Warumi
12:15 “Furahini pamoja nao wafurahio; lieni pamoja nao waliao”.
“rejoice with Those who rejoice;
mourn with those who mourn”
Utangulizi.
Mungu anapendezwa sana pale anapoona
wanadamu wakisaidiana kupendana na kuchukuliana katika kila jambo, Mungu anamtegemea
kila mwanadamu kuwa mbali na ubinafsi na kuishi kwa kusaidiana kwa kadiri ya
neema yake, Furahini na wanaofurahi na lieni na wanaolia ni amri ya kibiblia
inayotufunza kuwa na ushirika na wengine na kuwasaidia wengine ni amri
inayohusu kuwa mbali na ubinafsi.
Israel walipokuwa karibu na kuingia
katika inchi ya kanaani baadhi ya makabila ya wana wa Israel walikuwa na
utajiri mkubwa sana wa mifugo kuliko kabila nyingine na waliona nchi nzuri
inayofaa kuiweka mifugo yao ng’ambo ya Yordani hivyo walimuomba Musa kuwa
wangependa kukaa magharibi ya mto Yordan
kwajili ya mifugo yao, Musa hakufurahi kwani alijua kuwa jambo hili lingeweza
kuwavunja moyo wengine, Lakini wao waliahidi kuwa wako tayari kuvaa silaha na kupigana
kwaajili ya ndugu zao mpaka nao wafanikiwe kupata urithi wao angalia :-
Hesabu
32:16-18 “Basi
wakamwendea karibu, na kusema, Sisi tutafanya mazizi hapa kwa ajili ya wanyama
wetu wa mifugo, na kujenga miji kwa ajili ya watoto wetu; lakini sisi wenyewe tutakuwa tayari na silaha
zetu kutangulia mbele ya wana wa Israeli, hata tutakapowafikisha mahali pao; na
watoto wetu watakaa katika hiyo miji yenye maboma, kwa sababu ya wenyeji wa
nchi.Sisi hatutarudia nyumba zetu, hata wana wa Israeli watakapokuwa wamekwisha
kurithi kila mtu urithi wake.”
Mfano.
Huko Afrika ya kusini baadhi ya
Wanafunzi wa chuo kimoja cha Ualimu waliamua kwenda katika vijiji vya ndani
sana vya Wazulu ili kutoa msaada wa Elimu kwa watu waliokuwa hawana elimu,
waliamua kuchagua vijiji vilivyokuwa juu kabisa katika milima katika makabila
ya watu waishio milimani.
Walimu walipofika katika vijiji hivyo
walipokelewa vizuri sana na kwa ukarimu mkubwa na kuchezewa ngoma, kisha
walipelekwa mahali pa kupumzika, wanakijiji walikuwa na ukarimu na waliishi kwa
furaha licha ya kuwa hawakuwa na umeme na vifaa vya kisasa, lakini walikuwa
wakarimu kiasi ambacho walimu wale walifurahi sana.
Walimu walijieleza kwa mkuu wa
kijiji juu ya kusudi lao na mpango wao wa kuwaelimisha watoto, Wanakijiji walifurahi
sana kusikia hilo, waliwakusanya watoto na kutengeneza ratiba kwaajili ya
kujifunza, hata hivyo walimu walipata changamoto ya kuwahamasisha sana wanafunzi
wao kujifunza kwani ilikuwa ngumu sana, walitumia mbinu nyingi sana lakini
wanafunzi wachache ndio walioonyesha mwitikio.
Mwalimu mmoja aliamua kutoa
Chocolate kwa kila mtoto katika darasa lake, na wanafunzi wao waliipenda sana
chocolate kwa vile hawajawahi kula hata siku moja tangu kuzaliwa, ilihamasisha
sana hivyo waliamua kuanzisha shindano, ili kujipatia boxi la Chocolate
waliweka Boxi moja la chocolate mbali karibu na mti kama mita 200 hivi ili
kuhamasisha wanafunzi kupenda masomo.
Walitangaza kuwa mtoto atakayekuwa
wa kwanza atapata chocolate boxi zima, walihesabu mojaaaa! Mbiliiiiii! Tatuuuu!
Unajua kilichotokea?
Watoto wote wa kijiji kile
walishikana mikono na wakakimbia kwa pamoja kama upepo na kuokota boxi la
Chocolate kwa pamoja na wakagawana wote sawa kabisa.
Jambo hili liliwashangaza sana
walimu wao kwani hakukuwa na mshindi, wote walikimbia kwa pamoja na wote
waligawana sawa chocolate zile.
Mwalimu mmoja akawauliza wale watoto
mbona mmefanya hivyo mwanafunzi yule akajibu “UBUNTU!”
Walimu waliuliza wanakijiji UBUNTU ndio nini wakaambiwa kuwa UBUNTU maana yake “When others are sad
how can you Stay Happy?” yani kama wenzako wana huzuni wewe unafurahije?” UBUNTU NI UMOJA "UNITY" ni ushirikiano usio na ubinafsi.
Walimu walishangazwa sana!
Unawezaje kuwa na furaha hali
wengine wana huzuni “When others are sad, how can you
stay happy?’”
Huu ni wakati wa kusaidiana na
kuinuana kama ni wakati wa mitihani unakaribia ni muhimu kuhakikisha kuwa wenye uwezo mkubwa
wanawasaidia wenye uwezo mdogo na kuwasaidia kuelewa, kuna faida gani mnapata
division one huku wengine wana division IV ni muhimu kusaidiana katika masomo,
kumbuka sisemi msaidiane vibomu wakati wa mitihani hapana tusaidiane kuelewa
masomo wakati wa kujisomea, tusaidiane kuinuana kiuchumi kama wachaga na wahindi, mwingine
anapoharibikiwa, tusaidiane kujengana katika ndoa wengine wanapokuwa na
mafarakano, tusaidiane kuhakikisha kuwa watanzania wote, wakenya wote na majirani
zetu Rwanda, Burundi, Kongo na kadhalika zinakuwa na amani, Mwalimu Nyerere
alisema, Tanzania (Tanganyika) haiwezi kuwa huru Mpaka Afrika nzima imekuwa
huru.
Wana wa Reuben na Gadi na nusu ya
Manase walitii kile walichomuahidi Musa
walishika silaha na kutangulia mbele ya Israel ili kuwapigania nao wapate
urithi wao kama wao ilivyokua,
Yoshua
4:12-13 “Na wana wa Reubeni, na wana wa Gadi na
hiyo nusu ya kabila ya Manase, wakavuka, hali ya kuvaa silaha mbele ya wana wa
Israeli, kama Musa alivyowaambia; walipata kama watu arobaini elfu hesabu yao,
wenye kuvaa silaha tayari kwa vita, waliovuka mbele ya Bwana, waende vitani,
hata nchi tambarare za Yeriko”.
Na. Rev. Innocent Kamote.
Mkuu wa wajenzi Mwenye Hekima.