Zaburi 31:14-18 “Lakini mimi nakutumaini
Wewe, Bwana, Nimesema, Wewe ndiwe Mungu wangu. Nyakati zangu zimo mikononi
mwako; Uniponye na adui zangu, nao wanaonifuatia. Umwangaze mtumishi wako Kwa
nuru ya uso wako; Uniokoe kwa ajili ya fadhili zako. Ee Bwana, nisiaibishwe,
maana nimekuita; Waaibishwe wasio haki, wanyamaze kuzimuni. Midomo ya uongo iwe
na ububu, Imneneayo mwenye haki maneno ya kiburi, Kwa majivuno na dharau.”
Utangulizi:
Ni muhimu kufahamu kuwa hapa
Duniani hasa Afrika sio kila mtu anaweza kufurahia mafanikio yako, mazungumzo
ya watu wengi kukuhusu wewe au mimi hufanyika zaidi pale tunapokuwa tumeharibu
au kuharibikiwa hayo ndio watu huyazungumza na kuyapa kipaumbele na kuyafurahia
zaidi, kuliko tunapokuwa na mafanikio, na kama wako watu katika nafasi ambayo
wanaweza kuhakikisha kuwa wanaharibu mafanikio yako wako tayari kuhakikisha ya
kuwa wanakuharibia hawa wanaitwa kwa kiingereza DESTINY KILLERS, yaani waua ndoto, au watu ambao hawafurahii kuona unafanikiwa
hawa ni wengi sana duniani kuliko wale wanaotaka ufanikiwe, hii ni kawaida tu
kwa sababu wanadamu wana tabia ya wivu na hawawezi kufurahia mafanikio yako!,
wengi wanafurahia tuwe sawa au uwe chini lakini usiwazidi wala usifanikiwe
kuliko wao, wako pia watu ambao hujipanga kwa namna mbalimbali ili kuhakikisha
ya kuwa hutoboi hawa wanaweza kuwa ni watu wanaotumiwa na shetani aidha
wakijijua au wakiwa hawajijui, lakini wanakuwepo tu katika jamii kuhakikisha
kuwa wanaharibu, wanaua, wanasambaratisha au wanahakikisha kuwa hufiki mbali au hufikii na katika
nyakati ambazo Mungu ameziandaa kwaajili yako!, wao wanaandaliwa kuhakikisha ya
kuwa wanakukwamisha, wanachelewesha, wanaharibu juhudi zako au wanadhoofisha Nyakati
ambazo Mungu anakusudia kwako, na hawaoni lolote jema kwako, wanazungumza
mabaya kukuhusu, wanakutakia kuharibikiwa, wanatamani wakukwamishe na hata
kuidhoofisha Imani yako, wakati huo wakidhani kuwa nyakati zako ziko katika
mikono yao na wanasahau kabisa kuwa ni Mungu ndiye anayeshika majira na nyakati
na mipango ya mtu ni Mungu peke yake
mwenye nyakati zetu!
Wafilipi 1:6 “Nami niliaminilo ndilo hili,
ya kwamba yeye aliyeanza kazi njema mioyoni mwenu ataimaliza hata siku ya
Kristo Yesu;”
Kumbuka ni Mungu ndiye aliyeanza
kazi njema na wewe, na ni yeye ndiye atakayeimaliza, hakuna mwanadamu anayeweza
kudai, au kujidai au kujisifu kuwa anashikilia hatima yako, wote wanaosema
ngoja tuone, hatoboi, ameisha, tumemaliza hakuna anayeweza kumaliza kile
ambacho Mungu amekisimamisha, mambo ya Mungu hukamilishwa na Mungu mwenyewe na
wanaoshindana nawe wanajiweka katika madhara kwani wanaweza kujikuta kuwa
wanapingana na Mungu heri wajiepushe
Matendo 5: 38-39 “Basi sasa nawaambia,
Jiepusheni na watu hawa, waacheni; kwa kuwa shauri hili au kazi hii ikiwa
imetoka kwa binadamu, itavunjwa, lakini ikiwa imetoka kwa Mungu hamwezi
kuivunja; msije mkaonekana kuwa mnapigana na Mungu.”
Akiyajua haya Daudi anasema
Nyakati zangu ziko mikononi mwako Ee bwana na anamuomba Mungu amlinde na maadui
zake, wala asimuache kuaibishwa, na wote wanaomfuatia wawe bubu,
wanyamazishishwe kuzimu, leo tutachukua muda kujifunza somo hili NYAKATI ZANGU KATIKA MIKONO YA BWANA kwa
kuzingatia vipengele vitatu vifuatavyo:-
1.
Maana
ya zangu katika mikono ya Bwana
2.
Mifano
ya uweza wa Mungu katika nyakati za watu mbalimbali
3.
Nyakati
zangu katika mikono ya Bwana
Maana ya Nyakati zangu katika Mikono ya Bwana
Zaburi 31:14-18 “Lakini mimi nakutumaini
Wewe, Bwana, Nimesema, Wewe ndiwe Mungu wangu. Nyakati zangu zimo mikononi
mwako; Uniponye na adui zangu, nao wanaonifuatia. Umwangaze mtumishi wako Kwa
nuru ya uso wako; Uniokoe kwa ajili ya fadhili zako. Ee Bwana, nisiaibishwe,
maana nimekuita; Waaibishwe wasio haki, wanyamaze kuzimuni. Midomo ya uongo iwe
na ububu, Imneneayo mwenye haki maneno ya kiburi, Kwa majivuno na dharau.”
Neno nyakati linalotumika hapo katika maandiko ya kiingereza linasomeka
katika namna hii
Psalm 31:14-18 “But I trust in you, O Lord:
I say You are my God” MY TIMES ARE IN YOUR HANDS Deliver me from my enemies and
from those who pursue me. Let your face shiner on your servant; save me in your
unfailing love. Let me noy be put to shame O Lord, for I have cried out to you,
but let the wicked be put to shame and lie silent in the grave. Let their lying
lips be silenced, for with pride and contempt they speak arrogantly against the
righteous”
Kifungu hiki cha maandiko ni
mojawapo ya kifungu cha Muhimu sana katika zaburi hii, Mwandishi alikuwa
akifanya maombi yanayoonyesha ya kuwa anamuamini Mungu na kuwa anamtegemea kwa
Ulinzi wake na mafanikio ya maisha yake dhidi ya watu wote wale wanaiomtakia
mabaya, Mwandishi sio tu kuwa alikuwa anatakiwa mabaya na adui zake lakini adui
zake walikuwa wamekwishakuchukua hatua kadhaa kuhakikisha kuwa hafanikiwi,
hatoboi hatoki na anamalizwa kwa namna yoyote ile, ni kama walikuwa wanafikiri
kuwa wameshamuweza, Lakini mwandishi
anamwambia Mungu kwamba yeye anamwamini na kwamba alikuwa anafahamu wazi kuwa NYAKATI ZAKE ZIKO KATIKA MKONO WA MUNGU hivyo
alipokuwa akikutana na vita na upinzani kutoka kwa maadui alikuwa anafahamu
kuwa yeye anatakiwa tu Kumuomba Mungu, kwa sababu yeye alifahamu kuwa alizaliwa
kwa kusudi la Mungu na kuwa yuko duniani kutimiza mpango wake katika wakati
uliokusudiwa na Mungu!
Neno Nyakati zangu Katika mikono
ya Bwana au kwa kiingereza My times in the hands of Lord kwa kiebrania linasomeka kama ETH kimatamshi AYTH ambalo maana yake ni
Majira na Makusudi, katika biblia ya kiingereza ya KJV limetumika mara 257 kumaanisha muda, mara 16 kumaanisha majira, mara 7 kumaanisha kusudi na mara 10 kumaanisha Kazi maalumu, hii maana
yake ni nini ? Mungu anapotupa muda wa kuishi ndani yake anatoa majira, muda
kazi na majukumu ambayo kila mwanadamu anatakiwa ayatimize awapo duniani
unaona! Na ili uyatimize kuna HATIMA yaani kilele cha kutimizwa kwa
majukumu hayo maalumu ambayo Mungu anayatoa kwa kila mtu kwa majira na nyakati
zake!
Kwa hiyo Mwandishi anapojieleza
kuwa Nyakati zangu zimo Mikononi mwake anamaanisha Hatima yaani Destiny, kusudi, wajibu, muda na kazi
maalumu aliyopewa na iliyokusudiwa kwake iko mikononi mwa Mungu, na kama ni
hivyo basi ni wazi kuwa juhudi na jitihada za maadui na wapinzani, na wanena
mabaya, na wanga, na wachawi, na majeshi, na wazandiki
na wafitini, na wapika majungu, na walozi, na wenye chuki, na wenye wivu na
wenye husuda kamwe haziwezi kuharibu wala kukatisha kusudi la Mungu
lililokusudiwa na Mungu kwa wakati wake na kuwa ni lazima litatimia, hafi mtu
wala haaribikiwi mtu, kwa sababu hao woote hawana hatimiliki ya Nyakati
zilizokuduiwa kwako
-
Habakuki
2:3 “Maana njozi hii bado ni kwa wakati ulioamriwa,
inafanya haraka ili kuufikilia mwisho wake, wala haitasema uongo; ijapokawia,
ingojee; kwa kuwa haina budi kuja, haitakawia.”
-
Isaya 46:9-10
“kumbukeni mambo ya zamani za kale; maana mimi ni
Mungu, wala hapana mwingine; mimi ni Mungu, wala hapana aliye kama mimi; nitangazaye
mwisho tangu mwanzo, na tangu zamani za kale mambo yasiyotendeka bado;
nikisema, Shauri langu litasimama, nami nitatenda mapenzi yangu yote.”
-
Hesabu
23:19 “Mungu si mtu, aseme uongo; Wala si
mwanadamu, ajute; Iwapo amesema, hatalitenda? Iwapo amenena, hatalifikiliza?”
Kwa hiyo ni Mungu ndiye
aliyekusudia uzaliwe hapo ulipozaliwa, ni Mungu aliyekusudia uzaliwe mwanamke
au mwanaume, ni Mungu aliyekusudia uzaliwe katika familia uliyozaliwa, ni Mungu
aliyekusudia ufanye kazi unayoifanya ni Mungu aliyekusudia ufanye huduma
unayoifanya, ni Mungu aliyekusudia uwe na mume uliye naye na mke uliye naye ni
Mungu aliyekusudia uwe na cheo ulicho nacho na mambo haya yote Mungu
aliyakusudia tangu kuwekwa kwa misingi ya dunia, maana yake ni nini Hakuna mtu
au pepo au malaika au jambo lolote lile linaloweza kuharibu mpango wa Mungu
katika maisha yako kwa sababu hakuna adui anayeshikilia hatima yako, wala muda
wako, wala kazi maalumu ambayo Mungu ameikusudia katika maisha yako kwa nini
kwa sababu NYAKATI ZAKO ZIKO KATIKA
MIKONO YA BWANA !
Waefeso 2:10 “Maana tu kazi yake, tuliumbwa
katika Kristo Yesu, tutende matendo mema, ambayo tokea awali Mungu aliyatengeneza
ili tuenende nayo.”
Mifano ya uweza wa Mungu katika nyakati za watu mbalimbali
Maandiko yamejaa mifano mingi
sana ambayo Muda hauwezi kuruhusu kuipitia yote, lakini mifano michache
nitakayoitumia hapa inatosha kabisa kuonyesha kuwa adui zako hawakuwezi, na
hawana mamlaka ya kuharibu chochote na kama wakiharibu ujue tu Mungu alikusudia
waharibu, kwa sababu maandiko yanaonyesha kuwa hatua zetu zote yaani njia za
maisha yetu zote zinaratibiwa na Mungu ona
Mithali 20:24 “Mwenendo wa mtu watoka kwa
Bwana; Basi, awezaje mtu kuelewa na njia yake? ”
Mungu anapokuwa amekusudia jambo
kwa Mtu na kwa wakati wake kisha akatokea mtu kuingilia kati kwa makusudi ya
kuharibu, awe anajua au awe hajui, awe amatumiwa na shetani au awe hajatumiwa,
awe ni ajenti wa ibilisi au vyovyote vile ni aidha mipango yao ifeli, au
kupitia hila zao Mungu akupeleke katika mpango wake mwingine anaoukusudia kwa
wakati huo kwanini kwa sababu Nykati zetu zimo katika mikono yake, hapa iko
mifano ya watu waliozaliwa kwa wakati maalumu kwa kusudi la kufanya kazi
maalumu katika majukumu maalimu kwa nyakati alizokuwa amekusudia Mungu kisha
watu wakajitokeza na mikakakati ya kuharibu au kuzuia na haya ndio waliyokutana
nayo:- ona
1.
Herode
dhidi ya Mwana wa Mungu Yesu Kristo
Moja ya watu
waliojaribu kuharibu maisha ya mtu mwingie ni pamoja na Herode Mfalme yeye
alikuwa amekusudia kuyaharibu kabisa maisha ya Mwana wa Mungu Yesu Kristo,
baada ya kusikia habari za kuzaliwa kwake na unabii aliosomewa na matamko ya
wanajibu yaani mamajusi kuhusu hatima ya Yesu Kristo kuwa ni Mfalme mkuu wa
wayahudi anayestahili kusujudiwa yeye alifadhaika na aliadhimia kuwa na mkakati
wa kuharibu maisha ya Mwana wa Mungu
Mathayo 2:1-3 “Yesu
alipozaliwa katika Bethlehemu ya Uyahudi zamani za mfalme Herode, tazama,
mamajusi wa mashariki walifika Yerusalemu, wakisema, Yuko wapi yeye aliyezaliwa
mfalme wa Wayahudi? Kwa maana tuliiona nyota yake mashariki, nasi tumekuja
kumsujudia. Basi mfalme Herode aliposikia hayo, alifadhaika, na Yerusalemu pia
pamoja naye.”
Wako watu
wanaotuzunguka wako kama Herode badala ya kufurahia mafanikio yako wao
wanafadhaika wanaumwa na mafanikio yako, wanaumwa wanapoona ya kuwa unaenda
kutoboa, wanaumwa wanaposikia kuwa
unaenda kuoa au kuolewa, au kupata kazi, au kupewa cheo au wanapogundua kuwa
wewe ni tishio la mafanikio kwao wanatumia kila hila na ujanja ili yamkini
ikiwezekana waharibu Mpango wa Mungu ndani yako lakini ashukuriwe Mungu kuwa
hekima yake haichunguziki yeye anajua kuifanya kuwa upuuzi hekima ya dunia hii
nay a shetani nay a wanadamu, wewe kama ni mwana wa Mungu kama ilibyokuwa kwa
Yesu Kristo Mungu ataandaa mpango wa kukuokoa na kuchepusha njia za adui kile
wanachokifikiri, sio kile ambacho Mungu atakifanya
Mathayo 2:8-14 “Akawapeleka
Bethlehemu, akasema, Shikeni njia, mkaulize sana mambo ya mtoto; na mkiisha
kumwona, nileteeni habari, ili mimi nami niende nimsujudie.Nao waliposikia
maneno ya mfalme, walishika njia; na tazama, ile nyota waliyoiona mashariki
ikawatangulia, hata ikaenda ikasimama juu ya mahali alipokuwapo mtoto. Nao
walipoiona ile nyota, walifurahi furaha kubwa mno. Wakaingia nyumbani,
wakamwona mtoto pamoja na Mariamu mamaye, wakaanguka wakamsujudia; nao
walipokwisha kufungua hazina zao, wakamtolea tunu; dhahabu na uvumba na
manemane. Nao wakiisha kuonywa na Mungu katika ndoto wasimrudie Herode,
wakaenda zao kwao kwa njia nyingine. Na hao walipokwisha kwenda zao, tazama,
malaika wa Bwana alimtokea Yusufu katika ndoto, akasema, Ondoka, umchukue mtoto
na mama yake, ukimbilie Misri, ukae huko hata nikuambie; kwa maana Herode
anataka kumtafuta mtoto amwangamize. Akaondoka akamchukua mtoto na mama yake
usiku, akaenda zake Misri;”
Mungu alifanya
njia kuhakikisha kusudia aliloliweka ndani ya Mwana wake linatimia na kuwa
hakuna mpumbavu anaweza kuliharibu, kiburi cha Herode kilifanywa kuwa ujinga
pale Mungu alipotokeza njia na kusema na mamajusi lakini vile vile alisema na
Yusufu, nataka nikuhakikishie kile ambacho Adui zako wanadhani kuwa
watafanikiwa hakitafanikiwa na Mungu ana njia na mpango mkakati wa kuhakikisha
kuwa anajitokeza kwako, kwa njia nyingine kuhakikisha ya kuwa kazi ile njema
aliyoianza anaikamilisha hakuna anayeweza kushindana na kusudi la Mungu na
kubadili mpango na nyakati alizozikusudia Bwana !
2.
Farao
dhidi ya wana wa Israel
Farao alikwishakuambiwa
mara kadhaa kusudi la Mungu kuhusu Israel, alielezwa wazi kuwa israel ni
mzaliwa wa kwanza wa Mungu wa Ibrahim Isaka na Yakobo, na kuwa kusudi la Mungu
wa waebrania ni kuwapeleka Israel katika inchi ya mkanaani aliyowaapia baba zao
Ibrahim na Isaka na Yakobo, lakini kwa makusudi kabisa farao alikuwa akipingana
na kusudi hili na akapigwa kwa mapigo kumi, hata baada ya pigo la mwisho yeye
bado alitaka kuwaendea Israel na kuwarejesha tena katika inchi ya utumwa
Kutoka 14:5-8 “Mfalme
wa Misri aliambiwa ya kuwa wale watu wamekwisha kimbia; na moyo wa Farao, na
mioyo ya watumishi wake, iligeuzwa iwe kinyume cha hao watu, nao wakasema, Ni
nini jambo hili tulilotenda, kwa kuwaacha Waisraeli waende zao wasitutumikie
tena? Akaandalia gari lake, akawachukua watu wake pamoja naye; tena akatwaa
magari mia sita yaliyochaguliwa, na magari yote ya Wamisri, na maakida juu ya
magari hayo yote.Na BWANA akaufanya moyo wake Farao mfalme wa Misri kuwa mgumu,
naye akawafuata wana wa Israeli; kwa sababu wana wa Israeli walitoka kwa ujeuri.”
Unaweza kuuona
moyo wa farao,? Bado walifikiri yeye na watumishi wake kuwa wanaweza kuamua
hatima ya watu wa Mungu, wanaweza kuwarejesha nyuma wanaweza kuzuia mpango wa
Mungu na neno lake na kiapo chake kuwa
anawapeleka katika inchi ya mkanaani na hivyo hata Mungu alipoigawa bahari ya
shamu kwa ujinga walitaka kupita mle mle kinyume na kusudi la Mungu na hiki
ndicho kilichowakuta
Kutoka 14:22-28 “Wana
wa Israeli wakaenda ndani kati ya bahari katika nchi kavu; nayo maji yalikuwa
ukuta kwao mkono wa kuume, na mkono wa kushoto. Na wale Wamisri wakawafuatia,
wakaingia ndani kati ya bahari, farasi zote za Farao, na magari yake, na
wapanda farasi wake. Ikawa katika zamu ya alfajiri, BWANA akalichungulia jeshi
la Wamisri katika ile nguzo ya moto na ya wingu, akalifadhaisha jeshi la
Wamisri. Akayaondoa magurudumu ya magari yao, hata yakaenda kwa uzito; na
Wamisri wakasema, Na tukimbie mbele ya Israeli; kwa kuwa BWANA anawapigania,
kinyume cha Wamisri. BWANA akamwambia Musa, Nyosha mkono wako juu ya bahari,
ili maji yarudi tena juu ya Wamisri, juu ya magari yao, na juu ya farasi zao.
Musa akaunyosha mkono wake juu ya bahari, na kulipopambazuka, bahari ikarudi
kwa nguvu zake; Wamisri wakakimbia mbele yake; na BWANA akawakukutia mbali hao Wamisri
kati ya bahari. Yale maji yakarudi yakafunikiza magari na wapanda farasi, hata
jeshi lote la Farao lililoingia katika bahari nyuma yao; hakusalia hata mtu
mmoja.”
Unaona hatima ya
farao na majesi yake yote yalizikwa katika bahari ya shamu kwa nini kwa sababu
alikuwa akishindana na kusudi lililokuwa ndani ya watu wa Mungu, nimefurahi
Musa anavyomalizia mstari huu HAKUSALIA
HATA MTU MMOJA Bwana akufanyie hivyo
na kuzidi mtu wa Mungu wote ambao wanakufuatilia ili kuhakikisha kuwa
unaharibikiwa Bwana asimwache hata mmoja asisalie hata wa kutoa taarifa ya
kilichotokea, awaye yote ambaye anazani kuwa ana mamlaka ya kushika Nyakati
zako ajue wazi kuwa nyakati zako ziko katika mikono ya Bwana !
3.
Mawaziri
dhidi ya Daniel
Wakati mwingine
watu wanaodhani wanaweza kuharibu Nyakati zako kwaajili ya sifa zako hupatwa na wivu tu, na kutafuta
kuwa maarufu, au kutafuta kukuchafua ili wao waonekane au wawe na cheo kama
ulichonacho hawajui kuwa wewe una upako wa huduma tofauti au niseme una kitu
cha ziada ndivyo aklivyokuwa Daniel alipendwa aliwazidi watu katika sifa na
cheo na uaminifu na watu wakawa wanatafuta namna ya kumpaka matope ili achafuke
ili tu wamuharibie
Daniel 6:1-5 “Ilimpendeza
Dario kuweka juu ya ufalme maliwali mia na ishirini, wawe juu ya ufalme wote;
na juu yao akaweka wakubwa watatu, na Danieli alikuwa mmoja wao; ili maliwali
hawa watoe hesabu kwao, mfalme asipate hasara. Basi Danieli huyo alipata sifa
kuliko wakubwa na maliwali, kwa kuwa roho bora ilikuwa ndani yake; naye mfalme
akaazimu kumweka juu ya ufalme wote. Basi mawaziri na maamiri wakatafuta sana
kupata sababu za kumshitaki Danieli kwa habari za mambo ya ufalme; lakini
hawakuweza kuona sababu wala kosa; kwa maana alikuwa mwaminifu, wala
halikuonekana kosa wala hatia ndani yake. Ndipo wale watu wakasema, Hatutapata
sababu ya kumshitaki Danieli huyo, tusipoipata katika mambo ya sheria ya Mungu
wake.”
Ukiona watu
wanatafuta kuchafua jina lako au kuwafanya wengine waamini kuwa haufai ujue
kuna kitu cha ziada umewazidi, katika maisha yangu nimekutana na watu wengi
sana wenye wivu wenye uchungu ambao sio tu wanatamani uharibikiwe lakini
wanatamani usambaratike, wanatamani hata ndoa yako ife, wanatamani kazi zako
ziharibike, ufukuzwe, uumwe, ufe upatwe na majanga na sio hivyo tu watakuandama
wakiwa na wivu wenye uchungu, watatumia hata uchawi na majungu wakifikiri ya
kuwa wamekuweza hivi ndivyo ilivyokuwa kwa Daniel lakini mwisho wa siku Daniel
aliyetupwa katika tundu la simba alipona na wao wakaliwa na simba na kutoweka
duniani kwa nini kwa sababu nyakati za mtu wa Mungu ziko mikononi mwa Mungu
Daniel 6:20-24 “Naye
alipolikaribia lile tundu, akamlilia Danieli kwa sauti ya huzuni; mfalme
akanena; akamwambia Danieli, Ee Danieli, mtumishi wa Mungu aliye hai, je! Mungu
wako, unayemtumikia daima, aweza kukuponya na simba hawa? Ndipo Danieli
akamwambia mfalme, Ee mfalme, uishi milele. Mungu wangu amemtuma malaika wake,
naye ameyafumba makanwa ya simba, nao hawakunidhuru; kwa kuwa mbele zake mimi
nalionekana kuwa sina hatia; tena, mbele yako, Ee mfalme, sikukosa neno. Basi
mfalme akafurahi sana, akaamuru wamtoe Danieli katika lile tundu. Ndipo Danieli
akatolewa katika lile tundu, wala dhara lo lote halikuonekana mwilini mwake,
kwa sababu alikuwa anamtumaini Mungu wake. Mfalme akaamuru, nao wakawaleta wale
watu waliomshitaki Danieli, wakawatupa katika tundu la simba, wao, na watoto
wao, na wake zao; na wale simba wakawashinda wakaivunja mifupa yao vipande
vipande, kabla hawajafika chini ya tundu.”
Wwatu wote
waliokuwa wakiwafuatia watu wenye kusudi la Mungu hatima ya maisha yao ilikuwa
mbaya sana, Ndugu usiogope wote waliokuonea Mungu atawalipia maovu yao yatakuwa
juu ya vichwa vyao, hawawezi kukuharibu, hawawezi kukufitini, hawawezi kukuzika
na badala yake utawazika wewe, muda usingeweza kutosha kusema habari za Hamani
na Esta na wayhaudi walokuwako shushani Ngomeni, wala muda wa balaamu dhidi ya
waisraeli, wala musa wa Yusufu na kaka zake, wala Sanbalati na tobia dhidi ya
Nehemia, na kadhalika wewe kama mwanafunzi wa biblia unajua yaliyowakuta Mungu
hataacha uonelewe atawakemea wote na kuwachafulia usemi wao wote wanaoinuka
kinyume nao na wote wanaojenga mnara wa babeli dhidi yako watachafuliwa usemi
Nyakati zangu katika Mikono ya Bwana
Zaburi 31:14-18 “Lakini mimi nakutumaini
Wewe, Bwana, Nimesema, Wewe ndiwe Mungu wangu. Nyakati zangu zimo mikononi
mwako; Uniponye na adui zangu, nao wanaonifuatia. Umwangaze mtumishi wako Kwa
nuru ya uso wako; Uniokoe kwa ajili ya fadhili zako. Ee Bwana, nisiaibishwe,
maana nimekuita; Waaibishwe wasio haki, wanyamaze kuzimuni. Midomo ya uongo iwe
na ububu, Imneneayo mwenye haki maneno ya kiburi, Kwa majivuno na dharau.”
Kwa misingi hiyo utaweza kuona
kuwa kadiri unavyokaribia au unapofikia kilele cha kusudi lile ambalo Mungu
amelikusudia au hatima ile ya Muhimu ndio utaweza kuona vita kali sana
inainuka, Mungu anapotaka kukuinua au anapokuwa amekuinua unakuta watu
hawapendezwi, hawafurahii wanazungumza vibaya, wanakuchafua wanakuchukia, njia
yako inatiwa tope inawekwa giza, upinzani unakuwa mkubwa dharau, masengenyo,
majungu, mateso, au vita kali sana jua sasa kuwa unakaribia Baraka kubwa ambazo
Mungu amezikusudia kwako, na nataka nikuhakikishie kuwa Mungu yule yule
anayetupa neema kupenya atakupa neema izidiyo na kukusaidia wakati wa mahitaji
yako watu hawashindani na mtu mwenye
nyota ndogo, watu wenye nyota ndogo siku zote hupiga vita watu wenye nyota
kubwa kumbuka nyota ya Yesu na Herode!
Waebrania 4:16 “Basi na tukikaribie kiti
cha neema kwa ujasiri, ili tupewe rehema, na kupata neema ya kutusaidia wakati
wa mahitaji.”
Wakati huo mtegemee Mungu ukiwa
na ufahamu kama aliokuwa nao Daudi mtumaini yeye, mfanye kuwa ndie Mungu wako
jua kuwa nyakati zako ziko mikononi mwake kwa hiyo atakuponya na adui zako, atakupa
kibali, atashughulika na wanaokufuatilia, atakuokoa kwa upendo wake, hatakuacha
uaibike, wataaibishwa wao na kunyamazishwa katika kuzimu, na wanaosema mabaya
watapigwa ububu!
Hatupaswi kuogopa lolote wala mtu
yeyote wala manenmo yoyote ya wapuuzi na wajinga walio kinyume na mapenzi ya
Mungu katika maisha yetu, hakuna mtu anayeshika hatima ya maisha yako isipokuwa
Mungu mwenyewe
Kila mtu anaweza kupanga lolote
analoweza kulipanga lakini shauri la bwana ndio litakalosimama Mithali 19:21 “Mna
hila nyingi moyoni mwa mtu; Lakini shauri la Bwana ndilo litakalosimama.”
Haijalishi wanadamu wanajenga
nini la msingi ni lile Mungu analolijenga
Zaburi 127:1 “Bwana asipoijenga nyumba Waijengao wafanya kazi bure.
Bwana asipoulinda mji Yeye aulindaye akesha bure.”
Fahamu ya kuwa unaweza kuwa na
vita kubwa na nyingi lakini ukimwambia Bwana yeye ndiye atakayepigana kwa niaba
yako, Mungu ndiye aliyekusudia hakuna anayeweza kutangua kusudi, kupigana nawe
adui zako ni kama wameamua kupigana na Mungu mwenyewe, kwa kila jaribu uko mlango wa kutokea, Mwana
wa Mungu alikuwa na maadui wengi walioinuka pasipo sababu lakini Yesu
hakupoteza muda kujibizana nao alikuwa busy na majukumu ambayo Mungu amempa,
ninaposema nyakati zangu katika mikono ya Mungu nina maana pana sana hakuna mtu anaweza kudhibiti, kuongeza au
kupunguza lolote lile katika makusudi ambayo kwayo Mungu ameyakusudia katika
maisha yangu na yako kwa hiyo usiogope, Hakuna aibu itatutawala, hakuna vita
hatutashinda, hakuna kikwazo hatutavuka, hakuna aibu haitazimishwa, hakuna
kivywa hakitazibwa, hakuna kifo, hakuna kurudi nyuma, sio kwa sababu mimi na
wewe ni wakamlilifu bali kwa sababu yeye ni mkamilifu, mpango wa Mungu ndani
yetu hauwezi kuzimishwa na wazushi, ni fimbo yake na gongo lake ndilo linalotuongoza,
tumeumbwa na Mungu na sio na watu, mimi na wewe tu wana wa Mungu wagomvi wetu wanagombana na
baba yetu haupaswi kuogopa kwa sababu NYAKATI
ZAKO ZIKO KATIKA MIKONO YA MUNGU.
Na. Rev Innocent Samuel Kamote
Mkuu wa wajenzi mwenye Hekima