Alhamisi, 6 Oktoba 2016

Nabii Obadiah


OBADIA MTUMISHI WA MUNGU NABII WA HAKI

Mwandishi wa kitabu cha Obadia.

A.     MWANDISHI NI NABII OBADIA MWENYEWE

-          Jina lake maana yake ni mtumishi wa Mungu sawa na “Abdullah” la kiarabu
-          Ni maarufu kama nabii wa haki
-          Kitabu chake hakina nukuu yoyote kuhusu yeye kazi yake  na wito wake
-          Tunajua kuwa alikuwa ni Nabii aliyetumwa huko Edomu kusini mashariki ya Yordani
-          Kitabu chake ndio kifupi kuliko vyote katika agano la kale
-          Tareha ya uandishi inakadiriwa kuwa mwaka wa 586 k.k.
-     Obadia haelezi ni lini alipata maono  na ingawaje ni kutokana na yale anayoelezea unaweza  kuhisi kuwa huenda ni baada ya anguko la Yerusalem

B.     UPEKEE WA KITABU CHA OBADIA 

-          Ni kitabu cha pekee katika ujumbe wake na urefu wake
-          Ni kifupi kuliko vyote katika Agano la kale na kinabeba Tangazo na hukumu nzito kuhusu dhambi
-          Ujumbe wa Obadia kimsingi uliihusu Edomu wana wa Esau  ingawa aligusia na kurejezwa tena kwa Wayahudi ambako kutatimia kwa ukamilifu atakapokuwa anarudi Kristo baada ya dhiki ile kuu

C.     HISTORIA YA MATUKIO KATIKA KITABU CHA OBADIA

-          Mwanzo 25;21-34,27;32-33 Hesabu 20;14-21, 2samuel 8;11-14-14, 2Nyakati 20;1-24,21;8-16
-          Ili kukifahamu kitabu cha Obadia Vizuri msomaji anapaswa kurudi nyuma na kuangalia maisha ya Mapacha wa Isaka yaani Yakobo na Esau
-          Mashindano yao yalianza tangu tumboni mwa mama yao na yaliendelea kwa karne nyingi katika ya vizazi vyao Mwanzo 25;21-34 watoto wote walikuwa na wazazi wacha Mungu na haki sawa ingawaje Esau alikuwa na shauku kwa mambo ya mwilini zaidi wakati Yakobo alikuwa na shauku ya mambo ya kiroho licha ya kuwa mwenye dhambi alikuwa na shauku katika Mungu na ahadi zake Waebrania 12;16 inasema Esau hakuwa mcha Mungu
-          Mungu aliona tabia zao hata kabla ya Kuzaliwa Mwanzo 25;23 Tabia tofauti na mitazamo Tofauti iliwapelekea vijana hao katika muelekeo Tofauti kidini, kiuchumi, na kimafanikio.
-          Upendeleo ulionyeshwa na kila mzazi ulichangia katika kuelekea kwenye migogoro wao
-          Baraka ambazo Isaka baba yao alikusudia kumpa Esau na zikaibiwa na Yakobo zilipelekea Chuki kubwa ya Esau dhidi ya Nduguye, Esau aliapa kuwa atamuua Yakobo na hii ilipelekea Yakobo kukimbia mpaka Padan- aram kwa mjomba wake Labani
-          Esau alitunza kisasi hicho kwa miaka 20 hivi mpaka wakati Yakobo  alipokuwa anarudi na Esau alituma kikosi cha askari 400 kumuua Lakini kwa neema ya Mungu, Mungu aliingilia kati na  wakapatana
-          Ingawa Esau na kizazi chake chote hawakuweza kuushinda uchungu waliokuwa nao dhidi ya Yakobo na kizazi chake
-          Miaka 300 baadaye kwa ajili ya uchungu na chuki Edomu haikuwaruhusu Israel kupita katikati yao walipokuwa wakitoka Misri Hesabu 20;14-21.
-          Mwaka 1042 k.k yaani kama miaka 700 hivi baadaye Daudi alizipiga nchi jirani na kupanua mipaka ya Israel na kuwafanya wana wa Esau yaani Edomu kulipa kodi yaani kutimiza unabii kuwa Esau angemtumikia Yakobo.
-          Wakati wa utawala wa Yehoramu Edomu waliasi 2Falme 8;20-22 na miaka 146 ilipita ndipo Edomu wakiungana na Waamoni na Wamoabu waliivamia Yuda wakati wa utawala wa Yehoshafati lakini Mungu alimpa Yuda ushindi.
-          Mwaka wa 586 k.k Edomu walifurahia ilipoanguka Yerusalem Zaburi 137;7 Ezekiel 35;15
-          Inaonekana kuwa baada ya Waedomu kushirikiana na Wakaldayo waliruhusiwa kukaa kusini mwa Israel baada ya wayahudi kuchukuliwa mateka huko Babeli
-          Walifanikiwa sana, lakini Makabayo baadae aliwashinda na kuwalazimisha kushika sheria za kiyahudi na baadaye wayunani na Warumi walipotawala waliliita eneo hilo Idumeya
-          Inasemekana kwamba Mfalme Herode mkuu anatokea katika jamii hiyo na eneo hilo
-          Baada ya mwaka wa 70 B.K Waedomu walimezwa na waarabu na wametoweka leo hawako kama Taifa au kabila.

D.     MISTARI YA MUHIMU

-          Msatari wa 3-4
-          15
-          17
-          21

E.     MIGAWANYO YA KITABU CHA OBADIA

-          Kuanguka kwa Edomu Mstari wa 1-16
-          Kuhuishwa kwa Israel Mstari wa 17-21

F.      UCHAMBUZI
*      Hukumu ya Mungu dhidi ya Edomu mstari wa 1-14.
-          Unabii unahusu kuanguka kwa Edomu  mstari wa kwanza unaonyesha kuwa kile Mwandishi aliandika sio mawazo yake lakini Mungu alikuwa amemfunulia “Tumesikia ujumbe kutoka kwa Bwana” hii inaweza kuhusu  Obadia kusikia kutoka kwa Mungu kabla ya kuandika na huenda Yeremia na Ezekiel pia walipokea ujumbe kama huo.
-          Mjumbe aliyetumwa inaweza kuwa Malaika au Roho wa Bwana aliyetumwa kuyachochea mataifa  kuinuka dhidi ya Edom


G.    HALI YA EDOMU
-          Walikuwa na kiburi Mstari wa 2-4 walijiinua kwa sababu walikuwa na eneo lisiloweza kuvamiwa na mafanikio ya kijeshi na kisiasa waliyokuwa nayo iliwapelekea Kujiamini na kuacha kumtumaini Mungu Zaburi 127;1 Bwana asipoulinda mji aulindaye akesha bure.


                 
Mabaki ya mji wa wa Petra ambao ulikuwa chini ya serikali ya Edomu kama ngome zake zinavyoonekana leo Picha na maelezo kwa hisani ya Maktaba ya Mchungaji Innocent Kamote.

-          Ingawa mji wao ulikuwa jangwani lakini mataifa mengi yaliionea wivu Edomu kwani walikuwa matajiri  wa visima vya maji na mabonde mazuri
-          Walikuwa na madini ya chuma na shaba na njia kuu za kibiashara  hata kwa njia ya bahari  hivyo utajiri wao pia ulichangia kiburi walichokuwa nacho Mstari wa 5,-6.
-          Edomu waliifanya biashara na Syria, Ashuru, India, Misri, Arabuni na Afrika
-          Mstari wa 5-6 unaonekana katika maono ya Obadia  kwamba wangepoteza utajiri wao moja ya mji wao mzuri ungetekwa  na huu ni mji wa Petra kiyunani au Sela kiibrania ambalo jina hilo maana yake ni mwamba,
-          Ilikuwa ni ngome kabambe isiyoweza kuanguka, tajiri na yenye kuzungukwa na mawe kila upande Linganisha Edom na ushauri unaotolewa katika 1Timotheo 6;1-19 hasa 17.
-          Kumbuka maagizo ya Mungu kwa Israel walipokuwa wakitoka Misri katika Kumbukumbu 2;4-5 na 23;7 na kitendo cha Waedom Hesabu 20;14-21 lakini pamoja na hayo chuki yao iliendelea Zaburi 137;7 na kulingana na  Ezekiel 35;1-11 Kitendo cha Edomu kilitokana na chuki na wivu wa kale  Galatia 6;7wenye uchungu.
-          Kumbuka!
           Mungu atayahukumu au huukumu mataifa kulingana na jinsi yanavyoshughulika na watu wengine na hususani watu wake aliowachagua Edomu walihukumiwa kutokana na tendo lao la kuwa kinyume na wanaoteseka katika Mathayo 25;31-46 Yesu alifundisha kuwa tuwasaidie wale wanaoteseka au wenye uhitaji kama wakimbizi, wathirika, masikini na wenye vita sasa ukilinganisha Matendo ya Edomu na Mathayo 5;43-45 na 1Yohana 3;15-18 tunajifunza kanuni za kuwapenda maadui zetu na chuki zinatufanya kuwa wauaji mbele ya macho ya Mungu kama hatia iliyowapata Edomu.

H.    SIKU YA BWANA MSTARI WA 15-17. 

Kwa ujumla hii inazungumzia swala la siku ya hukumu ya Mungu dhidi ya Maadui zake, Pia hutumiwa na Manabii kuelezea matukio ya mwisho wa dunia ambayo hujumuisha
·         Kunyakuliwa kwa kanisa
·         Dhiki kuu
·         Vita vya Armageddon
·         Kurudi kwa Yesu mara ya pili katika utukufu
·         Kuokolewa kwa Israel
·         Hukumu ya mataifa
·         Utawala wa Yesu Kristo wa miaka 1000 duniani
              Kwa ajili ya Edomu siku ya Bwana ilimaanisha siku ya hukumu ya Edomu kwa ajili ya uchungu dhidi ya Ndugu zao
-          Kiburi kingine cha Edomu ilikuwa ni rafiki zao Mstari wa 7 Waarabu walikuwa ndio rafiki wa karibu wa Waedomu  na walijiunga nao katika kuishambulia Yuda Zaburi 83;5-6 pia rafiki zao Waamini, Wamoabu, na wengine waliifanya biashara nao hawa waliwageuka
-          Kiburi cha kisiasa Mstari wa 8-9 Waliwategemea wenye Hekima, Viongozi wao wa kisiasa washauri na majeshi wataalamu wa Vita wa mlima Seiri  walijulikana sana kwa Hekima na maarifa ya ulimwengu inasemekana watu Rafiki wa karibu wa Ayubu mwenye Hekima Elifazi Mtemani alitokea Temani  ambazo ni sehemu za Edomu Linganisha msatari wa 9 na  Ayubu 2;11. Hekima ya kibinadamu inaweza kutumiwa kwa ajili ya Mungu na kwa utukufu wake kuufanya ulimwengu kuwa mahali pa salama Yakobo 1;5 Ingawaje maarifa na Hekima pasipo Mungu  haiwezi kusaidia katika kuikwepa hukumu yake.
-          Kiburi kilichotokana na nguvu za kijeshi mstari wa 9; na kuwa na makomandoo wa kivita  mashujaa watemani vilitilia hofu mataifa mengine Yeremia 49;16 walijitumainia katika hali hiyo lakini ilitabiriwa kuwa askari wake wangechinjwa na watu wangeachwa bila ya ulinzi
-          Sababu kuu za Maangamizi ya Edomu ni Mstari wa 10-14.

*      Uasi dhidi ya Ndugu zao
*      Kusimama peke yao kujitenga kiburi cha Kujiamini
*      Kufurahia maangamizi ya ndugu zao
*      Kuwadharau ndugu zao na kuwasengenya siku ya taabu zao
*      Kufurahia utajiri na mali za ndugu zao na Kuwashambuilia mateka waliosalia.

Hakuna maoni: