Alhamisi, 1 Oktoba 2026

Mtu akiwa ndani ya Kristo!

 


2Wakorintho 5:16-17 “Hata imekuwa, sisi tangu sasa hatumjui mtu awaye yote kwa jinsi ya mwili. Ingawa sisi tumemtambua Kristo kwa jinsi ya mwili, lakini sasa hatumtambui hivi tena. Hata imekuwa, mtu akiwa ndani ya Kristo amekuwa kiumbe kipya; ya kale yamepita tazama! Yamekuwa mapya.”



Utangulizi:

Paulo mtume alikuwa anaandika waraka huu kwaajili ya kuitetea huduma yake ya upatanisho ambayo Mungu ameifanya kupitia Yesu Kristo, anaeleza jinsi ambavyo kifo cha Yesu Kristo na ushindi wake dhidi ya kifo jinsi unavyobadili kabisa maisha ya mwanadamu hususani wale wanaomuamini Yesu Kristo kama Bwana na mwokozi wa maisha yao, mtu huyo sio tu anaboreshwa au kukarabatiwa lakini ni ukweli ulio wazi kuwa amekuwa kiumbe kipya kisicho na historia ya kale au zamani zilizopita

Yohana 1:12-13 “Bali wote waliompokea aliwapa uwezo wa kufanyika watoto wa Mungu, ndio wale waliaminio jina lake; waliozaliwa, si kwa damu, wala si kwa mapenzi ya mwili, wala si kwa mapenzi ya mtu, bali kwa Mungu.”

Pamoja na mambo mengine leo tutachukua muda wa kutosha kutafakari fungu hili la msingi Mtu akiwa ndani ya Kristo amekuwa kiumbe kipya ya kale yote yamepita tazama yamekuwa mapya kwa kuzingatia vipengele muhimu vikuu vitatu vifuatavyo:-

·         Tangu sasa hatumjui mtu awayeyote kwa jinsi ya mwili.

·         Ingawa sisi tumemtambua Kristo kwa jinsi ya mwili, lakini sasa hatumtambui hivi tena

·         Mtu akiwa ndani ya Kristo.

Tangu sasa hatumjui mtu awayeyote kwa jinsi ya mwili.

2Wakorintho 5:16 “Hata imekuwa, sisi tangu sasa hatumjui mtu awaye yote kwa jinsi ya mwili. Ingawa sisi tumemtambua Kristo kwa jinsi ya mwili, lakini sasa hatumtambui hivi tena.”

Paulo mtume anaonyesha jinsi ambavyo injili ya Kristo ikipokelewa na mwanadamu inauwezo wa kufanya mageuzi makubwa ya kutisha na kushangaza, anaeleza kuwa mtu aliyeokolewa anakuwa na mtazamo mpya kabisa anapowatazama wenzake ambao wameokolewa, sijui wewe unamtazamaje mtu ndugu katika Bwana aliyeokoka lakini hiki ndicho Paulo mtume anachokitazama linapokuja swala la ndugu zake katika Bwana, Yeye hamwangalii mtu kwa jinsi ya mwili, Kulikuwa na shida katika Kanisa la Korintho Kanisa ambalo lilianzishwa na Paulo mwenyewe lakini kwa sababu ya changamoto za uchanga wao wa kiroho wako watu ambao walikuwa wanamkosoa na kumuona kama mtu asiye na uwezo wa kuzungumza kwa ufasaha, mtu ambaye ni mwoga kwa kuwa alijitegemea kifedha alipokuwa Korintho, mtu dhaifu, mwenye historia ya kuliudhi Kanisa mwoga, anapokuwa katika mwili lakini mkali anapoandika nyaraka zake, baadhi walimuona kama kiongozi wa kiroho mwenye mamlaka kamili na wakasema sisi ni wa Paulo, wengine walimuona sio mzungumzaji mzuri kwa sababu Wakorintho walikuwa wameathiriwa na tamaduni za Kigiriki zilizokuwa zikiheshimu wanenaji wazuri na wenye hekima, na walimuona yeye kuwa sio mzungumzaji kama hao,(wanafalsafa) na wengine walitilia mashaka utume wake,  kwa sababu hakuwa miongoni mwa wanafunzi walioambatana na Yesu alipokuwa duniani kabla ya kupaa mbinguni, akijibu hoja hizo katika waraka huu Paulo anaonyesha jinsi mtu aliyeokoka kwanza anavyopaswa kuwaangalia watu wengine, yeye anasema, mtu aliyebadilishwa na Yesu Kristo hamwangalii mtu yeyote kwa jinsi ya mwili neno hili lina maana gani hasa? Hebu tuone na kufanya uchunguzi wa kimaandiko kupata maana husika!

2Wakorintho 5:16 “Hata imekuwa, sisi tangu sasa hatumjui mtu awaye yote kwa jinsi ya mwili. Ingawa sisi tumemtambua Kristo kwa jinsi ya mwili, lakini sasa hatumtambui hivi tena.”

Maneno “Hata imekuwa, sisi tangu sasa hatumjui mtu awaye yote kwa jinsi ya mwili”, yanasomeka hivi katika Biblia ya kiingereza ya King James Version (KJV) “wherefore henceforth know we no man after the flesh”  kwa Kiyunani hatumjui mtu awaye yote kwa jinsi ya mwili linasomeka hivi  “eidō hēmeis de kata sarx” ambalo tafasiri yake ni kuwa watu waliookoka kweli kweli hawamwangalii mtu katika picha ya mtazamo wa kibinadamu bali katika jicho la Mungu aliyewaokoa “In salvation radically alters human perception not based on fleshly”  neno Flesh au mwili ndio kwa Kiyunani SARX, baada ya kuokolewa hatumwangalii mtu awaye yote kwa sababu ya rangi yake, utajiri wake, umasikini wake, kabila yake, elimu yake, taifa lake, wala hadhi yake wala historia yake ya nyuma, kila mtu aliyeokolewa anapaswa kumtazama mwingine katika namna ambayo Mungu anamtazama na tuache mara moja kujifikiri kuwa wewe unaweza kuwa bora kuliko wengine katika Kristo, leo hii unaweza kuona hata miongoni mwa watu wanaomuamini Yesu Kristo watu wa kabila fulani au dhehebu fulani wakijifikiri kuwa wao ni maalumu sana kuliko watu wa kabila nyingine au dhehebu lingine, wakati mwingine unaweza kubaki katika imani kwa sababu ya ujuzi wako kuhusu Kristo tu lakini wako watu wa makabila fulani, na madhehebu fulani, ambao wanadhani kuwa wao na babu zao na ukoo wao ndio wenye uwezo wa kumtumikia Mungu peke yao na akitokea mtu wa kabila lingine au dhehebu lingine ambaye anakiri kuwa ameokoka, wanadhani kuwa huyo hawezi na wanampiga vita, kuna wakati hata waimbaji wakiinuliwa kutokea kabila lingine watu waanza kuhoji kuwa hata wakabila hii nao wanaimba? Huku wakisahau kuwa kumbe Mungu anaweza kuinua waimbaji kutokea kabila lolote lile, unajua ni kwa nini ni kwa sababu wanadhani ni wao tu ndio wameitwa kumuimbia Mungu au ndio wanajua kuimba kuliko watu wa kabila zingine, Paulo mtume aliutetea utume wake ambao watu waliupiga vita wakifikiri kuwa hakuwa na Yesu kwa jinsi ya mwili na hivyo ana mapungufu, akilinganishwa na mitume wengine waliotembea na Bwana bega kwa bega, Ni muhimu kufahamu kuwa Mungu hapokei uso wa mwanadamu! Hatishwi na vyeo wala utajiri, wala wingi au ucheche wala mvuto wa nje, watu wote ambao Kristo amewafia msalabani wako sawa na hakuna aliye bora kuliko wengine hata kama injili ilianzia kwenu, kumbuka ilianza kwa Wayahudi na imetufikia sisi sote, Mungu sio wa Kusini na Kaskazini peke yake pia ni Mungu wa Mashariki na Magharibi, Mungu ni wa wote wenye mwili asomaye na afahamu yeye hana upendeleo!

Wagalatia 2:6-9 “Lakini wale wenye sifa ya kuwa wana cheo; (walivyokuwa vyo vyote ni mamoja kwangu; MUNGU HAPOKEI USO WA MWANADAMU); nasema, hao wenye sifa hawakuniongezea kitu; bali, kinyume cha hayo, walipoona ya kuwa nimekabidhiwa injili ya wasiotahiriwa, kama vile Petro ya waliotahiriwa; (maana yeye aliyemwezesha Petro kuwa mtume wa waliotahiriwa ndiye aliyeniwezesha mimi kwenda kwa Mataifa); tena walipokwisha kuijua ile neema niliyopewa; Yakobo, na Kefa, na Yohana, wenye sifa kuwa ni nguzo, walinipa mimi na Barnaba mkono wa kuume wa shirika; ili sisi tuende kwa Mataifa, na wao waende kwa watu wa tohara;”

Matendo 10:34-35 “Petro akafumbua kinywa chake, akasema, Hakika natambua ya kuwa MUNGU HANA UPENDELEO; bali katika kila taifa mtu amchaye na kutenda haki hukubaliwa na yeye.”

Warumi 2:5-11 “Bali kwa kadiri ya ugumu wako, na kwa moyo wako usio na toba, wajiwekea akiba ya hasira kwa siku ile ya hasira na ufunuo wa hukumu ya haki ya Mungu, atakayemlipa kila mtu kwa kadiri ya matendo yake; wale ambao kwa saburi katika kutenda mema wanatafuta utukufu na heshima na kutokuharibika, watapewa uzima wa milele; na wale wenye fitina, wasioitii kweli, bali wakubalio dhuluma, watapata hasira na ghadhabu; dhiki na shida juu ya kila nafsi ya mwanadamu atendaye uovu, Myahudi kwanza na Myunani pia; bali utukufu na heshima na amani kwa kila mtu atendaye mema, Myahudi kwanza na Myunani pia; KWA MAANA HAKUNA UPENDELEO KWA MUNGU.”

Waefeso 6:9 “Nanyi, akina bwana, watendeeni wao yayo hayo, mkiacha kuwaogofya, huku mkijua ya kuwa yeye aliye Bwana wao na wenu yuko mbinguni, WALA KWAKE HAKUNA UPENDELEO.”

Wakolosai 3:23-25 “Lo lote mfanyalo, lifanyeni kwa moyo, kama kwa Bwana, wala si kwa wanadamu,mkijua ya kuwa mtapokea kwa Bwana ujira wa urithi. Mnamtumikia Bwana Kristo. Maana adhulumuye atapata mapato ya udhalimu wake, WALA HAKUNA UPENDELEO.”

Tunajifunza ya kuwa Mungu hana upendeleo, na kuwa ndani ya Yesu Kristo kila mtu aliyeokolewa ana thamani kubwa sana mbele za Mungu thamani ambayo iko sawa na mwingine, tunatofautiana neema, vipawa na huduma kwa kadiri apendavyo Mungu yeye yule katika mwili wa Kristo, lakini hii haimaanishi kuwa mtu aliyeokoka anaweza kumdharau mwingine au kulinganisha mtu na mtu au mtu wa kabila fulani la kabila fulani au dhehebu fulani na fulani linalohubiri wokovu, ni mbaya sana katika wokovu kufikiri kuwa watu fulani tu ndio wana haki ya kumtumikia Mungu na wa aina fulani hawana haki, Katika wokovu hatumwangalii mtu kwa jinsi ya kibinadamu bali kama ndugu katika Kristo bila kujali mtu huyu ameitwa namna gani.

Ingawa sisi tumemtambua Kristo kwa jinsi ya mwili, lakini sasa hatumtambui hivi tena

2Wakorintho 5:16 “Hata imekuwa, sisi tangu sasa hatumjui mtu awaye yote kwa jinsi ya mwili. Ingawa sisi tumemtambua Kristo kwa jinsi ya mwili, lakini sasa hatumtambui hivi tena.”

Paulo anakwenda ndani zaidi sana kwamba mtu aliyeokoka vema sio tu kuwa hatazami watu kwa jinsi ya Mwili lakini pia hata utambuzi wake kuhusu Yesu Kristo unakwenda ndani zaidi ya kuwa hatumtambui Yesu kwa jinsi ya mwili “Ingawa sisi tumemtambua Kristo kwa jinsi ya mwili, lakini sasa hatumtambui hivi tena”

Wengine katika Korintho walijisifu kuwa wanamjua Kristo kwa jinsi ya mwili, na wengine waliokuwa wakijivunia walijivunia kwa sababu wao walimuona Kristo na walimjua kwa jinsi ya mwili walikuwa karibu naye ni wa kabila yao kwa hiyo baadhi ya watu kule Korintho walimuona Paulo mtume kama asiye na ubora kwa vile hakumuona Kristo kwa jinsi ya mwili wakati mitume wengine, walimuona Paulo anawaonyesha kuwa hilo pia halina maana na wala halina mashiko, wako watumishi ambao wamebahatika pia kumuona Kristo akiwatokea na kuwaita moja kwa moja katika wito maalumu wa kumtumikia na wanadhani kwa sababu hiyo wanaweza kuwa na umaalumu sana, Paulo anaonyesha ya kuwa ukiisha kuokolewa kuna namna unaweza kumtambua Yesu Kristo kwa jinsi nyingine na sio lazima iwe ile ya mwili, kutokewa na Kristo hakukufanyi wewe uwe maalumu  na wa kipekee sana kuliko asiyetokewa, kwa hiyo Paulo anaonyesha ya kuwa ingawa yeye hakutembea na Yesu moja kwa moja kama mitume wengine wakati wa maisha ya Yesu Duniani lakini Kristo alimtokea kwa njia ya pekee na kumteua kuwa mtume hata kama kule Korintho wanamuona yeye ni mdogo au hana sifa!

1Wakorintho 15:3-10 “Kwa maana naliwatolea ninyi hapo mwanzo yale niliyoyapokea mimi mwenyewe, ya kuwa Kristo alikufa kwa ajili ya dhambi zetu, kama yanenavyo maandiko; na ya kuwa alizikwa; na ya kuwa alifufuka siku ya tatu, kama yanenavyo maandiko; na ya kuwa alimtokea Kefa; tena na wale Thenashara; baadaye aliwatokea ndugu zaidi ya mia tano pamoja; katika hao wengi wanaishi hata sasa, ila baadhi yao wamelala; baadaye akamtokea Yakobo; tena na mitume wote; na mwisho wa watu wote, alinitokea mimi, kama ni mtu aliyezaliwa si kwa wakati wake. Maana mimi ni mdogo katika mitume, nisiyestahili kuitwa mitume, kwa sababu naliliudhi Kanisa la Mungu. Lakini kwa neema ya Mungu nimekuwa hivi nilivyo; na neema yake iliyo kwangu ilikuwa si bure, bali nalizidi sana kufanya kazi kupita wao wote; wala si mimi, bali ni neema ya Mungu pamoja nami.”

2Wakorinto 12:1-4 “Sina budi kujisifu, ijapokuwa haipendezi; lakini nitafikilia maono na mafunuo ya Bwana. Namjua mtu mmoja katika Kristo, yapata sasa miaka kumi na minne, (kwamba alikuwa katika mwili sijui; kwamba alikuwa nje ya mwili sijui; Mungu ajua). Mtu huyo alinyakuliwa juu mpaka mbingu ya tatu. Nami namjua mtu huyo, (kwamba alikuwa katika mwili sijui; kwamba alikuwa nje ya mwili sijui; Mungu ajua); ya kuwa alinyakuliwa mpaka Peponi, akasikia maneno yasiyotamkika, ambayo haijuzu mwanadamu ayanene.”

Yohana 20:29 “Yesu akamwambia, Wewe, kwa kuwa umeniona, umesadiki; wa heri wale wasioona, wakasadiki.”

Kila mtu ana namna yake anavyomjua Kristo, wale waliomuona kwa mwili au waliomuona kwa maono hawawezi kwa namna yoyote kuwa bora kuliko yule asiyemuona, lakini ameamini kwa hiyo kimsingi Yesu alisema amebarikiwa yule asiyeniona lakini akaniamini, hata kama ulimjua Kristo kwa jinsi ya mwili kuna namna kila mmoja anamjua kwa jinsi yake  na kuna namna kila mtu aliyeokolewa anamtambua si kwa namna ile ya mwilini tena, mtazamo wa mtu aliyeokoka baada ya kuwamini Yesu, haumtazami Yesu kihistoria tu wala kwa utamaduni na kabila yake ndani ya watu waliookoka kuna ufahamu mpya na mtazamo mpya wa kiroho kuhusu Yesu Kristo, hakuna mtu mwenye hati miliki ya Kristo yeye ni mwokozi wa ulimwengu, wako wanaomtazama kwa jinsi ya mwili na wanamjua kwa jinsi ya tamaduni na historia wako wanaomuona kama Mwanadamu, wako wanaomuona kama Myahudi, wako wanaomuona kama Rabi mkubwa, wako wanaomuona kama mwana wa Mariamu, wako wanaomuona kama mtume tu wa kawaida, Sisi tuliomuamini kuna namna yetu, tunavyomtambua, hatumtambui kwa jinsi ya mwili kuna namna nyingine tunamtambua Bwana Yesu wala si kwa akili za kibinadamu, uko ufunuo wa kipekee unaowekwa na Mungu ndani yetu, Ingawa sisi tumemtambua Kristo kwa jinsi ya mwili, lakini sasa hatumtambui hivi tena kuna namna mpya ambayo mtu aliyeokoka anamjua Yesu Kristo na hii ndio ya muhimu na ndiyo anayoizungumzia Paulo Mtume

Mathayo 16:13-17 “Basi Yesu akaenda pande za Kaisaria-Filipi, akawauliza wanafunzi wake akasema, Watu hunena Mwana wa Adamu kuwa ni nani? Wakasema, Wengine hunena u Yohana Mbatizaji, wengine Eliya, wengine Yeremia au mmojawapo wa manabii. Akawaambia, Nanyi mwaninena mimi kuwa ni nani? Simoni Petro akajibu akasema, Wewe ndiwe Kristo, Mwana wa Mungu aliye hai.Yesu akajibu, akamwambia, Heri wewe Simoni Bar-yona; kwa kuwa mwili na damu havikukufunulia hili, bali Baba yangu aliye mbinguni.”

Yohana 3:31 “Yeye ajaye kutoka juu, huyo yu juu ya yote. Yeye aliye wa dunia, asili yake ni ya dunia, naye anena mambo ya duniani. Yeye ajaye kutoka mbinguni yu juu ya yote.”

Mtu akiwa ndani ya Kristo

2Wakorintho 5:16-17 “Hata imekuwa, sisi tangu sasa hatumjui mtu awaye yote kwa jinsi ya mwili. Ingawa sisi tumemtambua Kristo kwa jinsi ya mwili, lakini sasa hatumtambui hivi tena. Hata imekuwa, mtu akiwa ndani ya Kristo amekuwa kiumbe kipya; ya kale yamepita tazama! Yamekuwa mapya.”

Paulo mtume anakwenda ndani zaidi na kumzungumzia sasa mtu aliyeokoka na ambaye anaendelea kudumisha uhusiano wake na Kristo kuwa mtu huyo sio wa kawaida maneno ya Kiyunani yanayotumika hapo ni “en Christō Kainē ktisis” maana yake mtu aliye ndani ya Kristo ni uumbaji mpya, ni maisha mapya, ni mwanzo mpya, ni tabia mpya, ni utambulisho mpya, mtu aliyeokoka hafanyiwi ukarabati au marekebisho kwa hiyo sahau utambulisho wake wa zamani, mwenendo wake wa zamani, dhambi zake za zamani  ya kale yanafutwa kabisa na hapo haimaanishi kuwa kumukumbuki zimefutika la hasha bali kila aina ya utawala na nguvu za zamani zimeharibiwa ni ukurasa mpya unaanza, kwa hiyo mtu asikuhukumu kwa maswala ya jana au juzi au historia yako ya zamani, Paulo mtume alikuwa na historia ngumu ya kuliudhi Kanisa lakini Mungu alipomuokoa na kumuita mambo ya kale yalipita hali kadhalika wewe na mimi kuna namna tunapaswa kutazamwa katika mtazamo mwingine baada ya kuokoka, waliookoka wanapaswa kutazamwa katika jicho lingine, hatupaswi kufikiri kwa sababu mtu huyu alikuwa muuaji basi hawezi kuwa chombo cha Mungu, Paulo mtume aliliudhi kanisa n ahata alipookolewa Mwanafunzi wa Bwana Anania aliogopa hata kumuhudumia lakini Mungu alimweleza kuwa mtu huyu ni chombo changui kiteule

Matendo 9:10-16 “Basi palikuwapo Dameski mwanafunzi jina lake Anania. Bwana akamwambia katika maono, Anania. Akasema, Mimi hapa, Bwana. Bwana akamwambia, Simama, enenda zako katika njia iitwayo Nyofu, ukaulize katika nyumba ya Yuda mtu aitwaye Sauli, wa Tarso; maana, angalia, anaomba; naye amemwona mtu, jina lake Anania, akiingia, na kumwekea mikono juu yake, apate kuona tena. Lakini Anania akajibu, Bwana, nimesikia habari za mtu huyu kwa watu wengi, mabaya mengi aliyowatenda watakatifu wako Yerusalemu; hata hapa ana amri itokayo kwa wakuu wa makuhani awafunge wote wakuitiao Jina lako. Lakini Bwana akamwambia, Nenda tu; kwa maana huyu ni chombo kiteule kwangu, alichukue Jina langu mbele ya Mataifa, na wafalme, na wana wa Israeli. Maana nitamwonyesha yalivyo mengi yatakayompasa kuteswa kwa ajili ya Jina langu.” 

Paulo mtume alibadilishwa kabisa kama kila mtu aliyemuamini Kristo anavyobadilishwa, mtuime ahkupaswa kutiliwa mashaka kuwa hayuko sawa na wengine kwa sababui kinachomtokea kila mtu aliyeokoka ndicho kilichomtokea na yeye, mtu aliyeokoka anapatwa na maswala yafuatayo ambayo humfanya kuwa kiumbe kipya:-

Amesamehewa dhambi zake – Wakolosai 1:13-14 “Naye alituokoa katika nguvu za giza, akatuhamisha na kutuingiza katika ufalme wa Mwana wa pendo lake; ambaye katika yeye tuna ukombozi, yaani, msamaha wa dhambi;”

Amekuwa mwana wa Mungu – Yohana 1:12-13 “Bali wote waliompokea aliwapa uwezo wa kufanyika watoto wa Mungu, ndio wale waliaminio jina lake; waliozaliwa, si kwa damu, wala si kwa mapenzi ya mwili, wala si kwa mapenzi ya mtu, bali kwa Mungu.”

Anahesabiwa haki -  Warumi 5:1-2 “Basi tukiisha kuhesabiwa haki itokayo katika imani, na mwe na amani kwa Mungu, kwa njia ya Bwana wetu Yesu Kristo, ambaye kwa yeye tumepata kwa njia ya imani kuifikia neema hii ambayo mnasimama ndani yake; na kufurahi katika tumaini la utukufu wa Mungu.”

Anatakaswa katika Kristo – 1Wakorintho 1:2 “kwa kanisa la Mungu lililoko Korintho, wale waliotakaswa katika Kristo Yesu, walioitwa wawe watakatifu, pamoja na wote wanaoliitia jina la Bwana wetu Yesu Kristo kila mahali, Bwana wao na wetu.”

Ana uzima wa milele – Yohana 3:16 “Kwa maana jinsi hii Mungu aliupenda ulimwengu, hata akamtoa Mwanawe pekee, ili kila mtu amwaminiye asipotee, bali awe na uzima wa milele.”

Hana hukumu ya adhabu – Warumi 8:1 “Sasa, basi, hakuna hukumu ya adhabu juu yao walio katika Kristo Yesu.”

Na. Rev. Innocent Samuel Kamote

Mkuu wa wajenzi mwenye Hekima

Hakuna maoni: