Matendo 23:1-3 “Paulo akawakazia macho watu
wa baraza, akasema, Ndugu zangu, mimi kwa dhamiri safi kabisa nimeishi mbele za
Mungu hata leo hivi. Kuhani Mkuu Anania akawaamuru wale waliosimama karibu naye
wampige kinywa chake. Ndipo Paulo akamwambia, Mungu atakupiga wewe, ukuta
uliopakwa chokaa. Wewe umeketi kunihukumu sawasawa na sheria, nawe unaamuru
nipigwe kinyume cha sheria?”
Utangulizi
Leo tutachukua muda kwa kutosha
kujifunza na kuchambua kwa kina maneno yaliyozungumzwa na Paulo Mtume dhidi ya
Kuhani mkuu waliyekuwako wakati huo kama tulivyoweza kuona katika mstari wa
msingi
Matendo 23:1-3 “Paulo akawakazia macho watu
wa baraza, akasema, Ndugu zangu, mimi kwa dhamiri safi kabisa nimeishi mbele za
Mungu hata leo hivi. Kuhani Mkuu Anania akawaamuru wale waliosimama karibu naye
wampige kinywa chake. Ndipo Paulo akamwambia, Mungu atakupiga wewe, ukuta
uliopakwa chokaa. Wewe umeketi kunihukumu sawasawa na sheria, nawe unaamuru
nipigwe kinyume cha sheria?”
Katika tafakari yetu leo kuhusu
kifungu hiki cha maandiko tunajifunza somo hili KUPIGWA KWA UKUTA ULIOPAKWA CHOKAA Kwa kuzingatia vipengele vitatu
vifuatavyo:-
·
Agizo la kutenda haki
·
Paulo hakutendewa haki
·
Kupigwa kwa ukuta uliopakwa chokaa
Agizo la Kutenda haki
Mojawapo ya maagizo ya Mungu kwa
mtu awaye yote mwenye mamlaka, ni kuhakikisha kuwa anatenda haki, kila ngazi ya
mamlaka duniani ni ngazi ya maamuzi, kwa msingi huo ni muhimu kwa kila mmoja
mwenye mamlaka kuhakikisha kuwa anatenda haki, Kutokutenda haki ni kinyume na
mapenzi ya Mungu, Mungu aliagiza watu wasitende yasiyo haki katika hukumu ona
Mambo ya walawi 19:15 “Msitende yasiyo haki
katika hukumu, usimpendelee mtu maskini, wala kumstahi mwenye nguvu; bali
utamhukumu jirani yako kwa haki”
Mungu ndiye hakimu wetu mkuu
atakayemuhukumu kila mmoja sawa na kutenda kwake na hivyo ni muhimu kwetu
tunapokuwa katika ngazi za maamuzi kutenda haki au kuhakikisha kuwa haki
inatendeka bila kufanya upendeleo tukikumbuka kuwa Mungu ndiye mtoa sheria na
ndiye mwenye kuhukumu, hivyo kila aliye kwenye ngazi ya maamuzi na ajiangalie.
Yakobo 4:12 “Mtoa sheria na mwenye kuhukumu ni mmoja tu, ndiye awezaye
kuokoa na kuangamiza. U nani wewe umhukumuye mtu mwingine?”
Na ndio maana maandiko yanatuonya
kwamba tujihadhari na hukumu kwa kuwa nasi tutahukumiwa, na kujihadhari na
kipimo kile tukipimacho kwani kipimo kilekile tupimacho ndicho tutakachopimiwa,
Mungu ndiye Muhukumu wa ulimwengu mzima
na kwake ni lazima atatenda haki na kuisimamia na kuhakikisha kuwa inakuja
kufanyiwa malipizo kwa namna yoyote (Karma)
Mwanzo
18:25 “Hasha usifanye hivyo, ukamwue mwenye haki
pamoja na mwovu, mwenye haki awe kama mwovu. Hasha; Mhukumu ulimwengu wote
asitende haki? ”
Ulikuwa ni utambuzi kamili wa
Ibrahimu kuwa Mungu wa Mbinguni Mungu wake ana sifa kadhaa wa kadhaa lakini
mojawapo yeye ni Muhukumu wa Ulimwengu ni Jaji mkuu nani mwenye haki hivyo
alimsihi Mungu kutenda haki wakati anapotaka kuangamiza watu wote katika miji
ya Sodoma na Gomora ya kwamba kwa vyovyote hataangamiza watu wema pamoja na
waovu, Tabia hii ya uungu ya kutenda haki inapaswa kuwa na kila kiongozi aliyeko
katika nafasi ya kufanya maamuzi duniani kwamba ni lazima atende haki, kutenda
haki huambatana na Baraka kubwa sana.
Lakini kutokutenda haki ni hatari
sana Katika imani ya Kiislamu, Kitabu chao Quran kina Sura maalumu inayoitwa Al
– Qariah maana yake hukumu au mizani,
mkazio wake ni kuhukumu kwa haki au kutenda usawa kama inavyofanya mizani,
Katika kitabu cha Mithali, Maandiko yanaonya kuhusu Mizani ya hadaa ikiwa na
maana ya kutokutenda haki ni chukizo kwa Mungu ona
Mithali 11:1 “Mizani ya hadaa ni chukizo
kwa Bwana; Bali vipimo vilivyo sawasawa humpendeza.”
Kwa msingi huo maandiko
yanatukumbusha hapa umuhimu wa kutenda, haki na kuhukumu kwa haki, na kufanya
mambo sawasawa na Mapenzi ya Mungu na kutokuwahukumu wenzetu katika namna isiyo
sahihi
Paulo hakutendewa Haki!
Matendo 23:1-3 “Paulo akawakazia macho watu
wa baraza, akasema, Ndugu zangu, mimi kwa dhamiri safi kabisa nimeishi mbele za
Mungu hata leo hivi. Kuhani Mkuu Anania akawaamuru wale waliosimama karibu naye
wampige kinywa chake. Ndipo Paulo akamwambia, Mungu atakupiga wewe, ukuta
uliopakwa chokaa. Wewe umeketi kunihukumu sawasawa na sheria, nawe unaamuru
nipigwe kinyume cha sheria?”
Mahakama ya kitahudi ambayo
huongozwa na kuhani mkuu ikiwa na wataalamu wapatao 70 ambayo ilijulikana kama baraza la wazee (Sanhedrin) ilikuwa imeketi kusikiliza
mashauri ya Paulo mtume yaliyoletwa kwa hila na masingizio ya wayahudi, wakati
Paulo anapewa nafasi ya kujitetea alianza kwa kuonyesha wazi kuwa ameishi kwa
dhamiri safi maana yake yeye hana hatia hata sasa, Neno hilo likiwa kinywani
mwa Paulo alipokuwa akianza utetezi wake mara moja hatujui ni kwa chuki au kwa
dhamiri gani Kuhani mkuu Anania hakufurahishwa na neno hilo akaamuru
waliosimama karibu naye wampige mara moja makofi katika kinywa chake, kwa
kitendo hiki Paulo alimwambia Mungu atakupiga wewe, ukuta uliopakwa chokaa, kwa
sababu ameketi katika kiti cha hukumu ili ahukumu sawa na sharia lakini
anaamuru apigwe kinyume cha Sheria, haki haikutendeka mahali hapo! Paulo kwa
ujasiri mkubwa na ushuhuda kuwa anaifanya kazi ya injili sawasawa na wito wake
katika Kristo kwa hiyo kimsingi hakuwa na hatia zaidi ya upofu uliokuweko
katika baraza ka wazee wa kiyahudi kuhusu mtazamo wao kinyume na injili ya
Bwana Yesu! Paulo hakutendewa haki ni kutokana na na jambo hili Paulo mtume alijua wazi kuwa
Mungu atasimama na kumtetea bila kujali
kuwa Anania alikuwa kuhani mkuu andiko linasema hivi
Zaburi 12:5 “Kwa ajili ya kuonewa kwao
wanyonge, Kwa ajili ya kuugua kwao wahitaji, Sasa nitasimama, asema Bwana, Nitamweka
salama yeye wanayemfyonya.”
Kama haki haipatikani mahali
ambapo haki inatakiwa ipatikane maana yeke mahali hapo hapana ustaarabu na
yanayofanyika hayana tofauti na yanayofanywa na wanyama, Mwanadamu anapaswa
kuwa kiumbe kilicho staarabika na kama hakuna ustaarabu maana yake hakuna
tofauti na ulimwengu wa wanyama Mungu anataka haki itendeke
Muhubiri 3:16 “Zaidi ya hayo, nikaona tena
chini ya jua ya kwamba, Mahali pa hukumu upo uovu, Na mahali pa haki upo
udhalimu. Nikasema moyoni mwangu, Mungu atawahukumu wenye haki na wasio haki;
kwa kuwa kuna wakati huko kwa kila kusudi na kwa kila kazi. Nikasema moyoni
mwangu, Ni kwa sababu ya wanadamu, ili Mungu awajaribu, nao waone ya kuwa wao
wenyewe wafanana na wanyama.”
Muhubiri 4:1 “Kisha nikarudi na kuona madhalimu
yote yanayotendeka chini ya jua; na tazama, machozi yao waliodhulumiwa, ambao
walikuwa hawana mfariji; na upande wa wale waliowadhulumu kulikuwa na uwezo,
walakini wale walikuwa hawana mfariji.”
Dhuluma inapotendeka na haki
inapopotoshwa Mungu hataweza kutulia ataingilia kati na kuileta hukumu kwa
haraka kama ilivyosema Zaburi 12:5
kwa hiyo ni muhimu kufuatilia na kuona kuwa haki inatendeka katika jamii, Je
swala la kumpiga kofi mtume Paulo mdomoni ili asijitetee na na asiendelee kusema kuwa hana hatia je ni
swala dogo? Mbele za Mungu haikuwa jambo jema na hata mbele za Paulo mwenyewe
na ndio maana Paulo aliamua kumuachoa Mungu na kumhakikishai kuhani mkuu kuwa
Mungu Atampiga! Je kuhani mkuu alipigwa
na Mungu kama Paulo alivyosema?
Kupigwa kwa ukuta uliopakwa chokaa!
Kabla ya kuangalia kama Kuhani
mkuu alipigwa na Mungu au la jambo la kwanza ni jina alilopewa na Paulo mtume
kwa kuitwa ukuta uliopakwa chokaa! Hii ilikuwa na maana gani, kwa kawaida usemi
huu hauna tofauti na ule usemi wa Yesu Kristo alipokuwa akiwakemea Mafarisayo
kutokana na tabia zao za kinafiki aliwaita makaburi yaliyopakwa chokaa
Mathayo 23:27-28 “Ole wenu, waandishi na
Mafarisayo, wanafiki! Kwa kuwa mmefanana na makaburi yaliyopakwa chokaa, nayo
kwa nje yaonekana kuwa mazuri, bali ndani yamejaa mifupa ya wafu, na uchafu
wote. Vivyo hivyo ninyi nanyi, kwa nje mwaonekana na watu kuwa wenye haki, bali
ndani mmejaa unafiki na maasi.”
Unaona mwanadamu awaye yote anayeketi
katika kiti cha hukumu na kuhukumu wengine wakati nay eye mwenyewe akiwa sio
mkamilifu, ana dhambi tena chafu kuliko za wale anaowahukumu huyo ni ukuta
uliopakwa chokaa ni kaburi ambalo limepakwa chokaa kwa nje linaonekana kuwa
jema lakini kwa ndani limejaa mifupa ya wafu, ukuta uliopakwa chokaa ni wa watu
ambao ndani ni waovu wana hatia, lakini hawatendi haki, wanajidai haki lakini
ni wanafiki wakubwa! Paulo alimkemea kuhani mkuu kwa tabia ya kinafiki ya
kuamuru apigwe kinyume cha Sheria wakiwa katika mahakama ya kiyahudi kwaajili
ya kutafuta haki lakini pamoja na hayo alitabiri kuwa Mungu atampiga kuhani
mkuu je hili lilitimia?
Kwa mujibu wa Historia Mwana
historia Mashuhuri aitwaye A.C Harvey anamuelezea Ananias kuwa alikuwa mtu
Jeuri sana, mwenye kiburi, mroho mwenye uchu, akiamua ameamua na mwenye utawala
wa kiimla maneno anayotumia kumueleza katika ikiingereza ni a Violent, Haughty,
gluttonous and rapacious man. Japo alikubalika kwa wayahudi,kwa maelekezo hayo
na kwa vyovyote vile mtu huyu hakuwa na wema ndani yake, Mungu alimpiga kwa
maelezo ya Mwanahistoria mashuhuri wa kiyahudi wa karne ya Kwanza alitwaye
Flavious Josephus , Annania alijihusisha na uasi dhidi ya serikali ya kirumi na
kushutumiwa vikali na gavana wa Syria alishitakiwa huko Roma na kupelekwa kwa
Kaisari Claudius kati ya mwaka wa 52 baada ya Kristo, Claudius alimuongeza muda
wa kuendelea na ukuhani mpaka mwaka wa 58, akiwa kibaraka mkubwa wa warumi,
alikamatwa na kuuawa na wayahudi wenye msimamo mkali mwanzoni mwa vita kati ya
wayahudi na warumi, Na hivyo kutimizwa kwa maneno ya Mtume Paulo kuwa Bwana
atakupiga ukuta uliopakwa chokaa, Mungu hatawaqacha watu wake hususani
watumishi wake waonewe, haki tasimama hata kama hao wanaoonea watumishi wa
Mungu ni wenye mamlaka ya kifalme au la Zaburi
105:14-15 “Hakumwacha mtu awaonee, Hata wafalme
aliwakemea kwa ajili yao. Akisema, Msiwaguse masihi wangu, Wala msiwadhuru
nabii zangu.”
Na Rev. Innocent Samuel Kamote
Mkuu wa wajenzi Mwenye Hekima!