Jumatatu, 16 Oktoba 2023

Unirehemu mimi, maana nafsi yangu imekukimbilia wewe!


Zaburi 57:1-3 “Unirehemu, Ee Mungu, unirehemu mimi, Maana nafsi yangu imekukimbilia Wewe. Nitaukimbilia uvuli wa mbawa zako, Hata misiba hii itakapopita. Nitamwita MUNGU Aliye juu, Mungu anitimiziaye mambo yangu.  Atapeleka toka mbinguni na kuniokoa, Atukanapo yule atakaye kunimeza. Mungu atazipeleka Fadhili zake na kweli yake” 



Utangulizi:

Hakuna jambo lililozuri kulipokea duniani kama Rehema, Kila mwanadamu anapenda kurehemiwa na ndio maana katika zaburi hii ya 57 tunamuona Daudi, akiomba rehema kwa Mungu, kwa mujibu wa historia ya kimaandiko zaburi hii ilitokana na Maisha ya Daudi nyikani wakati alipokuwa katika miaka ya kumkimbia Sauli, ambaye alikuwa anataka kumuua kwa sababu ya wivu, Daudi alikuwa akikimbia kuyaokoa maisha yake na kujificha katika mapango huko Engedi magharibi mwa pwani ya bahari iliyokufa. Ni katika mazingira ya aina hiyo yaliyokuwa magumu katika maisha ya Daudi ndio tunaona akimuomba Mungu katika zaburi hii akihitaji rehema za Mungu kwake!

1Samuel 24:1-3 “Ikawa, Sauli aliporudi baada ya kuwafuatia Wafilisti, aliambiwa ya kwamba, Daudi yuko katika nyika ya Engedi. Ndipo Sauli akatwaa watu elfu (tatu) waliochaguliwa katika Israeli wote, akaenda kumtafuta Daudi na watu wake juu ya majabali ya mbuzi-mwitu. Akafika penye mazizi ya kondoo kando ya njia, na huko kulikuwa na pango; Sauli akaingia ndani ili kuifunika miguu. Na Daudi na watu wake walikuwa wakikaa mle pangoni ndani sana.”            

Kuomba rehema za Mungu hakuhitajiki tu wakati ambapo tumetenda dhambi na tuko katika toba na basi kwaajili hiyo tunaomba Rehema Hapana hapa Daudi kuna kitu kingine cha tofauti anatufundisha kuhusu utajiri wa rehema, tunaweza kumuomba Mungu rehema hata wakati wa mapito yetu na mahitaji yetu, wote tunakumbuka ombi la Batrimayo kwa Yesu Kristo Mwana wa Daudi aliomba arehemiwe lakini kwaajili ya nini kwaajili ya ukarabati wa macho yake ili aweze kuona ona 

Luka 18:35-43 “Ikawa alipokaribia Yeriko, mtu mmoja kipofu alikuwa ameketi kando ya njia, akiomba sadaka; na alipowasikia makutano wakipita, aliuliza, Kuna nini? Wakamwambia, Yesu wa Nazareti anapita. Akapiga kelele, akisema, Yesu, Mwana wa Daudi, unirehemu. Basi wale waliotangulia wakamkemea ili anyamaze; lakini yeye alizidi sana kupaza sauti, Ee Mwana wa Daudi, unirehemu. Yesu akasimama, akaamuru aletwe kwake; na alipomkaribia, alimwuliza, Wataka nikufanyie nini? Akasema, Bwana, nipate kuona. Yesu akamwambia, Upewe kuona; imani yako imekuponya. Mara hiyo akapata kuona, akamfuata, huku akimtukuza Mungu. Na watu wote walipoona hayo walimsifu Mungu.”

Kwa hiyo tunaweza kuinua macho yetu katika mtazamo mwingine na kujifunza umuhimu wa rehema za Mungu katika maisha yetu na utaweza kufurahia mpango wa Mungu katika maisha yetu na kujua kuwa kila wakati katika changamoto yoyote tunayokutana nayo tunahitaji rehema za Mungu na zitatupa upenyo tunaouhitaji siku zote katika maisha yetu. Tutajifunza somo hili kwa kuzingatia maswala matatu muhimu yafuatayo:-

1.       Umuhimu wa rehema za Mungu

2.       Madhara  ya kukosekana kwa rehema

3.       Unirehemu maana nafsi yangu imekukimbilia wewe

Umuhimu wa rehema za Mungu.

Ni muhimu kufahamu kuwa hakuna jambo muhimu duniani Kama rehema! Rehema inapokosekana katika dunia kila kitu kinaweza kuharibika na picha la kutisha likajitokeza Duniani, kwa kuelewa umuhimu wa rehema Daudi anaomba rehema wakati akiwa anapita katika mateso na majaribu makali sana

Rehema ni nini? Neno rehema alilolitumia Daudi katika zaburi ya 57 katika biblia ya kiebrania linasomeka kama CHANAN kimatamshi Khaw-nan ambalo maana yake ni kuomba kuhurumiwa katika wakati wa mgandamizo wa mawazo, hususani wakati unapitia hali ngumu au mateso, au kuomba kuhurumiwa kutoka kwa mtu mwenye uwezo na mamlaka na nguvu ya kukuadhibu au kukudhuru, Neno hilo kwa kilatini ni Merced au merces kwa kiingereza Mercy

Daudi alihitaji rehema za Mungu wakati alipokuwa amekimbilia katika nyika ya Engedi ambayo ilikuwa na mapango mengi yeye alikuwa na watu wapatao mia sita tu wakati Sauli alikuwa akimtafuta na askari wapatao 3000 tena hawa walikuwa ni wateule yaani watu hodari na wataalamu wa vita kama ungekuwepo katika uwanja wa vita ungeweza kuona mapango kila mahali na upelelezi ulikuwa umeonyesha wazi kuwa Daudi yuko huko na hivyo Sauli alikuwa na uhakika wa kumpata na kumla nyama au kumfanya akitakacho!

Daudi alisali sala hii katika zaburi 57 Yeye alihitaji rehema alijua kuwa Mungu atatuma rehema zake na kuwa rehema hiyo hiyo ndiyo itakayomuokoa na majanga yanayomkabili, Mungu alijibu vipi Mungu alimpiga Sauli upofu yeye na majeshi yake walifanya mapumziko katika pango lilelile ambalo Daudi na watu wake walikuwa kwa ndani zaidi ona kilichojitokeza

1Samuel 24:3-6 “Akafika penye mazizi ya kondoo kando ya njia, na huko kulikuwa na pango; Sauli akaingia ndani ili kuifunika miguu. Na Daudi na watu wake walikuwa wakikaa mle pangoni ndani sana. Nao watu wa Daudi wakamwambia, Tazama, hii ndiyo siku ile aliyokuambia Bwana, Angalia, nitamtia adui yako mikononi mwako, nawe utamtenda yo yote utakayoona kuwa mema. Basi Daudi akainuka, akaukata upindo wa vazi lake Sauli kwa siri. Lakini halafu, moyo wake Daudi ukamchoma, kwa sababu amekata upindo wa vazi lake Sauli. Akawaambia watu wake, Hasha! Nisimtendee bwana wangu, masihi wa BWANA,neno hili,kuunyosha mkono wangu juu yake,kwa maana yeye ni masihi wa BWANA.”          

Unaona matokeo ya kuomba rehema yalisababisha majibu ya kushangaza Mungu alimleta Sauli katika pango lilelile alilokuwepo Daudi na tayari kulikuwa na neno la unabii ya kuwa siku moja bwana angentia Sauli mikononi mwa Daudi angalia sentensi hii - hii ndiyo siku ile aliyokuambia Bwana, Angalia, nitamtia adui yako mikononi mwako Ilikuwa wazi kabisa kuwa Mungu alikuwa ameshasema wazi kuwa Daudi afanye anachoweza kukifanya na washirika wa Daudi walimkumbusha lakini yeye aliwakataza, Daudi alikumbuka rehema, yeye alikuwa amemuomba Mungu rehema na hivyo aliziamini rehema za Mungu na fadhili za Mungu kuwa zinaweza kumlipia. Rehema ni tabia ya uungu, Daudi alionyesha ukomavu na alikuwa na ujuzi kuwa Mungu wa Ibrahimu Isaka na Yakobo ni Mungu wa rehema Biblia inasema katika Maombolezo 3:22 “Ni huruma za Bwana kwamba hatuangamii, Kwa kuwa rehema zake hazikomi.” Unaona hatuwezi kukwepa huruma na rehema za Mungu kabisa hata wakati wa majanga maana hii ndio tabia ya Mungu ndio rehema ndio jina lake kwa kweli na

Kutoka 34:5-7 “BWANA akashuka ndani ya lile wingu, akasimama pamoja naye huko, akalitangaza jina la BWANA. BWANA akapita mbele yake, akatangaza, BWANA, BWANA, Mungu mwingi wa huruma, mwenye fadhili, si mwepesi wa hasira, mwingi wa rehema na kweli; mwenye kuwaonea huruma watu elfu elfu, mwenye kusamehe uovu na makosa na dhambi; wala si mwenye kumhesabia mtu mwovu kuwa hana hatia kamwe; mwenye kuwapatiliza watoto uovu wa baba zao, na wana wa wana wao pia, hata kizazi cha tatu na cha nne.”

Bila rehema za Mungu hakuna mwanadamu angestahili kuwepo, Bila rehema za Mungu hakuna mwanadamu angeweza kuhesabiwa haki, Bila rehema za  Mungu tungeweza kuangamia, kila mmoja wetu anapaswa kukumbuka rehema, rehema zinabeba, reheema zinafungua njia, rehema za Mungu zinatutunza rehema ni uhai wetu!

Madhara ya kukosekana kwa rehema

Ni ukweli uio wazi kuwa hakuna mtu anaweza kumfikia Mungu na hata kuomba kama hakuna rehema, rehema za Mungu zingekosekana hali ya kila mtu na kila mwanadamu ingekuwa mbaya sana duniani, tunaweza kuona wakati wa agano a kale Mungu alipotaka kukaa kati kati ya wanadamu kupitia hema ya kukutania alitoa maelekezo kwa Musa kutengeneza Sanduku la agano ili ipatikane njia ya rehema za Mungu kuwafikia wana wa Israel Mungu alielekeza kuwa ni lazima kiwepo kiti cha rehema, maelekezo haya ni muhimu sana kwa sababu yanaonyesha wazi kuwa Mungu anakaa juu ya kiti cha rehema, niseme hivi ofisini kwa Mungu anapokuwa kazini na kufanya kazi zake zote kiti alichokikalia ni Rehema, bila rehema huwezi kufanikiwa kuwa na mawasiliano yoyote na Mungu.  

Kutoka 25:17-22 “Nawe fanya kiti cha rehema cha dhahabu safi; urefu wake utakuwa dhiraa mbili na nusu, na upana wake dhiraa moja na nusu. Nawe fanya makerubi mawili ya dhahabu; uyafanye ya kazi ya kufua, katika hiyo miisho ya kiti cha rehema, huku na huku. Weka kerubi moja mwisho mmoja, na kerubi la pili mwisho wa pili; fanya hayo makerubi ya kitu kimoja na kiti cha rehema, mwisho huku na mwisho huku. Na hayo makerubi yatainua mabawa yao juu, na kukifunika hicho kiti cha rehema kwa mabawa yao, na nyuso zao zitaelekeana hili na hili; nyuso za hayo makerubi zitaelekea kiti cha rehema. Weka kiti cha rehema juu ya hilo sanduku, kisha utie huo ushuhuda nitakaokupa ndani ya sanduku. Nami nitaonana nawe hapo, na kuzungumza nawe pale nilipo juu ya kiti cha rehema, katikati ya hayo makerubi mawili yaliyo juu ya sanduku la ushuhuda, katika mambo yote nitakayokuagiza kwa ajili ya wana wa Israeli.”               

Watu wa agano la kale waliweza kumfikia Mungu kupitia kiti cha rehema, Mungu ni mtakatifu mno, usafi wake na utakatifu wake unamtenga kwa wazi na kutoa sababu sahihi ya yeye kuwa mbali na wanadamu na hata akitakiwa kutokujali, lakini watu wabaya wasiokombolewa na damu ya Yesu waliweza kumfikia Mungu kwa damu za mafahari ya mbuzi na kondoo na sadaka za kuteketezwa na damu ya kunyunyizwa iliyomwaga juu ya kiti cha rehema, hii ilikuwa ni picha ya agano la kale yenye kutusaidia kufahamu umuhimu wa rehema sisi watu wa agano jipya, kuvunjwa kwa amri kumi za Mungu kukosekana kwa uadilifu kungepelekea kifo cha kila mtu lakini kabla Mungu hajaziangalia amri zake tulizozivunja anaangalia  anatuangalia sisi kupitia kiti chake cha rehema ambacho unajua wazi kuwa kwa damu ya Yesu Kristo iliyomwagiza pale msalabani tunawezeshwa kuwa na haki ya kupata rehema

Waebrania 4:14-16 “Basi, iwapo tunaye kuhani mkuu aliyeingia katika mbingu, Yesu, Mwana wa Mungu, na tuyashike sana maungamo yetu. Kwa kuwa hamna kuhani mkuu asiyeweza kuchukuana nasi katika mambo yetu ya udhaifu; bali yeye alijaribiwa sawasawa na sisi katika mambo yote, bila kufanya dhambi. Basi na tukikaribie kiti cha neema kwa ujasiri, ili tupewe rehema, na kupata neema ya kutusaidia wakati wa mahitaji.”

Unaona maandiko yako wazi kuwa sisi katika agano jipya sasa tunaweza kukaribia kiti cha rehema na kupewa rehema na neema ya kutusaidia wakati wa mahitaji yetu, kwa hiyo utakubaliana nami kuwa hatuhitaji rehema tu wakati tumefanya dhambi, lakini pia tunahitaji rehema ya Mungu wakati wa mahitaji yetu, na tunaweza kuwasiliana na Mungu pia kwa kupitia rehema,  na hivyo usishangazwe na Daudi kuomba rehema wakati akiwa anawindwa na adui au kuomba rehema akiwa vitani, zaburi yake inatufunulia wazi umuhimu mkubwa wa rehema ya Mungu na madhara makubwa ambayo yangetupata endapo Mungu angekuwa sio mwingi wa rehema! Kama sio rehema za Mungu hali ya kila mmoja wetu ingekuwa mbaya. Mungu alipokaa juu ya kiti cha rehema damu ilifunika madhaifu ya kibinadamu na kusababisha Mungu asijali wala kuruhusu hasira yake kuwaka dhidi ya wanadamu, unakumbuka ni alama ya damu katika miimo ya milango iliyowaokoa wanadamu wote waliokuwa ndani ya nyumba zilizowekwa alama ya damu bila kujali ni jinsia gani iko ndani, ni kabila gani iko ndani na nyumba zote misiri ambazo hawakuwa na alama ya damu waliangamizwa, ni alama ya damu ndio iliyomuokoa kahaba Rahabu na familia yake yote, wote waliokuwamo katika nyumba yake walisalimika kwa sababu ya alama ya damu, asante sana Yesu kuhani mkuu kama sio damu yake aliyoimwaga msalabani leo tungekuwa pabaya Yesu ndio kiti cha rehema damu yake ina nguvu, ina uwezo wa kututetea kama sio damu yake leo hii tunapoigwa kwa hukumu, kwa magonjwa, kwa laana, kwa hasira ya Mungu, kwa majini, kwa mapepo kwa wachawi kwa nguvu za giza na changamoto nyingi sio hivyo tu hata tusingeweza kusamehewa dhambi zetu pia

Waebrania 9:22-28 “Na katika Torati karibu vitu vyote husafishwa kwa damu, na pasipo kumwaga damu hakuna ondoleo. Basi ilikuwa sharti nakala za mambo yaliyo mbinguni zisafishwe kwa hizo, lakini mambo ya mbinguni yenyewe yasafishwe kwa dhabihu zilizo bora kuliko hizo. Kwa sababu Kristo hakuingia katika patakatifu palipofanyika kwa mikono, ndio mfano wa patakatifu halisi; bali aliingia mbinguni hasa, aonekane sasa usoni pa Mungu kwa ajili yetu; wala si kwamba ajitoe mara nyingi, kama vile kuhani mkuu aingiavyo katika patakatifu kila mwaka kwa damu isiyo yake; kama ni hivyo, ingalimpasa kuteswa mara nyingi tangu kuwekwa msingi wa ulimwengu; lakini sasa, mara moja tu, katika utimilifu wa nyakati, amefunuliwa, azitangue dhambi kwa dhabihu ya nafsi yake. Na kama vile watu wanavyowekewa kufa mara moja, na baada ya kufa hukumu; kadhalika Kristo naye, akiisha kutolewa sadaka mara moja azichukue dhambi za watu wengi; atatokea mara ya pili, pasipo dhambi, kwa hao wamtazamiao kwa wokovu.”

Ni damu ya Yesu pekee inayoweza na ambayo inalia kwake ili tupate rehema ndio yenye nguvu, inatupa kibali, inatupa mamlaka dhidi ya uovu inatuthibitishia usalama, inavunja vifungo vya kila aina inasafisha, inatupa uhakika wa kusamehewa na kuondolewa hatia zetu za mambo yaliyopita yaliyopo na yajayo inavunja minyororo yote na misiba na huzuni, inaondoa utumwa wa aina yoyote katika maisha yetu inawafanya majini na mapepo kutuogopa ni damu ya Yesu ndio kiti cha rehema                

Ikikosekana rehema maisha huwa na majuto  na uchungu mkubwa sana, visasi na mikasa na maisha ya uadui kati ya wanadamu kwa wanadamu yanaweza kutokea pale rehema inapokosekana, kama shetani anataka kuangamiza maisha yako moja ya njia atakayoifanya ni kuhakikisha ya kuwa unakosa Rehema, anapoitwa mshitaki wetu na kazi anayoifanya ya kushitaki ni kuhakikisha kuwa tunakosa rehema kwa Mungu alafu tunaangamizwa au kupitia machungu na hali ngumu,  ni jambo baya sana Mungu anapokubali kuacha kutuangalia kupitia rehema zake

Zekaria 11:6 “Maana mimi sitawahurumia tena wenyeji wa nchi hii, asema Bwana; bali, tazama, nitawatia, kila mmoja wao, mikononi mwa mwenzake, na mikononi mwa mfalme; nao wataipiga hiyo nchi, wala mimi sitawaokoa mikononi mwao.”

Ezekiel 7:8-9 “Basi hivi karibu nitamwaga ghadhabu yangu juu yako, nitazitimiza hasira zangu juu yako, nami nitakuhukumu sawasawa na njia zako; nami nitakupatiliza machukizo yako yote. Jicho langu halitaachilia, wala sitaona huruma; nitakupatiliza njia zako na machukizo yako yote yatakuwa katikati yako; nanyi mtajua ya kuwa mimi, BWANA, napiga.”

Unaweza kuona ulinzi wetu na usalama wetu uko katika rehema za Mungu, Rehema zikikosekana utaweza kuona tukipatilizwa, tukishughuikiwa, tukinyooshwa, ghadhabu ya Mungu itakuwa juu yetu hasira zake zitawaka, tutahukumiwa, kila njia yetu itanyooshwa, tutalipia kila dhambi, tutakosa msaaada tutakutana na machukizo, tutapigwa, tutaonewa, tutakuwa hatarini, tutatiwa mikononi mwa adui zetu, tutadhalilishwa, na kutendewa mabaya na uonevu wa kila aina kwa hiyo utakubaliana nami kuwa kuna madhara makubwa sana ikikosekana rehema! Kanisani kukikosekana rehema, waliookoka wakikosa rehema, taasisi zikikosa rehema, hospitali kukikosa rehema, shuleni na nyumbani katika ndoa ikikosekana rehema hakuna kitu kinaweza kusimama Daudi alielewa umuhimu wa Rehema akasema unirehemu ee bwana unirehemu maana nafsi yangu imekukimbilia wewe!

Unirehemu maana nafsi yangu imekukimbilia wewe

Zaburi 57:1-3 “Unirehemu, Ee Mungu, unirehemu mimi, Maana nafsi yangu imekukimbilia Wewe. Nitaukimbilia uvuli wa mbawa zako, Hata misiba hii itakapopita. Nitamwita MUNGU Aliye juu, Mungu anitimiziaye mambo yangu.  Atapeleka toka mbinguni na kuniokoa, Atukanapo yule atakaye kunimeza. Mungu atazipeleka Fadhili zake na kweli yake

Daudi alikuwa anajua anachokiomba na sio tu alikuwa akiomba rehema kwa Mungu yeye mwenyewe alikuwa mstari wa mbele kuishi kile anachokiomba, kama hujawahi kuishi maisha ya kuwa na maadui nataka nikuambie hakuna jambo baya sana duniani kama kuwa na maadui, vilevile kama hujawahi kuchukiwa nataka nikuambie hakuna jambo baya duniani kama kuchukiwa, na pia kama hujawai kuona madhara ya kisasi nataka nikujulishe kuwa hakuna jambo baya kama kulipa kisasi, Daudi alichagua rehema alijua kuwa rehema inalipa Mwanaye mkuu baadaye Yesu Kristo mwana wa Daudi alikazia wazi kuwa rehema kwa wengine inatuzalishia rehema kwa Mungu ona Mathayo 5:7Heri wenye rehema; Maana hao watapata rehema.”  Rehema inatusaidia kutokulipa mabaya kwa mabaya rehema ndio inayoongoza kusamehe, kuachilia maumivu yote, uwezo wetu wa kutokuinua mkono wetu juu ya adui zetu ndio unaoonyesha ukomavu wetu wa kiroho ni rehema, Daudi alimua kumuachia Mungu, kuhusu Sauli, alikuwa na uzoefu kuwa hata Nabali aliyemtukana matusi pamoja na kuwa alimtendea wema alitaka kumuua kwa mikono yake Mwenyewe lakini alipotulizwa na Abigaili Mungu alinyoosha mkono wake juu ya Nabali yeye mwenyewe kwa niaba ya Daudi, chochote ambacho tunataka Mungu atufanyie Yesu alionyesha kuwa Mungu anaweza kutupa kama pia tunawafanyia wengine Mathayo 6:14-15 “Kwa maana mkiwasamehe watu makosa yao, na Baba yenu wa mbinguni atawasamehe ninyi. Bali msipowasamehe watu makosa yao, wala Baba yenu hatawasamehe ninyi makosa yenu.”

Kwa lugha nyingine ili tupate rehema kwa Mungu hatuna budi kuwa na rehema kwa wanadamu wenzetu, Daudi aliifahamu siri hii, angeweza kumuua Sauli, angeweza kumdhuru kwa sababu alipewa pia neno la unabii kuwa nitamtia adui yako mikononi mwako nawe utamfanya vyovyote upendavyo hata hivyo aliamua kuchagua njia iliyobora zaidi ambayo ni Kumuachia Mungu, anapoomba rehema yeye mwenyewe alielewa kuwa anahitaji sana rehema , ndugu mpenzi msomaji wangu tunahitaji rehema sana, rehema kila mahali, katika ndoa katika malezi katika maongozi ni rehema za Mungu tu ndio maana hatuangamii kila mmoja wetu anahitaji rehema na rehema inalipa.

Mithali 11:17-18 “Mwenye rehema huitendea mema nafsi yake; Aliye mkali hujisumbua mwili wake. Mtu mwovu hupata mshahara wa udanganyifu; Apandaye haki ana thawabu ya hakika.”

Kuwa na Rehema kwa Daudi dhidi ya Sauli kulisababisha apate rehema pale alipokuja kufanya makosa makubwa, kuna benki ya rehema mbinguni, na hivyo kila mmoja wetu ajifunze kutoka kwa Daudi na kuachia rehema au kutunza rehema katika maisha yake hifadhi rehema ili baadaye uje upate faida ya rehema kutoka benki ya mbinguni, rehema ni ufunguo wa kila aina ya muujiza, tukikosa rehema tunajifungia Baraka zetu, liko gereza na taabu ya kulipia katika ulimwengu wa roho kama tumekosa rehema  ona mfano wa mtumishi asiye na rehema kuna vitu vya kujifunza

Mathayo 18:21-35 “Kisha Petro akamwendea akamwambia, Bwana, ndugu yangu anikose mara ngapi nami nimsamehe? Hata mara saba? Yesu akamwambia, Sikuambii hata mara saba, bali hata saba mara sabini. Kwa sababu hii ufalme wa mbinguni umefanana na mfalme mmoja aliyetaka kufanya hesabu na watumwa wake.  Alipoanza kuifanya, aliletewa mtu mmoja awiwaye talanta elfu kumi. Naye alipokosa cha kulipa, bwana wake akaamuru auzwe, yeye na mkewe na watoto wake, na vitu vyote alivyo navyo, ikalipwe ile deni. Basi yule mtumwa akaanguka, akamsujudia akisema, Bwana, nivumilie, nami nitakulipa yote pia. Bwana wa mtumwa yule akamhurumia, akamfungua, akamsamehe ile deni. Mtumwa yule akatoka, akamwona mmoja wa wajoli wake, aliyemwia dinari mia akamkamata, akamshika koo, akisema Nilipe uwiwacho. Basi mjoli wake akaanguka miguuni pake, akamsihi, akisema, Nivumilie, nami nitakulipa yote pia. Lakini hakutaka, akaenda, akamtupa kifungoni, hata atakapoilipa ile deni. Basi wajoli wake walipoyaona yaliyotendeka, walisikitika sana, wakaenda wakamweleza bwana wao yote yaliyotendeka. Ndipo bwana wake akamwita, akamwambia, Ewe mtumwa mwovu, nalikusamehe wewe deni ile yote, uliponisihi; nawe, je! Haikukupasa kumrehemu mjoli wako, kama mimi nilivyokurehemu wewe? Bwana wake akaghadhibika, akampeleka kwa watesaji, hata atakapoilipa deni ile yote. Ndivyo na Baba yangu wa mbinguni atakavyowatenda ninyi, msiposamehe kwa mioyo yenu kila mtu ndugu yake.”

Daudi anatufunza jambo kubwa sana kuhusu rehema, hatuna budi kumuomba Mungu na kumshihi aturehemu, kila eneo la maisha yetu lijawe na rehema na maisha yetu na kila tulifanyalo tukumbuke umuhimu wa kujawa na rehema weka rehema katika maisha ya watu ili Mungu naye akutunzie katika akaunti yako ya akiba za rehema maana ni rehema ya Mungu inayohitajika kila wakati na zaidi sana wakati wa mahitaji yetu, Bwana ampe neema kila mmoja wetu kuwa mtu aliyejaa rehema ili tuweze kupata rehema katika jina la Yesu Kristo, Amen

Rev. Innocent Samuel Kamote

Mkuu wa wajenzi mwenye hekima!

Alhamisi, 5 Oktoba 2023

Usinifanye laumu ya Mpumbavu!


Zaburi 39:7-9 “Na sasa ninangoja nini, Ee Bwana? Matumaini yangu ni kwako, Uniokoe na maasi yangu yote, Usinifanye laumu ya mpumbavu.  Nimenyamaza, sitafumbua kinywa changu, Maana Wewe ndiwe uliyeyafanya.



Utangulizi:

Ni muhimu kufahamu ya kwamba tuwapo duniani kama wanadamu tunakutana na changamoto nyingi, na changamoto hizi vyovyote iwavyo ni za kawaida tu wala usiogope, hakuna jambo jipya linalokupata kila jambo linalokupata ni la kawaida, na wala hauko peke yako wako wengi wanapitia au wamekwisha kupitia hivyo usiogope.

1Wakorintho 10:13 “Jaribu halikuwapata ninyi, isipokuwa lililo kawaida ya wanadamu; ila Mungu ni mwaminifu; ambaye hatawaacha mjaribiwe kupita mwezavyo; lakini pamoja na lile jaribu atafanya na mlango wa kutokea, ili mweze kustahimili.”

Daudi alikuwa mojawapo ya watu wa Mungu ambaye alipitia changamoto nyingi sana  na katika zaburi zake utaweza kugundua maswala kadhaa wa kadhaa ambayo sisi nasi tunayapitia katika maisha yetu, uko wakati ambapo Daudi alikuwa laumu yaani alifanywa LAUMU au alikuwa akilaumiwa kwa njia mbalimbali na kusemwa au kufanywa kuwa mfano wa matukio mabaya na yasiyofaa, au mfano wa watu ambao Mungu ni kama alikuwa akishughulika naye au kumuadhibu,  alilaumiwa sana Daudi kiasi cha kufikia kuvunjika moyo, aliumia au kuugua sana na hakukuwa na mtu wa kumuhurumia  wala kumsaidia hatimaye aliamua kumlilia Mungu  kama msaada wake ili asaidike naye ona:-

Zaburi 69:16-20 “Ee Bwana, unijibu, maana fadhili zako ni njema, Kwa kadiri ya rehema zako unielekee. Wala usinifiche uso wako, mimi mtumishi wako, Maana mimi nimo taabuni, unijibu upesi. Uikaribie nafsi yangu, uikomboe, Kwa sababu ya adui zangu unifidie. Wewe umejua kulaumiwa kwangu, Na kuaibika na kufedheheka kwangu, Mbele zako Wewe wako watesi wangu wote. Laumu imenivunja moyo, Nami ninaugua sana. Nikangoja aje wa kunihurumia, wala hakuna; Na wa kunifariji, wala sikumwona mtu.”           

Yawezekana nawe pia unapitia hali kama ya Daudi mwana wa Yese, unalaumiwa kila mahali, unaonekana kama sababu ya mabaya yaliyotokea katika jamii,  na hivyo unalaumiwa unaweza kulaumiwa kwa sababu ya  ndoa yako kuvunjika, unaonekana kama wewe ndio sababu ya kifo cha yule mgonjwa, unaonekana kama wewe ni sababu ya migogoro, unaonekana kuwa wewe ndio sababu ya ubadhirifu, unaonekana kama wewe ndio uliye changia ajali ile kutokea, au wewe ndio sababu ya mambo kwenda vibaya, unaweza kulaumiwa kwa sababu zozote zile, lawama wanafunzi wakifeli, lawama kwaya ikiharibu, lawama mboga ikiungua, chumvi ikizidi lawama, chumvi ikipungua, lawama, sukari ikizidi lawama, sukari ikipungua, lawama kwa sababu ya anguko la mtu Fulani, lawama ya kufukuzwa kazi kwa mtu Fulani, lawama timu yako imefungwa, lawama wewe ni kocha, lawama wewe ni kiongozi, lawama lawama lawama Daudi alipoona lawama zimeuvunja moyo wake alimuomba Mungu amsaidie lakini vilevile asiruhusu yeye kuwa laumu au mithali hata kwa watu wapumbavu!, tuwapo duniani hatuwezi kukwepa lawama, lakini si kila mtu ana haki ya kutulaumu,  tutajifunza somo hili zuri kwa kuzingatia vipengele vitatu vifuatavyo:-

·         Maana ya Laumu

·         Mambo yanayoweza kusababisha lawama

·         Usinifanye Laumu ya mpumbavu

Maana ya Laumu

Zaburi 39:7-9 “Uniokoe na maasi yangu yote, Usinifanye laumu ya mpumbavu. Nimenyamaza, sitafumbua kinywa changu, Maana Wewe ndiwe uliyeyafanya.

Neno laumu au lawama linalotumika katika maandiko hususani katika biblia ya kiebrania ambayo ndiyo iliyoleta tafasiri ya biblia kwetu upande wa agano la kale linatumika neno “CHERPAH”  kimatamshi KHER- PAW unaweza kutamka KEPAH neno hili maana yake KUZUNGUMZWA VIBAYA, KUSEMWA VIBAYA KWA SABABU FULANI, KUSEMWA KWA KULAUMIWA, KUSUKUMIZIWA LAWAMA, KUSHUTUMIWA, KUFANYWA KUWA MFANO WA TABIA MBAYA KWA, KUSEMWA VIBAYA KWA SABABU WEWE NDIO UNAEONEKANA UMESABABISHA JAMBO BAYA KUTOKEA, KUSEMWA KWA SABABU YA MATUKIO YA AIBU, KUSEMWA KWA MAKUSUDI YA KUSHUSHA NA KUHARIBU HESHIMA YAKO, KUSEMWA NA KUSHUTUMIWA KWA KUSUDI LA KUKUHARIBIA SIFA Kiingereza Shame, au reproach, Neno Reproach linatafasiriwa kama Disapproval, Kushutumiwa kwa makusudi ya kukataliwa, na hii sio kwa sababu tu ulifanya jambo baya hapana wakati mwingine hata kwa sababu ya ubora au uzuri au mafanikio au muonekano wako, kutokana na mvuto mkubwa ulionao na jinsi jamii inavyokukubali au wanavyokubali huduma yako na kazi zako na nyimbo zako na lolote lile unalolifanya, wako watu kwa sababu zao moyoni wanaweza kutafuta namna ya kukulaumu tu, wanatafuta cha kusema kwa kusudi la kukuharibia sifa ambazo Mungu amekupa

Mfano Luka 23:35-39 “Watu wakasimama wakitazama. Wale wakuu nao walikuwa wakimfanyia mzaha, wakisema, Aliokoa wengine; na ajiokoe mwenyewe, kama ndiye Kristo wa Mungu, mteule wake. Wale askari nao wakamfanyia dhihaka, wakimwendea na kumletea siki, huku wakisema, Kama wewe ndiwe mfalme wa Wayahudi, ujiokoe mwenyewe. Na juu yake palikuwa na anwani; HUYU NDIYE MFALME WA WAYAHUDI. Na mmoja wa wale wahalifu waliotungikwa alimtukana, akisema, Je! Wewe si Kristo? Jiokoe nafsi yako na sisi.”

Unaona lawama wakati mwingine inakuja tu kwa sababu ya wivu, Yesu hakuwa amefanya lolote baya lakini alilaumiwa, alishutumiwa alidhihakiwa na kukosolewa hata mtu aliyekuwa anasulubiwa pamoja naye alisema kama wewe ndiye Masihi basi jiokoe nafsi yako na sisi pia, hii ilikuwa ni lawama, siku ya mateso yake Yesu alilaumiwa, alilaumiwa kwa mambo mengi ya uongo, alilaumiwa kwa nukuu mbaya kutoka katika mahubiri yake, alilaumiwa kuwa alisema anaweza kulijenga katika siku tatu! na lawama nyingine nyingi zikiwa na makusudi ya kumvunjia heshima, kumdhihaki, kumuaibisha, kumfedhehi,  na kuharibu sifa zake aonekane mbaya, hafai na anatahili kuuawa

Je umewahi kukwepa maisha ya lawama? Mimi sijawahi kuyakwepa, lakini sio hivyo tu wakati mwingine hata sisi wenyewe huwalaumu watu wengine na kuwaona kama wao ndio sababu  ya kushindwa kwetu, mume anaweza kumlaumu mkewe kwa sababu ya tabia za watoto, watoto wanaweza kuwalaumu walimu kwa sababu ya kufeli kwao, na walimu pia wanaweza kuwalaumu wanafunzi kwa kusingizio kuwa ni wazito, lawama ziko kila mahali, Kanisani, katika ndoa, kazini, na hata ukiwa rais wa nchi watu watalaumu, maisha yakiwa magumu wanaweza kudhani kuwa wewe ndio sababu, hata ukiwa waziri wa Nishati umeme ukikatika watu wanaweza kukulaumu na hata kukutukana wakisema tayari waziri keshatuzimia umeme, katika maisha haya ni lawama lawama lawama, kukwepa maisha ya lawama kwa kiyunani ni ANEPILEPTONblameless, kutokushutumiwa au kulaumiwa!  Jambo hilo sio jepesi hata kidogo tuwapo duniani, tutalaumiwa sana jambo hili ni jambo la kawaida tu na hupaswi kuvunjika moyo!

Mambo yanayoweza kusababisha lawama.

Lawama ni tabia ya kibinadamu, lawama haitakuja iishie mpaka tunapoondoka Duniani, Hata mwanadamu anapofariki dunia watu wengi sana huuliza sababu ya kifo chake na kitu fulani kitabebeshwa lawama ya kifo hicho, maralia, presha, sukari, HIV, ajali uzembe, ujinga na kadhalika lazima kitakuwepo kitu cha kubebeshwa lawama ndipo mwanadamu aweze kupumua, mwanadamu hawezi kusikia Amani mpaka apate kitu cha kukisingizia, na kukipa lawama, mwanadamu analaumu ili kujisikia nafuu,  kutupia lawama wengine ni tatizo la kiroho na kisaikolojia ni njia ya kutafuta unafuu, Nini kinaweza kusababisha lawama?

Lawama ilijitokeza kwa mara ya kwanza kabisa baada ya anguko la Mwanadamu katika bustani ya Edeni Mara baada ya Mungu kuhoji sababu ya anguko la mwanadamu na kwanini Adamu na Eva walijificha walimpomsikia  ona

Mwanzo 3:9-13 “BWANA Mungu akamwita Adamu, akamwambia, Uko wapi? Akasema, Nalisikia sauti yako bustanini, nikaogopa kwa kuwa mimi ni uchi; nikajificha. Akasema, Ni nani aliyekuambia ya kuwa u uchi? Je! Umekula wewe matunda ya mti niliyokuagiza usiyale? Adamu akasema, Huyo mwanamke uliyenipa awe pamoja nami ndiye aliyenipa matunda ya mti huo, nikala. BWANA Mungu akamwambia mwanamke, Nini hili ulilolifanya? Mwanamke akasema, Nyoka alinidanganya, nikala.”

Kila mwanadamu mwenye upungufu, huwa anatafuta kujazilizia udhaifu wake kwa kutafuta visingizio, wanadamu wote katika uchanga wao na udhaifu wao hawako tayari kubeba lawama za wengine, marazote watu hutafuta wa kulaumu, ni wanadamu wachache sana ambao wanaweza kukubali kubeba adhabu au kuwajibika kwaajili ya watu wengine, ukomavu wa juu zaidi wa kiroho unatupeleka katika kiwango cha kufunika lawama za wengine na sisi kuwa mstari wa mbele katika kukubali kuzibela lawama. Bwana wetu Yesu ni kielelezo cha kubeba lawama sio za wanafunzi wake tu na lawama zetu zote wakati wote amekubali kuwajibika kwaajili yetu hata mbele za baba yake ona:-

Mathayo Luka 22:50-51 “Mmoja wao akampiga mtumwa wa Kuhani Mkuu, akamkata sikio la kuume. Yesu akajibu akasema, Mwe radhi kwa hili. Akamgusa sikio, akamponya.”

Yesu hakutaka moja ya wanafunzi wake bila shaka (Petro) alaumiwe na kuwajibishwa kuwa alimkata mtu sikio na badala yake aliomba radhi kwa niaba yake na kumponya mtu aliyekatwa sikio, huku ni kuwajibika kwa kiwango kikubwa na cha juu zaidi katika hali ya ukomavu wa mtu wa rohoni, aidha alipokuwa Msalabani hakutaka kuwalaumu Askari kwa kitendo cha kumsulubisha na badala yake alijitishwa lawama na kuwaombea msamaha kwa baba yake!

Lawama nyingine tunaweza kusababisha sisi wenyewe kwa sababu ya makosa yetu na dhambi zetu Mfano Daudi alipofanya dhambi na Bathsheba Nabii nadhani alimweleza wazi kuwa kosa lake linaweza kuwapa adui zake na adui za Bwana sababu ya kulaumu/kukufuru ona

2 Samuel 12: 13-14Daudi akamwambia Nathani, Nimemfanyia Bwana dhambi. Nathani akamwambia Daudi, Bwana naye ameiondoa dhambi yako; hutakufa. Lakini, kwa kuwa kwa tendo hili umewapa adui za Bwana nafasi kubwa ya kukufuru, mtoto atakayezaliwa kwako hakika yake atakufa.”

Unaona  Neno kukufuru linalotumika hapo Kiebrabia ni NAATS  ambalo maana yake umewapa kudhihaki, umewapa kutukana umewapa kusema vibaya umewapa sababu za kulaumu,  unaona hapo ni kutokana na makosa aliyokuwa ameyafanya hapa, watu walipata nafasi ya kulaumu au kukufuru, watu hawakumlaumu Daudi tu bali walimlaumu na Mungu wake kwa sababu Mungu alijivunia Daudi kuliko mtu mwingine yeyote alisema nimemwona Daudi mwana wa Yese mtu anayeupendeza moyo wangu, wakati mwingine kwa sababu ya neema na rehema za Mungu zilizo juu yetu na wakati mwingine kwa sababu ya uhusiano wetu ulio karibu sana na Mungu adui wanaweza kupata sababu ya kulaumu, uko wakati wanaweza kutafuta hata namna ya kukuchafua ili mradi tu wapate sababu ya kukulaumu, hata hivyo Daudi alikuwa mtu wa toba alikwisha tubu na Mungu alikubali kumsamehe lakini kwa kuwa adui zake hawajui njia za Mungu ni wajinga ni wapumbavu hawajui njia za Mungu Yeye alimuomba Mungu asimfanye kuwa laumu ya mpumbavu.

Tuwapo duniani hatuwezi kukwepa lawama kwa sababu yako mambo mengi sana tunayoweza kuyafanya au kufanyiwa, kusababisha au kusababishiwa lawama, kuishi kwa kukwepa lawama sio jambo jepesi hata ukijifungia sana ndani watu wanalaumu kuwa unajitenga na watu,  na kwa bahati mbaya sasa wako watu wengine kama ilivyokuwa kwa Daudi wanaongoza kwa kulaumiwa, wakati mwingine unaweza kulaumiwa hata bila ya sababu na wakati mwingine kwa sababu, Daudi alikuwa anapitishwa na Mungu katika shule Fulani ili aweze kuwa bora zaidi, katika wakati huo wa mapito yake alikuwa akilaumiwa kila sehemu na kila mahali mpaka akazidiwa na lawama, naye aligundua kuwa anapaswa kumuomba Mungu kwaajili ya lawama anazokutana nazo, alihesabu kuwa ni Mungu ameruhusu yeye awe lawama na anamuomba Mungu asimfanye kuwa lawama  alimsihi Mungu mara kadhaa asimuache akawa lawama wala asiabike, Mungu hatakuacha ulaumiwe hata milele tangu zamani Mungu alikuwa amekusudia kumkomboa mwanadamu kutoka katika lawama, lawama zinazotokana na sisi, au jamaa zetu wanaotuzunguka  ama lawama za aina yoyote ile, lawama ni alama ya madhaifu kibinadamu.

Usinifanye Laumu ya mpumbavu

Kwa nini Daudi alimuomba Mungu asimfanye kuwa Laumu ya Mpumbavu? Daudi jambo la kwanza Kabisa alikuwa akimlilia Mungu ili kwamba mapito anayoyapitia yasifikiriwe kuwa anapita kwa sababu yeye ni mwenye dhambi, Daudi anamuomba Mungu kuwa ni wachache sana wanaomjua Mungu wanaoweza kuzielewa njia za Mungu na kujua sababu ya mapito yake, lakini wengi na hasa watu wajinga na wapumbavu wanaweza wasielewe njia za Mungu na hivyo wanaweza kufikiri kuwa Mungu anamfanya Daudi kuwa somo la mtu aliyeivunja torati  na hivyo Mungu anamnyoosha au anamfanyia kama mtu mwenye dhambi au kama mtu ambaye hajasamehewa! Au mtu ambaye Mungu ameondoa mkono wake kwake, au mtu ambaye Mungu anaona hasira juu yake, badala yake yeye ni mtu mwenye kibali kwa Mungu Zaburi 39:8 “Uniokoe na maasi yangu yote, Usinifanye laumu ya mpumbavu.”

Mpumbavu ni mtu ambaye kwa mujibu wa maandiko hana hekima au ufahamu kuhusu njia za Mungu, au mtu ambaye amekataa maarifa au mtu asiyemcha Mungu Mithali 1:7 “Kumcha Bwana ni chanzo cha maarifa, Bali wapumbavu hudharau hekima na adabu.”  Mpumbavu ni mtu asiyemjua Mungu au hata kuamini kuwa Mungu yupo, Zaburi 14:1-3 “Mpumbavu amesema moyoni, Hakuna Mungu; Wameharibu matendo yao na kuyafanya chukizo, Hakuna atendaye mema. Toka mbinguni Bwana aliwachungulia wanadamu, Aone kama yuko mtu mwenye akili, Amtafutaye Mungu. Wote wamepotoka, wameoza wote pamoja, Hakuna atendaye mema, La! Hata mmoja.” Mpumbavu pia anaweza kuwa mtu aliyeamini lakini hazijui njia za Mungu!

Wapumbavu ni watu wenye dhambi, wasiomcha Mungu watu wenye sifa mbaya, wenye kutenda machukizo, wasiotenda mema, wasio na akili, wasiomtafuta Mungu, au waliopotoka hawa hueneza lawama kwa kusudi la kumshutumu Mungu kupitia udhaifu wa kibinadamu, walio nao watumishi wake, Mungu ni baba kwetu uhusiano wetu na baba hakuna anayeweza kuuvunja, kwani we inakuuma nini Baba wa nyumba ya jirani akiwa anamuadhibu mwanaye?  Kuadhibiwa kwa Daudi na Mungu hakukuwa na maana kuwa Mungu hakuwa amesamehe dhambi zake bali Mungu alikuwa na kusudi la kutengeneza nidhamu kwa Daudi, Mungu alikuwa anashughulika na mtoto wake lilikuwa ni jambo jema sana kwani alitakiwa kufa lakini hata adhabu ya kifo ilifutwa, dhambi yake ilifutwa lakini Mungu alimuingiza katika shule ya Nidhamu tu, Mungu alikuwa anamkemea Daudi asirudie kufanya madudu, Mungu alikuwa anamkumbusha kuwa mnyenyekevu, anamkumbusha kutikutumia madaraka yake vibaya, anamkumbusha kuwa anaye baba wa kimbingu ambaye hataruhusu Israel iwe na wafalme wanaofanana na wafalme wa dunia hii

Waebrania 12:6-11 “Maana yeye ambaye Bwana ampenda, humrudi, Naye humpiga kila mwana amkubaliye. Ni kwa ajili ya kurudiwa mwastahimili; Mungu awatendea kama wana; maana ni mwana yupi asiyerudiwa na babaye? Basi kama mkiwa hamna kurudiwa, ambako ni fungu la wote, ndipo mmekuwa wana wa haramu ninyi, wala si wana wa halali. Na pamoja na hayo tulikuwa na baba zetu wa mwili walioturudi, nasi tukawastahi; basi si afadhali sana kujitia chini ya Baba wa roho zetu na kuishi? Maana ni hakika, hao kwa siku chache waliturudi kama walivyoona vema wenyewe; bali yeye kwa faida yetu, ili tuushiriki utakatifu wake. Kila adhabu wakati wake haionekani kuwa kitu cha furaha, bali cha huzuni; lakini baadaye huwaletea wao waliozoezwa nayo matunda ya haki yenye amani.”        

Wakristo pamoja na watumishi wa Mungu wanaaswa katika maandiko, kutokuwa laumu, au wasiwe wenye kulaumiwa hata pamoja nakuishi katika ulimwengu huu wenye kizazi cha ukaidi na kilichopotoka ona

1Timotheo 3:2 “Basi imempasa askofu awe mtu asiyelaumika, mume wa mke mmoja, mwenye kiasi na busara, mtu wa utaratibu, mkaribishaji, ajuaye kufundisha;” 

Wafilipi 2:14-15 “Yatendeni mambo yote pasipo manung'uniko wala mashindano, mpate kuwa wana wa Mungu wasio na lawama, wala udanganyifu, wasio na ila kati ya kizazi chenye ukaidi, kilichopotoka; ambao kati ya hao mnaonekana kuwa kama mianga katika ulimwengu,”           

Katika nyakati zetu ni muhimu zaidi kuwa na maombi kama ya Daudi ya kumsihi Mungu asituifanye kuwa laumu kwa wapumbavu  na pia kwa wenye hekima, ni muhimu kuomba maombi kama haya kama hayajawahi kukuta Mshukuru Mungu lakini wenzako mara kadhaa watu wasio na nia njema wametutafuta sana ili watuchafue wapate cha kulaumu, Lakini ashukuriwe Mungu kwa neema yake ametutunza, Lakini nasema kama ilivyo kwa Daudi maombi yake yalikuwa ni muhimu sana  na yanatufunza kitu cha ziada katika nyakati zetu, Hii ni dua yangu na ninakuombea na wewe Mungu akutunze usiwe na lawama katika maisha yako na huduma ambayo bwana ameiweka ndani yako, waimbaji, wahubiri, viongozi, na wasanii pamoja na watumishi wote wa Mungu na wakristo kwa ujumla mtu asitulaumu!, Mungu amtunze kila mmoja wetu ili kwamba asipatikane mtu wa kutulaumu kwa habari ya utumishi wetu kwa Mungu, na kwa habari ya karama hii tunayoitumikia, kama tutakuwa na nidhamu na Munu ametufunza nidhamu kamwe Bwana hatatuacha tuangukie katika lawama za wapumbavu,

2Wakorintho 8:20-21 “Tukijiepusha na neno hili, mtu asije akatulaumu kwa habari ya karama hii tunayoitumikia; tukitangulia kufikiri yaliyo mema, si mbele za Bwana tu, ila na mbele ya wanadamu.”

Wapumbavu, tukitoa pepo watasema tunatoa kwa mkuu wa pepo, wapumbavu tukifanikiwa watasema sisi ni freemason, wapumbavu ukipitia changamoto mbalimbali wanasema tuna dhambi, hawajui njia za Mungu!, Daudi alikuwa na uhusiano na Mungu kama mtu na baba yake na Mungu alikuwa ameahidi kuwa akikosea atashughulika naye mtu mpumbavu hawezi kuelewa Daudi aliomba kwamba asifanyike laumu ya mpumbavu, mtu asiyeelewa njia na uhusiano alionao Daudi na Mungu

2Samuel 7:14-15 “Mimi nitakuwa baba yake, naye atakuwa mwanangu; akitenda maovu nitamwadhibu kwa fimbo ya binadamu na kwa mapigo ya wanadamu; lakini fadhili zangu hazitamwondoka, kama vile nilivyomwondolea Sauli, niliyemwondoa mbele yako.”

Daudi au mwana wa Daudi awaye yote anaposhughulikiwa na Mungu mpumbavu na anyamaze, kwani haimaanishi kuwa Mungu ameondoa fadhili zake, kwa mtumishi wake lakini baba yuko kwenye chuo cha Nidhamu na mtumishi wake

 1Wakorintho 11:32 “Ila tuhukumiwapo, twarudiwa na Bwana, isije ikatupasa adhabu pamoja na dunia.” Katika kiingereza mstari huu unasomeka hivi 1Corinthians 11:32 “But when we are judged by the Lord we are being disciplined so that we will not be condemned with the worldkwa msingi huo Mtu wa Mungu anapopita katika majaribu ni Mungu mwenyewe ndiye anayejua kwanini anapitia hayo, labda Mungu anampa mtu shule ya nidhamu ili asihukumiwe na watu wa dunia au kama watu wa dunia hii, Hivyo Daudi alikuwa na uelewa kuwa anapitia njia ngumu lakini bado ana uhusiano mzuri na Mungu, na hivyo wasio haki wanyamaze kimya hawana hadhi ya kumlaumu Daudi, Ndugu yangu Hakuna mtu mwenye hadhi ya aina yoyote ile mwenye haki ya kuinua mdomo wake kuhusu maisha yako, mtu akikushutumu ajue wazi kuwa hana haki, wala hadhi ya kuinua kinywa chake kuhusu maisha yako, Mungu sio wa mtu Fulani tu Mungu ni Mungu wa wote wenye mwili, ninapochapwa na baba yangu wewe inakuhusu nini, kila mmoja na familia yake na kila famuilia na sharia zake, mwache kuwashutumu wengine kama hamuwaombei, wala kuwashauri, wala kuwatakia Amani, kwani hakuna mtu awaye yote ajuaye uhusiano wako na Mungu, siri ya mapito yako iko kati yako wewe na baba yako wa mbinguni, USINIFANYE LAUMU YA MPUMBAVU!

 

Na Rev. Innocent  Kamote

Mkuu wa wajenzi mwenye Hekima


Jumatatu, 2 Oktoba 2023

Mwacheni alaani, Kwa sababu Bwana ndiye aliyemwagiza


2Samuel 16:5-12 “Basi mfalme Daudi alipofika Bahurimu, tazama, kulitoka huko mtu wa jamaa ya nyumba ya Sauli, jina lake akiitwa Shimei, mwana wa Gera; alitoka, akalaani alipokuwa akienda. Tena akamtupia Daudi mawe, na watumishi wote wa mfalme Daudi; na watu wote na mashujaa wote walikuwako mkono wake wa kuume na mkono wake wa kushoto. Na Shimei alipolaani, alisema hivi, Nenda zako! Nenda zako! Ewe mtu wa damu! Ewe mtu usiyefaa!  Bwana amerudisha juu yako damu yote ya nyumba ya Sauli ambaye umetawala badala yake; naye Bwana ametia ufalme katika mkono wa Absalomu mwanao; kisha, angalia, wewe umetwaliwa katika uovu wako mwenyewe, kwa sababu umekuwa mtu wa damu.  Ndipo Abishai mwana wa Seruya, akamwambia mfalme, Mbona mbwa mfu huyu amlaani mfalme bwana wangu? Na nivuke, nakusihi, nikaondoe kichwa chake. Mfalme akasema, Nina nini na ninyi, enyi wana wa Seruya? Kwa sababu yeye analaani, na kwa sababu Bwana amemwambia, Mlaani Daudi, basi, ni nani atakayesema, Mbona umetenda haya?Daudi akamwambia Abishai, na watumishi wake wote, Angalieni, huyu mwanangu, aliyetoka viunoni mwangu, anautafuta uhai wangu; si zaidi Mbenyamini huyu sasa? Mwacheni alaani, kwa sababu Bwana ndiye aliyemwagiza.  Labda Bwana atayaangalia mabaya yaliyonipata, naye Bwana atanilipa mema kwa sababu ya kunilaani kwake leo



Utangulizi:

Absalom Mwana wa Daudi alikuwa ameinuka kinyume na baba yake kwa kusudi la kumpindua na kumuua na kuchukua utawala wake, Hivyo ilimuazimu Daudi na majeshi yake kukimbia kwanza, akiwa njiani anakutana na mtu anaitwa Shimei yeye ni wa jamaa ya familia ya Sauli, Mtu huyu ghafla anaanza kurusha mawe na mavumbi akimlaani Daudi na kumtukana kama mtu aliyechukua madaraka baada ya Sauli, akimshutumu ya kuwa ni Mungu amesababisha machafuko kwa sababu ya Damu ya Sauli na watu wake (Damu ya nyumba ya Sauli), Baadhi ya mashujaa wa Daudi walimkemea na kumuomba Daudi waondoe kichwa cha mbwa mfu huyu, anayemtukana na kumlaani mfalme  jambo hili lilikuwa ni kinyume cha sheria na kinyume cha maagizo ya torati Kutoka 22:28 “Usimtukane Mungu, wala usimlaani mkuu wa watu wako.”

Kumlaani mfalme au kumtukana ni kosa ambalo kwa mujibu wa torati lilikuwa linahalalisha hukumu ya kifo, kama mtu akikubambikizia kesi ya kumtukana mfalme katika Israel pia ilihesabika kuwa umemtukana Mungu unaona?

 1Wafalme 21:8-14.  Basi, akaandika nyaraka kwa jina la Ahabu, akazitia muhuri yake, akazipeleka zile nyaraka kwa wazee, na kwa watu wenye nguvu waliokuwa katika mji wake, waliokaa pamoja na Nabothi. Akaandika katika zile nyaraka, akasema, Pigeni mbiu ya watu kufunga, mkamweke Nabothi juu mbele ya watu,  mkainue watu wawili, watu wasiofaa, ili wamshitaki, na kumshuhudia, kunena, Umemtukana Mungu na mfalme. Kisha mchukueni nje, mkampige kwa mawe, ili afe. Wale wazee wa mji wake, na walio wenye nguvu waliokaa mjini mwake, wakafanya kama Yezebeli alivyowaagiza, kama ilivyoandikwa katika nyaraka alizowapelekea. Wakapiga mbiu ya watu kufunga, wakamweka Nabothi juu mbele ya watu. Na hao watu wawili, watu wasiofaa, wakaingia, wakaketi mbele yake; wale watu wasiofaa wakamshuhudia Nabothi mbele ya watu, wakasema, Nabothi amemtukana Mungu na mfalme. Ndipo wakamchukua nje ya mji, wakampiga kwa mawe hata akafa. Wakampelekea Yezebeli habari, wakasema, Nabothi amepigwa kwa mawe, amekufa.”

Pamoja na kuwa ilikuwa halali kabisa kwa mujibu wa Torati mtu huyo kuuawa na ingekuwa ni makosa kwa mfalme kumuachia kwani naye angekuwa hajaitimiza torati, lakini kwa amri ya kifalme Daudi alimkinga mtu huyo na kuamuru kuwa aachiwe alaani kwa sababu Bwana ndiye aliyeagiza! Daudi hakutaka mtu huyo alipwe apatwe na mabaya wakati ule kwani alikuwa anaamini katika uaminifu wa Mungu, Yeye aliyetoa sheria ana haki ya kuhukumu kwa sheria yake “mwacheni alaani kwa sababu Bwana ndiye aliyemtuma”! Tutajifunza somo hili kwa kuzingatia vipengele vitatu vifuatavyo:-

·         Puuzia laana zisizo na maana au sababu

·         Kufuata njia ya Mungu

·         Kanuni ya Mungu kuhusu laana na Baraka.

Puuzia laana zisizo na maana au sababu.

Wote tunakubalina ya kuwa tukio kama hili halikuwa tukio rahisi, mara nyingi kama mtu anakulaani au kukutukana wengi wetu tungependa kujibu mapigo mara moja  na wakati huo huo tungeweza kutukana au kulaani mara moja  au tungemuomba Mungu amshughulikie mara moja hili ni jambo la kawaida la kibinadamu hata mimi napenda!

Lakini haikuwa hivyo kwa Daudi, mwana wa Yese yeye alimsamehe mtu huyu, na kuipuuzia laana yake na matukano yake na aliamini katika Mungu ya kuwa Mungu atamlipia na alitazamia kuwa Mungu atamrehemu yeye Daudi na rehema zake zitakuwa juu yake, Daudi aliiona laana ya Shimei na mabaya anayomtakia hayakuwa na mashiko kiasi cha kumfanya Mungu ashawishike kumlaani Daudi kwani laana hiyo haikuwa na maana wala sababu za haki, kwani Daudi hakufanya kosa katika familia ya Sauli iliyokuwa na mashiko ya yeye kulaanika kwa hiyo matusi na laana  za Shimei alizozitoa ilikuwa kama mbayuwayu tu katika kuruka kwake ona Daudi hakuwahi kuinua upanga wake njuu ya Sauli wala familia yake, Ni sauli ndiye aliyekuwa anataka kumuua Daudi lakini Daudi hakufanya hivyo hata kidogo!

Mithali 26:6 “Kama shomoro katika kutanga-tanga kwake, Na kama mbayuwayu katika kuruka kwake; Kadhalika laana isiyo na sababu haimpigi mtu.”

Shomoro na mbayu wayu ni ndege wadogo sana ndege hawa huwa na tabia aidha ya kufukuza wadudu au wakati mwingine kucheza kwa kukimbia hewani na kugeuka geuka unaweza kudhani kuwa wataanguka au kutua lakini huishia kugeuka ama unaweza kudhani wataenda moja kwa moja kumbe wanarudi, ukweli kama huu ndivyo ilivyo laana isiyo na maana au sababu, laana ni sawa na  uchawi ni hukumu, Ni tamko ni shambulizi linaloweza kutolewa na mtu na inaweza kumpata mtu kama ziko sababu za  haki za kufanyika hivyo, Daudi alikuwa na ujuzi huo wazi kuwa hakuna mtu anaweza kumlaani akalaanika yeye alianza harakati yake ya kwanza kabisa kwa kulaaniwa na Goliath ona

1Samuel 17:42-43 “Hata Mfilisti alipotazama huku na huku, akamwona Daudi akamdharau; kwa kuwa ni kijana tu mwekundu, tena ana sura nzuri. Mfilisti akamwambia Daudi, Je! Mimi ni mbwa hata umenijia kwa fimbo? Mfilisti akamlaani Daudi kwa miungu yake.”

Hata pamoja na Goliath kumlaani Daudi kwa miungu yale laana hiyo haikuweza kufanya kazi na kinyume chake akiwa anapigana vita kwa jina la Bwana ni Goliath ndiye aliyeishia kupigwa vibaya yeye na wafilisti wakifuatia  

1Samuel 17:45-50 “Ndipo Daudi akamwambia yule Mfilisti, Wewe unanijia mimi na upanga, na fumo, na mkuki, bali mimi ninakujia wewe kwa jina la Bwana wa majeshi, Mungu wa majeshi ya Israeli uliowatukana. Siku hii ya leo Bwana atakuua mkononi mwangu, nami nitakupiga, na kukuondolea kichwa chako, nami leo nitawapa ndege wa angani na wanyama wa nchi mizoga ya majeshi ya Wafilisti, ili kwamba dunia nzima wajue ya kuwa yuko Mungu katika Israeli. Nao jamii ya watu wote pia wajue ya kwamba Bwana haokoi kwa upanga wala kwa mkuki; maana vita ni vya Bwana, naye atawatia ninyi mikononi mwetu. Ikawa, hapo Mfilisti alipojiinua, akaenda akamkaribia Daudi, ndipo Daudi naye akapiga mbio, akalikimbilia jeshi ili akutane na yule Mfilisti. Daudi akatia mkono wake mfukoni, akatwaa humo jiwe moja, akalitupa kwa kombeo lake, akampiga Mfilisti katika kipaji cha uso; jiwe hilo likamwingilia kipajini, akaanguka chini kifudifudi. Hivyo Daudi akamshinda yule Mfilisti kwa kombeo na jiwe, akampiga Mfilisti, akamwua; walakini Daudi hakuwa na upanga mkononi mwake.”

Hakuna mtu anaweza kukulaani, ni Mungu pekee mwenye uwezo wa kufanya hayo, hakuna mwanadamua anaweza kukutakia mabaya ni Mungu tu, Adui au mtu awaye yote anapokulaani Mungu ana uwezo wa kuigeuza laana hiyo kuwa Baraka ona

Zaburi 109:27-28. “Nao wakajue ya kuwa ndio mkono wako; Wewe, Bwana, umeyafanya hayo. Wao walaani, bali Wewe utabariki, Wameondoka wao wakaaibishwa, Bali mtumishi wako atafurahi.”

Kumbukumbu 28:20 “Bwana atakuletea laana na mashaka, na kukemewa, katika yote utakayotia mkono wako kuyafanya, hata uangamie na kupotea kwa upesi; kwa ule uovu wa matendo yako, uliyoniacha kwayo.”    

Unaona kwa msingi huo hakuna manadamu ana mamlaka ya kulaani kile ambacho Mungu amekibariki, Daudi alikuwa na uhakika kuwa laana ya Shimei na matukano yake yote kinyume na Mfalme Havingeweza kuathiri lolote katika maisha ya Daudi, hata hivyo kisheria Shimei alipaswa kuuawa lakini Daudi alichagua rehema na alichagua kuachia kesi kwa Mungu, msomaji wangu mpendwa usiogope hakuna mtu anaweza kubadili mwenendo wa maisha yako kwa maneno yake yasiyo na maana, wako watu duniani ambao ni wepesi sana kulaani, ukimuudhi kidogo tu anamwaga laana nyingi na wengi wetu tunadhani kuwa laana hizo zimefanya kazi katika maisha yetu n ahata watu wengine wanadani kwa kukubali kuwa ulilaaniwa, nataka nikueleze ukweli wa kibiblia Hakuna laana inaweza kuwa na nguvu juu yako isipokuwa kama tutamuasi Mungu, au kuhusika katika dhuluma au kama kuna mashiko katika hilo

1Petro 3:13-17 “Naye ni nani atakayewadhuru, mkiwa wenye juhudi katika mema? Lakini mjapoteswa kwa sababu ya haki mna heri. Msiogope kutisha kwao, wala msifadhaike; bali mtakaseni Kristo Bwana mioyoni mwenu. Mwe tayari siku zote kumjibu kila mtu awaulizaye habari za tumaini lililo ndani yenu; lakini kwa upole na kwa hofu. Nanyi mwe na dhamiri njema, ili katika neno lile mnalosingiziwa, watahayarishwe wale wautukanao mwenendo wenu mwema katika Kristo. Maana ni afadhali kuteswa kwa kutenda mema, ikiwa ndiyo mapenzi ya Mungu, kuliko kwa kutenda mabaya.”  

Kufuata njia ya Mungu.

Ni muhimu kufahamu kuwa tuwapo hapa duniani wako watu wanaweza kuinuka kama shimei katika maisha yetu na kujiweka katika nafasi ya uadui katika maisha yetu, Hatukuja duniani kutengeneza maadui lakini wako watu kutokana na matukio kadha wa kadha duniani wanaweza kujiweka katika nafasi ya adui wao wenyewe linapokuja swala la namna hii ni muhimu kama ilivyokuwa kwa Daudi kuchagua njia ya Mungu, Shimei alikuwa amemlaani Daudi na kumlaumu kama mtu wa damu, lakini ni ukweli ulio wazi kuwa Sauli aljaribu kumuua Daudi karibu mara saba na Daudi alijaribu kuokoa maisha yake mara kadhaa, akiacha kila kitu kiwe katika mikono ya Mungu yeye aliamini kuwa Mungu ana njia iliyo bora zaidi ya kushughulika na wote wanaojiweka katika njia ya maisha yake kama adui zake na ndio Maana Yesu mwana wa Daudi alifundisha kuwa inatupasa kuwaombea maadui zetu na kuwapenda  Mwalimu alikuwa na maana gani hapa, kwa vyovyote vile alikuwa na maana ya kuwaacha katika mikono ya Mungu, kumuachia Mungu hakimu mwenye haki na mwenye hekima yake kuamua namna njema na nzuri itakayofaa Kwa adui zetu!

Mathayo 5:43-44 “Mmesikia kwamba imenenwa, Umpende jirani yako, na, Umchukie adui yako; lakini mimi nawaambia, Wapendeni adui zenu, waombeeni wanaowaudhi,”

Yesu mwenyewe alituachia kielelezo, hata waliokuwa wakimsulubisha aliwaombea rehema kwa Mungu kwa sababu ni Mungu pekee ndiye anayeweza kulaani, na sio kila mtu anaweza kulaanika kwa sababu wako ambao Mungu alikusudia kuwabariki tu uweza huo uko katika mikono ya Mungu hakuna mtu anaweza kukulaani bila Mungu kutoa kibali au wewe mwenyewe kuvunja maagizo kadhaa ya kiungu yanayoweza kuruhusu kanuni ya kuvuna na kupanda ikafanya kazi katika maisha yako, lakini ukweli unabaki wazi kuwa Mungu hana kigeugeu akimbariki mtu amembariki

Hesabu 23:8 “Nimlaanije, yeye ambaye Mungu hakumlaani? Nimshutumuje, yeye ambaye Bwana hakumshutumu?”

Hesabu 23:12 “Naye akajibu, akasema, Je! Hainipasi kuangalia, niseme neno lile Bwana atialo kinywani mwangu?

Daudi alikuwa na ufahamu huu wote kuhusu Neno la Mungu alielewa wazi kuwa hakuna mtu anaweza kumlaani na kuwa kama mtu atafanya hayo anaweza kufanya hayo kwa kibali kutoka kwa Mungu, na ndio maana akawa na ujasiri wa kusema mwacheni alaani Bwana ndiye aliyemuagiza, alijua wazi kuwa kama ni Bwana sawa lakini kama si Bwana hakuna mtu anayeweza kuudhuru kwa sababu zozote zile

Kunaweza kuwako nyakati katika maisha yetu ambapo watu wanaweza kupandisha kichaa na kuanza kutulaani  laana hizo zote zitakuwa ni maneno ya mkosaji tu yatakuwa ni maneno ya kusema mabaya yanaweza kutoka kwa ndugu, jamaa majirani, kazini na hata kanisani, watu wanaweza kukushambulia hadharani au sirini na vyovyote vile lakini tuna njia ambayo tunaweza kuichagua tusiwe kama watu wa ulimwengu huu, ambao wanaweza kujibu tukio kama hilo kwa mtindo wanaotaka wao, au tunaweza kuchagua njia ya Mungu kwa kuiga mfano wa Daudi na Yesu mwana wa Daudi,  na kupuuzia maneno ya kipuuzi na kuonyesha upendo kwa kumuachia Mungu tukijua wazi kuwa hawana madhara yoyote katika maisha yetu!

Kanuni ya Mungu Mtu kuhusu laana na Baraka.

Daudi alikuwa ni mfalme wakati anatukanwa mtu aliyemtukana alikuwa anastahili kufa, Daudi alionyesha kushughulika na kuhitaji Rehema zaidi kwa Mungu kuliko kuruhusu hukumu kwa mtu aliyemtukana, alionyesha uvumilivu, alionyesha unyenyekevu, alitarajia Mungu mwenyewe anaweza kuigeuza laana yake kuwa Baraka kutakiwa mabaya kuwa neema na rehema za Mungu, Mungu atatulipia sio tu huduma tunazofanya bali hata mateso tunayoyapitia  hivyo hatuna budi kumuamini Mungu kuwa atatulipia  2Wathesalonike 1:6 “Kwa kuwa ni haki mbele za Mungu kuwalipa mateso wale wawatesao ninyi Daudi alitambua kuwa ziko kanuni za kiungu mtu anapolaani alijihisi kuwajibika yeye kwa makosa yake  na kukubali mapenzi ya Mungu kuliko kushughulika na wengine, Yeye kama Mwanadamu alikosea sana na Mungu alikuwa amesema upanga hautaondoka nyumbani mwako sasa ulikuwa ni wakati ambapo mtoto wake mwenyewe ameinuka kinyume naye, na kama mtu baki tu anamtukana si shani sana ukilinganisha kuwa hata mwana wake wa kumzaa amefanya mapinduzi:-

-          Kuna wakati ambapo ni vema tukashughulika sana na changamoto zetu, kuliko kutaka kuna wengine wakiadhibiwa, wakati sisi tunapoangukia katika mikono ya Mungu na kunyooshwa, sio vema sana katika wakatio huo huo kutaka Mungu awanyooshe wengine, hatuna budi kutafuta kibali cha kiungu kwaajili ya maisha yetu na kumuhitaji Mungu awe msaada wetu zaidi, atupe rehema, aondoe kiburi, atunyenyekeshe, aondoe ile hali ya kujiona bora kuliko wengine, atupe utambuzi ya kuwa sisi sio wa thamani sana kuliko wengine, Hata hivyo uelewa katika neno la Mungu ulimsaidia sana Daudi kutambua kuwa maneno ya Shimei hayana nguvu kwake Hawezi mtu wa Mungu kulaaniwa na mtu awaye yote bila kibali cha Mungu

 

Hesabu 22:10-12 “Balaamu akamwambia Mungu, Balaki mwana wa Sipori, mfalme wa Moabu, amewatuma kwangu, akisema, Tazama, kuna watu waliotoka Misri, wanaufunika uso wa nchi; basi njoo unilaanie watu hawa; labda nitaweza kupigana nao, na kuwafukuza. Mungu akamwambia Balaamu, Usiende pamoja nao; wala usiwalaani watu hawa, maana wamebarikiwa.”

 

-          Mungu mwenyewe atambariki kila mtu anayetubarikia na atamlaani kila anayetulaani kwa sababu tumekusudiwa kuwa Bwaraka kwa mataifa yote Mwanzo 12:3 “nami nitawabariki wakubarikio, naye akulaaniye nitamlaani; na katika wewe jamaa zote za dunia watabarikiwa.”

 

-          Watu wote wanaopenda kulaani kwa mujibu wa maandiko wanajiweka katika hatari ya kupatwa wao na laana hizo na ndio maana maandiko yanatutaka tupendezwe na kubariki Zaburi 109:17-20 “Naye alipenda kulaani, nako kukampata. Hakupendezwa na kubariki, kukawa mbali naye, Alijivika laana kana kwamba ni vazi lake. Ikamwingilia moyoni kama maji, Na kama mafuta mifupani mwake. Na iwe kwake kama vazi ajivikalo, Na kama mshipi ajifungao daima. Ndiyo malipo ya washitaki wangu toka kwa Bwana, Na ya hao wanaoisingizia nafsi yangu mabaya.”

 

-          Hakuna silaha inayoweza kufanikiwa juu yakow ewe na mimi na hakuna ulimi au laana inayoweza kuinuka juu yetu kwani laana hiyo itahukumiwa Isaya 54:17 “Kila silaha itakayofanyika juu yako haitafanikiwa na kila ulimi utakaoinuka juu yako katika hukumu utauhukumu kuwa mkosa. Huu ndio urithi wa watumishi wa Bwana, na haki yao inayotoka kwangu mimi, asema Bwana.”

 

-          Laana isiyo na mashiko yaani sababu haimpigi mtu “Mithali 26:6 “Kama shomoro katika kutanga-tanga kwake, Na kama mbayuwayu katika kuruka kwake; Kadhalika laana isiyo na sababu haimpigi mtu.”

 

-          Mungu anauwezo wa kutangua laana hata iliyotoka kwa mzazi, Mwanzo 49: 3-4 “Reubeni, u mzaliwa wangu wa kwanza, Nguvu zangu, na malimbuko ya uwezo wangu. Umewapita wengine kwa ukuu na kwa nguvu. Umeruka mpaka kama maji, basi usiwe na ukuu, Kwa sababu ulikipanda kitanda cha baba yako, Ukakitia unajisi; alikipandia kitanda changu.” Maandiko yanaonyesha wazi kuwa Yakobo hakumbariki Reubeni kwa sababu alivuka mpaka alikipanda kitanda cha baba yake ni wazi kuwa kulikuwa na laana iliyojificha na hivyo ukoo huu ungefutika kabisa katika Israel na kuwa dhaifu sana lakini katika jicho la Rohoni baba wa kiroho Musa alitamka Baraka kuwa reubeni asife lakini angalau awe na watu wachache ona  Kumbukumbu 33:6 “Reubeni na aishi, asife; Lakini watu wake na wawe wachache.” Baba wa kimwili alimlaani Reuben na huenda alimfuta katika Hesabu zake lakini baba wa kiroho alibadilisha kauli na kutamka Baraka kuwa Reuben na aishi          

 

-          Usilitumie jina la Mungu kwa kulaani Kutoka 20:7 “Usilitaje bure jina la BWANA, Mungu wako, maana BWANA hatamhesabia kuwa hana hatia mtu alitajaye jina lake bure.” Neno usilitaje bure jina la Bwana Mungu wako katika lugha nyingine linamaanisha pia usilitumie jina lake kulaani No Using the name of God, your God, in curses or silly banter

 

-          Endapo tuliwahi kulaani watu ni vema ukatubu na kufuta laana hizo, kwa sababu kama watu hao walihesabiwa haki na Mungu kuliko wewe yanaweza kukurudia

 

 Yakobo 3:10-11 “Katika kinywa kile kile hutoka baraka na laana. Ndugu zangu, haifai mambo hayo kuwa hivyo. Je! Chemchemi katika jicho moja hutoa maji matamu na maji machungu?

 

Kristo anawatarajia wakristo kuwa watu wenye moyo kama wa Daudi, japo tunafahamu katika mazingira Fulani tunaweza kuzitumia zaburi kama zile zaburi za kulaani, lakini hata hivyo haipaswi kuwa jambo jepesi sana kukimbilia kulaani, na badala yake tunaweza kuonyesha wema wa Mungu kwa wale wanaotupinga ili yamkini ikiwezekana Mungu aweze kulete rehema kwetu pale tunapokuwa na rehema kwa wengine Mathayo 5:7 “Heri wenye rehema; Maana hao watapata rehema.”

 

-          Kataa kurudisha laana kwa anayekulaani – Warumi 12:14 “Wabarikini wanaowaudhi; barikini, wala msilaani.” Na 17-21 “Msimlipe mtu ovu kwa ovu. Angalieni yaliyo mema machoni pa watu wote. Kama yamkini, kwa upande wenu, mkae katika amani na watu wote. Wapenzi, msijilipize kisasi, bali ipisheni ghadhabu ya Mungu; maana imeandikwa, Kisasi ni juu yangu mimi; mimi nitalipa, anena Bwana. Lakini, Adui yako akiwa na njaa, mlishe; akiwa na kiu, mnyweshe; maana ufanyapo hivyo, utampalia makaa ya moto kichwani pake. Usishindwe na ubaya, bali uushinde ubaya kwa wema.”

 

-          Jifunze kubariki – Kubariki ni tabia ya uungu, Mungu alipokuwa anauumba ulimwengu mara kwa mara alikibariki kila alichokiumba, kubariki ni unabii, unatamka maneno mazuri ili yaweze kuwapata na wengine  unatamka kwa Imani, unahakikisha kuwa kile unachokiamuru kama Baraka kinakuwa kwa wengine nawe utabaki kama nabii wa Bwana kwa sababu unachokitamka kizuri kitawapata wengine,

 

Waebrania 11:20-21 “Kwa imani Isaka akawabariki Yakobo na Esau, hata katika habari ya mambo yatakayokuwa baadaye.Kwa imani Yakobo, alipokuwa katika kufa, akambariki kila mmoja wa wana wa Yusufu, akaabudu akiegemea kichwa cha fimbo yake.”     

 

Ukiyajua hayo Heri wewe ukiyatenda!

Na. Rev. Innocent Samuel Kamote

Mkuu wa wajenzi mwenye Hekima!

Jumatatu, 25 Septemba 2023

Hata Daudi Mwana wa Yese alirukwa !


1Samuel 16:10-11 “Yese akawapitisha wanawe saba mbele ya Samweli. Samweli akamwambia Yese, Bwana hakuwachagua hawa. Kisha Samweli akamwambia Yese, Watoto wako wote wapo hapa? Naye akasema, Amesalia mdogo wao, na tazama, anawachunga kondoo. Basi Samweli akamwambia Yese, Tuma watu, wamlete; kwa sababu hatutaketi hata atakapokuja huku.”


Utangulizi:

Je wewe umewahi kukataliwa? Umewahi Kurukwa? Umewahi kufanya kazi kwa bidii sana mahali na kwa moyo wako wote lakini hakuna mtu aliyetambua mchango wako, na hatimaye ukawa unapuuziwa tu?  Daudi alikuwa mmojawao! Yeye alikuwa ni kijana wa mwisho kati ya vijana nane wa Mzee Yese, ambaye alikuwa ni Mkulima na mfugaji kutoka kabila la Yuda huko Bethelehemu, lakini kijana huyu aliyekuwa mchunga kondoo alipuuzwa tu, hakujaliwa alirukwa, hakuehesabika kuwa ni kitu! Mungu alipomuagiza Nabii Samuel kwenda kumpaka mafuta mfalme ajaye wa Israel kwa Mzee aitwaye Yese, kila kijana wa Yese alisogezwa mbele ya Samuel katika ibada maalumu ya kumtia mafuta mfalme ajae vijana saba wote waliletwa kwa nini kwa sababu nadhani Karibu wote walikuwa na sifa zinazofaa kwa wao kuwa wafalme na wanadamu walikubali nadhani hata Samuel aliweza kufikiri wazi kuwa mpakwa mafuta angekuwepo pale bila shaka ona !

1Samuel 16:1-3 “Bwana akamwambia Samweli, Hata lini utamlilia Sauli, ikiwa mimi nimemkataa asiwamiliki Israeli? Ijaze pembe yako mafuta, uende, nami nitakupeleka kwa Yese, Mbethlehemi; maana nimejipatia mfalme katika wanawe. Samweli akasema, Nawezaje kwenda? Sauli akipata habari, ataniua. Basi Bwana akasema, Chukua ndama pamoja nawe, ukaseme, Nimekuja ili kumtolea Bwana dhabihu. Ukamwite Yese aje kwenye dhabihu, nami nitakuonyesha utakayotenda; nawe utamtia mafuta yule nitakayemtaja kwako.”

1Samuel 16:4-10 “Samweli akafanya hayo aliyosema Bwana, akaenda Bethlehemu. Wakaja wazee wa mji kumlaki, wakitetemeka, nao wakasema, Je! Umekuja kwa amani? Naye akasema, Naam, kwa amani; nimekuja kumtolea Bwana dhabihu; jitakaseni; njoni pamoja nami kwenye dhabihu. Akawatakasa Yese na wanawe, akawaita kwenye dhabihu. Ikawa walipokuja, alimtazama Eliabu, akasema, Yakini masihi wa BWANA yupo hapa mbele zake. Lakini Bwana akamwambia Samweli, Usimtazame uso wake, wala urefu wa kimo chake; kwa maana mimi nimemkataa. Bwana haangalii kama binadamu aangaliavyo; maana wanadamu huitazama sura ya nje, bali Bwana huutazama moyo. Ndipo Yese akamwita Abinadabu, akampitisha mbele ya Samweli. Naye akasema, Bwana hakumchagua huyu. Ndipo Yese akampitisha Shama. Naye akasema, wala Bwana hakumchagua huyu. Yese akawapitisha wanawe saba mbele ya Samweli. Samweli akamwambia Yese, Bwana hakuwachagua hawa.”

Unaweza kuona kwa vipimo vya kibinadamu wote waloisogezwa ilifikiriwa kuwa wanafaa lakini hata hivyo kwa bahati mbaya Mungu hakuwa amewakusudia hao  Mungu alimuonya Samuel kuwa yeye haaangalii kama wanadamu wanavyoangalia yeye ana mtazamo tofauti na wanadamu kwani yeye anaona tangu moyoni na hazingatii mtazamo wa nje peke yake!

1Samuel 16:7 “Lakini Bwana akamwambia Samweli, Usimtazame uso wake, wala urefu wa kimo chake; kwa maana mimi nimemkataa. Bwana haangalii kama binadamu aangaliavyo; maana wanadamu huitazama sura ya nje, bali Bwana huutazama moyo.”

Unaona aliyekusudiwa alidharauliwa, hakuwa ameonekana kuwa na sifa za kimaongozi, hakuna mtu aliyewajua watoto hawa kwa ukaribu kama  baba na kwa mawazo ya baba mzazi Yese alikuwa anaelewa vizuri sana watoto wenye kufaa kuongoza Israel pengine mapendekezo yake kwa Samuel na hata Kwa Mungu tukinena kiwazimu Yese alikuwa sahihi, yeye ni mzazi hivyo anajua , aliyebaki alikuwa ni mchungaji wa kondoo na kwa nyakati zile wachungaji wa kondoo na mifugo hawakudhaniwa kuwa ni watu safi, walikuwa wachafu ni watu wa porini na ni ngumu kumualika mtu kama huyo kwenye sherehe ya ibada kubwa mbele ya nabii aliyeheshimika sana Samuel hivyo zilikuwepo kila sababu za kumruka au kurukwa kwa kijana yule hii inaweza kumtokea mtu awaye yote miaka ya zamani kufaulu darasa la saba halikuwa jambo rahisi watu wengi sana walirukwa, kwenda kidato cha tano pia halikuwa jambo rahisi kama ilivyo leo na watu wengi walirukwa, wenginehawakwenda hata vyuo vya kawaida walirukwa lakini wengi katika hao Mungu amewatumia kuwa msaada mkubwa kwa taifa letu na makanisani pia, hapa simaanishi kuwa vyeti vya kitaaluma havina maana hapana hata kidogo Mungu alikuwa amemuandaa Daudi kwa namna vyingine hukohuko Porini kuwa kijana jasiri mwenye kuhurumia kondoo ambaye angeweza pia kuwa na huruma kwa kondoo wa Israel Mungu huwaandaa watumishi wake kwa muda mrefu na wa kutosha ili waweze kuja kuwa wenye kufaa kwa utumishi aliowakusudia ilimchukua Mungu miaka 80 kumuandaa Musa, Miaka 30 kumuandaa Yohana kwa huduma ya miezi sita tu Paulo mtume miaka 14 kwaajili ya injili ! Daudi naye alikuwa anaandaliwa kipekee na Mungu na alikuwa amehitimu shule hiyo ambayo hakuwa amemsimulia mtu na sasa Mungu anamuona mtu huyu kuwa anafaa lakini kwa vipimo vya kibinadamu anaonekana kuwa hafai

Wewe ndiye mtu yule !

Kurukwa  na wanadamu sio sababu ya Mungu kutokukutumia, Mungu anamtazamo wake mwingine tofauti sana, Hekima yake ni tofauti sana na Hekima ya kibinadamu, Mungu huchagua vitu vinyonye, vyenye mapungufu, vilivyodarauliwa na au kukataliwa katika hekima ya wanadamu ili avitumie kwa utukufu wake ona

1Wakorintho 1:25-29 “Kwa sababu upumbavu wa Mungu una hekima zaidi ya wanadamu, na udhaifu wa Mungu una nguvu zaidi ya wanadamu. Maana, ndugu zangu, angalieni mwito wenu, ya kwamba si wengi wenye hekima ya mwilini, si wengi wenye nguvu, si wengi wenye cheo walioitwa; bali Mungu aliyachagua mambo mapumbavu ya dunia awaaibishe wenye hekima; tena Mungu alivichagua vitu dhaifu vya dunia ili aviaibishe vyenye nguvu; tena Mungu alivichagua vitu vinyonge vya dunia na vilivyodharauliwa, naam, vitu ambavyo haviko, ili avibatilishe vile vilivyoko; mwenye mwili awaye yote asije akajisifu mbele za Mungu.”

Je wewe umewahi kurukwa? Umewahi kupotezewa? Umewahi kuonekana mbele za watu kuwa hufai hii ilitokea kwa Daudi mwana wa Yese na inawezekana pia ukawa unakubali moyoni mwako kuwa wewe sio mkubwa, wewe sio kama kaka zako, wao wana ujuzi mkubwa wao ni safi wewe ni mchunga mbuzi tu unaweza kujiweka katika daraja lolote la chini unalolitaka na watu pia wanaweza kukuweka katika mzani huo  lakini Mungu anakuita leo na anataka uchangamke kwa sababu wewe ndiye mtu yule wewe ndiye uliyechaguliwa wewe ndiye mtumishi wake  wewe ndiye mtu yule ambaye Mungu ameona moyo wako  na ndiye mtumishi wake aliyekuchagua!

Matendo 13:22-23 “Na alipokwisha kumwondoa huyo, akamwinua Daudi awe mfalme wao ambaye alimshuhudia, akisema, Nimemwona Daudi, mwana wa Yese, mtu anayeupendeza moyo wangu, atakayefanya mapenzi yangu yote. Katika uzao wake mtu huyo Mungu amewaletea Israeli Mwokozi, yaani, Yesu, kama alivyoahidi;”

Unaona Mungu alimuona Daudi tena alipendezwa naye na ni kupitia yeye na katika uzao wake Mungu alimleta Yesu Krito Bwana na Mwokozi wetu  Duniani, Kama Mungu aliweza kumtumia Daudi mchunga kondoo wa kawaida kabisa Mungu hashindwi kukutumia wewe! Iwe unajidharau au iwe umedharaulika au umerukwa!  

Wakati watu wanakutazama kwa jeuri, na kukuona kama hufai katika eneo hili au lile Yeye aliyekuumba anajua wapi unafiti kwa sababu ndiye aliyekuumba anakujua kuliko baba yako mzazi, anakujua kuliko manabii, anajua namna alivyokuandaa anajua uwanja wako wa mafunzo ya vita ulikuwa wapi na hivyo ni yeye ndiye anayependezwa nawe  hata kama wanadamu wanakukataa na kukuona haufai Mungu aliyekuumba anauona moyo wako naye anapendezwa nawe ona :-

Isaya 49:6-10 “naam, asema hivi, Ni neno dogo sana wewe kuwa mtumishi wangu ili kuziinua kabila za Yakobo, na kuwarejeza watu wa Israeli waliohifadhiwa; zaidi ya hayo nitakutoa uwe nuru ya mataifa, upate kuwa wokovu wangu hata miisho ya dunia. Bwana, mkombozi wa Israeli, Mtakatifu wake, amwambia hivi yeye anayedharauliwa na wanadamu; yeye anayechukiwa na taifa hili; yeye aliye mtumishi wao watawalao; Wafalme wataona, watasimama; wakuu nao watasujudu; kwa sababu ya Bwana aliye mwaminifu, Mtakatifu wa Israeli aliyekuchagua Bwana asema hivi, Wakati uliokubalika nimekujibu, na siku ya wokovu nimekusaidia; nami nitakuhifadhi, nitakutoa uwe agano la watu hawa, ili kuiinua nchi hii, na kuwarithisha urithi uliokuwa ukiwa; kuwaambia waliofungwa, Haya, tokeni; na hao walio katika giza, Jionyesheni. Watajilisha katika njia, na juu ya majabali watapata malisho. Hawataona njaa, wala hawataona kiu; hari haitawapiga, wala jua; kwa maana yeye aliyewarehemu atawatangulia, naam, karibu na chemchemi za maji atawaongoza.”

Mungu yuko tayari kumuinua mtumishi wake anayedharauliwa na wanadamu, anayechukiwa na kumfanya kuwa nuru kubwa sana kwa mataifa yote na hivi ndivyo alivyomfanyia Daudi ambaye kweli alidharauliwa lakini sasa ni mwenye sifa kubwa saba duniani, sio yeye tu Hata kristo alikataliwa na kudharauliwa lakini sasa jina la Yesu ni msaada mkubwa kwa watu wote duniani, hiki ndicho Mungu anachiokikusudia kwako wewe unayesioma ujumbe huu na unayepitia changamoto kama hii!         

Leo hii hakuna mtu maarufu sana katika Israel Kama Daudi, Bendera ya Israel ina nyota ya buluu katikati inaitwa nyota ya Daudi amekuwa ni kiongozi maarufu sana hata Yesu aliitwa mwana wa Daudi, alitumiwa na Mungu alikuwa na sifa za kiungu, alimsifu Mungu katika maisha yake, hakufanya jambo bila kumuuliza Mungu, alijaa neno, alikuwa mwenye msamaha, aliwapenda maadui, alipigana vita vingi vya bwana, alipokosea kama wanadamu alitubu, alijinyeneykeza kwa Mungu na Mungu alimtumia katika watu ambao Mungu anajivunia kuwa anapendezwa nao Daudi alikuwa ni mmoja wao, Mungu anakuamini anajua utatenda kwa busara naye atakuinua juu nawe utakuwa juu sana

Isaya 52:13 “Tazama, mtumishi wangu atatenda kwa busara, atatukuzwa, na kuinuliwa juu, naye atakuwa juu sana    

Kama ilivyo kwa Daudi Endelea kuwa hodari, jifunze njia za Mungu, mwamini Mungu jiungamanishe na Mungu katika dua na sala na maombi Na Mungu yule nimwabuduye kwa dhamiri safi atakutokea  na kuifuta aibu yako na kukuweka panapo nafasi na kukuinua juu sana kama yeye mwenyewe alivyokuandaa kwa utukufu wake !

Na Rev. Innocent Kamote

Mkuu wa wajenzi Mwenye Hekima. !