Mwanzo 50:24-26 “Yusufu akawaambia nduguze,
Mimi ninakufa, lakini Mungu atawajia ninyi bila shaka, atawapandisha toka nchi
hii, mpaka nchi aliyowaapia Ibrahimu, na Isaka, na Yakobo. Yusufu akawaapisha
wana wa Israeli, akasema, Bila shaka Mungu atawajia ninyi, nanyi mtaipandisha
huko mifupa yangu. Basi Yusufu akafa, mwenye miaka mia na kumi; wakampaka dawa,
wakamtia katika sanduku, huko Misri.”
Utangulizi:
Kaka zangu na dada zangu katika
Kristo! Leo tunachukua Muda kujifunza kwa kina na mapana na marefu kuhusu
kutimizwa kwa mojawapo ya agizo la Muhimu sana la Yusufu kwa wana wa Israel,
wote tunakumbuka habari za Mtu huyu Muhimu aliyeitendea mema familia yake na
mataifa mengi kwa kuyaokoa na njaa kupitia uwezo wake mkubwa wa kiutawala na
mipango chini ya Farao iliyoleta wokovu kwa wengi, Pamoja na kuwa ndugu zake
walimfanyia vibaya lakini wote tunaukumbuka Moyo wa Yusufu jinsi ulivyokuwa
mwema kwani hakuthubutu kulipa mabaya, alihesabu yaliyomkuta kama mapenzi ya
Mungu, jambo lililopelekea kuwa mtu wa kuheshimiwa sana katika familia yake,
Lakini akiwa anakaribia kufa mtu huyu aliwakusanya Israel wote na akiwa
amezungukwa na wana wa Israel pamoja na wanae na wajukuu zake aliwaeleza habari
za Muhimu sana na akazisisitiza kwa kuwaapisha kwamba ni lazima Bwana atawatokea
tena na Bila shaka atawapandisha kutoka katika inchi hii Misri, na kuwa
atawapandisha katika inchi ile aliyowaapia baba zao yaani Ibrahimu, Isaka na
Yakobo, na ya kuwa wakati huo utakapowadia wahakikishe wanaipandisha Mifupa
yake huko na aliwaapisha kuwa jambo hili ni lazima walitimize.
Mwanzo 50:24-26 “Yusufu akawaambia nduguze, Mimi ninakufa, lakini Mungu
atawajia ninyi bila shaka, atawapandisha toka nchi hii, mpaka nchi aliyowaapia
Ibrahimu, na Isaka, na Yakobo. Yusufu akawaapisha wana wa Israeli, akasema,
Bila shaka Mungu atawajia ninyi, nanyi mtaipandisha huko mifupa yangu. Basi
Yusufu akafa, mwenye miaka mia na kumi; wakampaka dawa, wakamtia katika
sanduku, huko Misri.”
Tunaweza kujiuliza swala la
msingi sana kwanini mtu huyu aliyekuwa na mafanikio makubwa sana kule Misri,
aliyestawi sana na kuwastawisha ndugu zake wote lakini bado hataki kusahau
inchi ya Urithi wa baba zake? Yusufu
alikuwa na ujuzi mkubwa sana kuhusu Mungu wa baba zake ya kuwa hakuna neno
ambalo Mungu wetu ataahidi likaanguka bure yaani likapita bila kutimizwa, Yusufu
anamjua wazi Mungu wa Ibrahimu na Isaka na Yakobo kuwa hakuna neno linalotoka
katika kinywa chake ambalo liliwahi kuanguka bure, Mungu alikuwa ameahidi kwa
kinywa chake Tangu zamani ya kuwa atawapa Israel Inchi ya Mkanaani, Nchi
iliyojawa na maziwa na asali. Yusufu alikuwa na Imani kuwa neno hilo lazima
litakuja kutimizwa, Hivyo hata kama yu katika hali ya kufa anajua kuwa Mungu
atatimiza ahadi zake, Yusufu aliendelea kumuamini Mungu kwamba atawaokoa watu
wake na kuwaondoa katika inchi ile ambayo wangetumikishwa kwa utumwa mzito
ambao kimsingi pia waliujua kuwa utakuja na ya kuwa ni lazima atawaleta tena
katika inchi ya ahadi. Nadhani Yusufu alikuwa anakumbuka kile ambacho Mungu
alizungumza na baba zake Ibrahimu na Isaka na Yakobo.
Mwanzo 15:13-16 “BWANA akamwambia Abramu,
Ujue hakika ya kwamba uzao wako utakuwa mgeni katika nchi isiyo yake,
watawatumikia watu wale, nao watateswa muda wa miaka mia nne. Hata na taifa
lile, watakaowatumikia, nitawahukumu; baadaye watatoka na mali mengi. Lakini
wewe utakwenda kwa baba zako kwa amani, utazikwa katika uzee mwema. Na kizazi
cha nne kitarudi hapa, maana haujatimia uovu wa Waamori bado.”
Tutajifunza somo hili kupandishwa
kwa mifupa ya Yusufu kwa kuzingatia vipengele viwili vifuatavyo:-
1.
Kwanini
Mifupa ya Yusufu katika inchi ya Kanaani?
2.
Kupandishwa
kwa mifupa ya Yusufu
Kwanini Mifupa ya Yusufu katika inchi ya Kanaani?
Yusufu aliinuliwa sana katika
inchi ya Misri, alikuwa maarufu mno? Aliwasaidia wengi na kuheshimika sana na
alipata mafanikio makubwa, aliwapa ndugu zake inchi ya Gosheni mahali ambapo
Mto Nile unamwaga maji yake katika bahari ya Mediteraniani, ni eneo lenye
rutuba na ustawi mkubwa sana kwa wana wa Israel na kwa kweli walifanikiwa sana,
walimiliki mali nyingi mpaka wenyeji wao waliona wivu, waliongezeka sana
walistawi na walikuwa na Nguvu, Gosheni
lilikuwa eneo lenye kufaa kwa malisho pia, unaweza kujiuliza kwanini Yusufu
anawaapisha Israel na kuwahakikishia kuwa watakuja kuondoka na hivyo waikumbuke
mifupa yake na kuipeleka katika inchi ya ahadi?
1.
Yusufu alikuwa amejifunza ya kuwa Mungu wa baba zake ni Muaminifu, Hakuna
neno hata moja amewahi kuliahidi lisitimizwe bila kujali kuwa itachukua muda
gani, Yeye mwenyewe alikuwa amejifunza uaminifu wa Mungu kwani Ndoto zile
alizooteshwa na Mungu Japokuwa zilimpitisha katika mapito Mengi lakini zilikuja
kutimia, alikuwa amejifunza kivitendo kwamba ni Mungu asiyeweza kusema uongo na
ya kuwa neno lake haliwezi kwenda bure, uaminifu wake na fadhili zake ni za
milele nazo hudumu kizazi hata kizazi!
Hesabu 23:19 “Mungu
si mtu, aseme uongo; Wala si mwanadamu, ajute; Iwapo amesema, hatalitenda?
Iwapo amenena, hatalifikiliza?”
Isaya 55:10 -11 “Maana
kama vile mvua ishukavyo, na theluji, kutoka mbinguni, wala hairudi huko; bali
huinywesha ardhi, na kuizalisha na kuichipuza, ikampa mtu apandaye mbegu, na
mtu alaye chakula; ndivyo litakavyokuwa neno langu, litokalo katika kinywa
changu; halitanirudia bure, bali litatimiza mapenzi yangu, nalo litafanikiwa
katika mambo yale niliyolituma.”
Kwa hiyo Yusufu
alikuwa na uhakika wa Mungu wa baba zake ya kuwa hakuna kitu anaahidi kisha
asikitimize, kwa hiyo tukio la kuagiza mifupa yake kuzikwa katika inchi ya
kanaani ni wazi kuwa alikuwa na Imani ya kuwa wana wa Israel watatoka katika
inchi ya utumwa na kuwa Mungu atawarejesha katika inchi ya ahadi.
Waebrania 11: 22 “Kwa
imani Yusufu, alipokuwa amekaribia mwisho wake,
alitaja habari za kutoka kwao wana wa Israeli, akaagiza kwa habari ya mifupa
yake.”
2.
Yusufu anatumika kama alama ya kisayuni kwa wana wa Israel, Israel leo wametawanyika kila
mahali duniani, na nafahamu na wote tu mashahidi kuwa wengi wamerudi nyumbani,
wako pale Israel leo katika inchi ambayo dunia inachanganyikiwa kuhusu
mustakabali wa inchi ile, Lakini Yusufu anawakumbusha Wayahudi wote duniani
hata pamoja na mafanikio makubwa wanayoyapata kokote waliko duniani,
wanaheshimika sana wanafanikisha inchi hizo huko waliko lakini ni lazima wakumbuke
kuwa wao ni Wayahudi na kuwa Mungu anatoa wito kwao kurudi Nyumbani, kuchelewa
kwao kurudi nyumbani kunachelewesha kutimia kwa unabii na mapenzi mengi ya
Mungu, Mungu aliahidi kuwatawanya lakini vile vile Mungu aliahidi kuwa
atawarudisha,
Kumbukumbu 30:4-6“Watu
wako waliotawanyika wakiwako katika ncha za mbingu za mwisho, kutoka huko
atakukusanya Bwana, Mungu wako; kutoka huko atakutwaa; atakuleta Bwana, Mungu
wako, uingie nchi waliyomiliki baba zako, nawe utaimiliki; naye atakutendea
mema, na kukufanya uwe watu wengi kuliko baba zako. Bwana, Mungu wako,
atautahiri moyo wako, na moyo wa uzao wako, ili umpende Bwana, Mungu wako, kwa
moyo wako wote, na kwa roho yako yote, upate kuwa hai.”
Haijalishi vizazi
vingapi vimepita, haijalishi wana siasa wa dunia wanawaza nini Lakini Israel ni Inchi
ya ahadi kwa Ibrahimu, Isaka, Yakobo na Yusufu pia, kila anayeshindana na agizo
hili anashindana na agizo la Mungu, Yusufu anaonyesha moyo wa kizalendo,
anajitanabahisha kuwa Myahudi halisi nyumbani ni Israel, alijua kuwa Israel
watakuwa watumwa, lakini Misri sio inchi salama kiroho wala sio kwao, ina
miungu mingi inayoabudiwa, walipitia magumu mengi, watoto wao wa kiume waliuawa
na Yusufu anaonyesha kwamba anatamani nyumbani na nyumbani halisi ni Israel
sawasawa na Neno la Mungu kwa baba zao.
Mwanzo 15: 18-21 “Siku
ile BWANA akafanya agano na Abramu, akasema, Uzao wako nimewapa nchi hii,
kutoka mto wa Misri mpaka huo mto mkubwa, mto Frati, Mkeni, na Mkenizi, na
Mkadmoni, na Mhiti, na Mperizi, na Mrefai,na Mwamori, na Mkanaani, na
Mgirgashi, na Myebusi.”
Mwanzo 17:7-8 “Agano
langu nitalifanya imara kati ya mimi na wewe, na uzao wako baada yako, na
vizazi vyao, kuwa agano la milele, kwamba nitakuwa Mungu kwako na kwa uzao wako
baada yako. Nami nitakupa wewe na uzao wako baada yako nchi hii unayoikaa
ugeni, nchi yote ya Kanaani, kuwa milki ya milele; nami nitakuwa Mungu wao.”
Mwanzo 28:11-17 “Akafika
mahali fulani akakaa huko usiku kucha, maana jua lilikuwa limekuchwa; akatwaa
jiwe moja la mahali pale akaliweka chini ya kichwa chake, akalala usingizi pale
pale. Akaota ndoto; na tazama, ngazi imesimamishwa juu ya nchi, na ncha yake
yafika mbinguni. Tena, tazama, malaika wa Mungu wanapanda, na kushuka juu yake.
Na tazama, BWANA amesimama juu yake, akasema, Mimi ni BWANA, Mungu wa Ibrahimu
baba yako, na Mungu wa Isaka; nchi hii uilalayo nitakupa wewe na uzao wako. Na
uzao wako utakuwa kama mavumbi ya nchi, nawe utaenea upande wa magharibi, na
mashariki, na kaskazini, na kusini; na katika wewe, na katika uzao wako, jamaa
zote za dunia watabarikiwa. Na tazama, mimi nipo pamoja nawe, nitakulinda kila
uendako, nami nitakuleta tena mpaka nchi hii, kwa maana sitakuacha, hata nitakapokufanyia
hayo niliyokuambia. Yakobo akaamka katika usingizi wake, akasema, Kweli BWANA
yupo mahali hapa, wala mimi sikujua. Naye akaogopa akasema, Mahali hapa
panatisha kama nini! Bila shaka, hapa ni nyumba ya Mungu, napo ndipo lango la
mbinguni.”
Mwanzo 48:3-4 “Yakobo
akamwambia Yusufu, Mungu Mwenyezi alinitokea huko Luzu, katika nchi ya Kanaani,
akanibariki, akaniambia, Mimi hapa, nitakuongezea uzao wako, na kukuzidisha,
nami nitakufanya uwe kundi la mataifa; kisha nitawapa wazao wako nchi hii baada
yako, iwe milki ya milele.”
Israel ni ya
Mungu, Israel (Kanaani) ni Mungu alimpa Ibrahimu na Isaka na Yakobo, kila
anayetaka Israel isiwepo anashindana na agizo la Mungu, Wayahudi wenyewe
wanapaswa kuwa mstari wa Mbele kutii agizo la Mungu ambalo Ibrahimu, Isaka na
Yakobo walilitii, na Yusufu hakutaka kuwa sababu ya wayahudi kubakia Misri
hivyo kwa kiapo aliwaapisha kwamba akifa haijalishi watakaa muda gani Misri,
lakini Lazima Mungu ataitimiza ahadi yake naye hataki kubaki ugenini, huu ni
moyo wa uzalendo mkubwa na nitoe wito kwa kila myahudi kokote aliko duniani wakumbuke
Kanaani, kwa sababu Mungu ameagiza hivyo.
3.
Yusufu alikuwa ni Mwalimu mzuri sana,
alitumia kifo chake na mifupa yake kuwa alama muhimu kwa kizazi na kizazi,
kumbuka Tangu walipofika Misri Israel waliishi miaka karibu 430 na Yusufu
aliishi miaka 110 tu lakini Fundisho lake na kazi yote ambayo Mungu aliifanya
Yusufu alihakikisha kuwa kumbukumbu yake haitafutika alihakikisha kuwa kupitia
mifupa yake kila kizazi kitakumbuka umuhimu wake, na uaminifu wa Mungu na
unabii wake, Yeye aliagiza siku watakapoondoka Misri aliwaapisha wakumbuke
mifupa yake hivyo kizazi na kizazi katika jamii ya wayahudi kila mmoja kabla
hajafa alimkubusha mtoto wake kila nyumba kulikuwa na mafundisho ya kuwa Mungu
atatutoa utumwani na atakapotimiza hilo kumbukeni mifupa ya Yusufu, kila
familia ilionywa jamani jamani msisahau mifupa ya Yusufu, na ndio maana Musa
alipotoka Misri japo alikuwa wa kabila
la Lawi hakusahau kamwe mifupa ya Yusufu, na Wana wa Israel hata alipokufa Musa
huko jangwani bado wana wa Israel chini ya Yoshua walipewa inchi na
walihakikisha wanaizika mifupa ya Yusufu huko Shekemu nchini Israel yaani inchi ya mkanaani nchi ya
ahadi.
Kutoka 13:19 “Musa
akaichukua ile mifupa ya Yusufu pamoja naye; maana, alikuwa amewaapisha sana
wana wa Israeli, akisema, Mungu hana budi atawajilia ninyi; nanyi mtaichukua
mifupa yangu kutoka hapa pamoja nanyi.”
Yoshua 24:31-32 “Nao
Israeli wakamtumikia Bwana siku zote za Yoshua, na siku zote za hao wazee
walioishi baada ya kufa kwake Yoshua, hao walioijua kazi yote ya Bwana,
aliyowatendea Israeli. Na hiyo mifupa ya Yusufu, ambayo wana wa Israeli
walikuwa wameileta kutoka Misri, wakaizika huko Shekemu katika ile sehemu ya
nchi, Yakobo aliyoinunua kwa wana wa Hamori, babaye Shekemu, kwa vipande mia
vya fedha; nayo ikawa ni urithi wa wana wa Yusufu.”
Vizazi vingi
vilikuwa vimepita Lakini Israel walikumbuka umuhimu wa Yusufu na agizo lake,
walilishika walilitii na walilitimiza kama walivyoapishwa na Yusufu!
Kupandishwa kwa mifupa ya Yusufu!
Kupandishwa kwa
mifupa ya Yusufu katika inchi ya kanaani kunatufundisha maswala kadhaa ya
Muhimu sisi kama wakristo, huu ni mfano Muhimu sana wenye vitu vya kutufunza.
1.
Lazima
tuendelee kumuamini Mungu na ahadi zake – iwe mvua iwe jua, iwe
tumefanikiwa iwe hatujafanikiwa bado Mungu ni mwaminifu, Yusufu alikuwa
amebarikiwa sana na alikuwa na mafanikio makubwa sana, lakini hii haikumfanya
asahau uaminifu wa Mungu. Wala haikumfanya asahau kwao! Alikuwa amejifunza kuwa Mungu ni mwaminifu na
kila alisemalo litatimia aliamini kuwa Mungu atafanya alilolisema, Ni wangapi
tunaamini katika kile ambacho Bwana amekisema? Yesu Kristo ni mwaminifu kila
neno lake aliloliahidi litatimia kila kitu kitapita lakini maneno yake Bwana
wetu Yesu hayatapita kamwe. Ni lazima kila mtu wa Mungu awe na Imani katika
Neno la Mungu. Yesu Kristo anaitwa shahidi aliye mwaminifu, ni lazima tuziamini
ahadi zake na kujua ya kila alilolisema atalitimiza.
Ufunuo 1:4-6 “Yohana, kwa yale makanisa saba yaliyoko Asia; Neema na
iwe kwenu na amani, zitokazo kwake yeye aliyeko na aliyekuwako na atakayekuja;
na zitokazo kwa roho saba walioko mbele ya kiti chake cha enzi; tena zitokazo
kwa Yesu Kristo, shahidi aliye mwaminifu, mzaliwa wa kwanza wa waliokufa, na
mkuu wa wafalme wa dunia. Yeye atupendaye na kutuosha dhambi zetu katika damu
yake, na kutufanya kuwa ufalme, na makuhani kwa Mungu, naye ni Baba yake;
utukufu na ukuu una Yeye hata milele na milele. Amina.”
2. Yusufu alifikiri yajayo – Yusufu
hakujifikiri yeye mwenyewe tu, alitaka kizazi na kizazi kimuelewe Mungu, hakuwa
anafanya mambo kwaajili yake, tendo lake la kuamuru kwa nguvu na lazima yaani
kwa kuwaapisha lilikuwa linaonyesha anawaza maisha zaidi ya maisha haya, kila
Mkristo anapaswa kuhakikisha ya kuwa injili inarithishwa kwa kizazi kijacho kwa
watu waaminifu ambao watafaa kuwafundisha na wengine, Israel walikuwa waaminifu
kurudia tena na tena kiapo cha Yusufu kwao kwa kizazi kilichofuata waliogopa
kupata madhara endapo hawatawashirikisha watu wengine, Injili yetu inapaswa
kukabidhiwa watu wengine ili kizazi na kizazi kiweze kulijua neno la Mungu vile
vile kama tulivyoagizwa tangu enzi za mitume
2Timotheo 2:2 “Na mambo yale uliyoyasikia kwangu mbele ya mashahidi
wengi, hayo uwakabidhi watu waaminifu watakaofaa kuwafundisha na wengine.”
3. Umuhimu wa inchi ya kanaani – Wakristo
wanapaswa kuwa Mstari wa mbele kuelewa mapenzi ya Mungu kuhusu Israel ile nchi
ni lango la Mbinguni, Baraka zote zilizokusudiwa duniani kwa wanadamu wote
zinapitia Israel, kwa hiyo kila mmoja anapaswa kuwatendea mema wayahudi na
kuwasaidia kurudi kwao na kuisimamia inchi yao, Wamarekani na Waingereza na
Wafaransa na Wajerumani wanaijua siri hii, ni afadhali kukaa kimya linapokuja
swala la Israel kuliko kuropoka ropoka Israel ni ya Mungu na amewapa wana wa
Ibrahimu Milele, Waarabu wanapaswa kulijua hilo, Waafrika wanapaswa kulijua
hilo, Wazungu wanapaswa kulijua hilo na zaidi sana Wakristo na kuwa watetezi
wakubwa kwa wayahudi, Yusufu aliipa kipaumbele inchi ya Kanaani kwa sababu ni
inchi waliyoahidiwa na Mungu, makao makuu ya Bwana wetu Yesu Kristo na serikali
ya ufalme wake duniani itatawala kutokea Israel na Yerusalem yakiwa makao makuu
yake, linaweza kuwa jambo la kusikitisha na la kushangaza mtu yeyote yule
akisimama kinyume na Mapenzi ya Mungu kuhusu Israel, waarabu wanapaswa
kukumbuka hilo ya kuwa endapo wanamuheshimu Mungu basi pia wakumbuke kuiacha
Israel kwa wana wa Israel na waarabu kubakia katika mataifa mengine, vinginevyo
Ibrahimu na Isaka na Yakobo na Yusufu watashangaa sana wakati wa Hukumu kukuta
watu wengine wakiidai inchi ya kanaani kuwa yao kinyume na mapenzi ya Mungu
mwenye nguvu sana !
Mathayo 5:34-35
“lakini mimi nawaambia, Usiape kabisa; hata kwa
mbingu, kwa maana ndicho kiti cha enzi cha Mungu; wala kwa nchi, kwa maana
ndiyo pa kuwekea miguu yake; wala kwa Yerusalemu, kwa maana ndio mji wa Mfalme
mkuu.”
4. Kuwaza kuhusu uzima wa milele – Swala la
mifupa ya Yusufu liatukumbusha kuwa maisha yanaendelea hata baada ya kifo, kila
mtu anapaswa kufikiri zaidi ya mazingira ya kawaida kwa sababu hata baada ya
uzima huu uko uzima wa milele. Mungu ameahidi uzima wa milele kwa kila
anayemuamini Yesu Kristo aliyetolewa pale msalabani kwa niaba ya watu wote
watakaoamini ahadi hii ni ya kweli, kwa hiyo katika kuishi kwetu duniani pamoja
na mafanikio yetu yote na umaarufu wetu wote tusisahau kujiwekeza katika uzima
wa milele, Yusufu hakusahau inchi ya ahadi, Hatupaswi kusahau uzima wa umilele,
hatuna budi kuwekeza katika uzima wa milele na kuamini ya kuwa Mungu atatufufua
kutika kwa wafu na kutupa neema ya kuketi katika mkono wake wa kuume katika
ufalme wake
Yohana 3:16 “Kwa maana jinsi hii Mungu aliupenda ulimwengu, hata
akamtoa Mwanawe pekee, ili kila mtu amwaminiye asipotee, bali awe na uzima wa
milele.”
5. Imani ni zaidi ya kawaida ya Muda – Ni
swala la Muda tu, Yusufu hakujali kuwa Israel wataondoka lini Misri lakini
alikuwa na Imani kuwa iko siku Mungu atawatokea, Nasema Mungu atakutokea bila
kujali muda, kila mkristo anapaswa kukumbuka kumsubiri Mungu na kuishi kwa
Imani, Mwamini Mungu biola kujali Muda, mwamini Mungu kuwa atafanya kitu,
mwamini Mungu kuwa atakujibu, mwamini mungu kuwa atatkutokea, mwamini Mungu
kuwa atafanya, Yusufu aliishi kwa Imani, aliamini katika maneno ya Mungu wa
baba yake na babu zake alihesabiwa haki kwa Imani hii
Waebrania 10:38
“Lakini mwenye haki wangu ataishi kwa imani; Naye
akisita-sita, roho yangu haina furaha naye.”
6. Agizo kuu – Agizo la Yusufu ambalo
ilishikwa na kizazi na kizazi cha wana wa Israel ni fundisho kwa kanisa ya kuwa
sisi nasi tunapaswa kulikumbuka agizo la Bwana wetu Yesu Kristo na kuihubiri
injili duniani na kwa kila kiumbe, kama wana wa Israel vizazi na vizazi walilishika
agizo la Yusufu, wakristo hawana budi kuhakikisha wanalishika agizo la Bwana
Yesu, kuhakikisha kuwa kwa nguvu zetu zote tunarithisha injili au habari njema
za wokovu ulioletwa kwetu na Bwana wetu
Yesu Kristo kwa kufa kwake Msalabani, Neno la Mungu ni lazima lienee na
kurithishwa kwa watu wote Duniani na kwa vizazi vyetu vyote kwa kufanya hizi
sisi nasi tutakuwa tumeipandisha mifupa ya Yusufu katika inchi ya kanaani, Musa
hakuisahau mifupa, na hata Yoshua na wazee baada ya Yoshua walihakikisha Mifupa
ya Yusufu inafika Shekemu inchi ya urithi wa wana Israel Efraimu na nusu ya
Manase na Israel wote.
Mathayo
28:18-20 “Yesu akaja kwao, akasema nao, akawaambia,
Nimepewa mamlaka yote mbinguni na duniani. Basi, enendeni, mkawafanye mataifa
yote kuwa wanafunzi, mkiwabatiza kwa jina la Baba, na Mwana, na Roho Mtakatifu;
na kuwafundisha kuyashika yote niliyowaamuru ninyi; na tazama, mimi nipo pamoja
nanyi siku zote, hata ukamilifu wa dahari.”
Na. Rev. Innocent Samuel Kamote
Mkuu wa wajenzi mwenye Hekima!