2Samuel
11:1-4 “Hata ikawa, mwanzo wa mwaka mpya, wakati
watokapo wafalme kwenda vitani, Daudi akampeleka Yoabu, na watumishi wake
pamoja naye, na Israeli wote; wakawaangamiza wana wa Amoni, wakauhusuru Raba.
Lakini Daudi mwenyewe akakaa Yerusalemu. Ikawa wakati wa jioni, Daudi akaondoka
kitandani, akatembea juu ya dari ya jumba la mfalme; na alipokuwa juu ya dari
aliona mwanamke anaoga; naye huyo mwanamke alikuwa mzuri sana, wa kupendeza
macho. Naye Daudi akapeleka, akauliza habari za yule mwanamke. Mtu mmoja
akasema, Je! Huyu siye Bath-sheba, binti Eliamu, mkewe Uria, Mhiti? Basi Daudi
akapeleka wajumbe, akamtwaa; naye akaingia kwake; naye akalala naye; (maana
yule mwanamke amekwisha kutakasika unajisi wake); kisha akarudi nyumbani kwake.”
Utangulizi:
Ni muhimu kufahamu kuwa kifungu hiki
cha maandiko kina jambo kubwa la msingi la kutufundisha ambalo mwandishi wa
kifungu hiki alikuwa anakusudia kukileta kwetu! Wengi wetu tunafahamu sana
habari ya anguko la Daudi katika zinaa, na tunafahamu madhara makubwa
yaliyompata kutokana na dhambi hii, lakini vilevile tunaweza kukubaliana wazi
kuwa Daudi alikuwa na udhaifu sawa na ule walionao wanaume wengine, kwamba
aliona mwanamke mzuri anaoga akamtamani, na kuzini naye na wengi wameweza
kumalumu Daudi kwa sababu mbalimbali hata ikiwa ni pamoja na kujenga Ghorofa
lenye dari ya kutembelea na kusababisha kuona mke wa jirani yake ambaye alikuwa
anaoga, tunaweza kuwa na sababu lukuki kuhusu anguko la Mfalme Daudi na sababu
hizo zikawa na mashiko kadhaa, Lakini mwandishi wa kifungu hiki ana sababu
mojawapo ya muhimu zaidi ambayo kimsingi ndio nataka tuiangalie kwa kina katika
siku kama hii ya leo!
Ikawa
Mwanzo wa Mwaka mpya!
Mwandishi anaanza kwa kueleza Habari
ya anguko la Daudi akiwa na sababu nyingine tofauti mno Ikawa Mwanzo wa Mwaka
Mpya! Wakati watokapo wafalme kwenda vitani!
Majira ya nchi katika mashariki ya kati yanafanana sana kwa kiwango
kikubwa na majira ya Afrika ya mashariki, Mwezi wa Januari na February Mpaka
March ndio miezi ambayo tunaweza kuyaita majira ya Mwanzo wa mwaka kunakuwa na
Joto kali na ukavu wa aina Fulani, katika majira haya kwa wana wa Israel
huangukia kati ya mwezi wa Abibu au
mwezi (Nisani) katika majira haya
ardhi huwa kame na kavu, na hivyo ndio majira ambayo wafalme wengi waliyatumia
kuingia vitani kwa kusudi la kupanua mipaka ya mataifa yao, kuteka nyara,
kulipisha kodi wale utakaowashinda au kulinda mipaka yako, wakati huu ulikuwa
ni wakati muafaka kwa vita kwa sababu ardhi ilikuwa kavu, na hivyo iliweza kurahisisha
vita vya miguu, magari ya kukokotwa na farasi lakini pia kusafirisha silaha na
wanajeshi kwa urahisi zaidi kuliko wakati wa baridi na wakati wa mvua ambapo
ardhi huwa na matope na vita vinakuwa ni ngumu, wakati huu pia ilikuwa ni rahisi kuteka nyara
vitu na kuvibeba kwa hiyo ilikuwa ni desturi ya Wafalme kutoka kwenda kupigana
vita mwanzoni mwa mwaka mpya, Hata Mungu aliwaokoa wana wa Israel kutoka Misri
katika majira kama haya.
Kutoka
12;1-2”BWANA akanena na Musa na Haruni katika nchi
ya Misri, akawaambia, Mwezi huu utakuwa mwanzo wa miezi kwenu; utakuwa ni mwezi
wa kwanza wa mwaka kwenu”.
Kwa hiyo wataalamu wa nyakati waliweza
kuuelewa vema kuwa ulikuwa ni wakati gani na wanapaswa kufanya nini, Mwandishi anataka kutuonyesha kuwa
Sababu zilizopelekea Daudi kufanya dhambi au kuanguka dhambini ilikuwa ni pamoja na:-
1. Aliudharau wakati – kumbe
ilikuwa wazi kabisa na ilikuwa inajulikana kabisa kwamba Mwanzo wa mwaka mpya
ni lazima wafalme watoke kwenda kupigana vita, Lakini yeye aliupuuzia wakati Moja ya tatizo kubwa linaloweza kumleta
mwanadamu katika anguko la maisha yake ni kutokujua kuutumia wakati, kuna
madhara mengi na majuti makubwa sana kwa kila mwanadamu ambaye hakujua kuutumia
wakati, wakati tuliopewa duniani ni mfupi sana na unaenda haraka mno, wastaafu
wengi wanajua leo kwa sababu hawakujua kuutumia wakati, vijana wengi wanafikiri
wataendelea kuwa vijana tu, wasichana wengi wanadhani wataendelea kuwa
wasichana tu, wanafunzi wengi sana wanadhani iko siku watakaa ajipange na
kusoma kwa bidii na sasa wengi wanalala na kupoteza muda wakifikiri uko wakati,
Hakuna jambo linaumiza sana kama kuja kugundua baadaye kuwa sikuutumia wakati,
nilikuwa wapi mimi? Hakuna jambo linaumiza kama kupotezewa wakati! Kila mmoja wetu anapaswa kufahamu kuwa wakati
usipoutumia vema anguko lake ni kubwa na
lenye kuleta madhara makubwa sana duniani, kwa hiyo ni vema kuutumia wakati na
kutokuupuuza Yesu alilalamika kwa njia ya kinabii kwa mji wa Yerusalem kwamba
utabomolewa na kuharibiwa vibaya sana na Majeshi ya warumi tukio ambalo
lilitimizwa mwaka wa 70 baada ya Kristo lakini malalamiko ya Yesu kwa Yerusalem
ni kwa sababu tu ya kutokuujua majira na wakati hususani Mwokozi wa ulimwengu
alipowatembelea.
Luka 19:41-44 “Alipofika
karibu aliuona mji, akaulilia, akisema, Laiti ungalijua, hata wewe katika siku
hii, yapasayo amani! Lakini sasa yamefichwa machoni pako. Kwa kuwa siku
zitakuja, adui zako watakapokujengea boma, likuzunguke; watakuzingira na
kukuhusuru pande zote; watakuangusha chini wewe na watoto wako ndani yako,
wasikuachie jiwe juu ya jiwe, kwa sababu hukutambua majira ya kujiliwa kwako.”
Daudi
alifahamu wazi kuwa ulikuwa ni wakati wa wafalme kwenda vitani lakini yeye
hakwenda vitani, alibaki anarandaranda mjini tu na hiki ndio moja ya sababu
ambayo mwandishi anaiona kuwa Daud alikosea!
2. Aliudharau wajibu - Kupigania watu ulikuwa ni moja ya
wajibu wa waamuzi na wafalme Daudi alikuwa anawajibika kabisa kwenda vitani,
huu ulikuwa ni wajibu wake na wajibu wa wafalme wa mataifa yote, ndio kuna
wakati unaweza kumtuma mtu aende, Lakini mwandishi anaonyesha kuwa tatizo hapa
lililopelekea habari kuwa nyingine kwa Mfalme Daudi ni kutokwenda vitani yeye
alimtuma Yoabu aende, wakati
mwingine ili Mungu aweze kuleta ukombozi kwa jamii ni lazima waweko watu
watakaokubali kubeba wajibu, kama kila mmoja wetu akibeba wajibu wake kwa
ufanisi tutaweza kuona mwanga
Luka 1:38 “Mariamu
akasema, Tazama, mimi ni mjakazi wa Bwana; na iwe kwangu kama ulivyosema. Kisha
malaika akaondoka akaenda zake.”
Mariam
alikubali kuubeba wajibu wa kumzaa Yesu na akaleta faida Kubwa sana Duniani,
walimu wakifanya wajibu wao, wanafunzi wakifanya wajibu wao, wanasiasa
wakifanya wajibu wao na wananchi wakifanya
wajibu wao hakuna kitakachoshindikana, mke naye afanye wajibu wake na mume naye
afanya wajibu wake kila mmoja atimize wajibu, wake kila mmoja akitimiza wajibu
wake hakuna changamoto itakayojitokeza popote, Daudi alikwepa wajibu, na
kudharau muda na majira aliyotakiwa kwenda vitani na matokeo yake alipatwa na
anguko la kihistoria, hatuwezi kumlaumu yeye kwa sababu zozote zile kwani kuna
kitu cha kujifunza kutoka kwake lakini mwandishi anatuonyesha kuwa moja ya
sababu ya anguko lake ni kudharau wajibu, inapotokea kuwa shetani akatutia
katika kishawishi cha kutokuzingatia kutimiza wajibu tunaweza kujikuta
tunajutia maisha yetu yote na kusema laiti ningelijua kwa msingi huo ni muhimu
kwetu tukatimiza wajibu, najua ziko ndoa nyingi sana zinapitia kwenye changamoto
ambazo kimsingi ni kwa sababu tu watu hawataki kutimiza wajibu wao, kila mmoja
akimfanyia mwenziwake kile ambacho maandiko yameagiza basi, katika jamii yetu
kama kila mmoja wetu atatimiza wajibu kamwe haitakuja tuone madhara na majuto
baadaye timiza wajibu.
3.
Kupenda
rahisi/au uvivu – kupenda rahisi au uvivu kuna madhara makubwa
sana katika maisha yetu tunaambiwa kuwa Daudi alikaa tu ona “Lakini Daudi mwenyewe akakaa Yerusalemu.”Maana
yake alikaa tu hakufanya kazi, Daudi aliingiwa na uvivu, mtu akikaa tu bila
jambo la Muhimu la kufanya, kinachofuata sasa ni kumpa ibilisi nafasi, “Idlenes gives great adavantage to the
temper “ Neno la Mungu linapingana
vikali sana na swala zima la la uvivu, na wakati wote neno la Mungu linatutaka
kupingana na tatizo la uvuvi na linawataka watu wafanye kazi likiwa na mifano
mingi sana na maelekezo mengi sana mfano
Mithali 6:6-11 “Ewe
mvivu, mwendee chungu, Zitafakari njia zake ukapate hekima. Kwa maana yeye hana
akida, Wala msimamizi, wala mkuu, Lakini hujiwekea akiba ya chakula wakati wa
jua; Hukusanya chakula chake wakati wa mavuno. Ewe mvivu, utalala hata lini?
Utaondoka lini katika usingizi wako? Bado kulala kidogo, kusinzia kidogo, Bado
kukunja mikono upate usingizi! Hivyo umaskini wako huja kama mnyang'anyi, Na
uhitaji wako kama mtu mwenye silaha.”
Biblia ina la kusema kuhusu uvivu. Kitabu cha Mithali imejawa
na hekima kuhusu uvivu na onyo kwa mtu mvivu. Mithali inatuambia kwamba mtu
mvivu anachukia kazi:
Mithali 21:25 "Matakwa yake
mtu mvivu humfisha, kwa maana mikono yake hukataa kufanya kazi."
Mithali
26:13-14 “Mtu mvivu husema, Simba yuko njiani, Simba yuko katika njia
kuu. Kama vile mlango ugeukavyo katika bawaba zake; Kadhalika mtu mvivu katika
kitanda chake.“
Mithali 18:9 Yeye naye aliye mvivu katika kazi yake, Ni ndugu yake aliye
mharabu. Newton's first law states that, “if a body is at rest or moving at a
constant speed in a straight line, it will remain at rest or keep moving in a
straight line at constant speed unless it is acted upon by a force”.
Mwandishi anaonyesha kuwa taabu nyingine ambayo Daudi ilimpelekea kuingia
katika hali hii nzito ya anguko ni kukaa tu bila kufanya shughuli 2 Wathesalonike 3:10 “Kwa kuwa hata wakati ule tulipokuwapo
kwenu tuliwaagiza neno hili, kwamba ikiwa mtu hataki kufanya kazi, basi, asile
chakula”. Kila mmoja wetu anapaswa kuhakikisha kuwa hatumpi ibilisi
nafasi, kila mmoja ahakikishe kuwa anaukomboa wakati na hapotezi muda, muda sio
wa kuchezea muda ni mali, lakini wakati huo huo kila mmoja atimize wajibu wake
na mwisho tuhakikishe kuwa tunapiga vita uvizu, maswala haya yalipodharauliwa
na daudi yalileta anguko kwake ashukuriwe Mungu yeye alianguka katika zinaa
lakini anguko baya kuliko yote ni kushindwa maisha hili linaleta majuto makubwa
na machungu sana Duniani kuliko naguko la iana nyinguine lolote tunaweza
kujiokoa kwa kujituma kwa bidii kwa kutumia nafasi na vipawa tulivyopewa na
Mungu na kukamilisha kusudi la Mungu alilolikusudia kwetu Duniani, Neema ya
Mungu na ikufunike ikiwa unataka kuishi kama Mfalme katika wakati ujao ni vema
ukiyazingatia hayo!
Rev. Innocent
Samuel Kamote.
Mkuu wa wajenzi
mwenye Hekima!