Jumamosi, 4 Mei 2019

Imetupasa kumtii Mungu kuliko wanadamu!

Mstari wa Msingi:- Matendo 5:29Petro na mitume wakajibu, wakisema, Imetupasa kumtii Mungu kuliko wanadamu.”


Mstari wa Somo:- Kutoka 1:15-21Kisha mfalme wa Misri akasema na wazalisha wa Waebrania, mmoja jina lake aliitwa Shifra, na wa pili jina lake aliitwa Pua;  akasema, Wakati mwazalishapo wanawake wa Kiebrania na kuwaona wa katika kuzaa, ikiwa ni mtoto mwanamume, basi mwueni, bali ikiwa ni mtoto mwanamke, na aishi. Lakini wale wazalisha walikuwa wakimcha Mungu, wasifanye kama walivyoamriwa na huyo mfalme wa Misri, lakini wakawahifadhi hai wale wanaume. Basi mfalme wa Misri akawaita wale wazalisha na kuwauliza, Kwa nini kufanya jambo hili, na kuwahifadhi watoto waume wawe hai? Wazalisha wakamwambia Farao, Ni kwa sababu hao wanawake wa Kiebrania si kama wanawake wa Kimisri; kwa kuwa ni hodari hao, nao huzaa kabla mzalisha hajapata kuwafikilia. Basi Mungu akawatendea mema wale wazalisha; na hao watu wakaongezeka sana, wakaendelea na kuzidi kuwa na nguvu nyingi. Ilikuwa kwa sababu wale wazalisha walikuwa wakimcha Mungu, akawasimamishia nyumba.”


Utangulizi:


Ni muhimu kufahamu kuwa wako watu ambao wametajwa katika maandiko kwa ufupi sana lakini wanatufundisha somo pana sana lenye kuweza kutufaa katika nyakati zetu, Miongoni mwa watu hao ni Shiphrah na Puah ambao wanatufundisha mambo ya msingi katika kumpendeza Mungu, Leo tutachukua muda kujifunza kuwa wao ni nani na mambo muhimu ya kujifunza kutoka kwao:-

Shiphra na Puah ni nani?

Tofauti na Mashujaa wengine katika maandiko Shiphra na Puah wanatajwa kwa kifupi sana katika maandiko katika kitabu cha Kutoka 1:15-21, Hawa walikuwa wanawake waliookoa maisha ya wengi kabla ya kuzaliwa kwa Musa huko Misri, wanawake hawa walikuwa ni wakunga, (Wauguzi wanaohusika na kuzalisha wanawake wajawazito)

Wanatheolojia wanapata utata mkubwa sana kugundua asili ya Shiphrah na Puah kwamba walikuwa Waebrania au walikuwa Wamisri, hii ni kwa sababu Biblia ya kiyahudi inawaita wazalisha wa kiibrania “Hebrew Midwives” kwa kiibrania “ Meyaldot Haiviyot  Meyaldot Haiviyot” Wataalamu wa maandiko wa kiyahudi akiwemo Rabbi Abrabanel  ameweka wazi katika mawazo yake kuwa wanawake hao walikuwa wamisri isipokuwa waliokuwa wanamcha Mungu, kama wangekuwa waebrania neno Mcha Mungu lisingeliweza kutumika hapo, lakini neno hilo ndilo linalosaidia kujua kuwa wanawake hao walikuwa wamisri, kwa vile neno wacha Mungu mara nyingi lilitumika katika biblia kumaanisha mataifa waliomuamini au waliomcha Mungu wa waebrania, sasa swali linaweza kuja kwa nini waliitwa wazalisha wa kiibrania lugha hii inaweza kuwa na maana ya “Wakunga waliokuwa wakiwazalisha waebrania” na kwa sababu hiyo haikuwa na ulazima sana wao wenyewe wawe waebrania Kama hivyo ndivyo basi, Shiphra na Puah wanakuwa watu wa kwanza wasiokuwa waenrabia kuhatarisha maisha yao kwaajili ya Wayahudi. Msomi mmoja wa kiyahudi ambaye ni mwalimu mwenye kuheshimika sana ajulikanaye kama Nechama Leibowitaz  anasema kama wanawake hao walikuwa wamisri hapo ndipo somo hili linapokuwa tamu na kupata maana iliyo njema zaidi, na somo kuu tunajifunza kuwa mtu yeyote yule wa taifa lolote lile na jamii yeyote ile anaweza kusimama katika kweli linapokuja sala la kusimamia haki, bila kujali kuwa anatoka katika historia gani.


Ni wanawake waliompendeza Mungu.


Wanawake hawa mashujaa waliagizwa kwa amri ya mfalme katika Kutoka 1:15-17 “Kisha mfalme wa Misri akasema na wazalisha wa Waebrania, mmoja jina lake aliitwa Shifra, na wa pili jina lake aliitwa Pua; akasema, Wakati mwazalishapo wanawake wa Kiebrania na kuwaona wa katika kuzaa, ikiwa ni mtoto mwanamume, basi mwueni, bali ikiwa ni mtoto mwanamke, na aishi. Lakini wale wazalisha walikuwa wakimcha Mungu, wasifanye kama walivyoamriwa na huyo mfalme wa Misri, lakini wakawahifadhi hai wale wanaume.Unaona Maandiko yanasema wanawake wale walikuwa wacha Mungu na hivyo hawakufanya kama ilivyokuwa amri ya mfalme, wao kwa imani waliamua kumtii Mungu kuliko kuwatii wanadamu waliwatunza wayahudi bila kujalia amri ya mfalme jambo hili lilihatarisha sana maisha yao, zamani ilikuwa usipotii amri ya mfalme ilikuwa lazima uuawe, lakini wanwake hawa walisimama katika kweli walisimama katika haki na Mungu aliwatetea, Ziko nyakati katika maisha yetu ambazo tunatakiwa kuwa na msimamo thabiti kwamba heri ya lawama kuliko fedhea kuwa tayari kuhatarisha maisha yetu kwaajili ya utii wetu kwa Mungu, hili ni somo ambalo wanawake hao wanatufunza leo, walikuwa na ujasiri, hawakuogopa, walifanya yaliyo wajibu wao, sawa na Petro alivyojibu wakati baraza la wazee wa kiyahudi wakiwapiga marufuku wasihubiri injili, Petro alijibu kwa ujasiri “Imetupasa kumtii Mungu kuliko wanadamu

Somo kutoka kwa Shiphra na Puah


1.       Imetupasa kumtii Mungu kuliko wanadamu – wanawake hao walihatarisha maisha yao kwaajili ya kuikiuka amri ya mfalme kwa kweli walipaswa kukatwa shingo, lakini walikuwa tayari kupoteza kila kitu kwa sababu WALIKUWA WANAMCHA MUNGU tunajifunza kuwa kama tunamcha Mungu kama tunamuogopa Mungu tunaweza kusimama na kupingana na dhuluma na udhalilishaji wa aina yoyote ile bila kujali nini kitatukuta ila kwa sababu kubwa moja tu tunamcha Mungu.


2.       Walitamini umuhimu wa uhai na maisha - Bila kujali kuwa wanaozalishwa ni wamisri au wayahudi wanawake hawa walionyesha kuwa wanathamini uhai na kuwa wako tayari kutoa uhai kwaajili ya uhai, hawakuogopa waliwahurumia watoto hao wachanga walioma huruma jinsi ambavyo mama amebeba mimba miezi tisa na sasa anataka kuunganishwa na mwanaye na kitoto kipya kinakuja ulimwenguni bado hakujaunganishwa na mama yake, bila kujali ni wa aina gani ni wakabila gani uhai wa mwanadamu una thamani kuwa sana, wao walijua kuwa wameapa kuokoa uhai wa mwanadamu na hivyo walikuwa wana haki ya kuhakikisha kuwa wanafanya hivyo bila kujali nani ameagiza vitoto visivyo na hatia viuawe, siku nhizi watu hawathamini uhai unaweza kusikia watu wakiwaxchinja wake zao, au kuua vitoto na kuwachoma moto wezi kabla hata ya kuwafikisha katika vyombo vya kisheria kuua limekuwa jambo la kawaida tu Mithali 31:8-9 inasema “Fumbua kinywa chako kwa ajili yake aliye bubu; Uwatetee watu wote walioachwa peke yao; Fumbua kinywa chako, uhukumu kwa haki; Uwapatie maskini na wahitaji haki yao” Neno la Mungu linatutaka tuseme kwa aajili ya wale wasiosema, tuwatetee wasioweza kujitetea, tusimame katika haki na kuhakikisha kuwa masikini wanapata haki zao, Hii ndio kazi iliyofanywa na Shiphrah na Puah, walisimama kwa niaba ya wanyonge na masikini vitoto visivyoweza kujitetea, watu wengine kwa kuwa Mungu amekuweka katika mikono yake basi ndio utaipata fresh. 


3.       Mungu anaona Mawazo yetu na Matendo yetu – Hwa wanawake wakunga walikataa kutii amri ya mfalme wao muovu, na kutokukubalia kuuwa watoto wasio na hatia na Mungu aliona na kuwabariki, Sio tu kuwa mungu aliona matendo yao hapa lakini pia aliisoma nia yao namawazo yao, Zaburi 139:1-4 “Ee Bwana, umenichunguza na kunijua. Wewe wajua kuketi kwangu na kuondoka kwangu; Umelifahamu wazo langu tokea mbali. Umepepeta kwenda kwangu na kulala kwangu, Umeelewa na njia zangu zote.  Maana hamna neno ulimini mwangu Usilolijua kabisa, Bwana.” Kumbe Mungu anaona na anayajua mawazo yetu anatufahamu kwa undani zaidi hakuna cha kujificha katika mawazo yetu wala katika ulimi wetu, hivyo ni muhimu katika maisha yetu kuishi maisha ya kupendeza yeye popote tulipo na kisimama upande wake hata kama lile tunalolisimamia litahatarisha maisha yetu, hatuna budi kuisimiamia kwaajili ya Mungu.


4.       Lazima tusimame na Israel. – Shiphra na Puah hawakuwa Wayahudi, lakini waliwahudumia waliwalinda na kutokana na matendo yao mema Mungu aliwabariki aliwasimamishia nyumba , walipate neema waliolewa, walikuwa na familia nzuri. Walibarikiwa, Bilia ina ahadi nyingi kuhusu kusimama na Israel, Bila kujali wewe ni mtu wa namna gani, ni wa asili ipi ni wa imani ipi linapokuja swala la mtu anataka kuiharibu Israel simama na Israel simama na watu wa Mungu, hata siku moja usithubutu kuwashutumu na kuwazomea na kuwalaani


Mwanzo 12: 1-3 “BWANA akamwambia Abramu, Toka wewe katika nchi yako, na jamaa zako, na nyumba ya baba yako, uende mpaka nchi nitakayokuonyesha; nami nitakufanya wewe kuwa taifa kubwa, na kukubariki, na kulikuza jina lako; nawe uwe baraka; nami nitawabariki wakubarikio, naye akulaaniye nitamlaani; na katika wewe jamaa zote za dunia watabarikiwa.”

Isaya 62:1 “Kwa ajili ya Sayuni sitanyamaza, na kwa ajili ya Yerusalemu sitatulia, hata haki yake itakapotokea kama mwangaza, na wokovu wake kama taa iwakayo.”

Isaya 62:6-7 “Nimeweka walinzi juu ya kuta zako, Ee Yerusalemu; hawatanyamaza mchana wala usiku; ninyi wenye kumkumbusha Bwana, msiwe na kimya;  wala msimwache akae kimya, mpaka atakapoufanya imara Yerusalemu, na kuufanya kuwa sifa duniani.”

Zaburi 122:6 “Utakieni Yerusalemu amani; Na wafanikiwe wakupendao;

Warumi 15:27 “Naam, imewapendeza, tena wamekuwa wadeni wao. Kwa maana ikiwa Mataifa wameyashiriki mambo yao ya roho, imewabidi kuwahudumu kwa mambo yao ya mwili.

Shiphrah na Puah walisimam na wayahudi na wakabarikiwa, kila taifa linapaswa kuwa na uelewa na kujifunza na kufahamu kuwa mataifa mengi yaliyobarikiwa na Mungu na watu wengi waliofanikiwa sana ni wale wanaosimama na Israel, viongozi wa taifa letu ni lazima wahakikishe kuwa linapokuja swala la Israel kama huna cha kusema ni afadhali kunyamaza kimya, kuna uhusiano mkubwa wa Baraka za watu wote Duniani na mataifa yote Duniani kubarikiwa kutokana na msimamo wako katika Israel, Marekani na mataifa mengine makubwa yanaifahamu siri hii na ndio maana unawaona kama wanaojipendekeza kwa wayahudi, Kupitia wanawake wale wakunga waliosiamama na Waisrael nataka kumuonya kila mtu kuhakikisha kuwa katika maisha yake ili kuzivuta Baraka waza mema na watakie heri Israel waombee amani, fanya amani nao na utaona Baraka alizoahidiwa Ibrahimu zikimiminika katika maisha yako Shipra na pua walifanya hivyo walisimama na Israel licha ya kuwa wao hawakuwa waebrania.

I stand with Israel forever
Rev. Innocent Kamote
Mkuu wa wajenzi mwenye Hekima.

Jumatatu, 29 Aprili 2019

Imekwisha !



Yohana 19:28-30Baada ya hayo Yesu, hali akijua ya kuwa yote yamekwisha kumalizika ili andiko litimizwe, akasema, Naona kiu. Kulikuwako huko chombo kimejaa siki; basi wakatia sifongo iliyojaa siki juu ya ufito wa hisopo, wakampelekea kinywani.  Basi Yesu alipokwisha kuipokea ile siki, alisema, IMEKWISHA. Akainama kichwa, akaisalimu roho yake.


Utangulizi:
Mojawapo kati ya usemi wenye maana sana kati ya semi saba za Yesu alizozisema akiwa msalabani na ambazo zinatajwa katika sehemu mbalimbali za injili, moja ya usemi huo wa muhimu ni usemi wa sita wenye Neno IMEKWISHA  ambalo leo katika siku ya pasaka tutachukua muda kulijadili kwa undani na kupata maana iliyokusudiwa, maneno mengine kati ya maneno saba aliyoyasema Yesu msalabani ni pamoja na:-
·         Baba uwasamehe kwa maana hawajui walitendalo Luka 23:34
·         Amin nakuambia leo hii utakuwa pamoja nani peponi Luka 23:43
·         Mama tazama mwanao, mwana tazama mama yako Yohana 19:26-27
·         Mungu wangu Mungu wangu mbona umeniacha Mathayo 27:46
·         Nina kiu Yohana 19:28
·         Imekwisha Yohana 19:30
·         Baba mikononi mwako naiweka roho yangu Luka 23:46
Maana ya neno IMEKWISHA
Ni muhimu kufahamu kuwa Neno IMEKWISHA ambalo katika kiingereza kiingereza linasomeka “IT IS FINISHED  katika Biblia ya kiyunani yaani Kigiriki linasomeka kama “TETELESTAI  Neno hili ndio neno la Mwisho kabisa katika maneno aliyoyatamka Yesu pale msalabani kabla ya kutamka neno “Baba mikononi mwako naiweka roho yangu” na kufariki dunia pale msalabani, Neno hili Imekwisha TETELESTAI limetokana na neno TELEO la kiyunani ambalo maana yake ni Kukamilisha kazi, kumaliza kazi, kutimiza kazi, to complete or to accomplish, neno hili lina umuhimu mkubwa kwa sababu linazungumzia kumaliza kazi kwa furaha, au kwa mafanikio, utamu wa neno hili ni kama vile mtu anapokuwa amemaliza mtihani wa mwisho katika kozi ya mwisho, au mtihani wa mwisho kabisa wa kumaliza shule au chuo au kama vile mtu aliyekamilisha malipo ya mwisho ya ununuzi wa nyumba au gari, (Paid in Full) au kukamilisha kwa usahihi kile ulichowaza au kufikiri kuwa utakifanya na ukakifanya kwa usahihi kabisa, Kama vile Mungu alivyosema tazama kila kitu kimekuwa chema, well done, kazi imefanyika kwa ufasaha.

Lakini ni muhimu kufahamu kuwa neno hili IMEKWISHA liko katika wakati uliopita kwa namna linavyoonekana hapa  lakini katika kiyunani ni sentensi kamili Perfect tense na kwa sababu hiyo neno hili linapata umuhimu mkubwa kwa sababu lina maanisha imekwisha katika wakati uliopita, uliopo na ujao kwa msingi huo neno hili linaendelea kufanya kazi kila siku na kila wakati, Neno hili pia lilimaanisha kuwa kama kulikuwa na deni, basi deni hilo limelipwa milele, wale wamuaminio Yesu hawana wanachodaiwa, kama ilikuwa ni kesi imefutwa na hati za mashitaka zimeharibiwa kabisa Wakolosai 2:14-15 akiisha kuifuta ile hati iliyoandikwa ya kutushitaki kwa hukumu zake, iliyokuwa na uadui kwetu; akaiondoa isiwepo tena, akaigongomea msalabani; akiisha kuzivua enzi na mamlaka, na kuzifanya kuwa mkogo kwa ujasiri, akizishangilia katika msalaba huo”.Neno hili ni kama kupewa ruhusa kutoka hospitalini baada ya kuugua kwa muda na kulazwa katika chumba cha wagonjwa mahututi kila mtu akijua umekwisha kisha ukainuka tena ukiwa mzima wa afya. Ni neno muhimu sana katika kazi ya ukombozi wa mwanadamu na wokovu wetu.

Umuhimu wa neno IMEKWISHA.

Yesu alipolia kwa sauti kuu IMEKWISHA alimaanisha katika wakati uliopita, sasa na itaendelea kuwa imekwisha hata baadaye. Kumbuka kuwa hakusema nimekwisha hii ingemaanisha kuwa ameshindwa na kifo, lakini alilia akisema IMEKWISHA! maana yake nimeikamilisha kwa ufasaha kazi niliyokuja kuifanya. Kwa msingi huo neno imekwisha lina maana ya hakuna kilichosazwa katika kazi ya ukombozi aliyokuja kuifanya na hivyo alikuwa akizungumza ukweli kuwa kila kitu kimekamilishwa sasa ni mambo gani Yesu aliyakamilisha yako mengi mno lakini baadhi ni pamoja na:-
1.       Alikamilisha kazi yote aliyokuwa ametumwa na baba yake kuja kuifanya duniani Yohana 17:4 “Mimi nimekutukuza duniani, hali nimeimaliza kazi ile uliyonipa niifanye.

2.       Alikamilisha kazi ya kuja kutafuta na kuokoa kile kilichopotea Luka 19:10 “Kwa kuwa Mwana wa Adamu alikuja kutafuta na kuokoa kile kilichopotea.”

3.       Alikamilisha kazi ya kutukomboa sisi na adui zetu Luka 1:68-74 “Atukuzwe Bwana, Mungu wa Israeli, Kwa kuwa amewajia watu wake, na kuwakomboa. Ametusimamishia pembe ya wokovu Katika mlango wa Daudi, mtumishi wake. Kama alivyosema tangu mwanzo Kwa kinywa cha manabii wake watakatifu; Tuokolewe na adui zetu Na mikononi mwao wote wanaotuchukia; Ili kuwatendea rehema baba zetu, Na kulikumbuka agano lake takatifu; Uapo aliomwapia Ibrahimu, baba yetu, Ya kwamba atatujalia sisi, Tuokoke mikononi mwa adui zetu, Na kumwabudu pasipo hofu,

4.       Alikamilisha unabii katika torati na manabii uliozungumza kumuhusu yeye kwa unabii, ishara, alama na vivuli kuhusu ujio wake na kazi zake kutoka kitabu cha Mwanzo mpaka kitabu cha Malaki ambako kuna nabii zaidi ya 300 kuhusu Masihi Mwanzo 3:15 na Isaya 53

Kwa msingi huo hatupaswi tena kuteseka, kuwa watumwa, kukandamizwa, kuonewa, kuugua na kuteswa na magonjwa, kuwa watumwa wa dhambi na shetani, hatupaswi kumuogopa awaye yote, Nguvu za giza, na wachawi na washirikina na waganga, na mapepo na majini na mashetani na shetani hazina uwezo juu yetu kwa imani katika kazi aliyoifanya Bwana Yesu pale msalabani, laana ya torati, na sheria, hatuna deni, hatuna deni la jana wala la leo wala la kesho kazi imekamilika yakikutokea majanga angalia msalaba kumbuka kazi iliyofanyika msalabani, kumbuka kuwa mwanaume huyu amemaliza amakamilisha kazi ya ukombozi huna hatia hata kidogo hakuna wa kukuhukumu, wewe hata kama ulikuwa na historia mbaya sana yeye anawweza kuifuta na kuiandika upya endapo utamwamini Bwan Yesu, Neno imekwisha ni neno lenye nguvu kama vile siku unapotangazwa uhuru wa taifa lililotawaliwa na wakoloni, tunapoadhimisha siku ya kufa na kufufuka kwa Yesu Kristo yaani katika siku hii ya pasaka ni lazima tujikumbushe kuwa Yesu amekamilisha kazi ya kutuweka huru na kuvitangazia vifungo vinavyotuzunguka kwa kuvitangazia kuwa imekwisha, Mateso yamekwisha, kazi za shetani zimekwisha, majini na mapepo kazi zao zimekwisha kila aina ya vifungo na utumwa wa ibilisi ni lazima zisikie na kukumbuka kuwa imekwisha

Rev. Innocent Kamote

Mkuu wa wajenzi mwenye Hekima!

Wamisri wakatuonea, wakatutesa, !


Kumbukumbu la torati 26:6-9 “Wamisri wakatuonea, wakatutesa, wakatutumikisha utumwa mzito.  Tukamlilia Bwana, Mungu wa baba zetu; Bwana akasikia sauti yetu, akaona na taabu yetu, na kazi yetu, na kuonewa kwetu.  Bwana akatutoa kutoka Misri kwa mkono wa nguvu, na kwa mkono ulionyoshwa, na kwa utisho mwingi, na kwa ishara, na kwa maajabu; naye ametuingiza mahali hapa, na kutupa nchi hii, nchi ijaayo maziwa na asali.”

 Sinagogi la Kiyahudi huko San Diego, lililoshambuliwa kwa Risasi 28/04/2019

Utangulizi:
Jana tarehe 28 April 2019  sawa na mwezi Nisan 23 5779 kwa kalenda ya kiyahudi, nilipata habari ya kuuawa kwa Myahudi mmoja kutokana na shambulio la risasi lililofanyika huko San Diego katika mojawapo ya sinagogi la kiyahudi, na wengine watatu kujeruhiwa vibaya, nilikuwa bado sijasahau tukio la kuuawa kwa wakristo wakati wa Pasaka Nchini Sri-lanka nikafikiri na kuwaza kwamba bado dunia ya leo iliyoendelea kuna watu bado wanafikiri wanaweza kuwepo duniani peke yao bila kuchanganyika na watu wanaotofautiana nao kimawazo kifikira kiitikadi na kiimani? Dunia inapaswa kutafakari kwa kina kuhusu ukomavu na uwezo wa kuchukuliana katika jamii na kupendana bila kujali tofauti zetu,
Biblia inasema katika 1Yohana 4:8Yeye asiyependa, hakumjua Mungu, kwa maana Mungu ni upendo.” Hii ni wazi kuwa bado dunia haijamjua Mungu, na kuwa jamii inapaswa kukumbuka na kuhimiza na kufundisha kuhusu upendo, ni muhimu kufanya kilalinalowezekana kuing’oa chuki miongoni mwa wakazi wa dunia, na kukumbuka kuwa Yesu hakuwa mjinga alipokuwa akifundisha Upendo, alikuwa anajua wazi kuwa dunia itakuja kufikia na kuwa na matukio haya tunayoyashuhudia leo katika jamii iliyoendelea.
Katika kifungu cha maandiko ya msingi, Musa alikuwa anawakumbusha wana wa Israel sheria za Mungu na hususani kwa kizazi kipya ambao wengi waoa walizaliwa Jangwani au na wale waliotoka Misri wakiwa vijana na waliokuwa wadogo, Musa alikuwa akizungmzia kumtolea Mungu sadaka za shukurani watakazomtolea Mungu watakapokuwa katika nchi ya amani nchi iliyojaa maziwa na asali nchi ya Israel aliwalekeza kwamba watakapotoa wamkumbushe Mungu kuwa walionewa huko Misri, lakini walipomlilia Mungu akawaokoa na kuwaleta katika inchi hii iliyojaa maziwa na asali
Katika kifungu hiki Kumbukumbu la Torati 26:6 ““Wamisri wakatuonea, wakatutesa, wakatutumikisha utumwa mzito. .”
Biblia ya kiingereza  NIV inasomeka hivi Deuteronomy 26:6But the Egyptians mistreated us and made us suffer, subjecting us to harsh labor.”
Biblia ya Kiyahudi iitwayo (The Israel Bible) inasomeka hivi Deuteronomy 26:6The Egyptians DEALT HARSHLY WITH US and oppressed us; they imposed heavy labor upon us.”
Musa aliwakumbusha Jambo hili la msingi walikumbuke watakapokuwa wakiabudu, kwa sadaka ya shukurani, wamkumbushe Mungu kuwa walitendwa vibaya na wamisri neno kuonewa, kuteswa na kutendwa vibaya katika lugha ya Kiebrania linatumika neno “VAYAREIU”  likimaanisha kuwa lakini rafiki zetu walitugeuka,walitutenda mabaya, wakatuonea, wakatutesa, wakatudhulumu kisha wakatugeuza  kuwa watumwa kwa utumwa mbaya na mzito” Hii ilimaanisha kuwa Israel hawakushuka Misri wakiwa watumwa walikuwa rafiki wa wamisri, walikuwa wapendwa, walikuwa jamaa na ndugu wa waisrael, lakini hatimaye ukafika wakati wakawageuka, wakavunja urafiki, wakaanza kuwabagua na kutengeneza sheria za kuwabana, na kuwaonea na kuwatesa na kuwakandamiza na hatimaye kuwafanya watumwa wao, Ndipo ulipofika wakati wayahudi wakamlilia Mungu awatoe katika utumwa ule mzito na Mungu akawaokoa akawapeleka katika nchi ya ahadi, ambako huko npekee ndipo mahali ambapo Wayahudi watakuwa salama na wakamfurahia Mungu.
Leo hii sio Misri tu ambao wamewakaribisha Wayahudi kisha wakawaonea baadaye, ziko nchi nyingi tu ambazo zimewapokea wayahudi wakiwa kama marafiki, kama ilivyotokea Ujerumani na Uganda, lakini baadaye katika namna isiyoweza kueleweka watu hao waliwageuka nakuwaona wayahudi kama adui na watu wasiofaa, ili mtahudi aweze kuwa salama ni lazima popote pale walipo warudi katika nchi yao ya asili nchi yao ya ahadi ili wamuabudu Mungu pasipo hofu na watoe sadaka ya shukurani na mateso yao yote yatageuka kuwa historia
Wako watu wengi sana leo wanateseka lakini chanzo cha mateso yao hakikuwa chuki na majuto na dhuluma ambazo wanaziona sasa, inawezekana wewe ni House girl ulichukuliwa kama dada wa kazi kwa nia nzuri, ukaenda mjini kama rafiki na ndugu, na ukapokelewa vema huko ulikokwenda mama na baba wa nyuma uliyofikia walikataa kuitwa anko walisema utuite mama au baba, lakini baada ya siku kadhaa hali ilibadilika umeanza kuitwa hili, limbwa, paka , nyau. Fala na kadhalika.

Inawezekana ulioa au kuolewa kwa nia nzuri kabisa, wakati unachumbiwa ulikuwa ni rafiki, hukuwa mtumwa mliitana majina mazuri, sweetie, asali wangu, maua, dear, dally na kadhalika lakini hapa unaposoma ujumbe huu mambo yamegeuka wewe sasa ni jibwa, fala, lione, liangalie, sijui nililioa la nini, mlango wa nane, balaa nuksi, mwiba na kadhalika.
Inawezekana wakati uaajiliwa ulikaribishwa kwa furaha, bosi aliwataka wenyeji wakupe saada mkubwa utakaouhitaji, ulidekezwa, ulifanywa kama moja ya wamiliki wa kampuni, ulikuwa ni wakati wa furaha umepata kazi mpya, lakini baada ya sikukadhaa, Mambo yamebadilika, unaonekana kama mzigo, unateseka, unapelekeshwa unaonekana hifai tena.
Kila mahali walikokwenda Wayahudi walikaribishwa walipokelewa kwa ukarimu lakini leo watu wanawalipua, wanawapiga risasi, kama majambazi au watu wasiofaa, huko san diego wayahudi wameuawa katika sabato ya kwanza ya Pasaka walipokuwa katika ibada na mama mmoja mwenye miaka 60 alifariki na wengine watatu kujeruhiwa vibaya, mmoja akiwa kiongozi wa kidini Rabbi na mkuu wa sinagogi husika kinawafanya wengine wawe na chuki dhidi ya wengine, kwa nini wakristo wameuawa Srilanka na kwa nini waqyahudi wameshambuliwa nani atawasemea
Hujawahi kuona unakaribishwa mahali vizuri, unapeewa na ofisi, unasifiwa kila mahali unahesabika kama mtu mwema kisha baada ya muda wewe ndio unaonekana kama mwiba wa kila mmoja pale ulipo?
Hali hii ndio inayowatokea Israel Duniani kote, ndio inayoatokea Wakristo, watu wanaona kuwa ni haki kuvaa mabomu na kuwalipua
Iko siri moja kubwa na ya kipekee, ni kukaa katika ahadi za Mungu tu, Ili Israel iweze kuwa salama hawana budi kuungana na kukaa Israel pekee ili wajilinde wakae katika nchi ya ahadi waliyoahidiwa baba zao Ibrahimu Isaka na Yakobo ndio wanaweza kujithibitishia usalama wao.
Wako watu wengi leoa hawako salama kwa sababu walifanya urafiki na shetani, walipokelewa na shetani , ibilisi kwa furaha sana wakiwa kama marafiki, Lakini kumbuka kuwa shetani hana urafiki na mtu awaye yote lazima atakugeuka tu atakutesa atakugeuza kuwa mtumwa na atakudhulumu, shetani anataka ufanye mambo kwa faida yake na maslahi yake hakuna mafanikio ya kweli kwa shetani, ili uwe salama huna budi kurudi kwa Yesu kristo na kujificha kwake, yeye ndio nchi halisi ya ahadi na kwake kuna usalama, Kwa ibilisi haijalishi kuwa wewe ni mwenye haki au la kwake nifuraha kubwa ukiangamia yeye na watu wake hawatajali haki yako, wakati umefika wa wewe kukaa katika uwepo wa Mungu kwa usalama wako, ili amani ipatikane katika ndoa yako hakikisheni mnamkaribisha Mungu na kujifunza upendo kama yeye alivyoagiza.
Isaya 5:1 Mwenye haki hupotea, wala hakuna atiaye hayo moyoni; na watu watauwa huondolewa, wala hakuna afikiriye ya kuwa mwenye haki ameondolewa asipatikane na mabaya
Hakuna wanaojali kile kinachowapata wayahudi leo. Lakini Palestina ikiguswa tu dunia itapiga kelele hata kama wakati mwingine wao ndio wachokozi na ndio wanaoanzisha kurusha maroketi, Israel ikijibu kama sehemu na wajibu wa kujihami na kujilinda, Israel ikijilipizia kisasi kwa adui zake dunia inapiga kelele je wadhani Wayahudi sio watu, nani atawapigia kelele na kuielimsha jamii duniani kuwa nao wanastahili kutetewa na kuangaliwa kwa maslahi yao duniani, Mimi sisemi kwa sababu nina asili ya Kiebrania tu hapana bali nataka haki itetendeke duniani ifikie hatua tujifunze pendo lake Yesu na kuielimisha katika jamii yetu, kila mmoja anapaswa kujua kuwa kama tunampenda Mungu tutathamini uhai wa watu wake kuliko imani zetu, Dunia pia inapaswa kuelewa kuwa ili Israel iweze kuwa salama  nilazima waelekee katika nchi ya ahadi na kukaa katika taifa lao wenyewe, ili sisi nasi tuweze kuwa salama turudi katika uwepo wa Mungu. Tutafanikiwa. Israel walimlilia Mungu, akawasikia akaziona taabu zao na kuonewa kwao aakawaokoa kwa mkono wa nguvu ulionyooshwa na wakajiliwa na kipindi cha neema  I stand with Israel.”
Rev. Innocent Kamote.
Mkuu wa wajenzi mwenye hekima