Jumatatu, 25 Aprili 2022

Yesu anaposimama katikati!


Yohana 20:19-23 “Ikawa jioni, siku ile ya kwanza ya juma, pale walipokuwapo wanafunzi, milango imefungwa kwa hofu ya Wayahudi; akaja Yesu, akasimama katikati, akawaambia, Amani iwe kwenu. Naye akiisha kusema hayo, akawaonyesha mikono yake na ubavu wake. Basi wale wanafunzi wakafurahi walipomwona Bwana. Basi Yesu akawaambia tena, Amani iwe kwenu; kama Baba alivyonituma mimi, mimi nami nawapeleka ninyi. Naye akiisha kusema hayo, akawavuvia, akawaambia, Pokeeni Roho Mtakatifu. Wo wote mtakaowaondolea dhambi, wameondolewa; na wo wote mtakaowafungia dhambi, wamefungiwa.”


Utangulizi:

Ni muhimu kufahamu kuwa katika ubinadamu wetu, mara kadhaa tunaweza kuwa na wakati wa amani na vilevile tunaweza kuwa na wakati, tukapoteza amani na kuwa na mashaka kutokana na majaribu ya aina mbalimbali na changamoto za aina mbalimbali tunazokutana nazo, wakati mwingine tunaweza kujawa na hofu na mashaka hata kufikia kiwango cha kujifungia, kwa woga na hofu huku tukiwa hatujui hatima yetu, ni katika hali ya namna kama hiyo wanafunzi wa Yesu Kristo walikuwa na wakati mgumu sana wakati Yesu alipokamatwa na kuteswa kwa kusulubiwa na kufa na kuzikwa, kulikuwa na hali ya mashaka makubwa mno, huku taarifa za kufufuka kwake zikiwa bado hazijathibitika kwa uwazi kwa wanafunzi wote, lakini vilevile Bado kulikuwa na wasiwasi kama wayahudi watawaacha salama wanafunzi ama walianza na Kristo kisha wamalizie kundi lake hivyo walipoteza matumaini kabisa! Na kukata tamaa! Wakiwa katika hali kama hiyo maandiko yanasema Yesu akasimama katikati yao!, kumbe Yesu anaposimama katikati hali inakuwa tofauti, huyu ni Yesu aliyefufuka mara baada ya kusulubiwa na kufa na kuzikwa:-

o   Yesu akisimama katikati mahali ambapo watu wamepoteza tumaini, matumaini yanarejea

o   Yesu akisimama katikati mahali penye hofu hofu inaondoka

o   Yesu akisimama katikati mahali ambapo watu wamepoteza amani, amani inarejea

o   Yesu akisimama katikati mahali penye changamoto za aina mbalimbali, changamoto hizo zinatoweka

o   Yesu akisimama katikati wakati watu wanapopata shida na kuingilia kati, shida hizo zinaondoka

o   Yesu akisimama katikati anabadilisha hali ya mashaka na kuyaondoa kabisa, kwanini Yesu husimama katikati ni  kwa sababu anajali na kuguswa sana na mahitaji yetu:-

Maandiko yanasema na tumtwike yeye fadhaa zetu zote maana yeye hujishughulisha sana na mambo yetu,

1Petro 5:7” huku mkimtwika yeye fadhaa zenu zote, kwa maana yeye hujishughulisha sana kwa mambo yenu.”


Ni muhimu kukumbuka hili ya kuwa Mungu wetu ni Mungu muelewa sana wakati mambo yanapoonekana kuwa ni yenye kuvunja moyo, yeye husimama katikati na kubadilisha hali ya hewa, Tuna Mungu anayejali, na mambo huwa tofauti wakati wote anapojitokeza,  wakati wa pasaka unapoadhimisha kufufuka kwa Yesu ni vema ukakumbuka kuwa Yesu aliyefufuka ni wa tofauti yeye anauwezo wa kuibuka katikati ya shida yako na kuyafanya mambo kuwa tofauti, Krito alipokuwa katika mwili alikuwa na tabia hiyohiyo ya kuingilia kati na kubadili hali ya hewa pale mambo yanapoharibika kwa wanadamu, Yesu anauwezo wa kubadilisha Msiba kuwa furaha, anauwezo wa kuhahirisha mazishi na kurudisha furaha na amani iliyopotea ona:-

Luka 7:11-16 “Baadaye kidogo alikwenda mpaka mji mmoja uitwao Naini, na wanafunzi wake walifuatana naye pamoja na mkutano mkubwa. Na alipolikaribia lango la mji, hapo palikuwa na maiti anachukuliwa nje, ni mwana pekee wa mamaye ambaye ni mjane, na watu wa mjini wengi walikuwa pamoja naye. Bwana alipomwona alimwonea huruma, akamwambia, Usilie. Akakaribia, akaligusa jeneza; wale waliokuwa wakilichukua wakasimama. Akasema, Kijana, nakuambia, Inuka. Yule maiti akainuka, akaketi, akaanza kusema. Akampa mama yake. Hofu ikawashika wote, wakamtukuza Mungu, wakisema, Nabii mkuu ametokea kwetu; na, Mungu amewaangalia watu wake.”

Yesu anauwezo wa kutuliza dhoruba ya aina yoyote itakayojitokeza katika maisha yetu na kutuondolea wasiwasi

Marko 4:36-41 “Wakauacha mkutano, wakamchukua vile vile alivyo katika chombo. Na vyombo vingine vilikuwako pamoja naye. Ikatokea dhoruba kuu ya upepo, mawimbi yakakipiga chombo hata kikaanza kujaa maji. Naye mwenyewe alikuwapo katika shetri, amelala juu ya mto; wakamwamsha, wakamwambia, Mwalimu, si kitu kwako kuwa tunaangamia? Akaamka, akaukemea upepo, akaiambia bahari, Nyamaza, utulie. Upepo ukakoma, kukawa shwari kuu. Akawaambia, Mbona mmekuwa waoga? Hamna imani bado? Wakaingiwa na hofu kuu, wakaambiana, Ni nani huyu, basi, hata upepo na bahari humtii?

Yesu aliweza kuyafanya hao alipokuwa katika hali yake ya kawaida ya mwilini hapa duniani tena akiwa na mipaka katika Israel, Lakini Yesu aliyefufuka hana mipaka na haitaji mlango ufunguliwe yeye anauwezo wa kuingilia kati mahali popote pale na kufanya lolote lile iwe mashariki au magharibi, kasikazini au kusini yeye anaposimama katikati hubadilisha hali ya mambo:-

Yesu anaposimama katikati ya hali Fulani yeye anafanya nini kuna mambo ya kujifunza kutoka katika kifungu hiki

1.       Anaonyesha Makovu, unajua kwanini Yesu huonyesha makovu,? Mimi ninalo kovu Fulani katika mkono wangu wa kushoto ambalo nililipata Tarehe 01/05/2000 kule Dodoma nilipokuwa naelekea chuo cha biblia, nilivamiwa na majambaza zaidi ya nane na wakanikaba na kuniumiza kisha wakapora kila nilichokuwa nacho wakati huo nilipopoteza fahamu kwaajili ya uvamizi ule, kila ninapoliona lile kovu nakumbuka tukio lile na ninakumbuka namna Mungu alivyoniokoa na mauti, lakini kama Haitoshi Tarehe 01/05/2015 Binti yangu wa kwanza Irene alizaliwa hivyo kwenye Tarehe ile ambayo nilipaswa kukumbuka tukio baya sasa ninakumbuka tukio zuri la kuzaliwa kwa binti yangu, kovu lile limekuwa historia, Yesu aliwaonyesha makovu yake wanafunzi wake ili kwamba wajue kuwa mateso yake yamebaki historia tu, Yesu amefufuka yu hai haijalishi aliumizwa kwa kiwango gani,

 

Yohana 20:20 “Naye akiisha kusema hayo, akawaonyesha mikono yake na ubavu wake. Basi wale wanafunzi wakafurahi walipomwona Bwana.”

 

Mungu anajua hali unayoipitia na Yesu aliyefufuka anakuthibitishia kuwa hali unayoipitia itakuwa historia tu, Mungu atakufanyia muujiza mkubwa wa kupita kawaida kinyume kabisa na matarajio ya maadui zako, watuoenee wanavyoweza kutuonea, watutese wanavyoweza kututesa lakini hali yeyote unayoipitia sasa itakuwa Historia tu unaweza usiwe na majeraha na makovukatika mwili wako lakini unaweza kuwa na majeraha na makovu makubwa katika moyo wako, Yesu alityefufuka anapoonyesha makovu namaanisha mashaka yako na mateso yako na majeraha yako atayabadili kuwa historian a wewe utakuwa na kiwango kingine tunapoadhimisha kufufuka kwa Yesu tukumbuke pia kuwa atatuonyesha makovu yake nah ii ni sihara ya kuwa mauti na mateso na majeraha yetu yatabakia kuwa historia tu!.

 

2.       Anatangaza Amani, Ni muhimu kufahamu kuwa Mstari wa 19 na wa 21 Yesu anasema Amani iwe kwenu, hawa walikuwa wamepoteza amani, walikuwa na fadhaa, walikuwa na woga, walikuwa na hofu, Yesu alikuwa amewaambia mapema kuwa anawapa amani  na akarudia tena amani iwe kwenu!, kwa nini alifanya alitangaza vile ni kwa sababu alikuwa anataka kuwaondolea haki ya kuchanganyikiwa na hali ya hofu na woga ambao uliwaondolea amani, kumbuka amani hii ni maalumu kutoka kwa Mungu

 

Yohana 14:27 “Amani nawaachieni; amani yangu nawapa; niwapavyo mimi sivyo kama ulimwengu utoavyo. Msifadhaike mioyoni mwenu, wala msiwe na woga.”

 

Amani itokayo kwa Mungu ni zawadi ni tofauti na amani ya dunia hii neno la kiebrania alilolitumia Yesu ni Shalom! Au Irene kwa kiyunani ambayo ni amani ya kipekee itokayo kwa Mungu, amani hii huilinda mioyo yetu kwa kiwango cha hali ya juu Paulo mtume anaiita amani hii kuwa inapita akili za kibinadamu amani hii inauwezo wa kutulinda na kutuhifadhi!

 

Wafilipi 4:6-7 “Msijisumbue kwa neno lo lote; bali katika kila neno kwa kusali na kuomba, pamoja na kushukuru, haja zenu na zijulikane na Mungu. Na amani ya Mungu, ipitayo akili zote, itawahifadhi mioyo yenu na nia zenu katika Kristo Yesu.

 

Amani ipitayo akili zote itatuhifadhi hii ni amani inayotumika kuhifadhi na kuilinda mioyo yetu isijeruhiwe hali yoyote ya kuchanganyikiwa na kutokuelewa kwamba hali itakuwaje hali hiyo na hofu hiyo inaondolewa na Yesu Kristo aliyefufuka, wanafunzi walikuwa wamejifungia na hawajui itakuwaje, walikuwa wamechanganyikiwa na hali ngumu ya kuuawa kwa Mwalimu wao kupitia mateso mazito lakini zaidi na habari tata ya kwamba Yesu yuko hai au la au mwili wake umeibiwa je amefufuka kwelikweli au hali ikoje? Kusimama katikati kwa Yesu kristo na kuwatangazia amani kuliondoa mashaka yote, Yesu atatuondolea mashaka yote yanayotukabili maishani.

 

3.       Yesu anatupa Mamlaka, Yohana 20:22-23 “Naye akiisha kusema hayo, akawavuvia, akawaambia, Pokeeni Roho Mtakatifu. Wo wote mtakaowaondolea dhambi, wameondolewa; na wo wote mtakaowafungia dhambi, wamefungiwa”.

 


Yesu anapoingilia kati anatupa mamlaka kupitia Roho wake Mtakatifu tunakuwa mawakili wa siri za Mungu kiasi ambacho tunaweza kuwapa watu mbingu au kuwanyima, kuruhusu wasamehewe dhambi au wasisamehewe, ni Roho Mtakatifu aliyekuja kubadilisha maisha ya watu kama Petro ambaye alitoka kumkana Yesu mara tatu siku chache zilizopita sasa ni jambo la kustaabisha kuwa anapewa mamlaka miongoni mwa waliopewa mamlaka na uweza na nguvu za Roho Mtakatifu, Roho Mtakatifu anatupa maisha ya ushindi na ujasiri anatupa kujiamini na uweza na mamlaka ya kutenda mambo makubwa na ya ajabu ni yeye atakayetupa ushindi katika siku zote za maisha yetu!

 

Ni muhimu kufahamu kuwa Yesu anaposimama katikati, hofu zetu, katikati ya mashaka yetu, katikati ya changamoto zetu, katikati ya mateso yetu, katikati ya shida zetu, katikati ya vifungo vyetu, katikati ya mashaka yetu, katikati ya masomo yetu katikati ya jambo lolote lile maombi yetu yanajibiwa na kupata ufumbuzi lolote lile majibu ya maswali yetu katika maisha,  na Mungu anageuza kila kitu kwa njia ya kutisha, anajibu maombi, anafanya kwa wakati wake, anatikisa, anaweka huru anaokoa, anawezesha, anapatanisha anaweka mambo yote kuwa sawa, anavunja magereza, na minyororo analainisha malango yanafunguka ana anatetemesha na anaokoa!

Matendo 16:22-31 “Na walipokwisha kuwapiga mapigo mengi, wakawatupa gerezani, wakamwamuru mlinzi wa gereza awalinde sana. Naye akiisha kupata amri hii akawatupa katika chumba cha ndani, akawafunga miguu kwa mkatale. Lakini panapo usiku wa manane Paulo na Sila walikuwa wakimwomba Mungu na kumwimbia nyimbo za kumsifu, na wafungwa wengine walikuwa wakiwasikiliza. Ghafula pakawa tetemeko kuu la nchi, hata misingi ya gereza ikatikisika, na mara hiyo milango ikafunguka, vifungo vya wote vikalegezwa. Yule mlinzi wa gereza akaamka, naye alipoona ya kuwa milango ya gereza imefunguka, alifuta upanga, akataka kujiua, akidhani ya kuwa wafungwa wamekimbia. Ila Paulo akapaza sauti yake kwa nguvu, akisema, Usijidhuru, kwa maana sisi sote tupo hapa. Akataka taa ziletwe, akarukia ndani, akitetemeka kwa hofu, akawaangukia Paulo na Sila; kisha akawaleta nje akasema, Bwana zangu, yanipasa nifanye nini nipate kuokoka? Wakamwambia, Mwamini Bwana Yesu, nawe utaokoka pamoja na nyumba yako.”  

Namuomba Mungu asimame katikati katika maisha yako na kuleta majibu ya maombi yako na kukutana na haja ya moyo wako, wakati wote tunapopita katika changamoto za aina mbalimbali ni muhimu kwetu tukakumbuka kuliitia jina la Bwana na kumtwika yeye fadhaa zetu zote, naye ataingilia kati maisha yetu kwa kusimama katikati yetu na kutupa ufumbuzi wa mahitaji yetu ! uongezewe neema

Rev. Innocent Samuel Kamote

Mkuu wa wajenzi mwenye Hekima


Jumapili, 17 Aprili 2022

Baba Mikononi mwako Naiweka Roho yangu!


Luka 23:44-46 “Hapo ilikuwa yapata saa sita, kukawa giza juu ya nchi yote hata saa kenda, jua limepungua nuru yake; pazia la hekalu likapasuka katikati. Yesu akalia kwa sauti kuu, akasema, Ee Baba, mikononi mwako naiweka roho yangu.”


Utangulizi:

Tunaendelea kujifunza kuhusu maneno ya Yesu aliyoyasema pale msalabani, ambayo yana maana pana sana kama utapata nafasi ya kujifundisha moja baada ya jingine, Leo nataka kuzungumzia kuhusu maneno ya mwisho miongoni mwa maneno saba aliyoyazungumza Yesu pale msalabani ambalo ni BABA MIKONONI MWAKO NAIWEKA ROHO YANGU!, Maneno haya ni sehemu ya maombi aliyokuwa akiyaomba Bwana Yesu Pale msalabani kwa kutumia Zaburi, yeye alipaza sauti kubwa sana na kuyasema maneno haya na kisha akakata roho, watu wengi sana huyaogopa maneno haya wakidhani ya kuwa ukiyasema basi utakuwa unajitakia kifo, au unaweza ukayasema inapofika saa yako ya mwisho, lakini maneno haya yana maana tofauti kabisa na namna ambavyo wengi wetu tumefikiri kwa siku nyingi, hata hivyo kabla ya kuyafanyia uchambuzi na upembuzi yakinifu ni vema kwanza tukajikumbusha tena maneno mengine katika maneno yote saba aliyoyasema Bwana Yesu Pale msalabani, maneno hayo ni pamoja na :-

·         Baba uwasamehe kwa maana hawajui walitendalo Luka 23:34

·         Amin nakuambia leo hii utakuwa pamoja nani peponi Luka 23:43

·         Mama tazama mwanao, mwana tazama mama yako Yohana 19:26-27

·         Mungu wangu Mungu wangu mbona umeniacha Mathayo 27:46

·         Nina kiu Yohana 19:28

·         Imekwisha Yohana 19:30

·         Baba mikononi mwako naiweka roho yangu Luka 23:46 


Baba mikononi mwako naiweka roho yangu

Kama tulivyoona ya kwamba maneno haya BABA MIKONONI MWAKO NAIWEKA ROHO YANGU Yalizungumzwa na Bwana Yesu kama maneno ya mwisho pale msalabani na kisha Yesu akakata roho na matukio mengi ya kushangaza yakajitokeza wakati mwana wa Mungu akikata roho, Maandiko haya ya msingi yanatuambia hivi tuone tena:-

 Luka 23:46 “Yesu akalia kwa sauti kuu, akasema, Ee Baba, mikononi mwako naiweka roho yangu

kimsingi maneno haya yana asili ya Lugha ya kiibrania na yanatoka moja kwa moja katika Zaburi ya 31:5 thelathini na moja, mstari wa tano, Na hivyo kimsingi Mwandishi au waandishi wa agano jipya waliruka maneno muhimu kutoka katika zaburi hii ambayo yana maana pana sana nay a muhimu  linapokuja swala la kufufuka kwa Yesu na sikukuu ya Pasaka, labda waandishi walikuwa na dhana kama yetu ya kufikiri kuwa Yesu alikuwa amevuta pumzi yake ya mwisho ya uhai na kuamua kufa kwa kukabidhi roho yake kwa baba yake, basi. Lakini maneno haya yanasomeka namna hii katika Zaburi yenyewe ya asili ambayo Yesu alikuwa akiinukuu kama maombi pale msalabani  ona -

Zaburi ya 31:5 “Mikononi mwako naiweka roho yangu; Umenikomboa, Ee Bwana, Mungu wa kweli.”

Aidha ili ieleweke vema pia zaburi hii katika kiingereza inasiomeka namna hii hasa kwa tafasiri ya Biblia ya kiingereza ya ESV yaani “English Standard Version” yanasomeka hivi Psalm 31:5 “Into your hand I commit my spirit; you have redeemed me, O LORD, Faithful God”, Kwa msingi huo pale msalabani Yesu alikuwa anasali kwa kunukuu Zaburi ya 31:5 akiwa katika hali ya mateso makali mno wakati akiwa katika hali yake ya mwilini duniani akiteseka maneno aliyoyasema Yesu kwa tafasiri ya ESV yalitakiwa kusomeka hivi MIKONONI MWAKO NAIWEKA ROHO YANGU,UMENIKOMBOA EE BWANA, MUNGU MWAMINIFU, Kwa hiyo utakubaliana nami kuwa kuna maneno ya msingi yalirukwa au yalipoteza maana wakati wa kufanya tafasiri katika lugha mbalimbali, nataka sasa nikuchukue taratibu ili iweze kujua kwa uwazi maneno haya na maana yake namna yalivyo na nguvu kuliko tunavyoweza kufikiri utanielewa tu, kwanza tuangalia neno NAIWEKA kwa undani kisha tuunganishe na maneno yaliyorukwa katika Luka 23:46 na kuyaona kwa uhalisia wake katika Zaburi 31:5

Usemi huo unakubaliana wazi kabisa na Lugha za kiibrania na kiyunani ambapo neno NAIWEKA ROHO YANGU kwa kiingereza “I COMMIT” katika lugha ya Kiibrania linatumika neno “AFKID” na kiyunani neno “DIAPRATO”, Neno la kiibrania AFKID kwa kiingereza linasomeka kama “I DEPOSIT” ambalo Kiswahili chake ni kuweka amana au kuacha kitu cha thamani kubwa mfano fedha kwa mtu au taasisi unayoiamini kwa kusudi la kuja kuchukua kitu hicho baadaye, mfano ni kama vile tunavyoweka fedha zetu bank na kisha tunakuwa na haki au uhakika wa kuzichukua wakati wowote unaona!, na neno la kiyunani “DIAPRATO” kwa kiingereza “ENTRUST” ambalo maana yake kukabidhi jukumu Fulani muhimu kwa mtu unayemuamini kuwa atalifanya, atalinda na kukuwakuilisha salama, Hatakuangusha. Kama Neema ya Mungu itakuwa imefunuliwa kwako sasa utakuwa umefahamu kuwa  Yesu aliposema BABA MIKONONI MWAKO NAIWEKA ROHO YANGU, kama alinukuu Zaburi 31:5 Basi Yesu alikuwa akisema maneno haya “BABA MIKONONI MWAKO NAIWEKA AMANA ROHO YANGU, UMENIKOMBOA EE BWANA, MUNGU MWAMINIFU.

Hii maana yake ni nini maana yake Yesu alipaza Sauti yake kwa imani pasipo shaka akatamka kwa uhakika kuwa anaiweka Roho yake amana kwa Mungu mwaminifu na ambaye anaweza kumrejeshea na sio anaweza kukaa nayo jumla jumla, Yesu aliamini katika uweza wa baba yake ya kuwa anauweza wa kuirejesha Roho yake tena na sio hivyo tu yeye mwenyewe anauwezo wa kuichukua atakapokua anaitaka kama wewe unavyoweza kuchukua fedha zako kutoka katika bank wakati unapotaka, Hii maana yeke ni kuwa Yesu kristo aliutoa uhai wake yeye mwenyewe  na hakuna mtu anayeweza kumuondolea uhai, lakini licha ya kuutoa mwenyewe yeye pia anauwezo wa kuutwaa tena uhai wake au roho yake, Aidha tunajifunza kuwa maneno yale yalikuwa na maana ya kuiweka roho yake kwa muda tu, na kisha ataichukua tena, kwa hiyo kukata roho kwa Yesu kulikuwa ni kwa muda na kuwa angafufuka tena !

Yohana 10:17-18 “Ndiposa Baba anipenda, kwa sababu nautoa uhai wangu ili niutwae tena. Hakuna mtu aniondoleaye, bali mimi nautoa mwenyewe. Nami ninao uweza wa kuutoa, ninao na uweza wa kuutwaa tena. Agizo hilo nalilipokea kwa Baba yangu.”

Kwa msingi huo Yesu alimaanisha kuwa hakuna anayeweza kuuondoa uhai wake hapa inajumuisha kila kitu mbinguni na duniani hakuna anayeweza kuiondoa uhai wake, kifo cha Msalabani ilikuwa ni hiyari yake mwenyewe kwaajili ya kuwakomboa wanadamu na ndio maana anapendwa na baba  kwa sababu hakuna aliyemshurutisha, Yesu anayo mamlaka ya kuyatoa maisha yake na anayo mamlaka ya kuyachukua tena, hivyo ni kwa hiyari yake mwenyewe kwa kawaida yeye humuheshimu baba yake, na hafanyi neno Bila kuagizwa na baba hasa alipokuwa Duniani neno linasema:-

Yohana 5;19  Mwana hawezi kutenda neno mwenyewe ila lile ambalo amwona Baba analitenda; kwa maana yote ayatendayo yeye, ndiyo ayatendayo Mwana vile vile.”

Yesu anazungumza hii katika hali ya ubinadamu wake hali ya kumtegemea baba yake akiwa duniani, hali ya kujinyenyekeza, lakini neno lake baba mikononi mwako naiweka roho yangu linatufungulia akili kujua uweza na mamlaka kubwa aliyonayo Yesu Kristo, lakini linatuthibitishia kuwa alikuwa na uhakika wa kufufuka!

Yesu hakufa kama afavyo mchuuzi, ulikuwa ni mpango wake kamili wa kumuokoa mwanadamu, mpango ambao baba wa mbinguni alifurahishwa nao, kwa mamlaka hii, tunaweza kukabidhi chochote kwake, na anauwezo wa kuturejeshea, kama kuna vitu tulipokonywa au kuumizwa au kuibiwa au kudhulumiwa vyovyote iwavyo tunaye Yesu mwenye uwezo wa kuturejeshea maradufu yeye anauwezo wa kufisha na kuuhisha, anajeruhi na anaponya, nani yeye mwenye uwezo wa kuokoa hivyo kama kuna kitu kimepotea katika maisha yetu iwe amani, furaha na kadhalika Huyu Yesu anauwezo mkubwa ana mamlaka kubwa yeye ni Mungu na anajitambulisha kuwa hakuuawa isipokuwa ilikuwa kwa hiyari yake ni sadaka aliyojitoa yeye anauwezo wa kuutoa uhai wake na kuuchukua tena na anaweza kufanya hivyo na lolote kwa yeyote akimtumainia yeye, Maandiko yanasema!  

Kumbukumbu 32:39 “Fahamu sasa ya kuwa Mimi, naam, Mimi ndiye, Wala hapana Mungu mwingine ila Mimi; Naua Mimi, nahuisha Mimi, Nimejeruhi, tena naponya; Wala hapana awezaye kuokoa katika mkono wangu,”

Hakuna jambo la Msingi kama kukabidhi maisha yetu, mali zetu, ndoa zetu, kazi zetu, watoto wetu, waume zetu, wake zetu, mashamba yetu, magari yetu, afya zetu, na lolote lila katika mikono salama ya baba wa mbinguni ambaye tunajua anaweza kulinda kile tunachiomkabidhi, hakikisha kuwa katika maisha yako unamkabidhi Mungu mwaminifu maisha yako kwa sababu yeye anauwezo wa kutunza, kulinda na kukurejeshea kila kinachopotea ni kwa Mungu pekee ndipo tunapokuwa na uhakika wa kurejezewa kila kilichopotea endapo kweli katika maisha yetu tulimkabidhi yeye, watu wengi wamekabidhi maisha yao na mali zao kwa watu mabaradhuli na wakapoteza Yesu anatukumbusha kuwa ukijikabidhi kwa Mungu mwaminifu hakuna cha kupoteza ! ni muhimu wakati huu wa msimu wa Pasaka kukabidhi maisha yetu kwa Mungu mwaminifu yeye atayarejesha tena yatakapopotea kwa sababu yoyote ile, tukiamini kazi aliyoifanye Yesu Msalabani hakika yeye naye atatufufua siku ya mwisho

Yohana 6:53-54 “Basi Yesu akawaambia, Amin, amin, nawaambieni, Msipoula mwili wake Mwana wa Adamu na kuinywa damu yake, hamna uzima ndani yenu. Aulaye mwili wangu na kuinywa damu yangu anao uzima wa milele; nami nitamfufua siku ya mwisho.”

Na Rev Innocent Kamote

Mkuu wa wajenzi mwenye hekima!



Ijumaa, 15 Aprili 2022

Baba uwasamehe, kwa kuwa hawajui watendalo!


Luka 23:33-37 “Na walipofika mahali paitwapo Fuvu la Kichwa, ndipo walipomsulibisha yeye, na wale wahalifu, mmoja upande wa kuume, na mmoja upande wa kushoto. Yesu akasema, BABA, UWASAMEHE, KWA KUWA HAWAJUI WATENDALO. Wakagawa mavazi yake, wakipiga kura. Watu wakasimama wakitazama. Wale wakuu nao walikuwa wakimfanyia mzaha, wakisema, Aliokoa wengine; na ajiokoe mwenyewe, kama ndiye Kristo wa Mungu, mteule wake. Wale askari nao wakamfanyia dhihaka, wakimwendea na kumletea siki, huku wakisema, Kama wewe ndiwe mfalme wa Wayahudi, ujiokoe mwenyewe



Utangulizi:


Mojawapo kati ya usemi wenye maana sana kati ya semi saba za Yesu alizozisema akiwa msalabani na ambazo zinatajwa katika sehemu mbalimbali za injili, ni pamoja ya usemi huo wa muhimu ni usemi wa Kwanza wenye Neno BABA UWASAMEHE KWA MAANA HAWAJUI WALITENDALO ambalo leo katika msimu huu wa pasaka tutachukua muda kulijadili kwa undani na kupata maana Muhimu sana iliyokusudiwa, maneno mengine kati ya maneno saba aliyoyasema Yesu msalabani ni pamoja na:-

1.       Baba uwasamehe kwa maana hawajui walitendalo Luka 23:34

2.       Amin nakuambia leo hii utakuwa pamoja nani peponi Luka 23:43

3.       Mama tazama mwanao, mwana tazama mama yako Yohana 19:26-27

4.       Mungu wangu Mungu wangu mbona umeniacha Mathayo 27:46

5.       Nina kiu Yohana 19:28

6.       Imekwisha Yohana 19:30

7.       Baba mikononi mwako naiweka roho yangu Luka 23:46



BABA UWASAMEHE KWA MAANA HAWAJUI WALITENDALO.


Leo ni siku ya ijumaa kuu, ni siku ambayo wakristo wote duniani, tunaungana katika kuadhimisha na kukumbuka kusulubiwa kwa Yesu Kristo huko Golgota miaka zaidi ya 2000 iliyopita katika siku hii basi basi sisi tutachukua Muda kuangalia usemi huu wa Kwanza katika maneno saba yaliyozungumzwa na Yesu Pale Msalabani wakati wa mateso yake , Neno hili ni miongoni mwa maneno saba ya Yesu akiwa matesoni ambayo yamekusanywa kutoka maeneo mbalimbali ya vitabu vya injili na hili mojawapo tutaangalia umuhimu wake katika msimu huu wa Pasaka. Hapa tunazungumzia Msamaha.


Kila mmoja wetu kwa namna moja ama nyingine amewahi kujeruhiwa moyo na mtu mwingine, kila mmoja amewahi kujeruhiwa na kuathiriwa kiakili, kihisia na hata kimwili, na kwa sababu hiyo tunaweza kujawa na maumivu ya aina Fulani mioyoni mwetu, ama uchungu wa aina Fulani, vyovyote vile iwavyo ukomavu wa kiroho katika maisha yetu ya ukristo unapimwa na namna tunavyoweza kusamehe, uwezo wa kusamehe ukiwa pamoja nasi  unatuwezesha kuishi kwa furaha na amani duniani na huku tukiwa huru bila kifungo chochote endapo tutakuwa na uwezo wa kusamehe wengine.


Yesu Kristo akiwa Msalabani aliangalia chini na kutafakari katika hali ya ukimya akiwaangalia wote waliokuwa wanahusika katika kumtesa, Askari ambao walisimamia mateso yake wakigawana nguo yake kwa kuipigia kura, Yesu hakuwahi kutenda neno lolote ovu, siku zote alikuwa akiwafundisha watu neno la Mungu na kuwaponya watu magonjwa yao, aliwahudumia watu akifufua, akiponya, akilisha akihurumia na kurehemu, hata hivyo kwajili ya wivu wakuu wa dini walikusudia kumuua, waliandaa mpango mkakati wa kumuua, walitoa rushwa kwa Yuda ili aweze kumsaliti, waliandaa mashahidi wa uongo ili wamshitaki, walimuweka katima mikono ya wenye dhambi ili asulubiwe, hakimu aliyekuwepo alipindisha hukumu ilihali akijua wazi kuwa Yesu hakuwa na hatia, zaidi ya yote aliamuru Yesu apigwe mijeledi 


Yohana 19:1-6 “Basi ndipo Pilato alipomtwaa Yesu, akampiga mijeledi. Nao askari wakasokota taji ya miiba, wakamtia kichwani, wakamvika vazi la zambarau. Wakawa wakimwendea, wakisema, Salamu! Mfalme wa Wayahudi! Wakampiga makofi. Kisha Pilato akatokea tena nje, akawaambia, Mtu huyu namleta nje kwenu, mpate kufahamu ya kuwa mimi sioni hatia yo yote kwake. Ndipo Yesu alipotoka nje, naye amevaa ile taji ya miiba, na lile vazi la zambarau. Pilato akawaambia, Tazama, mtu huyu! Basi wale wakuu wa makuhani na watumishi wao walipomwona, walipiga kelele wakisema, Msulibishe! Msulibishe! Pilato akawaambia, Mtwaeni ninyi basi, mkamsulibishe; kwa maana mimi sioni hatia kwake.”


Ni ukweli usiopingika kuwa Yesu aliharibiwa sana kiasi ambacho ilikuwa ni ngumu kumtamani sawa kabisa na alivyotabiri Isaya katika Isaya 53:2-5Maana alikua mbele zake kama mche mwororo, Na kama mzizi katika nchi kavu; Yeye hana umbo wala uzuri; Na tumwonapo hana uzuri hata tumtamani. Alidharauliwa na kukataliwa na watu; Mtu wa huzuni nyingi, ajuaye sikitiko; Na kama mtu ambaye watu humficha nyuso zao, Alidharauliwa wala hatukumhesabu kuwa kitu. Hakika ameyachukua masikitiko yetu, Amejitwika huzuni zetu; Lakini tulimdhania ya kuwa amepigwa, Amepigwa na Mungu, na kuteswa. Bali alijeruhiwa kwa makosa yetu, Alichubuliwa kwa maovu yetu; Adhabu ya amani yetu ilikuwa juu yake, Na kwa kupigwa kwake sisi tumepona.”


Pamoja na mateso haya na suluba kali pia walimfanyia dhihaka za namna nyingi, mateso yake yamerekodiwa na Mel Gobson katika filamu yake ijulikanayo kama Passion of Jesus ambayo wayahudi walipoiona kwa mara ya kwanza waliikataa na kusema kuwa inaweza kuchochea chuki kati ya wakristo na wayahudi wakifikiri kuwa Mel Gibson ametia chumvi, lakini kitaalamu Mel Gibson ameonyesha karibu robo tatu tu ya mateso halisi aliyoyapata Kristo, mateso mengine :- 


Yohana 19:23-24, “Nao askari walipomsulibisha Yesu, waliyatwaa mavazi yake, wakafanya mafungu manne, kwa kila askari fungu lake; na kanzu nayo. Basi kanzu ile haikushonwa, ilikuwa imefumwa yote pia tangu juu. Basi wakaambiana, Tusiipasue, lakini tuipigie kura, iwe ya nani. Ili litimie andiko lile linenalo, Waligawanya nguo zangu, Na vazi langu wakalipigia kura. Basi ndivyo walivyofanya wale askari.” 


Mathayo 27:27-31 “Ndipo askari wa liwali wakamchukua Yesu ndani ya Praitorio, wakamkusanyikia kikosi kizima.Wakamvua nguo, wakamvika vazi jekundu. Wakasokota taji ya miiba, wakaiweka juu ya kichwa chake, na mwanzi katika mkono wake wa kuume; wakapiga magoti mbele yake, wakamdhihaki, wakisema, Salamu, Mfalme wa Wayahudi! Kisha wakamtemea mate, wakautwaa ule mwanzi, wakampiga-piga kichwani. Walipokwisha kumdhihaki, wakalivua lile vazi, wakamvika mavazi yake, wakamchukua kumsulibisha.” 


Wahalifu wawili waliokuwa kulia kwake na kushoto kwake wakimshutumu, Mathayo 27:44, “Pia wale wanyang'anyi waliosulibiwa pamoja naye walimshutumu vile vile.” Viongozi wa dini waliofanya fitina na kutengeneza ushahidi wa uongo na kushinikiza kwamba Yesu asulubiwe na waliokuwa wakimdhihaki Mathayo 27:41-43,“Kadhalika na wale wakuu wa makuhani wakamdhihaki pamoja na waandishi na wazee, wakisema, Aliokoa wengine, hawezi kujiokoa mwenyewe. Yeye ni mfalme wa Israeli; na ashuke sasa msalabani, nasi tutamwamini. Amemtegemea Mungu; na amwokoe sasa, kama anamtaka; kwa maana alisema, Mimi ni Mwana wa Mungu” 


Hakimu Pilato ambaye alifahamu kabisa kuwa Yesu hakuwa na hatia, lakini akapindisha kesi haya yote na ile aina ya mateso kwa mwana wa Mungu, kungeweza kwa namna yoyote ile kuleta hisia za maumivu, uchungu, kinyongo, kisasi, ugumu wa moyo, hasira, ghadhabu, ubaridi, kujihami na kuhakikisha kuwa unawashughulikia wote waliokutenda uovu, Lakini Bwana Yesu anatangaza kusamehe na kuwaombea wakosaji wote kwa BABA KUWA WASAMEHEWE, Hali hii inaashiria uwezo mkubwa wa ukomavu mkubwa wa kiroho aliokuwa nao Yesu wa kutangaza Msamaha, ni ngazi ya juu sana ya Rehema na upendo, kwamba hata katika hali ngumu kama hii ya kuteseka bado Yesu anatangaza Msamaha dhidi ya maadui zake ! wote tunafahamu kuwa msamaha sio jambo rahisi, lakini katika msimu huu wa Pasaka Bwana Yesu anatukumbusha kwamba tunapaswa kuachilia na kutangaza msamaha kwa wote waliotukosea lakini vilevile kuwaomba radhi wale ambao tumewakosea, wakati huu wa Kwaresma ni wakati wa kuachilia ni wakati wa kusamehe ni wakati wa kuonyesha kuwa tumekomaa kiroho na kiakili na kuwa kusamehe ndio njia ya juu kabisa ya kuonyesha tabia ya uungu na ukomavu wetu, tusamehe.! 


Kusamehe ni nini hasa? 


Kusamehe ni kuachilia, unaachilia mambio yaende, unaacha kuhesabu ubaya uliofanyiwa unaufunika kwa kuendelea kupenda, unaacha kutafuta kulipa kisasi au nkulipiwa kisasi, unaondoa moyoni mwako hali ya kumfikiri mtu aliyekukosea unajiweka huru mbali na kifungo cha aina yoyote cha kuwa na mtu moyoni, unamuhurumia mtu, unachukuliana naye, unamuhesabu kuwa yeye ni dhaifu, hivyo unamuachilia 


Faida za kusamehe 


·         Unadumisha mahusiano, mahusiano yanakuwa mazuri, Ndoa inakuwa nzuri, unampata ndugu yako

·         Unaiweka akili yako kufikiri mambo ya msingi na kuzungumza mambo ya msingi

·         Unajiweka huru kutoka kwenye migandamizo na msongo wa mawazo

·       Unakuwa na afya nzuri, unakuwa mwenye furaha, hutakuwa na pressure, hutaugua magonjwa ya moyo, na unakuwa mtu mwenye uwezio wa juu wa kujitambua 


·         Kusamehe kunakufanya wewe nawe usamehewe na Mungu 


Mathayo 18:21-35Kisha Petro akamwendea akamwambia, Bwana, ndugu yangu anikose mara ngapi nami nimsamehe? Hata mara saba? Yesu akamwambia, Sikuambii hata mara saba, bali hata saba mara sabini. Kwa sababu hii ufalme wa mbinguni umefanana na mfalme mmoja aliyetaka kufanya hesabu na watumwa wake. Alipoanza kuifanya, aliletewa mtu mmoja awiwaye talanta elfu kumi.Naye alipokosa cha kulipa, bwana wake akaamuru auzwe, yeye na mkewe na watoto wake, na vitu vyote alivyo navyo, ikalipwe ile deni.Basi yule mtumwa akaanguka, akamsujudia akisema, Bwana, nivumilie, nami nitakulipa yote pia. Bwana wa mtumwa yule akamhurumia, akamfungua, akamsamehe ile deni. Mtumwa yule akatoka, akamwona mmoja wa wajoli wake, aliyemwia dinari mia akamkamata,akamshika koo,akisema Nilipe uwiwacho.Basi mjoli wake akaanguka miguuni pake, akamsihi, akisema, Nivumilie, nami nitakulipa yote pia. Lakini hakutaka, akaenda, akamtupa kifungoni, hata atakapoilipa ile deni. Basi wajoli wake walipoyaona yaliyotendeka, walisikitika sana, wakaenda wakamweleza bwana wao yote yaliyotendeka. Ndipo bwana wake akamwita, akamwambia, Ewe mtumwa mwovu, nalikusamehe wewe deni ile yote, uliponisihi; nawe, je! Haikukupasa kumrehemu mjoli wako, kama mimi nilivyokurehemu wewe? Bwana wake akaghadhibika, akampeleka kwa watesaji, hata atakapoilipa deni ile yote. Ndivyo na Baba yangu wa mbinguni atakavyowatenda ninyi, msiposamehe kwa mioyo yenu kila mtu ndugu yake.” 


Kutokusamehe hasara zake. 


Hakuna sababu ya kuwabeba watu moyoni, hii hali kiroho inakuweka wewe mwenyewe gerezani na kukunyima furaha, dua, sala, sadaka na maombi yetu vinakutana na kikwazo kama hatujawasamehe wengine Mathayo 6:12 “Utusamehe deni zetu, kama sisi nasi tuwasamehevyo wadeni wetu.” Mathayo 6:14-15 “Kwa maana mkiwasamehe watu makosa yao, na Baba yenu wa mbinguni atawasamehe ninyi.Bali msipowasamehe watu makosa yao, wala Baba yenu hatawasamehe ninyi makosa yenukuna hasara nyingi sana za kiroho na kimwili kama watu hawatasamehe na kuna faida nyingi sana kama watu watasamehe.Lakini kama mtu hatasamehe yafuatayo yatamkabili:- 


·         Unakuwa na moyo wenye uchungu, huwezi kufurahia mahusiano hata katika ndoa

·         Unakuwa na mawazo mabaya kwa kudhani Fulani ni adui yako

·         Utakuwa na mgandamizo wa mawazo

·         Unafungua mlango wa kuvamiwa na mapepo, unafukuza uwepo wa Mungu

·         Unazuia Baraka za Mungu na kufanya ibada zako zikataliwe

Bwana na ampe neema kila Mmoja wetu, kuwa na uwezo wa kusamehe ili tuweze kuwa wana wa Mungu sawasawa na mafundisho ya Bwana wetu Yesu!

 

Na. Rev. Innocent Kamote

Mkuu wa wajenzi mwenye Hekima



Jumatano, 13 Aprili 2022

Litanijiaje Sanduku la Bwana Mungu wangu!


1Nyakati 13:9-12 “Hata walipofika penye uga wa Nakoni, Uza akaunyosha mkono wake alishike sanduku; kwa maana wale ng'ombe walikunguwaa. Ndipo hasira ya Bwana ikawaka juu ya Uza, naye akampiga, kwa sababu alilinyoshea sanduku mkono wake, hata akafa pale pale mbele za Mungu. Naye Daudi akaona uchungu, kwa kuwa Bwana amemfurikia Uza; akapaita mahali pale Peres-uza hata leo. Naye Daudi akamwogopa Mungu siku ile, akasema, NITAJILETEAJE SANDUKU LA MUNGU KWANGU?


Utangulizi:

Moja ya mazingira ya kusikitisha sana katika Historia ya maandiko ni Pamoja na historia ya kufa kwa kuhani aliyeitwa Uza kifo chake kimeelezewa kwa kina katika 1Nyakati 13:1-14, Kifo cha kuhani huyu kilikuwa ni matokeo ya uamuzi wa Daudi kulileta Sanduku la Agano la Mungu kutoka mji ulioitwa Kiriath Yearimu kuja Yerusalem mwendao wa miles kama kumi hivi (10). Sanduku lililetwa likiwa limebebwa kwenye mkokoteni uliokuwa ukikokotwa na ngombe!

Walipokuwa wakisafiri kuja Yerusalem ng’ombe wale walikunguwaa yaani walijikwaa na ikawa kama wanataka kuangusha Sanduku la agano, ndipo Uza aliyekuwa karibu na sanduku la agano la Mungu akanyoosha mkono wake kujaribu kulizuia ili lisianguke, Hasira za Mungu zikawaka na Bwana akampiga Uza kwa sababu ile na akafa mbele za Bwana pale pale, Jambo hili lilikuwa la kusikitisha sana na kila mmoja aliogopa Daudi naye aliogopa akajawa na uchungu sana akaliacha sanduku la Agano katika nyumba ya Obedi- Edom na akaanza kuwaza nitaliletaje Sanduku la Mungu kwangu! Ama linanijiaje Sanduku la Bwana Mungu wangu!

2Samuel 6:6-11 “Hata walipofika kwa uga ya Nakoni, Uza akalinyoshea mkono sanduku la Mungu, akalikamata kwa maana wale ng'ombe walikunguwaa. Ndipo hasira ya Bwana ikawaka juu ya Uza; naye Mungu akampiga huko kwa kosa lake; hata akafa pale pale penye sanduku la Mungu. Daudi akaona uchungu kwa kuwa Bwana amemfurikia Uza; akapaita mahali pale Peres-uza hata leo. Naye Daudi akamwogopa Bwana siku ile; akasema, LITANIJIAJE SANDUKU LA BWANA? Basi Daudi hakutaka kulileta sanduku la Bwana kwake mjini mwa Daudi; ila Daudi akalihamisha nyumbani kwa Obed-edomu, Mgiti. Sanduku la Bwana akalitia katika nyumba ya Obed-edomu, Mgiti, muda wa miezi mitatu; naye Bwana akambarikia Obed-edomu, na nyumba yake yote.”

Wanatheolojia wengi sana hujiuliza sasa ni lipi kosa la Uza? Je Mungu hakuwa mwema kwa kumuua Uza lipi lilikuwa jema kuliacha sanduku la agano lianguke? Au kuzuia lisianguke? Kwanini Uza alikuwa akifanya jambo jema na Mungu akamkasirikia na kumuua? Kwanini, bila shaka kuna mambo ya msingi ya kujifunza katika tukio hili, tutajifunza somo hili kwa kuzingatia vipengele vitatu vifuatavyo:-

·         Ufahamu kuhusu Sanduku la Agano

·         Litanijiaje Sanduku la Bwana Mungu wangu!

·         Mambo ya kujifunza katika tukio hili.

Ufahamu kuhusu Sanduku la Agano.

Sanduku la agano, ambalo pia huitwa Sanduku la ushuhuda au sanduku la Mungu, kilikuwa ni moja ya chombo muhimu sana na kitakatifu mno kwa wana wa Israel, Miongoni mwa Thamani zlizokuwa zikikaa katika hema la kukutania au hekaluni Chombo hiki kilijengwa wa mti wa mshita (Acacia)  na kufunikwa kawa dhahabu  kutokana na maelekezo ya Mungu kwa Musa, Ndani yake kulihifadhiwa mbao mbili za mawe zenye amri kumi zilizoandikwa na Mungu, mwenyewe na ile fimbo ya Haruni iliyochipuka pamoja na kopo la dhahabu lenye mana iliyohifadhiwa, Chombo hiki juu kilikuwa na Makerubi wawili walioinamisha mbawa zao na kufunika kiti cha Rehema cha Mungu, na ni kutoka Hapo ndio mahali Mungu alikuwaakizungumza na Musa ona:-

Kutoka 25:10-22 “Nao na wafanye sanduku la mti wa mshita; urefu wake na uwe dhiraa mbili na nusu, na upana wake dhiraa moja na nusu, na kwenda juu kwake dhiraa moja na nusu. Nawe ulifunike kwa dhahabu safi, ulifunike ndani na nje, nawe tia na ukingo wa dhahabu kulizunguka pande zote. Nawe subu vikuku vinne vya dhahabu kwa ajili yake, na kuvitia katika miguu yake minne; vikuku viwili upande mmoja, na vikuku viwili upande wake wa pili. Nawe fanya miti mirefu ya mshita na kuifunika dhahabu. Nawe tia hiyo miti katika vile vikuku vilivyo katika pande mbili za sanduku ili kulichukua hilo sanduku. Hiyo miti itakaa katika vile vikuku vya sanduku; haitaondolewa. Kisha tia ndani ya sanduku huo ushuhuda nitakaokupa. Nawe fanya kiti cha rehema cha dhahabu safi; urefu wake utakuwa dhiraa mbili na nusu, na upana wake dhiraa moja na nusu. Nawe fanya makerubi mawili ya dhahabu; uyafanye ya kazi ya kufua, katika hiyo miisho ya kiti cha rehema, huku na huku. Weka kerubi moja mwisho mmoja, na kerubi la pili mwisho wa pili; fanya hayo makerubi ya kitu kimoja na kiti cha rehema, mwisho huku na mwisho huku. Na hayo makerubi yatainua mabawa yao juu, na kukifunika hicho kiti cha rehema kwa mabawa yao, na nyuso zao zitaelekeana hili na hili; nyuso za hayo makerubi zitaelekea kiti cha rehema. Weka kiti cha rehema juu ya hilo sanduku, kisha utie huo ushuhuda nitakaokupa ndani ya sanduku. Nami nitaonana nawe hapo, na kuzungumza nawe pale nilipo juu ya kiti cha rehema, katikati ya hayo makerubi mawili yaliyo juu ya sanduku la ushuhuda, katika mambo yote nitakayokuagiza kwa ajili ya wana wa Israeli.”               

Kimsingi kuna mambo mengi sana tunaweza kujifunza kutoka katika chombo hiki kitakatifu na cha thamani mno,mbao mbili za mawe zilizoandikwa Amri kumi zinatufundisha wazi kuwa Mungu ni Mungu wa Utaratibu, Fimbo ya haruni iliyochipuka inatufundisha kuwa Mungu anaheshimu itifaki uongozi aliouchagua, Kopo la dhahabu na ile mana iliyohifadhiwa inatufundhisha kuwa Mungu anashughulika na mahitaji yetu kila siku, kwa ujumla kuna mambo mengi ya kujifunza kutoka katika chombo hiki lakini kwa leo itoshe tu kusema maana kuu hasa ya chombo hiki ilikuwa ni uwakilishi unaoonekana wa uwepo wa Mungu asiyeonekana, Chombo kiliwakilisha “UWEPO WA MUNGU” chombo hiki kilikuwa na uwezo mkubwa sana wa kusababisha Baraka na madhara, Baraka kama kitapewa heshima inayostahili na madhara endapo ukiukwaji wa Heshima yake utafanyika!

2Samuel 6:10-12 “Basi Daudi hakutaka kulileta sanduku la Bwana kwake mjini mwa Daudi; ila Daudi akalihamisha nyumbani kwa Obed-edomu, Mgiti. Sanduku la Bwana akalitia katika nyumba ya Obed-edomu, Mgiti, muda wa miezi mitatu; naye Bwana akambarikia Obed-edomu, na nyumba yake yote. Kisha mfalme Daudi akaambiwa ya kwamba, Bwana ameibarikia nyumba ya Obed-edomu, na vitu vyote alivyo navyo kwa ajili ya sanduku la Mungu. Daudi akaenda, akalileta sanduku la Mungu, toka nyumba ya Obed-edomu mpaka mji wa Daudi, kwa shangwe.”

Kutokana na tukio la kifo cha kuhani Uza watu waliingiwa na Hofu na Daudi pia alimuogopa Mungu siku ile lakini aliingiwa na uchungu sio wa kuchukizwa na Mungu lakini kujutia na kujiuliza imekuwaje Mungu akafanya vile! Hili lilimpa kujiuliza swali kubwa kuwa litanijiaje Sanduku la Bwana Mungu wangu!

Litanijiaje Sanduku la Bwana Mungu wangu!     

Swala kubwa hapa ni namnagani sanduku la Mungu litafika Yerusalem, kwani walipokuwa katika kulileta Ndio kuhani Uza akauawa na Mungu kwa kulinyooshea mkono Sanduku, na Daudi aliogopa sasa kulileta na alipoliacha kwa Obed- Edom mtu huyu ndani ya miezi mitatu tu alibarikiwa sana kwa nini hasa sanduku la agano lilishindwa kufika Yerusalem katika wakati uliokusudiwa na kusababisha madhara njiani?

Tukio linatukumbusha umuhimu wa kufuata maagizio ya Mungu na kufanya sawasawa na Mapenzi yake, Mungu alikuwa ametoa maagizo yaliyokuwa wazi namna na jinsi sanduku la agano linavyopaswa kubebwa katika Torati

Kutoka 25:14-15 “Nawe tia hiyo miti katika vile vikuku vilivyo katika pande mbili za sanduku ili kulichukua hilo sanduku. Hiyo miti itakaa katika vile vikuku vya sanduku; haitaondolewa.”

Katika maelekezo ya ujenzi wake sanduku lilipaswa kuwa na vikuku ambavyo vingechomekwa miti ya dhahabu kwa kusudi la kuichomeka na kulibeba sanduku la agano mabegani mwa makuhani maalumu walioteuliwa kufanya kazi hiyo wengi wakiwa ni walawi na hususani kabila la walawi wa wakohathi

Hesabu 7:9 “Lakini hakuwapa wana wa Kohathi; maana, utumishi wa vile vitu vitakatifu ulikuwa ni wao; nao wakavichukua mabegani mwao.”

Daudi pamoja na kuhani Uza walisahahu kufuata maelekezo ya Mungu, na Mungu akamshughulikia Uza mara moja kwa kifo, jambo hili lilimfanya Daudi kumuogopa sana Mungu, Mungu yuko Sirius/Makini na maagizo yake, yeye alitaka Sanduku la agano liheshimiwe kwa kiwango kikubwa sana chochote ambacho Mungu amakitangaza kuwa ni kitakatifu hakipaswi kuchukuliwa kimzaha mzaha, Ulimwengu wa kiroho uwe wa giza au wa nuru unazingatia sana masharti wakati wote kama ukivunja mashari au miiko au kutokufuata maelekezo huwezi kutoboa! Ona madhara;-

1Samuel 6:19 “  Basi Bwana aliwapiga baadhi ya watu wa Beth-shemeshi, kwa sababu wamechungulia ndani ya hilo sanduku la Bwana, wapata watu sabini, na watu hamsini elfu; nao watu wakalalamika, kwa kuwa Bwana amewapiga watu kwa uuaji mkuu.”

Daudi alikuwa amejifunza kuwa ubebwaji wa sanduku la Mungu mwanzoni haukuwa umefuata maelekezo yake na sasa Daudi akawa amejifunza kupitia uchungu alioupata kwa kifo cha Uza ilikuwa ni lazima sanduku la Agano libebe Mabegani tena na makuhani kama Bwana alivyoagiza, wao walibeba kama wafilisti wasiomjua Mungu walivyolirudisha Sanduku la Agano

 1Nyakati 15:2 “Ndipo Daudi akasema, Haimpasi mtu awaye yote kulichukua sanduku la Mungu, isipokuwa Walawi peke yao; kwa kuwa hao ndio aliowachagua Bwana, ili walichukue sanduku la Mungu, na kumtumikia daima. 15 Na wana wa Walawi wakalichukua sanduku la Mungu mabegani mwao kwa miti yake, kama vile Musa alivyoamuru, sawasawa na neno la Bwana.”

Walipofuata maelekezo ya Mungu kwa uaminifu ndipo walipokuwa na uwezo wa kulibeba sabduku la Bwana bila kusababisha madhara  na safari yao ikawa salama tofauti na mwenendo wao wa Mwanzo, watu wengi sana hawafanikiwi kwa sababu hawafuati maelekezo, huwezi kubeba uwepo wa Mungu kama Mungu hajakuchagua uubebe, Kama hujali kuhusu maelekezo na kufuata utaratibu hakuna mafanikio mahali popote ambapo watu hawafuati utaratibu Mungu ni Mungu wa utaratibu, Sanduku la agano litakujiaje ni kwa kufuata maelekezo, mafanikio katika maisha, kujibiwa maombi na kufurahia Baraka na uwepo wa Mungu vitatujia katika maisha yetu endapo tutakuwa makini kufuata maelekezo na kuyatii na kuacha kutumaini hekima yetu na ujuzi wetu wa kibinadamu.

Mambo ya kujifunza katika tukio hili.

Mungu ni mwema nani mwenye upendo mwingi sana na rehema zake ni kubwa kwa wanadamu lakini linapokuja swala la kutokufuata Maelekezo yake Mungu anachukizwa sana na yuko tayari hata kuahirisha mpango wake kwa mtu asiyefuata maelekezo, Endapo mtu anataka kufanikiwa katika njia za Mungu basi ni vema akafuata maelekezo.

·         UTII: 1Samuel 15:22-23 “Naye Samweli akasema, je! Bwana huzipenda sadaka za kuteketezwa na dhabihu Sawasawa na kuitii sauti ya Bwana? Angalia, kutii ni bora kuliko dhabihu, Na kusikia kuliko mafuta ya beberu. Kwani kuasi ni kama dhambi ya uchawi, Na ukaidi ni kama ukafiri na vinyago; Kwa kuwa umelikataa neno la Bwana, Yeye naye amekukataa wewe usiwe mfalme.”

 

Lazima wakati wote watu wajifunze, kukubali kujifunza sio dhambi, Yesu alikubali kujifunza Kabla ya kuwa Mwalimu mzuri na kiongozi mzuri alichukua Muda kukaa na walimu na aliuliza maswali  na hivyo tunamuona yeye baadaye anakuja kuwa kiongozi na mwalimu mwema na bora zaidi Duniani

 


·         KUJIFUNZA: Luka 2:52 “Ikawa baada ya siku tatu wakamwona hekaluni, ameketi katikati ya waalimu, akiwasikiliza na kuwauliza maswali.”  Watu wengi sana wanaponzwa kwa sababu ya kujifikiri kuwa wanajua maandiko yanasema mtu akidhani ya kuwa anajua hajui bado kama impasavyo kujua ni lazima kila kitu tujifunze

 

1Wakoritho 8:2 “Mtu akidhani ya kuwa anajua neno, hajui neno lo lote bado, kama impasavyo kujua.”

 

Daudi mwanzoni alikuwa hajui na alipokubali kujifunza akafanikiwa wako watu wanaona noma kujifunza wanafikiri kuwa watakuwa duni sana wakijifunza na kuuliza wanataka waonekane kuwa wanajua, Mungu hamfurahii mtu awayeyote anayekataa maarifa

 

Hosea 4:6 “Watu wangu wanaangamizwa kwa kukosa maarifa; kwa kuwa wewe umeyakataa maarifa, mimi nami nitakukataa wewe, usiwe kuhani kwangu mimi; kwa kuwa umeisahau sheria ya Mungu wako, mimi nami nitawasahau watoto wako.”

 

·         KUMTEGEMEA MUNGU SIO AKILI:  Mungu hapandezwi na mtu anayezitegemea akili zake mwenyewe, kutegemea akili zako mwenyewe ni kiburi, Kanuni ya Mungu inatutaka kuyatafuta mapenzi yake na kuyafuata tunapoanza kujifanya tuna akili na tunazitumainia akili zetu na hekima zetu basi madhara yake ni pamoja na kuharibikiwa Lazima tumtegemee Mungu katika njia zetu zote

 

Mitahli 3:5-8 “Mtumaini Bwana kwa moyo wako wote, Wala usizitegemee akili zako mwenyewe; Katika njia zako zote mkiri yeye, Naye atayanyosha mapito yako.Usiwe mwenye hekima machoni pako; Mche Bwana, ukajiepushe na uovu. Itakuwa afya mwilini pako, Na mafuta mifupani mwako.”

 

Maandiko yanatuonya sana tuache kujiamini kupita kawaida na kufikiri kuwa yale tunayoyaona sisi ni sahihi wakati wote kumbe wakati mwingine yako kinyume na mapenzi ya Mungu, kujifikiri kuwa sisis ni smart mno tuko vizuri kichwani kunatupelekea kuumbuka kwa sababu tunaweza kudhani njie yetu ni sahihi kumbe njia ile ni njia ya mauti

 

Mithali 14:12 “Iko njia ionekanayo kuwa sawa machoni pa mtu, Lakini mwisho wake ni njia za mauti.”

 

Ilionekana ni sahihi kwa Uza kulinyooshea mkono Sanduku la agano ndio kwani ng’ombe walikuwa wamejikwaa na Sanduku lingeanguka isingekuwa vema machoni pa Uza ilikuwa ni sahihi lakini kumbe tukio hilo lingeleta mauti, Jambo linaweza kuonekana sahihi machoni pako lakini likawa sio sahihi machoni pa Mungu, kama mtu anataka kuufurahia uwepo wa Mungu, amani yake na uvumilivu wake hatuna budi klujifunza kutoka katika neno la Mungu na kulitendea kazi katika maisha yetu.

 

 

Na. Rev. Innocent Samuel Kamote

Mkuu wa wajenzi mwenye Hekima!


Jumanne, 29 Machi 2022

Mbweha wadogo waiharibuo mizabibu


Wimbo uliobora 2:15 “Tukamatie mbweha, Wale mbweha wadogo, Waiharibuo mizabibu, Maana mizabibu yetu yachanua.”


Utangulizi:

Kitabu cha wimbo uliobora ni mojawapo ya kitabu katika vitabu vijulikanavyo kama vitabu vya mashairi, vitabu vingine ni pamoja na Ayubu, Zaburi, Mithali, Muhubiri na kitabu hiki cha wimbo ulio bora, Katika vitabu hivi kuna mafunzo mengi sana ya hekima kuhusu maisha, na kwa kuwa ni vitabu vya mashairi wakati mwingine unaweza kukutana na lugha au misemo yenye kushangaza lakini yenye mafunzo muhimu sana kwa jamii!, kitabu cha wimbo ulio bora hata hivyo mashairi yake ni mashairi ya kimapenzi na ni mtu na mpenzi wake waliokuwa wakiimbiana na kujibizana, katikati ya mahaba yao wakaambiana maneno haya Wimbo Ulio Bora 2:15 “Tukamatie mbweha, Wale mbweha wadogo, Waiharibuo mizabibu, Maana mizabibu yetu yachanua.” Kimsingi lugha hii ni lugha ya kimashairi na inatufunza mamswala ya msingi katika Nyanja nyingi za maisha katika maeneo mbalimbali, Wafasiri wengi wa maandiko na wanatheolojia wanakiri kuwa mahusiano haya ya kimapenzi yalikuwa ni kati ya kijana wa kifalme Suleimani na mwanamke Mshulami, hata hivyo kitheolojia wimbo huu unahusu vilevile mahusiano yaliyoko kati ya Yesu na Kanisa lake. Tunajifunza somo hili kwa kuzingatia vipengele vifuatavyo:- 

1.       Mbweha wadogo waiharibuo mizabibu!

2.       Maana ya mbweha wadogo waiharibuo Mizabibu


Mbweha wadogo waiharibuo mizabibu!

Nyakati za Biblia katika Isarael hasa kutokana na geographia ya nchi ya Kanaani au Israel Mbweha walijulikana kama wanyama wadogo waharibifu, hususani kwa sababu wao walijihusisha na kilimo ikiwemo kilimo cha mizabibu, Na wanyama hawa walikuwa miongoni mwa wanyama waharibifu kwa mizabibu hususani pale inapoanza kutoa maua au kuchanua !, inawezekana kuwa wako wanyama wengi wakubwa zaidi na waharibifu, kama ilivyo Afirka tembo wanaweza kuingia kwenye mashamba ya watu na wakafanya uharibifu mkubwa kwa dakika chache, Mashariki ya kati mashamba ya mizabizu yalikuwa yakizungushiwa wigo wa mawe ili kuyalinda na wanyama waharibifu na hivyo yalikuwa salama, ona

Marko 12:1-2 “Akaanza kusema nao kwa mifano; Mtu mmoja alipanda shamba la mizabibu, akazungusha ugo, akachimba shimo la shinikizo, akajenga mnara, akapangisha wakulima, akasafiri. Hata kwa wakati wake akatuma mtumwa kwa wale wakulima, ili apokee kwa wakulima katika matunda ya mizabibu”.  

Lakini huenda hata hivyo Mbeha ndio walikuwa adui wakubwa wa mizabibu na labda zaidi sana wakati yakichanua maua. Lakini hata hivyo watu wengi waliwadharau mbweha kama wanayama wasi hatarishi sana, ukilinganisha na wengine, Kimsingi unapoiangali Biblia inaweza kumaanisha kuwa Mbweha alitumika pia au kuhesabiika miongoni mwa wanyama wanaoweza kutumika kwa uharibifu  na hivyo pamoja na kujilinda dhidi ya wanyama wengine wakubwa na waharibifu wakulima wa mizabibu hawakupaswa kabisa kuwadharau mbweha kwani nao wanachangia uharibifu hata kama watacheza cheza kwenye mashamba ya zabibu na kuangusha maua ambayo ndio asili ya kupata matunda, Ki biblia Mbweha ni mnyama aliyetumika kuonyesha hali ya uharibifu mfano Samsoni aliwatumia Mbweha kuchoma mashamba ya ngano ya wafililisti

Waamuzi 15:3-5 “Samsoni akasema, Safari hii nitakuwa sina hatia katika habari za hawa Wafilisti, hapo nitakapowadhuru. Samsoni akaenda akakamata mbweha mia tatu; kisha akatwaa vienge vya moto akawafunga mbweha mkia kwa mkia, akatia kienge kati ya kila mikia miwili. Alipokwisha kuviwasha moto vile vienge, akawaachia mbweha kati ya ngano ya Wafilisti, akayateketeza matita, na ngano, hata na mashamba ya mizeituni.”

Pia mbweha walitumika kama ishara ya dharau kubwa sana, kama kitu kilikuwa cha uongo, au chenye viwango vya chini sana au mtu mwoga kupita kawaida au chenya kuzuia mapenzi ya Mungu kilichodharaulika mno kama manabii wa uongo, au ujenzi ulio chini ya kiwango, au mtu mwoga kuliko kawaida manabii na watu wa nyakati za biblia walilitumia neno mbweha kwa kitu kilicho dharaulika mfano ona

Nehemia 4:1-5 “Lakini ikawa, Sanbalati aliposikia ya kwamba tulikuwa tukiujenga ukuta, akaghadhibika, akaingiwa na uchungu sana, akawadhihaki Wayahudi. Akanena mbele ya nduguze na mbele ya jeshi la Samaria, akisema, Wayahudi hawa wanyonge wanafanyaje? Je! Watajifanyizia boma? Watatoa dhabihu? Au watamaliza katika siku moja? Je! Watayafufua mawe katika chungu hizi za kifusi, nayo yameteketezwa kwa moto? Basi Tobia, Mwamoni, alikuwa karibu naye, akasema, Hata hiki wanachokijenga, angepanda mbweha, angeubomoa ukuta wao wa mawe. Sikia, Ee Mungu wetu; maana tunadharauliwa; ukawarudishie mashutumu yao juu ya vichwa vyao, ukawatoe watekwe katika nchi ya uhamisho; wala usiusitiri uovu wao, wala isifutwe dhambi yao, mbele zako; kwa maana wamekukasirisha mbele ya hao wanaojenga.”

Ezekiel 13:1-4 “Kisha neno la BWANA likanijia, kusema, Mwanadamu, tabiri juu ya manabii wa Israeli wanaotabiri, uwaambie wanaotabiri kwa mioyo yao wenyewe, Lisikieni neno la BWANA; Bwana MUNGU asema hivi; Ole wao manabii wajinga, wanaoifuata roho yao wenyewe, wala hawakuona neno lo lote!Ee Israeli, manabii wako wamekuwa kama mbweha, mahali palipo ukiwa.”

Luka 13:31-33 “Saa ile ile Mafarisayo kadha wa kadha walimwendea, wakamwambia, Toka hapa, uende mahali pengine, kwa sababu Herode anataka kukuua. Akawaambia, Nendeni, mkamwambie yule mbweha, Tazama, leo na kesho natoa pepo na kuponya wagonjwa, siku ya tatu nakamilika. Pamoja na hayo imenipasa kushika njia yangu leo na kesho na kesho kutwa; kwa kuwa haimkini nabii aangamie nje ya Yerusalemu.”              

Kwa hiyo suleimani na mpenzi wake walipokuwa wakiimbiana wimbo wa mapenzi na kuona kuwa penzi lao limechanua waliimbina na kupeana tahadhari kuwa watajilinda na maadui wakubwa wa mapenzi yao lakini fvilevile wasidharau maadui wadogo ambao nao wanaweza kuathiri pezni lao lisiweze kuzaa marunda, Maadui wakubwa wa mapenzi walifanannishwa na wanyama wakubwa huko Misri maadui wakubwa wa mapenzi walifananishwa na mamba, na Israel maadui wadogowadogo wa mapenzi walifananishwa na mbwea, kwa hiyo katika wimbo wao wa kimapenzi Suleimani hakutaka hata vitu vidogovidogo vinavyodhauliwa na watu,  wengi kwao visiharibu mapenzi yao kwa gharama yoyote wala viziwe tishio la mapenzi yao,  ili mahusiano yaweze kuwa imara kuna vitu vidogo vidogo vingi ambavyo havipaswi kupuuziwa, kwani vikipuuzwa navyo vinaweza kufifisha upendo, na vinaweza kuwa hatari sana hivyo wapendanao lazima wahakikishe kuwa wanajilinda dhidi ya maadui wakubwa na wale wadogowadogo ili kutunza mahusiano mema katika upendo wao,  Upendo haulindwi na kumnunulia mtu nguo pekee, au kumnunulia chakula, au kumtunza, au kumzalisha, au kumpa fedha ya saloon, au kumuachia fedha mezani, au kufanya kazi kwa bidii ili uitunze familia yako, au kushughulika sana katika tendo la ndoa au kumpa mumeo au mkeo kila siku, kuna vitu vidogovidogo sana ambavyo vinaweza kumfanya mwenzi wako ajisikie yuko peponi, leo hii watu wanagombana sana, hawasameheani, kila mmoja na simu yake, hakuna kupokeana, hakuna mazungumzo na vitu vingi ambavyo ni vya muhimu katika kujenga uhusiano hata hivyo kumbuka sitaki kuzungumzia mapenzi katika somo langu hili mimi nazungumzia maswala ya rohoni

Maana ya mbweha wadogo waiharibuo Mizabibu

Ni muhimu kufahamu kama tulivyosema awali kuwa Mbweha sio wanyama wakubwa sana wanaoweza kusababisha uharibifu mkubwa kama tembo au dubu na kadhalika, mbweha wana urefu wa inchi kama 20 na uzito kama wa kilo nane hivi, lakini tatizo lao kubwa ni kuwa wana uwezo wa kuharibu maua lakini pia kutafuna na kusababisha mzabibu kukauka na ukakosa matunda na ndio maana nyakati za Biblia licha ya kuwadharau mbweha lakini pia walikuwa na kampeni ya kuwakamata na kuwaua kabisa kutokana na uwezo wao mkubwa wa kusababisha uharibifu

Wimbo Ulio Bora 2:15 “Tukamatie mbweha, Wale mbweha wadogo, Waiharibuo mizabibu, Maana mizabibu yetu yachanua.”

Jambo kubwa analolizungumza Suleimani hapa ni kuwa mapenzi yake na Mshulami ndio yanaanza kuchanua hivyo anatoa tahadhari kwa maswala ambayo kimsingi ynaweza kuleta uharibifu mkubwa katika mahusiano  yawe ya kimapenzi yawe na watu au na Mungu, watu wengi sana wanaompokea Yesu wanaweza kuwashinda maadui wakubwa wanaoonekana kwa nje wanaweza kuwa sio waizi, wanaweza kuwa sio wazinzi, wanaweza kuwa sio walevi, wanaweza kuwa hawaviti sigara, wanaweza kuwa sio wasengenyaji, wala sio wafitini, wala sio wachonganishi, wanaweza kuwa sio wenye tamaa ya fedha lakini kuna vitu ambavyo watu wengi wanavidharau, Maswala ambayo yanaharibu maisha yetu, na kuharibu ndoa zetu, yanayoharibu ushuhuda wetu, au yanayotutia gizani, yanayoharbu mahisiano wakati mwingine sio yale yanayoonekana kwa macho wakati mwingine ni yale yaliyoko mioyoni mwetu

1.       Ubinafsi -  wanadamu wengi sana wanasumbuliwa na ubinafsi, wanataka kujitukuza wenyewe, wanataka wao wenyewe ndio wabaki juu, wajitumikie wenyewe wajifurahishe wenyewe na wawe juu yaw engine tu  Biblia inaonyesha kuwa ni watu wachache sana ambao huangalia mambo ya wengine lakini wengi sana huangalia maslahi yao

 

2Timotheo 3:2-4 “Maana watu watakuwa wenye kujipenda wenyewe, wenye kupenda fedha, wenye kujisifu, wenye kiburi, wenye kutukana, wasiotii wazazi wao, wasio na shukrani, wasio safi, wasiowapenda wa kwao, wasiotaka kufanya suluhu, wasingiziaji, wasiojizuia, wakali, wasiopenda mema, wasaliti, wakaidi, wenye kujivuna, wapendao anasa kuliko kumpenda Mungu;”

 

Kujipenda mwenyewe ni moja ya dhambi ambayo inaweza kuonekana kuwa ni ndogo lakini inaweza kusababisha madhara makubwa sana katika ndoa, familia na hata taifa au kanisa ni rahisi kufikiri kuwa ubinafsi sio tatizo lakini ni tatizo kubwa sana ambalo kwa hili wengi watakosa nafasi ya kuingia mbinguni hii ni ile hali ya mimi kwanza, mtu anaweza kuwa sio mzinzi, wala mlevi wala mwizo lakini akawa ni mbinafsi kuliko kawaida mchoyo anataka afanikiwe yeye tu

 

Luka 18:18-25 “Tena, mtu mkubwa mmoja alimwuliza, akisema, Mwalimu mwema, nifanye nini ili nipate kuurithi uzima wa milele? Yesu akamwambia, Mbona unaniita mwema? Hakuna aliye mwema ila mmoja, naye ndiye Mungu. Wazijua amri; Usizini, Usiue, Usiibe, Usishuhudie uongo, Waheshimu baba yako na mama yako. Akasema, Hayo yote nimeyashika tangu utoto wangu. Yesu aliposikia hayo alimwambia, Umepungukiwa na neno moja bado; viuze ulivyo navyo vyote, ukawagawanyie maskini, nawe utakuwa na hazina mbinguni; kisha, njoo unifuate. Lakini aliposikia hayo alihuzunika sana, maana alikuwa na mali nyingi. Yesu alipoona vile alisema, Kwa shida gani wenye mali watauingia ufalme wa Mungu! Kwa maana ni vyepesi ngamia kupita katika tundu la sindano kuliko tajiri kuingia katika ufalme wa Mungu.”

 

Tatizo kubwa la huyu tajiri ilikuwa iko dhambi ya choyo na umimi na ubinafsi ambayo yeye aliiona kama sio tatizo kubwa kwa sababu ameshika mari zote lakini kumbe alikuwa na mbweha anayeharibu mzabibu wake ambayo ni choyo na umimi na ubinafsi mkubwa kujikana nafsi sio jambo jepesi

 

Mathayo 16:24-26 “Wakati huo Yesu aliwaambia wanafunzi wake, Mtu ye yote akitaka kunifuata, na ajikane mwenyewe, ajitwike msalaba wake, anifuate. Kwa kuwa mtu atakaye kuiokoa nafsi yake, ataipoteza; na mtu atakayepoteza nafsi yake kwa ajili yangu, ataiona. Kwani atafaidiwa nini mtu akiupata ulimwengu wote, na kupata hasara ya nafsi yake? Au mtu atatoa nini badala ya nafsi yake?

 

Ubinafsi umeharibu maisha ya watu wengi duniani umeharibu mahusiano ya watu, umeharibu ndoa, umeharibu na kusababisha vita, mafarakano na migawanyiko mikubwa katika jamii, imeleta misiba mikubwa na hata vifo kwa sababu ya ubinafsi tu japo linaonekana ni jambo dogo

 

2.       Uchungu:

Watu wengi sana wanadhani ni haki wao kuwa na uchungu na hawaoni kuwa kuwa na uchungu ni dhambi inaonekana ndogo lakini ina madhara makubwa, kwa sababu ya uchungu na hofu mtu anajikuta akakosoa tu kila kitu au anakosoa mtu, linaweza lisiwe tatizo kubwa lakini biblia imaonya kwamba ni shina ambalo likiwemo ndani ya mtu linaweza kuleta madhara makubwa kwa jamii

 

Waebrania 12:14-15 “Tafuteni kwa bidii kuwa na amani na watu wote, na huo utakatifu, ambao hapana mtu atakayemwona Bwana asipokuwa nao; mkiangalia sana mtu asiipungukie neema ya Mungu; shina la uchungu lisije likachipuka na kuwasumbua, na watu wengi wakatiwa unajisi kwa hilo.”

               

3.       Kutokusamehe:

 

Kusamehe ni swala la kutangaza msamaha kwa mtu mwingine, bila kujali amakukosea nini katika maandiko kibiblia msamaha wa Mungu unahusiana na dhambi zetu lakini ili tusamehewe na Mungu sharti lake ni kuwa lazima tuwasamehe wengine  kutokuwasamehe wengine kunakuweka katika magereza ngumu ya kukufanya nawe usisamehewe na Mungu

 

Mathayo 18:21-35 “Kisha Petro akamwendea akamwambia, Bwana, ndugu yangu anikose mara ngapi nami nimsamehe? Hata mara saba? Yesu akamwambia, Sikuambii hata mara saba, bali hata saba mara sabini. Kwa sababu hii ufalme wa mbinguni umefanana na mfalme mmoja aliyetaka kufanya hesabu na watumwa wake.Alipoanza kuifanya, aliletewa mtu mmoja awiwaye talanta elfu kumi. Naye alipokosa cha kulipa, bwana wake akaamuru auzwe, yeye na mkewe na watoto wake, na vitu vyote alivyo navyo, ikalipwe ile deni. Basi yule mtumwa akaanguka, akamsujudia akisema, Bwana, nivumilie, nami nitakulipa yote pia. Bwana wa mtumwa yule akamhurumia, akamfungua, akamsamehe ile deni. Mtumwa yule akatoka, akamwona mmoja wa wajoli wake, aliyemwia dinari mia akamkamata,akamshika koo,akisema Nilipe uwiwacho. Basi mjoli wake akaanguka miguuni pake, akamsihi, akisema, Nivumilie, nami nitakulipa yote pia. Lakini hakutaka, akaenda, akamtupa kifungoni, hata atakapoilipa ile deni. Basi wajoli wake walipoyaona yaliyotendeka, walisikitika sana, wakaenda wakamweleza bwana wao yote yaliyotendeka. Ndipo bwana wake akamwita, akamwambia, Ewe mtumwa mwovu, nalikusamehe wewe deni ile yote, uliponisihi; nawe, je! Haikukupasa kumrehemu mjoli wako, kama mimi nilivyokurehemu wewe? Bwana wake akaghadhibika, akampeleka kwa watesaji, hata atakapoilipa deni ile yote. Ndivyo na Baba yangu wa mbinguni atakavyowatenda ninyi, msiposamehe kwa mioyo yenu kila mtu ndugu yake.

 

Sio rahisi kusamehe lakini inahitajika neema ya Mungu, kuachia makosa ya aina mbalimbali ambayo tumetendewa na wenzetu watu wengi sana wanafikiri kuwa wa haki ya kutokusamehe wakidhani kuwa kununa kwao na kukasirika kwao ni halali kwa Mungu, lakini ni ukweli ulio wazi kuwa mtu asiposamehe anaharibu kabisa maombi mfano katika sala ya Bwana

 

Mathayo 6: 12. “Utusamehe deni zetu, kama sisi nasi tuwasamehevyo wadeni wetu.” Watu wengi kwaajili ya kutokusamehe wamepoteza kwa Mungu na wanadamu.

 

4.       Hasira

Hasira ni mojawapo ya udhaifu ambao watu wengi wanafikiri ni sifa kuwa nazo kumbe ni moja ya tabia mbaya sana, Mtu anayeweza kujizuia asikasirike ni mtu mwenye nguvu sana kuliko anayekasirika hovyo maandiko yanatuagiza kuwa tusiache jua likachwa kabla hatujaondoa hasira vifuani mwetu  andiko hili halitii moyo kuwa na hasira lakini linatia moyo kuhakikisha kuwa tunafanya mapatano na wale tuliowakosea kwa sababu ya hasira zetu kabla jua halijachwa  na kama tutashindwa kufanya hayo mapema tunampa shetani nafasi ya kupanda mbegu ya uchungu ambayo itakuwa na kuathiri wenguine

 

Waefeso 4:26-27 “Mwe na hasira, ila msitende dhambi; jua lisichwe na uchungu wenu bado haujawatoka; wala msimpe Ibilisi nafasi.

 

Maandiko yanataka tuweke mbali na kuzifisha kabisa dhambi mbalimbali kubwa na nyinginezo tunazozidharau ikiwepo hasira na ghadhabu

 

Wakolosai 3:5-8 “Basi, vifisheni viungo vyenu vilivyo katika nchi, uasherati, uchafu, tamaa mbaya, mawazo mabaya, na kutamani, ndiyo ibada ya sanamu; kwa ajili ya mambo hayo huja ghadhabu ya Mungu. Katika hayo ninyi nanyi mlitembea zamani, mlipoishi katika hayo. Lakini sasa yawekeni mbali nanyi haya yote, hasira, na ghadhabu, na uovu, na matukano, na matusi vinywani mwenu

 

Ni hasira iliyomfanya Musa na Haruni kukataliwa na Mungu kuingia katika inchi ya mkanaani 


Hesabu 20:12 “Bwana akamwambia Musa na Haruni, Kwa kuwa hamkuniamini mimi, ili kunistahi mbele ya macho ya wana wa Israeli, basi kwa sababu hiyo, hamtawaingiza kusanyiko hili katika ile nchi niliyowapa.”Hasira za Musa zikamfanya azungumze na kutenda mambo yasiyopasa ona 


Zaburi 106:32-33. “Wakamghadhibisha penye maji ya Meriba, Hasara ikampata Musa kwa ajili yao, Kwa sababu waliiasi roho yake, Akasema yasiyofaa kwa midomo yake.”Kutokana na kujaa ghadhabu Nabii Musa alimkosea Mungu na kupata hasara kwa kuzungumza na kutenda yasiyofaa watu wengi sana wamepata hasara kwa sababu ya hasira zilizowapelekea kutenda na kunena yasiyofaa hao ni mbweha wadogo wanaoharibu mizabibu

 

5.       Wivu.

 

Ni hali ya kutokujisikia vizuri kwa sababu ya mafanikio ya mtu mwingine, ubora wake, mafanikio yake na kibali chake au bahati yake wako watu wanaumia sana wanapoona wengine wamefanikiwa, wameolewa wao hawajaolewa, wamefanikiwa wao bado, wamefaulu wao wamefeli, wanakibali wao hawana, wanakubaliwa na Mungu wao hawana kitu na wanajisikia vibaya kiasi cha kukasirika kukosoa na hata kubeza ana wakati mwingine hata kuua kwa sababu ya wivu wenye uchungu ona

 

Mwanzo 4:3-5 “Ikawa hatimaye Kaini akaleta mazao ya ardhi, sadaka kwa BWANA. Habili naye akaleta wazao wa kwanza wa wanyama wake na sehemu zilizonona za wanyama. BWANA akamtakabali Habili na sadaka yake; bali Kaini hakumtakabali, wala sadaka yake. Kaini akaghadhibika sana, uso wake ukakunjamana.”

 

Hali kama hii ilimtokea pia kaka mkubwa katika Mfano ule wa mwana mpotevu pale alipoona ndugu yake aliyepotea na akarudi japo alichukua mali za baba yake kama sehemu ya urithi unaomuangukia akaenda kuzitapanya na makahaba aliporejea baba yake alimpokea kwa furaha lakini kaka mkubwa aliposikia alisusa na kulaumu maamuzi ya baba yake

 

Luka 15:11-32 “Akasema, Mtu mmoja alikuwa na wana wawili; yule mdogo akamwambia babaye, Baba, nipe sehemu ya mali inayoniangukia. Akawagawia vitu vyake. Hata baada ya siku si nyingi, yule mdogo akakusanya vyote, akasafiri kwenda nchi ya mbali; akatapanya mali zake huko kwa maisha ya uasherati. Alipokuwa amekwisha tumia vyote, njaa kuu iliingia nchi ile, yeye naye akaanza kuhitaji. Akaenda akashikamana na mwenyeji mmoja wa nchi ile; naye alimpeleka shambani kwake kulisha nguruwe.Akawa akitamani kujishibisha kwa maganda waliyokula nguruwe, wala hapana mtu aliyempa kitu. Alipozingatia moyoni mwake, alisema, Ni watumishi wangapi wa baba yangu wanaokula chakula na kusaza, na mimi hapa ninakufa kwa njaa. Nitaondoka, nitakwenda kwa baba yangu na kumwambia, Baba, nimekosa juu ya mbingu na mbele yako;sistahili kuitwa mwana wako tena; nifanye kama mmoja wa watumishi wako. Akaondoka, akaenda kwa babaye. Alipokuwa angali mbali, baba yake alimwona, akamwonea huruma, akaenda mbio akamwangukia shingoni, akambusu sana. Yule mwana akamwambia, Baba, nimekosa juu ya mbingu na mbele yako; sistahili kuitwa mwana wako tena. Lakini baba aliwaambia watumwa wake, Lileteni upesi vazi lililo bora, mkamvike; mtieni na pete kidoleni, na viatu miguuni;mleteni ndama yule aliyenona mkamchinje; nasi tule na kufurahi; kwa kuwa huyu mwanangu alikuwa amekufa, naye amefufuka; alikuwa amepotea, naye ameonekana. Wakaanza kushangilia. Basi, yule mwanawe mkubwa alikuwako shamba na alipokuwa akija na kuikaribia nyumba, alisikia sauti ya nyimbo na machezo. Akaita mtumishi mmoja, akamwuliza, Mambo haya, maana yake nini? Akamwambia, Ndugu yako amekuja, na baba yako amemchinja ndama aliyenona, kwa sababu amempata tena, yu mzima. Akakasirika, akakataa kuingia ndani. Basi babaye alitoka nje, akamsihi. Akamjibu baba yake, akasema, Tazama, mimi nimekutumikia miaka mingapi hii, wala sijakosa amri yako wakati wo wote, lakini hujanipa mimi mwana-mbuzi, nifanye furaha na rafiki zangu;  lakini, alipokuja huyu mwana wako aliyekula vitu vyako pamoja na makahaba, umemchinjia yeye ndama aliyenona. Akamwambia, Mwanangu, wewe u pamoja nami sikuzote, na vyote nilivyo navyo ni vyako. Tena, kufanya furaha na shangwe ilipasa, kwa kuwa huyu ndugu yako alikuwa amekufa, naye amefufuka; alikuwa amepotea, naye ameonekana.”

 

Wako watu wana wivu wa ajabu sana kwa sababu wanachukizwa na neema ya Mungu iliyojuu yako hata wanaposikia umekosea wanatamani kama Mungu angekuua au kukutupilia mbali jehanamu ya moto, hawataki kabisa kuona Mungu amekurehemu na anaendelea kukubariki hii ni tabia mbaya sana na hawa ni mbweha waharibuo mzabimu, Bwana ampe neema kila mmoja kuwa mbali na wivu wenye uchungu katika jina la Yesu.

 

6.       Unafiki.

 

Watu wengi sana ni wanafiki, unafiki ni tabia ya kuigiza pretending Mungu hapandezwi na unafiki, kujipendekeza na kutaka sifa ili hali moyo wako uko mbali naye au na mapenzi yake 


Mathayo 15:7-9 “ Enyi wanafiki, ni vema alivyotabiri Isaya kwa habari zenu, akisema, Watu hawa huniheshimu kwa midomo; Ila mioyo yao iko mbali nami. Nao waniabudu bure, Wakifundisha mafundisho Yaliyo maagizo ya wanadamu.” 


Unafiki ni dhambi inayooenakana kuwa ni ya kawaida sana kwa watu wengi wanaodai kuwa wanamcha Mungu, bila kujua kuwa Mungu anachukizwa na jambo hili na Mungu alimuadhibu vikali Anania na mkewe kwa sababu ya dhambi ya unafiki 


Matendo ya mitume 5:1-10 “Lakini mtu mmoja jina lake Anania, pamoja na Safira mkewe, aliuza mali,akazuia kwa siri sehemu ya thamani yake, mkewe naye akijua haya, akaleta fungu moja akaliweka miguuni pa mitume. Petro akasema, Anania, kwa nini Shetani amekujaza moyo wako kumwambia uongo Roho Mtakatifu, na kuzuia kwa siri sehemu ya thamani ya kiwanja?Kilipokuwa kwako, hakikuwa mali yako? Na kilipokuwa kimekwisha kuuzwa, thamani yake haikuwa katika uwezo wako? Ilikuwaje hata ukaweka neno hili moyoni mwako? Hukumwambia uongo mwanadamu, bali Mungu. Anania aliposikia maneno haya akaanguka, akafa. Hofu nyingi ikawapata watu wote walioyasikia haya. Vijana wakaondoka, wakamtia katika sanda, wakamchukua nje, wakamzika. Hata muda wa saa tatu baadaye mkewe akaingia, naye hana habari ya hayo yaliyotokea. Petro akamjibu, Niambie, Mlikiuza kiwanja kwa thamani hiyo? Akasema, Ndiyo, kwa thamani hiyo. Petro akamwambia, Imekuwaje hata mkapatana kumjaribu Roho wa Bwana? Angalia, miguu yao waliomzika mumeo ipo mlangoni, nao watakuchukua nje wewe nawe.Mara akaanguka miguuni pake akafa; wale vijana wakaingia wakamkuta amekufa, wakamchukua nje, wakamzika pamoja na mumewe.”

 

Kwa hiyo utaweza kuona dhambi zile tunazazidharau na kuzifikiri kuwa ni ndogo zina athari kubwa sana katika kuharibu uhusiano wetu na Mungu na hivyo nazo Mungu anataka tuzishughulikie

 

7.       Choyo:

 

Maandiko yanatahadharisha sana kuhusu choyo, watu wengi sana ni wachoyo, na watu wengi sana wanapenda kujimilikisha vitu vingi wakifikiri kuwa kwa kuwa na vitu watakuwa na uzima Yesu aktika mafundisho yake alionya kuhusu choyo anasema katika Luka 12:15 “Akawaambia, Angalieni, jilindeni na choyo, maana uzima wa mtu haumo katika wingi wa vitu vyake alivyo navyo.” Wako watu wana masanduku na nguo zimejaa kwenye begi zao masanduku mengine yamejaa mpaka zipu zimeachia au wanashundilia kwa miguu wakati wa kuyafunga lakini hawagawi Yesu akikolezea mungu mafundisho yake alionya kuwa sisi ni wapitaji tu katika ulimwengu huu na hivyio kujilimbikizia au mpango wa kujilimbikizia hautatufikisha kokote 


Luka 12:16-20 “Akawaambia mithali, akisema, Shamba la mtu mmoja tajiri lilikuwa limezaa sana;akaanza kuwaza moyoni mwake, akisema, Nifanyeje? Maana sina pa kuyaweka akiba mavuno yangu.  Akasema, Nitafanya hivi; nitazivunja ghala zangu, nijenge nyingine kubwa zaidi, na humo nitaweka nafaka yangu yote na vitu vyangu. Kisha, nitajiambia, Ee nafsi yangu, una vitu vyema vingi ulivyojiwekea akiba kwa miaka mingi; pumzika basi, ule, unywe, ufurahi. Lakini Mungu akamwambia, Mpumbavu wewe, usiku huu wa leo wanataka roho yako! Na vitu ulivyojiwekea tayari vitakuwa vya nani?                


choyo ni moja ya mbweha wadogo na waharibifu, kuna choyo za aina nyingi, moja ya choyo maarufu sana katika mapenzi na inayokera na kuharibu mahusiano ni pamoja na kunyimana tendo la ndoa aina hii ya choyo imeharibu mapenzi sana na watu wengi wameachana kwa sababu wako wanaotumia fursa ya tendo la ndoa kuwekea mgomo na kuesa nafsi za wengine aina hii ya choyo imekemewa vikali katika maandiko 


1Wakoritho 7:1-5 “Basi kwa habari ya mambo yale mliyoandika, ni heri mwanamume asimguse mwanamke. Lakini kwa sababu ya zinaa kila mwanamume na awe na mke wake mwenyewe, na kila mwanamke na awe na mume wake mwenyewe. Mume na ampe mkewe haki yake, na vivyo hivyo mke na ampe mumewe haki yake. Mke hana amri juu ya mwili wake, bali mumewe; vivyo hivyo mume hana amri juu ya mwili wake, bali mkewe. Msinyimane isipokuwa mmepatana kwa muda, ili mpate faragha kwa kusali; mkajiane tena, Shetani asije akawajaribu kwa kutokuwa na kiasi kwenu.”  Neno la  Mungu linatahadharisha pia kuhusiana na jambo hili na ain azote za choyo Bwana na ampe neema kila mmoja wetu kujilinda na choyo za aina mbalimbali ili tuwe na mahusiano imara kwa Mungu na wanadamu        

Athari za kutokukamata mbweha wadogo:-

-          Kunatokea kumzimisha Roho Mtakatifu Wathesalonike 5:19Msimzimishe Roho;”

-          Tunashindwa kuzaa matunda ya Roho Wagalatia 5:19-23 “Basi matendo ya mwili ni dhahiri, ndiyo haya, uasherati, uchafu, ufisadi, ibada ya sanamu, uchawi, uadui, ugomvi, wivu, hasira, fitina, faraka, uzushi, husuda, ulevi, ulafi, na mambo yanayofanana na hayo, katika hayo nawaambia mapema, kama nilivyokwisha kuwaambia, ya kwamba watu watendao mambo ya jinsi hiyo hawataurithi ufalme wa Mungu. Lakini tunda la Roho ni upendo, furaha, amani, uvumilivu, utu wema, fadhili, uaminifu, upole, kiasi; juu ya mambo kama hayo hakuna sheria.”

-          Tunapoteza furaha Zaburi 51:11-12Usinitenge na uso wako, Wala roho yako mtakatifu usiniondolee. Unirudishie furaha ya wokovu wako; Unitegemeze kwa roho ya wepesi.”

-          tunapoteza amani Wafilipi 4:7 “Na amani ya Mungu, ipitayo akili zote, itawahifadhi mioyo yenu na nia zenu katika Kristo Yesu.”

-          inaharibu uhusiano na Mungu 1Yohana 1:3 “hilo tuliloliona na kulisikia, twawahubiri na ninyi; ili nanyi pia mpate kushirikiana nasi: na ushirika wetu ni pamoja na Baba, na pamoja na Mwana wake Yesu Kristo.”


-          Tunapoteza ujasiri katika maombi Warumi 8:26Kadhalika Roho naye hutusaidia udhaifu wetu, kwa maana hatujui kuomba jinsi itupasavyo, lakini Roho mwenyewe hutuombea kwa kuugua kusikoweza kutamkwa.”

-          tunakuwa waoga 1Yohana 2:28Na sasa, watoto wadogo, kaeni ndani yake, ili kusudi, atakapofunuliwa, mwe na ujasiri, wala msiaibike mbele zake katika kuja kwake.”

Dhambi hizo tunazofikiri kuwa sio tatizo katika maisha yetu zinatuletea athari na kuharibu hali yetu ya kiroho na wakati mwingine kuturudisha nyuma na kuharibu uhusiano wetu na Yesu, hatuna budi kuhakikisha tunashughulikia maswala ya ndani tunayofafikiri kuwa ni madogo madogo na kumbe yanaharibu sana uhusiano wetu na Mungu, ukiyajua hayo heri wewe ukiyatenda.

Na mkuu wa wajenzi mwenye Hekima!

Rev. Innocent Samuel Kamote