Ijumaa, 15 Julai 2016

Mwana wa faraja!



Andiko: Matendo 4:36. “Na Yusufu, aliyeitwa na mitume Barnaba, (maana yake, Mwana wa faraja), Mlawi, asili yake ni mtu wa Kipro,”

 "Ndani ya Yesu Kristo kulikuwa na huduma ya Faraja, watu walifurahi kumsikia kumgusa na kumuona, ilikuwa Huzuni kwa wanafunzi wake alipowaambia kuwa ataondoka, lakini aliwaahidi kuwaletea mfariji yaani Roho Mtakatifu, ambaye hufanya kazi ya kuwahudumia watu waliomuamini"

UTANGULIZI:

Kufariji maana yake ni tendo endelevu la kuendelea kutia moyo, kutia matumaini, kutia nguvu, kila mtu duniani anahitaji kutiwa moyo, kuishi kwa matumaini, na kutokukata tamaa katika maisha yetu ya kila siku, Tunaishi katika ulimwengu wenye changamoto nyingi sana na bila huduma ya kutiana moyo ulimwengu hauwezi kuwa mahali pa kupendeza sana kuishi, Tunahitaji watu wenye huduma ya kutia moyo wawepo kila mahali, Nyakati za Kanisa la Kwanza Mungu alilipa Kanisa zawadi ya mtu mwenye karama ya kutia moyo wengine, Mtu huyu alijulikana kama Yusuphu Mlawi mzaliwa wa Cyprus.

·         Mitume walimuita mtu huyu “Barnabas” kuonyesha umuhimu wa huduma hii ya faraja
·         Tunawezaje kutiana moyo kila mmoja na mwingine? Ni kwa kujifunza kutoka kwa “Barnaba” na kuangalia kila alichokifanya:-

Huduma ya Barnaba.
I.       Alitia moyo kanisa kwa kuonyesha mfano wa matendo yake.
·         Aliuza shamba lake  na kutoa fedha Matendo 4:37 alionyesha mfano katika kanisa, Kutoa kwake ulikuwa ni moyo wenye kuonyesha kuwa anawajali wengine, lilikuwa ni jambo gumu sana kuuza shamba Yerusalem kwa ajili ya umuhimu wa kumiliki ardhi katika jiji hilo lakini Barnaba alifanya akionyesha kujali wengine.
·         Aliwatia moyo waliokataliwa katika jamii na kanisa Matendo 9:26-30, Paulo mtume ambaye ndiye Sauli alipookoka na kujiunga na wanafunzi pale Yerusalem watu walikuwa na mashaka naye Lakini Barnaba alikuwa na ujasiri wa ajabu alimchukua Sauli na kumtambulisha kwa mitume, Je tufanyeje kwaajili ya watu wanaokataliwa katika jamii au kanisani lazima wawepo wenye huduma ya kufariji na kutia moyo kama Barnaba.
·         Aliwatia moyo washirika kukaa katika kweli kwa Bwana Matendo 11:22-24, kudumu kwetu katika wokovu pia kunahitaji watu wa kukujenga na kukutia Moyo Barnaba alikuwa mtu wa namna hiyo alilitoia moyo kanisa la Antiokia kudumu katika imani
·         Alimtia moyo Muhubiri mwenye kipawa na kuhudumu naye Matendo 11:25-26, wakati jamii inawapiga vita watu wenye vipawa the talented people na wakati mwingine kuwachukia ni rahisi kuwapoteza watu wa aina hii kama hakuna huduma ya kutia moyo Paulo mtume alikuja kuwa muhubiri mkubwa sana na mwenye huduma kubwa sana lakini ilifanyiwa malezi na kutiwa moyo na Mchungaji Barnaba, watumishi wengi wa Mungu wameshindwa kulea watu wenye vipawa kwa kuhofia kuwa watameza huduma zao, au wameshindwa kuwasaidia waimbaji kwa kufikiri kuwa ni watu wasiochungika, kama tukiwaelewa na kuwatia moyo na kuwajenga watakuwa wenye kufaa sana katika kazi na ujenzi wa ufalme wa Mungu
·         Alitumika kuyatia moyo makanisa yaliyopata shida kwa kupeleka zawadi Matendo 11;27-30, Wakati kanisa la Uyahudi linapitia shida Kanisa la Antiokia lilimtuma Barnaba kupeleka msaada na kanisa likafarijiwa kwa nini Barnaba kwa sababu alikuwa na moyo wa kweli wa kujali na kuwajenga wengine.
·         Alilitia moyo Kanisa kwa ibada za kufunga na kuomba pamoja na mafundisho Matendo 13:1-3,  Namna nyingine ya kulitia moyo kanisa ni kukaa katika maombi, kufunga na kuabudu na kufundisha Barnaba alikuwa mstari wa mbele kufanya hayo mimi naamimi kwa vyovyote vile aliutafuta uso wa Bwana na kuwaombea wengine, alitumiwa na Mungu pia kwa ishara na miujiza maana yake aliwaponya watu wengine na pia kujitoa katika kazi ngumu sana ya umisheni.
II.       Alilitia moyo kanisa kwa kutumia neno la Mungu
·         Alilitia moyo waamini kukaa katika imani bila kujali dhiki Matendo 14:21-22 Barnaba na Paulo walilikumbusha kanisa kuwa imetupasa kuingia katika ufalme wa Mungu kwa njia ya dhiki nyingi, waliwakumbusha kuvumilia na kuwatia moyo, fikiria kama unapitia majaribu ya aina mbalimbali na hakuna wa kukutia moyo, je ungedumu katika imani?
·         Alilitia moyo kanisa kwa kutafuta suluhu ya kanisa la mataifa kuhusu tohara Matendo 15:1-2 Injili mbaya ya kutahiriwa kwanza ndipo uokoke ilipolivamia kanisa Barnaba akiwa na Paulo walibishana na waalimu hao wa uongo, lakini pia walikwenda Yerusalem kwaajili ya kutafuta suluhu ili kanisa liweze kufarijika
·         Alilitia moyo kanisa kupitia shuhuda za matendo makuu ya Mungu Matendo 15:12
·         Alilitia moyo kanisa kupitia waraka na maneno Matendo 15:31-32 baada ya maamuzi ya mitume waliyarudia makanisa yaliyosumbuliwa na fundisho baya na kuyaimarisha kwa misimamo ya mafundisho sahii na maamuzi ya kanisa kutoka mkutano wa Yerusalem
III. Alilitia moyo kanisa kupitia kuwepo kwake
·         Ulimwengu huu ni ulimwengu wa changamoto mbalimbali una dhiki nyingi Yohana 16:33
·         Ayubu ni moja ya mfano wa watu waliokutana na mambo magumu sana kiasi ambacho hata waliokuja kumfariji walikaa kimya kwa siku saba Ayubu 1;13-19,2;7-11-13
·         Kuwa na watu kama kina Barnabas ni kwa muhimu sana kwa sababu ziko nyakati ambazo kama wanadamu tunahitaji faraja kwani yako mambo yanatuelemea Majukumu ya kifamilia, watoto wasiosikia na kutii, mikwaruzo katika ndoa, Hofu za kupoteza ajira, mishahara isiyotosheleza mahitaji yetu, hasara za kibiashara, kazi nyingi nyumbani, upweke, kuvunjika kwa uchumba, lawama kutoka kwa ndugu, lawama kazini, lawama kwa bosi, mahitaji ya ada za wanafunzi, Bili za umeme, bili za maji, kodi ya mwenye nyumba mahitaji ya wazee kijijini, mahitaji ya palizi au maandalizi ya mashamba kupanda kwa bei ya vyakula, nguo za watoto, kusengenywa, mafarakano, visa vya majirani, mashambulizi ya wachawi, kuuguliwa, madeni ya vikundi vya mikopo saccos, kupigwa nyundo Kanisani, shida za washirika na wachungaji hali kama hizi na nyinginezo nyingi ndizo zinazopelekea Kuweko na hitaji la kufarijiwa au kutiwa moyo hili ni jambo muhimu sana na linahitajika sana katika wakati huu tulionao kuliko nyakati nyingine zozote, Huduma za watumishi kama Barnaba zinahitajika sana wakati wa maswala mzito kama hayo.

