Waefeso 3:14-17 “Kwa hiyo NAMPIGIA BABA
MAGOTI, ambaye kwa jina lake ubaba wote wa mbinguni na wa duniani unaitwa,
awajalieni, kwa kadiri ya utajiri wa utukufu wake, kufanywa imara kwa nguvu,
kwa kazi ya Roho wake katika utu wa ndani. Kristo akae mioyoni mwenu kwa imani
mkiwa na shina na msingi katika upendo;”
Utangulizi:
Wote tunafahamu kuwa maombi ni
moja ya njia ya muhimu inayotumiwa na watu wengi sana katika kuunganisha
ulimwengu wa roho na mwanadamu, tunaweza kusema kuwa maombi ndio pumzi ya uhai
wa kila anayeamini, maombi yana nguvu, maombi yanaweza kuombwa kwa staili,
mikao na mitindo mbalimbali inayotajwa pia katika maandiko, kwa mfano kufumba
macho, au kufumbua, kusimama au kukaa, kuinua mikono au kukunja, kulala
kifudifudi, au kuketi kimya, kuomba kwa sauti au kimya, laniki pia kuna kuomba
kwa kupiga magoti, hata hivyo pamoja na kuwa mwanadamu anaweza kumuomba Mungu
kwa mitindo mbalimbali leo nataka kuzungumzia swala la kuomba kwa kupiga
magoti, watu wengi wanataka kuomba maombi yenye matokeo, yenye nguvu, lakini
hawajui njia, Neno la Mungu linazungumzia maombi ya kupiga magoti kwa njia na
namna ya kipekee sana kuna nguvu ya ziada wakati mwanadamu anapomuomba Mungu au
kumuabudu Mungu huku akiwa amepiga magoti.
Luka 22:39-43 “Akatoka akaenda mpaka mlima
wa Mizeituni kama ilivyokuwa desturi yake; wanafunzi wake nao wakafuatana naye.
Alipofika mahali pale aliwaambia, Ombeni kwamba msiingie majaribuni. Mwenyewe
akajitenga nao kama kiasi cha kutupa jiwe, AKAPIGA MAGOTI AKAOMBA, akisema, Ee
Baba, ikiwa ni mapenzi yako, uniondolee kikombe hiki; walakini si mapenzi
yangu, bali yako yatendeke. Malaika kutoka mbinguni akamtokea akamtia nguvu.”
Kumbe kuna matokeo katika maombi
ya kupiga magoti,Kwa msingi huo basi leo tutachukua muda kujifunza kwa kina na
mapana na marefu somo hili Nguvu ya kuomba kwa kupiga magoti kwa kuzingatia vipengele
vitatu vifuatavyo:-
·
Maana ya
kupiga magoti kimaandiko.
·
Mifano ya
watu walioomba kwa kupiga magoti.
·
Nguvu ya
kuomba kwa kupiga magoti.
Maana ya kupiga magoti kimaandiko.
Neno kupiga magoti katika lugha
ya Kiebrania linatumika kama neno
“Barak” na kwa Kiyunani linatumika
neno “Gonypeteo” Neno “Barak” la Kiebrania maana yake ni
Kupiga magoti, au kuonyesha unyenyekevu, kuonyesha
heshima au kujishusha mbele ya mtu unayemuheshimu, mtu mkubwa au Mungu, kwa
hiyo kwa ujumla wake kupiga magoti maana yake ni tendo la kuonyesha unyenyekevu
mbele za Mungu, kutambua ukuu wake na
kukubali kuwa wewe na mimi tunamtegemea Mungu, kwa hiyo kupiga magoti ni tendo
linalotakiwa kuanzia moyoni na kujitokeza kwa nje katika jinsi ya mwili, Neno
la Mungu linatoa wito wa kumuabudu kwa kumsujudia na kwa kumpigia magoti Mungu
wetu, Kumbuka imeandikwa utamwabudu na kumsujudia Bwana Mungu wake peke yake!
Zaburi 95:6-7 “Njoni, tuabudu, tusujudu, TUPIGE
MAGOTI MBELE ZA BWANA aliyetuumba. Kwa maana ndiye Mungu wetu, Na sisi tu watu
wa malisho yake, Na kondoo za mkono wake. Ingekuwa heri leo msikie sauti yake!”
Kupiga magoti au goti katika
Lugha ya Kiyunani linatumika neno
“Gonypeteo” ambalo ni muunganiko wa maneno mawili ya kiyunani yaani “Gonu” na “Pipto”. “Gonu” ikiwa na
maana ya Goti na “Pipto” ikiwa na
maana ya anguka au kuanguka kwa kiingereza “fall
on Knee” au “Kneel down” au “Bow the knee” Hili ni tendo la kuonyesha, unyenyekevu na
utii, au kukubali kuwa chini ya maelekezo ya Mungu, ni njia inayotumika katika
maombi hususani nyakati za agano jipya kuonyesha heshima kwa Yesu Kristo,
lakini ni ishara ya kuonyesha kuwa una hitaji la muhimu na zito na linalohitaji
msaada wa haraka au kupewa kipaumbele cha aina yake.
Mathayo 17:14-18 “Nao walipoufikia mkutano,
mtu mmoja akamjia, AKAMPIGIA MAGOTI, akisema, Bwana, umrehemu mwanangu, kwa
kuwa ana kifafa, na kuteswa vibaya; maana mara nyingi huanguka motoni, na mara
nyingi majini. Nikamleta kwa wanafunzi wako, wasiweze kumponya. Yesu akajibu,
akasema, Enyi kizazi kisichoamini, kilichopotoka, nitakaa pamoja nanyi hata
lini? Nitachukuliana nanyi hata lini? Mleteni huku kwangu. Yesu akamkemea pepo,
naye akamtoka; yule kijana akapona tangu saa ile.”
Kupiga magoti ni heshima kubwa na
ni tendo la nje linalotoka moyoni lenye kuonyesha kuwa unakubali kunyenyekea
kwa mwenye mamlaka, Maandiko yanaonyesha na kutabiri kuwa kwa Yesu Kristo
kutokana na mamlaka kubwa sana aliyopewa kila goti la vitu vyote iwe ni
mbinguni au duniani litapigwa kwake kwa sababu ya heshima kubwa aliyotunukiwa
na Mungu Baba yake ona:-
Wafilipi 2:9-11 “Kwa hiyo tena Mungu
alimwadhimisha mno, akamkirimia Jina lile lipitalo kila jina; ILI KWA JINA LA
YESU KILA GOTI LIPIGWE, la vitu vya mbinguni, na vya duniani, na vya chini ya
nchi; na kila ulimi ukiri ya kuwa YESU KRISTO NI BWANA, kwa utukufu wa Mungu
Baba.”
Mifano ya watu walioomba kwa kupiga magoti.
Neno la Mungu limejaa mifano
kadhaa ya watu kadhaa wa kadha ambao waliomba kwa kupiga magoti na kupata
matokeo makubwa sana katika maombi yao, kimsingi kabla ya kuangalia nguvu ya
maombi ya kupiga magoti au umuhimu wa maombi ya kupiga magoti eneo hili
linatuonyesha moja kwa moja matokeo nguvu na umuhimu wa kupiga magoti wakati wa
kuomba.
1.
Yesu
Kristo - Alipokuwa katika wakati
mgumu sana kibinamu wa kukabiliwa na mauti ya msalaba na mateso yaliyojaa dhihaka na kuvunjiwa
heshima kwa kuwa alitambua ni mauti ya aina gani na mateso ya aina gani
yalikuwa yanamkabili, moyo wake na hisia zake zilijawa na maumivu makali ya
kupita kawaida, alikuwa na wakati mgumu alikuwa na wakati wa vita kali ya
kiroho, wakati huu alitumia maombi ya kupiga magoti na mbingu zilimtia nguvu kwani
alitumiwa malaika kutoka mbinguni mara moja ili kumtia nguvu ona!
Luka 22:39-43. “Akatoka
akaenda mpaka mlima wa Mizeituni kama ilivyokuwa desturi yake; wanafunzi wake
nao wakafuatana naye. Alipofika mahali pale aliwaambia, Ombeni kwamba msiingie
majaribuni. Mwenyewe akajitenga nao kama kiasi cha kutupa jiwe, AKAPIGA MAGOTI
AKAOMBA, akisema, Ee Baba, ikiwa ni mapenzi yako, uniondolee kikombe hiki;
walakini si mapenzi yangu, bali yako yatendeke. Malaika kutoka mbinguni
akamtokea akamtia nguvu.”
Ukichunguza kwa
kina tukio hili utagundua ya kuwa maombi ya kupiga magoti yanafaa sana wakati
mwanadamu akiwa katika shinikizo zito na hali ngumu kihisia na mambo ya kutisha
yanapokukabili au unapokuwa na vita kubwa, wakati huo utahitaji kujinyenyekeza
zaidi kwa kupiga magoti lakini pia unaweza kuona matokeo ya kupiga magoti kwani
Malaika wa Bwana kutoka mbinguni alimtokea na kumtia nguvu.
2.
Daniel
– Kulikuwa na mswada mkali wa kiserikali uliopitishwa kukataza watu kuomba
kwa mungu yoyote kwa muda wa mwezi mmoja na mtu ambaye angekiuka swala hilo
angetupwa katika tundu la simba wakali wenye njaa, tunamuona Daniel
hakubadilisha kabisa mfumo wa maisha yake ya maombi na hata katika wakati huu wa sheria kali
kiasi hicho la tishio la maisha na kifo kwa simba wakali aliendelea kuomba kwa
kupiga magoti mara tatu kila siku akiwa mwaminifu kwa Mungu wake na matokeo
yanaonekana simba hawakumuweza, Mungu aliwatuma malaika wake wakayafunga
makanwa ya simba na hawakumdhuru.
Daniel 6:6-11 “Basi
wale mawaziri na maamiri wakakusanyika pamoja mbele ya mfalme, wakamwambia
hivi, Mfalme Dario, uishi milele.
Mawaziri wote wa ufalme, na manaibu, na maamiri, na madiwani, na
maliwali wamefanya shauri pamoja ili kuweka amri ya kifalme; na kupiga
marufuku, ya kwamba mtu ye yote atakayeomba dua kwa Mungu awaye yote, au kwa
mtu awaye yote, katika muda wa siku thelathini, ila kwako, Ee mfalme atatupwa
katika tundu la simba. Sasa, Ee mfalme, piga marufuku, ukatie sahihi maandiko
haya, yasibadilike, kama ilivyo sheria ya Wamedi na Waajemi, isiyoweza
kubadilika. Basi mfalme Dario akayatia sahihi maandiko yale, na ile marufuku.
Hata Danieli, alipojua ya kuwa yale maandiko yamekwisha kutiwa sahihi, akaingia
nyumbani mwake, (na madirisha katika chumba chake yalikuwa yamefunguliwa
kukabili Yerusalemu;) AKAPIGA MAGOTI MARA TATU KILA SIKU, AKASALI, akashukuru
mbele za Mungu wake, kama alivyokuwa akifanya tokea hapo. Basi watu hao
wakakusanyika pamoja, wakamwona Danieli akiomba dua, na kusihi mbele za Mungu
wake.”
Daniel 6:19-24 “Asubuhi
mfalme akaondoka mapema, akaenda kwa haraka mpaka penye lile tundu la simba.
Naye alipolikaribia lile tundu, akamlilia Danieli kwa sauti ya huzuni; mfalme
akanena; akamwambia Danieli, Ee Danieli, mtumishi wa Mungu aliye hai, je! Mungu
wako, unayemtumikia daima, aweza kukuponya na simba hawa? Ndipo Danieli
akamwambia mfalme, Ee mfalme, uishi milele. MUNGU WANGU AMEMTUMA MALAIKA WAKE,
NAYE AMEYAFUMBA MAKANWA YA SIMBA, nao hawakunidhuru; kwa kuwa mbele zake mimi
nalionekana kuwa sina hatia; tena, mbele yako, Ee mfalme, sikukosa neno. Basi
mfalme akafurahi sana, akaamuru wamtoe Danieli katika lile tundu. Ndipo Danieli
akatolewa katika lile tundu, wala dhara lo lote halikuonekana mwilini mwake,
kwa sababu alikuwa anamtumaini Mungu wake. Mfalme akaamuru, nao wakawaleta wale
watu waliomshitaki Danieli, wakawatupa katika tundu la simba, wao, na watoto
wao, na wake zao; na wale simba wakawashinda wakaivunja mifupa yao vipande
vipande, kabla hawajafika chini ya tundu.”
3.
Petro
– Mwanafunzi mmoja aliyekuwa mwema sana nyakati za Kanisa la kwanza huko
Yafa kwa matendo yake mazuri kwa wajane na yatima aliyeitwa Thabita au Dorkas
aliugua na kufa na walipokuwa wamemuosha walimuweka katika chumba na kumuita
Petro, Petro alipokuja moja ya njia aliyoitumia kumuombea marehemu ilikuwa ni
kwa maombi ya kupiga magoti na kwa kweli kwa kutumuia maombi hayo yaliyojaa
unyenyekevu mkubwa maiti (Drkas aliyekuwa amekufa)alifufuka
Matendo 9:36-42 “Na
mwanafunzi mmoja alikuwako Yafa, jina lake Tabitha, tafsiri yake ni Dorkasi
(yaani paa); mwanamke huyu alikuwa amejaa matendo mema na sadaka alizozitoa.
Ikawa siku zile akaugua, akafa; hata walipokwisha kumwosha, wakamweka orofani.
Na kwa kuwa mji wa Lida ulikuwa karibu na Yafa, nao wanafunzi wamesikia ya
kwamba Petro yuko huko, wakatuma watu wawili kwake, kumsihi na kusema, Usikawie
kuja kwetu. Petro akaondoka akafuatana
nao. Alipofika, wakampeleka juu orofani wajane wote wakasimama karibu naye,
wakilia na kumwonyesha zile kanzu na nguo alizozishona Dorkasi wakati ule
alipokuwa pamoja nao. Petro akawatoa nje wote, AKAPIGA MAGOTI, AKAOMBA, kisha
akaelekea yule maiti, akanena, Tabitha, ondoka. Naye akafumbua macho yake, na
alipomwona Petro akajiinua, akaketi. Akampa mkono, akamwinua; hata akiisha
kuwaita wale watakatifu na wajane akamweka mbele yao, hali yu hai. Ikajulikana
katika mji mzima wa Yafa; watu wengi wakamwamini Bwana.”
Ni kama
tunajifunza hapo kuwa maombi ya kupiga magoti yanaweza kusababisha muujiza
mkubwa sana na kuleta nguvu ya ajabu kwani sio tu mtu alifufuka lakini wengi pia
waliosikia habari za tukio hilo katika mji huo na vitongoji vyake walimuamini
Bwana kupitia muujiza ule, Unyenyekevu mkubwa kwa Mungu kwa njia ya kupiga
magoti unaweza kufungua udhihirisho mkubwa sana wa nguvu za Mungu.
4.
Suleimani
– alikuwa ni mfalme mwenye utukufu mkubwa na wa hali ya juu lakini hakuacha
kuonyesha unyenyekevu kwa Mungu wake siku ya kuweka wakfu Hekalu alipiga magoti
na kuomba maombi maalumu sana mbele ya watu wote bila kujali heshima yake na
cheo chake jambo lililopeleka siku ile moto wa Mungu ukashuka na kuteketeza
sadaka ya kutekeketezwa na utukufu wa Mungu ukashuka katika nyumba ya Mungu
siku ile ilipokuwa inawekwa wakfu jambo
lililosababisha makuhani kushindwa kutekeleza majukumu yao
2Nyakati 6:13-17. “(maana
Sulemani alikuwa amefanya mimbari ya shaba, urefu wake mikono mitano, na upana
wake mikono mitano, na kwenda juu kwake mikono mitatu, na kuisimamisha katikati
ya ua; akasimama juu yake, AKAPIGA MAGOTI MBELE YA MKUTANO WOTE WA ISRAELI,
AKAIKUNJUA MIKONO YAKE KUELEKEA MBINGUNI); akasema, Ee Bwana, Mungu wa Israeli,
hakuna Mungu kama wewe, mbinguni, wala duniani; ushikaye maagano na rehema kwa
watumishi wako, waendao mbele zako kwa moyo wao wote; uliyemtimizia mtumishi
wako Daudi, baba yangu, ahadi uliyomwahidi; naam, ulinena kwa kinywa chako,
ukayatimiza kwa mkono wako, kama ilivyo leo. Sasa, Ee Bwana, Mungu wa Israeli,
umfikilizie mtumishi wako Daudi, baba yangu, ahadi uliyomwahidia, ukisema,
Hutakosa kuwa na mtu machoni pangu, wa kuketi katika kiti cha enzi cha Israeli;
wakiwa tu watoto wako wataiangalia njia yao, ili kuiendea torati yangu, kama
wewe ulivyokwenda mbele zangu.Basi sasa, Ee Bwana, Mungu wa Israeli,
ulithibitishe neno lako, ulilomwambia mtumishi wako Daudi.”
2Nyakati 7:1-4. “Basi
Sulemani alipokwisha maombi hayo, moto ukashuka kutoka mbinguni, ukateketeza
sadaka ya kuteketezwa na dhabihu; utukufu wa Bwana ukaijaza nyumba. Wala
makuhani hawakuweza kuingia nyumbani mwa Bwana, kwa kuwa utukufu wa Bwana
umeijaza nyumba ya Bwana. Wakatazama wana wa Israeli wote, uliposhuka ule moto,
utukufu wa Bwana ulipokuwapo juu ya nyumba; wakasujudu kifulifuli hata nchi
sakafuni, wakaabudu, wakamshukuru Bwana, wakisema, Kwa kuwa ni mwema; kwa maana
fadhili zake ni za milele. Ndipo mfalme na watu wote wakatoa dhabihu mbele za
Bwana.”
Ni kama tunajifunza
hapo kuwa kumbe maombi ya unyenyekevu ya kumpigia Mungu magoti yanaweza
kusababisha Mungu kushuka kwa utukufu na uwepo wake katika namna ambayo ni ya
kipekee na ni nani asiyependa kuuona utukufu wa Bwana? Mungu alishuka na Mungu
anaweza kushuka kwa kumpigia magoti
Stephano – Alikuwa anazingirwa na
maadui na walikuwa wamekusudia kumuua baada ya kushindwa kwa hoja kutokana na
ukinzani wa kidini, walimkasirikia sana Stephano, walimsagia meno na wakiwa
wamekusudia kutaka kumuua na akiwa katika mateso na kukabiliwa na hali ya kifo
alipiga magoti, aliwasamehe adui zake alimuona Yesu amesiamama tayari kumpokea
na walipomkazia macho waliona uso wake ni kama wa malaika haya yanamtokea mtu
huyu wa Mungu wa kipekee akiwa amepiga magoti na kumuomba Mungu
Matendo 6:8-15 “Na
Stefano, akijaa neema na uwezo, alikuwa akifanya maajabu na ishara kubwa katika
watu. Lakini baadhi ya watu wa sinagogi lililoitwa sinagogi la Mahuru, na la
Wakirene, na la Waiskanderia, na la wale wa Kilikia na Asia, wakaondoka na
kujadiliana na Stefano; lakini hawakuweza kushindana na hiyo hekima na huyo
Roho aliyesema naye. Hata wakashawishi watu waliosema, Tumemsikia mtu huyu
akinena maneno ya kumtukana Musa na Mungu. Wakawataharakisha watu na wazee na
waandishi, wakamwendea, wakamkamata, wakampeleka mbele ya baraza. Wakasimamisha
mashahidi wa uongo waliosema, Mtu huyu haachi kusema maneno ya kufuru juu ya
mahali hapa patakatifu na juu ya torati; maana tumemsikia akisema kwamba Yesu
huyo Mnazareti atapaharibu mahali hapa, na kuzibadili desturi tulizopewa na
Musa. Watu wote walioketi katika ile baraza wakamkazia macho yao, wakamwona uso
wake kuwa kama uso wa malaika.”
Matendo 7:57-60 “Wakapiga
kelele kwa sauti kuu, wakaziba masikio yao, wakamrukia kwa nia moja, wakamtoa
nje ya mji, wakampiga kwa mawe. Nao mashahidi wakaweka nguo zao miguuni pa
kijana mmoja aliyeitwa Sauli. Wakampiga kwa mawe Stefano, naye akiomba,
akisema, Bwana Yesu, pokea roho yangu. AKAPIGA MAGOTI, AKALIA KWA SAUTI KUU, BWANA,
USIWAHESABIE DHAMBI HII. Akiisha kusema haya akalala. Na Sauli alikuwa akiona
vema kwa kuuawa kwake.”
Paulo – Akiwa katika mafundisho na
mkazo wa kiroho kwa wazee na washirika wa kanisa la Efeso wakati anakamilisha
huduma yake huko hatimaye Paulo na wote waliokuwa wakimsindikiza walipiga
magoti na kumuomba Mungu Neema kwa pamoja
Matendo 20:31-38 “Kwa
hiyo kesheni, mkikumbuka ya kwamba miaka mitatu, usiku na mchana, sikuacha
kumwonya kila mtu kwa machozi. Basi, sasa nawaweka katika mikono ya Mungu, na
kwa neno la neema yake, ambalo laweza kuwajenga na kuwapa urithi pamoja nao
wote waliotakaswa. Sikutamani fedha wala dhahabu, wala mavazi ya mtu. Ninyi
wenyewe mnajua ya kuwa mikono yangu hii imetumika kwa mahitaji yangu na ya wale
waliokuwa pamoja nami. Katika mambo yote nimewaonyesha ya kuwa kwa kushika kazi
hivi imewapasa kuwasaidia wanyonge, na kuyakumbuka maneno ya Bwana Yesu, jinsi
alivyosema mwenyewe, Ni heri kutoa kuliko kupokea. ALIPOKWISHA KUNENA HAYA
AKAPIGA MAGOTI, AKAOMBA PAMOJA NAO WOTE. Wakalia sana wote, wakamwangukia Paulo
shingoni, wakambusu-busu, wakihuzunika zaidi kwa sababu ya neno lile alilosema,
ya kwamba hawatamwona uso tena. Wakamsindikiza hata merikebuni.”
Tunajifunza hapa
kuwa kupiga magoti pia inaweza kuwa ni hali ya kawaida ya maisha ya kila siku
ya kumuomba Mungu kwa wakristo na viongozi wa kanisa, sio tu wakati wa
changamoto lakini kwaajili ya kijiumbia tabia ya unyenyekevu tunaweza kuitumia
njia hii kila wakati na Mungu akajali na kusikiliza dua zetu.
Yakobo Ndugu yake Bwana – Kwa mujibu wa
masimulizi ya tamaduni za nyakati za kanisa la Kwanza inaelezewa kuwa Yakobo
Ndugu yake Bwana alikuwa ni moja ya watu waliokuwa waombaji hodari sana kwa
kupiga magoti, kiasi ambacho alipewa jina la Mtu mwenye magoti ya ngamia, kwa mujibu
wa maelezo ya mwanahistoria wa kanisa wa karne ya pili aliyeitwa Eusebius alinukuu maelezo ya Hegesippus yakieleza kuwa Yakobo ndugu
yake Yesu alikuwa na tabia ya kupiga magoti hekaluni na kuomba kwa muda mrefu
kiasi ambacho magoti yake yalishika sugu kama magoti ya ngamia, aliheshimiwa
sana kwa sababu alisikika akiwaombea watu na kutubia dhambi zao, kwa kupiga
magoti pembezoni mwa hekalu hii ilikuwa ni desturi yake ya maisha mpaka
alipouawa kwa kupigwa mawe ambapo pia alipiga magoti na kuomba Baba uwasamehe,
tunajifunza kwake kuwa kanisa pamoja na maombi mengine wakati mwingine ni vema
kuwa na muda wa unyenyekevu na kukaa magotini kwa muda wa kutosha ili tuweze
kupata rehema kwa Mungu wetu
Nguvu ya kuomba kwa kupiga magoti.
Kupiga magoti kama kutaanza
kutokea ndani yaani moyoni ni moja ya silaha yenye nguvu sana katika maombi,
sisemi kwamba kila anayepiga magoti maombi yake yanaweza kujibiwa, wala sisemi
kuwa maombi ya kupiga magoti ni muhimu kuliko ya iana nyingine lakini nasema kile maandiko yamekionyesha swala
Muhimu hapa ni kuvunjika moyo, ni kunyenyekea, ni kupondeka mbele za Mungu
ishara yake ya nje ndio kupiga magoti, Kuna nguvu ya kusikilizwa na Mungu mtu
anapokwenda mbele za Mungu au wakili wa Mungu kwa kuvunjika au kwa unyenyekevu
ni kama kunahusisha toba, unyenyekevu
ibada na kuvunjiia vunjika mbele za Mungu, ni tendo ambalo likifanyika kuanzia
moyoni linakupatia kibali na linaongezea neema hii ni kwa sababu Mungu
huangalia moyo, kwa kupiga magoti kutoka moyoni unajitengenezea kibali kwa
Mungu na kumfanya Mungu akuhurumie kwa haraka hitaji lako:-
2Wafalme 1:9-14 “Ndipo mfalme akatuma akida
wa askari hamsini pamoja na hamsini wake, wamwendee Eliya. Akamwendea, na
tazama, ameketi juu ya kilima. Akamwambia, Ewe mtu wa Mungu, mfalme asema,
Shuka. Eliya akajibu, akamwambia yule akida wa hamsini, Ikiwa mimi ni mtu wa
Mungu, na ushuke moto kutoka mbinguni, ukuteketeze wewe na hamsini wako. Moto
ukashuka, ukamteketeza, yeye na hamsini wake. Akatuma tena akida wa hamsini
mwingine pamoja na hamsini wake, wamwendee. Akajibu, akamwambia, Ewe mtu wa
Mungu, mfalme asema, Shuka upesi. Eliya akajibu, akamwambia, Ikiwa mimi ni mtu
wa Mungu, na ushuke moto kutoka mbinguni, ukuteketeze wewe na hamsini wako.
Moto wa Mungu ukashuka kutoka mbinguni, ukamteketeza, yeye na hamsini wake.
Tena akatuma akida wa hamsini wa tatu, pamoja na hamsini wake. Yule akida wa
hamsini wa tatu akapanda, AKAENDA AKAPIGA MAGOTI mbele ya Eliya, akamsihi sana,
akamwambia, Ee mtu wa Mungu, nakusihi, roho yangu, na roho za watumishi wako
hawa hamsini, ziwe na thamani machoni pako. Tazama, moto ulishuka kutoka
mbinguni, ukawateketeza wale akida wa hamsini wawili wa kwanza pamoja na
hamsini wao; laiti sasa roho yangu na iwe na thamani machoni pako. Malaika wa
Bwana akamwambia Eliya, Shuka pamoja naye; usimwogope. Akaondoka, akashuka
pamoja naye hata kwa mfalme.”
Akida hawa wa askari wa kikosi
chenye askari 50 wa kwanza na wa pili waliuawa
kwa sababu ya tabia na mwenendo wao wa kutokujali mamlaka ya kiungu,
walimuamuru Nabii ashuke na kumtii mfalme lakini nabii alikuwa anawakilisha
mamlaka ya Mungu, na Mungu aliangalia kutoka moyoni na kuwaona maakida hao kuwa kwa maneno na
vitendo walikuwa hawana adabu, wala moyo
wa unyenyekevu, moyo wa akida wa 3 wa kikosi cha 50 mwengine yeye alikuwa na
unyenyekevu wa hali ya juu sana na kwa sababu hiyo alipata neema kwa hiyo tabia
ya kiburi kutoka moyoni inaweza kusababisha dua yako au yangu isisikilizwe na tabia
ya unyenyekevu na kuvunjika kutoka moyoni huvutia neema ya Mungu, kwa hiyo kupiga
magoti ni lazima kuwe kumetoka moyoni mtu anaweza kupiga magoti kwa nje lakini
kwa nia na lengo la kudhihaki kama askari waliomsulubisha Yesu walivyomfanyia,
walipiga magoti kwa dhihaka na sio kwaajili ya kunyenyekea bali kudhalilisha,
hii ilikuwa ni jeuri ya wazi ya mwanadamu dhidi ya mwana wa Mungu ambaye kila
goti litapigwa kwake
Mathayo 27:27-31 “Ndipo askari wa liwali
wakamchukua Yesu ndani ya Praitorio, wakamkusanyikia kikosi kizima.Wakamvua nguo,
wakamvika vazi jekundu. Wakasokota taji ya miiba, wakaiweka juu ya kichwa
chake, na mwanzi katika mkono wake wa kuume; WAKAPIGA MAGOTI MBELE YAKE,
WAKAMDHIHAKI, wakisema, Salamu, Mfalme wa Wayahudi! Kisha wakamtemea mate,
wakautwaa ule mwanzi, wakampiga-piga kichwani. Walipokwisha kumdhihaki,
wakalivua lile vazi, wakamvika mavazi yake, wakamchukua kumsulibisha.”
Mtu mwenye ukoma aliyechoshwa na
hali ya kukaa na ukoma alimjia Yesu na kumpigia magoti akihitaji rehema za
Mungu na kwa huruma kubwa sana, Yesu alimkubalia ombi lake kwa huruma na
akatakakaswa ukoma kwa mamlaka
Marko 1:40-42 “Akaja kwake mtu mwenye
ukoma, akamsihi na kumpigia magoti, na kumwambia, Ukitaka, waweza kunitakasa.
Naye akamhurumia, akanyosha mkono wake, akamgusa, akamwambia, Nataka, takasika.
Na mara ukoma wake ukamtoka, akatakasika.”
Uko umuhimu wa kumuendea Mungu
kwa heshima na unyenyekevu mkubwa, sisi hatuwezi lolote kwake yeye ni Muumba na
sisis ni viumbe, kuokolewa kwetu kusitufanye sisi kujifikiri kuwa ni wa Muhimu
sana na hata kama tutajifikiri kuwa ni wa Muhimu kwa Mungu wetu bado inatupasa
kutambua kuwa yeye ni Bwana wa Mabwana na kuwa tukimuheshimu naye atatuheshimu,
kupiga magoti ni ishara ya heshima kwa Mungu wetu naye anastahili, wote
waliokwenda Mbele zake kwa unyenyekevu Mungu hakuwahi kuwaangusha na hii ndio
nguvu ya kumuendea tukiwa tumepiga magoti mbele zake kama ishara kutoka moyoni kuwa tunavunjika
mbele zake, tu wanyonge mbele zake hebu kuanzia sasa jaribu kujifunza namna na
jinsi tunavyopaswa kukaa magotini kwake
1Samuel 2:30 “Kwa sababu hiyo, Bwana, Mungu
wa Israeli, asema, Ni kweli, nalisema ya kuwa nyumba yako, na nyumba ya baba
yako itakwenda mbele zangu milele; lakini sasa Bwana asema, Jambo hili na liwe
mbali nami; kwa maana wao wanaoniheshimu nitawaheshimu, na wao wanaonidharau
watahesabiwa kuwa si kitu.”
Isaya 66:2 “Maana mkono wangu ndio
uliofanya hivi vyote, vitu hivi vyote vikapata kutokea, asema Bwana; lakini mtu
huyu ndiye nitakayemwangalia, mtu aliye mnyonge, mwenye roho iliyopondeka,
atetemekaye asikiapo neno langu.”
Na. Rev. Innocent Samuel Kamote
Mkuu wa wajenzi mwenye Hekima

Hakuna maoni:
Chapisha Maoni