Andiko
la Msingi: Ufunuo 12:10 “Nikasikia sauti kuu
mbinguni, ikisema, Sasa kumekuwa wokovu, na nguvu, na ufalme wa Mungu wetu, na
mamlaka ya Kristo wake; kwa maana ametupwa chini MSHITAKI wa ndugu zetu, yeye
AWASHITAKIYE mbele za Mungu wetu, mchana na usiku.”
Marko 15:3 “Nao wakuu wa Makuhani walikuwa WAKIMSHITAKI mambo mengi”
Ni
muhimu kufahamu kuwa shetani ndiye adui mkuu wa kila mwanadamu na kwa watu wa
Mungu, Naye hufanya kazi kwa mbinu mbalimbali katika kuwashambulia wanadamu na
watu wa Mungu moja ya mbinu kuu anayoitumia katika kufanya mashambulizi kwetu
ni kutushitaki, au kutushutumu au kutulaumu, Leo tutachukua muda kutafakari kwa
kina moja ya mbinu hii anayoitumia shetani kutushambulia ili asipate kutushinda
kwa kukosa kuzijua Fikra zake au mbinu zake katika Jina la Yesu. 2Wakoritho 2:11 “Shetani asije akapata kutushinda kwa maana
hatukosi kuzijua fikira zake.” Tutajifunza somo hili kwa kuzingatia
vipengele vitatu vifuatavyo:-
·
Maana ya neno
Mshitaki.
·
Makusudi makuu
ya mshitaki wetu.
·
Jinsi ya kumshinda
Mshitaki wetu.
Maana ya neno Mshitaki.
Neno
mshitaki kwa asili linatokana na neno la Kiyunani “Kategoros” au “Kategor”
ambalo kwa kiingereza ni “An accuiser”
which means one who blames another, or charges another with crime ambalo maana yake ni “Yeye mwenye kutafuta na kuinua lawama kwa Mwingine” au yeye mwenye kushitaki
mwingine kwa uhalifu, Unaweza kuona ni katika namna ya kushangaza sana shetani
mwenyewe au kupitia maajenti wake huitumia mbinu hii katika kuhakikisha
anabomoa kazi ya injili, au sifa za mtu, au kanisa, ili lisiweze kukubalika kwa
wasioamini au kuwafanya walioamini kupungukiwa na imani. Neno hili limetajwa
mara kadhaa katika biblia likionyesha kusudi la Ibilisi au maajenti wake
wakilifanya kwa kusudi la kuharibu mpango wa Mungu!. Mfano:-
Yohana 8:10 Biblia inasema hivi “Yesu
akajiinua asimwone mtu ila yule mwanamke, akamwambia Mwanamke, wako wapi wale WASHITAKI wako? Je Hakuna aliyekuhukumu
kuwa na Hatia? Akamwambia Hakuna Bwana
Yesu akamwambia, Wala mimi sikuhukumu. Enenda zako wala usitende dhambi tena”
Katika
kifungu hicho hapo juu mwanamke huyu alikamatwa katika kosa la zinaa na kwa
mujibu wa Torati wazinzi walipaswa kupigwa mawe hata kufa, hata hivyo katika
nyakati hizi serikali ya Warumi ndio ilikuwa inatawala Dunia na Israel pia, wao
walikuwa wamepiga marufuku mtu yeyote kuendesha hukumu ya kifo isipokuwa
serikali ya Rumi, katika kisa hicho hapo juu shetani aliitumia dhambi ya
mwanamke huyu na washitaki wake ili kumtega Yesu aingie katika mtego wa
kuruhusu hukumu ya kifo na hatimaye Yesu apate kushitakiwa unaona? Kisa
kinaonekana kumlenga mtu mwingine lakini ndani yake kinamlenga Yesu Kristo ili
ashitakiwe yeye, Mungu alimpa Hekima namna ya kuwasaidia wote akiwemo mwanamke
huyo, shetani ndiye mshitaki wetu mkuu kumbuka, swala la kumtega Yesu ili
aingie hatiani lilikuwa ni swala la kila siku la shetani na maajenti wake ili
wapate kisa cha kumshitaki
Mathayo 12:10 “Na tazama yumo mtu mwenye
mkono umepooza: wakamwuliza, wakisema Ni halali kuponya watu siku ya Sabato? Wapate KUMSHITAKI.”
Marko3:2 “Wakamvizia ili kuona kama atamponya siku ya sabato wapate KUMSHITAKI”
Marko 12:13-15 “Wakatuma baadhi ya Mafarisayo na Maherodi, ili wamnase kwa
maneno, Kumnasa kwa maneno maana yake wapate namna ya KUMSHITAKI”
Marko 15:3 “Nao wakuu wa Makuhani walikuwa WAKIMSHITAKI mambo mengi”
Muda
usingeliweza kutosha kuweza kuangalia maandiko mengi zaidi yanayoonyesha neno
hilo Mshitaki linavyotumiwa katika Biblia katika maeneo mengoi sana kote huko
shetani akitafuta hatia dhidi ya watu wa Mungu.
Makusudi makuu ya Mshitaki wetu!
Shetani
kuitwa mshitaki wetu sio jambo geni katika agano jipya tangu zamani hizi
zimekuwa sifa zake kubwa na tabia yake kuu mno, shetani ameonekana katika
maandiko mengi ya kale akifanya kazi ya kuwashitaki wenye haki mfano katika :-
Ayubu 1:6-11 Bilia inasema hivi “Ilikuwa, siku moja ambayo hao wana wa Mungu
walikwenda kujihudhurisha mbele za Bwana, Shetani naye akaenda kati yao. Bwana
akamwuliza Shetani, Umetoka wapi wewe? Ndipo Shetani akamjibu Bwana, na kusema,
Natoka katika kuzunguka-zunguka duniani, na katika kutembea huku na huku humo.
Kisha Bwana akamwuliza Shetani, Je! Umemwangalia huyo mtumishi wangu Ayubu? Kwa
kuwa hapana mmoja aliye kama yeye duniani, mtu mkamilifu na mwelekevu, mwenye
kumcha Mungu na kuepukana na uovu. Ndipo Shetani akamjibu Bwana, na kusema, Je!
Huyo Ayubu yuamcha Bwana bure? Wewe hukumzingira kwa ukigo pande zote, pamoja
na nyumba yake, na vitu vyote alivyo navyo? Kazi za mikono yake umezibarikia,
nayo mali yake imeongezeka katika nchi. Lakini nyosha mkono wako sasa, uyaguse hayo
yote aliyo nayo, naye atakukufuru mbele za uso wako.
Ayubu 2:1-5 Biblia inasema hivi “Tena kulikuwa na siku hao wana wa Mungu
walipokwenda kujihudhurisha mbele za Bwana, Shetani naye akaenda kati yao, ili
kujihudhurisha mbele za Bwana. Bwana akamwuliza Shetani, Umetoka wapi? Shetani
akamjibu Bwana, na kusema, Natoka katika kuzunguka-zunguka duniani, na katika
kutembea huku na huku humo. Bwana akamwuliza Shetani, Je! Umemwangalia huyo
mtumishi wangu Ayubu? Kwa kuwa hapana mmoja aliye kama yeye duniani, mtu
mkamilifu na mwelekevu, mwenye kumcha Mungu na kuepukana na uovu; naye hata
sasa anashikamana na utimilifu wake, ujapokuwa ulinichochea juu yake, ili nimwangamize
pasipokuwa na sababu. Shetani akamjibu Bwana, na kusema, Ngozi kwa ngozi, naam,
yote aliyo nayo mtu atayatoa kwa ajili ya uhai wake. Lakini sasa nyosha mkono
wako, uuguse mfupa wake na nyama yake, naye atakukufuru mbele za uso wako.
Bwana akamwambia Shetani, Tazama, yeye yumo mkononi mwako; lakini tunza tu uhai
wake”
Zekaria 3:1-5 “Kisha akanionyesha Yoshua, kuhani mkuu, amesimama mbele ya
malaika wa Bwana, na Shetani amesimama mkono wake wa kuume ili kushindana naye.
Bwana akamwambia Shetani, Bwana na akukemee Ewe Shetani; naam, Bwana,
aliyechagua Yerusalemu, na akukemee; je! Hiki si kinga kilichotolewa motoni?
Basi, Yoshua alikuwa amevaa nguo chafu sana, naye alikuwa akisimama mbele ya
malaika. Naye huyo akajibu, akawaambia wale waliosimama mbele yake, akisema,
Mvueni nguo hizi zenye uchafu. Kisha akamwambia yeye, Tazama, nimekuondolea
uovu wako, nami nitakuvika mavazi ya thamani nyingi. Nikasema, Na wampige
kilemba kizuri kichwani pake. Basi, wakampiga kilemba kizuri kichwani pake,
wakamvika mavazi; naye malaika wa Bwana akasimama karibu”.
1Nyakati 21:1 “Tena shetani akasimama juu ya Israeli, akamshawishi Daudi
kuwahesabu Israeli.”
Unaweza
kuona kazi za shetani katika vifungu vyote vya maandiko hapo juu kwa nini
shetani hutumia lawama, mashitaka, na masingizio kwa wanadamu na kwa jamii ya
wenye haki ambao maandiko yanawaita Ndugu zetu yaani waamini? Kusudi kubwa ni
kuharibu sifa na kuvunjilia mbali ushawishi walionao waamini katika jamii ili
Mungu azomewe na kazi zake za ukombozi zionekane kuwa bure, Hii ndio imekuwa
sifa ya Shetani na maajenti wake siku zake zote Kazi hii Maandiko yanaonyesha kuwa
shetani huifanya Usiku na Mchana
Kwa
kutumia maandiko hayo utaweza kuliona wazi kusudi la shetani kuwashitaki
wateule
Ø Anamshitaki Daudi ili Israel wapigwe wakataliwe na
Mungu, Mungu awakasirikie watu wake na wapate hasara na shetani kufurahia
angamizo la watu wa Mungu
Ø Anamshitaki Zakaria ili asihesabiwe haki, aonekane
hana sifa kwa Mungu aliyemchagua
Ø Anamshitaki Ayubu kuonyesha kuwa mungu haabudiwi
tupu, kwamba watu wake wanamuabudu kwa sababu Mungu amewapa Maisha mema, ili
ionekanane kwamba binadamu akikosa kitu hawezi kumuweka Mungu mbele.
Ø Kushitaki pia huja kwa kusudi la kutuletea Mateso
katika jamii, akipata kitu cha kutusingizia na tukauhumiwa tutateseka sana
kwaajili ya Kristo.
Ø Anataka kuharibu mioyo yetu na kutujengea mazingira
ya kuwa wenye hatia na usijione kuwa unastahili. Kisha upoteze Haki zako. Na kuleta
aibu kubwa
Ø Jumla ya yote ni ili karama tunayoitumikia iweze
kulaumiwa yaani watu waone kuwa hakuna wokovu
Jinsi ya kumshinda Mshitaki wetu.
1. Biblia inaonya kwamba tuwe na kiasi na wenye
kukesha! 1Petro 5:8 “Mwe na kiasi na
kukesha; kwa kuwa MSHITAKI wenu Ibilisi, kama simba angurumaye, huzunguka-zunguka,
akitafuta mtu ammeze.” Njia pekee ya Kumshinda ni kuishi maisha ya
kiasi, Mungu alituokoa ili tupate kuishi kwa kiasi, tusizidiwe na mambo ya
ulimwengu huu kiasi ya kwamba yatatutoa katika mapenzi yake na adui akapata
sababu ya kulaumu, Tito 2:11-12 Biblia
inasema hivi “Maana
neema ya Mungu iwaokoayo wanadamu wote imefunuliwa; nayo yatufundisha kukataa
ubaya na tamaa za kidunia; tupate kuishi kwa kiasi, na haki, na utauwa, katika
ulimwengu huu wa sasa;” Unaweza kuona Mungu anatutaka tuishi kwa
kiasi na kwa haki adi Yetu shetani asipate la kutushitaki Mungu anapokuwa
ametuokoa anatupa nguvu dhidi ya mamlaka na utawala wa shetani na shetani
hawezi kufurahia kuanguka kwetu au kupatikana kwetu katika lawama ni njia yake
ya kututamani ili kwamba turejee katika utawala wake, njia pekee ni kujitia
nidhamu ni kuishi kwa kiasi.
2. Biblia inatukumbusha namna nyingine ya kumshinda
mshitaki wetu ni kuendelea kumwangalia Yesu Kristo ambaye kwa upendo wake
mkubwa alitufia msalabani na zaidi ya yote ndiye anayetuombea, lazima tujue
kuwa ni vigumu kutenganishwa na upendo huu Warumi
8:33- 39 “Ni
nani atakayewashitaki wateule wa Mungu? Mungu ndiye mwenye kuwahesabia haki. Ni
nani atakayewahukumia adhabu? Kristo Yesu ndiye aliyekufa; naam, na zaidi ya
hayo, amefufuka katika wafu, naye yuko mkono wa kuume wa Mungu; tena ndiye
anayetuombea. Ni nani atakayetutenga na upendo wa Kristo? Je! Ni dhiki au
shida, au adha, au njaa, au uchi, au hatari, au upanga? Kama ilivyoandikwa, ya
kwamba, Kwa ajili yako tunauawa mchana kutwa, Tumehesabiwa kuwa kama kondoo wa
kuchinjwa. Lakini katika mambo hayo yote tunashinda, na zaidi ya kushinda, kwa
yeye aliyetupenda. Kwa maana nimekwisha kujua hakika ya kwamba, wala mauti,
wala uzima, wala malaika, wala wenye mamlaka, wala yaliyopo, wala
yatakayokuwapo, wala wenye uwezo, wala yaliyo juu, wala yaliyo chini, wala
kiumbe kinginecho chote hakitaweza kututenga na upendo wa Mungu ulio katika
Kristo Yesu Bwana wetu”. Ni
nani atakayewashitaki wateule wa Mungu, Mungu ndiye mwenye kuwahesabia haki,
iko wazi kuwa haki tuliyonayo sio haki yetu wenyewe ni haki inayotokana na
Kristo, ni muhimu kwetu kuendelea kuwa kuishi kwa imani na kuendelea kuaminikatika
upendo wake nayeye mwenyewe atamkemea Shetani, kama ilivyokuwa kwa kuhani mkuu
Zekaria, Shetani alipomshitaki Malaika alimtetea na kumtaka bwana amkemee,
lazima tuendelee kumwangalia Yesu kama mtetezi wetu aliye hai.
3. Damu ya Yesu
ni jibu lingine la kumshinda mshitaki wetu, Yohana 12:10-11 “Nikasikia sauti kuu mbinguni, ikisema, Sasa kumekuwa wokovu,
na nguvu, na ufalme wa Mungu wetu, na mamlaka ya Kristo wake; kwa maana
ametupwa chini mshitaki wa ndugu zetu, yeye awashitakiye mbele za Mungu wetu,
mchana na usiku. Nao wakamshinda kwa damu ya Mwana-Kondoo, na kwa neno la
ushuhuda wao; ambao hawakupenda maisha yao hata kufa.” Kama tukiwa
na hisia za hatia tusiogope hatia sio jambo baya kusudi lake ni kutuleta katika
toba, na toba hii inatupa wepesi wa kusamehewa na kuitumia damu ya Yesu kwa
imani iliyomwagika msalabani tu narudi katika kuhesabiwa haki na shetani
anapoteza nafasi ya kutushitaki.
4. Yesu Kristo ni mpatanishi wetu Ni lazima tuelewe
kuwa tunaye mpatanishi anayestahili yeye ndiye anayeweza kusimama mahali
palipobomoka kati yetu na Mungu na kutupatanisha hatupaswi kuogopa turudi kwa
mung mara tunapogundua kuwa tumemkosea na Kristo kama wakili wetu anatuombea
kwa baba na kutupatanisha na Mungu kabla ibilisi hajapata la kutushitaki 1Yohana 2:1-2 “Watoto wangu wadogo, nawaandikia haya ili
kwamba msitende dhambi. Na kama mtu akitenda dhambi tunaye Mwombezi kwa Baba,
Yesu Kristo mwenye haki, naye ndiye
kipatanisho kwa dhambi zetu; wala si kwa dhambi zetu tu, bali na kwa dhambi za
ulimwengu wote.”
Hatupaswi
kuogopa na kufikiri kuwa kila kitu kimeisha eti kwa sababu tulikosea jambo la
msingi ni kurudi kwa Mungu na pia kuelewa kuwa tunaye mpatanishi na atafanyia
upatanisho na Mungu.
5. Usishitaki watu wa Mungu bali uwaombee, watu wengi
wa Mungu hasa wana tabia ya kushutumu sana wanapoona makosa ya wengine badala
ya kuwaombea Mungu kamwe hafurahii tabia ya aina hiyo, Mungu anaweza kukuhukumu
wewe kwa vile unageuka na kusimama katika nafasi ya shetani kosa kama hili
liliwahi kufanywa na Nabii Eliya Warumi
11: 2-4 “Mungu
hakuwasukumia mbali watu wake aliowajua tokea awali. Au hamjui yale yaliyonenwa
na maandiko juu ya Eliya? Jinsi anavyowashitaki Waisraeli mbele za Mungu, Bwana,
wamewaua manabii wako, wamezibomoa madhabahu zako, nami nimesalia peke yangu,
nao wananitafuta roho yangu. Lakini ile jawabu ya Mungu yamwambiaje?
Nimejisazia watu elfu saba wasiopiga goti mbele ya Baali”. Wakristo
ni lazima wajifunze kuombeana na kusamehe kwa haraka kutokusamehe kwa haraka ni
kumpa ibilisi nafasi Efeso 4:26-27 inasema “Mwe na hasira,
ila msitende dhambi; jua lisichwe na uchungu wenu bado haujawatoka; wala msimpe
Ibilisi nafasi.” Shetani anapataje nafasi ni kwa watu
kutokusameheana nah ii inaweza kumpa yeye wakati wa kutushitaki kwa kulijua
hili Paulo mtume aliagiza msamaha kwa ndugu aliyefanya dhambi na kupokea maonyo,
alilisihi kanisa kumsamehe mtu huyo, kwani kama wasingelifanya hilo shetani
angeweza kuwashinda angalia 2Wakoritho 2:10-11 “Lakini kama mkimsamehe mtu neno lo lote, nami
nimemsamehe; kwa maana mimi nami, ikiwa nimemsamehe mtu neno lo lote,
nimemsamehe kwa ajili yenu mbele za Kristo, Shetani asije akapata kutushinda;
kwa maana hatukosi kuzijua fikira zake.” Unaweza kuona kumbe
kutokusamehe kunaweza kumpa ushindi mshitaki wetu ni lazima tuwe wenye kusamehe
na kutokuwashutumu na kuwalaumu wengine, na badala yake kuwaombea vinginevyo
shetani atapata nafasi kwetu pia.
Itaendelea na Rev. Innocent Kamote Mkuu wa wajenzi mwenye Hekima!