Mstari wa Msingi: Luka 1:26-33 “Mwezi wa sita, malaika Gabrieli alitumwa na
Mungu kwenda mpaka mji wa Galilaya, jina lake Nazareti, kwa mwanamwali bikira
aliyekuwa ameposwa na mtu, jina lake Yusufu, wa mbari ya Daudi; na jina lake
bikira huyo ni Mariamu. Akaingia nyumbani kwake akasema, Salamu, uliyepewa
neema, Bwana yu pamoja nawe. Naye akafadhaika sana kwa ajili ya maneno yake,
akawaza moyoni, Salamu hii ni ya namna gani? Malaika akamwambia, Usiogope,
Mariamu, kwa maana umepata neema kwa Mungu.
Tazama, utachukua mimba na kuzaa mtoto mwanamume; na jina lake utamwita
Yesu. Huyo atakuwa mkuu, ataitwa Mwana wa Aliye juu, na Bwana Mungu atampa kiti
cha enzi cha Daudi, baba yake. Ataimiliki nyumba ya Yakobo hata milele, na
ufalme wake utakuwa hauna mwisho”
Maana ya jina Mariam.
Jina Mariam au Maria limetokana
na jina la Kiyunani Maria na kwa kiaram Maria, kwa kiibrania Miriam kwa kiarabu
Maryam ni Jina maarufu sana katika maandiko ya Kikristo na Kiislamu, Mariam ni
mwanamke anayesadikiwa kuwa alibarikiwa sana kutokana na kupata neema ya Kumzaa
mwokozi wa Ulimwengu yaani Bwana Yesu Kristo (Masihi). Jina hili Mariam maana
yake ni mtumishi wa Mungu!
Mariam anatajwa kama mwanamke
aliyekuwa mwanamwali yaani Bikira aliyekuwa anakaribia kuolewa au aliyekuwa
amechumbiwa anasifiwa kwa sifa kubwa ya kuwa mwanamke mwaminifu aliyejitunza na
mnyenyekevu aliyekuwa na uelewa wa juu sana kuhusu Neno la Mungu na Mapenzi ya
Mungu. Mwanamke huyu alikuwa na asili ya ukoo wa Daudi ingawa aliishi Galilaya
katika mji mdogo wa Nazareth kama yanenavyo maandiko yaani Agano jipya na Quran
Mwanamke huyu shujaa anatwaja na
maandiko yote agano jipya na Quran kwamba alikuwa Bikira na alikuwa amebakiza
muda tu wa kufungishwa ndoa kwa Yusufu ambaye naye pia alikuwa wa ukoo wa
Mfalme Daudi, Bikira wa aina hii aliitwa PARTHENOS
kwa kiyuinani yaani mwana mwali, aliyekuwa tayari kwa kutimiza tu ibada ya
ndoa, alionekana kuwa ana mimba ni mimba ambayo vitabu vitakatifu vinaeleza
wazi kuwa haikutokana na uashetari wala mbegu za kiume za mwanamume awaye yote,
bali zilitokana na muujiza wa kiungu sawasawa na jinsi alivyotabiri nabii Isaya
“TAZAMA BIKIRA ATACHUKUA MIMBA NAYE
ATAZAA MWANA WA KIUME NAYE WATAMUITA JINA LAKE IMANUEL YAANI MUNGU PAMOJA NASI”
Isaya 7:14 “Kwa
hiyo Bwana mwenyewe atawapa ishara. Tazama, bikira atachukua mimba, atazaa
mtoto mwanamume, naye atamwita jina lake Imanueli.”
Tukio hili halikuweza kumuumiza
Yusufu kwa vile alikuwa na uelewa mpana wa Mapenzi ya Mungu aidha malaika wa
bwana mjumbe wa Mungu Gabriel alimtokea na kumpa ufafanuzi kuhusu ujauzito huo,
ni kutokana na hali hii Mariam aliambatana na Yusufu mpaka Bethelehemu kwaajili
ya kuhesabiwa kutokana na amri ya Kaisari Augusto kwamba wahesabiwe watu wa
utawala wake kila mmoja kwao na kwa vile Yusufu na Mariamu kwa asili ni watu wa
Bethelehemu huko Uyahudi walikwenda huko ili wahesabiwe na kwa bahati nzuri
Masihi alizaliwa huko, ili kutimiza Unabii wa Mika katika Mika 5:2 kwamba “Bali wewe, Bethlehemu Efrata, uliye mdogo kuwa miongoni mwa
elfu za Yuda; kutoka kwako wewe atanitokea mmoja atakayekuwa mtawala katika
Israeli; ambaye matokeo yake yamekuwa tangu zamani za kale, tangu milele.”
Mwanamke huyu maarufu anatajwa
kama mara 50 hivi katika injili, Quran imempa Sura maalumu iitwayo Surat
al Maryam na inasemekana Quran inamtaja mara nyingi
zaidi kama mwanamke mtakatifu katika Quran Maryam ametajwa mara 70
Mariam alitokewa Malaika Gabriel
na kuelezwa rasmi kuwa amechaguliwa na Mungu kuwa mama wa Masihi, ni mwanamke
mwenye uwezo mkubwa sana wa kuvumilia kwani licha ya kuwa na mtoto mwema mno
kama Yesu injili imethibitisha kuwa alikuwepo wakati mwanae anasulubiwa na
kuuawa kwaajili ya dhambi za ulimwengu hili lilikuwa ni tukio chungu sana na
lilihitaji kuyajua mapenzi ya Mungu hasa na kwa uwazi Mariamu huenda katika
kipindi hiki alikumbuka maneno ya nabii mzee aliyeitwa simeon ambaye aliahidiwa
na Mungu kuwa hatakufa mpaka atakapomuona Masihi mzee huyu alimweleza maneno
mazito Mariamu kumuandaa tayari kwa machungu ya kusulubiwa kwa mwanae miaka
michache ijayo.
Luka 2:21-35 “Hata zilipotimia
siku nane za kumtahiri, aliitwa jina lake Yesu; kama alivyoitwa na malaika
kabla hajachukuliwa mimba. Kisha, zilipotimia siku za kutakasika kwao, kama
ilivyo torati ya Musa walikwenda naye hata Yerusalemu, wamweke kwa Bwana, (kama
ilivyoandikwa katika sheria ya Bwana, Kila mtoto mwanamume aliye kifungua mimba
ya mamaye na aitwe mtakatifu kwa Bwana), wakatoe na sadaka, kama ilivyonenwa
katika sheria ya Bwana, Hua wawili au makinda ya njiwa wawili. Na tazama, pale
Yerusalemu palikuwa na mtu, jina lake Simeoni, naye ni mtu mwenye haki, mcha
Mungu, akiitarajia faraja ya Israeli; na Roho Mtakatifu alikuwa juu yake. Naye
alikuwa ameonywa na Roho Mtakatifu ya kwamba hataona mauti kabla ya kumwona
Kristo wa Bwana. Basi akaja hekaluni ameongozwa na Roho; na wale wazazi
walipomleta mtoto Yesu ndani, ili wamfanyie kama ilivyokuwa desturi ya sheria,
yeye mwenyewe alimpokea mikononi mwake, akamshukuru Mungu, akisema, Sasa,
Bwana, wamruhusu mtumishi wako, Kwa amani, kama ulivyosema; Kwa kuwa macho yangu yameuona wokovu wako,
Uliouweka tayari machoni pa watu wote; Nuru ya kuwa mwangaza wa Mataifa, Na
kuwa utukufu wa watu wako Israeli. Na babaye na mamaye walikuwa wakiyastaajabia
hayo yaliyonenwa juu yake. Simeoni akawabariki, akamwambia Mariamu mama yake, TAZAMA,
HUYU AMEWEKWA KWA KUANGUKA NA KUINUKA WENGI WALIO KATIKA ISRAELI, NA KUWA
ISHARA ITAKAYONENEWA. NAWE MWENYEWE, UPANGA UTAINGIA MOYONI MWAKO, ili
yafunuliwe mawazo ya mioyo mingi.”
Mariamu hata baada ya kufufuka
kwa Yesu alijiunga na wanafunzi wa kanisa la kwanza pale Yerusalem na maandiko
yanamtaja kuwa aliungana katika maombi na wanafunzi na alikuwa miongozi mwa
watu 120 waliojazwa Roho Mtakatifu japo kwa Mariamu huenda tukio hilo lilikuwa
likijirudia kwa mara nyingine kwani Raoho wa Mungu alikuwa juu yake mapema
zaidi ili aweze kukabidiwa jukumu la Kumbeba Bwana Yesu.
Kwa mujibu ya masimulizi ya
kihistoria hasa ya wakatoliki na makanisa ya Othodox wanaamini kuwa mwili wake
ulinyakuliwa Mbinguni moja kwa moja lakini swala hili linaitwa “Assumption”
yaani inasadikiwa tu lakini hakuna uthibitisho wa moja kwa moja, Masimulizi
mengine yanaeleza kuwa huenda alikuweko mpaka mwaka wa 70 AD wayahudi
walipotawanywa na kupoteana na kutokuweko kwa uhakika kuwa ni wapi alifia,
Mtume Yohana alipewa jukumu la kumlea Mariam lakini hata hivyo hajawahi kueleza
lolote kuhusu Mwisho wake aidha baadhi ya wanawe kama Yuda aliyeandika waraka
na Yakobo pia ndugu zake bwana
hawajawahi kueleza lolote kuhusu mama yao.
Mariamu anaheshimika na watu
wengi sana na mamilioni ya watu wanaamini kuwa ni moja ya watakatifu muhimu
sana katika dini, wengine wanaamini kuwa amewahi kuwatokea kimuujiza katika
karne kadhaa, makanisa ya Othodox na Catholic na Anglican na Lutheran yanaamini
kuwa kwa kuwa yesu ni Mungu na alizaliwa na Mariam basi Mariamu ni mama wa
Mungu, baadhi ya mashirika ya kikatoliki kama Marian wao wanaamini na kumuita
kuwa ni mama wa Mungu na wanaamini kuwa hata yeye kama ilivyo kwa yesu Kristo
hakuwa na dhambi na kuwa alizaliwa pasipokuwa na dhambi, siwezi kusema lolote
katika hili lakini ukweli ni kuwa Quran pia imemkubali sana Maryam na kuonyesha
heshima kubwa sana juu yake akitetewa kuwa hakuwa na dhambi tofauti na mama wa
Muhamad ambaye hatajwi kabisa katika kitabu hichi ukicha khadithi.
Pamoja na ubora wote huu kuhusu
Mariamu na utakatifu wake kwetu sisi na kwangu mimi Mariamu ni mtakatifu kama
walivyo watakatifu wote katika biblia, nakubali kuwa Yesu alimuheshimu sana
mama yake lakini vilevile sisi nasi tunamuheshimu sana na kama mbingu
zilivyomuheshimu sana kuwa ni Mtakatifu hilo hatuna mashaka nalo, kila mtu
anaweza kuwa kama Mariamu tu kama tukiyashika maneno ya Mungu Yesu alisema
“MAMA NA NDUGU ZANGU NI AKINA NANI? NI WALE WANAOLISIKIA NENO LA MUNGU NA
KULISHIKA” ni imani yangu pia kuwa
furaha atakayokuwa nayo Mariamu inaweza kuwa furaha ya kila mmoja anayelisikia
neno la Mungu na kulishika Yesu akasema
alipoulizwa ni furaha gani aliyonayo mwanamke aliyekuzaa na kukulea
alijibu AMA NI FURAHA GANI WALIYONAYO WANAOLISIKIA NENO LA MUNGU NA KULITII”
Katika kitabu cha matendo Mariamu
anaonekana akiwa muombaji sawa na waombaji wengine kama Petro na wengineo,
mariamu amebarikiwa hatuna shaka na hilo, Mariamu ytuko mbinguni kama
watakatifu wengine hatuna shaka na hilo, Lakini Mariamu sio njia na kweli na uzima,
yeye sio njia ya kumfikia Mungu aliye hai, yeye sio njia ya kutumika kutuombea
kwa baba mbinguni, yeye sio mama wa Mungu, wala sio mke wa Mungu, yeye
aliendelea kuwa mke wa Yusufu na alizaa watoto sita zaidi ukiacha Yesu mwanawe
wa kwanza aliyemzaa kwa muujiza soma Mathayo
13:54-56 “ Na
alipofika nchi yake, akawafundisha katika sinagogi lao, hata wakashangaa,
wakasema, Huyu amepata wapi hekima hii na miujiza hii? Huyu si mwana wa
seremala? Mamaye si yeye aitwaye Mariamu? Na nduguze si YAKOBO, NA YUSUFU, NA
SIMONI, NA YUDA? Na MAUMBU (Dada zake) yake
wote hawapo hapa petu? Basi huyu amepata wapi haya yote?”
Kama u mwanafunzi wa Biblia
utaona wazi kuwa ndugu zake Yesu wametajwa katika Biblia Yakobo. Yusufu, Simoni
na Yuda yaaninkaka wane na neno maumbu maana yeke dada zake ambao inakisiwa
walikuwa wawili hivyo jumla ya wana wa Mariamu ni Saba na aliozaa na Yusufu ni
sita, so kama Mariamu ni mama wa Mungu basi pia ni mama wa wanadamu! Kumbuka ni
Yesu pekee ndie alikuwa mwana wa miujiza na yusufu aliendelea kuzaa na kufurahia
maisha yake na Mariam inasadikiwa tu kuwa Yusufu alifariki mapema zaidi.
Wakati watu wanakazania kumuomba
Mariamu ni muhimu kujikumbusha kuwa Mariamu alikuwa akimuomba Yesu pamoja na
wanafunzi wake aliungana nao katika maombi Matendo
ya Mitume 1:12-14 “Kisha wakarudi kwenda Yerusalemu kutoka mlima ulioitwa wa
Mizeituni, ulio karibu na Yerusalemu, wapata mwendo wa sabato.Hata walipoingia,
wakapanda orofani, walipokuwa wakikaa; Petro, na Yohana, na Yakobo, na Andrea,
Filipo na Tomaso, Bartholomayo na Mathayo, Yakobo wa Alfayo, na Simoni Zelote,
na Yuda wa Yakobo. Hawa wote walikuwa wakidumu kwa moyo mmoja katika kusali,
pamoja nao wanawake, na Mariamu mama yake Yesu, na ndugu zake.” Unaona Mariamu mama yake Yesu na ndugu zake
walikuwa miongoni mwa watu waombaji waliokuwa wakimuomba Mungu kwa jina la Yesu,
dhana inayojengwa na baadhi ya watu wanaotaka kupotoshja maandiko wakisema kuwa
Mariamu ni muombezi wanajenga hoja kupitia muujiza wa kana ya Galilaya wakati
Yesu alipohudhuria harusini na kisha watu wakatindikiwa na Divai, Mariamu
alikuja kumuomba Yesu na kumpa taarifa ya kutoikuweko kwa Divai Yesu hakukubali
kwa urahisi kwani mariamu alitaka Yesu atumie uwezo wake wa kimuuijiza kabla ya
wakati wa Mungu, hata hivyo alimuomba kwa imani na kuwagiza wanafunzi wake kuwa
atakalowaagiza walifanye dhana hii haitufundishi kumuomba mariamu aku kumfanya
mariamu kuwa ni muombezi bali inatufundisha kuwa tukiwa na uhitaji wowote ni
lazima tumweleze Bwana yesu kwa imani naye ataenda Yohana 2:1-9 “Na siku ya tatu
palikuwa na arusi huko Kana, mji wa Galilaya; naye mama yake Yesu alikuwapo.
