Yohana 16:7-13 “Lakini mimi nawaambia iliyo kweli; yawafaa ninyi mimi
niondoke, kwa maana mimi nisipoondoka, huyo Msaidizi hatakuja kwenu; bali mimi
nikienda zangu, nitampeleka kwenu. Naye akiisha kuja, huyo atauhakikisha
ulimwengu kwa habari ya dhambi, na haki, na hukumu. Kwa habari ya dhambi, kwa
sababu hawaniamini mimi; kwa habari ya haki, kwa sababu mimi naenda zangu kwa
Baba, wala hamnioni tena; kwa habari ya hukumu, kwa sababu yule mkuu wa
ulimwengu huu amekwisha kuhukumiwa. Hata bado nikali ninayo mengi ya kuwaambia,
lakini hamwezi kuyastahimili hivi sasa. Lakini yeye atakapokuja, huyo Roho wa
kweli, atawaongoza awatie kwenye kweli yote; kwa maana hatanena kwa shauri lake
mwenyewe, lakini yote atakayoyasikia atayanena, na mambo yajayo atawapasha
habari yake.”
Utangulizi:
Ni
muhimu kufahamu kuwa Yesu Kristo alikuwa anazungumza maneno haya mwishoni
kabisa mwa huduma yake akiwa amewaaga wanafunzi wake ya kuwa yeye ameikamilisha
kazi aliyotumwa kuifanya na kuwa anarudi kwa Baba, Yesu alikuwa amewaeleza
wanafunzi wake kuwa atasulubiwa, kufa na kufufuka, na kuikamilisha kazi ya
ukombozi wa mwanadamu, na baada yake nini kingelifuata. Yesu anaonyesha kwa
uwazi umuhimu wa kuja kwa Roho Mtakatifu, hili lilikuwa ni jambo la muhimu sana
kwani lingeondoa hofu ya wanafunzi wake na kuifanya kazi ya Mungu kupanuka kwa
kina zaidi na hivyo kuondoka kwake kulikuwa na faida zaidi kuliko hasara ambayo
wanafunzi wake walikuwa wakiifikiria, Yesu alikuwa anafahamu changamoto ambazo
zingewakabili wanafunzi wake baada yake na hivyo alitaka kuwathibitishia kuwa
uwepo wa Roho Mtakatifu utakuwa na umuhimu zaidi na suluhu kwa hofu yao
Yohana 14:16-17 “Nami nitamwomba Baba, naye atawapa Msaidizi mwingine, ili
akae nanyi hata milele; ndiye Roho wa kweli; ambaye ulimwengu hauwezi kumpokea,
kwa kuwa haumwoni wala haumtambui; bali ninyi mnamtambua, maana anakaa kwenu,
naye atakuwa ndani yenu.”
Kimsingi
Yesu Kristo alilizungumzia swala na ujio wa Roho Mtakatifu kama swala muhimu
sana na hitaji la msingi katika maisha
ya kiroho ya wanafunzi wake na kila
aaminiye baadaye na huduma, Yesu alitaka
wanafunzi wake wawe na uelewa mpana kuhusu umuhimu wa Roho Mtakatifu na
kuonyesha wazi kuwa hatuwezi kwa namna yoyote ile kuishi duniani na kutimiza
kusudi la Mungu bila msaada wa Roho Mtakatifu na nguvu zake mwenyewe, kwa
msingi huo katika msimu huu wa juma la Pentekoste tutachukua muda kutafakari kwa kina na mapana na marefu umuhimu wa Roho Mtakatifu katika
maisha yetu, na kujumuika kwa pamoja katika maombezi ya ubatizo wa Roho
Mtakatifu na hivyo tutajifunza somo hili
“Yawafaa ninyi mimi niondoke” kwa
kuzingatia vipengele vitatu vifuatavyo:
·
Yawafaa ninyi mimi niondoke
·
Kazi za Roho Mtakatifu Duniani
·
Ubatizo wa Roho Mtakatifu
Yawafaa ninyi
mimi niondoke!
