Waefeso 4: 27 “Wala msimpe Ibilisi nafasi”.
Utangulizi:
Ni muhimu kufahamu kuwa Kila mtu
wa Mungu yuko katika vita na shetani, Shetani anatajwa katika maandiko kuwa
ndiye adui yetu mkubwa yeye anatajwa kama simba aungurumaye akitafuta mtu apate
kummeza 1Petro 5:8 “Mwe na kiasi na kukesha; kwa
kuwa mshitaki wenu Ibilisi, kama simba angurumaye, huzunguka-zunguka, akitafuta
mtu ammeze.” Shetani amejaa hila na mbinu za kuwasumbua watu wa Mungu
kila wakati na kuhakikisha kuwa hakuna mtu anaishi kwa amani au kukaa kwa amani
hivyo ni muhimu tukawa tayari kupambana naye kila wakati Waefeso 6:11 “Vaeni silaha zote za Mungu,
mpate kuweza kuzipinga hila za Shetani.” 2Wakoritho 2:11 “Shetani asije akapata
kutushinda; kwa maana hatukosi kuzijua fikira zake”. Biblia
inatufundisha kuwa tuna uwezo wa kumshinda kwa sababu tunazijua sana fikra zake
yaani mbinu anazozitumia ili aweze kutushinda
Paulo mtume anakazia kuwa tusimpe
nafasi, tusimpe mlango, tusiifanye njia yake kuwa rahisi katika kutujia na
kutushambulia, tumnyime njia kwa kuangalia kuwa tunambana kiasi ambacho ni
lazima asiwe na nafasi hata ya kuchungulia
Mtu mmoja alikuwa anauza nyumba
yake kwa shilingi za kitanzania milioni 30. Na mtu mmoja akajitokeza akasema
yeye atainunua nyumba hiyo kwa kuwa amaeipenda sana lakini yeye alikuwa
masikini na hakuwa na uwezo wote wa kuinunua nyumba ile, hivyo alibembeleza
sana sana ili auziwe nyumba ile, na hivyo mwenye nyumba aliamua kumuuzia kwa
nusu ya bei yaani miliioni 15 lakini kwa sharti moja tu kwamba anataka awe
anamiliki msumari mmoja uliokuwa sebuleni mwa nyumba ile nyuma ya mlango hivyo
walikubaliana.
Baada ya miaka kadhaa yule mwenye
nyumba wa zamani alitaka kuinunua nyumba ile tena, lakini mwenye nyumba mpya
hakukubali kuiuza, kwa hiyo mwenye nyumba wa zamani aliondoka na baada ya muda
alirudi akiwa na mzoga wa mnyama aliyekufa na akaomba autundike katika msumari
anaoumiliki, mara nyumba yote ikawa inanuka na imejaa harufu mbaya na nyumba
ile ikawa ngumu sana kuishi familia ile ililazimika kuiuza nyumba ile tena kwa
mmiliki wa msumari
Hivi ndivyo ilivyo ikiwa
tutakubali kumpa ibilisi nafasi hata kama nafasi hiyo ni ndogo sana, ayaitumia
nafasi hiyo hiyo kutuharibia maisha yetu na uhusiano wetu, shetani hutumia vitu
vidogo vidogo kuharibu uhusiano wetu hatupaswi kumpa nafasi kwa namna yoyote
kutushambulia.
Mungu ametupa nguvu
ya kumpinga shetani, Biblia inaposema wala msimpe ibilisi nafasi ni wazi kuwa
jambo hili liko katika uwezo wetu, Mungu ametupa mamlaka juu yake tunaweza
kumkatalia kabisa asituguse wala asimguse awaye yote katika maisha yetu, hii
ina maana kuwa shetani anaweza kutukaribia iwapo tu tutamruhusu kutusogelea Yakobo 4:7 Biblia
inasema “Basi mtiini Mungu. Mpingeni Shetani, naye atawakimbia.”
Uwe hodari na ushujaa
mwingi uwe na imani na ujasiri, unapokuwa vitani hupaswi kumpa kisogo adui ni
muhimu kumkabili uso kwa uso tukishindwa adui atafurahi, ssisi ndio tunapaswa
kumpa shetani wakati mgumu na sio yeye atupe sisi wakati mgumu Luka 10:19
“Tazama, nimewapa amri ya kukanyaga nyoka na nge, na nguvu zote za yule adui,
wala hakuna kitu kitakachowadhuru.”
Wakristo wengi sana
huwa wanasahau kuwa zile dhambi zinazofikiriwa kuwa ndogo kwamba zinamadhara
makubwa sana kwani kuna uwezekano kabisa mtu asiwe mlevi, au mwesharati, au
mchawi, au mpiganaji lakini wakawa na mawazo machafu, wakawa na uadui, wakawa
na husuda na wivu, wakawa na uchungu, na ulafi na uzushi, na mafarakano, na
kufitiniana, na majungu, na kusengenyana na kusemana vibaya na hasira na kiburi
na majivuno na kujisifu, hivi vinapuuziwa lakini vina madhara Makubwa kwani
ibilisi anaweza kabisa kuvitumia kwa kusudi la kuharibu maisha yetu.
Bwana na ampe neema
kila mmoja wetu kutokumpa ibilisi nafasi katika jina la Yesu amen!
Na mkuu wa wajenzi
mwenye hekima.
Rev. Innocent Kamote.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni