Mathayo
16:13-17 “Basi
Yesu akaenda pande za Kaisaria-Filipi, akawauliza wanafunzi wake akasema, Watu
hunena Mwana wa Adamu kuwa ni nani? Wakasema, Wengine hunena u Yohana
Mbatizaji, wengine Eliya, wengine Yeremia au mmojawapo wa manabii. Akawaambia,
Nanyi mwaninena mimi kuwa ni nani? Simoni Petro akajibu akasema, Wewe ndiwe
Kristo, Mwana wa Mungu aliye hai. Yesu akajibu, akamwambia, Heri wewe Simoni
Bar-yona; kwa kuwa mwili na damu havikukufunulia hili, bali Baba yangu aliye
mbinguni.”
Utangulizi:
Moja ya njia pekee ya kutambua mtu au kitu kwa kina
na mapana na marefu ni pamoja na kuangalia majina ambayo mtu huyo anaitwa au
anajiita, katika somo la uungu, unapomzungumzia Mungu baba na mwana na Roho
Mtakatifu, moja ya nafsi ambayo inasumbua sana wanazuoni wengi wa Kikristo na
zaidi wasio wakristo ni kujua asili ya Kristo, na ni kutokana na kuwepo kwa
utata mwingi sana kuhusu asili ya Yesu, kumekuwepo na somo katika vyuo vya
Biblia linalojaribu kuchambua kwa undani ili kumjua Yesu ni nani, somo hilo
kitaalamu huitwa CHRISTOLOGY ambalo
ni muunganiko wa misamiati miwili ya kiyunani CHRIST na LOGOS ikiwa
na maana ya MAARIFA KUHUSU KRISTO – Knowledge about Christ, Somo hilo
kimsingi linahusika na kuchambua kwa undani sana kuhusu Yesu Kristo na asili
yake, kumjua Yesu na Mungu baba yetu wa Mbinguni yalikuwa ni moja ya sehemu ya
muhimu ya maombi ya Yesu Kristo kwetu!.
Yohana
17:1-3 “Maneno
hayo aliyasema Yesu; akainua macho yake kuelekea mbinguni, akasema, Baba, saa
imekwisha kufika. Mtukuze Mwanao, ili Mwana wako naye akutukuze wewe; kama vile ulivyompa mamlaka juu ya
wote wenye mwili, ili kwamba wote uliompa awape uzima wa milele. Na uzima wa
milele ndio huu, Wakujue wewe, Mungu wa pekee wa kweli, na Yesu Kristo
uliyemtuma.”
Kumjua Yesu Kristo kwa kawaida sio swala Jepesi kama
tunavyofikiri, huwezi kumjua Yesu bila msaada wa Mungu, maandiko au Yesu
Mwenyewe na katika maandiko pia wakati mwingine ni mpaka yeye mwenyewe ahusike
kukufunulia andiko husika kwa neema yake. Leo tutachukua muda kujifunza somo
hili muhimu KWANINI YESU ALIJIITA MWANA WA ADAMU tutajifunza somo hili
kwa kuzingatia vipengele vitatu vifuatavyo:-
·
Jinsi kuijua
asili ya Yesu Kristo kulivyowasumbua wasomi
·
Jinsi
ya kumjua Yesu Kristo
·
Kwanini
Yesu alijiita mwana wa Adamu
Jinsi
kuijua asili ya Yesu kulivyowasumbua wasomi
Moja ya swala ambalo lilisumbua sana mnamo karne ya
kwanza mpaka karne ya tatu kwa wanazuoni wakubwa sana katika kanisa la Mungu,
ilikuwa ni pamoja na kuijua nafsi ya Mungu mwana, utata kuhusu Yesu ni nani sio
tu ulisumbua vichwa vya wasomi, lakini hata wakati wa Yesu mwenyewe kila mmoja
alikuwa akisema lake kuhusu Yesu ni nani ona :-
Mathayo
16:13-17 “Basi
Yesu akaenda pande za Kaisaria-Filipi, akawauliza wanafunzi wake akasema, Watu
hunena Mwana wa Adamu kuwa ni nani? Wakasema, Wengine hunena u Yohana Mbatizaji,
wengine Eliya, wengine Yeremia au mmojawapo wa manabii. Akawaambia, Nanyi
mwaninena mimi kuwa ni nani? Simoni Petro akajibu akasema, Wewe ndiwe Kristo,
Mwana wa Mungu aliye hai. Yesu akajibu, akamwambia, Heri wewe Simoni Bar-yona;
kwa kuwa mwili na damu havikukufunulia hili, bali Baba yangu aliye mbinguni.”
Katika karne ya tatu swali kuhusu Masihi ni nani
bado liliendelea kuwasumbua wasomi na kila mtu alikuwa na maoni yeke kuhusu
asili ya Yesu kuwa ikoje na ni nani? Kama tunavyoweza kujionea maoni mbalimbali
ya wanazuoni wakiumiza kichwa kumjua Yesu.
1. Waebionite – (Ebionites) – Hili ni kundi la wakristo
wa kiyahudi ambao walikuweko karne za mwanzoni wakiishi maisha ya kimasikini
wakiwa na Imani kuwa umasikini una uhusiano na maisha matakatifu, waoa walikuwa
wakiamini kuwa YESU NI MASIHI LAKINI SIO MUNGU na kuwa kuzaliwa kwake na
Mariamu kunasisitiza umuhimu wa kuishika na kuitii Torati ya Musa, Hivyo Yesu
ni Mwanadamu aliyetii torati yote ya Musa na kutunukiwa kuwa masihi.
2. Waanostisizim – (Gnosticism) – Hili ni kundi la watu
walioamini kuwa Maarifa yanaleta wokovu na dhambi ni ujinga, kundi hili
liliamini kuwa YESU ALIKUWA NI ROHO NA HAJAWAHI KUUTWAA MWILI Fundisho
la aina hii lilipingwa vikali na Mtume Yohana na alilionya kanisa kuwa makini
na aina ya fundisho kama hilo ona
1Yohana
4:1-3 “Wapenzi,
msiiamini kila roho, bali zijaribuni hizo roho, kwamba zimetokana na Mungu; kwa
sababu manabii wa uongo wengi wametokea duniani. Katika hili mwamjua Roho wa
Mungu; kila roho ikiriyo kwamba Yesu Kristo amekuja katika mwili yatokana na
Mungu. Na kila roho isiyomkiri Yesu haitokani na Mungu. Na hii ndiyo roho ya
mpinga Kristo ambayo mmesikia kwamba yaja; na sasa imekwisha kuwako duniani.”
3. Waariyan – (Arianism) – Ni kundi la Wakristo
waliofuata fundisho la Mwanatheolojia aliyeitwa Arius ambaye alikuwa
mwangalizi na msomi wa chuo kikuu cha Kikristo huko Alexandria nchini
Misri kati ya mwaka 256-336 Baada ya Kristo, wao waliamini kuwa Yesu sio
Mungu ni kiumbe cha kwanza kuumbwa na Mungu na hivyo hayuko sawa na Mungu
lakini yuko chini kidogo ya Mungu na juu ya malaika, walimuita Yesu Mwanzo wa
kuumba kwa Mungu sawa na
Ufunuo 3:14c “Na kwa malaika wa kanisa lililoko Laodikia andika;
Haya ndiyo anenayo yeye aliye Amina, Shahidi aliye mwaminifu na wa kweli,
MWANZO WA KUUMBA KWA MUNGU.”
Pia wanatumia andiko hili
kutoka injili ya Yohana Yesu akisema baba ni Mkubwa kuliko Yeye
Yohana 14:28 “Mlisikia ya kwamba mimi naliwaambia, Naenda zangu,
tena naja kwenu. Kama mngalinipenda, mngalifurahi kwa sababu naenda kwa Baba,
KWA MAANA BABA NI MKUU KULIKO MIMI.”
4. Wanestorian – (Nestorianism) – Hili ni kundi lingine la
wasomi wa Kikristo, waliokuwa na mtazamo tofauti kuhusu asili ya Yesu, wao
waliona kuwa uungu na ubinadamu hauwezi kuwa na muunganiko kwa hiyo Yesu hawezi
kuwa Mungu mwanadamu, au kuwa Mungu wakati huo huo na wakati huo huo mwanadamu.
5. Waapolonari – (Apollinarian) – Aplonari alikuwa ni
askofu kijana wa kanisa la Laodekia lililokuwako huko Syria mwaka wa 361 baada
ya Kristo, yeye aliamini pamoja na watu wake kuwa Yesu alikuwa mwanadamu lakini
akili yake ilikuwa akili ya kiungu, kwa hiyo asili hizi mbili hazikuweza
kujitokeza kwa pamoja ni kama anataka kusema kuwa kuna wakati Yesu alikuwa
mwanadamu na alisema na kundenda kibinadamu na kuna wakati alikuwa Mungu na
alitenda na kusema kama Mungu.
6. Waeutiko – ( Eutychians) - Hili ni kundi la Wakristo waliofuata mafundisho ya Eutychus
ambaye aliishi huko Constantinople, kati ya mwaka 380 - 456 baada ya Kristo, wao walikuwa na fundisho kuwa Yesu alikuwa na
asili mpya yaani Mungu + Mwanadamu = Asili mpya, kwa hiyo Yesu sio Mungu
wala sio Mwanadamu
7. Waorthodox – (Orthodox) – Hili ni Kundi la wakristo
wanaoamini kuwa wanafundisho sahihi neno Orthodox maana yake ni Right
opinion wao waliamini kuwa Yesu ni
Mungu mwanadamu na kwa sababu hiyo Yeye ni Mwanadamu kwa asilimia 100% na ni
Mungu kwa asilimia 100% fundisho hili ndilo lililosalia kuwa fundisho
sahihi mpaka sasa kwa mujibu wa kanisa la Mungu wao wanasimamia andiko la Yohana 1:1-3,
13-14
Yohana 1:1-3 “Hapo mwanzo kulikuwako Neno, naye Neno alikuwako
kwa Mungu, naye Neno alikuwa Mungu. Huyo mwanzo alikuwako kwa Mungu. Vyote
vilifanyika kwa huyo; wala pasipo yeye hakikufanyika cho chote kilichofanyika.”
Yohana 1:14 “Naye Neno alifanyika mwili, akakaa kwetu; nasi
tukauona utukufu wake, utukufu kama wa Mwana pekee atokaye kwa Baba; amejaa
neema na kweli.”
Unaweza kuona makundi
hayo yalikuwa na mijadala mikali sana kuhusu Asili ya Kristo, na hii
inatufundisha wazi kuwa kumjua Yesu Kristo sio kazi nyepesi kama watu wengi
wanavyodhani inahitajika neema maalumu ya kiungu kuweza kumjua Yesu, na ndio
maana watu wengi sana huwa wanachanganyikiwa kuhusu, nafsi na asili ya Yesu
mpaka leo, Ni muhimu sana tunapoendelea kujifunza somo hili kuwa na maombi ya
kutaka kumjua Yesu zaidi, kama mwandishi wa Tenzi za injili namba 92 alivyoimba
kuwa anataka kumjua Yesu na azidu kumfahamu, tunahitaji neema ya Mungu kumjua
bwana wetu Yesu.
Jinsi ya
kumjua Yesu Kristo
Kumjua Yesu Kristo kamwe hakuwezi kuja kwa akili za
kawaida za kibinadamu, wala kwa kujenga hoja za kisomi, maandiko na Yesu Kristo
Mwenyewe anaonyesha wazi kuwa kumjua Yesu Kristo kunaweza kuletwa kwetu kwa
msaada wa Mungu na ufunuo wa Mungu Baba mwenyewe kwetu kupitia Roho wake
Mtakatifu, maandiko au Yesu Kristo mwenyewe moja kwa moja tunaweza kupata
ushahidi wa jambo hili kwa kuangalia tena andiko letu la Msingi
Mathayo
16:16-17 “Simoni
Petro akajibu akasema, Wewe ndiwe Kristo, Mwana wa Mungu aliye hai. Yesu
akajibu, akamwambia, Heri wewe Simoni Bar-yona; kwa kuwa mwili na damu
havikukufunulia hili, bali Baba yangu aliye mbinguni.”
Unaona? Yesu alipouliza swali watu wanasema kuwa
mwana wa Adamu ni nani, kulikuwa na majibu mbali mbali kuhusu Masihi, lakini
hatimaye Simioni Petro akajibu, wewe ndiwe Kristo Mwana wa Mungu aliye hai, na
mara baada ya jibu hili ambalo lilikukuwa jibu sahihi Yesu alijibu kwa
kumwambia HERI
WEWE SIMONI BAR-YONA; KWA KUWA MWILI NA DAMU HAVIKUKUFUNULIA HILI, BALI BABA
YANGU ALIYE MBINGUNI Maneno haya yana maana
gani? Rahisi tu huwezi kumjua Yesu bila kufunuliwa na Mungu mwenyewe, na kule
kusema mwili na damu havikukufunulia hili, Yesu alikuwa akimaanisha Akili ya
kawaida ya kibinadamu na uweza katika uhai wa mwanadamu hauwezi kutambua siri
hii ya kuwa Yesu Kristo ni nani, na ndio maana umeweza kuona wasomi wengi
walisumbuka kutambua asili ya Kristo na hata leo, watu wa dini nyingine hususani
wakiwemo waislamu wanahangaika sana na kutatizwa mno na ukweli kuhusu asili ya
Yesu Kristo, na huwa wanadhani tuna haja
ya kumkuza sana au kukufuru kwa kumpa Heshima ambayo wanadhani haistahili, jambo
kubwa la Msingi ni kuwa tunamjua Mungu kupitia ufunuo kutoka kwa Mungu
mwenyewe! Na neema yake wakati tunapotafakari na kumruhusu yeye atufunulie
maandiko!
Au wakati mwingine Yesu mwenyewe huwa anahusika
kutufunulia yeye mwenyewe ili tuweze kumjua au kutufunulia maandiko ili tuweze
kuelewa, jambo hili linadhihirika wazi kuwa hata wanafunzi wa Yesu, waliomuona
mubashara alipokuwa hai, alipofufuka ilikuwa ngumu kwao kumjua na hata kujua
kile ambacho kimeandikwa kumuhusu, lakini kwa msaada wake yeye mwenyewe waliweza
kubaini ukweli uliokuweko na kwa hiyo kwa kupitia ufunuo wake katika maandiko
unaweza kumjua kumhusu! Angalia maandiko hapa:-
Luka
24:13-32 “Na tazama, siku ile ile watu wawili miongoni mwao walikuwa wakienda
kijiji kimoja, jina lake Emau, kilichokuwa mbali na Yerusalemu kama mwendo wa
saa mbili. Nao walikuwa wakizungumza wao kwa wao habari za mambo hayo yote
yaliyotukia. Ikawa katika kuzungumza na kuulizana kwao, Yesu mwenyewe
alikaribia, akaandamana nao. Macho yao yakafumbwa wasimtambue. Akawaambia, Ni
maneno gani haya mnayosemezana hivi mnapotembea? Wakasimama wamekunja nyuso
zao. Akajibu mmoja wao, jina lake Kleopa, akamwambia, Je! Wewe peke yako u
mgeni katika Yerusalemu, hata huyajui yaliyotukia humo siku hizi? Akawauliza,
Mambo gani? Wakamwambia, Mambo ya Yesu wa Nazareti, aliyekuwa mtu nabii, mwenye
uwezo katika kutenda na kunena mbele za Mungu na watu wote; tena jinsi wakuu wa
makuhani na wakubwa wetu walivyomtia katika hukumu ya kufa, wakamsulibisha.
Nasi tulikuwa tukitumaini ya kuwa yeye ndiye atakayewakomboa Israeli. Zaidi ya
hayo yote, leo ni siku ya tatu tangu yalipotendeka mambo hayo; tena, wanawake
kadha wa kadha wa kwetu walitushitusha, waliokwenda kaburini asubuhi na mapema,
wasiuone mwili wake; wakaja wakasema ya kwamba wametokewa na malaika waliosema
kwamba yu hai. Na wengine waliokuwa pamoja nasi walikwenda kaburini wakaona
vivyo hivyo kama wale wanawake walivyosema, ila yeye hawakumwona. Akawaambia,
Enyi msiofahamu, wenye mioyo mizito ya kuamini yote waliyoyasema manabii! Je!
Haikumpasa Kristo kupata mateso haya na kuingia katika utukufu wake? Akaanza
kutoka Musa na manabii wote, akawaeleza katika maandiko yote mambo yaliyomhusu
yeye mwenyewe. Wakakikaribia kile kijiji walichokuwa wakienda, naye alifanya
kama anataka kuendelea mbele. Wakamshawishi wakisema, Kaa pamoja nasi, kwa kuwa
kumekuchwa, na mchana unakwisha. Akaingia ndani kukaa nao. Ikawa alipokuwa
ameketi nao chakulani, alitwaa mkate, akaubariki, akaumega, akawapa.
Yakafumbuliwa macho yao, wakamtambua; kisha akatoweka mbele yao. Wakaambiana,
Je! Mioyo yetu haikuwaka ndani yetu hapo alipokuwa akisema nasi njiani, na
kutufunulia maandiko? ”
Kwa hiyo hata maandiko kumbe tunaweza tu tukayasoma
lakini kama Mungu Baba, au Mwana au Roho Mtakatifu hatakufunulia jambo au
utafichwa jambo huwezi kulibaini au kulijua, wanafunzi wa Yesu ni mpaka
yalipofumbuliwa macho yao ndio wakaweza kuelewa na macho yao yakafunguliwa
wakamtambua, lakini pia alipokuwa akiwafunulia maandiko tena akiwakemea ENYI
MSHIOFAHAMU WENYE MIOYO MIZITO YA KUAMINI YOTE WALIYOYASEMA MANABII,
ukifungwa ufahamu, ukawa na moyo mzito huwezi kuelewa na kuamini hata kilichoandikwa
na manabii, Yesu akikufunulia maandiko utamuelewa kwa undani, na anaweza
kufanya hivyo kwa wale waliokuwa pamoja naye n ahata kwa wale wasiokuwa pamoja
naye yaani hata sisi leo Yesu yu aweza kutuelekeza kitu kupitia Roho wake
Mtakatifu na tukaweza kuelewa yale yaliyofichika ona hii:-
Wagalatia
1:11-12 “Kwa
maana, ndugu zangu, injili hiyo niliyowahubiri, nawajulisha ya kuwa siyo ya
namna ya kibinadamu. Kwa kuwa sikuipokea kwa mwanadamu wala sikufundishwa na
mwanadamu, bali kwa ufunuo wa Yesu Kristo.”
Paulo Mtume pia katika kifungu hiki anatuhakikishia
kuwa aliihubiri injili ambayo haikuwa ya namna ya kibinadamu kwa sababu
aliipokea na kufundishwa na Yesu Kristo mwenyewe kwa ufunuo, kwa hiyo unaweza
kukubaliana nami wazi kuwa bila kufunuliwa jambo kuhusu Kristo ni vigumu kwa
akili za kawaida kuweza kutambua kitu au jambo kuhusu Yesu Kristo, Hasa kama
Bwana amekusudia kulificha au kama hatuna muda wa kusoma na kutafakari na
kutaka kumjua. Bwana ampe neema kila mmoja wetu kuwa na ufunuo kumhusu Kristo
ili tuweze kuwa na uelewa mpana kwa kina na mapana na marefu kumuhusu Yesu!,
katika somo hili sio nia yangu kumuelezea Yesu Kristo labda nitafanya hivyo
wakati mwingine leongo langu kuu ni kujibu swali la Msingi kwanini Yesu
alijiita mwana wa Adamu hili tutalitafakari kwa kina katika kipengele
kinachofuata:-
Kwanini
Yesu alijiita mwana wa Adamu
Kama umeweza kunifuatilia tangu mwanzo, leo
sitaki kujibu swali Yesu ni nani, lakini nataka kujibu na kuweka wazi kwanini
Yesu alijiita Mwana wa Adamu, moja ya
njia ya kumjua Yesu ni pamoja na kuyajua maandiko, kwamba yanasema nini
Kumuhusu yeye, kwa hiyo katika somo la ufahamu kuhusu Yesu Kristo yaani
Christology waalimu wanafanya kazi kubwa sana ya kuchambua majina yoote ya
Yesu Kristo yaliyotumika katika maandiko kumuelezea, na moja ya majina hayo ni
MWANA WA ADAMU tena inaonekana wazi kuwa jina hili Yesu Kristo mwenyewe
ndiye aliyelitumia zaidi kuliko wanafunzi wake wala watu wengine, kwa hiyo kuna
swali kubwa sana la msingi la kujiuliza kwanini Yesu alikuwa akijiita mwana wa
Adamu? Na kabla ya kuangalia swala hilo tuone sehemu kadhaa katika maandiko
Yesu akijiita mwana wa Adamu na tukio hili la kujiita mwana wa Adamu
limeonekama mara zaidi ya 82 katika maandiko hususani agano jipya
Mathayo
12:31-32 “Kwa
sababu hiyo nawaambia, Kila dhambi na kila neno la kufuru watasamehewa wanadamu,
ila kwa kumkufuru Roho hawatasamehewa. Naye mtu ye yote atakayenena neno juu ya
MWANA WA ADAMU atasamehewa, bali yeye atakayenena neno juu ya Roho Mtakatifu
hatasamehewa katika ulimwengu wa sasa, wala katika ule ujao.”
Mathayo
13:37 “Akajibu,
akasema, Azipandaye zile mbegu njema ni MWANA WA ADAMU;”
Marko
14:62 “Yesu
akasema, Mimi ndiye, nanyi mtamwona MWANA WA ADAMU ameketi mkono wa kuume wa
nguvu, akija na mawingu ya mbinguni.”
Luka
12:8-10 “Nami
nawaambia, kila atakayenikiri mbele ya watu, MWANA WA ADAMU naye atamkiri yeye
mbele ya malaika wa Mungu; na
mwenye kunikana mbele ya watu, huyo atakanwa mbele ya malaika wa Mungu. Na kila
mtu atakayenena neno juu ya MWANA WA ADAMU atasamehewa, bali aliyemkufuru Roho
Mtakatifu hatasamehewa.”
Yohana
1:51 “Akamwambia,
Amin, amin, nawaambia, Mtaziona mbingu zimefunguka na malaika wa Mungu wakikwea
na kushuka juu ya MWANA WA ADAMU.”
Yohana
3:13-15 “Wala
hakuna mtu aliyepaa mbinguni, ila yeye aliyeshuka kutoka mbinguni, yaani, MWANA
WA ADAMU. Na kama vile Musa alivyomwinua yule nyoka jangwani, vivyo hivyo MWANA
WA ADAMU hana budi kuinuliwa; ili kila mtu aaminiye awe na uzima wa milele
katika yeye.”
Mathayo
8:20 “Yesu
akamwambia, Mbweha wana pango, na ndege wa angani wana viota; lakini MWANA WA
ADAMU hana pa kulaza kichwa chake.”
Marko
10:45 “Kwa
maana MWANA WA ADAMU naye hakuja kutumikiwa, bali kutumika, na kutoa nafsi yake
iwe fidia ya wengi.”
Luka
5:24 “Lakini,
mpate kujua ya kwamba MWANA WA ADAMU anayo amri duniani ya kusamehe dhambi,
(alimwambia yule mwenye kupooza). Nakuambia, Ondoka, ujitwike kitanda chako,
ukaende zako nyumbani kwako.”
Mathayo
26:64 “Yesu
akamwambia, Wewe umesema; lakini nawaambieni, Tangu sasa mtamwona MWANA WA
ADAMU ameketi mkono wa kuume wa nguvu, akija juu ya mawingu ya mbinguni.”
Hayo ni baadhi ya maandiko machache tu ambayo
yanamtaja Yesu kama Mwana wa Adamu, na
baadhi ya mikazo hii aliitaja yeye mwenyewe, swali kubwa linabaki kwanini Yesu
anajiita Mwana wa Adamu? Na ni
watu wachache sana ambao walimuita Yesu mwana wa Adamu baada ya kumuona akiwa
amesimama mkono wa kuume wa Mungu ona
Matendo
7:55-56 “Lakini
yeye akijaa Roho Mtakatifu, akakaza macho yake, akitazama mbinguni, akauona
utukufu wa Mungu, na Yesu akisimama upande wa mkono wa kuume wa Mungu. Akasema,
Tazama! Naona mbingu zimefunguka, na MWANA WA ADAMU amesimama mkono wa kuume wa
Mungu.”
Kwa mujibu wa utafiti wa kimaandiko na michango ya
wanazuoni wengi kuhusu tafasiri ya kwanini Yesu alijiita Mwana wa Adamu kwa
mkazo na msisitizo mkubwa? Ziko sababu kadhaa ambazo wanatheolojia wanajaribu
kuelezea Kama nitakavoainisha hapa
1. Kusisitiza uhusiano wake na wanadamu
Moja ya tafasiri
inayoelezwa na wanazuoni ni kwanini Yesu alijiita mwana wa Adamu inasemekana ni
kusisitiza uhusiano wake na wanadamu, hii ni kwa sababu neno Mwana wa Katika
Kiibrania linasomeka BEN ambalo lina maana kubwa mbili, Mtoto wa, na
uhusiano na, Kwamfano watu waliookoka wao huitwa wana wa Ufalme ona
Mathayo 8:11-12 “Nami nawaambieni, ya kwamba wengi watakuja kutoka
mashariki na magharibi, nao wataketi pamoja na Ibrahimu, na Isaka, na Yakobo
katika ufalme wa mbinguni; bali wana wa ufalme watatupwa katika giza la nje,
ndiko kutakuwako kilio na kusaga meno.”
Wakati wale
watakaofufuliwa na Bwana wetu Yesu Kristo wanaitwa wana wa Ufufuo
Luka 20: 35-36 “lakini, wale wahesabiwao kuwa wamestahili kuupata
ulimwengu ule, na kule kufufuka katika wafu, hawaoi wala hawaolewi; wala
hawawezi kufa tena; kwa sababu huwa sawasawa na malaika, nao ni wana wa Mungu,
kwa vile walivyo wana wa ufufuo.”
Hali kadhalika wale
wanaopenda Amani, Yesu aliwaita wana wa Amani unaweza kuona katika
Luka 10:5-65. “Na nyumba yo yote mtakayoingia, semeni kwanza,
Amani iwemo nyumbani humu; na akiwamo mwana wa amani, amani yenu itamkalia; la,
hayumo, amani yenu itarudi kwenu.”
Na mtu ambaye ameandikiwa
hukumu ya Mungu, huitwa mwana wa uharibifu mfano ni Yuda ona
Yohana 17:12 “Nilipokuwapo pamoja nao, mimi naliwalinda kwa jina
lako ulilonipa, nikawatunza; wala hapana mmojawapo wao aliyepotea, ila yule
mwana wa upotevu, ili andiko litimie.”
Kwa hiyo Yesu anapotumia
neno Mwana wa Adamu anammaanisha kimsingi uhusiano wake na wanadamu, au
uhusuano wake na Adamu aliye baba ya wanadamu wote, kwa msingi huo katika mkazo
huu Yesu ambaye ni Mungu anataka kuonyesha ushirika wake na wanadamu, anataka
kutuonyesha kuwa aliacha enzi na utukufu na kukubali kuwa mwanadamu ambaye
kimsingi ni dhaifu na hivyo ni jambo la unyenyekevu sana
Wafilipi 2: 6-8 “ambaye yeye mwanzo alikuwa yuna namna ya Mungu,
naye hakuona kule kuwa sawa na Mungu kuwa ni kitu cha kushikamana nacho; bali
alijifanya kuwa hana utukufu, akatwaa namna ya mtumwa, akawa ana mfano wa
wanadamu; tena, alipoonekana ana umbo kama mwanadamu, alijinyenyekeza akawa
mtii hata mauti, naam, mauti ya msalaba.”
Kwa msingi huo jina hili
Mwana wa Adamu linaunganisha au kuonyesha ubinadamu wote wa Bwana Yesu, akiwa
anakula, anachoka, analala, anasalitiwa, anateswa, anadhihakiwa, anateswa na
anauawa na hatimaye Mungu anamfufua kutoka kwa wafu, kwa hiyo moja yaw azo la
kitheolojia ni kuwa Yesu ambaye ni Mungu alikuwa anafurahia kuushiriki
ubinadamu na akawa anaweza mkazo Mwana wa Adamu.
2. Kwaajili ya Kutimiza unabii
Jambo lingine
linalozungumzwa na wanazuoni kwamba ni kwanini Yesu alijiita Mwana wa Adamu
ilikuwa ni kujitambulisha kuwa yeye ndiye Masihi sawa na nabii mbalimbali
katika maandiko ukiwemo unabii wa Daniel tunaweza kuliona hilo wazi katika
Daniel 7:13-14 “Nikaona katika njozi za usiku, na tazama, mmoja
aliye mfano wa mwanadamu akaja pamoja na mawingu ya mbingu akamkaribia huyo
mzee wa siku, wakamleta karibu naye. Naye akapewa mamlaka, na utukufu, na
ufalme, ili watu wa kabila zote, na taifa zote, na lugha zote, wamtumikie;
mamlaka yake ni mamlaka ya milele, ambayo hayatapita kamwe, na ufalme wake ni
ufalme usioweza kuangamizwa.”
Ni uwazi kuwa unabii huu
wa Daniel pamoja na maeneo mengine umesema wazi kuwa masihi atakuwa ni wa namna
gani, ni aliye mfano wa Mwanadamu na akapewa Mamlaka na utukufu na ufalme,
hivyo ni vya milele, kwa hiyo wanatheolojia wengi wanahisia ya kuwa Yesu
alupokuwa akijiita mwana wa Adamu alikuwa pia akijidhihirisha kuwa yeye ni
Masihi sawa na namna na jinsi alivyotabiri nabii Daniel.
Kwa ujumla kupitia Yesu
kuwa mwanadamu, ameweza kufanya kazi kubwa ya kuandaa njia ya ukombozi wa
mwanadamu, ukiacha kuja kuwa na Enzi na mamlaka ya utawala wa kiungu duniani
lakini Masihi ameweza kufanya mengi kwaajili ya wanadamu, ameweza kuufunua
uungu na wema na tabia ya Mungu kupitia uanadamu wake kwa hiyo kuna faida kubwa
sana ya Yesu kuwa mwanadamu mfano
Kusamehe dhambi wanadamu kwa sababu ameonja
unanadamu anajua udhaifu wa mwanadamu – Marko 2:10 “Lakini mpate kujua ya kwamba Mwana wa Adamu anayo
amri duniani ya kusamehe dhambi, (hapo amwambia yule mwenye kupooza),”
Kumtafuta mwanadamu na kumuokoa – Luka 19:9-10 “Yesu akamwambia, Leo wokovu umefika nyumbani humu,
kwa sababu huyu naye ni mwana wa Ibrahimu. Kwa kuwa Mwana wa Adamu alikuja
kutafuta na kuokoa kile kilichopotea.”
Kushiriki mateso kwa niaba ya wanadamu ili kuleta
ukombozi – Marko 8:31 “Akaanza kuwafundisha kwamba imempasa Mwana wa Adamu
kupatikana na mateso mengi, na kukataliwa na wazee, na wakuu wa makuhani, na
waandishi, na kuuawa, na baada ya siku tatu kufufuka.”
Kumfunua Mungu kwetu – Yesu alipokuwa na mwili
wa kibinadamu alisema wazai kuwa kazi ananozifanya na maneno yote aliyokuwa
anawafundisha yalikuwa yanafunua matendo ya Mungu kwa wanadamu
Yohana 5:19-20 “Mwana hawezi kutenda neno mwenyewe ila lile ambalo
amwona Baba analitenda; kwa maana yote ayatendayo yeye, ndiyo ayatendayo Mwana
vile vile.Kwa kuwa Baba ampenda Mwana, naye humwonyesha yote ayatendayo
mwenyewe; hata na kazi kubwa zaidi kuliko hizo atamwonyesha, ili ninyi mpate
kustaajabu.”
Kuonyesha shauku ya Mungu kushirikiana na wanadamu –
Mathayo 1L22-23 “Hayo
yote yamekuwa, ili litimie neno lililonenwa na Bwana kwa ujumbe wa nabii
akisema, Tazama, bikira atachukua mimba, Naye atazaa mwana; Nao watamwita jina
lake Imanueli; Yaani, Mungu pamoja nasi.”
3. Kwaajili ya Kufunua asili yake ya uungu
Tunaelewa wazi kuwa Yesu
ni Mungu, kule kuitwa mwana wa Mungu maana yake anashiriki uungu, kwa hiyo Yesu
alikuwa akijionea fahari kuushiriki uanadamu, huku yeye akiwa na asili ya
uungu, Mungu anamjua mwanadamu kama kiumbe dhaifu na mara kadhaa alilitumia neno
mwanadamu akimuita Ezekiel, inasemekana Mungu anamtaja Ezekiel kama mwanadamu
mara 93 kwa msingi huo Mungu alikuwa akimaanisha Ezekiel ni mwanadamu
lakini sivyo Ilivyo Kwa Kristo. Yesu hakuwa dhaifu Kama Ezekiel Yeye alikuja
kumfunua Mungu kwetu, alikuwa Mungu aliyeishi katika ubinadamu
Wakolosai 2:9 “Maana katika yeye unakaa utimilifu wote wa Mungu,
kwa jinsi ya kimwili.”
Kwaajili ya haya aliweza
kusamehe dhambi, aliweza kuonyesha ubwana dhidi ya sabato, aliweza kuonyesha
kuwa amekuja kumuokoa mwanadamu, aliweza kuonyesha kuwa ana uwezo wa kufufua
wafu, aliweza kuonyesha kuwa anamamlaka ya kuhukumu, na kuonyesha kuwa atarudi
tena siku moja duniani, aliweza kuonyesha kuwa ana mamlaka ya kubadili sharia ya
Musa kwa kuitimiza na ana mamlaka ya kumuweka huru Mwanadamu na kumkomboa kama
mwana wa Mfalme wa Mbinguni
Mathayo 26:64 “Yesu akamwambia, Wewe umesema; lakini nawaambieni,
Tangu sasa mtamwona Mwana wa Adamu ameketi mkono wa kuume wa nguvu, akija juu
ya mawingu ya mbinguni.”
Kwa sababu hizi na nyinginezo
nyingi wanatheolojia wanazitumia kumuelezea Yesu na kujaribu kujibu kuwa ndio
sababu kubwa na za Msingi za Yesu kujiita mwana wa Adamu. Kwa hiyo katika
tafiti nyingi na vitabu vingi na wajenga hija wengi wanaishia kwenye jambo hilo
na sababu hizo kwanini Yesu alijiita mwana wa Adamu!
Hitimisho:
Kwa mtazamo wangu mimi ambao ndio umenisukuma
kuandaa somo hili, Yesu alipokuwa akijiita Mwana wa Adamu, kuna tofauti kabisa
na Mungu alivyokuwa akimuita Ezekiel nabii Mwanadamu, Yesu alikuwa akijiita Mwana
wa Adamu, katika mtazamo uleule wa namna anavyojiita au alivyoitwa Mwana wa
Abraham, au Mwana wa Daudi, unapoangalia maandiko katika Kitabu za Ezekiel
Mungu anapomuita Ezekiel Mwanadamu kuna tofauti na neno Mwana wa Adamu
linavyotumika katika Agano jipya tunaweza kuona kwa kitambo kiasi
Ezekiel
3:1-4 “Akaniambia,
Mwanadamu, kula uonacho; kula gombo hili, kisha enenda ukaseme na wana wa
Israeli. Basi nikafunua kinywa changu, naye akanilisha lile gombo. Akaniambia,
Mwanadamu, lisha tumbo lako, ulijaze tumbo lako kwa hili gombo nikupalo. Ndipo
nikalila, nalo kinywani mwangu lilikuwa tamu, kama utamu wa asali. Akaniambia,
Mwanadamu, haya! Waendee wana wa Israeli ukawaambie maneno yangu.”
Mathayo
12:31-32 “Kwa
sababu hiyo nawaambia, Kila dhambi na kila neno la kufuru watasamehewa
wanadamu, ila kwa kumkufuru Roho hawatasamehewa. Naye mtu ye yote atakayenena
neno juu ya MWANA WA ADAMU atasamehewa, bali yeye atakayenena neno juu ya Roho
Mtakatifu hatasamehewa katika ulimwengu wa sasa, wala katika ule ujao.”
Katika kiingereza wakati kwa Ezekiel wanatumia son
of man au a son of man kwa Yesu linatumika neno The Son of Man,
kwa Ezekiel ikimaanisha mwanadamu, na Kwa Yesu Kristo ikimaanisha Mwana wa
Adamu, hii maana yake ni nini? Huyu
ni mwana wa Adamu wa Ahadi ambaye Adamu alikuwa ameahidiwa, kama ilivyokuwa kwa
Abrahamu ambaye alikuwa ameahidiwa na Daudi ambaye naye alikuwa ameahidiwa,
mwana huyu wa Ahadi aliyeahidiwa Adamu katika kitabu cha Mwanzo:-
Mwanzo
3:14-15 “BWANA
Mungu akamwambia nyoka, Kwa sababu umeyafanya hayo, umelaaniwa wewe kuliko
wanyama wote, na kuliko hayawani wote walioko mwituni; kwa tumbo utakwenda, na
mavumbi utakula siku zote za maisha yako; nami nitaweka uadui kati yako na huyo
mwanamke, na kati ya uzao wako na uzao wake; huo utakuponda kichwa, na wewe
utamponda kisigino.”
Ijapokuwa mwana huyu wa ahadi anaitwa uzao wa
Mwanamke, lakini kwa uwazi kabisa alikuwa ni mtoto wa Adamu kwa hiyo Tangu
wakati huu katika wazo la Adamu na wazo la Mwanamke walikuwa wanafahamu kuwa
kuna moja ya mtoto wao ambaye atakuwa suluhisho la mgogoro kati yao na Shetani,
Kwa hiyo alikuwa ni mtoto wa ahadi za kinabii, fahamu kuwa katika agano la kale
mwanzoni kabisa hakukuwa na nabii na hivyo Mungu baba mwenyewe ndiye aliyekuwa
nabii kwa Adamu na Eva na unabii wa kwanza ni Mwanzo 3:15 uzao wa mwanamke,
kwa hiyo Yesu alipokuwa akijiita mwana wa Adamu
alikuwa akimaanisha mwana wa Ahadi wa Adamu, na Mwana wa Ahadi wa Abraham na
mwana wa Ahadi wa Daudi, huyu kwa vyovyote vile angetokea katika mti wa uzao wa
Adamu, mti wa uzao wa Ibrahimu na mti wa uzao wa Daudi. Kwa hiyo Yesu alipokuwa
akijita Mwana wa Adamu alikuwa anamanisha mwana wa Ahadi wa Adamu ambaye Mungu
alikuwa amemkusudia kwa ukombozi, hii ni moja ya sababu ya kujiita mwana wa
Adamu, na ni mwana wa adamu ambaye atateseka angalia neno KUPONDA KISIGINO
na kupitia maumivu haya ya kupondwa kisigino yeye atakomesha mateso kwa
kumaliza uadui kati yetu na shetani angalia neno KUPONDA KICHWA. Yesu alitumia jina Mwana wa Adamu mara nyingi
sana akitaka akili za watu zifunguke na kumwangalia mtoto wa Adamu aliyeahidiwa
unaona!
Sababu nyingine kubwa ya Msingi ya Yesu kujiita
mwana wa Adamu ilikuwa ni maalumu sana akijilinganisha na Mwana wa Adamu
aliyeuawa na Ndugu yake, Mwana huyu wa Adamu alikuwa mwenye haki, hakuwa na
kosa lolote lakini aliuawa tu kwa sababu alipata kibali kwa Mungu, mwana huyu
wa Adamu ni Habili, ambaye aliuawa na kaka yake Kaini, kwa msingi huo mara kwa mara Yesu alipojiita
mwana wa Adamu alikuwa maalumu anajidhihirisha kuwa Yeye ndiye yule Mwenye haki
aliyeuawa katika mikono ya watu wabaya, Mwana huyu wa Adamu alimuuma sana Adamu,
hasa damu yake ilipomwagika hii ndio picha halisi ambayo wanatheolojia wengi
hawajawahi kuizungumzia, lakini Roho Mtakatifu alinifundisha kuwa Yesu
anapojiita mwana wa Adamu kwa hakika alikuwa akimaanisha MTOTO WA ADAMU
MWENYE HAKI ALIYEUAWA kwa mikono ya ndugu yake na wakati huo huo msisitizo
ukiwa katika kuuawa kwake ambako kimsingi kunafanana na kuuawa kwa Habili, tumeona maswala kadhaa kumuhusu Habili katika
maandiko
Mtoto huyu wa Adamu alikuwa Mchungaji wa wanyama – Mwanzo
4:2 “Akaongeza
akamzaa ndugu yake, Habili. Habili alikuwa mchunga kondoo, na Kaini alikuwa
mkulima ardhi.”
Mtoto huyu wa Adamu alikubaliwa na Mungu kutokana na
Sadaka yake - Mwanzo 4:4 “Habili naye akaleta wazao wa kwanza wa wanyama wake na sehemu zilizonona
za wanyama. BWANA akamtakabali Habili na sadaka yake;”
Mtoto huyu wa Adamu alisalitiwa na kuuawa na ndugu
yake - Mwanzo 4:8-10 “Kaini akamwambia Habili nduguye, [Twende uwandani]Ikawa walipokuwapo
uwandani, Kaini akamwinukia Habili nduguye,akamwua. BWANA akamwambia Kaini,
Yuko wapi Habili ndugu yako? Akasema, Sijui, mimi ni mlinzi wa ndugu yangu?
Akasema, Umefanya nini? Sauti ya damu ya ndugu yako inanililia kutoka katika
ardhi.”
Mtoto huyu wa Adamu alikuwa mwenye haki - Mathayo
23:32-36 “Kijazeni
basi kipimo cha baba zenu. Enyi nyoka, wana wa majoka, mtaikimbiaje hukumu ya
jehanum? Kwa sababu hiyo, angalieni, mimi natuma kwenu manabii na wenye hekima
na waandishi; na wengine wao ninyi mtawaua na kuwasulibisha, na wengine wao
mtawapiga katika masinagogi yenu, na kuwafukuza mji kwa mji; hivyo ije juu yenu
damu yote ya haki iliyomwagika juu ya nchi, tangu damu ya Habili, yule mwenye
haki, hata damu ya Zakaria bin Barakia, mliyemwua kati ya patakatifu na
madhabahu. Amin, nawaambieni, Mambo hayo yote yatakuja juu ya kizazi hiki.”
Mtoto huyu wa Adamu Damu yake ilidai haki - Waebrania
12:24 “na
Yesu mjumbe wa agano jipya, na damu ya kunyunyizwa, inenayo mema kuliko ile ya
Habili.”
Mtoto huyu wa Adamu alikuwa tumaini la ukombozi wa
Wazazi wake - Mwanzo 4:25-26 “Adamu akamjua mke wake tena; akazaa mwana mwanamume, akamwita jina lake
Sethi; maana alisema, MUNGU AMENIWEKEA UZAO MWINGINE MAHALI PA HABILI; kwa
sababu Kaini alimwua. Sethi naye akazaa mwana; akamwita jina lake Enoshi. Hapo
ndipo watu walipoanza kuliitia Jina la BWANA.”
Mtoto huyu wa Adamu alifanya matendo yake kwa Imani
- Waebrania 11:4 “Kwa
imani Habili alimtolea Mungu dhabihu iliyo bora kuliko Kaini; kwa hiyo
alishuhudiwa kuwa ana haki; Mungu akazishuhudia sadaka zake, na kwa hiyo,
ijapokuwa amekufa, angali akinena.”
Jambo hili Muhimu sana linalomuhusu Mwana huyu wa
kipekee wa Adamu lina umuhimu mkubwa sana ukiunganisha na matukio yaliyomkuta
Bwana wetu Yesu Kristo, Habili alichunga Kondoo, Yesu ndiye Mchungaji mwema, Habili
alitoa sadaka iliyokubaliwa na Mungu, Na Yesu mjumbe wa Agano jipya aliyetoa
damu inenayo mema kuliko ile ya Habili, Kuuawa kwake kulileta mtoto wa
matumaini ambaye baada yake watu walianza kuliitia jina la bwana, ni baada ya
kifo cha Yesu Kristo wanadamu wanapata nafasi ya kumfikia Mungu na kumuabudu
pasipo hofu, Habili alikuwa mwenye haki, akauawa na ndugu yake, Na Yesu hakuwa
na hatia akauawa na ndugu zake kwa hiyo kwa mujibu wa maelekezo niliyopewa mimi
kama mkuu wa wajenzi, Mungu alinielekeza niieleze dunia leo, jambo ambalo wanazuoni
na wanatheolojia huwa hawalielezei, au hawakuwa wamefunuliwa ya kuwa Yesu
anapojiita mwana wa Adamu ni ukweli ulio wazi kuwa katika ubongo wake hakuna na
wazo la mtu yule katika Daniel, wala wazo la Mtu yule katika Isaya, wala wazo
la kutwaa mwili, wala hakuwa na wazo lingine zaidi ya wazo la mtoto wa Adamu
aliyeuawa na ndugu yake akijitaja kama Yeye ambaye atauawa na Nduguze kwaajili
ya ukombozi wa ulimwengu!
Wanatheolojia wengi wanamtumia Habil kama alama
kivuli au unabii kuhusu Kristo na wanakubali kuwa kama Habili alivyouawa na
ndugu yake na sababu kubwa ikiwa ni kwa sababu Habili alikuwa mwenye haki,
kadhalika Kristo naye aliuawa na Ndugu zake wayahudi akiwa hana hatia, Mungu
alimkabili Kaini akihoji Yuko wapi ndugu yako angalia
Mwanzo
4:10-11 “BWANA akamwambia Kaini, Yuko wapi Habili ndugu yako? Akasema, Sijui, mimi
ni mlinzi wa ndugu yangu?Akasema, Umefanya nini? Sauti ya damu ya ndugu yako
inanililia kutoka katika ardhi.”
Damu ya habili ililia kwaajili ya kutaka kisasi au
haki, lakini Damu yake Yesu inalia kwaajili ya rehema na msamaha na wokovu, Waebrania
12:24 “na
Yesu mjumbe wa agano jipya, na damu ya kunyunyizwa, inenayo mema kuliko ile ya
Habili.”
Waefeso
1:6-7 “Na
usifiwe utukufu wa neema yake, ambayo ametuneemesha katika huyo Mpendwa. Katika
yeye huyo, kwa damu yake, tunao ukombozi wetu, masamaha ya dhambi, sawasawa na
wingi wa neema yake.”
Kwa msingi huo utakubaliana nami kuwa kama Yesu
alivyokuwa akisisitiza ni kwa mauti ya namna gani atauawa na katika dhana hiyo
hiyo Yesu alikuwa akijiita Mwana wa Adamu, ni kama Yesu alikuwa akitaka makutano
waelewe kuwa YEYE NDIYE HABILI WA PILI, na kama vile kifo hakikuweza
kunyamazisha uhai wa Habili, kifo vilevile kimeshindwa kunyamazisha uhai wa
Yesu Kristo. Nasisistiza tena na tena Yesu alipokuwa akijiita mwana wa Adamu
alikuwa akimuwaza Habili akilini mwaka na kile ambacho wakuu wa makuhani
wangemfanyia na kazi ya ukombozi ambayo angeikamilisha kwamkifo chake, aidha
masikitiko na maneno ya Adamu alipomzaa Sethi aliposema MUNGU AMENIWEKEA UZAO MWINGINE MAHALI PA HABILI katika mtazamo finyu mtoto huyo ni
SETHI na katika mtazamo mpana mtoto huyo ni YESU KRISTO, mtoto wa tumaini la Adamu lililopotea.
Na Rev.
Innocent Samuel Kamote
Mkuuu
wa wajenzi mwenye Hekima