Marko 3:13-15 “Akapanda mlimani, akawaita
aliowataka mwenyewe; wakamwendea. Akaweka watu kumi na wawili, wapate kuwa
pamoja naye, na kwamba awatume kuhubiri, tena wawe na amri ya kutoa pepo.”
Pichani ni Reverend Innocent Samuel Kamote, aka. Mkuu wa wajenzi Mwenye Hekima
Utangulizi:
Leo tutachukua muda kuzungumzia
miongozo inayoweza kutusaidia na kutukumbusha wajibu wetu kama wahudumu katika
jamii, namna na jinsi inavyotupasa kuenenda miongoni mwa wale tunaowahudumia,
kuwa Muhudumu wa jamii na hasa kiongozi wa kiimani, kisiasa na katika jamii
kunahitaji neema ya Mungu, na nidhamu ya hali ya juu, na muongozo
utakaotusaidia kuweza kuifanya huduma hii kwa unyenyekevu na ufanisi mkubwa
tukimpendeza Mungu na wanadamu, hii ni muhimu sana kwetu kusudi tusiwe watu wa
kukataliwa hususani na baba yetu wa Mbinguni.
1Wakorintho 9:25-27 “Na kila ashindanaye
katika michezo hujizuia katika yote; basi hao hufanya hivyo kusudi wapokee taji
iharibikayo; bali sisi tupokee taji isiyoharibika. Hata mimi napiga mbio vivyo
hivyo, si kama asitaye; napigana ngumi vivyo hivyo, si kama apigaye hewa; bali
nautesa mwili wangu na kuutumikisha; isiwe, nikiisha kuwahubiri wengine,
mwenyewe niwe mtu wa kukataliwa.”
Falsafa za utumishi ni muongozo
au dondoo zinazotusaidia kutupa picha ya utumishi wetu mzima kwa jamii, na kutusaidia
kujua wajibu wetu kama viongozi namna na jinsi inavyotupasa kuenenda ili
kutimiza kusudi letu kubwa ambalo Mungu ametupa kwaajili ya kuitumikia jamii,
wajibu huo unahitaji nidhamu, nidhamu ambayo wanamichezo wanayo na huishika ili
wapokee taji au kombe liharibikalo, na pia kwaajili ya kulinda umahiri wao
wakati wanaposhiriki michezo, lakini sisi tunahitaji kujitia nidhamu ili
tupokee taji isiyoharibika. Paulo anasema naye ana fanya zoezi (Nidhamu ya kiroho) hilo kila siku la kujitia
nidhamu ili hatimaye asijekuwa mtu wa kukataliwa, anataka kuwaongoza wengine
lakini bila kuingia matatani na mwajiri wetu ambaye ni Mungu kwa hiyo ili jambo
hili liweze kufanikiwa tunahitaji muongozo wa kutusaidia kuelewa sisi ni nani,
tunapaswa kufanya nini, tunafanyaje na tunatimizaje kusudi zima la huduma
ambayo Mungu ametupa kuwasaidia watu wake, tutajifunza somo hili Falsafa za
Huduma kwa kuzingatia vipengele viwili vifuatavyo:-
·
Maana ya
Falsafa
·
Falsafa
za utumishi
Maana ya Falsafa:
Neno falsafa limetokana na Neno
la kiingereza Philosophy ambalo kwa asili ni neno la Kiyunani Philosophy yaani Muungangiko wa neno “Phileo” na “Sophia” Phileo ni Upendo na Sophia
ni Hekima neno hili liligunduliwa na
Mwanafalsafa wa kiyunani aliyejulikana kama Pythagoras ambaye yeye
alisema kwa kuwa Mungu ndiye Mwanzilishi wa Hekima basi ukimcha Mungu au
ukimpenda Mungu utakuwa na hekima au maarifa, Neno Philosophy kwa hiyo ni kupenda Hekima, au kwa ufupi ni Hekima tukilitohoa neno hilo
tunapata neno Falsafa katika Kiswahili.
Mithali 1:5-7 “mwenye hekima asikie na
kuongezewa elimu, na mwenye ufahamu ayafikie mashauri yenye njia. Kufahamu
mithali na kitendawili, na maneno ya wenye hekima na mafumbo yao. Kumcha Bwana
ni chanzo cha maarifa, Bali wapumbavu hudharau hekima na adabu.”
Kazi kubwa ya falsafa ni kutoa
muongozo, na kutatua changamoto zozote zinazowakuta wanadamu kwa kutoa kweli
zitakazodumu milele zikiwaongoza wanadamu kuishi na kutenda na kuenenda kwa
busara, Falsafa inafanya kazi katika mazingira yote na pasipo falsafa jamii
inapoteza muelekeo, kila jamii yenye maendeleo makubwa ni jamii iliyofuata
falsafa iliyo bora, walijiwekea falsafa wakaifanyia kazi ikawaongoza na kuleta
matokeo yanayokusudiwa!
Kwa hiyo katika somo hili
tutakuwa tukijifunza sasa dondoo au falsafa za utumishi, yaani miongozo ambayo
itatusaidia kama viongozi wa jamii, siasa na imani, kutupa hekima na akili ya
namna ya kuwahudumia watu na watu hawa wakaridhika huku sisi nasi tukibaki kuwa
salama katika utumishi wetu na huduma zetu.
Falsafa za utumishi.
# 1. Kwaajili ya utukufu wa Mungu.
Utumishi wowote
ule ambao Mungu ametupa, iwe ni katika siasa, au jamii au kanisa yaani kiimani
kusudi lake kubwa ni ili Mungu atukuzwe, ili Mungu ainuliwe, ili sifa na
utukufu na heshima zimrudie Mungu.
Isaya 43:7 “Kila
mmoja aliyeitwa kwa jina langu, niliyemwumba kwa ajili ya utukufu wangu; mimi
nimemwumba, naam, mimi nimemfanya.”
Kila mtu duniani
ameumbwa kwaajili ya utukufu wa Mungu, kwa hiyo viongozi wote wa kijamii,
kisiasa na kiimani ni lazima tukumbuke kumpa Mungu utukufu, kuhakikisha ya kuwa
kila tunalolifanya katika jamii kutoka moyoni tunalifanya kwaajili ya utukufu
wa Mungu, Yesu aliwafundisha wanafunzi wake wakati wote kukumbuka kuwa
wanapofanya jambo wajiambie nafsi zao kuwa wao ni watumishi tu wasio na faida
Luka 17:7-10 “Lakini,
ni nani kwenu mwenye mtumwa alimaye au achungaye ng'ombe, atakayemwambia mara
arudipo kutoka shambani, Njoo upesi, keti, ule chakula? Je! Hatamwambia,
Nifanyie tayari chakula, nile; jifunge unitumikie, hata niishe kula na kunywa,
ndipo nawe utakapokula na kunywa? Je! Atampa asante yule mtumwa, kwa sababu
ameyafanya aliyoagizwa? Vivyo hivyo nanyi, mtakapokwisha kuyafanya yote
mliyoagizwa, semeni, Sisi tu watumwa wasio na faida; tumefanya tu yaliyotupasa
kufanya.”
Mungu
atakapokuwa anatoa hukumu yake kwa kazi zetu tulizozifanya hatahukumu si tu kwa
kile tulichokifanya lakini atahukumu kwanini tunafanya, yaani nia yetu ya
kufanya tunachokifanya.
Katika nyakati
zetu za leo tulizo nazo kumekuweko watu wanaotafuta kubeba utukufu kwa sababu
zisizo hata na msingi, wakati Fulani Mke wangu alikwenda kuombewa na nabii
mmoja ambaye alivuma sana katika mji wa Tanga, kwa hiyo mke wangu alikuwa na
hitaji lake ambalo kimsingi mimi nalifahamu na Mungu alishasema na mimi kuhusu
changamoto ya mke wangu hata kabla ya kumuoa, Lakini alishawishiwa na baba
yangu mzazi kwenda kwa nabii huyo na kwa heshima ya baba yangu na hitaji la mke
wangu nilimuacha aende, kwa nasibu baada ya maombezi ya nabii yule alimwambia
mke wangu amlete mumewe, na kwa sababu ya kuheshimu watu wa Mungu niliamua
kwenda kwa nabii yule, nilihudhuria ibada ambapo kulikuwa na ibada ya sifa na
neno la utangulizi kabla nabii hajatokea, ibada ya sifa ilikuwa nzuri sana na
kisha neno la Utangulizi, neno la utangulizi lilikuwa likiwaandaa waamini
kukutana na nabii na kumuamini nabii, “hakuna shaka katika hilo kwa sababu neno
linasema mwaminini Mungu nanyi mtathibitika waaminini manabii wake nanyi
mtafanikiwa” Lakini katika ibada ile maandiko
mengi sana yalitumika kutuelekeza namna ya kumpokea nabii na kulikuwa na
vitisho vingi sana ikiwa ni pamoja na maelekezo kuwa nabii akikuchagua kama
anataka kukuhudumua utapiga magoti chini wakati wa kuzungumza naye, hayo
hayakuwa na shida yoyote, ibada ile ya utangulizi iliisha na kisha nabii
alikuja alikuwa ni kijana mdogo na ukilinganisha na umri wangu, alikuwa ameanza
huduma miaka kama mitatu tu na mimi nikiwa katika huduma zaidi ya miaka 20 sina
neno na umri wa kihuduma kwa sababu hayana msingi katika Kristo, lakini ibada
ya kinabii ilipoisha nilitakiwa kwenda ofisini kuonana naye kwa sababu yeye
ndiye aliniita, nilikuwa nimevaa suti yangu nyeusi safi sana na nabii alikuwa
na shati lake na jinsi wala hakuwa amechomekea shati lile mimi nilivaa kiatu
cheusi cha kupiga kiwi na nabii alikuwa na raba tu, hilo nalo halikuwa na
shida, wakati nikielekea ofisini kwake niliambiwa na binti mdogo sana kwamba
nivue viatu vyangu ninapokwenda ofisini kwa nabii, nilisita sana kwa sababu
nabii mwenyewe alikuwa na viatu na aliingia navyo ofisini kwake na jingo lile
halikuwa kanisa lingekuwa kanisa nadhani hakungekuwa na shida kuvua viatu,
nimewahi kuvua viatu nilipotembelea msikiti wa wahindu kwa sababu nilipeleka
wanafunzi wangu wa somo la dini za ulimwengu kujifunza Imani za watu mbalimbali
hivyo kule haikuwa shida, kwani hata shekhe wa wahindu nay eye alivua viatu, lakini kwa vile ni ofisi za watu na
niliamuriwa kuvua viatu vyangu, nilivua viatu vyangu na kuingia, nilisalimiana
naye na akanijulia hali na akaniuliza vipi mtumishi wa Mungu nilimueleza kuwa
changamoto ya mke wangu ilitoka kwa Mungu na Mungu alishasema na mimi hata
kabla sijamuoa, kwa hiyo hakuna nabii anaweza kuitangua! tulisalimiana na kisha
tuliagana hakuthubutu hata kuniombea, kwa sababu na mimi nilimuomba Mungu upako
na utishio mkubwa sana kwa hiyo aliniogopa, nilitoka na kuvaa viatu vyangu na
nilipotoka katika mlango wa ofisi nilimkazia macho binti yule aliyeniambia
nivue viatu, ilihali nabii mwenyewe yeye hakuvua viatu vyake, kisha nikaondoka
zangu. Kitu nilichojifunza pale ni kuwa watu wanatishiwa sana ili watuone sisi
watumishi wa Mungu kama malaika au kuwa sisi ni watu maalumu sana, wakati
ukweli unabaki tu kuwa sisi ni wanadamu
ni watumwa wa Yesu Kristo tusio na faida watu wana mbwembwe nyingi sana, na
makeke mengi ya kujitangaza wao kuliko Kristo, mimi nimelelewa kiroho Pale
Mwenge kwa Akofu @Zachary Kakobe, tangu nikiwa Makongo secondary kidato cha
pili, na kanisani nilikuwa nakaa viti vya mbele mstari wa kwanza kabisa katika ukumbi namba moja naujua UTISHO wa kimungu na mimi mwenyewe nimetembea na utisho wa kimungu
kwa hiyo, Na nilimuona Mchungaji wangu
Kakobe akiwa na utisho na mimi haukunisumbua, ila pepo ndio walisumbuka, mimi
mwenyewe naujua utisho wa Mungu na nimetembea nao, niliwahi kwenda hoteli moja
na rafiki yangu na tukaongea na muhudumu aliyetuhudumia na kisha tulifurahi kwa
huduma yake na hivyo tulitaka kumbariki wakati tunatamka Baraka kumuombea kumbe
alikuwa na mapepo aliagunshwa chini na kupiga makelele nikamkemea pepo nab inti
yule akawa huru, kumbuka ilikuwa tu hotelini, sio ile mikwara ya kibinadamu, watu
tunaomtumikia Mungu tuache vitimbi vyovyote vya kutafuta utukufu usio sahihi,
tunaweza kujitengenezea mauti kwa sababu tu ya kuchukua utukufu wa Mungu au
kutaka sifa kutoka kwa wanadamu, watu wote walionizidi umri mimi huwaamkia shikamoo,
hata baada ya salamu za kidini, siwezi kumpigisha magoti mtu aliyenizidi umri,
lakini naogopa pia magoti kwa sababu yameumbwa kwaajili ya ibada nayaona magoti
ni kama mali ya Mungu, tusiharibu utumishi wetu kwa kujifanya kuwa sisi ji
miungu watu au watu maalumu sana. Upako kama upo upo tu na kama hakuna hakuna
Matendo 12:20-23 “Naye
Herode alikuwa amewakasirikia sana watu wa Tiro na Sidoni; wakamwendea kwa nia
moja, na wakiisha kufanya urafiki na Blasto, mwenye kukitunza chumba cha mfalme
cha kulalia, wakataka amani; kwa maana nchi yao ilipata riziki kwa nchi ya
mfalme. Basi siku moja iliyoazimiwa, Herode akajivika mavazi ya kifalme,
akaketi katika kiti cha enzi, akatoa hotuba mbele yao.Watu wakapiga kelele,
wakisema, Ni sauti ya Mungu, si sauti ya mwanadamu. Mara malaika wa Bwana
akampiga, kwa sababu hakumpa Mungu utukufu; akaliwa na chango, akatokwa na roho.”
Herode alikuwa
kiongozi wa kisiasa katika jamii, alikuwa na mamlaka aliweza hata kuwafunga na
kuwahukumu watu wa kanisa, siku moja alipokuwa akihutubia watu walishangilia
hutuba yake wakasema si mwanadanu anayenena ni Mungu, akiwa katika mavazi yake
ya kifahari, Malaika wa bwana alikuja kumpiga na stroke na akafa pale pale,
Mungu anapokuweka katika nafasi yoyote ile kumbuka kujishusha na ukiona watu
wanakusifia sana kataa sifa hizo zisizo na msingi, wakumbushe watu kuwa ni
wajibu wangu/wetu kuwahudumia kwa sababu Mungu ameniweka niwahudumie, lakini
kama tunafanya huduma hizi katika jamii na tukalewa sifa kiasi cha kujisahau
kuwa sisi ni wanadamu tunaweza kupatwa na mabaya, Paulo Mtume na Barnaba
walikataa kupokea ibada walirarua mavazi yao na kuwakumbusha watu kuwa wao sio
Mungu, wao ni wanadamu kama walivyo wanadamu wengine wenye mwili na nyama
Matendo 14:8-15 “Na
huko Listra palikuwa na mtu mmoja, dhaifu wa miguu, kiwete tangu tumboni mwa
mamaye, ambaye hajaenda kabisa. Mtu huyo alimsikia Paulo alipokuwa akinena;
ambaye akamkazia macho na kuona ya kuwa ana imani ya kuponywa, akasema kwa
sauti kuu, Simama kwa miguu yako sawasawa. Akasimama upesi akaenda. Na makutano
walipoona aliyoyafanya Paulo wakapaza sauti zao, wakisema kwa Kilikaonia,
Miungu wametushukia kwa mifano ya wanadamu. Wakamwita Barnaba, Zeu, na Paulo,
Herme, kwa sababu ndiye aliyekuwa mnenaji. Kuhani wa Zeu ambaye hekalu lake lilikuwa
mbele ya mji, akaleta ng'ombe na taji za maua hata malangoni, akitaka kutoa
dhabihu pamoja na makutano. Walakini mitume Barnaba na Paulo, walipopata
habari, wakararua nguo zao, wakaenda mbio wakaingia katika makutano, wakipiga
kelele, wakisema, Akina bwana, mbona mnafanya haya? Sisi nasi tu wanadamu hali
moja na ninyi; twawahubiri habari njema, ili mgeuke na kuyaacha mambo haya ya
ubatili na kumwelekea Mungu aliye hai, aliyeumba mbingu na nchi na bahari na
vitu vyote vilivyomo;”
Kwa hiyo ni
muhimu kukumbuka kuwa tunawahudumia watu wa Mungu, sisi ni watumishi wa Mungu
yaani watumwa wa Mungu, hatuko kwaajili ya kutafuta mambo makubwa, kuhudumia watu
ni wajibu wetu hatupaswi, kulazimisha kutafuta heshima Mungu mwenyewe
atatuheshimu kadiri tunavyojitoa katika utumishi wetu, na kufanya kila
tulifanyalo hakikisha ya kuwa unalifanya kwa utukufu wa Mungu na upendo.
Yeremia
45:5 “Je! Unajitafutia mambo makuu? Usiyatafute;
kwa maana tazama, nitaleta mabaya juu ya wote wenye mwili, asema Bwana; lakini
roho yako nitakupa iwe nyara, katika mahali pote utakapokwenda.”
1Wakorintho 10:31 “Basi,
mlapo, au mnywapo, au mtendapo neno lo lote, fanyeni yote kwa utukufu wa Mungu.”
Yohana 12:26 “Mtu
akinitumikia, na anifuate; nami nilipo, ndipo na mtumishi wangu atakapokuwapo.
Tena mtu akinitumikia, Baba atamheshimu.”
Kwa hiyo falsafa
ya kiutumishi inatukumbusha kuwa wacha Mungu, inatukumbusha ubinadamu wetu sisi
ni wadhaifu Mungu ni Muumba, kiumbe kamwe hakiwezi kulinganishwa na Mungu kwa
sababu zozote zile, wakati wote hatunabudi kuhakikisha kuwa sisi tunapungua na
Mungu anazidi.
Yohana 3:27-30 “Yohana
akajibu, akasema, Hawezi mtu kupokea neno lo lote isipokuwa amepewa kutoka
mbinguni. Ninyi wenyewe mwanishuhudia ya kwamba nalisema, Mimi siye Kristo,
bali nimetumwa mbele yake. Aliye naye bibi arusi ndiye bwana arusi; lakini
rafiki yake bwana arusi, yeye anayesimama na kumsikia, aifurahia sana sauti
yake bwana arusi. Basi hii furaha yangu imetimia. Yeye hana budi kuzidi, bali
mimi kupungua.”
Isaya 42:6-8 “Mimi,
Bwana, nimekuita katika haki, nami nitakushika mkono, na kukulinda, na kukutoa
uwe agano la watu, na nuru ya mataifa; kuyafunua macho ya vipofu, kuwatoa
gerezani waliofungwa, kuwatoa wale walioketi gizani katika nyumba ya kufungwa.
Mimi ni Bwana; ndilo jina langu; na utukufu wangu sitampa mwingine, wala
sitawapa sanamu sifa zangu.”
# 2. Kwaajili ya kuwa Pamoja na Mungu
Moja ya sababu
kubwa kwanini Mungu alimuumba mwanadamu, ilikuwa ni pamoja na kuwa na ushirika
naye, Mungu anatamani sana kufanya kazi pamoja na mwanadamu duniani, ile dhana
ya Mungu pamoja na wanadamu yaani Imanuel (Mungu Pamoja nasi) lilikuwa ni wazo
la Mungu la zamani sana na ambalo lilihariiwa katika bustani ya Edeni baada ya
anguko, baadaye Mungu atakuja kulitimiza mwisho wa nyakati.
Ufunuo 21:1-3 “Kisha
nikaona mbingu mpya na nchi mpya; kwa maana mbingu za kwanza na nchi ya kwanza
zimekwisha kupita, wala hapana bahari tena. Nami nikauona mji ule mtakatifu,
Yerusalemu mpya, ukishuka kutoka mbinguni kwa Mungu, umewekwa tayari, kama
bibi-arusi aliyekwisha kupambwa kwa mumewe. Nikasikia sauti kubwa kutoka katika
kile kiti cha enzi ikisema, Tazama, maskani ya Mungu ni pamoja na wanadamu,
naye atafanya maskani yake pamoja nao, nao watakuwa watu wake. Naye Mungu
mwenyewe atakuwa pamoja nao.”
Yesu Kristo
alipokuwa anawachagua viongozi yaani mitume ambao wangekuwa wasaidizi wa kazi
zake duniani mwandishi wa injili anaonyesha kuwa pamoja na kuwatuma wale mitume
ambao ni viongozi moja ya maswala ya msingi ni pamoja na watu hao kuwa pamoja
naye angalia mkazo wa neno wapate kuwa pamoja naye kama msingi kwa kwanza,
kisha wafanye kazi yake, kisha wawe na mamlaka dhidi ya Pepo wabaya!
Marko 3:13-15 “Akapanda
mlimani, akawaita aliowataka mwenyewe; wakamwendea. Akaweka watu kumi na
wawili, wapate kuwa pamoja naye, na kwamba awatume kuhubiri, tena wawe na amri
ya kutoa pepo.”
Hii maana yake
ni nini? Mungu anataka viongozi wa
kisiasa na kijamii na kimani kuwa wenziwake maana yake wawe na ushirika wa
kudumu pamoja na yeye, Kimsingi hatuwezi kuzaa matunda kama tunakuwa nje ya
uwepo wa Mungu, Ili amani na uwiano wa kibnadamu ulio bora uwepo viongozi ni
lazima wawe marafiki wa Mungu, (wawe wacha Mungu) Baba yetu Ibrahimu alikuwa
rafiki yake Mungu, Daudi mfalme yule mkuu katika Israel aliyekuwa na mafanikio
makubwa sana alikuwa katika moyo wa Mungu, kwa hiyo alipokuwa akiwaongoza watu
mara kwa mara alihitaji ushauri kutoka kwa Mungu, alikuwa na manabii maalumu
kwaajili ya kuyajua mapenzi ya Mungu, hali ya Daudi ya Kiroho iliathiri hali ya
taifa zima japo alikuwa kiongozi wa Kisiasa kwa hiyo ni lazima tumtegemee
Mungu, lazima tuwe na yeye kwaajili ya mafanikio yetu na maandiko yanaonyesha
kuwa peke yetu hatuwezi lakini pamoja na Mungu tutatenda makuu
Yohana 15:4-5 “Kaeni
ndani yangu, nami ndani yenu. Kama vile tawi lisivyoweza kuzaa peke yake,
lisipokaa ndani ya mzabibu; kadhalika nanyi, msipokaa ndani yangu. Mimi ni
mzabibu; ninyi ni matawi, akaaye ndani yangu nami ndani yake, huyo huzaa sana;
maana pasipo mimi ninyi hamwezi kufanya neno lo lote.”
Zaburi 60:11-12. “Utuletee
msaada juu ya mtesi, Maana wokovu wa binadamu haufai. Kwa msaada wa Mungu
tutatenda makuu, Maana Yeye atawakanyaga watesi wetu.”
Sasa ili kudumisha
ushirika huo na Mungu viongozi wa kijamii, kiimani na kisiasa wanapaswa kuwa
karibu na Mungu. Na ni kwa jinsi gani tunaweza kwa neno la Mungu na kwa maombi,
huduma zetu zitakuwa na ukavu kama hatutakuwa na neno la Mungu na maombi, kwa
hiyo huduma ya kudumu katika kuomba na kulihudumia neno haipaswi kupuuzwa kwa
kila kiongozi anayetaka mafanikio makubwa katika uongozi wake
Matendo 6:2-4 “Wale
Thenashara wakawaita jamii ya wanafunzi, wakasema, Haipendezi sisi kuliacha
neno la Mungu na kuhudumu mezani. Basi ndugu, chagueni watu saba miongoni
mwenu, walioshuhudiwa kuwa wema, wenye kujawa na Roho, na hekima, ili tuwaweke
juu ya jambo hili; na sisi tutadumu katika kuomba na kulihudumia lile Neno.”
Yoshua 1:7-9 “Uwe
hodari tu na ushujaa mwingi, uangalie kutenda sawasawa na sheria yote
aliyokuamuru Musa mtumishi wangu; usiiache, kwenda mkono wa kuume, au wa
kushoto, upate kufanikiwa sana kila uendako. Kitabu hiki cha torati kisiondoke
kinywani mwako, bali yatafakari maneno yake mchana na usiku, upate kuangalia
kutenda sawasawa na maneno yote yaliyoandikwa humo; maana ndipo
utakapoifanikisha njia yako, kisha ndipo utakapositawi sana. Je! Si mimi
niliyekuamuru? Uwe hodari na moyo wa ushujaa; usiogope wala usifadhaike; kwa
kuwa Bwana, Mungu wako, yu pamoja nawe kila uendako.”
1Wafalme 2:1-3. “Basi
siku ya kufa kwake Daudi ikakaribia, akamwusia Sulemani mwanawe, akasema, Mimi
naenda njia ya ulimwengu wote; basi uwe hodari, ujionyeshe kuwa mwanamume;
uyashike mausia ya Bwana, Mungu wako, uende katika njia zake, uzishike sheria
zake, na amri zake, na hukumu zake, na shuhuda zake, sawasawa na ilivyoandikwa
katika torati ya Musa, upate kufanikiwa katika kila ufanyalo, na kila utazamako;”
Maandiko
yanatuonyesha umuhimu wa neno la Mungu ambalo likijumuishwa na maombi na utii litaleta mafanikio makubwa sana
yatakayosaidia kuzalisha matunda yanayokusudiwa, watu tunaowaongoza ni watu wa Mungu bila kujali
wanatokea wapi, na sisi timewekwa na Mungu kuwahudumia hatuwezi kutumia fimbo
ya kibinadamu kuwaongoza lakini tunaweza kuwaongoza tukijishikamanisha na
mwenye watu wake ambaye ni Mungu mwenyewe, tulitumie neno la Mungu kuwaongoza,
kuwaelekeza na kuwatendea haki, jamii inafurahi anapotawala mtu wa Mungu na
jamii huugua atapotawala mtu muovu, Mithali 29:2 “Wenye
haki wakiwa na amri, watu hufurahi; Bali mwovu atawalapo, watu huugua.” Hivyo
kumcha Mungu ni lazima.
# 3. Kwaajili ya kuwatumikia
watu.
Kusudi kubwa
la Mungu kuwachagua watu miongoni mwa watu wake ili kuwasimamia watu wengine
kijamii, kisiasa na kiimani ni ili watu hao watumikiwe, wako viongozi kadhaa
duniani ambao ni kama miungu watu, wako mbali sana na jamii, wako juu ya jamii,
ni maboss na ili uwakute huna budi kupanda na ngazi, jamii inajua kuwa
wanapaswa kuwaheshimu viongozi, wanaelewa lakini viongozi hawapaswi kuitafuta
heshima hiyo na Yesu Kristo alituonyesha mfano kivitendo ya kuwa alikuja
kuwatumikia watu
Marko 10:42-45 “Yesu
akawaita, akawaambia, Mwajua ya kuwa wale wanaohesabiwa kuwa wakuu wa Mataifa
huwatawala kwa nguvu, na wakubwa wao huwatumikisha. Lakini haitakuwa hivyo
kwenu; bali mtu anayetaka kuwa mkubwa kwenu, atakuwa mtumishi wenu, na mtu
anayetaka kuwa wa kwanza wenu, atakuwa mtumwa wa wote. Kwa maana Mwana wa Adamu
naye hakuja kutumikiwa, bali kutumika, na kutoa nafsi yake iwe fidia ya wengi.”
Wafilipi 2:5-11 “Iweni
na nia iyo hiyo ndani yenu ambayo ilikuwamo pia ndani ya Kristo Yesu; ambaye
yeye mwanzo alikuwa yuna namna ya Mungu, naye hakuona kule kuwa sawa na Mungu
kuwa ni kitu cha kushikamana nacho; bali alijifanya kuwa hana utukufu, akatwaa
namna ya mtumwa, akawa ana mfano wa wanadamu; tena, alipoonekana ana umbo kama
mwanadamu, alijinyenyekeza akawa mtii hata mauti, naam, mauti ya msalaba. Kwa
hiyo tena Mungu alimwadhimisha mno, akamkirimia Jina lile lipitalo kila jina;
ili kwa jina la Yesu kila goti lipigwe, la vitu vya mbinguni, na vya duniani,
na vya chini ya nchi; na kila ulimi ukiri ya kuwa YESU KRISTO NI BWANA, kwa
utukufu wa Mungu Baba”
1Petro 5:1-3 “Nawasihi
wazee walio kwenu, mimi niliye mzee, mwenzi wao, na shahidi wa mateso ya
Kristo, na mshirika wa utukufu utakaofunuliwa baadaye; lichungeni kundi la
Mungu lililo kwenu, na kulisimamia, si kwa kulazimishwa, bali kwa hiari kama
Mungu atakavyo; si kwa kutaka fedha ya aibu, bali kwa moyo. Wala si kama
wajifanyao mabwana juu ya mitaa yao, bali kwa kujifanya vielelezo kwa lile
kundi.”
2Nyakati 10:6-8 “Mfalme
Rehoboamu akataka shauri kwa wazee, waliosimama mbele ya Sulemani baba yake,
alipokuwa hai bado, akasema, Mwanipa shauri gani la kuwajibu watu hawa?
Wakamwambia, wakasema, Ukiwa mwema kwao watu hawa, na kuwapendeza, na kuwaambia
maneno mazuri, ndipo watakapokuwa watumishi wako siku zote. Lakini akaliacha
shauri lile la wazee walilompa, akataka shauri kwa wale vijana waliokua pamoja
naye, waliosimama mbele yake.”
Mafanikio
makubwa kwa viongozi wote waliofanikiwa
ni wale ambao walikuwa ni viongozi watumishi, Yesu alifanikiwa sana na
kuheshimika sana mbinguni na duniani kwa sababu ya moyo wake mkubwa wa
unyenyekevu, na kujishusha na kuamua kuwatumikia watu, falsafa hii itafanya
kazi kwa wafalme, makuhani na manabii namaanisha viongozi wote wa kijamii,
kisiasa na kiimani. Tufuate njia na nyayo ya Bwana Yesu na tutaona aina ya
uongozi wetu itakuwa nyepesi na Mungu ataweka mkono wake kutufanikisha.,
tuwatue watu mizigo yao, tutatue matatizo yao, tuwasikilize na tujihadhari
kuwatwisha mizigo isiyo na sababu (Mfano katika nchi yetu kuna malalamiko ya
kikokotoo, ambacho wabunge hakiwahusu, lakini wala kinaowahusu wanaumia na
wanalia lakini hakuna mtu wa kuwasikiliza, viongozi wanaosimama kwaajili ya
watu watasimama kuwatetea watu na sio kuwakandamiza)
#4. Kwaajili
ya Upendo:
Iko dhana
potofu duniani ambayo imejengeka katika jamii kwamba watu wengi sana hudhani ya
kuwa mtu anapokuwa kiongozi basi ameuchinja! Dhana hii ni ya kipumbavu kwa
mtazamo wa Mungu, kwani jambo hili husababisha watu wautake uongozi na ama
wanapokuwa viongozi wawe na ubinafsi, tamaa ya fedha na ushindani, nia ya kweli
inayokubaliwa na Mungu katika swala zima la uongozi ni upendo na huruma, na sio
kuwaendesha watu wa Mungu badala ya kuwaongoza, maandiko yanatuonyesha ya kuwa
bila upendo kila kitu kinakuwa hakina maana
1Wakorintho 13:1-3 “Nijaposema kwa lugha za wanadamu na za malaika, kama sina upendo,
nimekuwa shaba iliayo na upatu uvumao. Tena nijapokuwa na unabii, na kujua siri
zote na maarifa yote, nijapokuwa na imani timilifu kiasi cha kuweza kuhamisha
milima, kama sina upendo, si kitu mimi. Tena nikitoa mali zangu zote kuwalisha
maskini, tena nikijitoa mwili wangu niungue moto, kama sina upendo, hainifaidii
kitu.”
Upendo
unapaswa kuongoza nia zetu za ndani za kuwatumikia watu, wakati ubinafsi
unataka tuchukue, badala ya kutoa, kuwa waovu badala ya kuwa wema, kulazimisha
badala ya kusihi, kuwaongoza watu kwa upendo kunahusisha uwazi, kuwa tayari
kuwa baba mwenye huruma kwa jamii, au mama mwenye huruma, lazima tuwahurumie watu
na kuwaongoza tukijua kuwa ni watu wa Mungu na sio watu wetu, Yesu kila
alichokifanya kwa watu alikifanya kwa sababu aliongozwa na upendo. Aliwaona
wanadamu kuwa ka amkondoo wa baba yake, na hivyo hakuwahi kuweka maslahi yake
mbele hata siku moja moyo wake ulijali
Mathayo 9:36-38 “Na
alipowaona makutano, aliwahurumia, kwa sababu walikuwa wamechoka na kutawanyika
kama kondoo wasio na mchungaji.Ndipo alipowaambia wanafunzi wake, Mavuno ni
mengi, lakini watenda kazi ni wachache. Basi mwombeni Bwana wa mavuno, apeleke
watenda kazi katika mavuno yake.”
Ni nini
kinakusukuma kuwaongoza watu Mungu anachunguza moyo, na anaiona nia yako ya
kuwatumikia watu basi iwapo nia yako ni njema hakikisha kuwa nia hiyo inadumu
na tusibadilike mpaka mwisho.
# 5. Kwa kuwezeshwa na Mungu
Kuhudumia watu
sio kazi nyepesi ni Mzigo, uongozi ni mzigo, viongozi hukutana na changamoto
nyingi, shida za watu ni shida zao, maumivu ya watu ni maumivu yao, wanapoumia
wao viongozi huumia, wanapopatwa na shida nao huweza kuhisi zile shida kama ni
zao, kwa hiyo wajibu huo ni mlima, katika mpango wake Mungu viongozi wote wa
kisiasa, kijamii na kiimani Mungu hakuwahi kuwatuma bila kuwapaka mafuta yaani
bila nguvu za Roho Mtakatifu, Yesu Kristo alifanya wanafunzi wengi lakini
aliandaa viongozi 12 na wengine 70, na wengie
120, na wengine 500, na kadhalika na hata baada ya mafunzo mengi ya
nadharia na vitendo aliwataka wasiondoke bila ujazo wa Roho Mtakatifu.
Luka 24:49 “Na
tazama, nawaletea juu yenu ahadi ya Baba yangu; lakini kaeni humu mjini, hata
mvikwe uwezo utokao juu.”
Matendo 1:8 “Lakini
mtapokea nguvu, akiisha kuwajilia juu yenu Roho Mtakatifu; nanyi mtakuwa
mashahidi wangu katika Yerusalemu, na katika Uyahudi wote, na Samaria, na hata
mwisho wa nchi.”
Zakaria 4:6-7 “Akajibu
akaniambia, akisema, Hili ndilo neno la Bwana kwa Zerubabeli, kusema, Si kwa uwezo,
wala si kwa nguvu, bali ni kwa roho yangu, asema Bwana wa majeshi.Nani wewe, Ee
mlima mkubwa? Mbele ya Zerubabeli utakuwa nchi tambarare; naye atalileta lile
jiwe la kuwekwa juu kabisa pamoja na vigelegele vya, Neema, neema, ilikalie.”
Roho Mtakatifu
ni Mungu na anahusika na kitengo cha maongozi, hakuna kiongozi anaweza kuona
mambo kuwa mepesi bila kuvikwa uwezo huu utokao juu, uwezo huu ndio unaomfanya
kiongozi kuwa mtu mwingine, ndio unaomfanya kiongozi kubeba mzigo wa uongozi,
ndio unaomfanya kiongozi kuwa na hekima, fahamu na ujuzi, na maarifa na uchaji
wa Mungu na kuwa na mzigo wa kukataa udhalimu na uonevu wa watu, wafalme
waamuzi na mashujaa wengi katika biblia waliifanya kazi waliyoifanya kwa sababu
Roho Mtakatifu alikuwa juu yao
1Samuel 16:1-3,13. “Bwana akamwambia Samweli, Hata lini utamlilia Sauli, ikiwa mimi
nimemkataa asiwamiliki Israeli? Ijaze pembe yako mafuta, uende, nami
nitakupeleka kwa Yese, Mbethlehemi; maana nimejipatia mfalme katika wanawe. Samweli
akasema, Nawezaje kwenda? Sauli akipata habari, ataniua. Basi Bwana akasema,
Chukua ndama pamoja nawe, ukaseme, Nimekuja ili kumtolea Bwana dhabihu. Ukamwite
Yese aje kwenye dhabihu, nami nitakuonyesha utakayotenda; nawe utamtia mafuta
yule nitakayemtaja kwako”. “Ndipo Samweli akaitwaa pembe yenye mafuta,
akamtia mafuta kati ya ndugu zake; na roho ya Bwana ikamjilia Daudi kwa nguvu
tangu siku ile. Basi Samweli akaondoka, akaenda zake Rama.”
Uweza, mamlaka
na nguvu zako zitakazokurahisishia kazi wakati unapoelekea kutekeleza majukumu
yako ni Roho Mtakatifu kuwa juu yako, yeye ni nyenzo muhimu katika utumishi
tulioitiwa, usifanye kazi mwenyewe hakikisha kuwa una nguvu za Mungu, dumisha
uhusiano wako na Roho Mtakatifu atakusaidia kukabiliana na kila aina ya
upinzani na kukupa hekima ambayo Mungu anaikusudia na ndio maana nyakati za kanisa la kwanza
wakati wote walizingatia sana kuwachagua viongozi ambao wana uhusiano mzuri na
Roho Mtakatifu
Matendo 6:3-6 “Basi
ndugu, chagueni watu saba miongoni mwenu, walioshuhudiwa kuwa wema, wenye
kujawa na Roho, na hekima, ili tuwaweke juu ya jambo hili; na sisi tutadumu
katika kuomba na kulihudumia lile Neno. Neno hili likapendeza machoni pa
mkutano wote; wakamchagua Stefano, mtu aliyejaa imani na Roho Mtakatifu, na
Filipo, na Prokoro, na Nikanori, na Timoni, na Parmena, na Nikolao mwongofu wa
Antiokia; ambao wakawaweka mbele ya mitume, na walipokwisha kuomba wakaweka
mikono yao juu yao.”
Ningeweza
kusema mengi na kutoa mifano Mingi lakini kila asomaye na ahafamu wote tunajua
umuhimu wa Mungu Roho Mtakatifu katika utumishi wetu basi na tusimzimishe,
tujiulize tu hapa duniani kuna kiongozi aliyekuwa bora kushinda Yesu Kristo? Na
ikiwa Yesu Kristo tu alihitaji kuwa na Roho Wa Mungu juu yake kabla ya kufanya
huduma je sembuse wewe na mimi, hatuwezi
kufika kokote bila yeye watu hawa ni
mali yake na Yeye ndiye Bwana wa mavuno yote tutakayoyafanya kwaajili ya
kuhudumia watu ni matokeo ya nguvu hizo za uungu kuwa juu yetu
Luka 4:18-19 “Roho
wa Bwana yu juu yangu, Kwa maana amenitia mafuta kuwahubiri maskini habari
njema. Amenituma kuwatangazia wafungwa kufunguliwa kwao, Na vipofu kupata kuona
tena, Kuwaacha huru waliosetwa, Na kutangaza mwaka wa Bwana uliokubaliwa.”
# 6. Kwaajili ya kuufuata mfano wake
Zamani sana
nilikuwa napenda sana kuwaweka watu Fulani ambao kwangu walikuwa ni mashujaa wa
Imani kama mfano wangu wa kuwafuata, na ndivyo wengi tulivyo, tunaweza kuwataja
hapa wahubiri wakubwa sana na kuwaita kama mfano wetu na wakati mwingine
tukawaita baba zetu wa kiroho!, yako mafundisho pia siku hizi ambayo
yanasisitiza kwamba kila mtu awe na baba wa kiroho na wakati mwingine
tunaambiwa ni hatari sana kama mtu hana baba wa kiroho, maandiko hayako kinyume
sana na kuwa na baba wa kiroho lakini
yako mazingira ambayo wakati mwingine yanaweza yakakunyima kuwa na hao na ni hatari sana kuwa na baba wa kiroho
mwanadamu, nadhani neno zuri ni kuwa na Mchungaji. Au mchungaji rafiki ambaye
anaweza kukushauri, au Mchungaji mwenye umri uliozidi wako, kukuongoza na
kukukosoa au kukukemea na kukuonya. Biblia haijawahi kutuagiza kuwa na baba wa
kiroho, wala hajaituamuru wakristo kuitwa baba tunaambiwa tunaye baba mmoja tu
aliye mbinguni, lakini maandiko yanataka tuwakumbuke waliotuongoza, na kuiga
Imani yao, lakini kwa kuuchunguza sana mwenendo wao
Mathayo 23:8-12 “Bali
ninyi msiitwe Rabi, maana mwalimu wenu ni mmoja, nanyi nyote ni ndugu. Wala
msimwite mtu baba duniani; maana Baba yenu ni mmoja, aliye wa mbinguni. Wala
msiitwe viongozi; maana kiongozi wenu ni mmoja, naye ndiye Kristo. Naye aliye mkubwa wenu atakuwa mtumishi wenu.
Na ye yote atakayejikweza, atadhiliwa; na ye yote atakayejidhili, atakwezwa.”
Waebrania 13:7 “Wakumbukeni
wale waliokuwa wakiwaongoza, waliowaambia neno la Mungu; tena, kwa kuuchunguza
sana mwisho wa mwenendo wao, iigeni imani yao.”
Kwanini kwa sababu
wao ni binadamu, naweza nikajivunia mtu Fulani, lakini ukashangaa watu
wanaomjua kwa ukaribu wakawa wanakushangaa, kwa sababu wote hao ni binadamu, Abrahamu
anaitwa baba wa Imani kwa mujibu wa maandiko, lakini hata hivyo yako mambo
tunaweza kujifunza kutoka kwake na mengine tunaona ubinadamu wake sasa nani
anaweza kuwa kielelezo chetu katika huduma na utumishi wetu ni Yesu Kristo peke
yake kwa sababu yeye alijaribiwa katika
mambo yote kama tujaribiwavyo lakini hakutenda dhambi. Kwa sababu yeye Peke yake
ni mkamilifu nay eye pekee anafaa kuwa mfano wa kuigwa!
Zaburi 37:37 “Umwangalie
sana mtu mkamilifu, Umtazame mtu mnyofu, Maana mwisho wake mtu huyo ni amani.”
Yakobo 3:1-2 “Ndugu
zangu, msiwe waalimu wengi, mkijua ya kuwa mtapata hukumu kubwa zaidi. Maana
twajikwaa sisi sote pia katika mambo mengi. Mtu asiyejikwaa katika kunena, huyo
ni mtu mkamilifu, awezaye kuuzuia na mwili wake wote kama kwa lijamu”.
Waebrania 4:14-15 “Basi,
iwapo tunaye kuhani mkuu aliyeingia katika mbingu, Yesu, Mwana wa Mungu, na
tuyashike sana maungamo yetu. Kwa kuwa hamna kuhani mkuu asiyeweza kuchukuana
nasi katika mambo yetu ya udhaifu; bali yeye alijaribiwa sawasawa na sisi
katika mambo yote, bila kufanya dhambi.”
Yesu peke yake
ndiye anayeweza kuwa mfano wetu, (rolemodel)
yeye hana mapungufu katika idara yoyote ile na kwa sababu hiyo tunaweza
kumfuata yeye, tuache kuwa na tabia ya kutukuza wanadamu kwa sababu hatuwezi
kusoma nia zao wala mioyo yao, ni Mungu peke yake ndiye aujua moyo wa mwanadamu
na tunaambiwa kuwa moyo wa mwanadamu una ugonjwa wa kufisha kwa hiyo Yesu na
awe kielelezo chetu katika utumishi wetu, tabia na mwenendo, kiongozi wako wa
mfano ni nani ni Yesu, huku tukiwaheshimu wale aliowaweka yeye katika mamlaka
ili watuongoze, Yesu ndiye baba yetu wa kiroho.
Yeremia 17:9-10 “Moyo
huwa mdanganyifu kuliko vitu vyote, una ugonjwa wa kufisha; nani awezaye
kuujua? Mimi, Bwana, nauchunguza moyo, navijaribu viuno, hata kumpa kila mtu
kiasi cha njia zake, kiasi cha matunda ya matendo yake.”
# 7. Kwa unyenyekevu
Nimekataza
hapo juu kuwa na baba kwa sababu neno la Mungu linaeleza kuwa baba yetu ni
mmoja tu Mathayo 23:8-12 “Bali ninyi msiitwe Rabi, maana mwalimu wenu ni mmoja,
nanyi nyote ni ndugu. Wala msimwite mtu baba duniani; maana Baba yenu ni mmoja,
aliye wa mbinguni. Wala msiitwe viongozi; maana kiongozi wenu ni mmoja, naye
ndiye Kristo. Naye aliye mkubwa wenu atakuwa mtumishi wenu.Na ye yote
atakayejikweza, atadhiliwa; na ye yote atakayejidhili, atakwezwa.”
Yesu alikataza
wanafunzi wake kutokujiita Rabbi, baba, au viongozi, kwa sababu ya tabia ya
mafarisayo ambao walijiita majina hayo kwa sababu ya kukosa unyenyekevu na
kutaka kujikweza kwaajili ya kutaka heshima kwa watu, kwa hiyo ni lazima
kuchukua tahadhari juu ya hilo, Na
nimekazia hapo juu ya kuwa Yesu ndiye mfano wetu pekee wa kuufuata, hata hivyo
tunao viongozi wetu waliowekwa na Mungu, ambao ni wanadamu wanaotuongoza
maandiko yanataka tuwaheshimu na kujitiisha chini yao hii kwa lugha ya
kiingereza inaitwa Submission
Waebrania 13:17 “Watiini
wenye kuwaongoza, na kuwanyenyekea; maana wao wanakesha kwa ajili ya roho zenu,
kama watu watakaotoa hesabu, ili kwamba wafanye hivyo kwa furaha wala si kwa
kuugua; maana isingewafaa ninyi.” 1Wakorintho 14:32 “Na roho za manabii huwatii manabii.”
Kama tunaufuta
mfano wa Yesu Kristo kamwe hatutaacha kutii mamlaka, na kuzinyenyekea hiyo
ndiyo kanuni ya mafanikio ya uongozi wetu ni lazima tujitiishe chini ya mamlaka
zilizoko, katika maisha yake yote na huduma Yesu Kristo alijinyenyekeza kwa
baba yake, kwa hiyo Kristo anatufundisha kutembea kwa unyenyekevu, hata wale
wenye huduma zao binafsi wanapaswa kuwa na watu watakaowashauri, kuwakemea na
kuwaonya, ni salama sana kuwa na mtu juu yetu anayetuangalia, mimi hujisikia
salama sana nikifanya kazi chini ya mtu, lakini asiwe mtu katili, au mwenye
wivu, sina hatari kwa mtu yeyote yule, na ninaweza kumnyenyekea mtu yeyote yule
lakini sipendi kuonewa au kunyanyaswa,
isipokuwa kama Mungu amekutuma uninyanyase, huduma yako itakuwa na thamani
kama utajinyenyekeza huku watu wakiheshimiana na sio kuvunjiana heshima.
Kumbuka kuwa unyenyekevu sio ujinga.
# 8. kwaajili ya kujitoa dhabihu.
Uthamani wa kitu
chochote kile duniani na katika Imani unapimwa kwa jinsi mtu anavyoweza
kujidhabihu, Ibrahimu alihesabiwa kuwa na haki baada ya kuwa radhi kumtoa
sadaka mwanae wa ahadi Isaka huu ulikuwa moyo mkunjufu na ukarimu wa hali ya
juu hakuna anayeweza kuuiga, Mungu peke yake alimuiga Ibrahimu kwa kuwa tayari
kumtoa mwana wake wa pekee kwaajili ya ulimwengu, katika utumushi wetu kwa
jamii, siasa, na Imani utagundua kuwa huduma inahitaji kujidhabihu, hii sio
kazi ya kivivu kama watu fulani wanavyoweza kufikiri, unaweza kuvutiwa tu na
watu Fulani katika huduma hata kutamani kuwa kama wao lakini chunguza sana
mapito yao utagundua kuwa waligharimika sana au wanagharimika sana, mpaka
kufikia hapo walipofika, ukitaka kuwa na huduma kama ya Paulo Mtume ukumbuke
pia mapito yake kwa kweli sio vitu vya kutia moyo hata kidogo, kuna gharana za kulipa,
2Wakorintho 2:21-33 “Nanena kwa jinsi ya kujidhili kana kwamba sisi tulikuwa
dhaifu. Walakini, akiwa mtu anao ujasiri kwa lo lote, (nanena kipuuzi), mimi
nami ninao ujasiri. Wao ni Waebrania? Na mimi pia. Wao ni Waisraeli? Na mimi
pia. Wao ni uzao wa Ibrahimu? Na mimi pia. Wao ni wahudumu wa Kristo? (Nanena
kiwazimu), mimi ni zaidi; katika taabu kuzidi sana; katika vifungo kuzidi sana;
katika mapigo kupita kiasi; katika mauti mara nyingi. Kwa Wayahudi mara tano
nalipata mapigo arobaini kasoro moja. Mara tatu nalipigwa kwa bakora; mara moja
nalipigwa kwa mawe; mara tatu nalivunjikiwa jahazi; kuchwa kucha nimepata kukaa
kilindini; katika kusafiri mara nyingi; hatari za mito; hatari za wanyang'anyi;
hatari kwa taifa langu; hatari kwa mataifa mengine; hatari za mjini; hatari za
jangwani; hatari za baharini; hatari kwa ndugu za uongo; katika taabu na
masumbufu; katika kukesha mara nyingi; katika njaa na kiu; katika kufunga mara
nyingi; katika baridi na kuwa uchi. Baghairi ya mambo ya nje, yako yanijiayo
kila siku, ndiyo maangalizi ya makanisa yote. Ni nani aliye dhaifu, nisiwe
dhaifu nami? Ni nani aliyekwazwa nami nisichukiwe? Ikinibidi kujisifu, nitajisifia mambo ya
udhaifu wangu. Mungu, Baba wa Bwana Yesu, aliye mtukufu hata milele, anajua ya
kuwa sisemi uongo. Huko Dameski liwali wa mfalme Areta alikuwa akiulinda mji wa
Wadameski, ili kunikamata;nami nikatelemshwa ndani ya kapu, katika dirisha la
ukutani, nikaokoka katika mikono yake.”
Kazi ya huduma
ina gharama zake na unapokuwa kiongozi ni lazima ukubali kulipa gharama hizo na
ili ulipe lazima ukubali kujidhabihu, upweke, mbali na familia, kujinyima na kadhalika
wakati mwingine tunachukua muda mwingi sana kuandaa jumbe kama hizi ambazo
zinakuwa baraka kwa wengi, ujumbe unaoweza kuhubiriwa kwa dakika 45 wakati
mwingine unaweza kugharimu kwa ufinyu masaa nane ya maandalizi, na masomo
marefu huchukua wakati mwingine majuma kadhaa, wiki kadhaa, au siku nzima,
inagharimu muda na kukaa katika computa kwa muda mrefu, kuchapa na kuandaa ni
lazima ujitoe kama kuku anayelalia ili uweze kutotoa bila kujidhabihu wakati
mwingine maisha ya huduma hayawezi kuwa rahisi. Huduma pia inaambatana na vita, na wakati
mwingine kusema vibaya, kutukana kusingiziwa, tunaweza hata kuambiwa kuwa ni
freemason au unatumia nguvu za giza, au kutuhumiwa kuwa mzinzi, na kusingiziwa,
mimi niliwahi kusingiziwa kuwa nilitaka kubaka, na sijawahi kuwaambia watu hao
watubu kwangu au wakae kimya wala
sihitaji kujitakasa kwa wanadamu kwa sababu ni kawaida kutuhumiwa, ni kawaida
kunenwa vibaya ni kawaida kuchafuliwa na
hatuwezi kumthibitishia kila mtu kuwa tuna wema isipokuwa Mungu ajuae mioyo ya
watu, hakuna sababu ya kujibu lolote au kunyamazisha wanaotutukana au kusema
vibaya, kwa sababu hiyo ni sehemu ya dhabihu ya kujitoa kwa Mungu, kunenwa
vibaya na kusingiziwa ni sehemu ya utumishi wetu nah ii inakuja ili
kutunyenyekesha na kwaajili ya Mungu kutuongezea neema nyingi zaidi.
1Wakorintho 4:9-13 “Maana nadhani ya kuwa Mungu ametutoa sisi mitume mwisho, kama watu
waliohukumiwa wauawe; kwa sababu tumekuwa tamasha kwa dunia; kwa malaika na
wanadamu. Sisi tu wapumbavu kwa ajili ya Kristo, lakini ninyi ni wenye akili
katika Kristo; sisi tu dhaifu, lakini ninyi mna nguvu; ninyi mna utukufu,
lakini sisi hatupati heshima. Hata saa hii ya sasa, tuna njaa na kiu, tu uchi,
twapigwa ngumi, tena hatuna makao; kisha twataabika tukifanya kazi kwa mikono
yetu wenyewe. Tukitukanwa twabariki, tukiudhiwa twastahimili; tukisingiziwa
twasihi; tumefanywa kama takataka za dunia, na tama ya vitu vyote hata sasa.”
9 #. Kwaajili ya kuwakamilisha
Watakatifu
Ukuaji ni tabia
ya kitu chochote chenye uhai, maendeleo ni dalili ya afya ya jamii yenye akili
nzuri, kila kitu chenye uhai kinapaswa kukua, jamii ya watu wa Mungu wanapaswa
kukua kiroho, kiidadi na kijiografia, ni kazi ya viongozi kuhakikisha kuwa hilo
linatokea, na ndio maana Yesu aliweka huduma kadhaa ndani ya kanisa kwaajili ya
ustawi wa jamii ya kanisa.
Waefeso 4:11-15 “Naye
alitoa wengine kuwa mitume, na wengine kuwa manabii; na wengine kuwa
wainjilisti na wengine kuwa wachungaji na waalimu; kwa kusudi la kuwakamilisha
watakatifu, hata kazi ya huduma itendeke, hata mwili wa Kristo ujengwe; hata na
sisi sote tutakapoufikia umoja wa imani na kumfahamu sana Mwana wa Mungu, hata
kuwa mtu mkamilifu, hata kufika kwenye cheo cha kimo cha utimilifu wa Kristo;
ili tusiwe tena watoto wachanga, tukitupwa huku na huku, na kuchukuliwa na kila
upepo wa elimu, kwa hila ya watu, kwa ujanja, tukizifuata njia za udanganyifu.
Lakini tuishike kweli katika upendo na kukua hata tumfikie yeye katika yote,
yeye aliye kichwa, Kristo.”
Karama za huduma
zimetolewa katika kanisa ambazo pia ni karama za maongozi ya kanisa ili
kuwaandaaa watu wa Mungu kwaajili ya kazi njema, ili mwili wa Kristo ujengwe,
kwa hiyo karama hizi na vipawa hivi sio njia ya kujinufaisha,lakini zimetolewa
kwaajili ya ujenzi, ujenzi wa mwili wa Kristo, ni kwaajili tu ya kufaidiana
kuufaidisha mwili wa Kristo
1Wakorintho 12:4-7 “Basi pana tofauti za karama; bali Roho ni yeye yule. Tena pana tofauti
za huduma, na Bwana ni yeye yule. Kisha pana tofauti za kutenda kazi, bali
Mungu ni yeye yule azitendaye kazi zote katika wote. Lakini kila mmoja hupewa
ufunuo wa Roho kwa kufaidiana.”
Karama hizi za
huduma zimetolewa ili tuweze kuwasaidia wengine na kuwatumikia ili wakue, kwa
hiyo sio huduma za kitawala ni huduma za kujenga, lengo lake kubwa ikiwa ni
matokeo na matokeo hayo ni ukomavu katika tabia na mwenendo ili watu wawe kama
Kristo, yaani Kristo aumbike katika tabia na mwenendo wetu na kumzalia matunda.
Kwa mujibu wa Paulo
Mtume kuwakamilisha watakatifu ndio lengo kuu la Bwana wetu Yesu Kristo, na
sisi kama watu mishi wake ni muhimu kwetu kuhakikisha tunalifanyia kazi lengo
hili, kuwakamilisha watakatifu maana yake ni pamoja na kuhakikisha kuwa
wanakuwa kiroho, na kuondoka katika uchanga na kukomaa, na hili ndio kusudi
kubwa la karama za Huduma, hatujazaliwa kama wakamilifu, na hivyo tunapaswa
kukulia neema na maarifa katika kumjua Mungu na Mwokozi wetu Yesu
2Petro 3:18a “Lakini,
kueni katika neema, na katika kumjua Bwana wetu na Mwokozi Yesu Kristo. Utukufu
una yeye sasa na hata milele.”
Kuwakamilisha
watakatifu ni kitendo cha kuwaongoza watu wa Mungu katika kukua kiroho na
kuishi maisha matakatifu, kuwasaidia kukua kiimani, kuwa na maarifa ya namna ya
kuishi sawa na neno la Mungu, na
mafundisho yake, kwa hiyo ili
kukamilisha swala hili, Kufundisha, kutia moyo kusimamia nidhamu, na kuwasaidia
waamini zaidi sana kuwapunguzia mizigo yao! Utatatua vipi changamoto zao kwa
kuhubiri, na kufundisha na kuwaombea na kufanya semina mbalimbali, kuwafundisha
kuomba, kufunga kujitiisha na kuishi maisha ya kumpendeza Mungu na jamii.
# 10. kwaajili ya kutoa hesabu
Waebrania 13:17 “Watiini
wenye kuwaongoza, na kuwanyenyekea; maana wao wanakesha kwa ajili ya roho zenu,
kama watu watakaotoa hesabu, ili kwamba wafanye hivyo kwa furaha wala si kwa
kuugua; maana isingewafaa ninyi.”
Kazi hii ina
hatima na hatima yake ni kutoa hesabu kwaajili ya kila kitu ambacho Mungu
ametukabidhi, ikiwemo watu ambao Mungu ametupa
Yohana 17:11-13 “Wala
mimi simo tena ulimwenguni, lakini hawa wamo ulimwenguni, nami naja kwako. Baba
mtakatifu, kwa jina lako ulilonipa uwalinde hawa, ili wawe na umoja kama sisi
tulivyo. Nilipokuwapo pamoja nao, mimi naliwalinda kwa jina lako ulilonipa,
nikawatunza; wala hapana mmojawapo wao aliyepotea, ila yule mwana wa upotevu,
ili andiko litimie.Na sasa naja kwako; na maneno haya nayasema ulimwenguni, ili
wawe na furaha yangu imetimizwa ndani yao.”
Maandiko
yanatufundisha ya kuwa tutawajibika tutatoa hesabu mbele za Mungu kama kaka na
dada namna na jinsi tunavyohudumiana na kuuhudumia mwili wa Kristo, tunamuona
Yesu Mwana wa Mungu akiwajibika kutoa hesabu ya wale aliopewa sisi nasi tutatoa
hesabu ya namna tulivyoishi na namna tulivyochukuliana na wenzetu,
Warumi 14:11-13 “Kwa
kuwa imeandikwa, Kama niishivyo, anena Bwana, kila goti litapigwa mbele zangu;
Na kila ulimi utamkiri Mungu. Basi ni hivyo, kila mtu miongoni mwetu atatoa
habari zake mwenyewe mbele za Mungu. Basi tusizidi kuhukumiana, bali afadhali
toeni hukumu hii, mtu asitie kitu cha kumkwaza ndugu au cha kumwangusha.”
2Wakorintho 5:9-10 “Kwa hiyo, tena, ikiwa tupo hapa, au ikiwa hatupo hapa, twajitahidi
kumpendeza yeye.Kwa maana imetupasa sisi sote kudhihirishwa mbele ya kiti cha
hukumu cha Kristo, ili kila mtu apokee ijara ya mambo aliyotenda kwa mwili,
kadiri alivyotenda, kwamba ni mema au mabaya.”
Hivyo
tunapoishi maisha ya huduma na utumishi lazima tuyakumbuke haya na kujua ya
kuwa tutayatolea hesabu mbele za Mungu na mafanikio ya huduma zetu yanategemeana
na namna na jinsi tunavyotembea katika falsafa hizo, Bwana ampe neema kila
mmoja wetu kuyazingatia haya na kuzidi katika jina la Yesu Kristo amen!
Na. Rev. Innocent Mkombozi Kamote
Mkuu wa wajenzi mwenye Hekima!