Luka 4:16-30 “Akaenda Nazareti, hapo alipolelewa; na siku ya sabato
akaingia katika sinagogi kama ilivyokuwa desturi yake, akasimama ili asome.
Akapewa chuo cha nabii Isaya, akakifungua chuo, akatafuta mahali palipoandikwa,
Roho wa Bwana yu juu yangu, Kwa maana amenitia mafuta kuwahubiri maskini habari
njema. Amenituma kuwatangazia wafungwa kufunguliwa kwao, Na vipofu kupata kuona
tena, Kuwaacha huru waliosetwa, Na kutangaza mwaka wa Bwana uliokubaliwa.
Akakifunga chuo, akamrudishia mtumishi, akaketi; na watu wote waliokuwamo
katika sinagogi wakamkazia macho. Akaanza kuwaambia, Leo maandiko haya
yametimia masikioni mwenu. Wakamshuhudia wote, wakiyastaajabia maneno ya neema
yaliyotoka kinywani mwake, wakasema, Huyu siye mwana wa Yusufu? Akawaambia,
Hapana shaka mtaniambia mithali hii, Tabibu, jiponye nafsi yako; mambo yote
tuliyosikia kwamba yametendeka Kapernaumu, yatende na hapa pia katika nchi yako
mwenyewe. Akasema, Amin, nawaambia ya kwamba, Hakuna nabii mwenye kukubaliwa
katika nchi yake mwenyewe. Lakini, kwa hakika nawaambia, Palikuwa na wajane
wengi katika nchi ya Israeli zamani za Eliya, wakati mbingu zilipofungwa miaka
mitatu na miezi sita, njaa kuu ikaingia nchi nzima; wala Eliya hakutumwa kwa
mmojawapo, ila kwa mjane mmoja wa Sarepta katika nchi ya Sidoni. Tena, palikuwa
na wenye ukoma wengi katika Israeli zamani za nabii Elisha, wala hapana
aliyetakaswa ila Naamani, mtu wa Shamu.Wakajaa ghadhabu wote waliokuwa katika
sinagogi walipoyasikia hayo. Wakaondoka wakamtoa nje ya mji, wakampeleka mpaka
ukingo wa kilima ambacho mji wao umejengwa juu yake, wapate kumtupa chini;
lakini yeye ALIPITA KATIKATI yao, akaenda zake.”
Utangulizi:
Moja ya maswala ya kushangaza
sana ambayo huwa tunayasoma katika maandiko na kisha yakatuacha aidha
hatujaelewa, au yakatushangaza sana ni pamoja na muujiza huu, wa Yesu kupita
kati kati ya waliokuwa wamejaa ghadhabu
na wamepania kummaliza, lakini wakashangaa kuwa ametoweka katika mazingira ya
kutatanisha!
Hii sio mara ya kwanza tunasoma katika maandiko ya kwamba Yesu
amewahi kuwepo au kupita kati kati ya watu tena watu waliojaa ghadhabu na hasira ili
wamdhibiti na kumwangamiza na bado yeye
akapita kati kati yao bila wao kutambua na kwenda zake waandishi wengi wa injili
wanapata taabu namna ya kuelezea tukio hili na hivyo kuwafanya wasomaji wao
kushindwa kuelewa au kupata kile kilichofanyika ona
Yohana
8:48-59 “Wayahudi
wakajibu, wakamwambia, Je! Sisi hatusemi vema ya kwamba wewe u Msamaria, nawe
una pepo? Yesu akajibu, Mimi sina pepo;
lakini mimi namheshimu Baba yangu, na ninyi mwanivunjia heshima yangu. Wala
mimi siutafuti utukufu wangu; yuko mwenye kutafuta na kuhukumu. Amin, amin,
nawaambia, Mtu akilishika neno langu, hataona mauti milele. Basi Wayahudi
wakamwambia, Sasa tumeng'amua ya kuwa una pepo. Ibrahimu amekufa, na manabii
wamekufa; nawe wasema, Mtu akilishika neno langu, hataonja mauti milele. Wewe u
mkuu kuliko baba yetu Ibrahimu, ambaye amekufa? Nao manabii wamekufa. Wajifanya
u nani? Yesu akajibu, Nikijitukuza mwenyewe, utukufu wangu si kitu; anitukuzaye
ni Baba yangu, ambaye ninyi mwanena kuwa ni Mungu wenu. Wala ninyi hamkumjua;
lakini mimi namjua. Nikisema ya kwamba simjui, nitakuwa mwongo kama ninyi;
lakini namjua, na neno lake nalishika. Ibrahimu, baba yenu, alishangilia kwa
vile atakavyoiona siku yangu; naye akaiona, akafurahi. Basi Wayahudi wakamwambia,
Wewe hujapata bado miaka hamsini, nawe umemwona Ibrahimu? Yesu akawaambia,
Amin, amin, nawaambia, Yeye Ibrahimu asijakuwako, mimi niko. Basi wakaokota
mawe ili wamtupie; lakini Yesu AKAJIFICHA, akatoka hekaluni.”
Ni muhimu kufahamu kuwa Biblia ya
kiingereza ya King James katika maandiko au maneno AKAPITA KATI KATI YAO AKAENDA ZAKE yanasomeka katika Luka 4:30 “But HE PASSING THROUGH THE MIDST OF THEM and
went his way” na Katika hali kama hiyo tena Yohana 8:59 andiko lile LAKINI YESU AKAJIFICHA, linasomeka kwa
kiingereza “then
took they up stones to cast him, BUT JESUS HID HIMSELF and went out of the
temple, GOING THROUGH OF THEM and so passed by” Yohana 10:39 “Wakatafuta tena kumkamata;
lakini akatoka mikononi mwao.” Kumkamata Yesu halikuwa jambo rahisi
kama watu wengi wanavyoweza kudhani, Hapa huu ulikuwa ni muujiza wa wazi, aidha
kwa mujibu wa wanatheolojia wengi, walipigwa upofu, au walipigwa gazi, au Yesu
alitoweka kwa jinsi ya muujiza biblia ya kiyunani inatumia maneno haya “DIELTHON DIA MESOU EPOREUETO” kwa kiingereza “But Passing through their
midst he went his way” kwa hiyo neno EPOREUETO ambalo kiingereza klinasomeka “WENT HIS WAY” pia linasomeka kama “TRAVERSE”
ambalo tafasiri yake inaweza kusomeka kama KUTOKOMEA, kama vile kitu kinapopotelea mwisho wa mto, au ndege
inapopaa na ikapotelea angani, au meli inavyosafiri na kutokomea nje ya upeo wa
macho ya kibinadamu kwa hiyo ukiangalia kwa undani sana swala hili utaweza
kuona “HE BECAME INVISIBLE” yaani
alitoweka na kuendelea na shughuli zake sehemu nyingine, kwa kukosa neno zuri
la kuelezea ndio Yiohana anatumia neno kujificha au kutoweka mikononi mwao na Luka
anaelezea vema kupita katikati yao na kwenda zake!
Katika maandiko hayo ya msingi
utaweza kujiuliza maswali mengi kwamba ilikuwaje kuwaje Yesu, akapita kati ya
watu waliokuwa wamekusudia kumdhuru, na kumuumiza, au inawezekanaje mtu ambaye
watu wote wanamuangalia anajificha kama biblia ya Kiswahili ilivyotumia neno
hilo kwenye injili ya Yohana na watu walikuwa wamekusudia kumkamata na kumtupa
nje ya kilima wakiwa wamejaa ghadhabu?, watu wenye nguvu na ambao tayari
walikuwa wamekwisha muweka mikononi mwao, ukweli ni kuwa kulikuwa na nguvu ya
ziada na ya kiungu ya kupita kawaida ambayo wakati mwingine iliwafanya maadui
wasimuone, yaani walipigwa upofu na kufanywa wasimtambue na hili lilikuwa ni
jambo la kawaida kuweza kufanyika mfano,
angalia watu hawa:-
Luka 24:13-16 “Na tazama, siku ile ile watu wawili miongoni mwao
walikuwa wakienda kijiji kimoja, jina lake Emau, kilichokuwa mbali na
Yerusalemu kama mwendo wa saa mbili. Nao walikuwa wakizungumza wao kwa wao
habari za mambo hayo yote yaliyotukia. Ikawa katika kuzungumza na kuulizana
kwao, Yesu mwenyewe alikaribia, akaandamana nao. Macho yao yakafumbwa
wasimtambue.”
Mungu katika mpango wake anazo
njia zake za kuwaficha wapendwa wake ili wasidhurike na hatari ya aina yoyote
ile, Ndio maana tunapokuwa na Mungu hatupaswi kuogopa jambo lolote lile,
hatupaswi kuogopa wingi wa majeshi ya maadui, wala mipango mikakati ya adui zetu
kutuangamiza na kututupilia mbali, tunapaswa, tu kufahamu kuwa kuna wakati
Mungu yu aweza kuwapiga upofu maadui zetu na wasituone na kuwa tunaweza kupita
katikati yao na kuendelea na shughuli zetu bila madhara, Mungu ameahidi kutuokoa
na mitego yote ya adui ona Zaburi
124:6-7 “Na ahimidiwe Bwana; Asiyetutoa kuwa
mawindo kwa meno yao. Nafsi yetu imeokoka kama ndege Katika mtego wa wawindaji,
Mtego umevunjika, nasi tumeokoka” Mungu ameahidi kutuokoa kama nudge
anavyonusurika katika mitego ya adui, Jambo alilolifanya Yesu Kristo ni jambo
la kawaida sana lililoweza kufanywa na manabii hata katika agano la kale,
Wakati wa nabii Elisha yeye alitafutwa na jeshi kubwa sana la nchi ya shamu, na
walikwenda maalumu kwaajili ya kumtafuta Elisha, na Elisha alizungumza nao
vizuri tu na kuwalisha kisha akwaacha
waende zao ona
2Wafalme 6:8-23 “Basi, mfalme wa Shamu
alikuwa akifanya vita na Israeli. Akafanya mashauri na watumishi wake, akasema,
Kituo changu kitakuwapo mahali fulani. Yule mtu wa Mungu akapeleka habari kwa
mfalme wa Israeli, kusema, Jihadhari, usipite mahali fulani; kwa sababu ndiko
wanakoshukia Washami. Mfalme wa Israeli akapeleka watu mpaka mahali pale
alipoambiwa na yule mtu wa Mungu, na kuhadharishwa; akajiokoa nafsi yake, si mara
moja, wala si mara mbili. Basi mfalme wa Shamu moyo wake ukamfadhaika sana kwa
ajili ya jambo hili; akawaita watumishi wake, akawaambia, Je! Hamtanionyesha,
ni mtu yupi miongoni mwenu aliye upande wa mfalme wa Israeli? Mmojawapo wa
watumishi wake akasema, La, bwana wangu, mfalme; lakini Elisha, yule nabii
aliye katika Israeli, humwambia mfalme wa Israeli maneno uyanenayo katika
chumba chako cha kulala. Akasema, Enendeni, mkamwangalie aliko, nipate kupeleka
watu kwenda kumchukua. Akaambiwa ya kwamba, Tazama, yuko Dothani. Kwa hiyo
akapeleka huko farasi, na magari, na jeshi kubwa; wakafika usiku, wakauzingira
mji ule pande zote. Hata asubuhi na mapema mtumishi wake yule mtu wa Mungu
alipoondoka, na kwenda nje, kumbe! Pana jeshi la watu, na farasi na magari,
wameuzingira mji ule. Mtumishi wake akamwambia, Ole wetu! Bwana wangu,
tufanyeje? Akamjibu, Usiogope; maana walio pamoja nasi ni wengi kuliko wale
walio pamoja nao. Elisha akaomba, akasema, Ee Bwana, nakusihi, mfumbue macho
yake, apate kuona. Bwana akamfumbua macho yule mtumishi; naye akaona; na
tazama, kile kilima kilikuwa kimejaa farasi na magari ya moto yaliyomzunguka
Elisha pande zote. Na walipomtelemkia Elisha akamwomba Bwana, akasema, Uwapige,
nakusihi, watu hawa kwa upofu. Akawapiga kwa upofu sawasawa na neno la Elisha.
Elisha akawaambia, Njia hii siyo, na mji huu sio, nifuateni mimi, nami
nitawapeleka kwa mtu yule mnayemtafuta. Akawapeleka Samaria. Hata walipokwisha
kuingia Samaria, Elisha akasema, Bwana wafumbue macho watu hawa, wapate kuona.
Bwana akawafumbua macho wakaona; kumbe! Walikuwa katikati ya Samaria. Naye
mfalme wa Israeli alipowaona, akamwambia Elisha, Ee baba yangu, niwapige?
Niwapige? Akamjibu, Usiwapige; je! Ungetaka kuwapiga watu ambao umewatwaa
mateka kwa upanga wako na uta wako? Weka chakula na maji mbele yao, wapate kula
na kunywa, na kwenda kwa bwana wao. Basi akawaandalia chakula tele; nao
walipokwisha kula na kunywa, akawaacha, wakaenda zao kwa bwana wao. Na vikosi
vya Shamu havikuja tena katika nchi ya Israeli”
Haijalishi kuwa leo mpendwa
unapitia katika hali ya namna gani, inawezekana umebanwa kila upande,
umezingirwa, na hali tata ambazo hujui utapenya vipi, kila kilicho kibaya
kinakuandama na kukutafuta, adui wamejipanga kwamba wanakuharibia lakini leo
nataka nikutie Moyo, ya kuwa upo muujiza wa kupita kati kati yao na kuenda zako,
kwa amani, Muujiza huu unatuthibitishia ya kuwa adui hatatuona; Lakini sisi
tutamuona na kuamua wapi pa kumpeleka na au wapi pa kupita, adui atadhani kuwa
hatutaiona njia lakini Muuijza huu unatufundisha ya kuwa iko njia hata katikati
ya kibano, ambacho kwa akili zako unaweza kudhani ya kuwa hutapenya lakini kwa
neema ya Mungu utapenya, wiki hii kidato cha nne watakuwa na mitihani ya
kitaifa na wengi wanaweza kuwa wanaogopa kwamba itakuwaje au wanafikiri
itakuwaje hata wazazi wanaogopa na walimu vilevile tunawaza itakuwaje hofu
inatufunika kana kwamba ule mtihani tunakwenda kufanya sisi, tunawaza
tunavukaje? na pengine ibilisi amekusudia kukukwamisha na kukutupilia mbali ili
kwamba historia yako isiwepo tena lakini nataka kukuthibitishia ya kuwa bwana
anakusudia kukupitisha katikati ya mtihani huu wa kitaifa na uende zako
Hekaluni ukamtukuze Mungu, hatupaswi kuogopa kwa sababu Mungu ana njia nyingi”
atakusaidia. Na nafsi yako itaokoka katika mikono ya adui zako kwa namna ya
kushangaza!
Isaya 43:1-2 “Lakini sasa, Bwana
aliyekuhuluku, Ee Yakobo, yeye aliyekuumba, Ee Israeli, asema hivi, Usiogope,
maana nimekukomboa; nimekuita kwa jina lako, wewe u wangu. Upitapo katika maji
mengi nitakuwa pamoja nawe; na katika mito, haitakugharikisha; uendapo katika
moto, hutateketea; wala mwali wa moto hautakuunguza.”
Na Rev. Innocent Kamote.
Mkuu wa wajenzi mwenye hekima!