Warumi 2:1-8 “Kwa hiyo, wewe mtu uwaye yote
uhukumuye, huna udhuru; kwa maana katika hayo umhukumuyo mwingine wajihukumu
mwenyewe kuwa na hatia; kwa maana wewe uhukumuye unafanya yale yale. Nasi
twajua ya kuwa hukumu ya Mungu ni ya kweli juu yao wafanyao hayo. Wewe
binadamu, uwahukumuye wale wafanyao hayo na kutenda yayo hayo mwenyewe, je!
Wadhani ya kwamba utajiepusha na hukumu ya Mungu? Au waudharau wingi wa wema
wake na ustahimili wake na uvumilivu wake, usijue ya kuwa wema wa Mungu
wakuvuta upate kutubu? Bali kwa kadiri ya ugumu wako, na kwa moyo wako usio na
toba, wajiwekea akiba ya hasira kwa siku ile ya hasira na ufunuo wa hukumu ya
haki ya Mungu, atakayemlipa kila mtu kwa kadiri ya matendo yake; wale ambao kwa
saburi katika kutenda mema wanatafuta utukufu na heshima na kutokuharibika,
watapewa uzima wa milele; na wale wenye fitina, wasioitii kweli, bali wakubalio
dhuluma, watapata hasira na ghadhabu;”
Utangulizi:
Hukumu ya Mungu kwa wanadamu ni
jambo lisiloepukika,Tangu mwanzo Mwanadamu na viumbe wengine walipokosea Mungu
mara moja alitoa hukumu, alimuhukumu Shetani, alimuhukumu mwanadamu,
Alimuhukumu mwanaume na alimuhukumu mwanamke kila mmoja kwa kadiri ya uhusika
wake katika kosa lile la bustanini mwa Edeni, kwa hiyo hukumu ya Mungu ni jambo
lisiloepukika, ukweli kuhusu hukumu ya Mungu ni jambo lenye kutisha sana kwa
wanadamu, hata hivyo leo tutachukua Muda kutafakari kwa undani kuhusu hukumu ya
Mungu na umuhimu wake katika mtazamo wa upendo wake na rehema zake na tabia
yake ya uungu ambayo itakushangaza!
Warumi 2:12-16 “Kwa kuwa wote waliokosa
pasipo sheria watapotea pasipo sheria, na wote waliokosa, wenye sheria,
watahukumiwa kwa sheria. Kwa sababu sio wale waisikiao sheria walio wenye haki
mbele za Mungu, bali ni wale waitendao sheria watakaohesabiwa haki. Kwa maana
watu wa Mataifa wasio na sheria wafanyapo kwa tabia zao yaliyo ndani ya torati,
hao wasio na sheria wamekuwa sheria kwa nafsi zao wenyewe. Hao waionyesha kazi
ya torati iliyoandikwa mioyoni mwao, dhamiri yao ikiwashuhudia, na mawazo yao,
yenyewe kwa yenyewe, yakiwashitaki au kuwatetea; katika siku ile Mungu
atakapozihukumu siri za wanadamu, sawasawa na injili yangu, kwa Kristo Yesu.”
Swala zima la hukumu kwa mujibu
wa maandiko Mungu hakuwapa wanadamu, na tumekatazwa kuhukumu, bali amepewa Yesu
Kristo na Baba yake aliye mbinguni, kwa hiyo hakuna mtu awaye yote mwenye
mamlaka ya kuhukumu isipokuwa mwana wa Adamu yaani Yesu Kristo mwenyewe,
kuhukumu ni kukaa katika kiti cha Mungu. Fundisho kuhusu hukumu linatawala
maandiko yote katika agano la kale na jipya, Utukufu wa Mungu unaonekana na
kufunuliwa katika namna anavyohukumu, Mungu anamtaka kila mmoja awajibike na
kwa sababu hiyo hakuna mwanadamu wala taifa litakaloweza kuiepuka hukumu ya
Mungu na Yesu ndiye Mwamba wa hukumu hiyo:-
Yohana 5:22-30 “Tena Baba hamhukumu mtu ye
yote, bali amempa Mwana hukumu yote; ili watu wote wamheshimu Mwana kama vile
wanavyomheshimu Baba. Asiyemheshimu Mwana hamheshimu Baba aliyempeleka. Amin,
amin, nawaambia, Yeye alisikiaye neno langu na kumwamini yeye aliyenipeleka
yuna uzima wa milele; wala haingii hukumuni, bali amepita kutoka mautini
kuingia uzimani. Amin, amin, nawaambia, Saa inakuja, na sasa ipo, wafu
watakapoisikia sauti ya Mwana wa Mungu, na wale waisikiao watakuwa hai. Maana
kama vile Baba alivyo na uzima nafsini mwake, vivyo hivyo alimpa na Mwana kuwa
na uzima nafsini mwake. Naye akampa amri ya kufanya hukumu kwa sababu ni Mwana
wa Adamu. Msistaajabie maneno hayo; kwa maana saa yaja, ambayo watu wote
waliomo makaburini wataisikia sauti yake. Nao watatoka; wale waliofanya mema
kwa ufufuo wa uzima, na wale waliotenda mabaya kwa ufufuo wa hukumu.Mimi siwezi
kufanya neno mwenyewe; kama nisikiavyo ndivyo nihukumuvyo; na hukumu yangu ni
ya haki, kwa sababu siyatafuti mapenzi yangu mimi, bali mapenzi yake
aliyenipeleka.”
Kwa nini Masihi amepewa kuhukumu?
Kwa sababu uwezo wake wa kuhukumu ni mkubwa sana na uko juu na sio wa
kibinadamu, na kwa sababu yeye amepitia uanadamu anatujua vema lakini pia kwa
sababu kuhukumu kwake hakutokani na yale yanayoonekana kwa macho, wala yale
ayasikiayo kwa masikio yake lakini hukumu yake ni ya haki kama alivyosema
mwenyewe na uwezo wake ni mkubwa sana kwa sababu ya Roho wa Mungu na hekima
yake kuu
Isaya 11:1-5 “Basi litatoka chipukizi
katika shina la Yese, na tawi litakalotoka katika mizizi yake litazaa
matunda.Na roho ya Bwana atakaa juu yake, roho ya hekima na ufahamu, roho ya
shauri na uweza, roho ya maarifa na ya kumcha Bwana; na furaha yake itakuwa
katika kumcha Bwana; wala hatahukumu kwa kuyafuata ayaonayo kwa macho yake,
wala hataonya kwa kuyafuata ayasikiayo kwa masikio yake;bali kwa haki
atawahukumu maskini, naye atawaonya wanyenyekevu wa dunia kwa adili; naye
ataipiga dunia kwa fimbo ya kinywa chake, na kwa pumzi ya midomo yake atawaua
wabaya. Na haki itakuwa mshipi wa viuno vyake, na uaminifu mshipi wa kujifungia.”
