Luka 14:21-23 “Yule mtumwa akaenda, akampa
bwana wake habari ya mambo hayo. Basi, yule mwenye nyumba akakasirika,
akamwambia mtumwa wake, Toka upesi, uende katika njia kuu na vichochoro vya
mji, ukawalete hapa maskini, na vilema, na vipofu, na viwete. Mtumwa akasema,
Bwana, hayo uliyoagiza yamekwisha tendeka, na hata sasa ingaliko nafasi. Bwana
akamwambia mtumwa, Toka nje uende barabarani na mipakani, ukawashurutishe
kuingia ndani, nyumba yangu ipate kujaa.”
Lakewood Church ni Kanisa linaloongozwa na Mchungaji Joel Osteen,
jijini Houston Texas Nchini Marekani ni
kanisa kubwa lenye washirika wapatao 45,000, Kanisa hili lina uwezo wa
kuketisha watu 16,800 kwa wakati wa ibada moja na wana ibada nne za kiingereza
na ibada mbili za Kihispania kwa wiki, hii ni moja ya mfano wa Kanisa kubwa
Utangulizi:
Ni muhimu kufahamu kwamba mara
nyingi sana tunajifunza jinsi ya kupanda makanisa, na aina ya makanisa
tunayopaswa kupanda, Lakini vile vile tunajifunza kuhusu uamsho, kukua kiroho
na maswala yanayofanana na hayo, tukihimiza kuhusu uinjilisti umisheni na
mengineyo, Hata hivyo wazo la kuwa na kanisa kubwa mara nyingi limeachwa
kuzungumziwa, kimsingi maswala yote ni muhimu kama kupanda makanisa, kufanya
uinjilisti, kutuma wamishionari, na uamsho mkubwa kutokea haya yote yanaweza
kufanyika kwa wepesi sana kama washirika wa makanisa na Watumishi wa Mungu
wataingiziwa wazo la kuwa na kanisa kubwa (Mega
Church) Roho wa Bwana tangu mwanzo katika mpango wake anaonyesha kuwa
anapendezwa na uwepo wa kanisa kubwa (Mega Church)
Kanisa kubwa kwa kawaida ni
kanisa lenye washirika wengi sana ambao hawapungui washirika 2,000 wanaohudhuria ibada ya mahali
pamoja na kushiriki katika maswala mbalimbali ya kielimu na kijamii kila wiki,
Mungu anapokuwa amekuamini anakupa kuchunga zaidi ya watu 2000 na kuendelea mpaka kufikia maelfu kwa maelfu, Yesu Kristo
wakati mwingine alikuwa na ibada zenye makusanyiko yenye watu wengi sana na
wakati Fulani maelfu kwa maelfu mpaka wakakanyagana
Luka 12:1a “Wakati huo, makutano
walipokutanika elfu elfu, hata wakakanyagana,” unaona elfu elfu
maana yake ni Elfu mara Elfu ni idadikubwa sana ya watu waliokusanyika
wakihitaji huduma ya kiroho kutoka kwa Yesu Kristo, Mungu anataka kila
mchungaji akue kiroho na abadilishe mtazamo na kuanza kufikiri mikakati ya kuwa
na Kanisa kubwa, lenye watu wengi sana kuanzia na kundi hilo dogo ambalo Mungu
amekupa, mpaka kufikia kuwa wengi sana
Ayubu 8:5 -7 “Wewe ukimtafuta Mungu kwa
bidii, Na kumsihi huyo Mwenyezi; Ukiwa wewe u safi na mwelekevu; Hakika yeye
sasa angeamka kwa ajili yako, Na kuyafanya makazi ya haki yako kufanikiwa. Tena
ujapokuwa huo mwanzo wako ulikuwa ni mdogo, Lakini mwisho wako ungeongezeka
sana.”
Unaona kimsingi Mungu anataka
kumfanikisha kila mchungaji na kila kanisa kuwa na maelfu ya watu, ni mapenzi
ya Mungu kila kanisa liwe na washirika wengi sana, idadi ya watu wanaookolewa
na idadi ya watu wanaopotea ikilinganishwa utaweza kuona kuwa wanaopotea ni
wengi sana kuliko wanaookolewa
Mathayo 7:13-14 “Ingieni kwa kupitia mlango
ulio mwembamba; maana mlango ni mpana, na njia ni pana iendayo upotevuni, nao
ni wengi waingiao kwa mlango huo. Bali mlango ni mwembamba, na njia imesonga
iendayo uzimani, nao waionao ni wachache.”
Yesu aliposema maneno haya hakuwa
na maana kuwa wakristo wawe wachache, au wanaookolewa wawe wachache, wala
hakutukataza kanisa kuridhika na watu wachache, kusudi lake ni kuonyesha tu
kuwa njia ya uzima haipendwi sana na sio rahisi kwa watu kuichagua kutokana na
ugumu wake, lakini linapokuja swala la kuokoa Roho Mtakatifu ameonyesha kuwa
ana uwezo wa kuokoa maelfu ya watu na kumfanya kila mchungaji kuwa na kanisa
kubwa sana, kuna faida kubwa san asana za kuwa na kanisa kubwa nitazizungumza
baadaye lakini nataka uelewe kwanza uelewe
kuwa ni mapenzi ya Mungu kuwa na kanisa kubwa na ni jambo ambalo
linawezekana na ni jambo la Baraka sana! Mungu anataka tuwe na makanisa makubwa sana
yajae watu mpaka wamwagike, ndio maana Mungu hajakupa mji Fulani pekee wala nchi
Fulani Mungu alitupa ulimwengu mzima
endendeni ulimwenguni kote Mungu anataka utukufu wake na habari za
mwanae Yesu Kristo zienezwe kila mahali mijini na vijijini kila mahali hata
mwisho wa nchi, hii maana yake nini kila unayemuona ni wako, kila unayemuona
anastahili kuwa mshirika wako, kila unayemuona fanya mkakati awe wako, Roho Mtakatifu ni Bwana wa Mavuno na Hashindwi
kuokoa maelefu kwa maelfu
Matendo 2:40-47 “Akawashuhudia kwa maneno
mengine mengi sana na kuwaonya, akisema, Jiokoeni na kizazi hiki chenye ukaidi.
Nao waliolipokea neno lake wakabatizwa; na siku ile wakaongezeka watu wapata
elfu tatu. Wakawa wakidumu katika fundisho la mitume, na katika ushirika, na
katika kuumega mkate, na katika kusali. Kila mtu akaingiwa na hofu; ajabu
nyingi na ishara zikafanywa na mitume. Na wote walioamini walikuwa mahali
pamoja, na kuwa na vitu vyote shirika, wakiuza mali zao, na vitu vyao
walivyokuwa navyo, na kuwagawia watu wote kama kila mtu alivyokuwa na haja. Na
siku zote kwa moyo mmoja walidumu ndani ya hekalu, wakimega mkate nyumba kwa
nyumba, na kushiriki chakula chao kwa furaha na kwa moyo mweupe, wakimsifu
Mungu, na kuwapendeza watu wote. Bwana akalizidisha kanisa kila siku kwa wale
waliokuwa wakiokolewa.”
Kwa hiyo utaweza kuona kuwa ni
mapenzi ya Mungu kuwa na kundi kubwa la washirika katika kanisa moja, Shetani
amefanikiwa sana kuwapa moyo wa kuridhika wachungaji wetu wengi, wengi wetu
tukishafanikiwa kumiliki Prado, kama Fulani, na kulipwa vizuri, na kujenga
nyumba nzuri na kuwa na uwezo wa kubadilisha mboga, basi watu wanaanza
kuridhika, na kufikiri kuwa wamekwisha kuvuka na wamefika, Ni jambo zuri
watmishi wa Mungu kuwa na unafuu wa maisha lakini tusikubali kabisa kuisikiliza
sauti ya shetani ikitunong’oneza “You
have made it” ushatoboa na kuwa kila kitu kwako kiko vizuri, shetani
akifanikiwa kukunongoneza na hayo tayari amekwisha kupiga upofu usitazame
mbele, Yeye anataka ubaki na kijikanisa kidogo na usahau kabisa kuwa kuna
maelfu kwa maelfu ya watu wanaenda jehanamu kila iitwapo leo, Idadi ya washirika
wako ni kipimo kidogo sana cha watu unaowapunguza wasiende motoni, Mungu
anataka uwe na macho mapana na yanayoona mbali, Maandiko hayaonyeshi kuwa ni
lazima uwe na idadi Fulani ya watu, lakini pia hayakatai wewe kuwa na idadi
kubwa sana ya watu, na Mungu
akikuamini unaweza kuwa na kanisa kubwa
hapa nikimaanisha kanisa lenye idadi kubwa sana ya watu wanaookolewa!
Historia ya kanisa inathibitisha
tu kwa mfano kanisa lililokuwako Antiokia lililochungwa na Barnaba na Paulo na
wenzao lilikuwa na washirika wapatao laki tano wanaoabudu mahali pamoja, Na kule Korea ya kusini Kanisa alilokuwa
akichunga David Yong Choi linauwezo wa kuketisha watu wapatao laki
saba 700,000 katika ibada moja, mchungaji huyu aliaminiwa na Mungu kiasi cha
kuwa na washirika zaidi ya milioni mbili, kwa hiyo wazo la kuwa na kanisa kubwa
linawezekana na sasa tunapozungumzia uamsho na mikazo ya kupanda makanisa
tusisahau kupanua mawazo ya watumishi wa Mungu kuwa na maeneo makubwa, majengo
makubwa, na maono makubwa ya kuhakikisha kuwa tunawafikia watu wengi sana na
kuwaleta kwa Yesu, jambo ambalo litaleta uamsho mkubwa zaidi. Uamsho ni ajenda
yetu! Tutajifunza somo hili Kanisa kubwa kwa kuzingatia maswala ya msingi
yafuatayo:-
·
Misingi ya kuwa na Kanisa kubwa
·
Faida za kuwa na kanisa kubwa
·
Jinsi ya kuwa na kanisa kubwa
Misingi ya kuwa na kanisa kubwa
Tumeona kuwa kuwa na kanisa kubwa
ni mapenzi ya Mungu, lakini hata hivyo ni muhimu kufahamu kuwa ili Mungu aweze
kulikuza kanisa kwanza inapaswa kuwa ndoto ya kila mchungaji kiongozi wa kanisa
la mahali pamoja, Kila mchungaji aanze kufikiri na kuwaza kuwa na MEGA CHURCH kuwa na Kanisa kubwa, Kwa
sababu Mungu ametupa shamba kubwa la mavuno kama Shamba letu la mavuno
lingekuwa dogo tungevuna kidogo lakini Shamba ambalo tumepewa ni ulimwengu mzima
Mathayo 28:18-20 “Yesu akaja kwao, akasema
nao, akawaambia, Nimepewa mamlaka yote mbinguni na duniani. Basi, enendeni,
mkawafanye mataifa yote kuwa wanafunzi, mkiwabatiza kwa jina la Baba, na Mwana,
na Roho Mtakatifu; na kuwafundisha kuyashika yote niliyowaamuru ninyi; na
tazama, mimi nipo pamoja nanyi siku zote, hata ukamilifu wa dahari.”
Shamba alilotupa Mungu sio pale
kilosa, tu wala sio Liwale tu, wala sio kiomboi, wala tambukareli, wala
misozwe, wala kule mndemo, sio nyegezi, wala Isanga, wala kilindoni, wala mafia
pekee Mungu ametupa ulimwengu mzima, Mungu ametupa mataifa yote, kumbuka basi
enendeni mkawafanye mataifa yote kuwa wanafunzi, kwa hiyo ni agizo la kibiblia
kufanya wanafunzi wengi maandiko sio tu yametupa uwanja mpana, lakini vile vile
tyunaelezwa kuwa mavuno ni mengi sana
Mathayo 9:36-38 “Na alipowaona makutano,
aliwahurumia, kwa sababu walikuwa wamechoka na kutawanyika kama kondoo wasio na
mchungaji. Ndipo alipowaambia wanafunzi wake, Mavuno ni mengi, lakini watenda
kazi ni wachache. Basi mwombeni Bwana wa mavuno, apeleke watenda kazi katika
mavuno yake.”
Unaona? mavuno ni mengi
tunaaambiwa na Mwalimu, na tena Bwana wa Mavuno Roho Mtakatifu yupo, na nadhani
uliona kasi yake ya mavuno kuanzia siku ya Pentekoste, kwa hiyo hatuna udhuru,
tunahitaji kwanza kuwa na ndoto, tunahitaji tu kuwa na maono, tunahitaji tu
kufanya maandalizi yanayolingana ili Mungu aweze kutuamini na kutupa watu wengi
sana, washirika wakiwa wengi sana maelfu kwa maelfu kuna mambo mengi sana
yatarahisishwa na kunakuwa na faida kubwa sana ambazo nitazielezea baadaye,
lakini wote lazima tukubaliene kuwa tumepokea kiasi, na bado tunataka Mungu
apanue mipaka yetu ili aweze kutujaza, lazima upanue hozi, yako ili Mungu
akuongeze
Zaburi 81:10 “Mimi ndimi Bwana, Mungu wako,
Niliyekupandisha toka nchi ya Misri; Fumbua sana kinywa chako nami nitakijaza.”
Zaburi 2:7-8. “Nitaihubiri amri; Bwana
aliniambia, Ndiwe mwanangu, Mimi leo nimekuzaa. Uniombe, nami nitakupa mataifa
kuwa urithi wako, Na miisho ya dunia kuwa milki yako.”
1Nyakati 4:9-10 “Naye Yabesi alikuwa mwenye
heshima kuliko nduguze; na mamaye akamwita jina lake Yabesi, akisema, Ni kwa
sababu nalimzaa kwa huzuni. Huyo Yabesi akamlingana Mungu wa Israeli, akisema,
Lau kwamba ungenibarikia kweli kweli, na kunizidishia hozi yangu, na mkono wako
ungekuwa pamoja nami, nawe ungenilinda na uovu, ili usiwe kwa huzuni yangu!
Naye Mungu akamjalia hayo aliyoyaomba.”
Unaona! Mungu yuko tayari
kutubariki, lakini sisi nasi tunasehemu yetu ya kufanya, ukifumbua sana kinywa
Mungu atakijaza, ukimuomba Bwana atakupa mpaka miisho ya dunia kuwa milki yako,
na ukiomba akuzidishie hozi (territory,
a boundary, a land mark, a state kwa
kiibrania Gebul Gebul) Mungu atazidisha, sasa maono haya hayawezi kuanzia
chini yanapaswa kuwa malengo ya kichwa cha kanisa n ahata ukiwa nayo moyoni tu,
athari zake zitaanza kuonekana kwa jamii ya kanisa la mahali pamoja, sasa basi
licha ya kuwa na ndoto hii yako mambo ya msingi ya kuyafanyia kazi ili tuweze
kuona matokeo yanayokusudiwa yakifumuka !
a.
Maombi
– Ni muhimu kufahamu kuwa hakuna mahali kokote ambako jambo lolote
linalohusiana na uamsho lilitokea bila maombi, wote tunajua kuwa Israel
waliokolewa kutoka utumwani baada ya kuuugua sana, walipolia na kuugua kwaajili
ya utumwa ule mzito Ndipo Mungu akashuka ili awaokoe, uamsho nyakati za kanisa
la kwanza yalikuwa ni matokeo ya watu kuomba kwa siku kumi walipokuwa wakiomba
siku ya Pentekoste Roho Mtakatifu alishuka na siku hiyo hiyo watu wapatao 3000
waliokoka na kanisa lilikuwa na kuongezeka kwa kasi
Matendo 1:12-14 “Kisha
wakarudi kwenda Yerusalemu kutoka mlima ulioitwa wa Mizeituni, ulio karibu na Yerusalemu,
wapata mwendo wa sabato. Hata walipoingia, wakapanda orofani, walipokuwa
wakikaa; Petro, na Yohana, na Yakobo, na Andrea, Filipo na Tomaso, Bartholomayo
na Mathayo, Yakobo wa Alfayo, na Simoni Zelote, na Yuda wa Yakobo. Hawa wote
walikuwa wakidumu kwa moyo mmoja katika kusali, pamoja nao wanawake, na Mariamu
mama yake Yesu, na ndugu zake.”
Unaona tunasoma
kwamba baada ya Yesu kupaa, jamaa walirudi katika chumba kilichokuwepo Oriofani
na kwa moyo mmoja walianza kuomba, maombi haya yakiwemo ya mama yake Yesu na
wanafunzi wengine na wengine waliokuwepo ndiyo yaliyokuwa sababu ya kuandaa
utayari wa Roho Mtakatifu kufanya kazi na wao, ni maombi ndiyo Daniel ndiyo
yaliyoleta matokeo ya uamshi wa Israel kurudi kwao baada ya miaka 70, ni Maombi
ya Mordekai na esta yaliyosababisha wayahudi waliohukumiwa kuuawa, kuwa na
nguvu dhidi ya adui zao, ni maombi ya Nehemia ndiyo yaliyoleta uamsho wa ujenzi
wa ukuta Yerusalem na maombi ya ezra yaliteta uamsho wa kiroho na kuwafanya
watu kutubu na kuanza kumcha bwana, hakunamkinaweza kutokea bkla maombi ya
dhati ya kuutaka uamsho, maombi ndio yanayosababisha kanisa kutuma wainjilisti,
manabii na mitume katika kazi zinazokusudiwa
Matendo 13:1-3 “Na
huko Antiokia katika kanisa lililokuwako palikuwa na manabii na waalimu, nao ni
Barnaba, na Simeoni aitwaye Nigeri, na Lukio Mkirene, na Manaeni aliyekuwa
ndugu wa kunyonya wa mfalme Herode, na Sauli. Basi hawa walipokuwa wakimfanyia
Bwana ibada na kufunga, Roho Mtakatifu akasema, Nitengeeni Barnaba na Sauli kwa
kazi ile niliyowaitia. Ndipo wakiisha kufunga na kuomba, wakaweka mikono yao
juu yao, wakawaacha waende zao.”
Matendo 4:24-33 “Nao
waliposikia, wakampazia Mungu sauti zao kwa moyo mmoja, wakisema, Mola, wewe
ndiwe Mungu, ndiwe uliyefanya mbingu na nchi na bahari na vitu vyote vilivyomo;
nawe ulinena kwa Roho Mtakatifu kwa kinywa cha babaetu Daudi, mtumishi wako,
Mbona mataifa wamefanya ghasia, Na makabila wametafakari ubatili? Wafalme wa
dunia wamejipanga, Na wakuu wamefanya shauri pamoja Juu ya Bwana na juu ya
Kristo wake. Maana ni kweli, Herode na Pontio Pilato pamoja na Mataifa na watu
wa Israeli, walikusanyika katika mji huu juu ya Mtumishi wako mtakatifu Yesu,
uliyemtia mafuta, ili wafanye yote ambayo mkono wako na mashauri yako
yamekusudia tangu zamani yatokee. Basi sasa, Bwana, yaangalie matisho yao;
ukawajalie watumwa wako kunena neno lako kwa ujasiri wote, ukinyosha mkono wako
kuponya; ishara na maajabu vifanyike kwa jina la Mtumishi wako mtakatifu Yesu.
Hata walipokwisha kumwomba Mungu, mahali pale walipokusanyika pakatikiswa, wote
wakajaa Roho Mtakatifu, wakanena neno la Mungu kwa ujasiri. Na jamii ya watu
walioamini walikuwa na moyo mmoja na roho moja; wala hapana mmoja aliyesema ya
kuwa kitu cho chote alicho nacho ni mali yake mwenyewe; bali walikuwa na vitu
vyote shirika. Na mitume wakatoa ushuhuda wa kufufuka kwake Yesu kwa nguvu
nyingi, na neema nyingi ikawa juu yao wote.”
Maombi yana
matokeo makubwa sana katika historia ya uamsho kokote pale utaweza kuona kuwa
uamsho huo ulisababishwa na maombi, kwa hiyo baada ya kuwa na ndoto au maono ya
kanisa kubwa mzigo mkubwa lazima uelekezwe katika kuomba maombi maombi maombi
na Roho Mtakatifu atashuka na kuanza kutimiza kiu na kutoa nguvu ya kutimiza
maono na mzigo ambao kimsingi ni wake kupitia sisi
b.
Ukuaji
wa ndani – Ukuaji wa Kanisa kiidadi utakuwa na maana sana kama utaanza na
ukuaji mkbwa wa ndani, Hapa nazungumzia ukuaji wa kiroho, Mungu hawezi kukupa
washirika wengi na ukawa na kanisa kubwa
kama kwanza bado hujahakikisha wale wachache wanakomaa kiroho, achana na haya
makusanyiko ya watu wanaohitaji mazingaombwe tu, wanaohitaji kuponywa tu,
wanaomfuata Yesu kwa sababu walikula mikate wakashiba, wale washirima wachache
tulionao lazima waandaliwe kuwa nguzo itakayokuwa na uwezo wa kubeba kanisa
kubwa, kwa msingi huo ni lazima waandaliwe kuwa viongozi, Yesu alikuwa na
wanafunzi wa aina nyingi, alikuwa na watatu muhimu, alikuwa na wote 12,
thenashara, alikuwa na wale 70 na alikuwa na wale 120, kisha walikuwepo 500 na
pia alikuwa na umati mkubwa sana wa
wanafunzi, Muhimu sana ni wale 12, hawa waliandaliwa kwa muda mrefu zaidi
kuliko wale wengine hii ni kwa sababu wao walikuwa ni Msingi wa kanisa, ni
nguzo,
Marko 3:13-19 “Akapanda
mlimani, akawaita aliowataka mwenyewe; wakamwendea. Akaweka watu kumi na
wawili, wapate kuwa pamoja naye, na kwamba awatume kuhubiri, tena wawe na amri
ya kutoa pepo. Akawaweka wale Thenashara; na Simoni akampa jina la Petro; na
Yakobo, mwana wa Zebedayo, na Yohana nduguye Yakobo, akawapa jina la Boanerge,
maana yake, wana wa ngurumo; na Andrea, na Filipo, na Bartholomayo, na Mathayo,
na Tomaso, na Yakobo wa Alfayo, na Thadayo, na Simoni Mkananayo, na Yuda
Iskariote, ndiye aliyemsaliti. Kisha akaingia nyumbani.”
Luka 10:1-12 “Basi,
baada ya hayo Bwana aliweka na wengine, sabini, akawatuma wawili wawili
wamtangulie kwenda kila mji na kila mahali alipokusudia kwenda mwenyewe.
Akawaambia, Mavuno ni mengi, lakini watenda kazi ni wachache; basi mwombeni
Bwana wa mavuno apeleke watenda kazi katika mavuno yake. Enendeni, angalieni, nawatuma
kama wana kondoo kati ya mbwa-mwitu. Msichukue mfuko, wala mkoba, wala viatu;
wala msimwamkie mtu njiani. Na nyumba yo yote mtakayoingia, semeni kwanza,
Amani iwemo nyumbani humu; na akiwamo mwana wa amani, amani yenu itamkalia; la,
hayumo, amani yenu itarudi kwenu. Basi, kaeni katika nyumba iyo hiyo, mkila na
kunywa vya kwao; maana, mtenda kazi amestahili kupewa ujira wake. Msihame-hame
kutoka nyumba hii kwenda nyumba hii. Na mji wo wote mtakaouingia,
wakiwakaribisha, vileni vyakula viwekwavyo mbele yenu; waponyeni wagonjwa
waliomo, waambieni, Ufalme wa Mungu umewakaribia. Na mji wo wote mtakaouingia,
nao hawawakaribishi, tokeni humo, nanyi mkipita katika njia zake semeni, Hata
mavumbi ya mji wenu yaliyogandamana na miguu yetu tunayakung'uta juu yenu.
Lakini jueni hili, ya kuwa Ufalme wa Mungu umekaribia. Nawaambia ya kwamba siku
ile itakuwa rahisi zaidi Sodoma kuistahimili adhabu yake kuliko mji huo.”
Muda hauwezi
kutosheleza kuinyesha aina zote za wanafunzi Yesu aliokuwa nao, lakini jambo
kubwa la Msingi ni kuwa wanafunzi wake walitofautiana viwango vya maandalizi
kwa makusudi mbalimbali, nafurahia sana kuwa makanisa mengi yana madarasa ya
jumapili ambapo watu hujifunza maandiko, lakini changamoto kubwa au dosari
kubwa ni kuwa hakuna madarasa ya biblia ya kuwatofautisha wanafunzi hao, katika
shule nyingi za jumapili makanisani mtu aluyeokoka miaka 20 iliyopita anakuwa
darasa moja tu na mtu aliyeokoma juzi, ndani ya kanisa kwa kawaida ukiacha
watoto ambao huwa na madarasa yao , na laba vijana ambao huwa na madarasa yao,
kunapaswa kuwepo na makundi kama manne kama sio matano ya watu tofauti kwa
mafundisho tofauti, mfano darasa la kwanza wanaweza kuwa watu wanaojifunza
masomo ya Mwanzo ya wokovu, kisha ubatizo, na meza ya bwana na kadhalika, dara
sa la pili wakawa ni watu wanaojifunza namna ya kuhubiri injili, kushuhudia,
kulea wanaookolewa na kadhalika, darasa la tatu likawa ni jamii ya watu
wanaojifunza kuhudumia wengine yaani watendakazi, hawa wanakuwa na uwezo wa
kuchaguliwa kuma wazee, mashemasi, na kusimamia makanisa ya nyumbani na kufanya
huduma hata za maziko na kadhalika, na kundi la nne likawa ni jamii ya watu
ambao wanaweza kuhudumu pamoja na Mchungaji, wanaweza kutumwa kufungua
makanisa, wanaweza kwenda kwenye shule za kupanda makanisa, n ahata kupelekwa
chuo cha Biblia kwa maandalizi ya utumishi wa juu zaidi, kisaikolojia ukiweka
watu wote darasa moja huwezi kupata ukuaji wa kiroho unaolingana na wengine
watachoshwa kujifunza mambo yale yale kwa miaka mingi, waumbie kiu ya kutamani
kuja darasa la juu kila wakati, tengeneza miundo itakayosaidia watu kukua
kiroho, kitabia na upendo, watu wakiandaliwa katika mtindo huo tutapata watu
wenye sifa kuwa ni nguzo, ambao watabeba mzigo mkubwa wa usimamizi wa kanisa,
na mchungaji utatoka kwenye ngazi ya kuchunga kundi dogo kwa fimbo na makubazi
na utakwenda kwenye kiwango cha kuchunga ukiwa juu ya farasi na mabuti na kofia
cowboy unayechunga ranch, Mungu akufunulie, yako makanisa unakuta mchungaji
ameita watu mbele anaombea watu wanaanguka na hakuna wahudumu, mapepo
yanafumuka watu mapaja yanaonekana hakuna hata watu wa kuwafunika, mapepo
yanapiga ngumi, hakuna mtu wa kuwabana, katika hali kama Hiyo Mungu katika
hekima yake atakuacha usubiri sana, huna watu, huna viongozi, huna wahudumu,
bado Imani yako iko kwenye kuwekea mikono tu, ukipewa watu elfu utawekea mikono
wangapi, kuna kiwango Mungu anataka ukifikie ukue na kanisa likue kazi ya
huduma itendeke, ukuaji wa watu ni muhimu sana, ukuaji wa kiroho wa Mchungaji
na wazee wa kanisa unatupa nafasi kubwa ya kukua kwa kanisa
Waefeso 4:11-15 “Naye
alitoa wengine kuwa mitume, na wengine kuwa manabii; na wengine kuwa
wainjilisti na wengine kuwa wachungaji na waalimu; kwa kusudi la kuwakamilisha
watakatifu, hata kazi ya huduma itendeke, hata mwili wa Kristo ujengwe; hata na
sisi sote tutakapoufikia umoja wa imani na kumfahamu sana Mwana wa Mungu, hata
kuwa mtu mkamilifu, hata kufika kwenye cheo cha kimo cha utimilifu wa Kristo;
ili tusiwe tena watoto wachanga, tukitupwa huku na huku, na kuchukuliwa na kila
upepo wa elimu, kwa hila ya watu, kwa ujanja, tukizifuata njia za udanganyifu.
Lakini tuishike kweli katika upendo na kukua hata tumfikie yeye katika yote,
yeye aliye kichwa, Kristo.”
Wagalatia 2:6-9 “Lakini
wale wenye sifa ya kuwa wana cheo; (walivyokuwa vyo vyote ni mamoja kwangu;
Mungu hapokei uso wa mwanadamu); nasema, hao wenye sifa hawakuniongezea kitu;
bali, kinyume cha hayo, walipoona ya kuwa nimekabidhiwa injili ya
wasiotahiriwa, kama vile Petro ya waliotahiriwa; (maana yeye aliyemwezesha
Petro kuwa mtume wa waliotahiriwa ndiye aliyeniwezesha mimi kwenda kwa
Mataifa); tena walipokwisha kuijua ile neema niliyopewa; Yakobo, na Kefa, na
Yohana, wenye sifa kuwa ni nguzo, walinipa mimi na Barnaba mkono wa kuume wa
shirika; ili sisi tuende kwa Mataifa, na wao waende kwa watu wa tohara;”
c.
Ukuaji
wa Hekima – Luka 2:52 “Naye Yesu akazidi kuendelea
katika hekima na kimo, akimpendeza Mungu na wanadamu.” Hakuna jambo
la msingi na la Muhimu kama kukua katika Hekima! wote tunafahamu umuhimu wa
Hekima, nimewahi kusikia watu wakimsifia mchungaji mmoja kwamba ana misimamo
mizuri, anafundisha vizuri lakini hana Hekima washirika walikuwa wakimteta
Mtumishi huyo Mzuri wa Mungu, na nilipokuwa nikitafakari na kujiuliza nilikuja
kusikia kuwa alikuwa alikuwa mkali na wakati mwingine alikuwa akiwashushua
washirika mbele ya watu na kuwafanya wajisikie kuaibishwa, anafokea mafundi
mitambo sauti inapokuwa haijakaa vizuri, anafokea mashemasi wake ambao
hajawafundisha vena kujua wajibu wao, ni wat utu wameambiwa wewe ni shemasi
kuanzia leo, lakini hawana mafunzo, tayari watu mia tatu tu wanamtoa jasho,
mzigo umemuelemea yeye, hajawafunza watu wabebe mzigo pamoja naye anabeba peke
yake anaelemewa na akiwa katika mifungo hasira na stresses zinamuelemea zaidi,
na katika kanisa lake ana majukumu mengine ya uangalizi wa makanisa mengine
tayari hajaandaliwa kuwa nguzo lakini amebebeshwa mzigo mkubwa kuliko uwezo
wake na hekima inakosekana, tunapojiandaa kuongoza umati mkubwa sana wa
watu basi Hekima ni ya muhimu sana Mfalme sulemani alipotawazwa kuwa mfalme na
kugundua kuwa anaongoza watu wengi sana alihitaji hekima kukua katika hekima ni
jambo la Muhimu sana! Ona
2Nyakati 1:7-12 “Usiku
ule Mungu akamtokea Sulemani, akamwambia, Omba utakalo nikupe. Sulemani
akamwambia Mungu, Umemfanyia baba yangu Daudi fadhili kuu, nawe umenimilikisha
mimi badala yake. Basi sasa, Ee Bwana Mungu, na limyakinie baba yangu Daudi
neno lako; maana umenitawaza niwe mfalme juu ya watu wengi kama mavumbi ya
nchi. Basi sasa nipe hekima na maarifa, nijue kutoka na kuingia mbele ya watu
hawa; kwa kuwa ni nani awezaye kuwahukumu watu wako hawa walio wengi? Naye
Mungu akamwambia Sulemani, Kwa sababu neno hili lilikuwamo moyoni mwako, wala
hukujitakia mali, wala utajiri, wala utukufu, wala maisha za wakuchukiao, wala
hukujitakia maisha ya siku nyingi; bali umejitakia hekima na maarifa, upate
kuwahukumu watu wangu, niliokutawaza juu yao; basi hekima na maarifa umepewa;
nami nitakupa mali, na utajiri, na utukufu, kupita walivyokuwa navyo wafalme
wote waliokuwa kabla yako, wala baada yako hapatakuwa na mtu atakayekuwa navyo.”
Kusimamia watu
walio wengi kunahitaji hekima, na maarifa, lazima uwe na neema kubwa ya
kukusaidia katika mazingira hayo, Kusimamia kanisa kubwa kama alivyo @Bishop Barnabas Mtokambali, au @Bishop
Zachary Kakobe, na wengineo rafiki zangu ambao sijawataja hapo kunahitaji
uwe na ukomavu mkubwa sana wa kiroho, lakini zaidi sana hekima, watu haw ahata
kama unaabudu katika kanisa lake hata kama hakujua lakini upendo wake unakuguza
moja kwa moja wanaongoza taasisi kubwa sana lakini wanauwezo wa kumfikia kwa
upendo mtu mmoja mmoja na kumgusa binafsi bila hata ya kujali wana heshima
kiasi gani, ili uongoze kanisa kubwa lazima tuombe hekima
Yakobo 1:5-6 “Lakini
mtu wa kwenu akipungukiwa na hekima, na aombe dua kwa Mungu, awapaye wote, kwa
ukarimu, wala hakemei; naye atapewa. Ila na aombe kwa imani, pasipo shaka yo
yote; maana mwenye shaka ni kama wimbi la bahari lililochukuliwa na upepo, na
kupeperushwa huku na huku.”
Hekima itakusaidia katika mifumo yote ya
i.
Kuweka maono na mipango mkakati ya kanisa na
ku9nyesha muongozo huku ukiwasaidia washirika kuelewa wanakokwenda
ii.
Kuwashirikisha washirika katika maswala mazima
ya huduma na kukusaidia kuongoza makundi madogo madogo kwa hiyari na kubeba
mzigo wa kanisa pamoja nawe
iii.
Kuhakikisha kuwa wanaifikia jamii, kwa kunda
matukio mbalimbali, kukutana na mahitaji yao, na kujihusisha na maswala ya
kijamii
iv.
Kufanya mawasiliano yenye tija na washirika na
watu wanaoizunguka taasisi, matumizi mazuri ya emails,mitandao ya kijamii
v.
Mpangilio mzuri na wenye kuvutia wa ibada, wenye
maana na unaotosheleza mahitaji ya kundi kwa watu wanaohudhuria kila siku n
ahata wageni, kuna kanisa moja alikwenda mgeni mmoja akakuta mchungaji anafoka
sana kiasi ambacho mgeni alijihisi anafokewa yeye na hakurudi tena, mawasiliano
mabaya
vi.
Jinsi na namna ya kuendeleza viongozi,
mipangilio ya kundi la maombi, kundi la kuabudu, kundi la kwaya, maombi na
ibada zinazotoa ukuaji wa kiroho wa binafsi na kuwaletea ahueni ya maisha
wanaohudhuria, watu wanakuja na mizigo yao kanisani na hivyo wanahitaji
kutuliwa wanapokuja kanisani
vii.
Kusimamia kweli za misingi ya kiroho za
kanisa lako, lakini vilevile kwenda na mabadiliko yaliyioko duniani, mfano
nyakati za leo madhabahu nyingi zinapambwa kwa mvuto wa kipekee wa mifumo ya
jipsum na taa za kuvutia, na kadhalika, wewe miaka yote uko namipazia ya
mirangi rangi kama mganaga wa kienyeji, be flexible badilika kutokana na
ukisasa ulioko, weka Priojectors au monitor za television zinazoonyesha nyimbo,
matangazo, na mahubiri ili wanaoandika waweze kufuatilia kwa kwa ukaribu bila
kupitwa na kitu, Mafundi mitambo wako wakipata semina nzuri kutoka kwa watu
wenye ujuzi sahihi wa vyombo vya music, wapigaji na kadhalika tutakuwa na ibada
zenye utulivu na kila kitu kitaenda vema na hekima yako itadhihirika katika
utaratibu mzima unaouweka.
Faida za kuwa na kanisa kubwa
1.
Huduma
mbalimbali – mojawapo ya faida ya kanisa kubwa ni pamoja na kuwa na huduma
mbalimbali, unakuwa na washirika wenye vipawa vyote, na karama nyingi sana, ujuzi
mwingi, elimu kubwa, wataalamu mbalimbali ambao kimsingi wanaweza kutumia
vipawa vyao katika kulisaidia kanisa, Kanisa la Full Gospel nilikokuwako zamani
kwa Askofu kakobe kwa mfano Engineer Mbwambo, aliyekuwa moja ya viongozi wa
kanisa hilo aliweza kutumia ujuzi wake huo katika kusimamia ujenzi wa Kanisa,
Fundi Mvungi kule Tanga Full Gospel, aliweza kusimamia ujenzi wa kanisa la
Nguvumali pale tanga, Profesa Kimeme katika kanisa la TAG anasaidia sana katika
ustawi wa shule za kanisa, idadi kubwa ya watu wanaokuwako kanisani inasaidia
kuwa na idadi kubwa ya watu wanaolifanya kanisa kuwa imara kama
wakishirikishwa, chukulia tu una walimu waliookoka wa sekondari na msingi wako
kanisani wameokoka umewafundisha Imani vizuri je huwezi kufurahia kipawa hicho
hicho kiktumiwa katika madarasa ya biblia jumapili?, kanisa kubwa lenye idadi
kubwa ya watu linaruhusu kuwa na watu wengi na huduma nyingi na zikipangiliwa
vizuri, huwezi kukosa watu wa kuratibu mambio mbalimbali na kuifanya huduma
kuwa na mvuto, uimbaji, utakuwa na waimbaji wa kutosha, wapiga vyombo, mafundi
mitambo, waandaaji wa matangazo, wanasheria wa kanisa, na wataalamu wa kila
aina.
2.
Nguvu
kubwa ya maombi - kanisa lenye watu
wengi linakuwa na nguvu kubwa sana ya maombi, mnaweza hata kuwa na mfumo wa maombi
ya mnyororo ambapo kila saa linaweza kuwa na watu wanaooomba kwa uaminifu na
kumnyima pumzi shetani, hata hivyo katika hali ya kawaida tu watu wanapokuwa
wengi na mkafanya maombi ya pamoja kunakuwa na nguvu kubwa sana ya uwepo wa
Mungu kwa kanuni za kibiblia
Mathayo 18:19-20 “Tena
nawaambia, ya kwamba wawili wenu watakapopatana duniani katika jambo lo lote
watakaloliomba, watafanyiwa na Baba yangu aliye mbinguni. Kwa kuwa walipo
wawili watatu wamekusanyika kwa jina langu, nami nipo papo hapo katikati yao.”
Maandiko
yanasema wawili au watatu wakipatana katika jambo lolote watakaloliomba
watafanyiwa sasa unapokuwa umati mkubwa sana wa watu maana yake nguvu ya maombi
ya umoja inakuwa kubwa kuliko maelezo. Mkuu wa anaga katiika eneo hilo anapigwa
na kusambaratishwa na kuleta mpenyo kwa haraka, kwa hiyo kadiri kanisa
linavyokuwa kiroho na kiidadi linajiweka katika nafasi kubwa ya ushindi
kutokana na muungano wetu na umoja wetu
Kumbukumbu 30:29-30 “Laiti wangekuwa na akili, hata wakafahamu haya, Ili
watafakari mwisho wao. Mmoja angefukuzaje watu elfu, Wawili wangekimbizaje elfu
kumi, Kama Mwamba wao asingaliwauza, Kama Bwana asingaliwatoa? ”
Andiko laonyesha
nguvu ya mtu mmoja ni 1000 na nguvu ya watu wawili ni 10,000 je wakiwa 1000?
Tunapokuwa wengi tunakuwa na nguvu kuibwa sana ya kiroho kuliko kawaida na ndio
maana shetani katika hekima yake hatataka kanisa lolote la mahali pamoja liwe
kubwa n ahata mawazo ya kuwa na kanisa kubwa kwa wachungaji haiwezi kupangwa kwa
urahisi.
3.
Umati
huvutia umati – Kwa kawaida unapokuwa na umati mkubwa sana wa watu, umati
huo unatabia ya kuvuta umati, mfano unapokuwa na kanisa lenye watu mia tano
nadhani huwezi kukosa wageni 25 kwa kiwango cha chini sana kwa mwezi, lakini
sio hivyo tu matarajio ya watu huwa ni makubwa na Imani hupanda sana, Imani ya
kila mmoja inakuwa kwa kasi sana na kupaa juu, kuliko Imani ya mtu mmoja, kuna
kanuni hii ya kuwa Mungu pia hujitukuza kwenye umati mkubwa sana wa watu,
thamani ya muhubiri inapanda kila mtu mwenye shida yake anataka kukufikia na
kuutumia muda mfupi sana ulionao kukutana na mahitaji yao
Luka 5:18-24 “Na
tazama, wakaja watu wanamchukua kitandani mtu mwenye kupooza; wakataka
kumpeleka ndani na kumweka mbele yake. Hata walipokosa nafasi ya kumpeleka
ndani kwa ajili ya lile kundi la watu, walipanda juu ya dari wakampisha katika
matofali ya juu, wakamshusha yeye na kitanda chake katikati mbele ya Yesu. Naye
alipoiona imani yao, alimwambia, Ee rafiki, umesamehewa dhambi zako. Basi, wale
waandishi na Mafarisayo wakaanza kuhojiana wakisema, Ni nani huyu asemaye
maneno ya kukufuru? N'nani awezaye kusamehe dhambi isipokuwa Mungu peke yake?Na
Yesu alijua hoja zao, akajibu akawaambia, Mnahojiana nini mioyoni mwenu? Lililo
jepesi ni lipi? Kusema, Umesamehewa dhambi zako, au kusema, Ondoka, uende?
Lakini, mpate kujua ya kwamba Mwana wa Adamu anayo amri duniani ya kusamehe
dhambi, (alimwambia yule mwenye kupooza). Nakuambia, Ondoka, ujitwike kitanda
chako, ukaende zako nyumbani kwako.”
Yesu alikuwa
amezingirwa na umati mkubwa sana kiasi ambacho ilikuwa ni ngumu kufikia mijamaa
ikaamua kutoboa dari kumshusha mgonjwa wao pale alipo Yesu Imani yao ikiwa
kubwa sana, mahali popote ambapo watu wanakusanyika kwa wingi hii inamaanisha
pana kitu, watu wanasaidika hapo na hivyo watu hujaa, sana Peto ulifikia wakati
hata muda wa kugusa watu hana watu wakabuni kulaza wagonjwa ili kivuli chake tu
kikipita kiwaguse unaona hii maana yake nini Thamani ya Muhubiri inapanda,
Imani ya muhubiri inakuwa na huduma yako inakuwa Mungu hataruhusu tena uwekee
watu mikono utachoka sasa Mungu ataruhusu hata kivuli chako kisaidie watu
Matendo 5:12-16 “Na
kwa mikono ya mitume zikafanyika ishara na maajabu mengi katika watu; nao wote
walikuwako kwa nia moja katika ukumbi wa Sulemani; na katika wote wengine
hapana hata mmoja aliyethubutu kuambatana nao; ila watu waliwaadhimisha;
walioamini wakazidi kuongezeka kwa Bwana, wengi, wanaume na wanawake; hata
ikawa katika njia kuu hutoa nje wagonjwa, na kuwaweka juu ya majamvi na
magodoro, ili Petro akija, ngawa kivuli chake kimwangukie mmojawapo wao. Nayo
makutano ya watu wa miji iliyoko kandokando ya Yerusalemu wakakutanika,
wakileta wagonjwa, nao walioudhiwa na pepo wachafu; nao wote wakaponywa.”
Kumbuka ni Petro
huyu huyu ambeye sura ya tatu alimsika mtu aliyepooza mikono na kumuombea
asimame kwa jina la Yesu, sasa wahitaji wamekuwa wengi hawezi kugusa watu wote
sasa watu wanahitaji japo kivuli chake tu, umati unasababisha Imani za watu
zikue na huduma yako inakuwa unatoka katika hali ya kuchunga vikondoo vichache
unakwenda kuchunga ranchi, toka kwenye makubazi na fimbo, chunga juu ya farasi
ukiwa na viatu mchingoko na kofia ya kuziia jua Rancher, hiki ndio kiwangi
Mungu anataka ukifikie sijui mnanielewa? Neno
lile ILA WATU WALIWAADHIMISHA katika kiyunani linatumika neno MEGALUNO ambalo
kwa kiingereza ni MAGNIFY Yaani waliwakuza, waliwaona sio watu wa kawaida
waliwahehimu sana, unapoadhimia kuwa na kanisa Kubwa Mungu atafanya mambo
makubwa na wewe atakukuza pia, hali ya heaa ya kiroho kwenye kanisa dogo na
hali ya hewa kwenye kanisa kubwa ni vitu viwili tofauti kama utakuwa umewahi
kuhubiri,
4.
Kanisa
kubwa kazi kubwa – unapokuwa katika kanisa kubwa Utendaji wa Mungu
kimiujiza unakuwa mkubwa na matarajio ya watu kupokea yanakuwa na kazi
inayofanyika inakuwa kubwa, hii
haimaanishi Mungu hafanyi kwenye kanisa dogo anafanya lakini kuna tofauti kubwa
sana, linapokuja swala la watu wengi sana Imani inakuwa kubwa sana , matarajio
ni makubwa sana, nguvu ya Mungu inakuwa kubwa sana miujiza inakuwa mikubwa
sana shuhuda zinakuwa nyingi sana, Mungu
anatukuzwa kikubwa sana, Baraka za Mungu zinakuwa nyingi sana, Michango inakuwa
mingi sana, uchumi unatrahisishwa sana, mtafanya uinjilisti kirahisi sana,
mnaweza kushuhudia nyumba kwa nyumba kwa nyumba nyingi sana, mnaweza kupeleka
chuo cha biblia wachungaji wengi sana,mnaweza kupanda makanisa mengi sana,
mnaweza kuhudumia watu wengi sana, kanuni ya wingi inatumiwa sana na hawa jamaa
wanaokusanya watu wengi, ukifanikiwa kukusanyha watu wengi sana mahali pamoja
Mungu hujitukuzwa kwa kiwango kikubwa sana, hawa watu wenye makusanyiko makubwa
hakuna chochote walichokuzidi isipikuwa watu wengi, nah ii ni kwa sababu
walikuwa na maono hayo, na hawakuridhika, wana matangazo kwenye redio wana
vituo vya televisheni, na kupitia umati walionao wanavutia umati mkubwa sana
angalia @Bishop Dickson Kaganga pale
Zanzibar he is coming, angalia hekima yake, ndugu tunapozungumzia uamsho
natuwezi kuacha kuzungumzia kuwa na makanisa makubwa Maga church Hebu na
tumuamini Mungu sasa kwaajili ya kanisa kubwa, usiridhike tu kwa sababu
jnabadili mboga, una prado, una kigorofa wenzako wana mpaka personal jet Mungu akutoe hapo ulipo wewe na mimi na
tuanze kufikiri mambo makubwa “Attempt Great things for God” alisema Missionary William Carey na
Mungu anapokufanikisheni kiuchumi endelea kuutumia uchumi huo kwa kuendeleza
kazi ya Mungu cha kujilimbikizia mali, hatukuja na kitu duniani wala
hatutaondoka na kitu, tunapowaza kanisa kubwa mwenye kanisa anakuona
anakuchunguza unachowaza kanisa kubwa ni uchumi mkubwa uchumi huu sio wa
Mchungaji ni uchumi wa kazi ya Mungu, tutajali mpaka yatima, tutasomesha yatima
tutajali wajene, tutajali wenye ulemavu tutafanya mambo mengi na mfano mzuri ni
Marehemu @TB Joshua hakuwa na choyo,
Mungu akipombariki taifa zima lilibarikiwa na ulimwengu mzima, Kanisa linaweza kutuma
wamishionari kila mahali na tukawalipa mshahara
5.
Kanisa
kubwa watendakazi wengi – Kanisa inapokuwa kubwa kunakuwa na wafanyakazi
wengi sana wa serikalini na watu wenye ajira, lakini pia wafanya biashara na watu mbali mbali kwa
msingi huo kanisa linakuwa na kipato kikubwa zaidi, uchumi mkubwa katika kanisa
unapelekea kufanikisha kazi nyingi za Mungu, hata hivyo watakuwepo wengine kama
watazamaji, na wengine , lakini mwisho wa siku kundi kubwa la watenda kazi pia
litapatikana watu ambao watayatoa maisha yao pamoja na kazi nyingine kumtumikia
Mungu, hawa ni watu wa maana bila kupuuzia wale wengine umuhmu wao unakuja kuwa
wanaweza kujihusisha na kazi ya Mungu moja kwa moj a na kusaidia ukuaji wa
kanisa zaidi, na Mchungaji kiongozi atakuwa na nafasi kubwa ya kutuma
watendakazi katika shamba la Mungu
Mattayo 9:37-38 “Ndipo
alipowaambia wanafunzi wake, Mavuno ni mengi, lakini watenda kazi ni
wachache.Basi mwombeni Bwana wa mavuno, apeleke watenda kazi katika mavuno yake.”
Wahudumu katika
maeneo mbalimbali ya ukuaji wa kanisa watapatikana, jambo ambalo sio rahisi
kuwapata kwenye kanisa dogo, kumbuka hapa ninapozungumzia kanisa kubwa na dogo
nazungumzia ukubwa kiidadi na namaanisha wingi wa watu, Kanisa litaweza kuwa na
nguvu hata ya kuwahudumia masikini na kusababisha Baraka kubwa sana
Zaburi 41:1-2 “Heri
amkumbukaye mnyonge; Bwana atamwokoa siku ya taabu. Bwana atamlinda na
kumhifadhi hai, Naye atafanikiwa katika nchi; Wala usimtie katika hali
wamtakiayo adui zake. Bwana atamtegemeza alipo mgonjwa kitandani. Katika ugonjwa
wake umemtandikia.”
Kanisa litakuwa
na baraka kubwa kama wataweza kufanya huduma kwa watu wenye mahitaji muhmu na
maalumu, na fedha hazitakuwa tatizo kutokana na wingi wa watu kile kidogo
anachojitoa kila mtu kama mkiwa wengi kinakuwa kitu kikubwa ! wenye vipindi vua
televisheni wataweza kufadhili uwepo wa hewani, na redioni na matangazo ya
injili na kwenye magazeti, na huduma nyinginezo za maedeleo ya kanisa
6.
Kanisa
kubwa mamlaka kubwa - Kanisa kubwa
linakuwa na nguvu kubwa sana katika jamii, na sio hivyo tu linakuwa na mamlaka
kubwa sana na linakuwa taifa lenye nguvu, wanasiasa hupapatikia sana Kanisa
kubwa, mchungaji mwenye kanisa kubwa huwa na mamlaka kubwa na thamani yako
haitaruhusu kugombea uaskofu, zaiti ya kujitiisha katika ushirika wa kanisa
lako na skofu wako huku ukifanya huduma zako, kila Mchungaji akikusudia kuwa na
kanisa mkubwa anakuwa mkubwa katika jumuia ya kanisa lake la mahali pamoja, na
hivyo ni ngumu sana kwa mtu aliye busy kuanza kuwania ngazi za kisiasa za
kanisa namaanisha uongozi wa kikanisa hapa, Serikali huanza kuwa na hofu kwa
kanisa lenye watu wengi, Mchungaji mwenye kanisa kubwa huwa kama serikali,
washirika wenye taaluma mbalimbali hata za usalama wa taifa, ni nadra kumficha
Mchungaji wao kitu, unaweza kualikwa kwenye matukio makubwa sana na hata
kukaribishwa ikulu, Mchungaji mwenye kanisa kubwa la mahali pamoja anakubwa mtu
mkubwa sana, wanasiasa wanajua kuwa kanisa kubwa maana yake ni umati mkubwa wa
watu, maana yake kura nyingi za watu, lakini kikanisa kidogo, kinadharaulika,
wanasiasa wanajua kuwa neno lako na maelekezo yako yanaweza kuwapa kura au
kuwanyima kura na watakuwa wakikujia kusalimu au kwa maombi na kadhalika,
wanasiasa huogopa sana na hawawezi kwa namna yoyote kupuuzia ushawishi wa Mtu
anayeaminiwa kama wewe,
Luka 13:31-33 “Saa
ile ile Mafarisayo kadha wa kadha walimwendea, wakamwambia, Toka hapa, uende
mahali pengine, kwa sababu Herode anataka kukuua. Akawaambia, Nendeni,
mkamwambie yule mbweha, Tazama, leo na kesho natoa pepo na kuponya wagonjwa,
siku ya tatu nakamilika. Pamoja na hayo imenipasa kushika njia yangu leo na
kesho na kesho kutwa; kwa kuwa haimkini nabii aangamie nje ya Yerusalemu.”
Marko 6:17-20 “Kwa
maana Herode mwenyewe alikuwa ametuma watu, akamkamata Yohana, akamfunga
gerezani, kwa ajili ya Herodia, mkewe Filipo ndugu yake, kwa kuwa amemwoa; kwa
sababu Yohana alimwambia Herode, Si halali kwako kuwa na mke wa nduguyo. Naye
yule Herodia akawa akimvizia, akataka kumwua, asipate.Maana Herode alimwogopa
Yohana; akimjua kuwa ni mtu wa haki, mtakatifu, akamlinda; na alipokwisha
kumsikiliza alifadhaika sana; naye alikuwa akimsikiliza kwa furaha.”
Mtumishi wa
Mungu mwenye watu wengi anaogopewa na mfalme na mfalme huwatendea haki na kuwachukualia
kwa uzito mkubwa watu hawa wenye ushawishi mkubwa katika jamii, Yesu hakuwahi
kumuogopa kabisa herode wala Pilato, hali kadhalika Yohana Mbatizaji na
ushawishi wako unajulikana
7.
Kanisa
kubwa jamii kubwa – Kanisa linapokuwa kubwa watu wanakuwa jamii kubwa, ni
rahisi kupata mchumba na kuolewa, makanisa makubwa hufunga ndoa nyingi mpaka
ndoa sitini kwa wakati mmoja, kunapatikana muunganiko wa kupata kazi, na
uhusiano mkubwa na watu wa jamii mbalimbali, mambo mengi duniani yanafanikishwa
na kujuana amini usiamini, watu wanapenda kukaa mahali ambapo wanahisi usalama
Amani na baraka, na mnapokuwa katika kanisa moja na imani moja ni rahisi
kuinuana na kufikia malengo ya kimaisha kwa namna nyepesi sana tunaweza tisiwe
kama kanisa la Kwanza kwa kuuza kila tulicho nacho na kushiriki pamoja, lakini
tunaweza kushirikiana katika maswala ya msingi, ikiwa ni pamoja na ushirika
kikazi, kibiashara, makampuni na kadhalika na kama wakristo hawa wakipata
maelekezo mazuri na malezi mazuri hakuna mtu atajuitia kuajiri wapendwa katika
kampuni yake
Jinsi ya kuwa na kanisa kubwa
1.
Watu
wawe watendaji - Mchungaji yeyote
anayetaka kuwa na kanisa kubwa hatakubali kuwaacha washirika wawe ni watu
wanaoketi na kusikiliza neno kila siku na badala yake atasababisha kazi ya huduma
itendeke, yaani kila mtu ndani ya kanisa awe na jambo la kufanya katika huduma,
au afanye kivitendo, ukuaji wa kiroho wa wakristo hauko katika kuwapatia tu
maarifa lakini maarifa ya namna ya kutumika, hivyo kila mtu ahusike katika
utumishi, kila mtu amtumikie Mungu kivitendo, Yesu hakuwa tu Mwalimu lakini
alikuwa mtendaji, Maandiko yanahamashisha utendaji zaidi ona
Matendo 1:1 “Kitabu
kile cha kwanza nalikiandika, Theofilo, katika habari ya mambo yote aliyoanza
Yesu kufanya na kufundisha,”
Waefeso 4:11-12 “Naye
alitoa wengine kuwa mitume, na wengine kuwa manabii; na wengine kuwa
wainjilisti na wengine kuwa wachungaji na waalimu; kwa kusudi la kuwakamilisha
watakatifu, hata kazi ya huduma itendeke, hata mwili wa Kristo ujengwe;”
Yakobo 1:22-25 “Lakini
iweni watendaji wa neno, wala si wasikiaji tu, hali mkijidanganya nafsi
zenu.Kwa sababu mtu akiwa ni msikiaji wa neno tu, wala si mtendaji, mtu huyo ni
kama mtu anayejiangalia uso wake katika kioo. Maana hujiangalia, kisha huenda
zake, mara akasahau jinsi alivyo. Lakini aliyeitazama sheria kamilifu iliyo ya
uhuru, na kukaa humo, asiwe msikiaji msahaulifu, bali mtendaji wa kazi, huyo
atakuwa heri katika kutenda kwake.”
Neno la Mungu
linasisitiza sana katika kutenda, mwanafunzi halisi wa Yesu sio yule anayesikia
tu ni yule anayetenda, kama watu watajifunza kuomba, kisha hawaombi, au
kushuhudia kisha hawashuhudii, au kufanya umisheni kisha hawaendi, utoaji kisha
hawatoi, ukarimu kisha hawafanyi, Imani bila matendo imekufa, Kanisa lenye
malengo ya kuzaa matunda linapaswa kuwa kanisa la watu wanaolitendea kazi neno
la Mungu, watu wanasikia sana lakini wanaotenda ni wachache, Mungu anapendezwa
na watu wanaotenda. Tukiwa wasikiaji tu na sio watendaji swala la kuwa kanisa
kubwa litasalia kuwa ndoto, mwanafunzi halisi wa Yesu ambaye ana hekima ni yule
anayelitendea kazi neno la Mungu
Mathayo 7:24-27 “Basi
kila asikiaye hayo maneno yangu, na kuyafanya, atafananishwa na mtu mwenye
akili, aliyejenga nyumba yake juu ya mwamba; mvua ikanyesha, mafuriko yakaja,
pepo zikavuma, zikaipiga nyumba ile, isianguke; kwa maana misingi yake imewekwa
juu ya mwamba. Na kila asikiaye hayo maneno yangu asiyafanye, atafananishwa na
mtu mpumbavu, aliyejenga nyumba yake juu ya mchanga; mvua ikanyesha, mafuriko
yakaja, pepo zikavuma, zikaipiga nyumba ile, ikaanguka; nalo anguko lake likawa
kubwa.”
Kanisa ambalo
watu wake wanalitendea kazi neno la Mungu kivitendo, linaweza kutimiza mapenzi
ya Mungu na kufanikiwa sana katika matokeo ya wazi yatakayolipeleka katika
ngazi nyingine ikiwepo kuyatimiza mapenzi ya Mungu na kuwa Kanisa kubwa!
2.
Lisha
kondoo wa Bwana – Wajibu mkubwa wa mtumishi wa Mungu aliyeaminiwa na Bwana
ni kuwalisha kondoo wake Yohana 21:15-17
“Basi walipokwisha kula, Yesu akamwambia Simoni
Petro, Je! Simoni wa Yohana, wewe wanipenda kuliko hawa? Akamwambia , Naam
,Bwana, wewe wajua kuwa nakupenda. Akamwambia, Lisha wana-kondoo wangu.
Akamwambia tena mara ya pili, Simoni wa Yohana, wanipenda? Akamwambia, Ndiyo,
Bwana, wewe wajua kuwa nakupenda. Akamwambia, Chunga kondoo zangu. Akamwambia
mara ya tatu, Simoni wa Yohana, wanipenda? Petro alihuzunika kwa vile
alivyomwambia mara ya tatu, Wanipenda? Akamwambia, Bwana, wewe wajua yote; wewe
umetambua ya kuwa nakupenda. Yesu akamwambia, Lisha kondoo zangu.”
Hutatoa hesabu
kwa programu nyingine zaidi ya Programu ya kulisha kundi na kulichunga kundi,
Mchungaji anayelenga kuwa na kanisa kubwa atahakikisha anatoa muda wake mwingi
kwa kanisa la mahali pamoja, hata kuliko kanisa la kitaifa, watu wengi sana
wanatafuta umaarufu wakifikiri kuwa wanaweza kuwa maarufu kwa kuwa waangalizi,
au maaskofu wa kanda au maaskofu wakuu, kuwa askofu ni wito mwingine mkubwa na
mgumu zaidi, hakuna sababu ya kuwasumbua waangalizi wako, wala maaskofu wako,
wala cheo chochote, wewe lenga tu kuwa na kanisa kubwa, ukiwa na kanisa kubwa
watu wote watakujua Pale Kenya Yuko mtu
mmoja wa Mungu simfahamu sana lakini anajulikana sana kama @Evangelist Ezekiel mtu huyu hajiiti askofu, tena wala hajiiti
mchungaji, anajiita Mwinjilisti Ezekiel, ni maarufu sana huyu mtu, mimi simjui kwa undani sana
lakini nimejikuta namjua sio kwa sababu ni askofu la hasha bali kwa sababu ana
kanisa kubwa, @Joel Osteen kule
Marekani tunamjua sio kwa sababu ni askofu bali kwa sababu ana kanisa kubwa,
ukiwa na kanisa kubwa san ahata askofu wako atakujua unaona, uwe mwaminifu kwa kanisa lako, tii taratibu
za kitaifa na za kikatiba za kanisa lako lakini moyo wako uweke kwenye kukuza
kanisa lako la mahali pamoja na Huduma yako kubwa itakuwa na kuwafikia watu
wengi na hutahitaji kujiita jina kubwa bali, utakuwa maarufu tu kwa sababu Baba
mwenyewe atakuheshimu, waheshimu sana wale unaowahudumia wajali, walishe
wasaidie, wainue wakuze na utabarikiwa sana.
3. Tufanye kazi kwa bidii – Maono ya kuwa
na kanisa kubwa hayawezi kutokea kwa mtu mvivu, lazima kazi kubwa ifanyike ,
viongozi na watumishi wa Mungu wote duniani wanaofanya kazi sana utaweza
kugundua kuwa walikuwa na bidi sana Mchungaji Zachary Tenee aliyekuwa na kanisa
kubwa sana kule Younde Cameroon alikuwa ni mchapa kazi, yeye na washirika wake
walikuwa na bidi, siku aliyokufa Zachary Tenee mkewe alisema maneno haya
kaburini, “Mungu wangu ulinipokonya mume wangu alipokuwa akali hai, wakati wote
alifanya kazi zako na sasa kama haitoshi umeamua kunipokonya kabisa hata
nisimuone” hii maana yake ni nini alikuwa anachapa kazi, maandiko hayaungi
mkono uvivu,
Mithali 12:24 “Mkono
wa mwenye bidii utatawala; Bali mvivu atalipishwa kodi.”
Yeremia 48:10. “Na
alaaniwe mtu afanyaye kazi ya Bwana kwa ulegevu; na alaaniwe auzuiaye upanga
wake usimwage damu.”
Warumi 12:11- “kwa
bidii, si walegevu; mkiwa na juhudi katika roho zenu; mkimtumikia Bwana;”
4.
Maombi
- Kanisa halikui kwa sababu tu ya maono bali kwa mbinu za kibiblia, kuna
mambo mengi ya kimikakati naweza kuyaweka hapa lakini yanaweza yasikusaidie,
napenda sana njia za kibiblia ambazo zikitumiwa zinaweza kuleta matokeo, na
moja ya njia ya ajabu sana ni Maombi, unapoomba Mungu mwenyewe atatoa njia ya kufanya
atakupa na mbinu za kufanya ili kanisa liwe kubwa lakini maombi maombi maombi,
Lazima umuamini Mungu kwaajili ya kanisa kubwa na maombi ni moja ya njia
muhimu.
Isaya 56:5-8. “Nitawapa
hawa nyumbani mwangu, na ndani ya kuta zangu, kumbukumbu na jina, lililo jema
kuliko kuwa na wana na binti; nitawapa jina lidumulo milele, lisilokatiliwa
mbali. Na wageni, walioandamana na Bwana ili wamhudumu, na kulipenda jina la
Bwana, kuwa watumishi wake; kila aishikaye sabato asiivunje, na kulishika sana
agano langu; Nitawaleta hao nao hata mlima wangu mtakatifu, na kuwafurahisha
katika nyumba yangu ya sala; makafara yao na dhabihu zao zitakubaliwa juu ya
madhabahu zangu; kwa maana nyumba yangu itaitwa nyumba ya sala kwa mataifa
yote. Bwana MUNGU, akusanyaye waliofukuzwa katika Israeli asema, Pamoja na hayo
nitamkusanyia na wengine, zaidi ya hao walio wake waliokusanywa.”
Ili Mungu
akukusanyie watu mbalimbali na kuwaleta katika kuta za nyumba yake lazima
nyumba hiyo iwe nyumba ya sala yaani uwekezaji mkubwa uwe ni maombi, maombi
hurahisisha kazi na wakati watu wanaomba Mungu mwenyewe atasema ni namna gani
mnaweza kuifanya kazi yake na atakupa mwelekeo
Matendo 13:1-3 “Na
huko Antiokia katika kanisa lililokuwako palikuwa na manabii na waalimu, nao ni
Barnaba, na Simeoni aitwaye Nigeri, na Lukio Mkirene, na Manaeni aliyekuwa
ndugu wa kunyonya wa mfalme Herode, na Sauli. Basi hawa walipokuwa wakimfanyia
Bwana ibada na kufunga, Roho Mtakatifu akasema, Nitengeeni Barnaba na Sauli kwa
kazi ile niliyowaitia. Ndipo wakiisha kufunga na kuomba, wakaweka mikono yao
juu yao, wakawaacha waende zao.”
Matendo 16:6-10 “Wakapita
katika nchi ya Frigia na Galatia, wakikatazwa na Roho Mtakatifu, wasilihubiri
lile neno katika Asia. Walipofika kukabili Misia wakajaribu kuenda Bithinia,
lakini Roho wa Yesu hakuwapa ruhusa, wakapita Misia wakatelemkia Troa. Paulo
akatokewa na maono usiku; alimwona mtu wa Makedonia amesimama, akimsihi, na
kumwambia, Vuka, uje Makedonia utusaidie. Basi alipokwisha kuyaona yale maono,
mara tukataka kutoka kwenda Makedonia, kwa kuwa tuliona hakika ya kwamba Mungu
ametuita tuwahubiri Habari Njema.”
Nyakati za
kanisa la Kwanza wao waliomba na kumtii Mungu na wakaweka neno la Mungu na
agizo la krist kivitendo, Roho wa Mungu aliwaongoza aliwajulisha wapi pa kwenda
na pale ambapo hakutaka waende aliwakataza, maombi yataleta kila kitu mbinu na
njia za kufanya kwa kadiri ya kutaka kwetu kuyatimiza mapenzi ya Mungu, Kwa hiyo
mchungaji anayetaka kanisa kubwa asipuuzie kamwe swala la maombi.
Na. Rev Innocent
Samuel Kamote
Mkuu wa wajenzi
mwenye Hekima
0718990796