Mstari wa Msingi: Muhubiri 2:3 “Ndipo nilipoona
ya kuwa kweli hekima hupita upumbavu, kwa kadiri nuru ipitavyo giza”
Utangulizi:
Wengi wetu tumewahi kusikia habari za Sulemani kwamba
alikuwa mfalme mwenye hekima, lakini wengi wetu tunaweza tusiwe na uelewa wa
kutosha kuhusu faida ya hekima, tunapojifunza somo hili fupi sana Pende tu
utaiona faida ya Hekima na utagundua umuhimu wa kuomba Hekima.
Zamani sana katika inchi fulani watu waliishi kwa furaha
chini ya mfalme mmoja, watu wa ufalme ule walikuwa na maisha ya furaha na amani
na walibarikiwa kwa utajiri mwingi sana na hakukuwa na majuto.
Siku moja mfalme aliamua kufanya ziara katika maeneo ya
kihistoria ya taifa lile na katika sehemu mbalimbali za makumbusho, aliamua
kwamba atatembea kwa miguu ili kwamba apate nafasi ya kusalimiana na watu wake
na kuwafahamu kwa ukaribu, watu wa maeneo mbalimbali walifurahia sana kupata
nafasi ya kuongea na hata kumuona mafalme kwa ukaribu, walifurahi na kujivunia
moyo mwema wa mfalme wao.
Baada
ya majuma kadhaa ya ziara ya mfalme, hatimaye alirejea ikulu katika makazi
yake, Alikuwa na furaha sana kwa ziara aliyoifanya na kwa kutembelea maeneno
muhimu ya taifa lile. Alifurahi kushuhudia watu wake wakiishi maisha ya amani
na furaha huku wakiwa wametajirika sana lakini jambo moja tu lilikuwa
likimsikitisha sana.
Hakuweza
kuvumilia maumivu katika miguu yake, na hasa kwa sababu ilikuwa ni mara yake ya
kwanza kufanya ziara ya miguu, alilalamika na kuwaelezea mawaziri wake na
kuwaambia kwamba Barabara zetu sio nzuri na nyingi ni za mawe na hivyo
yanaumiza sana, alisema nawahurumia sana wananchi wangu ambao wanatumia
barabara hizo kwa sababu nao watapata au huwa wanapata maumivu kama
niliyoyapata mimi.
Walipofikiri
kuhusu hilo, Mfalme aliamuru watumishi wake kupitia wizara ya ujenzi watandaze
ngozi katika barabara za nchi yake yote ili watu wa ufalme wake watembee kwa
raha!
Mawaziri
wote wa mfalme walishitushwa na jambo hili na wakawaza kwa agizo hili ili
liweze kutekelezeka hatuna budi kuwa tutachinja ngombe wote inchi nzima ili
kupata ngozi ya kutosha kutandaza katika barabara zote, waitafakari kuwa jambo
hili litagharimu fedha nyingi sana.
Mwisho
waziri mmoja mwenye hekima alikuja na wazo kwa mfalme na kumwambia mfalme nina
wazo, Mfalme alimwambia sawa elezea wazo lako, Waziri yule alisema badala ya
kufunika barabara zote kwa ngozi, kwa nini tusitumie kipande cha ngozi na
kukikata vizuri kwa umbile la kupendeza kisha wewe uvae na kufunika miguu yako?
Mfalme
alishangaa sana kwa wazo hilo na hekima aliyokuwa nayo waziri wake akaagiza
atengenezewe viatu kwaaajili yake na kisha wakaamuru kila mtu katika ufalme ule
avae viatu, watu wote wakaanza kuvaa viatu tangu wakati huo.
Unaona
huwezi kuubadili ulimwengu kabla ya wewe mwenyewe kubadilika!, kama tutakuwa na
hekima tutaweza kutatua matatizo mengi sana katika kila eneo la maisha yetu kwa
njia ya usahii zaidi, tunaweza kuwa na mawazo mazuri, lakini bila hekima mawazo
hayo yakawa yanatumika vibaya na kutugharimu, nd ndio maana Mfalme Sulemani
aliona kuwa ni Muhimu kwanza amuombe Mungu hekima
1Wafalme 3:6-10“Sulemani
akasema, Umemfanyia mtumwa wako Daudi baba yangu fadhili kuu, kadiri
alivyoenenda mbele zako katika kweli, na katika haki, na katika unyofu wa moyo
pamoja nawe; nawe umemwekea na fadhili hii kubwa, maana umempa mwana wa kuketi
kitini pake kama ilivyo leo. Na sasa, Ee Bwana, Mungu wangu, umenitawaza niwe
mfalme mimi mtumwa wako badala ya Daudi baba yangu; nami ni mtoto mdogo tu;
sijui jinsi inipasavyo kutoka wala kuingia. Na mtumwa wako yu katikati ya watu
wako uliowachagua, watu wengi wasioweza kuhesabiwa, wala kufahamiwa idadi yao,
kwa kuwa ni wengi. Kwa hiyo nipe mimi mtumwa wako moyo wa adili niwahukumu watu
wako, na kupambanua mema na mabaya; maana ni nani awezaye kuwahukumu hawa watu
wako walio wengi? Neno hili likawa jema machoni pa Bwana, ya kuwa Sulemani
ameomba neno hili.”
Tunawezaje
kuwa na Hekima Biblia inasema tunaweza kumuomba Mungu Hekima lakini pia
tunaweza kujifunza hekima
Yakobo 1:5
“Lakini mtu wa kwenu akipungukiwa na hekima, na
aombe dua kwa Mungu, awapaye wote, kwa ukarimu, wala hakemei; naye atapewa”.Unaona
tunaweza kuwa na hekima kwa kumuomba Mungu, Mungu ndiye chanzo cha hekima na
maarifa yote,
Mithali 1:7 “Kumcha Bwana ni chanzo cha maarifa, Bali wapumbavu
hudharau hekima na adabu.”
Na. Rev. Innocent Kamote
Mkuu wa wajenzi mwenye hekima!
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni