1Wakorintho 1:18-24 “Kwa sababu neno la
msalaba kwao wanaopotea ni upuzi, bali kwetu sisi tunaookolewa ni nguvu ya
Mungu. Kwa kuwa imeandikwa, Nitaiharibu hekima yao wenye hekima, Na akili zao
wenye akili nitazikataa.Yu wapi mwenye hekima? Yu wapi mwandishi? Yu wapi mlete
hoja wa zamani hizi? Je! Mungu hakuifanya hekima ya dunia kuwa ni upumbavu? Kwa
maana katika hekima ya Mungu, dunia isipopata kumjua Mungu kwa hekima yake,
Mungu alipenda kuwaokoa waaminio kwa upuzi wa lile neno linalohubiriwa. Kwa
sababu Wayahudi wanataka ishara, na Wayunani wanatafuta hekima; bali sisi
tunamhubiri Kristo, aliyesulibiwa; kwa Wayahudi ni kikwazo, na kwa Wayunani ni
upuzi; bali kwao waitwao, Wayahudi kwa Wayunani, ni Kristo, nguvu ya Mungu, na
hekima ya Mungu.”
Utangulizi:
Leo ni siku ya ijumaa kuu,
wakristo wote nchini wanaungana na wakristo wenzao duniani kuadhimisha na
kukumbuka Mateso ya Bwana wetu Yesu Kristo na kuuawa kwake msalabani kwaajili
ya ukombozi wa wanadamu kulikotokea huko Yerusalem zaidi ya miaka 2000
iliyopita, Katika siku hii ya leo nataka kuzungumzia Ufahamu kuhusu njia ya
Msalaba.
Huenda wewe umewahi kusikia au
kuhusika kwa namna moja ama nyingine katika ibada iitwayo ibada ya njia ya
Msalaba! Na huenda umewahi kujiuliza ibada hii ni ibada ya namna gani, asili
yake ni nini na je ni mapokeo au ni mafundisho ya kibiblia, ina kweli gani na
ina dosari gani ni mambo gani mazuri tunaweza kujifunza kutoka katika ibada hii,
yepi ya kibiblia na yepi sio ya kibiblia, kwa wakristo wa makanisa ya kikatoliki
na Anglican ya High Church njia ya msalaba inaweza kuwa sio kitu kigeni, Hususani
katika wakati ule wa Kwaresma na katika siku ya leo ya ijumaa kuu – Kwaresma
maana yeke ni (40), lakini kwa makanisa ya kipentekoste inaweza kuwa kitu
kigeni, vyovyote iwavyo vile kuna mambo ya kujifunza kwa kila mmoja wetu uwe ni
mpentekoste au mkatoliki na muanglikan na wengineo, yako mambo ambayo Roho
Mtakatifu anataka tujifunze kwa msingi huo basi Leo basi Mwalimu Mkuu Mungu Roho
Mtakatifu ametupa neema ya kujifunza maswala muhimu katika ibada hii ya njia ya
msalaba na tutajifunza kwa kina na mapana na marefu kwa kusudi tu la kuelewa
yale yaliyoko katika njia ya msalaba na kufaidika. Kwa ufahamu na maarifa.
Tutajifunza somo hili Ufahamu kuhusu njia ya msalaba kwa kuzingatia vipengele vinne
vifuatavyo:-
·
Historia
ya njia ya Msalaba.
·
Mafundisho
Muhimu katika njia ya msalaba.
·
Mambo
yasiyo ya kibiblia katika njia ya Msalaba.
·
Faida ya
mafundisho ya njia ya Msalaba.
Historia ya njia ya Msalaba
Ni muhimu kufahamu kuwa ibada ya
njia ya msalaba asili yake ilitokana na ibada ya kutafakari kwa kina na
kujifunza maswala mbali mbali kuhusu mateso ya Bwana wetu Yesu Kristo tangu
alipohukumiwa na Pilato hadi wakati alipokufa Msalabani na alipozikwa, ibada
hii huadhimishwa kwa kirefu aidha wakati wa Kwaresma (40) ama wakati wa sikukuu
ya ijumaa kuu, Katika wakati huo watu waliomwamini Yesu hujumuika kwa pamoja
katika kujifunza na kutafakari Mateso ya Yesu na hivyo kujiimarisha kiroho,
kiimani,toba na kiufahamu, wakati wa kutafakari mateso hayo lakini lengo kuu
likiwa ni kupandikiza fundisho hilo Muhimu kuhusu kuteswa kusulubiwa na kufufuka
kwa Bwana wetu Yesu Kristo fundisho ambalo ni msingi mkuu wa ukombozi wa
Mwanadamu, na Imani yetu, kwani kama Kristo asingelisulubiwa na kufa na
kufufuka katika wafu Imani yetu ingelikuwa ni bure.
1Wakorintho 15:13-20 “Lakini kama hakuna
kiyama ya wafu, Kristo naye hakufufuka; tena kama Kristo hakufufuka, basi,
kuhubiri kwetu ni bure na imani yenu ni bure. Naam, na sisi tumeonekana kuwa
mashahidi wa uongo wa Mungu; kwa maana tulimshuhudia Mungu ya kuwa alimfufua
Kristo, ambaye hakumfufua, ikiwa wafu hawafufuliwi. Maana kama wafu
hawafufuliwi, Kristo naye hakufufuka. Na kama Kristo hakufufuka, imani yenu ni
bure; mngalimo katika dhambi zenu. Na hapo wao nao waliolala katika Kristo
wamepotea. Kama katika maisha haya tu tumemtumaini Kristo, sisi tu maskini
kuliko watu wote. Lakini sasa Kristo amefufuka katika wafu, limbuko lao
waliolala.”
Ibada hii ilianza mnamo karne ya
4 baada ya Yesu Kristo, kama matokeo ya wakristo waliokuwa na tabia ya kutembelea
Yerusalem na kupita katika njia ile halisi aliyopitia Yesu Kristo kutoka jumba
la hukumu la Anthonio akielekea Golgotha
au Kalvari mahali ambako
alisulubiwa, wakristo hao wa kale walikuwa na tabia ya kutembelea Yerusalem (Kufanya hija) na kupita hatua kwa hatua
na kusimama katika kila eneo la kihistoria kwa kutafakari kujifunza na kufanya
maombi kwa kukumbuka mateso ya Yesu Kristo.
Moja ya watu mashuhuri waliokuwa
wakifanya ibada hii na baadaye kuyatambua maeneo hayo muhimu ya mateso ya Yesu
ni pamoja na mama wa Mfalme Constantine aliyejulikana kama Malkia Hellena ambaye alikuwa ni Mkristo kabla ya mwanae kumuamini
Bwana Yesu Baadaye.
Mnamo karne ya 13-14 watawa wa
Kifransisko (Franciscans) walipewa
jukumu la kuyahifadhi maeneo hayo ya njia ya Msalaba huko Yerusalem chini ya
utawala wa Sultan wa Ottoman 1342 na
wao walifanya kazi hii ikiwa ni pamoja na kuieneza ibada hii katika maeneo
mbali mbali ya ulaya, mpaka karne ya 18 Papa
Clement XIV alikubali kupitisha vituo 14 rasmi katika ibada hii ya njia ya
msalaba vinavyotambulika mpaka leo, hata hivyo baadhi ya wakristo waliongeza
kituo cha 15 kuzungumzia kuhusu kufufuka kwa Yesu na wengine huona kuwa wakati
ibada ya njia ya msalaba hufanyika ijumaa kuu, basi kituo cha 15 kinaweza
kuadhimishwa sikukuu ya pasaka. Vituo tisa tu kati ya vituo vile 14 ni matukio
ya kweli ya kibiblia wakati vituo vitano 5 matukio yake si ya kibiblia bali
yanatokana na masimulizi ya kale yaliyoaminiwa na watu kwa miaka na kwa taarifa
za kimapokeo.
Ibada hii ya njia ya Msalaba ilipewa
umuhimu mkubwa katika nyakati za pasaka kwa sababu ilikuwa ikiwasaidia wakristo
kupata nafasi ya kutafakari kwa undani mateso ya Yesu Kristo kama njia ya
kujiimarisha kiimani katika maisha ya kiroho. Katika lugha ya kilatini njia hii
ya Msalaba inajulikana kama “Via
Dolorosa” kwa kiingereza “Sorrowful
Way” au “Way of Suffering” au “The Painful Path” yaani njia ya huzuni
au njia ya mateso, au njia ya maumivu, hapa tunaiita njia ya msalaba, njia hii
iko katika mji wa zamani wa Yerusalem na inaaminika njia hiyo ndiyo ile
aliyoipitia Yesu kuelekea mahali alikosulubiwa.
Isaya 53:3 “Alidharauliwa na kukataliwa na
watu; MTU WA HUZUNI NYINGI, AJUAYE SIKITIKO; Na kama mtu ambaye watu humficha
nyuso zao, Alidharauliwa wala hatukumhesabu kuwa kitu.”
Mafundisho Muhimu katika njia ya msalaba
Kutokana na mwamko mkubwa wa
kiinjili tulio nao leo, Njia ya msalaba inaweza kuonekana kuwa ni ibada ya
kimapokeo, lakini ukiichunguza kwa undani utaweza kugundua kuwa kulikuwa na nia
njema ya kutaka kuwafundisha watu kwa kina sana kuhusu mateso ya Yesu Kristo,
japo kutokana na ufinyu wa kiufahamu uliokuwako nyakati hizo, na upungufu
mkubwa wa Elimu na maarifa ya wakati ule, uwezo wa kufikisha mafundisho hayo
ulikuwa duni, na wa kitoto hata pamoja na kuhusisha picha, lengo kuu lilikuwa
halijafikiwa na sasa Roho Mtakatifu aliniamuru kuwa wakati wa kuweka sawa
fundisho hili kwa faida ya kizazi cha sasa na kijacho umewadia nami kwa neema
ya Mungu niliyopewa kama mkuu wa wajenzi ninafanya kazi hii leo ya kuliweka
wazi fundisho hilo kwa maarifa yake katika msingi wa kimaandiko.
