Ijumaa, 9 Mei 2025

Maana ya kuchovya mguu wako katika Mafuta!


Kumbukumbu 33:24-27 “Na Asheri akamnena, Na abarikiwe Asheri kwa watoto; Na akubaliwe katika nduguze, Na achovye mguu wake katika mafuta. Makomeo yako yatakuwa ya chuma na shaba; Na kadiri ya siku zako ndivyo zitakavyokuwa nguvu zako. Hapana aliyefanana na Mungu, Ee Yeshuruni, Ajaye amepanda juu ya mbingu ili akusaidie. Na juu ya mawingu katika utukufu wake. Mungu wa milele ndiye makazi yako, Na mikono ya milele i chini yako. Na mbele yako amemsukumia mbali adui; Akasema, Angamiza.”




Utangulizi:

Moja ya tahadhari inayotolewa kwa wahubiri wa neno la Mungu ni pamoja na kuhakikisha kuwa tunalitumia neno la Mungu kwa halali, Neno la Mungu linatahadharisha kuwa walimu wa neno la Mungu watapata hukumu iliyokubwa zaidi, kwa sababu hiyo ni muhimu kwa kila mtafasiri wa neno la Mungu kulitafasiri kwa halali neno la kweli ili watu wa Mungu wasipotoshwe na kujikuta wakipotezwa kwa kutokuwa na maarifa ya kuifahamu kweli ya neno la Mungu, na kanuni zake za kulitafasiri! Neno la Mungu likitafasiriwa kwa usahihi linaleta mwelekeo sahihi kwa watu wa Mungu. Tafasiri sahihi na njema kwa neno la Mungu huwajengea watu makuzi sahihi ya kiroho, kuikulia Imani sahihi na kujenga uhusiano imara na Mungu na kujiepusha na matumizi mabaya ya maandiko yatakayopelekea kuzuka kwa Imani potofu au Imani za kizushi na kuwafanya wadamu wasitimize kusudi sahihi la Mungu katika maisha yao!

2Timotheo 2:14-15 “Uwakumbushe mambo hayo, ukiwaonya machoni pa Mungu, wasiwe na mashindano ya maneno, ambayo hayana faida, bali huwaharibu wasikiao. Jitahidi kujionyesha kuwa umekubaliwa na Mungu, mtenda kazi asiye na sababu ya kutahayari, ukitumia kwa halali neno la kweli.”         

Yakobo 3:1-2 “Ndugu zangu, msiwe waalimu wengi, mkijua ya kuwa mtapata hukumu kubwa zaidi. Maana twajikwaa sisi sote pia katika mambo mengi. Mtu asiyejikwaa katika kunena, huyo ni mtu mkamilifu, awezaye kuuzuia na mwili wake wote kama kwa lijamu.”

Kwa msingi huo basi leo nataka tuchukue muda kujifunza kwa kina na mapana na marefu tafasiri ya Maana ya kuchovya mguu wako katika Mafuta! Ili kwamba kila mwanafunzi wa Yesu Kristo aweze kuwa na ufahamu wa kutosha  na uliosahihi kuhusu fundisho linaloendelea mitaani ambapo kumekuwako na watumishi wa Mungu wanaowakanyagisha watu mafuta wakifikiri kuwa kwa kufanya hivyo wanaweza kusababisha mabadiliko ya maisha ya watu kiroho, kiuchumi na kimwili jambo ambalo sio sahihi,  na wakristo wengi sana wasomi kwa wasio wasomi lakini wasio na ujuzi kuhusu neno la Mungu wameshawishika kukanyaga mafuta halisi kwa kutumia tafasiri isiyo halisi ya neno la Mungu, tutajifunza somo hili Maana ya kuchovya mguu wako katika Mafuta! Kwa kuzingatia vipengele vitatu vifuafuatayo:-

 

·         Umuhimu wa kuzingatia kanuni za kutafasiri maandiko.

·         Tafasiri halisi ya Maana ya kuchovya mguu wako katika Mafuta!

·         Jinsi ya kuchovya mguu wako katika Mafuta!

 

Umuhimu wa kuzingatia kanuni za kutafasiri maandiko.

Moja ya changamoto kubwa inayolikumba kanisa la Mungu katika nyakati za leo ni pamoja na kuweko kwa kundi kubwa la mashambulizi ya mafundisho ya uongo ambayo yamekuwa mwiba na usumbufu mkubwa katika kanisa la Mungu kwa miaka mingi, unaweza ukalichukulia swala hili kuwa ni swala la kawaida, lakini ni ukweli usioweza kupingika kuwa Mungu hafurahii watu wanaojitafasiria neno lake kama wapendavyo, Biblia ni kitabu cha Heshima kubwa sana ni neno la Mungu na kwa sababu hiyo haipendezi hata kidogo kila mtu tu akijitafasiria maandiko kama apendavyo kamwe huo sio mpango wa Mungu, Roho Mtakatifu ndiye mwandishi mkuu wa Biblia na bila shaka hangeweza kufurahia watu wajitafasirie neno lake kama watakavyo tu kwa mapenzi yao wenyewe!

2Petro 1:19-21 “Nasi tuna lile neno la unabii lililo imara zaidi, ambalo, mkiliangalia, kama taa ing'aayo mahali penye giza, mwafanya vyema, mpaka kutakapopambazuka, na nyota ya asubuhi kuzuka mioyoni mwenu. Mkijua neno hili kwanza, ya kwamba hakuna unabii katika maandiko upatao kufasiriwa kama apendavyo mtu fulani tu. Maana unabii haukuletwa po pote kwa mapenzi ya mwanadamu; bali wanadamu walinena yaliyotoka kwa Mungu, wakiongozwa na Roho Mtakatifu.”

Mungu anachukizwa sana pale watu wanaposema kile ambacho yeye hajawahi kukisema, nakumbuka niliwahi kuwa na Muhasibu ambaye alikuwa akiandika jina langu katika namna ambayo mimi mwenyewe sikuwahi kuitwa hivyo, Mimi naitwa INNOCENT SAMUEL KAMOTE Lakini muhasibu wangu yeye alikuwa akiandika jina langu INNOCENT SAMWELI KAMMTTE  nililalamika mara kadhaa kuwa Jina langu unavyoliandika sivyo linavyopaswa kuwa lakini hata hivyo hakujali na aliendelea kuliandika jina langu katika namna hiyo hiyo aliyokuwa anataka yeye, mimi sio mwepesi wa hasira lakini hata hivyo nilianza kumtafasiri vibaya muhasibu huyu aliyekazania kuliandika jina langu katika namna anayoitaka yeye hata pamoja na kumuonyesha vitambulisho vyangu vilivyo na jina sahihi,yeye aliendelea kuliandika jina langu katika namna hiyo hiyo aliyoikubali yeye na hakukubali masahihisho, kimsingi nilianza kumchukia na kumuona kama mtu mwenye nia ovu kwa maslahi yangu kwani nafahamu kuwa dosari katika jina la mtu hasa ikiachwa hivyo katika documents muhimu linaweza kuwa na athari kubwa sana baadaye utakapohitajika kuthibitisha uhalisi wa mtu anayetajwa hapo na ukweli kuhusu jina lako, sio hivyo tu nilianza kuingia shaka kuhusu elimu yake na aidha akili zake, kwa hiyo sikuwa namfurahia tena, na alipoteza umuhimu wake kwangu, katika maumivu kama hayo ni ukweli ulio wazi kuwa Mungu anachukizwa sana watu wanapomnukuu vibaya tofauti na maana aliyokuwa anaikusudia kwenye neno lake, Mungu anataka neno lake lisemwe kwa uaminifu na kama mtu hataki aache, Mungu hataki kusingiziwa kwamba amesema kitu ambacho yeye hakukisema, iwe ni kwa misingi ya ndoto wala mafunuo anataka atendewe haki katika tafasiri halali kwa neno lake ili watu wake wasipotoshwe ona  

Yeremia 23:25-32.“Nimesikia waliyoyasema manabii wanaotabiri uongo kwa jina langu, wakisema, Nimeota ndoto; nimeota ndoto. Je! Mambo hayo yatakuwa katika mioyo ya manabii wanaotabiri uongo hata lini, manabii hao wenye udanganyifu katika mioyo yao wenyewe? Wanaodhania ya kuwa watawasahaulisha watu wangu jina langu kwa ndoto zao, wanazomhadithia kila mtu jirani yake, kama vile baba zao walivyolisahau jina langu, kwa ajili ya Baali. Nabii aliye na ndoto, na aseme ndoto yake; na yeye aliye na neno langu, na aseme neno langu kwa uaminifu. Makapi ni kitu gani kuliko ngano? Asema Bwana. Je! Neno langu si kama moto? Asema Bwana; na kama nyundo ivunjayo mawe vipande vipande? Basi kwa sababu hiyo mimi ni juu ya manabii hao, asema Bwana, wanaompokonya kila mtu jirani yake maneno yangu. Tazama, mimi ni juu ya manabii, asema Bwana, wanaotumia ndimi zao na kusema, Yeye asema, Tazama, mimi ni juu ya hao wanaotabiri ndoto za uongo, asema Bwana, na kuzisema, na kuwakosesha watu wangu kwa uongo wao, na kwa majivuno yao ya upuzi, lakini mimi sikuwatuma, wala sikuwapa amri; wala hawatawafaidia watu hawa hata kidogo, asema Bwana.”

Kwa msingi huo hatuwezi kulichezea neno la Mungu na kuruhusu litafasiriwe vyo vyote vile kama watu wanavyotaka, ziko kanuni zinazoongoza tafasiri halali kwa neno la Mungu, katika karne ya 20 wa NAZI wa Ujerumani waliona kuwa kuna uhalali wa kuwaangamiza wayahudi na kuwaua kwa sababu walitumia andiko la Mathayo 27:24-25 vibaya:-

Mathayo 27:24-25 “Basi Pilato alipoona ya kuwa hafai lo lote, bali ghasia inazidi tu, akatwaa maji, akanawa mikono yake mbele ya mkutano, akasema, Mimi sina hatia katika damu ya mtu huyu mwenye haki; yaangalieni haya ninyi wenyewe. Watu wote wakajibu wakasema, Damu yake na iwe juu yetu, na juu ya watoto wetu.”

Tafasiri yoyote mbaya ya kimaandiko inaweza kuleta matokeo mabaya yasiyokusudiwa katika jamii wala yasiyo sawa na mapenzi ya Mungu, kama kila mwanadamu anapenda kunukuliwa vizuri basi Mungu anapenda kunukuliwa vizuri zaidi. Katika mtindo kama huo Madaktari wanafahamu athari zinazoweza kutokea endapo mtu atazidishiwa dozi au kupewa dozi chini ya kiwango wakati wa kumtibu mgonjwa kufanya hivyo kunaweza kusababisha madhara ya usugu wa dawa au kumuumiza mgonjwa, kadhalika neno la Mungu linaagizwa litafasiriwe kwa halali na sio kwa maslahi ya mtu na mafunuo yake au ndoto zake, sio kila mtu ana sifa ya kuwa mtafasiri wa maandiko, na sio kila mtu anaweza kuelewa neno la Mungu bila msaada wa mtu mwingine, na wako watu Mungu amewaweka ili waifanye kazi hiyo ya kuelewesha wengine neno la Mungu ili malengo yake yaweze kufikiwa. Kwa hiyo usipuguze wala kuongeza neno.

Matendo 8:29-35 “Roho akamwambia Filipo, Sogea karibu na gari hili, ukashikamane nalo. Basi Filipo akaenda mbio, akamsikia anasoma chuo cha nabii Isaya; akanena, Je! Yamekuelea haya unayosoma? Akasema, Nitawezaje kuelewa, mtu asiponiongoza? Akamsihi Filipo apande na kuketi pamoja naye. Na fungu la Maandiko alilokuwa akilisoma ni hili, Aliongozwa kwenda machinjoni kama kondoo, Na kama vile mwana-kondoo alivyo kimya mbele yake amkataye manyoya, Vivyo hivyo yeye naye hafunui kinywa chake. Katika kujidhili kwake hukumu yake iliondolewa. Ni nani atakayeeleza kizazi chake? Kwa maana uzima wake umeondolewa katika nchi. Yule towashi akamjibu Filipo, akasema, Nakuomba, nabii huyu; asema maneno haya kwa habari ya nani; ni habari zake mwenyewe au za mtu mwingine? Filipo akafunua kinywa chake, naye, akianza kwa andiko lilo hilo, akamhubiri habari njema za Yesu.”

Kumbukumbu 4:1-2 “Na sasa, Ee Israeli, zisikilizeni amri na hukumu niwafundishazo, ili mzitende; mpate kuishi na kuingia na kuimiliki nchi awapayo Bwana, Mungu wa baba zenu. Msiliongeze neno niwaamurulo wala msilipunguze, mpate kuzishika amri za Bwana, Mungu wenu, niwaamuruzo.”  

Wakati mwingine ili mtu aelewe neno la Mungu anahitaji kuongozwa na wale ambao Mungu ameweka neema maaalumu ya kuwa wakufunzi wa neno la Mungu, kumbuka sisi ni wanafunzi wa Yesu na tunapaswa kujifunza kila iitwapo leo, tukiwa na moyo wa unyenyekevu na kuweka kiburi pembeni Mungu anaweza kutufundisha njia yake kwa usahihi zaidi.

Matendo 18:24-28 “Basi Myahudi mmoja, jina lake Apolo, mzalia wa Iskanderia, mtu wa elimu, akafika Efeso; naye alikuwa hodari katika maandiko. Mtu huyo alikuwa amefundishwa njia ya Bwana; na kwa kuwa roho yake ilikuwa ikimwaka, alianza kunena na kufundisha kwa usahihi habari za Yesu; naye alijua ubatizo wa Yohana tu. Akaanza kunena kwa ujasiri katika sinagogi; hata Prisila na Akila walipomsikia wakamchukua kwao, wakamweleza njia ya Bwana kwa usahihi zaidi. Na alipotaka kuvuka bahari aende mpaka Akaya, ndugu wakamhimiza, wakawaandikia wale wanafunzi wamkaribishe, naye alipofika akawasaidia sana wale waliokwisha kuamini kwa neema ya Mungu. Kwa maana aliwashinda Wayahudi kabisa kabisa mbele ya watu wote, akionyesha kwa maneno ya maandiko ya kuwa Yesu ni Kristo.”

Kwa hiyo wakristo tunakubaliana kuwa mtu anaweza kusoma neno la Mungu na asielewe bila uongozi, na pia mtu anaweza kuwa muhubiri lakini asihubiri kwa usahihi kama hajafundishwa vizuri na tunakubaliana kuwa maandiko yana kanuni zake katika kulitafasiri neno la Mungu ili yamkini liweze kutendewa haki katika tafasiri zake na kutumika kwa halali jambo ambalo linamfurahisha Mungu pia, tusiruhusu kitabu chetu kitakatifu kikatafasiriwa kama apendavyo mtu tu kwa mapenzi yake mwenyewe bali sawa na kanuni za kiungwana na kiungu sawasawa na mapenzi ya Mungu.  Kwa sababu hiyo ziko kanuni rahisi kumi zinazoongoza watu wa Mungu katika kutafasiri maandiko na ingawa hatutakuwa na muda wa kuzifafanua sana kwa undani lakini zinaweza kukupa mwanga wa namna ya kusimamia tafasiri njema na sahihi ya maandiko:-

1.       Lazima mtafasiri wa maandiko awe na Kanuni ya utii (The Principle of Obidience) – hii ni kanuni ya dhamiri njema, mtafasiri wa maandiko lazima ahakikishe kuwa ana moyo wenye dhamiri njema na kuwa mpango wake ni kumtii Mungu,  na kumtumikia kwa dhati, Kila mwanadamu mwenye utii kwa mapenzi ya Mungu na mwenye dhamiri njema Mungu humsaidia muelekeo wake wa moyo kuwa na uweza wa kuifahamu kweli na hata akikosea kwa sababu alikuwa na dhamiri safi rehema za Mungu huwa juu yake, kwa sababu Mungu akiiangalia nia yake anaona kuwa ni mtu mwenye mapenzi mema, Mungu hawezi kuwa radhi na mtu anayekusudia mabaya wakati wanapotaka kulitafasiri neno la Mungu, hata hivyo utii na dhamiri njema havitoshi peke yake vinaweza kutosha kwa Mungu anayechunguza mioyo lakini havitoshi kwetu kwa sababu tutajuaje kuwa ulikuwa na dhamiri njema iwapo fundisho lako limesababisha upotofu miongoni mwa jamii? Kwa hiyo kanuni ya utii inaweza kukuweka salama kwa Mungu tu lakini haikuachi salama kwetu sisi tuliosomea utaalamu wa kutafasiri maandiko haikuweki salama  kwa sababu neno la Mungu linasema Moyo una ugonjwa wa kufisha

 

Yeremia 17:9-10 “Moyo huwa mdanganyifu kuliko vitu vyote, una ugonjwa wa kufisha; nani awezaye kuujua? Mimi, Bwana, nauchunguza moyo, navijaribu viuno, hata kumpa kila mtu kiasi cha njia zake, kiasi cha matunda ya matendo yake.”

 

Kwa hiyo wakristo wana haki ya kuyachunguza maandiko ili waone kama kile kinachohubiriwa na kusemwa ni kitu sahihi ama hapana! Hapo haijalishi anayehubiri ni nani na ana mamlaka gani lazima tumpime katika maandiko ili tuone yale anayotupa ndio mapenzi ya Mungu hasa, kinyume cha hapo tutakuwa tumekosa uungwana, watu wa Beroya hawakuwahi kujali kuwa Paulo ana mafunuo gani laiki waliyachunguza maandiko wajionee wenyewe kama mambio ndivyo yalivyo, usiamini katika moyo wa mtu.

 

Matendo 17:10-11 “Mara hao ndugu wakawapeleka Paulo na Sila usiku hata Beroya. Nao walipofika huko wakaingia katika sinagogi la Wayahudi. Watu hawa walikuwa waungwana kuliko wale wa Thesalonike, kwa kuwa walilipokea lile neno kwa uelekevu wa moyo, wakayachunguza maandiko kila siku, waone kwamba mambo hayo ndivyo yalivyo.”                                

 

2.       Lazima mtafasiri wa neno la Mungu awe na uelewa kuhusu Kanuni ya uvuvio (The Principle of Inspiration) – hii ni kanuni inayomsaidia kujua kuwa kila andiko lenye pumzi ya Mungu linafaa kwa mafundisho, kwa hiyo tunaweza kuwafundisha watu neno la Mungu kwa njia nyepesi tu na kama tuna mapenzi mema tutawaelekeza watu wake katika mapenzi yake kwa kutumia neno la Mungu  kwa sababu lijna pumzi ya Mungu

 

2Timotheo 3:16-17 “Kila andiko, lenye pumzi ya Mungu, lafaa kwa mafundisho, na kwa kuwaonya watu makosa yao, na kwa kuwaongoza, na kwa kuwaadibisha katika haki; ili mtu wa Mungu awe kamili, amekamilishwa apate kutenda kila tendo jema.”

 

Kanuni hii haitoshi ingawa kuna ukweli kuwa kila andiko lenye pumzi ya Mungu linafaa kwa mafundisho, lakini maandiko yanahitaji ulinganifu wa kina na ndio maana shetani pia alipoona Yesu anatumia maandiko naye akayatumia lakini si kwa nia nzuri kwa hiyo uko ulinganifu maalumu unaohitajika katika kujua andiko fulani linatumikaje na kwa wakati gani

 

Mathayo 4:5-7 “Kisha Ibilisi akamchukua mpaka mji mtakatifu, akamweka juu ya kinara cha hekalu,akamwambia, Ukiwa ndiwe Mwana wa Mungu jitupe chini; kwa maana imeandikwa, Atakuagizia malaika zake; Na mikononi mwao watakuchukua; Usije ukajikwaa mguu wako katika jiwe.Yesu akamwambia, Tena imeandikwa, Usimjaribu Bwana Mungu wako.”

 

3.       Lazima mtafasiri wa Maandiko pia awe na uelewa kuhusu Historia  na mazingira ya andiko (Mukhtadha) (Principle of Historical Context) – hapa mtafasiri anapaswa kujifunza historia ya Mazingira yanayozunguka andiko husika mfano historia ya mji wa Korintho, lugha zao, wakati ambapo neno linaandikwa, tamaduni zao, jamii yao na kadhalika , sio hivyo tu lazima mtafasiri aelewe kitu kilichoandikwa au kusemwa pamoja na maneno yote na maana zake zinazozunguka andiko husika, mazingira yaliyopelekea kutamkwa kwa maneno hayo huo ndio muktadha,  tafasiri hii inakulazima uwe msomi ili uweze kujua lugha za wakati ule, tamaduni za wakati ule, jamii ya wakati ule, na jinsi tunavyoweza kulitumia andiko hilo kwa sasa, lazima uwe na kamusi au ujuzi wa lugha za asili kwaajili ya kupata maana sahihi iliyokusudiwa na mwandishi

 

4.       Lazima mtafasiri aweze pia kufanya uchunguzi wa kimaandiko yaani “ajue yaliyomo” lugha zilizotumika misamiati iliyotumika na maana ya maneno yanayotumika,- (Principle of content) mfano lugha hiyo ni ya namna gani, maneno yake yana maana gani anaweza pia kwenda kwenye lugha za asili kama kiebrania, kiaramu, kiyunani na kilatini ili kupata matumizi ya lugha halisi ya wakati ule na jinsi inavyoweza kutumika katika wakati wa sasa, lazima uchunguze kuwa lugha hiyo ni ya kimafumbo au ya kawaida inaweza kutafasiriwa kama kawaida au inaweza kuwa fumbo? Na madhara gani yanaweza kujitokeza, ni lazima uwe na ujuzi kuhusu kitabu unachotaka kukitafasiri kama ni cha kinabii, kimashairi, kihistoria, sheria, nyaraka, au injili na msemaji alikuwa akizungumza na jamii ya watu wa aina gani, kwa wakati gani, kwa tamaduni gani na inaweza kutuhusu vipi sisi katika nyakati za leo, Lazima uwe na ujuzi kuhusu stori nzima, somo zima, wazo zima, mpangilio mzima, mtiririko mzima na nia nzima ya mwandishi na yote yaliyomo kabla na baada ya andiko husika.    

 

5.       Lazima mtafasiri pia wakati mwingine achukue “lugha rahisi” tu iliyoko kama ilivyo bila kutumia utaalamu kutafasiri japo kwa kufanya hivyo mtafasiri anaweza anaweza kujikuta yuko katika wakati mgumu kwa sababu sio kila lugha iliyotumika inaweza kuwa na maana hizo, ziko lugha za mficho, za kimashairi, za kimafumbo, za kinabii, na kadhalika  (The principle of simplicity) ziko Lugha au maana katika biblia ambazo hazihitaji tafasiri yoyote kwa hiyo ukizichukulia kama zilivyo bila kutafasiri unakuwa salama, huitaji kuyafanya mambo kuwa magumu, lakini yako maandiko ambayo yanahitaji kutokuchukuliwa kirahisi au kama yalivyo mfano:-

 

-          Jicho lako likikukosesha ling’oe – Mathayo 18:8-9 “Basi mkono wako au mguu wako ukikukosesha, ukate ukautupe mbali nawe; ni afadhali kuingia katika uzima hali umepungukiwa na mkono au mguu, kuliko kuwa na mikono miwili au miguu miwili, na kutupwa katika moto wa milele. Na jicho lako likikukosesha, ling'oe, ukalitupe mbali nawe; ni afadhali kuingia katika uzima una chongo, kuliko kuwa na macho mawili, na kutupwa katika jehanum ya moto.”

 

-          Je unaweza kulichukua andiko hilo hapo juu na kulitafasiri kama lilivyo? Je andiko hilo ni la kawaida au ni la kimafumbo? Sasa ukichukulia kila kitu kama kilivyoandikwa hutaweza kupata tafasiri sahihi ya andiko hilo hali kadhalika   neno na “Na achovye mguu wake katika mafuta”.  Haliwezi kuchukuliwa katika maana yake nyepesi au rahisi kama ilivyo hiyo ilikuwa lugha inayohitaji ufafanuzi, ukiichukulia kama ilivyo wajinga watakanyaga mafuta

 

6.       Lazima mtafasiri pia ajifunze kufanya ulinganifu wa kimaandiko (The Principle of Harmonisation) yaani ili uweze kufanya fundisho kutoka katika andiko basi andiko hilo liwe na mashahidi wawili au watatu, ni lazima ufanye ulinganifu wa fundisho unalotaka kulitengeneza kutoka katika ushahidi wa maandiko mengine (Combination of scriptures references) Biblia imekaa katika mfumo unaotegemeana sana kwa sababu hiyo huwezi kuchomoa uzi mmoja wa nguo kisha ukadai kuwa hii ni nguo, nguo kamili ni mfungamano wa nyuzi nyingi zinazoifanya nguo kuwa nguo kwa hiyo mzani wako wa ulinganifu wa maandiko utakusaidia kuwa na fundisho sahihi  na hupaswi kusingizia kila kitu kuwa kimetokana na ufunuo wa kiungu

 

Isaya 28:9-10 “Atamfundisha nani maarifa? Atamfahamisha nani habari hii? Je! Ni wale walioachishwa maziwa, walioondolewa matitini? Kwa maana ni amri juu ya amri, amri juu ya amri; kanuni juu ya kanuni, kanuni juu ya kanuni; huku kidogo na huku kidogo.”

 

2Wakorintho 13:1 “Hii ndiyo mara ya tatu ya mimi kuja kwenu. Kwa vinywa vya mashahidi wawili au watatu kila neno litathibitishwa.”

Kumbukumbu 19:15 “Shahidi mmoja asimwinukie mtu awaye yote kumshuhudia kwa uovu wo wote, wala kwa dhambi yo yote, katika makosa akosayo yo yote; jambo na lithibitishwe kwa vinywa vya mashahidi wawili, au watatu.”

 

7.       Lazima uwe na utaalamu wa kutosha kuhusu ulinganifu wa maswala ya agano la kale na agano jipya, (The Principles of Covenants) uwe na ufahamu kuwa ni mafundisho gani hasa yaliweza kuwahusu watu wa agano la kale na kwa wakati gani na  wale wa agano jipya, sheria zipi zilifaa kwa wakati ule na zipi hazifai kwa wakati huu na ni yapi mapenzi ya Mungu hasa kwa wakati wetu

 

Matendo 17:30-31 “Basi, zamani zile za ujinga Mungu alijifanya kama hazioni; bali sasa anawaagiza watu wote wa kila mahali watubu. Kwa maana ameweka siku atakayowahukumu walimwengu kwa haki, kwa mtu yule aliyemchagua; naye amewapa watu wote uthabiti wa mambo haya kwa kumfufua katika wafu.”            

8.       Lazima uwe na utaalamu wa kujua ni mambo gani hasa yametimizwa katika ufalme wa Mungu na yale ambayo bado hayajatimizwa, Kanuni za ufalme wa Mungu (The Principle of the Kingdom) yako maswala kadhaa katika maswala yahusuyo ufalme wa Mungu ambayo yametimizwa na ambayo bado, kwa hiyo mtaalamu wa neno la Mungu anapaswa kuwa na uelewa huo.

 

9.       Lazima mtaalamu wa kutafasiri maandiko awe na ujuzi wa kina na wa kutosha kuhusu kutafasiri mifano ya ufalme wa Mungu (The Principle of Parables) mifano ya ufalme wa Mungu ina kanuni zake na taratibu zake na inabeba maana moja kubwa iliyokusudiwa na hivyo huwezi kuitafasiri kama unayefanya uchambuzi

 

10.   Lazima mtaalamu wa neno la Mungu awe na ujuzi wa kina kuhusu maswala ya unabii, (The Principle of Prophecy) ajue kuwa ni unabii gani umeshatimizwa na upi ambao bado haujatimizwa ili kujua ni namna gani anaweza kuyaweka sawa maswala ya kinabii asikosee au kwenda kinyume na zile kanuni za kimungu na ile tabia za unabii kujirudia kwa mfumo za zaidi ya mara moja.

Hizo hapo juu ni kanuni kumi muhimu zinazomuongoza mtafasiri wa maandiko kulitafasiri neno la Mungu kwa halali, sina muda mkubwa sana wa kuzielezea hapa kwa  kina lakini zinapatikana katika somo maalumu la kitheolojia linalohusika na namna na jinsi ya kuyatafasiri maandiko kwa halali somo hilo kitaalamu katika vyo vya Biblia linaitwa the “Principles of Biblical interpretations”  au “Hermaneutics”  the sientifical study of the methodological principles of interpretation of the Bible kwa Kiswahili hizo ni sayansi za ufundi na njia au kanuni za kimatumizi katiika kutafasiri maandiko au Biblia,  kwa hiyo watumishi wa Mungu wanaokuwa wameitwa na Mungu na kukubali kwenda katika vyuo vya Biblia hufundishwa masomo hayo kwa kusudi au lengo la kupunguza changamoto za kutafasiri vibaya maandiko, Uchungaji hausomewi, lakini yeye aliyeitwa anapaswa kuupeleka witio wake katika vyuo vya Biblia kwa walimu kwa kusudi la kuunoa wito wako ili uyatumie maandiko kwa halali au kwa mujibu wa kanuni kwa hiyo mtu anyezingatia kanuni hizo sasa anakuwa katika nafasi nzuri sasa ya kulitendea haki neno la Mungu kwa kuitafasiri Biblia katika njia iliyo njema, hairuhusiwi kutengeneza maana yako ya kibiblia kisha ukalisingizia andiko, to guide in “EISOGESIS”  na badala yake unatakiwa kutafuta maana iliyokusudiwa na mwandishi na kuiweka wazi kwa jamii unayoifundisha to guide out “EXEGESIS” wale wanaotafuta maana iliyokusudiwa na mwandishi kwa wakati wake kisha wakatafuta namna ya kuitumia maana ile kwa wakati huu wa sasa wako salama kabisa katika kulitafasiri neno la Mungu kwa usahihi, kwa hiyo tafasiri ya maandiko ni sayansi na sio swala la kukurupuka tu!

Sasa baada ya kujenga msingi huo wa ufahamu nataka twende moja kwa moja tukaaangalie sasa tafasiri ya kimaandiko kuhusu “Tafasiri halisi ya Maana ya kuchovya mguu wako katika Mafuta!” je andiko hili lilimaanisha nini kwa wakati wa Musa na linaweza kutafasiriwa vipi na linaweza kutendewa kazi katika mazingira yapi? Katika wakati wetu wa leo?

Tafasiri halisi ya Maana ya kuchovya mguu wako katika Mafuta!

Ni muhimu kwanza kufahamu kuwa andiko la msingi linatoka katika Kumbukumbu 33:24-25 “Na Asheri akamnena, Na abarikiwe Asheri kwa watoto; Na akubaliwe katika nduguze, Na achovye mguu wake katika mafuta. Makomeo yako yatakuwa ya chuma na shaba; Na kadiri ya siku zako ndivyo zitakavyokuwa nguvu zako.”

Andiko hili kwa asili linatokana na lugha ya kiebrania kwa sababu ndio lugha ya asili iliyotumika kuandikia agano la kale tofauti na agano jipya ambalo kimsingi liliandikwa kwa lugha ya kiyunani sasa basi katika lugha ya kiebrania andiko hilo linasomeka namna hii:-

Âshr âmar âshr bârak bn râtsâh âch ţâbal regel shemen “24 âshr âmar âshr bârak bn râtsâh âch ţâbal regel shemen” kwa kiingereza ingetakiwa kusomeka Of Asher he said May Asher be most blessed of sons, may he be favorite among his brothers and bathe his feet in oil

KJV inasomeka hivi “And Asher he said, Let Asher be blessed with children; let him be acceptable to brethren, and let him dip his foot in oil”

SUV inasomeka hiviNa Asheri akamnena, Na abarikiwe Asheri kwa watoto; Na akubaliwe katika nduguze, Na achovye mguu wake katika mafuta.

Kwa asili andiko hili limetokana na Musa nabii ambaye alikuwa akitamka Baraka za aina mbalimbali kwa makabila 12 ya Israel sawa tu na jinsi Yakobo baba yao alivyowatabiria watoto wake kuhusu maswala yatakayowapata siku za mwisho kwa hiyo haya yalikuwa ni maneno ya kinabii  kutoka kwa Musa akiongezea yale yaliyotoka kwa Yakobo ona

Mwanzo 49:1-2 “Yakobo akawaita wanawe, akasema, Kusanyikeni, ili niwaambie yatakayowapata siku za mwisho. Kusanyikeni, msikie, enyi wana wa Yakobo, Msikilizeni Israeli, baba yenu.”

Mwanzo 49:20 “Asheri, chakula chake kitakuwa kinono, Naye atatoa tunu za kifalme.” Kimsingi Musa alikuwa akijazilizia Baraka zilizokuwa zimetamkwa na Baba yao Israel kwa kabisa zote 12 za wana wa Israel lakini linapokuja swala la kabila la Asheri inaonekana wazi kuwa Musa pamoja na Yakobo walikuwa wanalizungumzia kabila hili kama kabila ambalo Bwana angelibariki sana  kwa hiyo maneno “Thy feet in the oil or and let him dip his foot in Oil” au kwa KiswahiliNa achovye mguu wake katika mafutayana maana ya kinabii inayoashiria kuwa kabila la Asheri katika Israel ni kabila ambayo imetamkiwa kutembea katika utajiri mkubwa sana kwa chakula na tunu au madini  hiyo lugha inayotumika hapo ni lugha ya kinabii au pia inaweza kuitwa (figurative language) au figurative expression, yaani lugha ya mficho au lugha ya kimafumbo inayoashiria kuwa Asheri litakuwa ni kabila litakalokanyaga mafanikio makubwa sana, Asheri watakuwa una utajiri mkubwa wa mafuta ya mzeituni.

Nyakati za agano la kale mtu aliyekuwa anamiliki mafuta hasa yaliyotokana na mzeituni, alikuwa ni mtu ambaye anaweza kutengeneza fedha nyingi sana na kuwa vizuri kiuchumi, kwa nyakati zile, kwa hiyo lugha kubwa ya mafanikio na utajiri pia ililinganishwa na wingi wa mafuta ya mizeituni ambao mtu aliweza kuwa nao kama mtu angekuwa na mafuta ya kutosha angeweza kuyamudu maisha yake na kuondokana kabisa na madeni au kupoteza mali na rasilimali alizokuwa nazo, kuchovya mguu katika mafuta kulimaanisha ni kuwa juu ya Baraka zilizopitiliza, kabila la Asheri wanabarikiwa kuwa kabila lenye mafanikio na utajiri unaomwagika, pia mbaraka huu uliashiria kuwa mipaka ya kabila la Asheri itakuwa ni mipaka inayozingirwa na utajiri wa ardhi yenye rutuba na yenye kustawi mizeituni kwa wingi jambo ambalo litawapa utajiri wa mafuta. Kwa hiyo kuchovya mguu wake katika mafuta kunamaanisha kutembea katika mafanikio na maisha ya starehe, mafuta yalikuwa ni ishaya ya mafanikio makubwa nyakati za zamani kwa ichi za mashariki ya kati, ukibarikiwa kuwa uchovye mguu wako katika mafuta maana yake Mungu akufanikishe kwa njia rahisi na isiyo ya taabu.

2Wafalme 4:1-7 “Basi, mwanamke mmoja miongoni mwa wake za wana wa manabii alimlilia Elisha, akasema, Mtumishi wako mume wangu amekufa; nawe unajua ya kuwa mtumishi wako alikuwa mcha Bwana; na aliyemwia amekuja ili ajitwalie wana wangu wawili kuwa watumwa. Elisha akamwambia, Nikufanyie nini? Niambie; una kitu gani nyumbani? Akasema, Mimi mjakazi wako sina kitu nyumbani, ila chupa ya mafuta. Akasema, Nenda, ukatake vyombo huko nje kwa jirani zako wote, vyombo vitupu; wala usitake vichache. Kisha uingie ndani, ukajifungie mlango wewe na wanao, ukavimiminie mafuta vyombo vile vyote; navyo vilivyojaa ukavitenge. Basi akamwacha, akajifungia mlango yeye na wanawe; hao wakamletea vile vyombo, na yeye akamimina.Ikawa, vilipokwisha kujaa vile vyombo, akamwambia mwanawe, Niletee tena chombo. Akamwambia, Hakuna tena chombo. Mafuta yakakoma.Ndipo akaja akamwambia yule mtu wa Mungu. Naye akasema, Enenda ukayauze mafuta haya, uilipe deni yako; nayo yaliyosalia uyatumie wewe na watoto wako.”

Mtu alipokuwa amebarikiwa sana nyakati za agano la kale mafanikio yalionekana ni kama kukanyaga siagi au kumiminiwa mito ya mafuta, wakati huo ulikuwa unaitwa wakati wa ustawi mkubwa sana mfano Ayubu alipokuwa amebarikiwa sana kabla ya mapito yake alizikumbuka nyakati zake za Baraka kubwa na kuzitaja kama nyakati za kukanyaga siagi au kuoshwa hatua zako kwa siagi ona

Ayubu 29:4-6 “Kama nilivyokuwa katika siku zangu za kukomaa, Hapo siri ya Mungu ilipokuwa hemani mwangu; Wakati Mwenyezi alipokuwa akali pamoja nami, Nao watoto wangu walipokuwa wakinizunguka; Wakati hatua zangu zilipokuwa zikioshwa kwa siagi, Nalo jabali liliponimiminia mito ya mafuta!

Kwa hiyo katika andiko la msingi ni muhimu kila mwanafunzi wa maandiko akawa na uelewa kuwa hakuna mahali maaandiko yameagiza au kutoa amri au agizo la kukanyaga mafuta, andiko hili ni sehemu kamili ya maneno ya Baraka ya Musa kwa kabila kadhaa za Israel kabla ya kufa kwake, Musa alikuwa akifanya hivyo kama kiongozi wa kiroho kama ilivyokuwa kwa Israel au Yakobo ambaye ilipofika saa yake ya mwisho pia aliwaita watoto wake na kuwatamkia Baraka  kwa hiyo maneno  naNa achovye mguu wake katika mafuta yana uhusiano na Baraka ya moja kwa moja kwa kabila la Asheri  na ni lugha ya kinabii inayohusiana na mafanikio yao utajiri mkubwa ambao Mungu amewapa Kabila la Asheri, kabila hili lilibarikiwa sana kimwili, na kiroho na kwa maelezo ya marabi wa kiyahudi ni kuwa kabila hili pia lilikuwa na wanawake wazuri na waliokuwa na adabu na wala hawana maringo, kabila hili lilibarikiwa kwa utajiri, mafanikio na ongezeko kubwa lakini pia walibarikiwa kama watu ambao hawapigiki kirahisi vitani  na watakuwa na ulinzi wa uhakika Makomeo yako yatakuwa ya chuma na shaba  Asheri litakuwa ni kabila la watu wenye mafanikio makubwa sana na wingi wa mafuta unaashiria utajiri mkubwa sana wa Ardhi yenye kuzalisha mizeituni kwa wingi bna ambay ingewabeba kiuchumi.

Mafuta ya mzeituni nyakati za Biblia ilikuwa ni bidhaa adimu na ya thamani sana, mafuta yalitumika kwa kupikia, kuwashia taa, kutibu, kujipaka na kwa sababu mbali mbali kwa hiyo kabila hili kuwabarikiwa kiasi cha kukanyaga mafuta kulimaanisha wingi wa utajiri wa bidhaa hii adimu waliyokuwa nayo, kukanyaga mafuta au zabibu pia kulikuwa na maana ya kuendesha mtambo wa kukamulia Mafuta au zabibu kwaajili ya mvinyo, Mashine ya kutengenezea Zabibu au Mafuta ya mzeituni ilitengenezwa kwa mawe makubwa mawili ambapo jiwe moja kubwa lilikaa chini na jiwe moya lilikuwa juu na lile la juu lingesukumwa ili kusaga zaituni zilizovunwa na kuoshwa vizuri kisha zilikamuliwa katika mashinde (Shinikizo) na hivyo kuendesha mashine ya kukamua mafuta au Zabibu kwaajli ya juisi ya zabibu pia kuliitwa kukanyaka shinikizo

Isaya 63:1-2. “Ni nani huyu atokaye Edomu, Mwenye mavazi ya kutiwa damu kutoka Bosra? Huyu aliye na nguo za fahari, Anayekwenda katika ukuu wa uweza wake? Kwani mavazi yako kuwa mekundu, Na nguo zako kama za mtu akanyagaye zabibu? Nalikanyaga shinikizoni peke yangu; Wala katika watu hakuwapo mtu pamoja nami; Naam, naliwakanyaga kwa hasira yangu, Naliwaponda kwa ghadhabu yangu; Na mavazi yangu yametiwa madoa kwa damu yao, Nami nimezichafua nguo zangu zote.”          

Unaona kukanyaga Zabibu hapo maana yake ni kusaga zabibu kwaajili ya kupata juisi ya zabibu, na kukanyaga mafuta ya zeituni ni kukanyaga shinikio (Mashine za kizamani) za kukamulia mafuta ua mizabizu, kwa hiyi utaweza kuona kama Mungu alikuwa anamaaisha kuchovya mguu katika mafuta ni tukio halisi basi kukanyaka Zabibu nalo lingekuwa ni tukio halisi unaelewa?

 

Kwa hiyo Kabila la Asheri linatamkiwa na Musa kuwa kabila lenye wingi wa mafanikio na utajijiri wa mafuta ya zeituni na watu wasiopigika kirahisi, kabila la Asehri walikuwa na sifa njema sana nyakati za biblia kimwili na kiroho maana walitabiriwa kukubalika pia na kupata kibali kwa ndugu zao wakati Yesu alipokuwa anazaliwa mwanamke mmoja mcha Mungu aliyekuwa wa kiroho sana mwenye umri mkubwa sana na tabia njema na uvumilivu alijitokeza pia kutoa unabii kumuhusu Yesu Kristo mwanamke huyu maarufu alitokea kabila la Asheri ona

Luka 2:36-38 “Palikuwa na nabii mke, jina lake Ana, binti Fanueli, wa kabila ya Asheri, na umri wake ulikuwa miaka mingi, alikuwa amekaa na mume miaka saba baada ya uanawali wake. Naye ni mjane wa miaka themanini na minne; haondoki katika hekalu, ila huabudu usiku na mchana kwa kufunga na kuomba. Huyu alitokea saa ile ile akamshukuru Mungu, na wote waliokuwa wakiutarajia ukombozi katika Yerusalemu akawatolea habari zake.”

Kwa sababu hiyo ni muhimu wakristo wakawa na uelewa kuwa hakuna agizo la kibiblia la aina yoyote lile linaloamuru wanadamu wakanyage mafuta, hii ilikuwa ni lugha ya kinabii ya kumtakia mtu mafanikio hata kama utakuwa ulikanyaga mafuta mahali na ukaona mafanikio fulani kumbuka tu kuwa Mungu aliweza kukuhurumia tena alikuhurumia kwa sababu ya ujinga wako na kwa kufilisika kwako kimawazo na kwa tafasiri mbovu za kibiblia, na kwa sababu ya jina lake ambalo lilitajwa huko lakini, andiko hilo halina uhusiano wowote na kukanyaga mafuta kunakofanywa na watumishi kadhaa leo.  Maandiko hayajakakataza mtu kupakwa mafuta miguuni baada ya kunawa au kuoga, lakini hilo sio agizo la kibiblia kwamba tukanyage mafuta, Nayaweka haya hadharani kwa sababu nimeagizwa kuihubiri kweli, nimeagizwa kuwafungua watu akili ili watoke gizani na kumgeukia Yesu Kristo mzima mzima sawa sawa na mapenzi yake nimeagizwa kuweka kweli ya Mungu kwa uwazi kwa kusudu la kuleta uelewa ulio wazi ili watu waifahamu kweli na kweli iwaweke huru maandiko yanaonyesha wazi kuwa wakati wa Yoshua alipopiga kura ya kugawa ardhi watu wa kabila la Asheri walipata inchi yenye utajiri mkubwa wa madini pamoja na ustawi wa miti ya mizeituni na chakula cha kutosha, kwa hiyo unabii kuhusu kubarikiwa kwa kabila hilo la Asheri ulitimizwa!

Yoshua 19:24-31 “Kisha kura ya tano ilitokea kwa ajili ya kabila ya wana wa Asheri kwa kuandama jamaa zao. Na mpaka wao ulikuwa ni Helkathi, na Hali, na Beteni, na Akishafu; na Alameleki, na Amadi, na Mishali; nao ukafikilia hata Karmeli upande wa magharibi, tena ulifikilia hata Shihor-libnathi; kisha ukazunguka kuelekea maawio ya jua mpaka Beth-dagoni, nao ukafikilia hata Zabuloni, tena mpaka bonde la Iftaeli upande wa kaskazini hata Bethemeki na Neyeli; kisha ukatokea hata Kabuli upande wa kushoto; na Ebroni, na Rehobu, na Hamoni, na Kana, hata kufikilia Sidoni mkuu; kisha mpaka ulizunguka kuelekea Rama, na mji wa Tiro ulio na boma; kisha mpaka ulizunguka kuelekea Hosa; na matokeo yake yalikuwa baharini katika nchi ya Akzibu; na Uma pia, na Afeka, na Rehobu; miji ishirini na miwili, pamoja na vijiji vyake.Huu ndio urithi wa kabila ya wana wa Asheri kwa kuandama jamaa zao; miji hii pamoja na vijiji vyake.”

Tafasiri ya Kabila la Asheri kuchovya mguu wao katika mafuta inaweza kutafasiriwa leo kama kutembea katika Baraka za Mungu, kubarikiwa na kupata kibali kiroho, kiuchumi na wingi wa mafanikio, kufurahia neema ya Mungu na kuwa na mapito yasiyo na taabu na masumbufu, lakini kamwe andiko hilo haliwezi kutafasiriwa kama lisemavyo moja kwa moja kwa kufanya hivyo ni kufanya mambo ya kijinga kwani mnakanyaga chakula, kukanyaga chakula kunaleta laana kubwa sana  kwa hiyo Mwandishi au Musa hakuagiza watu wakanyage chakula au wakanyage mafuta mwandishi hajawahi kukusudia hivyo! Msipoelewa maneno ya Mungu mtakanyagishwa mpaka ugali, Bwana ampe neema kila mmoja kutembea katika Baraka za Mungu kama kabila ya Asheri katika jina la Yesu Kristo amen!

Jamani swala la kuchovya mguu katika mafuta tafasiri yake sio kukanyaka mafuta halisi, hii ni lugha ya kimafumbo yenye maana kuwa kabila la Asheri watafanikiwa sana kwa utajiri mwingi utakaopatikana kwao naomba ieleweke kwa njia hiyo!

Naomba niseme kwa kiingereza hapa labda nitaeleweka pia

My brothers and Sisters the phrase is not a literal instruction to dip feet in oil, but rather a metaphor for the tribe of Asher’s Prosperity and abundance of resouces available to them I beg to be understood in that way!

Jinsi ya kuchovya mguu wako katika Mafuta!

Kuchovya mguu wako katika mafuta maana yake ni kutembea katika Baraka za Mungu, matokeo ya kutembea katika Baraka za Mungu sio tukio linalokuja kama kufumba na kufumbua bali ni mchakato unaotokana na mtindo wa maisha ya kila siku, unaoendana na utii kwa Mungu. Badala ya kuwakanyagisha watu chakula watumishi wa Mungu wawafundishe watu jinsi ya kutembea katika Baraka za Mungu na kutembea katika Baraka za Mungu kuna kanuni zake.

Wakati Musa au Yakobo anawabariki kabla la Asheri kumbuka kuwa alikuwa amewasoma mtindo wao wa maisha tabia na mwenendo wao kwa Bwana, Imani yao, ushirika wao na kujitoa kwao katika maisha ya kila siku na safari ya kila siku ya maisha yao kwa hiyo Yakobo alipofikia mwisho aliwatabiria Asheri na Musa naye alipokuwa anafikia mwisho aliwatabiria Asheri Baraka nyingi sana kwa hiyo mtu awaye yote anayetaka Baraka za Mungu atapaswa kukanyaga katika kanuni za Mungu kwa kufanya yafuatayo katika maisha yake ya siku zote:-

1.       Ishi maisha ya utii kwa neno la Mungu – Baraka za Mungu huja kwetu pale tunapotii, huenda Musa alikuwa amewaangalia sana wana wa Asheri na kubaini kuwa walikuwa watii katika sheria za Mungu na sheria ya Mungu ilikuwa na ahadi kwamba kama mtu ataisikiliza sauti ya Bwana Mungu wake na kuyatunza maagizo yake basi Mungu angeamuru Baraka zije juu ya mtu huyu au kabila hiyo, utii wetu kwa Mungu katika mambo yote hata madogo madogo utawapelekea watu kufurahia matunda ya utii huo.

 

Kumbukumbu 28:1-2 “Itakuwa utakaposikia sauti ya Bwana, Mungu wako, kwa bidii, kutunza kuyafanya maagizo yake yote nikuagizayo leo, ndipo Bwana, Mungu wako, atakapokutukuza juu ya mataifa yote ya duniani; na baraka hizi zote zitakujilia na kukupata usikiapo sauti ya Bwana, Mungu wako.”

 

Isaya 1:19-20 “Kama mkikubali na kutii mtakula mema ya nchi; bali kama mkikataa na kuasi mtaangamizwa kwa upanga; maana kinywa cha Bwana kimenena haya.”      

 

2.       Ishi maisha  ya Imani – Mwamini na kumtegemea Mungu, hakuna namna iwayo yote mtu anaweza kuishi kwa imani bila kutii na kutegemea, tunaelezwa kuwa Mungu alimuahidi Ibrahimu Baraka lakini ili Baraka hizo ziweze kumjilia Ibrahimu yeye alimuamini Mungu na kutii na ikahesabiwa kwake kuna na haki, hakuna namna yoyote ile ambayo tunaweza kumpendeza Mungu pasipo Imani

 

Mwanzo 12:1-4 “BWANA akamwambia Abramu, Toka wewe katika nchi yako, na jamaa zako, na nyumba ya baba yako, uende mpaka nchi nitakayokuonyesha; nami nitakufanya wewe kuwa taifa kubwa, na kukubariki, na kulikuza jina lako; nawe uwe baraka; nami nitawabariki wakubarikio, naye akulaaniye nitamlaani; na katika wewe jamaa zote za dunia watabarikiwa. Basi Abramu akaenda, kama BWANA alivyomwamuru; Lutu akaenda pamoja naye. Naye Abramu alikuwa mtu wa miaka sabini na mitano alipotoka Harani.”

 

Waebrania 11:6 “Lakini pasipo imani haiwezekani kumpendeza; kwa maana mtu amwendeaye Mungu lazima aamini kwamba yeye yuko, na kwamba huwapa thawabu wale wamtafutao.”

 

Yeremia 17:5-8 “Bwana asema hivi, Amelaaniwa mtu yule amtegemeaye mwanadamu, Amfanyaye mwanadamu kuwa kinga yake Na moyoni mwake amemwacha Bwana. Maana atakuwa kama fukara nyikani, Hataona yatakapotokea mema; Bali atakaa jangwani palipo ukame, Katika nchi ya chumvi isiyokaliwa na watu. Amebarikiwa mtu yule anayemtegemea Bwana, Ambaye Bwana ni Tumaini Lake. Maana atakuwa kama mti uliopandwa kando ya maji, Uenezao mizizi yake karibu na mto; Hautaona hofu wakati wa hari ujapo, Bali jani lake litakuwa bichi; Wala hautahangaika mwaka wa uchache wa mvua, Wala hautaacha kuzaa matunda.

 

3.       Ishi maisha ya utoaji – hakikisha kuwa unatoa kwa ukarimu na sio kwa sheria maandiko yanaonyesha kuwa Mungu huwabariki watu wake wote wanaotoa kwa moyo wa upendo na kwa ukarimu unapokuwa na moyo wa kuwasaidia wengine Mungu huamuru Baraka zake zikujie.

 

Matendo 20:34-35 “Ninyi wenyewe mnajua ya kuwa mikono yangu hii imetumika kwa mahitaji yangu na ya wale waliokuwa pamoja nami. Katika mambo yote nimewaonyesha ya kuwa kwa kushika kazi hivi imewapasa kuwasaidia wanyonge, na kuyakumbuka maneno ya Bwana Yesu, jinsi alivyosema mwenyewe, Ni heri kutoa kuliko kupokea.”            

 

Luka 6:38 “Wapeni watu vitu, nanyi mtapewa; kipimo cha kujaa na kushindiliwa, na kusukwa-sukwa hata kumwagika, ndicho watu watakachowapa vifuani mwenu. Kwa kuwa kipimo kile kile mpimacho ndicho mtakachopimiwa.”                                        

Hitimisho:

Kutembea katika Baraka za Mungu ni matokeo ya maisha endelevu yenye kudumisha uhusiano wako na Mungu, kumpenda Mungu kwa moyo wako wote, kumtii na kumtumikia huku ukiendelea kumuamini, Mungu sio mchoyo kwani yeye amekusudia kumbariki kila mtu na yuko tayari kumimina Baraka zake katika maisha yako ili hatimaye wewe nawe uchovye mguu wako katika mafuta yaani utembee katika Baraka za Mungu, wakristo ni lazima wakumbuke kuwa hakuna njia ya mkato, lakini iko njia ya mchakato, usikubali kudanganywa hata kama watu wanayatumia maandiko, kama kukanyaka mafuta ingekuwa ni njia halisi ya kibiblia ya kufunguliwa na kupata Baraka za Mungu wengi tungekanyaga mafuta hayo, lakini je tangu umenza kukanyaga mafuta halisi kuna badiliko lolote la kiroho, kiafya au kiuchumi? Watumishi wa Mungu tuamke na kutembea katika nuru kwani saa ya kutoka gizani imekwisha kuwadia asomaye na afahamu!, iwapo kukanyaga mafuta lingekuwa agizo halisi la kimaandiko, mitume wa Bwana wangefanya hivyo, na Yesu angeagiza hivyo, na ingekuwa rahisi tu tungekanyaga mafuta na kupata mafanikio lakini hakuna njia ya mkato kwa Mungu kanyaga njia halisi za mapenzi yake na utafanikiwa, kama bado hujamwamini Yesu tafuta kwanza ufaome wake na haki yake na mengine yote mtazidishiwa jiulize  je ni wapi Yesu ameagiza katika agano jipya? Tuchovye mguu katika mafuta?  Je Yesu alipowaosha wanafunzi wake miguu alikuwa akimaanisha na sisi tuoshane miguu? La hasha alikuwa akijibu swali la wanafunzi wake ni yupi aliye mkubwa na akajibu kwa vitendo ni yule atumikaye au anayewahudumia wengine, hebu tulitendee haki neno la Mungu na tusikubali kudanganyika kila tunachofundishwa duniani tuhoji na tujiulize kikoje katika maandiko na je ndivyo kilivyo? Imekuwaje wakristo wa kipindi hiki ambao ni wasomi na maarifa nyameongezeka wanadanganyika kwa njia rahisi? Do you think that to think critical is sin? Je unafikiri kwamba kufikiri kwa kuhoji au kujiuliza ni dhambi? Amka kuanzia sasa na jaribu kila fundisho au roho uone kama ndivyo ilivyo, Mafundisho huwa yana roho nyuma yake

Yohana 6:63 “Roho ndiyo itiayo uzima, mwili haufai kitu; maneno hayo niliyowaambia ni roho, tena ni uzima.”

1Yohana 4:1-4 “Wapenzi, msiiamini kila roho, bali zijaribuni hizo roho, kwamba zimetokana na Mungu; kwa sababu manabii wa uongo wengi wametokea duniani. Katika hili mwamjua Roho wa Mungu; kila roho ikiriyo kwamba Yesu Kristo amekuja katika mwili yatokana na Mungu. Na kila roho isiyomkiri Yesu haitokani na Mungu. Na hii ndiyo roho ya mpinga Kristo ambayo mmesikia kwamba yaja; na sasa imekwisha kuwako duniani. Ninyi, watoto wadogo, mwatokana na Mungu nanyi mmewashinda, kwa sababu yeye aliye ndani yenu ni mkuu kuliko yeye aliye katika dunia.”

                                 

Na. Rev. Innocent Samuel Kamote

Mkuu wa wajenzi mwenye Hekima!

Ijumaa, 2 Mei 2025

Nafasi ya wafanya kazi wa ndani katika nyumba za wachungaji!


2Wafalme 5:1-5 “Basi Naamani, jemadari wa jeshi la mfalme wa Shamu, alikuwa mtu mkubwa mbele ya bwana wake, na mwenye kuheshimiwa, kwa sababu kwa mkono wake Bwana alikuwa amewapa Washami kushinda; tena alikuwa mtu hodari wa vita; lakini alikuwa mwenye ukoma. Na Washami walikuwa wametoka vikosi, wakachukua mfungwa mmoja kijana mwanamke kutoka nchi ya Israeli; naye akamhudumia mkewe Naamani. Akamwambia bibi yake, Laiti bwana wangu angekuwa pamoja na yule nabii aliyeko Samaria! Maana angemponya ukoma wake.” 



  

Utangulizi:

Ni muhimu kufahamu kwamba mojawapo ya nafasi ya Muhimu sana katika utumishi wa Mungu ni pamoja na kupata nafasi ya kuwa mfanyakazi wa ndani katika nyumba ya Mchungaji au mtumishi awaye yote wa Mungu, hii ni nafasi ya kipekee sio tu ya kupata neema ya kuwahudumia watumishi wa Mungu lakini pia ya kupitia kujifunza kwa namna ya kipekee na kushuhudia maisha ya utumishi wa watu wa Mungu na kujiletea baraka  na heshima kutoka kwa Mungu, hii ni kwa sababu neno la Mungu limesema yeye amuhudumiaye nabii kwa kuwa ni nabii atapata thawabu ya nabii.


Mathayo 10:40-42 “Awapokeaye ninyi, anipokea mimi; naye anipokeaye mimi, ampokea yeye aliyenituma. Ampokeaye nabii kwa kuwa ni nabii, atapata thawabu ya nabii; naye ampokeaye mwenye haki kwa kuwa ni mwenye haki, atapata thawabu ya mwenye haki. Na mtu awaye yote atakayemnywesha mmojawapo wa wadogo hawa ngaa kikombe cha maji ya baridi, kwa kuwa ni mwanafunzi, amin, nawaambia, haitampotea kamwe thawabu yake.”


Wafanyakazi wa ndani katika nyumba za watumishi wa Mungu wanahitaji maelekezo maalumu ili waweze kutambua wajibu wao na baraka ambazo Mungu amezikusudia kwao, wasipoelekezwa vema wanaweza kutumika kinyume na mapenzi ya Mungu na kusababisha changamoto kubwa za kihuduma kwa mtu wa Mungu na hata na kanisa lake kwa ujumla na huduma ya Mchungaji na mama Mchungaji, Ni lazima watumishi wa ndani katika nyumba za wachungaji watambue kuwa kazi yao ni huduma kamili na ni ibada kamili mbele za Mungu na kwa sababu hiyo wanapaswa kuifanya kwa moyo na ni nafasi ya kipekee sana na kwa sababu hiyo hawapaswi kuichukulia kama nafasi isiyo ya heshima, wao wanaweza kuyatumia mazingira ya kiroho yapatikanayo katika nyumba ya mtumishi wa Mungu kama njia ya Baraka kubwa katika maisha yao.


Kwa msingi huo leo tutachukua Muda kujifunza maswala ya msingi ambayo wafanyakazi wa ndani katika nyumba za watumishi wa Mungu wanaweza kuyaishi ili waweze kuwa Baraka katika mwili wa Kristo na kwa kanisa la Mungu bila kusababisha madhara katika nyumba za watumishi wa Mungu na huduma walizoaminiwa na Mungu katika maisha yao. Huduma ya kichungaji inapaswa kulindwa na kwa sababu hiyi mtenda kazi wa ndani ni moja ya walinzi wa huduma ya kichungaji, ni walinzi wa madhabahu iliyo hai yaani moyo na maisha ya Mchungaji.

1.       Watumishi wa ndani katika nyumba ya mchungaji ni watenda kazi pamoja na mtumishi wa Mungu.

 

Inapotokea kuwa kwa njia yoyote ile umepata nafasi ya kuishi katika nyumba ya Mchungaji au nabii, Mtume na kadhalika kwaajili ya kazi za ndani ni lazima utambue kuwa wewe ni mtumishi wa Mungu katika nafasi uliyo nayo, kwa sababu umepata neema ya kumtumikia Mungu pamoja na mtumishi wake na familia yake, na kwa sababu hiyo kazi yako sio kazi ya kawaida bali ni ibada mbele za Mungu na Mungu atakubariki endapo utaifanya kazi hiyo kwa uaminifu na uchaji wa Mungu, kwa hiyo fanya kazi hiyo kama sehemu ya utumishi wako kwa Mungu na kamwe acha kujifikiri kuwa u mtumwa au mjakazi.

 

Wakolosai 3:23-24 “Ninyi watumwa, watiini hao ambao kwa mwili ni bwana zenu, katika mambo yote, si kwa utumwa wa macho, kama wajipendekezao kwa wanadamu, bali kwa unyofu wa moyo, mkimcha Bwana. Lo lote mfanyalo, lifanyeni kwa moyo, kama kwa Bwana, wala si kwa wanadamu,mkijua ya kuwa mtapokea kwa Bwana ujira wa urithi. Mnamtumikia Bwana Kristo.”    

 

Nimeishi na wasichana wa kazi wengi katika maisha yangu na wengi wa wale waliokaa na mimi vizuri Mungu aliwabariki na waliolewa na sasa wana nyumba zao na wanaishi maisha mazuri na yenye utulivu, nay a kuvutia sana, vijana  wengi waliamini kuwa mambinti hao wako salama  na wote waliooa kutoka katika nyumba za wachungaji hawakuwahi kujutia hii ni moja ya Baraka kubwa, wakati mwingine kutokana na kuishi katika utumishi wa Mtumishi wa Mungu, Mungu amewafanya wafanyakazi katika nyumba za watu wa Mungu kuja kuwa na huduma ya kitumishi vile vile na wengi wameinuliwa kutoka kuwa watumishi wa ndani na hata kuwa mama wachungaji, mama maaskofu na kadhalika  

 

Roho ya utumishi wa Mungu imewahi kuwakalia wale waliokuwa watumishi wa watumishi wa Mungu, hii ni kwa sababu watumishi wa waliokuwa watumishi wa Mungu wanajua mapito na mateso yote ambayo Bwana zao waliyapitia kwa hiyo haishangazi kuona Mungu akijitwalia viongozi kutoka wale waliokuwa wakifanya kazi kama za utumwa tu, kimsingi wakati mwingine huwezi kuwa mtumishi wa Mungu kabla ya kuwa mtumishi wa mwanadamu.

 

Kutoka 3:1-4 “Basi huyo Musa alikuwa akilichunga kundi la Yethro mkwewe, kuhani wa Midiani; akaliongoza kundi nyuma ya jangwa, akafika mpaka mlima wa Mungu, hata Horebu. Malaika wa BWANA akamtokea, katika mwali wa moto uliotoka katikati ya kijiti; akatazama, na kumbe! Kile kijiti kiliwaka moto, nacho kijiti hakikuteketea. Musa akasema, Nitageuka sasa, niyaone maono haya makubwa, na sababu kijiti hiki hakiteketei. BWANA alipoona ya kuwa amegeuka ili atazame, Mungu akamwita kutoka katikati ya kile kijiti, akasema, Musa! Musa! Akasema, Mimi hapa.”  

 

Hesabu 11:28-29 “Yoshua mwana wa Nuni, mtumishi wa Musa tangu ujana wake, akajibu akasema, Ee bwana wangu Musa, uwakataze. Musa akamwambia, Je! Umekuwa na wivu kwa ajili yangu; ingekuwa heri kama watu wote wa Bwana wangekuwa manabii na kama Bwana angewatia roho yake.”

 

Yoshua 1:1-3 “Ikawa baada ya kufa kwake Musa, mtumishi wa Bwana, Bwana akamwambia Yoshua, mwana wa Nuni, mtumishi wa Musa, akasema, Musa mtumishi wangu amekufa; haya basi, ondoka, vuka mto huu wa Yordani; wewe na watu hawa wote, mkaende hata nchi niwapayo wana wa Israeli.Kila mahali zitakapopakanyaga nyayo za miguu yenu, nimewapa ninyi, kama nilivyomwapia Musa.”

 

Ni jambo la kushangaza kuwa Musa alikuwa akifanya kazi ya kulichunga kund la Yethro mkwewe ambaye alikuwa kuhani wa Midian, Lakini Mungu alimuita Musa akiwa katika hali ya kumtumikia mkwewe na kufanya kazi hiyo ambayo kimtazamo ilionekana ni kama kazi ya chini sana, Yoshua alikuwa mtumishi wa Musa na baadaye Musa alipokufa Yoshua ndiye aliyekuwa kiongozi mkubwa aliyewaingiza Israel katika inchi ya mkanaani  hii inaweza isiwe kanuni lakini inatufunza Mungu anajali utumishi wako dhidi ya watumishi wake.               

 

2.       Watumishi wa ndani katika nyumba ya mchungaji ni lazima wajifunze kuwaheshimu wachungaji na familia zao.

 

Kila anayefanya kazi katiia nyumba ya mtumishi wa Mungu ni lazima awe na uelewa kuwa watumishi hao wa Mungu wanahitaji kuheshimiwa sana wao pamoja na familia zao, Mchungaji au nabii au mtume ni mtu aliyeitwa na Mungu na ni mtu anayestahili heshima yeye pamoja  na mkewe pia na watoto wao, kwa sababu hiyo kila anayefanya kazi ndani ya nyumba za watumishi wa Mungu anapaswa kujiheshimu, ni marufuku kuutumia udhaifu wa mke wa Mchungaji kama nafasi ya kutaka kumvunjia Heshima mama Mchungaji na au mchungaji, Moja ya mgogoro mkubwa uliompata Sara na Hajiri hata kufikia ngazi ya kuanza kutesana ni pamoja na Hajiri kuanza kumdharau Bibi yake.

 

Mwanzo 16:6-9 “Naye Abramu akamwambia Sarai, Tazama, mjakazi wako yu mkononi mwako, mtendee lililo jema machoni pako. Sarai akamtesa, naye akakimbia kutoka mbele yake. Malaika wa BWANA akamwona kwenye chemchemi ya maji katika jangwa, chemchemi iliyoko katika njia ya kuendea Shuri. Akamwambia, Hajiri, wewe mjakazi wa Sarai, unatoka wapi, nawe unakwenda wapi? Akanena, Nakimbia mimi kutoka mbele ya bibi yangu Sarai. Malaika wa BWANA akamwambia, Rudi kwa bibi yako, ukanyenyekee chini ya mikono yake.”

 

Wafanyakazi wa ndani watapaswa kuishi na mke wa mchungaji vizuri na kujiepusha na migogoro isiyo na msingi, aidha wao ni waajiriwa wa mwanamke na kamwe halitakuwa jambo lenye kupendeza Mchungaji kujihusisha na malipo ya mshahara wa mfanyakazi, wafanyakazi wa ndani wanapaswa kuheshimu mamlaka ya kiroho ya kichungaji sawa tu na ilivyo Kanisani na nyumbani pia.

 

1Timotheo 5:17 “Wazee watawalao vema na wahesabiwe kustahili heshima maradufu; hasa wao wajitaabishao kwa kuhutubu na kufundisha.”

 

Aidha kila msichana wa kazi katika nyumba ya mtumishi wa Mungu anapaswa kuwa kielelezo kwa kuishi maisha matakatifu na yaliyo kielelezo kwani watu wanaitazamia nyumba ya mchungaji kuwa kielelezo, wako mambinti wengi katika nyumba za watumishi wa Mungu ambao wametia aibu kwa kuishi maisha yasiyokuwa na kielelezo na kwa sababu hiyo kusababisha maswali yasiyoyokuwa na majibu, wengine walipata ujauzito na wakarudhishwa makwao huku washirika wakibaki na maswali kwamba waliwezaje kufanya matukio ya aina hiyo ili hali wanaishi katika nyumba za watu wa Mungu, huku ni kufanya uchafuzi wa kimazingira na kuleta shaka juu ya usimamizi wa huduma ya kichungaji kwani Mchungaji na mama Mchungaji wana wajibu wa kuisimamia nyumba ya Mchungaji ili iwe kielelezo kwa waamini.

 

1Timotheo 3:4-5 “mwenye kuisimamia nyumba yake vema, ajuaye kutiisha watoto katika ustahivu; (yaani, mtu asiyejua kuisimamia nyumba yake mwenyewe, atalitunzaje Kanisa la Mungu?)

 

3.       Watumishi wa ndani katika nyumba ya mchungaji ni lazima wawe kielelezo katika Uadilifu, Nidhamu na kutunza siri za nyumbani

 

Ukiacha kuwa ni jukumu la kila mfanyakazi wa ndani katika nyumba ya Mchungaji kuishi maisha yaliyo kielelezo na ya uadilifu na nidhamu, pia kila msichana wa kazi katika nyumba za watumishi wa Mungu anapaswa kuwa mstari wa mbele katika kutunza siri za changamoto zinazojitokeza katika nyumba ya mtumishi wa Mungu, Nyumbani Mchungaji ni Baba, ni Mume  na ni kiongozi wa familia, lakini sio hivyo tu Nyumba ya mchungaji ina mapito mengi, wanaweza kulala na njaa, kufunga, kula vibaya yaani chakula kisicho na hadhi, kupungukiwa na kadhalika pia Mchungaji anao ndugu na jamaa ambao wanaweza kuwa hawajaokoka, hivyo watendakazi nyumbani kwa mchungaji hupita mapito hayo pamoja na familia ya Mchungaji na kwa sababu hiyo wakati mwingine usiri unahitajika kuhusiana na mapito hayo, Ni lazima mfanyakazi wa ndani katika nyumba ya mchungaji awe mwaminifu kwa kila linaloendelea nyumbani, hupaswi kulianika nje? Usieneze siri ya matatizo au mapito ya ndani ya nyumba ya mchungaji, hakikisha kuwa washirika wengine hawatengenezi nafasi ya udadisi ya kutaka kujua yanayoendelea katika nyumba ya mchungaji wewe endelea kuwa mwaminifu na kufanya kazi kwa heshima, usafi na kwa moyo acha kueneza fitina hususani kati ya nyumba ya mchungaji na washirika wake, waache waguswe wenyewe kuihudumia nyumba ya Mchungaji na usiwaeleze watu kabisa hata kama mmeshinda na njaa. Aidha kama kuna jambo watu wanajaribu kulidadisi kuhusu Mchungaji au mama Mchungaji waelekeze watu kuwaona wasemaji wa familia ya Mchungaji na wewe baki kama mtu usiyejua kinachoendelea!

 

Mithali 11:13 “Mwenye kitango akisingizia hufunua siri; Bali mwenye roho ya uaminifu husitiri mambo.”

 

Mithali 25:2 “Ni utukufu wa Mungu kuficha jambo; Bali ni utukufu wa mfalme kuchunguza jambo.”

 

Aidha ishi na watoto wa Mtumishi wa Mungu sawa na makusudi ambayo kwayo watoto hao wamezaliwa, wewe kama yaya wa watoto wa Mchungaji usijihusishe katika kuwapandikizia watoto wa Mchungaji uharibifu, lilikuwa ni jambo la kusikitisha kuwa Hajiri yeye alianza kumnyanyasa Isaka na akiwa na mwanae Ishmael walianza kutumiwa na shetani kumdhihaki Isaka na kumfanya mtoto yule wa ahadi asiyafurahie maisha nyumbani kwao jambo lililompelekea Sara kuamuru kutimuliwa kwa mjakazi na mwanae.

 

Mwanzo 21:8-12 “Mtoto akakua, akaachishwa kunyonya; Ibrahimu akafanya karamu kuu siku ile Isaka alipoachishwa kunyonya. Sara akamwona yule mwana wa Hajiri Mmisri, ambaye alimzalia Ibrahimu, anafanya dhihaka. Kwa hiyo akamwambia Ibrahimu, Mfukuze mjakazi huyu na mwanawe, maana mwana wa mjakazi hatarithi pamoja na mwanangu, Isaka. Na neno hilo lilikuwa baya sana machoni pa Ibrahimu, kwa ajili ya mwanawe. Mungu akamwambia Ibrahimu, Neno hili lisiwe baya machoni pako, kwa ajili ya huyo mwana, na huyo mjakazi wako. Kila akuambialo Sara, sikiza sauti yake, kwa maana katika Isaka uzao wako utaitwa.”

 

Aidha uzembe uliowahi kufanya na yaya wa Yonathan mwana wa Sauli kwa kijana wake Methiboehseth ulisababisha ulemavu usio wa lazima kwa mtoto wa Mtumishi wa Mungu Yonathan, kwa hiyo hata yaya katika nyumba za watumishi wa Mungu anapaswa kuwa mtu mwangalifu kwa familia ya Mchungaji, watoto wke mkewe na nduguze na kuchukua tahadhari za kutokuwasababishia matatizo au changamoto watumishi wa Mungu zikiwemo changamoto za kiafya!

 

2Samuel 4:4 “Naye Yonathani, mwana wa Sauli alikuwa na mwana aliyekuwa na kilema cha miguu. Alikuwa amepata miaka mitano, habari za Sauli na Yonathani zilipofika Yezreeli, na yaya wake akamchukua akakimbia ikawa, alipokimbia kwa haraka, huyo mtoto akaanguka, akawa kilema. Na jina lake aliitwa Mefiboshethi.”       

 

4.       Watumishi wa ndani katika nyumba ya mchungaji ni lazima waishi kwa kutumia fursa za kiroho zinazopatikana katika nyumba ya mtumishi

 

Kuishi na watumishi wa Mungu kwa uzuri ubora na uaminifu kunaleta Baraka kubwa sana kutokana na utendaji wako uliotukuka wewe unaweza kufanikisha watumishi wa Mungu kuhudhuria ibada kwa wakati huku wakiwa wameshiba, kuwapikia chakula bora, kuitumia nafasi ya kufunga kwao na kuomba kukua kiroho, kuhudhuria ibada pamoja nao na kujifunza maisha ya utumishi, kwa ujumla ni Baraka kubwa sana kuwatumikia watumishi wa Mungu wale waliotumika kwa uaminifu walipata Baraka na wale walioshindwa kuwa waaminifu walipata madhara kwa sababu hiyo wewe itumie nafasi ya kuishi kwa mchungaji kwa nia njema, usikubali kuwaacha watumishi wa Mungu kwa sababu zozote zile hata wanapopitia changamoto wewe ni lazima uwe mtu wa kwanza kusimama nao

 

2Wafalme 2:9-15 “Hata ikawa, walipokwisha kuvuka, Eliya akamwambia Elisha, Omba kwangu lo lote utakalo nikutendee, kabla sijaondolewa kwako. Elisha akasema, Nakuomba, sehemu maradufu ya roho yako na iwe juu yangu. Akasema, Umeomba neno gumu; lakini, ukiniona nitakapoondolewa kwako, utalipata; la hukuniona, hulipati. Ikawa, walipokuwa wakiendelea mbele na kuongea, tazama! Kukatokea gari la moto, na farasi wa moto, likawatenga wale wawili; naye Eliya akapanda mbinguni kwa upepo wa kisulisuli. Naye Elisha akaona, akalia, Baba yangu, baba yangu, gari la Israeli na wapanda farasi wake! Asimwone tena kabisa; akashika mavazi yake mwenyewe, akayararua vipande viwili. Kisha akaliokota lile vazi la Eliya lililomwangukia, akarudi, akasimama katika ukingo wa Yordani. Akalitwaa lile vazi la Eliya lililomwangukia, akayapiga maji, akasema, Yuko wapi Bwana, Mungu wa Eliya? Naye alipoyapiga maji, yakagawanyika huku na huku, Elisha akavuka.Na hao wana wa manabii, waliokuwako Yeriko wakimkabili, walipomwona, walisema, Roho ya Eliya inakaa juu ya Elisha. Wakaja kuonana naye, wakainama kifudifudi mbele yake.”

 

Elisha alikuwa ni mtumishi binafsi wa Eliya, alitumika kwa uaminifu mpaka dakika ya mwisho, jambo hili lilimletea Baraka kubwa sana wakati wa kuagana ulipofika kwa kweli Eliya alikuwa amekusudia kumbariki Elisha na Elisha aliomba sehemu maradufu ya roho ya Eliya imkalie juu yake na kwa kweli Mungu alifanya hivyo na wote waliokuwa wakimtambua Elisha kama mtumishi wa Eliya walimuinamia mpaka nchi wakijua kuwa Roho ya Eliya inakaa juu ya Elisha

 

Wakati Elisha akiwa anafaidika na utumishi wake mambo yalikuwa kinyume kwa Gehazi ambaye aliweka maslahi yake mbele na kutokufuata maelekezo ya Bwana wake na kwa sababu hiyo aliambulia kuwa na ukoma siku zote za maisha yake

 

2Wafalme 5:20-27 “Lakini Gehazi, mtumishi wa Elisha mtu wa Mungu, akasema, Tazama, bwana wangu amemwachilia huyo Naamani Mshami, asivipokee mikononi mwake vile vitu alivyovileta; kama Bwana aishivyo, mimi nitamfuata mbio, nipokee kitu kwake. Basi Gehazi akamfuata Naamani. Naye Naamani, alipoona mtu apigaye mbio anakuja nyuma yake, alishuka garini amlaki, akasema, Je! Ni amani? Akasema, Amani. Bwana wangu amenituma, kusema, Tazama, sasa hivi wamenijia kutoka milimani mwa Efraimu vijana wawili wa wana na manabii; uwape, nakuomba, talanta ya fedha, na mavazi mawili. Naamani akasema, Uwe radhi, ukatwae talanta mbili. Akamshurutisha, akafunga talanta mbili za fedha ndani ya mifuko miwili, na mavazi mawili, akawatwika watumishi wake wawili; nao wakayachukua mbele yake. Naye alipofika kilimani, alivitwaa mikononi mwao, akaviweka nyumbani; akawaacha wale watu kuondoka, nao wakaenda zao. Lakini yeye akaingia, akasimama mbele ya bwana wake. Elisha akamwambia, Watoka wapi, Gehazi? Akanena, Mtumwa wako hakuenda mahali. Akamwambia, Je! Moyo wangu haukuenda na wewe, hapo alipogeuka yule mtu katika gari ili akulaki? Je! Huu ndio wakati wa kupokea fedha, na kupokea mavazi, na mashamba ya mizeituni, na mizabibu, na kondoo, na ng'ombe, na watumwa, na wajakazi? Basi ukoma wa Naamani utakushika wewe, na wazao wako hata milele. Naye akatoka usoni pake mwenye ukoma kama theluji.”

 

Kutokuitumia fursa ya kiroho ya kuishi na watumishi wa Mungu kunaweza kutuletea laana na wazao wetu, lakini tukiwa na akili na kujua mapenzi ya Mungu neema ya Mungu itatuinua na watumishi hao wa Mungu watatuachia Baraka kubwa sana katika maisha yetu, kama ukiitambua siri ya kuishi na watumishi wa Mungu na ukajua Baraka zinazopatikana kwa kweli utasema kama Daudi kuwa siku moja katika nyua zako ni bora kuliko siku 1000, kuitumikia nyumba ya mtumishi wa Mungu ni kuitumikia madhabahu ya Bwana

 

Zaburi 84:10 “Hakika siku moja katika nyua zako Ni bora kuliko siku elfu. Ningependa kuwa bawabu nyumbani mwa Mungu wangu, Kuliko kukaa katika hema za uovu.”

 

5.       Watumishi wa ndani katika nyumba ya mchungaji ni lazima waitumie nafasi ya kuishi kwa maombi na neno la Mungu

 

Kupata nafasi ya kuishi katika nyumba ya mtumishi wa Mungu kusikufanye wewe kubweteka na kuishi maisha ya kiburi na majivuno, badala yake lazima uitumie nafasi hiyo kwa kuishi kwa maombi huku ukiwa mtu uliyejaa neno la Mungu, lazima mtu anayeishi katika nyumba ya mchungaji awe msikilizaji na mtendaji mzuri wa neno la Mungu, huku ukiwa kielelezo cha maisha ya kiroho, kushiriki ibada na mafundisho na hata kuandika notes, watu wanaokaa kwa mchungaji hawachukuliwi kuwa watu wa kawaida kwa hiyo ni lazima uwe kielelezo.

 

Kutoka 33:11 “Naye BWANA akasema na Musa uso kwa uso, kama vile mtu asemavyo na rafiki yake. Kisha akageuka akarejea hata maragoni; bali mtumishi wake Yoshua, mwana wa Nuni, naye ni kijana, hakutoka mle hemani.”

 

Mathayo 4:4 “Naye akajibu akasema, Imeandikwa, Mtu hataishi kwa mkate tu, ila kwa kila neno litokalo katika kinywa cha Mungu.”

 

6.       Watumishi wa ndani katika nyumba ya mchungaji ni lazima kuitumia nafasi ya kuishi kwa Mchungaji kama sehemu ya huduma na Upendo kwa wengine.

 

Kufanya kazi katika nyumba ya Mchungaji kunahitaji hekima, uvumilivu na upendo kwa wengine lakini zaidi sana kwa Mchungaji, wachungaji wakati  mwingine hukosa nafasi ya Mapumziko mfanyakazi katika nyumba ya Mchungaji anapaswa kuwa na hekima sio kila wakati utamwamsha mchungaji au kuwakaribisha wageni katika nyumba yake, utawahoji wageni kwa hekima na upendo iwapo wana ahadi ya kukutana na Mchungaji nyumbani kwake au ofisini, Afya ya Mchungaji ni lazima ilindwe kwa gharama yoyote, muda wake binafsi na Mungu, muda wake wa kujiandaa kwaajili ya neno la Mungu, utulivu wake kula kwake na mapumziko yake kwa hiyo ni wajibu wa mfanyakazi katika nyumba ya Mchungaji ni kusimamamia ratiba za mtumishi wa Mungu badala ya kumwamsha kila anapokuja mtu yoyote na hata matapeli tu kwa hiyo tunaaswa kuwa na huduma na moyo wa upendo lakini tukiyanusuru na kuyalinda maisha ya mtumishi wa Mungu yasiiingiliwe kama mtu atakavyo

 

Wagalatia 5:13-14 “Maana ninyi, ndugu, mliitwa mpate uhuru; lakini uhuru wenu usiwe sababu ya kuufuata mwili, bali tumikianeni kwa upendo. Maana torati yote imetimilika katika neno moja, nalo ni hili, Umpende jirani yako kama nafsi yako.”

 

7.       Watumishi wa ndani katika nyumba ya mchungaji ni lazima wafanyike Baraka katika nyumba ya Mchungaji.     

 

Katika mstari wa msingi wa somo hili nimenukuu habari za binti mmoja kijakazi katika nyumba ya Naamani ambaye alichukuliwa mateka huko Syria, lakini binti huyu aligeuka Baraka kubwa kwa sababu kupitia yeye na imani yake Bwana wake aliponywa ukoma wake, mfanyakazi huyu alichukuliwa mateka kutoka Israel lakini jambo la kushangaza hajawahi kuweka kinyongo chochote alikubali maisha ya ujakazi na utumwa huku akiwa mwaminifu kwa Bwana wake huku akimtakia afya njema na mafanikio zaidi, Naaman tunaelezwa kuwa alikuwa mzuri sana kwani jina Naaman maana yake ni mzuri lakini alipougua ukoma hali yake iliharibika na sasa kijakazi huyu anamtakia bibi yake na bwana wake furaha ya kweli kwa kujali afya ya Naamani

 

2Wafalme 5:1-5 “Basi Naamani, jemadari wa jeshi la mfalme wa Shamu, alikuwa mtu mkubwa mbele ya bwana wake, na mwenye kuheshimiwa, kwa sababu kwa mkono wake Bwana alikuwa amewapa Washami kushinda; tena alikuwa mtu hodari wa vita; lakini alikuwa mwenye ukoma. Na Washami walikuwa wametoka vikosi, wakachukua mfungwa mmoja kijana mwanamke kutoka nchi ya Israeli; naye akamhudumia mkewe Naamani. Akamwambia bibi yake, Laiti bwana wangu angekuwa pamoja na yule nabii aliyeko Samaria! Maana angemponya ukoma wake.”

 

Kila mfanyakazi katika nyumba ya mtumishi wa Mungu anapaswa kuwa sababu ya Baraka na uponyaji wa nyumba ya mtumishi badala ya kutumika kama ajenti wa shetani na kusababisha maafa na anguko la mtumishi wa Mungu au huduma yake, aidha kuwa na moyo wa shukurani na subira kuacha tamaa, wivu na kutokuyatenda majukumu yako ipaswavyo, binti yule wa kiyahudi alikuwa mwaminifu na mwenye moyo wa kweli kwani licha ya kuwa alikuwa amechukuliwa mateka lakini alikuwa ni mtu aliyethamini utumishi wa Naamani na kutamani kama angeponywa ukoma wake, alikuwa na imani kubwa kwani haijawahi kusikika kokote kuwa mtu amewahi kuponywa ukoma wake lakini yeye alimuamini Elisha na kusaidiki kuwa bwana wake anaweza kupata msaada Endapo angekutana na mtu wa Mungu na ikawa hivyo kwani Naamani aliponywa na sio mwili wake tu na alimuamini Mungu wa Israel hata ushindi wake ulitokana na Mungu wa Israel

 

8.       Watumishi wa ndani katika nyumba ya mchungaji ni lazima wavae kwa kujisitiri

 

Kama mtumishi wa Mungu ndani ya nyumba ya mchungaji hakikisha kuwa unavaa kwa heshima na kujisitiri, haiwezekani unakaa katika nyumba ya Mtu wa Mungu kisha ukawa unavaa mavazi ya kikahaba na kutumika kama chombo cha ibilisi kwaajili ya kumaliza huduma ya kichungaji swala hilo halitaleta Baraka kwako na kwa mwili wa Kristo, acha kujifikiri mwenyewe na starehe zako na baadala yake fikiri kuhusu faida za mwili wa Kristo na ufalme wa Mungu.

               

1Timotheo 2:9-10 “Vivyo hivyo wanawake na wajipambe kwa mavazi ya kujisitiri, pamoja na adabu nzuri, na moyo wa kiasi; si kwa kusuka nywele, wala kwa dhahabu na lulu, wala kwa nguo za thamani; bali kwa matendo mema, kama iwapasavyo wanawake wanaoukiri uchaji wa Mungu.”

 

Mithali 7:10-18 “Na tazama, mwanamke akamkuta, Ana mavazi ya kikahaba, mwerevu wa moyo; Ana kelele, na ukaidi; Miguu yake haikai nyumbani mwake. Mara yu katika njia kuu, mara viwanjani, Naye huotea kwenye pembe za kila njia. Basi akamshika, akambusu, Akamwambia kwa uso usio na haya, Kwangu ziko sadaka za amani; Leo hivi nimeziondoa nadhiri zangu; Ndiyo maana nikatoka nikulaki, Nikutafute uso wako kwa bidii, nami nimekuona. Nimetandika kitanda changu, magodoro mazuri, Kwa matandiko ya Kimisri yenye mistari. Nimetia kitanda changu manukato, Manemane na udi na mdalasini. Haya, na tushibe upendo hata asubuhi, Tujifurahishe nafsi zetu kwa mahaba.”

 

9.       Watumishi wa ndani katika nyumba ya mchungaji wasijaribu kuwa mrithi wa mama Mchungaji

 

Hakuna sheria inayokataza Mchungaji kumuoa binti wake wa kazi endapo itatokea Mungu ametaka iwe hivyo, hata hivyo litakuwa ni jambo lenye kuchukiza na kuleta utata mkubwa sana endapo itatokea unaolewa na Mchyhungaji baada ya mama Mchungaji, maandiko yanaonyesha kuwa ni chukizo kwa mjakazi kumrithi bibi yake, Muombe Mungu akupe mumeo na usijihusishe na maisha ya Mchungaji wale mke wake hata kama uliyasoma  madhaifu yake, watmishi wa Mungu tafadhali Mungu akupe hekima usilitupia jicho lako kwa binti wa kazi yeye na awe kama moja ya mabinti zako tu nyumbani, Mwandishi wa kitabu cha Mithali alionyesha kuwa kuoa housegirl ni jambo lisilovumilika na linaweza kutetemesha nchi

 

Mithali 30:21-23 “Kwa ajili ya mambo matatu nchi hutetemeka, Naam, kwa ajili ya manne haiwezi kuvumilia. Mtumwa apatapo kuwa mfalme; Mpumbavu ashibapo chakula; Mwanamke mwenye kuchukiza aolewapo; Na mjakazi aliye mrithi wa bibi yake.”

 

10.   Watumishi wa ndani katika nyumba ya mchungaji Wanaweza kumjua Mchungaji vema zaidi kuliko watu wengine wote

 

Watumishi wa ndani katika nyumba ya Mchungaji wanauwezo wa kumjua Mchungaji na mahitaji yake vema zaidi kuliko watu wengine, Nyakati za kanisa la kwanza wakati Mchungaji Yakobo na Petro walipokuwa wamekamatwa, na Yakobo akauawa na Herode ni ukweli uliokuwa wazi kuwa kanisa lilimuomba Mungu kwa bidii sana lakini hata hivyo hawakuwa na Imani kuwa Mungu angefanya muujiza, Hata hivyo Mungu alimtuma malaika akamfungua Petro Gerezani na hata alipokuwa akigonga mlango mtu aliyetambua kuwa Petro anagonga mlango alikuwa ni Roda mfanyakazi wa ndani katika nyumba ya Mariamu mama yake Yohana, binti huyu kwa furaha aliacha kufungua mlango na kuwapasha wote kuwa Petro anagonga mlango, hata hivyo kila mmoja katika kanisa walifikiria kuwa binti huyo ana wazimu ni kichaa, hayuko sawasawa,  lakini ni ukweli ulio wazi yeye ndiye aliyekuwa sahihi kuliko watu wote, moyo wake upendo na Imani yake kwa Mungu ilimfanya kuwa na mtazamo tofauti na watu wengine wote yeye alimjua Petro vizuri na hata sauti yake na alipogonga pia alikuwa anajua namna Petro anavyogonga mlango wa nyumba

 

Matendo 12:11-16 “Hata Petro alipopata fahamu akasema, Sasa nimejua yakini ya kuwa Bwana amempeleka malaika wake na kunitoa katika mkono wa Herode na katika kutazamia kote kwa taifa la Wayahudi. Na alipokuwa akifikiri haya akafika nyumbani kwa Mariamu, mamaye Yohana, ambaye jina lake la pili ni Marko; na watu wengi walikuwa wamekutana humo wakiomba. Naye alipobisha kilango cha lango, kijakazi, jina lake Roda, akaja kusikiliza. Alipoitambua sauti ya Petro, hakukifungua lango, kwa ajili ya furaha, bali alipiga mbio, akaingia ndani akawaambia kwamba Petro anasimama mbele ya lango. Wakamwambia, Una wazimu. Lakini yeye akakaza sana, akasema ya kwamba ndivyo hivyo. Wakanena, Ni malaika wake. Petro akafuliza kugonga, hata walipokwisha kumfungulia wakamwona, wakastaajabu.”

 

Hii inatukumbusha na kutufundisha kuwa watumishi wa ndani katika nyumba ya Mchungaji wanaweza kuwa na ufahamu mkubwa na wa kina kumuhusu mtumishi wa Mungu nahata kumjua Mungu na utendaji wake kuliko mtu mwingine yeyote na Mungu amewapa wao neema ya kutambua mwenendo na uhitaji wa Mchungaji wakati mwingine kuliko wengine katika kanisa, na tunakumbushwa hapa kuwa hatupaswi kuwafikiria kuwa ni wenye wazimu hata kidogo, na kuwapuuzia au kuipuuzia mitazamo yao ya kiroho

 

11.   Watumishi wa ndani katika nyumba ya mchungaji ni lazima wawe waaaminifu kwa mama Mchungaji

 

Ruthu ni mfano wa kuigwa kwa uaminifu wake aliokuwa nao kwa Mkwewe, alisimama na mkwewe katika mazingira yaliyokuwa magumu sana na kujionyesha kuwa mwaminifu hata kwa gharama yoyote, Yeye alikuwa ni Mmoabu na hakukuwa na kitu cha kupoteza endapo angemuacha Naomi lakini alisimama na mkwewe katika mazingira magumu sana ambo lililomletea sifa za kipekee na faraja kubwa sana hapo baadaye, simama na mama Mchungaji katikamhali zote iwe njema au mbaya usikubali kumuacha mama Mchungaji isipokuwa kama utaolewa na kuwa na majukumu yako mengine yanayokulazimu

 

Ruthu 1:16-18 “Naye Ruthu akasema, Usinisihi nikuache, Nirejee nisifuatane nawe; Maana wewe uendako nitakwenda, Na wewe ukaapo nitakaa. Watu wako watakuwa watu wangu, Na Mungu wako atakuwa Mungu wangu; Pale utakapokufa nitakufa nami, Na papo hapo nitazikwa; Bwana anitende vivyo na kuzidi, Ila kufa tu kutatutenga wewe nami.Basi alipomwona kuwa amekaza nia yake kufuatana naye, aliacha kusema naye.”       

 

Ufunuo 2:10 “Usiogope mambo yatakayokupata; tazama, huyo Ibilisi atawatupa baadhi yenu gerezani ili mjaribiwe, nanyi mtakuwa na dhiki siku kumi. Uwe mwaminifu hata kufa, nami nitakupa taji ya uzima.”  
           

Hitimisho:

Wafanyakazi wa ndani hasa katika nyumba za watumishi wa Mungu wameitwa kuwa mabalozi wa Baraka za Mungu, kwa Imani yao, mwenendo na tabia zao, kamwe hatuwatarajii wao kuwa sababu ya kusambaratika kwa huduma za wachungaji au kusababisha kero na ugomvi katika nyumba ya Mchungaji, haipendezi wao kuwa sababu ya dharau, na uchonganishi kati ya huduma ya Mchungaji na washirika wake, somo hili linatoa mwanga tu wa namna na jinsi iwapaswavyo kuishi kwaajili ya Mungu na wala si kwaajili yao, aidha na kuwaonyea ili kwamba waache kutumika kama chombo cha shetani na badala yake waweze kutumika kuiinua huduma ya kichungaji na kuiweka kwenye heshima inayostahili, ni imani yangu kuwa kama unafanya kazi katika nyumba za watumishi wa Mungu hutakata tamaa na kujidharau na kujifikiri kuwa huna maana nataka nikutie moyo ili ujue ya kuwa Mungu anakuzingatia sana anajua umuhimu wako katika kuitumikia familia ya mtumishi wake!


Wengi wa waliofanya kazi katika nyumba za watumishi wa Mungu kamwe Mungu hakuwahi kuwapuuzia kwani wengine alijifunua kwao na kuwabariki na wengine walimuona Mungu hata pale walipopita katiia changamoto ngumu Mungu aliwatokea


Wakati Sara alipomtendea vibaya Hajiri malaika wa Bwana hawakumuacha Hajiri na badala yake walimuelekeza njia sahihi ya kufanya na kuyalinda maisha yake na ya mtoto wake, Mungu hajawahi kuwadharau wajakazi na kuwaona kama watu wasio na maana na badala yake aliwahusisha katika Baraka zake alizozikudsudia sawa na nyumba za watumishi wake  


Mwanzo 16:6-11 “Naye Abramu akamwambia Sarai, Tazama, mjakazi wako yu mkononi mwako, mtendee lililo jema machoni pako. Sarai akamtesa, naye akakimbia kutoka mbele yake. Malaika wa BWANA akamwona kwenye chemchemi ya maji katika jangwa, chemchemi iliyoko katika njia ya kuendea Shuri. Akamwambia, Hajiri, wewe mjakazi wa Sarai, unatoka wapi, nawe unakwenda wapi? Akanena, Nakimbia mimi kutoka mbele ya bibi yangu Sarai. Malaika wa BWANA akamwambia, Rudi kwa bibi yako, ukanyenyekee chini ya mikono yake. Malaika wa BWANA akamwambia, Hakika nitauzidisha uzao wako, wala hautahesabika kwa jinsi utakavyokuwa mwingi.Malaika wa BWANA akamwambia, Tazama! Wewe una mimba, utazaa mwana wa kiume, nawe utamwita jina lake Ishmaeli, maana BWANA amesikia kilio cha mateso yako.”


1Timotheo 4:12 “Mtu awaye yote asiudharau ujana wako, bali uwe kielelezo kwao waaminio, katika usemi na mwenendo, na katika upendo na imani na usafi.”

               

Na. Rev. Innocent Samuel Kamote

 Mkuu wa wajenzi mwenye Hekima