Kimsingi
Roho Mtakatifu ametolewa na Mungu Baba yetu ili akae nasi milele na
kuikamilisha ile kazi iliyoanzishwa na Yesu Kristo hapa duniani, Yesu alikuwa
hana budi kuteswa na kufa msalabani kisha kufufuka siku ya tatu na kupaa kwenda
mbinguni mpaka wakati ulioamriwa, Ujio wa Roho Mtakatifu ulikuwa ni wa Muhimu
sana kwa sababu kuweko wa Yesu Duniani katika mwili wa kibinadamu kulimpa
mipaka ya kihuduma na alilazimika kuweko mahali pamoja kwa wakati mmoja lakini
kwa kitendo cha kupaa na kurudi kwa Baba angetoa ruhusa kwa Roho Mtakatifu kuja
na kukaa na sisi daima na kuuleta uwepo
wa Mungu kwa kila mmoja kokote aliko Duniani, Kutokana na umuhimu wa Roho
Mtakatifu, Yesu aliwaagiza wanafunzi wake kutokuianza kazi ya Mungu kwanza
mpaka wamepokea ubatizo wa Roho Mtakatifu ambaye angewageuza, kuwapa nguvu na kuwafanya kuwa mashahidi wake
Matendo 1:4-8 “Hata alipokuwa amekutana nao aliwaagiza wasitoke
Yerusalemu, bali waingoje ahadi ya Baba, ambayo mlisikia habari zake kwangu; ya
kwamba Yohana alibatiza kwa maji, bali ninyi mtabatizwa katika Roho Mtakatifu
baada ya siku hizi chache. Basi walipokutanika, wakamwuliza, wakisema, Je!
Bwana, wakati huu ndipo unapowarudishia Israeli ufalme? Akawaambia, Si kazi
yenu kujua nyakati wala majira, Baba aliyoyaweka katika mamlaka yake mwenyewe.
Lakini mtapokea nguvu, akiisha kuwajilia juu yenu Roho Mtakatifu; nanyi mtakuwa
mashahidi wangu katika Yerusalemu, na katika Uyahudi wote, na Samaria, na hata
mwisho wa nchi.”
Luka 24:46-49 “Akawaambia, Ndivyo ilivyoandikwa, kwamba Kristo atateswa
na kufufuka siku ya tatu; na kwamba mataifa yote watahubiriwa kwa jina lake
habari ya toba na ondoleo la dhambi, kuanza tangu Yerusalemu. Nanyi ndinyi
mashahidi wa mambo haya. Na tazama, nawaletea juu yenu ahadi ya Baba yangu;
lakini kaeni humu mjini, hata mvikwe uwezo utokao juu.”
Wanafunzi
wa Yesu Kristo walikuwa pamoja naye kwa zaidi ya miaka mitatu na nusu,
wakijifunza maarifa elimu na uwezo wa kufanya huduma lakini pamoja na yote haya
Yesu anawaamuru wasitoke kufanya lolote mpaka wapokee ahadi ya Baba, hii
ilikuwa na maana iliyo wazi ya kuwa Elimu, ujuzi na maarifa pekee hautoshi,
uzoefu hautoshi, vipawa vya kibinadamu havitoshi ili tuwe wanafunzi wa Yesu
waliokamilika tunamuhitaji sana Roho Mtakatifu. Uwepo wa Roho Mtakatifu ambaye
haonekani kwa macho katika maisha ya wanafunzi wa Yesu ni wa muhimu zaidi
kuliko uwepo wa Yesu katika hali ya mwili, Roho Mtakatifu asingeliweza kuja
kama Yesu angeendelea kubaki, Kupaa kwa Yesu Kristo, na kutukuzwa kwake
mbinguni kungeruhusu ujio wa Roho Mtakatifu ambaye uwepo wake ungesababisha
uwepo wa Mungu kukaa ndani ya kila mwamini kokote aliko duniani, lakini pia
kazi ya kutukuzwa kwa Yesu Kristo Duniani
ingeanza kupitia Roho Mtakatifu sawasawa na jinsi ambavyo Yesu
ametukuzwa Mbinguni.
Kazi za Roho
Mtakatifu Duniani
-
Roho Mtakatifu ni Msaidizi
mwingine – Yesu
Kristo alikuwa anafahamu kuwa Wanafunzi wake wangekabiliwa na changamoto
kali na kubwa na upinzani mkali wa aina
mbalimbali na wangekata tamaa hasa baada ya kuondoka kwake, Yeye alipokuwa
pamoja nao alikuwa ni mtetezi mkubwa sana wa wanafunzi wake na mashambulizi
yote ya adui yalielekezwa kwake, Kuondoka kwake Yesu Kristo ilikuwa sababu ya huzuni
nyingi sana hofu na mashaka na walikata tamaa, Yesu aliwaahidi kuwa atawaletea
msaidizi mwingine
Yohana
14:16-17 “Nami nitamwomba Baba, naye atawapa
Msaidizi mwingine, ili akae nanyi hata milele; ndiye Roho wa kweli; ambaye
ulimwengu hauwezi kumpokea, kwa kuwa haumwoni wala haumtambui; bali ninyi
mnamtambua, maana anakaa kwenu, naye atakuwa ndani yenu.”
Neno Msaidizi mwingine katika
lugha ya kiyunani (Koine Greek)
linasomeka kama “Paraklētos” ambalo maana yake Msaidizi,
mtetezi, mfariji, mshauri au mtu anayesimama karibu na wewe kwa kusudi la
kukutetea wakili (Advocate) Kazi hii
inafanywa na Roho Mtakatifu kwa kila mtu aliyemuamini hata leo, kwa sababu hiyo
kila mtu aliyeokoka anamuhitaji yeye kama uwepo wa Mungu katika maisha yetu ya
kila siku.
-
Roho Mtakatifu anauwezo wa
kubadilisha maisha
– Wanafunzi wa Yesu Kristo walikuwa wanahitaji mabadiliko makubwa ya maisha
yao, wengine walikuwa waoga, wasiojiamini, wenye ukali, wenye kisasi, wasioweza
kusamehe na walihitaji mabadiliko makubwa sana, Roho Mtakatifu ndiye njia
inayohusika katika mfumo mzima wa kubadili maisha ya mtu na kumfanya afae kwa
kazi ile ambayo Mungu anaihiitahi katika maisha, ni pale tu Roho wa Mungu
anapokuwa juu ya mtu kwa ubatizo ndipo anapoweza kubadilisha maisha ya mtu huyo
na kumfanya afae kwa matumizi ya kazi ya ufalme wa Mungu.
1Samuel
10:5-7 “Baada ya hayo utafika Gibea ya Mungu, hapo
palipo na ngome ya Wafilisti; kisha itakuwa, utakapofika mjini, utakutana na
kundi la manabii wakishuka kutoka mahali pa juu, wenye kinanda, na tari, na
kinubi, na filimbi mbele yao, nao watakuwa wakitabiri; na roho ya Bwana
itakujilia kwa nguvu, nawe utatabiri pamoja nao, nawe utageuzwa kuwa mtu
mwingine. Basi, hapo ishara hizi zitakapokutukia, fanya kama uonavyo vema; kwa
kuwa Mungu yu pamoja nawe.”
Wagalatia
5:16-25 “Basi nasema, Enendeni kwa Roho, wala
hamtazitimiza kamwe tamaa za mwili. Kwa sababu mwili hutamani ukishindana na
Roho, na Roho kushindana na mwili; kwa maana hizi zimepingana, hata hamwezi
kufanya mnayotaka. Lakini mkiongozwa na Roho, hampo chini ya sheria. Basi
matendo ya mwili ni dhahiri, ndiyo haya, uasherati, uchafu, ufisadi, ibada ya
sanamu, uchawi, uadui, ugomvi, wivu, hasira, fitina, faraka, uzushi,husuda,
ulevi, ulafi, na mambo yanayofanana na hayo, katika hayo nawaambia mapema, kama
nilivyokwisha kuwaambia, ya kwamba watu watendao mambo ya jinsi hiyo
hawataurithi ufalme wa Mungu.Lakini tunda la Roho ni upendo, furaha, amani,
uvumilivu, utu wema, fadhili, uaminifu, upole, kiasi; juu ya mambo kama hayo
hakuna sheria. Na hao walio wa Kristo Yesu wameusulibisha mwili pamoja na
mawazo yake mabaya na tamaa zake.Tukiishi kwa Roho, na tuenende kwa Roho.”
Ubatizo wa Roho Mtakatifu
unatubadilisha maisha na kutufanya au kutusaidia kuishi maisha matakatifu siku
hadi siku, kutembea katika Roho Mtakatifu kutayafanya maisha yetu yaachane na
zile hali za mwili na kuruhusu ukomavu na kuzaliwa kwa matunda ya Roho
Mtakatifu katika maisha yetu na kumlingania Yesu.
-
Roho Mtakatifu hutuvika uwezo
au Nguvu kutoka juu
– Kuihubiri injili na kuishi maisha ya ushuhuda kunahitaji nguvu za Mungu,
Mungu anapowatuma watu katika ulimwengu huu anawavika nguvu kwa sababu kuna
nguvu za upinzani ambazo tutakabiliana nazo duniani nguvu hii tunayovikwa na Roho wa Mungu katika lugha ya
kitaalamu ya maandiko ya agano jipya inaitwa “Dunamis” hili ni neno la Kiyunani (Koine Greek) ambalo lina
maanisha uwezo, nguvu za Mungu, Nguvu zenye matokeo na mamlaka, nguvu hii
husaidia waamini kukabiliana na upinzani wa anaina yoyote na kuwa tayari hata
kufa kwaajili ya jina la Bwana na kwaajili ya ufalme wa Mungu, Wale waliokuwa
na hofu na woga waliweza kutiwa nguvu na kuwa majasiri mara baada ya kubatizwa
katika Roho Mtakatifu, tutakuwa na uwezo wa kukabiliana na upinzani wa aina
yoyote na kuwa tayari hata kufa kwaajili ya jina la Bwana kama tutabatizwa kwa
Roho Mtakatifu.
Luka
24:46-49 “Akawaambia, Ndivyo ilivyoandikwa, kwamba Kristo
atateswa na kufufuka siku ya tatu; na kwamba mataifa yote watahubiriwa kwa jina
lake habari ya toba na ondoleo la dhambi, kuanza tangu Yerusalemu. Nanyi ndinyi
mashahidi wa mambo haya. Na tazama, nawaletea juu yenu ahadi ya Baba yangu;
lakini kaeni humu mjini, hata mvikwe uwezo utokao juu.”
Matendo
1:8 “Lakini mtapokea nguvu, akiisha kuwajilia juu
yenu Roho Mtakatifu; nanyi mtakuwa mashahidi wangu katika Yerusalemu, na katika
Uyahudi wote, na Samaria, na hata mwisho wa nchi.”
-
Roho Mtakatifu atatuongoza
katika kweli yote – Kweli
yote ya Mungu haiwezi kueleweka kwa akili za kawaida peke yake, Lakini Roho
Mtakatifu ni Mwalimu, yeye ni mwandishi wa neno la Mungu, ni Mwalimu na anaweza
kutupa ufunuo wa kweli, lakini sio hivyo
tu Roho Mtakatifu atatukumbusha katika maswala yote muhimu na ya msingi katika
mafundisho ya Yesu Kristo, Yeye hufanya kazi ya kutufunulia maswala yote kuhusu
Mungu na mapenzi yake, Katika ulimwengu huu kila mtu anadai anayo kweli lakini
ni kazi ya Roho Mtakatifu ambaye anaitwa Roho wa kweli kuufunua ukweli halisi
sawasawa na ufunuo wa neno la Mungu.
Yohana
14:26 “ Lakini
huyo Msaidizi, huyo Roho Mtakatifu, ambaye Baba atampeleka kwa jina langu,
atawafundisha yote, na kuwakumbusha yote niliyowaambia.”
1Wakorintho
2:10-14 “Lakini Mungu ametufunulia sisi kwa Roho.
Maana Roho Huchunguza yote, hata mafumbo ya Mungu, Maana Ni nani katika
binadamu ayajuaye mambo ya binadamu ila roho ya binadamu iliyo ndani yake?
Vivyo hivyo na mambo ya Mungu hakuna ayafahamuye ila Roho wa Mungu. Lakini sisi
hatukuipokea roho ya dunia, bali Roho atokaye kwa Mungu, makusudi tupate kuyajua
tuliyokirimiwa na Mungu. Nayo twayanena,
si kwa maneno yanayofundishwa kwa hekima ya kibinadamu, bali yanayofundishwa na
Roho, tukiyafasiri mambo ya rohoni kwa maneno ya rohoni. Basi mwanadamu wa
tabia ya asili hayapokei mambo ya Roho wa Mungu; maana kwake huyo ni upuzi,
wala hawezi kuyafahamu, kwa kuwa yatambulikana kwa jinsi ya rohoni.”
-
Roho Mtakatifu humshuhudia Yesu
Kristo – Kumshuhudia
Yesu Kristo katika lugha ya asili ya kiyunani linatumika neno “martureō” ambalo kwa kiingereza ni sawa
na neno “giving evidence”, au “well
report about me”, maana yake ni kuwa Roho Mtakatifu atathibitisha ukweli
kuhusu Yesu Kristo ni nani au ataelezea vizuri kuhusu Yesu Kristo, ana ushahidi
wa kina kuhusu Yesu Kristo, kwa hiyo kama Mwalimu wa kweli atawaelekeza watu
kumjua Yesu Kristo kwa kina zaidi ya
alivyojulikana kwa wakati ule, na anavyoelezewa katika maandiko, atamuinua Yesu
Kristo atathibitisha mafundisho yake kwa hiyo huduma yoyote ya kiroho au
inayoongozwa kiroho haitakuwa na malengo ya kumuinua mtu bali itakuwa inamuinua
Yesu Kristo, huduma yoyote ambayo haimuinui Yesu Kristo inahitaji kupimwa , na
mtumishi yoyote ambaye hamuinui Yesu hatuna budi kumwangalia kwa makini na
nabii yeyote ambaye anajitukuza yeye kuliko Kristo naye ni wa kuangaliwa kwa
makini, ukiona imani yoyote inamuinua yeyote zaidi ya Kristo basi ni imani
yenye mashaka.
Yohana
15:26 “Lakini ajapo huyo Msaidizi,
nitakayewapelekea kutoka kwa Baba, huyo Roho wa kweli atokaye kwa Baba, yeye
atanishuhudia.”
1Wakorintho
12:3 “Kwa hiyo
nawaarifu, ya kwamba hakuna mtu anenaye katika Roho wa Mungu, kusema, Yesu
amelaaniwa; wala hawezi mtu kusema, Yesu ni Bwana, isipokuwa katika Roho
Mtakatifu.”
-
Roho Mtakatifu hutoa nyenzo za
kutendea kazi – Ziko
nyenzo za kutendea kazi ya Mungu ambazo hutolewa na Roho Mtakatifu ni maarufu
sana kama karama za Roho Mtakatifu, hizi husaidia kurahisisha kazi ya Mungu na
kulithibitisha neno na kuufaidia mwili wa Kristo, bila karama na utendaji wa
Roho Mtakatifu kupitia karama hizo maneno yetu yatakuwa ni maneno yasiyo na
uthibitisho au yanaweza kuwa kama hekima tu za wanadamu (Yaani Falsafa) au
maneno ya kushawishi, lakini litakuwa ni neno lenye kuthibitishwa
1Wakorintho
2:4-5 “Na neno langu na kuhubiri kwangu hakukuwa
kwa maneno ya hekima yenye kushawishi akili za watu, bali kwa dalili za Roho na
za nguvu, ili imani yenu isiwe katika hekima ya wanadamu, bali katika nguvu za
Mungu.”
1Wakorintho
12:7-11 “Lakini kila mmoja hupewa ufunuo wa Roho
kwa kufaidiana. Maana mtu mmoja kwa Roho apewa neno la hekima; na mwingine neno
la maarifa, apendavyo Roho yeye yule; mwingine imani katika Roho yeye yule; na
mwingine karama za kuponya katika Roho yule mmoja; na mwingine matendo ya
miujiza; na mwingine unabii; na mwingine kupambanua roho; mwingine aina za
lugha; na mwingine tafsiri za lugha; lakini kazi hizi zote huzitenda Roho huyo
mmoja, yeye yule, akimgawia kila mtu peke yake kama apendavyo yeye.”
-
Roho Mtakatifu ni njia ya
kurahisisha ukomavu wa kiroho – Roho
Mtakatifu anahusika katika kuzaliwa kwetu mara ya pili, lakini pia anahusika
katika kusaidia ukomavu wetu wa kiroho, endapo Mkristo atakomaa kiroho matendo
yote ya mwili yanapukutika na matunda ya kiroho yanaanza kujichomoza katika maisha
ya mwamini, Roho Mtakatifu hatoi karama tu bali anatoa na matunda ambayo
kimsingi hutuumbia tabia kama ya Kristo
Wagalatia
5:22-25 “Lakini tunda la Roho ni upendo, furaha,
amani, uvumilivu, utu wema, fadhili, uaminifu, upole, kiasi; juu ya mambo kama
hayo hakuna sheria. Na hao walio wa Kristo Yesu wameusulibisha mwili pamoja na
mawazo yake mabaya na tamaa zake. Tukiishi kwa Roho, na tuenende kwa Roho.”
-
Roho Mtakatifu hutupa hekima ya
utawala na maamuzi – Ili
dunia iweze kuongozwa vema na maamuzi yaweze kufanyika kwa haki bila upendeleo
wala kuumiza watu tunamuhitaji Roho Mtakatifu ambapo yeye hutoa hofu ya Mungu,
haki, ufahamu, ushauri, uweza na maarifa yatakayosaidia kuujenga ufalme wa
Mungu na kuiongoza dunia katika haki.
Isaya
11:1-5 “Basi litatoka chipukizi katika shina la
Yese, na tawi litakalotoka katika mizizi yake litazaa matunda. Na roho ya Bwana
atakaa juu yake, roho ya hekima na ufahamu, roho ya shauri na uweza, roho ya
maarifa na ya kumcha Bwana; na furaha yake itakuwa katika kumcha Bwana; wala
hatahukumu kwa kuyafuata ayaonayo kwa macho yake, wala hataonya kwa kuyafuata
ayasikiayo kwa masikio yake; bali kwa haki atawahukumu maskini, naye atawaonya
wanyenyekevu wa dunia kwa adili; naye ataipiga dunia kwa fimbo ya kinywa chake,
na kwa pumzi ya midomo yake atawaua wabaya. Na haki itakuwa mshipi wa viuno
vyake, na uaminifu mshipi wa kujifungia.”
Matendo
6:3-4 “Basi ndugu, chagueni watu saba miongoni
mwenu, walioshuhudiwa kuwa wema, wenye kujawa na Roho, na hekima, ili tuwaweke
juu ya jambo hili; na sisi tutadumu katika kuomba na kulihudumia lile Neno.”
-
Roho Mtakatifu hutupa nguvu za
kukabiliana na uchawi – Katika
ulimwengu huu tulio nao ziko nguvu kubwa mbili zinazotawala, nguvu za Mungu na
nguvu za Giza, ili mwanadamu wa kawaida aweze kuwa na nguvu za Mungu zinazoweza
kukabiliana na nguvu za giza ni lazima abatizwe katika Roho Mtakatifu, nguvu za
Mungu kwetu ziko pia kwaajili ya kukabiliaana na nguvu pinzani mfano
Matendo
13:6-12 “Walipokwisha kupita katikati ya kisiwa
chote mpaka Pafo, wakaona mtu mmoja, mchawi, nabii wa uongo, Myahudi jina lake
Bar-Yesu; mtu huyu alikuwa pamoja na liwali Sergio Paulo, mtu mwenye akili.
Yeye liwali akawaita Barnaba na Sauli waje kwake, akataka kulisikia neno la
Mungu. Lakini Elima, yule mchawi (maana ndiyo tafsiri ya jina lake),
akashindana nao, akitaka kumtia yule liwali moyo wa kuiacha ile imani. Lakini
Sauli, ambaye ndiye Paulo, akijaa Roho Mtakatifu, akamkazia macho, akasema, Ewe
mwenye kujaa hila na uovu wote, mwana wa Ibilisi, adui wa haki yote, huachi
kuzipotoa njia za Bwana zilizonyoka? Basi, angalia, mkono wa Bwana u juu yako,
nawe utakuwa kipofu, usilione jua kwa muda. Mara kiwi kikamwangukia na giza,
akazunguka-zunguka na kumtafuta mtu wa kumshika mkono na kumwongoza.Ndipo yule
liwali, alipoyaona yaliyotendeka, akaamini, akiyastaajabia mafundisho ya Bwana.”
2Timotheo
3:8 “Na kama vile Yane na Yambre walivyopingana na
Musa, vivyo hivyo na hawa wanapingana na ile kweli; ni watu walioharibika akili
zao, wamekataliwa kwa mambo ya imani.”
1Wafalme
18 :21-24 “Naye Eliya akawakaribia watu wote, akanena,
Mtasita-sita katikati ya mawazo mawili hata lini? Bwana akiwa ndiye Mungu,
mfuateni; bali ikiwa Baali ni Mungu, haya! Mfuateni yeye. Wale watu hawakumjibu
neno. Ndipo Eliya akawaambia watu, Mimi nimesalia, mimi peke yangu, nabii wa
Bwana; lakini manabii wa Baali ni watu mia nne na hamsini. Kwa hiyo na
watutolee ng'ombe wawili; wao na wajichagulie ng'ombe mmoja, wamkate-kate na
kumweka juu ya kuni, wasitie moto chini; nami nitamtengeza huyo ng'ombe wa
pili, na kumweka juu ya kuni, wala sitatia moto chini. Nanyi ombeni kwa jina la
mungu wenu, nami nitaomba kwa jina la Bwana; na Mungu yule ajibuye kwa moto, na
awe ndiye Mungu. Watu wote wakajibu wakasema, Maneno haya ni mazuri.”
Ubatizo wa Roho
Mtakatifu.
Fahamu
ya kuwa anayebatiza kwa Roho Mtakatifu Ni Bwana Yesu mwenyewe, Na ubatizo huu
ni mpango wa Mungu, ni ahadi ya Mungu kwa waaminio kwa hiyo kila mmoja
anastahili kupokea kwa Imani na kufungua moyo wake kuhakikisha kuwa maisha yake
yanajaa na kufunikwa na uwepo wa Mungu Roho Mtakatifu sawa na neno lake
lisemavyo:-
a. Mathayo
3:11 “Kweli mimi nawabatiza kwa maji kwa ajili ya
toba; bali yeye ajaye nyuma yangu ana nguvu kuliko mimi, wala sistahili hata
kuvichukua viatu vyake; yeye atawabatiza kwa Roho Mtakatifu na kwa moto.”
b. Ubatizo
huu ni ahadi ya Mungu mwenyewe kwa kila mtu amwaminiye
Yoel
2:28 “Hata itakuwa, baada ya hayo, ya kwamba
nitamimina roho yangu juu ya wote wenye mwili; na wana wenu, waume kwa wake,
watatabiri, wazee wenu wataota ndoto, na vijana wenu wataona maono;”
Luka
24:49 “Na tazama, nawaletea juu yenu ahadi ya Baba
yangu; lakini kaeni humu mjini, hata mvikwe uwezo utokao juu.”
Matendo
2:38-39 “Petro akawaambia, Tubuni mkabatizwe kila
mmoja kwa jina lake Yesu Kristo, mpate ondoleo la dhambi zenu, nanyi mtapokea
kipawa cha Roho Mtakatifu. Kwa kuwa ahadi hii ni kwa ajili yenu, na kwa watoto
wenu, na kwa watu wote walio mbali, na kwa wote watakaoitwa na Bwana Mungu wetu
wamjie.”
c. Lazima
uwe na nia ya kutumika – Ubatizo
wa Roho Mtakatifu ni kwaajili ya utumishi, Roho wa Mungu anatabia ya
kutaharakisha watu kwaajili ya utumishi, Pale tunapokuwa tayari kwa huduma na
kukubali kutumika huku na huko Roho Mtakatifu atakuwa radhi nasi, Ubatizo huu
hauwafai watu ambao wakataa tu, unawafaa watu ambao wako tayari kwa kazi kwa
sababu Roho Hatakupa kutulia
Waamuzi
13:24-25 “Basi yule mwanamke akamzaa mtoto
mwanamume akamwita jina lake Samsoni, mtoto huyu akakua, Bwana akambarikia. Roho
ya Bwana ikaanza kumtaharakisha katika Mahane-dani, katikati ya Sora na
Eshtaoli.”
Yeremia
47:6-7 “Ee upanga wa Bwana, Siku ngapi zitapita
kabla hujatulia? Ujitie katika ala yako; Pumzika, utulie. Utawezaje kutulia,
Ikiwa Bwana amekupa agizo? Juu ya Ashkeloni na juu ya pwani, Ndipo alipoyaamuru
hayo.”
d. Kwa
maombi bila kuchoka – Kama
itatokea hujabatizwa katika Roho mtakatifu wakati Fulani huo usiwe mwisho au
mwanzo wa kukata tamaa maandiko yanatutia moyo kuendelea kung’ang’ania mpaka
tumpokee Roho Mtakatifu, aidha huwezi kupokea Roho Nyingine zaidi ya kile
unachokiomba, iko dhana ya watu kufikiri kuwa ukiwekewa mikono wakati wa maombi
utapokea roho Nyingine, Mungu atakupoa sawasawa na kuomba kwako
Luka
18:9-13 “Nami nawaambia, Ombeni, nanyi mtapewa;
tafuteni, nanyi mtaona; bisheni, nanyi mtafunguliwa. Kwa kuwa kila aombaye
hupokea; naye atafutaye huona; naye abishaye atafunguliwa. Maana ni yupi kwenu
aliye baba, ambaye mwanawe akimwomba mkate, atampa jiwe au samaki, badala ya
samaki atampa nyoka? Au akimwomba yai, atampa nge? Basi, ikiwa ninyi mlio waovu
mnajua kuwapa watoto wenu vipawa vyema, je! Baba aliye mbinguni hatazidi sana
kuwapa Roho Mtakatifu hao wamwombao?”
e. Lazima
uwe na imani
Maswala yote ya kiroho
yanapokelewa kwa Imani, wakati wote mtu akiwa na mashaka hawezi kupokea kitu
kutoka kwa Mungu, kwani pasipo Imani haiwezekani kumpendeza Mungu, kwa hiyo Mtu
anayemuhitaji Roho wa Mungu ni lazima aombe kwa Imani,
Waebrania
11:6 “Lakini pasipo imani haiwezekani kumpendeza;
kwa maana mtu amwendeaye Mungu lazima aamini kwamba yeye yuko, na kwamba huwapa
thawabu wale wamtafutao.”
Wagalatia
3:2 “Nataka kujifunza neno hili moja kwenu. Je!
Mlipokea Roho kwa matendo ya sheria, au kwa kusikia kunakotokana na imani? ”
f.
Kuna umuhimu wa kuomba kwa
kupaaza sauti – watu
wanaoomba kimyakimya maombi ya ubatizo wa Roho Mtakatifu ni vigumu sana kujazwa
maandiko yanaonyesha kuwa wale waliobatizwa katika Roho Mtakatifu walikuwa
wakiomba kwa sauti ya kusikika kubwa na ndio maana walijazwa na wakasikika
wakisema kwa lugha nyingine
Zaburi
81:10 “Mimi ndimi Bwana, Mungu wako,
Niliyekupandisha toka nchi ya Misri; Fumbua sana kinywa chako nami nitakijaza.”
Matendo
10:45-46 “Na wale waliotahiriwa, walioamini,
wakashangaa, watu wote waliokuja pamoja na Petro, kwa sababu Mataifa nao
wamemwagiwa kipawa cha Roho Mtakatifu. Kwa maana waliwasikia wakisema kwa
lugha, na kumwadhimisha Mungu. Ndipo Petro akajibu,”
Kwa
hiyo baada ya kujifunza namna hii na kusikia neno la Mungu kuhusu Ubatizo wa
Roho Mtakatifu unapaswa kuamini na kuyatendea kazi yale yote ambayo umeyasikia
na ninakuhakikishia hutakuwa kama ulivyo.
Yesu
alisisitiza juu ya ahadi hii ya ujio wa Roho Mtakatifu kwa sababu
Roho
Mtakatifu ni Msaidizi mwingine, Roho Mtakatifu ana uwezo wa kubadilisha maisha,
Roho Mtakatifu hutuvika uwezo au Nguvu kutoka juu, Roho Mtakatifu atatuongoza
katika kweli yote Roho Mtakatifu humshuhudia Yesu Kristo, Roho Mtakatifu hutoa
nyenzo za kutendea kazi, Roho Mtakatifu ni njia ya kurahisisha ukomavu wa
kiroho, Roho Mtakatifu hutupa hekima ya utawala na maamuzi, Roho Mtakatifu
hutupa nguvu za kukabiliana na uchawi, kuna na mambo mengine mengi sana ambayo
kibinadamu hatuwezi kuyatakeleza bila msaada wa Roho Mtakatifu hivyo ubatizo wa
Roho Mtakatifu unabaki kuwa nyenzo Muhimu sana kwa kanisa tangu jana leo na hata
milele. Uongezewe neema unapochukua majukumu ya kulitendea kazi neno la Mungu
kivitendo, wako katika utumishi.
Na Rev. Innocent
Samuel Kamote
Mkuu wa wajenzi
Mwenye hekima

Hakuna maoni:
Chapisha Maoni