Luka 13:34.
“Ee Yerusalemu, Yerusalemu,
uwauaye manabii na kuwapiga kwa mawe waliotumwa kwako, mara ngapi nimetaka
kuwakusanya watoto wako kama vile kuku avikusanyavyo vifaranga vyake chini ya
mbawa zake, wala hamkutaka.”
Mathayo 23:37
“Ee
Yerusalemu, Yerusalemu, uwauaye manabii, na kuwapiga kwa mawe wale
waliotumwa kwako! Ni mara ngapi nimetaka kuwakusanya pamoja watoto wako,
kama vile kuku avikusanyavyo pamoja vifaranga vyake chini ya mabawa
yake, lakini hamkutaka!”
Utangulizi:
Leo
tutachukua muda kujifunza na kutafakari kwa kina kuhusu maneno haya ya
Yesu, ambayo kitaalamu inaaminika yalizungumzwa wakati Yesu anaulilia
mji wa Yerusalem siku chache kabla ya kusulubiwa kwake
Luka 19:41- 44 “Alipofika
karibu aliuona mji, akaulilia, akisema, Laiti ungalijua, hata wewe
katika siku hii, yapasayo amani! Lakini sasa yamefichwa machoni pako.
Kwa kuwa siku zitakuja, adui zako watakapokujengea boma, likuzunguke;
watakuzingira na kukuhusuru pande zote; watakuangusha chini wewe na
watoto wako ndani yako, wasikuachie jiwe juu ya jiwe, kwa sababu
hukutambua majira ya kujiliwa kwako”
wataalamu
wengi wa kimaandiko tunaamini kuwa huenda Yesu alizungumza maneno yale
pale juu katika wakati huu, ingawa waandishi waliyaweka katika vifungu
vingine kwaajili ya kusisitiza umuhimu wa kile walichotaka kukiwakilisha
chini ya uongozi wa Roho Mtakatifu, kwa vyovyote vile Yesu alikuwa
akifanya maombolezo kwaajili ya jiji la Yerusalem ambalo lingeshuhudia
hukumu kubwa miaka michache kama 37 ijayo, Yesu alikuwa akiulilia mji
wa Yerusalem kutokana na tabia yake ya kuwaua Manabii, wenye hekima na
walimu,(waandishi). Lakini sio hivyo tu bali pia kulikuwa na mpango wa
kumuua Yesu mwenyewe na Yesu alitambua mpango huo, sio tu Yesu angeuawa
bali hata wale atakaowatuma wangeuawa
Mathayo 23:34 “Kwa
sababu hiyo, angalieni, mimi natuma kwenu manabii na wenye hekima na
waandishi; na wengine wao ninyi mtawaua na kuwasulibisha, na wengine wao
mtawapiga katika masinagogi yenu, na kuwafukuza mji kwa mji”
Yesu
alikuwa akitabiri kuwa tabia ya watu wa Israel kuwatendea vibaya
manabii, siku moja ingefikia mwisho na kuwa hukumu kwaajili ya mji wa
Yerusalem ingefika na kila kitu kingesambaratishwa, Yesu anatangaza
hukumu mbaya sana katika Yerusalem na Israel kutokana na tabia na
mwenendo wake mbaya wa kile inachokifanya dhidi ya watu wa Mungu. Lakini
katika maonyo hayo Mazito hakukuwa na nafasi ya rehema tena kwani neno
la Yesu lilitimizwa sawa sawa na unabii wake Katika mwaka wa 70 AD
Yerusalem uliteketezwa kwa moto na wayahudi waliuawa kila mahali na
waliikimbia inchi yao mpaka waliporejea tena miaka ya 1940 na kupata
uhuru 1948. Israel ilikuwa imekataa mpango wa Mungu. Miaka 27 tu ilipita
tangu YESU alipopaa mwaka wa 33
Yesu
katika maonyo yake alibainisha wazi sababu za Israel kuangukia katika
hukumu ya Mungu ni kwa sababu ilikataa mpango wa Mungu wa upendo. Mungu
alikuwa na Mapenzi mema na Israel kila ambacho Mungu alikuwa
amekikusudia kimefichwa katika Mfano wa kuku akusanyaye vifaranga vyake
Kwanini
wakati huu Mungu anatumia mfano wa kuku avikusanyee vifaranga vyake?
Ukweli ni kuwa kuku ana mambo kadhaa muhimu ya kujifunza na Yesu
aliutumia mfano huu kwa sababu katika mazingira ya kawaida ya wakati huo
Israel walifuga kuku sawa na mazingira ya kawaida ya kitanzania na
Afrika kwa siku za zamani, kuku wa kienyeji walifugwa kwa njia ya asili
na ya kawaida tofauti na nyakati za leo.
Mfano wa kuku avikusanyae vifaranga vyake
Kuku anapotaka kuwa na vifaranga jambo la kwanza anataka mayai ya kutosha Jambo hili linatufundisha MPANGO MWEMA – Mungu ana mpango mwema na kila mmoja kama alivyokuwa na mpango mwena na Israel Yeremia 29:11-13. “Maana
nayajua mawazo ninayowawazia ninyi, asema Bwana, ni mawazo ya amani
wala si ya mabaya, kuwapa ninyi tumaini siku zenu za mwisho. Nanyi
mtaniita, mtakwenda na kuniomba, nami nitawasikiliza. Nanyi mtanitafuta
na kuniona, mtakaponitafuta kwa moyo wenu wote”.
Kuku anapoanza kulalia ili aweze kutotoa anapunzuza mizunguko yaani hazuruli hovyo jambo hili linatufundisha kujitia NIDHAMU
Wakati kuku anapolalia mayai yake huwa anapungua uzito anakonda KUJIKANA
Kuku anapolalia huwa hajali analalia mayai ya kuku mwingine au hata ya kanga yeye hulalia tu bila ubaguzi hii inatufundisha UKARIMU hana UBAGUZI wala UPENDELEO.
Kuku ili aweze kutotoa anapaswa kulalia kwa siku 21 kwa kuvumilia hii inatufundisha UVUMILIVU
Kuku anapolalia anaweza kujua yai lenye kifaranga na yai lililoviza hii inatufundisha kuwa anauwezo wa KUPAMBANUA na KUTABIRI
Kuku baada ya kutotoa anaacha mayai viza na anatunza vifaranga vyake hii inatufundisha kuwa kuku ana HEKIMA huwezi kumbeba asiyebebeka.
Hakuna anayeweza kukigusa kifaranga chake hii inatufundisha kuwa uko ULINZI WA MUNGU Na upendo wake na kujali
Anakusanya vifaranga vyake chini ya Mbawa zake ni hali ya kuhakikisha wanakuwa na UMOJA na kuwatunza hawagawanyi ili awatawale
Hawezi kuwaacha mpaka wakue yaani inatufundisha kuwa kuku anafundisha UALIMU
Mungu
alikuwa ana makusudi mema na Israel, alikuwa nawqwawazia mema na amani,
Mungu alitoa muda wake kwa israel zaidi kuliko mataifa mengine, Mungu
alimleta masihi kwa Israel na ulimwengu mzima ili, Mungu alitoa neema
yake bila upendeleo, Mungu alikuwa akiwavumilia ili wazae matunda, Mungu
aliamini kuwa siku moja watu wake watakomaa, Mungu alikusudia kuwa
mwalimu kwa kila mmoja lakini kutokana na Israel kuendelea kukataa
mapenzi ya Mungu, Yesu alitangaza hukumu, na maangamizi kutokana na
jeuri ya kuendelea kukataa maonyo na kuwakataa manabii.
Je
ni mara ngapi tumekataa maonyo kutoka kwa watumishi wa Mungu ambao
Mungu aliwatuma kwetu kwa makusudi mema ni mara ngapi tumewaua na
kuwapiga kwa mawe wale wanaotumwa kwetu, hali ya kutokukubali maonyo
itatuletea hukumu ya Mungu
Na mkuu wa wajenzi mwenye Hekima!
Rev. Innocent Kamote.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni