Alhamisi, 4 Februari 2016

Jinsi ya Kuukulia Wokovu !



Mstari wa msingi 1Petro 2;2 “ Kama watoto waliozaliwa sasa yatamanini maziwa ya akili yasiyoghoshiwa ili kwa hayo mpate kuukulia wokovu”

Ni muhimu kufahamu kuwa tangu ulipoamua kuokoka wewe sasa umekuwa mtoto wa Mungu Biblia inasema katika Yohana 3;6 “ Kilichozaliwa kwa mwili ni mwili na kilichozaliwa kwa Roho ni roho wewe umezaliwa kwa roho ndiyo maana inatajwa pia kuwa umezaliwa mara ya pili , hapo mwanzo ulizaliwa katika mwili na kilichozaliwa kwa mwili ni mwili  na kamwe hakiwezi kuishinda dhambi, lakini sasa umezaliwa mara ya pili na ufalme wa Mungu ni wako, kwa msingi huo sasa tungependa kutafakari jambo moja la msingi sana 

 wokovu ni hatua

Mtoto mchanga wa kimwili anapozaliwa  yaani katika hali ya kawaida ya kibinadamu  ili aendelee kuishi anapaswa au analazimika kupewa maziwa ili aweze kuishi jambo kama hili ni sawa kwa mtoto wa kiroho pia vinginevyo anaweza kufa au kudumaa na hatimaye kuwa dhaifu na kufa, kufa kiroho ni kurudi nyuma na kumtumikia shetani sasa ili mtu aliyezaliwa mara ya pili aweze kuendelea katika wokovu ni lazima anywe maziwa ya Kiroho 1Wakoritho 3;1-2 na Waebrania 5;13 “Kwa maana kila mtu atumiaye maziwa hajui sana neno la haki kwa kuwa ni mtoto mchanga” Hivyo mara baada ya kuzaliwa kiroho au kuokoka tunakuwa bado hatujui sana neno la haki tunahitaji maziwa ili tuweze kukua katika wokovu.

Maana ya maziwa
Maziwa haya ni kinywaji cha kiroho Kutoka kwa Yesu Kristo ni neno la Mungu au neno la Kristo soma 1Wakoritho 10;4 wote wakanywa kinywaji kile cha roho kwa maana waliunywea mwamba wa roho uliowafuatia na mwamba ule ulikuwa ni Kristo” Mtu awaye yote aliyeokoka kama hatapata mafundisho ya neno la Mungu  atadumaa nakujiweka katika hali ya kufa kiroho na kurudi tena katika utumwa wa dhambi, hakuna uwezekano  wowote wakuendelea na wokovu bila mafundisho ya neno la Mungu  Neno la Mungu lina sehemu kubwa sana katika maisha ya kiroho ya mtu.

1.       Ni chakula cha kiroho.
Biblia inasema mtu hataishi kwa mkate tu bali kwa kila neno litokalo katika kinywa cha Mungu, kwa msingi huo kusudi la kuishi kwetu halitegemei kula chakula cha kawaida tu bali na chakula cha kiroho ambalo ni neno la Mungu Yeremia 15;16 “maneno yako yalionekana nami nikayala…” Neno la Mungu ni chakula halisi Yesu alisema amlaye yeye ataishi kwanini kwa sababu Yesu ni neno la Mungu Yohana 1;1 Ufunuo 1913 Yohana 6;48-58 Tukiacha kulila Neno la Mungu  baada ya kuzaliwa mara ya pili  hatutaweza kuishi milele ili kuishi milele ni lazima tumle Yesu Kristo Yohana 6;48-49,57-58, Yeye ndiye chakula cha uzima  Mathayo 4;4 Yesu alisema mtu hataishi kwa mkate tu…” Kumbukumbu la torati 8;3 Mungu aliwafundisha Israel kuwa hawawezi kuishi kwa mkate tu bali kwa kila litokalo katika kinywa cha Mungu ni kwa ujuzi huu watatakatifu waliotutangulia walifahamu umuhimu wa kulishika Neno kama chakula Ayubu 23;12, wao waliiona sheria ya Mungu yaani neno kuwa la thamani kuliko maelfu ya dhahabu na fedha”

2.       Ni taa na mwanga wa njia yetu ya Mbinguni
Njia ya mbinguni ni nyembamba sana  kwa maana nyingine imesonga  na mlango ni mwembamba sana Mathayo 7;14 ili wakati wote tuweze kutembea  bila kuanguka au kuteleza  na kuingia katika njia iendayo upotevuni  inatupasa kuwa na mwanga Mathayo 7;13, tusipolizingatia Neno la Mungu tunaweza kupotea  katika wokovu Zaburi 119;105 Neno lako ni taa ya miguu yangu, Mithali 6;21-23 sheria ya Mungu ni nuru…”

3.       Ni silaha ya ushindi dhidi ya dhambi.
      Ni vigumu kabisa kuishinda dhambi bila kujaa neno la Mungu Yesu Kristo alimshinda shetani katika mathayo sura ya 4 kwa kutumia neno la Mungu aliposema imeandikwa, kumbe kumshinda adui na kuishinda dhambi kunahitaji uwe na ujuzi pia wa neno la Mungu  Huwezi kuishinda dhambi na adui shetani kama hupendi kuhudhuria mafundisho na ibada ambako tunajifunza Neno la Mungu, Zaburi ya 119;11 Biblia inasema Moyoni mwako nimeliweka Neno lako nisije nikakutenda dhambi kumbe kujifunza neno la Mungu na kulifanyia kazi yaani kulitii kunatusafishia njia ya kwenda mbinguni Zaburi ya 119;9 Jinsi gani kijana aisafishe njia yake ni kwa kutii Neno la Mungu na kulifuata daima, Neno la Mungu pia hufanya maisha yetu kuwa safi Yohana 15;3,Yohana 17;17, kuacha kujifunza neno la Mungu kunaweza kutufanya pia kufanya dhambi bila kujua Mambo ya walawi 5;17

4.       Ni Afya ya miili yetu na nyundo ya kuyavunja matatizo tuliyo nayo
Ikiwa tuliponywa kwa Neno la Mungu katika mikutano ya injili au katika maombezi yoyote ni neno la Mungu linalotuhakikishia uzima wakati wowote, mara nyingi shetani anapotuona kuwa tunaujuzi wa Neno la Mungu hawezi kurudi kutufuata fuata tena Luka 11;24-26, hata kama hatujapokea uponyaji wa miili yetu bado ni muhimu kufahamu kuwa Neno la Mungu ndio ufunguo wa uponyaji wetu Mithali 4;20-22 Yohana 6;63. Yatafute maneno ya Mungu na kuyaweka moyoni.
 Unapokuwa umebanwa na matatizo ya aina yoyote  dawa siyo kuacha kutafuta mafundisho ya Neno la Mungu  tumia kila inavyowezekana kulitafuta Neno na kulitumia lenyewe ni kama nyundo ya kuvunja vunja kila aina ya matatizo matatizo yote yanayoonekana kama mawe magumu Neno linauwezo wa kuyavunja Yeremia 23;29 Je Neno langu si kama moto? Asema Bwana na kama nyundo ivunjayo mawe vipande vipande?

Vizuizi vya kukuzuia kupata mafundisho au chakula cha kiroho yaani Neno la Mungu.
Tumeona jinsi ambavyo neno la Mungu lina faida nyingi sana katika maisha yetu ikiwa ni pamoja na kutufanya tuishi milele na milele kwa msingi huo basi ni muhimu kufahamu kuwa shetani hatapedezwa na sisi kulipata Neno la Mungu kwa msingi huo kutakuwa na vizuizi vya kila aina kutoka kwake ili tusiwezi kulielewa na kulijifunza Yeye anajuwa wazi kabisa kuwa hawezi kumshinda mtu aliyejaa neno kama ilivyokuwa kwa Bwana Yesu Mathayo 4;1-11 kwa msingi huo atahakikisha kuwa kwa gharama yoyote ile anatuzuia kulipata Neno  na ndio maana hukusudia kutuua kiroho mapema katika uchanga wetu ili tusifikie ngazi ya kulijua Neno ambalo kwalo anajua kuwa hataweza kutushinda tena alikusudia kumuua Yesu mapema  Mathayo 2;13,16, sisi nasi tunapookolewa ni muhimu kufahamu kuwa tunakuwa tumezaliwa kwa Roho na hivyo ibilisi atahakikisha kuwa anatuua mapema kabla hatujalijua sana neno kwa kuwa tunazifahamu fikra zake ni muhimu kujifunza mbinu zake mapema kabla hajaanza kuzitumia na kutupata 2Wakorotho 2;11 tukizifahamu mbinu anazozitumia basi hatutampa nafasi ya kukuua mpinge naye atakukimbia Waefeso 4;27.Yakobo 4;7.

Njia Tano anazozitumia shetani Kumzuia mtoto mchanga kupata Neno la Mungu ili kumuua.
·         Kumfanya ajione anajua na akatae kufundishwa
Biblia inasema mtu akidhani kuwa anajua neno  hajui bado kama impasavyo kujua  1Koritho 8;2 Mtu awaye yote akikosa ladha ya chakula na kukataa kula akisema kuwa anajisikia kuwa ameshiba  maisha ya mtu huyo yako hatarini hiki ndicho shetani anachokifanya kwa watu wengi waliookoka   huwafanya wajione kuwa wanajua na hawahitaji kujifunza tena  na kutokukubali kujifunza neno la Mungu na hatimaye hujikuta wanakufa kiroho mtu akitaka kujifunza siku zote ni lazima ujifanye kuwa mjinga Zaburi 73;22,24 na ni lazima ukubali kufundishwa na Mungu siku hadi siku Zaburi 143 ;10 Tunapokuwa katika hali ya kukubali kufundishwa ndipo tunapata nafasi ya kumpendeza Mungu Zaburi 25;4-5,Yohana 6;45 Isaya 54;13 Kuangamizwa kwetu kunatokana na kukosa maarifa Hosea 4;6 kwa msingi huo ni lazima tukubali kufanya sehemu yetu na kukubali kujifunza Neno la Mungu na kamwe tusikubali kulizoea Neno kila siku kubali kujifunza kana kwamba ndio unaanza sasa ukifanya hivyo ushindi utakuwa ni wako.

·         Kumfanya asongwe na shughuli za dunia na udanganyifu wa mali.
Mathayo 13;22 tunajifunza mfano wa mbegu zilizoangukia kwenye miiba kuwa ni watu wanaoshindwa kukua kiroho kwa sababu ya kushindwa kudumu katika neno na kusongwa na shughuli za dunia na udanganyifu wa mali, kwa msingi huo ni lazima uwe mwerevu katika mema fahamu kuwa lolote lile linalokuzuia kujifunza Neno la Mungu wakati mwingine ni kifungo cha kukufanya usikue kiroho na huyo ni adui 3Yohana 1;2 Mungu anapenda tufanikiwe katika mambo yote  lakini msingi wa mafanikio ya kweli huanzia rohoni na ndio maana Yesu alisema tutafute kwanza ufalme wa Mungu na haki yake na mengine yote tutazidishiwa  Mathayo 6;33 kumbuka kuwa haitakufaidia kitu kama utaupata ulimwengu mzima na kupoteza nafsi yako ? Marko 8;36 ni muhimu kufanya kazi na kujishughulisha kwani Biblia inasema asiye fanya kazi kula na asile lakini ni muhimu kutokutawaliwa na utafutaji wa mali na kujikosesha mambo ambayo ndio msingi wa baraka za mwili pia kwa kila jambo kuna majira yake Muda wa ibada uwe ibada na Muda wa kazi na biashara na uwe muda wa kazi na biashara Muhubiri 3;1 kwa msingi huo wakati wa kipindi cha neno acha shughuli zako nyingine maana neno la Mungu ndio uhai wa maisha yetu hivyo ni muhimu likapewa kipaumbele.
·         Kuwafanya watu wawe wanatoa udhuru wakati wote wanapohitajika kwenda kwenye neno
Una weza kushangaa kuwa siku za ibada ya kujifunza maneno ya Mungu ndio kunatokea sababu kadhaa wa kadhaa ili mradi tu kukufanya usione umuhimu wa kuja kujifunza neno la Mungu inapotokea hali hiyo fahamu kuwa ni hila za adui  Luka 14;16-20 Yesu alitoa mfano wa watu walioalikwa harusini lakini kila mmoja alionekana ana sababu za msingi za kumfanya asihudhuria sherehe ile  hali iliyomuudhi mwenye harusi Luka 14;33 Yesu alihitimisha kwa kuonya kuwa “basi kadhalika kila mmoja wenu asiyeacha vyote  alivyo navyo hawezi kuwa mwanafunzi wangu” 

·         Kumletea mtu dhiki au udhia kwa ajili ya wokovu.
Mathayo 13;20-21 ni mfano wa Yule aliyepandwa kwenye miamba kwa kukosa mizizi  inapotukia dhiki huchukizwa , hiii ni mbinu nyingine ya adui ili kwamba aweze kuwakatisha watu tamaa ya kujifunza neno la Mungu kisha wafe kiroho inakupasa kuvumilia yanapotokea magumu  na wala uusiliache neno la Mungu  heri ni wale wanaostahimili Mathayo 5;11-12,1Petro 4;12-16 Yakobo 5;10

·         Kukufanya utafute mafundisho yaliyo karibu na nyumbani
Katika hali isiyokuwa ya kawaida wakati mwingine shetani anaweza kuleta ushawishi unaoonekana kama wenye busara kwa kukushawishi kufuata mafundiho yanayopatikana karibu na nyumbani  ili kukupeperusha  kwa kupenda njia ya mkato Mungu alipandisha Israel kutoka Misri aliwapitisha katika njia iliyo ndefu na ya mbali kwenda kanaani Kutoka 13;17-18 si vibaya kusali karibu na nyumbani kwako kama wana mafundisho mazuri lakini ni vema kukaa na wale waliokuzaa kiroho kwani hao ndio wana uchungu na wewe na pia endapo mafundisho ya mahali hapo ni dhaifu basi ni afadhali kwenda mbali kwa faida ya roho yako  hekima ya Mungu wakati mwingine hutafutwa kwa gharama Mathayo 12;42 ukitaka ukue kiroho wakati mwingine uwe kama malikia wa sheba.

Umuhimu wa kunywa maziwa Yasiyoghoshiwa Incorrupt Gospel 1Petro 2;2
Maziwa yasiyoghoshiwa ni neno la Mungu halisi lisilochanganywa na chochote, neno la Mungu ambalo limechanganywa na mapokeo ya wanadamu halifai katika malezi ya kiroho, baada ya kuokolewa kama utakuweko mahali ambapo neno la Mungu linachanganywa na mapokeo ya wanadamu mahali hapo panaandaa mauti yako ya Kiroho, ni muhimu kwako kukaa mahali ambapo unajifunza Neno la Mungu safi lisilochanganywa na mapokeo ya kidini kwani hayo ni sumu ya kuua watu wa kirohon kaa mahali penye mafundisho ambayo ni neno la Mungu halisi.

Uchungu wa mwana aujuaye ni mzazi wagalatia 4;19-20
Neno la Mungu linatufundisha kuwa Mzazi wa kiroho kama ilivyo kwa mzazi wa kimwili anakuwa na uchungu wa mtoto wake kuliko Yule asiyekuzaa ili uweze kupata huduma nzuri kaa na wale waliokuzaa kiroho wao wana uchungu wa kweli kwaajili yako, hudhuria ibada hapo njoo na kalamu na daftari andika mafundisho yote unayojifunza ukijua ya kuwa nawe utakuwa kiroho na kuwa mwalimu wa wengine huo ndio mpango wa Mungu kwaa jili yako Ubarikiwe.

Furaha katika Maisha ya Wokovu !



Mstari wa msingi Mithali 16;20 “ …….Na kila amuaminiye ana Heri”

Ni vigumu kujifunza katika somo moja kama hili furaha zinzoambatana na wokovu, hata hivyo tutaangalia kwa ufupi sana maeneo machache katika furaha hii maana furaha hii haina mwisho, inaanzia hapa duniani na itaendelea mbinguni milele na milele,siku ile ulipokata shauri ulifanyika kuwa mtoto wa Mungu  Yohana 1;12-13, “Bali wote waliompokea aliwapa uwezo kufanyika watoto wa Mungu ndio wale waliaminio jina lake waliozaliwa si kwa mapenzi ya mwili wala si kwa mapenzi ya mtu bali kwa Mungu” wewe sasa ni mtoto wa Mungu hapo mwanzo wewe ulikuwa mtoto wa Ibilisi kwa sababu kila atendaye dhambi ni wa Ibilisi na tamaa za ibilisi ndizo apendazo kuzitenda Yohana 8;44,1Yohana 3;7-8 sasa basi kwakuwa wewe ni mtoto wa Mungu Mungu anajishughulisha sana mambo yako yote na hivyo mkono wa Mungu uko juu yako katika maswala kadhaa wa kadhaa kama yafuatayo.

                                                             Nanyi mnalindwa na Nguvu za Mungu!

*      ULINZI
Wewe sasa unalindwa na nguvu za Mungu kwa sababu umekuwa mtoto wake na umtii kwake alipokuita ulikubali kutubu dhambi zako na kumfuata hivyo tangu sasa inakupasa kumtegemea yeye kwa ulinzi wa kila aina haupaswi kuogopa Uchawi wala wachawi, nguvu za giza hazina nguvu kwako tena unapoonewa sasa Mungu ndiye ngao yako yeye ndiye anayekutetea moja kwa moja huna haja ya kuogopa tena 

§  Zekaria 2;8 “…………..awagusaye ninyi aigusa mboni ya jicho langu”
§  Zaburi 34;7 “Malaika wa Bwana hufanya kituo akiwazunguka wamchao na kuwaokoa”
§  2Nyakati 16;9 “Kwa maana macho ya Bwana hukimbia kimbia duniani mwote ili ajionyeshe mwenye nguvu kwaajili ya hao, waliokamilika moyo kuelekea kwake”
§  Zaburi 91;4-7 “Kwa manyoya yake atakufunika , chini ya mbawa zake utapata kimbilio…”
§  Zaburi 125;2 “Kama milima inavyoizunguka Yeruselem Ndivyo Bwana anavyowazunguka watu wake tangu sasa na hata milele”

*      WATU WANAOKUPIGA VITA AU KUKUONEA MUNGU ATASHUGHULIKA NAO.
Kuanzia ulipokata shauri kuokoka wewe ni wa thamani mno machoni pa Mungu  hivyo vita si vyako tena bali ni vya Bwana  wako Yesu Kristo 2Nyakati 20;15 Yeye Bwana ni mtu wa Vita Kutoka 15;3 na anauwezo wa kukupigania wewe nawe utanyamaza kimya  Kutoka 14;14  yafuatayo ni maandiko kwaajili yako
§  Yeremia 15;20-21 “nami nitakufanya kuwa kama ukuta wa  boma la shaba juu ya watu hawa nao watapiganna nawe lakini hawatakushinda maana mimi nipo pamoja nawe  ili nikuokoe na kukuponya asema Bwana , nami nitakuokoa na mkono wa watu wabaya  nami nitakukomboa katika mkono wao wenye kutisha”
§  Isaya 54;17 “Kila silaha itakayofanyika juu yako haitafanikiwa, na kila ulimi utakaoinuka juu yako katika hukumu utauhukumu kuwa mkosa huu ndio urithi wa watumishi wa Bwana na haki yao inayotoka kwangu mimi asema Bwana”
§  Isaya 43;1-2 “Lakini sasa Bwana aliyekuhuluku Eee Yakobo yeye aliyekuumba Ee Israel asema hivi Usiogope maana nimekukomboa , nimekuita kwa jina lako,wewe u wangu, upitapo katika maji mengi nitakuwa pamoja nawe na katika mito haitakugharikisha, uendapo katika moto hutateketea wala mwali wa moto hautakuunguza”

*      KWA HABARI YA MAGONJWA AU MATESO
Mapenzi yake Bwana aliyetuokoa ni wewe uwe na uzima  tena uwe nao tele Yohana 10;10 kazi za magonjwa ni kazi za Ibilisi lakini Kristo alidhihirishwa ili azivunje kazi za Ibilisi 1Yohana 3;8 kwa msingi huo litumie jina la Yesu kukemea mateso ya aina yoyote na magonjwa yanayokutesa wakati wote amini maandiko yafuatayo kwa ajili ya uzima wako.
§  Zaburi 34;19 “Mateso ya mwenye haki ni mengi lakini Bwana humponya nayo yote”
§  Kutoka 15;26 “Akawaambia kwamba utaisikiza kwa bidii sauti ya Bwana Mungu wako na kuyafanya yaliyoelekea mbele zake na kutega masikio usikie maagizo yake na kuzishika amri zake, mimi sitatia juu yako maradhi yo yote niliyowatia wamisri Kwa kuwa mimi ni Bwana Mungu wako nikuponyaye”
§  Yeremia 30;17 “Maana nitakurudishia afya asema Bwana Kwa sababu wamekuita mwenye kutupwa wakisema Ni sayuni ambao hapana mtu autakaye”
§  Torati 7;15 “ Na Bwana atakuondolea ugonjwa wote wala hatatia juu yako maradhi yoyote mabaya uyajuayo ya Misri”

*      KWA HABARI YA MAOMBI.
Maombi yako kabla ya kuokoka Mbele za Mungu yalikuwa ni kama kelele tu Mungu alikuwa hakusikilizi dhambi zilikuwa zimekutenga mbali naye Isaya 59;2 “Lakini maovu yenu yamewafarikisha ninyi na Mungu wenu na dhambi zenu zimeuficha  uso wake msiuone hata hataki kusikia” sasa baada ya kuokolewa anashughulika na maombi yako hivyo lolote utakaloliomba atashughulika nalo zaburi 55;22, Umtwike Bwana mzigo wako naye atakutegemeza hatamwacha mwenye haki aondoshwe milele 1Petro 5;7 Yohana 16;24 tumuombe Mungu kwa jina lake Yesu naye atatusikia huu ndio ujasiri tulio nao kwake kuwa tukiomba kitu sawa na mapenzi yake anatusikia  1Yohana 5;14-15, Hatupaswi kumuomba Mungu kupitia majina ya watakatifu waliotutangulia na Badala yake tunamuomba Mungu kwa jina la Yesu tu si Petro, au Paulo au Mariam kuomba kupitia wao sio mpango wa Mungu Yohana 14;13-14 kumbuka mitume na hata Mariam naye alimuomba Yesu soma Matendo 1;14 Kumuomba Mungu kupitia mtu mwingine ni machukizo kwa Mungu  na ni kulitia unajisi  jina la Bwana Isaya 48;11 Jina la Yesu ni jina lililo juu ya majina Yote Wafilipi 2;9-10.
Wewe tangu sasa umekuwa kiumbe kipya  2Koritho 5;17  na kwamba unao ndugu wengi kwa kuwa sasa umaeingia katika familia ya Mungu kila aliye katika kristo Yesu yeye ni ndugu yako  undugu huo hauna mipaka ya nchi ,wala rangi wala kabila  sote ni mwili wa Kristo sisi tu wana wa Mungu na Mungu alituchagua tangu asili  soma Warumi 8;29 “Maana wale aliowajua tangu asili aliwachagua tangu asili wafananishwe na mfano wa Mwana wake ili yeye awe mzaliwa wa kwanza miongoni mwa ndugu wengi” Karibu sana katika familia ya Mungu.

Kuteswa kwaajili ya Kristo !



Mstari wa Msingi Wafilipi 1;29 “ Maana mmepewa kwa ajili ya Kristo si kumwamini tu ila na kuteswa kwaajili yake “

Kuchukiwa baada ya kuokoka
Baada ya kumuamini bwana Yesu na kuanza kuukiri wokovu ulioupokea hadaharani, kutafuata kila aina ya kebehi kutukanwa na kila namna ya kuchukiwa na ndugu walio karibu ni muhimu kuvumilia mpaka mwisho kwani Yesu alituambia kuwa tukichukiwa kwaajili yake tuna heri Mathayo 10;22.
   Katika hali ya kawaida ungefikiri kuwa ndugu mume au mke au wazazi wangelifurahia uamuzi wako wa kuokoka lakini jambo la kushangaza ni kuwa haitakuwa hivyo wengi wataanza kusema umeiacha imani yako ya kwanza uliyozaliwa nayo? Au dini ya ukoo wako hali inaweza kuvuruga sana hata mahusiano yako na mumeo yanaweza kuingia utata ni muhimu kufahamu kuwa si kila wakati watafurahia watu uamuzi wako ndio maana Yesu alisema hakuja kuleta amani duniani Luka 12;51-53. 

                                                Kwaajili ya Kristo wengine wanakubali kuuawa kinyama


Wakati mwingine kwa sanbabu ya wokovu amani itaondoka utashangaa unaweza kufanyiwa hata vikao  na kuanza kutishwa au kuteswa kwaajili ya bwana na mwokozi wako Yesu Kristo hayo yasikukatishe tamaa fahamu ya kuwa tumepewa si kumwamini tu bali na kuteswa kwaajili yake wanaweza kukupa kila aina ya majina hata kuitwa mchawi isikusumbue kwani hata Yesu aliitwa kuwa anatoa pepo kwa kutumia mkuu wa pepo Mathayo 10;24-25,28 hayo yatatupata mara baada tu ya kulikubali neno la Mungu 

Fahamu kuwa wewe si wa ulimwengu huu na hivyo ndio maana ulimwengu unakuchukia ungelikuwa wa ulimwengu huu ulimwengu ungekupenda  Yohana 17;14 kwa msingi huo ni muhimu kuwa tayari kwa mateso ya namna yoyote ile na kuvumilia huku tukihakikisha kuwa hayatupotezei wokovu wetu Ufunuo 3;11

Biblia inatufundisha kuwa watu wanaokwenda mbinguni ni lazima wapitie dhiki adha  na mateso mengi ndio maana mitume waliwafundisha wanafunzi wao mapema kujua hayo Matendo 14;22 Imetupasa kuingia katika ufalme wa Mungu kwa njia ya dhiki nyingi, aidha katika mafundisho yake Bwana Yesu alisema Heri weri wenye kuudhiwa kwaajili ya haki maana ufalme wa mbinguni ni wao Mathayo 5;10  yeyote ambaye amechagua maisha ya utauwa yaani maisha ya wokovu lazima ataudhiwa soma 2Timotheo 3;12  dhiki hizi tumewekewa na na tusifadhaishwe 1Thesalonike 3;3, Petro anasema katika 1Petro 3;14 Lakini mjapoteswa kwaajili ya haki mna heri kwa hiyo tusiogope kutisha kwao

Mtu anayekata tamaa haraka kwaajili ya dhiki hizi anafananishwa na mbegu zile zilizoangukia juu ya mwamba na kwa kukosa mizizi ikitukia dhiki wanachukizwa soma Mathayo 13; 20-21, tunapaswa kuwa wavumilivu na kamwe hatupaswi kuwajibu vibaya wala kwa hasira  kwa sababu hawajui walitendalo wewe subiri thawabu yako ambayo ni kubwa sana Mbinguni  Mathayo 5;11-12, Ni sifa kubwa mbele za Mungu  kupigwa makofi kwaajili ya wema 1Petro 2;19 dhiki hizi tulizo nazo sisi ni nyepesi na za Muda tu  ukilinganisha na thawabu kubwa ambayo Mungu atakwenda kutulipa huko Mbinguni 2Wakoritho 4;17-18  inatupasa kufurahi tunaposhiriki mateso kama Kristo ili siku akifunuliwa  utukufu mkubwa wa Mungu  na roho wake anatukalia hii ndio maana ulimwengu unatuchukia 1Petro 4;13-14 trukumbuke kuwa yanayotupata yaliwapata pia wale waliokuwa wametutangulia na biblia inatutaka kuchukua manabii waliotutangulia kama mfano wa kustahimili mabaya na wa uvumilivu Yakoboo 5;10, mitume wengi waliuawa kwaajili ya Kristo katika historia za kanisa inaonekana kuwa Petro aliuawa wakati wa mtawala aliyeitwa Nero kwa kusulubiwa kichwa chini miguu juu,huko Roma Andrea alisulubiwa huko Misri na Simon Mkananayo aliyeshurutishwa kuubeba msalaba wa Yesu naye alisulubiwa  na wengine wengi walipata mateso ya namna mbalimbali  kweli ufalme wa Mungu unapatikana kwa njia ya dhiki nyingi nasi inatupasa kuwa wavumilivu sana hata kama kila mtu atatuchukia iwe ni kazini ama popote pale kumbuka kuwa taji kubwa inakungoja 

Kumbuka kuendelea kuwaombea wale wanaotutesa ili kwamba Mungu awaokoe na pia wakati wote huu wa mateso shirikisha wenzako katika Bwana ili mshirikiane katika kuomba kwani kiungo kimoja kikiumia katika Kristo ni viungo vyote Jipe moyo kwani ushindi ni lazima Ubarikiwe sana
Maana mmepewa kwa ajili ya Kristo si kumwamini tu ila na kuteswa kwaajili yake.

Wenyeji wetu uko Mbinguni!



Mstari wa msingi wafilipi 3;20 “Kwa maana sisi wenyeji weytu uko mbinguni kutoka huko tena tunamtazamia mwokozi Bwana Yesu Kristo”

 kwa maana sisi wenyeji wetu uko Mbinguni

Tumaini letu kuu watu tuliookoka ni kwamba Yesu Kristo Mwokozi wetu atakuja mara ya pili, safari hii hatakuja kwa ajili ya kutufia bali anakuja na utukufu mkuu kuja kuwachukua watu waliookoka kwa kuwanyakua ili tumlaki yeye mawinguni Waebrania 9;28  “ Kadhalika Kristo naye akiisha kutolewa sadaka mara moja azichukue dhambi za watu wengi  atatokea mara ya pili pasipo dhambi kwa hao wamtazamiao kwa wokovu”

 Kwa sasa Kristo amekwenda kutuandalia makao soma Yohana 14;3 ili pale alipo na sisi tuwepo
1Wathsalonike 4;17 Kisha atakuja tena na kutunyakua  ili tumlaki yeye mawinguni  ni siku gani au lini Yesu anakuja kutuchukua swala hili ni siri kwani Kristo atakuja kama mwivi 1Wathesalonike 5;1-4, ujio wa Kristo utakuwa wa ghafla sana  na hakuna mtu ajuaye siku wala saa Mathayo 24;36 Biblia inatuambia kuwa bado kitambo kidogo sana atakuja wala hatakawia Waebrania 10;37

 Ni mambo gani ya kufanya ili kujiandaa na ujio wa Kristo?
·         Dumu katika wokovu ili usiaibike 1Yohana 2;28, Yakobo 5;7-8
·         Kuhakikisha kuwa tunajiweka tayari kila iitwapo leo Luka 12;40

Jinsi ya kujiweka tayari
Mathayo 3;8 Inatupasa kuzaa matunda yapasayo toba  lolote ambalo ni dhambi ni muhimu kuliacha kabisa  ishi maisha yanayoendana na kutubu kwako pia chukua hatua zifuatazo ili kujihadhari na kurudi dhambini
i.                     Punguza urafiki na marafiki wa zamani ulioshirikiana nao katika dhambi Zaburi 119;63. Mithali 22;24-25
ii.                   Waeleze rafiki zako wa zamani kuwa wewe sasa umeokoka , kumbuka kuwa wokovu ni kitu cha thamani hivyo hatupaswi kuuonea aibu Marko 8;38, 1Petro 3;15
iii.                  Endelea kutamani mafundisho ya neno la Mungu ili uweze kuukulia wokovu 1Petro 2;2. “ Kama watoto wachanga waliozaliwa sasa yatamanini maziwa ya akili yasiyoghoshiwa ili kwa hayo mpate kuukulia wokovu”