Jumapili, 25 Novemba 2018

Moto wa Kigeni!


Walawi 10:1-2Na Nadabu na Abihu, wana wa Haruni, wakatwaa kila mtu chetezo chake, wakatia moto ndani yake, wakatia na uvumba, nao wakatoa moto wa kigeni mbele ya BWANA, ambao yeye hakuwaagiza. Kisha moto ukatoka hapo mbele za BWANA, nao ukawala, nao wakafa mbele za BWANA.”


Utangulizi:

Mojawapo ya matukio mazito ya kutisha ambayo yamerekodiwa katika Biblia hususani wakati wa agano la kale ni pamoja na tukio la kifo cha wana wa Haruni Nadabu na Abihu, Hili ni tukio lenye kutisha na kuogofya kama lilivyokuwa tukio la kifo cha Anania na Safira katika Agano jipya. Tukio hili kwa mujibu wa maandik lilisababishwa na tendo la Nadabu na Abihu kutoa Moto wa Kigeni mbele za Bwana, kutoa moto wa kigeni kuna maanisha nini hasa? Hili ndilo jambo la msingi na kuliangalia kwa undani na kujifunza katika nyakati zetu leo kuwa lina maanisha nini.

Maana ya Moto wa Kigeni.

Neno moto wa kigeni Katika Biblia ya kiebrania linatajwa kama “esh zarah” Kwa kiingereza “Alien Fire” yaani moto ulio tofauti na maagizo “Strange fire” Jambo ambalo liko kinyume na kawaida, Jambo lisiloagizwa, jambo lililo kinyume na mamlaka, Jambo lisilojali heshima au utukufu wa Mungu, tukio la aina hii ndilo limeitwa moto wa kigeni. Yaani wana wa Haruni walifanya jambo ambalo halikuagizwa na Mungu. Biblia ya kiingereza ya King James Version KJV na New American Standard Bible NASB yanatumia neno “Strange Fire” na Biblia ya kiingereza ya New International Version NIV inatumia neno “unauthorized fire” Kwa hiyo Mungu sio tu alikataa sadaka yao (Ibada yao) lakini aliwaangamiza kwa moto na kifo kwa kutokufuata maagizo yake.

Moto wa Mungu na Moto wa Kigeni.

Ni muhimu kufahamu kuwa Biblia imetaja aina mbili za Moto, kwanza kulikuwa na Moto uliotoka kwa Mungu na pili Nadabu na Abihu walitumia moto wa kigeni

Unaposoma maandiko katika Mambo ya walawi 9:22-24 “Kisha Haruni akainua mikono yake na kuielekeza kwa hao watu, akawabariki; kisha akashuka akisha isongeza sadaka ya dhambi, na sadaka ya kuteketezwa, na sadaka za amani. Kisha Musa na Haruni wakaingia ndani ya hema ya kukutania, kisha wakatoka nje, na kuwabarikia watu; na huo utukufu wa BWANA ukawatokea watu wote. Kisha moto ukatoka hapo mbele za BWANA, na kuiteketeza sadaka ya kuteketezwa, na yale mafuta juu ya madhabahu; watu wote walipouona huo moto wakapiga kelele wakainama kifudifudi.

Huu ulikuwa Moto ulioshuka kutoka kwa Mungu, Mto huu ulitokana na Musa na haruni pamoja na wanawe kufuata maelekezo yote ambayo Mungu alikuwa amewapa jinsi na namna ya kumuabudu, Moto huu ulileta Baraka kubwa sana kwa watu wa Mungu, Haruni kuhani mkuu aliwabariki watu, Mto huu uliposhuka watu waliuona walipiga kelele za utukufu kwa Mungu na waliinama na kumuabudu Mungu, Huu ulikuwa moto wa ushindi

Unaposoma maandiko Katika Mambo ya walawi 10:1-2 “Na Nadabu na Abihu, wana wa Haruni, wakatwaa kila mtu chetezo chake, wakatia moto ndani yake, wakatia na uvumba, nao wakatoa moto wa kigeni mbele ya BWANA, ambao yeye hakuwaagiza. Kisha moto ukatoka hapo mbele za BWANA, nao ukawala, nao wakafa mbele za BWANA” 

Biblia haijaweka wazi kwamba Nadabu na Abihu walitumia aidha moto waliotumia walichukua kutoka nje au kama huu ulikuwa Moto uleule ambao ulishuka kutoka kwa Mungu lakini safari hii ulitumiwa na Nadabu na Abihu kwaajili ya kuwashia vyetezo vya kufukizia uvumba, Moto ukashuka kutoka kwa Munngu ukawaua nao wakafa, Moto huu ulisababishwa na Nadabu na Abihu kuasi na kutokufuata maelekezo ya Mungu na hivyo Haukuleta utukufu kwa Mungu na badala yake ulileta laana majuto na majonzi, ulikuwa ni moto wa hukumu, vyovyote vile kama walitumia moto wa Mungu au walitumia Moto kutoka nje ni wazi kuwa hawakuwa wanyenyekevu kutaka maelekezo kutoka kwa Mungu kwamba vyetezo vilipaswa kutumia moto wa aina gani, uwazi ni kuwa hawakuwa wamepokea maelekezo hivyo waliwasha moto usiamriwa na Mungu hawakufuata maelekezo,lakini pia kulikuwa na sababu kadhaa zifuatazo:-

Nabadu na Abihu waliuawa kwa sababu kadhaa zifuatazo za kibiblia.

1. Waliasi na kutokufuata maelekezo sahihi waliyopewa na Mungu na hivyo walishindwa kuonyesha heshima kwa Mungu Walawi 10: 3Ndipo Musa akamwambia Haruni, Jambo hili ni hilo BWANA alilolinena, akisema, Nitatakaswa mimi katika hao wanikaribiao, nami nitatukuzwa mbele ya watu hao wote. Haruni akanyamaza kimya.”

2. Hawakumuheshimu Mungu; Walihudhuria ibada waliwa wamelewa na hivyo walishindwa kukumbuka maagizo ya Mungu kwa usahihi Walawi 10: 8-9 “Kisha BWANA akanena na Haruni, na kumwambia, Usinywe divai wala kileo cho chote, wewe, wala wanao pamoja nawe, hapo mwingiapo ndani ya hema ya kukutania, ili kwamba msife; amri hii itakuwa ni amri ya milele katika vizazi vyenu; kisha, mpate kupambanua kati ya yaliyo matakatifu na hayo yaliyo ya siku zote, na kati ya yaliyo najisi na hayo yaliyo safi;” Ni wazi kuwa tabia yao ya ulevi wa pombe na kuingia katika nyumba ya Bwana ndiko kulikopelekea wasitiikwa usahihi maagizo ya Mungu na Mungu aliwashughulikia kwa hukumu yenye kutisha iliyopelekea kufutwa kwao.

Fundisho:

Kwa kifo cha hukumu ya Nadabu na Abihu kwaajili ya Moto wao wa kigeni , Mungu anamfundisha kila mmoja wetu kuwa Mungu hakubalkiani na namna yoyote ya uasi na kuvunjamaagizo yake, Hatupaswi kuwa na kiburi na kujifikiri kuwa tuna hati miliki ya Mungu, Hakuna jambo baya duniani kama uasi, Biblia haikubaliana kabisa na uasi wa aina yoyote kwa sababu zozote zile, Mungu anataka atukuzwe na sisi au kupitia sisi katika mazingira yoyote yale, hakuna sababu yoyote ambayo inaweza kukubaliwa na Mungu ya kutufanya sisi tuasi, Hata kama tunaonewa Mungu yupo na atatulipia, lakini kuonewa kwetu kusiwe sababu ya kumuasi Mungu na kuacha Mungu atukanwe kupitia maisha yetu.

Mungu anaijua mioyo yetu vema Ni sadaka ya utii na unyenyekevu tu inayoweza kutuletea Baraka kutoka kwake na kuuleta utukufu wake, Lakini hatuwezi kumtolea Mungu Sadaka ya Kiburi na kutokutii kisha Mungu atuvumilie tu, Mungu huwapinga wenye kiburi na kuwapa neema wanyenyekevu, Tunaponyenyekea kwake na kumtii Mungu hutubariki na kutukubali, lakini linapokuja swala la Utukufu na Heshima yake Mungu hawezi kukubali kuona vinaharibiwa
Mungu anachukizwa sana na watu wasiofuata maelekezo yake , watu wasiofuata maelekezo ya Mungu maana yake wamekataa kuwa chini ya utawala wa Mungu na hivyo Mungu huwadhibu au kuwakataa.

1Samuel 15:22-23 “Naye Samweli akasema, je! Bwana huzipenda sadaka za kuteketezwa na dhabihu Sawasawa na kuitii sauti ya Bwana? Angalia, kutii ni bora kuliko dhabihu, Na kusikia kuliko mafuta ya beberu. Kwani kuasi ni kama dhambi ya uchawi, Na ukaidi ni kama ukafiri na vinyago; Kwa kuwa umelikataa neno la Bwana, Yeye naye amekukataa wewe usiwe mfalme.” 

Popote pale unapoona watu wanachochea kuasi uongozi wa shule, au serikali, au wazazi au Mungu, au mamlaka fahamu kwa haraka kuwa hao wanatumia moto wa kigeni na kuwa hukumu ya Mungu haiko mbali, popote pale ambapo injili ya aina nyingine inahubiriwa na sio ile tuliyowahubiri mjue ya kuwa huo ni moto wa kigeni,Mafundisho potofu yaliyo kinyume na mpango halkisi wa Mungu ni moto wa kigeni, Mungu hatoruhusu Heshima yake iharibiwe kwa kufuata kile watu wanachokitaka na sio kile Mungu alichoagiza, Popote pale ambapo watu wanafungisha ndoa za jinsia moja au wanakubali kwa namna yoyote maswala ua ushoga na usagaji huo ni moto wa kigeni, Popote pale ambapo wanapinga watoto kuadhibiwa kwa fimbo, au walimu kushika fimbo kwaajili ya kuwaelekeza watoto sawasawa na neno la Mungu huo ni moto wa kigeni, ppopote pale wanapotumia mziki ambao sio wa kupiga moja kwa moja wakati wa kumsifu Mungu huo ni moto wa kigeni, popote pale ambapo watu wanaoongoza ibada wanavaa nusu uchi huo nao ni moto wa kigeni na utaharibu maisha yetu, utatuua hautaleta utukufu wa Mungu, kwetu utatunyima Baraka zilizokusudiwa kwetu, ni lazima tutubu kwa dhati na kumuomba Mungu atusamehe kila inapotokea mbegu ya uasi dhidi ya Mungu katikati yetu na kila linapotokea swala linalofanywa ambalo liko kinyume na Maagizo ya Mungu.

Musa alikuwa ni nabii aliyeheshimika sana na Mungu lakini Mungu hakumuachia aingie kanaani pale aliposhindwa kutii maagizo ya Mungu, ni lazima watu wa Mungu waogope kufuata maelekezo mengine ambayo sio ya neno lake.

Kumbukumbu 34:10 “Wala hajainuka tena katika Israeli nabii kama Musa, ambaye Bwana alimjua uso kwa uso;”

Pamoja na ukuu wote aliokuwa nao Musa aliadhibiwa vikali pale aliposhindwa kuyatii maagizo ya Mungu .

Hesabu 20: 7-13 “Bwana akasema na Musa, akinena, Twaa ile fimbo, ukawakusanye mkutano, wewe na Haruni ndugu yako, ukauambie mwamba mbele ya macho yao utoe maji yake, nawe utawatokezea maji katika mwamba, na hivyo utawanywesha maji mkutano na wanyama wao. Musa akaitwaa hiyo fimbo kutoka mbele za Bwana kama alivyomwamuru. Musa na Haruni wakawakusanya kusanyiko mbele ya mwamba, akawaambia, Sikieni sasa, enyi waasi; je! Tuwatokezee maji katika mwamba huu? Musa akainua mkono wake akaupiga ule mwamba kwa fimbo yake mara mbili; maji yakatoka mengi, mkutano wakanywa na wanyama wao pia. Bwana akamwambia Musa na Haruni, Kwa kuwa hamkuniamini mimi, ili kunistahi mbele ya macho ya wana wa Israeli, basi kwa sababu hiyo, hamtawaingiza kusanyiko hili katika ile nchi niliyowapa. Maji haya ni maji ya Meriba; kwa sababu wana wa Israeli waliteta na Bwana, naye alijionyesha kuwa mtakatifu kati yao”.

Mtu anayeweza kufurahia Baraka za Mungu kwa vyovyote vile atakuwa mtu yule ambaye anafuata maagizo ya Mungu na kuyashika vilevile bila kuangalia mkono wa kushoto au wa kiume, ni muhimu kukaza injili tuliyoipokea na kukaa katika utuu na maagizo ya Bwana, 

Joshua 1:5-8 “Hapatakuwa mtu ye yote atakayeweza kusimama mbele yako siku zote za maisha yako; kama nilivyokuwa pamoja na Musa, ndivyo nitakavyokuwa pamoja na wewe; sitakupungukia wala sitakuacha. Uwe hodari na moyo wa ushujaa, maana ni wewe utakayewarithisha watu hawa nchi hii niliyowaapia baba zao ya kwamba nitawapa. Uwe hodari tu na ushujaa mwingi, uangalie kutenda sawasawa na sheria yote aliyokuamuru Musa mtumishi wangu; usiiache, kwenda mkono wa kuume, au wa kushoto, upate kufanikiwa sana kila uendako. Kitabu hiki cha torati kisiondoke kinywani mwako, bali yatafakari maneno yake mchana na usiku, upate kuangalia kutenda sawasawa na maneno yote yaliyoandikwa humo; maana ndipo utakapoifanikisha njia yako, kisha ndipo utakapositawi sana. Je! Si mimi niliyekuamuru? Uwe hodari na moyo wa ushujaa; usiogope wala usifadhaike; kwa kuwa Bwana, Mungu wako, yu pamoja nawe kila uendako.” 

Mungu atupe neema leo kukumbuka kufuata maagizo ya Mungu na kuyatii katika jina la Yesu Kristo wa Nazareth mwana wa Mungu aliye hai, Amen!

Rev. Innocent Kamote.

Mkuu wa wajenzi mwenye Hekima.

0718990796

Hata sasa Bwana ametusaidia!


1Samuel 7:12 “Ndipo Samweli akatwaa jiwe, na kulisimamisha kati ya Mispa na Sheni, akaliita jina lake Eben-ezeri, akisema, Hata sasa Bwana ametusaidia.


Utangulizi:
Ni muhimu kufahamu kuwa wana wa Israel, waliwahi kupigwa vibaya sana na kusambaratishwa mbele ya adui zao, swalala Israel kushindwa lilikuwa swala la aibu kubwa sana katika maisha yao, Wao walitambua kuwa Mungu yuko pamoja nao na hivyo isingeliweza kuwa rahisi kwao kushindwa vita, lakini bilia inaonyesha kuwa Israel walipigwa vibaya na wazee walifikiri kuwa endapo watalileta sanduku la agano labda huenda wangeweza kupata ushindi hata hivyo safari hii walipigwa vibaya na hata sanduku la agano lilichukuliwa mateka
1Samuel 4:1-11 “[Ikawa siku zile Wafilisti walikusanyika ili kupigana na Israeli,] nao Waisraeli wakatoka juu ya Wafilisti kwenda vitani;wakatua karibu na Ebenezeri ,nao Wafilisti wakatua huko Afeki. Nao Wafilisti wakajipanga juu ya Israeli; na walipopigana, Israeli wakapigwa mbele ya Wafilisti; wakauawa watu wa jeshi lao lililokuwa uwandani wapata watu elfu nne. Hata watu walipofika kambini, wazee wa Israeli wakasema, Mbona Bwana ametupiga leo mbele ya Wafilisti? Twende tukalilete sanduku la agano la Bwana toka Shilo hata huku, lije kati yetu, na kutuokoa katika mikono ya adui zetu. Basi wakatuma watu kwenda Shilo, nao wakalileta toka huko sanduku la agano la Bwana wa majeshi, akaaye juu ya makerubi; na Hofni na Finehasi, wana wawili wa Eli, walikuwako huko pamoja na sanduku la agano la Mungu. Na sanduku la agano la Bwana lilipoingia kambini, Israeli wote wakapiga kelele kwa sauti kuu, hata nchi ikavuma. Nao Wafilisti waliposikia mshindo wa zile kelele, walisema, Maana yake nini mshindo wa kelele hizi kubwa katika kambi ya Waebrania? Wakatambua ya kuwa sanduku la Bwana limefika kambini. Wafilisti wakaogopa, maana walisema, Mungu ameingia kambini. Wakasema, Ole wetu! Kwani halijawa jambo kama hili tangu hapo. Ole wetu! Ni nani atakayetuokoa na mkono wa miungu hawa walio hodari? Hawa ndio miungu waliowapiga Wamisri kwa mapigo ya kila namna jangwani. Iweni hodari, na kufanya kiume enyi Wafilisti, msije mkawa watumwa wa Waebrania, kama wao walivyokuwa watumwa wenu; fanyeni kiume, mkapigane nao. Wafilisti wakapigana nao, Israeli wakapigwa, wakakimbia kila mtu hemani kwake; wakauawa watu wengi sana; maana katika Israeli walianguka watu thelathini elfu wenye kwenda vitani kwa miguu. Hilo sanduku la Mungu Likatwaliwa; na Hofni na Finehasi, wale wana wawili wa Eli, wakauawa.”
Unaweza kuona tukio hili la kusikitisha ambalo lilitokea kabla Samuel hajawa Mwamuzi wa Israel, lilikuwa tukio la kusikitisha na lililoleta simanzi kubwa sana kwa wana wa Israel, jambo hili liliwapa kujitafakari kwa nini wamepoteza ushindi katika maisha yao! Israel waligundua siri ya kushindwa kwao vibaya katika vita hii na hivyo chini ya Samuel walijipanga tena kuutafuta uso wa Mungu wa Israel, kwani sababu ilikuwa wazi kuwa kushindwa kwao kulitokana na maisha yao ya kuabudu miungu na kumuacha Mungu wa kweli, sasa Israel walitambua kuwa wamekosa na hivyo walianza kutafuta ushindi. Kanuni za ushindi.

Mungu aliweza kuwajilia tena baada ya kufuata kanuni kadhaa na kuweza kuwasaidia na kuwapa Ushindi.
1Samuel 7:3-12Basi Samweli akawaambia nyumba yote ya Israeli, akasema, Ikiwa mnamrudia Bwana kwa mioyo yenu yote, basi, iondoleeni mbali miungu migeni, nayo Maashtorethi yatoke kwenu, mkamtengenezee Bwana mioyo yenu, mkamtumikie yeye peke yake; naye atawaokoa katika mikono ya Wafilisti. Ndipo wana wa Israeli wakayaondoa Mabaali na Maashtorethi, wakamtumikia Bwana peke yake. Samweli akasema, Wakusanyeni Israeli wote Mispa, nami nitawaombea ninyi kwa Bwana. Wakakusanyika huko Mispa, wakateka maji na kuyamimina mbele za Bwana; wakafunga siku ile, wakasema huko, Tumemfanyia Bwana dhambi. Samweli akawaamua wana wa Israeli huko Mispa. Hata Wafilisti waliposikia ya kuwa wana wa Israeli wamekusanyika huko Mispa, mashehe wa Wafilisti walipanda juu ili kupigana na Israeli. Nao wana wa Israeli waliposikia, wakawaogopa Wafilisti. Wana wa Israeli wakamwambia Samweli, Usiache kumlilia Bwana, Mungu wetu, kwa ajili yetu, kwamba atuokoe na mikono ya Wafilisti. Ndipo Samweli akatwaa mwana-kondoo mchanga, akamtolea Bwana sadaka ya kuteketezwa nzima; Samweli akamlilia Bwana kwa ajili ya Israeli; Bwana akamwitikia. Hata Samweli alipokuwa akiitoa hiyo sadaka ya kuteketezwa, Wafilisti wakakaribia ili kupigana na Israeli; walakini Bwana akapiga ngurumo, mshindo mkubwa sana, juu ya Wafilisti siku ile, akawafadhaisha; nao wakaangamizwa mbele ya Israeli.Nao watu wa Israeli wakatoka Mispa, wakawafuatia Wafilisti, wakawapiga, hata walipofika chini ya Beth-kari. Ndipo Samweli akatwaa jiwe, na kulisimamisha kati ya Mispa na Sheni, akaliita jina lake Eben-ezeri, akisema, Hata sasa Bwana ametusaidia. Hivyo Wafilisti walishindwa, wasiingie tena ndani ya mipaka ya Israeli; na mkono wa Bwana ulikuwa juu ya Wafilisti siku zote za Samweli. Nayo miji ile Wafilisti waliyokuwa wamewapokonya Waisraeli ilirudishwa tena kwa Israeli, tokea Ekroni mpaka Gathi; na Waisraeli wakauokoa mpaka wake mikononi mwa Wafilisti. Tena kulikuwa na amani kati ya Israeli na Waamori. Naye huyo Samweli akawaamua Israeli siku zote za maisha yake.”
Unaweza kuona Israel walipata ushindi mkubwa baada ya kuchukua hatua za kurejea katika kanuni za kimungu zilizowapa ushindi.
1. Waloimrudia Bwana kwa Moyo yaani walitubu na kuacha dhambi zao hususani za kuabudu miungu.
2. Walimtumikia Mungu yaani walimuabudu kwa moyo safi.
3. Waliteka maji na kuyamimina mbele za Bwana – kumimina maji ni lugha ya fumbo ambayo maana yake ni kuanguka chini na kuomba Zaburi 22:14 “Nimemwagika kama maji, Mifupa yangu yote imeteguka, Moyo wangu umekuwa kama nta, Na kuyeyuka ndani ya mtima wangu.” Hivyo Israel walianguka chini na kufanya maombi ya unyenyekevu yaliyoambatana na kufunga.
4. Walimuomba Samuel Nabii awaombeee kwa Mungu na kuwa asiache kuwa mwombezi katikati yao Samuel aliwaombea na Mungu alimjibu.
5. Kisha Maadui wa Israel waliinuka tena na safari hii walipigwa vibaya na kutolewa nje kabisa.
Ni ukweli ulio wazi kuwa Mungu aliwasaidia sana Israel, katika mji uleule mahali walipopigwa vibaya waliwashinda adui zao na kuwapiga vinbaya na kujikomboa, ni ukweli uliowazi kuwa Samuel alijua kuwa Mungu nsasa ameanza kuwasaidia watu wake, na alitaka kuweka kumbukumbu ya ushindi ule kwa jiwe alilolisimamisha na Kupaita mahali Pale EBEN-EZER yaani hata sasa Mungu ametusaidia.
Je maisha yako ni ya ushindi? Ni wapi umekwama Mungu anakupa nafasi ya kumrudia yeye na kuumimina moyo wako kwake, ni muhimu kukumbuka kuwa tunaye mwomnbezi, Yesu Kristo yeye ni Jiwe lililo hai, yeye ni muombezi wetu anatuombea na atatupa ushindi tukiwa naye hakuna kitu kitaweza kusimama mbele yetu, Israel waliwezakupata ushindi na adui hakuweza kusimama mbele yao siku zote za Samuel, Tunaweza kuwa na ushindi tukiwa na kuhani mwombezi aliyeketi mkono wa kuume wa Mungu baba naye anatuombea siku zote yeye ndiye kipatanisho kati yetu na Mungu, yeye ndiye chanzo cha ushindi wetu, Yeye ni Ebenezaer Jiwe la ushindi wetu, hata kama kulikuwa na historia ya kushindwa yeye Mungu wetu atatupa ushindi, na kuifuta historia ya kushindwa kwetu na kuwa ushindi wetu.
Na Rev. Innocent Kamote.
Mkuu wa Wajenzi mwenye Hekima.

Msijisumbue kwa neno lo lote; bali katika kila neno kwa kusali na kuomba

Wafilipi 4:6-7 “Msijisumbue kwa neno lo lote; bali katika kila neno kwa kusali na kuomba, pamoja na kushukuru, haja zenu na zijulikane na Mungu. Na amani ya Mungu, ipitayo akili zote, itawahifadhi mioyo yenu na nia zenu katika Kristo Yesu."
 
 Unapokuwa umemtegemea Mungu huna sababu ya kuogopa Yeye yu pamoja nawe Zaburi 118:6

Utangulizi:
Neno usijisumbue lilikuwa ni moja ya Misingi mikubwa katika Mafundisho ya Bwana Yesu Mathatyo 6:25, 34 zinasema “Kwa sababu hiyo nawaambieni, Msisumbukie maisha yenu, mle nini au mnywe nini; wala miili yenu, mvae nini. Maisha je! Si zaidi ya chakula, na mwili zaidi ya mavazi?, Basi msisumbukie ya kesho; kwa kuwa kesho itajisumbukia yenyewe. Yatosha kwa siku maovu yake.”

Msisumbuke!

Mungu katika mapenzi yake hataki sisi tusumbuke yaani tujiumize kwa mashaka na wasiwasi kama wasioamini, Usumbufu huu ni usumbufu wa Moyo uitwao “ANXIETY”ambalo maana yake ni kuogopa au kuhofia au kutetemeka kwaajili ya jambo fulani linalohuisiana na maisha, Kama tutafikiri kwa akili zetu za kibinadamu kwa jambo lolote gumu katika maisha yetu ni dhahiri kuwa tutazama katika masumbufu na mashaka , lakini kama tutamshirikisha Mungu ukweli wa kimaandiko ni kuwa tutakuwa juu ya mashaka yetu

Mithali 3:5-6 “.Mtumaini Bwana kwa moyo wako wote, Wala usizitegemee akili zako mwenyewe; Katika njia zako zote mkiri yeye, Naye atayanyosha mapito yako.”

Watakatifu waliotutangulia walikuwa na ufahamu wa kutosha kuwa kila unapokutana na changamoto za aina yoyote hupaswi kujisumbua katika jambo lolote zaidi ya kuomba na kumshukuru Mungu yaani kumfanyia bwana ibada, Petro huenda alikuwa na ujuzi na uzoefu kuwa kila changamoto mitume waliweza kuikabili kwa maombi, walipofadhaika walimwambia Mungu,lakini sio hivyo tu bali hata manabii walipokuwa na changamoto waliweza kuomba Ndugu zango hata leo maombi ndio ufunguo wa kukomesha aina yoyote ya mashaka na wasiwasi, hofu na kuleta majibu ya maswali magumu katika masha yetu.

1. Tumtwike yeye fadhaa zetu zote 1Petro 5:6-7Basi nyenyekeeni chini ya mkono wa Mungu ulio hodari, ili awakweze kwa wakati wake; huku mkimtwika yeye fadhaa zenu zote, kwa maana yeye hujishughulisha sana kwa mambo yenu.” Mtume Petro alikuwa na ujuzi wa kutosha kuwa kila unapokutana na changamoto zozote unapaswa kumtwika Mungu swala hilo kisha kustarehe ku “relax” ni wazi kuwa mitume na watakatifu waliotutangulia walikuwa na uelewa huu wazi kuwa linapokuja swala linalosumbua moyo unalipeleka katika maombi kisha unaamini kuwa Mungu atashughulikia na ni kweli atalishughulikia! Unaona angalia walivyofanya walipokutana na changamoto hapa chini katika Matendo 4;24-31 waliomba na Mungu aliwatia nguvu.

2. Matendo 4:24-31Nao waliposikia, wakampazia Mungu sauti zao kwa moyo mmoja, wakisema, Mola, wewe ndiwe Mungu, ndiwe uliyefanya mbingu na nchi na bahari na vitu vyote vilivyomo; nawe ulinena kwa Roho Mtakatifu kwa kinywa cha babaetu Daudi, mtumishi wako, Mbona mataifa wamefanya ghasia, Na makabila wametafakari ubatili? Wafalme wa dunia wamejipanga, Na wakuu wamefanya shauri pamoja Juu ya Bwana na juu ya Kristo wake. Maana ni kweli, Herode na Pontio Pilato pamoja na Mataifa na watu wa Israeli, walikusanyika katika mji huu juu ya Mtumishi wako mtakatifu Yesu, uliyemtia mafuta, ili wafanye yote ambayo mkono wako na mashauri yako yamekusudia tangu zamani yatokee. Basi sasa, Bwana, yaangalie matisho yao; ukawajalie watumwa wako kunena neno lako kwa ujasiri wote, ukinyosha mkono wako kuponya; ishara na maajabu vifanyike kwa jina la Mtumishi wako mtakatifu Yesu. Hata walipokwisha kumwomba Mungu, mahali pale walipokusanyika pakatikiswa, wote wakajaa Roho Mtakatifu, wakanena neno la Mungu kwa ujasiri.”

3. Daniel 6:10Hata Danieli, alipojua ya kuwa yale maandiko yamekwisha kutiwa sahihi, akaingia nyumbani mwake, (na madirisha katika chumba chake yalikuwa yamefunguliwa kukabili Yerusalemu;) akapiga magoti mara tatu kila siku, akasali, akashukuru mbele za Mungu wake, kama alivyokuwa akifanya tokea hapo.” Unaweza kuona pia kwa Daniel ni wazi kuwa ni mapenzi ya Mungu kwamba tusijisumbue katika neno lolote, tusiogope lolote, tuombe Mungu hata kama swala hilo liko kinyume na serikali, liko kinyume na wafalme, madam liko kinyume na mapenzi ya Mungu wewe omba tu kisha Mungu atalijibu mtegemee yeye, relax kama mtu aliyeruka na parachute.

Ushindi wetu na uthabiti wetu uko katika maombi na kumtegemea Mungu na sio kuogopa, na Ukiisha kumuomba Mungu furahi na kutulia.

Na mkuu wa wajenzi mwenye Hekima
Rev. Innocent Kamote

Jumatatu, 15 Oktoba 2018

Maisha ya Nabii Yusufu:


1.Timotheo 4:12 “Mtu awaye yote asiudharau ujana wako, bali uwe kielelezo kwao waaminio, katika usemi na mwenendo, na katika upendo na imani na usafi.”


Yakobo alikuwa makini wakati wa Kuweka Mikono Mkono wa kuume ni Yule unayekusudia kumfanya kuwa kicha na Mkono wa Kushoto ni Yule unayekusudia awe mdogo Je wachungaji nwa leo wanaweka vipi Mikono? Wakati wa kubariki Ndoa ua viongozi wa kanisa, usiweke mikono hovyo hovyo kuna kanuni Yusufu na Yakobo walizijuaMwanzo 48:1-22

Utangulizi:

Maisha ya Yusufu ni moja ya Maisha ya mfano, na ya kuigwakatika Biblia, Tunaona Biblia ikizungumza kwa upana kuhusu uumbaji kwatika Mwanzo 1-2, wakati Mwanzo 3 pekee ikizungumzia Anguko la Mwanadamu, Mwanzo 4-5 habari ya kaini na Habili pamoja na kuongezeka kwa maasi, Mwanzo 6-9 Ni habari za Gharika na Nuhu mtu wa Mungu, Mwanzo 10-11 ni habari za Mnara wa Babeli na kutawanyika kwa mataifa, Mwanzo 12-24 ni Habari za Ibrahimu baba wa Imani,  Mwanzo 25-36 Kidogo Isaka, Esau lakini zaidi sana Yakobo, Mwanzo37:1-50:26 Ni habari za Yusufu, Kwa hiyo utaweza kuona Kuwa Neno la Mungu linamzungumzia Yusufu kwa upana na urafu zaidi, huku Biblia ikiwa haijawahi kuonyesha uzaifu wowote aliokuwa nao Yusufu, Kuna kitu cha ziada cha kujifunza katika maisha yake.

Yusufu anapewa Madaraka makubwa sana Katika Biblia, Miongoni mwa mababa wa Isarel Yusufu ni Mmojawao “The Patriarchs” hii ilikuwa nafasi ambayo labda Ruben angepewa Lakini kutokana na uaminifu wa Yusufu baba yake alimpa mbaraka huu kwa hiyo wakitajwa Mababa wa taifa la Israel basi Yusufu Ni mmojawao

a.      Abraham baba wa imani
b.      Isaka Mwana wa Ahadi
c.       Yakobo (Israel) Baba wa taifa la kiyahudi baba wa Kabila 12 za Israel
d.      Yusufu Mwokozi wa Israel na Misri Baba wa Kabila mbili za Israel Manaseh na Efraimu

Pamoja na umuhimu wao wote utaweza kuona habariza Yusufu zinaandikwa kwa kina zaidi kuliko wengine na hakuna dhambi yoyote inaonyeshwa kuhusu Maisha ya Yusufu, Maisha yake yenye uadilifu wa hali ya juu, Usafi wa Moyo, na maisha, kutokulipiza Kisasi, kuelewa vema makusudi na mipango ya Mungu, kuna mfanya kuwa mtu wa kuigwa miongoni mwa watu wa agano la kale na kufananishwa na Yesu Kristo kwa kile alichokifanya kwa ulimwengu.

Tutajifunza somo hili Muhimu kuhusu Maisha ya yusufu kwa Kuzingatia vipengele vine vifuatavyo:-

1.      Maisha ya Yusufu Katika nchi ya kanaani
2.      Maisha ya Yusufu Katika Nchi ya Ugeni kama Mtumwa
3.      Maisha ya Yusufu Katika Nchi ya Ugeni kama Mtawala.

Maisha ya Yusufu Katika Inchi ya Kanaani.

A.     Alichukiwa na Kaka zake
a.      Alifanya kazi za baba yake kwa bidii na uaminifu Mwanzo 37:2
b.      Alitoa ripoti ya kazi zilizofanyanyika kwa baba yake Mwanzo 37:2
Hivi ndivyo vizazi vya Yakobo. Yusufu, aliyekuwa mwenye miaka kumi na saba, alikuwa akichunga kondoo pamoja na ndugu zake; naye alikuwa kijana pamoja na wana wa Bilha, na wana wa Zilpa, wake wa baba yake. Yusufu akamletea baba yao habari zao mbaya”.
c.       Yakobo alikuwa na wana kumi na mbili na binti mmoja, Dina (Mwanzo 29:31;30:24; 35:16-18). Wanawe walikuwa:-
·         Wana wa Lea: Reubeni, Simeoni, Lawi, Yuda, Isakari na Zabuloni
·         Wana wa mjakazi wa Lea (Zilpa): Gadi na Asheri
·         Wana wa Mjakazi wa Raheli (Bilha): Dani na Naftali
·         Wana wa Raheli: Yusufu na Benyamini
d.      Kutokana na uaminifu wake pia mzaliwa wa kwanza wa Raheli mke aliyependwa sana na Yakobo, Baba yake alimpenda sana na kumtengenezea vazi maalumu Mwanzo 37:3-4, Maisha ya Yusufu sio yalimpendeza babaye tu Bali hata Mungu na hivyo Mungu alisema naye kuhusu Maisha yake ya baadaye Mwanzo 37:5-11, Mungu alisema naye kwa Njia ya Ndoto kuhusu kusujudiwa na ndugu zake, yaani kuwa mfalme dhidi yao lakini wao walimchukia upeo.
e.      Yusufu aliuza Misri baada ya kunusurika jaribio la kuuawa Mwanzo 37:12-36
f.        Ruben alitaka kumuokoa lakini Mpango wake ulishindikana Mwanzo 37:21-22
g.   Yuda alitaka kumuokoa nduguye na kifo kwa kutoa wazo auzwe utumwani Mwanzo 37:26-27 na mpango wake ulifanikiwa
Yusufu alimtii baba yake na hakutaka kuwapendeza ndugu zake kwa kufunika maovu yao, Pamoja na Yusufu kufanyiwa mabaya na ndugu zake aliendelea kuwa mwaminifu hata mbali na mzazi wake huko Utumwani Misri.

Maisha ya Yusufu Katika Nchi ya Ugeni kama Mtumwa

A.     Mungu alikuwa pamoja naye
a.      Alinunuliwa kama mtumwa katika nyumba ya Potifa, Mungu alimpa kibali Mwanzo 39:1-6, aliweza kuwa mwenye kuleta faida na Baraka na kuaminiwa
b.      Yusufu alikuwa Mzuri sana “Handsome” kwa sababu hiyo alivutia watu akiwemo mke wa Potifa Mwanzo39:b-20
c.       Mara kwa mara au mara kadhaa mke wa Potifa alimjaribu Yusufu ili alale naye
d.      Lakini Yusufu alikataa kwa sababu alimuheshimu Potifa lakini alimuheshimu Mungu pia Mwanzo 39:8-9
Je wewe kama kijana wa leo unaliweza hili? Leo hii ulimwengu umebadilika wanawake wenye uwezo wa kifedha kama ilivyo kwa potifa wanafuata vijana wadogo wanawashawishi na kutembea nao wanaviita “VIBENTEN” zamani Serengeti Boys, sio rahisi kwa vijana kushinda katika hili, maswala ya mapenzi ni yenye kvutia sana hususani kama mwanamke ndiye anayekutongoza, inawezekana pia haikuwa rahisi kwa Yusufu na ndio maana alikimbia na kuacha vazi lake huko Biblia inasema “Ikimbieni Zinaa” 1Wakoritho 6:18 “Ikimbieni zinaa. Kila dhambi aitendayo mwanadamu ni nje ya mwili wake; ila yeye afanyaye zinaa hutenda dhambi juu ya mwili wake mwenyewe.”
1.      Kutokana na singizio hilo Yusufu aliwekwa Gerezani
2.      Hasira za Potifa ziliwaka juu ya Yusufu.

B.      Maisha ya Yusufu Gerezani.
a.      Mungu aliendelea kuwa Pamoja na Yusufu Mwanzo 39:21-23
b.      Alipata kibali mbele ya mkuu wa Gereza na kuamini wa sana
c.       Alifanikiwa katika kila alilolifanya
d.      Alijihusisha na maisha ya ndani kabisa ya wafungwa wenzake aliwaonea huruma na alijua kusoma nyuso zao ili kujua kuwa wana huzuni, wana furaha na amani au la?, Mungu alimpa karama ya neno la Maarifa na aliitumia kuweza Kufasiri Ndoto
Wakati wote Alimpa Mungu utukufu na hakuchukua utukufu wa Mungu, Tumeumbwa ili tumtukuze Mungu, Mungu na awe kipaumbele chetu cha kwanza katika maisha yetu Mwanzo 40:1-41:36
e.      Yusufu alitafasiri Ndoto za Muokaji na Mnyweshaji gerezani na ndoto zilikuwa za kweli na zilitimia
f.        Mungu ndiye mwenye kutafasiri Ndoto alisema Yusufu Mwanzo 40:8
g.      Alitafasiri Ndoto ya mnyweshaji na kumuomnba amkumbuke Mwanzo 40:20-23
Wanadamu wana uwwezo mkubwa sana wa kuwasahau wenzao, tenda mema bila kutarajia kitu ni Mungu pekee ambaye hataweza kukusahau Isaya 49:15 “Je! Mwanamke aweza kumsahau mtoto wake anyonyaye, hata asimhurumie mwana wa tumbo lake? Naam, hawa waweza kusahau, lakini mimi sitakusahau wewe.” Ni Mungu pekee anayeweza kutufadhili na kutulipia kwa wema wetu wote tunaoufanya yeye fadhili zake zinadumu milele, Mungu hawezi muacha mtu mwenye haki Zaburi 37:25Nalikuwa kijana nami sasa ni mzee, Lakini sijamwona mwenye haki ameachwa Wala mzao wake akiomba chakula.

C.      Mungu anamkumbuka Yusufu.
a.      Mungu alimpa Ndoto Farao Mwanzo 41:1-7
b.      Wenye hekima, waganga, na wachawi  wote wanashindwa kuitafasiri Mwanzo 41:8
c.       Mungu anaweka mazingira ya lazima kwa mnyweshaji kumkumbuka Yusufu Mwanzo 41:9-13,.Wanadamu wasipokuwa waaminifu kwetu Mungu ni Mwaminifu
d.      Yusufu aliitwa kutafasiri Ndoto, alimpa Mungu utukufu Mwanzo 41: 16, 25, 32 Wakati wote Yusufu alitambua kuwa Mungu ndiye mwenye kutenda kila jambo
e.      Yusufu alibadilishwa mavazi yake, huwezi kumkaribia mfalme ukiwa katika hali ya mfungwa Mwanzo 41:14.
f.        Licha ya Kufasiri Ndoto alikuwa na majibu ya tatizo kwa farao Mwanzo 41:33-36
g.      Maisha yalikuwa magumu na yenye uchungu, alikataliwa na nduguze, aliuzwa kama mtumwa, alihukumiwa kifungo kwa uonevu, alisahaulika hata na wale aliowatendea wema, kuna haja gani tena ya kuendelea kuwa mwaminifu katika mazingira kama haya? Lakini Yusufu aliendelea kutenda haki, alijua kuwa Mungu hawezi kumsahau, Wagalatia 6:9 “Tena tusichoke katika kutenda mema; maana tutavuna kwa wakati wake, tusipozimia roho.” Mungu alimpa kibali Farao na hatimaye farao hakuona mtu mwingine sahihi wa kusaidia jamii yake isipokuwa Yusufu. Ndugu usipozimia roho utavuna mema yote unayowatendea watu.

Maisha ya Yusufu Katika Nchi ya Ugeni kama Mtawala.

Mungu si Athumani akiwa na miaka 30 Yusufu anakuwa mtawala wa Misri chini ya farao anainuliwa sana Mwanzo 41:38-46 
a.      Alitawazwa kuwa kuwa mkuu katika nchi yote ya Misri Mwanzo 41:38-40
b.      Aliwekwa juu ya Ncho yote, akavishwa Pete ya Mamlaka Mwanzo 41:41-45
c.       Aliozwa mke Mzuri sana aliyeitwa Asenath
d.      Watu wote walimpigia Magoti, akiwemo Potifa, Mnyeshwaji, Askari wa Magereza na  raia wote
e.      Aliongoza kwa Hekima kubwa sana, alianza kufanya wajibu wake hakulipiza kisasi kwa Mtu
f.        Mungu alimbariki kwa watoto wawili wa Kiume Mwanzo 41:50-52
g.      Yusufu anafanyika Mwokozi sio wa Misri tu na ulimwengu mzima Mwanzo 41:55-57, Kuwa Baraka kwa wengine kunaanzia katika maisha ya uaminifu tangu nyumbani, shuleni, kazini, na hata ugenini Mungu alimbariki kweli kweli.

Kutimia kwa Ndoto ya Yusufu.

Baada ya miaka ipatayo 13 sasa Yusufu alkiwa na miaka 30 anakuwa ameinuliwa sana na Mungu na kuwa mtawala mwenye heshima ya kifalme Misri Mwanzo 41:38-46, Hekima aliyopewa na Mungu inaonekana katika Utendaji wa uongozi wake
a.      Alijua nini cha kufanya wakati wa Miaka ya mavuno Mwanzo 41:47-49
b.      Alijua nini cha kufanya wakati wa Miaka ya njaa Mwanzo 41:53-57, 47:13-26
c.       Aliunganisha maisha yake na Mambo aliyotendewa na Mungu Mwanzo 41:50-52
·         Manase Mungu amenisahaulisha taabu za nyumba ya Baba yangu
·         Efraimu Mungu amenineemesha Katika Nchi ya Ugeni
d.      Ndugu zake wanakuja Misri kwaajili ya kununua Chakula
·         Mwanzo 42:1-13 Yusufu aliwagundua Ndugu zake walipokuja na Kumuinamia na aliikumbuka Ndoto yake yaani ile ahadi ya Mungu aliyoahidiwa kwa Ndoto
·         Yusufu alitaka kuwakumbusha Ndugu zake Tatizo lao na kujua kama wamebadilika Mwanzo 42:14-24
·         Reben alikuwa Tayari kupoteza watoto wake wawili ili waende na Benjamin ambaye Yusufu alimdai waende naye wakati Simeon aliwekwa kizuizini, Mwanzo 42:36-38
·         Yuda naye anaonyesha kuwajibika kwa Maisha ya Ndugu zake Mwanzo 43:1-14
·         Mungu anataka tuwe mbali kabisa na maisha ya ubinafsi, ukomavu wa kweli unakuja pale tunapoonyesha kujali wengine na hata kuwa tayari kuyapoteza maisha yetu kwaajili ya wengine
·         Yuda anaonekana kuwa Tayari kuwajibika pia kwaajili ya Benjamin na kwaajili ya baba yake Mwanzo 44:18-34
·         Yusufu alishindwa kujizuia Mwanzo 45:1-4
·         Alihesabu kuwa kila kilichotokea ilikuwa ni mpango wa Mungu Mwanzo 45:5-15
·         Anawaahidi kuwatunza katika Nchi ya Gosheni Mwanzo 46:16-20,28-34;47:1-12
·         Yusufu alionyesha Moyo wa Msamaha Mwanzo 45:4-8, 50:15-21

Mungu huweza kutumia njia Mbaya kuleta jambo zuri Mwanzo 50:20
Mungu ni mwaminifu katika kutunza ahadi zake Mwanzo 50:24-25

Hitimisho:
Katika maisha ya Yusufu kuna mambo ya msingi ya Kujifunza
a.      Alimwamini Mungu na Kumtegemea
b.      Alijitoa kumtumikia Mungu na Mwanadamu kwa Heshima naUaminifu
c.       Hakukubali kumezwa na Chuki,Usaliti,Kusahaulika alionyesha upendo na hakulipiza kisasi
d.      Alikuwa tayari kuwasamehe wengine
e.      Alikuwa na akili na uwezo wa kujua Mapenzi ya Mungu katika kila alichokuwa anakipitia
f.        Alikuwa mwaminifu tangu ujana wake, na hata alipokuwa mbali na Nyumbani
g.      Alitambua kuwa Israel waterejea katika inchi ya ahadi na kuomba mifupa yake izikwe Israel
h.      Kupitia yeye tunaweza kujifunza namna ya kuwa Kielelezo katika. usemi na mwenendo, na katika upendo na imani na usafi.

Limeandaliwa na Rev. Innocent Kamote
Mkuu wa wajenzi mwenye Hekima.