Esta 4:13-14 “Naye Mordekai akawaagiza wampelekee Esta jibu la kusema, Wewe usijidhanie kuwa wewe utaokoka nyumbani mwa mfalme, zaidi ya Wayahudi wote. Kwa maana wewe ukinyamaza kabisa wakati huu, ndipo kutakapowatokea Wayahudi msaada na wokovu kwa njia nyingine; ila wewe utaangamia pamoja na mlango wote wa baba yako; walakini ni nani ajuaye kama wewe hukuujia ufalme kwa ajili ya wakati kama huo?”
Utangulizi.
Katika Historia ya Dunia moja ya
watu au jamii au kabila au taifa la watu waliopitia katika mateso na
mashambulizi makali sana duniani ni Wayahudi, Wayahudi wamekuwa watu wa
kuchukiwa kila mahali Duniani, Mifumo yote ya kishetani duniani, imepangwa na
kukusudia kuharibu kabisa mpango wa Mungu kupitia taifa hilo kuanzia na mpango
wa ukombozi wa wanadamu ambao ulikuja pia kupitia Yesu Ktisto kupitia taifa
hilo, lakini sio hivyo tu hata mpango wa Mungu wa baadaye.
Katika maisha yetu vilevile wako
watu wengine ambao Mungu ana mpango na makusudi makubwa na maisha yao kwaajili
ya kuwahudumia watu wengine! Lakini hata hivyo wamekutana na mashambulizi
makali sana kutoka kwa watu mbalimbali kwaajili ya kupambana na maisha yao, na
kusudi lile ambalo Mungu ameliweka ndani yao, kokote kule waliko wanachukiwa na
kupigwa vita nani tamaa ya shetani na maajenti wake kuona watu hao
wanaharibikiwa wanakwenda mbali na nyuso zao na hata kuwaua, Mwalimu alisema
kwamba sote tutachukiwa kwaajili ya jina lake.
Yohana 16:1-3 “Maneno hayo nimewaambia,
msije mkachukizwa. Watawatenga na masinagogi; naam, saa yaja atakapodhania kila
mtu awauaye ya kuwa anamtolea Mungu ibada. Na hayo watawatenda kwa sababu
hawakumjua Baba wala mimi.”
Kama ilivyo kwa wayahudi na
wanafunzi wa Yesu Kristo watachukiwa vilevile, na mtu mmoja mmoja kwa kadiri
unavyompenda Mungu utachukiwa na wakati mwingine hata na wakristo wenzako, na
au hata watumishi wenzako na wakati mwingine hata watu waliokuzidi kila kitu
wanaweza kuchukizwa nawe kumbuka maneno ya Paulo mtume “Ndugu za uongo” hawa
watakuchukia na kukuonea wivu na kukutengenezea zengwe ili yamkini uharibikiwe
na kuangamizwa nah ii ndio furaha yao au kwa ujinga wakidhani wanafanya mapenzi
ya Mungu, katika mazingira kama hayo bado tunapaswa kukumbuka kuwa Mungu yupo
naye ndiye tumaini letu na tegemeo letu na ya kuwa ataleta msaada na wokovu kwa
njia nyingine hata nje ya zile tunazozitegemea!
Ni ahadi ya Mungu ya kuwa njia
moja ikifungwa atafungua na njia nyingine
1Wakoritho 10:13 “Jaribu halikuwapata
ninyi, isipokuwa lililo kawaida ya wanadamu; ila Mungu ni mwaminifu; ambaye
hatawaacha mjaribiwe kupita mwezavyo; lakini pamoja na lile jaribu atafanya na
mlango wa kutokea, ili mweze kustahimili.”
Kuujia Ufalme kwa wakati.
Kitabu cha Esta kiliandikwa kwa
makusudi ya kuwafundisha wayahudi sababu ya kuwepo kwa sikukuu ya Purim,
Neno hilo Purim ni neno la Kiibrania ambalo kwa kiingereza ni “LOTS” kwa Kiswahili ni Kura au Muswada,
ni sikukuu ya wayahudi kukumbuka au kufurahia ukombozi uliotokea karne tano
hivi kabla ya Kristo kwa wayahudi wachache waliokuwa wakikaa huko uajemi ambao
walipitishiwa Mswada na ukapigiwa kura kwamba watu wa kabila hilo wauawe, ni
kutokana na wokovu mkubwa walioupata ndipo Mordekai akaamuru waikumbuke siku
hiyo na kuiadhimisha kokote waliko
Esta 9:20-26 “Basi Mordekai aliyaandika
mambo hayo; naye akapeleka barua kwa Wayahudi wote waliokaa katika majimbo yote
ya mfalme Ahasuero, waliokuwa karibu na waliokuwa mbali, kuwaonya wazishike
siku ya kumi na nne ya mwezi wa Adari, na siku ya kumi na tano yake, mwaka kwa
mwaka, ambazo ni siku Wayahudi walipojipatia raha mbele ya adui zao, na mwezi
uliogeuzwa kwao kuwa furaha badala ya huzuni, na kuwa sikukuu badala ya kilio;
wazifanye siku hizo ziwe za karamu na furaha, za kupeana zawadi na za kuwapa
maskini vipawa. Nao Wayahudi wakakubali kufanya kama walivyoanza, na kama
Mordekai alivyowaandikia; kwa sababu Hamani bin Hamedatha, Mwagagi, adui ya
Wayahudi wote, alikuwa amefanya shauri juu ya Wayahudi ili kuwaangamiza,
akapiga Puri, yaani kura, ili kuwakomesha na kuwaangamiza pia; bali mfalme
alipoarifiwa, aliamuru kwa barua ya kwamba hilo shauri baya alilolifanya juu ya
Wayahudi limrudie kichwani pake mwenyewe; na ya kwamba yeye na wanawe
watundikwe juu ya mti. Hivyo wakaziita siku hizo Purimu, kwa jina la Puri.
Basi, kwa ajili ya maneno yote ya barua hiyo, na kwa yale waliyoyaona wenyewe
juu ya jambo hilo, na mambo yenyewe yaliyowajia”,
Katika wakati wa tukio hilo la
ukombozi Mungu alikuwa ameinua binti wa kiyahudi akliyeitwa Esta kuwa malikia
wa uajemi baada ya kuolewa na aliyekuwa mfalme kwa wakati huo, Mordekai mjomba
wake alikuja kumtumia binti huyu kuwa sababu ya wokovu mkubwa wa wayahudi
alipokuwa madarakani, kuingia kwake madarakani ulikuwa ni mpango wa Mungu ili
kwamba aweze kuja kuwa msaada katika wakati mgumu wa saa ya kujaribiwa kwa
Israel nani kupitia yeye kweli Mungu alileta wokovu mkubwa, baada ya Mjomba
wake Mordekai kumfunulia mpango mbaya uliokuwa umepitishwa wa kuwaabngamiza
wayahudi! Esta alikuwa tayari kuyatoa maisha yake kwaajili ya Ndugu zake kwani
ilikuwa ni desturi ngumu kuwa kumuendea mfalme bila kibali chake hata kama wewe
ni malikia kungekugharimi kifo isipokuwa kama mfalme atakunyooshea fimbo ya
dhahabu
Esta 4:15-16 “Basi Esta akawatuma ili
wamjibu Mordekai,Uende ukawakusanye Wayahudi wote waliopo hapa Shushani,
mkafunge kwa ajili yangu; msile wala kunywa muda wa siku tatu, usiku wala
mchana, nami na wajakazi wangu tutafunga vile vile; kisha nitaingia kwa mfalme,
kinyume cha sheria; nami nikiangamia, na niangamie”
Kwa nini Esta alikubali kujitoa
muhanga kwaajili ya watu wake ni baada ya Mordekai kumjulisha kuwa emekuwepo
madarakani katika ufalme ule huenda kwa mpango wa Mungu ili awaletee watu wake
wokovu, jambo ambalo pia lilimpa heshima kubwa mwanamke huyu!
