Alhamisi, 28 Septemba 2017

Nguvu ya Umoja!



Andiko la Msingi: Yohana 17:21Wote wawe na umoja; kama wewe, Baba, ulivyo ndani yangu, nami ndani yako; hao nao wawe ndani yetu; ili ulimwengu upate kusadiki ya kwamba wewe ndiwe uliyenituma.”


Umoja ni hali ya kuungana kushikamana na kushirikiana au kufanya mambo kwa nia moja hata kuwa kitu kimoja, kadiri watu wanavyokuwa na umoja wanakuwa na mwanya mkubwa sana wa kufanikiwa katika kila jambo wanalolifanya na kulikusudia hakuna cha kuwazuia kwa kufahamu umuhimu wa Umoja Yesu aliwaombea wanafunzi wake wawe na umoja.

Ujumbe.

Wakati fulani kulikuwa na Mzee mmoja aliyeishi na vijana wake watatu huko kijijini, vijana hao walikuwa ni wachapa kazi hodari, hata hivyo walikuwa na tabia ya kugombana sana kila wakati, Mzee wao alijaribu kufanya kila njia ili kuwapatanisha lakini ilishindikana. Ingawa wanakijiji walishukuru na kufurahia utendaji wao wa kazi na bidii waliyokuwa nayo, lakini waliwatania kutokana na ugomvi wao.

Miezi ilipita ikatokea kuwa yule mzee alianza kuugua, aliwaita vijana wake na kuwataka wawe na umoja , lakini hawakusikiliza, aliamua kuwafundisha kivitendo, ili kwamba wasahau tofauti zao na kuungana

Mzee aliwaita vijana na kuwaambia “Nitawapa fimbo nyingi sana na kuzigawanya kwa kila mmoja nataka avunje fimbo hiyo mara mbili, yeye atakayevunja fimbo kwa haraka atapata zawadi”.
Vijana wakakubali.

Mzee aliwapa kundi la fimbo kumikumi kila mmoja na aliwaambia wazivunje vipande vipande, vija na walifanya hivyo kwa dakika chahe sana na kisha wakaanza kugombana kuwa ni nani amekuwa wakwanza

Mzee aliwaambia “wanangu wapendwa kazi bado, Sasa nitawapa kundi moja moja lenye fimbo kumikumi zilizofungwa pamoja na sasa utatakiwa kuvunja kundi zima la fimbo bila kuzitenganisha”
Vijana walikubali na kuanza kutaka kuvunja kundi la fimbo kumikumi kila mmoja na lake, kila mmoja alijaribu kufanya kila aliwezalo ili wazivunje lakini ilishindikana, kisha walitoa taarifa kwa baba yao.

Mzee wao aliwaambia wanangu angalia jinsi mlivyoweza kuvunja fimbo moja moja zilizokuwa peke yake kila moja  kwa urahisi sana, lakini hamkuweza kuzivunja fimbo za aina hiyohiyo zililipokuwa pamoja, kama mtakuwa mnagombana kila wakati na kutengana ni rahisi kwenu kushindwa , Lakini kama mtaungana na kuwa kitu kimoja hakuna atakayewaweza tafadhali sana nawaomba make pamoja

Vijana walielewa nguvu ya umoja na wakamuahidi mzee wao kuwa watakaa pamoja kwa gharama yoyote!.

Kuna nguvu ya mafanikio makubwa katika umoja, kuna siri katika umoja, Kanisa likikaa kwa umoja, ndugu wakikaa kwa umoja, wanandoa wakikaa kwa umoja, familia zikikaa kwa umoja kwaya zikikaa kwa umoja bendi zikikaa kwa umoja, wafanya kazi wakikaa kwa umoja, na taifa letu tukiungana na kuwa kitu kimoja hakuna jambo litaweza kuzuiliwa kwetu

Mwanzo 11:1-7Nchi yote ilikuwa na lugha moja na usemi mmoja. Ikawa watu waliposafiri pande za mashariki waliona nchi tambarare katika nchi ya Shinari; wakakaa huko.Wakaambiana, Haya, na tufanye matofali tukayachome moto. Walikuwa na matofali badala ya mawe, na lami badala ya chokaa. Wakasema, Haya, na tujijengee mji, na mnara, na kilele chake kifike mbinguni, tujifanyie jina; ili tusipate kutawanyika usoni pa nchi yote. BWANA akashuka ili auone mji na mnara waliokuwa wakiujenga wanadamu. BWANA akasema, Tazama, watu hawa ni taifa moja, na lugha yao ni moja; na haya ndiyo wanayoanza kuyafanya, wala sasa hawatazuiliwa neno wanalokusudia kulifanya. Haya, na tushuke huko, tuwachafulie usemi wao ili wasisikilizane maneno wao kwa wao.”

“Ni wazi kuwa Mungu mwenyewe anatambua Nguvu ya umoja anasema wala sasa hawatazuiliwa neno wanalokusudia kulifanya” kumbe watu wakiwa na umoja kuna kuwa na nguvu kubwa ya mafanikio na ndio maana shetani hupenda kupanda mbegu ya mafarakano ili yasiwepo mafanikio. Umoja unaleta upako wa kiroho kama upako wa Haruni, Zaburi 133:1-3Tazama, jinsi ilivyo vema, na kupendeza, Ndugu wakae pamoja, kwa umoja.Ni kama mafuta mazuri kichwani, Yashukayo ndevuni, ndevu za Haruni, Yashukayo mpaka upindo wa mavazi yake. Kama umande wa Hermoni ushukao milimani pa Sayuni. Maana ndiko Bwana alikoamuru baraka, Naam, uzima hata milele”.

Unaona kuna Baraka katika kukaa kwa umoja kinyume chake kuna laana katika mafarakano kaangalie nyumba na familia na ndoa ambazo hawaishi kugombana uone kama kuna maendeleo, angalia pia mataifa wanaopigana wenyewe kwa wenyewe, tukikaa kwa umoja Upako utatiririka kutoka kwa kuhani mkuu Yesu Kristo na kutuletea Baraka wote

Walawi 26:8Na watu watano wa kwenu watawafukuza watu mia, na watu mia wa kwenu watawafukuza watu elfu kumi; na adui zenu wataanguka mbele yenu kwa upanga.

Na Kumbukumbu la torati 32:3 inasema “Mmoja angefukuzaje watu elfu, Wawili wangekimbizaje elfu kumi….

Umoja unaleta ushindi wa kiroho, kupitia umoja kunakuwa na nguvu kubwa ya kumshinda shetani, umoja unazalisha nguvu iitwayo “Mastermind” ambayo ni kama nguvu ya nyuklia inayosababisha kusudi lake liweze kutimia, hakuna kitakachozuiliwa kama watu watakuwa na umoja katika lile wanalokusudia kulifanya.

Na Rev. Innocent Kamote
Mkuu wa wajenzi mwenye Hekima.  

Jumatano, 27 Septemba 2017

Hekima hupita Upumbavu!



Mstari wa Msingi: Muhubiri 2:3 “Ndipo nilipoona ya kuwa kweli hekima hupita upumbavu, kwa kadiri nuru ipitavyo giza



Utangulizi:

Wengi wetu tumewahi kusikia habari za Sulemani kwamba alikuwa mfalme mwenye hekima, lakini wengi wetu tunaweza tusiwe na uelewa wa kutosha kuhusu faida ya hekima, tunapojifunza somo hili fupi sana Pende tu utaiona faida ya Hekima na utagundua umuhimu wa kuomba Hekima.
Zamani sana katika inchi fulani watu waliishi kwa furaha chini ya mfalme mmoja, watu wa ufalme ule walikuwa na maisha ya furaha na amani na walibarikiwa kwa utajiri mwingi sana na hakukuwa na majuto.

Siku moja mfalme aliamua kufanya ziara katika maeneo ya kihistoria ya taifa lile na katika sehemu mbalimbali za makumbusho, aliamua kwamba atatembea kwa miguu ili kwamba apate nafasi ya kusalimiana na watu wake na kuwafahamu kwa ukaribu, watu wa maeneo mbalimbali walifurahia sana kupata nafasi ya kuongea na hata kumuona mafalme kwa ukaribu, walifurahi na kujivunia moyo mwema wa mfalme wao.

Baada ya majuma kadhaa ya ziara ya mfalme, hatimaye alirejea ikulu katika makazi yake, Alikuwa na furaha sana kwa ziara aliyoifanya na kwa kutembelea maeneno muhimu ya taifa lile. Alifurahi kushuhudia watu wake wakiishi maisha ya amani na furaha huku wakiwa wametajirika sana lakini jambo moja tu lilikuwa likimsikitisha sana.

Hakuweza kuvumilia maumivu katika miguu yake, na hasa kwa sababu ilikuwa ni mara yake ya kwanza kufanya ziara ya miguu, alilalamika na kuwaelezea mawaziri wake na kuwaambia kwamba Barabara zetu sio nzuri na nyingi ni za mawe na hivyo yanaumiza sana, alisema nawahurumia sana wananchi wangu ambao wanatumia barabara hizo kwa sababu nao watapata au huwa wanapata maumivu kama niliyoyapata mimi.

Walipofikiri kuhusu hilo, Mfalme aliamuru watumishi wake kupitia wizara ya ujenzi watandaze ngozi katika barabara za nchi yake yote ili watu wa ufalme wake watembee kwa raha!

Mawaziri wote wa mfalme walishitushwa na jambo hili na wakawaza kwa agizo hili ili liweze kutekelezeka hatuna budi kuwa tutachinja ngombe wote inchi nzima ili kupata ngozi ya kutosha kutandaza katika barabara zote, waitafakari kuwa jambo hili litagharimu fedha nyingi sana.

Mwisho waziri mmoja mwenye hekima alikuja na wazo kwa mfalme na kumwambia mfalme nina wazo, Mfalme alimwambia sawa elezea wazo lako, Waziri yule alisema badala ya kufunika barabara zote kwa ngozi, kwa nini tusitumie kipande cha ngozi na kukikata vizuri kwa umbile la kupendeza kisha wewe uvae na kufunika miguu yako?

Mfalme alishangaa sana kwa wazo hilo na hekima aliyokuwa nayo waziri wake akaagiza atengenezewe viatu kwaaajili yake na kisha wakaamuru kila mtu katika ufalme ule avae viatu, watu wote wakaanza kuvaa viatu tangu wakati huo. 

Unaona huwezi kuubadili ulimwengu kabla ya wewe mwenyewe kubadilika!, kama tutakuwa na hekima tutaweza kutatua matatizo mengi sana katika kila eneo la maisha yetu kwa njia ya usahii zaidi, tunaweza kuwa na mawazo mazuri, lakini bila hekima mawazo hayo yakawa yanatumika vibaya na kutugharimu, nd ndio maana Mfalme Sulemani aliona kuwa ni Muhimu kwanza amuombe Mungu hekima 

1Wafalme 3:6-10Sulemani akasema, Umemfanyia mtumwa wako Daudi baba yangu fadhili kuu, kadiri alivyoenenda mbele zako katika kweli, na katika haki, na katika unyofu wa moyo pamoja nawe; nawe umemwekea na fadhili hii kubwa, maana umempa mwana wa kuketi kitini pake kama ilivyo leo. Na sasa, Ee Bwana, Mungu wangu, umenitawaza niwe mfalme mimi mtumwa wako badala ya Daudi baba yangu; nami ni mtoto mdogo tu; sijui jinsi inipasavyo kutoka wala kuingia. Na mtumwa wako yu katikati ya watu wako uliowachagua, watu wengi wasioweza kuhesabiwa, wala kufahamiwa idadi yao, kwa kuwa ni wengi. Kwa hiyo nipe mimi mtumwa wako moyo wa adili niwahukumu watu wako, na kupambanua mema na mabaya; maana ni nani awezaye kuwahukumu hawa watu wako walio wengi? Neno hili likawa jema machoni pa Bwana, ya kuwa Sulemani ameomba neno hili.”

Tunawezaje kuwa na Hekima Biblia inasema tunaweza kumuomba Mungu Hekima lakini pia tunaweza kujifunza hekima

Yakobo 1:5Lakini mtu wa kwenu akipungukiwa na hekima, na aombe dua kwa Mungu, awapaye wote, kwa ukarimu, wala hakemei; naye atapewa”.Unaona tunaweza kuwa na hekima kwa kumuomba Mungu, Mungu ndiye chanzo cha hekima na maarifa yote,  

Mithali 1:7Kumcha Bwana ni chanzo cha maarifa, Bali wapumbavu hudharau hekima na adabu.”

Na. Rev. Innocent Kamote

Mkuu wa wajenzi mwenye hekima!  

Jumanne, 26 Septemba 2017

Heri wenye moyo safi!



Mathayo 5:8 “Heri wenye moyo safi; Maana hao watamwona Mungu
 
Injili maalumu kwa watoto: “Waacheni watoto wadogo waje kwangu msiwazuie maana watoto kama hawa ufalme wa Mungu ni wao”




Siku moja katikati ya umati mkubwa sana wa watu kijana mmoja alisimama na akapiga kelele akisema Jamani niangalieni mimi kwakweli nina moyo Mzuri kuliko watu wote Duniani
Watu wote walishituka na kumwangalia na kweli walishangaa kuona kwamba ana moyo mzuri sana na ulikuwa mkamilifu katika umbile lake na haukuwa na mikwaruzo ya aina yoyote, wote walishangazwa na uzuri wa moyo wake na walimsifu sana. 
 
Hata hivyo baada ya muda kidogo mzee mmoja alisimama na kumwambia kijana Hapana mwanangu mimi nina moyo safi na mzuri zaidi kuliko wa kwako na nina moyo mzuri zaidi kuliko wote duniani
Kijana akamwambia nionyeshe moyo wako! Tuuone

Mzee yule alionyesha Moyo wake, kwa kweli ulikuwa mbaya hauna sura nzuri una majeraha na makovu makubwa ulikuwa umeharibika kiasi ambacho hata ile sura ya moyo haikueleweka vizuri, ulikuwa kama vipande vipande vilivyoungwa.

Kijana alimcheka sana na kumwambia Babu yangu umechanganyikiwa angalia moyo wangu jinsi ulivyo mzuri kweli unaweza kufananisha na wako? Moyo wangu hauna hata mkwaruzo ni mkamilifu katika kila eneo, unaweza kulinganisha na wa kwako kweli? Una majeraha mengi umeungwaungwa umepoteza sura yake kabisa unawezaje kusema kuwa una moyo mzuri kuliko wote Duniani?

Mwanangu moyo wangu ni mzuri kuliko wa kwako alisema mzee yule, umeona majeraha? Umeona makovu, umeona ulivyoungwaungwa?umeona ulivyopoteza sura? Nilinyofoa nyofoa moyo wangu kwa kuwasaidia wengine, nilionyesha matendo ya huruma na upendo kwa watu mbalimbali, lakini wengine hawakunirudishia, niliwatendea watu mema lakini wengine walinirudishia mabaya, kwa hiyo nilitafuta vipande vya nyama nyingine na kuziba sehemu za moyo wangu nilizowapa wengine,

Kijana alishangaa!

Nisikilize kijana wangu moyo wangu ni mzuri kama wa kwako tu unaona makovu haya? Kila kovu linawakilisha sehemu ya moyo wangu nilioutoa kwa wengine, wakati mwingine nilitoa kipande cha moyo kilichokuwa kikubwa zaidi, lakini sikurudishiwa! Kwa sababu niliowapenda wengine walinilipa mabaya, wengine hawakunirudishia, wengine waliuumiza moyo wangu zaidi wengine waliuchoma kwa mkuki na kuufanyia moyo wangu kila walichokitaka,Sehemu nyingine nilitoa moyo wangu wote na wakanirudishia kidogo au wasirudishe kabisa, sehemu nyingine niliwakopesha sehemu ya moyo wangu hawakurudisha aidha wengine niliwapa wakauchezea, nililazimika kuachilia kusamehe na kusahau na kuushona moyo wangu na kuuungauunga na kuutibu ndio maana moyo wangu una majeraha na makovu makubwa, na hauna sura nzuri ya kupendeza kama wako, Moyo wako wewe unaonekana kuwa mzuri kwa sababu hujawahi kutoa hata kipande ukawapa wengine je hili sio kweli?

Kijana alitulia kimyaa na akaishiwa maneno, alianza kutokwa na machozi, alimkumbatia mzee yule na kuuchana moyo wake na kumpa mzee yule kipande.

ISamuel 16:7Lakini Bwana akamwambia Samweli, Usimtazame uso wake, wala urefu wa kimo chake; kwa maana mimi nimemkataa. Bwana haangalii kama binadamu aangaliavyo; maana wanadamu huitazama sura ya nje, bali Bwana huutazama moyo.”

Watu wengi sana huangalia watu kwa umbile la nje na kuwasifu watu kwa umbile la nje lakini Mungu huangalia moyo, umeutumiaje moyo wako kwa wengine moyo wako umejaa nini utu wa mtu utapimwa kulingana na kile anachokitoa kutoka moyoni mwake je wewe unatoa nini kwa watu Mungu huitazama mioyo Marko 7: 15-23Hakuna kitu kilicho nje ya mtu ambacho kikimwingia chaweza kumtia unajisi, bali vile vimtokavyo, ndivyo vimtiavyo unajisi yule mtu.Mtu akiwa na masikio ya kusikilia, na asikie.] Hata alipoingia nyumbani, ameuacha mkutano, wanafunzi wake wakamwuliza habari za ule mfano. Akawaambia, Hivi hata ninyi hamna akili? Hamfahamu ya kwamba kila kitu kilicho nje ya mtu, kikimwingia, hakiwezi kumtia unajisi; kwa sababu hakimwingii moyoni, ila tumboni tu; kisha chatoka kwenda chooni? Kwa kusema hivi alivitakasa vyakula vyote. Akasema, Kimtokacho mtu ndicho kimtiacho unajisi. Kwa maana ndani ya mioyo ya watu hutoka mawazo mabaya, uasherati, wivi, uuaji, uzinzi, tamaa mbaya, ukorofi, hila, ufisadi, kijicho, matukano, kiburi, upumbavu.Haya yote yaliyo maovu yatoka ndani, nayo yamtia mtu unajisi.”

Na mkuu wa Wajenzi mwenye Hekima

Rev. Innocent Kamote.

Jumapili, 24 Septemba 2017

Rafiki aliye na Msaada!

Mstari wa Msingi: Yohana 15:13 “Hakuna aliye na upendo mwingi kuliko huu, wa mtu kuutoa uhai wake kwa ajili ya rafiki zake

Injli Maalumu kwa Watoto. Waacheni watoto wadogo waje kwangu msiwazuie kwa maana watoto kama hawa Ufalme wa Mungu ni wao!


Sungura mmoja mcheshi sana aliishi msituni, kutokana na ucheshi wake aliweza kujipatia marafiki wengi sana wenye nguvu na maarufu sana aliwapenda na kujivunia sana Marafiki zake

Siku moja sungura Mcheshi alikumbana na kundi la mbwa mwitu wakali ambao walikusudia kumla, Sungura mcheshi aliogopa sana na alikimbilia kwa moja ya marafiki zake kwa kusudi la kutafuta msaada, haraka sana alikimbilia kwa swala dume rafki yake wa karibu na kumwambia tafadhali rafiki yangu mpendwa nisaidie kuna kundi la mbwa mwitu wakali wamekudia kunila nyama, najua unaweza kuwafukuzia mbali kupitia pembe zako ndefu ulizo nazo.

Swala alijibu na kusema ni kweli nina pembe ndefu na ninaweza kuwashambulia mbwa mwitu kwa pembe zangu lakini nina shughuli nyingi sana tafadhali mwambie Dubu akusaidie.

Sungura mcheshi alikimbilia kwa Dubu na kumwambia Tafadhali rafiki wewe una nguvu za kutosha niokoe kutoka kwa mbwa mwitu hawa wakali tafadhali, wafukuze tafadhali alimuomba Dubu

Dubu alimjibu, pole sana rafiki yangu nina njaa na nimechoka sana nahitaji kutafuta namna ya kula tafadhali muombe tumbili akusaidie.

Sungura mcheshi alimuendea tumbili, tembo, na nyati na rafiki zake wengine lakini hakuna aliyemsaidia

Alitambua kuwa anapaswa kutafuta namna ya kujitoa katika tatizo hilo mwenyewe, aliamua kupambana na hali yake na kuliitia jina la Mungu aliyemuumba, na kumwambia ee Mungu wagu je uliniumba ili nije kuwa kitowewo cha wengine duniani? ndipo Mungu akamjibu na akamuelekeza kuchimba shimo na kujificha kimyaa ikawa kila Sungura anapoona hali ya Hatari hukimbilia shini ya shimo lile na kuwa salama na kuokoka, Ndipo mbwa mwitu waliendelea kufukuza wanyama wengine na walimkosa Sungura, aliyekuwa salama chini ya shimo!

Sungura alijifunza kumtegemea aliyemuumba kwaajili ya kutunza uhai wake na sio kuwategemea rafiki zake, sungura alitambua kuwa mwenye uchungu na yeye ni yule aliyemuumba tu!

Yeremia 17:5 “Bwana asema hivi, Amelaaniwa mtu yule amtegemeaye mwanadamu, Amfanyaye mwanadamu kuwa kinga yake Na moyoni mwake amemwacha Bwana. Maana atakuwa kama fukara nyikani, Hataona yatakapotokea mema; Bali atakaa jangwani palipo ukame, Katika nchi ya chumvi isiyokaliwa na watu. Amebarikiwa mtu yule anayemtegemea Bwana, Ambaye Bwana ni tumaini lake. Maana atakuwa kama mti uliopandwa kando ya maji, Uenezao mizizi yake karibu na mto; Hautaona hofu wakati wa hari ujapo, Bali jani lake litakuwa bichi; Wala hautahangaika mwaka wa uchache wa mvua, Wala hautaacha kuzaa matunda.

Tunajifunza: “Kumtegemea Mungu na kumfanya aliyetuumba kuwa rafiki yetu wa Kweli”
Mkuu wa wajenzi mwenye Hekima

Rev. Innocent Kamote
Yesu kwetu ni rafiki,
Huambiwa haja pia,
Tukiomba kwa Babaye
Maombi asikia,
Lakini twajikosesha,
Twajitweka vibaya,
Kwamba tukimwomba Mungu,
Dua atasikia.

Una dhiki na maonjo?
Una mashaka pia?
Haifai kufa moyo,
Dua atasikia.
Hakuna mwingine mwema
Wa kutuhurumia
Atujua tu dhaifu,
Maombi asikia.

Je, hunazo hata nguvu,
Huwezi kwendelea?
Ujapodharauliwa,
Ujaporushwa pia,
Watu wangekudharau,
Wapendao dunia
Hukwambata mikononi,
Dua atasikia

Jumatatu, 18 Septemba 2017

Mfano wa kuku avikusanyae vifaranga vyake!


Luka 13:34.

Ee Yerusalemu, Yerusalemu, uwauaye manabii na kuwapiga kwa mawe waliotumwa kwako, mara ngapi nimetaka kuwakusanya watoto wako kama vile kuku avikusanyavyo vifaranga vyake chini ya mbawa zake, wala hamkutaka.”
 
Mathayo 23:37

Ee Yerusalemu, Yerusalemu, uwauaye manabii, na kuwapiga kwa mawe wale waliotumwa kwako! Ni mara ngapi nimetaka kuwakusanya pamoja watoto wako, kama vile kuku avikusanyavyo pamoja vifaranga vyake chini ya mabawa yake, lakini hamkutaka!

Utangulizi:

Leo tutachukua muda kujifunza na kutafakari kwa kina kuhusu maneno haya ya Yesu, ambayo kitaalamu inaaminika yalizungumzwa wakati Yesu anaulilia mji wa Yerusalem siku chache kabla ya kusulubiwa kwake 

Luka 19:41- 44 “Alipofika karibu aliuona mji, akaulilia, akisema, Laiti ungalijua, hata wewe katika siku hii, yapasayo amani! Lakini sasa yamefichwa machoni pako. Kwa kuwa siku zitakuja, adui zako watakapokujengea boma, likuzunguke; watakuzingira na kukuhusuru pande zote; watakuangusha chini wewe na watoto wako ndani yako, wasikuachie jiwe juu ya jiwe, kwa sababu hukutambua majira ya kujiliwa kwako 

wataalamu wengi wa kimaandiko tunaamini kuwa huenda Yesu alizungumza maneno yale pale juu katika wakati huu, ingawa waandishi waliyaweka katika vifungu vingine kwaajili ya kusisitiza umuhimu wa kile walichotaka kukiwakilisha chini ya uongozi wa Roho Mtakatifu,  kwa vyovyote vile Yesu alikuwa akifanya maombolezo kwaajili ya jiji la Yerusalem ambalo lingeshuhudia hukumu kubwa miaka michache kama 37  ijayo,  Yesu alikuwa akiulilia mji wa Yerusalem kutokana na tabia yake ya kuwaua Manabii, wenye hekima na walimu,(waandishi). Lakini sio hivyo tu bali pia kulikuwa na mpango wa kumuua Yesu mwenyewe na Yesu alitambua mpango huo, sio tu Yesu angeuawa bali hata wale atakaowatuma wangeuawa 

Mathayo 23:34 “Kwa sababu hiyo, angalieni, mimi natuma kwenu manabii na wenye hekima na waandishi; na wengine wao ninyi mtawaua na kuwasulibisha, na wengine wao mtawapiga katika masinagogi yenu, na kuwafukuza mji kwa mji

 Yesu alikuwa akitabiri kuwa tabia ya watu wa Israel kuwatendea vibaya manabii, siku moja ingefikia mwisho na kuwa hukumu kwaajili ya mji wa Yerusalem ingefika na kila kitu kingesambaratishwa, Yesu anatangaza hukumu mbaya sana katika Yerusalem na Israel kutokana na tabia na mwenendo wake mbaya wa kile inachokifanya dhidi ya watu wa Mungu. Lakini katika maonyo hayo  Mazito hakukuwa na nafasi ya rehema tena kwani neno la Yesu lilitimizwa sawa sawa na unabii wake Katika mwaka wa 70 AD Yerusalem uliteketezwa kwa moto na wayahudi waliuawa kila mahali na waliikimbia inchi yao mpaka waliporejea tena miaka ya 1940 na kupata uhuru 1948. Israel ilikuwa imekataa mpango wa Mungu. Miaka 27 tu ilipita tangu YESU alipopaa mwaka wa 33

Yesu katika maonyo yake alibainisha wazi sababu za Israel kuangukia katika hukumu ya Mungu ni kwa sababu ilikataa mpango wa Mungu wa upendo. Mungu alikuwa na Mapenzi mema na Israel kila ambacho Mungu alikuwa amekikusudia kimefichwa katika Mfano wa kuku akusanyaye vifaranga vyake 

Kwanini wakati huu Mungu anatumia mfano wa kuku avikusanyee vifaranga vyake? Ukweli ni kuwa kuku ana mambo kadhaa muhimu ya kujifunza na Yesu aliutumia mfano huu kwa sababu katika mazingira ya kawaida ya wakati huo Israel walifuga kuku sawa na mazingira ya kawaida ya kitanzania na Afrika kwa siku za zamani, kuku wa kienyeji walifugwa kwa njia ya asili na ya kawaida tofauti na nyakati za leo.

Mfano wa kuku avikusanyae vifaranga vyake 

Kuku anapotaka kuwa na vifaranga jambo la kwanza anataka mayai ya kutosha  Jambo hili linatufundisha MPANGO MWEMA – Mungu ana mpango mwema na kila mmoja kama alivyokuwa na mpango mwena na Israel Yeremia 29:11-13. “Maana nayajua mawazo ninayowawazia ninyi, asema Bwana, ni mawazo ya amani wala si ya mabaya, kuwapa ninyi tumaini siku zenu za mwisho. Nanyi mtaniita, mtakwenda na kuniomba, nami nitawasikiliza. Nanyi mtanitafuta na kuniona, mtakaponitafuta kwa moyo wenu wote”.


Kuku anapoanza kulalia ili aweze kutotoa anapunzuza mizunguko yaani hazuruli hovyo jambo hili linatufundisha kujitia NIDHAMU

Wakati kuku anapolalia mayai yake huwa anapungua uzito anakonda KUJIKANA 

Kuku anapolalia huwa hajali analalia mayai ya kuku mwingine au hata ya kanga yeye hulalia tu bila ubaguzi hii inatufundisha UKARIMU hana UBAGUZI wala UPENDELEO

Kuku ili aweze kutotoa anapaswa kulalia kwa siku 21 kwa kuvumilia hii inatufundisha UVUMILIVU

Kuku anapolalia anaweza kujua yai lenye kifaranga na yai lililoviza hii inatufundisha kuwa anauwezo wa KUPAMBANUA na KUTABIRI

Kuku baada ya kutotoa  anaacha mayai viza na anatunza vifaranga vyake hii inatufundisha kuwa kuku ana HEKIMA huwezi kumbeba asiyebebeka.

Hakuna anayeweza kukigusa kifaranga chake hii inatufundisha kuwa uko ULINZI WA MUNGU Na upendo wake na kujali

Anakusanya vifaranga vyake chini ya Mbawa zake ni hali ya kuhakikisha wanakuwa na UMOJA na kuwatunza hawagawanyi ili awatawale 

Hawezi kuwaacha mpaka wakue yaani inatufundisha kuwa kuku anafundisha UALIMU

Mungu alikuwa ana makusudi mema na Israel, alikuwa nawqwawazia mema na amani, Mungu alitoa muda wake kwa israel zaidi kuliko mataifa mengine, Mungu alimleta masihi kwa Israel na ulimwengu mzima ili, Mungu alitoa neema yake bila upendeleo, Mungu alikuwa akiwavumilia ili wazae matunda, Mungu aliamini kuwa siku moja watu wake watakomaa, Mungu alikusudia kuwa mwalimu kwa kila mmoja lakini kutokana na Israel kuendelea kukataa mapenzi ya Mungu, Yesu alitangaza hukumu,  na maangamizi kutokana na jeuri ya kuendelea kukataa maonyo na kuwakataa manabii.

Je ni mara ngapi tumekataa maonyo kutoka kwa watumishi wa Mungu  ambao Mungu aliwatuma kwetu kwa makusudi mema ni mara ngapi tumewaua na kuwapiga kwa mawe wale wanaotumwa kwetu, hali ya kutokukubali maonyo itatuletea hukumu ya Mungu

Na mkuu wa wajenzi mwenye Hekima!
Rev. Innocent Kamote.