Kumbukumbu 1:17 “Msitazame nafsi za watu
katika hukumu; mwasikize wadogo na wakubwa sawasawa; msiche uso wa mtu awaye
yote; kwa kuwa hukumu ni ya Mungu; na lile neno liwashindalo mniletee mimi,
nami nitalisikiza.”
Kumbukumbu 32:3-4 “Maana nitalitangaza Jina
la Bwana; Mpeni ukuu Mungu wetu.Yeye Mwamba, kazi yake ni kamilifu; Maana, njia
zake zote ni haki. Mungu wa uaminifu, asiye na uovu, Yeye ndiye mwenye haki na
adili.”
Leo tutachukua muda moja kwa moja
kutafakari kwa kina na mapana na marefu kuhusu hukumu za Mungu ambazo kimsingi
ziko aina nne za hukumu ambazo tutaziangalia kwa kuzingatia vipengele vinne
vifuatavyo sawa na ufunuo.
1.
Hukumu
iliyoko sasa – Paroúsa
Krisi
2.
Hukumu
ya adhabu – Krima
3.
Hukumu
isiyo ya adhabu – Krino
4.
Hukumu
isiyotarajiwa – Aprosmenos
Hukumu iliyoko sasa – Paroúsa
Krisi
Hukumu hii kwa kiingereza inaitwa Present Judgement kwa kiyunani Paroúsa
Krisi yaani hukumu hii inategemeana na mkao ulioko sasa wa hali ya kiroho
za wanadamu, kama mwanadamu ameukubali mpango wa Mungu wa ukombozi kwa
kumwamini Bwana Yesu kama Bwana na mwokozi wake huyo kwa sasa haukumiwi, na
yule ambaye hajaukubali mpango wa Mungu wa ukombozi kupitia Yesu Kristo huyo
amekwisha kuhukumiwa, Instant Judgement.au
“Quckly Decision” “quicly judgemnt”
Yohana 3:16-18 “Kwa maana jinsi hii Mungu
aliupenda ulimwengu, hata akamtoa Mwanawe pekee, ili kila mtu amwaminiye
asipotee, bali awe na uzima wa milele. Maana
Mungu hakumtuma Mwana ulimwenguni ili auhukumu ulimwengu, bali ulimwengu
uokolewe katika yeye. Amwaminiye yeye hahukumiwi; asiyeamini amekwisha
kuhukumiwa; kwa sababu hakuliamini jina la Mwana pekee wa Mungu.”
Yohana 5:24 “Amin, amin, nawaambia, Yeye
alisikiaye neno langu na kumwamini yeye aliyenipeleka yuna uzima wa milele;
wala haingii hukumuni, bali amepita kutoka mautini kuingia uzimani.”
Kwa hiyo katika ulimwengu huu
wako watu ambao wamehukumiwa tayari yaani hivi tunavyozungumza hapa wako watu
wa aina mbili duniani na wote wanaendelea na shughuli zao wakiwa wamehukumiwa
yaani wale wasiomwamini Yesu na kundi la pili ni watu ambao hawako chini ya
hukumu hawahukumiwi hawa ni wale waliomuamini Bwana Yesu na kumkubali kama
Bwana na mwokozi wao, Hukumu hii inaendelea ikiendeshwa na Roho Mtakatifu
kupitia kazi anayoifanya sasa ya kuwashuhudia watu kwa habari ya dhambi, haki
na hukumu, kila wakati na kila siku injili ihubiriwapo mtu akimpokea Yesu
anahama kutoka upande wa wale waliohukumiwa kwenda upande wa wale wasiohukumiwa,Injili
ikihubiriwa ukaikubali sasa uko nje ya hukumu, na ukiikataa uko hukumuni.
Yohana 16:7-8 “Lakini mimi nawaambia iliyo
kweli; yawafaa ninyi mimi niondoke, kwa maana mimi nisipoondoka, huyo Msaidizi
hatakuja kwenu; bali mimi nikienda zangu, nitampeleka kwenu. Naye akiisha kuja,
huyo atauhakikisha ulimwengu kwa habari ya dhambi, na haki, na hukumu.”
Hukumu ya adhabu – Krima
Hii ni moja ya kundi la hukumu (Judgement or Condemnation) ambayo
inahusiana na siku ya mwisho wakati Kristo atakapokalia kiti cha enzi cha
hukumu na kumuhukumu kila mmoja kwa kadiri ya matendo yake hukumu hii pia
inaitwa hukumu ya adhabu au hukumu ya aibu, siku ya hukumu hii kila mtu
atasimama mbele ya kiti hicho cha hukumu cha Mungu na kutoa hesabu yake
mwenyewe. Hukumu hii kiyunani Krima
au Krinete maana yake to Condemn, au making a negative
assessment of a person or thing, kufanya maamuzi hasi dhidi ya mtu au kitu.
Warumi 14:10-12 “Lakini wewe je! Mbona
wamhukumu ndugu yako? Au wewe je! Mbona wamdharau ndugu yako? Kwa maana sisi
sote tutasimama mbele ya kiti cha hukumu cha Mungu. Kwa kuwa imeandikwa, Kama
niishivyo, anena Bwana, kila goti litapigwa mbele zangu; Na kila ulimi utamkiri
Mungu. Basi ni hivyo, kila mtu miongoni mwetu atatoa habari zake mwenyewe mbele
za Mungu.”
2Wakorintho 5:10 “Kwa maana imetupasa sisi
sote kudhihirishwa mbele ya kiti cha hukumu cha Kristo, ili kila mtu apokee
ijara ya mambo aliyotenda kwa mwili, kadiri alivyotenda, kwamba ni mema au
mabaya.”
Daniel 12:2-3 “Tena, wengi wa hao walalao
katika mavumbi ya nchi wataamka, wengine wapate uzima wa milele, wengine aibu
na kudharauliwa milele. Na walio na hekima watang'aa kama mwangaza wa anga; na
hao waongozao wengi kutenda haki watang'aa kama nyota milele na milele.”
Muhubiri 12:14 “Kwa maana Mungu ataleta
hukumuni kila kazi, pamoja na kila neno la siri, likiwa jema au likiwa baya.”
Ufunuo 20:11-12 “Kisha nikaona kiti cha
enzi, kikubwa, cheupe, na yeye aketiye juu yake; ambaye nchi na mbingu
zikakimbia uso wake, na mahali pao hapakuonekana. Nikawaona wafu, wakubwa kwa
wadogo, wamesimama mbele ya hicho kiti cha enzi; na vitabu vikafunguliwa; na
kitabu kingine kikafunguliwa, ambacho ni cha uzima; na hao wafu wakahukumiwa
katika mambo hayo yaliyoandikwa katika vile vitabu, sawasawa na matendo yao.”
Ufufuo huu ni wa hukumu ya
adhabu,(Krima) na itakuwa ni hukumu
ya aibu kwa sababu Neno Krima linalotumika kuelezea hukumu ya adhabu lina maana
ya hukumu isiyohukumu matokeo tu bali inayohusu utafiti wa kina na uzingativu
wa kila kilichofanyika kuanzia kwenye dhamiri na machakato mzima wa tukio
pamoja na uzito wa ushahidi na mazingira
katika mtazamo wa kibinadamu, lakini katika mtazamo wa kiungu hukumu hii
inahusisha hukumu iliyo sawasawa na Haki ya Mungu na tabia yake, na kwa kuwa
Mungu ni mkamilifu hukumu yake itakuwa sahihi
na madhara au adhabu itakayoambatana na hukumu hii itakuwa ni sahihi,
kwa hiyo hukumu yake itakuwa ni matokeo na ufunuo ulio sahihi ukiingia ndani
katika dhamiri ya mwanadamu kwa hiyo itakuwa ni hukumu ambayo hata yeye
anayehukumiwa atakubaliana na ile adhabu atakayopewa au ataridhishwa na maamuzi
ya jaji mkuu Yesu Kristo.
Hukumu isiyo ya adhabu – Krino
Hukumu hii isiyo ya dhabu ni
hukumu inayowahusu wale wote ambao wamemuamini Yesu Kristo hawa kimaandiko
hawahusiki katika hukumu ya adhabu (Krima),
na badala yake hawa wana adhabu iitwayo Krino
hii ni hukumu isiyo ya adhabu imetajwa na Paulo Mtume katika:-
Warumi 8:1-2 “Sasa, basi, hakuna hukumu ya
adhabu juu yao walio katika Kristo Yesu. Kwa sababu sheria ya Roho wa uzima ule
ulio katika Kristo Yesu imeniacha huru, mbali na sheria ya dhambi na mauti”
Warumi 8:33-34. “Ni nani atakayewashitaki
wateule wa Mungu? Mungu ndiye mwenye kuwahesabia haki.Ni nani atakayewahukumia
adhabu? Kristo Yesu ndiye aliyekufa; naam, na zaidi ya hayo, amefufuka katika
wafu, naye yuko mkono wa kuume wa Mungu; tena ndiye anayetuombea.”
Krino ni hukumu isiyo ya adhabu
ambayo itawahusu watu waliookolewa, yaani wale waliomuamini Yesu hawatakutana
na hukumu ya adhabu lakini watakutana na hukumu itakayofuatilia kwa haki,
kwanini mtu Fulani alifanya jambo Fulani na thawabu yake itakuwa ni thawabu
gani? Hukumu hii katika tamaduni za kiyunani Mgeni rasmi hukaa katika kiti
kinachoitwa Bema au jukwaa au sehemu
maalumu iliyoinuka kwaajili ya kutoa thawabu, za kimichezo ambapo wanamichezo
wanapata thawabu au medali kulingana na kazi waliyoifanya na hakuna madhara kwa
waliokosa medali. Hii ni hukumu ya watakatifu ni hukumu ya kutoa hesabu mbele
za Kristo kwa kile tulichofanya. Katika somo la ufahamu kuhusu maswala ya
hukumu The doctrine of Judgement Krino kiyunani kwa kiingereza ni to separate,
put asunder, to pick out, Select, choose, to approve, esteem, to prefer, to
give an opinion, to determine, resolve, decree, ni hukumu ya kutenganisha,
kuchanganua, kuchagua, kuidhinisha, kuthaminisha, kupendelea, kutoa maoni,
kuazimia, kuthibitisha, kwa hiyo itakuwa ni hukumu ya kuja kuthibitisha nani
anafaa kuwa nini katika ufalme wa Mungu na sio kwa kusudi la kuadhibu.
1Wakorintho 3:12-15 “Lakini kama mtu
akijenga juu ya msingi huo, dhahabu au fedha au mawe ya thamani, au miti au
majani au manyasi, kazi ya kila mtu itakuwa dhahiri. Maana siku ile
itaidhihirisha, kwa kuwa yafunuliwa katika moto; na ule moto wenyewe utaijaribu
kazi ya kila mtu, ni ya namna gani. Kazi ya mtu aliyoijenga juu yake ikikaa,
atapata thawabu. Kazi ya mtu ikiteketea, atapata hasara; ila yeye mwenyewe
ataokolewa; lakini ni kama kwa moto.”
Mathayo 25:14-28 “Maana ni mfano wa mtu
atakaye kusafiri, aliwaita watumwa wake, akaweka kwao mali zake. Akampa mmoja
talanta tano, na mmoja talanta mbili, na mmoja talanta moja; kila mtu kwa kadiri
ya uwezo wake; akasafiri. Mara yule aliyepokea talanta tano akaenda, akafanya
biashara nazo, akachuma faida talanta nyingine tano. Vile vile na yule mwenye
mbili, yeye naye akachuma nyingine mbili faida. Lakini yule aliyepokea moja
alikwenda akafukua chini, akaificha fedha ya bwana wake. Baada ya siku nyingi
akaja bwana wa watumwa wale, akafanya hesabu nao. Akaja yule aliyepokea talanta
tano, akaleta talanta nyingine tano, akisema, Bwana, uliweka kwangu talanta
tano; tazama, talanta nyingine tano nilizopata faida. Bwana wake akamwambia,
Vema, mtumwa mwema na mwaminifu; ulikuwa mwaminifu kwa machache, nitakuweka juu
ya mengi; ingia katika furaha ya bwana wako. Akaja na yule aliyepokea talanta
mbili, akasema, Bwana, uliweka kwangu talanta mbili; tazama, talanta nyingine
mbili nilizopata faida. Bwana wake akamwambia, Vema, mtumwa mwema na mwaminifu;
ulikuwa mwaminifu kwa machache, nitakuweka juu ya mengi; ingia katika furaha ya
bwana wako. Akaja na yule aliyepokea talanta moja, akasema, Bwana, nalitambua
ya kuwa wewe u mtu mgumu, wavuna usipopanda, wakusanya usipotawanya;basi
nikaogopa, nikaenda nikaificha talanta yako katika ardhi; tazama, unayo iliyo
yako. Bwana wake akajibu, akamwambia, Wewe mtumwa mbaya na mlegevu, ulijua ya
kuwa navuna nisipopanda, nakusanya nisipotawanya; basi, ilikupasa kuiweka fedha
yangu kwa watoao riba; nami nikija ningalipata iliyo yangu na faida yake. Basi,
mnyang'anyeni talanta hiyo, mpeni yule aliye nazo talanta kumi ”
Mathayo 24:45-46 “Ni nani basi yule mtumwa
mwaminifu mwenye akili, ambaye bwana wake alimweka juu ya nyumba yake, awape
watu chakula kwa wakati wake? Heri mtumwa yule, ambaye bwana wake ajapo
atamkuta akifanya hivyo.”
Hukumu hii ni hukumu ya
watakatifu, kila mtu aliyeokolewa anapaswa kumtumikia Mungu, na Kristo
atakapokuja kulinyakua kanisa, pale mawinguni itakuwepo nafasi ya kutoa taji na
karamu ya mwana kondoo wakati huu kila mkristo atahukumiwa sawa na kazi
aliyoifanya na jinsi na namna alivyoitumia talanta aliyopewa kwa uaminifu au
vinginevyo na hapo thawabu zitatolewa, hakutakuwa na adhabu lakini kila mtu
atastahili heshima yake kulingana na bidii, akili, muda na namna tunavyojitoa
kwa Mungu ikiwa ni pamoja na kuwalisha watu wake, kwa hiyo kama sisi ni
wachungaji tuwalishe watu chakula yaani neno la Mungu kwa wakati wake, kama una
kipawa chochote kile kitumie kwa kadiri uwezavvyo na kwa kadiri ya neema huku
ukiwa na dhamiri safi kwa sababu hukumu hii ni hukumu isiyoepukika pia katika
hukumu hii hakuna mtu anayeweza kuwashitaki watu wa Mungu kwa sababu zozote
wala hakuna mtu anayeweza kutuhukumu na kudai kuwa hawa ni wakosa, hukumu hii
ni hukumu isiyo na madhara.
Hukumu isiyotarajiwa – Aprosmenos
Katika hukumu zote zilizotajwa
hapo juu, hii ndio hukumu itakayoshangaza watu kuliko hukumu zote, katika
hukumu hii maamuzi atakayoyatoa Yesu Kristo yatadhihirisha uwezo wake mkubwa na
hekima yake kubwa na ile hali ya kuwa yeye ni Bwana na hakuna mtu wa kumuamulia
lolote wala kutabiri lolote, hukumu hii inadhihirisha kwamba Mungu mwenyewe ana
haki ya kuamua na uwezo wake wa kuhukumu ni wa hali ya juu na wa tofauti sana.
Hukumu hii iko katika maamuzi ya
Mungu mwenyewe na inaitwa hukumu isiyotabirika katika lugha ya kiyunani linatumika
neno hilo Aprosmenos ambalo kwa
kiingereza ni unanticipated, unforeseen,
unexpected, difficulties predicted kwa
hiyo ni hukumu isiyotegemewa, ni hukumu isiyotarajiwa, ni hukumu isiyotabirika
ni hukumu ambayo ni ngumu kimatazamio, hukumu hii iko chini ya maamuzi ya Mungu
mwenyewe bila kujali kuwa kuna haki au hakuna haki mfano lakini iko haki ambayo
Mungu mwenyewe katika mtazamo wake huiona lakini wanadamu hawawezi.
Warumi 9:10-16 “Wala si hivyo tu, lakini
Rebeka naye, akiisha kuchukua mimba kwa mume mmoja, naye ni Isaka, baba yetu,
(kwa maana kabla hawajazaliwa wale watoto, wala hawajatenda neno jema wala
baya, ili lisimame kusudi la Mungu la kuchagua, si kwa sababu ya matendo, bali
kwa sababu ya nia yake aitaye), aliambiwa hivi, Mkubwa atamtumikia mdogo. Kama
ilivyoandikwa, Nimempenda Yakobo, bali Esau nimemchukia.Tuseme nini basi? Kuna
udhalimu kwa Mungu? Hasha! Maana amwambia Musa, Nitamrehemu yeye nimrehemuye,
nitamhurumia yeye nimhurumiaye. Basi, kama ni hivyo, si katika uwezo wa yule
atakaye, wala wa yule apigaye mbio; bali wa yule arehemuye, yaani, Mungu.”
Warumi 9:20-21 “La! Sivyo, Ee binadamu;
wewe u nani umjibuye Mungu? Je! Kitu kilichoumbwa kimwambie yeye aliyekiumba,
Kwani kuniumba hivi? Au mfinyanzi je! Hana amri juu ya udongo, kwa fungu moja
la udongo kuumba chombo kimoja kiwe cha heshima, na kimoja kiwe hakina heshima?”
Unaona ili lisimame kusudi la
Mungu la kuchagua Maneno haya yanaonyesha kuwa mwanadamu awaye yote anapokuwa
na kesi mahakamani awe amekosa au awe hajakosea bado anakuwa na mashaka kwa
sababu mwenye maamuzi ya mwisho ni hakimu au jaji mwenyewe, kwa hiyo ni muhimu
kufahamu kuwa iko mamlaka ya Mungu mwenyewe inayoweza kuamua na kuhukumu hata
kama jambo linaonekana kuwa sawa machoni pako mfano;
1.
Luka
10 38-42 “Ikawa katika kuenenda kwao aliingia
katika kijiji kimoja; mwanamke mmoja jina lake Martha akamkaribisha nyumbani
kwake.Naye alikuwa na umbu lake aitwaye Mariamu, aliyeketi miguuni pake Yesu,
akasikiliza maneno yake.Lakini Martha alikuwa akihangaika kwa utumishi mwingi;
akamwendea, akasema, Bwana, huoni vibaya hivyo ndugu yangu alivyoniacha
nitumike peke yangu? Basi mwambie anisaidie.Bwana akajibu akamwambia, Martha,
Martha, unasumbuka na kufadhaika kwa ajili ya vitu vingi; lakini kinatakiwa
kitu kimoja tu; na Mariamu amelichagua fungu lililo jema, ambalo hataondolewa.”
Kwa mila na
tamaduni za kimashariki wewe na mimi tunge muhukumu Mariamu kama binti mvivu na
tungemkubali Martha kama mwanamke mchapakazi, lakini pale Martha alipoinua
kinywa chake kumuhukumu Mariamu Bwana katika hukumu yake isiyotarajiwa
anahukumu kuwa Martha ni changamoto kubwa sana na Mariamu ndiye yuko sahihi.
Martha alikuwa na makosa makubwa sana kuliko Mariamu, Martha alikuwa akimfokea
Yesu! BWANA HUONI VIBAYA? Ndugu yangu alivyoniacha nitumike peke yangu?
Kumsikiliza Yesu
ndio tukio la Heshima kubwa sana, na alikuwa akipokea Baraka kubwa za ushirika
na Yesu, ambapo Martha kwa sababu ya kulalamika kwake alikuwa na msongo tu wa
mawazo, haikuwa vibaya kuandaa kwaajili ya mgeni, lakini alijaa hukumu dhidi ya
Yesu na Ndugu yake Mariamu, na kwa sababu hiyo alipoteza point katika hukumu
kwa sababu ya manung’uniko
Wafilipi 2:14-15 “Yatendeni
mambo yote pasipo manung'uniko wala mashindano,mpate kuwa wana wa Mungu wasio
na lawama, wala udanganyifu, wasio na ila kati ya kizazi chenye ukaidi,
kilichopotoka; ambao kati ya hao mnaonekana kuwa kama mianga katika ulimwengu,”
Yesu hakumwambia
Martha akae chini, kwani alikuwa anafanya jambo jema, na wala hakumwambia
Mariamu inuka kwani naye alikuwa akifanya jambo jema, mmoja akimtumikia na
mwingine akisikiliza, wako wakristo na
watumishi wa Mungu ambao hutumika sana, na wako ambao huomba sana na kutafakari
wote wanaitenda kazi iliyo njema, kosa kubwa ni pale unapoanza kuwakosoa
wengine na kufikiri kuwa wewe ndiye bora zaidi kwa sababu unafanya hicho
unachikifanya, Jambo kubwa na la msingi na la muhimu ni uhusiano na Yesu
Kristo, na Mariamu alikuwa ameligundua hilo, na hakuna mtu angeweza kumtenga na
hilo, Mariamu kwa jicho la kibinadamu alionekana ni mvivu lakini kwa jicho la
Yesu Mariamu alikuwa anampenda Yesu, alichukua muda kuwa na Yesu kwake Yesu
alikuwa muhimu kuliko kupika, unalolifanya linaweza kuwa sio tatizo, lakini
tatizo ni pale unapoanza kuamsha kinywa kwaajili ya wengine, Uhusiano wetu na
Mungu ni jambo jema ambalo hakuna mtu anaweza kutuondolea. Mariamu alichagua
fungu jema na hakuna wa kumuondolea, Ukichagua ushirika na Yesu hakuna mtu
atakuondolea ushirika huo watakuondoa kwenye mengine lakini hakuna
kitakachokutenga na Upendo wake Kristo.
2.
Marko
9:38-40 “Yohana akamjibu, akamwambia, Mwalimu,
tulimwona mtu akitoa pepo kwa jina lako, ambaye hafuatani nasi; tukamkataza,
kwa sababu hafuatani nasi. Yesu akasema, Msimkataze, kwa kuwa hakuna mtu
atakayefanya mwujiza kwa jina langu akaweza mara kuninenea mabaya;kwa sababu
asiye kinyume chetu, yu upande wetu.”
Hakuna mtu
aliyekwenda kwa Yesu Kristo/Mungu akiwa anamshutumu mwingine na Yesu
akakubaliana naye hata siku moja, kila wakati katika maisha ya Yesu alipoletewa
kesi, Kesi hiyo iliwageukia walioleta, na hukumu kuwapata wao, katika tamaduni
za kikanisa na madhehebu watu hujidhania kuwa wao ni wao na wao ndio wenye Yesu
peke yao kama Yohana hapo, kwa hiyo walivyoona kuna anayetoa pepo kama wao
lakini si wa dhehebu lao alitaka kuwazuia kuwanyima kibali, Lakini Yesu alikosoa
vikali mtazamo wao.Wako watu wanaofikiri kuwa ni wao tu ndio wenye mamlaka au
hatimiliki na Yesu, wao ndio bora, tabia ya aina hii inamuuzi sana Mungu,
unaposhindana na kila mtu anayetumia jina la Yesu kwa kujifikiria kuwa wewe
ndio wa muhimu na unapaswa kulitumia jina hilo unajiweka kwenye hatari ya
kupingana na Yesu mwenyewe.
3.
Warumi
11:2-4 “Mungu hakuwasukumia mbali watu wake
aliowajua tokea awali. Au hamjui yale yaliyonenwa na maandiko juu ya Eliya?
Jinsi anavyowashitaki Waisraeli mbele za Mungu,Bwana, wamewaua manabii wako,
wamezibomoa madhabahu zako, nami nimesalia peke yangu, nao wananitafuta roho
yangu.Lakini ile jawabu ya Mungu yamwambiaje? Nimejisazia watu elfu saba
wasiopiga goti mbele ya Baali.”
Eliya alikuwa
nabii mkubwa sana wa Mungu, aliwahukumu waisrael kuwa wamewaua manabii wote wa
Mungu na kuvunja madhabahu, zote za Bwana na kuabudu baali na kuwa ni yeye
pakee amesalia (1Wafalme 19:10) Lakini
Mungu alimjibu kuwa wako wengi ambao hawajapiga goti lao kwa baali, Mungu
alikuwa anamthibitishia Eliya kuwa asijidhanie kuwa yuko pake yake Mungu ana
watu wengi, hukumu ya Mungu wakati wote huthibitisha kuwa sisi ni wanadamu na
hatuko sawa katika mitazamo yetu, Mungu ana jicho lake la kipekee katika
kuyatazama mambo na hivyo tunapaswa kuwa wanyenyekevu sana na kuacha
kuwashitaki watu wengine kwa Mungu.
4.
Katika mifano ya ufalme wa Mungu pia ambayo
imebeba siri nyingi za Mungu utaweza kuona imejaa hekima na maarifa na uweza wa
kiungu katika maamuzi ya namna ya kuhukumu, Yesu anafunua kuwa kuhukumu kwake
kutakuwa mara zote kukiwaacha watu midomo wazi yatakuwa ni maamuzi ambayo
yatawashangaza wengi kwa matokeo yake.
a. Farisayo na mtoza ushuru – Luka 18:9-14 “Akawaambia
mfano huu watu waliojikinai ya kuwa wao ni wenye haki, wakiwadharau wengine
wote. Watu wawili walipanda kwenda hekaluni kusali, mmoja Farisayo, wa pili
mtoza ushuru. Yule Farisayo akasimama akiomba hivi moyoni mwake; Ee Mungu,
nakushukuru kwa kuwa mimi si kama watu wengine, wanyang'anyi, wadhalimu,
wazinzi, wala kama huyu mtoza ushuru.Mimi nafunga mara mbili kwa juma; hutoa
zaka katika mapato yangu yote. Lakini yule mtoza ushuru alisimama mbali, wala
hakuthubutu hata kuinua macho yake mbinguni, bali alijipiga-piga kifua akisema,
Ee Mungu, uniwie radhi mimi mwenye dhambi.Nawaambia, huyu alishuka kwenda
nyumbani kwake amehesabiwa haki kuliko yule; kwa maana kila ajikwezaye
atadhiliwa, naye ajidhiliye atakwezwa.”
Katika mfano huu tunajifunza juu ya watu wawili
waliopanda kwenda hekaluni kusali, mmoja alikuwa farisayo kwa hiyo ni wazi kuwa
alikuwa myahudi wa madhehebu ya mafarisayo, alikuwa mcha Mungu na mtu
aliyemwamini Mungu, pia alikuwa mtii kwa sheria (Torati) na aliielewa vema, na
alikuwa mtu wa haki, hakutii tu sheria lakini alifanya zaidi ya sheria, kwa
mujibu wa torati waisrael walitakiwa kufunga mara moja tu siku moja kwa mwaka
(Siku ya upatanisho) lakini yeye alifunga mara mbili kila wiki kwa hiyo alizidisha na kufanya zaidi ya
sheria, Sheria ilimtaka mtu atoe fungu la kumi angalau ya sehemu Fulani tu ya
mapato yake lakini yeye alitoa sehemu ya kumi ya kila aina ya kipato (mapato
yangu yote) kwa hiyo hakuwa na dhambi, hakuwa myang’anyi, wala hakuwahi kudhulumu
mtu, wala hakuwahi kuzini, kwa msingi huu basi kama ingelikuwa ni wewe na mimi
farisayo huyu ni peponi moja kwa moja au tungekubaliana na sala yake na katika
hukumu hatungemuhesabia kuwa hana shida yoyote Lakini hitimisho la Hakimu mkuu
ni kuwa ajikwezaye atatushwa na ajishushae atakwezwa, Farisayo alikataliwa
tatizo lilikuwa ni nini katika hukumu hii? Alijihesabia haki, alijidhania ya
kuwa yeye ni mtakatifu, alijivuna, alipata kiburi cha kidini, hakufikiri kuwa
naye anahitaji msamaha wa Mungu na rehema zake, alijifikiri ya kuwa anaweza
kununua rehema za Mungu kwa matendo yake, alipiga vita wengine na kujiona ni
mkamilifu kwa sababu ya matendo yake na kiburi, Katika macho ya Mungu
alikataliwa Mungu huwapinga wenye kiburi na kuwapa neema wanyenyekevu, sio
hivyo tu moyo wake ulijaa dharau dhidi ya watu wengine na alikuwa hana upendo,
na zaidi ya yote alikalia kiti cha Mungu kwa kujifanya ndiye muhukumu,
Mathayo 7:1-5 “Msihukumu, msije mkahukumiwa ninyi. Kwa kuwa hukumu ile
mhukumuyo, ndiyo mtakayohukumiwa; na kipimo kile mpimiacho, ndicho
mtakachopimiwa.Basi, mbona wakitazama kibanzi kilicho ndani ya jicho la ndugu
yako, na boriti iliyo ndani ya jicho lako mwenyewe huiangalii? Au utamwambiaje
nduguyo, Niache nikitoe kibanzi katika jicho lako; na kumbe! Mna boriti ndani
ya jicho lako mwenyewe? Mnafiki wewe, itoe kwanza ile boriti katika jicho lako
mwenyewe; ndipo utakapoona vema kukitoa kile kibanzi katika jicho la ndugu yako.”
Mathayo
23:23-24 “Ole wenu waandishi na Mafarisayo,
wanafiki! Kwa kuwa mnalipa zaka za mnanaa na bizari na jira, lakini mmeacha
mambo makuu ya sheria, yaani, adili, na rehema, na imani; hayo imewapasa
kuyafanya, wala yale mengine msiyaache. Viongozi vipofu, wenye kuchuja mbu na
kumeza ngamia.”
Farisayo alikataliwa katika hukumu, hii ndio hukumu ya
kushangaza na isiyoweza kutabirika, tuna watu wengi sana wanaopanda kwenda
kusali, tuna watu wengi sana wanafunga, sio wazinzi, ni wasafi lakini usafi huo
ni wakwao wenyewe mioyoni mwao Mungu atawakataa, hukumu isiyotarajiwa
itatufunulia mengi sana, tutaona mambo ya ajabu ya watu wote wanaojifikiria
kuwa hawahitaji toba wamekamilika na wako safi lakini Yesu atawakataa hii
itatushangaza ni hukumu isiyotarajiwa. Wote wenye juhudi ya kutenda mema na
kudharau wengine kwa kujifikiri kuwa wao ni safi kuliko wengine, mahubiri yao
yamejaa hukumu, maneno yao yamejaa kuhukumu wengine na kujifikiri kuwa wao wako
sahihi na ni wasafi mno kumbe katika macho ya Mungu tunahitaji kuwa
wanyenyekevu, na ni muhimu kwetu kukumbuka kuwa matendo mema sio kitu cha kushangaza
kwa Mungu, tuliumbwa tukiwa wema, kwa hiyo unaweza kukuta mtu jhajamuamini Yesu
na akawa ana matendo mema, Mungu anataka tuipokee zawadi ya wokobu kwa neema na
kwa Imani na kutembea kwa neema na Imani, pasipo hiyo huwezi kumpendeza Mungu.
Waefeso 2:8-10
“Kwa maana mmeokolewa kwa neema, kwa njia ya imani;
ambayo hiyo haikutokana na nafsi zenu, ni kipawa cha Mungu; wala si kwa
matendo, mtu awaye yote asije akajisifu. Maana tu kazi yake, tuliumbwa katika
Kristo Yesu, tutende matendo mema, ambayo tokea awali Mungu aliyatengeneza ili
tuenende nayo.”
b. Wafanyakazi katika shamba za mizabibu –
Mathayo 20:1-16 “Kwa maana ufalme wa mbinguni
umefanana na mtu mwenye nyumba aliyetoka alfajiri kwenda kuajiri wakulima
awapeleke katika shamba lake la mizabibu. Naye alipokwisha kupatana na wakulima
kuwapa kutwa dinari, aliwapeleka katika shamba lake la mizabibu. Akatoka mnamo
saa tatu, akaona wengine wamesimama sokoni wasiokuwa na kazi; na hao nao
akawaambia, Enendeni nanyi katika shamba langu la mizabibu, na iliyo haki
nitawapa. Wakaenda. Akatoka tena mnamo saa sita na saa kenda, akafanya vile
vile. Hata kama saa kumi na moja akatoka, akakuta wengine wamesimama,
akawaambia, Mbona mmesimama hapa mchana kutwa bila kazi? Wakamwambia, Kwa sababu hakuna mtu aliyetuajiri.
Akawaambia, enendeni nanyi katika shamba la mizabibu. Kulipokuchwa, yule bwana
wa shamba akamwambia msimamizi wake, Waite wakulima, uwalipe ujira wao,
ukianzia wa mwisho hata wa kwanza. Na walipokuja wale wa saa kumi na moja,
walipokea kila mtu dinari. Na wale wa kwanza walipokuja, walidhani kwamba
watapokea zaidi; na hao pia wakapokea kila mtu dinari. Basi wakiisha kuipokea,
wakamnung'unikia mwenye nyumba, wakisema, Hao wa mwisho wametenda kazi saa moja
tu, nawe umewasawazisha na sisi tuliostahimili taabu na hari za mchana
kutwa.Naye akamjibu mmoja wao, akamwambia, Rafiki, sikudhulumu; hukupatana nami
kwa dinari? Chukua iliyo yako, uende zako; napenda kumpa huyu wa mwisho sawa na
wewe.Si halali yangu kutumia vilivyo vyangu kama nipendavyo? Au jicho lako
limekuwa ovu kwa sababu ya mimi kuwa mwema? Vivyo hivyo wa mwisho watakuwa wa
kwanza, na wa kwanza watakuwa wa mwisho”
Kuna mengi ya kujifunza pia kuhusu hukumu ya Mungu
katika mfano huu, sitaki kueleza kila kitu kilichomo katika mfano huu lakini mfano
huu unazungumzia mwenye nyumba, Biblia ya kiingereza inatumia neno landowner
yaani mwenye shamba ambaye alikuwa amekusudia kazi yake iishe, alitoka kutafuta
wafanya kazi, kwaajili ya shamba lile, siku zile malipo ya siku nzima yalikuwa
ni dinari, mwenye shamba aliajiri yeye mwenyewe aliajiri watu wa saa 12
alfajiri, kisha saa 6 kisha Saa 9 na kisha saa 11, na alipatana
nao kuwalipa (zingatia malipo kwa siku ni Dinari) au unaweza kuweka Elfu kumi
kwa siku, kwa kazi ya masaa 12. Hawa
wengine waliajiriwa tu kwa mapenzi ya mwenye shamba na aliwaahidi atawapa haki
yao, ilipofika jioni aliamuru wote walipwe akianza na wale wa saa 11 ambao
kimsingi walifanya kazi saa moja tu. Hii ni kwa sababu mwenye shamba ni
mkarimu, lakini walipolipwa wale walioajiriwa wa saa 12 alfajiri walilalamika
na kulaumu kuwa mwenye shamba hakuwa ametenda haki kwa sababu wako watu
wamefanya kazi saa moja tu na amewalipa sawa na wao waliofanya kazi tangu
asubuhi, Kwa hiyo walimuhukumu mwenye shamba kwa kuwa mkarimu na mwema. Hii inatufundisha
nini? Mungu anauwezo wa kuamua na lolote atakaloliamua sawa na ukarimu wake
huna haki ya kulalamika kwa sababu hajakudhulumu yeye huweza kuamua kumrehemu
yeyote yule na hatupaswi kuwa na wivu?
Warumi 9:18-21
“Basi, kama ni hivyo, atakaye kumrehemu humrehemu,
na atakaye kumfanya mgumu humfanya mgumu. Basi, utaniambia, Mbona angali
akilaumu? Kwa maana ni nani ashindanaye na kusudi lake?La! Sivyo, Ee binadamu;
wewe u nani umjibuye Mungu? Je! Kitu kilichoumbwa kimwambie yeye aliyekiumba,
Kwani kuniumba hivi? Au mfinyanzi je! Hana amri juu ya udongo, kwa fungu moja
la udongo kuumba chombo kimoja kiwe cha heshima, na kimoja kiwe hakina heshima?”
Waefeso 2:8-9 “Kwa maana mmeokolewa kwa neema, kwa njia ya imani; ambayo
hiyo haikutokana na nafsi zenu, ni kipawa cha Mungu; wala si kwa matendo, mtu
awaye yote asije akajisifu.”
Dinari inazungumzia wokovu, ambapo Mungu anaweza
kumuokoa mtu wakati wowote na thawabu ikawa moja kama alivyomuokoa mwizi pale
msalabani, lakini wale waliokuweko kazini wali lalamika mbona unatulipa
sawa? Mara kadhaa tumekasirika na kuona
wivu pale Mungu anapombariki mwingine, na kumuinua kuliko sisi kwa mapenzi yake
tunalalamika kwa sababu ya wivu, tunalalama na kumuona Mungu kama hayuko sawa
vile ni kama anapendelea wakati tunapojilinganisha na wengine na wakati
mwingine tumewapiga vita watu kwa sababu ya wivu wetu, tunafanya ujinga na
Mungu anazo sababu za kutuhukumu kwa kuhukumu wema wake na ukarimu wake, wokovu
ni kwa neema tu na kamwe hatuwezi kuutendea kazi, wale wanaofikiri kuwa kwa
kazi zao watapata kibali kikubwa kwa Mungu wanajidanganya mfano huu unafunua
vilevile hukumu isiyotarajiwa ya Mungu.
c. Mfano wa yule kaka mkubwa – Luka 15:11-32 “Akasema,
Mtu mmoja alikuwa na wana wawili; yule mdogo akamwambia babaye, Baba, nipe
sehemu ya mali inayoniangukia. Akawagawia vitu vyake. Hata baada ya siku si
nyingi, yule mdogo akakusanya vyote, akasafiri kwenda nchi ya mbali; akatapanya
mali zake huko kwa maisha ya uasherati. Alipokuwa amekwisha tumia vyote, njaa
kuu iliingia nchi ile, yeye naye akaanza kuhitaji. Akaenda akashikamana na
mwenyeji mmoja wa nchi ile; naye alimpeleka shambani kwake kulisha nguruwe.
Akawa akitamani kujishibisha kwa maganda waliyokula nguruwe, wala hapana mtu
aliyempa kitu. Alipozingatia moyoni mwake, alisema, Ni watumishi wangapi wa
baba yangu wanaokula chakula na kusaza, na mimi hapa ninakufa kwa njaa.
Nitaondoka, nitakwenda kwa baba yangu na kumwambia, Baba, nimekosa juu ya mbingu
na mbele yako; sistahili kuitwa mwana wako tena; nifanye kama mmoja wa
watumishi wako. Akaondoka, akaenda kwa babaye. Alipokuwa angali mbali, baba
yake alimwona, akamwonea huruma, akaenda mbio akamwangukia shingoni, akambusu
sana.Yule mwana akamwambia, Baba, nimekosa juu ya mbingu na mbele yako;
sistahili kuitwa mwana wako tena. Lakini baba aliwaambia watumwa wake, Lileteni
upesi vazi lililo bora, mkamvike; mtieni na pete kidoleni, na viatu miguuni;
mleteni ndama yule aliyenona mkamchinje; nasi tule na kufurahi; kwa kuwa huyu
mwanangu alikuwa amekufa, naye amefufuka; alikuwa amepotea, naye ameonekana.
Wakaanza kushangilia. Basi, yule mwanawe mkubwa alikuwako shamba na alipokuwa
akija na kuikaribia nyumba, alisikia sauti ya nyimbo na machezo. Akaita mtumishi
mmoja, akamwuliza, Mambo haya, maana yake nini? Akamwambia, Ndugu yako amekuja,
na baba yako amemchinja ndama aliyenona, kwa sababu amempata tena, yu mzima.
Akakasirika, akakataa kuingia ndani. Basi babaye alitoka nje, akamsihi.
Akamjibu baba yake, akasema, Tazama, mimi nimekutumikia miaka mingapi hii, wala
sijakosa amri yako wakati wo wote, lakini hujanipa mimi mwana-mbuzi, nifanye
furaha na rafiki zangu;lakini, alipokuja huyu mwana wako aliyekula vitu vyako
pamoja na makahaba, umemchinjia yeye ndama aliyenona. Akamwambia, Mwanangu,
wewe u pamoja nami sikuzote, na vyote nilivyo navyo ni vyako.Tena, kufanya
furaha na shangwe ilipasa, kwa kuwa huyu ndugu yako alikuwa amekufa, naye
amefufuka; alikuwa amepotea, naye ameonekana.”
Nauita mfano wa kaka mkubwa kwa sababu katika mtazamo wa
Mungu ndiye aliyekuwa na matatizo makubwa zaidi ya Mwana mpotevu, Baba wa mwana
mpotevu alikuwa anasikitika kumpoteza kijana wake na aliporejea nyumbani alilia
akamkumbatia na kumvika mavazi mazuri kisha akamfanyia sherehe kubwa, Kaka
mkubwa alikasirika, akasusa na kugoma kuingia ndani, akamuhukumu baba yake na
mdogo wake, alimshutumu kuwa mdogo wake huyo ametapanya mali pamoja na
makahaba, na baba yake ameonyesha ukirimu jambo ambalo hajawahi kulifanya kwa
kaka mkubwa, kwa hiyo alijawa na hasira, na wivu na kulaumu ukarimu wa baba
yake mfano huu kama mingine iliyotangulia unatahadharisha kuwa Mungu
atakapohukumu wanadamu atafanya mapinduzi ambayo wale wanaojifikiria kuwa ni
wenye haki watalia na kushangaa, wale wanaojifikiria kuwa hawajawahi kumkosea
Mungu kwa lolote, basi wanaweza kumkosea Mungu kwa kuhukumu wengine, au kwa
kumlaumu Mungu au maamuzi ya Mungu ya kikarimu, iko mifano Mingi ambayo muda
usingeliweza kutosha kuichanganua lakini unaanza kuelewa
Kwaajili ya Hukumu hizi za
kushangaza za Mungu, na tabia zake ni muhimu sana kuwa wanyenyekevu na kuogopa
sana hukumu ya Mungu, hakuna kitu kinatisha kama hukumu ya Mungu, wakati wote
kujifikiri kuwa sisi ndio tuko sawa na wenzetu hawako sawa, kunakuweka katika
hatari ya kuingia katika hukumu isiyoepukika na hukumu za kushangaza kwaajili
ya aina hii ya mtazamo ni lazima tukubali na kuelewa ya kuwa hata siku ya
mwisho siku ya hukumu Mungu akisema nimekusudia kuwarehemu watu wote na watu
wote nataka waingie peponi au katika ufalme wake je wewe na Mimi tutakubaliana
na hukumu hiyo? Tutaona kuwa Mungu amehukumu kwa haki? au tutadhani kuwa Mungu
ana upendeleo acha kujifikiri kuwa wewe ni bora zaidi kuliko wengine, acha kukomalia
makosa ya wengine Mungu nadhani anataka tushughulike na maisha yetu zaidi
kuliko ya wengine.
Mathayo 7:3-5 “Basi, mbona wakitazama
kibanzi kilicho ndani ya jicho la ndugu yako, na boriti iliyo ndani ya jicho
lako mwenyewe huiangalii? Au utamwambiaje nduguyo, Niache nikitoe kibanzi
katika jicho lako; na kumbe! Mna boriti ndani ya jicho lako mwenyewe? Mnafiki
wewe, itoe kwanza ile boriti katika jicho lako mwenyewe; ndipo utakapoona vema
kukitoa kile kibanzi katika jicho la ndugu yako.”
Je utaweza kuiepuka hukumu ya
Mungu? Ni hukumu isiyoepukika inatutaka tuwe wanyenyekevu sana sisi kama
wanadamu hatuna cha kujivuna katika jambo lolote lile, wakati wote tuombe
rehema na neema ya Mungu na kuendelea kumtafuta bwana kwa mioyo yetu yote, na
zaidi ya yote turuhusu wakati wote neno la Mungu lituhukumu na kutubu pale
linaposhughulika na maovu yetu, Mungu atatubariki na kwa neema yake
atatufunulia kweli yetu yote Bwana yu karibu na moyo uliopondeka tutembee kwa
unyenyekevu na kujishusha mbele za Mungu aliye hai.
Na Rev. Innocent Samuel Kamote
Mkuu wa wajenzi mwenye hekima
Tafadhali naomba maoni yako 0718990796