1Samuel 22:1-2. “Basi Daudi akaondoka huko,
akakimbilia pango la Adulamu; na ndugu zake na watu wote wa mbari ya baba yake
waliposikia habari hiyo, wakamwendea huko. Na kila mtu aliyekuwa katika hali ya
dhiki, na kila mtu aliyekuwa na deni, na watu wote wenye uchungu mioyoni mwao,
wakakusanyika kwake; naye akawa jemadari wao; nao waliokuwa pamoja naye
walipata kama watu mia nne.”
Utangulizi:
Wengi wetu tutakua tunafahamu kuhusu
habari za Daudi kukimbilia katika pango la Adulamu, Pango hili liko maili 22.5
sawa na kilomita 36 kusini magharibi mwa jiji la Yerusalem na kilomita 13
magharibi mwa Bathelehemu, mipakani na nchi ya Wafilisti eneo hili ni maarufu
na linajulikana kama Mahali pa kujificha, hasa kutokana na tukio la Daudi
kukimbilia huko na kujificha alipokuwa anamkimbia mfalme Sauli aliyekuwa
anataka kumuua, Adulamu pakawa mahali salama kwa Daudi na watu wote wenye
huzuni, shida na madeni waliomuendea, Kimsingi Pango la Adulamu pamoja na tukio
hili halisimami kama sehemu ya historia na usalama tu lakini linasimama kama
eneo muhimu la maandalizi ya kiroho na uongozi na mabadiliko makubwa ya Daudi
na watu wake, Kwa hiyo Adulamu pamejulikana kama eneo muhimu la kimchakato
ambapo Mungu anawaandaa watu wake kabla hawajashika majukumu yao ya kimaongozi.
1Samuel 21:8-10 “Tena Daudi akamwambia
Ahimeleki, Na hapa chini ya mkono wako, je! Hapana mkuki, au upanga? Kwa maana
sikuleta upanga, wala silaha zangu, kwa sababu ile shughuli ya mfalme ilitaka
haraka. Yule kuhani akasema, upanga wa Goliathi, yule Mfilisti, uliyemwua
katika bonde la Ela, tazama, upo hapa, umefungwa ndani ya nguo nyuma ya
naivera; ukipenda kuuchukua, haya! Uchukue, maana hapa hapana mwingine ila huo
tu. Daudi akasema, Hapana mwingine kama ule; haya! Nipe. Basi Daudi akaondoka,
akakimbia siku ile, kwa hofu ya Sauli, akamwendea Akishi, mfalme wa Gathi.”
1 Samweli 22:1-2 “Basi Daudi akaondoka
huko, AKAKIMBILIA PANGO LA ADULAMU; na ndugu zake na watu wote wa mbari ya baba
yake waliposikia habari hiyo, wakamwendea huko. Na kila mtu aliyekuwa katika
hali ya dhiki, na kila mtu aliyekuwa na deni, na watu wote wenye uchungu
mioyoni mwao, wakakusanyika kwake; naye akawa jemadari wao; nao waliokuwa
pamoja naye walipata kama watu mia nne.”
Kwa msingi huo leo tutachukua
muda kujifunza somo hili muhimu, lenye kichwa “Umuhimu wa Pango la Adulamu” kwa kuzingatia vipengele vikuu vitatu
muhimu vifuatavyo:-
·
Maana ya
Adulamu
·
Umuhimu
wa Pango la Adulamu
·
Matokeo
ya kupita katika Pango la Adulamu
Maana ya Adulamu
Neno au jina Adulam linatokana na neno la asili la Kiebrania “Adullām” ambalo lina uhusiano na eneo
lililokuwa lililokaliwa na rafiki mkubwa wa Yuda mwana wa Yakobo aliyeitwa Hira, Hira alikuwa
rafiki mkubwa sana wa Yuda ambao walishirikiana katika kufuga wanyama na mambo
yao mengine ya kimaisha, Rafiki huyu mkubwa wa Yuda aliishi eneo hilo.
Mwanzo 38:1-3, 12 “Ikawa wakati ule, Yuda
akashuka kutoka kwa ndugu zake, akamfikia mtu Mwadulami, jina lake Hira. Yuda
akaona huko binti wa mtu Mkanaani, jina lake Shua. Akamtwaa, akaingia kwake.
Naye akapata mimba, akazaa mwana, akamwita jina lake Eri. 12 Siku nyingi
zikapita, akafa binti Shua, mkewe Yuda. Yuda akafarijika, akaenda kwa watu wake
wawakatao manyoya kondoo huko Timna, yeye na mwenzake Hira, Mwadulami.”
Neno au pango la “Adullām” limepata umaarufu sana baada ya
Daudi kukimbilia huko kwaajili ya kuokoa uhai wake akimkimbia mfalme Sauli
aliyekuwa anataka kumuua, huko aliungana na watu wengine wapatao 400
na baadae walifika 600 watu
waliokuwa na madeni, waliokata tamaa na wale ambao hawakuridhishwa na hali ya
mambo wakati wa utawala wa Sauli, kutokana na umaarufu wa tukio hili hata jina “Adullām” au Pango la Adulamu limebeba
maana ya Mahali pa siri, au mahali pa makimbilio, au mahali pa
kujificha, au mahali pa kujitenga na kujipanga kwa upya, au kimbilio la
waliovunjika moyo, The secret place, The
place of Refuge, the Hiding Place, Place of withdrawal, the place of retreat,
or a place of brokenness.
Adulamu kumejipatia umaarufu
kiroho kama mahali ambapo Mungu anamtenga mtu wake na kumuandaa kwaajili ya
mpango wake mkuu wa baadae, ni eneo la utulivu, usalama na la kujipanga kwa
upya ni kama shule ya Roho Mtakatifu, mahali ambapo ni kama Mungu anakuacha
upoteze kila kitu, kisha uishi maisha ya ukimbizi, na kujiepusha na watu, kisha
anakuweka na watu wanaoonekana kutokufaa ili uwabadilishe waweze kufaa, hivyo
kwa jicho la kinabii Adulamu ni
mahali muhimu ambapo sio tu kuwa mtu anakimbilia bali Mungu anampeleka mtu huko
ili kumjenga na kumuandaa kwa huduma.
Umuhimu wa Pango la Adulamu
Mungu hakumruhusu Daudi kwenda
Adulamu kama adhabu, lakini badala yake lilikuwa ni eneo muhimu kwaajili ya
maandalizi ya kimkakati ya kumfanya kuwa mfalme mwenye nguvu sana, mwanadamu
hajifunzi kuwa imara anapokuwa kwenye eno lenye starehe “Comfort zone” lakini mwanadamu anakuwa imara sana anapokuwa katika
mazingira magumu na tatanishi yasiyo na faraja yoyote, kusudi kubwa Mungu anataka
ukomae na usidumae, anataka ukue na hatimaye uje kuwa kiungo kizuri katika
kutimiza mpango wake, wakati ambapo kimsingi Adulamu hakuonekani kuwa kwenye
kufaa huko lakini ni shule ya Mungu ya kutengeneza sifa nzuri, na kuleta
mabadiliko, kuondoa njia za zamani na mitazamo ya zamani na kupewa mipya
itakayofaa kwaajili ya watu wa Mungu lakini zaidi ya mambo yote Adulamu ni
mahali ambapo watu wa Daudi walijifunza kufunga na kuomba na kuabudu
wakimtegemea Mungu, kuna mafunzo mengi ambayo Mungu aliwafunza watu wake waliokimbilia
Adulamu
1. Ni eneo la kukomazwa - Yakobo 1:2-3 “Ndugu zangu, hesabuni ya kuwa ni furaha tupu, mkiangukia
katika majaribu mbalimbali; mkifahamu ya kuwa kujaribiwa kwa imani yenu huleta
saburi. Saburi na iwe na kazi kamilifu, mpate kuwa wakamilifu na watimilifu
bila kupungukiwa na neno.”
Waebrania 12:11
“Kila adhabu wakati wake haionekani kuwa kitu cha
furaha, bali cha huzuni; lakini baadaye huwaletea wao waliozoezwa nayo matunda
ya haki yenye amani.”
Kwa nini kukomazwa au kuwa na uzoefu ni kwa
muhimu? Kukomazwa na kuzoezwa ni jambo
la Muhimu na ni mchakato ambao kimsingi hautokei kama muujiza inachukua muda au
inahitaji muda fulani, lakini muda huo utakujengea ukuaji katika Hekima, imani
na kuwa na tabia za uungu, jambo hili ni la Muhimu kwa sababu pia litakusaidia
kukupa uwezo wa kukabiliana na changamoto za aina mbalimbali na kukujengea
uwezo na ubora katika maswala ya mahusiano, upendo wa kujitoa, kumjua Mungu kwa
undani kuwa na Amani katika mazingira yote
na kuwa na uhusiano wa ndani sana na Mungu na watu wengine, hakuna jambo
baya duniani kama kuja kuongozwa na kiongozi aliyekosa mafunzo na ukomavu,
viongozi wengi wasiopitia Adulamu wamejawa na ubinafsi, choyo, kujihami, kukosa
kujiamini na kushindwa kuchukuliana lakini kwa Daudi Adulamu lilikuwa eneo zuri
la kuishi na watu na kuwavumilia.
2. Ni eneo la kujifunza kumtegemea Mungu - Kumbukumbu
8:2-3 “Nawe utaikumbuka njia ile yote Bwana, Mungu
wako aliyokuongoza miaka hii arobaini katika jangwa, ili akutweze, kukujaribu
kuyajua yaliyo moyoni mwako, kwamba utashika amri zake, au sivyo. Akakutweza,
akakuacha uone njaa, akakulisha kwa mana, usiyoijua wewe wala baba zako
hawakuijua; apate kukujulisha ya kuwa mwanadamu haishi kwa mkate tu, bali
huishi kwa kila litokalo katika kinywa cha Bwana.”
2Wakorintho 12:9
“Naye akaniambia, Neema yangu yakutosha; maana
uweza wangu hutimilika katika udhaifu. Basi nitajisifia udhaifu wangu kwa
furaha nyingi, ili uweza wa Kristo ukae juu yangu.”
Kujifunza kumtegemea Mungu kuna umuhimu wake kwa
sababu kutakujengea msingi usiotikisika hata pale Amani yako inapotikiswa,
matumaini yako yanapogeuka, kusudi linapoonekana kuchelewa na uwezo wako wa
kufanya mambo kwa nafsi yako unapoachwa katika mikono ya Yeye mwenye uwezo wa
kuamua majira na nyakati, hutaogopa, utakuwa na nguvu ya ndani, utapata
muelekeo sahihi na utakuwa na moyo wa unyenyekevu, Adulamu inatufunza
kumtegemea Mungu.
3. Ni eneo la mabadiliko makubwa - Kabla
Mungu hajaanza kumtumia mtu anaandaa mazingira ya kutubadilisha, Mungu anaondoa
kabisa kiburi na ubinafsi, anakufundisha kumtegemea yeye na sio swala la
kukubalika na dunia au walimwengu, kwa hiyo ataruhusu majaribu ya aina
mbalimbali ili akunoe na kukutengeneza, wakati mwingine ataruhusu upoteze kila
kitu, akupime katika hali zote akuone unapofanikiwa na unapokosa tabia yako
inakuwaje na baada ya vipimo vingi sana Mungu anakuamini na kukupa majukumu
anayoyakusudia kukupa kubwa ni mabadiliko!
Wafilipi
4:11-13 “Si kwamba nasema haya kwa kuwa nina
mahitaji; maana nimejifunza kuwa radhi na hali yo yote niliyo nayo. Najua
kudhiliwa, tena najua kufanikiwa; katika hali yo yote, na katika mambo yo yote,
nimefundishwa kushiba na kuona njaa, kuwa na vingi na kupungukiwa. Nayaweza
mambo yote katika yeye anitiaye nguvu.”
Daudi alikuwa ni kama mtu aliyepoteza kila kitu
alipokimbiilia Adulamu, Lakini Mungu alimfundisha kumtegemea yeye aliishi
alikula na aliendelea kuwa shujaa mwenye uwezo wa kuingia na kutoka na kuwasaidia
watu wote duni waliokuwa wamemkimbilia, Daudi aliwatunza, aliwajenga kiroho na
kuwafundisha vita, Mungu atatujaribu ili atunoe na kutupima kama dhahabu
inavyopimwa ili tutoke tukiwa tunang’aa zaidi, Daudi na watu wake walijifunza
vita, walijifunza ushujaa, walijifunza ukakamavu, walijifunza kufunga na
kuomba, walijifunza kuabudu walijifunza kumtegemea Mungu na kuishi kijamaa na
wakatoka huko wakiwa na mabadiliko makubwa tayari kwa kushika hatamu na
kuwahudumia watu wa Mungu Ayubu 23:10 “Lakini yeye aijua njia niendeayo; Akisha kunijaribu,
nitatoka kama dhahabu.”
4. Ni eneo la maandalizi ya kishujaa - Mungu
hutumia changamoto kutujengea maandalizi na ushujaa, ili tuwe na nidhamu,
subira uvumilivu na ujasiri, anaruhusu mazingira ambayo wewe ndie utakuwa
tegemeo lake na hutajitumainia kwa lolote, anakubadilisha mtazamo na fikra na
kukuandaa kivita, wayahudi ni taifa vumilivu na imara zaidi duniani kwa sababu
ya kukutana na changamoto kali na kadiri wanavyoshambuliwa ndivyo wanavyokuwa
imara na kujijengea uwezo mkubwa siku hadi siku, kupigana kwao sio kwaajili ya
kushambulia bali kwaajili ya kujihami.
2Wakorintho
10:5 “Maana ingawa tunaenenda katika mwili,
hatufanyi vita kwa jinsi ya mwili; (maana silaha za vita vyetu si za mwili,
bali zina uwezo katika Mungu hata kuangusha ngome ;) tukiangusha mawazo na kila
kitu kilichoinuka, kijiinuacho juu ya elimu ya Mungu; na tukiteka nyara kila
fikira ipate kumtii Kristo; tena tukiwa tayari kupatiliza maasi yote, kutii
kwenu kutakapotimia.”
Yeremia 29:10-13.
“Maana Bwana asema hivi, Babeli utakapotimiziwa
miaka sabini, nitawajilia ninyi, na kulitimiza neno langu jema kwenu, kwa
kuwarudisha mahali hapa. Maana nayajua mawazo ninayowawazia ninyi, asema Bwana,
ni mawazo ya amani wala si ya mabaya, kuwapa ninyi tumaini siku zenu za mwisho.
Nanyi mtaniita, mtakwenda na kuniomba, nami nitawasikiliza. Nanyi mtanitafuta
na kuniona, mtakaponitafuta kwa moyo wenu wote.”
5. Ni eneo la kuondoa udumavu - Mungu
hafurahii udumavu wetu kiroho, iwapo anaona ukuaji wetu unaweza kuathiriwa
anaondoa watu na mahali na hali zote
zinazoonekana kuwa na umuhimu wa kukulazimisha wewe ukue na kukomaa, kama mtu
au watu na mazingira yanayoonekana kuathiri ukuaji wako anakuondoa wewe,
anaondoa ulinzi, anaondoa faraja, anaondoa kuthibitishwa na watu anaweza hata
kukuhamisha mazingira kama anaona ni madogo kwake kukusaidia kwenda kwenye
kiwango kingine anaingilia mielekeo
yako, anafunga mlango, anakuweka kwenye chumba cha kusubiria, anaruhusu upate
maumivu, atakufanya uishi kwa imani, anaondoa udumavu na kukuoa ukuaji wa
kiroho.
Hosea 2:13 -17 “Nami nitamwadhibu kwa sababu ya siku za Mabaali,
aliowafukizia uvumba; hapo alipojipamba kwa pete masikioni mwake, na kwa vito
asema Bwana. Kwa hiyo angalia, mimi nitamshawishi, na kumleta nyikani, na
kusema naye maneno ya kumtuliza moyo. Nami nitampa mashamba yake ya mizabibu
toka huko, na bonde la Akori kuwa mlango wa tumaini; naye ataniitikia huko,
kama siku zile za ujana wake, na kama siku ile alipopanda kutoka nchi ya Misri.
Tena siku hiyo itakuwa, asema Bwana, utaniita Ishi, Kwa maana nitayaondoa
majina ya Mabaali kinywani mwake, wala hawatatajwa tena kwa majina yao.”
6. Ni eneo la kutengwa - Daudi alishakuwa mtu maarufu sana tangu
siku alipomuua Goliath, watu wa mijini na vijijini walikuwa wanamtambua,
wanawake waliimba na kumsifia kuwa amefanya kazi kubwa kuliko hata mfalme
mwenyewe kwa hiyo alitajwa kama mtu shujaa aliyeiletea Israel ushindi mkubwa
sana, aliozwa binti wa kifalme na alikuwa anakaa ikulu, na kwa kuwa alikuwa mtu
wa kutegemewa alitakiwa kukaa katika uwanja wa vita akipigana vita mbalimbali
mtu huyu mwenye sifa zote za kifalme badala ya kuwako ikulu sasa anaishi kama
mkimbizi na kuishi katika pango huko Adulamu, Mungu alimtenga na umaarufu,
Mungu alitaka kumtenga mtumishi wake kwa kazi maalumu
1Samuel 18:6-7
“Hata ikawa, walipokuwa wakienda, hapo Daudi
aliporudi baada ya kumwua yule Mfilisti, wanawake wakatoka katika miji yote ya
Israeli, kwa kuimba na kucheza, ili kumlaki mfalme Sauli; wakatoka na matari,
na shangwe, na vinanda. Nao wale wanawake wakaitikiana wakicheza, wakasema,
Sauli amewaua elfu zake, Na Daudi makumi elfu yake.”
Wimbo huu uliashiria kuwa Daudi ni Mpiganaji hodari
zaidi kuliko Sauli kwani wanawake walijaribu kumlinganisha na mtawala aliyekuweko
na kwa sababu ya wimbo huu Sauli alipatwa na wivu na kuanza njama na mikakati
ya kummaliza na kumuua Daudi, Mungu anaamua kumtenga Daudi na hatari hizo,
kwaajili ya kumuandaa kuwa kiongozi hodari zaidi, mnyenyekevu, mvumilivu mwenye
kujua wakati na majira ya Mungu, Mungu anaweza kukutenga na kukupeleka mahali
ambapo utapata muda na utaendeleza uwezo wa kumuomba na kujitambua na kukomaa
zaidi kwa ajili ya kazi yake
7. Ni eneo la mafunzo ya kiroho - Huko
Adulamu Daudi hakuwa Mchungaji wa kondoo tu na Shujaa wa vita bali sasa alikuwa
kiongozi, alifanyika kiongozi wa watu waliovunjika moyo, watu wenye uchungu
moyoni, wenye madeni na wenye mizigo. Mungu
alimtumia Daudi kuwafanya watu hao wanyonge kuwa mashujaa, walijigundua wao
ni kina nani bila ufalme na walijigundua wao ni akina nani bila sifa na umati
wa watu, Adulamu inaondoa sifa na kufunua kuwa wewe ni nani, Adulamu inakupa
nafasi ya kujitazama kwa jicho lingine na sio vile wanavyosema watu!
1Samuel 22:1-2.
“Basi Daudi akaondoka huko, akakimbilia pango la
Adulamu; na ndugu zake na watu wote wa mbari ya baba yake waliposikia habari
hiyo, wakamwendea huko. Na kila mtu aliyekuwa katika hali ya dhiki, na kila mtu
aliyekuwa na deni, na watu wote wenye uchungu mioyoni mwao, wakakusanyika
kwake; naye akawa jemadari wao; nao waliokuwa pamoja naye walipata kama watu
mia nne.”
2Samuel 23:8-39. ”Haya ndiyo majina ya mashujaa aliokuwa nao Daudi;
Yashobeamu Mhakmoni,mkuu wa maakida ;huyo aliliinua shoka lake juu ya watu mia
nane waliouawa pamoja.Na baada yake kulikuwa na Eleazari, mwana wa Dodai,
Mwahohi, mmojawapo wa wale mashujaa watatu waliokuwa pamoja na Daudi;
walipowatukana Wafilisti waliokuwa wamekusanyika huko ili kupigana, na watu wa
Israeli walikuwa wamekwenda zao; huyo aliinuka, akawapiga Wafilisti hata mkono
wake ukachoka, na mkono wake ukaambatana na upanga; naye Bwana akafanya wokovu
mkuu siku ile; nao watu wakarudi nyuma yake ili kuteka nyara tu.Na baada yake
kulikuwa na Shama, mwana wa Agee, Mharari; nao Wafilisti walikuwa wamekusanyika
huko Lehi, palipokuwapo konde lililojaa midengu; nao watu wakawakimbia
Wafilisti; ila huyo alisimama katikati ya konde lile, akalipigania, akawaua
Wafilisti; naye Bwana akafanya wokovu mkuu. Tena, watatu miongoni mwa wale thelathini
waliokuwa wakuu wakashuka, wakamwendea Daudi wakati wa mavuno mpaka pango la
Adulamu, na kikosi cha Wafilisti walikuwa wamefanya kambi katika bonde la
Warefai. Naye Daudi wakati ule alikuwako ngomeni, na jeshi la Wafilisti wakati
ule walikuwako Bethlehemu. Daudi akatamani, akasema, Laiti mtu angeninywesha
maji ya kisima cha Bethlehemu, kilicho karibu na lango! Basi hao mashujaa
watatu wakapenya jeshi la Wafilisti, wakateka maji kutoka kile kisima cha
Bethlehemu, kilicho karibu na lango, wakayachukua, wakamletea Daudi; walakini
yeye hakukubali kuyanywa, akayamimina mbele za Bwana. Akasema, Hasha, Bwana, nisifanye hivi; je! Si
damu hii ya watu hao waliohatirisha nafsi zao? Kwa hiyo hakukubali kuyanywa.
Hayo ndiyo waliyoyafanya wale mashujaa watatu. Tena, Abishai, nduguye Yoabu,
mwana wa Seruya, alikuwa mkuu wa wale watatu. Huyo aliuinua mkuki wake juu ya
watu mia tatu, akawaua, akawa na jina kati ya wale watatu. Je! Huyo hakuwa na heshima maalumu miongoni
mwa wale watatu? Kwa hiyo akawekwa kuwa akida wao; ila hakudiriki kuwamo katika
wale watatu. Tena Benaya, mwana wa Yehoyada, mtu hodari wa Kabseeli aliyekuwa
amefanya mambo makuu; aliwaua simba wakali wawili wa Moabu, pia akashuka
akamwua simba katikati ya shimo wakati wa theruji. huyo naye akamwua Mmisri,
mtu mrefu; naye huyo Mmisri alikuwa na mkuki mkononi; lakini yeye alimshukia na
gongo, akamnyakulia Mmisri mkuki mkononi mwake, akamwua kwa mkuki wake
mwenyewe. Hayo ndiyo aliyoyafanya Benaya, mwana wa Yehoyada, akawa na jina kati
ya wale mashujaa watatu. Alikuwa mwenye heshima kuliko wale thelathini, ila
hakudiriki kuwamo katika wale watatu. Naye Daudi akamweka juu ya walinzi wake.
Asaheli, nduguye Yoabu, alikuwa mmojawapo wa wale thelathini; na Elhanani,
mwana wa Dodo, wa Bethlehemu; na Shama, Mharodi, na Elika, Mharodi; na Helesi,
Mpeloni, na Ira, mwana wa Ikeshi, Mtekoi; na Abiezeri, Mwanathothi, na Sibekai,
Mhushathi; na Salmoni, Mwahohi, na Maharai, Mnetofathi; na Heledi, mwana wa
Baana, Mnetofathi, na Itai, mwana wa Ribai, wa Gibea wa wana wa Benyamini; na
Benaya, Mpirathoni, na Hurai, wa vijito vya Gaashi;na Abieli, Mwarbathi, na
Azmawethi, Mbarhumi; na Eliaba, Mshaalboni, na wana wa Yasheni; na Yonathani,
mwana wa Shama, Mharari, na Ahiamu, mwana wa Shalali, Mharari; na Elifeleti, mwana wa Ahasbai, na Heferi,
Mmaakathi, na Eliamu, mwana wa Ahithofeli, Mgiloni; na Hezro, Mkarmeli, na
Paarai, Mwarbi; na Igali, mwana wa Nathani, wa Soba, na Bani, Mgadi; na Seleki,
Mwamoni, na Naharai, Mbeerothi, ambao ni wachukua silaha wa Yoabu, mwana wa
Seruya; na Ira, Mwithri, na Garebu, Mwithri; na Uria, Mhiti; jumla yao ilikuwa
watu thelathini na saba.”
Matokeo ya kupita katika Pango la Adulamu
Adulamu kulizalisha Serikali
yenye nguvu sana, Daudi na watu wake waliokuwa wamekataliwa katika jamii tena
wanatafutwa kuuawa waligeuka kuwa watu wema, waadilifu, wenye uchungu na taifa
lao, na viongozi wa ufalme na majeshi ya kifalme na mashujaa wenye nguvu,
walitoka wakiwa watu wanaomcha Mungu na wanaomtegemea Mungu kwa asilimia
miamoja, Daudi aliwafunza watu wake kuwa kama yeye alivyo na kuwa na moyo kama
wake.
Zaburi 34:17-19 “Walilia, naye Bwana
akasikia, Akawaponya na taabu zao zote. Bwana yu karibu nao waliovunjika moyo,
Na waliopondeka roho huwaokoa. Mateso ya mwenye haki ni mengi, Lakini Bwana
humponya nayo yote.”
Zaburi 57:1-3 “Unirehemu, Ee Mungu, unirehemu mimi, Maana nafsi yangu
imekukimbilia Wewe. Nitaukimbilia uvuli wa mbawa zako, Hata misiba hii
itakapopita. Nitamwita MUNGU Aliye juu, Mungu anitimiziaye mambo yangu.
Atapeleka toka mbinguni na kuniokoa, Atukanapo yule atakaye kunimeza. Mungu
atazipeleka Fadhili zake na kweli yake”
- Adulamu Daudi
na wenzake walitoka wakiwa mwenye nguvu zaidi – Daudi alikimbilia Adulamu
akiwa Mkimbizi lakini alitoka akiwa kiongozi wa wakati mkamilifu uliokusudiwa
na Mungu kwa Israel kuwa na kiongozi mcha Mungu, Adulamu iliwajenga, iliwapa
uvumilivu, iliwafanya kuwa wa kiroho zaidi, iliwaimarisha kihisia, na kuwajengea
ujasiri.
- Adulamu
iliimarisha uhusiano wao karibu na Mungu – Walikimbilia Adulamu wakiwa
wenye mashaka, wenye wasi wasi, wenye woga na hofu, wakiwa na uchungu, wenye
madeni na walikata tamaa lakini walitoka wakiwa mashujaa, Kule Adulamu Mungu
atakuunganisha na watu utakaokuwa nao kiroho, watakaokupigania na watakaosimama
na wewe na wito wako
- Adulamu
lilikuwa ni eneo la kuendeleza kipawa cha uongozi, - Daudi alijifunza jinsi
ya kuongoza, jinsi ya kupangilia mfumo wa uongozi, jinsi ya kupanga wapiganaji,
jinsi ya kuwatia moyo watu waliokata tamaa na jinsi ya kumtegemea Mungu,
ukiweza kuongoza watu Adulamu hutasindwa kuongoza watu Hebroni wala Yerusalem
- Adulamu
lilikuwa ni eneo la kuimarisha uhusiano na Mungu – Adulamu lilikuwa ni eneo
la kujipanga upya kiroho, kulikuwa na ukimya, lilikuwa eneo la siri, sehemu
ambayo unaweza kufurahia uwepo wa Mungu, walitoka wakiwa wamejifunza kuomba,
kuimba zaburi, kumtegemea Mungu zaburi nyingi za Daudi zilitungwa na kuimbwa
kutoka katika pango la Adulamu
Adulamu sio kuzuri lakini ni kwa
Muhimu, ni kama sehemu ya upweke, ni kama sehemu ya kucheleweshwa, ni kama
sehemu ya ukimya lakini kiroho ni eneo la kukujenga na sio la kukubomoa, Mungu
akupeleke Adulamu lakini sio kwa kukutesa wala sio kwa adhabu wala sio
kukuchosha lakini kwaajili ya kukuendeleza, unafichwa ili uandaliwe, unavunjwa
ili utengenezwe, unasubiri ili utiwe nguvu, huwezi kuhitimu Adulamu kwa
kuikimbia unahitimu Adulamu kwa kukubali kuwa kile Mungu alichokikusudia ndani
yetu, kije kuwa dhahiri katika maisha yetu ya baadaye na kuwafaa watu wa Mungu.
Na. Rev. Innocent Samuel Kamote
Mkuu wa wajenzi mwenye Hekima

Hakuna maoni:
Chapisha Maoni