Hitimisho:                
Tafadhali kuwa mtu mwenye kutia moyo wengine na kuwafariji, usiwe mtu wa kuwaponda tu na kuwasema wengine vibaya utakuwa mwana wa uharibifu, Mungu anataka kina barnaba wawepo kila mahali , katika taifa, familia, mashuleni, majumbani na katika taasisi mbalimbali
Jihadhari kuwa mkosoaji na mvunjaji moyo watu yako maswala mazuri ambayo wanadamu wanayo hayo ndio vema yakajadiliwa kwa mujibu wa fundisho la kibiblia “Wafilipi 4:8
Uwepo wetu uwe na thamani kwa sababu kupitia kuwatia moyo wengine na kuwafariji dunia itakua mahali pazuri pa kukaa salama, utakumbukwa duniani kutokana na mchango wako mkubwa kwa jamii na dunia itaona ni afadhali umeondoka endapo utakuwa mtu mwenye kuharibu wengine

·         Barnaba alikuwa mwenye kujali wengine Caring
·         Barnaba alikuwa mwenye kutia matumaini wengine wasikate tamaa Consoler
·         Barnaba alikuwa ni mwenye kuwahurumia wengine Compassionate
·         Barnaba hakuwa mtu wa kubadilika badilika katika huduma aliyokuwa nayo Consistent
·      Alikuwa jasiri katika kile alichokiamini kuwajenga wengine na kuwatetea kwa gharama yoyote ile Convictions

Katika kuhudumia kwangu kanisa la Mungu mtu anayefanana na Barnaba ambaye mimi nimewahi kumuona ni rafiki yangu mmoja anaitwa Raphael Sallu Yeye ni Mchungaji wa TAG Mkanyageni huko Muheza huyu jamaa ni kama Barnaba siongei kumtetea kwa sababu ni rafiki yangu hapana lakini ndivyo alivyo.

Na Mkuu wa wajenzi mwenye Hekima

Rev. Innocent Kamote.

Jumapili, 10 Julai 2016

Ujumbe: Watu huninena mimi kuwa ni nani?


Marko 8:27-30 “27. Akatoka Yesu na wanafunzi wake, wakaenda kwenye vijiji vya Kaisaria-Filipi; na njiani akawauliza wanafunzi wake, akasema, Watu huninena mimi kuwa ni nani? 28. Wakamjibu, Yohana Mbatizaji; wengine, Eliya; wengine, Mmojawapo wa manabii. 29. Naye akawauliza, Na ninyi mnasema ya kuwa mimi ni nani? Petro akamjibu, akamwambia, Wewe ndiwe Kristo. 30. Akawaonya wasimwambie mtu habari zake.”



Utangulizi:

Wengi wetu huwa kuna mahali tumeanzia tunapotaka kujifunza kitu au jambo Fulani, Leo tunataka kujifunza kwa kina kuhusu Yesu Kristo, tunaweza iujifunza habari za Yesu katika namna ileile ambayo tunajifunza habari za watu wengine, tutajibu swali Watu huninena mimi kuwa ni nani? Kwa kusudi la kumfahamu Yesu Kristo, Tutajifunza somo hili kwa kuzingatia vipengele vitatu vifuatavyo:-

Ushahidi wa kutoka kwa wanadamu kuhusu Yesu Kristo
Ushahidi wa kutoka kwa Malaika kuhusu Yesu Kristo
Ushahidi wa kutoka kwa Yesu Kristo

Ushahidi wa kutoka kwa wanadamu kuhusu Yesu Kristo

1.      Matha Yohana 11:27
2.      Petrer Mathayo 16:16; 2Peter 1:16-17
3.      Yohana Yohana 1:1-3, Yohana 1:14, IYohana 1:1-2, Yohana 20:30-31
4.      Thomas Yohana 20:28
5.      Ndugu zake Yohana 7:5; 1Wakoritho 15:7, Wagalatia 1:19, Yakobo 1:1 Yuda 1
6.      Mama yake Matendo 1:14

Ushahidi wa kutoka kwa Malaika Kuhusu Yesu Kristo

1.      Kundi la malaika Luka 2:11
2.      Gabriel Luka 1:32
3.      Kutoka kwa Baba yake  “Huyu ni Mwanangu Mpendwa”Luka 1:32. Mathayo 17:5 na Matendo 2:22

Ushahidi wa kutoka kwa Yesu Kristo Mwenyewe

1.      Mimi ni njia na kweli na uzima Yohana 14;16
2.      Mimi ndio Ufufuo na uzima Yohana 11:25
3.      Kabla Ibrahimu ahajakuwako mimi niko Yohana 8:58

Hitimisho:
1.      Basi Yesu sio mwanadamu wa Kawaida
2.      Yesu sio Mzushi
3.      Yesu sio Muongo
4.      Yesu ni mwana wa Mungu
5.      Yesu ni Mungu na Mkuu wa wajenzi mwenye Hekima!

Jumanne, 28 Juni 2016

Birthday iliyonifanya nitumbuliwe na mke wangu!


Week iliyopita nilikuwa na birthday yangu lakini mke wangu, watoto wangu hata wazazi wangu wote hawakunitakia heri ya kuzaliwa.

 Mke wangu mara baada ya kunikuta nimechizika kwenye sofa!
 
Nilienda kazini lakini hakuna hata mfanyakazi hata mmoja aliyenitakia heri ya kuzaliwa, nilipokuwa naingia ktk ofisi yangu katibu muhtasi wangu (secretary) akaniambia "Happy birthday bosi wangu" hapo ndipo nilijihisi wa maalumu (special) mnoo.
 
Akaniomba mchana twende tukapate lunch pamoja! Nilimkubalia na kuona kuwa hakuna maana hata ya kuwaza nyumbani tena, Tulienda na baada ya lunch akanialika nyumbani kwake anakoishi nalo niliona halina shida hata nikikawia kurudi nyumbani haijalishi.
 
Tulienda kwake na tulipoingia kwake akaniambia kwa sauti ya mahaba "Naomba niende chumbani kwa dakika moja narudi sasa hivi"  alisikika akibembeleza kimahaba nilijibu sawa huku nikiwa na mchecheto mno na kiroho kilianza kwenda kwa kasi.

Nilijua wazi kuwa huyu demu atakuwa ameni mind na huenda anakwenda kujiandaa kwa sex na mimi, na nilihisi atarejea akiwa ameondoa suti yake nzuri aliyokuwa amevaa siku hiyo na kwa vyovyote atarejea akiwa katika hali ya kunipa mahaba mazito

Sasa, kutokana na kujawa na mawazo ya kingono nilikuwa tayari nimejiandaa kumpokea kwa mahaba mazito na tayari kujibu shambulizi lolote la kimapenzi mara mara atakaporudi!
 
Alitoka baada ya dakika tano hivi alirejea akiwa amebeba keki ya birthday  Lakini kama haitoshi huku alikuwa ameambatana  na mke wangu, watoto wangu, mama yangu,Msichana wetu wa kazi na baadhi ya rafiki zangu wote wakisema  kwa nguvu sana SUPRISEEE!!!
 
Na nilikuwa nikisubiri katika sofa pale sebuleni NIKIWA NSHAVUA SURUALI NA PEPO LA NGONO LISHENIPANDA!
 
Masikini mie! Mawazo ya Ngono yameniponza! 

Kwa akili zako finyu unadhani nitakuwa nimejitumbua au nimetumbuliwa?
 
Hapa ninapozungumza mwenzenu Sina mke hivi sasa na heshima yangu iko jalalani!.

"Heri wenye Moyo safi maana hao watamuona Mungu" Mathayo 5:8 

Na Kirima Gs Baba God!
Edited by Rev. Kamote Mkuu wa wajenzi Mwenye Hekima!

Jumapili, 26 Juni 2016

Bwana Ndiye Mchungaji wangu!


Zaburi 23:1-6 Biblia inasema
 1. Bwana ndiye mchungaji wangu, Sitapungukiwa na kitu. 2. Katika malisho ya majani mabichi hunilaza, Kando ya maji ya utulivu huniongoza. 3. Hunihuisha nafsi yangu; na kuniongoza Katika njia za haki kwa ajili ya jina lake. 4. Naam, nijapopita kati ya bonde la uvuli wa mauti, Sitaogopa mabaya; Kwa maana Wewe upo pamoja nami, Gongo lako na fimbo yako vyanifariji. 5.Waandaa meza mbele yangu, Machoni pa watesi wangu. Umenipaka mafuta kichwani pangu, Na kikombe changu kinafurika. 6. Hakika wema na fadhili zitanifuata Siku zote za maisha yangu; Nami nitakaa nyumbani mwa Bwana milele.”

 Bonde la Wadi Quelt linalotajwa na daudi kama Bonde la Uvuli wa Mauti katika Zaburi 23.

Zaburi hii ni moja ya zaburi muhimu sana na Yenye maneno ya maana sana yenye usalama, Ingawa maandiko yake ni machache lakini yamebeba maana pan asana na nzito mno isiyoweza kupimika kuhusu Upendo wa Mungu kwa watu/mtu wake, Ni zaburi ambayo inaweza kutufunulia kwa kina upana na urefu wa Hali halisi ya uhusiano wa Mfalme Daudi na Mungu. Tutajifunza Zaburi hii kwa kutafakari vipengele vitatu vifuatavyo:-

·         Historia ya Zaburi hii
·         Bwana ni Mchungaji wa Ajabu
·         Sitaogopa Mabaya

Historia ya Zaburi hii:-

Zaburi ziko za Aina mbalimbali, lakini zaburi hii inaangukia katika Kundi la Zaburi za kujitia moyo, Katika moja ya chanzo yaani Commentary ambayo niliiisoma, inatuhakikishia wazi kuwa zaburi hii ni ya Daudi aliyekuwa mfalme wa Israel, Lakini sababu ambazo zilipelekea Daudi kuandika zaburi hiii ambayo inaonekana aliiandika kabla ya kuwa mfalme inazungumzia mazingira ya Bonde liitwalo kwa Kiarabu Wadi Quelt unaweza kugoogle jina hilo katika wikipidia, Bonde hili liko katika ukanda wa Magharibi yaani West Bank wa Mto Jordani Karibu na Yerusalem njia ya kuelekea Yeriko karibu na bahari ya Chumvi, Eneo hilo lilikuwa ni eneo hatari sana na lenye majabali ambapo kama mtu angeangukia huko kifo tu ndio kingekuwa zawadi yake, ni Bonde la Kutisha sana na njia yake pia ilikuwa na vibaka na majambazi na huenda ilikuwa ni simulizi na maonyo kutokupita eneo hilo hatari lililoogopewa sana, Bonde hilo lenye kutisha lilikuwa ni halisi na ni halisi hata sasa kwa vile liko hata leo, Kwa vile lilikuwa ni Bonde lenye kuogopesha wengine waliliita Pango la Jabali au Bonde la Mauti, kuna uwezekano kuwa watu wengi walipoteza Maisha katika eneo hilo na hata wachungaji walipoteza mifugo yao huko na walishindwa kuiokoa.

Bwana Ni Mchungaji wa Ajabu:-

Daudi anataka kumfunua Mungu anayemjua Yeye na mwenye uhusiano naye Jinsi alivyomkuu na alivyo na ujasiri kumtegemea, anataka kuionyesha jamii kuwa yeye anaweza kupita katika Bonde hilo lenye harufu ya kifo na akatoka salama, kule ambako jamii nzima inaogopa yeye angeliweza kupita tu kwa  sababu hakuna jambo lolote lenye kuogopesha linaweza kulinganishwa na Mungu wa Daudi na Mchungaji mwema, Kuweza kufahamu kila Daudi anakizungumzia ni lazima tufanye uchambuzi wa Maneno mazito yaliyomo katika zaburi hii.

1.       Bwana ni Mchungaji wangu – Kwa ufupi sana Daudi anatumia Mfano huu (Metaphor) ambao mara nyingi umetumiwa sana na waandishi wa Biblia hususani katika Agano la kela kuonyesha jinsi Mungu anavyojali na kujihusisha na watu wake (Zaburi 28:9, 79:13, 80:1, 95:7 Isaya 40:11Yeremia 31:10 na Ezekiel 34:6-19) Yesu mwenyewe alikuja kuuweka wazi kabisa kuwa Yeye ndiye huyu Mchungaji mwema anayetajwa katika zaburi hii na maandiko mengine  Yohana 10:11-16, Ukweli unaofunuliwa hapa ni sisi ni watoto wa Mungu Mungu ni Baba na ni mwangalizi mkuu wa Maisha yetu, Yeye hutujali na kutuangalia kwa upendo mkubwa sana kuliko wachungaji wanavyoangalia mifugo, Jambo kubwa la Msingi ili kunufaika na Bwana kama ilivyokuwa kwa Daudi ni lazima uwe na uhusiano wa kudumu na Mungu wetu.

2.       Sitapungukiwa kitu – Mungu kama Mchungaji mwema yuko tayari kurupatia malisho, huu ndio ulikuwa wajibu mkuu wa wachungaji wa wanyama walipaswa kuhakikisha kuwa Konndoo wanashiba ipaswavyo, ni wazi kuwa Mungu hushughulkika na mahitaji yetu kiasi ambacho hatutapungukiwa na kitu

3.       Kando ya malisho ya majani mabichi hunilaza – Ulikuwa ni wajibu mwingine wa Mchungaji kuhakikisha kuwa anawapa raha mifugo yake, ikiwa Mungu ni Mchungaji mwema na sisi tu Kodnoo zake yeye hutupa kustarehe pia Yesu alisema Njooni kwangu ninyi nyote wenye kuelemewa na Mizigo nami nitawapumzisha “Mathayo 11:28” haingekuwa hekima ya kawaida common wisdom kwa Mchungaji kuwazungusha mifugo kutwa nzima bila kuwapa pumziko, Mungu anajua kuwa tunahitaji pumziko, ingawa tunapitia changamoto za aina mbalimbali katika ulimwengu huu, Mungu atatupa nyakati za Kuburudika, Acha kusema kuwa utapumzika Kaburini, au au Heri wafu wafao katika Bwana, hayo maneno Daudi hakuyatamka hata kidogo yeye alljua kuwa Mungu atampa pumziko sawa kuna hilo la baadaya lakini hapahapa duniani pia tutafaidika na kazi za Mchungaji mwema, Mungu atalitumia neno lake kama chakula kutulisha na kututia nguvu,Yohana 6:32

4.       Kando ya maji ya utulivu huniongoza. – Ni wazi kuwa Maji yanawakilisha uwepo na faraja ya Roho Mtakatifu, kwa wale wakristo amabao wamejazwa Roho mtakatifu wanafahamu jinsi anavyoburudisha na kuleta utulivu mioyoni mwetu hata kama twapitia majaribu ya aina mbalimbali, Yeye ndio Chemichemi ya uzima acha kujichimbia visima vyako Yeremia 2:13 Roho wa Mungu yuko kutupa faraja ya kweli, ambayo haipatikani kwa Pombe au zinaa au uvutaji wa Bangi kila aina ya burudiko na bubujiko lililo bora utalipata kwa Roho wa Mungu

5.       Hunihuisha nafsi yangu – katika ulimwengu huu tulio nao yako mambo mengi ya kukatisha tamaa na kuvunja Moyo na kuifanya nafsi kuinama, Mungu wa Daudi aliweza kumtia nguvu alimtia Moyo, Zaburi 42:11, Tunapokutana na wakati mgumu wa kukabiliana na changamoto mbalimbali kama tumemfanya Yehova kuwa Mchungaji wetu atatufariji na kuzihuisha nafsi zetu, Daudi alilifahamu hilo vema aliona wema wa Mungu ukifanya hayo katika maisha yake

6.       Huniongoza Katika njia za Haki – Ni muhimu kufahamu kuwa ni Mungu kupitia Roho wake mtakatifu ndiye anayetuongoza katikia njia ya haki Warumi 8;14, Kwaasili mwanadamu havutiwi sana na kutembea katika haki, moyo na nia ya kuhakikisha kuwa tunatembea katika haki hupatikana kwa msaada wa Roho Mtakatifu, na ndio maana ni muhimu ikaeleweka wazi kuwa haki tuliyo nayo haitokanani na uweza wetu na uamuzi wetu ni haki ya Yesu Kristo na tunatembea katika hiyo kwa neema na uongozi wake Daudi alilijua hili wazi,Warumi 8:5-14, alitambua nia ya mwili siku zote inafanya uadui dhidi ya Mungu na kuwa kama anatembea katika haki ni kwa sababu ya utii wake wa kukubali kumsikiliza Mchungaji mwema na so sauti ya Mgeni Yohana 10:3-4, 5.

7.       Kwaajili ya Jina lake:-  Mungu hutufanyia miujiza mikubwa na kutisha na kushangaza kwaajili ya jina lake, wema wote anaotutendea Mungu hufanya ili apate utukufu Zekaria 2:8Kwa maana Bwana wa majeshi asema hivi, Ili nitafute utukufu amenituma kwa mataifa wale waliowateka ninyi; maana yeye awagusaye ninyi aigusa mboni ya jicho lake” Mungu hututetea kwaajili ya Utukufu wake Daudi alijua wazi kuwa kuna kitu cha ziada ndani yake jina la bwana linatukuzwa na hivyo kamwe Mungu hataacha kumuongoza katika njia za haki kwa sababu ya Jina lake takatifu aliloliweka ndani ya Daudi, Mungu akiweka kitu ndani yetu atatuongoza kwaajili yake

8.       Naam, nijapopita kati ya bonde la uvuli wa mauti, Sitaogopa mabaya; Kwa maana Wewe upo pamoja nami:- Daudi sasa analitaja lie Bonde la Wadi Quelt Bonde lenye kutisha sana, ni wazi kuwa Daudi analitumia Bonde hilo kuonyesha kuwa kuna magumu katika ulimwengu huu kuna mambo ya kutisha katika ulimwengu huu, Mungu hatatuacha tusipitie katika magumu, na majaribu, kwamba iwe ni nyakati za hatari, Magumu au hata hatari za kifo Yeye hataogopa mabaya kwa sababu Mungu atakuwa npamoja nayeYeye ni Mlinzi wetu,na ni Mwaminifu kamwe hawezi kutuacha Mathayo  28:20 Nami nitakuwa pamoja nayi hata ukamilifu wa Dahari Mungu ataendelea kuwa pamoja nasi

9.       Gongo lako na fimbo yako vyanifariji.:-  Fimbo na gongo vinawakilisha Mamlaka na silaha za Mungu pia humaanisha kutia nidhamu, au kurudi, kuadhibu, pia inawakilisha nguvu na utendaji wa Mungu Kutoka 21:20, Ayubu 9:34 fimbo ilitumika katika kumrudisha kondoo katika njia au kundi sahihi na iliwaadhibu pale walipokuwa kinyuma na matakwa ya Mchungaji, Mungu huwadhibu wale wampendao ili kuwapa nidhamu yeye mwenyewe lakini pia huwalinda na kuwatetea Gongo liko kwaajili yanulinzi na Usalama wa Kondoo.

10.   Waandaa meza mbele yangu, Machoni pa watesi wangu. Umenipaka mafuta kichwani pangu, Na kikombe changu kinafurika.:- Ukweli ni kuwa wanadamu hawafurahii mafanikio ya wanadamu wengine hata siku moja, kutokana na ubinadamu wao ndani yao kuna wivu na hivyo ni rahisi kuwa na maadui unapobarikiwa na Mungu, Lakini sio hivyo tu Mashetani majini na mapepo hayafurahii uhusiano wetu na Mungu, Daudi alifahamu wazi swala hilo lakini kutokana na ukuu na wema wa Mungu Daudi anamuona mungu kuwa ni mwenye kujali sana , ni mwenye kujali na kulata usalama kiasi ambacho pamoja na hatari ya mashetani na majini na mapepo na madui wa kibinadamu, Bado Mungu anatoa neema na Baraka za Kutosha anakubariki na kukufanikisha mbele ya wanaokuchukia, na hata wale waliokubali kutumiwa na shetani kututesa, Licha ya Baraka zake dhidi ya wanaotuchukio Mungu aliendelea kuonyesha kuwa Daudi ni Mtumishi wake tu ni mtumishi maalumu aliyemchagua amempaka mafuta! Hii ilikuwa ni Dalili ya wazi kuwa yeye amechaguliwa na Mungu na ana upendeleo maalumu na wa kipekee ana uhusiano na Roho Mtakatifu ulio wa Pekee  na kwa sababu hiyo hapungukiwi na kitu, Kikombe kilichofurika kinazungumzia mabalasi yenye uwezo wa kuchukua Galoni 40 za maji, Daudi alimaanisha kuwa kombe lake linafurika ukiwa na Mungu huna shaka maana Balasi lako halipungui, Ukimtegemea Mungu hutapungukiwa na kitu neema na rehema na kufurika roho wa Bwana kutaendelea kububujika siku zote za maisha yetu.

11.   Hakika wema na fadhili zitanifuata Siku zote za maisha yangu; Nami nitakaa nyumbani mwa Bwana milele:- Mchungaji siku zote aliandamana na kondoo kila walikokwenda uhusiano ulistawi waliwapenda na kuwa kitu kimoja, Daudi amabaye ana ujuzi mkubwa wa Kuchunga anaelewa wazi kuwa Mungu yuko pamona naye anafuatana naye akiwa na uso wa wema akiwa yuko tayari kufadhili,alijua kuwa Mungu akiambatana nawe siku zote atatoa msaada wenye kudumu, wema na fadhili bila kujali nini kitatokea mbele yako, Mchungaji hufanya shughuli zake zote kwaajili ya kondoo wake, daudi anamalizia kwa kuonyesha kuwa Lengo lake kuu la kuambatana na mchungaji huyu mwema ni ili siku moja autazame uso wake amtumikie na kumuabudu yeye milele.

Sitaogopa Mabaya:-



Nataka kuhitimisha ujumbe huu kwa kukazia kuwa ukimjua Mungu katika viwango ambayo Daudi alimfahamu Mungu, Hutaogopa chochote katika maisha yako, Mungu ndio zindiko letu, yeye ndie Mwamba ngao na kimbilio hatupaswi kuogopa lolote unapotamka Neno hilo Bwana ndiyo Mchungaji wangu! Kifurushi hicho cha Bwana ndiye Mchungaji wangu kinabeba maswala kadhaa  Nina uhusiano wa kipekee na Mungu, Yeye ndio anayenitunza, yeye ndiye starehe yangu na faraja yangu, Yeye ni faraja yangu, yeye ndiye mlinzi wangu, yeye ni mwaminifu, atanishindia majaribu, nimewekwa wakfu kwake, amanibariki, amanipa upako, ananitosheleza, niko naye milele mpango wangu ni kutokumuacha haya yote yatakufanya usiogope kitu chochote katika maisha yako na yeyote atakayejifanya kuwa ni adui yako atashangaa ukiandaliwa Meza machoni pake, kwaajili ya utukufu wake.
 


Ujumbe na Mkuu wa wajenzi mwenye Hekima
Rev. Innocent Kamote!