Alhamisi, 12 Oktoba 2017

Furahini na wanaofurahi, lieni na wanaolia



Warumi 12:15Furahini pamoja nao wafurahio; lieni pamoja nao waliao”.


“rejoice with Those who rejoice; mourn with those who mourn”


Utangulizi.

Mungu anapendezwa sana pale anapoona wanadamu wakisaidiana kupendana na kuchukuliana katika kila jambo, Mungu anamtegemea kila mwanadamu kuwa mbali na ubinafsi na kuishi kwa kusaidiana kwa kadiri ya neema yake, Furahini na wanaofurahi na lieni na wanaolia ni amri ya kibiblia inayotufunza kuwa na ushirika na wengine na kuwasaidia wengine ni amri inayohusu kuwa mbali na ubinafsi.

Israel walipokuwa karibu na kuingia katika inchi ya kanaani baadhi ya makabila ya wana wa Israel walikuwa na utajiri mkubwa sana wa mifugo kuliko kabila nyingine na waliona nchi nzuri inayofaa kuiweka mifugo yao ng’ambo ya Yordani hivyo walimuomba Musa kuwa wangependa  kukaa magharibi ya mto Yordan kwajili ya mifugo yao, Musa hakufurahi kwani alijua kuwa jambo hili lingeweza kuwavunja moyo wengine, Lakini wao waliahidi kuwa wako tayari kuvaa silaha na kupigana kwaajili ya ndugu zao mpaka nao wafanikiwe kupata urithi wao angalia :-

Hesabu 32:16-18Basi wakamwendea karibu, na kusema, Sisi tutafanya mazizi hapa kwa ajili ya wanyama wetu wa mifugo, na kujenga miji kwa ajili ya watoto wetu;  lakini sisi wenyewe tutakuwa tayari na silaha zetu kutangulia mbele ya wana wa Israeli, hata tutakapowafikisha mahali pao; na watoto wetu watakaa katika hiyo miji yenye maboma, kwa sababu ya wenyeji wa nchi.Sisi hatutarudia nyumba zetu, hata wana wa Israeli watakapokuwa wamekwisha kurithi kila mtu urithi wake.”

Mfano.

Huko Afrika ya kusini baadhi ya Wanafunzi wa chuo kimoja cha Ualimu waliamua kwenda katika vijiji vya ndani sana vya Wazulu ili kutoa msaada wa Elimu kwa watu waliokuwa hawana elimu, waliamua kuchagua vijiji vilivyokuwa juu kabisa katika milima katika makabila ya watu waishio milimani.

Walimu walipofika katika vijiji hivyo walipokelewa vizuri sana na kwa ukarimu mkubwa na kuchezewa ngoma, kisha walipelekwa mahali pa kupumzika, wanakijiji walikuwa na ukarimu na waliishi kwa furaha licha ya kuwa hawakuwa na umeme na vifaa vya kisasa, lakini walikuwa wakarimu kiasi ambacho walimu wale walifurahi sana.

Walimu walijieleza kwa mkuu wa kijiji juu ya kusudi lao na mpango wao wa kuwaelimisha watoto, Wanakijiji walifurahi sana kusikia hilo, waliwakusanya watoto na kutengeneza ratiba kwaajili ya kujifunza, hata hivyo walimu walipata changamoto ya kuwahamasisha sana wanafunzi wao kujifunza kwani ilikuwa ngumu sana, walitumia mbinu nyingi sana lakini wanafunzi wachache ndio walioonyesha mwitikio.

Mwalimu mmoja aliamua kutoa Chocolate kwa kila mtoto katika darasa lake, na wanafunzi wao waliipenda sana chocolate kwa vile hawajawahi kula hata siku moja tangu kuzaliwa, ilihamasisha sana hivyo waliamua kuanzisha shindano, ili kujipatia boxi la Chocolate waliweka Boxi moja la chocolate mbali karibu na mti kama mita 200 hivi ili kuhamasisha wanafunzi kupenda masomo.
Walitangaza kuwa mtoto atakayekuwa wa kwanza atapata chocolate boxi zima, walihesabu mojaaaa! Mbiliiiiii! Tatuuuu! 

Unajua kilichotokea?

Watoto wote wa kijiji kile walishikana mikono na wakakimbia kwa pamoja kama upepo na kuokota boxi la Chocolate kwa pamoja na wakagawana wote sawa kabisa.

Jambo hili liliwashangaza sana walimu wao kwani hakukuwa na mshindi, wote walikimbia kwa pamoja na wote waligawana sawa chocolate zile.

Mwalimu mmoja akawauliza wale watoto mbona mmefanya hivyo mwanafunzi yule akajibu “UBUNTU!”

Walimu waliuliza wanakijiji UBUNTU ndio nini wakaambiwa kuwa UBUNTU maana yake “When others are sad how can you Stay Happy?” yani kama wenzako wana huzuni wewe unafurahije?” UBUNTU NI UMOJA "UNITY" ni ushirikiano usio na ubinafsi.

Walimu walishangazwa sana!

Unawezaje kuwa na furaha hali wengine wana huzuni “When others are sad, how can you stay happy?’”

Huu ni wakati wa kusaidiana na kuinuana kama ni wakati wa mitihani unakaribia ni muhimu  kuhakikisha kuwa wenye uwezo mkubwa wanawasaidia wenye uwezo mdogo na kuwasaidia kuelewa, kuna faida gani mnapata division one huku wengine wana division IV ni muhimu kusaidiana katika masomo, kumbuka sisemi msaidiane vibomu wakati wa mitihani hapana tusaidiane kuelewa masomo wakati wa kujisomea, tusaidiane kuinuana kiuchumi kama wachaga na wahindi, mwingine anapoharibikiwa, tusaidiane kujengana katika ndoa wengine wanapokuwa na mafarakano, tusaidiane kuhakikisha kuwa watanzania wote, wakenya wote na majirani zetu Rwanda, Burundi, Kongo na kadhalika zinakuwa na amani, Mwalimu Nyerere alisema, Tanzania (Tanganyika) haiwezi kuwa huru Mpaka Afrika nzima imekuwa huru. 

Wana wa Reuben na Gadi na nusu ya Manase walitii  kile walichomuahidi Musa walishika silaha na kutangulia mbele ya Israel ili kuwapigania nao wapate urithi wao kama wao ilivyokua,  

Yoshua 4:12-13Na wana wa Reubeni, na wana wa Gadi na hiyo nusu ya kabila ya Manase, wakavuka, hali ya kuvaa silaha mbele ya wana wa Israeli, kama Musa alivyowaambia; walipata kama watu arobaini elfu hesabu yao, wenye kuvaa silaha tayari kwa vita, waliovuka mbele ya Bwana, waende vitani, hata nchi tambarare za Yeriko”.

Na. Rev. Innocent Kamote.

Mkuu wa wajenzi Mwenye Hekima.

Hakuna maoni: