Jumamosi, 13 Julai 2024

Ninyi si wa ulimwengu huu!

 

Yohana 15:18-21 “Iwapo ulimwengu ukiwachukia, mwajua ya kuwa umenichukia mimi kabla ya kuwachukia ninyi. Kama mngekuwa wa ulimwengu, ulimwengu ungewapenda walio wake; lakini kwa kuwa ninyi si wa ulimwengu, bali mimi naliwachagua katika ulimwengu, kwa sababu hiyo ulimwengu huwachukia. Likumbukeni lile neno nililowaambia, Mtumwa si mkubwa kuliko bwana wake. Ikiwa waliniudhi mimi, watawaudhi ninyi; ikiwa walilishika neno langu watalishika na lenu. Lakini haya yote watawatenda kwa ajili ya jina langu, kwa kuwa hawamjui yeye aliyenipeleka.”




Utangulizi:

Iwapo ulimwengu ukiwachukia, mwajua ya kuwa umenichukia mimi kabla ya kuwachukia ninyi. Yesu alikuwa akimaanisha ulimwengu utatuchukia kabisa, kwa sababu kwanza ulimwengu ulimchukia Kristo, Kwa hiyo kila mwanafunzi wa Yesu Kristo hapaswi kuona jambo hilo kuwa ni jambo geni, Kama ulimwengu ulimchukia Kristo kwa vyovyote vile hauwezi kuwakubali wafuasi wake.

Mathayo 10:22-25 “Nanyi mtakuwa mkichukiwa na watu wote kwa ajili ya jina langu; lakini mwenye kuvumilia hata mwisho, ndiye atakayeokoka. Lakini watakapowafukuza katika mji huu, kimbilieni mwingine; kwa maana ni kweli nawaambia, Hamtaimaliza miji ya Israeli, hata ajapo Mwana wa Adamu. Mwanafunzi hampiti mwalimu wake, wala mtumwa hampiti bwana wake.Yamtosha mwanafunzi kuwa kama mwalimu wake, na mtumwa kuwa kama bwana wake. Ikiwa wamemwita mwenye nyumba Beelzebuli, je! Si zaidi wale walio wa nyumbani mwake?

Ulimwengu unachukizwa sana na watu waliomwamini Yesu na kumfuata, kwa sababu sio wa ulimwengu huu, wakati wanafunzi wa Yesu watatambulikwa kwa upendo wao kwa watu, watu wa ulimwengu huu watajulikana kwa chuki na wivu dhidi ya watu wa Mungu, wanafunzi wa Yesu sio wa ulimwengu huu kwa sababu wameitwa kutoka ulimwenguni kuingia katika ufalme wa mwana wa pendo lake, na kuuacha ufalme wa giza, kwa hiyo tuwapo katika maisha haya sisi wenyeji wetu uko mbinguni, na kwa sababu hiyo mkuu wa ulimwengu huu hawezi kuwa na furaha na watu waliookolewa, kwa sababu wao wameuacha ufalme wake, na hivyo anachukizwa nao, wale walio wa ulimwengu huu wao ndio wenyeji wa ufalme wa shetani au ufalme wa giza na hivyo hauwezi kuweko urafiki kati ya nuru na giza, kweli na uongo, na hivyo hakuwezi kuweko kwa Amani na upendo wa kweli kutoka katika dunia hii inayoongozwa na mfumo wa yule muovu, wala watu wa Mungu wasitarajie ya kuwa dunia itawatendea haki, kwa sababu mfumo wa ulimwengu huu unawatema!, Mfumo wa ulimwengu huu uko chini ya Shetani ambaye kimsingi hana nguvu kama za Bwana wetu Yesu, lakini hata hivyo anatawala mfumo wa uasi wa dunia na kunyunyizia ushawishi wake duniani. 

Yohana 14:30-31 “Mimi sitasema nanyi maneno mengi tena, kwa maana yuaja mkuu wa ulimwengu huu, wala hana kitu kwangu. Lakini ulimwengu ujue ya kuwa nampenda Baba; na kama vile Baba alivyoniamuru; ndivyo nifanyavyo. Ondokeni, twendeni zetu.”       

Tutajifunza somo hili ninyi si wa ulimwengu huu kwa kuzingatia vipengele vitatu vifuatavyo:-


·         Ufahamu kuhusu mkuu wa ulimwengu huu.

·         Kuchukiwa kwa watu wasio wa ulimwengu huu.

·         Jinsi watu wasio wa ulimwengu huu wanavyopaswa kuishi.


Ufahamu kuhusu mkuu wa ulimwengu huu.

Ni muhimu kufahamu kuwa Shetani ana majina mengi yanayomtambulisha kama mwenye mamlaka na ulimwengu huu, Katika maandiko Yesu anamtaja kama mkuu wa ulimwengu huu Katika

Yohana 14:30 Mimi sitasema nanyi maneno mengi tena, kwa maana yuaja mkuu wa ulimwengu huu, wala hana kitu kwangu.  

Katika biblia ya kiingereza maneno hayo yanasomeka “I will not speak with you much longer, for the PRINCE OF THIS WORLD is coming. He has no hold on me” kwa hiyo shetani anaitwa mkuu wa ulimwengu huu, au kwa jina lingine, mungu wa dunia hii angalia au mfalme wa dunia hii, Kwa hiyo kimsingi Shetani ni mtawala wa dunia hii.

2Wakorintho 4:3-4 “Lakini ikiwa injili yetu imesitirika, imesitirika kwa hao wanaopotea; ambao ndani yao mungu wa dunia hii amepofusha fikira zao wasioamini, isiwazukie nuru ya injili ya utukufu wake Kristo aliye sura yake Mungu.”  

Unaona katika andiko hili Shetani anaitwa MUNGU WA DUNIA HII.  Aidha katika maandiko mengine Shetani anaitwa MFALME WA UWEZO WA ANGA “The Prince of the air” hili unaweza kuliona katika kitabu cha Waefeso

Waefeso 2:1-3 Nanyi mlikuwa wafu kwa sababu ya makosa na dhambi zenu; ambazo mliziendea zamani kwa kuifuata kawaida ya ulimwengu huu, na kwa kumfuata mfalme wa uwezo wa anga, roho yule atendaye kazi sasa katika wana wa kuasi; ambao zamani, sisi sote nasi tulienenda kati yao, katika tamaa za miili yetu, tulipoyatimiza mapenzi ya mwili na ya nia, tukawa kwa tabia yetu watoto wa hasira kama na hao wengine.”

Hii ina maana gani? Ni muhimu kufahamu kuwa katika lugha ya Kiyunani neno Prince of this world, mkuu wa ulimwengu huu, god of this age, mungu wa dunia hii, ruler of the kingdom of air, mkuu wa uweza wa anga huyu kwa kwa kiyunani anaitwa KOSMOKRATOR  kwa kiingereza COSMOCRATOR  maana yake RULER OF THE WORLD  neno hilo Kosmokrator limetokana na lugha ya asili ya dini za kipagani hususani Wanostiki na Wamarcion wakimaanisha ni lugha ya kiufundi ya kumtambulisha Shetani kutokana na kazi zake za uendeshaji wa ulimwenguni kwa hivyo utaweza kuona jina hilo Kosmokrator ni mkuu wa anga, au mtawala wa dunia hii au mwenye ushawishi wa akili na tabia na mwenendo, malengo, matumaini, falsafa, elimu, biashara, mawazo, fikra, ujasusi, udhibiti, na utaratibu wa kila kitu hapa duniani. Katika ulimwengu wa watu wasiookolewa ni muhimu ikafahamika wazi kuwa ulimwengu uko chini ya huyu Kosmokrator yaani Shetani. Kwa hiyo mifumo yote ya uendeshaji wa dunia hii na ushawishi wake uko chini ya mkuu wa anga anayetenda kazi sasa kwa wana wa kuasi.

Yohana 12:31Sasa hukumu ya ulimwengu huu ipo; sasa mkuu wa ulimwengu huu atatupwa nje”. Kwa hiyo Mkuu wa anga anaitwa Kosmokrator wakati ulimwengu na mfumo wake wote unaitwa Kosmos,  Mapambo  na vipodozi vyote vinaitwa Kosmetikos, yaani art of beautification kwa hiyo neno Kosmos lilitumika pia kuelezea mfumo wa ulimwengu na ndio maana nyakati za kanisa la Kwanza mtu aliyeonyesha kuupenda sana ulimwengu alifikiriwa pia amekuwa adui wa Mungu.

Yakobo 4:4 . “Enyi wazinzi, hamjui ya kwamba kuwa rafiki wa dunia ni kuwa adui wa Mungu? Basi kila atakaye kuwa rafiki wa dunia hujifanya kuwa adui wa Mungu.”

Kwa hiyo Maandiko yanapomtaja shetani kama mkuu wa ulimwengu huu, yanafunua ule ukweli ya kuwa katika ulimwengu huu wako watu wanaoongozwa na mfumo wake na wanaofuata mfumo wake na wako chini ya mfumo huo na pia wale waliomwamini Yesu wako katika mfumo mwingine wanaishi duniani lakini wakiwa wamehamishwa katika ufalme huo wa giza na kuingizwa katika mfumo wa ufalme wa mwana wa pendo lake yaani Pendo la Mungu. Hii ina maana gani ina maana ya kuwa watu waliookoka hawako chini ya utawala wa shetani, kwa hiyo wao sio wa ulimwengu huu

Wakolosai 1:13-14 “Naye alituokoa katika nguvu za giza, akatuhamisha na kutuingiza katika ufalme wa Mwana wa pendo lake; ambaye katika yeye tuna ukombozi, yaani, msamaha wa dhambi;”             

Kuchukiwa kwa watu wasio wa ulimwengu huu

Kwa sababu mtawala wa ulimwengu huu yaani shetani amepokonywa mateka yaani watu waliookolewa, wakahamishwa katika ufalme wa Mungu, Shetani amekuwa adui mkubwa sana wa watu wa Mungu na anachukizwa nao sana. Yesu akilijua hilo anatuwekea wazi, kuwa nasi tutachukiwa sana na ulimwengu na hii ni kwa sababu ulimwengu huo huo haukumkubali Bwana Yesu.

Yohana 15:18-21 “Iwapo ulimwengu ukiwachukia, mwajua ya kuwa umenichukia mimi kabla ya kuwachukia ninyi.Kama mngekuwa wa ulimwengu, ulimwengu ungewapenda walio wake; lakini kwa kuwa ninyi si wa ulimwengu, bali mimi naliwachagua katika ulimwengu, kwa sababu hiyo ulimwengu huwachukia. Likumbukeni lile neno nililowaambia, Mtumwa si mkubwa kuliko bwana wake. Ikiwa waliniudhi mimi, watawaudhi ninyi; ikiwa walilishika neno langu watalishika na lenu. Lakini haya yote watawatenda kwa ajili ya jina langu, kwa kuwa hawamjui yeye aliyenipeleka.”

Yesu anaendelea kukazia kuwa mtumwa si mkubwa kuliko Bwana wake, maana yake hali ile ile ambayo watu wanamfanyia Bwana wako ni hali ile ile ndiyo watakayo mfanyia mtumwa wake, Hali anayofanyiwa mwenye nyumba, ndiyo hiyo hiyo watakayofanyiwa wale wa nyumbani mwake, ikiwa walimsulubisha Bwana wetu Yesu Kristo hali kadhalika wanafunzi wa Yesu Kristo watasulubiwa na kupata mateso mengi, kwa sababu nao wataishi na kufanya kazi kama zile zile alizozifanya Yesu Kristo, Yesu ni Nuru ya ulimwengu hali kadhalika watu wa Mungu ni nuru ulimwenguni, na watu wa dunia hii wanapenda giza na ndio maana walimsulubisha Yesu Kristo wote wapendao kuishi kwa hali itokanayo na Kristo Yesu wataudhiwa

2Timotheo 3:10-12 “Bali wewe umeyafuata mafundisho yangu, na mwenendo wangu, na makusudi yangu, na imani, na uvumilivu,na upendo, na saburi; tena na adha zangu na mateso, mambo yaliyonipata katika Antiokia, katika Ikonio, na katika Listra, kila namna ya adha niliyoistahimili, naye Bwana aliniokoa katika hayo yote.Naam, na wote wapendao kuishi maisha ya utauwa katika Kristo Yesu wataudhiwa.”

Kwa hiyo wapenzi msione kuwa ni ajabu watu waliompokea Yesu, wakikutana na vikwazo vingi, wakikataliwa, wakidharauliwa, wakichukiwa na dunia, wakifanyiwa fitina, wakizushiwa, wakidhulumiwa, wakifanyiwa hila, wakihuzunishwa kwa namna mbalimbali, wakibaniwa, wakisalitiwa, wakitafuta kuuawa, Wakristo watapata mateso na uonevu kwa sababu ya Imani yao, watakutana na vipingamizi kwa sababu ya mifumo ya kipinzani ya dunia hii,  watatengwa na jamii na familia zao na dini zao,  kwa sababu hawakubaliki na mfumo wa ulimwengu huu, mifumo ya Kosmokrator iko kuanzia ngazi ya ulimwengu, mabara, mataifa, mikoa, wilaya na kila kijiji, na katika kila eneo nguvu ya ushawishi wa mkuu wa anga katika eneo hilo atapingana vikali na wakristo wa eneo husika akitumia aina ya ushawishi wake, katika eneo husika kuwapiga vita wakristo na vita hii iko katika ulimwengu wa roho.

Waefeso 6:10-13 “Hatimaye, mzidi kuwa hodari katika Bwana na katika uweza wa nguvu zake. Vaeni silaha zote za Mungu, mpate kuweza kuzipinga hila za Shetani. Kwa maana kushindana kwetu sisi si juu ya damu na nyama; bali ni juu ya falme na mamlaka, juu ya wakuu wa giza hili, juu ya majeshi ya pepo wabaya katika ulimwengu wa roho.Kwa sababu hiyo twaeni silaha zote za Mungu, mpate kuweza kushindana siku ya uovu, na mkiisha kuyatimiza yote, kusimama.”

Katika vita hivi na mfumo wa ulimwengu huu wakristo hawapaswi kuogopa kwa sababu mkuu wa ulimwengu huu hana kitu kwa Yesu Kristo na zaidi ya yote neno la Mungu limetuthibitishia wazi ya kuwa aliye ndani yetu ni mkuu kuliko yeye aliye ulimwenguni.

1Yohana 4:4-6 “Ninyi, watoto wadogo, mwatokana na Mungu nanyi mmewashinda, kwa sababu yeye aliye ndani yenu ni mkuu kuliko yeye aliye katika dunia. Hao ni wa dunia; kwa hiyo wanena ya dunia na dunia huwasikia Sisi twatokana na Mungu. Yeye amjuaye Mungu atusikia; yeye asiyetokana na Mungu hatusikii. Katika hili twamjua Roho wa kweli, na roho ya upotevu.”

Watu wa Mungu wanapaswa kuwa hodari Duniani, wanapaswa kuwa na imani, wanapaswa kuwa wapambanaji, wanapaswa kutumia silaha zote walizopewa kushughulika na wakuu wa anga katika mazingira yetu na kuharibu nguvu ya ushawishi inayotenda kazi kulingana na mazingira yetu na kwa kufanya hivyo tutapata upenyo, aidha kila tunapoendelea kuihubiri injili tunaendelea kumpa shida mkuu wa anga na kumpokonya mateka wake.  

Jinsi watu wasio wa ulimwengu huu wanavyopaswa kuishi

1.       Kuishi kwa kiasi chini ya neema ya Mungu –  kila mtu aliyeokolewa, aliokolewa kwa neema na kwa sababu hiyo hiyo hatuna budi kuendelea kuishi kwa neema, shetani hatataka mtu aliyeokolewa kwa neema aendelee kufurahia neema hiyo na kwa vyovyote vile atatupandikizia falsafa za dunia hii za kututaka tupate kibali kwa Mungu kwa njia ya tendo au matendo fulani, ni muhimu kukumbuka na kufahamu kuwa dini zote za uongo duniani zina mfumo wa kukutaka upate kibali kwa Mungu kwa njia ya matendo, Uislamu unakazia matendo mema, Budha, Hindu, Confucianism, Sikhism,Taoism, Shintoism, Judaism n.k  au kuupata wokovu kwa kazi, au kwa matendo mema, jambo hilo ni kinyume na kweli ya Mungu kwa sababu wokovu, na uzima wa milele ni zawadi kutoka kwa Mungu, ni kipawa ni karama ambayo kamwe haitokani na nafsi zetu wala matendo yetu  bali neema ya Mungu, tunaokolewa kwa neema na tunaendelea kuishi kwa neema tukimpendeza na kusaidiwa na Roho wake Mtakatifu kumpendeza Mungu kwa neema yake.

 

Waefeso 2:8-9 “Kwa maana mmeokolewa kwa neema, kwa njia ya imani; ambayo hiyo haikutokana na nafsi zenu, ni kipawa cha Mungu; wala si kwa matendo, mtu awaye yote asije akajisifu.”

 

2.       Kuishi kwa Imani isiyotikisika -  watu wa Mungu watapitia dhiki na mateso mengi lakini mateso yao au yetu isiwe sababu ya kuyumba wala kuogopa mateso, watakatifu waliotutangulia waliishi kwa Imani isiyotetereka hata wakati wa majaribu Makubwa walichagua kupata mateso pamoja na watu wa Mungu badala ya kujifurahisha kwa anasa huku wakiikana Imani, Badala yake walikaza kumwangalia Mungu kwa matokeo.

 

Waebrania 11:24-27 “Kwa imani Musa alipokuwa mtu mzima, akakataa kuitwa mwana wa binti Farao; akaona ni afadhali kupata mateso pamoja na watu wa Mungu kuliko kujifurahisha katika dhambi kwa kitambo; akihesabu ya kuwa kushutumiwa kwake Kristo ni utajiri mkuu kuliko hazina za Misri; kwa kuwa aliyatazamia hayo malipo. Kwa imani akatoka Misri, asiogope ghadhabu ya mfalme; maana alistahimili kama amwonaye yeye asiyeonekana.”

               

3.       Kuishi kwa uvumilivu na ustahimilivu - Hakuna jambo linauma kama kuteseka ili hali hujakosea kitu, hata hivyo maandiko yanatutaka kutokuogopa na kutokufadhaika na badala yake kuendelea kustahimili tukivumilia mateso na shida huku tukiiga mfano wa wenzetu ambao walidhihakiwa, walipigwa mijeledi, walifungwa kwa minyororo, walitiwa gerezani, walipigwa kwa mawe, walikatwa kwa misumeno lakini kwaajili ya Imani katika Mungu na upendo wao kwa Kristo walikubali hata kuuawa kuliko kumkana Bwana.

 

1Petro 3:14 “Lakini mjapoteswa kwa sababu ya haki mna heri. Msiogope kutisha kwao, wala msifadhaike; bali mtakaseni Kristo Bwana mioyoni mwenu.”

 

Waebrania 11:35-38 “Wanawake walipokea wafu wao waliofufuliwa. Lakini wengine waliumizwa vibaya hata kuuawa, wasikubali ukombozi, ili wapate ufufuo ulio bora; wengine walijaribiwa kwa dhihaka na mapigo, naam, kwa mafungo, na kwa kutiwa gerezani; walipigwa kwa mawe, walikatwa kwa misumeno, walijaribiwa, waliuawa kwa upanga; walizunguka-zunguka wakivaa ngozi za kondoo na ngozi za mbuzi; walikuwa wahitaji, wakiteswa, wakitendwa mabaya; (watu ambao ulimwengu haukustahili kuwa nao), walikuwa wakizunguka-zunguka katika nyika na katika milima na katika mapango na katika mashimo ya nchi.”

 

4.       Kutokuifuta namna ya dunia hii –  Nyakati za kanisa la Kwanza wanafunzi wa Bwana walijitolea kuishi maisha ya uadilifu na kujitofautisha sana na mifumo ya ulimwengu huu, neno namna ya dunia hii maana yake  ni kushi chini ya kiwango, au chini ya uadilifu neno linalotumika hapo standard of this world au Pattern of this world kwa kiyunani suschēmatizo yaani Fashion au design au model, au alike  kwa hiyo lazima watu wa Mungu wajitofautishe na watu wa dunia hii katika mtindo wao wa maisha, neno la Mungu linaagiza hivyo na neema ya Mungu itatusaidia kutufundisha namna ya kuishi zaidi ya kiwango cha dunia hii nje ya muundo 

 

Warumi 12:2 “Wala msiifuatishe namna ya dunia hii; bali mgeuzwe kwa kufanywa upya nia zenu, mpate kujua hakika mapenzi ya Mungu yaliyo mema, ya kumpendeza, na ukamilifu.”

 

Tito 11:11-12 “Maana neema ya Mungu iwaokoayo wanadamu wote imefunuliwa; nayo yatufundisha kukataa ubaya na tamaa za kidunia; tupate kuishi kwa kiasi, na haki, na utauwa, katika ulimwengu huu wa sasa;”           

 

5.       Kuonyesha upendo uzidio – Pamoja na changamoto ambazo ulimwengu utatuletea kutokana na mfumo wake watu wa Mungu ambao wao sio wa ulimwengu huu wanapaswa kuendelea kuonyesha upendo mkubwa kwa wengine hususani wale wanaotuchukia na kufikiriwa kuwa ni adui zetu, kuwapenda maadui au kuwaombea wale wanaotuchukia na kuishi kwa kuonyesha upendo uzidio na hii sio hali ya kawaida kwa ulimwengu huu kwa kufanya hivyo tutawavuta wale watu wa ulimwengu huu kuona na kujua ya kuwa kuna kitu cha ziada katika Kristo.

 

Mathayo 5:43-46 “Mmesikia kwamba imenenwa, Umpende jirani yako, na, Umchukie adui yako; lakini mimi nawaambia, Wapendeni adui zenu, waombeeni wanaowaudhi, ili mpate kuwa wana wa Baba yenu aliye mbinguni; maana yeye huwaangazia jua lake waovu na wema, huwanyeshea mvua wenye haki na wasio haki. Maana mkiwapenda wanaowapenda ninyi mwapata thawabu gani? Hata watoza ushuru, je! Nao hawafanyi yayo hayo?

 

Matendo 7:58-60 “wakamtoa nje ya mji, wakampiga kwa mawe. Nao mashahidi wakaweka nguo zao miguuni pa kijana mmoja aliyeitwa Sauli. Wakampiga kwa mawe Stefano, naye akiomba, akisema, Bwana Yesu, pokea roho yangu. Akapiga magoti, akalia kwa sauti kuu, Bwana, usiwahesabie dhambi hii. Akiisha kusema haya akalala. Na Sauli alikuwa akiona vema kwa kuuawa kwake.”

 

6.       Kuvaa silaha zote za Mungu - watu wasio wa ulimwengu huu wako vitani, na hivyo maandiko yanaagiza kuwa wavae silaha zote za Mungu kama inavyoelezwa katika kitabu cha Waefeso

 

Waefeso 6:11-18 “Vaeni silaha zote za Mungu, mpate kuweza kuzipinga hila za Shetani. Kwa maana kushindana kwetu sisi si juu ya damu na nyama; bali ni juu ya falme na mamlaka, juu ya wakuu wa giza hili, juu ya majeshi ya pepo wabaya katika ulimwengu wa roho. Kwa sababu hiyo twaeni silaha zote za Mungu, mpate kuweza kushindana siku ya uovu, na mkiisha kuyatimiza yote, kusimama. Basi simameni, hali mmejifunga kweli viunoni, na kuvaa dirii ya haki kifuani, na kufungiwa miguu utayari tupatao kwa Injili ya amani; zaidi ya yote mkiitwaa ngao ya imani, ambayo kwa hiyo mtaweza kuizima mishale yote yenye moto ya yule mwovu. Tena ipokeeni chapeo ya wokovu, na upanga wa Roho ambao ni neno la Mungu; kwa sala zote na maombi mkisali kila wakati katika Roho, mkikesha kwa jambo hilo na kudumu katika kuwaombea watakatifu wote;”

 

Hiyo inaashiria kuwa tunapaswa kuwa tayari katika hali ya kiroho kukabiliana na utendaji wa mkuu wa anga na nguvu zake za ushawishi na uovu duniani, ili kujilinda katika vita tuliyonayo kiroho, Kila mkristo kwa kuwa anajua ya kuwa yuko katikati ya adui anapaswa kuwa na msimamo thabiti katika Imani na kupambana kwa ujasiri kwa neema ya Mungu kuweza kuzishinda hila zote za adui zinazozuia ukuaji wa ufalme wa Mungu kwa njia ya injili. Wewe mwenyewe pia ukiyalinda maisha yako kwa kuwa uko vitani, uongezewe neema!

Na Rev. Innocent Samuel Kamote

Mkuu wa wajenzi mwenye Hekima!      

Jumatatu, 8 Julai 2024

Wakamshinda kwa damu ya Mwana-Kondoo


Ufunuo 12:9-11 “Yule joka akatupwa, yule mkubwa, nyoka wa zamani, aitwaye Ibilisi na Shetani, audanganyaye ulimwengu wote; akatupwa hata nchi, na malaika zake wakatupwa pamoja naye. Nikasikia sauti kuu mbinguni, ikisema, Sasa kumekuwa wokovu, na nguvu, na ufalme wa Mungu wetu, na mamlaka ya Kristo wake; kwa maana ametupwa chini mshitaki wa ndugu zetu, yeye awashitakiye mbele za Mungu wetu, mchana na usiku. Nao wakamshinda kwa damu ya Mwana-Kondoo, na kwa neno la ushuhuda wao; ambao hawakupenda maisha yao hata kufa.”                



Utangulizi:

Ni muhimu kufahamu kuwa moja ya Silaha yenye nguvu kubwa sana kuliko zote duniani katika ulimwengu wa roho ni pamoja na damu ya Yesu. Bila damu ya Yesu hata Imani yetu isingeweza kuendelea kuwepo duniani, Damu ya Yesu Kristo inawakilisha kila kitu ambacho Yesu Kristo alikifanya pale msalabani, Kuhesabiwa haki, ukombozi, upatanisho, Msamaha, utakaso,Uhuru kutoka katika adhabu na hasira ya Mungu, na agano, Yote haya ni marupurupu yanayopatikana katika damu ya Yesu, kwa msingi huo basi, kuwa na ufahamu kuhusu utendaji wa Damu ya Yesu ni muhimu sana kwetu kama wakristo, kwaajili ya kuelewa haki zetu zipatikanazo kwa Damu ya Yesu ili tuweze kuwa na ushindi siku zote za maisha yetu. Tutajifunza somo hili Wakamshinda kwa damu ya Mwana-Kondoo kwa kuzingatia vipengele vitatu vifuatavyo:-

·         Kazi ya damu katika nyakati za agano la kale.

·         Kazi ya Damu ya Yesu katika nyakati za agano jipya.

·         Wakamshinda kwa damu ya Mwanakondoo.

Kazi ya damu katika nyakati za agano la kale.

Ni muhimu kufahamu, kwamba ili tuweze kuelewa vema Kazi ya Damu ya Yesu Kristo, uweza wake na nguvu zake ni muhimu kwetu kuchukua muda kidogo, kujifunza matumizi ya damu jinsi yalivyokuwa nyakati za agano la kale, ili tuweze kujua utendaji huo namna unavyokuwa sasa katika agano jipya, Nyakati za agano la kale Damu zilizotumika zilikuwa damu za wanyama na kazi ya damu ilikuwa ni moja ya ishara muhimu sana ya msingi sana katika ibada za agano la kale kwa sababu zifuatazo:-

1.       Ilikuwa sehemu muhimu ya dhabihu ya upatanisho – Damu ilikuwa ni kiini muhimu cha ibada za dhabihu ambayo iliagizwa katika torati ya Musa. Dhabihu/Kafara za wanyama zilikuwa zinatolewa na damu ya wanyama hao zilikuwa zinanyunyizwa katika madhabahu kama njia ya upatanisho kwaajili ya dhambi.

 

Mambo ya walawi 17:10-12 “Kisha mtu awaye yote wa nyumba ya Israeli, au miongoni mwa hao wageni wakaao kati yao, atakayekula damu, ya aina yo yote, nitakunja uso wangu juu ya mtu huyo alaye damu, nami nitamkatilia mbali na watu wake. Kwa kuwa uhai wa mwili u katika hiyo damu; nami nimewapa ninyi hiyo damu juu ya madhabahu, ili kufanya upatanisho kwa ajili ya nafsi zenu; kwani ni hiyo damu ifanyayo upatanisho kwa sababu ya nafsi. Kwa hiyo naliwaambia wana wa Israeli, Hapana mtu miongoni mwenu aliye na ruhusa kula damu, wala mgeni aketiye kati yenu asile damu.”

 

Damu ilikuwa ni nyenzo muhimu ya kufanya upatanisho, yaani kwa kuwa mwanadamu anapotenda dhambi mara moja dhambi huharibu uhusiano wao na Mungu na kudai kifo, kwanini kifo kwa sababu Mungu alikuwa amemuonya mwanadamu wa kwanza kuwa siku atakapofanya dhambi hakika atakufa, kwa hiyo Damu kama uhai inamwagika kwa niaba ya mwanadamu na kugeuka kuwa sadaka ya kumpatanisha mwanadamu na Mungu, Kwa hiyo Damu hufanya kazi ya upatanisho. nami nimewapa ninyi hiyo damu juu ya madhabahu, ili kufanya upatanisho kwa ajili ya nafsi zenu; Nafsi za wanadamu hupatanishwa na Mungu kwa njia ya Damu, uadui wetu na Mungu unapoozwa au kufunikwa kwa sababu ya Damu.

 

Upatanisho ni nini? neno upatanisho katika Biblia ya kiingereza limetumika neno atonement karibu mara 71 katika lugha ya kiebrania neno atonement linasomeka kama neno Kphar  ambalo hutamkwa Kaw-far sawa na neno la Kiswahili KAFARA ambalo maana yake ni kuwaleta pamoja watu waliokuwa maadui au waliotengana kwa kuwapatanishan, kwa hiyo neno atonement  at- one- ment  is reparation, au reconciliation ambalo maana yake ni bringng together into harmony of those who heve been separated or enemies, kwa hiyo damu ina nguvu ya kuvunja uadui  uiotokana na dhambi zetu kati yetu sisi wanadamu na Mungu na kumpa Mungu nafuu, uhalali, kibali, cha kukubali kutuachilia, na kuwa rafiki yetu.

 

2.       Alama muhimu ya agano – Damu katika agano la kale vilevile ilitumika kama alama ya agano kati ya watu na Mungu, Damu iliponyunyizwa juu ya watu iliwafanya wanadamu, kupata kibali kwa Mungu na kuzuia hasira za Mungu zisiwake juu ya watu wake, Damu iliwafanya watu hao kuwa mali ya Mungu, na kuwa na urafiki wa kudumu na Mungu!

 

Kutoka 24:7-11 “Kisha akakitwaa kitabu cha agano akakisoma masikioni mwa watu; wakasema, Hayo yote aliyoyanena BWANA tutayatenda, nasi tutatii. Musa akaitwaa ile damu, akawanyunyizia watu, akasema, Hii ndiyo damu ya agano alilolifanya BWANA pamoja nanyi katika maneno haya yote. Ndipo akakwea juu, Musa, na Haruni, na Nadabu, na Abihu, na watu sabini miongoni mwa wazee wa Israeli; wakamwona Mungu wa Israeli; chini ya miguu yake palikuwa na kama sakafu iliyofanyizwa kwa yakuti samawi, kama zile mbingu zenyewe kwa usafi wake. Naye hakuweka mkono wake juu ya hao wakuu wa wana wa Israeli; nao wakamwona Mungu, wakala na kunywa.”

 

Agano ni nini? Neno agano katika biblia ya kiingereza linatumika neno Covenant ambalo limetumiwa katika biblia mara 264 katika lugha ya kiibrania neno Covenant linatumika neno Beriyth ambalo maana yake ni muungano wa ushirikiano wa kirafiki au kisiasa confederation au alliancethe permanent union  yaani muungano wa kudumu mfano nchi zipatazo 50 au zaidi za America zilikubaliana kuwa kitu kimoja na kupatikana United States of America, kwa hiyo Damu husababisha watu na Mungu kuwa na serikali moja, jeshi moja, na ushirikiano wa kudumu wa kirafiki na kisiasa na Mungu

 

3.       Alama ya utakaso na wakfu – Damu katika agano la kale ilitumika kama alama ya utakaso na kuweka wakfu kwa Bwana, Mfano makuhani wale waliochaguliwa kwa kazi ya utumishi walitakaswa na kuwekwa wakfu ili watumikie Mungu kwa damu ya wanyama angalia:-

 

Kutoka 29:20-21 “Kisha utamchinja kondoo, na kuitwaa damu yake, na kuitia katika ncha ya sikio la Haruni la upande wa kuume, na katika ncha za masikio ya kuume ya wanawe, na katika vyanda vya gumba vya mikono yao ya kuume, na katika vidole vikuu vya miguu yao ya kuume, na kuinyunyiza hiyo damu katika madhabahu kuizunguka kando-kando. Kisha twaa katika hiyo damu iliyo juu ya madhabahu, na katika hayo mafuta ya kutiwa, na kumnyunyizia Haruni, juu ya mavazi yake, na wanawe, na mavazi yao pia, pamoja naye; naye atatakaswa, na mavazi yake, na wanawe, na mavazi ya wanawe, pamoja naye.”

 

Sio hivyo tu Damu ilitumika kama nyenzo katika ibada kama njia ya kusafisha na kutakasa kwa kutumia damu. Na pasipo kumwagika Damu hakuna ondoleo la Dhambi.

 

Waebrania 9:19-22 “Maana kila amri ilipokwisha kunenwa na Musa kwa hao watu wote, kama ilivyoamuru sheria, aliitwaa damu ya ndama na ya mbuzi, pamoja na maji na sufu nyekundu na hisopo, akakinyunyizia kitabu chenyewe, na watu wote, akisema, Hii ni damu ya agano mliloamriwa na Mungu. Na ile hema nayo na vyombo vyote vya ibada alivinyunyizia damu vivyo hivyo. Na katika Torati karibu vitu vyote husafishwa kwa damu, na pasipo kumwaga damu hakuna ondoleo.”          

 

Kutakaswa au kuwekwa wakfu ni kitendo cha kutengwa na Mungu kwaajili ya Mungu na kufanywa mtakatifu jambo ambalo pia linafanywa na Damu ya Yesu

 

Waebrania 13:11-12 “Maana wanyama wale ambao damu yao huletwa ndani ya patakatifu na kuhani mkuu kwa ajili ya dhambi, viwiliwili vyao huteketezwa nje ya kambi. Kwa ajili hii Yesu naye, ili awatakase watu kwa damu yake mwenyewe, aliteswa nje ya lango.”

 

4.       Alama ya Pasaka – Ukombozi mzima wa wana wa Israel kutokuuawa kwa wazaliwa wao wa Kwanza na kuruhusiwa kutoka utumwani, na kumtiisha Farao kulikuwa ni matokeo ya kazi ya Damu ya ukombozi ambayo mwanakondoo wa Pasaka alichinjwa na damu yake ikanyunyizwa katika miimo ya milango, na kwa tendo hilo na utii wake wana wa Israel waliokolewa kutoka pigo la mwisho, walipata ulinzi na waliokolewa kutoka utumwani na kutembea kwa ujeuri kurudi katika inchi yao.

 

Kutoka 12:3-13 “Semeni na mkutano wote wa Israeli, mkawaambie, Siku ya kumi ya mwezi huu kila mtu atatwaa mwana-kondoo, kwa hesabu ya nyumba ya baba zao, mwana-kondoo kwa watu wa nyumba moja; na ikiwa watu wa nyumba ni wachache kwa mwana-kondoo, basi yeye na jirani yake aliye karibu na nyumba yake na watwae mwana-kondoo mmoja, kwa kadiri ya hesabu ya watu; kwa kadiri ya ulaji wa kila mtu, ndivyo mtakavyofanya hesabu yenu kwa yule mwana-kondoo. Mwana-kondoo wenu atakuwa hana ila, mume wa mwaka mmoja; mtamtwaa katika kondoo au katika mbuzi. Nanyi mtamweka hata siku ya kumi na nne ya mwezi ule ule; na kusanyiko lote la mkutano wa Israeli watamchinja jioni. Nao watatwaa baadhi ya damu yake na kuitia katika miimo miwili na katika kizingiti cha juu, katika zile nyumba watakazomla. Watakula nyama yake usiku ule ule, imeokwa motoni, pamoja na mkate usiotiwa chachu; tena pamoja na mboga zenye uchungu. Msiile mbichi, wala ya kutokoswa majini, bali imeokwa motoni; kichwa chake pamoja na miguu yake, na nyama zake za ndani.  Wala msisaze kitu chake cho chote hata asubuhi, bali kitu kitakachosalia hata asubuhi mtakichoma kwa moto. Tena mtamla hivi; mtakuwa mmefungwa viuno vyenu, mmevaa viatu vyenu miguuni, na fimbo zenu mikononi mwenu; nanyi mtamla kwa haraka; ni pasaka ya BWANA. Maana nitapita kati ya nchi ya Misri usiku huo, nami nitawapiga wazaliwa wa kwanza wote katika nchi ya Misri, wa mwanadamu na wa mnyama; nami nitafanya hukumu juu ya miungu yote ya Misri; Mimi ndimi BWANA. Na ile damu itakuwa ishara kwenu katika zile nyumba mtakazokuwamo; nami nitakapoiona ile damu, nitapita juu yenu, lisiwapate pigo lo lote likawaharibu, nitakapoipiga nchi ya Misri.”

 

Neno Pasaka katika lugha kiingereza linatumika neno Passover sawa na neno la kiibrania Pesach na kiswahili Pasaka neno hilo katika tafasiri ya kiingereza linaweza kutamkwa “passed over” maana yake Skipping au Passing over yaani Mungu alikuwa napita katika inchi ya Misri kuhukumu kwa kuua wazaliwa wa kwanza wa kila mlango usiokuwa na alama ya Damu, lakini kila mlango uliokuwa na akama ya damu aliiruka au kupita juu yake bila kuhukumu, kwa sababu damu ilifanya tukio liitwalo Propitiation yaani kuacha kukasirikia au kuhukumu kwa hoyo damu husababisha tuache kukasirikiwa na Mungu.

 

5.       Alama ya uzima na mauti – Damu katika agano la kale ilitumiwa na Mungu kama alama ya uzima na mauti, Damu ilitumika kuyatakasa maisha ya mwanadamu, na ndio maana Mungu aliwakataza wana wa Israel na wanadamu wote mpaka leo kutokuitumia damu kama chakula kwa sababu inawakilisha uhai, Damu ilikuwa ikitolewa kama mbadala wa dhambi yaani uhai unatolewa ili mwingine apate uzima asiuawe.

 

Walawi 17:10-14 “Kisha mtu awaye yote wa nyumba ya Israeli, au miongoni mwa hao wageni wakaao kati yao, atakayekula damu, ya aina yo yote, nitakunja uso wangu juu ya mtu huyo alaye damu, nami nitamkatilia mbali na watu wake. Kwa kuwa uhai wa mwili u katika hiyo damu; nami nimewapa ninyi hiyo damu juu ya madhabahu, ili kufanya upatanisho kwa ajili ya nafsi zenu; kwani ni hiyo damu ifanyayo upatanisho kwa sababu ya nafsi. Kwa hiyo naliwaambia wana wa Israeli, Hapana mtu miongoni mwenu aliye na ruhusa kula damu, wala mgeni aketiye kati yenu asile damu. Mtu ye yote aliye wa wana wa Israeli, au wa hao wageni wakaao kati yenu, ambaye amemshika mnyama, au ndege ambaye huliwa, katika kuwinda kwake; atamwaga damu yake, na kuifunika mchanga. Kwa maana kuliko huo uhai wa mnyama, hiyo damu yake ni moja na uhai wake; kwa hiyo naliwaambia wana wa Israeli, Msile damu ya mnyama wa aina yo yote; kwa kuwa uhai wa wanyama wote ni katika hiyo damu yake; atakayeila awaye yote atakatiliwa mbali.”             

 

Kwa hiyo unaweza kuona kuwa nyakati za agano la kale Damu ilikuwa ni alama au ishara muhimu kwaajili ya upatanisho, agano, utakaso, maisha na uhai, na ilitumika kumpa mwanadamu haki zake zote kutoka kwa Mungu ambazo alizipoteza kwa sababu ya kuweko kwa dhambi, damu ilisimama mahali palipobomoka kuwapatanisha wanadamu kwa Mungu na lakini hata hivyo ilikuwa ni alama au ishara inayoonekana na ambayo ilisimama kama kivuli cha damu halisi na safi na kamilifu itakayokamilisha maswala hayo yote katika agano jipya.

Kazi ya Damu ya Yesu katika nyakati za agano jipya

1.        Damu ya Yesu inatupa Ondoleo la dhambi - Damu aliyoimwaga Bwana Yesu kupitia mateso yake pale msalabani inafanya kazi ya kufuta, kuondoa, kumaliza kabisa, kulipa kabisa Deni la dhambi, Damu ya Yesu inazifutilia mbali dhambi zote ambazo tumewahi kuzifanya jana, leo na hata milele.

 

Mathayo 26:27-28 “Akakitwaa kikombe, akashukuru, akawapa, akisema, Nyweni nyote katika hiki; kwa maana hii ndiyo damu yangu ya agano, imwagikayo kwa ajili ya wengi kwa ondoleo la dhambi.”

 

Ufunuo 1:5-6 “tena zitokazo kwa Yesu Kristo, shahidi aliye mwaminifu, mzaliwa wa kwanza wa waliokufa, na mkuu wa wafalme wa dunia. Yeye atupendaye na kutuosha dhambi zetu katika damu yake, na kutufanya kuwa ufalme, na makuhani kwa Mungu, naye ni Baba yake; utukufu na ukuu una Yeye hata milele na milele. Amina.”

               

1Yohana 1:7 “bali tukienenda nuruni, kama yeye alivyo katika nuru, twashirikiana sisi kwa sisi, na damu yake Yesu, Mwana wake, yatusafisha dhambi yote.”

 

Neno Ondoleo la dhambi linalotumika katika Mathayo 26:28  katika biblia ya kiingereza linasomeka kama neno for remission of sins yaani katika kiyunani ni Aphesis ambalo maana yake ni Msamaha wa dhambi, au kufutiwa deni kwa kiingereza the cancellation of debt, charge or penalty yaani kufutiwa deni, au kufutiwa kesi au kuondolewa adhabu, Kwa hiyo Mtu anapomwamini Bwana Yesu kwa kazi yake aliyoifanya pale msalabani dhambi zako zote zinasamehewa na anahesabika hana cha kulipa, hawezi kuadhibiwa tena hakuna tena hukumu ya adhabu juu yake  Warumi 8:1 “Sasa, basi, hakuna hukumu ya adhabu juu yao walio katika Kristo Yesu.”

 

Neno ondoleo la dhambi katika kiyunani linasomeka kama Aphesis – ambalo linaweza kutafasiriwa kwa maneno ya kiingereza kama Pardon, Deliverence, Forgiveness, Liberty and Remission, Lakini neno Remission linatumika kimahakama zaidi na neno Liberty linatumika kiutawala Neno lililotumika katika maandiko ni neno Remission ambalo limetumika zaidi ya mara tisa neno hili la kimahakama linahusiana na kumuachilia mfungwa mwenye hatia kwamba awe huru mbele ya sheria bila kubadili asili ya mashitaka yake Remission is to reduce without changing the nature of the sentence where by the prisoner is released with or without condition and in the eyes of the law he/she will be free man or woman, Na neno Liberty – is a state of civil or political freedom – ni Hali ya kuwa huru kiraia au kisiasa, ni kama vile Rais anapoamua kuwaachia watu huru wakati wa sikukuu za muungano au uhuru, kuna wafungwa ambao wanaachiliwa huru kwa matamko ya kisiasa, Kwa hiyo Damu ina mtindo huo wa kumtangaza au kumfanya mtu awe huru mbele za Mungu kwa mujibu wa sheria au kiutawala na kuhesabika kuwa raia wa kawaida bila kutumikia adhabu iliyokusudiwa au bila kulipa kodi.

 

Damu ya Yesu pia inaosha – neno kuosha katika kiyunani ni “Louō” ambalo maana yake ni kufua au kuogesha ni tendo la kumsafisha mwanadamu katika ukamilifu wake kwa jinsi ya mwili, nafsi na roho, kwa hiyo damu ya Yesu inawasafisha wale wanaomuamini, kuna maneno mawili yanayotumika kuhusu kuosha kuna neno kuosha “Louō” na “Katharizō” washed and Cleanses ambalo maana yake kutakasa au kufanya safi.(Purify)

 

2.       Damu ya Bwana Yesu pia inasababisha watu wahesabiwe haki - kuhesabiwa haki ni lugha ya kimahakama yenye maana ya kutokuonekana na hatia, ingawa sisi tulikuwa wenye hatia halisi lakini Mungu kwa amri ya kimahakama anakutangaza kuwa na haki kana kwamba hujawahi kukosea kwa sababu ya kumuamini Mwana wake kwa kazi aliyoifanya pale msalabani  Justification –  kwa kiyunani “Dikaioō” yaani kutangazwa kutokuwa na hatia you are innocent , free justify ni lugha ya kimahakama ya kukutangaza kuwa huna hatia. 

 

Warumi 5:1-2 “Basi tukiisha kuhesabiwa haki itokayo katika imani, na mwe na amani kwa Mungu, kwa njia ya Bwana wetu Yesu Kristo, ambaye kwa yeye tumepata kwa njia ya imani kuifikia neema hii ambayo mnasimama ndani yake; na kufurahi katika tumaini la utukufu wa Mungu.”

               

Warumi 5:8-9 “Bali Mungu aonyesha pendo lake yeye mwenyewe kwetu sisi, kwa kuwa Kristo alikufa kwa ajili yetu, tulipokuwa tungali wenye dhambi. Basi zaidi sana tukiisha kuhesabiwa haki katika damu yake, tutaokolewa na ghadhabu kwa yeye.”

 

Wagalatia 3:10-14 “Kwa maana wale wote walio wa matendo ya sheria, wako chini ya laana; maana imeandikwa, Amelaaniwa kila mtu asiyedumu katika yote yaliyoandikwa katika kitabu cha torati, ayafanye. Ni dhahiri ya kwamba hakuna mtu ahesabiwaye haki mbele za Mungu katika sheria; kwa sababu Mwenye haki ataishi kwa imani. Na torati haikuja kwa imani, bali, Ayatendaye hayo ataishi katika hayo. Kristo alitukomboa katika laana ya torati, kwa kuwa alifanywa laana kwa ajili yetu; maana imeandikwa, Amelaaniwa kila mtu aangikwaye juu ya mti; ili kwamba baraka ya Ibrahimu iwafikilie Mataifa katika Yesu Kristo, tupate kupokea ahadi ya Roho kwa njia ya imani.”

 

Tito 3:5-7 “si kwa sababu ya matendo ya haki tuliyoyatenda sisi; bali kwa rehema yake, kwa kuoshwa kwa kuzaliwa kwa pili na kufanywa upya na Roho Mtakatifu; ambaye alitumwagia kwa wingi, kwa njia ya Yesu Kristo Mwokozi wetu; ili tukihesabiwa haki kwa neema yake, tupate kufanywa warithi wa uzima wa milele, kama lilivyo tumaini letu.”

 

3.       Damu ya Yesu pia inatupa ukombozi - Neno ukombozi katika maandiko ya kiingereza ni Redemption neno hili katika lugha ya kibiblia Neno hilo Redemption kwenye kiyunani linatumika neno “Apolutrōsis” ambalo maana yake kwa kiingereza ni Ransom in full ambalo tafasiri yake  a sum of money demanded or paid for release of a captive,  lugha hii inaweza kutumika katika mazingira ya mfano, watekaji nyara wanamteka mtu na kumuweka kizuizini, kisha wanadai kiwango fulani cha gharama kilipwe ili mateka huyo aweze kuwa huru, lugha hiyo ya kulipia deni ili mtu huyo mfungwa au aliyetekwa aweze kuachiwa huru ndio lugha ya ukombozi inayotajwa katika maandiko, kwa hiyo adui hana uwezo wa kukumiliki tena kwa sababu madai yake yamelipwa yote kwa ukamilifu hawezi tena kukuweka kizuizini na hana madai tena, Kwa hiyo Damu ya Yesu pia hufanya kazi ya kutukomboa yaani kututoa kifungoni, au kutuweka huru bila madai yoyote kutoka kwa aliyekuwa anatuzuia yaani shetani.

 

Waefeso 1:6-8 “Na usifiwe utukufu wa neema yake, ambayo ametuneemesha katika huyo Mpendwa.Katika yeye huyo, kwa damu yake, tunao ukombozi wetu, masamaha ya dhambi, sawasawa na wingi wa neema yake. Naye alituzidishia hiyo katika hekima yote na ujuzi;”

 

Wakolosai 1:14 “Naye alituokoa katika nguvu za giza, akatuhamisha na kutuingiza katika ufalme wa Mwana wa pendo lake; ambaye katika yeye tuna ukombozi, yaani, msamaha wa dhambi; naye ni mfano wa Mungu asiyeonekana, mzaliwa wa kwanza wa viumbe vyote.”

 

1Petro 1:18-19 “Nanyi mfahamu kwamba mlikombolewa si kwa vitu viharibikavyo, kwa fedha au dhahabu; mpate kutoka katika mwenendo wenu usiofaa mlioupokea kwa baba zenu; bali kwa damu ya thamani, kama ya mwana-kondoo asiye na ila, asiye na waa, yaani, ya Kristo.”

 

Wagalatia 5:1 “Katika ungwana huo Kristo alituandika huru; kwa hiyo simameni, wala msinaswe tena chini ya kongwa la utumwa.”

 

Kwa hiyo tunaweza kuona kuwa Damu ya Yesu inafanya kazi ya ukombozi, ambao unajumuisha kusamehewa dhambi, urejesho kutoka katika nguvu za kitu chochote kile ambacho kilikuwa na haki ya kukushikilia, zikiwemo nguvu za giza, unapomjia Yesu nguvu hizo hazina mamlaka ya kukushika kwa sababu zozote zile, hauko tena chini ya utumwa, au ufungwa au mateka ya adui kwa kuwa sasa wewe ni mali ya Yesu.

 

4.       Damu ya Yesu inatuhuhisha tena na kutuweka karibu na Mungu -  Kabla ya kumuamini Yesu kila mkristo na asiye mkristo ambaye hajaokolewa anahesabika kuwa alikuwa mbali na alikuwa ni adui wa Mungu, hatungeweza kuwa karibu na Mungu na kupata msaada kwake kwa sababu dhambi humweka mtu mbali na Mungu, lakini baada ya kazi aliyoifanya Yesu pale Msalabani sisi tuliokuwa mbali sasa tunaletwa karibu na Mungu kwa damu ya Yesu

 

Waefeso 2:11-13 “Kwa ajili ya hayo kumbukeni ya kwamba zamani ninyi, mlio watu wa Mataifa kwa jinsi ya mwili, mnaoitwa Wasiotahiriwa na wale wanaoitwa Waliotahiriwa, yaani, tohara ya mwilini iliyofanyika kwa mikono; kwamba zamani zile mlikuwa hamna Kristo, mmefarakana na jamii ya Israeli, wageni wasio wa maagano ya ahadi ile. Mlikuwa hamna tumaini, hamna Mungu duniani. Lakini sasa, katika Kristo Yesu, ninyi mliokuwa mbali hapo kwanza mmekuwa karibu kwa damu yake Kristo.”

               

Wakolosai 1:21-22 “Na ninyi, mliokuwa hapo kwanza mmefarikishwa, tena adui katika nia zenu, kwa matendo yenu mabaya, amewapatanisha sasa; katika mwili wa nyama yake, kwa kufa kwake, ili awalete ninyi mbele zake, watakatifu, wasio na mawaa wala lawama;

 

5.       Damu ya Yesu inatupa kibali na ujasiri wa kupaingia patakatifu pa patakatifu – wote tutakuwa tunakumbuka ya kwamba Hekalu lilikuwa na maeneo makuu matatu, yaani uwa wa nje, kisha uwa wa ndani na ndani kabisa, uwa wa nje ni mahali ambapo watu walifika na kufanyiwa ibada za upatanisho za kila siku, na uwa wa ndani ni mahali ambapo makuhani waliingia kwa zamu kwaajili ya kufukiza uvumba kila siku, na uwa wa ndani kabisa mahali palipoitwa patakatifu pa patakatifu kuhani mkuu aliingia mara moja tu kwa mwaka na kuweka damu katika madhabahu ya Mungu ambacho ni kiti cha rehema kwaajili ya kuwaombea watu, eneo hili kuhani mkuu aliingia baada ya kuwa amejitakasa kwa siku saba, palikuwa ni mahali ambapo palikaa uwepo wa Mungu nyakati za agano la kale, hapa palitengwa kwa pazia maalumu lenye unene wa inchi sita sawa na unene wa tofali, lakini siku Yesu anakufa msalabani kwa kuimwaga damu yake Pazia hili lilipasuka vipande viwili na watu wakapaona mahali patakatifu ambapo ilikuwa sio rahisi kupaona, pazia hili liliwakilisha mwili wa Kristo uliosulubiwa na damu yake imetupa rehema na neema ya kuweza kumfikia Mungu moja kwa moja bila kizuizi wala bila kuhitaji mtu wa kuingia kwa niaba yako kwa kuwa wewe nawe umefanyika kuhani kwa nafsi yako.

 

Mathayo 27:51-54 “Na tazama, pazia la hekalu likapasuka vipande viwili toka juu hata chini; nchi ikatetemeka; miamba ikapasuka; makaburi yakafunuka; ikainuka miili mingi ya watakatifu waliolala; nao wakiisha kutoka makaburini mwao, baada ya kufufuka kwake, wakauingia mji mtakatifu, wakawatokea wengi. Basi yule akida, na hao waliokuwa pamoja naye wakimlinda Yesu, walipoliona tetemeko la nchi na mambo yaliyofanyika, wakaogopa sana, wakisema, Hakika huyu alikuwa Mwana wa Mungu

 

Waebrania 10:19-21 “Basi, ndugu, kwa kuwa tuna ujasiri wa kupaingia patakatifu kwa damu ya Yesu, njia ile aliyotuanzia iliyo mpya, iliyo hai, ipitayo katika pazia, yaani, mwili wake; na kuwa na kuhani mkuu juu ya nyumba ya Mungu;       

 

Waebrania 4:14-16 “Basi, iwapo tunaye kuhani mkuu aliyeingia katika mbingu, Yesu, Mwana wa Mungu, na tuyashike sana maungamo yetu. Kwa kuwa hamna kuhani mkuu asiyeweza kuchukuana nasi katika mambo yetu ya udhaifu; bali yeye alijaribiwa sawasawa na sisi katika mambo yote, bila kufanya dhambi.Basi na tukikaribie kiti cha neema kwa ujasiri, ili tupewe rehema, na kupata neema ya kutusaidia wakati wa mahitaji.”

 

Maandiko yanapotualika kukaribia kwa ujasiri katika kiti cha Rehema au patakatifu maana yake tunaalikwa kumkaribia au kuukaribia uwepo wa Mungu pasipo hofu sisi wenyewe mahali ambapo tutapokea msamaha na rehema na upendo wa Mungu, hii ni kwa sababu zamani kabla ya Yesu kufa Msalabani hakuna mtu aliruhusiwa kuukaribia uwepo wa Mungu pasipo kuhani au kuitwa na Mungu mwenyewe na ukikaribia ilikuwa ni kifo, kwa hiyo katika nyakati za agano jipya baada ya kifo cha Bwana Yesu sasa tunaweza kwenda kwa uwazi, kwa uhuru, pasipo hofu, wala pasipo kuhani au mpatanishi, bila woga, bila kuhukumiwa na kukabiliana na Mungu sisi wenyewe na kujielezea kwake bila mtu kuingilia kati na kumwaga mizigo yetu, mashaka yetu, fadhaa zetu na hatutauawa kwa sababu ya rehema zake na upendo wake mkubwa kwetu atatusaidia, kwa sababu ya rehema zake atatupokea bila kujali ukubwa wa makosa yetu, hatuhitaji kuigiza kuwa sisi ni wakamilifu, hatuhitaji kujitafutia haki kwa sababu hatuwezi kuwa na haki yetu wenyewe, Sadaka pekee na kibali pakee kinachotupa ujasiri huo ni Kazi ya Yesu iliyofanyika pale Msalabani. Yaani Damu yale aliyoimwaga, na kwa njia ya Imani damu hii iakupa ruhusa, kibali au tiketi ya kumfikia Mungu

 

6.       Damu ya Bwana Yesu inatupa Amani na Mungu – Damu ya Yesu Kristo inatupa Amani ya kweli, huwezi kuwa na Amani ya kweli kama hujasamehewa dhambi, huwezi kuwa na Amani ya kweli kama uko chini ya ufalme wa giza, huwezi kuwa na Amani ya kweli kama una uadui na Mungu, huwezi kuwa na Amani ya kweli kama huna ujasiri wa kupaingia patakatifu, huwezi kuwa na Amani ya kweli kama u mfungwa na mateka katika utawala wa ibilisi hivyo tunapomuamini Bwana Yesu, ambaye aliteseka kwa niaba yetu tunapata Amani ya kweli.

 

 Waebrania 9:12-14 “wala si kwa damu ya mbuzi na ndama, bali kwa damu yake mwenyewe aliingia mara moja tu katika Patakatifu, akiisha kupata ukombozi wa milele. Kwa maana, ikiwa damu ya mbuzi na mafahali na majivu ya ndama ya ng'ombe waliyonyunyiziwa wenye uchafu hutakasa hata kuusafisha mwili; basi si zaidi damu yake Kristo, ambaye kwamba kwa Roho wa milele alijitoa nafsi yake kwa Mungu kuwa sadaka isiyo na mawaa, itawasafisha dhamiri zenu na matendo mafu, mpate kumwabudu Mungu aliye hai?

 

Isaya 53:3-5 “Alidharauliwa na kukataliwa na watu; Mtu wa huzuni nyingi, ajuaye sikitiko; Na kama mtu ambaye watu humficha nyuso zao, Alidharauliwa wala hatukumhesabu kuwa kitu. Hakika ameyachukua masikitiko yetu, Amejitwika huzuni zetu; Lakini tulimdhania ya kuwa amepigwa, Amepigwa na Mungu, na kuteswa. Bali alijeruhiwa kwa makosa yetu, Alichubuliwa kwa maovu yetu; Adhabu ya amani yetu ilikuwa juu yake, Na kwa kupigwa kwake sisi tumepona.”                                                             

Wakamshinda kwa damu ya Mwana-Kondoo!

Ufunuo 12:9-11 “Yule joka akatupwa, yule mkubwa, nyoka wa zamani, aitwaye Ibilisi na Shetani, audanganyaye ulimwengu wote; akatupwa hata nchi, na malaika zake wakatupwa pamoja naye. Nikasikia sauti kuu mbinguni, ikisema, Sasa kumekuwa wokovu, na nguvu, na ufalme wa Mungu wetu, na mamlaka ya Kristo wake; kwa maana ametupwa chini mshitaki wa ndugu zetu, yeye awashitakiye mbele za Mungu wetu, mchana na usiku. Nao wakamshinda kwa damu ya Mwana-Kondoo, na kwa neno la ushuhuda wao; ambao hawakupenda maisha yao hata kufa.”                

Katika kifungu hiki cha maandiko tunapewa taarifa ya mfumo wa vita kubwa iliyoko katika ulimwengu wa roho na namna ya kuishinda vita hiyo, hii ni vita kati ya nuru na giza ni vita kati ya nguvu za uovu na wema wa Mungu, Kifungu kinafunua siri kubwa ya ushindi wa watu wa Mungu, kushinda kwa damu ya mwana kondoo kunajumuisha maswala yote muhimu ambayo tumeyapata kupitia damu hiyo ambayo yalikuwa yanampa nafasi shetani kutumia mfumo wa kimahakama na kibunge kutushinda kama mshitaki au mwendesha mashitaka na kwa sababu hiyo anapoteza haki na uwezo wa kutushitaki kwa sababu Damu ya Yesu Kristo imemaliza kila hati yake ya mashitaka anayotaka kuitumia ili tuharibiwe;-

Zakaria 3:1-4 “Kisha akanionyesha Yoshua, kuhani mkuu, amesimama mbele ya malaika wa Bwana, na Shetani amesimama mkono wake wa kuume ili kushindana naye. Bwana akamwambia Shetani, Bwana na akukemee Ewe Shetani; naam, Bwana, aliyechagua Yerusalemu, na akukemee; je! Hiki si kinga kilichotolewa motoni? Basi, Yoshua alikuwa amevaa nguo chafu sana, naye alikuwa akisimama mbele ya malaika. Naye huyo akajibu, akawaambia wale waliosimama mbele yake, akisema, Mvueni nguo hizi zenye uchafu. Kisha akamwambia yeye, Tazama, nimekuondolea uovu wako, nami nitakuvika mavazi ya thamani nyingi.”

Nyakati za agano la kale Shetani aliendelea kufanya kazi zake za kushitaki wateule wa Mungu hata sasa bado anaifanya kazi hiyo na ndio maana anaitwa mshitaki wetu

1Petro5:8-10. “Mwe na kiasi na kukesha; kwa kuwa mshitaki wenu Ibilisi, kama simba angurumaye, huzunguka-zunguka, akitafuta mtu ammeze. Nanyi mpingeni huyo, mkiwa thabiti katika imani, mkijua ya kuwa mateso yale yale yanatimizwa kwa ndugu zenu walioko duniani. Na Mungu wa neema yote, aliyewaita kuingia katika utukufu wake wa milele katika Kristo, mkiisha kuteswa kwa muda kidogo, yeye mwenyewe atawatengeneza, na kuwathibitisha, na kuwatia nguvu.”

Kwa hiyo shetani alipata haki ya kuwashitaki watu wa Mungu kwa sababu kulikuwako hakuna damu ya Yesu, alimshitaki kuhani mkuu Yoshua kwa sababu kweli alikuwa mchafu na Bwana alimkemea, lakini sasa katika agano jipya damu ya Yesu inafanya kazi ya kumkemea ibilisi kwa niaba yetu kama tutaitumia kwa Imani kwa hiyo andiko la msingi linaonyesha kutupwa kwa Mshitaki huyu na sababu kubwa ya kutupwa kwake na ushindi mkubwa kupatikana ni Damu ya mwanakondoo na neno la ushuhuda.

a.       Ametupwa chini Mshitaki wa Ndugu zetu – Ibilisi hufanya kazi katika ulimwengu wa roho kwa mfumo wa kimashitaka na kwa kweli tuna haki ya kushitakiwa kutokana na ukweli ya kuwa tuna dhambi, lakini mashitaka ya shetani hupoteza haki kwa sababu  damu ya Yesu iliyopatikana kwa kazi iliyofanyika msalabani  inafanya kitu cha tofauti

 

i.                    Inatunenea mema – Waebrania 12:22-24 “Bali ninyi mmeufikilia mlima Sayuni, na mji wa Mungu aliye hai, Yerusalemu wa mbinguni, na majeshi ya malaika elfu nyingi, mkutano mkuu na kanisa la wazaliwa wa kwanza walioandikwa mbinguni, na Mungu mwamuzi wa watu wote, na roho za watu wenye haki waliokamilika, na Yesu mjumbe wa agano jipya, na damu ya kunyunyizwa, inenayo mema kuliko ile ya Habili.”

 

Damu ya Yesu inauwezo wa kuzungumza maneno mema mazuri kwaajili yetu kuliko mashitaka ya adui, kupitia ushindi wake pale Msalabani, Yesu amechukua ushindi dhidi ya nguvu za giza, Kwa hiyo Kazi ya damu hii ni kutunenea mema na kwa sababu hiyo huwezi kuhesabiwa kuwa na hatia, au u mtumwa ama vyovyote vile huwezi kuangamizwa kwa sababu ya damu ya Yesu, kwa hiyo neno hilo ni mjumuisho wa ushindi tulio nao kupitia damu ya Yesu ambayo kwayo inatupa neema juu ya neema, sio hivyo tu Damu ya Yesu inamkemea shetani asiwe na nguvu ya kutushitaki wala kufanya uonevu wa namna yoyote katika nafsi mwili na roho zetu.

 

Wakolosai 2:13-15 “Na ninyi mlipokuwa mmekufa kwa sababu ya makosa yenu na kutokutahiriwa kwa mwili wenu, aliwafanya hai pamoja naye, akiisha kutusamehe makosa yote; akiisha kuifuta ile hati iliyoandikwa ya kutushitaki kwa hukumu zake, iliyokuwa na uadui kwetu; akaiondoa isiwepo tena, akaigongomea msalabani; akiisha kuzivua enzi na mamlaka, na kuzifanya kuwa mkogo kwa ujasiri, akizishangilia katika msalaba huo.”

 

Warumi 8:33-39 “Ni nani atakayewashitaki wateule wa Mungu? Mungu ndiye mwenye kuwahesabia haki. Ni nani atakayewahukumia adhabu? Kristo Yesu ndiye aliyekufa; naam, na zaidi ya hayo, amefufuka katika wafu, naye yuko mkono wa kuume wa Mungu; tena ndiye anayetuombea. Ni nani atakayetutenga na upendo wa Kristo? Je! Ni dhiki au shida, au adha, au njaa, au uchi, au hatari, au upanga? Kama ilivyoandikwa, ya kwamba, Kwa ajili yako tunauawa mchana kutwa, Tumehesabiwa kuwa kama kondoo wa kuchinjwa. Lakini katika mambo hayo yote tunashinda, na zaidi ya kushinda, kwa yeye aliyetupenda. Kwa maana nimekwisha kujua hakika ya kwamba, wala mauti, wala uzima, wala malaika, wala wenye mamlaka, wala yaliyopo, wala yatakayokuwapo, wala wenye uwezo, wala yaliyo juu, wala yaliyo chini, wala kiumbe kinginecho chote hakitaweza kututenga na upendo wa Mungu ulio katika Kristo Yesu Bwana wetu.”

 

Ni hatari sana kumshitaki au kumuhukumu mtu anayemuamini Yesu kwa sababu anahesabiwa haki na Mungu, Andiko katika Warumi 8:33 katika kiingereza NIV mstari huo unasomeka

 

Who will bring any charge against those whom God hase chosen? It is God who justifies.”

 

Maana yake ni nani atakaye wahesabia kuwa wana hatia watu ambao Mungu amewachagua “Charge against” (KATA) kiyunani. Na swala hili jibu lake Mungu ndiye mwenye kuwahesabia haki Justifies anouced Innocent (DIKAIOŌ) kiyunani.  yaani wale waliotangazwa na hakimu kuwa hawana hatia INNOCENT maandiko yanaonyesha kuwa kupitia kazi aliyoifanya Yesu pale Msalabani kwa kumwaga damu yake (Kristo Yesu Ndiye aliyekufa) alafu yeye ndiye kuhani mkuu anayefanya upatanisho kwaajili yetu (Tena ndiye anayetuombea) kwa hiyo awaye yote ambaye anatuhesabia hatia au kutuhukumu kuwa hatufai ili hali Yesu amefanya kazi ya ukombozi na anatuombea huyu anaunganishwa na ibilisi katika kushindwa

 

Alaaniwe mtu awaye yote anayekuhesabia kuna na dhambi wakati Yesu amekufia msalabani na kumwaga damu yake nasema alaaniwe, aharibikiwe mtu awaye yote anayeongea maovu yako ili hali Mungu amekutangaza kuwa huna hatia, Bwana na amkemee kila mtu anayeipuuzia kazi ya damu ya Yesu iliyofanyika kwaajili yetu pale msalabani na kujidhani kuwa yeye ndiye yuko sawa, Ni damu ya Yesu inayotupa kiburi cha kuuliza ni nani atakayetushitaki?  Ni damu ya Yesu ndiyo iliyotuleta katika neema hii, kwa hiyo mtu yeyote anayehubiri kinyume na kazi ya damu Amelaaniwa.

 

Wagalatia 1:6-9 “Nastaajabu kwa kuwa mnamwacha upesi hivi yeye aliyewaita katika neema ya Kristo, na kugeukia injili ya namna nyingine. Wala si nyingine; lakini wapo watu wawataabishao na kutaka kuigeuza injili ya Kristo. Lakini ijapokuwa sisi au malaika wa mbinguni atawahubiri ninyi injili yo yote isipokuwa hiyo tuliyowahubiri, na alaaniwe. Kama tulivyotangulia kusema, na sasa, nasema tena, mtu awaye yote akiwahubiri ninyi injili yo yote isipokuwa hiyo mliyoipokea, na alaaniwe.”          

 

ii.                  Na kwa neno la ushuhuda – Ushuhuda huu unaotolewa na waamini ni ushuhuda gani? Ushuhuda wetu ni kuhusu kazi iliyofanywa na damu ya Yesu katika maisha yetu, tunapozungumza habari za ukombozi mkubwa unaosababishwa au uliosababishwa na Damu ya Yesu katika maisha yetu, tunaposhuhudia habari za ukombozi huu tunaendelea kueneza habari mbaya katika ufalme wa ibilisi kwa jinsi Damu hii inavyoleta neema na wepesi wa kila mwanadamu kukubali njia hii sahihi ya ukombozi iliyowekwa na Mungu Msalabani, na ushuhuda huo unatia hasara kubwa sana kwa upande wa shetani na kumletea kushindwa, kumbuka wakamshinda kwa Damu ya mwana kondoo na kwa neno la ushuhuda. (Injili).

 

1Wakorintho 1:17-18 “Maana Kristo hakunituma ili nibatize, bali niihubiri Habari Njema; wala si kwa hekima ya maneno, msalaba wa Kristo usije ukabatilika. Kwa sababu neno la msalaba kwao wanaopotea ni upuzi, bali kwetu sisi tunaookolewa ni nguvu ya Mungu.”

 

Warumi 1:16-17 “Kwa maana siionei haya Injili; kwa sababu ni uweza wa Mungu uuletao wokovu, kwa kila aaminiye, kwa Myahudi kwanza, na kwa Myunani pia. Kwa maana haki ya Mungu inadhihirishwa ndani yake, toka imani hata imani; kama ilivyoandikwa, Mwenye haki ataishi kwa imani.”

 

iii.                Damu ya Yesu ni silaha – Damu ya Yesu inasimama kama silaha kubwa ya kivita ya hatari sana katika ulimwengu wa roho, inatumika kama ulinzi kwaajili yetu na silaha ya kumshinda shetani, anakosa nguvu kabisa tunapoikumbuka kazi aliyoifanya Yesu Pale msalabani, Damu hii ni ngao, damu hii inatulinda dhidi ya mashambulizi yote ya ibilisi, tunapokumbuka tu na kujua umuhimu wake na kazi yake ambayo imefanyika kila kitu katika ulimwengu wa roho hasa wa giza unaachia, kama liko giza haliwezi kusimama kwa kazi ya Msalaba, kila kikwazo chochote duniani ambacho kinatokana na mashambulizi ya ibilisi kinasambaratiswa kupitia Damu ya Yesu, tunachotakiwa ni kuitumainia Damu ya Yesu kwa Imani na kuendelea kuzungumzia utamu wa ushindi tunaoupata kupitia Damu ya Yesu, Nisikilize kazi yote ya msalabani na tangazo la Yesu Kristo kuwa imekwisha inakamilishwa katika Damu, ile iliyomwagika msalabani kwaajili yetu. Damu hii ni kitambulisho ya kuwa tuna uhuru, tumekombolewa, mfame ametangaza kuwa tuko huru, tuna ushirika wa kudumu na Mungu, hatudaiwi kodi, ni wageni tulioruhusiwa kufanya kazi zetu kwa kibali cha mfaome hapa duniani, tuna muungano wa kisera, kisiasa na ushirika na Mungu, tuna kibali, hatuna hatia, hatuna mashitaka, tumewekewa alama ya kutokuuawa, tuna utambulisho wa uhuru kwa sababu tumemuamini Mungu na tumeikubali kazi yake ya ukombozi.

 

Yoshua 2:18-19 “Angalia, tutakapoingia katika nchi hii, funga kamba hii nyekundu katika dirisha hili ulilotutelemshia; nawe uwakusanye kwako nyumbani mwako, baba yako, na mama yako, na ndugu zako, na watu wote wa nyumba ya baba yako. Itakuwa mtu awaye yote atakayetoka katika mlango wa nyumba yako kwenda njiani, damu yake itakuwa juu ya kichwa chake mwenyewe, na sisi tutakuwa hatuna hatia; na mtu atakayekuwa ndani ya nyumba yako damu yake itakuwa juu ya vichwa vyetu, mkono wa mtu ukimpata.”

 

Na Rev. Innocent Samuel Kamote

Mkuu wa wajenzi mwenye Hekima!