Mstari wa Msingi: Matendo 2:38 “Petro akawaambia, Tubuni mkabatizwe kila
mmoja kwa jina lake Yesu Kristo, mpate ondoleo la dhambi zenu, nanyi mtapokea
kipawa cha Roho Mtakatifu.”
Utangulizi:
“Tubuni” alisema Petro, Hii
ilikuwa sehemu muhimu ya ujumbe wa Petro iliyotolewa chini ya uwepo wa Roho
Mtakatifu siku ya Pentekoste siku ambayo ilikuwa sikukuu kwa Wayahudi lakini
Mungu katika mpango wake alikusudia Kanisa lizaliwe, Toba ilikuwa ni sehemu
muhimu kwa watu kupokea Roho Mtakatifu, Toba ilikuwa ni sehemu muhimu mara
kanisa lilipoanza, toba lilikuwa ni jibu Muhimu kwa swali muhimu lililoulizwa
katika Matendo 2:37 “Walipoyasikia haya wakachomwa mioyo yao, wakamwambia
Petro na mitume wengine, Tutendeje, ndugu zetu?”
Toba ni sehemu muhimu sana katika
msingi wa imani ya Kikristo, Mwandishi wa kitabu cha Waebrania anaiweka toba
kama moya ya mafundisho ya awali ya Kristo Waebrani
6:1-2 “Kwa sababu hiyo, tukiacha kuyanena
mafundisho ya kwanza ya Kristo, tukaze mwendo ili tuufikilie utimilifu;
tusiweke msingi tena wa kuzitubia kazi zisizo na uhai, na wa kuwa na imani kwa
Mungu, na wa mafundisho ya mabatizo, na kuwekea mikono, na kufufuliwa wafu, na
hukumu ya milele.” Waebrania 5:12 pia, kwa msingi huo
kama toba ni moja wapo ya msingi muhimu katika imani yetu haipaswi kupuuziwa
hata kidogo.
Kimsingi mafundisho na ukweli
kuhusu toba katika agano jipya hauwezi kupuuziwa Hasa ukizingatia kuwa toba
ilikuwa ni kiini kikuu au kilele cha mahubiri ya watu wote maarufu katika agano
jipya
·
Yohana mbatizaji alihubiri toba Mathayo 3:1-2 “Siku
zile aliondokea Yohana Mbatizaji akihubiri katika nyika ya Uyahudi, na kusema,
Tubuni; kwa maana ufalme wa mbinguni umekaribia.”
·
Yesu Kristo alihubiri toba Mathayo 4:17 “Tokea wakati huo Yesu
alianza kuhubiri, na kusema, Tubuni; kwa maana ufalme wa mbinguni umekaribia.”
·
Paulo Mtume alihubiri toba Matendo 20:21 “nikiwashuhudia Wayahudi
na Wayunani wamtubie Mungu, na kumwamini Bwana wetu Yesu Kristo”
Kwa msingi huo basi si jambo la
kushangaza kuona Yesu akiwaagiza wanafunzi wake kuhubiri na kuwafanya mataifa
yote kuwa wanafunzi huku kiini cha ujumbe kikiwa tubuni kwa maana ufalme wa
Mungu umekaribia Mathayo 28:19-20 “Basi, enendeni, mkawafanye mataifa yote kuwa wanafunzi,
mkiwabatiza kwa jina la Baba, na Mwana, na Roho Mtakatifu; na kuwafundisha
kuyashika yote niliyowaamuru ninyi; na tazama, mimi nipo pamoja nanyi siku
zote, hata ukamilifu wa dahari”
Luka 24:47 “na kwamba mataifa yote
watahubiriwa kwa jina lake habari ya toba na ondoleo la dhambi, kuanza tangu
Yerusalemu.”
Kwa hiyo unaweza kuona kuwa toba
ndio msingi wa mafundisho ya ukristo, awaye yote anayebatizwa katika ukristo
kwanza ni lazima awe na uelewa kamili wa maana ya toba, anapaswa aelewe wazi,
huzuni ya kimungu, Neema ya Mungu na imani iokoayo.
Kwani toba ni agizo kuu kwa watu
wote wa aina zote wa mahali popote Matendo
17:30 “Basi, zamani zile za ujinga Mungu
alijifanya kama hazioni; bali sasa anawaagiza watu wote wa kila mahali watubu.”
Kwa msingi huo basi ni muhimu
kufahamu kuwa Toba ni mojawapo ya somo linalotakiwa kufuatiliwa kwa makini na
kwa undani zaidi, toba ni sehemu muhimu sana katika kujiunga na ufalme wa Mungu
Dr, David A DeSilva alisema “toba ni neema ya Mungu yenye kurejesha uhusiano wa
Mungu na mwanadamu”
Zifuataza sasa ni siri kuu muhimu
kuhusu toba.
1.
Toba
ni badiliko la nia na tabia.
Tunzapozungumzia
toba kwa ufupi tunasema toba ni badiliko la nia na tabia, ni kuachana na njia
ya kwanza ya kawaida uliyokuwa ukiifuata kuelekea katika njia nyingine
unayopaswa kuifuata, kuacha kufuata nia ya mwili wako na kufuata nia ya Mungu,
mwanadamu anapoamua kubadilisha nia yake na mtazamo wake mara moja na tabia
yake hubadilika
Warumi 12:2 “Wala
msiifuatishe namna ya dunia hii; bali mgeuzwe kwa kufanywa upya nia zenu, mpate
kujua hakika mapenzi ya Mungu yaliyo mema, ya kumpendeza, na ukamilifu.”
Mathayo 21:28-32 “Lakini mwaonaje? Mtu mmoja alikuwa na wana wawili;
akamwendea yule wa kwanza, akasema, Mwanangu, leo nenda kafanye kazi katika
shamba la mizabibu. Akajibu akasema, Naenda, Bwana; asiende. Akamwendea yule wa
pili, akasema vile vile. Naye akajibu akasema, Sitaki; baadaye akatubu,
akaenda. Je! Katika hao wawili ni yupi aliyefanya mapenzi ya babaye?
Wakamwambia, Ni yule wa pili. Basi Yesu akawaambia, Amin nawaambia, watoza
ushuru na makahaba wanatangulia mbele yenu kuingia katika ufalme wa Mungu. .
Kwa sababu Yohana alikuja kwenu kwa njia ya haki, ninyi msimwamini; lakini
watoza ushuru na makahaba walimwamini, nanyi hata mlipoona, hamkutubu baadaye,
ili kumwamini.”
Toba huambatana
na kutii na kutenda mapenzi ya Mungu,toba inamtoa mtu kutoka katika mtazamo
hasi aliokuwa nao kuelekea katika mtazamo chanya toba inaleta badiliko kuu sana
katika maisha ya mtu, kwa mfano wote tunatambua jinsi Paulo mtume alivyokuwa
katika njia zake alikuwa tishio kubwa sana la Ukristo na alidhamiria
kuhakikisha kuwa anawashughulikia wakristo kama watu wahalifu
Matendo 9:1-2, “Lakini Sauli, akizidi kutisha na kuwaza kuwaua wanafunzi
wa Bwana, akamwendea Kuhani Mkuu, akataka ampe barua za kuenda Dameski
zilizoandikwa kwa masinagogi, ili akiona watu wa Njia hii, waume kwa wake,
awafunge na kuwaleta Yerusalemu.” Mtu huyuhuyu ambaye alikuwa na nia
mbaya kuhusu Wakristo na aliyetumia nguvu zake nyingi kuwasumbua wakristo sasa
alipotubu alibadilika na kuwa mtu mwingine akithibitisha kuwa Yesu kristo ni
Bwana
Matendo 9: 20-22 “20. Mara akamhubiri Yesu katika masinagogi, kwamba yeye
ni Mwana wa Mungu. Na wote
waliosikia wakashangaa, wakasema, Siye huyu aliyewaharibu walioliitia Jina hili
huko Yerusalemu? Na hapa alikuwa amekuja kwa kusudi hilo, awafunge na
kuwapeleka kwa wakuu wa makuhani? Sauli
akazidi kuwa hodari, akawatia fadhaa Wayahudi waliokaa Dameski, akithibitisha
ya kuwa huyu ndiye Kristo.”
Tunapozungumzia
toba maana yake ni ufunguo mkubwa wa mabadiliko ya akili yaani nia na tabia mtu
anapodai kuwa ametubu hatarajiwi kuonekana na tabia zile za kwanza tena lakini
anapaswa kuwa na matendo mapya yanayoendana na toba yake Matendo 26:20 “bali kwanza niliwahubiri
wale wa Dameski na Yerusalemu, na katika nchi yote ya Uyahudi, na watu wa
Mataifa, kwamba watubu na kumwelekea Mungu, wakiyatenda matendo yanayopatana na
kutubu kwao.”
2.
Toba
humfanya Mungu arudishe uhusiano na sisi.
Dhambi
zinaharibu uhusiano mwema na Mungu, Mungu hasikilizi wenye dhambi Yohana 9:31 “Twajua
ya kuwa Mungu hawasikii wenye dhambi; bali mtu akiwa ni mcha Mungu, na
kuyafanya mapenzi yake, humsikia huyo.” Yesu Kristo alihakikisha kuwa
anadumisha uhusiano wake na Mungu wakati wote alimtii Mungu na hivyo
alisikilizwa sana na Mungu na hatimaye kuwa sababu ya wokou kwa watu wote
Waebrania 5:7-9 “Yeye, siku hizo za mwili wake, alimtolea yule, awezaye
kumwokoa na kumtoa katika mauti, maombi na dua pamoja na kulia sana na machozi,
akasikilizwa kwa jinsi alivyokuwa mcha Mungu; na, ingawa ni Mwana, alijifunza
kutii kwa mateso hayo yaliyompata; naye
alipokwisha kukamilishwa, akawa sababu ya wokovu wa milele kwa watu wote
wanaomtii;” Toba ni kurejesha uhusiano na Mungu na ambao ulivunjika au
unavunjika kutokana na kutokutii au dhambi, ni mbaya sana kupoteza uhusiano na
Mungu. Hakuna jambo zuri sana duniani kama kuwa na uhusiano na Mungu, mwanadamu
kukosa uhusiano na Mungu ni sawa na kufariki dunia kabla ya wakati, hatuwezi
kuwa na amani ya kweli kama hatuna amani na Mungu, kwa hiyo ni muhimu sana
kurejesha uhusiano wetu na Mungu, watu wengi wanatamani lakini uhusiano wao na
Mungu umevunjika Dhambi zinazuia uhusiano mwema na Mungu na ndio maana Mungu
anatoa wito wa sisi kumrudia yeye
Isaya
59:1-2 “. Tazama, mkono wa Bwana haukupunguka,
hata usiweze kuokoa wala sikio lake si zito, hata lisiweze kusikia; lakini
maovu yenu yamewafarikisha ninyi na Mungu wenu, na dhambi zenu zimeuficha uso
wake msiuone, hata hataki kusikia.” Sababu kubwa ya watu wengi kupoteza
uhusiano na Mungu ni makosa na dhambi Lakini Mungu anasema ameweka njia ameweka
mwaliko ambao tunaweza kuutumia kurudisha uhusiano wetu na Mungu, njia hii ni
toba pekee, kupitia njia hii anaweza kutusamehe, kuturejesha na kutusafisha.
1Yohana 1: 8-10 “Tukisema kwamba hatuna dhambi, twajidanganya wenyewe,
wala kweli haimo mwetu. Tukiziungama dhambi zetu, Yeye ni mwaminifu na wa haki
hata atuondolee dhambi zetu, na kutusafisha na udhalimu wote.Tukisema kwamba
hatukutenda dhambi, twamfanya Yeye kuwa mwongo wala neno lake halimo mwetu”.
Mungu anatuthibitishia kuwa yuko tayari kusamehe na kutufikia na kuturudia
endapo sisi tutakubali kufanya sehemu yetu yaani kutubu kwa kumaanisha kuacha.
Zekaria 1:3 “Basi,
uwaambie, Bwana wa majeshi asema hivi, Nirudieni mimi, asema Bwana wa majeshi,
nami nitawarudia ninyi, asema Bwana wa majeshi.”
2Nyakati 7:12-14 “Bwana akamtokea Sulemani usiku, akamwambia, Nimesikia
uliyoyaomba, na mahali hapa nimejichagulia kuwa nyumba ya dhabihu. Nikizifunga
mbingu isiwe mvua, tena nikiamuru nzige kula nchi, au nikiwapelekea watu wangu
tauni; ikiwa watu wangu, walioitwa kwa jina langu, watajinyenyekesha, na
kuomba, na kunitafuta uso, na kuziacha njia zao mbaya; basi, nitasikia toka
mbinguni, na kuwasamehe dhambi yao, na kuiponya nchi yao.”
Wakati wote
Mungu ametamani sana kuwa na uhusiano thabiti na sisi, au na mimi na wewe
lakini kikwazo kikubwa ni dhambi na maovu ni wito wa rehema na neema ya Mungu
na ahadi zake kubwa kwetu kwamba tukimuita atatuitikia, Kama tunahitaji
uponyaji kwa taifa letu na maisha yetu na mafanikio na baraka na mvua nzuri ni
toba pekee inayoweza kufungua milango ya Baraka kwa Mungu wetu.
3.
Toba
ni ishara ya unyenyekevu.
Swala la kutubu
ni zawadi kutoka kwa Mungu ni karama sio swala rahisi kama tunavyofikiri,
wanadamu wengi hupenda kujihesabia haki, tunatabia ya kufikiri kuwa sisi ni
bora kuliko wengine na tunatabia ya kufikiri kuwa jambo hililinamuhusu mtu
fulani na halinihusu mimi tunayo tabia ya kukwepa kuwajibika tuna tabia ya
kufikiri kwamba tna ubora fulani kuliko wengine na kwa sababu hiyo tukakataa
kutubu bila kuelewa, toba sio kitu rahisi kwa mtu anayejihesabia haki, na
kujihesabia haki nintabia ya kiburi na kukosa unyenyekevu
Luka 18: 9-14 “Akawaambia mfano huu
watu waliojikinai ya kuwa wao ni wenye haki, wakiwadharau wengine wote. Watu wawili walipanda kwenda hekaluni kusali,
mmoja Farisayo, wa pili mtoza ushuru. Yule Farisayo akasimama akiomba hivi
moyoni mwake; Ee Mungu, nakushukuru kwa kuwa mimi si kama watu wengine,
wanyang'anyi, wadhalimu, wazinzi, wala kama huyu mtoza ushuru. Mimi nafunga mara mbili kwa juma; hutoa zaka
katika mapato yangu yote. Lakini yule mtoza ushuru alisimama mbali, wala
hakuthubutu hata kuinua macho yake mbinguni, bali alijipiga-piga kifua akisema,
Ee Mungu, uniwie radhi mimi mwenye dhambi. Nawaambia, huyu alishuka kwenda
nyumbani kwake amehesabiwa haki kuliko yule; kwa maana kila ajikwezaye
atadhiliwa, naye ajidhiliye atakwezwa.”
Unaona
sio rahisi kwa mtu anayejifikiria kuwa na haki kukubali toba , sio rahisi, sio
rahisi kwa mtu mwenye kiburi kutubu, toba inakaa na wanyenyekevu, watu
wanaovunjika moyo ka haraka ukiwa mtu wa toba unaweza kuomba msamaha kwa
wanadamu na hata kwa Mungu lakini vilevile unaweza kuomba radhi kwaajili ya
watu wengin.
Mungu
anafananisha toba na unyenyekevu, Mungu anaiona toba kama vunjiko la moyo,
Mungu anaiangalia toba kama unyenyekevu na kuwa nje ya kiburi jambo hili sio
jepesi bila neema ya Mungu.
Katika Biblia
hususani agano la kale maombolezo makubwa sana yenye kuonyesha kupoteza tumaini
yalifanyika kwa watu kuvaa Magunia na kujipaka majivu, au kurarua mavazi ya na
kurusha michanga juu, hii ilikuwa ni ishara ya nje ya maumivu makali na
kuonyehsa unyenyekevu, Yakobo alivaa magunia na kuomboleza kwa siku nyingi sana
alipofikiri kuhusu kifo cha mwanaye Yusufu, Daudi alimamuru watu kuvaa magunia
akiomboleza kwaajili ya Abneri alipouawa, wakati mwingine pia toba ilifanyika
kwa kiwango sawa na maombolezo kama ya kufiwa.
Moja ya stori ya
kusisimua katika agano la kale ilikuwa ni habari ya mfalme Ahabu 1Wafalme 21: 19-26 “Angalia, nitaleta mabaya juu yako; nami nitakuangamiza
kabisa, nitamkatia Ahabu kila mume, aliyefungwa na aliyeachwa katika Israeli.
Kisha nitaifanya nyumba yako iwe kama nyumba ya Yeroboamu mwana wa Nebati, na
kama nyumba ya Baasha mwana wa Ahiya, kwa ajili ya chukizo ulilonichukiza, hata
kunighadhibisha, ukawakosesha Israeli. Tena Bwana alinena habari za Yezebeli,
akisema, Mbwa watamla Yezebeli katika kiwanja cha Yezreeli. Mtu wa nyumba ya
Ahabu afaye mjini, mbwa watamla, na yeye afaye mashambani ndege wa angani
watamla. (Lakini hapakuwa na mtu kama
Ahabu, aliyejiuza atende maovu machoni pa Bwana ambaye Yezebeli mkewe
alimchocheaAkachukiza mno, kwa kuzifuata sanamu sawasawa na yote waliyoyafanya
Waamori, Bwana aliowafukuza mbele ya wana wa Israeli.).”
Ni wazi kabisa
katika stori hii kuwa hakuna mtu aliyewahi kuwa muovu katika wafalme wa Israel
nyakati za agano la kale kama Ahabu, na kutokana na maovu kadhaa wa kadhaa,
Mungu alimtuma nabii kutangaza hukumu mbaya dhidi ya Ahabu na familia yake lakini
Ahabu aliposikia hukumu hii mbaya badala ya kumshambulia nabii na au kuamuru
kumuua aliamua kuwa mnyenyekevu na kujinynyekeza kwa Mungu kwa njia ya toba
1Wafalme 21:27-29 “Ikawa, Ahabu alipoyasikia maneno hayo, akayararua mavazi
yake, akavaa magunia mwilini mwake, akafunga, akajilaza juu ya magunia, akaenda
kwa upole. Neno la Bwana likaja kwa Eliya Mtishbi, kusema, Huoni jinsi Ahabu
alivyojidhili mbele yangu? Basi kwa sababu amejidhili mbele yangu, sitayaleta
yale mabaya katika siku zake; ila katika siku za mwanawe nitayaleta mabaya hayo
juu ya nyumba yake.”
Mungu
aliheshimu toba ya ahabu na kuamini kuwa amenynyekea mbele zake, toba ni sihara
ya unyenyekevu, toba na unyenyekevu huenda pamoja Mithali 3:34 “Hakika yake huwadharau
wenye dharau, Bali huwapa wanyenyekevu neema.” Mungu huwapinga wajikwezao bali huwapa neema wanyenyekevu.
Yakobo 4:6
4.
Toba
humfukuzia shetani mbali nasi.
Mara tunapokuwa
tumemkosea Mungu, tunaweza kujikuta tunapungukiwa na imani, tunaacha kumuamini
Mungu na neno lake, tunasikia sauti za mashaka, hukumu katika mioyo yetu na
dhamira zetu, unahisi kama Mungu hatakupa nafasi nyingine tena au Mungu
amekuchoka, na kisha unakosa amani.
Lakini mara
mkristo anapotubu na kurejea kwa Mungu sauti hizo za kishetani hukimbia mbali
sana na wewe Biblia inasema mtiini Mungu mpingeni shetani naye atawakimbia Yakobo 4:7 “Basi
mtiini Mungu. Mpingeni Shetani, naye atawakimbia.” Katika mstari huo
maana na kumtii Mungu na kumpinga shetani ni nini? Maana yake ni kutubu,
kujinyenyekesha, kutubu, ni kuacha dhambi, ni kuacha kuwa vuguvugu angalia Yakobo 4:8-10 “Mkaribieni
Mungu, naye atawakaribia ninyi. Itakaseni mikono yenu, enyi wenye dhambi, na
kuisafisha mioyo yenu, enyi wenye nia mbili. Huzunikeni na kuomboleza na kulia.
Kucheka kwenu na kugeuzwe kuwa kuomboleza, na furaha yenu kuwa hamu. Jidhilini mbele za Bwana, naye atawakuza.”
Dhambi inampa
nguvu shetani ruhusa kuwa karibu nasi, Shetani huwa karibu na wale wanaotenda
mapenzi yake kama Mungu anavyokuwa karibu nwatendao mapenzi yake 1Yohana 3:8 “atendaye
dhambi ni wa Ibilisi; kwa kuwa Ibilisi hutenda dhambi tangu mwanzo. Kwa kusudi
hili Mwana wa Mungu alidhihirishwa, ili azivunje kazi za Ibilisi.” Shetani
huwa karibu na wale wanaotenda mapenzi yake Yohana 8;44 Ninyi ni wa baba yenu,
Ibilisi, na tamaa za baba yenu ndizo mpendazo kuzitenda. Yeye alikuwa mwuaji
tangu mwanzo; wala hakusimama katika kweli, kwa kuwa hamna hiyo kweli ndani
yake. Asemapo uongo, husema yaliyo yake mwenyewe; kwa sababu yeye ni mwongo, na
baba wa huo.”
Unaweza kuona
kwa msingi huo tunapotubu Shetani anakosa nafasi ya kushitaki na kutudai kama
mali yake na hivyo tunaweza kumpinga na kupambana naye na kuondoa nguvu yake
yote ya ushawishi katika maisha yetu.
5.
Toba
inatuweka huru kutoka katika mateso ya dhambi.
Yohana 8:34 -36 “Yesu akawajibu, Amin, amin, nawaambia, Kila atendaye
dhambi ni mtumwa wa dhambi. Wala mtumwa hakai nyumbani sikuzote; mwana hukaa
sikuzote. Basi Mwana akiwaweka huru, mtakuwa huru kweli kweli.”
Dhambi inampa
shetani kibali cha kututesa na kutuonea, inatoa kibali kwa kila kitu kuwa adui
yetu, inatoa kibali kwa magonjwa, jambo hili lina ukweli katika maisha yetu,
tunapoendelea na maisha yetu ya dhambi, utagundua kuwa anayeteseaka zaidi ni
wewe na mimi, ingawa dhambi huonekana kuwa njema na tamu tunapoitenda lakini
kilele chake kina maumivu makubwa sana kuliko ahadi ambayo dhambi imetuahidi, Na
ndio maana kwa kiasi kikubwa Yesu alipowasaidia watu waliokuwa na matatizo
mbalimbali kwa sababu ya dhambi aliwaonya kwamba wasifanye dhambi tena
Yohana 8:10-11 “Yesu akajiinua asimwone mtu ila yule mwanamke, akamwambia, Mwanamke,
wako wapi wale washitaki wako? Je! Hakuna aliyekuhukumu kuwa na hatia? Akamwambia, Hakuna, Bwana. Yesu akamwambia,
Wala mimi sikuhukumu. Enenda zako; wala usitende dhambi tena.]”
Yohana 5:14 “Baada
ya hayo Yesu akamkuta ndani ya hekalu, akamwambia, Angalia, umekuwa mzima;
usitende dhambi tena, lisije likakupata jambo lililo baya zaidi.”
Magonjwa, uvamizi
wa kipepo, mashambulizi ya ibilisi na hatari za mauti vinaruhusiwa kutuandama
tukiwa katika maisha ya dhambi, na ndio maana Yesu anatoa tahadhari
kutokuirudia dhambi tena ili kuepuka mateso yake, Ni jambo la kumshukuru Mungu kwamba
tunapotubu dhambi zetu tunapokea Rehema, na kwakuwa Yesu Kristo ndiye kuhani
wetu mkuu hutuombea kwa kuingilia kati kwaajili yetu
Waebrania 4:14-16 “Basi, iwapo tunaye kuhani mkuu aliyeingia katika
mbingu, Yesu, Mwana wa Mungu, na tuyashike sana maungamo yetu. Kwa kuwa hamna
kuhani mkuu asiyeweza kuchukuana nasi katika mambo yetu ya udhaifu; bali yeye
alijaribiwa sawasawa na sisi katika mambo yote, bila kufanya dhambi. Basi na
tukikaribie kiti cha neema kwa ujasiri, ili tupewe rehema, na kupata neema ya
kutusaidia wakati wa mahitaji.”
Waebrania 7:24-25 “bali yeye, kwa kuwa akaa milele, anao ukuhani wake
usioondoka. Naye, kwa sababu hii, aweza kuwaokoa kabisa wao wamjiao Mungu kwa
yeye; maana yu hai sikuzote ili awaombee.”
Ni kwa sababu
hiyo basi neno la Mungu linatuahidi kwamba toba inatuleta kwa Mungu na kumfanya
Mungu afutilie mbali dhambi zako na tusipotubu hatuwezi kuwa huru kutoka katika
mateso na vifungo vya dhambi. Matendo 3:
19 “Tubuni basi, mrejee, ili dhambi zenu
zifutwe, zipate kuja nyakati za kuburudishwa kwa kuwako kwake Bwana;”
6.
Toba
huongoza katika maisha na Yesu Kristo.
Kwa kawaida
dhambi huongoza katika mauti na mauti ya milele Biblia iko wazi kabisa kuwa
Mshahara wa dhambi ni mauti
Warumi 6:23 “Kwa
maana mshahara wa dhambi ni mauti; bali karama ya Mungu ni uzima wa milele
katika Kristo Yesu Bwana wetu.” Na Yesu alitoa maonyo kuwa tusipotubu
bila shaka nasi tutaangamia
Luka 13: 1-3
“Na wakati uo huo walikuwapo watu waliompasha habari ya Wagalilaya wale ambao
Pilato alichanganya damu yao na dhabihu zao. Akawajibu akawaambia, Je! Mwadhani
ya kwamba Wagalilaya hao walikuwa wenye dhambi kuliko Wagalilaya wote, hata
wakapatwa na mambo hayo? Nawaambia, Sivyo; lakini msipotubu, ninyi nyote
mtaangamia vivyo hivyo”.
Lakini inapokuwepo
toba maangamizi huahirishwa na wokovu hupatikana
Matendo 11:18 “Waliposikia
maneno haya wakanyamaza, wakamtukuza Mungu, wakisema, Basi, Mungu amewajalia
hata mataifa nao toba liletalo uzima.”
2 Wakoritho 7:10 “Maana huzuni iliyo kwa jinsi ya Mungu hufanya toba liletalo wokovu
lisilo na majuto; bali huzuni ya dunia hufanya mauti.
Toba ina tabia
ya kumkaribisha Yesu Kristo, na kumfanya Mungu awe na ushirika na sisi katika
maisha yetu, Yesu alikazania sana swala la toba kwa makanisa yale saba ya asia
katika ufunuo lakini hatimaye alisema
Ufunuo
3:19-20 “Wote niwapendao mimi nawakemea, na
kuwarudi; basi uwe na bidii, ukatubu. Tazama, nasimama mlangoni, nabisha; mtu
akiisikia sauti yangu, na kuufungua mlango, nitaingia kwake, nami nitakula
pamoja naye, na yeye pamoja nami.” Ni furaha kubwa sana kuwa na ushirika
na Yesu Kristo na Mungu, Yeye alishinda kifo na mauti ili aweze kutupa uzima
huu na uzima wa milele, Uzima wa milele haunza tutakapokuwa tumeenda mbinguni
bali unaanza sasa hivyo ni furaha kubwa sana kama tutatubu na kuacha dhambi
zetu kwa kumaanisha kuziacha ili tuwe na ushirika wa kudumu na Bwana wetu Yesu
Kristo.
7.
Toba
ni Agizo la Mungu ni ushauri wa Mungu.
Paulo mtume
alisumbuliwa sana na jamii ya watu waliokuwa wanafalsafa wa Areopago waliokuwa
wakiabudu sanamu pale Athenes Ugiriki na kuwaambia wazi mapenzi ya Mungu ni
kila mtu wa kila taifa popote pale anapaswa kutubu, Mungu alijifanya kuwa haoni
uovu wao zamani za ujinga lakini saasa anaagiza toba kwa kila mtu na kila taifa Matendo 17:30 “Basi, zamani zile za ujinga Mungu alijifanya kama hazioni; bali sasa
anawaagiza watu wote wa kila mahali watubu.” Mafundisho kuhusu toba yanamuhusu
nkila mmoja iwe ni mataifa au wayahudi iwe ni kanisa au wasio kanisa ili
kurejesha uhusiano wetu na Mungu tunapaswa kutubu, kumbuka hatupaswi
kumlazimisha mtu kutubu lakini tunapaswa kuhubiri toba na kuwapa watu uwezo na
maamuzi ya kuchagua, toba ni sehemu ya njia ya uzima na kutokutubu ni kuchagua
mauti Kumbukumbu la Torati 30:19 “Nazishuhudiza mbingu na nchi juu yenu hivi leo, kuwa
nimekuwekea mbele yako uzima na mauti, baraka na laana; basi chagua uzima, ili
uwe hai, wewe na uzao wako;” Unaona ili uwe hai uwe na uzima Mungu
anakushauri kuchagua toba hii ndio namna pekee utakayoweza kuepuka Mauti, Yesu
alipokuwa akiyaonya makanisa yaliyoko Asia ndogo aliwashauri mara kwa mara
faida za toba na kuwaonya madhara ya kutokutubia kile alichowashauri:-
Ufunuo 2:5 EFESO “Basi, kumbuka ni wapi ulikoanguka; ukatubu, ukayafanye
matendo ya kwanza. Lakini, usipofanya hivyo, naja kwako, nami nitakiondoa
kinara chako katika mahali pake, usipotubu.”
Ufunuo 2:14-16. Smirna “Lakini ninayo maneno machache
juu yako, kwa kuwa unao huko watu washikao mafundisho ya Balaamu, yeye
aliyemfundisha Balaki atie ukwazo mbele ya Waisraeli, kwamba wavile vitu
vilivyotolewa sadaka kwa sanamu, na kuzini. Vivyo hivyo wewe nawe unao watu
wayashikao mafundisho ya Wanikolai vile vile. Basi tubu; na usipotubu, naja
kwako upesi, nami nitafanya vita juu yao kwa huo upanga wa kinywa changu.”
Ufunuo 3:2-3 SARDI “Uwe
mwenye kukesha, ukayaimarishe mambo yaliyosalia, yanayotaka kufa. Maana sikuona
matendo yako kuwa yametimilika mbele za Mungu wangu. Basi kumbuka jinsi
ulivyopokea, na jinsi ulivyosikia; yashike hayo na kutubu. Walakini usipokesha,
nitakuja kama mwivi, wala hutaijua saa nitakayokuja kwako”
Ufunuo 3:19, Laodekia “Wote niwapendao mimi nawakemea, na kuwarudi; basi uwe na
bidii, ukatubu.”Wakati wote maandiko yanakazia na kutoa wito wa kutubu,
ushauri wa kutubu, maoni ya kutubu,hivyo toba inabaki kuwa agizo na ushauri wa
Mungu kwa faida ya mwanadamu katika ufalme wa Mungu.
8.
Toba
inaleta furaha kubwa sana Mbinguni.
Yesu kristo
katika mafundisho yake alikazia sana furaha na shangwe inayotokea Mbuinguni
pale mtu mmoja anapotubu, Luka 15: 1-7
biblia inasema “Basi watoza ushuru wote na
wenye dhambi walikuwa wakimkaribia wamsikilize.Mafarisayo na waandishi
wakanung'unika, wakisema, Mtu huyu huwakaribisha wenye dhambi, tena hula nao.
Akawaambia mfano huu, akisema, Ni nani kwenu, mwenye kondoo mia, akipotewa na
mmojawapo, asiyewaacha wale tisini na kenda nyikani, aende akamtafute yule
aliyepotea hata amwone? Naye akiisha kumwona, humweka mabegani pake akifurahi.
Na afikapo nyumbani kwake, huwaita rafiki zake na jirani zake, akawaambia,
Furahini pamoja nami, kwa kuwa nimekwisha kumpata kondoo wangu aliyepotea.
Nawaambia, Vivyo hivyo kutakuwa na furaha mbinguni kwa ajili ya mwenye dhambi
mmoja atubuye, kuliko kwa ajili ya wenye haki tisini na kenda ambao hawana haja
ya kutubu.” Biblia au Bwana Yesu
amerudia tenana tena kwamba kuna furaha mbinguni, kwa malaika wa Mungu kwaajili
ya mwenye dhambi mmoja tu anapotubu, ni wazi kuwa toba ni mapenzi ya Mungu
yanayopendeza na kusubiriwa sana mbinguni ili kwamba mtu aweze kuyatimiza. Mtu
anapokuwa dhambini kibiblia anaitwa mfu au anafananishwa na mtu aliyekufa kwa
sababu ya dhambi aidha toba inaleta neema ya Mungu inayotuokoa kama
tutakavyoona baadaye lakini neno la Mungu lasema dhambi hutufanya kuwa wafu na
tunapotubu neema ya Mungu hutusaidia kuokoka Waefeso 2:1-9 “Nanyi mlikuwa wafu kwa
sababu ya makosa na dhambi zenu; ambazo mliziendea zamani kwa kuifuata kawaida
ya ulimwengu huu, na kwa kumfuata mfalme wa uwezo wa anga, roho yule atendaye
kazi sasa katika wana wa kuasi; ambao zamani, sisi sote nasi tulienenda kati yao,
katika tamaa za miili yetu, tulipoyatimiza mapenzi ya mwili na ya nia, tukawa
kwa tabia yetu watoto wa hasira kama na hao wengine. Lakini Mungu, kwa kuwa ni
mwingi wa rehema, kwa mapenzi yake makuu aliyotupenda; hata wakati ule
tulipokuwa wafu kwa sababu ya makosa yetu; alituhuisha pamoja na Kristo; yaani,
tumeokolewa kwa neema. Akatufufua pamoja naye, akatuketisha pamoja naye katika
ulimwengu wa roho, katika Kristo Yesu; ili katika zamani zinazokuja
audhihirishe wingi wa neema yake upitao kiasi kwa wema wake kwetu sisi katika
Kristo Yesu. Kwa maana mmeokolewa kwa neema, kwa njia ya imani; ambayo hiyo
haikutokana na nafsi zenu, ni kipawa cha Mungu; wala si kwa matendo, mtu awaye
yote asije akajisifu.” Watu walioko dhambini Mungu,
anawatazamia kuwa watatubu kwani biblia inawaita wafu na waliopotea na
wanapotubu inawaita walifufuka na walioonekana Luka 15, 32 “Tena, kufanya furaha na shangwe ilipasa, kwa kuwa huyu
ndugu yako alikuwa amekufa, naye amefufuka; alikuwa amepotea, naye ameonekana.”
Mungu angeweza kuuhukumu ulimwengu kwa haraka na Yesu angeweza kurudi
mara ya pili kwa haraka lakini kukawia kwake ni uvumilivu kwa wanadamu ili
kwamba watu wote wafikie toba, 2Petro 3:9 “Bwana
hakawii kuitimiza ahadi yake, kama wengine wanavyokudhani kukawia, bali huvumilia
kwenu, maana hapendi mtu ye yote apotee, bali wote wafikilie toba.”
9.
Yesu
alikuja kwaajili ya wenye dhambi ili watubu.
Tumeona maana
halisi ya toba kwamba kutubu ni kugeuka Metanoia kwa kiyunani, kwamba mtu
anageuka na kuiacha njia mbaya na kuyatoa maisha yake kwa Mungu, Toba ni kama
wito na kwaasili unaanza na Mungu, anatufungua akili kwa neema yake na kisha
tunaitikia kwa kuomba naye analeta msaada kwetu,na kutubadilisha kupitia neno
lake, tunapolisoma neno lake tunaanza kurekebisha imani zetu, tamaduni zetu,
tabia zetu na namna na mwenendo wa kuishi kwetu neno la Mungu likiwa ndio
kipimo kikuu cha maisha yetu!
Kwa msingi huo
toba ni sehemu muhimu sana katika maisha yetu ya imani Yesu mwenyewe anaeleza
wazi kuwa kusudi kubwa la ujio wake duniani ni ili watu watubu Luka 5:32 “Sikuja
kuwaita wenye haki, bali wenye dhambi, wapate kutubu.”
Yesu licha ya
kusisitiza kuwa alikuja kuwaita wenye dhambi wapate kutubu pia alilihubiri
kusudi hili kila mara alipoihubiri injili Marko
1;14-15 “Hata baada ya Yohana kutiwa gerezani,
Yesu akaenda Galilaya, akiihubiri Habari Njema ya Mungu, akisema, Wakati
umetimia, na ufalme wa Mungu umekaribia; tubuni, na kuiamini Injili”. na Mathayo
4:17 “Tokea wakati huo Yesu alianza kuhubiri,
na kusema, Tubuni; kwa maana ufalme wa mbinguni umekaribia.” Yesu
alifundisha kuwa moja ya mambo muhimu sana ni kuurithi ufalme wa Mungu Mathayo 6:33 “Bali
utafuteni kwanza ufalme wake, na haki yake; na hayo yote mtazidishiwa.”
Yesu alisisitiza kuwa ufalme wa Mungu ndio wa Muhimu zaidi lakini njia pekee ya
kuupata alisisitiza kuwa ni toba, Maandiko yanasisitiza kuwa ufalme wa Mungu
unapatikana kwa wale wanaotubu.
10.
Toba
inaleta wokovu
Njia kuu ya
kupokea zawadi ya wokovu na kuingia katika ufalme wa Mungu nji kwa njia ya
toba, hakuna namna yoyote mtu anaweza kuokoka bila kutubu, toba ndio msingi
mkuu wamafundisho ya wokovu na ufalme wa Mungu, Waebrania 6:1-2. “Kwa sababu hiyo,
tukiacha kuyanena mafundisho ya kwanza ya Kristo, tukaze mwendo ili tuufikilie
utimilifu; tusiweke msingi tena wa kuzitubia kazi zisizo na uhai, na wa kuwa na
imani kwa Mungu, na wa mafundisho ya mabatizo, na kuwekea mikono, na kufufuliwa
wafu, na hukumu ya milele”. Kuzitubia
kazi zisizo na uhai maana yake ni kuacha dhambi, Yesu alikwisha kutoa maonyo
kuwa kama hatutatubu uko uwezekano mkubwa wa kuangamia Luka 13:1-5 “Na wakati uo huo
walikuwapo watu waliompasha habari ya Wagalilaya wale ambao Pilato alichanganya
damu yao na dhabihu zao. Akawajibu akawaambia, Je! Mwadhani ya kwamba
Wagalilaya hao walikuwa wenye dhambi kuliko Wagalilaya wote, hata wakapatwa na
mambo hayo?Nawaambia, Sivyo; lakini msipotubu, ninyi nyote mtaangamia vivyo
hivyo. Au wale kumi na wanane, walioangukiwa na mnara huko Siloamu, ukawaua,
mwadhani ya kwamba wao walikuwa wakosaji kuliko watu wote waliokaa Yerusalemu?
Nawaambia, Sivyo; lakini msipotubu, ninyi nyote mtaangamia vivyo hivyo.”
Onyo la Kristo halimaanishi kuwa anataka watu waangamia hapana anataka watu
watubu ili wasiangamie ni ushauri uliojaa upendo kama watu hawatatubu kweli
hawataokolewa Mungu ni mvumilivu kwa sababu anataka watu wote tufikie toba 2Petro3:9 “Bwana
hakawii kuitimiza ahadi yake, kama wengine wanavyokudhani kukawia, bali
huvumilia kwenu, maana hapendi mtu ye yote apotee, bali wote wafikilie toba.”
Maandiko yanatoa wito wa toba kwani Mungu atamuhukumu kila mtu kwa kadiri ya
matendo yake na ndio maana manabii walioonya wakati wote walitoa wito kwa watu
kutubu Ezekiel 18:30-32 “ Basi, nitawahukumu ninyi, nyumba ya Israeli, kila mmoja
kwa kadiri ya njia zake, asema Bwana MUNGU. Rudini, mkaghairi, na kuyaacha
makosa yenu yote; basi hivyo uovu wenu hautakuwa uharibifu wenu. Tupilieni mbali nanyi makosa yenu yote
mliyoyakosa; jifanyieni moyo mpya na roho mpya; mbona mnataka kufa, enyi nyumba
ya Israeli? Maana mimi sikufurahii kufa kwake afaye, asema Bwana MUNGU; basi
ghairini, mkaishi”. Unaona dhambi huleta maangamizi huleta kifo lakini
Mungu hafurahii kufa kwetu na ndio maana anatoa wito tutubu toba ina faida gani
toba inaleta wokovu, tunapomuamini Bwana Yesu maana yake tutatubu kwa imani
kupitia kazi za rehema zilizofanya na Yesu pale msalabani ili tuweze kuokolewa Matendo 16:30-31 “kisha akawaleta nje akasema, Bwana zangu, yanipasa
nifanye nini nipate kuokoka?
Wakamwambia, Mwamini Bwana Yesu, nawe utaokoka pamoja na nyumba yako.”
Rev. Innocent
Kamote
Mkuu wa wajenzi
mwenye Hekima!