Alhamisi, 6 Machi 2025

Hukumu zake ni za kweli na za haki


Ufunuo 19:1-2 “Baada ya hayo nikasikia sauti kama sauti ya makutano mengi, sauti kubwa mbinguni, ikisema, Haleluya; wokovu na utukufu na nguvu zina BWANA MUNGU wetu. kwa kuwa hukumu zake ni za kweli na za haki; maana amemhukumu yule kahaba mkuu aliyeiharibu nchi kwa uasherati wake, na kuipatiliza damu ya watumwa wake mkononi mwake.”



Utangulizi:

Timothy John Evans (20 November 1924-9 March 1950)  alikuwa ni Dereva wa Roli huko Welsh, aliwahi kushitakiwa kwa kosa la kumuua mkewe Beryl pamoja na binti yake mdogo Geraldine, kwenye makazi yake huko Notting Hill, London nchini Uingereza, January 1950 Evans alikamatwa na kushitakiwa kwa kosa la mauaji ya Binti yake mdogo na mke wake na tarehe 9 March 1950 alihukumiwa kunyongwa mpaka kufa, wakati wa Kesi hiyo Evans alilalamika kuwa jirani yake wa ghorofa ya chini Bwana John Christie ambaye alikuwa ndiye shahidi namba moja wa mauaji hayo dhidi yake kwamba yeye ndiye muuaji wa mkewe na binti yake.

Miaka mitatu baadaye baada ya kunyongwa hadi kufa kwa Evance, ilikuja kubainika kuwa kweli muuaji alikuwa ni Bwana John Christie, ambaye pia aliuwa wanawake wengine katika matukio yanayofanana na lile,  katika nyumba ile ile, akiwemo mke wake Ethel, Bwana Christie alihukumiwa adhabu ya kifo, na alipokuwa anakaribia kunyongwa alikiri kuwa ni kweli yeye ndiye pia alikuwa mtu aliyehusika na kifo cha binti na mke wa Timothy John Evans, Mahakama kuu ilikuja kupitia upya kesi ya Bwana Evans mnamo mwaka 2004 na kubaini kuwa alihukumiwa kimakosa,  na hivyo kubatilisha maamuzi ya mtu ambaye alikwisha hukumiwa kifo na kunyongwa miaka 54 iliyopita!  

Kwa nini nimeanza na habari hizi za kusikitisha za Timothy Evans?  ni kwa sababu nataka kukuthibitishia kuwa katika moja ya maswala magumu sana duniani ni pamoja na swala la kusimamia haki au swala zima la kutoa hukumu za kweli na za haki, akielewa swala hili na ugumu wake huku akiwa na moyo wa kutaka kusimamia watu wa Mungu na kuwahukumu kwa haki Mfalme Suleimani aliwaza sana juu ya swala hili na kuamua kuwa atamuomba Mungu Hekima ili ahukumu watu hao kwa haki, Na Mungu alifurahishwa sana na ombi la Suleimani kwa sababu Mungu hafurahii udhalimu

1Wafalme 3:4-10 “Basi mfalme akaenda Gibeoni, ili atoe dhabihu huko; kwa kuwa ndipo mahali pa juu palipo pakuu. Sulemani akatoa sadaka elfu za kuteketezwa juu ya madhabahu ile. Na huko Gibeoni Bwana akamtokea Sulemani katika ndoto ya usiku; Mungu akamwambia, Omba utakalo nikupe. Sulemani akasema, Umemfanyia mtumwa wako Daudi baba yangu fadhili kuu, kadiri alivyoenenda mbele zako katika kweli, na katika haki, na katika unyofu wa moyo pamoja nawe; nawe umemwekea na fadhili hii kubwa, maana umempa mwana wa kuketi kitini pake kama ilivyo leo. Na sasa, Ee Bwana, Mungu wangu, umenitawaza niwe mfalme mimi mtumwa wako badala ya Daudi baba yangu; nami ni mtoto mdogo tu; sijui jinsi inipasavyo kutoka wala kuingia. Na mtumwa wako yu katikati ya watu wako uliowachagua, watu wengi wasioweza kuhesabiwa, wala kufahamiwa idadi yao, kwa kuwa ni wengi. Kwa hiyo nipe mimi mtumwa wako moyo wa adili niwahukumu watu wako, na kupambanua mema na mabaya; maana ni nani awezaye kuwahukumu hawa watu wako walio wengi? Neno hili likawa jema machoni pa Bwana, ya kuwa Sulemani ameomba neno hili.”

Kutoa haki sio jambo rahisi katika ulimwengu huu ulioharibika na unaotawaliwa na shetani, Mwanadamu ni kiumbe chenye upungufu na kwa sababu hiyo sio rahisi sana wakati mwingine mwanadamu kutoa haki, kwa sababu mtazamo wa kibinadamu unatofautiana sana na wa Mungu. Maandiko yanaonyesha wazi kuwa ni Yesu Kristo pekee ndiye atakayekuja kutoka hukumu ya haki kwa sababu Roho wa Bwana atakuwa juu yake, na haki itakuwa mshipi wa viouno vyake ona:-

Isaya 11:2-5. “Na roho ya Bwana atakaa juu yake, roho ya hekima na ufahamu, roho ya shauri na uweza, roho ya maarifa na ya kumcha Bwana; na furaha yake itakuwa katika kumcha Bwana; wala hatahukumu kwa kuyafuata ayaonayo kwa macho yake, wala hataonya kwa kuyafuata ayasikiayo kwa masikio yake; bali kwa haki atawahukumu maskini, naye atawaonya wanyenyekevu wa dunia kwa adili; naye ataipiga dunia kwa fimbo ya kinywa chake, na kwa pumzi ya midomo yake atawaua wabaya. Na haki itakuwa mshipi wa viuno vyake, na uaminifu mshipi wa kujifungia.”

Unaposoma kisa hicho hapo juu cha Bwana Timothy John Evans utaweza kubaini na kugundua kuwa sio watu wote walioko magerezani wako huko kwa haki, wengine waliingia magerezani kwa uonevu na kwa sababu ya kuongozwa na waamuzi ambao wanasukumwa na misisimko, hawana hekima, wanasikiliza upande mmoja ama hawafanyi uchambuzi wa kina au kwa sababu ya kukosekana kwa ushahidi unaojitosheleza, na kwa bahati mbaya hata makanisani ziko hukumu za namna mbalimbali zinazotolewa na hasa katika makanisa ya kiroho, hukumu hizo hutolewa wakati mwingine kwa misisimko na bila kuzingatia misingi ya haki na uongozi wa Roho wa Mungu na matokeo yake kumekuweko na watu wengi sana walioumizwa na kujeruhiwa mioyo, Lakini jambo mojawapo kubwa la kumshukuru Mungu ni kuwa Yeye Mungu wetu Hukumu zake ni za kweli na za haki.

Zaburi 119:136-138 “Macho yangu yachuruzika mito ya maji, Kwa sababu hawaitii sheria yako. Ee Bwana, Wewe ndiwe mwenye haki, Na hukumu zako ni za adili.Umeziagiza shuhuda zako kwa haki, Na kwa uaminifu mwingi.”

Tutajifunza somo hili Hukumu zake ni za kweli na haki kwa kuzingatia vipengele viwili vifuatavyo:-


·         Kwa nini wanadamu hawawezi kuhukumu kwa haki?

·         Hukumu zake ni za kweli na haki!


Kwa nini wanadamu hawawezi kuhukumu kwa haki?

Mwanadamu ni kiumbe mwenye upungufu na mipaka na kwa sababu hiyo katika kutoa hukumu anazingirwa na vikwazo kadhaa vinavyopelekea kushindwa kutenda haki, hii ni tofauti na mtazamo wa Mungu ambaye yeye hana mipaka ya kibinadamu na kwa sababu hiyo anaweza kufanya hukumu za kweli na za haki kwa sababu yeye anajua yote na hana upungufu wa wema yeye amejaa wema (Omnibenevole)  na ni mkamilifu, hana upendeleo wala haendeshwi na hisia, hana vikwazo vya kuona tofauti na wanadamu ambao wao wanaweza kuona kwa mitazamo ya nje.

1Samuel 16:7 “Lakini Bwana akamwambia Samweli, Usimtazame uso wake, wala urefu wa kimo chake; kwa maana mimi nimemkataa. Bwana haangalii kama binadamu aangaliavyo; maana wanadamu huitazama sura ya nje, bali Bwana huutazama moyo.”

Tunaweza kujiuliza maswali ni kwa nini Mwanadamu hawezi kuhukumu kwa haki? hapa kuna sababu kadhaa zinazomuathiri mwanadamu na sababu ni kwanini mwanadamu hawezi kuhukumu kwa haki?


1.        Wanadamu wana ufahamu finyu

 

Tangu anguko la mwanadamu mwanadamu amekuwa kiumbe mwenye mapungufu mengi na mojawapo ni ufinyu wa maarifa na ufahamu, kwa sababu hiyo mwanadamu hawezi kufahamu kweli zote, nia ya moyo wa mtu, msukumo wa mazingira  hali na ukweli wa mambo, moyo wa mwanadamu unatajwa katika maandiko kuwa una ugonjwa wa kufisha,  nia ya mwanadamu inaweza kuwa sahihi machoni pake tu lakini zaidi ya yote hata pamoja na uwepo wa Roho Mtakatifu maandiko yanakiri kuwa tunafahamu kwa sehemu tu mpaka wakati ule utimilifu utakapokuja kwa sababu ya ufahamu huo finyu anaathirika kimaamuzi

 

Yeremia 17:9-10 “Moyo huwa mdanganyifu kuliko vitu vyote, una ugonjwa wa kufisha; nani awezaye kuujua? Mimi, Bwana, nauchunguza moyo, navijaribu viuno, hata kumpa kila mtu kiasi cha njia zake, kiasi cha matunda ya matendo yake.”              

 

Mithali 14:12 “Iko njia ionekanayo kuwa sawa machoni pa mtu, Lakini mwisho wake ni njia za mauti.”                

 

1Wakorintho 13:12 “Maana wakati wa sasa tunaona kwa kioo kwa jinsi ya fumbo; wakati ule tutaona uso kwa uso; wakati wa sasa nafahamu kwa sehemu; wakati ule nitajua sana kama mimi nami ninavyojuliwa sana.”

 

2.       Wanadamu wana ubaguzi na upendeleo.

 

Wanadamu kwa kawaida wanathiriwa na uzoefu wao, tamaduni zao, na historia zao, na wakati mwingine hisia na chuki katika mioyo yao,  na ubaguzi usiokuwa rasmi, maswala kama haya ya kibinadamu yanapotangulizwa mbele katika hukumu yanaweza kupelekea mwanadamu asitende haki wakati wa kuhukumu, wakati mwingine mtu anaweza kuhukumiwa kwa sababu ya kabila yake tu, kwa sababu wewe ni msonjo basi unaweza kufikiriwa kuwa u mkorofi, au kwa sababu wewe ni mbondei unaweza kutafasiriwa kuwa una kiburi, au kwa sababu wewe ni mgogo au mhaya mtu anaweza kuhitimisha tu kuwa u mzinzi na mpenda ngono, au kwa sababu wewe ni mnyiramba unaweza kuhesabika kuwa u mtu katili na kama wewe u mmachame unaweza kufikiriwa kuwa una roho mbaya hukumu ya mwanadamu inaweza kutanguliwa na mitazamo mingi isiyo sahihi na ambayo sio ya kiungu na ama wakati mwingine mtu anayetangulia kushitaki anaweza kufikiriwa kuwa ndio yuko sahihi.

 

Yakobo 2:1-4 “Ndugu zangu, imani ya Bwana wetu Yesu Kristo, Bwana wa utukufu, msiwe nayo kwa kupendelea watu. Maana akiingia katika sinagogi lenu mtu mwenye pete ya dhahabu na mavazi mazuri; kisha akiingia na maskini, mwenye mavazi mabovu; nanyi mkimstahi yule aliyevaa mavazi mazuri, na kumwambia, Keti wewe hapa mahali pazuri; na kumwambia yule maskini, Simama wewe pale, au keti miguuni pangu,je! Hamkufanya hitilafu mioyoni mwenu, mkawa waamuzi wenye mawazo mabovu?

               

Mithali 18:17 “Ajiteteaye kwanza huonekana kuwa ana haki; Lakini jirani yake huja na kumchunguza.”               

 

3.       Mwanadamu awaye yote ana asili ya dhambi.

 

Uwezo wa mwanadamu wa kuhukumu umeathiriwa na dhambi, dhambi inaweza kutuelekeza katika ubinafsi, hofu, ujinga na umimi, pia dhambi inaaathiri maisha yetu na kutufanya tujawe na kiburi na hata hali ya kutokutenda haki, na kwa sababu hiyo mwenendo wetu katika utoaji wa haki unaathiriwa na dhambi na kwahiyo wakati mwingi tunashindwa kusimama katika haki na kutohukumu kwa haki na kweli

 

Warumi 3:10-12, 23 “kama ilivyoandikwa, ya kwamba, Hakuna mwenye haki hata mmoja. Hakuna afahamuye; Hakuna amtafutaye Mungu. Wote wamepotoka, wameoza wote pia; Hakuna mtenda mema, la! Hata mmoja.23 “kwa sababu wote wamefanya dhambi, na kupungukiwa na utukufu wa Mungu;          

 

Yakobo 4:12 “Ndugu, msisingiziane; amsingiziaye ndugu yake, au kumhukumu ndugu yake, huisingizia sheria na kuihukumu sheria. Lakini ukiihukumu sheria, huwi mtenda sheria, bali umekuwa hakimu. Mtoa sheria na mwenye kuhukumu ni mmoja tu, ndiye awezaye kuokoa na kuangamiza. U nani wewe umhukumuye mtu mwingine?      

 

4.       Mwanadamu ana uoni hafifu

 

Uwezo wetu wa kuona mambo kamwe hauwezi kufananishwa na namna Mungu anavyoona mambo, yale tunayoyana sisi tunaona sehemu ndogo sana ya picha, wakati Mungu anaona picha zima kuanzia mwanzo, kati hadi mwisho, lakini kama haitoshi anaiona dhamira kwa mbali kwa sababu hiyo mwanadamu anakosa na kupoteza haki ya kuwa na hukumu za kweli na za haki, Mungu anauwezo wa kumuona mtu akali mbali mwanadamu hana uwezo huo

 

Ayubu 38:1-2 “Ndipo Bwana akamjibu Ayubu katika upepo wa kisulisuli, na kusema, Ni nani huyu atiaye mashauri giza Kwa maneno yasiyo na maarifa?

 

Isaya 55:8-9 “Maana mawazo yangu si mawazo yenu, wala njia zenu si njia zangu; asema Bwana. Kwa maana kama vile mbingu zilivyo juu sana kuliko nchi, kadhalika njia zangu zi juu sana kuliko njia zenu, na mawazo yangu kuliko mawazo yenu.”

 

Luka 15:17-20 “ Alipozingatia moyoni mwake, alisema, Ni watumishi wangapi wa baba yangu wanaokula chakula na kusaza, na mimi hapa ninakufa kwa njaa. Nitaondoka, nitakwenda kwa baba yangu na kumwambia, Baba, nimekosa juu ya mbingu na mbele yako; sistahili kuitwa mwana wako tena; nifanye kama mmoja wa watumishi wako. Akaondoka, akaenda kwa babaye. ALIPOKUWA ANGALI MBALI, BABA YAKE ALIMWONA, AKAMWONEA HURUMA, akaenda mbio akamwangukia shingoni, akambusu sana.”    

 

5.       Mwanadamu ana misukumo ya kihisia.

 

Kila mwanadamu ameumbwa na misikuko ya kihisia kama hasira, woga, wivu, na kadhalika misukumo hiyo ya kihisia inaweza kwa kiasi kikubwa sana kuathiri utoaji wa hukumu na hivyo kumfanya mwanadamu asihukumu kwa haki na kweli, tofauti na Mungu ambaye maandiko yanamtaja kuwa mwingi wa rehema na asiye mwepesi wa hasira

 

Mithali 29:11. “Mpumbavu hudhihirisha hasira yake yote; Bali mwenye hekima huizuia na kuituliza.”

 

Yakobo 1:19-20 “Hayo mnajua, ndugu zangu wapenzi. Basi kila mtu na awe mwepesi wa kusikia, bali si mwepesi wa kusema; wala kukasirika; kwa maana hasira ya mwanadamu haiitendi haki ya Mungu.

 

Zaburi 145:8-9 “Bwana ana fadhili, ni mwingi wa huruma, Si mwepesi wa hasira, ni mwingi wa rehema, Bwana ni mwema kwa watu wote, Na rehema zake zi juu ya kazi zake zote.”

 

6.       Wanadamu wana viwango visivyowiana

 

Viwango vya wanadamu kuhusu haki na uadilifu  havilingani au haviko katika uwiano sawa katika tamaduni moja na tamaduni nyingine, wakati kule Sumbawanga, ukiingia katika shamba la mtu na kukata mahindi ya kuchoma ukawasha moto na kujichomea ukala mwenye shamba akikukuta hawezi kukudhuru kwa sababu anajua ulikuwa na njaa, jambo kama hilo huko Muheza, Tanga, linaweza kuhesabika kuwa ni wizi unaoambatana na dharau ya hali ya juu kwamba mahindi uibe afu kisha uchome humo humo ndani ya shamba, Mungu anakusudia kila mwanadamu awe mtenda haki na haki kwake haiathiriwi na mazingira au tamaduni, viwango vya Mungu vimenyooka havuathiriwi na geografia wala mazingira.

 

Muhubiri 3:16-18 “ Zaidi ya hayo, nikaona tena chini ya jua ya kwamba, Mahali pa hukumu upo uovu, Na mahali pa haki upo udhalimu. Nikasema moyoni mwangu, Mungu atawahukumu wenye haki na wasio haki; kwa kuwa kuna wakati huko kwa kila kusudi na kwa kila kazi. Nikasema moyoni mwangu, Ni kwa sababu ya wanadamu, ili Mungu awajaribu, nao waone ya kuwa wao wenyewe wafanana na wanyama.”              

 

Mika 6:8 “Ee mwanadamu, yeye amekuonyesha yaliyo mema; na Bwana anataka nini kwako, ila kutenda haki, na kupenda rehema, na kwenda kwa unyenyekevu na Mungu wako!

 

7.       Mwanadamu anakosa upendo uliokamilika

 

Hukumu ya mwanadamu wakati mwingine inapungukiwa na upendo uliokamilika na kwa sababu hiyo wakati wa kuhukumu wanakosa rehema za Mungu, au rehema anayokuwa nayo Mungu wakati wa kushughulika na wanadamu, ukweli tukikosa rehema na upendo tunapoteza maana kabisa

 

1Wakorintho 13:1-3 “Nijaposema kwa lugha za wanadamu na za malaika, kama sina upendo, nimekuwa shaba iliayo na upatu uvumao. Tena nijapokuwa na unabii, na kujua siri zote na maarifa yote, nijapokuwa na imani timilifu kiasi cha kuweza kuhamisha milima, kama sina upendo, si kitu mimi. Tena nikitoa mali zangu zote kuwalisha maskini, tena nikijitoa mwili wangu niungue moto, kama sina upendo, hainifaidii kitu.”       

 

Mathayo 7:2 “Msihukumu, msije mkahukumiwa ninyi. Kwa kuwa hukumu ile mhukumuyo, ndiyo mtakayohukumiwa; na kipimo kile mpimiacho, ndicho mtakachopimiwa.”

 

8.       Mwanadamu hufanya makosa

 

Wakati Mungu huwa habadiliki wala hakosei, mwanadamu ana tabia ya kubadilika badilika na kufanya makosa, kutokana na hali hii ya uanadamu mara kadhaa watu wamefanya makosa, kumbuka kile kisa cha Timothy John Evans ambaye alinyongwa licha ya kuwa yeye ndiye aliyepoteza mke wake na binti yake mdogo, ona makosa yaliyofanyika! Kumbuka jinsi Pilato alivyonawa mikono na kuwa na uhakika kuwa Yesu hakuwa na hatia lakini kumbuka kuwa ni yeye aliyetoa hukumu ya Yesu kusulubiwa kwa sababu ya mashinikizo ya kisiasa na ubinadamu, kwa kweli unapojihusisha na hukumu au maneno ya kusikia na mambo tata na yasiyo na ushahidi, usikimbilie kuhukumu na badala yake tuiendee hukumu kwa unyenyekevu mkubwa, tegemea hekima ya Mungu au muombe Mungu hekima kila uwapo katika nafasi inayokuhusisha kufanya maamuzi, vinginevyo utakuja kujikuta unajuta                

 

Mithali 3:5-7 “Mtumaini Bwana kwa moyo wako wote, Wala usizitegemee akili zako mwenyewe; Katika njia zako zote mkiri yeye, Naye atayanyosha mapito yako. Usiwe mwenye hekima machoni pako; Mche Bwana, ukajiepushe na uovu.”

 

Hesabu 23:19 “Mungu si mtu, aseme uongo; Wala si mwanadamu, ajute; Iwapo amesema, hatalitenda? Iwapo amenena, hatalifikiliza?

Mungu anatuagiza katika neno lake kuacha kuhukumu kwa mitazamo ya kawaida, lakini Mungu anatutaka tuhukumu kwa usahihi

Yohana 7:24 “Basi msihukumu hukumu ya macho tu, bali ifanyeni hukumu iliyo ya hakileo vilio vya haki vinasikika kila kona watu wakiwa wameonewa na kutendewa visivyo haki, unapoona leo hii utitiri wa makanisa pamoja na dini kugeuzwa kuwa biashara au kuwepo kwa uamsho mkubwa lakini wengine wameondoka katika makanisa yao na kupoteza haki zao zote kwa sababu ya kuhukumiwa vibaya, katika kazi zetu hizi za kichungaji na kazi ya Mungu ndugu wa uongo wako kila kona na unaweza wakati mwingine kwa sababu ya siasa za kidini, ukachomekewa na kuonewa na kuhukumiwa pasipo haki na kwa kweli wakati mwingine makosa ya kibinadamu hayo yamewafanya watu wengine kuishi maisha ya kuteseka na kuumizwa sana huku wakisubiria wakati wa Mungu ufike, Je unamkumbuka Yusufu Mwana wa Israel aliyewekwa gerezani kwa sababu ya kushutumiwa kuwa alitaka kumbaka mke wa Potifa na ushahidi ulikuwa ni vazi lake aliloliacha chumbani ni nani ambaye angeliweza kuingilia kati ili haki ya Yusufu ipatikane?

Ukweli ni kuwa yuko Mungu, Ni Mungu peke yake ambaye Hukumu zake ni za kweli na za haki, uko wakati utafika katika maisha yako uatamshangilia Mungu na kusema haleluya kweli nimetambua kuwa hukumu zako ni za kweli na za haki. Abrahamu alimtambua Mungu kama mhukumu ulimwengu na alipokuwa akiomba aliamini kuwa Mungu atatenda haki na atahukumu kwa haki

Mwanzo 18:25-26 “Hasha usifanye hivyo, ukamwue mwenye haki pamoja na mwovu, mwenye haki awe kama mwovu. Hasha; MHUKUMU ULIMWENGU WOTE ASITENDE HAKI? BWANA akasema, Nikiona katika Sodoma wenye haki hamsini mjini, nitapaacha mahali pote kwa ajili yao.”

Mungu anaweza kuwahukumu adui zetu sawasawa na haki yake na neno lake, hata kama kuna wakati wanaonekana kustawi usiogope washindanao na Bwana watapondwa kabisa Bwana ataihukumu miisho ya nchi, naye atampa mfalme wake nguvu na kuitukuza pemba ya masihi wake Asante sana Mungu mwingi wa rehema, asante sana Mungu mwenye haki asante sana kwa fadhili zako asante sana kwa sababu kati kati ya miungu hakuna aliye kama wewe ni wewe pekee yako mwenye rula isiyopinda, ni wewe peke yako unayeweza kuishangaza dunia ni wewe peke yako uliyempa mtumwa wako uvumilivu, ni wewe peke yako uliyempa mtumwa wako kuvumilia adui zake ni wewe peke yako uhukumuye kwa haki fadhili zina wewe milele na milele!, haki imesimama na kisasi kimelipwa na sasa Bwana utamwangalia mtumishi wake na kumrejeshea kila kilichopotezwa na adui kwa sababu ya uonevu, Hakuna aliye mtakatifu kama Bwana Kwa maana hakuna yeyote ila wewe, wala hakuna mwamba kama Mungu wangu!, walinena wakatakabari, walijivuna wakatoa maneno ya kiburi vinywani mwao Lakini hawakujua kuwa Mungu ni mwingi wa maarifa  nay a kuwa matendo hupimwa nay eye, kwa mizani yake isiyo na upendeleo, nguvu za waonevu zimevunjika, waliojikwaa wamepigwa hofu, walioshiba wanaona njaa, Kwa sababu aliye mnyone amesimikwa na Bwana, yeye hulinda miguu ya watakatifu, na hunyamazisha miguu ya wqaovu gizani, washinanao naye watapondwa Bwana atawapiga kwa radi, yeye anaweza kuhukumu hata mwisho wan chi, yeye yu aweza kumtukuza masihi wake! ni yeye pekee Mungu wetu na Mungu wangu, Mungu wa baba zangu Mungu mwenye kuogofya Mungu ahukumuye kwa kweli na kwa haki, humu zako zimenifurahisha, matendo yako yamependezwa nami ninakupenda kuliko wazee wangu, maana rehema zako na fadhli zako ni za milele, hukumwacha mtakatifu wako ane uharibifu! Wala mwenye haki wako aende kuzimu fadhili zina wewe milelele na milele! Na hukumu zako nimezithibitisha haki kwako haipindi, kweli kwako zimenyooshwa tuma malaika zako walitangaze hili, tuma makerubi walibandike na maserafi waliimbe kwamba utukufu na nguvu zina wewe na hukumu zako ni za kweli na za haki hata milele na milele! (Zaburi ya Mwandishi).

Hukumu zake ni za kweli na haki!

Ufunuo 19:1-2 “Baada ya hayo nikasikia sauti kama sauti ya makutano mengi, sauti kubwa mbinguni, ikisema, Haleluya; wokovu na utukufu na nguvu zina BWANA MUNGU wetu. kwa kuwa hukumu zake ni za kweli na za haki; maana amemhukumu yule kahaba mkuu aliyeiharibu nchi kwa uasherati wake, na kuipatiliza damu ya watumwa wake mkononi mwake.”

Tofauti na Wanadamu ambao tumejifunza kwamba kwa asili wanaathiriwa na maswala mengi hivyo uwezo wao wa kutenda haki au kufanya hukumu za kweli na za haki hauwezi kukidhi vigezo na utendaji wa Mungu, kwa upande wake yeye Mungu anaweza kufanya hukumu za kweli na za haki kwa sababu zifuatazo;-

1.       Yeye anajua yote – kwa asili Mungu anajua mambo yote (Omniscience), anajua kila kitu tangu wakati uliopita uliopo na ujao, na zaidi ya yote anaijua nia ya mwanadamu moyo wake na mazingira yake, ujuzi wake mkamilifu unamfanya asiwe na makosa katika uchunguzi wala upelelezi, wakati mwanadamu anafungwa na mipaka na kuhitaji ushahidi Mungu yeye haitaji ushahidi, yeye mwenyewe ana uwezo mkubwa sana wa kufanya uchunguzi na kumjua mwanadamu katika kila jambo kuanzia kuingia kwake na kutoka kwake!

 

Zaburi 139:1-4 “Ee Bwana, umenichunguza na kunijua. Wewe wajua kuketi kwangu na kuondoka kwangu; Umelifahamu wazo langu tokea mbali. Umepepeta kwenda kwangu na kulala kwangu, Umeelewa na njia zangu zote. Maana hamna neno ulimini mwangu Usilolijua kabisa, Bwana.”

 

2.       Yeye ni mwema – Kwa asili Mungu ni mwema  na mwaminifu, wema wake hauna mipaka (omnibenevolence) kutokana na tabia yake ya asili ya wema unamfanya yeye Mungu kuwa mwenye haki katika njia zake zote bila dosari kama za kibinadamu, na kwa sababu hiyo anaweza kufanya maamuzi yasiyo na utata, Licha ya kuwa mwema yeye pia ni chanzo cha wema wote, ni chanzo cha upendo, na haki pia, anapohukumu yeye anahukumu katika haki kwa sababu ya tabia yake na mwenendo wake uliojawa na uadilifu, usio na hofu wala upendeleo, ulio na rehema na neema, na wenye viwango vya juu kabisa vya haki

 

Zaburi 145:17 “Bwana ni mwenye haki katika njia zake zote, Na mwenye fadhili juu ya kazi zake zote.”

 

Zaburi 100:5 “Kwa kuwa Bwana ndiye mwema; Rehema zake ni za milele; Na uaminifu wake vizazi na vizazi.

 

3.       Yeye hatazami kama wanadamu watazamavyo – Njia za Mungu ziko juu sana haziwezi kamwe kulinganishwa na njia za wanadamu kwa sababu hiyo yeye hufanya mambo katika njia na namna tofauti sana na ile inayodhaniwa au kukusudiwa na wanadamu,  Yeye ni mwenye haki na wanadamu ni waongo

 

Isaya 55:8-9 “Maana mawazo yangu si mawazo yenu, wala njia zenu si njia zangu; asema Bwana. Kwa maana kama vile mbingu zilivyo juu sana kuliko nchi, kadhalika njia zangu zi juu sana kuliko njia zenu, na mawazo yangu kuliko mawazo yenu.”               

Hitimisho!

Hukumu zake ni za kweli na za haki ni usemi maarufu ambao umejirudia mara kadhaa katika maandiko ukionyesha kuwa maamuzi ya Mungu ni ya kweli, ya haki ya adilifu, hii maana yake ni kwakuwa yeye ni Mungu uweza wake wa kiungu unaaminika kukaa katika misingi ya kutokuonea mtu wala kufanya mambo kwa upendeleo wala kupokea uso wa mwanadamu, hakuna nafasi ya kutazama mambo kwa mtazamo usio sahihi kama wanadamu yeye uhukumu kwa ukamilifu

Ufunuo 16:5-7 “Nami nikamsikia malaika wa maji akisema, Wewe u mwenye haki, uliyeko na uliyekuwako, Mtakatifu, kwa kuwa umehukumu hivi; kwa kuwa walimwaga damu ya watakatifu na ya manabii, nawe umewapa damu wainywe; nao wamestahili. Nikaisikia hiyo madhabahu ikisema, Naam, Bwana Mungu Mwenyezi, ni za kweli, na za haki, hukumu zako.”

Zaburi 19:9-10 “Kicho cha Bwana ni kitakatifu, Kinadumu milele. Hukumu za Bwana ni kweli, Zina haki kabisa. Ni za kutamanika kuliko dhahabu, Kuliko wingi wa dhahabu safi. Nazo ni tamu kuliko asali, Kuliko sega la asali.

Kwa kujua jinsi ambavyo Mungu uhukumu vizuri na kwa haki na kwa rehema Daudi alichagua kuangukia katika hukumu ya Mungu kwa sababu alielewa Mungu atamhukumu kwa rehema

1Nyakati 21:9-13 “Naye Bwana akanena na Gadi, mwonaji wake Daudi, akisema, Nenda ukanene na Daudi, ukisema, Bwana asema hivi, Nakuwekea mambo matatu; katika haya ujichagulie moja, nikutendee hilo. Basi Gadi akamwendea Daudi, akamwambia, Bwana asema hivi, Kubali upendavyo; miaka mitatu ya njaa; au miezi mitatu kuangamia mbele ya adui zako, ukipatwa na upanga wa watesi wako; au siku tatu upanga wa Bwana, yaani tauni katika nchi, na malaika wa Bwana akiharibu kati ya mipaka yote ya Israeli. Haya basi ufikiri ni jawabu gani nimrudishie yeye aliyenituma.Naye Daudi akamwambia Gadi, Nimeingia katika mashaka sana; basi sasa na nianguke katika mkono wa Bwana; kwa kuwa rehema zake ni nyingi sana; wala nisianguke katika mkono wa wanadamu.”

Siku zote wanadamu wanapokuhukumu kwa njia isiyo halali usilalamike Mwambie Bwana uwasamehe kwa maana hawajui walitendalo, Ni Mungu peke yake anapohukumu ndiye anayejua anachokitenda, lakini wanadamu hawajui walitendalo wao wana mipaka najua wako watu wengi sana wameumizwa serikalini, makanisani, mimi pia niliwahi kuumizwa, niliwahi kuhukumiwa, niliwahi kusemwa vibaya wanadamu walinihukumu sawa na midomo ya washitaki zangu, lakini nilinyamaza na namshukuru Mungu kwani amenifundisha mengi sasa najua wazi kuwa Mungu wangu ni Mungu mwenye kuogopwa sana kwa sababu Hukumu zake ni za kweli na za haki, kama Bwana alivyonitendea mimi akutendee na wewe pia, naelewa na nilielewa tangu zamani ya kuwa hakumwacha mtu aliwatendea haki wote walioonewa, Haki yako itapatikana kwa Mungu aliye hai usikate tamaa endelea kumtumainia yeye na kumuachia yeye naye atakushangaza, amenishangaza mara nyingi na namuomba Mungu akushangaze na wewe pia.

Zaburi 105:14-15 “Hakumwacha mtu awaonee, Hata wafalme aliwakemea kwa ajili yao. Akisema, Msiwaguse masihi wangu, Wala msiwadhuru nabii zangu.”

Rev. Innocent Samuel Kamote

Mkuu wa wajenzi mwenye Hekima!

Jumatano, 26 Februari 2025

Kwa kuvisoma vitabu!


Andiko Kuu: Danieli 9:1-2 “Katika mwaka wa kwanza wa Dario, mwana wa Ahasuero, wa uzao wa Wamedi, aliyetawazwa kuwa mfalme juu ya milki ya Wakaldayo; katika mwaka wa kwanza wa kumiliki kwake, mimi Danielii, kwa kuvisoma vitabu, nalifahamu hesabu ya miaka, ambayo neno la Bwana lilimjia Yeremia nabii, ya kuutimiza ukiwa wa Yerusalemu, yaani, miaka sabini.”



Utangulizi

Ni muhimu kufahamu kuwa moja ya njia kubwa ya kijiongezea ufahamu na kukua katika Hekima maarifa na hali ya kiroho ni Pamoja na kuwa na tabia ya kujisomea vitabu, Neno la Mungu linahimiza Wakristo kuwa na bidii ya kusoma vitabu, hasa vile vinavyoweka wazi mapenzi ya Mungu na maarifa muhimu kwa maisha yetu. Danieli aligundua wakati wa ukombozi wa Israeli kwa kusoma vitabu, kwa kuvisoma vitabu alipata ufahamu, jambo linaloonyesha kuwa kusoma kunafungua macho ya kiroho kiakili na kiufahamu na kutufanya tujue wakati na mapenzi ya Mungu. Sio hivyo tu Walimu na wahudumu wa neno la Mungu wanapaswa kuwa na bidii katika kusoma ili wawe na ujuzi wa mambo mengi na ni ukweli ulio wazi kuwa ujuzi mwingi umewekwa katika Makala mbali mbali duniani, kwa hiyo kusoma vitabu ni mapenzi ya Mungu na maandiko yanahimiza kuwa na tabia hiyo:-

1Timotheo 4:13-16 “Hata nitakapokuja, ufanye bidii KATIKA KUSOMA na kuonya na kufundisha. Usiache kuitumia karama ile iliyomo ndani yako, uliyopewa kwa unabii na kwa kuwekewa mikono ya wazee. Uyatafakari hayo; ukae katika hayo; ili kuendelea kwako kuwe dhahiri kwa watu wote. Jitunze nafsi yako, na mafundisho yako. Dumu katika mambo hayo; maana kwa kufanya hivyo utajiokoa nafsi yako na wale wakusikiao pia

Unaweza kuona Paulo mtume alimtia moyo Muhubiri wa injili, mtenda kazi pamoja naye na mwangalizi wa makanisa nyakati za kanisa la kwanza, Timotheo kwamba afanye bidii katika kusoma na kuonya na kufundisha, Kwa hiyo utakubaliana nami ya kuwa kusoma ni sehemu muhimu ya maisha ya mtumishi wa Mungu ni sehemu muhimu ya huduma. Tutajifunza somo hili muhimu lenye kichwa Kwa kuvisoma vitabu Kwa kuzingatia vipengele vitatu vifuatavyo:-

 

  • Kwa kuvisoma vitabu
  • Mifano ya watu walionufaika kwa kuvisoma vitabu.
  • Ufanye bidii katika kusoma.

 

 

Kwa kuvisoma vitabu

Tumeona katika utangulizi wa ujumbe huu ya kuwa Daniel aligundua wakati muhimu wa Ukombozi wa Taifa lake na kuchukua hatua ya kumuomba Mungu na kumkumbusha juu ya swala Hilo, hii inatufungua akili ya kuwa yako mambo ambayo ni ya kiroho kabisa na ya kimwili na kitaifa ambayo yanaweza kuwa bayana kwetu kupitia kusoma, Daniel alikuwa Nabii na Kuna mambo ambayo aliweza kumuomba Mungu ili afunuliwe, lakini maswala mengine aliyapata Kwa kusoma vitabu tena vya manabii kama Yeremia aliyekuwa Nabii kabla ya yeye na aliyekuwa kama yeye tu

Danieli 9:1-2 “Katika mwaka wa kwanza wa Dario, mwana wa Ahasuero, wa uzao wa Wamedi, aliyetawazwa kuwa mfalme juu ya milki ya Wakaldayo; katika mwaka wa kwanza wa kumiliki kwake, mimi Danielii, kwa kuvisoma vitabu, nalifahamu hesabu ya miaka, ambayo neno la Bwana lilimjia Yeremia nabii, ya kuutimiza ukiwa wa Yerusalemu, yaani, miaka sabini.”

Kumbe basi Kwa kusoma vitabu tunaweza kupata mambo mengi ya muhimu, Kwa ufupi Kuna faida kubwa nyingi mno zitokanazo na kusoma vitabu hapa nitataja baadhi Lakini kabla ya kutaja nitaelezea kwa kifupi vitabu ni nini hasa?:-

Kitabu au vitabu ni mkusanyiko wa maneno yaliyowekwa pamoja kwa kusudi la kufunga au kuainisha au kutaarifu ujumbe Fulani, au fundisho Fulani au maelekezo Fulani, ambayo yamekusudiwa kuwafikia watu kwa muda Fulani au maisha yote, kitabu kinaweza kusomwa au kuandikwa, inaweza kuwa ni kazi Fulani ambayo Mungu anataka iwekwe kwa kusudi Fulani 

Yohana 1:11 “Nalikuwa katika Roho, siku ya Bwana; nikasikia sauti kuu nyuma yangu, kama sauti ya baragumu, ikisema, Haya uyaonayo uyaandike katika chuo, ukayapeleke kwa hayo makanisa saba: Efeso, na Smirna, na Pergamo, na Thiatira, na Sardi, na Filadelfia, na Laodikia.”

Kitabu kinaweza kuwa maandhishi yanayoanzia ukurasa mmoja na zaidi ambayo yamefungwa katika kifuniko kimoja, au mgawanyo mkubwa sana wa vifungu, utenzi, kweli, jumbe, sheria, taratibu, maonyo au maelekezo. Zamani sana vitabu viliandikwa katika magombo ya ngozi na kwa sababu hiyo pia viliitwa chuo

Luka 4:16-17 “Akaenda Nazareti, hapo alipolelewa; na siku ya sabato akaingia katika sinagogi kama ilivyokuwa desturi yake, akasimama ili asome. Akapewa chuo cha nabii Isaya, akakifungua chuo, akatafuta mahali palipoandikwa,”

Pia viliandikwa katika mawe, na vilianza kujulikana kama vitabu kwenye karne nne baada ya Kristo 400 AD  na Karatasi zilikuja kugunduliwa kwenye karne ya 15 hivi  kwa sababu hiyo hata Biblia maana yake imetokana na neno la asili la kiyunani Biblos ambalo maana yake ni mkusanyiko wa vitabu au maktaba yaani Library, na katika biblia kujna mkusanyiko wa vitabi 66 yaani 39 katika agano la kale na 27 katika agano jipya, Biblia ni Library au maktaba ya neno la Mungu, nan je yako viko vitabu vingine, hata somo hili na jumbe ninazohubiri kwa njia ya maandishi ni vitabu    

Ndani ya vitabu kuna maarifa, kukuza ufahamu, kujenga uadilifu, kutia moyo, kuburudisha na kukuandaa kwaajili ya ubunifu, katika ulimwengu wa sasa vitabu vinaweza kuwa katika mtindo wa nakala laini zinazopatikana katika mtindo wa kidigitali maandiko yanapotutia moyo kujisomea ni pamoja na makala hizo. Baadhi ya faida zipatikanazo katika vitabu baadhi ni kama ifuatavyo:-

               

  1. Ufahamu wa Mapenzi ya Mungu

Danieli alipata maarifa kuhusu miaka 70 ya utumwa kwa wana wa Israel huko Babeli na kutambua kuwa wakati huo ulikuwa umetimia na hivyo akaanza kufunga na kuomba ili Mungu amfunulie nini cha kufanya, aliweza kuyajua mapenzi hayo ya Mungu kwake na taifa lake kwa kusoma unabii wa Yeremia yaani kwa kusoma vitabu vya manabii waliomtangulia  

Yeremia 25:8-12 “Basi Bwana wa majeshi asema hivi, Kwa kuwa hamkuyasikiliza maneno yangu, angalieni, nitapeleka watu na kuzitwaa jamaa zote za upande wa kaskazini, asema Bwana, nami nitatuma ujumbe kwa Nebukadreza, mfalme wa Babeli, mtumishi wangu, nami nitawaleta juu ya nchi hii, na juu yao wakaao ndani yake, na juu ya mataifa haya yote yaliyopo pande zote; nami nitawaangamiza kabisa, na kuwafanya kitu cha kushangaza, na kitu cha kuzomewa, na ukiwa wa daima. Tena, nitawaondolea sauti ya kicheko, na sauti ya furaha, sauti ya bwana arusi, na sauti ya bibi arusi, sauti ya mawe ya kusagia, na nuru ya mishumaa. Na nchi hii yote pia itakuwa ukiwa, na kitu cha kushangaza; nayo mataifa haya watamtumikia mfalme wa Babeli miaka sabini. Na itakuwa miaka hiyo sabini itakapotimia, nitamwadhibu mfalme wa Babeli, na taifa lile, asema Bwana, kwa sababu ya uovu wao, nayo nchi ya Wakaldayo pia; nami nitaifanya kuwa ukiwa wa milele.”

Hii inafundisha kuwa wakati mwingine ili kuyajua mapenzi ya Mungu na kujua mpango wa Mungu kunahitaji kusoma na kutafakari maandiko na vitabu vyenye hekima ya kiroho. Au vitabu vya watu wengine wenye roho wa Mungu kama sisi waliofunuliwa maswala kadhaa na kuamua au kusukumwa wayaweke maswala hayo katika vitabu, kusoma huku kunatuletea ufahamu wa maswala ya kiungu, Yesu alikuwa na ufahamu wa Tabia ya Daniel nay eye mwenyewe alikuwa anaufahamu unabii wa Daniel na hata alipokuwa akifundisha maswala kadhaa kuhusu Daniel alikazia kwa maneno asomaye na afahamu, kwa sababu alijua kuwa ndani ya kusoma kuna maarifa, kuna ujuzi na kuna ufahamu utapata ufahamu mwingine wa kiroho kupitia kusoma.

Mathayo 24:14-15 “Tena habari njema ya ufalme itahubiriwa katika ulimwengu wote, kuwa ushuhuda kwa mataifa yote; hapo ndipo ule mwisho utakapokuja. Basi hapo mtakapoliona chukizo la uharibifu, lile lililonenwa na nabii Danieli, limesimama katika patakatifu (asomaye na afahamu),            

Kumbe tunaweza kupata fahamu na maarifa ya kiroho kutoka katika vitabu, ni wazi kuwa Daniel alisoma kitabu cha nabii Yeremia, lakini vile vile sio jambo la kushangaza kwamba Yesu naye alisoma kitabu cha unabii wa Daniel na kunukuu kama unavyoweza kuona hapo kwa hiyo kwa kuvisoma vitabu tunaweza kupata maarifa na ufahamu na kutyajua mapenzi ya Mungu katika maisha yetu

2.       Kuongezea maarifa na ukuaji wa kiroho.

 

Kusoma vitabu yaani Biblia na vitavu vya kiroho kunakuongezea maarifa na ukuaji binafsi wa kiroho na kukupa mwanga, mwongozo, na ufahamu wa kina na uelewa mpana wa maswala ya kiroho, falsafa, Hekima na utendaji wa kitheolojia (Practical Theology), usomaji huu utakuongeza nguvu za kiroho, ufahamu kuhudu mapenzi ya Mungu na kutimiza kusudi la kuwako kwako duniani, sio hivyo tu utajengwa, utatiwa moyo na kupanua ufahamu wako ambao kimsingi utakufanya uwe tofauti na wahudumu wengine wa injili

 

2Timotheo 3:14-17 “Bali wewe ukae katika mambo yale uliyofundishwa na kuhakikishwa, kwa maana unajua ni akina nani ambao ulijifunza kwao; na ya kuwa tangu utoto umeyajua maandiko matakatifu, ambayo yaweza kukuhekimisha hata upate wokovu kwa imani iliyo katika Kristo Yesu. Kila andiko, lenye pumzi ya Mungu, lafaa kwa mafundisho, na kwa kuwaonya watu makosa yao, na kwa kuwaongoza, na kwa kuwaadibisha katika haki; ili mtu wa Mungu awe kamili, amekamilishwa apate kutenda kila tendo jema.”

 

Mithali 4:5-8 “Jipatie hekima, jipatie ufahamu; usiusahau; Wala usiyakatae maneno ya kinywa changu. Usimwache, naye atakuhifadhi; Umpende, naye atakulinda. Bora hekima, basi jipatie hekima; Naam, kwa mapato yako yote jipatie ufahamu. Umtukuze, naye atakukuza; Atakupatia heshima, ukimkumbatia.”

 

Unaona maandiko yanatukumbusha hapa kuhusu umuhimu wa hekima na maarifa ambayo yatakulinda, yatakuongoza, yatakuadabisha, yatakuhifadhi, na yatakukuza

 

3.       Kukuza Uwezo wa Kufundisha na Kuhubiri.

 

Kuwa Mwalimu wa neno la Mungu na Mwalimu katika fani nyinginezo, kunahitaji umahiri, kunahitaji taaluma na mbinu maalumu,  Yesu Kristo alikuwa Mwalimu kweli kweli  na Paulo Mtume pia alikuwa Mwalimu kweli kweli na Nabii Musa pia alikuwa Mwalimu kweli kweli, ili uweze kuwa Mwalimu mzuri mwenye uwezo mkubwa wa kufundisha na kuhubiri ni lazima USOME, sio lazima tu mfumo maalumu wa kielimu, Lakini pia mfumo binafsi wa kielumu ambao kimsingi ni pamoja na kujitia nidhambu ya kusoma vitabu, ili kupata ujuzi wa maswala mbalimbali, Mwalumu mzuri anaweza kusoma mpaka vitabu vingine vilivyoandikwa n ahata watu wa Imani potofu, sababu kubwa ni ili kujua yaliyomo kwa makudusi ya kuweka sawa kweli za kimungu, huwezi kufundisha kitu ambacho huna. Kwa hiyo ni lazima ujuzi wa neno la Mungu ukae kwa wingi ndani yako ili uweze kuwa na kitu cha kuwafunza wengine  na ili ufanikiwe katika hilo njia pekee na rahisi ni kwa kuvisoma vitabu, kuna sifa kubwa tano tu za Mwalimu mwema ambazo Yesu Kristo Mwalimu kuu alikuwa nazo Mwalimu mwema ni lazima awapende watu wake, Mwalimu mwema ni lazima awajue watu wake, Mwalimu mwema ni lazima alijue somo lake, Mwalimu mwema ni lazima ajue jinsi ya kufundisha na Mwalimu mwema ni lazima aishi kile anacho kifundisha, sasa ili uweze kuwa Mwalimu mwema ni aidha uwe mtu uliyechukua muda mrefu sana kujifunza na unayeeendelea kujifunza lakini ni laaimza kuvisoma vitabu iwe ni sehemu ya maisha yako ya kila siku ya kujitoa nay a kinidhamu

 

Matendo 7:22 “Musa akafundishwa hekima yote ya Wamisri, akawa hodari wa maneno na matendo.”

 

Luka 1:46-47 “Ikawa baada ya siku tatu wakamwona hekaluni, ameketi katikati ya waalimu, akiwasikiliza na kuwauliza maswali. Nao wote waliomsikia walistaajabia fahamu zake na majibu yake.”

 

Matendo 22:3 “Mimi ni mtu wa Kiyahudi, nalizaliwa Tarso, mji wa Kilikia, ila nililelewa katika mji huu, miguuni pa Gamalieli, nikafundishwa sheria ya baba zetu kwa usahihi, nikawa mtu wa jitihadi kwa Mungu kama ninyi nyote mlivyo leo hivi;”

 

1Timotheo 4:13 “Hata nitakapokuja, ufanye bidii katika kusoma na kuonya na kufundisha.”

 

Wote tunaowasoma katika maandiko waliokuwa watumishi wa Mungu na kurumiwa na Mungu kipekee walikuwa watu waliokuwa na bidi katika kujifunza na kusoma, Mwalimu hawezi kuwa na kitu cha kuwapa watu kama yeye mwenyewe hana vitu vilivyozidi, uwezo wetu wa kuhubiri na kufundisha na kuyapanda maarifa unaweza kuwa bora zaidi siku hadi siku kama tu endapo tutatia bidi katika kusoma vitabu na kwa kuvisoma vitabu tutakuwa na ujuzi wa mambo ambayo tunatamani katika huduma zetu kuwafundisha na kuwahubiri wengine, kila Mtumishi wa Mungu licha ya maswala mengine anapaswa kuwa na maisha yaliyojaa kusoma ili awe na ujuzi sahihi katika yote atakayokuwa anayazungumza kwa watu wenye uelewa na ufahamu na elimu tofauti tofauti.

 

4.       Kukuza uwezo wa kufanya uchambuzi wa kina

 

Kwa kuvisoma vitabu utaongeza uwezo wako wa kufanya uchambuzi wa kina, utakuwa na uwezo wa kuweka mambo bayana na kwa ufasaha, ukiwa na uwezo wa kutambua mawazo mbalimbali ya watu na kuwa kama mtu uliyeandaliwa ukiwa na majibu mbali mbali yenye ufumbuzi wa watu kwa jamii, wako watu katika maandiko ambao walikuwa hodari, lakini uhodari wao ulichangiwa kwa kiasi kikubwa na uwezo wa kujifunza na kusoma uliokuwa nyuma yao ambapo Roho Mtakatifu aliwawezesha kuwa na taarifa za kina na za kutosha kiasi cha kuweza kuvutia jamii zao za wakati ule

 

Matendo 6:8-10 “Na Stefano, akijaa neema na uwezo, alikuwa akifanya maajabu na ishara kubwa katika watu. Lakini baadhi ya watu wa sinagogi lililoitwa sinagogi la Mahuru, na la Wakirene, na la Waiskanderia, na la wale wa Kilikia na Asia, wakaondoka na kujadiliana na Stefano; lakini hawakuweza kushindana na hiyo hekima na huyo Roho aliyesema naye.”

 

Matendo 18:24-26 “Basi Myahudi mmoja, jina lake Apolo, mzalia wa Iskanderia, mtu wa elimu, akafika Efeso; naye alikuwa hodari katika maandiko. Mtu huyo alikuwa amefundishwa njia ya Bwana; na kwa kuwa roho yake ilikuwa ikimwaka, alianza kunena na kufundisha kwa usahihi habari za Yesu; naye alijua ubatizo wa Yohana tu. Akaanza kunena kwa ujasiri katika sinagogi; hata Prisila na Akila walipomsikia wakamchukua kwao, wakamweleza njia ya Bwana kwa usahihi zaidi.”

 

Matendo 17:11Mara hao ndugu wakawapeleka Paulo na Sila usiku hata Beroya. Nao walipofika huko wakaingia katika sinagogi la Wayahudi. Watu hawa walikuwa waungwana kuliko wale wa Thesalonike, kwa kuwa walilipokea lile neno kwa uelekevu wa moyo, wakayachunguza maandiko kila siku, waone kwamba mambo hayo ndivyo yalivyo.”

 

Watu wote hao walikuwa na uwezo mkubwa sana wa kufanya uchambuzi wa kimaandiko, uwezo mkubwa wa kujieleza na kuelezea kwa sababu walikuwa watu wenye hekima, walikuwa nawatu wa elimu na walikuwa watu waungwana hawa ni watu waliokuwa wakiitafuta kweli na kuwa na kiu ya kutaka kuwajulisha wengine kile walichokuwa wamemeza nguvu kubwa ya msukumo na utendaji mkubwa wa Roho wa Mungu ndani yao haukuwa tupu tu ulichangiwa na maarifa waliyokuwa wameyabeba na ni namna gani waliweza kuwa na uwezo huo ni kwa kuvisma vitabu

 

5.       Kusoma ni amri

 

Mungu aliwaamuru watu kusoma wakati huo kitabu pekee cha kusoma kilikuwa ni Torati tu na haikuwezekana kupatikana kwa kila mtu hivyo watu walijifunza na kusomewa na kuisikiliza  tu lakini leo hii Mungu ameamuru watumishi wengi wa Mungu kuandika wanaandika masomo mbalimbali, wanaandika vitabu, wanapewa jumbe na kutoa muda wao kuandika sana kwa hiyo leo hii tunaweza kujiongeza kuwa tuisome Biblia ambalo ni neno la Mungu, tuende katika vyoa vya biblia na kujifunza kutoka kwa walimu walioidhinishwa lakini vile vile tusiache kusoma vitabu vya kiroho na vipeperushi mbali mbali na maandiko mbalimbali ya kiroho ambayo kimsingi yanaandikwa kwa lengo na kusudi la kuujenga mwili wa Kristo, katika maandiko watu wengi sana waliamuriwa na Mungu kusoma kwaajili ya mafanikio ya huduma zao na maisha yao

 

Kumbukumbu 31:9-13 “Musa akaiandika torati hii, akawapa makuhani, wana wa Lawi, waliolichukua sanduku la agano la Bwana, na wazee wote wa Israeli. Musa, akawaamuru, akasema, Mwisho wa kila mwaka wa saba, wakati wa maachilio, wakati ulioamriwa wa sikukuu ya vibanda, Israeli wote wafikapo ili kuonekana mbele za Bwana, Mungu wako, mahali pale atakapopachagua, uisome torati hii mbele ya Israeli wote masikioni mwao. Wakusanye watu, wanaume na wanawake na watoto, na mgeni wako aliyemo malangoni mwako wapate kusikia na kujifunza, na kumcha Bwana, Mungu wenu, na kuangalia kutenda maneno yote ya torati hii; na watoto wao wasiojua, wapate kusikia na kujifunza kumcha Bwana, Mungu wenu, siku zote mtakazokaa katika nchi mnayoivukia Yordani ili kuimiliki.”

 

Yoshua 1:6-9 “Uwe hodari na moyo wa ushujaa, maana ni wewe utakayewarithisha watu hawa nchi hii niliyowaapia baba zao ya kwamba nitawapa. Uwe hodari tu na ushujaa mwingi, uangalie kutenda sawasawa na sheria yote aliyokuamuru Musa mtumishi wangu; usiiache, kwenda mkono wa kuume, au wa kushoto, upate kufanikiwa sana kila uendako. Kitabu hiki cha torati kisiondoke kinywani mwako, bali yatafakari maneno yake mchana na usiku, upate kuangalia kutenda sawasawa na maneno yote yaliyoandikwa humo; maana ndipo utakapoifanikisha njia yako, kisha ndipo utakapositawi sana. Je! Si mimi niliyekuamuru? Uwe hodari na moyo wa ushujaa; usiogope wala usifadhaike; kwa kuwa Bwana, Mungu wako, yu pamoja nawe kila uendako.”

 

1Wafalme 2:1-4 “Basi siku ya kufa kwake Daudi ikakaribia, akamwusia Sulemani mwanawe, akasema, Mimi naenda njia ya ulimwengu wote; basi uwe hodari, ujionyeshe kuwa mwanamume; uyashike mausia ya Bwana, Mungu wako, uende katika njia zake, uzishike sheria zake, na amri zake, na hukumu zake, na shuhuda zake, sawasawa na ilivyoandikwa katika torati ya Musa, upate kufanikiwa katika kila ufanyalo, na kila utazamako, ili Bwana afanye imara neno lake alilonena kwa habari yangu, akisema, Ikiwa watoto wako wataiangalia njia yao, wakienda mbele zangu kwa kweli, kwa moyo wao wote, na kwa roho yao yote, (akasema), hutakosa mtu katika kiti cha enzi cha Israeli.             

 

 

Mifano ya watu walionufaika kwa kuvisoma vitabu

Tumeona katika kipengele kilichotangulia umuhimu wa kuvisoma vitabu, licha ya kuwa na faida kadhaa nyingi ikiwepo pamoja na kupunguza stresses yaani mkandamizo wa mawazo, kuongeza ufanisi katika ujuzi wa lugha na kungezea misamiati na kukupa ujasiri na kukutia moyo vitabu pia vinaonekana kuwanufaisha watu mbali mbali katika maeneno mbalimbali duniani, lakini katika maandiko nitatoa hapa mifano michache sana ya watu walionufaika kwa usomaji, ambao kimsingi usomaji ulikuwa na manufaa katika maisha yao ya kimwili na kiroho

Yesu Kristo - kwa mfano maisha yake na maneno yake na matendo yake yote yalikuwa yametanguliwa kuandikwa kwa hiyo yeye alikuja duniani akiwa anajua wapi pa kukanyaga kwa sababu aliandikiwa yeye mambo yote

Zaburi 40:6-8 “Dhabihu na matoleo hukupendezwa nazo, Masikio yangu umeyazibua, Kafara na sadaka za dhambi hukuzitaka. Ndipo niliposema, Tazama nimekuja, (Katika gombo la chuo nimeandikiwa,) Kuyafanya mapenzi yako, Ee Mungu wangu, ndiyo furaha yangu; Naam, sheria yako imo moyoni mwangu.”

Waebrania 10:5-7 “Kwa hiyo ajapo ulimwenguni, asema, Dhabihu na toleo hukutaka, Lakini mwili uliniwekea tayari; Sadaka za kuteketezwa na sadaka za dhambi hukupendezwa nazo; Ndipo niliposema, Tazama, nimekuja (katika gombo la chuo nimeandikiwa) Niyafanye mapenzi yako, Mungu.”

Vifungu hivyo vya maandiko ni vya muhimu sana katika maisha ya Bwana wetu Yesu na kwetu wenyewe, Mungu alikuwa ameshachoshwa na matumizi ya wanyama na dhabihu za sadaka za kutekeketezwa na hivyo alikuwa ameandaa mpango ya kuwa mtu mmoja wa kipekee aliyeandikiwa mapenzi ya Mungu ataishi kwa utii kwa kila lililoandikwa katika neno la Mungu na kuwa atayatoa maisha yake kama sadaka kwaajili ya wengi  na hivyo kutimiza mpango au mapenzi yote ya Mungu, Yesu aliyatimiza yote na kila alilolofanya lilikuwa limeandikwa katika maandiko hakufanya jambo Fulani kwa mapenzi yake na nadhani ili aweze kuatimiza yote haya aliyasoma kwa umakini na kuyatendea kazi akitimiza yote kwa kufa kwake msalabani

Wewe na mimi kama tunataka kunufaika na kuyajua mapenzi ya Mungu nay ale ambayo Mungu ametuandikia tuyafanye hatuna budi kujisomea Biblia ambayo kmsingi ni Library/ Maktaba ya vitabu na kuchungulia yake tuliyoandikiwa ili tuyafanya na kuyatimiza, kwa hiyo Yesu alifaidika na kila alichokuwa ameandikiwa kukifanya kwa sababu viliwekwa katika gombo la chuo alisoma na kuishi kile alichokisoma

Luka 4:16-21 “Akaenda Nazareti, hapo alipolelewa; na siku ya sabato akaingia katika sinagogi kama ilivyokuwa desturi yake, akasimama ili asome. Akapewa chuo cha nabii Isaya, akakifungua chuo, akatafuta mahali palipoandikwa, Roho wa Bwana yu juu yangu, Kwa maana amenitia mafuta kuwahubiri maskini habari njema. Amenituma kuwatangazia wafungwa kufunguliwa kwao, Na vipofu kupata kuona tena, Kuwaacha huru waliosetwa, Na kutangaza mwaka wa Bwana uliokubaliwa. Akakifunga chuo, akamrudishia mtumishi, akaketi; na watu wote waliokuwamo katika sinagogi wakamkazia macho. Akaanza kuwaambia, Leo maandiko haya yametimia masikioni mwenu.”

Unaona je unafahamu kuwa mambo mengi ambayo tunapaswa kuyatimiza duniani tumeandikiwa? Lakini unawezaje kuyatimiza mapenzi hayo ya Mungu bila kuyasoma basi kila tuliloandikiwa na kuagizwa liko katika neno la Mungu na maandishi ya kiroho yaliyoandikwa na watu kwa kusudi la kukutoa katika hatua moja na kukupeleka katika hatua nyingine unaweza kufaidika vipi katika maisha yako ni kwa kuvisoma vitabu

Daniel – Aliweza kugudua kuwa wakati wa ukombozi wa wayahudi umetimia sawasawa na alivyotabiri nabii Yeremia, Daniel aliweza kuyajua mapenzi ya Mungu kwa klizazi chake n ahata kutujuza mapenzi ya Mungu ya wakati ujao kwa kusoma vitabu lakini pia kwa kuandika, kwa kusoma vitabu aligundua wakati wa kukaa utumwani Babeli umetimia na hivyo aliingia katika maombi ya kitaifa na kutubu kwaajili ya taifa lake akimdai Mungu haki ya watu wake

Daniel 9:3-19 “Katika mwaka wa kwanza wa Dario, mwana wa Ahasuero, wa uzao wa Wamedi, aliyetawazwa kuwa mfalme juu ya milki ya Wakaldayo; katika mwaka wa kwanza wa kumiliki kwake, mimi Danieli, kwa kuvisoma vitabu, nalifahamu hesabu ya miaka, ambayo neno la Bwana lilimjia Yeremia nabii, ya kuutimiza ukiwa wa Yerusalemu, yaani, miaka sabini. Nikamwelekezea Bwana Mungu uso wangu, ili kutaka kwa maombi, na dua, pamoja na kufunga, na kuvaa nguo za magunia na majivu. Nikamwomba Bwana, Mungu wangu, nikaungama, nikasema, Ee Bwana, Mungu mkuu, mwenye kutisha, ashikaye maagano na rehema kwao wampendao, na kuzishika amri zake; tumefanya dhambi, tumefanya ukaidi, tumetenda maovu, tumeasi, naam, hata kwa kuyaacha maagizo yako na hukumu zako; wala hatukuwasikiliza watumishi wako, manabii, ambao kwa jina lako walisema na wafalme wetu, na wakuu wetu, na baba zetu, na watu wote wa nchi. Ee Bwana, haki ina wewe, lakini kwetu sisi kuna haya ya uso, kama hivi leo; kwa watu wa Yuda, na kwa wenyeji wa Yerusalemu, na kwa Israeli wote, walio karibu na hao walio mbali, katika nchi zote ulikowafukuza, kwa sababu ya makosa yao waliyokukosa. Ee Bwana, kwetu sisi kuna haya ya uso, kwa wafalme wetu, na wakuu wetu, na baba zetu, kwa sababu tumekutenda dhambi. Rehema na msamaha ni kwa Bwana Mungu wetu, ingawa tumemwasi; wala hatukuitii sauti ya Bwana, Mungu wetu, kwa kwenda katika sheria zake, alizoziweka mbele yetu kwa kinywa cha watumishi wake, manabii. Naam, Israeli wote wameihalifu sheria yako, kwa kugeuka upande, wasiisikilize sauti yako; basi kwa hiyo laana imemwagwa juu yetu, na uapo ule ulioandikwa katika sheria ya Musa, mtumishi wa Mungu; kwa sababu tumemtenda dhambi. Naye ameyathibitisha maneno yake, aliyoyanena juu yetu, na juu ya waamuzi wetu waliotuamua, kwa kumletea mambo maovu makuu; maana chini ya mbingu zote halikutendeka jambo kama hili, lilivyotendeka juu ya Yerusalemu. Kama ilivyoandikwa katika sheria ya Musa, mabaya haya yote yametupata lakini hata hivyo hatukumwomba Bwana, Mungu wetu, atupe fadhili zake, ili tugeuke na kuyaacha maovu yetu, na kuitambua kweli yake. Basi Bwana ameyavizia mabaya hayo, akatuletea; maana Bwana, Mungu wetu ni mwenye haki katika kazi zake zote azitendazo; na sisi hatukuitii sauti yake. Na sasa, Ee Bwana Mungu wetu, uliyewatoa watu wako hawa katika nchi ya Misri kwa mkono hodari, ukajipatia sifa, kama ilivyo leo; tumefanya dhambi, tumetenda maovu. Ee Bwana sawasawa na haki yako yote, nakusihi, hasira yako na ghadhabu yako zigeuzwe na kuuacha mji wako Yerusalemu, mlima wako mtakatifu; maana kwa sababu ya dhambi zetu, na maovu ya baba zetu, Yerusalemu na watu wako wamepata kulaumiwa na watu wote wanaotuzunguka. Basi sasa, Ee Mungu wetu, yasikilize maombi ya mtumishi wako, na dua zake, ukaangazishe uso wako juu ya patakatifu pako palipo ukiwa, kwa ajili ya Bwana. Ee Mungu wangu, tega sikio lako, ukasikie; fumbua macho yako ukautazame ukiwa wetu, na mji ule ulioitwa kwa jina lako; maana hatukutolei maombi yetu kwa sababu ya haki yetu, lakini kwa sababu ya rehema zako nyingi. Ee Bwana, usikie; Ee Bwana, usamehe; Ee Bwana, usikilize, ukatende, usikawie; kwa ajili yako wewe, Ee Mungu wangu; kwa sababu mji wako na watu wako wanaitwa kwa jina lako. Basi hapo nilipokuwa nikisema, na kuomba, na kuiungama dhambi yangu, na dhambi ya watu wangu Israeli, na kuomba dua yangu mbele za Bwana, Mungu wangu, kwa ajili ya mlima mtakatifu wa Mungu wangu; naam, nilipokuwa nikinena katika kuomba, mtu yule, Gabrieli, niliyemwona katika njozi hapo kwanza, akirushwa upesi, alinigusa panapo wakati wa dhabihu ya jioni. Akaniagiza, akaongea nami, akasema, Ee Danieli, nimetokea sasa, ili nikupe akili upate kufahamu.”

Kutoka katika hatua ya kuvisoma vitabu Daniel anaonekana kugundua kuwa walifanya dhambi, walifanya makosa, hawakuwasikiliza manabii, alitubu aliomba alitambua kuwa yaliyowapata yameandikwa katika torati ya Musa, na pia yalitolewa kama maonyo na kina Yeremia, na kutokea hapo alijibiwa maombi yake na malaika Gabriel na kufunuliwa mambo muhimu sana yanaoihusu Israel na wakati wa Masihi n ahata sisi leo, Daniel aliwezaje kuwa nabii mzuri kiasi kile ni kwa sababu alinufaika katika kusoma vitabu, vitabu vya manabii waliomtangulia  

Towashi wa kushi – Alikuwa ni mtu wa Kushi yaani Ethiopia alikuwa mkazi wa Afrika lakini alikuwa mtu Mcha Mungu aliyemheshimu Mungu wa wayahudi kule Israel alikuwa akipanda siku za sikukuu kwaajili ya kuabudu na inaonekana wazi licha ya cheo chake kikubwa alikuwa anapenda kusoma, hata hivyo hakuwa amefahamu kwa ufasaha yale aliyokuwa anayasoma, lakini Mungu kwa Rehema zake alimtuma mwinjilisti Philipo kumwendea na kumfahamisha na alipoelewa maandiko maisha yake ya kiroho yalibadilika sana

Matendo 8: 26-39 “Malaika wa Bwana akasema na Filipo, akamwambia, Ondoka ukaende upande wa kusini hata njia ile itelemkayo kutoka Yerusalemu kwenda Gaza; nayo ni jangwa. Naye akaondoka, akaenda; mara akamwona mtu wa Kushi, towashi, mwenye mamlaka chini ya Kandake malkia wa Kushi, aliyewekwa juu ya hazina yake yote; naye alikuwa amekwenda Yerusalemu kuabudu, akawa akirejea, ameketi garini mwake akisoma chuo cha nabii Isaya. Roho akamwambia Filipo, Sogea karibu na gari hili, ukashikamane nalo. Basi Filipo akaenda mbio, akamsikia anasoma chuo cha nabii Isaya; akanena, Je! Yamekuelea haya unayosoma? Akasema, Nitawezaje kuelewa, mtu asiponiongoza? Akamsihi Filipo apande na kuketi pamoja naye. Na fungu la Maandiko alilokuwa akilisoma ni hili, Aliongozwa kwenda machinjoni kama kondoo, Na kama vile mwana-kondoo alivyo kimya mbele yake amkataye manyoya, Vivyo hivyo yeye naye hafunui kinywa chake. Katika kujidhili kwake hukumu yake iliondolewa. Ni nani atakayeeleza kizazi chake? Kwa maana uzima wake umeondolewa katika nchi. Yule towashi akamjibu Filipo, akasema, Nakuomba, nabii huyu; asema maneno haya kwa habari ya nani; ni habari zake mwenyewe au za mtu mwingine? Filipo akafunua kinywa chake, naye, akianza kwa andiko lilo hilo, akamhubiri habari njema za Yesu. Wakawa wakiendelea njiani, wakafika mahali penye maji; yule towashi akasema, Tazama, maji haya; ni nini kinachonizuia nisibatizwe? Filipo akasema, Ukiamini kwa moyo wako wote, inawezekana. Akajibu, akanena, Naamini ya kwamba Yesu Kristo ndiye Mwana wa Mungu.] Akaamuru lile gari lisimame; wakatelemka wote wawili majini, Filipo na yule towashi; naye akambatiza. Kisha, walipopanda kutoka majini, Roho wa Bwana akamnyakua Filipo, yule towashi asimwone tena; basi alikwenda zake akifurahi.”

Kwa hiyo kumbe unaweza kukubaliana nami pamoja na maandiko ya kwamba kuna faida kubwa sana zinazoweza kupatikana kwa mambo yaliyoandikwa, kwa hiyo maandiko yanatutia moyo kusoma, yanatutia moyo kizitafuta kweli na kweli nyingine zimeandikwa wazi na kuwekwa katika maandishi na watumishi wa Mungu mbalimbali nikiwemo mimi, ili kukufundisha na kukufunulia mapenzi ya Mungu na uweze kunufaika na kuenedna na kuishi kwa hayo, kwa kupitia kusoma vitabu Mungu anaweza kuanzia hapo na kukupeleka katika viwango vingine, Miaka mingi nyuma Mungu alisema na mimi na kuniambia na kuniamuru kuandika alisema na mimi katika njozi ya usiku na katika njozi hiyo alinilisha kalamu mdomoni mwangu na tangu wakati huo sisikii Amani kukaa kimya bila kuandika, ninatumia muda mwingi kuandika, na vocha nyingi kurusha masomo yangu bure katika mitandao ya kijamii, siweki namba zangu kuomba mchango wa kitu chochote, siuzi masomo yangu, sizuii mtu kujisomea na kuyahubiri kwa sababu sio ya kwangu, Mungu alinipa kwaajili ya kanisa lake, sipendelei mtu yeyete ninapoandika wala dhehebu lolote mimi nimeamriwa niseme tu kile Mungu anataka nikiseme na ameniamuru kuyaweka yote katika maandishi lakini ni nani atakayefaidika ni yule atakayeondoa uvivu na kusoma, na kwa kuvisoma vitabu na maandishi haya utajengeka na kunufaika kroho! Sio wewe tu na kanisa lako unalolihudumia, utanufaika kama walivyonufaika watu wengine, maarifa mengi sana yamefichwa katika vitabu hivyo hakikisha unajisomea ukiyapenda mafunsiho yangu chukua namba zangu yaombe omba somo lolote katika whatsapp nitakurushia bure kwa sababu neno la Mungu limesema mmepewa bure toeni bure

Ufanye bidii katika kusoma

Neno la Mungu linatutia moyo kuwa tusome, kusoma sio jambo lenye kufurahisha sana, kama ilivyo kuandika pia, ili usome au kuandika ni lazima uutoe sadaka Muda wako, ujifungie na utafute utulivu, ukae muda mrefu sana, na suome sana na kupitia maandiko mengi sana na chunguzi nyingi sana jambo hili bila bidi, unaweza kujikuta unaingia uvivu wa kusoma na kuandika pia, kwa hiyo neno la Mungu linatutaka tuwe na bidi katika kusoma Ezra alikuwa Mwalimu wa neno la Mungu, na Mungu alimtumia kuleta uamshi mkubwa sana kupitia mafundisho yake lakini kabla ya kutumiwa na Mungu Ezra alitia bidi katika kusoma na kufundisha

Ezra 7:6-10 “huyo Ezra akakwea kutoka Babeli; naye alikuwa mwandishi mwepesi katika sheria ya Musa, aliyokuwa ameitoa Bwana, Mungu wa Israeli; naye mfalme akamjalia matakwa yake yote, kama mkono wa Bwana, Mungu wake, ulivyokuwa pamoja naye. Nao wakakwea baadhi ya wana wa Israeli, na wa makuhani, na wa Walawi, na waimbaji, na mabawabu, na Wanethini, ili kwenda Yerusalemu, katika mwaka wa saba wa mfalme Artashasta. Naye Ezra akafika Yerusalemu mwezi wa tano katika mwaka wa saba wa huyo mfalme. Maana alianza kukwea kutoka Babeli siku ya kwanza ya mwezi wa kwanza, naye akafika Yerusalemu siku ya kwanza ya mwezi wa tano, kama mkono mwema wa Mungu wake ulivyokuwa pamoja naye. Kwa maana huyo Ezra alikuwa ameuelekeza moyo wake kuitafuta sheria ya Bwana, na kuitenda, na kufundisha maagizo na hukumu katika Israeli.”

Ezra alikuwa mwandishi yaani Mwalimu na ndiye mwanzilishi wa kundi la waandishi, yaani walimu wa Torati, maneni aliuelekeza moyo kuitafuta sheria ya bwana na kuitenda na kufundisha maagizo na hukumu katika Israel ni ushahidi wa moyo wake kuwa alijikita katika kusoma na kuyaishi yale aliyojifunza ili afundishe , jambo la namna hii linahitaji kujitia na linahitaji bidi alikuwa na bidii jambo hili ni sawa tu na Paulo mtume alivyomuagiza Timotheo kuwa anwe na bidi katika kusoma na kufundisha 1Timotheo 4:13 “Hata nitakapokuja, ufanye bidii katika kusoma na kuonya na kufundisha.”

Wote tutakuwa tunakumbuka na kufahamu kuwa Paulo mtume ndiye mtume aliyeandika vitabu vingi sana na kufanya kazi kubwa kuliko mitume wote lakini ni ukweli ulio wazi kuwa mtume huyu msomo licha ya kupata elimu mbali mbali na mafuno makubwa ya aina mbalimbali maisha yake yote mpaka uzee wake hakuacha kuwa na tabia ya kusoma vitabu

2Timotheo 4:9-13 “Jitahidi kuja kwangu upesi. Maana Dema aliniacha, akiupenda ulimwengu huu wa sasa, akasafiri kwenda Thesalonike; Kreske amekwenda Galatia; Tito amekwenda Dalmatia. Luka peke yake yupo hapa pamoja nami. Umtwae Marko, umlete pamoja nawe, maana anifaa kwa utumishi. Lakini Tikiko nalimpeleka Efeso. Lile joho nililoliacha kwa Karpo huko Troa, ujapo ulilete, na vile vitabu, hasa vile vya ngozi.”

Paulo mtume alikuwa gerezani, alimwandikia Timotheo waraka wa kumtia moyo, akimhimiza pia kumtembelea upesi hata hivyo aliagizia joho lake bila kusahau vitabu vyake hasa vile vya ngozi, yaani maana yake alitaka maktaba yake iwe karibu naye maisha yake yalijawa na kusoma vitabu kila wakati kama unataka kuwa wa kiroho kama Paulo mtume basi usiache pia kusoma vitabu na maandishi mbali mbali ili kujiimarisha katika maisha yako ya kiroho na huduma, kiufupi tu nilitakiwa nikuambie soma vitabu basi , Paulo alikuwa na mafunuo mengi sana aliandika nyaraka nyingi sana lakini alikuwa akisoma sana vitabu ndugu uwe na bidi katika kusoma vitabu

Uvivu wako sio wako ni kuwa shetani hataki usome vitabu, hataki uwe na maarifa kwa sababu mengi ya maarifa hayo watu wa Mungu na waliotembea na Mungu wameanika siri hizo katika vitabu shetani anajua utamwambia imeandikwa kwa hiyo atakuzuia uwe mvizu usijisomee ili usiwe na maarifa na hatimaye uweze kuishiwa, sasa kama wewe kuhani huongezi maarifa, hujisomei vipi kuhusu watu wako? 

Hosea 4:6-9 “Watu wangu wanaangamizwa kwa kukosa maarifa; kwa kuwa wewe umeyakataa maarifa, mimi nami nitakukataa wewe, usiwe kuhani kwangu mimi; kwa kuwa umeisahau sheria ya Mungu wako, mimi nami nitawasahau watoto wako.Kadiri walivyozidishwa, kwa kadiri iyo hiyo walinitenda dhambi; nami nitageuza utukufu wao kuwa aibu. Hujilisha dhambi ya watu wangu, hujifurahisha moyo kwa uovu wao.Hata itakuwa, kama walivyo watu, ndivyo atakavyokuwa kuhani; nami nitawaadhibu kwa ajili ya njia zao, na kuwalipa kwa matendo yao.”

Kusoma vitabu kutakusaidia kuongeza ufahamu, kujilinda na mapokeo ya wanadamu, kujilinda na taratibu za kidini, kuleta uamsho, kujijenga kiroho kuepuka ujinga wa kiroho na kadhalika lakini pia kuepuka mitego ya adui

Mafanikio yoyote ya kimwili na kiroho yanategemea na ustawi wako katika maarifa, Wakristo wanapaswa kuelewa kuwa wanatakiwa wawe na bidi katika kujisomea na kuyachunguza maandiko na pamoja na Biblia kusoma vitabu vingine vya kiroho ili wafunguliwe nataka nikuhakikishie kuwa kama umsomaji wa vitabu unaweza kuwa na maarifa makubwa sana kuliko hata wale viongozi wa kiroho ambao wako busy na masala ya maongozi wakihangaika huko na huko kwenye vikao na mikutano na maswala ya kikatiba na kuacha kuwa na Muda wa kujisomea ikiwa Paulo Mtume aliyekuwa gerezani aliagizia vitabu mimi ni nani nisiwe na Muda wa kujsomea kila nipatapo nafasi soma vitabu

HITIMISHO

Kama Danieli alivyosoma vitabu na kupata maarifa kuhusu mpango wa Mungu, vivyo hivyo Wakristo wanapaswa kuwa na tabia ya kusoma vitabu vya kiroho. Kusoma kunasaidia kujua mapenzi ya Mungu, kukua kiroho, na kuwa tayari kwa kazi ya Bwana.Je, unajipa muda wa kusoma vitabu vyenye maarifa ya kiroho? Kama hufanyi hivyo anza sasa katika jina la Yesu kristo na utakuja kunishukuru baadae

Na Mchungaji Innocent Samuel Kamote

Mkuu wa wajenzi mwenye Hekima!