maombi ni sawa na kuacha Ukristo!

Lakini kila mmoja anaweza kujiuliza kwa nini leo mkuu wa wajenzi anataka au anazungumzia Umuhimu wa maombi wakati wa mambo Magumu, Kwa ujumla maombi yanapaswa kuwa sehemu na tabia ya kila amwaminiye Yesu Kristo, Na pamoja na hayo binafsi sipendi kuomba wakati wa mambo magumu, nafurahia sana kuomba wakati wa amani, hata hivyo kibiblia wakati wa mambo magumu sio wakati wa kuacha kuomba ni wakati wa kuongeza bidii katika kuomba. Biblia inatufundisha kuwa nyakati za Kanisa la kwanza wakristo wa Karne ya kwanza walikuwa waombaji, sehemu kuu ya ibada ya kawaida ya kanisa ilikuwa ni maombi, waliomba Mungu siku zote, Biblia inasema walikuwa wakidumu kwa moyo mmoja katika kusali Matendo 2:14Hawa wote walikuwa wakidumu kwa moyo mmoja katika kusali,pamoja nao wanawake, na Mariamu mama yake Yesu na ndugu zake” Unaona! Biblia inaonyesha kuwa wanafunzi na mama yake Yesu na ndugu zake walidumu katika kuomba hii ndio ilikuwa tabia ya nyakati za kanisa la kwanza.

Lakini hata hivyo tunaweza kuona katika biblia Kanisa la kwanza wakiongeza Maombi zaidi wakati wa mambo magumu, kama andiko la msingi pale juu linaonyesha kuwa Mungu kwetu sisi ni kimbilio na nguvu, ni msaada utakaoonekana tele wakati wa Mateso, hii maana yake ni kuwa ni lazima na ni muhimu kuliitia jina la bwana zaidi wakati wa mateso na majaribu Matendo 4:23-31 Biblia inasema

 “23. Hata walipofunguliwa, wakaenda kwa watu wao, wakawapasha habari ya mambo yote waliyoambiwa na wakuu wa makuhani na wazee. 24. Nao waliposikia, wakampazia Mungu sauti zao kwa moyo mmoja, wakisema, Mola, wewe ndiwe Mungu, ndiwe uliyefanya mbingu na nchi na bahari na vitu vyote vilivyomo; 25. nawe ulinena kwa Roho Mtakatifu kwa kinywa cha babaetu Daudi, mtumishi wako, Mbona mataifa wamefanya ghasia, Na makabila wametafakari ubatili? 26. Wafalme wa dunia wamejipanga, Na wakuu wamefanya shauri pamoja Juu ya Bwana na juu ya Kristo wake. 27. Maana ni kweli, Herode na Pontio Pilato pamoja na Mataifa na watu wa Israeli, walikusanyika katika mji huu juu ya Mtumishi wako mtakatifu Yesu, uliyemtia mafuta, 28. ili wafanye yote ambayo mkono wako na mashauri yako yamekusudia tangu zamani yatokee. 29. Basi sasa, Bwana, yaangalie matisho yao; ukawajalie watumwa wako kunena neno lako kwa ujasiri wote, 30. ukinyosha mkono wako kuponya; ishara na maajabu vifanyike kwa jina la Mtumishi wako mtakatifu Yesu. 31. Hata walipokwisha kumwomba Mungu, mahali pale walipokusanyika pakatikiswa, wote wakajaa Roho Mtakatifu, wakanena neno la Mungu kwa ujasiri.”

 Unaweza kuona Kumbe wakati wa majaribu na mateso pia ni wakati mzuri wa kuongeza bidii na kumuomba Mungu kwa nguvu zaidi, Muda usingeliweza kutosha kwa nyongeza ya mifano zaidi ya kibiblia lakini biblia inaonyesha pia Paulo na Sila walipokuwa Gerezani yaani wakati wa mateso waliendelea kukazia ibada Matendo 16:25Lakini panmapo usiku wa manane Paulo na Sila walikuwa wakimwomba Mungu na kumwimbia nyimbo za kumsifu na wafungwa wengine walikuwa wakisikiliza” unaona ukiendelea kusoma utaweza kuona ni nini kilitokea Mungu alipowajibu maombi yao hivyo Biblia inatufundisha kuwa tusikate tamaa na kuwa hata wakati wa mambo magumu inatupasa kuomba 

1.       Kwa nini inatupasa kumuomba Mungu hata wakati wa Mambo Magumu
2.       Maombi ni msaada kutoka kwa Mungu wakati wa mambo Magumu Zaburi 3:3-8;34:4
1.Bwana, watesi wangu wamezidi kuwa wengi, Ni wengi wanaonishambulia, 2. Ni wengi wanaoiambia nafsi yangu, Hana wokovu huyu kwa Mungu. 3. Na Wewe, Bwana, U ngao yangu pande zote, Utukufu wangu na mwinua kichwa changu. 4. Kwa sauti yangu namwita Bwana Naye aniitikia toka mlima wake mtakatifu. 5. Nalijilaza nikalala usingizi, nikaamka, Kwa kuwa Bwana ananitegemeza. 6. Sitayaogopa makumi elfu ya watu, Waliojipanga juu yangu pande zote. 7. Bwana, uinuke, Mungu wangu, uniokoe, Maana umewapiga taya adui zangu wote; Umewavunja meno wasio haki. 8. Wokovu una Bwana; Baraka yako na iwe juu ya watu wako.

3.       Maombi ndio njia ya Mungu ya kutulinda na nguvu na utendaji wa yule muovu Mathayo 6:13, Efeso 6:12.
4.       Maombi ndio njia pekee ya kutuletea amani tunapokutana na Magumu na hali za kutisha na kukatisha tamaa Wafilipi 4:4-7
5.       Maombi yanaweza kupindulia mbali vikwazo vya aina zote Marko 11:23-24
6.       Maombi ndio njia ya kututia moyo wakati wa kuvunjika Moyo Wakolosai 1:9-11
7.       Maombi yana nguvu ya kuhairisha jambo baya Esta 4:15-17, Daniel 2:13-19
8.       Maombi ndio njia ya kupokea nguvu za kiroho na ujasiri wakati wa vita za kiroho Matendo 4:23-31

Bila shaka sasa unaweza kuona na kuamini kupitia maandiko, kuwa wakati wa mateso na Mapito na mambo magumu ya aina yoyote ile, huo sio wakati wa kukata tamaa na kuacha kuomba ni wakati wa kuzidisha maombi na kumtegemea Mungu, Na Mungu hujitokeza  kwa viwango vikubwa tukionyesha kumtegemea yeye katika maombi wakati wa Mahitaji yetu katika wakati mgumu.

Rev. Innocent Kamote
Mkuu wa wajenzi mwenye Hekima.