Zaburi 27:1-3. “Bwana ni nuru yangu na wokovu wangu, Nimwogope nani? Bwana ni ngome ya uzima wangu, Nimhofu nani? Watenda mabaya waliponikaribia, Wanile nyama yangu, Watesi wangu na adui zangu, Walijikwaa wakaanguka. Jeshi lijapojipanga kupigana nami, Moyo wangu hautaogopa. Vita vijaponitokea, Hata hapo nitatumaini.”
Utangulizi:
Ni muhimu kufahamu kuwa Neno la
Mungu yaani maandiko matakatifu yanakiri kupitia mwandishi wa zaburi hii ya
kuwa Bwana akiwa nuru na wokovu wetu, haijalishi kuwa maadui zetu na watesi
wetu hata wawe wengi kiasi gani na hata wajipange vipi, watajikwaa na kuanguka,
hii maana yake ni kuwa kumtegemea Mungu kunasababisha tuendelee kubaki wenye
nguvu hata kama kuna mashambulizi makali ya adui kutoka kila kona, Zaburi hii pia
inafunua Nguvu za Mungu ambazo maadui walipaswa kujiuliza kwanza katika mipango
yao kuwa Mungu yuko na nani kabla ya kuanza kujipanga dhidi yetu kwa
mashambulizi yoyote yale, Hakuna mtu mwenye hati miliki ya Mungu ati!
2Samuel 5:17-18 “Na hao Wafilisti
waliposikia kwamba wamemtia Daudi mafuta ili awe mfalme juu ya Israeli,
Wafilisti wote wakapanda kumtafuta Daudi; naye Daudi akapata habari, akashuka
akaenda ngomeni. Basi Wafilisti walikuwa wamekuja na kujitawanya bondeni mwa
Warefai. Basi Daudi akauliza kwa Bwana, akisema, Je! Nipande juu ya Wafilisti?
Utawatia mkononi mwangu? Naye Bwana akamwambia Daudi, Panda; kwa kuwa hakika
nitawatia Wafilisti mikononi mwako.”
Ni makosa makubwa sana kupigana vita,
kupanga maovu, na kumshambulia kumsema vibaya na kumchafua, mtu ambaye hujui
kama ana Mungu au hana, katika vita vya kiroho ni lazima ujue kuwa unayepigana
naye ni mwenye haki au mwovu, kama unayepigana naye Mungu yuko upande wake
utakufa vibaya, utasambaratika, utaporomoka, utafutika na hautakuwepo tena kwa kosa la kipuuzi kama
hilo lisilozingatia kanuni na utendaji wa Mungu! Watakatifu waliotutangulia
Hasa Daudi ambaye alikuwa mtaalamu wa vita alijifunza kuwa Bwana akiwa upande
wako atakusaidia, na wanaokuchukia watashindwa na kusambaratika vibaya,
Historia yao itafifia na watatoweka duniani!
Zaburi 118:6-8 “Bwana yuko upande wangu,
sitaogopa; Mwanadamu atanitenda nini? Bwana yuko upande wangu, msaidizi wangu, Kwa
hiyo nitawaona wanaonichukia wameshindwa. Ni heri kumkimbilia Bwana Kuliko
kuwatumainia wanadamu.”
Leo basi kwa uzito mkubwa tutatafakari pamoja somo hili muhimu lenye kichwa Kujikwaa kwa watesi wangu na adui zangu, ambalo linakazia ushindi wa ajabu unaowapata watu wa Mungu dhidi ya adui zao, na tutajifunza somo hili kwa kuzingatia vipengele vitatu muhimu vifuatavyo:-
·
Maana ya
kujikwaa kwa watesi.
·
Siri ya
kujikwaa kwa watesi wetu na adui zetu.
·
Kujikwaa
kwa watesi wetu na adui zetu!
Maana ya kujikwaa kwa watesi.
Zaburi 27:1-3. “Bwana ni nuru yangu na
wokovu wangu, Nimwogope nani? Bwana ni ngome ya uzima wangu, Nimhofu nani?
Watenda mabaya waliponikaribia, Wanile nyama yangu, Watesi wangu na adui zangu,
Walijikwaa wakaanguka. Jeshi lijapojipanga kupigana nami, Moyo wangu
hautaogopa. Vita vijaponitokea, Hata hapo nitatumaini.”
Ni muhimu kufahamu kuwa neno
linalotumika katika Lugha ya Kiebrania kuelezea watesi ni “Tzoreri” au “Oyevai” ambalo kwa Kiingereza ni enemies au oppressors, au adversaries, Maadui, watesaji, watu
wanaotaka kukusababishia mabaya katika maisha au wanaofurahia wewe upatwe na
mabaya au wanaopanga mipango mibaya juu yako na wenye kutaka kuchafua au
kuharibu kibali ulichonacho hawa ndio
wanaitwa watesi an maadui watu ambao hawakufurahii na wanakupinga hawataki
mafanikio yako au wanaogopa wewe kufanikiwa hawa Bwana ameahidi katika neno
lake kuwa wanapodhamiria kukufanyia mambo yao au hata kama watafanya mambo yao
hatimae watajikwaa
Kujikwaa hasa ni nini? Neno linalotumika kuelezea kujikwaa katika
lugha ya Kiebrania ni “Kāshal” ambalo maana yake ni kudhoofishwa, kupoteza nguvu, kurudishwa
nyuma, kushindwa kusimama, kukutana na kizuizi, kukutana na kikwazo, kukosa
uwiano, kuzimia chini ya shinikizo, kuanguka kwa namna isiyotegemewa kwa
kiingereza “stumble” au “Fall” kwa
hiyo mtu awaye yote anayepambana na watu wa Mungu au mtu wa Mungu anaweza
akaanguka na asiinuke tena, huku sio tu kujikwaa kimwili, lakini ni kuanguka
kwa mfumo mzima wa adui, kusambaratika kwa mipango, na mifumo ya utendaji wa
maadui kupitia nguvu na msaada wa Mungu kwa mtumishi wake.
Zaburi 18:36-40 “Umezifanyizia nafasi hatua
zangu, Na miguu yangu haikuteleza. Nitawafuatia adui zangu na kuwapata, Wala
sitarudi nyuma hata wakomeshwe. Nitawapiga-piga wasiweze kusimama, Wataanguka
chini ya miguu yangu. Nawe hunifunga mshipi wa nguvu kwa vita, Hunitiishia
chini yangu walioniondokea. Naam, adui zangu umewafanya wanipe visogo, Nao
walionichukia nimewakatilia mbali.”
Siri ya kujikwaa kwa watesi wetu na adui zetu
Neno la Mungu linafunua siri
kubwa ni kwa nini maadui hawakufanikiwa, kwanza maadui hawa walikuwa na chuki
kubwa na ya kiwango cha juu, walikuwa wamekusudia kuharibu kabisa au kufutilia
mbali hawa hawakuwa maadui wa kawaida bali watu waliodhamiria mabaya na katika
kudhamiria kwao mabaya walikuwa kama watu wanaokaribia kula nyama kwa uchu hii
ni lugha ya kuonyesha tamaa mbaya ya kusababisha uharibifu mkubwa kwa mtu au
watu wa Mungu. Walikuwa ni watesi waliokusudia mabaya lakini walijikwaa,
Mipango yao iliharibika, uharibifufu uliwapata kwa ghafla, hofu iliwaingia,
akili zao zilipigwa na wakachanganyikiwa, maamuzi yao yaligeuzwa kuwa makosa,
roho zao ziliingia hatiani, dhamiri zao ziliwasuta, ushindi wako mtu wa Mungu
utageuka kuwa ushuhuda kwao, Mwandishi anaeleza kuwa yeye Bwana ni Nuru yake na
wokovu wake, haogopi
Zaburi 27:1-3 “Bwana ni nuru yangu na
wokovu wangu, Nimwogope nani? Bwana ni ngome ya uzima wangu, Nimhofu nani?
Watenda mabaya waliponikaribia, Wanile nyama yangu, Watesi wangu na adui zangu,
Walijikwaa wakaanguka. Jeshi lijapojipanga kupigana nami, Moyo wangu
hautaogopa. Vita vijaponitokea, Hata hapo nitatumaini.”
Mungu anapokuwa upande wako
hakuna anayeweza kusimama kinyume na wewe, adui awaye yote anapokukaribia
anakutana na nguvu za Mungu zisizokuwa za kawaida na bila kujielewa wanaanza
kupoteza mwelekeo, Mungu hakuwahi kuacha watu wake waonewe, kila anayejipanga
kupigana na mtu wa Mungu atashughulikiwa mpaka wajue ya kuwa wewe una Mungu,
kama walidhani wao ndio wana Mungu basi Mungu ataonyesha ni kina nani aliwachagua
kwaajili ya utukufu wake, adui watapata somo kali ambalo watasimuliana kizazi
na kizazi wataelewa ya kuwa kushindana na Mungu ni kujitafutia kifo, ni
kupoteza umaarufu, ni kuangamia na kupotea, ni kujifuta katika ramani ya dunia
Zaburi 103:14-15 “Hakumwacha mtu awaonee,
Hata wafalme aliwakemea kwa ajili yao. Akisema, Msiwaguse masihi wangu, Wala
msiwadhuru nabii zangu.”
Isaya 54:14-17 “Utathibitika katika haki;
utakuwa mbali na kuonewa, kwa maana hutaogopa; na mbali na hofu, kwa maana
haitakukaribia. Tazama, yamkini watakusanyana; lakini si kwa shauri langu. Watu
wo wote watakaokusanyana juu yako wataanguka kwa ajili yako.Tazama, nimemwumba
mhunzi avukutaye moto wa makaa, akatoa silaha kwa kazi yake; nami nimemwumba
mharibu ili aharibu. Kila silaha itakayofanyika juu yako haitafanikiwa na kila
ulimi utakaoinuka juu yako katika hukumu utauhukumu kuwa mkosa. Huu ndio urithi
wa watumishi wa Bwana, na haki yao inayotoka kwangu mimi, asema Bwana.”
1Samuel 2:9-10 “Yeye atailinda miguu ya
watakatifu wake; Bali waovu watanyamazishwa gizani, Maana kwa nguvu hakuna
atakayeshinda; Washindanao na Bwana watapondwa kabisa; Toka mbinguni yeye
atawapigia radi; Bwana ataihukumu miisho ya dunia; Naye atampa mfalme wake
nguvu, Na kuitukuza pembe ya masihi wake.”
Kujikwaa kwa watesi
wangu na adui zangu!
Maandiko yanatuthibitishia ya
kwamba kila mtu anayekukusudia mabaya juu yako au anayekukaribia kwa nia ovu
Mungu atampa kupoteza mwelekeo, wanaopanga mabaya dhidi yako watakosea hatua
zao, wanaotaka kukuangusha au kukupoteza wao ndio watakaopotea, hii ni sheria
ya kiroho kama Mungu yuko upande wako, adui anapokuja na kukushambulia au
kukukaribia ataharibiwa na uwepo wa Mungu, hili sio tukio la bahati mbaya ni
tukio la uhakika, wewe na mimi tutamshukuru Mungu kwaajili ya matendo yake
makuu atakayotutendea na anayoendela kuyafanya akihukumu kwa haki dhidi ya wale
wanaotuchukia, na kujipanga kinyume nasi wao na kila anachojivunia itakuwa
historia
Zaburi 9:1-4 “Nitamshukuru Bwana kwa moyo
wangu wote; Nitayasimulia matendo yako yote ya ajabu;Nitafurahi na
kukushangilia Wewe; Nitaliimbia jina lako, Wewe Uliye juu. Kwa sababu adui
zangu hurudi nyuma; Hujikwaa na kuangamia mbele zako. Kwa maana umenifanyia
hukumu na haki Umeketi kitini pa enzi ukihukumu kwa haki.”
Rev. Innocent Samuel Kamote
Mkuu wa wajenzi mwenye Hekima

Hakuna maoni:
Chapisha Maoni