Mwanzo 15:12-16 “Na jua lilipokuwa likichwa
usingizi mzito ulimshika Abramu, hofu ya giza kuu ikamwangukia. BWANA
akamwambia Abramu, Ujue hakika ya kwamba uzao wako utakuwa mgeni katika nchi
isiyo yake, watawatumikia watu wale, nao watateswa muda wa miaka mia nne. Hata
na taifa lile, watakaowatumikia, nitawahukumu; baadaye watatoka na mali mengi. Lakini wewe utakwenda kwa baba zako kwa
amani, utazikwa katika uzee mwema. Na
kizazi cha nne kitarudi hapa, maana haujatimia uovu wa Waamori bado.”
Utangulizi:
Maisha ya mwanadamu yamejaa siri
kubwa sana ambayo majibu ya maswali mengi ambayo wanadamu hujiuliza yanajibika
tu kwa kuwa na ufahamu wa kutosha katika maandiko na katika kumjua Mungu na
kuwa na uhusiano wa kudumu na Mungu, haijalishi umepitia changamoto za aina
gani katika maisha au unapitia changamoto gani hata wakati huu somo kama hili linapokujia
lakini Roho Mtakatifu amenitaka leo nikujulishe ya kuwa Mungu anajua mwanzo
mwisho, Mungu anayo ramani ya maisha yako na anajua kila kitu kinachoendelea
katika maisha yako! Ni yeye pekee mwenye uwezo wa kutangaza mwisho wako tangu
mwanzo na sio wanadamu!
Isaya 46:9-10
“kumbukeni mambo ya zamani za kale; maana mimi ni
Mungu, wala hapana mwingine; mimi ni Mungu, wala hapana aliye kama mimi;
nitangazaye mwisho tangu mwanzo, na tangu zamani za kale mambo yasiyotendeka
bado; nikisema, Shauri langu litasimama, nami nitatenda mapenzi yangu yote.”
Kwa msingi huo hupaswi kuwa na
shaka wala kuogopa katika maisha yako kwamba unapitia changamoto za aina gani,
wala hupaswi kuogopa kuwa itakuwaje kesho na kesho kutwa kumbuka tu kuwa Mungu
yuko kwenye udhibiti wa kila jambo linalotendeka na linalotokea katika maisha
yako yeye pekee ndiye anayejua maisha yako mwanzo mwisho na sio wanadamu, leo
tutachukua Muda kujifunza somo hili Mungu anajua mwanzo mwisho kwa kuzingatia
vipengele vitatu vifuatavyo:-
·
Mungu anajua yote.
·
Hakuna utakachopoteza.
·
Mungu anajua mwanzo mwisho.
Mungu anajua yote:
Moja ya sifa kubwa ya Mungu aliye
hai na wa kweli ni kuwa ANAJUA YOTE tena
anajua mwisho wa kila jambo na anauwezo wa kulisema jambo hilo tangu mwanzo hii
ni kwa sababu yeye ana sifa ya kuwa mwanzo na mwisho, (Yaani Alfa na Omega). Hivyo
ni wazi kuwa anajua tunakotoka na tunakokwenda! Ramani yote ya maisha yetu iko
mikononi mwake na kwa ujumla yeye ndiye mwenye mpango mzima (Master Plan) ya maisha ya kila mtu
duniani,
Ufunuo 21:6 “Akaniambia, Imekwisha kuwa.
Mimi ni Alfa na Omega, Mwanzo na Mwisho. Mimi nitampa yeye mwenye kiu, ya chemchemi
ya maji ya uzima, bure.”
Mwanzo 25:21-23. “Isaka akamwomba BWANA kwa
ajili ya mke wake, maana alikuwa tasa. Naye BWANA akamwitikia, na Rebeka mkewe
akachukua mimba. Watoto wakashindana tumboni mwake. Naye akasema, Ikiwa ni
hivi, kuishi kwanifaa nini? Akaenda kumwuliza BWANA. BWANA akamwambia, Mataifa
mawili yamo tumboni mwako, Na kabila mbili za watu watafarakana tangu tumboni
mwako. Kabila moja litakuwa hodari kuliko la pili, Na mkubwa atamtumikia mdogo.”
Unaona hapo kalba hajazaliwa Esau
na Yakobo Mungu alishajua mwisho wao utakuwaje hivyo ni wazi kuwa Mungu anajua
mwanzo mwisho wa kila mtu, maisha yetu yameratibiwa na Roho wake Mtakatifu
tangu itakavyokuwa mwanzo mpaka mwisho! Mungu anajua mwanzo mwisho!
Kwa ujumla kuna maeneo makubwa
matano yanayotumika kuelezea sifa za Mungu ambazo hakuna kiumbe kingine
chochote kinaweza kuwa na sifa hizo isipokuwa Mungu peke yake, sifa hizo ni
pamoja na:-
-
Mwenye
nguvu zote – Omnipotence
-
Mwenye
kujua yote – Omniscience
-
Mwenye
kuweko mahali kote kwa wakati mmoja – Omnipresence
-
Asiyebadilika
– immutability
-
Ni wa
Milele na milele – Transcendence
Kwa Mujibu wa wanatheolojia hizo
ni sifa ambazo mwanadamu au kiumbe cha kawaida hakiwezi kuwa nazo isipikuwa
Mungu peke yake, hata hivyo sio kusudi langu leo kuelezea sifa zote tano za
Mungu lakini nataka kuchukua Muda kuelezea sifa moja tu ya MWENYE KUJUA YOTE kwa kusudi tu la kutimiza leongo la somo hili:-
Neno hilo MWENYE KUJUA YOTE Katika lugha ya kiingereza linatumika neno OMNISCIENCE ambalo kimsingi ni neno la asili ya lugha
ya kilatini linalojumuisha muunganiko wa maneno mawili Omnis - ambalo kwa
kiingereza ni ALL ikiwa na maana ya
Kiswahili YOTE/WOTE na neno SCIENTIA ambalo kwa kiingereza ni KNOWLEDGE ambalo kwa
Kiswahili ni MAARIFA, au UJUZI kwa
hiyo linapoungwanishwa pamoja tunapata neno OMNISCIENCE ambalo kwa
kiingereza ni ALL KNOWING na kwa
kiwahili KUJUA YOTE na sasa basi linapotumika kuelezea sifa za
Mungu linatumika kuelezea kuwa Mungu anajua yote hivyo hakuna jipya kwake wala
hakuna jambo wanadamu watagundua ambalo Mungu hakuwa analijua yeye anajua kila
kitu, kwa hiyo kila jambo linalokutokea katika maisha yako haimaanishi kuwa
Mungu hakuwa na taarifa nalo, wala Mungu hasahau kitu kwa sababu amekuwepo toka
milele na anaendelea kuwepo na yupo hata milele kwa hiyo Mungu anajua kila kitu
na hakuna cha kumshangaza !
Katika maisha yetu hakuna bahati
mbaya Mungu anaelewa mwisho na mwanzo wa kila kinachoendelea katika maisha
yako, hivyo hupaswi kuogopa na badala yake unapaswa kumsubiri Mungu kwa njia ya
maombi, Katika andiko la Msingi tulilolisoma tunaona Mungu akizungumza na
Abraham kuhusu uzao wake kizazi cha nne ambao wangeshuka Misri na kukaa huko
miaka 400 na kuwa kisha atawarejesha tena katika nchi ya mkanaani ona
Mwanzo 15:12-16 “Na jua lilipokuwa likichwa
usingizi mzito ulimshika Abramu, hofu ya giza kuu ikamwangukia. BWANA
akamwambia Abramu, Ujue hakika ya kwamba uzao wako utakuwa mgeni katika nchi
isiyo yake, watawatumikia watu wale, nao watateswa muda wa miaka mia nne. Hata
na taifa lile, watakaowatumikia, nitawahukumu; baadaye watatoka na mali
mengi. Lakini wewe utakwenda kwa baba
zako kwa amani, utazikwa katika uzee mwema.
Na kizazi cha nne kitarudi hapa, maana haujatimia uovu wa Waamori bado.”
Unaona ni karibu kati ya miaka
1632-2000 hivi kutoka Abraham mpaka wakati Musa anazaliwa na kuitwa kuwakomboa
wana wa Israel, Lakini Mungu anayejua yote anamwambia Abrahamu habari za wana
wa Israel namna watakavyoshuka Misri na kutumikishwa huko na kuwa
angewapandisha tena Miaka Mingi sana
hata Isaka hajazaliwa wala Yakobo hajazaliwa, huo ni uthibitisho ulio wazi kuwa
kila kinachotokea katika maisha yetu kimeratibiwa katika mpango na ratiba za
Mungu aliye hai, huna sababu ya kujuta wala kulia katika kila jambo
unalolipitia Mungu yuko kwenye udhibiti na makusudi yake yatatimizwa tu, na
lile ambalo halijakusudiwa halitatimia !
Hakuna utakachopoteza!
Kama Mungu anajua yote ni wazi
kuwa anayajua maisha yetu vema na hakuna lolote linaloweza kuharibu mpango wetu
kwake, yote yanayotutokea yawe mema au mabaya yote ni kwa makusudi yake na
mapenzi yake ni lazima yatatimizwa, kama Mungu amekuahidi jambo fahamu ya kuwa
atalitimiza bila kujali nini kinatokea katika maisha yako kwa sasa kitatimia
kwani Mungu ni mwaminifu na wanadamu ni waongo!
-
Hesabu
23:19 “Mungu si mtu, aseme uongo; Wala si
mwanadamu, ajute; Iwapo amesema, hatalitenda? Iwapo amenena, hatalifikiliza?”
-
2Wakorintho
1:20 “Maana ahadi zote za Mungu zilizopo katika
yeye ni Ndiyo; tena kwa hiyo katika yeye ni Amin; Mungu apate kutukuzwa kwa
sisi.”
-
2Samuel
2:31 “Mungu njia yake ni kamilifu; Ahadi ya Bwana
imehakikishwa; Yeye ndiye ngao yao Wote wanaomkimbilia.”
-
Isaya
46:9-10 “kumbukeni mambo ya zamani za kale; maana
mimi ni Mungu, wala hapana mwingine; mimi ni Mungu, wala hapana aliye kama
mimi; nitangazaye mwisho tangu mwanzo, na tangu zamani za kale mambo
yasiyotendeka bado; nikisema, Shauri langu litasimama, nami nitatenda mapenzi
yangu yote.”
-
Mithali
19:21 “Mna hila nyingi moyoni mwa mtu; Lakini
shauri la Bwana ndilo litakalosimama.”
-
Ayubu
42:2 “Najua ya kuwa waweza kufanya mambo yote, Na
ya kuwa makusudi yako hayawezi kuzuilika.”
-
Warumi
8:28 “Nasi twajua ya kuwa katika mambo yote Mungu
hufanya kazi pamoja na wale wampendao katika kuwapatia mema, yaani, wale
walioitwa kwa kusudi lake.”
Mungu anapokuwa amekusudia jambo
Fulani katika maisha yako, ni muhimu kufahamu kuwa jambo hilo halitaweza
kuzuiliwa na mtu, Mungu ana makusudi na maisha yako, kila kitu katika maisha
yako hata aina ya mapito unayoyapitia yanakuandaa kukuleta katika lile kusudi
kwa msingi huo lolote lililo jema au lililo baya lisikutishe wala simama katika
mapenzi ya Mungu, jitahidi usitende dhambi lakini naam hata ukitenda maana hakuna mwanadamu atendaye mema asitende
dhambi hiyo haimzuii Mungu kutuimiza mpango wake alioukusudia kwako kwa sababu yeye anajua mwanzo mwisho yeye ni
msaada ulio karibu atafanya njia, atarehemu, atasamehe atakuweka panapo nafasi
na kusudio lake lililokusudiwa ndani mwako litatimizwa Warumi 8:28-30 “Nasi twajua ya kuwa katika
mambo yote Mungu hufanya kazi pamoja na wale wampendao katika kuwapatia mema,
yaani, wale walioitwa kwa kusudi lake. Maana wale aliowajua tangu asili,
aliwachagua tangu asili wafananishwe na mfano wa Mwana wake, ili yeye awe
mzaliwa wa kwanza miongoni mwa ndugu wengi. Na wale aliowachagua tangu asili,
hao akawaita; na wale aliowaita, hao akawahesabia haki; na wale aliowahesabia
haki, hao akawatukuza.”
Mungu anajua mwanzo mwisho!
Ni muhimu sasa kuwa na ufahamu
kuwa Mungu anajua kila kitu, Mungu anajua mambo yote na ya kuwa makusudi yake
hayawezi kuzuilika, ikiwa tunafahamu wazi sasa jambo hilo ni muhimu kuelewa
kuwa hakuna kitu ambacho kinafanyika duniani katika maisha yetu ambacho Mungu
hajui, Mungu ana taarifa ya mambo mengi sana
na anajua vema kila kitu kwa kina na mapana na marefu, Mungu anajua
mambo makubwa na madogo, maandiko yanaonyesha wazi maswala ambayo Mungu
anayajua na kuyafuatilia na ukijiweka katika ulinganifu wake utakubaliana nami
kuwa Mungu anajua mwanzo mwisho ona:-
-
Anajua
idadi ya nywele zetu Mathayo 10:29-30 “Je!
Mashomoro wawili hawauzwi kwa senti moja? Wala hata mmoja haanguki chini
asipojua Baba yenu; lakini ninyi, hata nywele za vichwa vyenu zimehesabiwa zote.”
Maandiko tena kupitia Yesu Kristo mwenyewe yananyesha kuwa hata ndege wa angani
hawaanguki chini bila mbingu kuwa na taarifa yaani Mungu anajua kuwa kuna ndege
amepigwa, ametegwa, ameliwa na kadhalika pamoja na udogo walio nao, lakini sio
hivyo tu hata nywele zetu idadi yake inajulikana na Mungu hiii maaana yake nini
maana yake Mungu anajali kuanzia vitu vikubwa mpaka vitu vidogo vidogo
vingi na kama ni hivyo anayajali na
kuyajua maisha yako na kila unalilopitia na utakalolipitia na namna
utakavyotoka na utakavyotimiza mpango wake na makusudi yake duniani
-
Anatujua
Mwanzo mwisho Yeremia 1:4-5 “Neno la Bwana
lilinijia, kusema, Kabla sijakuumba katika tumbo nalikujua, na kabla hujatoka
tumboni, nalikutakasa; nimekuweka kuwa nabii wa mataifa.” Mungu
anatujua hata kabla hajaruhusu tuzaliwe duniani wewe na mimi tulikuweko katika
wazo lake tangu milele Mungu anamwambia Yeremia nabii kabla hajatungishwa mimba
kwenye tumbo la mama yake yeye alikwisha kumjua na alikwisha kuchagua kuwa
atakuwa nabii kwa mataifa mbalimbali, Kama Mungu anakujua kuumbwa kwako na
kuzaliwa kwako na kama anaweka kusudi lake ndani yetu hata kabla hatujazaliwa
ni Dhahiri alijua kila utakachokipitia pia anajua siku zetu za kuwepo duniani,
anajua matendo yetu yote mema na mabaya kila kitu katika maisha yetu
kimeratibiwa Mbinguni Zaburi 139:13-18 “Maana
Wewe ndiwe uliyeniumba mtima wangu, Uliniunga tumboni mwa mama yangu. Nitakushukuru kwa kuwa nimeumbwa Kwa jinsi ya
ajabu ya kutisha. Matendo yako ni ya ajabu, Na nafsi yangu yajua sana, Mifupa
yangu haikusitirika kwako, Nilipoumbwa kwa siri, Nilipoungwa kwa ustadi pande
za chini za nchi; Macho yako yaliniona kabla sijakamilika; Chuoni mwako
ziliandikwa zote pia, Siku zilizoamriwa kabla hazijawa bado. Mungu, fikira zako
zina thamani nyingi kwangu; Jinsi ilivyo kubwa jumla yake! Kama ningezihesabu
ni nyingi kuliko mchanga; Niamkapo nikali pamoja nawe.”
-
Anajua
uhusiano wetu na yeye umesimamaje -
Nahumu 1:7 “Bwana
ni mwema, ni ngome siku ya taabu; naye huwajua hao wamkimbiliao”
Warumi 8:16-17 “Roho
mwenyewe hushuhudia pamoja na roho zetu, ya kuwa sisi tu watoto wa Mungu; na
kama tu watoto, basi, tu warithi; warithi wa Mungu, warithio pamoja na Kristo;
naam, tukiteswa pamoja naye ili tupate na kutukuzwa pamoja naye.”
Yohana 10:27-29 “Kondoo wangu waisikia sauti yangu; nami
nawajua, nao wanifuata. Nami nawapa uzima wa milele; wala hawatapotea kamwe;
wala hakuna mtu atakayewapokonya katika mkono wangu. Baba yangu aliyenipa hao
ni mkuu kuliko wote; wala hakuna mtu awezaye kuwapokonya katika mkono wa Baba
yangu.”
Mungu anamjua
kila mtu anayemtegemea anayemkimbilia anayemuamini anajua umesimama wapi katika
uhusiano wako na yeye, anajua anavyotuhudumia na sisi tu mashahidi kwa kuwa
Roho wake Mtakatifu hutushuhudia kuwa sisi ni wana wa Mungu hivyo haki zetu
zinahifadhiwa ndani yake kwa nini kwa sababu anajua uhusiano wetu tulionao
kwake na njia tutakayoipitia na kule atakakotuongoza anajua mwanzo mwisho!
-
Anatujua
kwa majina yetu - alimjua Musa Kutoka 33:12 na 17 alimjua sauli na alimjua
Koreshi mfalme wa uajemi hata kabla hajazaliwa tena kwa jina lake kabisa wazi
wazi
Kutoka 33:11-12 “Naye BWANA akasema na Musa uso kwa uso,
kama vile mtu asemavyo na rafiki yake. Kisha akageuka akarejea hata maragoni;
bali mtumishi wake Yoshua, mwana wa Nuni, naye ni kijana, hakutoka mle hemani.
Musa akamwambia BWANA, Angalia, wewe waniambia, Wachukue watu hawa; nawe
hukunijulisha ni nani utakayemtuma pamoja nami. Walakini umesema, Nakujua jina
lako, nawe umepata neema mbele zangu.” Na
Kutoka 33:17’ “BWANA
akamwambia Musa, Nitafanya na neno hili ulilolinena, kwa maana umepata neema
mbele zangu, nami nakujua jina lako.”
Alimjua Sauli
aliyekuwa analiudhi kanisa ona Matendo
9:1-5 “Lakini Sauli, akizidi kutisha na kuwaza
kuwaua wanafunzi wa Bwana, akamwendea Kuhani Mkuu, akataka ampe barua za kuenda
Dameski zilizoandikwa kwa masinagogi, ili akiona watu wa Njia hii, waume kwa
wake, awafunge na kuwaleta Yerusalemu. Hata alipokuwa akisafiri, ikawa
anakaribia Dameski; ghafula ikamwangaza kote kote nuru kutoka mbinguni. Akaanguka
chini, akasikia sauti ikimwambia, Sauli, Sauli, mbona waniudhi? Akasema, U nani
wewe, Bwana? Naye akasema, Mimi ndimi Yesu unayeniudhi wewe.”
Alimjua Koreshi
hata kabla hajazaliwa Isaya 45:1-5 “Haya ndiyo Bwana amwambiayo Koreshi, masihi wake,ambaye
nimemshika mkono wake wa kuume,ili kutiisha mataifa mbele yake,name nitalegeza
viuno vya wafalme;ili kufungua milango mbele yake,hata malango hayatafungwa. Nitakwenda
mbele yako, na kupasawazisha mahali palipoparuza; nitavunja vipande vipande
milango ya shaba, na kukata-kata mapingo ya chuma; nami nitakupa hazina za
gizani, na mali zilizofichwa za mahali pa siri, upate kujua ya kuwa mimi ni
Bwana, nikuitaye kwa jina lako, naam, Mungu wa Israeli.Kwa ajili ya Yakobo, mtumishi
wangu, na Israeli, mteule wangu, nimekuita kwa jina lako; nimekupa jina la
sifa; ijapokuwa hukunijua. Mimi ni Bwana, wala hapana mwingine; zaidi yangu
mimi hapana Mungu; nitakufunga mshipi ijapokuwa hukunijua;”
Ni jambo la
kushangaza sana Mungu alimjua Musa kwa jina lake, Mungu alimjua Sauli ambaye
alikuwa analiudhi kanisa na kumuita ili awe mtume Mungu, alimjua mfalme Koreshi
wa uajemi kabla hajazaliwa, Isaya alitaja habari zake na Mungu alijua kuwa
atamtumiaje maandiko haya yote ni mjumuisho wa taarifa tu kuwa Mungu anatujua
anajua huduma alizotuitia anajua utumishi aliotuitia anajua mapito
tunayoyapitia anajua kila kitu kinachoendelea katika maisha yetu.
-
Anaijua
mioyo yetu.
Yeremia 17:9-10 “Moyo
huwa mdanganyifu kuliko vitu vyote, una ugonjwa wa kufisha; nani awezaye
kuujua? Mimi, Bwana, nauchunguza moyo, navijaribu viuno, hata kumpa kila mtu
kiasi cha njia zake, kiasi cha matunda ya matendo yake.”
1Falme 8:39 “basi,
usikie huko mbinguni, makao yako, ukasamehe, ukatende, ukampe kila mtu kwa
kadiri ya njia zake; wewe ujuaye moyo wake; (maana wewe peke yako ndiwe uijuaye
mioyo ya wanadamu wote)”
Mungu anaijua
mioyo yetu anajua kama uko uovu ndani yetu anajua kama mioyo yetu ni safi, ama ina
ugonjwa wa kufisha yaani kama tunayoyawaza yatapelekea mauti ni yeye pia aliye
tayari kuitakasa mioyo yetu kama tutakuwa radhi na kuwa na hiyari ya kuyadai na
kuyataka mapenzi yake.
-
Anayajua
mawazo yetu - Mungu anayajua mawazo yetu anajua kila jambo analoliwaza
mwanadamu anajua pia tunapokusudia kutenda uovu anajua Mwanzo 6:5-6 “BWANA akaona ya kuwa maovu ya
mwanadamu ni makubwa duniani na kwamba kila kusudi analowaza moyoni mwake ni
baya tu sikuzote. BWANA akaghairi kwa kuwa amemfanya mwanadamu duniani,
akahuzunika moyo.” Mungu aliyasoma mawazo ya wanadamu wakati wa Nuhu
na kuona kuwa ayoyakusudia ni maovu tu hii maana yake ni kuwa kila wazo
linalotembea katika akili zetu Mungu analiona na hakuna kilichofikichika Zaburi 139: 1-2 “Ee
Bwana, umenichunguza na kunijua. Wewe wajua kuketi kwangu na kuondoka kwangu;
Umelifahamu wazo langu tokea mbali.” Unaona Mungu anajua mwanzo
mwisho analiona wazo la mwanadamu tokea mbali, tunaweza kuwatisha watu kwa
kujifanya tunajua kila kitu na tunajua kila wanachokifikiri lakini Mungu tayari
anajua anaujua ukweli, hakuna kinachoweza kufichika.
-
Anajua
hofu zetu – achilia mbali kwamba Mungu anayajua mawazo yetu, Mungu anazijua
pia hofu zetu na kutuponya nazo zote, Mapema sana Yesu akijua mahitaji Muhimu
ya wanadamu ambayo wamekuwa wakihofia aliwaondoa wasi wasi kuwa Mungu
anajishughulisha sana na mambo yetu yawe
kwa heri au kwa shari atashughulika katika njia iliyobora na njema zaidi.
Mathayo 6:25-34 “Kwa
sababu hiyo nawaambieni, Msisumbukie maisha yenu, mle nini au mnywe nini; wala
miili yenu, mvae nini. Maisha je! Si zaidi ya chakula, na mwili zaidi ya
mavazi? Waangalieni ndege wa angani, ya kwamba hawapandi, wala hawavuni, wala
hawakusanyi ghalani; na Baba yenu wa mbinguni huwalisha hao. Ninyi je! Si bora
kupita hao? Ni yupi kwenu ambaye akijisumbua aweza kujiongeza kimo chake hata
mkono mmoja? Na mavazi, ya nini kuyasumbukia? Fikirini maua ya mashamba, jinsi
yameavyo; hayafanyi kazi, wala hayasokoti nami nawaambia, ya kwamba hata
Sulemani katika fahari yake yote hakuvikwa vizuri kama mojawapo la hayo. Basi, ikiwa
Mungu huyavika hivi majani ya kondeni, yaliyopo leo, na kesho hutupwa kalibuni,
je! Hatazidi sana kuwavika ninyi, enyi wa imani haba? Msisumbuke, basi,
mkisema, Tule nini? Au Tunywe nini? Au Tuvae nini? Kwa maana hayo yote Mataifa
huyatafuta; kwa sababu Baba yenu wa mbinguni anajua ya kuwa mnahitaji hayo
yote. Bali utafuteni kwanza ufalme wake,
na haki yake; na hayo yote mtazidishiwa. Basi msisumbukie ya kesho; kwa kuwa
kesho itajisumbukia yenyewe. Yatosha kwa siku maovu yake.”
1Petro 5:6-7 “Basi
nyenyekeeni chini ya mkono wa Mungu ulio hodari, ili awakweze kwa wakati wake;
huku mkimtwika yeye fadhaa zenu zote, kwa maana yeye hujishughulisha sana kwa
mambo yenu.”
Baba yetu wa
mbinguni anajua tunayoyahitaji kwa sababu hiyo wajibu wetu ni kuomba tu ambako
ndiko kumtwika yeye fadhaa zetu zote na tunaambiwa kuwa anajishughulisha sana
na mambo yetu maana yake anashughulika vema na hofu zetu na anajua njia sahihi
na namna sahihi iliyo bora ya kutupatia mahitaji yetu
-
Anayajua
matendo yetu – Kama Mungu anayajua mawazo yetu na anajua hofu yetu sembuse
matendo yetu? Mungu anayajua yote hata yale tuyatendayo sirini maandiko
yanatueleza kuwa wakati wa hukumu Mungu ataweka wazi kila tendo na kila neno la
siri tulilolitenda na pia kazi za wapendwa wote zitapimwa kulinga ana nia ya
kila mmoja Mungu anajua Mungu anajua alionya sana katika nyaraka saba kwa
makanisa saba kule Asia katika kitabu cha ufunuo kuwa anajua anajua na akatoa
maelekezo sasa kwao
Muhubiri 12:14 “Kwa
maana Mungu ataleta hukumuni kila kazi, pamoja na kila neno la siri, likiwa
jema au likiwa baya.”
2Wakorintho 5:9-10 “Kwa hiyo, tena, ikiwa tupo hapa, au ikiwa hatupo hapa, twajitahidi
kumpendeza yeye. Kwa maana imetupasa sisi sote kudhihirishwa mbele ya kiti cha
hukumu cha Kristo, ili kila mtu apokee ijara ya mambo aliyotenda kwa mwili,
kadiri alivyotenda, kwamba ni mema au mabaya.”
Ufunuo 3:8 “Nayajua
matendo yako. Tazama, nimekupa mlango uliofunguliwa mbele yako, ambao hapana
awezaye kuufunga, kwa kuwa unazo nguvu kidogo, nawe umelitunza neno langu, wala
hukulikana jina langu.”
Mungu hataleta
hukumuni mambo asiyoyajua ataleta hukumuni ushahidi ulio wazi wa matendo yetu
yote na maneno yetu yote lakini pia waamini watapimwa na Kristo katika kiti cha
hukumu so kwaajili ya hukumu bali kwaajili ya kazi tulizozifanya hapa duniani,
Mungu anajua pia tuyatendayo na nia yake kwa nini tunayatenda
-
Anayajua
maneno yetu - Mungu anayajua maneno yetu yote kama Mungu mwenye kujua yote
hakuna neno lolote tunalolisema katika ndimi zetu ambalo linampita anayajua
vema
Zaburi 139:1-4 “Ee
Bwana, umenichunguza na kunijua. Wewe wajua kuketi kwangu na kuondoka kwangu;
Umelifahamu wazo langu tokea mbali. Umepepeta kwenda kwangu na kulala kwangu,
Umeelewa na njia zangu zote. Maana hamna neno ulimini mwangu Usilolijua kabisa,
Bwana.”
Mathayo 12:35-37 “Mtu
mwema katika akiba njema hutoa mema; na mtu mbaya katika akiba mbaya hutoa
mabaya. Basi, nawaambia, Kila neno lisilo maana, watakalolinena wanadamu,
watatoa hesabu ya neno hilo siku ya hukumu. Kwa kuwa kwa maneno yako
utahesabiwa haki, na kwa maneno yako utahukumiwa.”
-
Anazijua
njia zetu – Kuna maandiko memngi sana yanayothibitisha au kuonyesha Mungu
akizungumza kuhusu njia zetu lakini maandiko hayo yanatutaka tumkabidhi yeye
njia zetu kwa kuwa anaijua njia tuiendeayo
Ayubu 23:10 “Lakini yeye aijua njia niendeayo;
Akisha kunijaribu, nitatoka kama dhahabu.” Yeye kama Mchungaji mwema
wakati wote hutuongoza katika njia inayofaa Zaburi 23:3-4 “Hunihuisha nafsi yangu; na
kuniongoza Katika njia za haki kwa ajili ya jina lake. Naam, nijapopita kati ya
bonde la uvuli wa mauti, Sitaogopa mabaya; Kwa maana Wewe upo pamoja nami,
Gongo lako na fimbo yako vyanifariji.” Mithali 16:9 “Moyo wa mtu huifikiri njia yake; Bali Bwana huziongoza
hatua zake.”
Kwa kuwa Mungu
anajua njia kwa usahihi hii maana yake mipango yetu yote ni vema tukimkabidhi
yeye mipango yetu yote au kuomba Muongozo kutoka kwake lakini vyo vyote iwavyo
Mungu anajua mwanzo mwisho .
