Walawi 10:1-2 “Na Nadabu na Abihu, wana wa
Haruni, wakatwaa kila mtu chetezo chake, wakatia moto ndani yake,
wakatia na uvumba, nao wakatoa moto wa kigeni mbele ya BWANA, ambao yeye
hakuwaagiza. Kisha moto ukatoka hapo mbele za BWANA, nao ukawala, nao
wakafa mbele za BWANA.”
Utangulizi:
Mojawapo ya matukio
mazito ya kutisha ambayo yamerekodiwa katika Biblia hususani wakati wa
agano la kale ni pamoja na tukio la kifo cha wana wa Haruni Nadabu na
Abihu, Hili ni tukio lenye kutisha na kuogofya kama lilivyokuwa tukio la
kifo cha Anania na Safira katika Agano jipya. Tukio hili kwa mujibu wa
maandik lilisababishwa na tendo la Nadabu na Abihu kutoa Moto wa Kigeni
mbele za Bwana, kutoa moto wa kigeni kuna maanisha nini hasa? Hili ndilo
jambo la msingi na kuliangalia kwa undani na kujifunza katika nyakati
zetu leo kuwa lina maanisha nini.
Maana ya Moto wa Kigeni.
Neno moto wa kigeni Katika Biblia ya kiebrania linatajwa kama “esh
zarah” Kwa kiingereza “Alien Fire” yaani moto ulio tofauti na maagizo
“Strange fire” Jambo ambalo liko kinyume na kawaida, Jambo lisiloagizwa,
jambo lililo kinyume na mamlaka, Jambo lisilojali heshima au utukufu wa
Mungu, tukio la aina hii ndilo limeitwa moto wa kigeni. Yaani wana wa
Haruni walifanya jambo ambalo halikuagizwa na Mungu. Biblia ya
kiingereza ya King James Version KJV na New American Standard Bible NASB
yanatumia neno “Strange Fire” na Biblia ya kiingereza ya New
International Version NIV inatumia neno “unauthorized fire” Kwa hiyo
Mungu sio tu alikataa sadaka yao (Ibada yao) lakini aliwaangamiza kwa
moto na kifo kwa kutokufuata maagizo yake.
Moto wa Mungu na Moto wa Kigeni.
Ni muhimu kufahamu kuwa Biblia imetaja aina mbili za Moto, kwanza
kulikuwa na Moto uliotoka kwa Mungu na pili Nadabu na Abihu walitumia
moto wa kigeni
Unaposoma maandiko katika Mambo ya walawi 9:22-24
“Kisha Haruni akainua mikono yake na kuielekeza kwa hao watu,
akawabariki; kisha akashuka akisha isongeza sadaka ya dhambi, na sadaka
ya kuteketezwa, na sadaka za amani. Kisha Musa na Haruni wakaingia ndani
ya hema ya kukutania, kisha wakatoka nje, na kuwabarikia watu; na huo
utukufu wa BWANA ukawatokea watu wote. Kisha moto ukatoka hapo mbele za
BWANA, na kuiteketeza sadaka ya kuteketezwa, na yale mafuta juu ya
madhabahu; watu wote walipouona huo moto wakapiga kelele wakainama
kifudifudi.”
Huu ulikuwa Moto ulioshuka kutoka kwa Mungu, Mto huu
ulitokana na Musa na haruni pamoja na wanawe kufuata maelekezo yote
ambayo Mungu alikuwa amewapa jinsi na namna ya kumuabudu, Moto huu
ulileta Baraka kubwa sana kwa watu wa Mungu, Haruni kuhani mkuu
aliwabariki watu, Mto huu uliposhuka watu waliuona walipiga kelele za
utukufu kwa Mungu na waliinama na kumuabudu Mungu, Huu ulikuwa moto wa
ushindi
Unaposoma maandiko Katika Mambo ya walawi 10:1-2 “Na
Nadabu na Abihu, wana wa Haruni, wakatwaa kila mtu chetezo chake,
wakatia moto ndani yake, wakatia na uvumba, nao wakatoa moto wa kigeni
mbele ya BWANA, ambao yeye hakuwaagiza. Kisha moto ukatoka hapo mbele za
BWANA, nao ukawala, nao wakafa mbele za BWANA”
Biblia haijaweka
wazi kwamba Nadabu na Abihu walitumia aidha moto waliotumia walichukua
kutoka nje au kama huu ulikuwa Moto uleule ambao ulishuka kutoka kwa
Mungu lakini safari hii ulitumiwa na Nadabu na Abihu kwaajili ya
kuwashia vyetezo vya kufukizia uvumba, Moto ukashuka kutoka kwa Munngu
ukawaua nao wakafa, Moto huu ulisababishwa na Nadabu na Abihu kuasi na
kutokufuata maelekezo ya Mungu na hivyo Haukuleta utukufu kwa Mungu na
badala yake ulileta laana majuto na majonzi, ulikuwa ni moto wa hukumu,
vyovyote vile kama walitumia moto wa Mungu au walitumia Moto kutoka nje
ni wazi kuwa hawakuwa wanyenyekevu kutaka maelekezo kutoka kwa Mungu
kwamba vyetezo vilipaswa kutumia moto wa aina gani, uwazi ni kuwa
hawakuwa wamepokea maelekezo hivyo waliwasha moto usiamriwa na Mungu
hawakufuata maelekezo,lakini pia kulikuwa na sababu kadhaa zifuatazo:-
Nabadu na Abihu waliuawa kwa sababu kadhaa zifuatazo za kibiblia.
1. Waliasi na kutokufuata maelekezo sahihi waliyopewa na Mungu na hivyo
walishindwa kuonyesha heshima kwa Mungu Walawi 10: 3 “Ndipo Musa
akamwambia Haruni, Jambo hili ni hilo BWANA alilolinena, akisema,
Nitatakaswa mimi katika hao wanikaribiao, nami nitatukuzwa mbele ya watu
hao wote. Haruni akanyamaza kimya.”
2. Hawakumuheshimu Mungu;
Walihudhuria ibada waliwa wamelewa na hivyo walishindwa kukumbuka
maagizo ya Mungu kwa usahihi Walawi 10: 8-9 “Kisha BWANA akanena na
Haruni, na kumwambia, Usinywe divai wala kileo cho chote, wewe, wala
wanao pamoja nawe, hapo mwingiapo ndani ya hema ya kukutania, ili kwamba
msife; amri hii itakuwa ni amri ya milele katika vizazi vyenu; kisha,
mpate kupambanua kati ya yaliyo matakatifu na hayo yaliyo ya siku zote,
na kati ya yaliyo najisi na hayo yaliyo safi;” Ni wazi kuwa tabia yao ya
ulevi wa pombe na kuingia katika nyumba ya Bwana ndiko kulikopelekea
wasitiikwa usahihi maagizo ya Mungu na Mungu aliwashughulikia kwa hukumu
yenye kutisha iliyopelekea kufutwa kwao.
Fundisho:
Kwa
kifo cha hukumu ya Nadabu na Abihu kwaajili ya Moto wao wa kigeni ,
Mungu anamfundisha kila mmoja wetu kuwa Mungu hakubalkiani na namna
yoyote ya uasi na kuvunjamaagizo yake, Hatupaswi kuwa na kiburi na
kujifikiri kuwa tuna hati miliki ya Mungu, Hakuna jambo baya duniani
kama uasi, Biblia haikubaliana kabisa na uasi wa aina yoyote kwa sababu
zozote zile, Mungu anataka atukuzwe na sisi au kupitia sisi katika
mazingira yoyote yale, hakuna sababu yoyote ambayo inaweza kukubaliwa na
Mungu ya kutufanya sisi tuasi, Hata kama tunaonewa Mungu yupo na
atatulipia, lakini kuonewa kwetu kusiwe sababu ya kumuasi Mungu na
kuacha Mungu atukanwe kupitia maisha yetu.
Mungu anaijua mioyo
yetu vema Ni sadaka ya utii na unyenyekevu tu inayoweza kutuletea Baraka
kutoka kwake na kuuleta utukufu wake, Lakini hatuwezi kumtolea Mungu
Sadaka ya Kiburi na kutokutii kisha Mungu atuvumilie tu, Mungu huwapinga
wenye kiburi na kuwapa neema wanyenyekevu, Tunaponyenyekea kwake na
kumtii Mungu hutubariki na kutukubali, lakini linapokuja swala la
Utukufu na Heshima yake Mungu hawezi kukubali kuona vinaharibiwa
Mungu anachukizwa sana na watu wasiofuata maelekezo yake , watu
wasiofuata maelekezo ya Mungu maana yake wamekataa kuwa chini ya utawala
wa Mungu na hivyo Mungu huwadhibu au kuwakataa.
1Samuel 15:22-23
“Naye Samweli akasema, je! Bwana huzipenda sadaka za kuteketezwa na
dhabihu Sawasawa na kuitii sauti ya Bwana? Angalia, kutii ni bora kuliko
dhabihu, Na kusikia kuliko mafuta ya beberu. Kwani kuasi ni kama dhambi
ya uchawi, Na ukaidi ni kama ukafiri na vinyago; Kwa kuwa umelikataa
neno la Bwana, Yeye naye amekukataa wewe usiwe mfalme.”
Popote
pale unapoona watu wanachochea kuasi uongozi wa shule, au serikali, au
wazazi au Mungu, au mamlaka fahamu kwa haraka kuwa hao wanatumia moto
wa kigeni na kuwa hukumu ya Mungu haiko mbali, popote pale ambapo injili
ya aina nyingine inahubiriwa na sio ile tuliyowahubiri mjue ya kuwa huo
ni moto wa kigeni,Mafundisho potofu yaliyo kinyume na mpango halkisi wa
Mungu ni moto wa kigeni, Mungu hatoruhusu Heshima yake iharibiwe kwa
kufuata kile watu wanachokitaka na sio kile Mungu alichoagiza, Popote
pale ambapo watu wanafungisha ndoa za jinsia moja au wanakubali kwa
namna yoyote maswala ua ushoga na usagaji huo ni moto wa kigeni, Popote
pale ambapo wanapinga watoto kuadhibiwa kwa fimbo, au walimu kushika
fimbo kwaajili ya kuwaelekeza watoto sawasawa na neno la Mungu huo ni
moto wa kigeni, ppopote pale wanapotumia mziki ambao sio wa kupiga moja
kwa moja wakati wa kumsifu Mungu huo ni moto wa kigeni, popote pale
ambapo watu wanaoongoza ibada wanavaa nusu uchi huo nao ni moto wa
kigeni na utaharibu maisha yetu, utatuua hautaleta utukufu wa Mungu,
kwetu utatunyima Baraka zilizokusudiwa kwetu, ni lazima tutubu kwa dhati
na kumuomba Mungu atusamehe kila inapotokea mbegu ya uasi dhidi ya
Mungu katikati yetu na kila linapotokea swala linalofanywa ambalo liko
kinyume na Maagizo ya Mungu.
Musa alikuwa ni nabii aliyeheshimika
sana na Mungu lakini Mungu hakumuachia aingie kanaani pale aliposhindwa
kutii maagizo ya Mungu, ni lazima watu wa Mungu waogope kufuata
maelekezo mengine ambayo sio ya neno lake.
Kumbukumbu 34:10 “Wala hajainuka tena katika Israeli nabii kama Musa, ambaye Bwana alimjua uso kwa uso;”
Pamoja na ukuu wote aliokuwa nao Musa aliadhibiwa vikali pale aliposhindwa kuyatii maagizo ya Mungu .
Hesabu 20: 7-13 “Bwana akasema na Musa, akinena, Twaa ile fimbo,
ukawakusanye mkutano, wewe na Haruni ndugu yako, ukauambie mwamba mbele
ya macho yao utoe maji yake, nawe utawatokezea maji katika mwamba, na
hivyo utawanywesha maji mkutano na wanyama wao. Musa akaitwaa hiyo
fimbo kutoka mbele za Bwana kama alivyomwamuru. Musa na Haruni
wakawakusanya kusanyiko mbele ya mwamba, akawaambia, Sikieni sasa, enyi
waasi; je! Tuwatokezee maji katika mwamba huu? Musa akainua mkono wake
akaupiga ule mwamba kwa fimbo yake mara mbili; maji yakatoka mengi,
mkutano wakanywa na wanyama wao pia. Bwana akamwambia Musa na Haruni,
Kwa kuwa hamkuniamini mimi, ili kunistahi mbele ya macho ya wana wa
Israeli, basi kwa sababu hiyo, hamtawaingiza kusanyiko hili katika ile
nchi niliyowapa. Maji haya ni maji ya Meriba; kwa sababu wana wa Israeli
waliteta na Bwana, naye alijionyesha kuwa mtakatifu kati yao”.
Mtu anayeweza kufurahia Baraka za Mungu kwa vyovyote vile atakuwa mtu
yule ambaye anafuata maagizo ya Mungu na kuyashika vilevile bila
kuangalia mkono wa kushoto au wa kiume, ni muhimu kukaza injili
tuliyoipokea na kukaa katika utuu na maagizo ya Bwana,
Joshua 1:5-8
“Hapatakuwa mtu ye yote atakayeweza kusimama mbele yako siku zote za
maisha yako; kama nilivyokuwa pamoja na Musa, ndivyo nitakavyokuwa
pamoja na wewe; sitakupungukia wala sitakuacha. Uwe hodari na moyo wa
ushujaa, maana ni wewe utakayewarithisha watu hawa nchi hii niliyowaapia
baba zao ya kwamba nitawapa. Uwe hodari tu na ushujaa mwingi, uangalie
kutenda sawasawa na sheria yote aliyokuamuru Musa mtumishi wangu;
usiiache, kwenda mkono wa kuume, au wa kushoto, upate kufanikiwa sana
kila uendako. Kitabu hiki cha torati kisiondoke kinywani mwako, bali
yatafakari maneno yake mchana na usiku, upate kuangalia kutenda sawasawa
na maneno yote yaliyoandikwa humo; maana ndipo utakapoifanikisha njia
yako, kisha ndipo utakapositawi sana. Je! Si mimi niliyekuamuru? Uwe
hodari na moyo wa ushujaa; usiogope wala usifadhaike; kwa kuwa Bwana,
Mungu wako, yu pamoja nawe kila uendako.”
Mungu atupe neema leo kukumbuka kufuata maagizo ya Mungu na kuyatii katika jina la Yesu Kristo wa Nazareth mwana wa Mungu aliye hai, Amen!
Rev. Innocent Kamote.
Mkuu wa wajenzi mwenye Hekima.