Ni muhimu kufahamu kuwa wako watu
ambao wakiingia madarakani wanaweza kugeuka na kuwa Baraka kubwa sana kwa jamii
na watu, na wako watu ambao wakiingia madarakani wanaweza kuwa sababu ya
majutio makubwa sana kwa wengine, ashukuriwe Mungu kuwa esta alikubali kuwa
Baraka kwa wengine, lakini wako viongozi ambao wewe na mimi tutaweza kuendelea
kuwakumbuka katika maisha yetu katika mazingira yoyote yale iwe serikalini, au
kwenye makanisa yetu, au idara zetu, au kazini kwako au kwenye biashara yako au
bosi wako, kwamba wao walipoingia madarakani aidha walikuwa Baraka kubwa sana
kwako kiasi ukashukuru na kusema wameujia ufalme kwa wakati, lakini wako
viongozi wengine ndio wamekuja wakiwa hawajui kusudi la Mungu ndani yako na
wote ni kama wakichukua mazoezi ya kufukuza wanataka kukufukuza wewe, wakitaka
kuchukua mazoezi ya umbeya wanakufanyia wewe, wewe ndio unakuwa adui mkubwa
wewe ndio unakuwa sababu ya vurugu na vujo na kupitishwa kwa miswada mibaya na
mipango mibaya na vita za kila aina hwa ni watu wasiojua kwanini wameujia
ufalme na wanadani wameujia ufalme ili wakutoe sadaka wewe wakidhani ya kuwa
watajipatia heshima kumbuka Mordekai alimuonya Esta kuwa kama wewe hutatambua
wajibu wako wakati huu ndipo utakapowajia wayahudi Msaada na wokovu kwa njia
nyingine na wewe na mlango wa baba yako utaangamia, ninawatangazia wote ambao
Mungu aliwaweka madarakani ili wawe Baraka kwako na kwangu ya kuwa kama hawajui
ni kwa nini wameujia ufalme kwa wakati huu kuwa Mungu atatuletea Msaada na wokovu
kwa njia nyingine nao wataabika
katika jina la Yesu!
Msaada na wokovu kwa
njia nyingine!
Ni muhimu kufahamu kuwa Mungu
anatumia watu, na shetani pia anatumia watu, kila mtu aliyeko katika nafasi ya
kuwafanyia mema wengine na awafanyie kwa nia njema na nia nzuri, watu wengi sana wakishapewa nafasi badala ya
kuzitumia nafasi hizo kwa kutenda, haki na kuwasaidia watu wa Mungu, kufikia
ndoto zao na kutoa msaada wanaingiwa na choyo, wivu, dhuluma, kiburi na kutaka
kuabudiwa kama miungu watu, wakati wote wanatafuta Heshima na kama huanguki
kuwaabudu wanakasirika sana hiki ndicho kilichowafanya wayahudi kuchukiwa ona
Esta 3:1-6 “Baada ya hayo mfalme Ahasuero
alimwongezea cheo Hamani bin Hamedatha, Mwagagi, akampandisha, akamwekea kiti
chake juu ya maakida wote waliokuwapo pamoja naye. Nao watumishi wote wa
mfalme, walioketi mlangoni pa mfalme, wakainama na kumsujudia Hamani, maana
ndivyo alivyoamuru mfalme kwa habari zake. Bali Mordekai hakuinama, wala
kumsujudia. Basi watumishi wa mfalme walioketi mlangoni pa mfalme wakamwambia
Mordekai, Mbona wewe waihalifu amri ya mfalme? Ikawa, waliposema naye kila siku
asiwasikilize, wakamwarifu Hamani, ili kuona kama mambo yake Mordekai
yatasimama; maana alikuwa amewaambia ya kuwa yeye ni Myahudi. Hata Hamani
alipoona ya kwamba Mordekai hainami wala kumsujudia, alighadhibika sana. Akaona
si shani kumtia mikono Mordekai peke yake; maana wamemjulisha kabila yake
Mordekai; kwa hiyo Hamani alitaka kuwaangamiza Wayahudi wote waliokuwa wakikaa
katika ufalme wote mzima wa Ahasuero, yaani, watu wake Mordekai.”
Unaona kwa sababu ya kutaka
Heshima na kutaka kuabudiwa Hamani Mwagagi alikasirika sana na kutaka kuona
mambo ya Mordekai yatasiamamaje kisa tu kwa mila na desturi za Kiyahudi
hawaruhusiwi kutoa heshima ya Mungu kwa wanadamu, wako kina hamani kila kona
katika maisha yetu ambao wamevimbaa, wana uchungu, wana hasira wana mipango
mibaya imekusudiwa kwaajili yako pale kazini, pale shuleni, pale kwenye
biashara, pale jirani, kila mahali wako watu wenye wivu wenye uchungu, wengine
wana kila kitu lakini wivu umewajaa, wanatamani kuwa wao tu maisha yao yote,
wako watu wengine wana vyeo kibao, kila taasisi yeye ni mtu mkubwa lakini
unaweza kushangaa anakufuatilia wewe ambaye huna hata kuku wa mayaini jambo la
kushangaza wako watu wanaotaka ukwame, wako wanaotaka uwe masikini, wako
wanaotaka usitoke, wako wanaokuroga, wataroga mpaka na watoto wako, wanataka
kuhakikisha kuwa kila kitu chako kinaharibika na hufanikiwi na hiyo ndio furaha
yao! Hiyo ni roho ya Hamani, ni wao Mungu aliwaweka ili wawe msaada na wokovu
katika maisha yako lakini hata kama wao hawako tayari kufanya hay oleo nataka
nikutangazie kuwa uko Msaada na wokovu kwa njia nyingine, Mungu atafanya njia
pasipo na njia, Mungu atakuinua sana, Mungu atakupeleka juu, sisi ni wale ambao
msaada wetu hautoki kwa wanadamu Msaada wetu u katika Bwana aliyezuiumba mbingu
na nchi
Zaburi 121:1-8 “Nitayainua macho yangu
niitazame milima, Msaada wangu utatoka wapi? Msaada wangu u katika Bwana,
Aliyezifanya mbingu na nchi. Asiuache mguu wako usogezwe; Asisinzie akulindaye;
Naam, hatasinzia wala hatalala usingizi, Yeye aliye mlinzi wa Israeli. Bwana
ndiye mlinzi wako; Bwana ni uvuli mkono wako wa kuume. Jua halitakupiga mchana,
Wala mwezi wakati wa usiku. Bwana
atakulinda na mabaya yote, Atakulinda nafsi yako. Bwana atakulinda utokapo na
uingiapo, Tangu sasa na hata milele.”
Unaona wakati wote na kwa karne
nyingi wayahudi na wakristo wametiana moyo kwamba wote wanaopitria magumu
wasiwaangalie wanadamu, tunajua kuwa Mungu huwatumia wanadamu lakini na shetani
pia huwatumia wanadamu, hivyo tunapopitia hatari na kukawa kuna mtu tyunamtegemea
atusaidie mtu huyu anaweza kusahau, Yuko mtu ambaye Yusufu alimtafasiria Ndoto
gerezani na akamwambia ya kuwa ndugu yangu utakaporudi katika kiti cha mfalme
unikumbuke na mimi maana nimefungwa mahali hapa kwa uonevu lakini mtu huyo
alisahau ona
Mwanzo 40: 13-23 “Baada ya siku tatu Farao
atakiinua kichwa chako, atakurudisha katika kazi yako; nawe utampa Farao
kikombe mkononi mwake, kama desturi ya kwanza, ulipokuwa mnyweshaji wake. Ila
unikumbuke mimi, utakapopata mema, ukanifanyie fadhili, nakuomba, ukanitaje kwa
Farao, na kunitoa katika nyumba hii. Kwa sababu hakika naliibiwa kutoka nchi ya
Waebrania, wala hapa sikutenda neno lo lote hata wanitie gerezani. Mkuu wa
waokaji alipoona ya kwamba hiyo tafsiri ni ya mema, akamwambia Yusufu, Mimi
kadhalika nilikuwa katika ndoto yangu, na tazama, ziko nyungo tatu za mikate
myeupe juu ya kichwa changu. Na katika ungo wa juu, mlikuwa na kila namna ya
chakula kwa Farao, kazi za mwokaji; ndege wakavila katika ungo juu ya kichwa
changu. Yusufu akajibu, akasema, Tafsiri yake ndiyo hii Nyungo tatu ni siku
tatu. Baada ya siku tatu Farao atakiinua na kukuondolea kichwa chako, na
kukutundika juu ya mti, na ndege watakula nyama yako. Ikawa siku ya tatu, siku
ya kuzaliwa kwake Farao, akawafanyia karamu watumwa wake wote; akakiinua kichwa
cha mkuu wa wanyweshaji, na cha mkuu wa waokaji, miongoni mwa watumwa wake.
Akamrudisha mkuu wa wanyweshaji katika kazi yake ya kunywesha, naye akampa
Farao kikombe mkononi mwake. Bali akamtundika mkuu wa waokaji, kama Yusufu
alivyowafasiria. Lakini huyo mkuu wa wanyweshaji hakumkumbuka Yusufu, alimsahau
”
Nadhani unaweza kuona mioyo ya
kibinadamu, wakati mwingine Mungu anafungua milango na kumuinua mtu ili aweze
kuwa baraka kwako lakini badala ya Mtu huyo kuwa Baraka anajibariki yeye, hii
ilimtokea Yusufu hata alipotoa maagizo unikumbuke mtu yule alimsahau, Biblia
inasema lakini mkuu huyo wa wanyweshaji hakumkumbuka Yusufu , wakati mwingine
Mungu atainua Mwanamke au mwanaume
katika mahali Fulani kwa kusudi fulani ili wabebe jukumu Fulani na
kuyatimiza mapenzi ya Mungu kwako na wanaweza kujisahau au wanaweza kusaidia
lakini yote katika yote ni ili Mungu atimize mpango wako kwake katika maisha
yako wakikusahau usisikitike, wakikujali usisikitike Mungu ataleta Msaada na
wokovu kwa njia nyingine, Mungu anaweza kumtumia kila mmoja wetu kwa nafasi
yake kutimiza mpango wake katika maisha yetu nan i muhimu sana kujiangalia
katika kila nafasi tulizo nazo tukijisahau basi tujue wazi ya kuwa makudui ya
Mungu hayawezi kuzuilika yeye ataleta Msaada na wokovu kwa njia nyingine na
sisi wahusika tunaweza kujikuta tunaaangamia
Esta 4:14 “Kwa maana wewe ukinyamaza kabisa
wakati huu, ndipo kutakapowatokea Wayahudi msaada na wokovu kwa njia nyingine;
ila wewe utaangamia pamoja na mlango wote wa baba yako; walakini ni nani ajuaye
kama wewe hukuujia ufalme kwa ajili ya wakati kama huo?”
Baraka Burton katika wimbo wake
NAOMBA NIWE BARAKA Anaimba maneno muhimu sana ambayo Mungu ametaka yaaambatane
na ujumbe wangu huu! Kama maombi ya sisi kukubali kutumiwa na Mungu kwa nia
njema badala ya kuacha Mungu alete Msaada kwa njia nyingine! ~
Wimbo: Naomba niwe Baraka kwa wengine Na Burton King
Na Rev. Innocent Samuel Kamote
Mkuu wa wajenzi Mwenye Hekima!