Anayajua madhaifu yetu – Mungu anayajua
madhaifu yetu na anajua namna nzuri ya kuchukuliana nasi tofauti na jinsi
wanadamu wanavyotuchukulia yeye hutuchukulia kwa rehema kwa sababu anatujua
kuwa sisi ni Mavumbi
Zaburi 103:8-14 “Bwana
amejaa huruma na neema, Haoni hasira upesi, ni mwingi wa fadhili. Yeye hatateta
sikuzote, Wala hatashika hasira yake milele. Hakututenda sawasawa na hatia
zetu, Wala hakutulipa kwa kadiri ya maovu yetu. Maana mbingu zilivyoinuka juu
ya nchi, Kadiri ile ile rehema zake ni kuu kwa wamchao. Kama mashariki ilivyo
mbali na magharibi, Ndivyo alivyoweka dhambi zetu mbali nasi. Kama vile baba
awahurumiavyo watoto wake, Ndivyo Bwana anavyowahurumia wamchao. Kwa maana Yeye
anatujua umbo letu, Na kukumbuka ya kuwa sisi tu mavumbi.”
2Wakorintho 12:9-10 “Naye akaniambia, Neema yangu yakutosha; maana uweza wangu
hutimilika katika udhaifu. Basi nitajisifia udhaifu wangu kwa furaha nyingi,
ili uweza wa Kristo ukae juu yangu. Kwa hiyo napendezwa na udhaifu, na
ufidhuli, na misiba, na adha, na shida, kwa ajili ya Kristo. Maana niwapo
dhaifu ndipo nilipo na nguvu.”
-
Anajua
siku za uhai wetu Duniani
Wanadamu kwa
kawaida hatujui siku za maisha yetu ni ngapi, Mungu ametuficha lakini yeye
mwenyewe anajua anajua siku za maisha yetu anaweza kutusaidia kutujulisha ili
kwamba tuzitumie kwa hekima ona Zaburi
90:12 “Basi, utujulishe kuzihesabu siku zetu,
Tujipatie moyo wa hekima.”
Yakobo 4:13-14 “Haya
basi, ninyi msemao, Leo au kesho tutaingia katika mji fulani na kukaa humo
mwaka mzima, na kufanya biashara na kupata faida; walakini hamjui
yatakayokuwako kesho. Uzima wenu ni nini? Maana ninyi ni mvuke uonekanao kwa
kitambo, kisha hutoweka.” Maisha ya uhai wetu uko mikononi mwa
Mungu, maisha yetu ni kama mvuke hatujui yatakayokuwako kesho, Lakini Mungu
anajua kila kitu anajua mambo yote, unaweza ukafichwa usijue siku yako lakini
kwa Mungu hakuna geni wala la kushangaza.
Hitimisho:
Kwa kuwa tumejifunza kwa kina na
kuelewa kuwa Mungu anajua mwanzo mwisho ni muhimu kwetu kutokuogopa
tunapokuwa katika mapito ya aina yoyote
duniani, ni lazima tuelewe na kukubali kuwa kila linalotutokea katika ulimwengu
huu liko chini ya uwezo wa kiungu kazi yetu ni kuomba na kumuacha yeye atimize
mapenzi yake, Mungu alimwambia Ibrahimu maswala yote yatakayojitokeza baadaye
kizazi chake cha nne ambao walishuka Misri na baada ya miaka 400 kuwa
angewapandisha tena walishuka kupitia Yusufu unajua yaliyomkuta Yusufu unajua
yaliyowakuta wana wa Israel safari haikuwa nyepesi lakini tumeelewa kuwa Mungu alikuwa
kwenye udhibiti, kila linalotutokea kwenye maisha yetu hatupaswi kuogopa tunaye
Mungu anayejua yote tukiyajua haya tutafahamu kuwa haupaswi kujisumbua katika
jambo lolote lile isipokuwa kwa kila jambo kwa kusali na kuomba na
kumuacha Mungu afanye kazi yake Mungu
anajua maisha yetu anajua uendako anajua utokako hakuna lililofichika kwake
kuhusiana na maisha yako hivyo usifadhaike! Wala usihuzunike moyoni mwako Mungu
anajua Mungu anaona na Yeye atatenda. Mapenzi yake yatimizwe katika maisha yetu
kwaajili ya utukufu wake.
Wafilipi 4:6-7 “Msijisumbue kwa neno lo
lote; bali katika kila neno kwa kusali na kuomba, pamoja na kushukuru, haja
zenu na zijulikane na Mungu. Na amani ya Mungu, ipitayo akili zote,
itawahifadhi mioyo yenu na nia zenu katika Kristo Yesu.”
Na. Rev. Innocent Mkombozi Kamote
Mkuu wa wajenzi mwenye Hekima!.