Yesu naye alikuwa amealikwa arusini pamoja na wanafunzi wake. Hata divai
ilipowatindikia, mamaye Yesu akamwambia, Hawana divai. Yesu akamwambia, Mama,
tuna nini mimi nawe? Saa yangu haijawadia. Mamaye akawaambia watumishi, Lo lote
atakalowaambia, fanyeni. Basi kulikuwako huko mabalasi sita ya mawe, nayo
yamewekwa huko kwa desturi ya Wayahudi ya kutawadha, kila moja lapata kadiri ya
nzio mbili tatu. Yesu akawaambia, Jalizeni mabalasi maji. Nao wakayajaliza hata
juu. Akawaambia, Sasa tekeni, mkampelekee mkuu wa meza. Wakapeleka. Naye mkuu
wa meza alipoyaonja yale maji yaliyopata kuwa divai, (wala asijue ilikotoka,
lakini watumishi walijua, wale walioyateka yale maji),”
Ni muhimu kufahamu kuwa Yesu
Kristo ni Mkuu kuliko Mariam, neema aliyopewa Mariamu ilikuwa ni kushiriki
Baraka kubwa ya kumleta masihi Duniani, Lakini Mungu hajamfanya Mariamu kuwa
mwombezi kwa sababu zozote zile Makuhani waombezi wote katika uyahudi walikuwa
wanaume, Mariamu hakuwa nabii kama ilivyokuwa kwa Miriam wa agano la kale
aliyekuwa Dada wa Musa na Haruni,
alikuwa ni mwanamke shujaa jasiri na mwenye imani katika kutunza neno na
ahadi za Mungu, Mungu hajawahi kumfanya Mariamu kuwa malkia wa Mbinguni wala
hajawahi kumfanya mariamu kuwa sehemu ya ibada, Mariam atasikitika sana kama
atarudi duniani na kukuta akuombwa na kuabudiwa kama Mungu kwa unyenyekevu
aliokuwa nao angeshangaa kukuta kufuru hii.
Njia pekee ya kumfikia Mungu ni
Yesu naye ndiye kipatanisho pekee kati ya Mungu na wanadamu, 1Yohana 2:1-2 “Watoto wangu wadogo, nawaandikia haya ili
kwamba msitende dhambi. Na kama mtu akitenda dhambi tunaye Mwombezi kwa Baba,
Yesu Kristo mwenye haki, naye ndiye kipatanisho kwa dhambi zetu; wala si kwa
dhambi zetu tu, bali na kwa dhambi za ulimwengu wote.”
Unapotumia Muda wako kumuomba
Mungu kupitia Mariamu unapoteza lengo la maombi yako huku ukiwa na nia nzuri
lakini sio ya kimaandiko ni vema dua zetu na maombi yetu tukamuombababa wa
Mbinguni kwa njia ya mwanae Yesu Kristo pekee
Yohana 16:23-24 “Tena siku ile hamtaniuliza neno lo lote. Amin, amin,
nawaambia, Mkimwomba Baba neno lo lote atawapa KWA JINA LANGU. Hata sasa hamkuomba neno KWA JINA LANGU;
ombeni, nanyi mtapata; furaha yenu iwe timilifu.”
Wengi hawana furaha hawajawahi
nkufurahia uwepo wa Mungu na utendaji wa Mungu kwa sababu hawajawahi kuomba kwa
jina la Yesu wamedanganywa na kudanganyika wakiomba kupitia majina mengine Yesu
Mwenye yu ashauri hivi Yohana 14:13-14
“Nanyi
mkiomba lo lote kwa jina langu, hilo nitalifanya, ili Baba atukuzwe ndani ya
Mwana. Mkiniomba neno lo lote kwa jina langu, nitalifanya”: ni jambo
la kusikitisha sana katika Karne hii ya uwazi na ukweli yautafiti na ujuzi ya
hekima na maarifa neno la mungu liko wazi kila mahali bado kuna watu wanatumia
jina la Mariamu katika maombezi, ni malizie kwa kusema kuwa Roho Mtakatifu
ndiye anayetuombea kwa kuugua kusikoweza kutamkwa.
Kama hujui kuomba ruhusu Roho
Mtakatifu akufundisha kuomba maana yeye ndio muombezi mkuu na sio Mariamu Warumi 8:26-27 “Kadhalika
Roho naye hutusaidia udhaifu wetu, kwa maana hatujui kuomba jinsi itupasavyo,
lakini Roho mwenyewe hutuombea kwa kuugua kusikoweza kutamkwa. Na yeye
aichunguzaye mioyo aijua nia ya Roho ilivyo, kwa kuwa huwaombea watakatifu kama
apendavyo Mungu.”
Ni imani yangu kuwa utaifahamu kweli nayo itakuweka Huru katika jina la
Yesu Kristo aliye hai amen!
Rev. Innocent Kamote