Jumapili, 31 Januari 2016

MTU ANAYEUPENDEZA MOYO WA MUNGU:


1Samuel 13:13-14 Biblia inasema hivi “Naye Samweli akamwambia Sauli, Umefanya upumbavu; hukuishika amri ya Bwana, Mungu wako, aliyokuamuru; kwa maana Bwana angaliufanya ufalme wako kuwa imara juu ya Israeli milele.  Lakini sasa ufalme wako hautadumu; BWANA AMEJITAFUTIA MTU AUPENDEZAYE MOYO WAKE, naye Bwana amemwamuru yeye kuwa mkuu juu ya watu wake, kwa sababu wewe hukulishika  Neno lile Bwana alilokuamuru” 

Daudi alikuwa Mtu aliyeupendeaza Moyo wa Mungu



Paulo Mtume alipohubiri kule Antiokia katika mahubiri yake aligusia kwa ufupi Historia ya Isarael na kugusa kile ambacho Mungu alikisema kuhusu Daudi Matendo 13:22 “ ….ambaye alimshuhudia akisema, Nimemwona Daudi mwana wa Yese, MTU ANAYEUPENDEZA MOYO WANGU,”
Kila mmoja wetu anagefurahi kuitwa na Mungu “MTU ANAYEUPENDEZA MOYO WANGU”  kila mkristo anapaswa kuhakikisha kuwa anaupendeza moyo wa Mungu, Yesu aliishi maisha ya ya kumpendeza Mungu kiasi ambacho wakati akibatizwa Mungu alisema “HUYU NDIYE MWANANGU MPENDWA NINAYEPENDEZWA NAYE” hii ni sifa kubwa mbele za Mungu Hususani katika ulimwengu huu wa sasa.

Hata hivyo ili sisi nasi tuweze kumpendeza Mungu na Mungu kuvutiwa nasi kama ilivyokuwa kwa Daudi  ni muhimu kwetu kutafakari kwa vipi Daudi aliupendeza moyo wa Mungu au kujiuliza Daudi alikuwa mtu wa namna gani kiasi cha kufikia kuitwa mtu aliyeupendeza Moyo wa Mungu, ili sisi nasi tuweze kufuata nyayo zake:  Yako mambo kadhaa ya kujifunza kutoka kwa Daudi
1.       Alilipenda Neno la Mungu
a.       Aliipenda sheria ya Mungu Zaburi 119:97 (Sheria ya Mungu ni Neno lake)
b.      Aliliweka moyoni neno la Mungu ili asitende dhambi Zaburi 119:11(Alilifanya kuwa Muongozo wake)
c.       Neno la Mungu lilikuwa ndio faraja yake wakati wa Mateso Zaburi 119:50 (kila tatizo alilisuluhisha kwa kuutafuta Uso wa Mungu)
d.      Neno la Mungu lilikuwa ndio chimbuko la amani ndani yake  Zaburi 119:165
Je wewe unaliweka neno la Mungu moyoni, unalisoma, unalipenda unaliishi unalitafakari? Ni muhimu kulifanya Neno la Mungu kuwa kinga yetu na dawa yetu kwa kila tatizo hata ikiwemo dhambi.
2.       Alipenda kuomba (Maombi)
a.       Alisema nitaliitia jina la Bwana maadamu ninaishi Zaburi 116:1-2
b.      Alitambua kuwa Mungu amembariki na atambariki sana Zaburi 116:12-13
c.       Alitambua kuwa maombi yanamuweka Mungu karibu naye Zaburi 145:18
d.      Yesu pia alikuwa mwombaji Luka 5:16
Je ni kiasi gani tunapenda maombi, je tunaomba bila kukoma kama yanenavyo maandiko je tunajilinda katika maombi?
3.       Alipenda Kumsifu Mungu
a.       Alimsifu Mungu kwa sababu ya haki yake Zaburi 119:164
b.      Alimpenda Mungu kwa sababu ya ukuu wake na wema wake Zaburi 95:1-7
c.       Aliamua kuwa atamsifu Mungu maadamu anaishi Zaburi 104:33
d.      Yesu alipenda kuimba na kumsifu Mungu Mathayo 11:25-26 na 26:30
Je ni kiasi gani unapenda kusifu na kuabudu ni kiasi gani unajishughulisha na kuimba na kusifu na kuabudu?
4.       Daudi alipenda Umoja miongoni mwa watu wa Mungu
a.       Alipenda ndugu wakae kwa umoja aliona inapendeza Zaburi 133:1
b.      Alikuwa na ushirika wa karibu sana na Jonathan 1Samuel 18:1
c.       Alitambua pia uchungu wa migawanyiko katika familia 2Samuel 13
d.      Yesu pia alipenda umoja alituombea tuwe na umoja Yohana 17:20-23 Alikufa msalabani  ili tuwe wamoja Efeso 2:13-16
Je wewe unapenda umoja, unawafanya watu kuwa kitu kimoja au unapendelea watu na kuuvunjavunja mwili wa Kristo? Wako watu wengine leo wanafurahia wengine kupatwa na mabaya, kutengwa na kuwa mbali nao na kuuharibu mwili wa Kristo
5.       Daudi hakupendezwa na njia za uongo
a.       Alichukia uwongo akiwa na ujuzi wa kutosha kuhusu mtazamo wa Mungu Zaburi 119:104
b.      Chuki yake dhidi uongo iliathiri shughuli za uchaguzi wa Marafiki na shughuli zake Zaburi 101:3-4,6-7.
Yesu alichukizwa na uongo na njia zisizo sahii za mafarisayo
Je wewe unachukia njia za udhalimu? Upendo haufurahii udhalimu, ni muhimu kwako kuukemea udhalimu kwa Upendo, bila kumsahmbulia mtu, bali kuishambulia tabia isiyofaa
Biblia inaeleza kuwa Daudi ndiye awezaye kufanya mapenzi ya Mungu yote, Mtu atakayefanya mapenzi yangu yote, alikuwa tayari kufanya yote aliyomuamuru Mungu. Moyo wa Daudi ulikuwa tayari kutimiza kusudi lote la Mungu alilolikusudia. Ni muhimu kuishi Duniani kwa kulitimiza kusudi lote lile ambalo kwalo Mungu ametukusudia

Mkuu wa wajenzi mwenye Hikima
Rev. Innocent Kamote.

SOMO: JINSI MUNGU ANAVYOCHAGUA VIONGOZI



Mstari wa Msingi: 1Samuel 16:7 “Lakini Bwana akamwambia Samuel, Usimtazame uso wake wala urefu wa kimo chake ; kwa maana mimi nimemkataa. Bwana haangaliikama binadamu aangaliavyo; Maana wanadamu huitazama sura ya nje, bali bwana huutazama moyo”

      Mfalme Daudi alipatikana kwa Mapenzi ya Mungu na sui kwa shinikizo la Wanadamu
 
Utangulizi:
Hivi Karibuni Nchi yetu itakuwa na uchaguzi mkuu wa Rais, wabunge na madiwani, na kwa upande wa uchaguzi wa Rais ni wazi kuwa nafasi hii inahitaji Rais mpya kwa mujibu wa utaratibu tuliojiwekea, ni wazi kuwa kwa Tanzania, Marais hutokana na vyama vya kisiasa na hivyo vyanzi vinavyoweza kuleta Rais ni vyama vya siasa, na iko wazi kuwa kuna vyama vya siasa kama CCM, CUF, NCCR, CHADEMA, UDP, DP, ADC, na kadhalika, wote tunakubali kuwa moja ya chanzo kikubwa kinachoweze kutupatia viongozi katika Tifa hili ni CCM, hili halina ubishi kutokana na mfumo mzima ulivyo kwa taifa hili, ingawa inaweza kutokea tofauti wakati mwinginine lakini kwa Tanzania sio sasa

Katika wakati huu wa uchaguzi kuna mambo mengi ya kujifunza, au ambayo tunaweza kuwa wote tumejifunza na ni dhambi kuyakalia kimya bila kuyatafakari, vinginevyo Historia itatuhukumu!

Katika chaguzi za nyuma zilizopita, vituko kadhaa vilivyopata kushuhudiwa ilikuwa ni pamoja na kutabiriwa kumwagika kwa Damu, tetesi za vita, maonyo dhidi ya taifa, na pia baadhi ya watu kutabiri kuwa Fulani ndio chaguo la Mungu n.k.

Uchaguzi wa mwaka huu pia kupitia ndani ya mchakato wa CCM wengi wetu, tuliona na kushuhudia watu walionyesha wazi kuwa ni nani amechaguliwa na Mungu kuiongoza Tanzania kupitia CCM, watumishi wa Mungu, wachawi, wanajimu na Mashehe kila mmoja alikuwa na majibu kuwa ni nani anafaa kuwa kiongozi wa Taifa hili wakati Kikwete akiondoka Madarakani
Neno la Mungu lina majibu ya kutosha kuondoa utata huo uliojitokeza, kwa kurudia Historia ambayo watanzania lazima tuikumbuke kila wakati na kujifunza kutoka katika Neno lake namna na jinsi MUngu anavyojipatia viongozi.

Biblia imejaa Mifano mingi jinsi Mungu alivyojipatia viongozi wa aina mbalimbali wengi wao wakiwa ni hodari, viongozi hao wanaume kwa wanawake, wafalme, waamuzi, makuhani, manabii na Mitume Je Mungu aliwapataje viongozi hao ni mfumo gani Mungu aliutumia kupata viongozi? Njia hii ya Mungu kujipatia viongozi ikitumika katika taifa letu tutaona viongozi wazuri na watakaotimiza mengi makubwa katika Taifa letu wakiendelea kupatikana

Jinsi Mungu anavyochagua viongozi
Katika Mstari wetu wa msingi pale juu tunaona kuwa Daudi ni moja ya mfano wa viongozi waliopata kuiongoza Israel na kuiletea heshima kubwa sana, aliongoza Israel kwa miaka 40, Isamuel 16. Israel walikuwa chini ya utawala wa Saul ambaye sasa alikuwa anafikia ukingoni, Na Mungu anamtuma Nabii Samuel katika Familia ya Yesse akimueleza wazi kuwa amejipatia mfalme katika wanawe ! 1Samuel 16:1. Hakuna mtu alimjua si Samuel wala hata Yese mwenyewe ambaye alikuwa ndio chanzo kikuu cha kumleta mfalme!
Kumbuka kuwa hakukuwa na uteuzi wa kiofisi, hakukuwa na Kampeni, wala mijadala wala kujitangaza kwa mbwembwe, wala kwa kueleza sera mipango na mikakati au nini wataufanyia utawala wa Israel, Bali Mungu mwenyewe aliangalia na kuchagua ni nani atakuwa mrithi wa Sauli, sio hivyo tu lakini hebu chunguza njia ambayo Mungu anaitumia kumpata kiongozi ambaye ni chagua lake!
Wakati Samuel anafika nyumbani kwa Yese, Yese ambaye ni chanzo kikuu cha kutoa kiongozi anawaleta mbele ya nabii wanae wote wakubwa akiwa na furaha sana, Kumbuka kuwa hata Samuel hakuwa anajua kuwa ni nani atakuwa mfalme licha ya kuwa Nabii mkubwa na mwenye uzoefu na ujuzi kuhusu sauti ya Mungu Mungu alimwambia wazi “USIMTAZAME USO WAKE,WALA UREFU WA KIMO CHAKE, KWA MAANA MIMI NIMEMKATAA” Ni maneno magumu sana haya kutoka kwa Mungu hasa kama yanaelekezwa kwako kukataliwa Mh? Ni kama ukatili Fulani hivi lakini Mungu yuko kazini tena makini kuhakikisha kiongozi bora anapatikana, kwa sababu yeye haangalii mbwembwe za nje anaangalia Moyo!

Ni wazi kuwa wana wote wa Yese waliopitishwa kwa Samuel Mungu aliwakataa Mstari 8-10 Mungu anauwezo wa kuchunguza moyo Ayubu 34:21, Waebrania 4:13, 1Yohana 3:10.  Mungu ana namna yake ya kuangalia mambo katika namna iliyo njema kabisa nay a kiungu, na hivyo wana wote wa Yese waliopitishwa hawakuwa wanafaa kwa kwa nafasi ya Ufalme, Mwisho Yese alimuita mwanae mdogo Daudi ambaye hakuna hata mmoja alidhania kuwa angefaa hata kuletwa mbele ya Samuel

Hakika Mungu huchagua viongozi katika namna tofauti kabisa na sifa na mitazamo ya kibinadamu
Kila mahali katika Biblia tunaweza kuona mifano hii ya jinsi Mungu alivyojipatia viongozi, Musa aliyekuwa na miaka 80 akichunga kondoo wa mkwewe jangwani, Malaika wa Bwana alimtokea na kumuagiza awaongoze Israel kutoka Misri Kutoka 3. Elisha alikuwa akilima kwa ngo’mbe kwa jozi 12 na Eliyanabii alipita na kumtupia vazi kama ishara ya kuwa mrithi wake (1Wafalme 19:15-21) kumbuka kuwa Eliya aliambiwa watu ambao alipaswa kuwatia mafuta ambao Mungu alikuwa amewachagua, wakiwemo wafalme wa Israel na Syria 

Katika agano jipya mitume walichagua mtume mwingine ili kujaza nafasi ya Yuda aliyemsaliti Yesu, kwa kura lakini waliomba Mungu awaonyeshe ni nani aliyemchagua kati ya wawili waliopendekezwa Matendo 1:24-25 waliomba Mungu anayejua mioyo ya watu awaonyeshe. Hilo ni la Muhimu sana!

Mungu pia aliamua kumchagua mtu mwingine aliyeitwa Sauli ili awe Mtume yeye mwenyewe Matendo 9 Sauli yaani Paulo alitambua mara moja kuwa alikuwa akiwatesa watu wa Mungu, aliokoka na kubatizwa na akawa mtume mkubwa sana ilileta mashaka sana kwa watu wa kanisa wakati huo lakini kumbuka maneno haya Matendo 9:15 “ Lakini Bwana akamwambia  Nenda tu kwa maana huyu ni chombo kiteule kwangu alichukue jina langu mbele ya mataifa , na wafalme na wana wa Israel”

Mtu anaweza kudai kuwa hawa walikuwa viongozi wa kiroho, na labda Mungu hajihusishi na uchaguzi wa viongozi wa kisiasa na wakuu wa serikali kwa nnjia hizo! Jibu ni Hapana Mungu pia hujihusisha kuchagua viongozi wa kisiasa kama tulivyoona kuhusu mfalme wa Israel na Syria pale juu Biblia iko wazi kabisa kuwa aliye juu ndiye anayetawala katika falme za wanadamu Daniel 4:17 “hukumu hii imekuja kwa agizo la walinzi, na amrihii kwa neno la watakatifu: kusudi walio hai wapate kujua ya kuwa Aliyejuu anatawala katika ufalme wa wanadamu naye humpa amtakaye tena humtawaza juu yake aliye  myonge (myenyekevu)”

Hata inapotokea kuwa wanadamu wanalazimisha kiongozi wa aina wanayemtaka Bado Mungu huchagua yeye mwenyewe lakini mabaya yatakayowapata yatakuwa ni matokeo ya kutaka kwenu, Mungu aliwafanyia Israel walipotaka ufalme kama mataifa mengine kinyume na Samuel 1Samuel 10:23-24 Mungu akiruhusu wanadamu wakajichagulia atakuacha upate somo kuwa uchaguzi wa mwanadamu ni wa kipuuzi na tutaumia! 1Samuel 9: 15-17
Ni muhimu kufahamu kuwa Mungu anapochagua wala haiitajiki kampeni wala uchaguzi kwa vile sio DEMOCRACY lakini ni THEOCRASY yaani sio Mfumo ambao watu wengi au wote wanapata nafasi ya kuchagua MKUMBO bali ni mfumo ambao Mungu anaibua kiongozi kwa jicho lake kutoka kusikotarajiwa, uchaguzi wa Mungu hautokei chini kwenda juu bali juu kuja chini, HIVYO SAUTI YA WENGI SIO SAUTI YA MUNGU! Nakazia tena  SAUTI YA WENGI SIO SAUTI YA MUNGU mwisho wa kujinukuu.

Kampeni na uchaguzi wa kupiga kura uko kwaajili ya kuendeleza tabia ya kiongozi na kutekeleza mapenzi ya Mungu, lakini ukweli Mungu anapochagua huitaji kuwashawishi wanadamu kwa namna yoyote wala kwa sera na mipango utakayoifanya Mungu anawaweka katika ofisi na watu wanatakiwa kumfuata.

JINSI GANI VIONGOZI WANAWEZA KUFANIKIWA?
Hili ni swali muhimu Je kila kiongozi anayetokana na Mungu anaweza kufanya vizuri jibu ni ndio ikiwa wataendelea kumfuata Mungu na maagizo yake “Yoshua 1:5-9, 1Wafalme 1:1-3” Hata baada ya kufa kwake Daudi ingawa aliwahi kufanya dhambi katika maisha yake anasifiwa na Mungu kama mtu aliyeupendeza Moyo wa Mungu Matendo 13:22, Musa pamoja na makubwa aliyoyafanya na madhaifu aliyokuwa nayo anatajwa kuwa mtu mnyenyekevu zaidi kuliko wote waliokuwa juu ya uso wa duni Hesabu 12:3, Mungu hutuchagulia viongozi wazuri wenye kuleta ufanisi mkubwa, wenye moyo na uzalendo atakaowatumia kwa namna ya kupita kawaida na kuleta mafanikio makubwa ambayo kila mtu anayataka na watu hupata faraja kubwa na kufurahi
Mithali 29:2 “ wenye haki wakiwa na amri watu hufurahi bali mwovu atawalapo watu huugua”
Je ungependa nani akuchagulie kiongozi ? Mungu huchagua viongozi

Kumbuka.
·         Kiongozi anayetoka kwa Mungu ni vigumu kumtambua mpaka Mungu amfichue, Samuel alikuwa nabii mkubwa lakini ilikuwa ngumu kwake kujua Mungu anamtaka yupi katika shina la Yese
·         Tuwasamehe viongozi wote wa dini waliotabiri na kutamka kuwa mtu Fulani ni chagua la Mungu na wengine Fulani asipokuwa Raisi mniue kwa vile hao ni wanadamu na huenda hawajui Mungu anajipatiaje viongozi
·         Tuwasamehe watabiri na wanajimu kwa vile inawezekana uwezo wao wa kuona uliishia kwenye nyumba ya Yese yaani walitabiri wale walioishia kwenye tano bora ua wengine waliokatwa mapema tuwasamehe kwa vile ni wanadamu na hawajui mapenzi ya Mungu

·         Tuache kujivuna na kujifikiri kuwa sisi ni watu maalumu tunayoweza kuyajua mapenzi kamili ya Mungu aidha tuache kwenda kwa Mkumbo kwa vile Mungu hachukuliwi na umati wa watu
·         Acha kuwaombea na kuwalilia wale ambao Mungu amewakataa Mungu hutazama Moyo, wajibu wetu siku zote ni kumuomba Mungu atuonyeshe ni nani aliye katika mapenzi yake na kujiandikisha na kwenda kupiga kura ya kumkubali Yule ambaye Mungu amemchagua, Niliwahi kusema katika mahubiri yangu kuwa Yule ambaye anatoka kwa Mungu atakuwa ni Yule ambaye wanadamu hawakumtarajia wala kumfikiria.
Haya ndio niliyojifunza katika mchakato mzima wa kupatikana kwa wagombea Urais katika Taifa letu na huku tukiyaangalia mapenzi ya Mungu Mungu ibariki Afrika Mungu ibariki Tanzania

Mkuu wa wajenzi Mwenye Hekima
Rev. Innocent Kamote.

UJUMBE: KWAAJILI YA HAYA NALIZALIWA!


Mstari wa Msingi Yohana 18:37.

Biblia inasema hivi katika Mstari huo “37. Basi Pilato akamwambia, Wewe u mfalme basi? Yesu akajibu, Wewe wasema, kwa kuwa mimi ni mfalme. MIMI NIMEZALIWA KWA AJILI YA HAYA, na kwa ajili ya haya mimi nalikuja ulimwenguni, ili niishuhudie kweli. Kila aliye wa hiyo kweli hunisikia sauti yangu. 38. Pilato akamwambia, Kweli ni nini?”


Kila mtu duniani anapaswa kuwa na ufahamu wa kutosha kuwa ni kwanini yuko Ulimwenguni!, kutokujua ni kwa nini uko Duniani ni tukio baya sana, watu wengi sana wamepoteza muelekeo na kufupisha maisha yao au kufa kabla ya wakati kwa vile hawajui kwanini wanaishi!,Aidha wengine wamekosa kugundua umaana wa maisha  na kufikiri kuwa labda huenda heri wasingalizaliwa ama walizaliwa kwa bahati mbaya kwa vile tu hawakujua kwa nini wamezaliwa? “Mjenzi mmoja alisema kama mtu hajui kwa nini anaishi amekufa tayari ingawa anaishi”

Mungu anapenda tuwe na ufahamu na tutambue umuhimu wa kuwepo Kwetu, ndani ya kila aina binadamu Mungu alikwisha kuweka kusudi lake, ili tulitumikie na kuliishi tukiwa duniani, wengine walielezwa mapema na kwa uwazi makusudi ya kuwepo kwao Mfano 

Yeremia 1:4-8 4. Neno la Bwana lilinijia, kusema,  Kabla sijakuumba katika tumbo nalikujua, na kabla hujatoka tumboni, nalikutakasa; nimekuweka kuwa nabii wa mataifa. Ndipo niliposema, Aa, Bwana MUNGU! Tazama, siwezi kusema; maana mimi ni mtoto. Lakini Bwana akaniambia, Usiseme, Mimi ni mtoto; maana utakwenda kwa kila mtu nitakayekutuma kwake, nawe utasema kila neno nitakalokuamuru. Usiogope kwa sababu ya hao maana mimi nipo pamoja nawe nikuokoe, asema Bwana”. 

Ni wazi kwamba Yeremia alifunuliwa Kusudi la Mungu katika maisha yake mapema sana akiwa kijana mdogo, wako wengine wazazi wao walifunuliwa kusudi la watoto wao hata kabla hawajazaliwa ili waweze kuwasaidia kulitimiza kusudi hilo Mfano Samsoni Waamuzi 13:2-5 Samsoni alizaliwa akiwa na kusudi la kuwaokoa Israel na mikono ya wafilisti, Yohana Mbatizaji Luka 1:5-17 Yohana Mbatizaji alizaliwa kukiwa na kusudi la kurejesha mioyo ya watu kwa Bwana, Muda usingaliweza kutosha kuona watu wengi waliozaliwa na waliopata neema ya kujua kusudi la kuwako kwao Mungu ana makusudi nawe pia!, hujazaliwa kwa bahati mbaya kuna kusudi la Mungu katika kuweko kwako!

Yesu alikuja Duniani kwa Makusudi makubwa na mengi na kwakuwa Yeye nikiongozi mkuu wa wokovu wetu tunapopitia kusudi la kuzaliwa kwake tunapata kugundua siri ya kwanini tuko ulimwenguni na hili litatusaidia sisi nasi kuishi kwa Makusudi KWA AJILI YA HAYA NALIZALIWA

1.       Kuwaokoa watu na dhambi zao Mathayo 1:21
Dhambi ni moja ya matatizo makubwa sana
2.       Kuwapatanisha watu na Mungu Yohana 1:35,29
3.       Kuharibu kazi za Ibilisi 1Yohana 3:7-8
4.       Kutafuta na kuokoa kilichopotea Luka 19:10
5.       Kufanya Mapenzi ya Baba yake Yohana 6:38
6.       Kuwa Nuru ya Ulimwengu Yohana 12:46
7.       Kutoa Uzima wa milele Yohana 10:10
8.       Kuhukumu Ulimwengu Yohana 9:39
9.       Kufunua kusudi la kweli la Maisha ambalo ni “ kutumika” Mathayo 20:28
10.   Kufa Msalabani ili awaokoe wanadamu Yohana 12:27

Kuifunua Hekima ya kweli na neno la Mungu, nah ii ndio kweli, ni muhimu kufahamu kuwa Israel walikaa na kuishika torati kwa maelfu ya miaka lakini hawakuielewa, ilikuwa kana kwamba imefichika machoni pao, katika neon la Mungu kuna siri ya ajabu ambayo mtu wa asili ya kawaida hawezi kuielewa siri hii ndio Kweli Mathayo 13:35, kweli hii ni siri inahitaji neema na ufunuo kutoka kwake kuielewa  Luka 24:27

Kazi na mkuu wa wajenzi mwenye Hekima

Nitaweka mkono wangu Juu ya Misri



Mstari wa Msingi Kutoka 7:4-5 “Lakini Farao hatawasikiza ninyi, nami nitaweka mkono wangu juu ya Misri, na kuyatoa majeshi yangu, watu wangu, hao wana wa Israeli, watoke nchi ya Misri kwa hukumu zilizo kuu. 5. Na Wamisri watajua ya kuwa mimi ndimi BWANA, hapo nitakapounyosha mkono wangu juu ya Misri na kuwatoa wana wa Israeli watoke kati yao”.

Hii ni lugha nyingine ya Kibiblia “NITAWEKA MKONO WANGU JUU YA MISRI” Maana yake ni nini ? Mungu ataihukumu Misri kwa sababu ya kiburi cha maendeleo yao ataleta anguko kubwa kwa vile Pharao amekuwa jeuri ana moyo mgumu hataki kuwaachia Israel Mungu napoihukumu Misri ana hukumu nini ni muhimu kulichambua hili!

Hali ya kiroho ya Taifa la Misri ilikuwa mbaya sana ingawa walikuwa na maendeleo makubwa sana, Mungu atalihukumu taifa lolote na kusababisha anguko kwa Dola hata kama ina nguvu kiasi gani endapo tu itamuacha Mungu, Historia inaonyesha sababu nyingine za kuanguka kwa dola la Misri


·     Mpaka miaka ya 1550 – 1200 hivi Utawala wa Misri ulikuwa umeenea mashariki ya kati na mbali mpaka mto Frat
·         Hata hivyo kwa haraka sana utawala huu ulianza kuanguka na kupoteza uwezo baadaye ukifuatiwa na tawala nyingine kama Ashuru Syria mwaka 750 KK
·         Kisha Babeli 606 BC
·         Kisha Uamedi/uajemi au Iraq na Iran 530 BC
·         Kisha uyunani au Ugiriki 332 BC
·         Kisha Rumi mwaka wa 30 BC
Dola zote zilizofuata baada ya misri hazikudumu kwa miaka mingi kama Misri, kwa mujibu wa kihistoria kuibuka kwa Dola hizo nyingine ndio ulikuwa mchango mkubwa wa kuanguka kwa Misri, ushahidi wa kibiblia unaonyesha kuwa taifa linalomuacha Mungu Mungu huweka mkono wake juu ya taifa hilo kwa hukumu Mungu ndiye aliyeihukumu Misri na mataifa mengineyo!

Ni lazima kila taifa litambue kuwa Mungu ndiye anayetawala na kuwa ndiye anayeweka wafalme na kuondoa na tena ndiye anayeyainua mataifa kwa makusudi yake na kuyasimamisha kwa kusudi lake na kuyaangusha kwa kusudi lake na utukufu wake

Warumi 9:17. Biblia inasema hivi “Kwa maana maandiko yasema juu ya Farao ya kwamba nilikusimamisha kwa kusudi hili, ili nionyeshe nguvu zangu kwako jina langu likatangazwe katika inchi yote” unaona kumbe kusimama kwa Misri ilikuwa ni kusudi la Mungu ili Mungu atangaze  nJina lake Duniani

Ni vema neno la Mungu likawa wazi kwa kila kiongozi na kila taifa kuwa mtu akiwa na madaraka au akiinuliwa akubali na kutambua kuwa kuna kusudi la Mungu nyuma yake, hivyo kila Mtu na kila taifa linapaswa kumuheshimu Mungu na kumpa Mungu kipaumbele, na kuwa na utambuzi na kunyenyekea na kuacha majivuno Lazima kila mtawala ajue yuko kwa kusudi la Mungu, na kuwa kama hatalitimiza Mungu ataweka Mkono wake na kuhukumu!

Biblia inasema Hivi Daniel 4:17 “Hukumu hii imekuja kwa agizo la walinzi, na amri hii kwa neno la watakatifu; kusudi walio hai wapate kujua ya kuwa Aliye juu anatawala katika ufalme wa wanadamu, naye humpa amtakaye, tena humtawaza juu yake aliye mnyonge”. Unaweza kuona?
Mungu anatumia wanyonge na kuwainua Mungu hapendezwi na kiburi na majivuno alimshughulikia Mfalme Nebukadreza kwa kusudi la kumyemyekesha ili ajue kuwa aliye Juu yaaani Mungu ndiye anayetawala,  Mwisho mfalme wa Babeli alisema Hivi katika Daniel 4:37 “….Basi mimi Nebukadreza namhimidi mfalme wa Mbinguni namtukuza na kumuheshimu maana matendo yake yote ni kweli na njia zake ni za adili na wale waendao kwa kutakabari (kiburi) yeye aweza kuwadhili! Unaoana

Biblia inaonyesha kuwa kiongozi jeuri asiyemnyenyekea Mungu, Mungu anauwezo wa kumuadhibu ni kwa sababu hizi Mungu aliweka mkono wake wa Hukumu dhidi ya Misri kwa sababu ya viongozi wake ambao walijichukulia heshima ya Mungu na kusahau kuwa wao ni binadamu tu Farao na majeshi yake yalifutiliwa mbali na Misri ilianguka, Historia kamwe haiwezi kuonyesha sababu hizi za kiroho, Ushahidi uliowazo kuwa Farao alikuwa na kiburi ni jinsi mara nyingi alikaidi agizo la Mungu la kuwaachia Israel waende zao mfalme huyu aliwahi kumjibu Musa kuwa Huyo Bwana ni nani? Kutoka 5:1-2 Biblia inasema hivi …..Bwana ni nani hata niisikilize sauti yake na kuwapa Israel ruhusa waende zao? Mimi simjui Bwana wala sitawapa Israel Ruhusa waende zao! Ni maneno ya Kiburi dhidi ya Mungu aliye hai hii ni kwasababu wamisri walimtukuza sana Farao na kumuabudu wakiamini ni mwana wa Mungu jua aliyeitwa Re akiwa katika mwili wa kibinadamu, Hivyo, kuwatumikisha Israel ilikuwa ni kashfa kwa Mungu wa Israel kwa vile farao anajilindanisha naye huku akiwa hatambui uwepo wa Mungu aliye hai ni kwa sababu hii Mungu alisema Nitaweka Mkono wangu juu ya Misri yaani nitaihukumu Misri, Kitu chochote kile kinachomdhalilisha mtu wa Mungu na kumtesa ni wazi kuwa kimejitukuza dhidi ya Mungu aliye hai Bwana na aweke mkono wake juu ya kila kitu kinachokusumbua na kukutweza na kukuonea na kukutawala huku kikiwa hakitaki kukuachia natangaza kuwa wakati umefika lazima vilivyojiinua vishushwe Bwana anaweka mkono wake juu ya usumbufu wote na kuhukumu kwaajili ya utukufu wa Jina lake Kutoka 14:3,17-18
Ujumbe na Mkuu wa wajenzi mwenye Hekima
Rev Innocent Kamote

Mashaka ya Nabii Musa!

Kutoka 3:1-4:17
1. Mungu alipomtokea Musa katika kijiti kilichokuwa na utukufu
a. Alimuita Musa ili kuwaongoza Israel kutoka katika Inchi ya Utumwa Misri
b. Musa alionyesha Mashaka Yake wazi na kutoa sababu zinazodhihirisha kwa nini hafai kwa Kazi hiyo
2. Musa alionyesha Mashaka yake wazi na Bwana Mungu alikuwa akimjibu Musa, Msahaka ya Musa ndio somo kubwa sana kwetu
a. Kwa sababu ni katika nia inayofanana watu wengi sana leo hupewa na Mungu wajibu Fulani na hata wito wa kumtumikia Mungu
b. Si kwaajili ya kuwatoa watu katika utumwa kama ilivyo kwa Musa kule Misri, lakini kwa Ulimwengu kwaajili ya kuwahubiri habari njema Marko 16:15 1Petro 2:9 ili waokolewe
c. Kama ilivyokuwa kwa Musa wengi wetu tunatoa Udhuru na kuonyesha Mashaka, Mashaka ya Musa yanaweza kugawanywa katika maeneo Matano yafuatayo

A. Mimi ni nani? Kutoka 3:11 Musa akamwambia Mungu, Mimi ni nani……
1. Ingawa Musa aliwahi kuishi katika Ikulu ya Farao mtawala wa Misri
a. Sasa alikuwa mchungaji wa mifugo ya mkwewe akiwa mtu duni
b. Miaka 40 ilikuwa imepita tangu alipoondoka kwa Farao
c. Sasa alikuwa mtu mzima mzee wa miaka 80, nguvu za ujana zimekwisha na yuiko na fimbo tu Musa aliweza kuwa na sababu za haki za kufikiri kuwa huenda yyeye si mtu sahii
2. Mungu alimjibu Musa Kutoka 3:12 asiwe na Mashaka kwani yeye atakuwa Pamoja naye
a. Bila shaka mimi nitakuwa Pamoja nawe
b. Mungu anapomuahidi mtu atakuwa Pamoja naye maana yake Yeye mwenyewe Mungu ni Utoshelevu wetu
c. Paulo mtume alisema kama Mungu akiwa Upande wetu yaani pamoja nasi ni nani atakayeweza kusimama kinyumenasi Warumi 8:31
B. Baadhi yetu leo tunatoa Udhuru au kuonyesha Mashaka kama Musa
1. Tunajiangalia wenyewe na kujipima na kuona kwamba hatutoshelezi/hatustahili kwa vigezo vya kuwa watumishi wa Mungu
a. Ni kweli kabisa hakuna mwanadamu anayetosheleza katika utumishi na huduma hii kimsingi hata mimi pamoja na kujiita Mkuu wa wajenzi katika Huduma hii kila siku najigundua kuwa sistahili kabisa kumtumikia Mungu, sio hivyo tu huwa namshangaa Mungu kwa nini anitumia mtu kama mie
b. Lakini Mungu ni Utoshelevu wetu 2Wakoritho 3:5-6 “ Si kwamba twatosha sisi wenyewe kufikiri neno lolote kwamba ni letu wenyewe, bali utoshelevu wetu watoka kwa Mungu, Naye ndiye aliyetutosheleza kuwa wahudumu wa agano jipya”
c. Unaudhuru gani Elimu? Angalia kuwa Mungu aliwatumia mitume ambao wengi wao walikuwa wasio na Elimu Matendo 4:13
d. Kama ilivyokuwa Mungu kwa Musa, Yesu Kristo anakutia moyo leo usiogope atakuwa pamoja nasi hata ukamilifu wa Dahari Mathayo 28:20
e. Kwa msaada wake tutayaweza yote Wafilipi 4:13.
C. Niwaambie Nini? Imekaa vema kwa kimombo what shall I say? Kutoka 3:13
1. Musa alijua kwamba anapaswa kuwaendea Israel, na wako kifungoni wakiwa na maswali lukuki
a. Wangemuuliza Mungu yupi aliye kutuma?
b. Kwa nini tuondoke hapa tumekuweko kwa miaka 400, tumezaliwa hapa haya ndio maisha yetu na tamaduni zetu
c. Ni kama Musa alukuwa akijiuliza ninaanzia wapi?
2. Mungu alilazimika tena kumjibu Musa, mwenye mashaka
a. Mimi niko ambaye niko, Utawaambia Kutoka 3:14-15
b. Mungu alikuwa na majibu kwa Musa kuhusu nini cha kusema
D. Baadhi yetu tunaweza kuwa na mashaka kuhusu nini cha kusema
1. Tuna mashaka kwa sababu wakati mwingine tunafikiri kuhusu maarifa yetu yasotosheleza
2. Lakini Mungu ataweka maarifa na nini cha kusema
a. Atakupa neno rahisi Marko 16:15-16
b. Na ni jinsi gani itakuwa Rahisi 1Koritho 15:1-4,2:2
c. Hata Musa alipokuwa ameelekezwa nini cha kusema akaibuka na sababu nyingine
E. Je wasiponiamini wala kunisikiliza?
1. Musa sasa amepewa Maarifa na anajua nini cha Kusema lakini anawasiwasi hawatamuamini walakumsikiliza?
a. Ni dhahiri kuwa Musa alikuwa anaogopa kukosea
b. Anaogopa matokeo magumu na amesahau kuwa Mungu alisema atakuwa Pamoja naye
2. Mungu alimsaidia Musa kuondoa mashaka na kumuaminisha kuwa yuko naye
a. Fimbo ya Musa iligeuka kuwa nyoka Kutoka 4:2-5
b. Mkono wake ulipatwa na ukoma
c. Maji yaliyogeuka Damu Kutoka 4:9.
F. Wengi wetu tunamashaka na majukumu na wajibu tuliopewa kuutumikia na kwa watu wa Mungu wana mashaka kama wanafaa kuwa chombo cha kuhubiri injili
1. kumbuka woga ni adui anayekuzuia katika kujaribu
2. Kama Mungu alivyomjibu Musa na kuondoa mashaka aliyokuwa nayo tunao ushahidi unaoweza kututhibitishia na kutuondolea mashaka juu ya kile Mungu anataka tukitimize
a. Neno la Mungu liko kwaajili yetu Warumi 10:17, Yohana 20:30-31
b. Yesu alikufa na maefufuka Yuko hai ni yeye anayetenda kazi ndani yetu
c. Migandamizo na kelele kutoka nje isikutie mashaka ukaacha kumuamini Mungu kuwa yu aweza kukusaidia na kuwa yuko pamoja nawe na kuwa vita si yako ni yake yeye na kuwa hata wajibu na kazi tuliyopewa ni kwa utukufu wake.
G. Mimi sio Msemaji, Mimi sio mwepesi wa Kusema!
1. Tunaona mashaka haya katika Kutoka 4:10
1. Musa alisema mimi sio mnenaji Mzuri? Je umeshawahi kuwasikia baadhi ya viongozi wakisema neno mimi sio Mwanasiasa? Unajua wanamaanisha nini? Wao sio wasemaji, sio wazungumzaji wazuri
2. Mungu hasukumwi na Udhaifu wa Mwanadamu anatujua tulivyo hata kabla hajakuita au kukupa wajibu
3. Anaujuzi wa kuwatumia hata waliodhaifu ndio si tuliumbwa kwa kusudi lake uwe na uwezo usiwe na uwezo yeye akiamua anakutumia
a. Mungu alimsaidia Musa kujua Yeye ndiye Muumba ndiye anayeruhusu mtu kuwa Bubu au kuwa msemaji, Mungu alikuwa anaelewa wazi udhaifu wake na kama udhaifu wake ungekuwa ni sababu ya yeye kushindwa kumtumia asingelimfuata
b. Mungu anauwezo wa kumsaidia kila mtu katika madhaifu yake
c. Mungu alimuahidi tena Musa kuwa atakuwa pamoja naye Kutoka 4:11
d. Mungu alimuandaa haruni kwaajili ya kumsaidia Musa Kutoka 4:14-16 Mungu wakati wote ataandaa watu wa kututia moyo na kufanya kazi pamoja nasi.
H. Sisi nasi tunaweza kuwa na mashaka na kutoa udhuru kama huu wa Musa,
1. Paulo mtume Hakuwa na ufasaha wa Maneno wala hekima kama zile za wagiriki, alikuwa dhaifu, mwenye hofu na mwenye kutetemeka sana 1Koritho 2:1-5, Lakini pamoja na hayo alimtegemea Mungu na sio hilo tu aliwatia moyo na wengine
“Imani yetu isiwe katika Hekima za wanadamu bali katika nguvu za Mungu”
Musa aliogopa kuwa mnenaji eti kwa vile alikuwa na Kigugumizi Kutoka 4:13 Mungu hakukiondoa kigugumizi kila japo angeweza kufanya hivyo Mungu alikusudia kumtumia pamoja na udhaifu wake
I. Tuma huyo utakayemtuma! Kutoka 4:13.
Mungu alikubaliana na Mashaka yote ya Musa na kila mashaka yake yalikuwa na Majibu lakini sasa Mungu anakasirishwa na tabia ya Musa wakati huu, Sasa Musa hataki kabisa kwenda!
1. Mungu ametuumba kwa kusudi lake ni lazima tutmika bila kujali udhaifu tulionao kwa vila kila aina ya udhaifu una majibu kwa Mungu
2. Ukikataa kumtumikia Mungu au kulitumikia kusudi la Mungu unajiweka katika wajibu wa kumtumikia shetani
3. Hasira za Mungu kwa Musa zilikuwa za upendo, Mungu alikuwa anataka kumtumia Musa ndiye aliyekuwa amamemuandaa kwa Muda mrefu kwa kusudi hilo
Ndugu zangu
a. Kila udhuru na kila sababu utakayoitoa kukwepa kutokumtumikia Mungu ni Upotoshaji wa haki ya Mungu
b. Ni kweli tungetamani kama Mungu angelimtumia mtu mwingine mbadala
c. Ni kweli hatupendi kutenda kila Mungu anachokitaka
d. Lakini ndugu hapo ndipo hasira za Bwana zinapowaka na kuwa kinyume nasi, hatuwezi kuacha kulitumikia kusudila Mungu wetu hata kama kuna hali zinazokataa endapo hali hizi zimetokea kwetu kutoa udhuru tunahitaji kutubu
Hatimaye!
Wote tunajua kuwa Musa alikubali, wito wa kwenda Misri
Wote tunajua kuwa Mungu alikuwa pamoja naye na kumsaidia
Wote tunajua dhahiri kuwa Musa sasa anaheshimika na kukubalika na watu wote kama kiongozi mkubwa sana wa manabii na baba wa taifa la Israel, Ukiondoa shaka na kumuamini Mungu atakutumia kwa viwango vya juu kwa utukufu wake.
Mungu hatuimii watu maalumu sana, Tunakuwamaalumu Mungu anapokuwa Pamoja nasi
God never use the superman, we became the superman when God is with us
Mkuu wa wajenzi mwenye Hekima
Rev. Innocent Kamote.