1Petro 3:10-12 “Kwa maana, Atakaye kupenda maisha, Na kuona siku njema, Auzuie ulimi wake usinene mabaya, Na midomo yake isiseme hila. Na aache mabaya, atende mema; Atafute amani, aifuate sana. Kwa kuwa macho ya Bwana huwaelekea wenye haki, Na masikio yake husikiliza maombi yao; Bali uso wa Bwana ni juu ya watenda mabaya.”
Utangulizi:
Ni muhimu kufahamu; kwamba ni
vigumu sana kuyapenda maisha hususani nyakati ambazo tunapitia maswala magumu, watu
wengi wanapopitia nyakati ngumu sana katika maisha yao huwa wanatamani kufa na
au wanakata tamaa kabisa hata kufikia hatua ya kufikiri kuwa Mungu hawajali na
kujishughulisha tena na maisha yao, Je umewahi kupitia maswala magumu sana
katika maisha hata kufikia ngazi ya kukata tamaa na kutamani kufa au kufikiria kuwa Mungu hakujali? watu wengi
wamewahi kufikiri hivyo, hata mimi pia katiika vipindi Fulani mbalimbali, maisha sio kitu rahisi lakini maisha ni ya
muhimu sana, maisha yana changamoto nyingi sana lakini bado maisha yanabaki
kuwa ni ya muhimu mno!. Mtume Petro
anawaandikia Wakrito ambao walikuwa wanapitia nyakati za Mateso na nyakati
ngumu sana na anatoa ushauri unaokwenda sambamba na Zaburi iliyoandikwa na Mfalme Daudi kuhusu Maisha:-
Zaburi 34:12-16 “Ni nani mtu yule
apendezwaye na uzima, Apendaye siku nyingi apate kuona mema? Uuzuie ulimi wako
na mabaya, Na midomo yako na kusema hila. Uache mabaya ukatende mema, Utafute
amani ukaifuatie. Macho ya Bwana huwaelekea wenye haki, Na masikio yake
hukielekea kilio chao. Uso wa Bwana ni juu ya watenda mabaya, Aliondoe
kumbukumbu lao duniani.”
Petro anaunga mkono kile
kilichosemwa na Daudi au anahubiri kitabu cha zaburi ya 34:12-16 akionyesha ni
namna gani watu wa Mungu wanapopita katika magumu wanapaswa kuyatazama maisha,
Petro pamoja na Daud mwandishi wa Zaburi wanatutia moyo kuwa na imani kwa ahadi
za Mungu wakati wote hata wakati tunapopitia changamoto za aina mbalimbali
katika maisha na kuendelea kuyapenda
maisha ili Mungu atukuzwe wakati wa Magumu yetu, tunaonyesha ukomavu na imani
badala ya kuchukizwa nayo kama ilivyokuwa kwa Suleimani mwandishi wa kitabu cha
Muhubiri ambaye aliyaiona maisha kuwa jambo lisilo na maana na hasa maisha ya
mtu wa kawaida asiye na imani huyaona maisha kama kujilisha upepo, Maisha yana
maana kubwa sana hata pamoja na magumu unayoyapitia! Hivyo hatuna budi
kuyapenda:-
Petro anaona kuwa ziko kanuni
ambazo angaweza kutushauri wote tunaoishi bila kujali kuwa tunaishi katika
mazingira mazuri au mabaya kiasi gani lakini Maisha ni zawadi ni neema ambayo
Mungu ametupa hivyo wakati wote tuwapo duniani, tunapaswa kumshukuru Mungu kwa
imani sasa katika kanuni hizo Petro anatuasa kwanza
1.
Kuuzuia
ulimi usinene mabaya !
Ni muhimu
kufahamu kuwa ulimi ndio kiungo chepesi zaidi kutumika katika maisha ya
mwanadamu, mtu mwenye ukomavu na busara
au mtu mkamilifu ni yule mwenye uwezo wa kujua namna na jinsi ya kuutunza
Ulimi, na kuutumia Biblia inaonyesha ya kuwa kiungo hiki kinabeba mamlaka kubwa
sana katika maisha yetu ikiwa ni pamoja na uzima na mauti ona Mithali 18:20-21 “Tumbo
la mtu litajazwa matunda ya kinywa chake; Atashiba mazao ya midomo yake. Mauti
na uzima huwa katika uwezo wa ulimi; Na wao waupendao watakula matunda yake.”
Kwa haraka sana ni ulimi ndio unaoweza kutubadilishia hali ya ulimwengu
wetu kuwa wa furaha au wa amani, kuyatawala mazingira ama kutawaliwa
kutengeneza hali ya hewa au kuiharibu, kunung’unika au kushangilia mwenendo
wetu mbele za Mungu na wanadamu unaweza kuathiriwa au kuwekwa sawa kwa ulimi!
Maneno ni silaha yenye nguvu sana inayoweza kuinua watu au kuwaharibu watu!
Patro ananyesha wazi kuwa tunaweza sana kujizuia maisha yetu na dhuruba za
ulimwengu kama endapo tu tutaweza kuzuia ndimi zetu ona Mithali 21:23 “Mtu azuiaye kinywa chake na
ulimi wake, Atajilinda nafsi yake na taabu.” Uwezo wa kuchagua nini
cha kuzungumza na nini cha kutokuzungumza uko katika uchaguzi wetu, lakini
wakati wote ni muhimu sana kukumbuka namna na jinsi tunavyoutumia ulimi, Ni
vigumu sana kumsoma na kumjua kwa undani mtu asiyezungumza, mara tu
unapozungumza ndipo watu wanapoweza kukujua wewe ni nani nani mtu wa namna
gani, Maneno yetu yanafichua kile kilichoko ndani yetu Moja ya hukumu watakayohukumiwa wanadamu
mbele za Mungu ni pamoja na kile wanachokizungumza Mathayo 12:33-37 “Ufanyeni mti kuwa mzuri
na matunda yake kuwa mazuri; au ufanyeni mti kuwa mbaya na matunda yake mabaya,
kwa maana kwa matunda yake mti hutambulikana. Enyi wazao wa nyoka, mwawezaje
kunena mema, mkiwa wabaya? Maana, kinywa cha mtu huyanena yaujazayo moyo wake.
Mtu mwema katika akiba njema hutoa mema; na mtu mbaya katika akiba mbaya hutoa
mabaya. Basi, nawaambia, Kila neno lisilo maana, watakalolinena wanadamu,
watatoa hesabu ya neno hilo siku ya hukumu. Kwa kuwa kwa maneno yako
utahesabiwa haki, na kwa maneno yako utahukumiwa.” Ni kutokana na
hekina na ujuzi wake Petro kuhusu Maisha yeye anaona ni vema kutuasa kutikunena
na hasa kunena mabaya, kila mtu mwenye hekima anapaswa kujua yampasayo kunena
na ikiwezekana azungumze maneno ya kujenga
sio mabaya au yenye hila ndani yake, Dhambi nyingi tunazozifanya na namna
tunavyowazunguzia watu kwa wema au kwa ubaya kwa kujenga au kwa kuibomoa
tunatumia ulimi, karibu kila iana ya dhambi ni lazima itauhusisha ulimi, kwa
msingi huo Daudi na Patro wanatutaka sisi kuutumia ulimi kuleta uponyaji duniani
na sio kuharibu Mithali 12:17-19 “ Atamkaye maneno ya kweli hufunua haki; Bali shahidi wa
uongo hutamka hila. Kuna anenaye bila kufikiri, kama kuchoma kwa upanga; Bali
ulimi wa mwenye haki ni afya. Mdomo wa kweli utathibitishwa milele; Bali ulimi
wa uongo ni wa kitambo tu.” Kama hakuna sababu ya kuzungumza ni vema
kutokuzungumza kuliko kuzungumza maneno ya kubomoa, kuna thawabu kubwa sana
Mbinguni kwa watu wa Mungu ambao watakuwa na ujuzi wa namna na jinsi ya
kuutumia ulimi, na ni vema vile vile kwa pamoja tukiwa tunatafakari na kujadili
mambo yaliyo mazuri, yaliyo ya staha, yenye kujenga , yenye wema, yenye
kupendeza, yenye sifa nzuri hayo ndio maswala ya kuyajadili na ndivyo neno la
Mungu linavyotutaka Wafilipi 4:8 “Hatimaye, ndugu zangu, mambo yo yote yaliyo ya kweli, yo
yote yaliyo ya staha, yo yote yaliyo ya haki, yo yote yaliyo safi, yo yote
yenye kupendeza, yo yote yenye sifa njema; ukiwapo wema wo wote, ikiwapo sifa
nzuri yo yote, yatafakarini hayo.” Tukitafakari mambo mema tutazungumza mambo
mema na tutaufanya ulimwengu uwe mahali pema pa kuishi na vilevile katika
maisha yajayo baada ya kufa tutakuwa na wakati mwema na Mungu, kwa msingi huo
basi kanuni ya kwanza ya kutufanya tuishi maisha mazuri na kuufurahia uumbaji wa Mungu na kuona siku
njema ni kuzungumza mambo mazuri yaliyo mema kwa msingi huo basin i vema mno
tukaangalia kile Daudi alikisema na kile ambacho Petro alikihubiri kwamba kama
tunapenda maisha na kutaka kuwa na siku njema katika kipindi hiki kifupi sana
ambacho Mungu ametupa kuwepo duniani basi ni vema tunayapokea maisha kwa
shukurani, kwa tabia njema tukiwa tumejaa neema na kuhakikisha kuwa tunawajenga
wengine kwa utukufu wa Mungu baba! Matumizi ya ulimi yanatujengea kanuni kubwa
na njema na nzuri ya kuyafurahia maisha kwa hiyo kuna umuhimu wa kujilinda na
kujihami tusinene mabaya, tusihukumu kwa haraka na kuhakikisha kuwa tunatenda
mema, Neno la Mungu linatutaka kwamba hata kama tunaishi katika nyakati ambazo
kila mtu anazungumza mabaya ni wakristo pekee na watu weme na wenye hekima
wanaoweza kuufanya ulimwengu kuwa mahali pema kwa kuzungumza maneno mema na
mazuri ya neema na tukatae kabisa kutumika kama chombo cha shetani kwa kuuujaza
ulimwengu maneno mabaya hata kama tunapitia mambo magumu Wakolosai 4:5-6 “Enendeni kwa hekima mbele
yao walio nje, mkiukomboa wakati. Maneno yenu yawe na neema siku zote,
yakikolea munyu, mpate kujua jinsi iwapasavyo kumjibu kila mtu.” Tunapozungumza
haya unaweza kujiuliza kwamba sasa nitafanyaje maana huenda mimi niko miongoni
mwa watu wenye midomo michafu sana yaani katika watu ambao wana majibu mabaya
mimi nimo, katika watu ambao wanajua kunya kwa mdomo, wanajua kutema vyondo na
mimi nimo na sasa nimeyaharibu maisha yangu kwa kuzungumza yasiyopaswa nawezaje
kuwa mwema tena? Usiogope kama uliutumia ulimi wako vibaya kabla hatujafika
katika hatua nyingine yako mambo muhuimu ya kufanya :-
a.
Muombe
Mungu akutakase Moyo wako, akili zako na maneno yako:
Ni vigumu kuishi maisha matakatifu na kumpendeza Mungu
kama maneno yetu ni mabaya meneno yetu ni kipimo ya kile kilichoko moyoni
mwetu, akilini kwetu na ndio huwa kinadhihirishwa kwa kusema kwetu ona Luka 6:45 “Mtu
mwema katika hazina njema ya moyo wake hutoa yaliyo mema, na mtu mwovu katika
hazina mbovu ya moyo wake hutoa yaliyo maovu; kwa kuwa mtu, kinywa chake hunena
yale yaujazayo moyo wake.” Yesu
anaonyesha wazi kuwa kile tunachokinena ni matokeo ya kile kilichoko moyoni,
Kwa msingi huo basi hatuna budi kumuomba Mungu atusafishe na kututakasa, mioyo
yetu, akili zetu na maneno yetu, Mungu akitusamehe na kutusafisha maneno yetu
yatakuwa na nguvu ya kuumba mambo mema kwaajili ya Mungu Ona Isaya 6:1-7 “Katika
mwaka ule aliokufa mfalme Uzia nalimwona Bwana ameketi katika kiti cha enzi,
kilicho juu sana na kuinuliwa sana, na pindo za vazi lake zikalijaza hekalu.
Juu yake walisimama maserafi; kila mmoja alikuwa na mabawa sita; kwa mawili
alifunika uso wake, na kwa mawili alifunika miguu yake, na kwa mawili aliruka.
Wakaitana, kila mmoja na mwenzake, wakisema, Mtakatifu, Mtakatifu, Mtakatifu,
ni Bwana wa majeshi; dunia yote imejaa utukufu wake. Na misingi ya vizingiti
ikatikisika kwa sababu ya sauti yake aliyelia, nayo nyumba ikajaa moshi. Ndipo
niliposema, Ole wangu! Kwa maana nimepotea; kwa sababu mimi ni mtu mwenye
midomo michafu, nami ninakaa kati ya watu wenye midomo michafu; na macho yangu
yamemwona Mfalme, Bwana wa majeshi. Kisha mmoja wa maserafi wale akaruka
akanikaribia; naye alikuwa na kaa la moto mkononi mwake, ambalo alikuwa
amelitwaa kwa makoleo toka juu ya madhabahu; akanigusa kinywa changu kwa kaa
hilo, akaniambia, Tazama, hili limekugusa midomo yako, na uovu wako
umeondolewa, na dhambi yako imefunikwa.” Isaya ni nabii aliyetumiwa
sana na Mungu, Lakini kabla ya kutumwa alijitakasa alitubia uovu wake na Mungu
akamtakasa kinywa chake na ndipo akamtumia, hatuna budi kuhakikisha kuwa
tunaomba na kujitakasa ili kwamba Mungu aweze kuyalinda mawazo yetu na
kutulinda na uharibifu. Kumbuka kwamba tumeumbwa kwa sura na mfano wa Mungu,
Mungu aliuumba ulimwengu huu kwa neno tu na mara kadhaaa laifanya miujiza kwa
kutamkqa neno ona Mwanzo 18:10-14 “Akamwambia, Hakika nitakurudia wakati huu huu mwakani, na
tazama, Sara mkeo atapata mwana wa kiume. Sara akasikia mlangoni pa hema
iliyokuwapo nyuma yake. Basi Ibrahimu na Sara walikuwa wazee, na umri wao
mkubwa, na Sara alikuwa amekoma katika desturi ya wanawake. Kwa hiyo Sara
akacheka moyoni mwake, akisema, Niwapo mkongwe, nitapata furaha, na bwana wangu
mzee? BWANA akamwambia Ibrahimu, Mbona Sara amecheka akisema, Mimi kweli
nitazaa mwana, nami ni mzee? Kuna neno gani lililo gumu la kumshinda BWANA? Kwa
muhula wake nitakurudia, wakati huu huu mwakani, na Sara atapata mwana wa kiume.”
Unaweza kuona Mungu hapa anatamka neno na lile neno linakuwa kama vile
alivyotamka, sisi nasi tumeumbwa kwa mfano wake Mungu akikitakasa kinywa chetu
na kujifunza nidhamu ya kutunza kinywa tutakuwa na mamlaka katika matamshi yetu
nan a kusababisha uumbaji, mimi ni Mwalimu pia wa chuo cha Biblia chuo cha
Biblia kibiblia huitwa chuo cha manabii, hivyo nafundisha manabii pia ni
Mwalimu wa manabii ili nabii aweze kuwa na mamlaka anapaswa kuwa na kinywa safi
ili kinywqa cheke kiwe na mamlaka na ndio maana kabala Mungu hajamtumia nabii
isaya alimtakasa kinywa cheke kisha akaweka neno lake hivyo isaya akatabiri
mambo mengi kuhusu masihi na yakatimia, Manabii wengi walikuwa wakijitunza
vinywa vyao na hivyo vinywa vyao vikawa na mamlaka kubwa sana ona, Nabii Elisha
alitamka tu kama Mungu alivyomtamkia Sara na kile alichokinena kikatimia 2Wafalme
4:16-17 “Akasema, Panapo wakati huu mwakani,
utamkumbatia mwana. Akasema, La! Bwana wangu, wewe mtu wa Mungu, usiniambie
mimi mjakazi wako uongo. Yule mwanamke akachukua mimba, akazaa mtoto mume
wakati uo huo mwakani, kama Elisha alivyomwambia.”Elisha
anatufundisha kuwa tunaweza kutamka kitu kama Mungu nqa kikawa vilevile
kwaajili ya hayo tujnaina kuwa kuna umuhimu mkubwa sana wa kuomba kutakaswa ili
kwamba vivywa vyetu viweze kuwa na mamlaka ona 1Wafalme 17:1 “Basi Eliya Mtishbi, wa
wageni wa Gileadi, akamwambia Ahabu, Kama Bwana, Mungu wa Israeli, aishivyo,
ambaye ninasimama mbele zake, hakutakuwa na umande wala mvua miaka hii, ila kwa
neno langu.” “2 Wafalme 6:24-30 “Ikawa baada
ya hayo, Ben-hadadi mfalme wa Shamu akakusanya majeshi yake yote, akakwea
akauhusuru Samaria. Njaa ikawa kuu huko Samaria; na tazama, wakauhusuru, hata
kichwa cha punda kikapata kuuzwa kwa vipande themanini vya fedha, na kibaba cha
mavi ya njiwa kwa vipande vitano vya fedha. Ikawa mfalme wa Israeli alipokuwa
akipita ukutani, mwanamke mmoja akamwita akisema, Unisaidie, bwana wangu,
mfalme. Akasema, Bwana asipokusaidia, nikusaidieje mimi? Ya sakafuni, au ya
shinikizoni? Mfalme akamwambia, Una nini? Akajibu, Mwanamke huyu aliniambia,
Mtoe mtoto wako, tumle leo, na mtoto wangu tutamla kesho. Basi, tukamtokosa
mtoto wangu, tukamla; nikamwambia siku ya pili, Mtoe mtoto wako, tumle; naye
amemficha mtoto wake. Ikawa, mfalme
alipoyasikia maneno ya huyo mwanamke, aliyararua mavazi yake; (naye alikuwa
akipita juu ya ukuta;) na watu wakaona, na tazama, alikuwa amevaa magunia ndani
mwilini mwake.” Tatizo la Njaa hapa lilikuwa kubwa sana mpaka
yakatokea hayo yaliyotokea lakini Elisha alitamka neno la matumaini ambalo ni
vigumu kuamini kuwa linaweza kutokea katika mazingira kama yale lakini kwakuwa
kinywa chake kilikuwa na mamlaka Mungu aliweza kutekeleza kile alichokisema ona 2 Wafalme 7:1-2 “Elisha
akasema, Lisikieni neno la Bwana; Bwana asema hivi, Kesho panapo saa hii,
kipimo cha unga mzuri kitauzwa kwa shekeli, na vipimo viwili vya shayiri kwa
shekeli, langoni pa Samaria. Basi yule akida, ambaye mfalme alikuwa akitegemea
mkono wake, akamjibu yule mtu wa Mungu, akasema, Tazama, kama Bwana angefanya
madirisha mbinguni, je! Jambo hili lingewezekana? Akamwambia, Angalia, wewe
utaliona kwa macho yako, lakini hutakula.” Hali kama hii hata sisi
tunaoishi zamani za siku hizi zama za agano jipya tunaweza kabisa kutumia ndimi
zetu kwa mamlaka makubwa endapo tutakubali Mungu atutakase ndimi zetu na
kututuimia Matendo 3:6 “Lakini Petro akasema, Mimi sina fedha, wala dhahabu,
lakini nilicho nacho ndicho nikupacho. Kwa jina la Yesu Kristo wa Nazareti,
simama uende.” Kwa msingi huo tunaona kuwa kuna faida kubwa sana
kuwa na nidhamu kwa kutunza ndimi zetu na kutakaswa kwa ndimi zetu ili kwamba
vinywa vyetu viweze kutumiwa na Mungu kwa mamlaka iliyokubwa zaidi, hata Pepo
huwa wanatii watu wanaojua kutumia vinywa vyao vyema .
b.
Omba
kwamba Mungu ailinde dhamiri yako:
Ni muhimu kuyapima maneno yetu kabla ya kuyazungumza,
Ni muhimu kwetu kumuomba Mungu azilinde dhamiri zetu ili kwamba wakati wote
tukusudie kuzungumza mambo mazuri wakati wote tunapokusudia kuzungumza na kama
ni mazingira ambayo hatupaswi kusema lolote itakuwa vema basi tukanyamaza au
kumuomba Mungu atulinde vinywa vyetu ona Zaburi
19:14 “Maneno ya kinywa changu, Na mawazo ya moyo
wangu, Yapate kibali mbele zako, Ee Bwana, Mwamba wangu, na mwokozi wangu.”
Mara kwa mara wanadamu tunapenda, na
kulalamika hususani mbele ya rafiki zetu, wanfanyakazi, wanafunzi, wageni na
kaedhalika kwa kawaida hakuna mwanadamu anayefurahia kimsingi kusikia
malalamiko yetu, malalamiko huinajisi mioyo, kwa msingi huo ni vema sana
tukazuia vinywa vyetu lakini kwa kuwa hatuwezi basin a tumuombe Mungu kama
mwandishi wa zaburi ili kwamba Mungu atusaidie kila tunalolizungumza lipate
kibali mbele za Mungu!, Watu wengi sana wanafikiri kuwa Musa hakwenda kanaani
kwa sababu aliupiga mwamba hapana Musa alizunguimza yasiyofaa Zaburi 106:32-33 “Wakamghadhibisha
penye maji ya Meriba, Hasara ikampata Musa kwa ajili yao, Kwa sababu waliiasi
roho yake, Akasema yasiyofaa kwa midomo yake.” Wana wa Israel kwa
sababu ya kunungunika kwao mara kwa mara walimkosesha Musa na kumfanya Musa
kutamka mambo yasiyofaa na kwa sababu hiyo, hakuruhusiwa kuingia Kanaani.
Ni muhimu kukumbuka kuwa maandiko yanatuambia katika
wingi wa maneno hapakosi kuwa na maovu kwa msingi huo ni muhimu kumuomba Mungu
atupe akili ya kijizuia Mithali 10:19 “Katika wingi wa maneno hapakosi kuwa na maovu; Bali yeye
azuiaye midomo yake hufanya akili.” Kama wewe ni mropokaji sana
katika maneno ni muhimu sana kumuomba Mungu akuwekee walinzi katika kinywa
chako maneno yasikuchomoke tu kama risasi katika bunduki iliyokwisha
kutenguliwa kitufe Zaburi 141:1-3 “Ee Bwana, nimekuita, unijie hima, Uisikie sauti yangu
nikuitapo. Sala yangu ipae mbele zako
kama uvumba, Kuinuliwa mikono yangu kama dhabihu ya jioni. Ee Bwana, uweke mlinzi kinywani pangu,
Mngojezi mlangoni pa midomo yangu.” Unaweza kuona mfano kwa
watakatifu waliotutangulia walijua hatari ya kuropoka walitaka Mungu aweke
mngojezi katika vinywa vyao, sisi nasi hatuna budi kumuomba Mungu aweke walinzi
kwenye vinywa vyetu
c.
Tujifunze
kuzungumza maneno ya kujenga:
Neno la Mungu linatufundisha ya kuwa tunaweza kutumia
vinywa vyetu kujenga, na hilo ndilo kusudi kubwa la Mungu kutuweka Duniani,
Biblia inaonya kuwa haifai kuzungumza maneno ya kubomoa, ulimi unafananishwa na
chemichemi, hakuna chemichemi moja inayoweza kutoa aina mbili za maji yaani
kama ni maji ya chumvi itakuwa ya chumvi na kama ni maji matamu itakuwa maji
matamu ona Yakobo 3:10-11 “Katika kinywa kile kile hutoka baraka na laana. Ndugu
zangu, haifai mambo hayo kuwa hivyo. Je! Chemchemi katika jicho moja hutoa maji
matamu na maji machungu?” Yakobo anataka kama tunazungumza jambo basi tuzungumze
kwa kusudi la kujenga, kwa msingi huo uko umuhimu wa kumuomba Mungu atuongoze
na kutusaidia ili tuzungumze maneno ambayo yatamjengea heshima yeye Waefeso
4:29 “ Neno lo lote lililo ovu lisitoke vinywani
mwenu, bali lililo jema la kumfaa mwenye kuhitaji, ili liwape neema wanaosikia.”
Kumbe tunapaswa kuzungumza maneno
mema yanayomfaa mwenye uhitaji kufaa mana yeke kujenga kutia ujasiri, kutia
moyo, kuleta tumaini, kuwatoa watu kwenye maumivu, kuwaendeleza kuwahuisha na
kuwainua,wakati wote
tujihadhari na mambo ushirika au maneno yatakayoharibu 1Wakoritho 15:33 “Msidanganyike; Mazungumzo
mabaya huharibu tabia njema.” Aidha biblia inatutaka tusiwe watu wa
mizaha kupitiliza Mithali inaonya kuwa kuna hukumu ambazozimewekwa tayari kwa
wenye mizaha Mithali 19:28-29 “Shahidi asiyefaa kitu hudhihaki hukumu, Na vinywa vya
wasio haki humeza uovu. Hukumu zimewekwa tayari kwa wenye mzaha; Na mapigo kwa
mgongo wa wapumbavu.”
Biblia inatufundisha kuwa wako vijana 42 ambao walipomuona nabii Elisha ambaye
alikuwa na upaa walimchokoza kwa kumtania na akachukizwa na jambo hilo kiasi ambacho
nabii aliweza kuamuru Dubu ambaye aliwararua vijana wale ona 1Wafalme 2:23-24 “Akakwea
kutoka huko mpaka Betheli; naye alipokuwa akienda njiani, wakatoka vijana
katika mji, wakamfanyizia mzaha, wakamwambia, Paa wewe mwenye upaa! Paa wewe
mwenye upaa! Akatazama nyuma akawaona, akawalaani kwa jina la Bwana. Wakatoka
dubu wawili wa kike mwituni, wakawararua vijana arobaini na wawili miongoni
mwao.” Kwa msingi huo tumeona kwa mujibu wa Petro kuwa ili mtu aweze
kufurahia maisha na kuona siku njema anapaswa auzuie ulimi wake usinene mabaya
au midomo yake isiseme hila na kwamba ni vema kutumia ulimi kwa kuijenga jamii
hapo tutayafurahia maisha.
2.
Na
midomo yake isiseme hila!
Mojawapo ya
tabia ambazo zimeumiza watu wengi sana duniani ni pamoja na hila au kutenda
hila au kusema hila Biblia ya kiingereza imetumia neno GUILE kuzungumzia hila ambalo tafasiri zake ni pamoja na Deceit, au cunning ambalo maana yake ni mbinu za kudanganya, au kwa lugha
nyingine ni kufanyiwa utapeli, udanganyifu, ujanja wenye nia ya kudanganya Biblia
ya Kiswahili inatumia neno hilo HILA,
Mungu anapendezwa sana na mtu ambaye hana hila ona Zaburi 32:1-2 “Heri aliyesamehewa dhambi,
Na kusitiriwa makosa yake. Heri Bwana asiyemhesabia upotovu, Ambaye rohoni
mwake hamna hila.” Kristo Yesu alipokuwa akiwachagua wanafunzi wake
alimuona mmoja wa wanafunzi wake akija na alimsifia kuwa ni Myahudi kwelikweli
ambaye hakuna hila ndani yake ona Yohana
1:47-48 “Basi Yesu akamwona Nathanaeli anakuja
kwake, akanena habari zake, Tazama, Mwisraeli kweli kweli, hamna hila ndani
yake. Nathanaeli akamwambia, Umepataje kunitambua? Yesu akajibu, akamwambia,
Kabla Filipo hajakuita, ulipokuwapo chini ya mtini nilikuona.”
Sasa basi ili
tuweze kuyafurahia maisha neno la Mungu linatuonya kuwa tujihadhari na hila
katika maisha yetu, tuhakikishe kuwa rohoni mwetu hakuna hila ili tuweze
kumpendeza Bwana, Yakobo ni mfano wa mtu aliyekuwa na hila, jina lake pia maana
yake ni mwenye hila alitumia hila kumlaghai kaka yake Esau ili kupata haki ya
uzaliwa wa kwanza ona Mwanzo 25:29-34 “Yakobo akapika chakula cha dengu. Esau akaja kutoka
nyikani, naye alikuwa amechoka sana. Esau akamwambia Yakobo, Tafadhali, unipe
hicho chakula chekundu nile, kwa kuwa ninazimia mimi. Kwa hiyo walimwita jina
lake Edomu. Yakobo akamwambia, Kwanza niuzie leo haki yako ya mzaliwa wa
kwanza. Esau akasema, Tazama, mimi ni karibu kufa, itanifaa nini haki hii ya
uzazi? Yakobo akamwambia, Uniapie kwanza. Naye akamwapia, akamwuzia Yakobo haki
yake ya mzaliwa wa kwanza. Yakobo akampa Esau mkate na chakula cha dengu, naye
akala, akanywa, kisha akaondoka, akaenda zake. Hivyo Esau akaidharau haki yake
ya mzaliwa wa kwanza.” Licha Yakobo kufanya hila kuupata haki ya
mzaliwa wa kwanza pia alitumia hila kupata Baraka kutoka kwa baba yake, Mwanzo 27:19-20 “Yakobo
akamwambia babaye, Mimi ni Esau, mzaliwa wako wa kwanza, nimefanya kama
ulivyoniambia. Ondoka, tafadhali, ukae kitako, ule mawindo yangu, ili roho yako
inibariki. Isaka akamwuliza mwanawe, Imekuwaje umepata upesi namna hii,
mwanangu? Akasema, Kwa sababu BWANA, Mungu wako, amenifanikisha.” Hata hivyo Hila alizokuwa nazo zilimtokea
puani katia maisha yake, aliishi maisha ya kudanganywa nay eye kwa miaika Mingi
sana kazi kubwa ilifanyika ya kumbadilisha kutoka kuacha hila na kuwa Israel,
ni kweli hila zinaweza kukufanikisha kwa kitambo na kutupa kile tunachofikiri
itatupa Lakini Mungu kwa namna yoyote ile hawezi kukubali kuibariki hila na
mwisho wa siku lazima tuvuine kile tulichokipanda Mwanzo 29:16-26 “Labani alikuwa na binti wawili, jina la mkubwa ni Lea, na
jina la mdogo ni Raheli. Naye Lea macho yake yalikuwa dhaifu, lakini Raheli
alikuwa mzuri wa umbo, na mzuri uso. Yakobo akampenda Raheli akasema,
Nitakutumikia miaka saba kwa kumpata Raheli, binti yako mdogo. Labani akasema,
Afadhali nikupe wewe kuliko mtu mwingine; kaa kwangu. Yakobo akatumika miaka
saba kwa kumpata Raheli. Ikawa machoni pake kama siku chache tu kwa vile
alivyompenda. Yakobo akamwambia Labani, Nipe mke wangu, maana siku zangu
zimetimia; niingie kwake. Labani akakusanya watu wote wa mahali pale, akafanya
karamu. Ikawa wakati wa jioni akamtwaa Lea, binti yake, akamletea Yakobo, naye
akaingia kwake. Labani akampa Lea mjakazi wake Zilpa, awe mjakazi wake. Ikawa,
kulipokuwa asubuhi, kumbe! Ni Lea. Akamwambia Labani, Nini hii uliyonitenda? Sikukutumikia
kwa Raheli? Mbona umenidanganya? Labani akasema, Havitendeki hivi kwetu, kumtoa
mdogo kabla ya mkubwa;” Hila sio njema na wakati wote inapotajwa
katika Biblia haielezwi kama kitu kizuri hakuna uzuri wowote katika hila , Hila
siku zote inahusishwa na kazi za ibilisi ona 2wakoritho 11:3 “Lakini nachelea; kama yule
nyoka alivyomdanganya Hawa kwa hila yake, asije akawaharibu fikira zenu,
mkauacha unyofu na usafi kwa Kristo.” Mungu ni mwaminifu naye
anapendezwa nasi tukiwa na tabia inayofanana na yeye hivyo anatoa wito kwetu
kuwa watu wasio na hila, Yesu Kristo mwenyewe hakuwa na hila ona 1Petro 2:21-22 “Kwa
sababu ndio mlioitiwa; maana Kristo naye aliteswa kwa ajili yenu, akawaachia
kielelezo, mfuate nyayo zake. Yeye hakutenda dhambi, wala hila haikuonekana
kinywani mwake”. Hila ndio moja ya dhambo mbaya ya kuepukwa Pale
Yesu alipomwambia Nathaniel kuwa hakuna hila ndani yake alikuwa amemaanisha
kuwa ni mtu mwenye kiwango cha juu sana cha uadilifu, Bwana ampe neema kila
mmoja wetu kuwa mbali na hila katika jina la Yesu amen
3.
Na
aache mabaya:
Wito wa Mungu
wakati wote kwa watu wake ni kuacha mabaya, ili mtu aweze kuwa na siku njema
aweze kuufurahia uumbaji na utendaji wa Mungu ni lazima aacha mabaya, Neno
kuacha mabaya katika lugha nyingine linatumika neno “Let him eschew evil” Lugha hii ina maana ya kujiepusha na maovu
mfano imetumika pia katiika Ayubu 1:1 “Palikuwa na mtu katika nchi ya Usi, jina lake alikuwa
akiitwa Ayubu; mtu huyo alikuwa mkamilifu na mwelekevu, ni mmoja aliyemcha
Mungu, na kuepukana na uovu.” Ingawa hatuwezi wakati wote kuepuka kukutana
na changamoto mbalimbali lakini hatuna budi kuhakikisha kuwa wakati wote
tunaendelea kuwa na huruma na upendo kwa jamii, na hakuna matu anayeweza kuishi
maisha ya raha moja kwa moja tuwapo duniani lakini ili tuweze kuyafurahia maisha
maisha ya uzima wa milele mbinguni basin i lazima tujiepushe au kuacha mabaya
hii ndio njia itakayotupatia maisha mema,
Kumbuka Petro alikuwa anawaandikia wakristo waliokuwa wanapoitia katika
mateso, kwa hivyo kwao hazikuwa siku njema lakini alikuwa akizungumza kuwa
uvumilivu wao utawaleta hatimaye katika kufurahia siku njema kwa hivyo aliwaasa
wasiache njia “ekklineo” – wasiende nje
ya njia njema, Zaburi 1:1-6 “Heri mtu yule
asiyekwenda Katika shauri la wasio haki; Wala hakusimama katika njia ya wakosaji;
Wala hakuketi barazani pa wenye mizaha. Bali sheria ya Bwana ndiyo impendezayo,
Na sheria yake huitafakari mchana na usiku. Naye atakuwa kama mti uliopandwa
Kandokando ya vijito vya maji, Uzaao matunda yake kwa majira yake, Wala jani
lake halinyauki; Na kila alitendalo litafanikiwa. Sivyo walivyo wasio haki; Hao
ni kama makapi yapeperushwayo na upepo. Kwa hiyo wasio haki hawatasimama
hukumuni, Wala wakosaji katika kusanyiko la wenye haki. Kwa kuwa Bwana anaijua
njia ya wenye haki, Bali njia ya wasio haki itapotea.” Ni wito wa
kiungu wakati wote kuwaita watu wageuke na kuacha njia zao mbaya ili aweze
kuwaponya na kuwabariki Ezekiel 33:11 “Waambie, Kama mimi niishivyo, asema Bwana MUNGU,
SIKUFURAHII kufa kwake mtu mwovu; bali aghairi mtu mwovu, na kuiacha njia, yake
mbaya, akaishi. Ghairini, ghairini, mkaache njia zenu mbaya; mbona mnataka
kufa, Enyi nyumba ya Israeli? ” ni ahadi ya Mungu kila wakati kuwabariki
watu na kuwatendea mema iwapo wataacha njia mabaya 2Nyakati 7:14 “ikiwa watu wangu, walioitwa kwa jina
langu, watajinyenyekesha, na kuomba, na kunitafuta uso, na kuziacha njia zao
mbaya; basi, nitasikia toka mbinguni, na kuwasamehe dhambi yao, na kuiponya
nchi yao.” Biblia inatutia moyo kuwa rehema za Mungu ziko haijalishi
kwamba umewahi kuwa muovu kwa kiwango gani lakini ukibadilisha njia yako leo
Mungu yuko tayari kuyabariki maisha yako na kuanza nawe ukurasa mbaya maandiko
yamesisitiza wakati wote kuacha njia mbaya, kuishi maisha ya toba kila wakati
na kuendelea kumpendeza yeye Isaya 55:6-8 “Mtafuteni Bwana, maadamu anapatikana, Mwiteni, maadamu yu
karibu; Mtu mbaya na aache njia yake, Na mtu asiye haki aache mawazo yake; Na
amrudie Bwana, Naye atamrehemu; Na arejee kwa Mungu wetu, Naye atamsamehe
kabisa. Maana mawazo yangu si mawazo yenu, wala njia zenu si njia zangu; asema
Bwana. ”
4. Atende mema!.
Petro anaonekana kuathiriwa sana na usomaji
wa zaburi, kwani anarejea tena katika kile ambacho alinukuu kutoka katika Zaburi
ya Daudi ambayo mara kadhaa imesisitiza kuwa sasa kwa kuwa tumeacha mabaya na
tutende mema ona Zaburi 37:1-4 “Usikasirike kwa
sababu ya watenda mabaya, Usiwahusudu wafanyao ubatili. Maana kama majani
watakatika mara, Kama miche mibichi watanyauka. Umtumaini Bwana ukatende mema,
Ukae katika nchi, upendezwe na uaminifu. Nawe utajifurahisha kwa Bwana, Naye
atakupa haja za moyo wako.” Ona pia Zaburi 37: 27-28 “Jiepue na uovu, utende mema, Na kukaa hata milele. Kwa kuwa Bwana hupenda haki, Wala hawaachi watauwa
wake. Wao hulindwa milele, Bali mzao wa wasio haki ataharibiwa.” Mara
kadhaa maandiko yameonyesha kile ambacho Mungu anakitaka kwetu na ambacho ni
kutenda mema Mika 6:8 “Ee mwanadamu, yeye
amekuonyesha yaliyo mema; na Bwana anataka nini kwako, ila kutenda haki, na
kupenda rehema, na kwenda kwa unyenyekevu na Mungu wako!”
5. Atafute amani.
Mwisho Petro anataka tuitafute amani, kwa
kweli neno la Mungu Biblia kwa mukhtasari ni kitabu cha amani, ili mtu awe
kamili anapaswa kuwa na amani na Mungu na amani na wanadamu, hili ndio agizo la
kibiblia, Waebrania 12:14 “Tafuteni kwa bidii
kuwa na amani na watu wote, na huo utakatifu, ambao hapana mtu atakayemwona
Bwana asipokuwa nao;” Amani ina faida kubwa sana kwetu tunapotaka
kustawisha uhusiano wetu kwa Mungu na wanadamu, hatuwezi kuwa sawa na Mungu
kama hatuna amani na mtu fulani 1Yohana 4:20-21 “Mtu
akisema, Nampenda Mungu, naye anamchukia ndugu yake, ni mwongo; kwa maana
asiyempenda ndugu yake ambaye amemwona, hawezi kumpenda Mungu ambaye hakumwona.
Na amri hii tumepewa na yeye, ya kwamba yeye ampendaye Mungu, ampende na ndugu
yake.” Mke na Mume wasipokaa kwa akili na kuhakikisha kuwa wana
amani maombi yao yanaweza kuzuiwa 1Petro 3:7 “Kadhalika
ninyi waume, kaeni na wake zenu kwa akili; na kumpa mke heshima, kama chombo
kisicho na nguvu; na kama warithi pamoja wa neema ya uzima, kusudi kuomba kwenu
kusizuiliwe.” Watu wanapokosa amani kati yao na akama
hawajatengeneza au kupatana jambo hilo husima a kama ukuta katika ain azote za
ibada ikiwepo sadaka Mathayo 5:23-24 “Basi
ukileta sadaka yako madhabahuni, na huku ukikumbuka ya kuwa ndugu yako ana neno
juu yako, iache sadaka yako mbele ya madhabahu, uende zako, upatane kwanza na
ndugu yako, kisha urudi uitoe sadaka yako.” Yesu alimaanisha wazi
kuwa hatuwezi kupokea Baraka zozote zile kama tumevuruga amani, hivyo ni muhimu
kupatana na mashitaki wako upesi ili asizuie Baraka zako katika ulimwengu wa
Roho, Maagizo ya kibiblia yanatutaka tuitafute sana amani kwa sababu kuna
gharama kubwa sana kuipata, amani inapaswa kutafutwa kwa bidii, Yakobo alikuwa
amemuuzi kaka yake Esau kiasi ambacho Esau aliapa kuwa atamuua, jambo hili
lilisabababisha akimbie mbali ujombani, lakini huko nako hakuwa na amani maisha
yake yalikuwa taabuni kwa sababu Esaua angemuua na Esau aliposikia kuwa Yakobo
anakuja alikuja na kikosi cha askari mia nne huu ulikuwa wakati mbaya sana
katika maisha ya Yakobo na hapa ndipo alipoutafuta uso wa Mungu na vilevile alitafuta
msamaha wa kweli kutoka kwa Esau ona Mwanzo 32: 1-8 “Yakobo akashika njia yake na malaika wa Mungu wakakutana naye. Naye
Yakobo alipowaona, alisema, Hili ni jeshi la Mungu. Akapaita mahali pale,
Mahanaimu. Basi, Yakobo akapeleka wajumbe mbele yake kwenda kwa Esau nduguye
mpaka nchi ya Seiri katika nyika ya Edomu. Akawaagiza akisema, Mwambieni hivi
bwana wangu, Esau, Hivi ndivyo asemavyo mtumwa wako, Yakobo; Nimekaa ugenini
kwa Labani, na kukawia huko hata sasa, nami nina ng'ombe, na punda, na kondoo,
na watumwa, na vijakazi; nami nimepeleka watu nimpashe bwana wangu habari,
nipate neema machoni pako. Wale wajumbe wakarudi kwa Yakobo wakisema, Tulifika
kwa ndugu yako, Esau, naye anakuja kukulaki, na watu mia nne pamoja naye.Ndipo
Yakobo akaogopa sana, na kufadhaika sana, akawagawanya watu waliopo pamoja
naye, na kondoo, na ng'ombe, na ngamia, wawe matuo mawili. Akasema, Akija Esau
kwa kundi la kwanza, akalipiga, kundi litakalosalia litaokoka.” Ni
wazi kuwa Esau angekuja kufanya vita na Yakobo na yakobo aliogopa na aliamua
kumuomba Mungu usiku ule na Mungu alimuelekeza namna ya kupata amani ilimgharimu
sana lakini alifabya bidii ili aweze kuwa na amani na ndugu yake, kila atakaye
kupenda maisha yaani maisha haya nay ale yajayo hana budi kujikita katika
kuitafuta amani kwa bidii, Yakobo aliiitafuta sana na Mungu akamfanikisha Mwanzo 33:1-11 “Yakobo
akainua macho yake, akaona, na tazama, Esau anakuja na watu mia nne pamoja
naye. Akawagawanyia Lea, na Raheli, na wale vijakazi wawili, wana wao.
Akawaweka hao vijakazi na wana wao mbele, na Lea na wanawe nyuma yao, na Raheli
na Yusufu mwisho. Akapita mwenyewe mbele yao, akainama mpaka nchi mara saba,
hata alipomkaribia ndugu yake. Esau akaja mbio kumlaki, akamkumbatia, na
kumwangukia shingoni, akambusu; nao wakalia. Akainua macho yake, akawaona wale
wanawake na watoto, akauliza, Ni nani hawa walio pamoja nawe? Akasema, Ni
watoto Mungu aliompa mtumwa wako kwa neema yake. Ndipo wale vijakazi, na wana
wao, wakakaribia wakainama.Lea naye, na wanawe, wakakaribia wakainama. Baadaye
Yusufu na Raheli wakakaribia, wakainama. Akasema, Kundi hili lote nililolikuta,
maana yake ni nini? Akasema, Kunipatia kibali machoni pa bwana wangu. Esau akasema, Ninayo tele, ndugu yangu, uliyo
nayo na yawe yako. Yakobo akasema, Sivyo; kama nimekubalika machoni pako
tafadhali upokee zawadi yangu mkononi mwangu, iwapo nimeona uso wako kama kuona
uso wa Mungu, ukapendezwa nami. Pokea, tafadhali, mbaraka wangu, ulioletewa,
kwa sababu Mungu amenineemesha, na kwa sababu ninavyo hivi vyote
Akamshurutisha, naye akapokea.”
1Petro 3:10-12 “Kwa maana, Atakaye kupenda maisha, Na kuona
siku njema, Auzuie ulimi wake usinene mabaya, Na midomo yake isiseme hila. Na
aache mabaya, atende mema; Atafute amani, aifuate sana. Kwa kuwa macho ya Bwana
huwaelekea wenye haki, Na masikio yake husikiliza maombi yao; Bali uso wa Bwana
ni juu ya watenda mabaya.”
Na. Rev. Innocent Kamote.
Mkuu wa Wajenzi mwenye Hekima!
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni