Mstari wa Msingi. Mithali 1:32-33 Biblia mahali hapo inasema;-
“Maana kurudi nyuma kwao wajinga kutawaua, Na
kufanikiwa kwao wapumbavu kutawaangamiza. Bali kila anisikilizaye atakaa
salama, Naye atatulia bila kuogopa mabaya.”
Ni muhimu kuwa na ufahamu kuwa
sio wakristo wote wanaopata neema ya kuzaliwa mara ya pili au kuokoka wanapata
neema vilevile ya kuukulia wokovu, wengine wanarudi nyuma na hata kufa kiroho
kutokana na sababu mbalimbali, wote tunafahamu kuwa ziko sababu mbalimbali za
kwanini, watu wanarudi nyuma na hatimaye
kufa kiroho, lakini katika somo hili tutajaribu kuchambua chache kati ya hizo.
Hatari ya maisha ya upotevuni, tafadhali baki nyumbani rudi nyumbani
1. KUKOSA MISINGI AU MIZIZI.
Luka 8: 13 Biblia inasema “Na wale penye mwamba ndio wale ambao wasikiapo hulipokea lile
neno kwa furaha; nao hawana mizizi, huamini kitambo kidogo, na wakati wa
kujaribiwa hujitenga.” Ni muhimu kufahamu kuwa mara baada ya kuokolewa
kila mtu aliyeokoka anapaswa kuhakikisha kuwa analifanyia kazi neno la Mungu na
kujijengea juu ya msingi huu, kila mmoja anapaswa kuota mizizi na sio tu kuota
lakini kuhakikisha kuwa mizizi yake inashuka chini sana, tatizo kuu la wakristo
wengi sana wako katika kundi hili linalotajwa na Yesu Kristo kama watu au mioyo
inayolipokea neno la Mungu kwa furaha lakini hawana mizizi, hawaendelei mbele
wanadumaa na hatimaye kuiacha imani, Hawa pia wanaweza kufananishwa na mtu
aliyejenga nyumba yake kwenye Mchanga Mathayo
7:24-27 “.Basi kila asikiaye hayo maneno yangu, na
kuyafanya, atafananishwa na mtu mwenye akili, aliyejenga nyumba yake juu ya
mwamba; mvua ikanyesha, mafuriko yakaja, pepo zikavuma, zikaipiga nyumba ile,
isianguke; kwa maana misingi yake imewekwa juu ya mwamba. Na kila asikiaye hayo
maneno yangu asiyafanye, atafananishwa na mtu mpumbavu, aliyejenga nyumba yake
juu ya mchanga; mvua ikanyesha, mafuriko yakaja, pepo zikavuma, zikaipiga
nyumba ile, ikaanguka; nalo anguko lake likawa kubwa.” Unaweza kuona
tatizo kubwa la wapendwa wengi sio tu kulitendea kazi neno lakini hata
kulielewa hawalielewi,wako wakristo ambao hata hawajui kwanini wanatoa sadaka,
kwa nini wanahudhuria ibada katika kanisa wanalohudhuria, kwa nini wanaomba, kwa
nini wanene kwa lugha? Na wakikutana na changamoto ndogo tu wanakwazika na
kuchanganyikiwa, Hwawezi kuitetea imani, Hawana ujuzi wala uzoefu katika
kutembea na Mungu ni wakristo ambao hawawezi kusema Mungu amezungumza name na
wakikusikia kuwa unasema umezungumza na Mungu wanashangaa, hawana ushuhuda wao
wenyewe.
Mkristo mwenye Misingi imara
anapaswa kusimama mwenyewe haijalishi hata kama mtu aliyekuingiza katika
ukristo amehama imani na kujiunga na imani potofu, yeye anaendelea kusimama kwa
gharama yoyote, wazazi ndugu jamaa au rafiki wa karibu hawezi kubadilisha
msimamo wa mtu mwenye mizizi, utashangaa kuona mtu aliyeokoka hajui hata
tofauti ya Mashahidi wa Yehova na hata wasabato yeye kila aina ya fundisho na
imani na kila aina ya upepo wa Elimu unamzoa tu!
Mkristo mwenye mizizi kamwe hawezi
kuyumbishwa na jaribu la aina yoyote,taarifa mbaya kuhusu kiongozi wako wa
kidini haiwezi kuwa sababu yaw ewe kuiacha imani, unaweza kuwepo kanisani
lakini kama mimani yako haijajengwa kwenye misingi na haijaota mizizi ni rahisi
kujikuta matatani, Dhambi za kiongozi wako wa kidini zinauhusiano gani na
wokovu wako?uwapo duniani je unafikiri unaweza kumuacha Yesu kwa sababu ya
dhambi ya kiongozi wako?mkristo anayeweza kumuacha Yesu kwa sababu ya tatizo la
mtumwingine huyo hana misingi wala hajaota mizizi hajakomaa.
Mkristo aliyesimama vema ni yule
ambaye amesimama hawezi kutikiswa na kurudi nyuma kwa wengine Yohana 6:66-69 “Kwa ajili ya hayo wengi miongoni mwa wanafunzi wake wakarejea nyuma,
wasiandamane naye tena. Basi Yesu akawaambia wale Thenashara, Je! Ninyi nanyi
mwataka kuondoka? Basi Simoni Petro akamjibu, Bwana! Twende kwa
nani? Wewe unayo maneno ya uzima wa milele. Nasi tumesadiki, tena tumejua, ya
kuwa wewe ndiwe Mtakatifu wa Mungu.”
Wanafunzi
wa Yesu wenye msimamo kama Petro hawakuweza kuacha kuandamana na Yesu kwa
sababu walitambua kuwa Yesu anao uzima wa milele, Mtu ambaye hajajengwa kwenye
msingi na hana mizizi kwake ni rahisi kukata tamaa, ni vigumu kwake kupokea
neno gumu na kusonga mbele kwao ni rahisi kukwazika tu na kungung’unika na kurudi
nyuma Biblia haitutii moyo kumfuata kiongozi awaye yote anapokuwa amekengeuka
badala yake inatutia moyo kumfuata Yesu au kumfuata kiongozi kama anamfuata
Yesu pale anapokengeuka sisi tunasonga mbele na Yesu tu, tukimuombea yeye au
kumuacha na ukengeufu wake Paulo mtume alisema tumfuate yeye kama anavyomfuata
Kristo 1Wakoritho 11:1 “Mnifuate mimi kama mimi ninavyomfuata Kristo.” Ukiwa
kiongozi wa kiroho ni rahisi sana washirika wako kukutii katika jambo lolote
utakalowaamuru, wanakutii wanakuheshimu wanakusikiliza, lakini ni muhimu
kuwafundisha washirika wetu kumfuata Yesu na sio mtu au dhehebu, wengi
tumewaharibu washirika katika makanisa kwa sababu ya kuwaaminisha katika
Dhehebu na katika mtu, badala ya Yesu na kuwafanya kuwa wanafunzi wa neno la
Mungu, sisi watumishi wa Mungu ni binadamu na tunauwezekano mkubwa sana wa
kufanya dhambi tena kubwa na za aibu tu, hivyo ni lazima ieleweke wazi kuwa
kama tutawaambia washirika wetu kutenda jambo ambalo sio la kibiblia basi wawe
na uwezo wa kusema hapana kubwa, na kama tutafundisha fundiso lisilo la
kibiblia pia wawe na uwezo wa kutuambia Mchungaji, Mwinjilisti, Nabii, Mtume,
Mwalimu na kadhalika je hili fundisho ni la msingi wa kibiblia?
Pasipo kuwajenga washirika katika
kuwa wanafunzi wa Yesu kumepelekea baadhi ya watumishi wanafikia ngazi hata ya
kuoga na mshirika kwa madai kuwa ni oga takatifu, wengine wameweza kuwaibia
wakristo mali zao zote kwa kisingizio cha kumtolea Bwana, haya na mauchafu
mengine mengi yanaweza kufanyika kwa sababu wakristo wengi wamedumaa kiroho na
hawataki kujijenga juu ya msingi na kuota mizizi mikali katikia imani hivyo
wanazolewa na kila mbwembwe za kila upepo wa kila elimu hata zile zisizo na
uungu ndani yake!
Nikwa sababu kama Hizi Paulo
alisema mnifuate mimi kama ninavyomfuata Kristo hii ni kwa sababu Paulo mtume
alikuwa na uhakika wa mwenedo na tabia yake katika Kristo, alikuwa mwaminifu,
wakristo ni lazima wajifunze neno la Mungu na kuwa na mizizi na kuwa ma misingi
imara ya kutokuyumbishwa na aina yoyote ya ukiroho wa mtu, kumbuka kuwa
kiongozi wa ngazi yoyote ya kiroho anaweza kukengeuka na kurudi nyuma, Je
hatusomi katika maandiko kuwa Haruni aliruhusu makutano kuabudu sanamu Hapo
Musa alipokuwa mlimani kuomba? Musa alipokawia mlimani je Israel wote
hawakugeuka na kushindwa kusimama katika zamu yao na kuabudu miungu ya sananu huku wakisema
kuwa ndio mungu aliyewaokoa katika mikono ya Farao huko Misri? Ni wazi kuwa
watu hawa walikuwa hawajajengeka katika imani, walikuwa hawana msingi na
walikuwa hawana mizizi katika ujuzi wao binafsi na Mungu kumbuka kuwa Mungu si
wa mkumbo, kila mmoja anapaswa kujijengea uzoefu binafsi katika kuwa na
uhusiano wako na Mungu bila kufuata mkumbo.
Mtu mwenye misingi au mizizi hawezi kufuata mkumbo.
Wengi wa walioabudu sanamu Chini
ya uongozi wa Haruni walikuwa ni watu waliofuata mkumbotu, wengi wa
walioangamizwa jangwani walikuwa ni watu walionung’unika kwa sababu ya taarifa
za wapelelezi, kumi waliokosa imani na hawakuwajali wawili waliokuwa na
imanikwa Mungu, wengi pia wa waliomfuata mkumbo wakati Yesu anasulubiwa na
kupiga kelele wakisema asulubiwe asulubiwe hawakuwa na msimamo wao thabiti bali
walikuwa watu walifuata umati au mkumbo, kufuata mkumbo katika kutenda uovu ni
tatizo kubwa sana kwa wakristo wa nyakati za leo hebu komaa kiroho, hebu kataa
kudumaa, hebu kubali kuongozwa na neno na uote mzizi ya ujuzi wako mwenyewe
mfanye Mungu kuwa Mungu wako na neno lake kuwa neno lako, usikubali kwenda kwa
mkumbo Muombe Mungu akupe neema ya kusimama kwa miguu yako na uwe mkristo
mwenye mizizi iliyozama sana chini katika imani.
2. KUWA DEBE TUPU.
1Wakoritho 13:1 “Nijaposema kwa lugha za
wanadamu na za malaika, kama sina upendo, nimekuwa shaba iliayo na upatu uvumao.”
Biblia inazungumzia kuhusu debe
la shaba linalolia na upatu uvumao upatu maana yake ni mwangwi,kwa ujumla
biblia inazunguzmia utupu, bure kutokuwa na kitu, tunapozungumzia wakristo
wenye hatari ya kurudi nyuma au ambao wamedumaa au wamesharudi nyuma inagwa
wako kanisani biblia inazungumzia utupu wa kiroho, hii ni jamii ya wakristo tulionao
leo makanisani bila kujali miaka yao ya wokovu, wala ngazi ya utumishi wako
jambo kubwa la kujiuliza je wamejaa neno la Mungu,? Je wamejaa Roho Mtakatifu? Wanaweza wakawa wananena kwa
lugha lakini tujiulize ni nini faida yake? Je wana upendo? Wanaweza kuwa wana
karama nyingi na wanatumika sana kuwaombea wengine lakini msingi wana nini
katika Mungu? Kuwa debe tupu la kiroho
ni jambo la hatari sana katika maisha ya Ukristo
Shetani anapendezwa sana na
nyumba iliyopambwa na kufagiliwa kisha iko tupu, unapokuwa ntupu kiroho shetani
atatafuta vya kukujaza, Luka 11:24-26
“Pepo mchafu amtokapo mtu, hupitia mahali pasipo maji,
akitafuta mahali pa kupumzika; asipoona, husema,Nitairudia nyumba yangu niliyotoka. Hata afikapo,
akaiona imefagiwa na kupambwa, ndipo huenda akachukua pepo wengine saba, walio
waovu kuliko yeye mwenyewe, wakaingia na kukaa humo; na mtu yule hali yake ya
mwisho huwa mbaya kuliko ya kwanza”.
Mkristo ambaye ni debe tupu ana
maisha hatarishi shetani atatafuta kila namna ili aweze kuhakikisha kuwa
anakujaza mambo yatakayokufanya uwe wa kawaida na kukurudisha nyuma, utajaa
kila namna ya udunia ambayo hujawahi hata kuwa nayo kwa sababu, huna kitu,
lazima mkristo awe mtu aliyejaa kitu na sio debe tupu
Matendo ya mitume 6:5a,8 “Neno hili
likapendeza machoni pa mkutano wote; wakamchagua Stefano, mtu aliyejaa imani na
Roho Mtakatifu, Na Stefano, akijaa neema na uwezo, alikuwa akifanya maajabu na
ishara kubwa katika watu” Unaona kumbe kama mkristo amekuwa debe tupu
anakuwa na kelele tu hakuna kitu cha ziada katika maisha yake, hana imani,
hajai roho, hana neema hana uwezo, wala nguvu za Mungu, wakristo ambao ni debe
tupu na upatu uvumao ni wapiga kelele tu lakini hakuna kitu cha ziada maishani
mwao,watapiga kelele za manunguniko, watapiga kelele za masengenyo, watapiga
kelele za ugomvi, watapiga keleleza elimu zao na nchi walizotembelea lakini
hawana kitu cha ziada , ni muhimu kukumbuka nini tunapaswa kukijaza katika maisha
Yetu, ni lzaima tujaze neno la Mungu maishani mwetu na akilini mwetu, ni lazima
tujae neema na kweli, nilazima tujae hekima ya Mungu, ni lazima tujae Roho
Mtakatifu, ni lazima tujae nyimbo za injili,ni lazima tujae upendo na matendo,
mema na kujaa upendo, tukatae kuwa tupu.
Kwani kinyume chake shetani
atatujaza na matakwa yake na mapenzi yake.
3. KUUPENDA ULIMWENGU.
2Timotheo 4:10 “Maana Dema aliniacha, akiupenda ulimwengu huu wa sasa,
akasafiri kwenda Thesalonike; Kreske amekwenda Galatia; Tito amekwenda Dalmatia.”
Kama mtu akikipenda kitu uko uwezekano mkubwa wa kukifuata, Dema aliupenda
ulimwengu akaacha kufuatana na Paulo mtume anauendea ulimwengu, binti akimpenda
kijana anaaacha wazazi wake na kuambatana na yule kijana kupenda kuna enda na
nguvu ya kufuata au kuambatana
Kama ukiipenda dunia na tamaa
zake, ukipenda fedha, ukipenda anasa, ukipenda wanawake au wanaume, na dunia
yote kwa ujumla utavutwa na kile unachokipenda, Wakristo wanapaswa kutokuvutwa
na kitu kingine nje ya Mungu, na neno lake, ni muhimu kupenda kile kilicho cha
Muhimu ikiwa ni pamoja na Mungu, mkeo au mumeo na watoto nk kulingana na
mapenzi ya Mungu kamwe usiruhusu aina nyingine ya upendo ulio kinyume na
mapenzi ya Mungu, 1Yohana 2:15-16 “Msiipende dunia,
wala mambo yaliyomo katika dunia. Mtu akiipenda dunia, kumpenda Baba hakumo
ndani yake. Maana kila kilichomo duniani, yaani, tamaa ya mwili, na tamaa ya
macho, na kiburi cha uzima, havitokani na Baba, bali vyatokana na dunia”.
-
Kutokuipenda dunia maana yake ni nini ?
kutokusahau kuwa dunia sio makazi yetu ya kudumu sisi ni wapitaji tu hatupaswi
kujisahau na kufikiri tutaishi duniani milele hivyo ni lazima kuzingatia na
kujiandaa kwa maandalizi ya makazi yetu ya milele mbinguni Wakolosai 3:1-2 “Basi mkiwa mmefufuliwa
pamoja na Kristo, yatafuteni yaliyo juu Kristo aliko, ameketi mkono wa kuume wa
Mungu. Yafikirini yaliyo juu, siyo yaliyo katika nchi” Lazima kila
mkristo anayetaka kusonga mbele awe na muda wa kumtafakari Yesu Kristo, na
kukumbuka kuwa kazi aliyoifanya msalabani sio ya bure, sio hilo tu lakini
tunapaswa kuishi duniani kama wasafiri na sio watu wenye makazi Waebrania 11:9-10 “Kwa imani alikaa ugenini katika ile nchi ya ahadi, kama
katika nchi isiyo yake, akikaa katika hema pamoja na Isaka na Yakobo, warithi
pamoja naye wa ahadi ile ile. Maana alikuwa akiutazamia mji wenye misingi,
ambao mwenye kuubuni na kuujenga ni Mungu.”
-
Wala vilivyomo ndani yake au tamaa zake hapa
biblia inazungumzia kila kinachoonekana kuwa raha katika dunia kinachoweza
kutufunga ni lazima kujihadhari, hatupaswi kujitoa kwa vitu vilivyomo duniani
ukilinganisha na jinsi tunavyopaswa kujitoa kwa vitu vya Mungu, kutokuutii
mwili katika kila kinachohitajika nao 1Petro
2:11 “Wapenzi, nawasihi kama wapitaji na wasafiri,
ziepukeni tamaa za mwili zipiganazo na roho.”