Ni ukweli ulio wazi na
usiopingika kuwa katika kufuatilia yale yaliyomo katika ibada ya njia ya
msalaba utaweza kugundua kuwa yako mafundisho muhimu sana na mazuri na ya kweli
ya kujifunza katika maswala kadhaa lakini vile vile yako maswala machache
ambayo tunaweza tusiyape kipaumbele kwa sababu hayana ushahidi wa kimaandiko na
sio ya msingi kwa sababu hiyo ingawa Papa
Clement XIV alikubali kupitisha vituo 14 vya kimafundisho, Mimi nitajadili
vifungu tisa tu na kuweka pembeni vile visivyo na ushahidi wa kimaandiko na
vilivyo na asili ya kimapokeo lakini vinakubalika katika masimulizi ya wakristo
wa kale. Baada ya maelezo hayo sasa tunangalie yale tunayoweza kujifunza kutoka
katika njia ya Msalaba:-
1.
Yesu
Kristo Mbele ya Pilato: # 1
Katika eneo la
kwanza tunapotafakari kuhusu mateso ya Bwana wetu Yesu Kristo, utagundua hukumu
iliyo mbaya zaidi kuwahi kutokea duniani, ni hukumu ya kifo kwa mtu ambaye
kimsingi hakuwa na hatia, Watu, wakuu wa makuhani pamoja na Pilato waliyaacha
maisha ya mtu mwenye haki kuingia hukumuni na kuuawa pasipo hatia kwa ujumla
ilikuwa ni hukumu ya uonevu mkubwa usioweza kusimuliwa, hii inathuthibitishia
kuwa uovu wa mwanadamu ulikuwa umefikia ngazi ya juu kabisa ambapo mtu mwema
alionekana kuwa mbaya na mtu mbaya alionekana kuwa mwema, jamii ilikuwa
ikishabikia uovu kuliko wema.
Mathayo 27:22-25 “Pilato
akawaambia, Basi, nimtendeje Yesu aitwaye Kristo? Wakasema wote, Asulibiwe.
Akasema, Kwani? Ni ubaya gani alioutenda? Wakazidi sana kupiga kelele,
wakisema, Na asulibiwe. Basi Pilato alipoona ya kuwa hafai lo lote, bali ghasia
inazidi tu, akatwaa maji, akanawa mikono yake mbele ya mkutano, akasema, Mimi
sina hatia katika damu ya mtu huyu mwenye haki; yaangalieni haya ninyi wenyewe.
Watu wote wakajibu wakasema, Damu yake na iwe juu yetu, na juu ya watoto wetu.”
Yohana 19:6-8 “Basi
wale wakuu wa makuhani na watumishi wao walipomwona, walipiga kelele wakisema,
Msulibishe! Msulibishe! Pilato akawaambia, Mtwaeni ninyi basi, mkamsulibishe;
kwa maana mimi sioni hatia kwake.Wayahudi wakamjibu, Sisi tunayo sheria, na kwa
sheria hiyo amestahili kufa, kwa sababu alijifanya kuwa Mwana wa Mungu. Basi
Pilato aliposikia neno hilo, akazidi kuogopa.”
Hukumu hii ya Yesu Kristo ina maswala
kadhaa ya kujifunza
a. Inatufundisha jinsi ambavyo Yesu asiye na
hatia alivyokubali adhabu mbaya zaidi ya kwenda kufa msalabani kwaajili ya
makosa yetu na dhambi zetu,- Hukumu hii ya Yesu inadhihirisha jinsi wanadamu
walivyo waovu na walivyooza na kupotoka katika kutenda dhuluma, tunajifunza
jinsi dhambi ilivyo mbaya na jinsi ilivyoweza kusababisha majeraha makubwa
katika moyo wa mwana wa Mungu, Hata hivyo kwa sababu ya upendo wake kwa
wanadamu Yesu kristo anaonekana kukubali kuiachia dhuluma ishinde.
Isaya 53:3-8 “Alidharauliwa na kukataliwa na watu; Mtu wa huzuni
nyingi, ajuaye sikitiko; Na kama mtu ambaye watu humficha nyuso zao,
Alidharauliwa wala hatukumhesabu kuwa kitu. Hakika ameyachukua masikitiko yetu,
Amejitwika huzuni zetu; Lakini tulimdhania ya kuwa amepigwa, Amepigwa na Mungu,
na kuteswa. Bali alijeruhiwa kwa makosa yetu, Alichubuliwa kwa maovu yetu;
Adhabu ya amani yetu ilikuwa juu yake, Na kwa kupigwa kwake sisi tumepona. Sisi
sote kama kondoo tumepotea; Kila mmoja wetu amegeukia njia yake mwenyewe; Na
Bwana ameweka juu yake Maovu yetu sisi sote. Alionewa, lakini alinyenyekea,
Wala hakufunua kinywa chake; Kama mwana-kondoo apelekwaye machinjoni, Na kama
vile kondoo anyamazavyo Mbele yao wakatao manyoya yake; Naam, hakufunua kinywa
chake. Kwa kuonewa na kuhukumiwa aliondolewa; Na maisha yake ni nani
atakayeisimulia? Maana amekatiliwa mbali na nchi ya walio hai; Alipigwa kwa
sababu ya makosa ya watu wangu.”
b. Inatufundisha jinsi Yesu alivyohukumiwa kwa
makosa ya uongo.- Kimsingi hukumu hii ilikuwa ya dhuluma, isiyo ya haki na
ambayo haikuzingatia sheria ya kiyahudi wala za kirumi, Mashitaka ya Yesu
Kristo kwa kweli yalitolewa na watu waliokuwa wamepikwa na wakuu wa makuhani
ili kutoa ushahidi wa uwongo, wala hakimu mwenyewe hakupata ushahidi wa wazi
ambao ungeweza kumtia Yesu hatiani na kupelekea kupata adhabu ya kifo kibaya
kuliko maelezo aidha hakukuwa na nafasi ya upelelezi wa kina kuhusu makosa
anayosingiziwa Yesu Kristo badala yake kwa kupitia ushahidi wa kuunga unga tu
yakafanyika maamuzi mabaya na ya kusikitisha sana !
Luka 23:1-4 “Wakasimama mkutano wote, wakampeleka kwa Pilato.Wakaanza
kumshitaki, wakisema, Tumemwona huyu akipotosha taifa letu, na kuwazuia watu
wasimpe Kaisari kodi, akisema kwamba yeye mwenyewe ni Kristo, mfalme. Pilato
akamwuliza, akisema, Wewe ndiwe mfalme wa Wayahudi? Akajibu akamwambia, Wewe
wasema. Pilato akawaambia wakuu wa makuhani na makutano, Sioni neno lililo ovu
katika mtu huyu.”
Mathayo
26:59-61 “Basi wakuu wa makuhani na baraza yote
wakatafuta ushuhuda wa uongo juu ya Yesu, wapate kumwua; wasiuone wangawa
walitokea mashahidi wa uongo wengi. Hata baadaye wawili wakatokea, wakasema,
Huyu alisema, Naweza kulivunja hekalu la Mungu, na kulijenga kwa siku tatu.”
Yohana 18:38 “Pilato akamwambia, Kweli ni nini? Naye akiisha kusema
neno hilo akawatokea Wayahudi tena, akawaambia, Mimi sioni hatia yo yote kwake.”
c. Tunajifunza kwamba hukumu yake ni matokeo
ya wivu na uhasama na sio haki – Wakuu wa makuhani na viongozi wa dini
walimuonea Yesu wivu, kwa sababu alikuwa anafanya wanafunzi wengi kuliko wao,
alikuwa maarufu kuliko wao, alikuwa na huduma yenye nguvu na upako kuliko wao,
alikuwa akifanya miujiza mingi na mikubwa wakati wao hawakuwa na kitu,
mafundisho yake yalijaa amri na mamlaka, Yesu alikemea sana dhambi ya unafiki
ambayo kimsingi ilikuwa ikiwatafuna mafarisayo na viongozi wa dini na kwa sababu
hizo walifanya njama za wazi za kutaka kumuua, na ni ukweli ulio wazi
kwamba hukumu hii ya kifo likuwa ni
mauaji ya makusudi na haikuwa haki.
Yohana 11:47-50
“Basi wakuu wa makuhani na Mafarisayo wakakusanya
baraza, wakasema, Tunafanya nini? Maana mtu huyu afanya ishara
nyingi.Tukimwacha hivi, watu wote watamwamini; na Warumi watakuja,
watatuondolea mahali petu na taifa letu. Mtu mmoja miongoni mwao, Kayafa,
aliyekuwa Kuhani Mkuu mwaka ule, akawaambia, Ninyi hamjui neno lo lote; wala
hamfikiri ya kwamba yafaa mtu mmoja afe kwa ajili ya watu, wala lisiangamie
taifa zima.”
Mathayo
23:13-16 “Ole wenu waandishi na Mafarisayo,
wanafiki! Kwa kuwa mnawafungia watu ufalme wa mbinguni; ninyi wenyewe
hamwingii, wala wanaoingia hamwaachi waingie. [Ole wenu waandishi na
Mafarisayo, wanafiki! Kwa kuwa mnakula nyumba za wajane, na kwa unafiki mnasali
sala ndefu; kwa hiyo mtapata hukumu iliyo kubwa zaidi.] Ole wenu waandishi na
Mafarisayo, wanafiki! Kwa kuwa mnazunguka katika bahari na nchi kavu ili
kumfanya mtu mmoja kuwa mwongofu; na akiisha kufanyika, mnamfanya kuwa mwana wa
jehanum mara mbili zaidi kuliko ninyi wenyewe. Ole wenu viongozi vipofu, ninyi
msemao, Mtu atakayeapa kwa hekalu, si kitu; bali mtu atakayeapa kwa dhahabu ya
hekalu, amejifunga.”
d. Tunajifunza ya kuwa hukumu hii ilikuwa ya kinafiki
na ya uovu – kimsingi haikuwa hukumu iliyozingatia sheria wala utaratibu,
Kesi iliendeshwa usiku, hii ilikuwa kinyume cha utaratibu na kudhihirisha kuwa
lilikuwa swala la njama na uovu,
hakukuwa na muda wa kujitetea, kesi ilihukumiwa kwa kura, ambapo jambazi na mashuhuri
Baraba aliachiwa huru na Yesu Mwalimu na mtenda miujiza alichaguliwa kufa,
hakimu aligundua kuwa Yesu hakuwa na hatia lakini hakuzingatia haki kwa sababu
ya hofu ya fitina za kiyahudi na kwa unafiki alitoa hati ya hukumu ya kifo.
Mathayo
27:16-22 “Basi palikuwa na mfungwa mashuhuri siku zile,
aitwaye Baraba. Basi walipokutanika, Pilato akawaambia, Mnataka niwafungulie
yupi? Yule Baraba, au Yesu aitwaye Kristo? Kwa maana alijua ya kuwa wamemtoa
kwa husuda. Na alipokuwa ameketi juu ya kiti cha hukumu, mkewe alimpelekea
mjumbe, kumwambia, Usiwe na neno na yule mwenye haki; kwa sababu nimeteswa
mengi leo katika ndoto kwa ajili yake. Nao wakuu wa makuhani na wazee
wakawashawishi makutano ili wamtake Baraba, na kumwangamiza Yesu. Basi liwali
akajibu, akawaambia, Mnataka niwafungulie yupi katika hawa wawili? Wakasema,
Baraba. Pilato akawaambia, Basi, nimtendeje Yesu aitwaye Kristo? Wakasema wote,
Asulibiwe.”
Pamoja na kuwa kuhukumiwa kwa Yesu Kristo kwa njia ya
uonevu ilikuwa ni njia ya Mungu ya kuleta ukombozi wa mwanadamu, Hukumu hii
inatukumbusha wajibu wa watu kuhukumu kwa haki, kuhukumu kwa kuangalia mambo
juu juu kunaweza kutuletea gharama kubwa sana na kutukosesha mbele za Mungu,
kitendo hiki cha kuhukumiwa vibaya kwa Yesu kinatukumbusha kuwa wakati wa
kukumbuka mateso ya Bwana Yesu tunakumbushwa kuhukumu kwa haki na kuacha
dhuluma na kufanya upepelezi wa kesi mbalimbali ili kupata ushahidi wa
kujiridhisha na sio kukimbilia kutoa uamuzi wa haraka haraka, umewahi kujiuliza
ni kwanini Baraba alikuwa amefungwa na haikuwa tatizo lakini kulikuwa na haja
gani ya kutokuchelewesha hukumu ya Bwana Yesu hata kwa kifungo tu? Neno la
Mungu linatutaka kama tunahukumu basi tuhukumu kwa haki.
Yohana 7:24-26
“Basi msihukumu hukumu ya macho tu, bali ifanyeni
hukumu iliyo ya haki. Basi baadhi ya watu wa Yerusalemu wakasema, Je! Huyu siye
wanayemtafuta ili wamwue? Na kumbe! Anena waziwazi, wala hawamwambii neno!
Yamkini hao wakuu wanajua hakika ya kuwa huyu ndiye Kristo?”
Tunajifunza ya kuwa Yesu Kristo ambaye alikuwa na
uwezo wa kuagiza malaika waje kumuokoa na hali iliyokuwa ikimkabili alikubali
kupoteza haki zake, wakati mwingine katika maisha haya ya uchaji wa Mungu
tutadhulumiwa na kupoteza haki zetu, haya yanaweza kutupata na wakati mwingine
wenye kukudhulumu wakawa ni wapendwa kabisa, lakini Neno la Mungu linasema ni
afhadli kudhulumiwa na ni afhadhali kupoteza wakati mwingine na kule kuachilia
kutatujengea heshima mbele za Mungu
1Wakorintho
6:6-7 “Bali mwashitakiana, ndugu kwa ndugu, tena
mbele yao wasioamini. Basi imekuwa
upungufu kwenu kabisa kwamba mnashitakiana ninyi kwa ninyi. Maana si afadhali
kudhulumiwa? Maana si afadhali kunyang'anywa mali zenu?”
e. Njia ya msalaba inatukumbusha wakristo
kumuomba Mungu ili watu wema na watenda haki watawale ikiwezekana sisi
wenyewe tuwepo madarakani ili kutawala kwa haki, inapendeza sana watu wenye
haki wakitawala na inachukiza sana na kuleta kuugua waovu wakitawala.
Mithali 29:2 “Wenye haki wakiwa na amri, watu hufurahi; Bali mwovu
atawalapo, watu huugua.”
Kanisa lina wajibu wa kuombea mihimili ya maamuzi
katika inchi ili haki iweze kutendeka kila mahali, na wale walioko kwenye
maamuzi wanapaswa kujifunza kuwa na ujasiri na kusimama katika haki kwa gharama
yoyote ile na kutokuiga mfano wa Pilato katika hukumu hii ya ajabu aliyoifanya.
Hata hivyo wote tunakumbuka kuwa ingawa Yesu alionewa katika kesi hii alionewa
kwa sbabu yetu na kwaajili ya ukombozi wetu.
2.
Yesu
Kristo anaubeba Msalaba: # 2
Kuubeba msalaba
ni ishara ya kujitoa dhabihu, kujikana kujitoa sadaka, kuwa tayari kwa majaribu
na taabu na masumbufu ya Imani, Msalaba ni ishara ya kuvumilia magumu na sio
kubeba mizigo, ni nafasi ya kumfuata Yesu Kristo, njia zake tabia zake na utii,
baada ya hukumu ya kifo iliyokuwanya uongo kutolewa Yesu alikabidhiwa Msalaba
wake na kukubali kuubeba alifanya hivyo kwa hiyari na kwaajili yetu!
Yohana 19:15-17 “Basi
wale wakapiga kelele, Mwondoshe! Mwondoshe! Msulibishe! Pilato akawaambia, Je!
Nimsulibishe mfalme wenu! Wakuu wa makuhani wakamjibu, Sisi hatuna mfalme ila
Kaisari. Basi ndipo alipomtia mikononi mwao ili asulibiwe; nao wakampokea Yesu.
Akatoka, hali akijichukulia msalaba wake, mpaka mahali paitwapo Fuvu la Kichwa,
au kwa Kiebrania, Golgotha.”
Kitendo cha Yesu
Kristo kukubali kuubeba msalaba kinatufundisha jinsi ambavyo Yesu Kristo
alikuwa tayari sasa kuyatii mapenzi ya baba yake, kumbuka kufa kwake msalabani
ulikuwa ni mpango wa Mungu na ni mapenzi yake, kukubali kuubeba msalaba
kulikuwa ni ishara ya kwanza kwamba Yesu Kristo sasa anakubaliana na mateso
ambayo kimsingi haikuwa rahisi kukubaliana na njia ile aliyoipitia
Luka 22:41-42 “Mwenyewe
akajitenga nao kama kiasi cha kutupa jiwe, akapiga magoti akaomba, akisema, Ee
Baba, ikiwa ni mapenzi yako, uniondolee kikombe hiki; walakini si mapenzi
yangu, bali yako yatendeke.”
Wafilipi 2:6-9 “ambaye
yeye mwanzo alikuwa yuna namna ya Mungu, naye hakuona kule kuwa sawa na Mungu
kuwa ni kitu cha kushikamana nacho; bali alijifanya kuwa hana utukufu, akatwaa
namna ya mtumwa, akawa ana mfano wa wanadamu; tena, alipoonekana ana umbo kama
mwanadamu, alijinyenyekeza akawa mtii hata mauti, naam, mauti ya msalaba. Kwa
hiyo tena Mungu alimwadhimisha mno, akamkirimia Jina lile lipitalo kila jina;”
Yesu kukubali
kuubeba msalaba ilikuwa ni ishara ya upendo mkubwa kwa wanadamu self- sacrificial love, Yeye alikuwa
tayari kuyapoteza maisha yake kwaajili yetu, alikubali kuabishwa na kuibeba
fedhea ya dhambi na kuteketeza maisha yeke kwaajili ya upendo wake kwetu
Yohana 15:13 “Hakuna
aliye na upendo mwingi kuliko huu, wa mtu kuutoa uhai wake kwa ajili ya rafiki
zake.”
Ni watu wachache
sana duniani ambao wanaweza kukubali kutatoa maisha yao kwaajili ya wengine,
kuubeba msalaba ilikuwa ni alama kubwa sana ya kuwa Yesu Kristo hakuwa na
ubinafsi, wakati huu wa maadhimisho ya pasaka tunapokumbuka mateso yasiyo na
kifani ya Bwana Yesu ni muhimu kukumbuka kuwa Mungu alituumba pia kwaajili ya wengine
na ya kuwa mtu aliyekomaa kiroho katika ngazi ya juu zaidi ni yule ambaye yuko
tayari kuyatoa maisha yake kwaajili ya wengine! Kama sio wengine kujitoa
kwaajili yetu huenda tusingelikuwa hapa leo, Lakini wokovu wetu, maisha yetu na
kuwepo kwetu kumetokana na watu wengine kutuvumilia na kuyatekekeza aisha yao
ili sisi tuwepo!
Isidor Straus alikuwa moja ya wafanya
biashara wakubwa sana mwenye asili ya kijerumani na alikuwa mbunge pia katika
baraza la wawakilishi huko Marekani mtu huyu alikuwa tajiri mkubwa na mwenye
mali nyingi sana wakati wa ajali ya meli maarufu ya Titanic ilipokuwa inazama waokoaji walitoa kipaumbele kwa watu
wenye uwezo mkubwa na matajiri ili kuokoa maisha yao kwanza watu ambao
walijulikana kama VIP. Katika namna ya kushangaza mfanya biashara huyu Isdor Straus aliyekuwa na uwezo mkubwa
hata wa kununua Meli kama Titanic mara sita, Yeye alikataa kuokolewa na boti za
uokoaji na kuomba waokolewe kwanza wanawake na watoto, Mkewe aliyeitwa Ida pia alikubali kubaki na mumewe na
kukataa nafasi ya kuokolewa na boti maalumu na hivyo walikubali kufa kwa kuzama
majini anaingia kwenye kumbukumbu ya watu waliokubali kufa kwaajili ya usalama
wa wengine huku ni kujitoa kwa
hiyari ya hali ya juu sana na kusikokuwa na ubinafsi.
Kuubeba msalaba
kwa Bwana wetu Yesu Kristo kunatufunza hapa kwamba kila mwanafunzi wa Yesu
anapaswa kuelewa kuwa tumeitwa sio kumwamini tu bali pia na kushiriki mateso
kwaajili ya kusudi la Mungu, maisha yetu katika Bwana yanapaswa kuwa ni maisha
ya kujitoa kwaajili ya wengina na kuwa mbali na ubinafsi.
Wafilipi 1:29 “Maana
mmepewa kwa ajili ya Kristo, si kumwamini tu, ila na kuteswa kwa ajili yake;”
Kila mwanafunzi
wa Yesu anapaswa kujua kuwa kuna nyakati utaubeba msalaba wake kwaajili ya
wengine na kwaajili ya utii kwa Mungu wetu, kuifuta njia ya Yesu Kristo njia ya
msalaba ni pamoja na kujikana na kukataa ubinafsi kwa faida yetu na ya mwili wa
Kristo, mambo mengi duniani leo yangefanyika kwa weledi mkubwa kama tu watu wataacha
ubinafsi na kujiangalia wenyewe na kwa kufanya hivyo neno la Mungu
linatufundisha kuwa tunapoteza badala ya kuingiza.
Luka 9:23-25 “Akawaambia
wote, Mtu ye yote akitaka kunifuata, na ajikane mwenyewe, ajitwike msalaba wake
kila siku, anifuate. Kwa kuwa mtu atakaye kuiponya nafsi yake ataiangamiza, na
mtu atakayeiangamiza nafsi yake kwa ajili yangu ndiye atakayeisalimisha. Kwa
kuwa yamfaa nini mtu kuupata ulimwengu wote, kama akijiangamiza, au kujipoteza
mwenyewe?”
Kukubali kuubeba msalaba kunatufundisha
vilevile uwezo mkubwa wa kuvumilia magumu, Mungu ana makusudi na mpango
wake mkubwa katika maisha ya kila mwanadamu aliyemuamini na wakati wingine
Baraka hizo zimefichwa katika njia ngumu tunazozipitia, kukubali msalaba
ilikuwa ni njia ya unyenyekevu ya hali ya juu sana na njia nzito ya kujifunza
kuvumilia, wakati wote kuvumilia kunaleta thawabu kubwa sana thawabu zilizojificha,
Yesu alistahimili mapingamizi makubwa sana na kwa uvumilivu huo aliinuliwa juu sana
Waebrania 12:2-3 “tukimtazama
Yesu, mwenye kuanzisha na mwenye kutimiza imani yetu; ambaye kwa ajili ya
furaha iliyowekwa mbele yake aliustahimili msalaba na kuidharau aibu, naye
ameketi mkono wa kuume wa kiti cha enzi cha Mungu. Maana mtafakarini sana yeye
aliyeyastahimili mapingamizi makuu namna hii ya watendao dhambi juu ya nafsi
zao, msije mkachoka, mkizimia mioyoni mwenu.”
Tendo la Yesu
kuukubali Msalaba sio tu la kihistoria lakini linatufundisha wakristo mtindo wa
maisha, tunajifunza kutii mapenzi ya Mungu na kuwa waaminifu hata kufa, Tunajifunza unyenyekevu, tunajifunza kuvumilia (uvumilivu), na
tunajifunza msamaha na kukubali njia na
mpango wa Mungu wa ukombozi wa Mwanadamu.
3.
Simon
yule Mkirene asaidia kubeba msalaba. # 5
Simon Mkirene
anajitokeza kama mtu aliyeshurutishwa na Askari katika kusaidia kuubeba msalaba
wa Yesu; hata hivyo katika namna ya kushangaza sana Mtu huyu kwa hiyari yake
alikubali kuubeba msalaba wa Yesu pamoja naye, angeliweza kukataa kwani
halikuwa swala lililomuhusu, lakini alimuhurumia Yesu Kristo, na kwa jambo hili
aliweza kuingia katika rekodi ya injili zinazofanana yaani “synoptic Gospel” zote kwa hiyo kuna kitu
cha muhimu sana cha kutufunza katika swala zima la njia ya msalaba. Kwanza
anatajwa kwa tukio lake hili katika injili zote tatu ona:-
a. Mathayo 27:32 “Hata
walipokuwa wakitoka, wakamwona mtu Mkirene, jina lake Simoni; huyu
wakamshurutisha auchukue msalaba wake.”
b. Marko 15:21 “Wakamshurutisha
mtu aliyekuwa akipita, akitoka mashamba, Simoni Mkirene, baba yao Iskanda na
Rufo, ili auchukue msalaba wake.”
c. Luka 23:26 “Na
walipokuwa wakimwondoa walimkamata mtu mmoja, Simoni Mkirene, aliyekuwa ametoka
shamba, wakamtwika msalaba, auchukue nyuma yake Yesu.”
Simon huyu
alikuwa ni mgeni kutoka Kirene (Cyrene)
ambako kunajulikana kama Libya leo hizi zilikuwa ni pande za Afrika ya kaskazini,
mtu huyu kama alikuwa myahudi basi alikuwa akiishi Afrika na huenda alipanda
Yerusalem kwaajili ya maadhimisho ya pasaka, Yeye alilazimishwa kuubeba msalaba
wa Yesu, Na kwa hiyari yake alikubali kwani angeweza kukataa lakini alishiriki
kuubeba msalaba wa Yesu pamoja naye, kimsingi tunajifunza jinsi mtu huyu
alivyokuwa tayari kushiriki taabu pamoja na wengine alimsaidia Yesu kubeba
msalaba na kushiriki mateso ya wengine, kwa sababu hiyo yeye alikuwa na moyo wa
kuchukuliana na mizigo ya wengine lakini pia alikuwa na uwezo wa kufurahi na
wanaofurahi na kulia pamoja na wanaolia, hapa alihuzunika na kulia pamoja na
Yesu Katika taabu yake.
Wagalatia 6:2 “Mchukuliane
mizigo na kuitimiza hivyo sheria ya Kristo.”
Warumi 12:15 “Furahini
pamoja nao wafurahio; lieni pamoja nao waliao.”
Simon Mkirene
licha ya kuwa mtu aliyekuwa tayari kuchukuliana mzigo na wengine, na kuwa mtu
anayelia na wale waliao pia anatukumbusha wajibu wetu wa kuyashiriki mateso ya
Kristo, kila mtu aliyeokolewa anapaswa kukumbuka ya kuwa tumeitwa au tumepewa
sio kumwamini tu bali na kuteswa kwaajili ya Kristo, kwaajili ya njia hii ya
wokovu wakati mwingine tutapata mateso na changamoto za aina mbalimbali lakini
hatuna budi kukubali kupita katika njia hizo:-
Wafilipi 1:29 “.Maana
mmepewa kwa ajili ya Kristo, si kumwamini tu, ila na kuteswa kwa ajili yake;”
2Timotheo 2:3-8 “Ushiriki
taabu pamoja nami, kama askari mwema wa Kristo Yesu. Hakuna apigaye vita
ajitiaye katika shughuli za dunia, ili ampendeze yeye aliyemwandika awe askari.
Hata mtu akishindana katika machezo hapewi taji, asiposhindana kwa halali.
Yampasa mkulima mwenye taabu ya kazi kuwa wa kwanza wa kupata fungu la matunda.
Yafahamu sana hayo nisemayo, kwa maana Bwana atakupa akili katika mambo yote.
Mkumbuke Yesu Kristo, aliyefufuka katika wafu, wa uzao wa Daudi kama inenavyo
injili yangu.”
Historia ya
kanisa inaonyesha kuwa Mzee huyu ambaye alikubali kuyashiriki mateso ya Bwana
Yesu hatimaye watoto wake yeye na familia yake waliokolewa na watoto wake
wakamuamini Bwana Yesu na kuwa watu maarufu sana nyakati za Kanisa la Kwanza,
watoto wa mzee Simeoni Mkirene walikuwa ni (Alexander na Rufus) Iskanda
na Rufo na walikuwa wanafunzi waaminifu sana wa Bwana Yesu, tukio la mtu huyu
mwenye huruma kutoka Afrika kumsaidia Yesu, kulisababisha muujiza wa yeye
kuokolewa pamoja na familia yake na wakawa maarufu sana katika kanisa lakini
pia walikuwa waaminifu na mama yao Rufo
akawa kama mama wa wakristo wengi na mitume wengi sana baadaye akiwepo Paulo
mtume ona
Warumi 16:18 “Nisalimieni
Trifaina na Trifosa, wenye bidii katika Bwana. Nisalimieni Persisi, mpenzi
aliyejitahidi sana katika Bwana. Nisalimieni Rufo, mteule katika Bwana, na
mamaye, aliye mama yangu pia.”
Mafundisho ya
njia ya msalaba hapa yanatufundisha kuwa kupitia Simeoni kwamba kila mwanadamu
anapaswa kuwa na matendo ya huruma kwa wahitaji, tunaposaidia watu kwa namna na
jinsi mbalimbali maana yake tunamsaidia Yesu bila sisi kujua, Ingawa Yesu peke
yake ndiye mwokozi wa ulimwengu Lakini kitendo cha Simeoni kusaidia msalaba
hakumfanyi yeye kuwa mwokozi bali kunamuweka yeye kuwa miongoni mwa watu
wanaosaidia wengine, kuokolewa, kumpokea Yesu, kukutana na mahitaji yao na kwa
sababu hiyo kushiriki kwa namna moja ama nyingine katika kuifikisha injili
duniani. tunapowatendea mema wengine kwa sababu ya Imani yetu katika Kristo
tunamtendea Yesu bila kujua:-
Mathayo 25:34-40 “Kisha
Mfalme atawaambia wale walioko mkono wake wa kuume, Njoni, mliobarikiwa na Baba
yangu, urithini ufalme mliowekewa tayari tangu kuumbwa ulimwengu; kwa maana
nalikuwa na njaa, mkanipa chakula; nalikuwa na kiu, mkaninywesha; nalikuwa
mgeni, mkanikaribisha; nalikuwa uchi, mkanivika nalikuwa mgonjwa, mkaja
kunitazama; nalikuwa kifungoni, mkanijia. Ndipo wenye haki watakapomjibu,
wakisema, Bwana, ni lini tulipokuona una njaa, tukakulisha, au una kiu
tukakunywesha? Tena ni lini tulipokuona u mgeni, tukakukaribisha, au u uchi,
tukakuvika? Ni lini tena tulipokuona u mgonjwa, au kifungoni, tukakujia? Na
Mfalme atajibu, akiwaambia, Amin, nawaambia, kadiri mlivyomtendea mmojawapo wa
hao ndugu zangu walio wadogo, mlinitendea mimi.”
Aidha Simeoni
Mkirene katika picha ya kinabii anatufundisha ya kuwa Mungu ataitumia Afrika
katika kuitangaza injili wakati wa uchungu na mateso au wakati mgumu dunia yote
itakapokuwa imeharibika kwa uovu na ukatili Mungu ataitumia Afrika kusaidia
kuenea kwa injili katika siku za mwisho wakati dunia ikiwa imeharibika kwa
sababu hiyo Afrika inakumbushwa kuwa tayari kuihubiri injili wakati wa
uharibifu wa dunia.
4.
Huruma
kwa wanawake wa Yerusalem! # 8
Akiwa katika
njia ya msalaba katikati ya mateso Yesu anakutana na wanawake wa Yerusalem
ambao kimsingi walikuwa wakimuhurumia kwa sababu ya mateso yake na hata
kumlilia, wao walikuwa wanakumbuka mambo yote mazuri ambayo Yesu aliwatendea
watu wasio na shukurani na kuwa sasa kwa wivu wanamuweka matatani wamama hawa
wanalia na kuomboleza lakini inaonekana Yesu anawahurumia wao zaidi na kuwaonya
Luka 23:27-31 “Mkutano
mkubwa wa watu wakamfuata, na wanawake waliokuwa wakijipiga vifua na
kumwombolezea. Yesu akawageukia, akasema, Enyi binti za Yerusalemu, msinililie
mimi, bali jililieni nafsi zenu na watoto wenu. Kwa maana tazama, siku zitakuja
watakaposema, Heri walio tasa, na matumbo yasiyozaa, na maziwa yasiyonyonyesha.
Ndipo watakapoanza kuiambia milima, Tuangukieni, na vilima, Tufunikeni. Kwa
kuwa kama wakitenda mambo haya katika mti mbichi, itakuwaje katika mkavu?”
Wakati
wanawake hawa wa Yerusalem wakiwa wanamsikitikia Yesu Kristo na kumuhurumia na
kumuombolezea na kumlilia, Yesu ambaye wakati huu alikuwa kwenye mateso na
akiwa amebeba msalaba na maumivu, Yesu anaonyesha kuyajali maisha yao hasa na
maisha yao ya baadaye, ingawa alikuwa katika maumivu makali lakini alikuwa na
huruma kwa kuwa alikuwa anajua yanayokuja mbeleni kama nabii, Yesu aliwaonya
wanawake hao kulia na kuomboleza sio kwaajili yake bali kwaajili yao na watoto
wao, Kimsingi Yesu alikuwa anaona hukumu kubwa inayokuja dhidi ya Yerusalem
miaka michache baadaye na hii ilikuwa inajumuisha kubomolewa na kuvunjiliwa
mbali kwa mji wa Yerusalm na Israel nzima tukio hilo lililotokea mwaka wa 70
baada ya Kristo wakati huu ikiwa ni mwaka wa 33 baada ya Kristo ukweli ni kuwa
ilipita miaka 37 tu na Yerusalem ulibomolewa vibaya na watu wengi kuuawa na
wayahudi kukimbilia uhamishoni wengi sana na Askari wa kirumi walipita kila mji
na kila kijiji wakiua watu na kuchinja kila myahudi, ulikuwa ni wakati wa historia
mbaya zaidi kuwahi kutokea, watoto wa wanawakw wale walioonywa na Yesu ndio
waliokutana na hukumu ile mbaya!
Jililieni
nafsi zenu na watoto wenu yalikuwa ni maonyo ya Yesu aliyekuwa katika mateso
akionya juu ya watoto wa Yerusalem ya kuwa watapitia mateso makali na makubwa
sana kutokana na kizazi kile kumsulubisha mwokozi, Yesu anaonya kuwa itakuwa
dhiki ya hatari ambayo watu watasema heri matumbo yaliyo tasa, kuashiria huzuni
kubwa itakayowapata wayahudi kwa kuona watoto wao wakiuawa, Yesu anawaonya wao
kuwa tayari kwa hukumu hiyo na kuwataka kuwa afadhali watubu na kujihurumia
wenyewe.
Aidha katika
somo hili la njia ya msalaba tunaonywa kuwa hatupaswi tu kuhuzunika kwaajili ya
kuteswa na kufa kwa Yesu Kristo badala yake tunapaswa kuwa na ufahamu kwanini
alikufa na faida ya kifo chake inatuletea wokovu, huzuni kubwa na mbaya zaidi
sio kwa sababu Yesu anateswa na kufa bali kama sisi tutakosa nafasi ya kuzifurahia
faida za msalaba.
Yesu
aliendelea kuonya kuwa ikiwa wanaufanyia hivi mti mbichi itakuwaje kwa mti
mkavu, lilikuwa ni onyo pia kuwa kama
mtu mwema kama Yesu anatendewa ukatili kama ule hebu jaribu kufikiri wale wasio
na toba, kama Mungu anaruhusu mateso kama haya kwa mtu mwenye haki, kutatokea
nini kwa wale wasio haki.
Yesu alionya
kuwa ni lazima watu watambue kuwa Mungu ni Mungu mwenye haki na atahukumu kwa
dhati, na kamwe watu wasichukulie uvumilivu wake kama nafasi ya kujifanyia
wanayoyataka, ni lazima tuwafundishe watoto wetu kuishi maisha ya haki na
kuikulia njia ya Bwana, aidha kile alichokisema Yesu kwa wanawake wa Yerusalem
alikwisha kukisema kwa kina kwa wanafunzi wake katika Mathayo 24 akiwaonya
kuhusu siku za mwisho na pia kuhusu Anguko la mji wa Yerusalem.
Mathayo 24:2-12 “Naye
akajibu akawaambia, Hamyaoni haya yote? Amin, nawaambieni, Halitasalia hapa
jiwe juu ya jiwe ambalo halitabomoshwa. Hata alipokuwa ameketi katika mlima wa
Mizeituni, wanafunzi wake wakamwendea kwa faragha, wakisema, Tuambie, mambo
hayo yatakuwa lini? Nayo ni nini dalili ya kuja kwako, na ya mwisho wa dunia?
Yesu akajibu, akawaambia, Angalieni, mtu asiwadanganye. Kwa sababu wengi
watakuja kwa jina langu, wakisema, Mimi ni Kristo; nao watadanganya wengi.
Nanyi mtasikia habari za vita na matetesi ya vita; angalieni, msitishwe; maana
hayo hayana budi kutukia; lakini ule mwisho bado. Kwa maana taifa litaondoka
kupigana na taifa, na ufalme kupigana na ufalme; kutakuwa na njaa, na
matetemeko ya nchi mahali mahali. Hayo yote ndiyo mwanzo wa utungu. Wakati huo
watawasaliti ninyi mpate dhiki, nao watawaua; nanyi mtakuwa watu wa kuchukiwa
na mataifa yote kwa ajili ya jina langu. Ndipo wengi watakapojikwaa, nao
watasalitiana, na kuchukiana. Na manabii wengi wa uongo watatokea, na
kudanganya wengi. Na kwa sababu ya kuongezeka maasi, upendo wa wengi utapoa.”
Kitendo cha
Yesu kukutana na wanawake wa Yerusalem na kuwaonya wajililie nafsi zao na
watoto wao kinatukumbusha wajibu wetu kama kanisa kuzingatia na kukumbuka
maonyo yote kuhusu unabii wa siku za mwisho, tunakumbushwa kuwa tunaishi katika
nyakati za hatari na kwa sababu hiyo kila mtu anapaswa kuchukua tahadhari na kujikumbusha kuwa
kanisa hatuko salama na badala yake ni jukumu la kila mkristo kujitazama na
kujihami na kuzipima roho/mafundisho ya watumishi wa Mungu katika nyakati hizi
za hatari.
1Timotheo 4:1-2 “Basi
Roho anena waziwazi ya kwamba nyakati za mwisho wengine watajitenga na imani,
wakisikiliza roho zidanganyazo, na mafundisho ya mashetani; kwa unafiki wa watu
wasemao uongo, wakichomwa moto dhamiri zao wenyewe;”
2Timotheo 3:1-5 “Lakini
ufahamu neno hili, ya kuwa siku za mwisho kutakuwako nyakati za hatari. Maana
watu watakuwa wenye kujipenda wenyewe, wenye kupenda fedha, wenye kujisifu,
wenye kiburi, wenye kutukana, wasiotii wazazi wao, wasio na shukrani, wasio
safi,wasiowapenda wa kwao, wasiotaka kufanya suluhu, wasingiziaji, wasiojizuia,
wakali, wasiopenda mema,wasaliti, wakaidi, wenye kujivuna, wapendao anasa
kuliko kumpenda Mungu;wenye mfano wa utauwa, lakini wakikana nguvu zake; hao
nao ujiepushe nao.”
Kristo pia
anatukumbusha wajibu wetu wa kuhakikisha kuwa tunajiangalia sisi wenyewe kuwa
tukoje na Mungu badala ya kunyoosha vidole kwa wengine, tunafundishwa kuacha
kufikiria wengine wanapopitia shida na changamoto kuwa labda huenda wana makosa
makubwa kuliko yetu na badala yake tunakumbushwa kujiangalia wenyewe na kutubu
kwa sababu kama wenye haki wanateseka ni zaidi sana kwa mtu asiye haki hataweza
kustahimili
Luka 6:41-42 “Basi,
mbona wakitazama kibanzi kilicho ndani ya jicho la ndugu yako, na boriti iliyo
ndani ya jicho lako mwenyewe huiangalii? Au, utawezaje kumwambia ndugu yako,
Ndugu yangu, niache nikitoe kibanzi kilicho ndani ya jicho lako, nawe huiangalii
boriti iliyo ndani ya jicho lako mwenyewe? Mnafiki wewe, itoe kwanza ile boriti
katika jicho lako mwenyewe, ndipo utakapoona vema kukitoa kile kibanzi
kilichomo katika jicho la ndugu yako.”
Luka 13:1-5 “Na
wakati uo huo walikuwapo watu waliompasha habari ya Wagalilaya wale ambao
Pilato alichanganya damu yao na dhabihu zao. Akawajibu akawaambia, Je! Mwadhani
ya kwamba Wagalilaya hao walikuwa wenye dhambi kuliko Wagalilaya wote, hata
wakapatwa na mambo hayo? Nawaambia, Sivyo; lakini msipotubu, ninyi nyote
mtaangamia vivyo hivyo. Au wale kumi na wanane, walioangukiwa na mnara huko
Siloamu, ukawaua, mwadhani ya kwamba wao walikuwa wakosaji kuliko watu wote
waliokaa Yerusalemu? Nawaambia, Sivyo; lakini msipotubu, ninyi nyote mtaangamia
vivyo hivyo.”
Tangu zamani
imekuwepo dhana Fulani ya kufikiri kuwa wale wanaopatwa na mabaya labda walikuwa
waovu kuliko sisi, au wanaopatwa na ajali, Lakini Yesu anatukumbusha kuwa wao
wanaweza kuwa sio waovu kuliko waliobaki na hivyo iko haja ya kuitumia nafasi
tuliyo nayo ya Amani na uhai kwaajili ya toba na kujiweka tayari kwaajili ya
Mungu wetu
5.
Yesu
anavuliwa nguo # 10
Tunajifunza
Nini Kupitia Kitendo cha Yesu Kuvuliwa Nguo Kabla ya Kusulubiwa? Kitendo cha
Yesu kuvuliwa nguo kabla ya kusulubiwa ni sehemu muhimu ya mateso yake, na kina
maana kubwa kiroho na kimaandiko. Tukio hili linatajwa katika Injili zote nne:
·
Mathayo
27:28, 35 – “Wakamvua nguo, wakamvika vazi
jekundu.35 Walipokwisha kumsulibisha, waligawa mavazi yake, wakipiga kura; [ili
litimie neno lililonenwa na nabii, Waligawa nguo zangu kati yao, na juu ya vazi
langu walipiga kura.]”
·
Marko
15:20, 24 – “Baada ya kumdhihaki, wakamvua lile
joho la rangi ya zambarau, wakamvika mavazi yake mwenyewe... Wakagawana nguo
zake, wakizipigia kura waone nani atakaye pata kitu gani.”
·
Luka
23:34 – “Yesu akasema, Baba, uwasamehe, kwa kuwa
hawajui watendalo. Wale wakagawana mavazi yake kwa kura.”
·
Yohana
19:23-24 – “Askari walipomsulubisha Yesu, walitwaa
mavazi yake, wakayagawa mafungu manne, kila askari Fungu Lake; na lile joho
lake pia. Na hilo joho halikuwa na mshono, limetengenezwa kwa kipande kimoja
tangu juu hata chini. Wakaambiana, ‘Tusilikate, ila tuzipige kura tupate kujua
litakuwa la nani.’ Hii ilikuwa ili andiko litimie, lililosema: Wamegawana mavazi
yangu kati yao, na nguo yangu wameipigia kura.”
Maana na
Mafundisho Tunayopata Kutoka kwa Kitendo hiki
a. Utimilifu wa Unabii wa Agano la Kale- Kitendo
hiki kilikuwa ni utimilifu wa Zaburi
22:18 – “Wamegawana mavazi yangu, na nguo yangu
wameipigia kura.”
Hii inaonyesha kuwa mateso ya Yesu hayakuwa ya bahati
mbaya bali ni sehemu ya mpango wa Mungu uliotabiriwa tangu zamani. Yesu alikuwa
akiyatimiza mapenzi ya Mungu, na kila andiko alilokuwa ameandikiwa, kwa hiyo
hakuna kilichotokea Msalabani ambacho kilitokea kwa bahati mbaya hii
inadhihirisha wazi kuwa haya yalikuwa ni mapenzi ya Mungu.
b. Yesu alihisi aibu na fedheha kwa ajili Yetu - Kuvuliwa nguo hadharani ni tendo
la aibu na fedheha. Kwa Wayahudi, kuona mtu akiwa uchi hadharani lilikuwa jambo
la kudhalilisha sana, kitendo cha kuwekwa uchi ni kitendo cha kuaibishwa ni
tukio la kudharaulika sana, hili ndio tukio lililomtokea Adamu na Eva katika
Bustani ya Edeni walipokula lile tunda walilokatazwa, wakati wote tunapotenda
dhambi tukumbuke kuwa tunajiweka katika aibu na tunajivua nguo, Yesu
anapovuliwa nguo anatukumbusha wajibu wetu ya kuwa ni yeye pekee anayeweza
kutuvalisha vazi lililo bora, kwani pale msalabani alivuliwa nguo kwaajili ya
matendo yetu, alifanywa vile kwa sababu dhambi zetu zilizowekwa juu yake na
dhambi kwa kweli ni aibu mbele za Mungu.
Isaya 47:3 “Uchi wako utafunuliwa, Naam, aibu yako itaonekana.
Nitalipa kisasi; simkubali mtu ye yote.”
Nahumu 3:5-6 “Tazama, mimi ni juu yako, asema Bwana wa majeshi; nami
nitafunua marinda yako mbele ya uso wako; nami nitawaonyesha mataifa uchi wako,
na falme aibu yako. Nami nitatupa uchafu uchukizao juu yako, kukufanya uwe
mchafu, nami nitakufanya kuwa kitu cha kutazamwa kwa dharau.”
Isaya 53:3-5 –
“Alidharauliwa na kukataliwa na watu; Mtu wa huzuni
nyingi, ajuaye sikitiko; Na kama mtu ambaye watu humficha nyuso zao,
Alidharauliwa wala hatukumhesabu kuwa kitu. Hakika ameyachukua masikitiko yetu,
Amejitwika huzuni zetu; Lakini tulimdhania ya kuwa amepigwa, Amepigwa na Mungu,
na kuteswa.Bali alijeruhiwa kwa makosa yetu, Alichubuliwa kwa maovu yetu;
Adhabu ya amani yetu ilikuwa juu yake, Na kwa kupigwa kwake sisi tumepona.”
Waebrania 12:2
– “tukimtazama Yesu, mwenye kuanzisha na mwenye
kutimiza imani yetu; ambaye kwa ajili ya furaha iliyowekwa mbele yake
aliustahimili msalaba na kuidharau aibu, naye ameketi mkono wa kuume wa kiti
cha enzi cha Mungu”
Hii inatufundisha kuwa Yesu alikubali fedheha yetu ili
sisi tupate heshima mbele za Mungu. Yesu Aliacha Kila Kitu kwa Ajili Yetu-Yesu
alipovuliwa nguo, alikuwa hana kitu chochote cha kidunia. Hii inatuonyesha kuwa
alijitoa kikamilifu kwa ajili ya wokovu wetu: Hili linatufundisha kuwa hakuna
kitu cha kidunia kinachopaswa kutuzuia kumfuata Kristo, lakini pia
tubakumbushwa ile kweli ya kuwa hatukuja duniani na kitu na tutaondoka duniani
bila kitu.
2 Wakorintho 8:9
– “Kwa kuwa mnajua neema ya Bwana wetu Yesu Kristo,
ya kwamba alipokuwa tajiri, alikubali kuwa maskini kwa ajili yenu, ili ninyi
mpate kuwa matajiri kupitia umaskini wake.”
Yesu analishauri kanisa kujificha kwake kwa toba
katika ulimwengu wa roho tunapotubu na kucha maovu yetu Yesu hutuvika mavazi
meupe na kutuficha dhidi ya aibu yetu na kutuondoa katika mashaka
Ufunuo 3:17-19
“Kwa kuwa wasema, Mimi ni tajiri, nimejitajirisha,
wala sina haja ya kitu; nawe hujui ya kuwa wewe u mnyonge, na mwenye mashaka,
na maskini, na kipofu, na uchi. Nakupa shauri, ununue kwangu dhahabu
iliyosafishwa kwa moto, upate kuwa tajiri, na mavazi meupe upate kuvaa, aibu ya
uchi wako isionekane, na dawa ya macho ya kujipaka macho yako, upate kuona.
Wote niwapendao mimi nawakemea, na kuwarudi; basi uwe na bidii, ukatubu.”
Kama Mungu alivyomfunika Adamu kwa mavazi yaliyo bora
katika bustani ya Edeni atatuhifadhi sisi kwa haki yake kwani yeye alifanyika
dhambi ili sisi tuwe haki
2 Wakorintho 5:21 –
“Yeye asiyejua dhambi alimfanya kuwa dhambi kwa
ajili yetu, ili sisi tupate kuwa haki ya Mungu ndani yake.”
Dunia
ilimnyima Yesu Heshima yake yote, Lakini yeye alituheshimisha, na kutokana na
kukubali kudharauliwa kwa kiwango hicho Yesu ameinuliwa juu kuliko mtu awaye
yote na amekekirimiwa jina lipitalo majina yote na ameketi mkono wa kuume wa
nguvu wa Mungu baba mwenyezi mbinguni.
6.
Yesu
anawambwa Msalabani na kusulubiwa # 11
Yohana 19:16-18 “Basi
ndipo alipomtia mikononi mwao ili asulibiwe; nao wakampokea Yesu. Akatoka, hali
akijichukulia msalaba wake, mpaka mahali paitwapo Fuvu la Kichwa, au kwa
Kiebrania, Golgotha.Wakamsulibisha huko, na wengine wawili pamoja naye, mmoja
huku na mmoja huku, na Yesu katikati.”
Yesu alifanya
kazi nyingi sana za kuponya na kufundisha watu neno la Mungu lakini moja ya
kazi muhimu kabisa aliyoifanya na kuikamilisha ni kufa msalabani kwaajili ya
dhambi za ulimwengu kupitia njia ya kusulubiwa msalabani
Mathayo 1:21 “Naye
atazaa mwana, nawe utamwita jina lake Yesu, maana, yeye ndiye atakayewaokoa
watu wake na dhambi zao.”
Yohana 1:29 “Siku
ya pili yake amwona Yesu anakuja kwake, akasema, Tazama, Mwana-kondoo wa Mungu,
aichukuaye dhambi ya ulimwengu!”
Pamoja na tukio
hili Mateso yake, kufa kwake na kufufuka kwake msalabani, Yesu ilikuwa sio tu
anapaswa kufa lakini pia analipaswa kufufuka kwaajili yetu, kitendo cha yeye
kufufuka kinampa nafasi ya kuwa kuhani mkuu na mwombezi na mpatanishi kwaajili
yetu huko mbinguni
Warumi 8:33-34 “Ni
nani atakayewashitaki wateule wa Mungu? Mungu ndiye mwenye kuwahesabia haki. Ni
nani atakayewahukumia adhabu? Kristo Yesu ndiye aliyekufa; naam, na zaidi ya
hayo, amefufuka katika wafu, naye yuko mkono wa kuume wa Mungu; tena ndiye
anayetuombea.”
Warumi 4:24-25 “bali
na kwa ajili yetu sisi mtakaohesabiwa vivyo hivyo, sisi tunaomwamini yeye
aliyemfufua Yesu Bwana wetu katika wafu; ambaye alitolewa kwa ajili ya makosa
yetu, na kufufuliwa ili mpate kuhesabiwa haki.”
Warumi 5:9-11 “Basi
zaidi sana tukiisha kuhesabiwa haki katika damu yake, tutaokolewa na ghadhabu
kwa yeye. Kwa maana ikiwa tulipokuwa adui tulipatanishwa na Mungu kwa mauti ya
Mwana wake; zaidi sana baada ya kupatanishwa tutaokolewa katika uzima wake.
Wala si hivyo tu, ila pia twajifurahisha katika Mungu kwa Bwana wetu Yesu
Kristo, ambaye kwa yeye sasa tumeupokea huo upatanisho.”
Kusulubiwa kwake
msalabani kunatukumbusha upendo mkubwa sana wa Mungu kwa wanadamu ambapo Mungu
kwa hiyari yake mwenyewe anaamua kuwakomboa wanadamu kwa adhabu aliyojipa yeye
mwenyewe kwa ajili ya upendo wake kwetu
Yohana 3:16 “Kwa
maana jinsi hii Mungu aliupenda ulimwengu, hata akamtoa Mwanawe pekee, ili kila
mtu amwaminiye asipotee, bali awe na uzima wa milele.”
7.
Yesu
Kristo anafia msalabani # 12
Mathayo 27:45-50. “Basi
tangu saa sita palikuwa na giza juu ya nchi yote hata saa tisa. Na kama saa
tisa, Yesu akapaza sauti yake kwa nguvu akisema, Eloi, Eloi, lama sabakthani?
Yaani, Mungu wangu, Mungu wangu, mbona umeniacha? Na baadhi yao waliohudhuria,
waliposikia, walisema, Huyu anamwita Eliya. Mara mmoja wao akaenda mbio,
akatwaa sifongo, akaijaza siki, akaitia juu ya mwanzi, akamnywesha. Wale
wengine wakasema, Acha; na tuone kama Eliya anakuja kumwokoa. Naye Yesu akiisha
kupaza sauti tena kwa nguvu, akaitoa roho yake.”
Kitendo cha Yesu
Kristo kufa msalabani kinathibitisha wazi kuwa Yesu aliikamilisha kazi yote na
unabii, hata alipopaza Sauti na kusema imekwisha Yesu alikuwa na maana ya
kuikamilisha kazi yote aliyokuwa ameandikiwa aikamilishe, Yesu alihakikisha
kuwa kila neno lililonena na Mungu limetimia na hivyo hakukuwa na unabii wowote
kuhusu mateso yake ambao ulikuwa haujatimia
-
Kazi ya upatanisho
kati ya Mungu na wanadamu ilikuwa imekamilishwa Warumi 5:10 “Kwa maana ikiwa tulipokuwa adui tulipatanishwa na Mungu
kwa mauti ya Mwana wake; zaidi sana baada ya kupatanishwa tutaokolewa katika
uzima wake.”
-
Kristo
alikuwa amefanyika sadaka kamili ya dhambi kwaajili yetu Waebrania 10:10-14 “Katika mapenzi hayo mmepata utakaso, kwa kutolewa mwili
wa Yesu Kristo mara moja tu. Na kila kuhani husimama kila siku akifanya ibada,
na kutoa dhabihu zile zile mara nyingi; ambazo haziwezi kabisa kuondoa dhambi.
Lakini huyu, alipokwisha kutoa kwa ajili ya dhambi dhabihu moja idumuyo hata
milele, aliketi mkono wa kuume wa Mungu; tangu hapo akingojea hata adui zake wawekwe
kuwa chini ya miguu yake. Maana kwa toleo moja amewakamilisha hata milele hao
wanaotakaswa.”
- Kazi ya kuwashinda maadui wakubwa wa mwanadamu,
Shetani, dhambi na mauti ilikamilishwa, kwa kifo chake msalabani alilipa deni
la dhambi, na kumvua shetani enzi na mamlaka
Wakolosai
2:14-15 “akiisha kuifuta ile hati iliyoandikwa ya
kutushitaki kwa hukumu zake, iliyokuwa na uadui kwetu; akaiondoa isiwepo tena,
akaigongomea msalabani; akiisha kuzivua enzi na mamlaka, na kuzifanya kuwa
mkogo kwa ujasiri, akizishangilia katika msalaba huo.”
Waebrania
2:14-15 “Basi, kwa kuwa watoto wameshiriki damu na
mwili, yeye naye vivyo hivyo alishiriki yayo hayo, ili kwa njia ya mauti
amharibu yeye aliyekuwa na nguvu za mauti, yaani, Ibilisi, awaache huru wale
ambao kwamba maisha yao yote kwa hofu ya mauti walikuwa katika hali ya utumwa.”
8.
Yesu
anashushwa Msalabani # 13
Yohana 19:38-40 “Hata
baada ya hayo Yusufu wa Arimathaya, naye ni mwanafunzi wa Yesu, (lakini kwa
siri, kwa hofu ya Wayahudi), alimwomba Pilato ruhusa ili auondoe mwili wake
Yesu. Na Pilato akampa ruhusa. Basi akaenda, akauondoa mwili wake. Akaenda
Nikodemo naye, (yule aliyemwendea usiku hapo kwanza), akaleta machanganyiko ya
manemane na uudi, yapata ratli mia. Basi wakautwaa mwili wake Yesu, wakaufunga
sanda ya kitani pamoja na yale manukato, kama ilivyo desturi ya Wayahudi katika
kuzika.”
Kitendo cha
mwili wa Bwana Yesu kushushwa kutoka msalabani na kufanyiwa maandalizi ya
kuzikwa kilikuwa ni kitendo kinachotufundisha unyenyekevu mkubwa, Kumbuka yeye
alikuwa ni mwana wa Mungu lakini hapa alikuwa amekufa, mtu aliyefariki dunia
huwa hajimudu kabisa, anafanyiwa kila kitu anasaidiwa na wanadamu wenzake, huu
ndio wakati ambapo tunawahitaji wanadamu wenzetu washughulike na sisi, wawe
masikini au matajiri, tunajifunza kuwaheshimu watu na kutembea duniani kwa
unyenekevu.
Wale waliokuja
kumzika Yesu Kristo kama rafiki yao na mwalimu wao, walionyesha upendo wa kweli
hata katika wakati mgumu lakini maziko makubwa ya heshima walioyafanya
yanatukumbusha kuwa kila mwanadamu duniani hata kama alizarauliwa kiasi gani
anapaswa kuzikwa kwa heshima zote, Yesu anatimiza unabii wa Samsoni ambaye
alikataliwa na kukosa heshima alipokuwa akali hai, lakini alipofariki nduguze
walikuja kuutwaa mwili wake na kumhifadhi, alidharauliwa alipokuwa hai na
aliheshimiwa sana baada ya kifo chake.
Waamuzi 16:31. “Ndipo
ndugu zake, na watu wote wa nyumba ya baba yake wakatelemka, wakamtwaa
wakamchukua, wakamzika kati ya Sora na Eshtaoli, katika kiwanja cha kuzikia cha
Manoa baba yake. Naye alikuwa mwamuzi wa Israeli muda wa miaka ishirini.”
Ingawa Yesu
alishushwa kama maiti isiyokuwa na uwezo wowote yeye bado alijua kuwa
atafufuka, Yesu anatufundisha kuwa kifo sio mwisho wa kila kitu, kwani liko
tumaini la maisha mapya, mtu akimuamini Yesu hafi bali anapita kutoka mautini
na kuingia uzimani
Yohana 11:25-16. “Yesu
akamwambia, Mimi ndimi huo ufufuo, na uzima. Yeye aniaminiye mimi, ajapokufa,
atakuwa anaishi; naye kila aishiye na kuniamini hatakufa kabisa hata milele.
Je! Unayasadiki hayo?”
9.
Kristo
Yesu anazikwa Kaburini # 14
Tendo la kuzikwa
kwa Yesu Kristo linathibitisha kuwa Yesu alikufa kweli kimwili kwaajili ya
dhambi zetu, Yesu alizikwa pia kama sehemu ya kutimiza unabii kuhusu kuzikwa
pamoja na waovu
Yohana 19:41-42 “Na
pale pale aliposulibiwa palikuwa na bustani; na ndani ya bustani mna kaburi
jipya, ambalo hajatiwa bado mtu ye yote ndani yake. Humo basi, kwa sababu ya
Maandalio ya Wayahudi, wakamweka Yesu; maana lile kaburi lilikuwa karibu.”
Isaya 53:8-9 “Kwa
kuonewa na kuhukumiwa aliondolewa; Na maisha yake ni nani atakayeisimulia?
Maana amekatiliwa mbali na nchi ya walio hai; Alipigwa kwa sababu ya makosa ya
watu wangu.Wakamfanyia kaburi pamoja na wabaya; Na pamoja na matajiri katika
kufa kwake; Ingawa hakutenda jeuri, Wala hapakuwa na hila kinywani mwake.”
1Wakorintho 15:3-4 “Kwa maana naliwatolea ninyi hapo mwanzo yale niliyoyapokea mimi
mwenyewe, ya kuwa Kristo alikufa kwa ajili ya dhambi zetu, kama yanenavyo
maandiko; na ya kuwa alizikwa; na ya kuwa alifufuka siku ya tatu, kama
yanenavyo maandiko;”
Mathayo 12:39-40 “Akajibu,
akawaambia, Kizazi kibaya na cha zinaa chatafuta ishara, wala hakitapewa
ishara, ila ishara ya nabii Yona.Kwani kama vile Yona alivyokuwa siku tatu
mchana na usiku katika tumbo la nyangumi, hivyo ndivyo Mwana wa Adamu
atakavyokuwa siku tatu mchana na usiku katika moyo wa nchi.”
Tendo la
kukubali kuzikwa linatufundisha unyenyekevu mkubwa aliokuwa nao Bwana wetu Yesu
Kristo, unyeyekevu huu hatimaye ulimuinua sana Bwana Yesu, kimsingi tunajifunza
hata kuwa njia mojawapo ya juu kabisa ya ukristo ni pamoja na unyenyekevu,
unyenyekevu hutupelekea kuinuliwa juu sana na Bwana.
Wafilipi 2:5-8 “Iweni
na nia iyo hiyo ndani yenu ambayo ilikuwamo pia ndani ya Kristo Yesu; ambaye
yeye mwanzo alikuwa yuna namna ya Mungu, naye hakuona kule kuwa sawa na Mungu
kuwa ni kitu cha kushikamana nacho; bali alijifanya kuwa hana utukufu, akatwaa
namna ya mtumwa, akawa ana mfano wa wanadamu; tena, alipoonekana ana umbo kama
mwanadamu, alijinyenyekeza akawa mtii hata mauti, naam, mauti ya msalaba.”
Mambo yasiyo ya kibiblia katika njia ya Msalaba.
Njia ya msalaba ni fundisho
muhimu sana linalohusiana na tafakari ya kile kilichomkuta Bwana wetu Yesu
Kristo wakati wa mateso yake, kutafakari kuhusu mateso ya Bwana Yesu
hakutufanyi sisi kuwa na huzuni bali kunatufanya kuwa na furaka kwa sababu ndio
njia iliyochaguliwa na Mungu kwa ukombozi wetu, kwa hiyo njia ya msalaba ina
mambo mengi muhimu ya kutufunza kibiblia, hata hivyo kuna mambo yasiyo ya
kibiblia ambayo tunaweza kuyachukulia tahadhari
-
Maandiko hayajaeleza kokote pale kwamba Yesu
aliwahi kuanguka na msalaba, tunaweza kuona kuwa ni kweli Yesu alikuwa dhaifu
kiasi cha kusaidiwa Msalaba wake na Simeoni Mkirene lakini swala la Yesu
kuanguka na msalaba mra ya kwanza na ya pili na ya tatu halina rekodi yoyote
katika maandiko na ingawa inaweza kuwa hivyo katika historia na masimulizi ya
kale lakini hatuwezi kuwa na msimamo thabiti kwa sababu Biblia iko kimya kuhusu
matukio hayo kwa sababu hiyo kituo cha
tatu Yesu kuanguka na msalaba mara ya kwanza
na kituo cha saba Yesu kuanguka na msalaba mara ya pili na kituo cha
tisa cha Yesu kuanguka na msalaba mara ya tatu hakiwezi kujumuishwa katika
fundisho la kibiblia kwa sababu hakuna mwanafunzi wa Yesu aliyeandika hilo wala
waandishi wengine wala mitume hawajawahi kugusia hilo kokote, Penginepo pia
hakuwezi kuwepo na fundisho zuri linalohusiana na kuanguka.
-
Kuhusu swala la Yesu kukutana na mama yake
njiani wakati wa mateso pia linaweza kuwa na utata kwa sababu Biblia iko kimya,
lakini tunao uhakika kuwa Mariamu na ndugu za Yesu zake Yesu Kristo walikuwepo
wakati Yesu anasulubiwa lakini hatujaelezwa kuwa walikutana mahali fulani
njiani isipokuwa kwa masimulizi ya wakristo wa nyakati za kanisa la Kwanza kwa
sababu hiyo tukio hili linalotengeneza kituo cha nne miongoni mwa wakatoliki na Anglican hatukiingizi
katika fundisho la njia ya msalaba, maandiko yanaonyesha ni kama Yesu alimuona
mama yake na wanafunzi wake akiwa tayari ametundikwa juu ya msalaba hata kama
inawezekana mama yake aliongozana na watu waliofuatilia mateso
Yohana 19:26-27
“Basi Yesu alipomwona mama yake, na yule mwanafunzi
aliyempenda amesimama karibu, alimwambia mama yake, Mama, tazama, mwanao. Kisha
akamwambia yule mwanafunzi, Tazama, mama yako. Na tangu saa ile mwanafunzi yule
akamchukua nyumbani kwake.”
-
Kuhusu swala la Yesu kukutana na Mwanamke
aliyeitwa Veronica na kuwa mwanamke
huyu alimfuta jasho lake na picha ya Yesu ikasalia katika kitambaa cha mama
huyu, pia ni swala la kimapokeo na masimulizi tu na hakuna taarifa za kibiblia,
aidha jina Veronica kimsingi sio
jina la asili la Kiyahudi jina hilo ni la kilatini, na katika kigiriki labda
jina Berenice la Ugiriki au
Makedonia lingeweza kutumika, jina Veronika
lina asili ya maneno mawili ya kilatini “Vera
Icon” ambalo tafasiri yake ni true
image kwa hiyo masimulizi kuhusu mwanamke huyu na tukio la picha ya Yesu
kubaki katika kitambaa chake halina uthibitisho wa kimaandiko kwa sababu hiyo
kituo cha sita kinachohusiana na uwepo wa Veronika hakina uhalali wa kimaandiko
kwa hivyo kuanguka wa Yesu mara tatu, kukutana na Mariamu na kukutana na
Veronica kunaingia katika kundi la mambo yasiyo ya kibiblia.
-
Jambo lingine ni kuwa hakuna sababu ya kutumia
picha au sanamu katika kuadhimisha au kujikumbusha kuhusu njia ya msalaba kwani
njia hiyo ipo kule Yerusalem na picha za kila kituo zipo kwa hiyo picha za
vituo zinaweza kutumika katika kufundisha mafundisho yote ya njia ya malaba
kwani siku hizi watu wanaelewa tofauti na miaka ya zamani ambapo watu wengi
walikuwa hawajui kusoma na kuandika, mfano picha niliyoitumia mimi katika
kielelezo hapo juu ni picha ya njia halisi hiyo aliyoitumia Yesu iitwavyo via
dolorosa na njia hiyo ipo hata leo kule Yerusalem nchini Israel
-
Fundisho kuhusu njia ya msalaba sio la
kikatoliki na Anglican pekee linauhusu mwili wa Kristo na hivyo kila Mwalimu wa
neno la Mungu anaweza kulitumia kwa mafundisho sahihi na semina za pasaka
katika kuwatafakarisha watu mateso na kifo cha Bwana Yesu na wakato wowote
tunapotaka kutafakari au kujikumbusha kuhusu aina ya mauti na mateso
aliyokutana nayo Yesu. Kupitia fundisho
hili ni Imani yangu kuwa walimu wa neno la Mungu watapata ufahamu mkubwa zaidi
wa kuyaweka sawa mafundizho haya kwa njia iliyo bora zaidi katika siku za
usoni.
Yohana 8:31-32 “Basi Yesu akawaambia wale
Wayahudi waliomwamini, Ninyi mkikaa katika neno langu, mmekuwa wanafunzi wangu
kweli kweli; tena mtaifahamu kweli, nayo hiyo kweli itawaweka huru.”
Na Rev. Innocent Samuel Kamote.
Mkuu wa wajenzi mwenye hekima.