Luka 22:39-44 “Akatoka akaenda mpaka mlima
wa Mizeituni kama ilivyokuwa desturi yake; wanafunzi wake nao wakafuatana naye.
Alipofika mahali pale aliwaambia, Ombeni kwamba msiingie majaribuni. Mwenyewe
akajitenga nao kama kiasi cha kutupa jiwe, akapiga magoti akaomba, akisema, Ee
Baba, ikiwa ni mapenzi yako, uniondolee kikombe hiki; walakini si mapenzi
yangu, bali yako yatendeke. Malaika kutoka mbinguni akamtokea akamtia nguvu.
Naye kwa vile alivyokuwa katika dhiki, akazidi sana kuomba; hari yake ikawa
kama matone ya damu yakidondoka nchini.]”
Utangulizi:
Katika msimu huu wa Pasaka bado
tunaendelea kujifunza maswala kadhaa muhimu na madogo madogo, ambayo wakati
mwingine kwa sababu ya kutazama mfumo mzima wa mateso ya Bwana tunaweza
kujikuta ni kama tunayapuuzia, lakini yana umuhimu Mkubwa, leo nataka
kuzungumzia kile ambacho kimejitokeza katika Mlima wa Mizeituni sehemu iitwayo
Gethsemane na kuhusiana na tukio zima la Yesu Kristo kuwa na huzuni na kuingia
katika maombi lakini zaidi sana hari yake kuwa kama matone ya damu. Mahali hapa muhimu panaitwa Mlima wa
Mizeituni, lakini vilevile sehemu muhimu ya mlima huu wa mizeituni pia
panajulikana kama Bustani iitwayo Gethsemane.
Mathayo 26:36-39 “Kisha Yesu akaenda pamoja
nao mpaka bustani iitwayo Gethsemane, akawaambia wanafunzi wake, Ketini hapa,
hata niende kule nikaombe. Akamchukua Petro na wale wana wawili wa Zebedayo,
akaanza kuhuzunika na kusononeka. Ndipo akawaambia, Roho yangu ina huzuni
nyingi kiasi cha kufa; kaeni hapa, mkeshe pamoja nami. Akaendelea mbele kidogo,
akaanguka kifulifuli, akaomba, akisema, Baba yangu, ikiwezekana, kikombe hiki
kiniepuke; walakini si kama nitakavyo mimi, bali kama utakavyo wewe.”
Mahali hapo ndio mahali ambapo
kimsingi tunaweza kusema ushindi halisi wa Msalaba ulikoanzia, akiwa hapo
kumbuka kuwa msaliti ndio alikuwa amekwenda kuwaleta maadui wa kumkamata Yesu,
Hapa ndio mahali ambapo, Pia angekamatwa, hapa ndio mahali ambapo angeweza
kukata tamaa, hapa ndio mahali ambapo alihitaji msaada wa Mungu, Malaika na
wanadamu, Ndipo mahali ambapo angehitaji maombi kutoka kwa wenzake wa karibu
ambao kimsingi walilala, hapa ndipo mahali ambapo wale walioahidi kwenda naye
gerezani na hata kuwa tayari kufa naye walimkimbia, Hapa ndio mahali ambapo
alizidiwa na msongo wa mawazo, hapa ndipo mahali ambapo shetani alisema naye
kuhusu msalaba kama anaweza kuukabili au kukinywea kikombe cha mateso, hapa
ndio mahali ambapo mipango ya adui iliyokuwa mibaya ilikuwa inaenda kufanikiwa,
Ndipo mahali ambapo alitiwa nguvu na kukubaliana kuukabili Msalaba, Kimsingi ni
kama Yesu alikuwa hapa katika chumba cha wangonjwa mahututi, mgonjwa ambaye
anapambania uhai wake aishi ama afe na kisha mgonjwa anakubali kifo kwa Amani,
kwa hiyo mlima wa mizeituni, Bustani ya Gethsemane ni eneo la maamuzi magumu.
Ni eneo ambalo wakati na Muda muafaka wa ukombozi wa mwanadamu unaenda kuanza,
ni eneo la mapito ya moyoni. Na ya kihisia, na ya hofu na ya kutisha zaidi
kuliko hata msalaba wenyewe. Kila mwanadamu katika maisha yake huwa anapitia
katika bustani hii, kwa namna moja ama nyingine, ni mahali ambapo tunapaswa
kuruhusu Mapenzi ya Mungu yatimizwe! Tunajifunza somo hili, Mpaka mlima wa Mizeituni
kwa kuzingatia vipengele viwili vifuatavyo:-
·
Mlima wa Mizeituni, Bustani iitwayo Gethsemane
·
Mpaka mlima wa Mizeituni
Mlima wa Mizeituni, Bustani iitwayo Gethsemane
Ni Muhimu kufahamu kuwa Neno la
Mungu, limekuja kwetu kwa uweza wa Roho Mtakatifu, na Ni Roho huyu wa Mungu aliyewaongoza
waandishi kuweka rekodi hizi kwa kusudi la kutufundisha maswala mbali mbali.
Katika injili zote tunaona wakiwa wameelezea kuhusiana na Mahali hapa
alipokamatwa Yesu, Pakiwa panajulikana kama mlima wa Mizeituni, au bustani ya
Gethsemane lakini pia panaitwa Mahali pale, Kama ilivyo umuhimu wa Golgotha au
Kalvari, Mlima wa Mizeituni na hasa hapo Gethsemane pana umuhimu mkubwa sana
katika safari ya ukombozi wa mwanadamu.
Mathayo 26:30 “Nao walipokwisha kuimba,
wakatoka nje kwenda mlima wa Mizeituni.”
Luka 22:39 “Akatoka akaenda mpaka mlima wa
Mizeituni kama ilivyokuwa desturi yake; wanafunzi wake nao wakafuatana naye.”
Marko 14:26 “Nao walipokwisha kuimba
walitoka kwenda mlima wa Mizeituni.”
Kwa hiyo tunaona Injili zote
zikitaja habari za Mlima wa Mizeituni, Ni mlima maarufu na wa zamani sana una
ukubwa wa kama kilomita mbili hivi, mlima huu uko upande wa Mashariki mwa mji
wa Yerusalem, Mlima huu una urefu wa mita 78
au futi 250 ni mrefu kuliko mlima wa
hekalu, na hivyo ni eneo zuri ambalo unaweza kukaa na kuliangalia hekalu vizuri,
Yesu alipenda kuutumia mlima huu kwa maombi, kwa hiyo palikuwa ni mahali ambapo
alipendelea kupatembelea mara kwa mara akiwa Yerusalem na alitumia mlima huo
kufanya maombi, mlima unaitwa mlima wa mizeituni kwa sababu unafunikwa na miti
hiyo ya mizeituni na kulifanya eneo hilo kupendeza kwa ukijani wa Miti hiyo,
Mahali hapa Ndipo mahali ambapo Yesu alipatumia kupaa mbinguni angalia
Matendo 1:9-12 “Akiisha kusema hayo,
walipokuwa wakitazama, akainuliwa, wingu likampokea kutoka machoni pao. Walipokuwa
wakikaza macho mbinguni, yeye alipokuwa akienda zake, tazama, watu wawili
wakasimama karibu nao, wenye nguo nyeupe, wakasema, Enyi watu wa Galilaya,
mbona mmesimama mkitazama mbinguni? Huyu Yesu aliyechukuliwa kutoka kwenu
kwenda juu mbinguni, atakuja jinsi iyo hiyo mlivyomwona akienda zake mbinguni.
Kisha wakarudi kwenda Yerusalemu kutoka mlima ulioitwa wa Mizeituni, ulio
karibu na Yerusalemu, wapata mwendo wa sabato.”
Na ni katika mlima huu huu Yesu
atakaporudi atashukia hapo akitokea mbinguni na kufanya vita na Mpinga Kristo,
na kusimamisha utawala wake, kwa hiyo Mlima huu ni mlima wa kihistoria katika
ukombozi wa mwanadamu na utawala wa Mungu yaani ufalme wa Mungu.
Zekaria 14:3-4 “Hapo ndipo atakapotokea
Bwana, naye atapigana na mataifa hayo, kama vile alipopigana zamani siku ya
vita. Na siku hiyo miguu yake itasimama juu ya mlima wa Mizeituni, unaoelekea
Yerusalemu upande wa mashariki, nao mlima wa Mizeituni utapasuka katikati yake,
upande wa mashariki na upande wa magharibi; litakuwako huko bonde kubwa sana; na
nusu ya mlima ule utaondoka kwenda upande wa kaskazini, na nusu yake itaondoka
kwenda upande wa kusini.”
Kwa hiyo mlima wa mizeituni ni
mahali, muhimu sana katika unabii na historia nzima ya ukombozi wa mwanadamu na
kusimama kwa serikali ya kiungu yaani ufalme wa Mbinguni, kwa msingi huo Yesu
hakwenda tu katika mlima wa mizeituni kwa bahati mbaya, katika eneo hili la
Mlima wa Mizeituni juu ilikuweko sehemu ambayo ilikuwa na bustani nzuri na
sehemu hiyo iliitwa Gethsemane, kwa hiyo utaweza kuona tena waandishi wa Injili
wakiitaja sehemu hiyo angalia tena katika neno la Mungu hususani baadi ya
vitavu vya injili.
Mathayo 26:36 “Kisha Yesu akaenda pamoja
nao mpaka bustani iitwayo Gethsemane, akawaambia wanafunzi wake, Ketini hapa,
hata niende kule nikaombe.”
Marko 14:32 “Kisha wakaja mpaka bustani
iitwayo Gethsemane; akawaambia wanafunzi wake, Ketini hapa muda niombapo.”
Kwa hiyo katika mlima huo wa
mizeituni vilevile kulikuwako bustani ambayo iliitwa Gethsemane na Luka
anapaita mahali pale hii ni kwa sababu mahali hapo palikuwa ni maarufu sana hata
leo
Luka 22:40 “Alipofika mahali pale
aliwaambia, Ombeni kwamba msiingie majaribuni.”
Kwa Msingi huo ni muhimu kufahamu
kuwa eneo hili muhimu katika historia ya ukombozi wa mwanadamu, linaitwa Mlima
wa Mizeituni, lakini Pia Bustani ya Gethsemane, lakini Luka anapaita mahali
pale, na kuonyesha kuwa Yesu alikuwa na desturi ya kwenda katika eneo hilo mara
kadhaa, eneo hili kwa maelezo ya kale na katika injili ya Yohana palikuwa
ng’ambo ya kijito Kedroni, ambapo ndipo bustani hii ilipokuwepo na Yesu
alipachagua kama mahali pa maombi unaweza kuona
Yohana 18:1 “Alipokwisha kusema hayo, Yesu
alitoka pamoja na wanafunzi wake kwenda ng'ambo ya kijito Kedroni, palipokuwapo
bustani; akaingia yeye na wanafunzi wake.”
Eneo hili linaloitwa GETHSEMANE ambalo ni jina lenye asili
ya Kiaram ambalo maana yake Sehemu ya kukamulia mafuta, (oil Press) kwa hiyo uko uwezekano ya kuwa katika bustani ile ya
Mizeituni, kulikuweko na mashine za kukamulia mafuta ya zeituni, na ndio sababu pakaitwa pia GETHSEMANE, lakini vile vile kwanini
Luka anapaita MAHALI PALE, mahali
hapo palikuwa na historia maarufu ya watu hasa Mfalme mkuu Daudi kwenda
kuabudu, lakini sio hivyo tu Ni eneo ambalo Daudi aliposalitiwa na Mwanae
Absalom alikimbia na kuvuka mto huu yeye na watu wake na wakapanda mlima huu wa
mizeituni wakiwa wanalia sana, wakiwa hawana viatu na wakiwa wamejifunika nguo
zao vichwani mahali hapa kimsingi palikuwa
na sehemu ambapo Mungu alikuwa akiabudiwa, Lakini Mfalme Daudi na watu wake
walipanda mahali hapa wakiwa wamekata tamaa, wakiwa wanalia machozi, wakiwa
hawajui mbele yao itakuwaje. Unaweza kuona katika andiko hili:-
2Samuel 15:30-32 “Daudi akapanda akishika
njia ya kuupandia mlima wa Mizeituni, akilia alipokuwa akipanda; naye alikuwa
amejifunika kichwa chake, akaenda hana viatu; na watu wote waliokuwa pamoja
naye wakajifunika vichwa vyao, kila mmoja wao, wakapanda juu, wakilia
walipopanda Mtu mmoja akamwambia Daudi ya kwamba, Ahithofeli yu
katika hao waliopatana na Absalomu; Daudi akasema, Ee Bwana, nakusihi, uligeuze
shauri la Ahithofeli liwe ubatili. Ikawa, Daudi alipofika juu, hapo Mungu
alipoabudiwa, tazama, Hushai, Mwarki, akaja kumlaki na joho Lake Limeraruliwa,
tena ana udongo kichwani mwake.”
Kwa hiyo unaweza kuona Gethsemane
katika mlima wa mizeituni. Zaituni zilikamuliwa na zikatoa mafuta, lakini
vilevile ulikuwa ni mlima wa kutoa machozi, Daudi na watu wake walipanda mlima
huu huku wanalia, na Yesu alipanda mlima huu akiwa Analia, Daudi alipanda mlima
huu akiwa amekata tamaa na kupoteza matumaini akiwa amesalitiwa na Mwanae
Absalom na Yesu anapanda mlima huu akiwa amekata tamaa na anapoteza tumaini
kuukabili Msalaba akiwa amesalitiwa na mmoja ya Mwanafunzi wake Muhimu, huku
roho yake ikiwa ina huzuni mno
Mpaka mlima wa Mizeituni
Luka 22:39-44 “Akatoka akaenda mpaka mlima
wa Mizeituni kama ilivyokuwa desturi yake; wanafunzi wake nao wakafuatana naye.
Alipofika mahali pale aliwaambia, Ombeni kwamba msiingie majaribuni. Mwenyewe
akajitenga nao kama kiasi cha kutupa jiwe, akapiga magoti akaomba, akisema, Ee
Baba, ikiwa ni mapenzi yako, uniondolee kikombe hiki; walakini si mapenzi
yangu, bali yako yatendeke. Malaika kutoka mbinguni akamtokea akamtia nguvu.
Naye kwa vile alivyokuwa katika dhiki, akazidi sana kuomba; hari yake ikawa
kama matone ya damu yakidondoka nchini.]”
Tunaona katika andiko letu la
msingi kuwa Yesu akaenda pamoja na wanafunzi wake mpaka mlima wa mizeituni,
Mahali hapa Yesu alikuwa ameelemewa na Huzuni, Huzuni kubwa kwa sababu
anakabiliwa na kifo na sio kifo cha kawaida ni kifo cha msalaba, hakuna mauti
mbaya kama mauti ya msalaba, katika historia za hukumu ya kifo, kila taifa
lilikuwa lina namna yake ya kuua
Waingereza mtu alipohukumiwa kifo
walitumia kitanzi, wakati warumi walitumia shoka lililotundikwa, na wayahudi
walitumia kupiga mawe mpaka kifo, warumi walikuwa na hukumu nyingine ya kifo
kwa raia asiyekuwa Mrumi ambayo ilikuwa ni kumtundika msalabani, kifo hiki
kilikuwa ni kibaya zaidi kwa sababu ni mauti ya polepole, ilikuwa pia ni mauti
ya aibu, kwa sababu watu walisulubiwa wakiwa tupu na kudhalilishwa, wayahudi
waliamini kuwa Mungu hawezi kuruhusu mtu mwema kufa msalabani, mtu
aliyehukumiwa kifo cha msalabani alihesabika kuwa amelaaniwa,
Wagalatia 3:13-14 “Kristo alitukomboa
katika laana ya torati, kwa kuwa alifanywa laana kwa ajili yetu; maana
imeandikwa, Amelaaniwa kila mtu aangikwaye juu ya mti; ili kwamba baraka ya
Ibrahimu iwafikilie Mataifa katika Yesu Kristo, tupate kupokea ahadi ya Roho
kwa njia ya imani.”
Kwa hiyo katika mawazo ya Kristo
kama Mwana wa Mariam yaani kibinadamu mauti hii ilikuwa ni ya kuiepuka,
angetamani sana kikombe hiki kimuepuka aliomba kwa hisia kali sana na hapa
alikuwa amejawa na msongo wa mawazo, na ni katika eneo hilo hilo ambapo zaituni
zilikuwa zinakamuliwa Yesu alikamuliwa na msongo wa mawazo, kiasi cha kutoka
jasho (Hari) la damu, tukio hili kisayansi linaitwa Agony – ambalo maana yake ni Msongo mkubwa wa mawazo unaoathiri
hali halisi ya mwili kiasi cha mishipa ya damu kuzidiwa na kupanuka kwa
vinyeleo na kuruhusu jasho na damu kutoka, tukio hili liliweza kuelezewa na Luka
pekee kwa vile yeye alikuwa tabibu, Kwa hiyo Yesu alikuwa ameleemewa na huzuni
kubwa kwa sababu aina ya mateso ilikuwa mbaya kubebeka, na malaika walikuja
kumtia nguvu kuwa anapaswa kubeba, kwa hiyo tunapata picha hii Yesu alipokuwa
Gethsemane
-
Ni mahali
ambapo mtu anaelemewa na huzuni kubwa na msongo mkubwa wa mawazo
-
Ni mahali
ambapo mtu anakuwa amesalitiwa na kuachwa peke yake
-
Ni mahali
ambapo unajaribu kuomba msaada watu hata wakuombee na wanalala
-
Ni mahali
ambapo mtu unakata tamaa na kupoteza matumaini
-
Ni mahali
ambapo unaweza kuchanganyikiwa kwa sababu mipango ya adui ndiyo inayokwenda
kufanikiwa
-
Ni mahali
ambapo ni kama Mungu anasikia maombi ya adui zako na mipango yao na ya kwako
haisikiwi
-
Ni mahali
ambapo hakuna faraja kutoka upande wowote
-
Ni mahali
ambapo shetani angependa ubaki hapo ili akulize akukamue
-
Ni mahali
ambapo manabii walipanda wakiwa wanalia, machozi wamekata tamaa
-
Ni mahali
ambapo Imani yako inakamuliwa ili ikiwezekana iishe na urudie hapo
-
Ni mahali
ambapo pamejaa mashaka na marafiki wamekuacha peke yako
-
Ni mahali
ambapo ni kama uko chumba cha wagonjwa mahututi na unaota ndoto za kugombea
uhai au kifo
-
Ni mahali
ambapo huwezi kuamua mambo, na mambo yako yanaamuliwa na adui zako
-
Ni mahali
ambapo unachokiona mbele yako ni kifo tu maombi hayajibiwi
-
Ni mahali
ambapo ni kama maamuzi yamepita na huwezi hata kukata rufaa tena
-
Ni mahali
ambapo utatiwa mikononi mwa adui na rafiki zako wote watakukimbia
-
Ni mahali
ambapo unakutana na vita ya kiakili, kihisia na kiroho, na ni mahali pa maamuzi
magumu!
Mungu katika hekima yake huruhusu
nyakati Fulani na sisi katika maisha yetu tupite tupande mpaka mlima wa
Mizeituni, tuende mpaka Gethsemane tukakamuliwe huko, tukalizwe huko, akili
zetu zizungumze na shetani, huku Mungu akiwa kimyaa, Katika hali ya kawaida wakati
wa mapito na mateso huwa hauonekani kuwa ni wakati mzuri, unakuwa ni wakati wa
kukamuliwa, unakuwa ni wakati wa taarifa mbaya, unakuwa ni wakati wa kuamua
kufanya mapenzi ya Mungu au kuyaacha taarifa njema ni kuwa Yesu hakukata tamaa,
Yesu hakuvunjika moyo na malaika wa Bwana walikuja kumtia nguvu na akawa yuko
tayari kuyakabili mateso ya Msalaba, Daudi alilia katika mlima huu, lakini
alifanikiwa kujipanga na kukabiliana na Absalom na Mungu alimpa ushindi, Mungu
alijibu maombi ya Yesu kwa kumtia nguvu aukabili Msalaba lakini alijua ya kuwa
siku ya tatu atamfufua na kumpeleka katika maisha yasiyozuilika Ushindi wa maisha yetu na furaha ya kweli
hupatikana, pia kwa kupitia njia ya mateso,
tumepewa sio kumwamini tu bali na kuteswa kwaajili yake
Wafilipi 1:28-29 “wala hamwaogopi adui
zenu, katika neno lo lote; kwao hao ni ishara mathubuti ya kupotea, bali kwenu
ninyi ni ishara ya wokovu, huo utokao kwa Mungu. Maana mmepewa kwa ajili ya
Kristo, si kumwamini tu, ila na kuteswa kwa ajili yake;”
Mungu atatuacha tupite katika
wakati Mgumu, ambao utatuletea ushindi mkubwa sana na hivyo hatupaswi kuogopa tunapopita
Gethsemane wakati ambapo umeachwa peke yako na hakuna wa kukushika mkono
usiogope Yesu Kristo anaijua njia hiyo na ni yeye aliyesema Twendeni mpaka mlima
wa mizeituni mlima huu sio wa mateso pekee bali ni mlima wa ushindi, ni mlima
wa mahali ambapo sio Yesu atakamatwa tu, na kugongwa kisigino, lakini ni mahali
ambapo Yesu atakanyaga tena na mlima huu utapasuka na watachinjiliwa mbali adui
zake ni mlima ambapo ufalme wa Mungu utastawi, kumbuka muda wa kupita hapa sio
mrefu ni mfupi sana
1Petro 5:8-11 “Mwe na kiasi na kukesha; kwa
kuwa mshitaki wenu Ibilisi, kama simba angurumaye, huzunguka-zunguka, akitafuta
mtu ammeze. Nanyi mpingeni huyo, mkiwa thabiti katika imani, mkijua ya kuwa
mateso yale yale yanatimizwa kwa ndugu zenu walioko duniani. Na Mungu wa neema
yote, aliyewaita kuingia katika utukufu wake wa milele katika Kristo, mkiisha
kuteswa kwa muda kidogo, yeye mwenyewe atawatengeneza, na kuwathibitisha, na
kuwatia nguvu. Uweza una yeye hata milele na milele. Amina.”
Baada ya mateso ya kihisia pale Gethsemane Yesu alitiwa nguvu kuukabili
Msalaba, alikwenda msalabani na alipitia dhihaka na mateso akiwa ana utulivu
mkubwa sana akijua faida ya mateso yale na kufufuka kwake
-
Alikuwa
na nguvu ya kuwaombea maadui zake
-
Alikuwa
na nguvu ya kuruhusu majambazi waende peponi
-
Alikuwa
na nguvu ya kutangaza kuwa kazi ya ukombozi umekamilika
-
Alikuwa
na nguvu ya kukabidhi roho yake kwa Amani akijua ya kuwa Baba yake atamfufua
-
Alikuwa
na nguvu ya kuruhusu pazia la hekalu kupasuka na watu kuifikia neema ya Mungu
-
Alikuwa
na nguvu ya kufufua watu waliokufa zamani na miili yao kuonekana kwa muda
-
Alikuwa
na nguvu dhidi ya Mauti akitupa waamini wote tumaini kubwa lenye Baraka
-
Alikuwa
na nguvu ya kusamehe dhambi
-
Alikuwa
na nguvu ya kututhibitishia na kutuhakikishia wokovu
-
Alikuwa
na nguvu ya kubadilisha maisha ya watu na kuleta mabadiliko makubwa katika
jamii zote duniani
-
Alikuwa
na nguvu ya kutioa faraja na tumaini kiasi cha kumuwezesha kila mtu kuwa tayari
kufa kama yeye
-
Alikuwa
na nguvu na mamlaka yote mbinguni na duniani
-
Alikuwa
anamejithibitishia kuwa atarudi tena na kukanyaga mlima wa mizeituni
-
Alikuwa
na nguvu ya kuwafanya adui zake na wote waliokuwa wakimtesa walikiri hakika
alikuwa mwema
Ushindi wote huo hapo juu ni kwa
sababu Pale Gethsemane Yesu alikubali Mapenzi ya Mungu, kwamba hata tunapopitia
katika njia zilizo ngumu sana hatuachi kuomba tunaomba na baba akiwa kimya
tunakubali mapenzi yake yatimizwe
Luka 22:41-43. “Mwenyewe akajitenga nao
kama kiasi cha kutupa jiwe, akapiga magoti akaomba, akisema, Ee Baba, ikiwa ni
mapenzi yako, uniondolee kikombe hiki; walakini si mapenzi yangu, bali yako
yatendeke. Malaika kutoka mbinguni akamtokea akamtia nguvu.”
Ni pale Gethsemane ndipo Yesu
alipotengeneza nguvu ya kukabiliana na hali zote zilizokuwa mbele yake kumbuka
alisema ombeni kusudi msiingie majaribuni, aliweza kuyashinda majaribu yote na
malaika wa Bwana walikuja kumtia nguvu
Ni pale Gethsemane ndipo Yesu
alipoonja hisia na mateso yetu ya kibinadamu tunapokuwa taabuni alionyesha
uanadamu wake na sisi tunapopita katika majaribu makali anaujua uanadamu wetu,
Ni hapa ndipo wanafunzi wa Yesu walipofahamu umuhimu wa maombi, ni hapa ndipo
alipowafundisha namna wanavyoweza kukabiliana na ushindi wanapokuwa matatani.
Mathayo 26:41 “Kesheni, mwombe, msije
mkaingia majaribuni; roho i radhi, lakini mwili ni dhaifu.”
Ni pale Gethsemane ndipo Yesu
alionyesha kuwa kweli yeye ni Mpakwa mafuta kwa sababu alikubali kuukabili
msalaba bila vurumai yoyote aliukabili msalaba kwa upole na unyenyekevu mkubwa
Isaya 53:3-7 “Alidharauliwa na kukataliwa
na watu; Mtu wa huzuni nyingi, ajuaye sikitiko; Na kama mtu ambaye watu
humficha nyuso zao, Alidharauliwa wala hatukumhesabu kuwa kitu. Hakika
ameyachukua masikitiko yetu, Amejitwika huzuni zetu; Lakini tulimdhania ya kuwa
amepigwa, Amepigwa na Mungu, na kuteswa. Bali alijeruhiwa kwa makosa yetu,
Alichubuliwa kwa maovu yetu; Adhabu ya amani yetu ilikuwa juu yake, Na kwa
kupigwa kwake sisi tumepona. Sisi sote kama kondoo tumepotea; Kila mmoja wetu
amegeukia njia yake mwenyewe; Na Bwana ameweka juu yake Maovu yetu sisi sote.
Alionewa, lakini alinyenyekea, Wala hakufunua kinywa chake; Kama mwana-kondoo
apelekwaye machinjoni, Na kama vile kondoo anyamazavyo Mbele yao wakatao
manyoya yake; Naam, hakufunua kinywa chake.”
Ni pale Gethsemane Ndipo Yesu
alipoanza harakati za ukombozi wa mwanadamu kwa kukabiliana na matukio yote
kuanzia mahakamani, kusulubiwa kufa na kufufuka akiwa sadaka kamili ya
upatanisho na msamaha wa dhambi zetu akitupatanisha sisi na Mungu
1Timotheo 2:5-6 “Kwa sababu Mungu ni mmoja,
na mpatanishi kati ya Mungu na wanadamu ni mmoja, Mwanadamu Kristo Yesu; ambaye
alijitoa mwenyewe kuwa ukombozi kwa ajili ya wote, utakaoshuhudiwa kwa majira
yake.”
Ni Gethsemane ndipo Yesu
alipoandaa ukamilisho wa eneo muhimu la huduma yake duniani akionyesha kumtii
Mungu hata mauti ya msalaba, akiwa tayari kukamilisha mapenzi ya Mungu, huruma
zake kubwa kwa wanadamu na wajibu wake mkubwa kama mwokozi wa ulimwengu jambo
ambalo limemletea sifa kubwa sana Mbinguni
Wafilipi 2:5-11 “Iweni na nia iyo hiyo
ndani yenu ambayo ilikuwamo pia ndani ya Kristo Yesu; ambaye yeye mwanzo
alikuwa yuna namna ya Mungu, naye hakuona kule kuwa sawa na Mungu kuwa ni kitu
cha kushikamana nacho; bali alijifanya kuwa hana utukufu, akatwaa namna ya
mtumwa, akawa ana mfano wa wanadamu; tena, alipoonekana ana umbo kama
mwanadamu, alijinyenyekeza akawa mtii hata mauti, naam, mauti ya msalaba. Kwa
hiyo tena Mungu alimwadhimisha mno, akamkirimia Jina lile lipitalo kila jina;
ili kwa jina la Yesu kila goti lipigwe, la vitu vya mbinguni, na vya duniani,
na vya chini ya nchi; na kila ulimi ukiri ya kuwa YESU KRISTO NI BWANA, kwa
utukufu wa Mungu Baba.”
Ndugu msomaji wangu, kumbuka
wakati wote unapopitia mateso, ni kama uko Gethsemane, ni kama Mwalimu
amekuambia upande mlima wa mizeituni, utakuwepo kwa Muda mfupi na ukimtii Mungu
katika wakati huo Mungu, atakupeleka katika maisha ya Gethsemane, na kukupeleka
katika maisha yasiyoweza kuzuilika, wote sasa tunaweza kuona umuhimu wa mlima
wa mizeituni na eneo la Gethsemane, tunajifunza kujitia nguvu katika Bwana,
kuwa na ujasiri na utayari wa kukabiliaba na mambo magumu ambayo kwa kawaida
Mungu huyafupiza sana lakini hutupa matokeo mazuri sana tunapokuwa tumeyatii
mapenzi yake. Mungu akutie nguvu wakati wote unapopanda mlima wa mizeituni na
kupita eneo la kukamuliwa, Malaika wa bwana watakutia nguvu utakuwa na moyo wa
ujasiri na utashinda na kuwa msaada mkubwa kwa ulimwengu unaokuzunguka
Uongezewe neema!
Na. Rev. Mkombozi Innocent Samuel bin Jumaa bin Athumani Sekivunga
Kamote
Mkuu wa wajenzi mwenye Hekima