-
Kutokufanya urafiki na waasi “Mtu akiipenda dunia kumpenda baba hakumo ndani yake” Yakobo 4:4 “Enyi
wazinzi, hamjui ya kwamba kuwa rafiki wa dunia ni kuwa adui wa Mungu? Basi kila
atakaye kuwa rafiki wa dunia hujifanya kuwa adui wa Mungu.” Aidha maandiko yanaonya vikali
kufungiwa nira na wasioamini 2Wakoritho
6:14-18 “Msifungiwe nira pamoja na wasioamini, kwa
jinsi isivyo sawasawa; kwa maana pana urafiki gani kati ya haki na uasi? Tena
pana shirika gani kati ya nuru na giza? Tena pana ulinganifu gani kati ya
Kristo na Beliari? Au yeye aaminiye ana sehemu gani pamoja na yeye asiyeamini?
Tena pana mapatano gani kati ya hekalu la Mungu na sanamu? Kwa maana sisi tu
hekalu la Mungu aliye hai; kama Mungu alivyosema, ya kwamba, Nitakaa ndani yao,
na kati yao nitatembea, nami nitakuwa Mungu wao, nao watakuwa watu wangu. Kwa
hiyo, Tokeni kati yao, Mkatengwe nao, asema Bwana, Msiguse kitu kilicho
kichafu, Nami nitawakaribisha. Nitakuwa Baba kwenu, Nanyi mtakuwa kwangu
wanangu wa kiume na wa kike”
-
Aidha kupenda fedha kuliko Mungu au kuacha
fedha itutawale maisha yetu, mfano tukiwa nayo na tukiwa hatuna hisia zetu
zinakuwaje? 1Timotheo 6:6-10 “6. Walakini utauwa pamoja na kuridhika ni faida kubwa. Kwa maana
hatukuja na kitu duniani, tena hatuwezi kutoka na kitu; ila tukiwa na chakula
na nguo tutaridhika na vitu hivyo. Lakini hao watakao kuwa na mali huanguka
katika majaribu na tanzi, na tamaa nyingi zisizo na maana, zenye kudhuru,
ziwatosazo wanadamu katika upotevu na uharibifu. Maana shina moja la mabaya ya
kila namna ni kupenda fedha; ambayo wengine hali wakiitamani hiyo wamefarakana
na Imani, na kujichoma kwa maumivu mengi”.
Ni hatari sana kupenda kwa tamaa,
ni hatari kudharau kanuni za Mungu kwa sababu ya maswala ya ulimwengu huu, wako
vijana wasichana ambao wanashauku na hamu kubwa sana ya kuolewa kiasi ambacho
wako tayari kuvunja kanuni na sheria na kukubali kufanya lolote eti ili mradi
waolewe, kupenda kitu kwa tamaa ni kuwa na shauku yenye nguvu kuelekea kitu
hicho, ni tamaa ya kutaka kukifikia kitu hicho kwa namna isiyoweza kuzuilika
tamaa ya aina hii haifugiki, watu wanaweza kufikia ngazi ya kutaka kushindana
na wengine kwa sababu ya tamaa, tamaa ni shina la mabaya mengi hatuna budi
kujihadhari nayo na kumpenda Mungu na kufanya kazi zetu kwa bidii kwa kadiri ya
neema Mungu aliyotupa. Rafiki yangu mmoja mwimbaji wa nyimbo za Injili alikuwa
akinisimulia jinsi kama mwimbaji mzuri wa nyimbo za injili na mrembo, mwenye
umbile zuri, kiuno kizuri, na amejengeka kwa sifa zote za uzuri ananiambia mkuu
wa wajenzi, majaribu ya kuinuliwa ni magumu sana mtu mmoja ananiambia nitakupa
milioni 20 ukikubali kulala name kwa usiku mmoja tu. “I will give you 20 TZshs
Million per one night of staying with me” Unaweza kuona je ungekuwa wewe
ungechagua nini Hapo Fedha au Kumuacha Mungu, huu ndio ulimwengu. Ni lazima
tumuombe Mungu atuokoe na tamaa za ulimwenguni katika sala ya bwana kula ile
sentensi usitutie majaribuni lakini utuokoe na yule muovu hapa ndipo
inapohitajika aina hii ya sala 2Petro1:4
“Tena kwa hayo ametukirimia ahadi kubwa mno, za
thamani, ili kwamba kwa hizo mpate kuwa washirika wa tabia ya Uungu, mkiokolewa
na uharibifu uliomo duniani kwa sababu ya tamaa”.
4. UCHUNGU.
Waebrania 12: 14-15 “Tafuteni kwa bidii
kuwa na amani na watu wote, na huo utakatifu, ambao hapana mtu atakayemwona
Bwana asipokuwa nao; mkiangalia sana mtu asiipungukie neema ya Mungu; shina la
uchungu lisije likachipuka na kuwasumbua, na watu wengi wakatiwa unajisi kwa
hilo”.
Uchungu uchungu uchungu umeharibu
watu wengi sana, makanisani na kila mahali watu wameharibu mahusiano kwa sababu
ya uchungu, wengine wamejitenga na kuiacha imani kwa sababu ya kufanyiwa mambo
ya uchungu, wengine wamedai au kutoa talaka kwa sababu ya uchungu, wengine
wameacha kazi kwa sababu ya kutendewa mambo machungu Biblia inataadharisha kuwa
neema inaweza kupunguka, yaani ule uwezo wa kustahimili kwa sababu ya kutendewa
machungu? Je kama Mkristo unapotendewa mambo machungu unafanya nini? Wengine walianzisha madhehebu yao kwa sababu
ya kukimbia kutendewa mambo machungu na wengine wamerudi nyuma kwa sababu ya
kutendewa mambo machungu Biblia inatufundisha kuwa Yusufu alitendewa Machungu
lakini kutokana na uvumilivu wake alipokea Baraka nyingi na kuwa mtawala dhidi
ya ndugu zake Mwanzo 49:22-26 “Yusufu ni mti mchanga
wenye kuzaa, Mti mchanga wenye kuzaa karibu na chemchemi, Matawi yake yametanda
ukutani. Wapiga mishale walimtenda
machungu, Wakamtupia, wakamwudhi, Lakini upinde wake ukakaa imara, Mikono yake
ikapata nguvu, Kwa mikono ya Mwenye Enzi wa Yakobo; Kwa jina la mchungaji, yeye
jiwe la Israeli, Naam, kwa Mungu wa baba yako atakayekusaidia; Kwa mibaraka ya
mbinguni juu. Mibaraka ya vilindi vilivyo chini, Mibaraka ya maziwa, na ya
mimba. Mibaraka ya baba yako Imepita mibaraka ya milima ya kale, Vitu
vinavyotamanika vya vilima vya milele; Na vikae juu ya kichwa cha Yusufu, Juu
ya utosi wa kichwa chake aliye mkuu kati ya ndugu zake”. Uchungu
umeumiza wengi uko ushuhuda wa Pastor Dag Heward aliyeanzisha huduma yake kule
Ghana anaeleza katika moja ya vitabu vyake sababu ya watu kuhama makanisa yao
na kwenda kujiunga au kuanzisha mengine ni pamoja na watu kuwa na uchungu,
Pastor Dag anasema wengine hawakuwahi hata kuhudhuria harusi yake ingawa
aliwaalika, Nakumbuka mchungaji wangu Zacharia Kakobe wakati mwingine alikuwa
akihudhuria mikutano ya wachungaji na kukaa pamoja nao alijikuta kila Mchungaji
ameondoka na kuhama alipokuwa amekaa, wengi wlimuita npepo na wengine walisema
anatumia nguvu za giza na wengine walimsema kuwa ni imani potofu, Niliwahi
kuhudhuria kanisa moja na nilipojitambulisha kuwa mimi ni mshirika wa Full
Gospel Bible Fellowship na tulipotoka ibadani hakuna mtu alinisalimia kwa
mkono, wengi walikuwa wakinong’ona kuwa ametokea kanisa lenye imani potofu, je
we umewahi kutendewa mambo machungu? Je umeweza kusamehe au unadhuru wengine
kutokana na uchungu? Mchungaji wangu Msaidizi aliwahi kuzusha kuwa nilitaka
kumbaka, na nikauhukumiwa na Askofu wangu wa jimbo kwa kutengwa miezi mitatu,
ulipotimia wakati wa kufunguliwa nilimuendea Mchungaji na askofu wangu na
kuomba anifungue lakini aliniambia kazi bado nakuongeza kifungo cha mwaka mmoja
zaidi, ulikuwa ni wakati mgumu, nilinyimwa mshahara, familia iliteseka mke
wangu aliuza maandazi, kanisa lilinipa elfu 50 tu kwa mwezi,nilipoteza haki
zangu zote sikulipwa kipato chochote katika miaka tisa niliyolitumikia kanisa, Nilijiuliza hivi kweli kuna wokovu? Hivi huu
ndio Ukristo, Lakini Mungu Roho Mtakatifu aliniambia usiniache mimi nitakuwa
pamoja nawe, nitakuwa ngao yako na thawabu yako kubwa sana nitakuongoza kila
utakako kwenda, nilitiwa moyo tu kujua kuwa Mungu yuko name, huu ndio ulikuwa
wakati rahisi kurudi nyuma, lakini misingi thabiti ya kujua neno na kujua kuwa
askofu pia ni wanadamu ilinipa nguvu kusonga mbele, uchungu uchungu uchungu?
Hatupaswi kurudi nyuma au kujiua kwa sababu ya uchungu badala yake na tusonge
mbele, “Usimlaumu mtu yeyote katika maisha, watu wazuri watakupa furaha, watu
wema watakufanya ukumbuke, watu wabaya watakupa uzoefu, na watu waovu
watakufundisha adabu,” Hatuwezi kumuacha Yesu kwa sababu ya watu wabaya. Siku
hizi ninauwezo wa kucheka watu wanaponitendea uchungu na kumwambia Mungu sasa
kuna level gani nyingine unataka kunipeleka mzee najua una mazuri mengine zaidi
hivyo ninafurahi.
5. MAISHA YA DHAMBI.
Mfano wa mwana mpotevu ni mfano
dhahiri wa mwana aliyetaka uhuru, aliyetaka kuishi kwa kujitegemea, mbali na
sheria za nyumbani, mbali na kibano, mali na kupangiwa mbali na kuwaziwa, mbali
na kuelekezwa,mbali na uwepo wa baba, mwana mpotevu alitaka kuwa huru kuishi
maisha ya dhambi, hatuwezi kujua ushawishi huu ulitoka wapi, lakini huenda marafiki
wabaya walichangia kumshauri vibaya Biblia inasema hivi Mithali 1:10 “Mwanangu, wenye dhambi
wakikushawishi, Wewe usikubali.” Maana yake ni kuwa kama u mcha Mungu ni
muhimu kwako kuchukua hatua stahiki ya kuacha kuambatana na watu waovu wenye
ushawishi, hatuwezikabisa kuhama ulimwenguni lakini ni muhimu kwako kuhakikisha
kuwa unajihadhari na ushawishi utakaokurudisha tena katika kuishi maisha ya
dhambi, au kuona kila kinachofanyika kuwa ni cha kawaida tu, 1Wakoritho 15:33 “Msidanganyike; Mazungumzo mabaya huharibu tabia njema”
ni Muhimu kufahamu kuwa katika biblia ya kiingereza neno mazungumzo linalotajwa
hapo linasomeka hivi kwa mfano NIV na matoleo mengine ya kiingereza yanatumia
neno “Bad Company” ambalo lingemaanisha marafiki wabaya, kumbe wakati mwingine watu wanaweza kuishi
maisha ya dhambi kutokana na mazingira yanayokuzunguka au kutokana na marafiki
na ushawishi ili mkristo aweze kudumu katika imani ni lazima ahakikishe kuwa
anavunja urafiki na watu waovu, Maisha ya dhambi yanaweza kuahribu ushirika
wako na Mungu hiki ndicho kilichotokea kwa mwana mpotevu Luka 15: 11-19 “Akasema, Mtu mmoja alikuwa
na wana wawili; yule mdogo akamwambia babaye, Baba, nipe sehemu ya mali
inayoniangukia. Akawagawia vitu vyake. Hata baada ya siku si nyingi, yule mdogo
akakusanya vyote, akasafiri kwenda nchi ya mbali; akatapanya mali zake huko kwa
maisha ya uasherati. Alipokuwa amekwisha tumia vyote, njaa kuu iliingia nchi
ile, yeye naye akaanza kuhitaji. Akaenda akashikamana na mwenyeji mmoja wa nchi
ile; naye alimpeleka shambani kwake kulisha nguruwe. Akawa akitamani
kujishibisha kwa maganda waliyokula nguruwe, wala hapana mtu aliyempa kitu.
Alipozingatia moyoni mwake, alisema, Ni watumishi wangapi wa baba yangu
wanaokula chakula na kusaza, na mimi hapa ninakufa kwa njaa. Nitaondoka,
nitakwenda kwa baba yangu na kumwambia, Baba, nimekosa juu ya mbingu na mbele
yako; sistahili kuitwa mwana wako tena; nifanye kama mmoja wa watumishi wako”
unaweza kuona katika mfano huu, maisha ya kutaka kuwa huru,ubinafsi na
majaribio yenye kuhatarisha vinaweza kukuleta katika maisha yenye majuto sana
Neema ya Mungu bado iko ni kwa toba ya kulia na kujuta kutoka moyoni tunaweza
kurejea tena katika ushirika na Mungu,
ingawa ni vema zaidi kama hatutauvunja ushirika huo na kuendelea kushikamana na
utimilifu wetu hata mwisho.
Wakristo wanaoishi katika maisha
ya dhambi pia hawawezi kufurahia kanisa ambalo linakaza kukataza dhambi,
hawawezi kujisikia salama kuweko mahali ambako dhambi zinakemewa,wanaweza
kusema sihitaji kumsikia muhubiri huyu mwenye mahubiri ya kizamani,sitaki
kumsikiliza Mchungaji yule na mambo yake ya kuvuana nguo hawataki kukemewa
wanahitaji jumbe za kuwatia moyo tu ukianza kunyoosha wanakuchukia kama uko
safi hutaogopa kukemewa ni muhimu kukubali kukemewa, kurudiwa na kuonywa hali
hii ndio itakayotupeleka kwenye uzima Waebrania
12:4-10 “Hamjafanya vita hata kumwagika damu,
mkishindana na dhambi; tena mmeyasahau yale maonyo, yasemayo nanyi kama kusema
na wana, Mwanangu, usiyadharau marudia ya Bwana, Wala usizimie moyo ukikemewa
naye; Maana yeye ambaye Bwana ampenda, humrudi, Naye humpiga kila mwana
amkubaliye. Ni kwa ajili ya
kurudiwa mwastahimili; Mungu awatendea kama wana; maana ni mwana yupi
asiyerudiwa na babaye? Basi kama mkiwa hamna kurudiwa, ambako ni fungu la wote,
ndipo mmekuwa wana wa haramu ninyi, wala si wana wa halali. Na pamoja na hayo
tulikuwa na baba zetu wa mwili walioturudi, nasi tukawastahi; basi si afadhali
sana kujitia chini ya Baba wa roho zetu na kuishi? Maana ni hakika, hao kwa
siku chache waliturudi kama walivyoona vema wenyewe; bali yeye kwa faida yetu,
ili tuushiriki utakatifu wake”. Nimuhimu kufahamu kuwa kukemewa ni
sehemu ya injili, kukemea zinaa, uongo, wizi, ujambazi, masengenyo, uchawi,
uadui, ugomvi, uzushi, na kila aina ya uovu ni sehemu ya injili, kanisa lolote
linalohubiri kweli bila kutia maji ni lazima waikemee dhambi, tabia endelevu ya
kuishi katika dhambi itatupelekea katika kurudi nyuma na kupoteza neema ya
Mungu.
6. UONGO
Uwongo ni dhambi, watu wengi sana
hujifunza kusema uongo tangu utoto, tunapookoka biblia inatutaka tuache kabisa
uongo na kuambiana ukweli, Mwanzo
37:31-35 “Wakaitwaa kanzu ya Yusufu, wakachinja
mwana-mbuzi, na kuichovya kanzu katika damu. Wakaenda nayo ile kanzu ndefu,
wakamletea baba yao, wakasema, Tumeona hii; basi, utambue kama kanzu hii ni ya
mwanao, ama siyo. Akaitambua, akasema, Ndiyo kanzu ya mwanangu, mnyama mkali
amemla; bila shaka Yusufu ameraruliwa. Yakobo akararua mavazi yake, akajivika
gunia viunoni, na kumlilia mwanawe siku nyingi. Wanawe wote, na binti zake
wote, wakaondoka wamtulize, lakini akakataa kutulizwa, akasema, La! Nitamshukia
mwanangu, nikisikitika, hata kuzimu. Baba yake akamlilia” Kabla ya
mabadiliko makubwa wana wa Israel walikuwa waongo, waliweza hata kumdanganya
baba yao kwa kupatana kwamba mtoto ameliwa na mnyama mkali, Israel alilia kwa
siku nyingi kwa uchungu na masikitiko kumbe alikuwa amedanganywa nilikuwa
nawaza inawezekanaje kutokuwa na huruma kwa
watoto wa mzee Yakobo walimuacha baba yao aamini uongo kwa muda mrefu
walikula matanga na kuomboleza msiba ambao hawakuwa na uhakika nao, watu wa
Mungu ni muhimu kukumbuka kutokudanganyana, kusema ukweli, na kuacha kusemezana
uongo, Wakolosai 3: 9-10 “Msiambiane uongo, kwa kuwa mmevua kabisa utu wa kale, pamoja
na matendo yake; mkivaa utu mpya, unaofanywa upya upate ufahamu sawasawa na
mfano wake yeye aliyeuumba”. Mungu ni mkweli hatupaswi kamwe kusema
uongo, Afrika inafahamu sana uongo wa wamisionari waliokuja kuleta dini,
walifundisha kuwa msiibe lakini wao walituibia madini, pembe za ndovu na mali
nyingi sana zilizokuwepo Afrika wakati huo, hii ilisababisha baadhi ya maeneo
afrika kuwa na ukristo mbaya, Kila alitajaye jina la Bwana na auache uovu, Maisha
ya wamishionari yanaangaliwa sana na wale wanao wahubiri, hivyo nilazima kuwa
wakweli, watu wote waseme kweli biblia ni ya wote Mungu anachukizwa na uongo
vilevile. “Kule Kenya Mzee Jomo Kenyata alisema walituletea Biblia lakini wao
wakachukua ardhi yetu” kwa sababu ya mfano mbaya wa wakristo wamisionari
waliotangulia Afrika imeathiriwa lakini sasa hakuna udhuru ni lazima tusimamem
katika kweli bilamkuwa na visingizio Mithali 6:16-17 “Kuna vitu sita anavyovichukia Bwana; Naam, viko saba vilivyo
chukizo kwake. Macho ya kiburi, ulimi wa uongo, Na mikono imwagayo damu isiyo
na hatia; Moyo uwazao mawazo mabaya; Miguu iliyo myepesi kukimbilia maovu;
Shahidi wa uongo asemaye uongo; Naye apandaye mbegu za fitina kati ya ndugu”. Unaona ni muhimu kwetu tuakajifunza
kuwa wakweli, kweli ni silaha mojawapo ya Mkristo kumshinda shetani Waefeso 6: 10 - 14. “Hatimaye, mzidi kuwa hodari katika
Bwana na katika uweza wa nguvu zake. Vaeni silaha zote za Mungu, mpate kuweza
kuzipinga hila za Shetani. Kwa maana
kushindana kwetu sisi si juu ya damu na nyama; bali ni juu ya falme na mamlaka,
juu ya wakuu wa giza hili, juu ya majeshi ya pepo wabaya katika ulimwengu wa
roho. Kwa sababu hiyo twaeni silaha zote za Mungu, mpate kuweza kushindana siku
ya uovu, na mkiisha kuyatimiza yote, kusimama. Basi simameni, hali mmejifunga
kweli viunoni, na kuvaa dirii ya haki kifuani,” hatuwezi kuwa na nguvu na mamlaka kama tunasema uongo ni muhimu
kwetu kujifunza na kukubali kubadilika na kuwa kweli katika maisha yetu ya
Ukristo ni lazima tujihoji wenyewe je sisi ni waaminifu?,sisi ni wakweli? Je
tunakubali kutubu tunapokosea? Je tunakasirika tunapoambiwa ukweli wakati
umefika sasa wa kuacha kusema uongo na kusema kweli.
7. KUASI
Dhambi moja tu katika biblia
inafananishwa na uchawi, dhambi hii ni dhambi ya kuasi,kuasi kwa ufupi ni
kushindana na kupinzana na kupingana na mamlaka iliyoko, wakati wote vikundi
vya aina hii vinavyopigana na serikali kwa sababu ya madai kadhaa kama mfano
hapa Afrika vimepewa jina la waasi, Hali kadhalika watu waliomtii Mungu huitwa
wana wa kutii na kinyume chake watu wanaomuasi Mungu huitwa wana wa kuasi 1Petro 1:14 “Kama
watoto wa kutii msijifananishe na tamaa zenu za kwanza za ujinga wenu;” Biblia
inawaita watoto wa Mungu kama watoto wa kutii lakini wakati mwingine hutokea
watoto wa Mungu wakamuasi, uasi ni dhambi mbaya sana na inakwamisha watu kupata
neema ya Mungu, uasi unaleta kukataliwa adhabu ya uasi au uhahini mara zote
huwa ni kifo hakuna rehema kwa muasi 1Samuel
15:22-23 “Naye Samweli akasema, je! Bwana huzipenda
sadaka za kuteketezwa na dhabihu Sawasawa na kuitii sauti ya Bwana? Angalia,
kutii ni bora kuliko dhabihu, Na kusikia kuliko mafuta ya beberu. Kwani kuasi
ni kama dhambi ya uchawi, Na ukaidi ni kama ukafiri na vinyago; Kwa kuwa
umelikataa neno la Bwana, Yeye naye amekukataa wewe usiwe mfalme.” Unaweza kuona watu wanaweza kuasi makanisa yao
na kuanzisha huduma, washirika wanaweza kuasi kanisa lao na kuhamia kanisa
lingine, Wachungaji wanaweza kuasi na kufungua makanisa mengine, wachungaji
wasaidizi wanaweza kuasi na kufanya mambo mengine, wana ndoa wanaweza kuasi na
kutoka nje ya ndoa zao, na kupeana talaka, na kuolewa na waume au kuoa wake
wengine, watoto wanaweza kuasi, wazazi wao, Mwana mpotevu pia anaweza kuingia
katika kundi la kuasi, Absalom alimuasi babaye Daudi, Shimei,na Ahithofeli,
shetani pia aliasi mbinguni uasi uliwanyima Israel nafasi ya kuingia kanaani ,
unapoasi sasa anayekuwa adui yako sasa sio shetani bali Mungu na Roho wake
mtakatifu wanapigana nawe, uasi unaanzia moyoni, uasi unaambukiza na unaenea na
kusambaa kwa haraka, Isaya 63:9-10 “Katika mateso yao yote yeye aliteswa, na malaika wa uso wake
akawaokoa; kwa mapenzi yake, na huruma zake, aliwakomboa mwenyewe; akawainua,
akawachukua siku zote za kale. Lakini wakaasi, wakamhuzunisha Roho yake
Mtakatifu; kwa hiyo akawageukia, akawa adui, akapigana nao.” Kufanya
uasi ni kujiweka katika wakati mgumu sana hatuwezi kupigana na Roho Mtakatifu
kisha tukafikiri kuwa tunaweza kufanikiwa,
Katika ujuzi wa kimungu unapojikweza Mungu anakupinga na kuondoa neema
yake kwako 1Petro 5:5-6 “Vivyo hivyo ninyi vijana, watiini wazee. Naam, ninyi nyote
jifungeni unyenyekevu, mpate kuhudumiana; kwa sababu Mungu huwapinga wenye
kiburi, lakini huwapa wanyenyekevu neema. Basi nyenyekeeni chini ya mkono wa
Mungu ulio hodari, ili awakweze kwa wakati wake;” Mungu huwapinga wenye
kiburi yaani waasi na kuwapa neema wanyenyekevu yaani watii, watu wengi sana
wamepoteza neema ya Mungu kwa sababu ya kuasi , Uasi ndio dhambi kuu ya
shetani. Hii inasababisha kurudi nyuma na hata kufa Kiroho na kutokufanikiwa.
Mungu alikataa kabisa ombi la Musa na haruni kutaka kuiona Kanaani na mara
kadhaa Mungu aliwakumbusha kosa lao la kuasi, Mungu anaweza kusahau dhambi zote
lakini anakumbuka sana mtu anapoasi Bwana atupe neema ya kuachan na uasi na
kuwa mbali nao katika jina la Yesu. Ukweli ni kuwa watu wengi katika biblia
waliasi na walilipa gharama kubwa sana wengine walikufa Jangwani na Yona nabii
alimezwa na Nyangumi Zaburi ya 68:6 “Biblia inasema
“Mungu huwakalisha wapweke nyumbani; Huwatoa wafungwa wakae hali ya kufanikiwa;
Bali wakaidi hukaa katika nchi kavu” Neno wakaidi hapo linatumika pia
kama “the rebellious dwell in a dry land” yaani waasi Mungu huwapa waasi
ukavu,jangwa, njaa wanakaukiwa kiroho uhusiano na Mungu unakufa na hakuna
uamsho katika roho zao, wanaishi maisha ya huzuni na vifungo vya aina
mbalimbali, ee Mungu tuokoe na dhambi ya uasi.
8. UZEMBE/ UJINGA./UPUMBAVU.
Biblia ina maneno magumu sana kwa
mtu aliyerudi nyuma anu kudumaa kiroho, hakuna maneno ya kutia moyo kwa mkristo
anayemuacha Yesu, watu wengi sana wanapoishi maisha ya dhambi hujifikiri kuwa
wao ni wajanja lakini biblia inamuita mtu anayerudi nyuma kama mjinga na mpumbavu
mimi naita uzembe, Mithali 1: 32-33 ““Maana kurudi nyuma
kwao wajinga kutawaua, Na kufanikiwa kwao wapumbavu kutawaangamiza. Bali kila
anisikilizaye atakaa salama, Naye atatulia bila kuogopa mabaya.”
Unaweza kuona na Yesu anaongezea maneno magumu zaidi kwa mtu asiyelifanyia kazi
neno lake anamuita Mpumbavu Mathayo 7:26-27
“Na kila asikiaye hayo maneno yangu asiyafanye,
atafananishwa na mtu mpumbavu, aliyejenga nyumba yake juu ya mchanga; mvua
ikanyesha, mafuriko yakaja, pepo zikavuma, zikaipiga nyumba ile, ikaanguka;
nalo anguko lake likawa kubwa.” Mtu aliyeokolewa akiacha kujiandaa kwa
maswala ya Mungu na akawa anaiwaza dunia kana kwamba atakaa humo milele biblia
haina muda wa pongezi dhidi ya mtu huyo bali anaitwa mpumbavu Luka 12:16-21 16. “Akawaambia mithali, akisema, Shamba la mtu mmoja tajiri
lilikuwa limezaa sana; akaanza kuwaza moyoni mwake, akisema, Nifanyeje? Maana
sina pa kuyaweka akiba mavuno yangu.
Akasema, Nitafanya hivi; nitazivunja ghala zangu, nijenge nyingine kubwa
zaidi, na humo nitaweka nafaka yangu yote na vitu vyangu. Kisha, nitajiambia,
Ee nafsi yangu, una vitu vyema vingi ulivyojiwekea akiba kwa miaka mingi;
pumzika basi, ule, unywe, ufurahi. Lakini Mungu akamwambia, Mpumbavu wewe,
usiku huu wa leo wanataka roho yako! Na vitu ulivyojiwekea tayari vitakuwa vya
nani? Ndivyo alivyo mtu ajiwekeaye nafsi yake akiba, asijitajirishe kwa Mungu.”
Neno la Mungu halina lugha nyepesi kwa mtu anayerudi nyuma zaidi ya neno
upumbavu na ujinga kumuacha Yesu na kuigeukia Dunia ni ujinga ni upumbavu mimi
nasema ni uzembe wa hali ya juu 2Petro
2:20-22 Biblia inasema maneno magumu zaidi angalia “Kwa maana wale waliokwisha kuyakimbia machafu ya dunia kwa kumjua Bwana na
Mwokozi Yesu Kristo, kama wakinaswa tena na kushindwa, hali yao ya mwisho
imekuwa mbaya kuliko ile ya kwanza. Maana ingekuwa heri kwao kama wasingaliijua
njia ya haki, kuliko kuijua, kisha kuiacha ile amri takatifu waliyopewa. Lakini
imetukia kwao sawasawa na ile mithali ya kweli, Mbwa ameyarudia matapiko yake
mwenyewe, na nguruwe aliyeoshwa amerudi kugaa-gaa matopeni”. Uwiii Mungu atusaidie Mithali ya kweli Mbwa
anayekula matapishi yake mwenyewe au nguruwe aliyeoshwa kugaa gaa matopeni”
Ndugu nyangu kumbe kurudi nyuma
ni upumbavu, ni ujinga ni kujikosesha Baraka za Mungu afadhali uendelee kukaa
na Yesu, na kumshikilia kamwe usiwaze kumuacha ni afadhali uendelee kushikamana
na Bwana endapo utetenda dhambi hakuna njia ya mkato tubu yeye ni mwaminifu
lakini usimuasi Bwana na kurejea nyuma
Na mkuu wa wajenzi mwenye Hekima
Rev.Innocent Kamote.