Andiko la Msingi: Mathayo 6:25 -27 “Kwa sababu hiyo nawaambieni, Msisumbukie
maisha yenu, mle nini au mnywe nini; wala miili yenu, mvae nini. Maisha je! Si
zaidi ya chakula, na mwili zaidi ya mavazi? Waangalieni ndege wa angani, ya
kwamba hawapandi, wala hawavuni, wala hawakusanyi ghalani; na Baba yenu wa
mbinguni huwalisha hao. Ninyi je! Si bora kupita hao? Ni yupi kwenu ambaye akijisumbua aweza
kujiongeza kimo chake hata mkono mmoja?”
Na maisha ya nini
kuyasumbukia!
Nyakati hizi tulizonazo ni
nyakati ambazo ni ngumu sana kimaisha, watu wengi sana wanaishi maisha ya
huzuni yasiyo na furaha na yaliyojawa na wingi wa migandamizo ya maisha, siku
inaweza kupita na ukajikuta hakuna ulichokamilisha kila wakati unafikiri labda
utapata siku nzuri ambayo unaweza kukamilisha maswala yako yote muhimu
unayotaka kuyakamilisha, lakini mambo
sivyo yalivyo, watu wengi wa kizazi hiki wamekuwa busy na maisha lakini ni wachache
wanaofurahia kuwa busy kwao, kwa mtindo huu utaweza kugundua kuwa Maisha
yanakuwa magumu na muda unakuwa hautoshi, Hakuna wa kulaumiwa muda wako
unapokuwa hautoshi, unapokuwa umekusudia kufanya mambo mengi lakini mwisho wa
siku unajikuta hakuna hata moja ulilolikamilisha, unaweza hata kumlaumu Mungu
unaweza kufikiri kuwa muda hautoshi kumbuka
hivyo sivyo maisha yanavyopaswa kuwa; Yesu alikusudia watu wake waishi
maisha mepesi yasiyo na mizigo mizito wala hofu wala kongwa la utumwa!
Ni muhimu kufahamu kuwa Yesu
alikusudia watu waishi maisha yaliyojaa pumziko na raha nafsini mwao na ili mtu
aweze kufurahia maisha hana budi kuzingatia maswala muhimu ya kibiblia na
mafundisho ya Yesu juu ya kuishi kwa raha bila usumbufu wa aina yoyote Mathayo 11:28-29 “Njoni kwangu, ninyi nyote msumbukao na
wenye kulemewa na mizigo, nami nitawapumzisha. Jitieni nira yangu, mjifunze
kwangu; kwa kuwa mimi ni mpole na mnyenyekevu wa moyo; nanyi mtapata raha
nafsini mwenu;”
Kama mungu alikusudia watu wawe
na furaha wasiwe na Mizigo, wasielemewe wasisumbuke kwanini watu wengi
wanasumbuka leo na kuishi maisha ya kujichosha? Yesu alihoji ni nani kwenu
ambaye kwa kujisumbua aweza kuongeza kimo chake hata mkono mmoja? Mungu
anatufundisha katika neno lake jnsi na namna ya kuishi kwa furaha? Yafuatayo
yatatusaidia kuishi maisha rahisi na kujikuta tunafurahi bila kuelemewa na
lolote
1.
Fanya
jambo moja tu kwa wakati.
Mathayo 6: 24 “Hakuna
mtu awezaye kutumikia mabwana wawili; kwa maana atamchukia huyu, na kumpenda
huyu; ama atashikamana na huyu, na kumdharau huyu. Hamwezi kumtumikia Mungu na
mali.” Ingawa mstari huu unaweza kuwa na maana pana nyingi lakini
moja ya maana rahisi anayotaka kuikazia Yesu Kristo ni kuwa kuna mafanikio ya
kufanya jambo moja kwa wakati mmoja kuliko kutamani kufanya mambo mengi kwa
wakati mmoja, watu wengi wanaojichosha katika maisha na kujikuta muda hautoshi
na wanaamka wakiwa wamechoka ni wale wanaotaka kufanya mambo mengi kwa wakati
mmoja, akili yetu inapokuwa katika jambo lingina na mikono yetu ikitenda kitu
kingine maisha yatakuwa magumu na tunaweza kumaliza siku hakuna
ulichokamilisha!
Wataalamu wa
mapishi wanasema kuwa unaweza kutenganisha kiini cheupe cha yai na kiini cha
manjano cha yai na ukavitumia kwa matumizi fulani ya mapishi yaliyo mazuri,
lakini hata hivyo utapoteza muda na ni vigumu kuliko kama utavuruga yai lote na
kulila moja kwa moja.
Mwanafunzi
amabaye anakusudia kufanya au kujisomea masomo mengi kwa wakati mmoja wa
maandalizi hawezi kuwa na ufanisi kama yule anayefanya moja baada ya jingine,
mwanafunzi ambaye atakuwa na simu ya mkononi, yenye kila kitu huku anasoma
atapoteza mwelekeo hata kama ni mzuri kiasi gani, mwanafunzi anayeshiriki
Mapenzi huku anasoma, atapoteza mwelekeo, kwa kanuni ya Yesu huwezi kutumikia
mabwana wawili, fanya jambo moja kwanza Mungu hataki ujisumbue Wafilipi 4:6
“Msijisumbue kwa neno lo lote; bali katika kila neno kwa kusali na kuomba,
pamoja na kushukuru, haja zenu na zijulikane na Mungu.” Jaribu
kufanya jambo moja tu kwa wakati mmoja na utaweza kuona unafanikiwa na
kuyafurahia maisha, na kisha
pumzika. Hutachanganyikiwa wala hutalala na stresses.
Mungu
aliifurahia kazi yake ya uumbaji aliyokuwa akiifanya na kuikamilisha kwa siku
ile ile, kila siku alitimiza wajibu wa uumbaji fulani na alipokamilisha
alifurahi na kupumzika Mwanzo 1:3-4, Mungu akasema, Iwe nuru; ikawa nuru. Mungu akaiona nuru,
ya kuwa ni njema;” Mungu akatenga nuru na giza. kila kitu alikuwa akikikamilisha na
kujipongeza siku moja baada ya nyingine hivyo kwa siku sita ulimwengu uliumbwa
2.
Usiogope
kuhusu kesho?.
Mathayo 6:34 “Basi
msisumbukie ya kesho; kwa kuwa kesho itajisumbukia yenyewe. Yatosha kwa siku
maovu yake.” Mungu anatutarajia tumuamini katika kiwango ambacho
hatutaogopa kuhusu kesho itakuwaje, aliwafundisha wana wa Israel kutokuogopa
maisha yao kwamba itakuwaje kesho kwani kila siku alikuwa amewaandalia riziki
yao, hii haimaanishi kuwa tusiweke akiba, hii haimaanishi kuwa tutumie vibaya
kile tulicho nacho, hapana hapa Mungu anatufundisha kwamba tusiogope kesho
itakuwaje, watu wanaoogopa kesho itakuwaje wanaishi maisha ya taabu sana nay a kujitesa na hivyo wanaweza kukosa raha,
Mungu aliwafundisha Israel Jangwani kwamba mtu hataishi kwa mkate tu, bali kwa
kila neno litokalo katika kinywa cha Mungu, Kutoka 16: 15-21 “Wana wa Israeli walipokiona, wakaambiana, Nini hiki?
Maana hawakujua ni kitu gani. Musa akawaambia, Ndio mkate ambao BWANA amewapa
ninyi, mle. Neno hili ndilo aliloagiza BWANA, Okoteni ninyi kitu hicho kila mtu
kama ulaji wake ulivyo; kichwa pishi, kama hesabu ya watu wenu ilivyo; ndivyo
mtakavyotwaa, kila mtu kwa ajili ya hao walioko hemani mwake.Wana wa Israeli
wakafanya hivyo, wakaokota wengine zaidi, wengine kupungua. Nao walipoipima kwa
pishi, yeye aliyekuwa ameokota kingi hakubakiwa na kitu, na yeye aliyekuwa
ameokota kichache hakupungukiwa; wakaokota kila mtu kama ulaji wake ulivyokuwa.
Musa akawaambia, Mtu awaye yote asikisaze hata asubuhi. Lakini hawakumsikiza
Musa; wengine miongoni mwao wakakisaza hata asubuhi, nacho kikaingia mabuu na
kutoa uvundo; Musa akawakasirikia sana. Basi wakaokota asubuhi baada ya
asubuhi, kila mtu kama ulaji wake ulivyokuwa; na hapo jua lilipokuwa ni kali,
kikayeyuka.”
Watu wengi sana
wanahofu kuhusu maisha ya baadaye kuwa yatakuwaje kiasi ambacho wanaweza
kusahahu kuhusu mapenzi ya Mungu, jambo hili ni hatari, kujiandaa kwa maisha ya
baadaye ni kwa muhimu sana, na biblia haikatazi hilo lakini ni uzembe mkubwa kumsahahu
Mungu kwaajili ya maisha haya kwa sababu yeye ndiye mwenye kuutunza uzima wetu,
watu wanaoogopa kesho pia wanakuwa wachoyo Luka
12: 15-26 “1Akawaambia,
Angalieni, jilindeni na choyo, maana uzima wa mtu haumo katika wingi wa vitu
vyake alivyo navyo. Akawaambia mithali, akisema, Shamba la mtu mmoja tajiri
lilikuwa limezaa sana; akaanza kuwaza moyoni mwake, akisema, Nifanyeje? Maana
sina pa kuyaweka akiba mavuno yangu. Akasema, Nitafanya hivi; nitazivunja ghala
zangu, nijenge nyingine kubwa zaidi, na humo nitaweka nafaka yangu yote na vitu
vyangu. Kisha, nitajiambia, Ee nafsi
yangu, una vitu vyema vingi ulivyojiwekea akiba kwa miaka mingi; pumzika basi,
ule, unywe, ufurahi. Lakini Mungu akamwambia, Mpumbavu wewe, usiku huu wa leo
wanataka roho yako! Na vitu ulivyojiwekea tayari vitakuwa vya nani? Ndivyo
alivyo mtu ajiwekeaye nafsi yake akiba, asijitajirishe kwa Mungu.Akawaambia
wanafunzi wake, Kwa sababu hiyo nawaambia, Msisumbukie maisha yenu, mtakula
nini; wala miili yenu, mtavaa nini. Kwa kuwa maisha ni zaidi ya chakula, na
mwili ni zaidi ya mavazi. Watafakarini kunguru, ya kwamba hawapandi wala
hawavuni; hawana ghala wala uchaga, na Mungu huwalisha. Bora ninyi mara nyingi
kuliko ndege! Na yupi kwenu ambaye akijisumbua
aweza kujiongeza kimo chake hata mkono mmoja? Basi, ikiwa hamwezi hata neno
lililo dogo, kwa nini kujisumbua kwa ajili ya yale mengine?” Unaona
Mungu hataki tusumbukie maisha Mungu hataki tuwe na hofu kuhusu kesho yeye
ndiye anayejua maisha yetu na hivyo anataka tuwe na furaha, furahia kila
unachokikamilisha kwa siku ile, na
usiogope kuhusu kesho itakuwaje Mungu anajua.
3.
Rizika
na ulichonacho.
Waebrania 13:5-6 “.Msiwe
na tabia ya kupenda fedha; mwe radhi na vitu mlivyo navyo; kwa kuwa yeye
mwenyewe amesema, Sitakupungukia kabisa, wala sitakuacha kabisa. Hata
twathubutu kusema, Bwana ndiye anisaidiaye, sitaogopa; Mwanadamu atanitenda
nini?”
Tamaduni za
dunia ya sasa zinafikiri kuwa na furaha ni kuwa na vitu vingi au kuwa na kila
kitu lakini ukweli umedhihirika kuwa wale wanaoishi maisha rahisi ndio wenye
furaha kubwa duniani kuliko wengine wote, utafiti umethibitisha kuwa watu
wanaoishi muda mrefu zaidi kuliko wote duniani ni Mabedui wanaishi jangwani
hawa wanauwezo wa kufikisha hata miaka 200 ya maisha yao, sababu kuu ni kuwa
wameridhika na maisha yao, Maisha yamebadilika sana kwa sababu watu wameharibu
tamaduni zao kuanzia namna mtu anapozaliwa mpaka namna mtu anavyozikwa. leo hii
hata kuzika mtu imekuwa ni gharama kubwa sana, Mungu anataka watu wafurahie
maisha na hivyo ni muhimu kuridhika na kile ulicho nacho Wafilipi 4:11-13 “Si kwamba nasema haya kwa kuwa nina mahitaji; maana
nimejifunza kuwa radhi na hali yo yote niliyo nayo. Najua kudhiliwa, tena najua
kufanikiwa; katika hali yo yote, na katika mambo yo yote, nimefundishwa kushiba
na kuona njaa, kuwa na vingi na kupungukiwa. Nayaweza mambo yote katika yeye
anitiaye nguvu.” Kumbuka kuwa sio dhambi kuwa na vitu lakini ni
dhambi kumezwa na tamaa, ni kwa sababu ya kutokuridhika watu wengi wameingia
katika mateso makubwa sana na hata kufarakana na imani, mioyo tetu
inapofungamanisha na maswala ya vitu vya dunia inaweza kutuletea maumivu
makubwa sana na tukafikia ngazi ya kutokuyafurahia maisha 1Timotheo 6:6-10 “Walakini utauwa pamoja na kuridhika ni faida kubwa. Kwa
maana hatukuja na kitu duniani, tena hatuwezi kutoka na kitu; ila tukiwa na
chakula na nguo tutaridhika na vitu hivyo. Lakini hao watakao kuwa na mali
huanguka katika majaribu na tanzi, na tamaa nyingi zisizo na maana, zenye
kudhuru, ziwatosazo wanadamu katika upotevu na uharibifu. Maana shina moja la
mabaya ya kila namna ni kupenda fedha; ambayo wengine hali wakiitamani hiyo
wamefarakana na Imani, na kujichoma kwa maumivu mengi.” Kama tutajifunza kumfurahia Mungu kwa kile
alichotupa tutaishi maisha ya raha na amani, hakuna sababu ya kushindana na
awaye yote, kila mtu ana maisha yake na hatuwezi kufanana kwa sababu
ninachikiwaza sio unachokiwaza, ninachoamini sio unachokiamini kwa hiyo kila
mmoja aepuke maisha ya mashindano na ajifunze kuridhika na kile alicho nacho.
Watu wakiishi hivi hakutakuwa na wizi na maisha yatakuwa mazuri.
4.
Muweke
Mungu mbele.
Mathayo 6: 31-33 “Msisumbuke,
basi, mkisema, Tule nini? Au Tunywe nini? Au Tuvae nini? Kwa maana hayo yote
Mataifa huyatafuta; kwa sababu Baba yenu wa mbinguni anajua ya kuwa mnahitaji
hayo yote. Bali utafuteni kwanza ufalme wake, na haki yake; na hayo yote
mtazidishiwa.” Yesu anatupa
kanuni nyingine ya namna ya kuishi bila kuhangaika au kusumbuka anatoa maangizo
ya aina mbili kwa wakati mmoja kumtafuta Mungu kwanza na haki yake na mengine
yote tutazidishiwa; maana yake ni nini?
kama tuko duniani kwa makusudi ya Mungu na kila tunachokifanya ni kwaajili ya
kutimiza kusudi hilo basi ni vema tukamtafuta Mungu kwanza, yaani “kama Mungu
ni chanzo cha kila kitu ni vema tukaacha kutafuta au kuhangaika na kila kitu na
tukampata Yeye aliye chanzo” Chakula na
mavazi pamoja na mahitaji yetu mengine ni jukumu la kawaida la baba mwenye
upendo, Yesu anaweka wazi kuwa ni afadhali kuhangaika na kumtafuta yeye au
kumsikiliza yeye inaweza kuwa muhimu zaidi kuliko kusumbuka na maswala
mengineyo Luka 10:38-42 “Ikawa katika kuenenda kwao aliingia katika kijiji kimoja;
mwanamke mmoja jina lake Martha akamkaribisha nyumbani kwake. Naye alikuwa na
umbu lake aitwaye Mariamu, aliyeketi miguuni pake Yesu, akasikiliza maneno
yake. Lakini Martha alikuwa akihangaika kwa utumishi mwingi; akamwendea,
akasema, Bwana, huoni vibaya hivyo ndugu yangu alivyoniacha nitumike peke
yangu? Basi mwambie anisaidie.Bwana akajibu akamwambia, Martha, Martha,
unasumbuka na kufadhaika kwa ajili ya vitu vingi; lakini kinatakiwa kitu kimoja
tu; na Mariamu amelichagua fungu lililo jema, ambalo hataondolewa.”
Unaona mtu
anapochagua kumsikiliza Mungu amechagua fungu lililojema, ni muhimu sana kupata
ujuzi kuhusu nini ni mapenzi ya Mungu na kuyafanya kwa wakati huo, na ni muhimu
kuwa na ushirika na Mungu kwanza kabla ya kuanza kusumbuka na kutimiza kusudi
lake, wakati mwingine tunaweza kusumbuka bila mafanikio kwaajili ya
kujishughulisha kutafuta mafanikio bila kusikia neno la mfanikishaji
Kwa akili zetu
wakati mwingine tunaweza kusumbuka sana kufanya mambo bila kufanikiwa lakini
kwa kutii na kufuata au kuomba uongozi wa Mungu tunaweza kupata mafanikio
makubwa katika jambo lilelile ambalo limeshindikana mwanzoni Luka 5:4-7 “Hata
alipokwisha kunena, alimwambia Simoni, Tweka mpaka kilindini, mkashushe nyavu
zenu mvue samaki. Simoni akajibu akamwambia, Bwana mkubwa, tumefanya kazi ya
kuchosha usiku kucha, tusipate kitu; lakini kwa neno lako nitazishusha nyavu.
Basi, walipofanya hivyo walipata samaki wengi mno, nyavu zao zikaanza kukatika;
wakawapungia mikono washirika wao waliokuwa katika chombo cha pili, waje
kuwasaidia; wakaja, wakavijaza vyombo vyote viwili, hata vikataka kuzama.” Unaona
tunapomtanguliza Mungu na kumtii yeye kwanza kwa kuwa yeye ndio chanzo cha
mambo yote hutupa maelekezo stahiki yanayoweza
kutupa mafanikio tunayoyataka
Biblia
inaonyesha kuwa kama tukimtumikia Mungu yaani kumuabudu na kumuweka yeye Mstari
wa mbele atatuponya Magonjwa, ataondoa utasa, na kutimiza siku zako za kuweko
duniani Kutoka 23:25-26 “Nanyi mtamtumikia BWANA, Mungu wenu, naye atakibarikia
chakula chako, na maji yako; nami nitakuondolea ugonjwa kati yako. Hapatakuwa
na mwenye kuharibu mimba, wala aliye tasa, katika nchi yako; na hesabu ya siku
zako nitaitimiza.” Torati inaonyesha kuwa kuna Baraka nyingi sana
kama watu wataitii sauti ya Mungu na kumuweka yeye mbele, Neno la Mungu moja tu
kwetu linaweza kubadilisha kabisa mfumo wa maisha yetu na tukaishi maisha ya
furaha.
5.
Sahahu
yaliyopita.
Wafilipi 3:13 “Ndugu,
sijidhanii nafsi yangu kwamba nimekwisha kushika; ila natenda neno moja tu;
nikiyasahau yaliyo nyuma, nikiyachuchumilia yaliyo mbele;”
Moja ya kikwazo kikubwa
sana katika maisha ya watu wengi kinachowakosesha wasiweze kuwa na furaha au
kusumbuka ni kutokusahau Historia, ingawa Historia ni nzuri lakini wote
tutakubaliana kuwa ziko historia nyingine haziwezi kutupa maisha yenye furaha,
kwa msingi huo Biblia inatutaka tusahau yakiyo nyuma na kuchuchumilia yaliyo
mbele, historia yetu ya maisha ya nyuma ni ya kuitupa.
Mara kadhaa wana
wa Israel walijikosesha Baraka za Mungu kwa sababu walikumbuka Misri katika
inchi ya utumwa na kudharau uhuru ambao Mungu alikuwa amewazawadia, Mungu
alikuwa amewapa ukombozi mkuu lakini mara kwa mara walimuhuzunisha kwa kukosa
shukurani Hesabu 14:1-4 “Mkutano wote wakapaza sauti zao wakalia; watu wakatoka
machozi usiku ule. Kisha wana wa Israeli wote wakamnung'unikia Musa na Haruni;
mkutano wote wakawaambia, Ingekuwa heri kama tungalikufa katika nchi ya Misri,
au, ingekuwa heri kama tungalikufa katika jangwa hili. Mbona Bwana anatuleta
mpaka nchi hii ili tuanguke kwa upanga? Wake zetu na watoto wetu watakuwa
mateka; je! Si afadhali turudi Misri?
Wakaambiana, Na tumweke mtu mmoja awe akida, tukarudi Misri.” Kutokana
na kuwa na hali ya manunguniko na kukosa shukurani kwa Mungu ugumu uliongezeka
katika maisha yao safari ya jangwani ilikuwa ndefu na yenye misiba Mingi
inakisiwa kuwakila siku waisrael 70 walikufa, ni lazima tusahahu tulikotoka na
nkuendelea kumtumikia Mungu kwa nguvu na kumuabudu yeye kwa nguvu, kamwe
tusiangalie nyuma kule alikotutoa Bwana Luka
17:32-33 “Mkumbukeni mkewe Lutu. Mtu ye yote
atakaye kuiponya nafsi yake, ataiangamiza; na ye yote atakayeiangamiza
ataiponya.” Yesu alikumbusha juu ya kujikana nafsi na kuendelea
kumcha yeye na kutimiza wajibu wetu kwa Mungu bila kugeuka nyuma, Yesu alitumia
mfano wa mkewe Lutu, na kuonya juu ya jkutaka kuiokoa nafsi yetu, Yesu
anazungumzia juu ya kujihurumia na kutokujikana kwa Mungu, wengi kwaajili ya kujihurumia
wamepoteza Baraka na uwepo wa Mungu Paulo Mtume alikuwa ni mtume aliyepata
neema kubwa ya Mungu kuliko mitume wote, alipelekwa mpaka mbigu ya tatu na
kupewa mafunuo makubwa sana hata hivyo hakuwahi kuridhika wala kuangalia
historia yake yeye alijua kuwa furaha yake inapatikana kwa kuendelea kusahau
yaliyo nyuma na kuchuchumilia yaliyo mbele, aliwataka kanisa la kolosai
kuangalia Wakolosai 3:1-2 “Basi mkiwa mmefufuliwa pamoja na Kristo, yatafuteni
yaliyo juu Kristo aliko, ameketi mkono wa kuume wa Mungu. Yafikirini yaliyo juu, siyo yaliyo katika nchi.”
Ni Muhimu kujifunza kuangalia mbele ondoa uchungu wote na hakikisha kuwa
unasamehe wote waliokukosea uchungu una tabia ya kutufungia Baraka na uwepo wa
Mungu hivyo kusahau yaliyopita ni pamoja
na kusamehe wale waliotukosea Hesabu
4:13 “Nao watayaondoa hayo majivu madhabahuni; na
kutandika nguo ya rangi ya zambarau juu yake;” Kusamehe na kuondoa
kila aina ya uchungu ni sawa na kazi za makuhani ambao walitakiwa kuhakikisha
wanaondoa majivu katika madhabahu ili moto uendelee kuwaka.
6.
Fanya
kila kitu kwa utukufu wa Mungu.
1Wakoritho 10:31 “Basi,
mlapo, au mnywapo, au mtendapo neno lo lote, fanyeni yote kwa utukufu wa Mungu.”
Moja ya mambo ambayo yanawaumiza watu wengi sana duniani ni kufanya mambo kwa
mashindano au kwa kutaka kushindana au kujilinganisha, watu wengi sana wanakosa
amani na kusumbuka katika maisha haya kwa sababu wanajilinganisha na wengine,
hawafanyi mambo kwa nia njema nia ya Mungu kutukuzwa.
Mara zote
mashindano yameleta kiburi, yameleta dharau yameleta maumivu na majuto,siku
hizi kuna mashindano mpaka ya kutoa sadaka tabia ya aina hii imeumiza wengi
Mungu hatahukumu kile tunachokifanya bali atahukumu kwa nini tumefanya, ni
muhimu nia yetu nadhamiri zetu za kutenda lolote tunalolitenda ikawa ni
kwaajili ya Mungu kutukuzwa, kamwe neno la Mungu haliitii moyo kufanya jambo
kwa mashindano, Wafilipi 2:3 “Msitende neno lo lote kwa kushindana wala kwa majivuno;
bali kwa unyenyekevu, kila mtu na amhesabu mwenziwe kuwa bora kuliko nafsi yake.”
Unaweza kuona tabia ya kushindana ikiingia kanisani au kwa watu wa Mungu
inaweza kuleta vita na magomvi hata kuomba kwetu kunaweza kugeuzwa kuwa kuomba
kubaya kuomba kwa tamaa kwa sababu ya mshindano na sio kwaajili ya utukufu wa
Mungu Yakobo 4:1-3 “Vita vyatoka wapi, na mapigano yaliyoko kati yenu yatoka
wapi? Si humu, katika tamaa zenu zifanyazo vita katika viungo vyenu? Mwatamani,
wala hamna kitu, mwaua na kuona wivu, wala hamwezi kupata. Mwafanya vita na
kupigana, wala hamna kitu kwa kuwa hamwombi! Hata mwaomba, wala hampati kwa
sababu mwaomba vibaya, ili mvitumie kwa tamaa zenu.” Kama kila kitu
tukifanyacho hakifanyiki kwaajili ya utukufu wa
Mungu maisha yetu yatakuwa yenye uchungu mwingi, na hata kuomba kwetu
kutaathiriwa tutakuwa tunaomba kwa sababu ya kutaka kitu fulani kwa tamaa na
sio kwaajili ya utukufu wa Mungu kanuni kuu ya msingi hapa ni kufanya kila
jambo kwaajili ya utukufu wa Mungu.
7.
Jifunze
kukataa.
Mathayo 5:37 “Bali
maneno yenu yawe Ndiyo, ndiyo; Siyo, siyo; kwa kuwa yazidiyo hayo yatoka kwa
yule mwovu.”
Yakobo 5:12 “Lakini
zaidi ya yote, ndugu zangu, msiape, wala kwa mbingu wala kwa nchi; wala kwa
kiapo kinginecho chote; bali ndiyo yenu na iwe ndiyo, na siyo yenu iwe siyo,
msije mkaangukia hukumu.”
Nyakati za
Biblia hususani wakati wa Yesu Kristo wayahudi wengi sana walikuwa wakiogopa
sana kuapa au kujifunga katika ahadi yoyote kwa kumuhusisha Mungu hii ni kwa
sababu waliogopa kuwa endapo watashindwa kutimiza ahadi basi watakuwa
wamejifunga kwa Mungu, hivyo hawakutaka kumuhusisha Mungu ili hata wakivunja
ahadi wasiweze kuwajibika kwa Mungu wakijua kuwa hawafungwi, swala hili
lilipunguza uaminifu wa watu na kuwanyima raha, tatizo la kutokuwa wakeli
linawatesa sana hata wafrika wengi wanaogopa kusema Ndio au sio inayotoka
Moyoni wanaweza kusema Ndio lakini kumbe moyonimwao hawako radhi na hilo, au
wanaweza kusema sio kumbe kuna kitu wanakihitaji
Neno la Mungu
kupitia Yesu Kristo linatutaka tuwe watu wenye maamuzi yaliyo wazi tu kuwa kama
jambo ni ndio iwe ndio kivitendo maana sisi ni wa Mungu na kama jambo sio iwe
sio kwa maana sisi ni watu wa Mungu hakuna sababu ya kupiga siasa, wengi
wanaogopa kusema sio kwa wake za, mabosi wao kwa kuogopa kuuwaumiza mioyo
lakini baadaye wanajuta kwa nini sikukataa au kwanini nilikubali Heri kama
ningelikataa
Kutokusema
HAPANA ni tatizo kubwa sana la kisaikolojia wana saikoloji wanaliita tatizo
hilo “CANT SAY NO SYNDROM” wengi wanaoogopa kusema hapana wanafikiri
kwamba labda wao sio Bora sana, hivyo wanafikiri kuwa wanaweza kuwapendeza
wengine kwa kuwakubalia kila wanachokitaka, au wanafikiri kuwa wanapaswa
kuwatumikia wengine na kuwa wema sana kiasi wakisema hapana watawaudhi, au
anafikiri kuwa akisema hapana atakataliwa, wanafikiri kuwa watu watawapenda
wakiwakubalia kila kitu, wanadhani kusema hapana ni swala la kikatiali sana,
wanafikiri kuwa wataonekana kuwa wabinafsi wakisema hapana, au wanafikiri kuwa
wengine hawatakiwi kuona yeye kuwa ni mkaidi, na tafasiri mbaya ya maandiko
heri wenye upole maana watairithi inchi.
Biblia imatupa
kweli muhimu au kanuni ya muhimu ya kuyafurahia maisha ambayo ni kusema Ndio au
Hapana
Vijana wengi wa
kiume wakiombwa na wasichana kuwa wapenzi inakuwa vigumu kwao kusema hapana kwa
sababu ya kuwaonea huruma biblia inatutaka tuseme hapana kwa hapana kweli na
ndio kwa ndio kweli na sio kutoa maelezo.
Kusema hapana
sio swala rahisi, wengi wanaogoipa kusema hapana, kiroho kutokusema hapana kuna
maanisha kuwa tuna roho ya woga; 2Timotheo
1:7 “Maana Mungu hakutupa roho ya woga, bali ya
nguvu na ya upendo na ya moyo wa kiasi.” Kutokana na woga huu hususani woga wa kuumiza wengine kwa sababu
kusema hapana mara nyingi kunaumiza wengine watu wengi sana wamejikuta au
tumejikuta katika matatizo ya aina mbali mbali
·
Dereva anaweza akawa anaendesha kwa kasi sana na
kuhatarisha maisha lakini ukaogopa kumwambia punguza mwendo
·
Jambo linaweza likawa liko kinyume cha
Sheria.lakini kwa vile wengine wanafanya ukashidwa kusema hapana
·
Jambo linaweza kuwa hukubaliani nalo, lakini kwa
vile wengi wamelikubali hutaki kuonekana tofauti
Inahitajika roho
ya ujasiri, bila kuumiza moyo wa mtu mwingine kusema Hapana tofauti na mtazamo
wake, au wakati mwingine kusema hapana hata kama jambo hilo litamuumiza
muhusika Daniel 3:13-18 “Basi
Nebukadreza akatoa amri kwa hasira na ghadhabu, waletwe hao Shadraka, na
Meshaki, na Abednego. Basi wakawaleta watu hao mbele ya mfalme. Nebukadreza
akajibu, akawaambia, Enyi Shadraka, na Meshaki, na Abednego, je! Ni kwa
makusudi hata hammtumikii mungu wangu wala kuisujudia sanamu ya dhahabu
niliyoisimamisha? Basi sasa, kama mkiwa tayari wakati mtakapoisikia sauti ya
panda, na filimbi, na kinubi, na zeze, na santuri, na zomari, na namna zote za ngoma,
kuanguka na kuisujudia sanamu niliyoisimamisha, ni vema; bali msipoisujudia,
mtatupwa saa iyo hiyo katika tanuru iwakayo moto; naye ni nani Mungu yule
atakayewaokoa ninyi na mikono yangu? Ndipo Shadraka, na Meshaki, na Abednego,
wakajibu, wakamwambia mfalme, Ee Nebukadreza, hamna haja kukujibu katika neno
hili. Kama ni hivyo, Mungu wetu tunayemtumikia aweza kutuokoa na tanuru ile
iwakayo moto; naye atatuokoa na mkono wako, Ee mfalme. Bali kama si hivyo,
ujue, Ee mfalme, ya kuwa sisi hatukubali kuitumikia miungu yako, wala
kuisujudia hiyo sanamu ya dhahabu uliyoisimamisha”. Shadraka na Meshaki na Abednego walijifunza
kusema hapana katikakweli waliweza kumkatalia mfalme katika kile
walichokiamini, kuwa kwao na kwa imani yao hakiko sahihi.
1Wafalme 21: 1-4 “Ikawa
baada ya hayo, Nabothi Myezreeli alikuwa na shamba la mizabibu katika Yezreeli,
karibu na nyumba ya kifalme ya Ahabu mfalme wa Samaria. Ahabu akasema na
Nabothi, akamwambia, Nipe shamba lako la mizabibu nilifanye shamba la mboga,
maana ni karibu na nyumba yangu; nami nitakupa badala yake shamba la mizabibu
lililo zuri zaidi; au ukipenda, nitakupa fedha sawasawa na thamani yake. Nabothi
akamwambia Ahabu, Bwana apishe mbali nikupe wewe urithi wa baba zangu. Basi
Ahabu akaenda nyumbani kwake, ana moyo mzito, tena amekasirika, kwa sababu ya
neno lile aliloambiwa na Nabothi Myezreeli, akisema, Sitakupa urithi wa baba
zangu. Akajilaza kitandani pake, akageuza uso wake, akakataa kula.” Unaona Nabothi pia alikuwa mtu mwenye ujasiri
wa kusema hapana katika jambo alilokuwa anaamini kuwa ni sahihi kwa utamaduni
wake na kwa mujibu wa mila zao.
Unaona kutokuwa
na uwezo wa kusema hapana ni tatizo linalowasumbua watu wengi duniani kwani
wanaogopa kuumiza wengine, wengi tunaogopa kusema hapana kwa viongozi wetu, kwa
wake zetu, kwa waume zetu, kwa wachumba zetu kwa wazazi wetu na kadhalika na
kutokna na hayo wengi wameishi maisha ya kinafiki au kufanya mambo yanayoweza
kumiza nafsi zao.
Matendo ya Mitume 5:27-29 “Walipowaleta, wakawaweka katika baraza. Kuhani Mkuu akawauliza,
akisema, Je! Hatukuwaamuru ninyi kwa nguvu, msifundishe kwa jina hili? Nanyi,
tazameni, mmeijaza Yerusalemu mafundisho yenu, na mnataka kuileta damu ya mtu
yule juu yetu. Petro na mitume wakajibu, wakisema, Imetupasa kumtii Mungu
kuliko wanadamu.”
8.
Kataa
kufanya jambo ambalo hutalikamilisha.
Luka 14:28-32 “Maana ni nani katika ninyi, kama akitaka
kujenga mnara, asiyeketi kwanza na kuhesabu gharama, kwamba anavyo vya
kuumalizia? Asije akashindwa kuumaliza baada ya kuupiga msingi, watu wote
waonao wakaanza kumdhihaki, wakisema, Mtu huyu alianza kujenga, akawa hana
nguvu za kumaliza. Au kuna mfalme gani, akitaka kwenda kupigana na mfalme
mwingine, asiyeketi kwanza na kufanya shauri, kwamba yeye pamoja na watu elfu
kumi ataweza kukutana na yule anayekuja juu yake na watu elfu ishirini? Na kama
akiona hawezi, hutuma ujumbe kutaka sharti za amani, mtu yule akali mbali.”
Maandiko
yanatufundisha kuwa ni tabia ya uungu kuanza jambo na kulikamilisha, Mungu hana
kigeugeu kama ameanza kazi njema mioyoni mwetu atahakikisha kuwa anaikamilisha Wafilipi 1:6 “Nami niliaminilo ndilo hili, ya kwamba yeye
aliyeanza kazi njema mioyoni mwenu ataimaliza hata siku ya Kristo Yesu;”
Yesu Kristo pia
anaitwa katika maandiko mwanzilishi na mwenye kutimiza imani yetu hii
inatukumbusha kuwa Mungu akianza jambo huwa haliachii njiani kwa msingi huo ni
muhimu kwa kila mmoja wetu kuhakikisha kuwa hauishii njiani katika maswala ya
aina mbalimbali, kuanzia maswala ya imani, miradi na lolote lile unalolianzisha
ni muhimu kuhakikisha kuwa haliishiinjiani, “Mtu atakumbukwa kwa kila
alichokamilisha na sio kwa kile alichojaribu”
Waebrania 12:2 “tukimtazama Yesu, mwenye
kuanzisha na mwenye kutimiza imani yetu; ambaye kwa ajili ya furaha iliyowekwa
mbele yake aliustahimili msalaba na kuidharau aibu, naye ameketi mkono wa kuume
wa kiti cha enzi cha Mungu.”
Mambo mengi sana
hapa duniani yanahitaji subira na uvumilivu, hakuna kitu kinaweza kutokea mara
moja tu vingine vinahitaji subira, watu wasio na subira hawawezi kukamilisha
mambo, kukomaa kwetu pia kiroho na kitabia na mwenendo hakutokei kwa usiku
mmoja tu ni mchakato, watu wengi wanaoshindwa kiroho ni wale ambao wanatarajia
kitu kitokee mara moja tu na kufanikiwa kwa haraka yako mambo buna budi kuwa na
subira na uvumilivu. Usianzishe jambo kwa msukumo wa kihisia tu hapana lazima
ufikiri kwa kina namna utakavyokamilisha mambo uwe na busara kama mkulima
ambaye analima na kisha anasubiria mavuno yake Yakobo 5:10-11 “Ndugu, watwaeni manabii
walionena kwa jina la Bwana, wawe mfano wa kustahimili mabaya, na wa uvumilivu.
Angalieni, twawaita heri wao waliosubiri. Mmesikia habari ya subira yake Ayubu,
mmeuona mwisho wa Bwana ya kwamba Bwana ni mwingi wa rehema, mwenye huruma.”
9.
Mwachie
Mungu Mizigo yako.
Ni muhimu
kufahamu kuwa ingawa tunamwanini Mungu na tunamwamini Yesu, hii haimaanishi
kuwa hatutapitia changamoto za namna mbalimbali, madamu tumo ulimwenguni bado
tunaweza kupitia dhiki na vikwazo na changamoto mbalimbali Yohana 16:33 “Hayo nimewaambieni mpate kuwa
na amani ndani yangu. Ulimwenguni mnayo dhiki; lakini jipeni moyo; mimi
nimeushinda ulimwengu.” Kwa nini Yesu anatuambia kuwa duniani
tunayodhiki? Yesu hataki tushangae tunapopitia majaribu ya namna mbalimbalia
hata kama sisi ni watu wake, Majaribu yanatufundisha kuvumilia na kutuleta
katika ukamilifu Yakobo 1:2-4 2. “Ndugu zangu, hesabuni ya kuwa ni furaha tupu, mkiangukia
katika majaribu mbalimbali; mkifahamu ya kuwa kujaribiwa kwa imani yenu huleta
saburi. Saburi na iwe na kazi kamilifu, mpate kuwa wakamilifu na watimilifu
bila kupungukiwa na neno”. Hata
hivyo pamoja na faida hizo za majaribu Mungu anataka tumtike yeye fadhaa zetu
zote
Zaburi 55:22 “Umtwike
Bwana mzigo wako naye atakutegemeza, Hatamwacha mwenye haki aondoshwe milele.”
1Petro 5:6-7 “Basi
nyenyekeeni chini ya mkono wa Mungu ulio hodari, ili awakweze kwa wakati
wake; huku mkimtwika yeye fadhaa zenu
zote, kwa maana yeye hujishughulisha sana kwa mambo yenu.”
Kwa mujibu wa
maandiko hayo tunapata picha iliyo wazi na ukweli kuhusu Mungu, kwamba yeye hatatuacha
tuondoshwe, yaani ahatatuachan tuaibike, Yeye anatujalia Mungu anaonyesha wazi
kuwa anauwezo wa kutusaidia kiakili, kihisia, kiroho na kimwili, yuko tayari na
anauwezo kama alivyoahidi katika neno lake Mungu huruhusu au hufanya mambo yote
yaani magumu na mepesi kwa kusudi la kutupatia mema sisi tumpendao Warumi 8:28 “Nasi
twajua ya kuwa katika mambo yote Mungu hufanya kazi pamoja na wale wampendao
katika kuwapatia mema, yaani, wale walioitwa kwa kusudi lake.” Kwa
msingi huo ni muhimu kupeleka kwake kila jamnbo linalosumbua maisha yetu, hata
wakati wa shida na tunapokuwa na mashaka hata ya kumuamini yeye , Yeye hubaki
mwaminifu na anafanya kazi kwaajili yatu kwa utukufu wake, na ametuahidi kuwa
hatatuacha tujaribiwe kuliko tuwezavyo na kwamba kwa kila jaribu ameweka mlango
wa kutokea kwa msingi huo hatatuangusha kama ilivyo ahadi yake 1Wakoritho 10:13
“Jaribu halikuwapata ninyi, isipokuwa lililo kawaida ya wanadamu; ila Mungu ni
mwaminifu; ambaye hatawaacha mjaribiwe kupita mwezavyo; lakini pamoja na lile
jaribu atafanya na mlango wa kutokea, ili mweze kustahimili.”
10.
Wewe
ni zaidi ya Mshindi.
Warumi 8:37 “Lakini
katika mambo hayo yote tunashinda, na zaidi ya kushinda, kwa yeye aliyetupenda.”
Wakristo wengi
sana wanaufahamu mstari huu au andiko hili na hulitaja mara kwa mara kwa
tafasiri mbalimbalui, kwa mujibu wa somo hili kuwa zaidi ya mshuindi maana yake
ni kuwa na ujasiri kwa jambo lolote linalokutokea katika maisha kupitia Yesu Kristo
au kwaajili ya Yesu Kristo tunaweza kabisa kulikabili kwa ushindi, hatutaogopa
na hatutaishi kwa kusumbuka kwa vile tunajua hata kama tutazamishwa katika hali
ngumu kwa kiwango chochote kila Kristo atatusaidia na kutupa ushindi
Mungu ni mkuu
kuliko Hofu zetu, kwa msingi huo maandiko yanatutaka
1.
Tuwe na furaha hata wakati wa taabu na masumbufu
ya ulimwengu huu tukijua ya kuwa Mungu anaweza kuyatumia kuzalisha uvumilivu,
kututunza, kuwa na tabia njema , sifa njema na matumaini Warumi 5:3-4 “Wala si hivyo tu, ila na mfurahi katika dhiki pia; mkijua
ya kuwa dhiki, kazi yake ni kuleta saburi; na kazi ya saburi ni uthabiti wa
moyo; na kazi ya uthabiti wa moyo ni tumaini;”
2.
Kwamba tutumia masumbufu yetu kama njia ya
kutukuza kiimani na ya kutupeleka katika ngazi nyingine ya kumtumaini Mungu
kuliko njia zetu na akili zetu kwaajili ya utukufu wake Mithali 3:5-6 “Mtumaini Bwana kwa moyo wako
wote, Wala usizitegemee akili zako mwenyewe; Katika njia zako zote mkiri yeye,
Naye atayanyosha mapito yako.”
3.
Njia ya kutii na kutufanya tuwe wema kwa kila
mtu, uwezo wa kusamehe na kuchukuliana Waefeso
4:31-32 “Uchungu wote na ghadhabu na hasira na
kelele na matukano yaondoke kwenu, pamoja na kila namna ya ubaya; tena iweni
wafadhili ninyi kwa ninyi, wenye huruma, mkasameheane kama na Mungu katika
Kristo alivyowasamehe ninyi.”
4.
Kwaajili ya kutuleta katika toba ili
tushughulikie dhambi zetu na kuwa wakeli na kuishi maisha ya haki 1Yohana 1:9 “Tukiziungama
dhambi zetu, Yeye ni mwaminifu na wa haki hata atuondolee dhambi zetu, na
kutusafisha na udhalimu wote.”
Maombi:
Mungu baba uliyejaa upendo na
fadhili, rehema zako zina wakuchao kizazi na hata kizazi, ututie nguvu wakati
wote wa masumbufu ya ulimwengu huu, uwe pamoja nasi hata tuwapo na mashaka,
utupe kujificha kwako wakati wa shida namasumbufu ya ulimwengu huu, utupe
kukukimbilia wewe ili tusiaibike kweli wanaokutumaini wewe ni kama mlima wa
Sayuni hawatatikisika milele, Katika
jina la Yesu Kristo mwana wako ninakurudishia sifa na utukufu, Amen
Na mkuu wa Wajenzi mwenye Hekima
Rev. Innocent Kamote.