Zaburi 88:3-5 “Maana nafsi yangu imeshiba
taabu, Na uhai wangu umekaribia kuzimu. Nimehesabiwa pamoja nao washukao
shimoni; Nimekuwa kama mtu asiye na msaada. Miongoni mwao waliokufa nimetupwa,
Kama waliouawa walalao makaburini. Hao ambao Wewe huwakumbuki tena, Wametengwa
mbali na mkono wako.”
Utangulizi:
Mwandishi wa zaburi anazungumza
maneno magumu sana kuelekea kwa Mungu Muumba, ni haki yake na ni haki ya watu
wasiomjua Mungu na wanaomjua Mungu kusema maneno mazito kwa Muumba pale
yanapokuwa yametukuta, Si kuwa mwandishi hakuwa mtu mwenye tumaini kwa Mungu
hapana lakini alikuwa ni mtu aliyekata tamaa sana AMESHIBA TAABU na maisha yake yako hatarini kiasi ambacho ni kaburi
tu ndio analoliona linamkabili, anajina amehesabiwa kama watu waliokufa tayari
ingawa bado yuko hai, hana msaada, na anajiona kama ni miongoni mwa wafu basi
yeye ni mfu aliyetupwa hana thamani hata ya kuzikwa, sawa tu na watu waliolala
kaburini na wamesahaulika, sio na wanadamu tu hata Mungu ni kama hawakumbuki
tena nje, mbali kabisa na uwepo wa Mungu, hali kama hii inawakuta wanadamu wote
walioko duniani bila kujali una haki au hauna haki, unamcha Mungu au la, lakini
tuwapo safarini hapa duniani sio kila jambo linaweza kuwa rahisi, wakati
mwingine tunaweza kuwa na majanga mpaka nafsi zetu zikashiba taabu nini maana
ya nafsi iliyoshiba taabu? Hilo ndio jambo la msingi tutakwenda kuliangalia
katika somo hili !
Nafsi iliyoshiba taabu maana yake
ni nafsi iliyoelemewa na hisia kali na za ndani sana za maumivu yanayopelekea
mtu ajione kuwa hana matumaini tena ya kuishi, au kama mtu ambaye hawezi tena
kupata msaada wowote kutoka kwa yeyote hapa duniani, unahisi uko mwenyewe na
umekataliwa na huwezi kuunganishwa tena na yeyote, huwezi kushaurika na yeyote,
huwezi kutiwa moyo na yeyote zaidi ya magumu yanayokukabili tu, kuwa katika
hali ya nafsi kuugua, kuteseka, kusononeka na kuhuzunika au kushiba taabu
kunakuweka katika nafasi ya kuhisi kuwa uko mwenyewe na hata wale uliowategemea
wamekuacha ! na unachokiona katika maisha yako ni mauti tu ni kifo pekee ndicho
kinachokukabili, huoni tumaini lolote unaona giza, heri hata wewe unaweza hata
kusoma maandiko na au hata kufuatilia somo kama hili lakini nafsi iliyoshiba
taabu huwa inajawa na huzuni nyingi kiasi cha kufa ona :-
Mathayo 26:37-39. “Akamchukua Petro na wale
wana wawili wa Zebedayo, akaanza kuhuzunika na kusononeka. Ndipo akawaambia,
Roho yangu ina huzuni nyingi kiasi cha kufa; kaeni hapa, mkeshe pamoja nami.
Akaendelea mbele kidogo, akaanguka kifulifuli, akaomba, akisema, Baba yangu,
ikiwezekana, kikombe hiki kiniepuke; walakini si kama nitakavyo mimi, bali kama
utakavyo wewe.”
Je hali kama hiyo imewahi
kukutokea? Watumishi wengi wa Mungu wanakutana na hali kama hiyo, Bwana wetu
Yesu Kristo alikutana na hali kama hii alipokuwa akiukabili Msalaba alihitaji
msaada hata wa rafiki zake lakini walilala, alitamani hata wangekesha na kuomba
kwaajili yake lakini hawakuweza hawakuweza kumsaidia kwa sala wala hata kwa
maombi wala ushauri! Yeye alimuomba Mungu na ni malaika wa Bwana tu waliokuja
kumtia nguvu, Lakini afadhali hata Yesu alitiwa nguvu na malaika wa Bwana,
Lakini mwandishi wa zaburi yeye hakukuwa na mawasiliano ya aina yoyote na
mbingu.
Tuwapo duniani tunaweza kukutana
na changamoto na mapito magumu sana kiasi cha kutufikisha katika hali kama hii,
uwe mtu unayemuamini Mungu au hata usiyemuamini Mungu, kuna vipindi ambavyo
unaweza kukutana navyo vikakujaza huzuni kiasi cha nafsi yako kushiba, na
ukakosa majibu na kuanza kumlilia Mungu, kwanini mimi? Kwanini mimi eee Bwana!
Mungu wangu mbona mimi tuuuu!. Hivi Mungu yupo kweli jamani, hivi Mungu anaona,
hivi huyu muumba aweza kweli kutoa haki katika hili? Tunaweza kulia na kufikia
ngazi ya kufikiri kuwa ni Mungu ameamua kututaabisha ametutupa!, asante katika
agano jipya angalau tuna ufunuo kuwa shetani yupo na tunaweza kufikiri kuwa
changamoto nyingine zinasababishwa nay eye, Lakini nyakati za agano la kale
hawakujua sana habari za shetani na hivyo Mungu tu alibeba lawama zote! Ona:-
Zaburi 88:14-16 “Bwana, kwa nini kuitupa
nafsi yangu, Na kunificha uso wako? Nateswa mimi hali ya kufa tangu ujana,
Nimevumilia vitisho vyako na kufadhaika. Hasira zako kali zimepita juu yangu,
Maogofyo yako yameniangamiza.”
Unaona mwandishi wa zaburi hii
alifikia hatua ya kufikiri Mungu amemtupa, Mungu ameficha uso wake, na aliona
ni kama maisha yake yanapita katika hasira kali za Mungu na akachoka, huenda
nawe msomaji na msikilizaji wangu unapitia hali kama hii, Nafsi yako imeshiba
taabu, hakuna wa kukujali, uzito wa hali yako ni kama hakuna anayehisi, uko
ulimwenguni kama umefutwa tu, Lakini ashukuriwe Mungu wetu ni Mungu anayejali,
yeye hamtupi mtu na Bwana anataka kuinua nafsi yako kupitia ujumbe huu, Bwana
akupe neema ya kufuatilia somo hili kwa kina ili tuweze kupata suluhu, nafsi
zetu zikaponywe na kuacha kufadhaika katika jina la Yesu, Amen! Tutajifunza
somo hili kwa kuzingatia vipengele vitatu vifuatavyo:-
·
Maana ya
nafsi iliyoshiba taabu!
·
Nafsi
iliyoshiba taabu.
·
Mambo ya
kufanya Nafsi inaposhiba taabu.
Maana ya nafsi iliyoshiba taabu.
Nafsi iliyoshiba taabu kama
nilivyogusia kwenye utangulizi ni nafsi iliyoelemewa na hisia kali na za ndani
sana za maumivu yanayopelekea mtu ajione kuwa hana matumaini tena ya kuishi, Na
mwandishi wa zaburi anaonyesha kuwa alikuwa katika taabu iliyopitiliza kiasi
cha kukata tamaa au kiasi cha kufa mwenyewe anasema MAANA NAFSI YANGU IMEJAA TAABU neno taabu linalotumika hapo katika lugha
ya Kiebrania linatumika neno RAAH
ambalo limetajwa katika maandiko mara 663 na kwa kiyunani ni PERILUPOS ambalo tafasiri
yake kwa kiingereza ni EXCEEDING
SORROWFUL au AGONY ambalo maana
yake kwa kiingereza ni Extreme physical,
mental, and psychological suffering
yaani kwa lugha yetu ni Hatua ya juu na ya mwisho kabisa katika maumivu
ya mwili, akili na nafsi kuelekea kufa ni huzuni ya kupita kawaida ni kuugua
kwa ndani kabisa kama ingetokea mtu ni mgojwa wa mwili tungeweza kusema kuwa
yuko mahututi!
Sa katika maisha haya ya dunia
hii iliyojaa taabu kwa kawaida ziko taabu ambazo tunaweza kuvumilia lakini
inapofikia hatua ya kushiba taabu, maana yake mtu amefikia hatua ya mwisho
kabisa ya kuvumilia taabu hizo na anatamani katika akili yake afe! Yaani ni mtu
aliyehemewa na kukata tamaa na amezidiwa amelemewa ametaabika kiasi cha kuona
kifo ndio suluhu ya changamoto yake Nafsi inaposhiba taabu huwezi kamwe kuhisi
uwepo wa Mungu, unakuwa tu na hisia kuwa Mungu amekutelekeza na kama unamcha
Mungu unafikia ngazi ya kuchanganyikiwa kwamba Mungu anawezaje kuachilia hali ngumu
na nzito kama hii? ukweli ni kwamba rafiki yako wa karibu anakuwa ni giza tu na
unapoteza uwezo wa kufikiria kuwa utaokolewa, hata wanaojaribu kukutia moyo
unaweza kushangazwa na Imani yao kwani wewe unaona tu yasiyowezekana kwa ujumla
hakuna jambo baya duniani kama kuwa na nafsi iliyoshiba taabu, watu wengi
wanaojiua ni wale ambao nafsi zao zilijaa taabu na wakakosa msaada au hata watu
wa kuwatia moyo hii ni hali ngumu sana duniani
Mwandishi wa zaburi hii
anaonyesha kuwa alikuwa amefikia kiwango cha juu kabisa cha taabu na huzuni na
katika zaburi zinazoonyesha kiwango cha huzuni hii ni zaburi ya juu zaidi katika zaburi zote zenye hisia kali za
kuelemewa jambo kubwa la msingi ni kuwa zaburi hii imeandikwa kutundisha ya
kuwa Mungu hawezi kuatuacha hata kama tunapita katika hali ngumu kwa kiasi gani
kama tunamtegemea yeye ni lazima
atafanya njia na kutuokoa watoto wake bila kujali hali zetu
Kumbukumbu 31:6 “Iweni hodari na moyo wa
ushujaa, msiogope wala msiwahofu; kwa maana Bwana, Mungu wako, yeye ndiye
anayekwenda pamoja nawe, hatakupungukia wala kukuacha.”
Waebrania 13:5 “Msiwe na tabia ya kupenda
fedha; mwe radhi na vitu mlivyo navyo; kwa kuwa yeye mwenyewe amesema,
Sitakupungukia kabisa, wala sitakuacha kabisa.”
Mungu hatakuacha katika hali
yoyote ngumu endapo utaliitia jina lake, huyu ni baba anayejali, anayeona,
anayefuatilia, anayefundisha na anayetuwazia mema hata katika mazingira yasiyo
na matumaini, Mwandishi wa nyimbo za
injili namba 122 anasema umechoka umeshushwa moyo, mwambie Yesu, wote
tunajua kuwa tukimwambia Yesu hataweza kutuacha atashughulika nasi.
Nafsi iliyoshiba taabu.
Maisha sio kila wakati yana weza
kuwa ya furaha, mateso na kupoteza ni moja ya fungu la maisha ya mwanadamu,
Hata watu waliojitoa kwa Mungu na kutumiwa na Mungu kwa kiasi kikubwa walikutwa
na maisha ya taabu wakati Fulani, mwandishi wa zaburi hii alikuwa katika kilele
cha juu zaidi cha taabu yake, kwa kawaida kila mwanadamu kwa kiwango chake
anapofikia katika kiwango cha kuwa na huzuni yajuu kabisa au nafsi yake kushiba
taabu haoni nuru tena, anaona giza, haoni faida ya siku yake ya kuzaliwa na
kilele cha juu kabisa cha suluhisho lake huona ni kifo, Kuwa na uhusiano mzuri
au mbaya na Mungu sio sababu hata kidogo ya kukufanya usikutane na taabu, asili
ya taabu na masumbufu ya maisha haya ni anguko la Mwanadamu, Tangu Adamu na Eva
wazazi wetu walipoasi walifungua mlango wa kifo, mlango wa kifo hutafuta kuua
kila kitu katika maisha yetu, kila kitu kina pigwa vita ya mauti, tangu
unazaliwa, masomo yako, malezi yako, maisha yako, biashara zako, ndoa yako,
kazini kwako, familia yako, mke wako, mume wako, watoto wako, mazingira yako, chakula chako, biashara zako,
kanisa lako na chochote kile kwa namna yoyote ile vitatafuta kupingana nawe na
ndipo tunapojikuta tuko katika mazingira ya taabu, “Niliwahi kumwambia mke wangu hivi laiti ingekuwa maisha yanasomewa
kwanza kisha ukihitimu ndio unaishi, basi watu wengi tungechagua kutokuzaliwa
na kuishi duniani nadhani nikiwamo mimi!”, Lakini kwa bahati mbaya au njema
maisha ni zawadi ambayo hatukuichagua, lakini ni zawadi ya thamani na hivyo
kama tumepewa ni lazima tukubali kupambana na kila linalotukabili kwaajili ya
utukufu wa Mungu,
Yakobo maisha yake yalijaa taabu
alipoulizwa una miaka mingapi jibu lake lilikuwa refu kuliko swali lenyewe
Mwanzo 47:7-9 “Yusufu akamleta Yakobo
babaye ndani akamweka mbele ya Farao Yakobo akambariki Farao. Farao akamwuliza
Yakobo, Je! Siku za miaka ya maisha yako ni ngapi? Yakobo akamjibu Farao, Siku
za miaka ya kusafiri kwangu ni mia na thelathini; siku za miaka ya maisha yangu
zimekuwa chache, tena za taabu, wala hazikufikilia siku za miaka ya maisha ya
baba zangu katika siku za kusafiri kwao.”
Unaona huyu ni Mtumishi wa Mungu,
Yakobo au Israel, anapoulizwa swali kuhusu maisha anajibu hapa akiwa na miaka
130 anaonyesha kuwa afadhali siku za baba zake wao waliishi sana na changamoto
hazikuwa kubwa lakini yeye maisha yake YALIJAA
TAABU, kwa lugha nyingine alishiba taabu, Neno taabu lililotumika hapo ni
neno la Kiebrania RAAH, yaani mbaya,
za taabu, za shida, za maumivu, za mateso, za kukatisha tamaa, zisizopendeza,
zenye msongo wa mawazo, zenye huzuni, nzito, ngumu, sio za kupendeza, mbaya
sana, njaatupu, za hovyo, za kilio, za masononeko, za vitisho, za misiba, za
majanga, za bahati mbaya, zisizofaa, zenye madhara, hatarishi, huo ndio
ufafanuzi wa neno hilo RAAH yaani kuhuzunisha kupita kawaida unaona
Akieleza kuhusu maisha Ayubu
anasema katika kitabu chake Ayubu 14:1 “Mwanadamu aliyezaliwa na mwanamke Siku zake za kuishi si
nyingi, naye hujaa taabu.” Unaona Ayubu anatumia neno HUJAA TAABU kwa lugha ya Kiebrania
kumetumika neno ROGEZ linalotamkwa ROGHEZ akimaanisha siku za maisha ya
Mwanadamu hazina starehe, hazina utulivu, zinatisha, ni za hasira
Unajua Ayubu alikuwa Mcha Mungu
aliishi maisha matakatifu, alikuwa kuhani wa Mungu wa ngazi yajuu sana, lakini
hilo haliwezi kuwa sababu ya kutokuonja taabu naye maisha yake unafahamu nafsi
yake ilishiba taabu anasehema ni kama mwanadamu anazaliwa ili akutane na
mashaka tu
Ayubu 5:7-11 “Lakini mwanadamu huzaliwa ili
apate mashaka, Kama cheche za moto zirukavyo juu. Lakini mimi ningemtafuta
Mungu, Ningemwekea Mungu daawa yangu; Yeye afanyaye mambo makuu,
yasiyotambulikana; Mambo ya ajabu yasiyo na hesabu; Yeye atoaye mvua inyeshe
juu ya nchi, Na kuyapeleka maji mashambani; Awainuaye juu hao walio chini; Na
hao waombolezao hukuzwa wawe salama.”
Unaona Bahati nzuri yeye anasema
atamchagua Mung utu anapopita katika hali ngumu, wengine kwa sababu ya nafsi
kutaabika na kukosa matumaini ndipo wanapoamua kwenda kwa waganga, na wachawi
kutafuta msaada, wakati nafsi inapotaabika mtihani wa moyo unapita kupima kuwa
utamwangalia nani?
jambo kubwa zaidi la kumshukuru
Mungu mwandishi wa zaburi 88 hakuwahi kutaka kujiua, wala kuwaendea waganga, lakini alikuwa anaona kuwa Mungu ana wajibika
na taabu zote anazozipitia na kuwa ni yeye Mungu ambaye hajajibu maombi yake,
wakati nafsi yake imekaribia kufa, Nafsi yake imeshiba taabu, na amekuwa kama
mfu hata miongoni mwao waliokufa yeye ametupwa, ametengwa mbali na watu, watu
wanamchukia, yupo kwenye kifungo asichoweza kutoka, na anaanza kuwa na shaka
kama atamsifu Mungu na kusimulia matendo yake akiwa kaburini na inaonekana kuwa
tangu ujana wake maisha yamejaa taabu tu
hii ndio hali ya mtu anapofikia ngazi ya nafsi kushiba taabu
Ndugu yangu nafsi yako inapojaa
taabu wewe unakimbilia wapi? Nani anakuwa kuhani wako, je unadhani kujiua ndio
suluhu? Je unadhani wewe ndio pekee unayapitia haya? Hapana wewe sio wa kwanza,
wala wewe huko peke yako tofauti zetu ni kuwa wengine hawasimulii yanayowakuta lakini
kila mwanadamu hata waliofanikiwa wakikuelezea wanayoyapitia utajua kuwa watu
wengi wana nafsi zilizojaa taabu!
Mambo ya kufanya Nafsi inaposhiba taabu.
Najua kuwa umepitia changamoto
ngumu sana na wako watu wamepitia hata mimi pia, kila mmoja anesema aelezee
anayoyapitia nadhani kila mmoja sawa na mzani wake anaweza kukiri kuwa yeye
ndiye mwanadamu aliyepitia changamoto nyingi zaidi kuliko mwingine, vyovyote
iwavyo, masiha yangu pia yamekuwa na taabu zisizoweza kuelezeka, naweza kusema
pia kama Yakobo nadhani ni afadhali ya siku za baba zangu, hata hivyo sijawahi
kupungukiwa na wema wa Mungu, wakati wote nilipopoteza tumaini hata wakati wa
mambo magumu sana, niliziona fadhili za Bwana hakika wema nza fadhili zake
zinanifuata mimi siku zote za maisha yangu, nawe pia ndugu yangu Mungu
hatapunguza wema wake kwako yeye atakupa kutoboa, na hatimaye ataandaa meza
katikati ya watesi wako, nini unatakiwa kufanya wakati huu
1.
Mtumaini
Mungu – Mithali 3:5-6 “Mtumaini Bwana kwa moyo wako
wote, Wala usizitegemee akili zako mwenyewe; Katika njia zako zote mkiri yeye,
Naye atayanyosha mapito yako.”
2.
Mkimbilie
Mungu – Mwandishi wa zaburi 88 anaanza kwa kuliitia jina la Bwana hata
pamoja na nafsi yake kushiba taabu hakuwaza kwenda kwa waganga na badala yake
aliendelea kuliitia jina la Bwana kwaajili ya wokovu wake, Ni Yesu tu anayeweza
kuwa jibu la taabu zetu zote Zaburi
46:1-3 “Mungu kwetu sisi ni kimbilio na nguvu,
Msaada utakaoonekana tele wakati wa mateso.Kwa hiyo hatutaogopa ijapobadilika
nchi, Ijapotetemeka milima moyoni mwa bahari. Maji yake yajapovuma na kuumuka,
Ijapopepesuka milima kwa kiburi chake.”
3.
Ifundishe
nafsi yako kuabudu – Wakati unapofikia ngazi ya kuzidiwa na taabu kwa kuwa
ni nafsi ndiyo inayosumbuka nafsi hiyo useme nayo, uishirikishe kumuabudu
Mungu, uishirikishe kukumbuka mambo kadhaa hata kama ni machache aliyoyafanya
Mungu, ikumbushe nafsi isisahau kuwa na shukurani, ikumbushe nafsi matendo
makuu ya Mungu
Zaburi 103:1-4 “Ee
nafsi yangu, umhimidi Bwana. Naam, vyote vilivyo ndani yangu Vilihimidi jina
lake takatifu. Ee nafsi yangu, umhimidi Bwana, Wala usizisahau fadhili zake
zote. Akusamehe maovu yako yote, Akuponya magonjwa yako yote, Aukomboa uhai
wako na kaburi, Akutia taji ya fadhili na rehema,”
4.
Usijiombee
kufa – Maisha yetu ni zawadi, hatukuchagua kuzaliwa kwa hiyo unapokuwa
katika wakati wa taabu ni rahisi kumshutumu Mungu na kumwambia inatosha niondoe HAPANA usiombe hivyo kuomba hivyo ni
kukosa shukurani ni kumjibu Mungu kuwa ulituumba bure tu huna makusudi nasi, ni
afadhali kujua kuwa taabu yako ina somo gani baada ya kumaliza na Mungu katika
shule yake kuliko kujiombea kufa hata hivyo Mungu huwa hajibu dua za namna hiyo
-
Ayubu alijua
kuwa baada ya moto wa taabu yake atatoka akiwa angaa zaidi kama dhahabu ona
Ayubu 23:10-12 “Lakini
yeye aijua njia niendeayo; Akisha kunijaribu, nitatoka kama dhahabu. Mguu wangu
umeshikamana sana na hatua zake; Njia yake nimeishika, wala sikukengeuka. Sikurudi
nyuma kuiacha amri ya midomo yake; Nimeyatunza maneno ya kinywa chake zaidi ya
riziki yangu,”
-
Musa
alijiombea kufa – alipozidiwa na majukumu na taabu za uongozi wa kuongoza
watu wanaonung’unika Musa aliona taabu sana na akamuomba Mungu ikiwezekana afe
ona Hesabu 11:4-15. “Kisha mkutano wa wafuasi waliokuwa kati yao, wakashikwa
na tamaa; wana wa Israeli nao wakalia tena, wakasema, N'nani atakayetupa nyama
tule? Twakumbuka samaki tuliokula huko Misri bure; na yale matango, na
matikiti, na mboga, na vitunguu, na vitunguu saumu; lakini sasa roho zetu
zimekauka; hapana kitu cho chote; hatuna kitu cha kutumaini isipokuwa hii mana
tu. Na hiyo mana ilikuwa mfano wa chembe za mtama na kuonekana kwake kulikuwa
kama kuonekana kwake bedola. Watu wakazunguka-zunguka na kuikusanya, kisha
wakaisaga kwa mawe ya kusagia, au kuitwanga katika vinu, kisha wakaitokosa nyunguni,
na kuandaa mikate; na tamu yake ilikuwa kama tamu ya mafuta mapya. Umande
ulipoyaangukia marago wakati wa usiku, hiyo mana ilianguka pamoja nao. Basi
Musa akawasikia watu wakilia katika jamaa zao zote, kila mtu mlangoni pa hema
yake; na hasira za Bwana zikawaka sana; Musa naye akakasirika. Musa akamwambia
Bwana, Mbona umenitenda uovu mimi mtumishi wako? Kwa nini sikupata neema
machoni pako, hata ukanitwika mzigo wa watu hawa wote juu yangu? Je! Ni mimi
niliyewatungisha mimba watu hawa wote je! Ni mimi niliyewazaa, hata ikawa wewe
kuniambia, Haya, wachukue kifuani mwako, mfano wa baba mwenye kulea achukuavyo
mtoto anyonyaye, uende nao mpaka nchi uliyowaapia baba zao? Nipate wapi nyama
ya kuwapa watu hawa wote? Kwani wanililia, wakisema Tupe nyama, tupate kula. Mimi
siwezi kuwachukua watu hawa wote peke yangu, kwa kuwa ni mzigo mzito sana wa
kunishinda. Na kama ukinitenda hivi, nakuomba uniulie mbali, kwamba nimepata
fadhili mbele ya macho yako; nami nisiyaone haya mashaka yangu.” Ni hali ya kawaida wakati mtu anapokuwa
katika taabu na nafsi yakle ikalemewa huwa hawazi kuhusu uweza wa Mungu na
hivyo hufikiri kuwa suluhisho ni kufikia mwisho kuliko kuona aibu au uchungu
ulioko mbele lakini Musa hakujua kuwa Mungu alikuwa na mpango mwema nasema hivi
usikufe wala usiombe kufa kwa sababu Mungu anataka kutukuzwa katika njia
unayoipitia
-
Eliya – alikuwa
nabii aliyeweza kufanya mambo makubwa sana lakini ulipokuja mtihani wa taabu
alikata tamaa sana alitishiwa tu na malikia Yezebeli kuwa atamkata kichwa,
Eliya alikimbia mbio aligoma hata kula na maombi yake yakawa anataka tu afe ona
1Wafalme 19:
2-4 “Ndipo Yezebeli akampelekea Eliya mjumbe,
kusema, Miungu wanifanyie hivyo na kuzidi, nisipokufanya roho yako kesho,
panapo wakati huu, kama roho ya mmojawapo wa hao. Naye alipoona hayo,
aliondoka, akaenda aihifadhi roho yake, akafika Beer-sheba, mji wa Yuda,
akamwacha mtumishi wake huko. Lakini yeye mwenyewe akaendelea katika jangwa
mwendo wa siku moja, akaenda akaketi chini ya mretemu. Akajiombea roho yake
afe, akasema, Yatosha; sasa, Ee Bwana, uiondoe roho yangu; kwa kuwa mimi si
mwema kuliko baba zangu.”
Unaweza kumcheka Eliya ukisoma kisa kizima cha ushujaa
wake na mkwara kutoka kwa mwanamke, lakini zingatia kila mwanadamu ana kiwango
chake cha mwisho cha uvumilivu huyu alipotumiwa ujumbe tu kuwa kesho nitakuua
naapa kwa miungu yangu, Tayari aliogopa na kukimbia na kugoma kula na kulalal
chini ya mti akisubiri kufa, Mungu ndiye anayetoa maisha na ni mpaka kusudi
lake litimie ndani yetu Mungu hakukubali ombi hili, n ahata kifo kiliahirishwa
kwake, hivyo usijiombee kufa wala usiogope
5. Usiogope – kila wakati wito wa Mungu
katika maandiko unatutaka tusiogope hii ni kwa sababu Mungu yuko pamoja nasi
hata katika wakati tukiwa na hisia za kuwa peke yetu Mungu ni Roho kuna wakati
anaruhusu tuhisi uwepo wake hivyo hata miili yetu inahisi kuwa yuko pamoja nasi
lakini kuna wakati hatoruhusu tumhisi, tunahitaji Imani wakati huo, tunahitaji
kutupilia mbali hofu, tunahitaji kutembea katika shuhuda zake tu tuikijua kuwa
yupo na anashughulika na maisha yetu hata kama tunaiona mauti kumbuka yupo!
Zaburi 23:1-6 “Bwana
ndiye mchungaji wangu, Sitapungukiwa na kitu. Katika malisho ya majani mabichi
hunilaza, Kando ya maji ya utulivu huniongoza. Hunihuisha nafsi yangu; na kuniongoza
Katika njia za haki kwa ajili ya jina lake. Naam, nijapopita kati ya bonde la
uvuli wa mauti, Sitaogopa mabaya; Kwa maana Wewe upo pamoja nami, Gongo lako na
fimbo yako vyanifariji. Waandaa meza mbele yangu, Machoni pa watesi wangu.
Umenipaka mafuta kichwani pangu, Na kikombe changu kinafurika. Hakika wema na
fadhili zitanifuata Siku zote za maisha yangu; Nami nitakaa nyumbani mwa Bwana
milele.”
Hitimisho:
Mungu hatakusaliti – Mwandishi wa zaburi
hii ya 88 ni HERMAN Mwana wa KORAH huyu ndiye mwandishi wa zaburi hii ni
zaburi miongoni mwa zaburi zilizokuwa zinaimbwa wakati watu wanapopanda kwenda
Hekaluni zinaitwa zaburi za KUPANDIA hii
ndio zaburi chungu zaidi kuliko zote wayahudi waliita zaburi ya GIZA iliimbwa kwa machozi na watu
waliokuwa wanahitaji msaada wa Mungu wakiwa hawajui maisha yatakuwaje, wakiwa
na maswali mengi yasiyo na majibu wakifikiri kuwa Mungu pia amewaacha HERMAN anatuwakilisha sisi wote
tunaweza kulalamika nadhani mimi ni mlalamikaji zaidi kuliko hata ninyi
wasomaji wangu, nampenda Mungu lakini wakati mwingine simuelewi anaponipitisha
katika magumu namuona kama ameniacha namuona kama amenisaliti, HERMAN mimi na wewe msomaji wangu
tunamuona kama Mungu ametusaliti, na rafiki yetu ni giza tu nafsi imetupwa,
maombi hayajibiwi, wanaotujua wametuacha, fadhaa zimetujaa? Je umewahi kufikia
hali kama hii? Herman mwandishi wa zaburi hii Mwana wa kora aliifikia akidhani
Mungu amemsaliti,
Zaburi 88:14-18 “Bwana,
kwa nini kuitupa nafsi yangu, Na kunificha uso wako? Nateswa mimi hali ya kufa
tangu ujana, Nimevumilia vitisho vyako na kufadhaika. Hasira zako kali zimepita
juu yangu, Maogofyo yako yameniangamiza. Yamenizunguka kama maji mchana kutwa,
Yamenisonga yote pamoja. Mpenzi na rafiki umewatenga nami, Nao wanijuao wamo
gizani.”
Mungu ni
mwaminifu katika ahadi zake kwa vyovyote vila haitakuja itokee akuache na
asijali kuhusu maisha yako na yangu yeye hataweza kutusaliti wala kutuacha
gizani yuko pamoja nasi hata ukamilifu wa Dahari, atatutia nguvu, atatusaidia
na atatushika mkono na kutuinua hii ni ahadi yake na ndivyo itakavyokuwa katika
maisha yetu siku zote Amen
Isaya 41:10 . “usiogope,
kwa maana mimi ni pamoja nawe; usifadhaike, kwa maana mimi ni Mungu wako;
nitakutia nguvu, naam, nitakusaidia, naam, nitakushika kwa mkono wa kuume wa
haki yangu.”
Na. Mkuu wa wajenzi mwenye Hekima
Rev. Innocent Mkombozi Kamote.