Jumapili, 10 Mei 2026

Mimi sina mtu wa kunitia birikani!


Yohana 5:5-8 “Na hapa palikuwa na mtu, ambaye amekuwa hawezi muda wa miaka thelathini na minane.  Yesu alipomwona huyu amelala, naye akijua ya kuwa amekuwa hali hiyo siku nyingi, alimwambia, Wataka kuwa mzima?  Yule mgonjwa akamjibu, Bwana, mimi sina mtu wa kunitia birikani, maji yanapotibuliwa; ila wakati ninapokuja mimi, mtu mwingine hushuka mbele yangu.  Yesu akamwambia, Simama, jitwike godoro lako, uende.”




Utangulizi:

Ni muhimu kufahamu kuwa wakati mwingine hapa duniani mtu anaweza kukwama katika mambo fulani fulani tu kwasababu ya kukosa mtu wa kukusaidia, inawezekana unahitaji matibabu ya tatizo fulani la kiafya na linahitaji fedha nyingi lakini ukakosa mtu, au unatafuta kazi mahali fulani na umehangaika kwa muda mrefu lakini ukaikosa kwa sababu tu huna mtu, wako watu wengi sana wamekwama katika maisha na huduma na mambo mbalimbali kwa sababu tu hawana mtu, usipokuwa na mtu hapa duniani wa kukusaidia wakati mwingine unaweza kujikuta umekwama tu unaweza hata kupitia katika mateso na kuwekewa zengwe kwa sababu huna mtu anayekufahamu.

Kutoka 2:8-10 “Basi akainuka mfalme mpya kutawala Misri, asiyemjua Yusufu. Akawaambia watu wake, Angalieni, watu wa wana wa Israeli ni wengi tena wana nguvu kuliko sisi. Haya! Na tuwatendee kwa akili, wasije wakaongezeka; tena, ikitokea vita, wao nao wasije wakashikamana na adui zetu na kupigana nasi, na kutoka katika nchi hii.”

Wana wa Israel waliteseka sana kule Misri na kugeuzwa kuwa watumwa kwa mateso mazito kwa sababu hakukuwa na mtu aliyewatambua, au asiyetambua mchango wa Yusufu huko nyuma, unapokosa mtu anayekufahamu, anayekujua anayeweza kuwa msaada katika dunia hii ya sasa unaweza kuteseka sana. Katika maandiko ya msingi tunasoma habari za mtu mmoja ambaye jina lake halikuweza kufahamika mara moja, lakini mtu huyu alikuwa amepooza na alikuwa akitarajia kupokea uponyaji kutoka katika kisima kiitwacho Bethzatha mtu huyu amekuwa katika hali hii ya mateso kwa miaka 38 na kwa sababu ya jambo hili alipoteza kila kitu huenda aliishi kwa msaada wa wasamaria wema waliompa chakula lakini haja ya moyo wake haikuweza kutimizwa kwa sababu ilihitaji mtu, na hakukuwa na mtu wa kumjali kwa sababu watu walikuwa na watu wao, unaweza kuteseka kwa miaka mingi sana kwa sababu tu hauna mtu, kuna watu wengi sana wamekwama kwa sababu hawana mtu, jamii haikuoni, marafiki hawahusiki na wewe ndugu hawahusiki na wewe uko peke yako na hakuna wa kukutoa kwa sababu huna mtu! 
        

·         Katika Birika la Bethzatha

·         Mimi sina mtu wa kunitia birikani!

·         Kukosa mtu sio kikwazo kwa Yesu


Katika Birika la Bethzatha

Yohana 5:2-9 “Na huko Yerusalemu penye mlango wa kondoo pana birika, iitwayo kwa Kiebrania Bethzatha, nayo ina matao matano. Ndani ya hayo jamii kubwa ya wagonjwa walikuwa wamelala, vipofu, viwete, nao waliopooza, [wakingoja maji yachemke. Kwa maana kuna wakati ambapo malaika hushuka, akaingia katika ile birika, akayatibua maji. Basi yeye aliyeingia wa kwanza baada ya maji kutibuliwa, akapona ugonjwa wote uliokuwa umempata.] Na hapa palikuwa na mtu, ambaye amekuwa hawezi muda wa miaka thelathini na minane. Yesu alipomwona huyu amelala, naye akijua ya kuwa amekuwa hali hiyo siku nyingi, alimwambia, Wataka kuwa mzima? Yule mgonjwa akamjibu, Bwana, mimi sina mtu wa kunitia birikani, maji yanapotibuliwa; ila wakati ninapokuja mimi, mtu mwingine hushuka mbele yangu. Yesu akamwambia, Simama, jitwike godoro lako, uende. Mara yule mtu akawa mzima, akajitwika godoro lake, akaenda. Nayo ilikuwa ni sabato siku hiyo.”

Katika kisa hiki tunajifunza habari za mtu mmoja aliyekuwa amepooza na kuteseka katika mateso hayo kwa muda wa miaka 38 huku mtu huyu akihitaji uponyaji kabla ya kukutana na Yesu, Neno la Mungu linatueleza kuwa kutokana na haja ya moyo wake kuhitaji uponyaji alipelekwa mahali sahihi kabisa ambapo angeweza kupata uponyaji wake mahali hapo ni katika Birika la Bethzatha, Kimsingi mahali hapo palikuwa ndio mahali sahihi pa kupokea muujiza wake lakini hata hivyo hali yake ilizidi kuwa mbaya na aliendelea kudhoofika siku hadi siku, kimsingi angefia mahali ambapo alitakiwa kupokea uponyaji wake na kinyume chake zaidi aliendelea kusota hapo bila ya msaada kwa nini?

“Bethzatha” lilikuwa  ni jina la Kiyunani la kisima maalumu cha uponyaji ambacho kwa lugha ya Kiebrania na Kiaramu kiliitwa “Bethesda” kimsingi jina hili ni muunganiko wa maneno mawili ya kiebrania Beth na Chesed au Hesed neno Beth ni nyumba House na neno Chesed/Hesed ni Rehema Mercy kwa hiyo yanapounganishwa pamoja maneno hayo unapata neno Bethesda  ambalo maana yake ni nyumba ya rehema (House of Mercy)  hapa palikuwa ni mahali pa ajabu sana kwani kisima hiki kilikuwa jijini Yerusalem katika mlango uitwao Lango la kondoo, kisima hiki kilikuwa na matawi matano ambapo maji ya mvua yalikingwa na kupelekwa katika visima vikubwa viwili hapo kulikuwa na wakati kila siku Malaika wa Bwana alishuka na kuyatibua yale maji na mtu anayekuwa wa kwanza kuingia kwa kuwahi huyu alipokea uponyaji, kwa sababu hiyo wagonjwa wengi sana hususani vipofu, viwete na waliopooza walikusanyika hapo na palikuwa na mashindano makali ya yule atakayefanikiwa kuingia kwanza maji yanapotibuliwa alipona, jambo hili lilipelekea wengine hasa wale waliokuwa dhaifu kusubiria hapo kwa miaka mingi, na kama ulikuwa na mtu basi mtu huyo angelikusaidia kuingia kisimani kwa haraka kabla yaw engine na ungepokea uponyaji na kuondoka zako, sasa hapa alikuweko mtu ambaye amesota kwa miaka 38 na hana mtu wa kumsaidia, kimsingi tunapona kuwa mtu huyu alikuwa mahali sahihi ambapo angepokea uponyaji na angeweza kuhurumiwa lakini kinyume chake mambo hayakuwa hivyo badala ya kupata uponyaji na rehema aliendelea kuteseka, aliendelea kusubiri mtu, mahali hapa pakawa mahali pa ushindani, wenye nguvu walidumbukiza ndugu zao, wasio na nguvu na dhaifu walisubiri na wengine walisubiri miaka wakakata tamaa, ndipo siku hii Yesu alikuja maalumu kwaajili ya mtu huyu!

Yohana 5:6-7 “Yesu alipomwona huyu amelala, naye akijua ya kuwa amekuwa hali hiyo siku nyingi, alimwambia, Wataka kuwa mzima? Yule mgonjwa akamjibu, Bwana, mimi sina mtu wa kunitia birikani, maji yanapotibuliwa; ila wakati ninapokuja mimi, mtu mwingine hushuka mbele yangu.”

Mimi sina mtu wa kunitia birikani!

Tunaona kuwa changamoto kubwa hapa ilikuwa ni mtu, hiki ni kilio cha watu wengi leo wanatamani kufanya mambo fulani ya muhimu katika maisha yao lakini hawana mtu, unatamani kusoma lakini huna mtu wa kukulipia ada, unatamani kupata kazi, Lakini huna mtu wa kukuunganisha, unatamani kuanza huduma lakini huna mtu wa kukusapoti, unatamani kurekodi studio lakini huna mtu, unahitaji kuchapa vitabu vyako lakini huna mtu, unatamani, kuolewa au kuoa lakini hauna mtu, unatamani kufanya biashara lakini huna mtu, unatamani, kupata kiti cha magurudumu lakini hauna mtu, unatamani kwenda shule ya ufundi lakini hauna mtu, unatamani kupata dawa za gharama fulani lakini huna mtu, unatamani kujiendeleza lakini huna mtu, unatamani kujishughulisha na kilimo lakini huna mtu, unatamani kufungua ofisi yako lakini huna mtu, unatamani kuanza biashara lakini huna mtu wa kukupa mtaji, unatamani kulima lakini huna mtu, unatamani kufuga lakini huna mtu, unahitaji kufungua ofisi ya ujuzi ulionao lakini huna mtu, mtu yule aliyepooza alikuwa hana mtu wa kusimama naye, alikuwa hana mtu wa kumuinua, alikuwa hana mtu wa kumuunganisha na fursa iliyokuwa mbele yake, una elimu sahihi kabisa lakini huna mtu, una ujuzi sahihi kabisa lakini huna mtu, umesomea shughuli hiyo lakini huna mtu kwaajili ya haya mtu huyu alikata tamaa, inasikitisha kuwa mtu huyu hakuwa na watu watu walimsahau, watu walimuacha, watu hawakumtafuta watu hawakujishughulisha naye, birikika lilikuwa sahihi, na maji yalikuwa sahihi lakini tatizo lake ilikuwa mtu! Kumbe duniani unaweza ukapata shida kwa sababu huna mtu, unaweza ukasota kwa sababu huna mtu, unaweza ukapoteza muda kwa sababu huna mtu, Yesu aliitambua hali aliyopitia mtu yule na hivyo alikuja moja kwa moja kwa mtu yule tena akijua hali halisi kwamba mtu huyu amekosa huduma kwa sababu hana mtu tena ameteseka muda mrefu amelala pale amepigwa na baridi na ameng’atwa na mbu, Godoro lale limechakaa, amesubiri muda mrefu, mpaka amesahau kuwa anahitaji uzima yeye anaona sababu zake ni watu, unaweza kupita katika hali ngumu sana duniani na wewe ukadhani ni kwa sababu ya watu, nisingelikuwa hivi kama sio mtu, haya yote yamenipata kwa sababu ya watu, watu, mtu, watu, mtu, watu, mtu, watu, mtu, hiki ndio kilio cha watu wengi sana, niko hivi nilivyo leo kwa sababu watu au kwa sababu ya mtu! Nisingelikuwa hivi leo ila ni kwa sababu ya mtu au watu! 

Yohana 5:6-7 “Yesu alipomwona huyu amelala, naye akijua ya kuwa amekuwa hali hiyo siku nyingi, alimwambia, Wataka kuwa mzima? Yule mgonjwa akamjibu, Bwana, mimi sina mtu wa kunitia birikani, maji yanapotibuliwa; ila wakati ninapokuja mimi, mtu mwingine hushuka mbele yangu.”

Kukosa mtu sio kikwazo kwa Yesu

Ni muhimu kuelewa kuwa Yesu alikuja moja kwa moja kwa mtu yule mwenye uhitaji, hatusomi kokote kuwa alitaarifiwa habari zake lakini tunaona kuwa Yesu alikuwa na uelewa kamili, alijua shida ya mtu yule na kwa sababu hiyo alikuja kumsaidia shida yake ilikuwa uzima alikuwa nahitaji uponyaji lakini yeye alikuwa anaona watu, Yesu alimwambia wataka kuwa mzima? Yesu alijua kuwa mtu huyu amekuweko kwenye nyumba ya rehema na wala hakupata rehema, alikuwa karibu na birika, na maji lakini havikuweza kumsaidia, malaika walitibua maji lakini hawakumsaidia mgonjwa kuingia kwenye maji, Yesu alikuja kufanya uhamisho wa mtu yule kutoka hospitalini kwenda nyumbani na kuendelea na shughuli zake, inawezekana unahitaji mtu leo nakujulisha yuko mtu huyu ni Yesu

Yohana 5:6-9 “Yesu alipomwona huyu amelala, naye akijua ya kuwa amekuwa hali hiyo siku nyingi, alimwambia, Wataka kuwa mzima? Yule mgonjwa akamjibu, Bwana, mimi sina mtu wa kunitia birikani, maji yanapotibuliwa; ila wakati ninapokuja mimi, mtu mwingine hushuka mbele yangu. Yesu akamwambia, Simama, jitwike godoro lako, uende. Mara yule mtu akawa mzima, akajitwika godoro lake, akaenda. Nayo ilikuwa ni sabato siku hiyo.”

Kimsingi Yesu anaonyesha kuwa anauwezo wa kuingilia mfumo na kufanya mambo nje ya mfumo, Mungu hafungwi na njia za wanadamu wala njia ulizozizoea, Mungu anaweza kukufanyia jambo hata bila ya msaada wa kibinadamu, Mungu anaweza kufanya jambo peke yake jambo lolote ambalo wanadamu wameshindwa, Mungu haitaji mzunguko, wala hataki kukuchelewesha, Mungu hutenda mambo kwa wakati, Mungu anaweza kugeuza mambo kwa ghafla, dakika moja ya Yesu ni bora kuliko masaa elfu, ya kusubiria mtu, unapokuwa hauna mtu kwa taarifa yako Yesu ndiye anakuwa mtu yule, yeye anachotaka ni wewe kuamka na kuchukua hatua, kukosa msaada sio sababu za Mungu kushindwa kutimiza kusudi lake, Mungu anaposema wewe chukua hatua  yeye anapoona hakuna mtu huchukua hatua yeye mwenyewe

Isaya 59:16 “Akaona ya kuwa hapana mtu, akastaajabu kwa kuwa hapana mwombezi; basi, mkono wake mwenyewe ndio uliomletea wokovu; na haki yake ndiyo iliyomsaidia.”

Zaburi 46:1-3 “Mungu kwetu sisi ni kimbilio na nguvu, Msaada utakaoonekana tele wakati wa mateso. Kwa hiyo hatutaogopa ijapobadilika nchi, Ijapotetemeka milima moyoni mwa bahari. Maji yake yajapovuma na kuumuka, Ijapopepesuka milima kwa kiburi chake.”

Mungu anaweza kufanya yeye mwenyewe bila msaada wa kibinadamu, Mungu anaweza kufungua njia bila connection za wanadamu, wanadamu wanaweza kukusahau, lakini Mungu hawezi kukusahau wala kukuacha, watu wanaweza kukupita lakini Mwokozi hatokupita kamwe, watu wanaweza wasikuone lakini Mungu anakuona, unaweza kukaza macho yako kwa Mungu huko ndiko unakoweza kutoka msaada acha kuwalaumu wanadamu mwangalie Yesu, mwambie Mungu naomba unisimamie wewe mwenyewe, mwambie Mungu naomba muda wangu usipotezwe na watu hata kama nimechelewa wewe ndiye msaada wangu mwambie Bwana njoo moja kwa moja wewe mwenyewe naomba unikwamue hapa nilipo, kwaajili ya watu Eee bwana unipe neema nisiwaangalia bali nikuone wewe na kila ninachikihitaji ee bwana fupisha michakato hii unifanyie njia  katika jina la Yesu Kristo wa Nazareth aliye hai Aamen!   kumbuka Bwana ni mtu wa vita atakupigania katika vita yako

“Roho wa Bwana twakualika utawale, karibu Roho wa Bwana fanya mapenzi ya Bwana”

Rev. Innocent Samuel Kamote

Mkuu wa wajenzi mwenye Hekima

Hakuna maoni: