Zaburi 103:14-16 “Kwa maana Yeye anatujua
umbo letu, Na kukumbuka ya kuwa sisi tu mavumbi. Mwanadamu siku zake zi kama
majani; Kama ua la kondeni ndivyo asitawivyo. Maana upepo hupita juu yake,
kumbe haliko! Na mahali pake hapatalijua tena.”
Utangulizi:
Ni muhimu kujikumbusha tena na
tena Japokuwa haipendezi ya kuwa maisha ya mwanadamu duniani yamefupizwa sana, Kimsingi
maisha ya mwanadamu ni mafupi mno ukilinganisha na maisha ya milele, ambayo
Mungu amekusudia kuwapa wanadamu kama watamuamini Bwana Yesu,
Yohana 3:16 “Kwa maana jinsi hii Mungu
aliupenda ulimwengu, hata akamtoa Mwanawe pekee, ili kila mtu amwaminiye
asipotee, bali awe na uzima wa milele.”
Kufupishwa kwa maisha ya
mwanadamu kumetokana na Mungu mwenyewe kuyapunguza kama adhabu Baada ya
kuongezeka kwa maasi yaani dhambi zetu wanadamu hapa ulimwenguni!
Mwanzo 6:1-3 “Ikawa wanadamu walipoanza
kuzidi usoni pa nchi na wana wa kike walizaliwa kwao, wana wa Mungu waliwaona
hao binti za wanadamu ya kuwa ni wazuri; wakajitwalia wake wo wote
waliowachagua. BWANA akasema, Roho yangu haitashindana na mwanadamu milele, kwa
kuwa yeye naye ni nyama; basi siku zake zitakuwa miaka mia na ishirini.”
Mwanzoni mwanadamu alikuwana
uwezo wa kuishi kwa karne tisa (9) yaani
miaka mia tisa na zaidi, na Mwanadamu aliyepata kuishi sana kuliko wanadamu
wote aliitwa Methusela ambaye aliishi miaka
969 (mia tisa sitini na tisa)
Mwanzo 5:22-27 “Henoko akaenda pamoja na Mungu baada ya kumzaa Methusela
miaka mia tatu, akazaa wana, waume na wake. Siku zote za Henoko ni miaka mia
tatu na sitini na mitano. Henoko akaenda pamoja na Mungu, naye akatoweka, maana
Mungu alimtwaa. Methusela akaishi miaka mia na themanini na saba, akamzaa
Lameki. Methusela akaishi baada ya kumzaa Lameki miaka mia saba na themanini na
miwili, akazaa wana, waume na wake. Siku zote za Methusela ni miaka mia kenda
na sitini na kenda, akafa.”
Hata hivyo maisha ya mwanadamu
siku za leo yamekuwa mafupi zaidi kama maua au majani au mvuke, japokuwa kila
mwanadamu anatamani kuishi milele, Kwa msingi huo haijalishi mwanadamu ataishi
muda mrefu kiasi gani bado maisha hayo ni mafupi kwa nini kwa sababu maandiko
yanasema pia yanaenda kwa kasi sana yaani kama kivuli, kwa hiyo maisha haya
hayatoshi, bado uko uhitaji wa maisha ya milele, na ndio maana Mungu katika
hekima yake alituumba tuishi milele na kwa sababu hiyo kila mwanadamu kwaasili
hapendi kifo milele iko katika mioyo yetu.
Muhubiri 3:11-14 “Kila kitu amekifanya
kizuri kwa wakati wake; tena ameiweka hiyo milele ndani ya mioyo yao; ila kwa
jinsi mwanadamu asivyoweza kuivumbua kazi ya Mungu anayoifanya, tangu mwanzo
hata mwisho. Mimi najua ya kwamba hakuna jema kwao kupita kufurahi, na kufanya
mema maadamu wanaishi. Tena ni karama ya Mungu kila mtu apate kula na kunywa,
na kujiburudisha kwa mema katika kazi yake yote. Najua ya kwamba kila kazi
aifanyayo Mungu itadumu milele; haiwezekani kuizidisha kitu, wala kuipunguza
kitu; nayo Mungu ameifanya ili watu wamche Yeye.”
Kwa nini tunajifunza somo hili?
Kujikumbusha ufupi wa siku zetu sio kitu kibaya kwani kunatupa hekima ya kujua
namna ya kuishi kwa Amani na kutumia siku zetu kwa hekima tuwapo hapa duniani Zaburi 90:12 “Basi,
utujulishe kuzihesabu siku zetu, Tujipatie moyo wa hekima.” Kwa hiyo
somo hili lina baadhi ya mwaswala Muhimu yanayotuongoza jinsi na na mna ya
kuzitumia siku zetu chache duniani kwa hekima, uchahce huu pia unachangiwa na
kuwa zinapita haraka sana hata kama utaishi miaka mia, bado utaona ni kama
zimepita haraka sana, Na kule kujifunza somo hili hakuna uhusiano wowote na
unabii wa kifo cha mtu hapa, hapana ni kwaajili ya kuishi maisha mazuri tuwapo
duniani!. Tutajifunza somo hili
Mwanadamu siku zake zi kama majani kwa kuzingatia vipengele viwili vifuatavyo:-
·
Mwanadamu
siku zake zi kama majani
·
Jinsi ya
kutumia muda tuliopewa Duniani
Mwanadamu siku zake zi kama majani.
Moja ya mifano ya asili
inayoonyesha ufupi wa maisha ya Mwanadamu ni pamoja na majani na maua katika
miti na mimea ya kondeni, majani na maua huishi kwa muda mfupi sana na ndio
maana utaweza kuona katika maandiko majani na maua yakitumiwa kama mfano halisi
au mfano hai wa kufananisha maisha mafupi ya mwanadamu
1Petro 1:24 “Maana, Mwili wote ni kama
majani, Na fahari yake yote ni kama ua la majani. Majani hukauka na ua lake
huanguka;”
Kwa msingi huo maandiko yanatumia
majani na maua kama mfano wa asili wa kuonyesha kitu kinachodumu kwa muda mfupi
zaidi. Kwa kiyunani kitu kinachodumu kwa muda mfupi zaidi kinaitwa Ephemeral Neno hilo Ephemeral kwa kiyunani yaani Greek ni Muunganiko wa maneno mawili EPI na HEMEROS, EPI kwa kiingereza
maana yake ni Upon or For na HEMEROS kwa
kiingereza maana yake ni Day kwa
hiyo neno Ephemeral maana yake ni “For a day” “kwa siku tu” ikiwa na
maana kitu kinachoishi kwa muda mfupi sana. Ephemeral is something that lasting for a very short time yaani ni
kama mwendo wa kivuli cha jua, Kwa hiyo Ephemeral
maana yake ni kitu kinachoishi kwa muda mfupi sana! Kama majani, au kama maua, na pia kinachopita kwa kasi sana kama
kivuli!
Zaburi 102:11-12 “Siku zangu zi kama kivuli
kilichotandaa, Nami ninanyauka kama majani. Bali Wewe, Bwana utaketi ukimiliki
milele, Na kumbukumbu lako kizazi hata kizazi.”
Ayubu 14:1-2 “Mwanadamu aliyezaliwa na
mwanamke Siku zake za kuishi si nyingi, naye hujaa taabu. Yeye huchanua kama
vile ua, kisha hukatwa; Hukimbia kama kivuli, wala hakai kamwe.”
Muhubiri 6:12 “Kwa maana ni nani ajuaye
yaliyo mema ya mwanadamu katika maisha yake, siku zote za maisha yake ya
ubatili, anayoishi kama kivuli? Kwa maana ni nani awezaye kumweleza mwanadamu
mambo yatakayofuata baada yake chini ya jua? ”
Zaburi 39:4-6 “Bwana, unijulishe mwisho
wangu, Na kiasi cha siku zangu ni kiasi gani; Nijue jinsi nilivyo dhaifu.
Tazama, umefanya siku zangu kuwa mashubiri; Maisha yangu ni kama si kitu mbele
zako. Kila mwanadamu, ingawa amesitawi, ni ubatili.Binadamu huenda tu huko na huko
kama kivuli; Hufanya ghasia tu kwa ajili ya ubatili; Huweka akiba wala hajui ni
nani atakayeichukua.”
Kwa hiyo katika mtazamo wa
kifalsafa, maisha ya mwanadamu hutazamwa kuwa mafupi sana bila kujali mtu
ameishi maisha ya miaka mingapi hapa duniani, hii inathibitisha ukweli ya kuwa
tunapaswa kujua namna na jinsi ya kutumia wakati wetu huu mfupi tulio nao kwa
busara zaidi sana tukijifunza kuacha majivuno na maringo kwa sababu zozote.
Zaburi 90:10-12 “Siku za miaka yetu ni
miaka sabini, Na ikiwa tuna nguvu miaka themanini; Na kiburi chake ni taabu na
ubatili, Maana chapita upesi tukatokomea mara. Ni nani aujuaye uweza wa hasira
yako? Na ghadhabu yako kama ipasavyo kicho chako? Basi, utujulishe kuzihesabu
siku zetu, Tujipatie moyo wa hekima.”
Jinsi ya kutumia muda tuliopewa Duniani
Tunawezaje kutumia kwa busara
muda huu mfupi sana tuliopewa duniani? Ili kutumia muda huu vema tunapaswa
kufikiri katika maana nzima kuhusu maisha na kulenga kutimiza kusudi kuu la
maisha tulilopewa na Mungu, Maisha ni dhamana kwa hiyo:-
1.
Ishi
sawa na kusudi la Mungu - Tambua ni jambo gani la Muhimu duniani ambalo
Mungu anataka ulifanye?, Mungu alikuumba ili iweje? Mungu amekuleta ufanye
nini? Ukiisha kutambua simamia katika siku zako zote za kuishi, kumbuka kila
mwanadamu hapa duniani ana kusudi lake ambalo Mungu amemkusudia kulifanya basi
kaa katika kusudi hilo, huku ukihakikisha unadumisha uhusiano wako na Mungu
mapema!
Mhubiri 12:1-7 “Mkumbuke
Muumba wako siku za ujana wako, Kabla hazijaja siku zilizo mbaya, Wala
haijakaribia miaka utakaposema, Mimi sina furaha katika hiyo.Kabla jua, na
nuru, na mwezi, Na nyota, havijatiwa giza; Kabla ya kurudi mawingu baada ya
mvua; Siku ile walinzi wa nyumba watakapotetema; Hapo wenye nguvu
watakapojiinamisha; Na wasagao kukoma kwa kuwa ni haba; Na hao wachunguliao
madirishani kutiwa giza; Na milango kufungwa katika njia kuu; Sauti ya kinu
itakapokuwa ni ndogo; Na mtu kusituka kwa sauti ya ndege; Nao binti za kuimba
watapunguzwa; Naam, wataogopa kilichoinuka Na vitisho vitakuwapo njiani; Na mlozi
utachanua maua; Na panzi atakuwa ni mzigo mzito; Na pilipili hoho itapasuka;
Maana mtu aiendea nyumba yake ya milele, Nao waombolezao wazunguka njiani.
Kabla haijakatika kamba ya fedha; Au kuvunjwa bakuli la dhahabu; Au mtungi
kuvunjika kisimani; Au gurudumu kuvunjika birikani; Nayo mavumbi kuirudia nchi
kama yalivyokuwa, Nayo roho kumrudia Mungu aliyeitoa.”
Kumkumbuka Mungu
maana yake ni kulitumikia kusudi la Mungu au kutumikia shauri la Mungu yaani
kufanya kile ambacho Mungu amateka tukifanye katika maisha yetu na kubwa zaidi
tukiwatumikia watu na kuacha alama katika maisha yao, na moyo wa Mungu baba
yetu aliyetuumba. Utatufurahia
Matendo 13:36 “Kwa
maana Daudi, akiisha kulitumikia shauri la Mungu katika kizazi chake, alilala,
akawekwa pamoja na baba zake, akaona uharibifu.”
2.
Tengeneza
mahusiano mazuri – Ni muhimu katika maisha haya kuwekeza katika mahusiano,
usiwe na maadui wala uadui na mtu wala usiwe na uadui na Mungu na watu, Neno la
Mungu linatutaka tuwe na mahusiano mema na watu wote lakini na Mungu pia, Neno
la Mungu limekazia sana uhusiano mwema, baba zetu wa Imani Ibrahimu na Isaka na
Yakobo wakati wote katika maisha yao walitafuta amani kwa bidii hata baada ya
kufanya makosa makubwa sana ya kibinadamu walitafuta Amani!
Waebrania 12:14 “Tafuteni
kwa bidii kuwa na amani na watu wote, na huo utakatifu, ambao hapana mtu
atakayemwona Bwana asipokuwa nao;”
Marko 12:29-31 “Yesu
akamjibu, Ya kwanza ndiyo hii, Sikia, Israeli, Bwana Mungu wetu ni Bwana mmoja;
nawe mpende Bwana Mungu wako kwa moyo wako wote, na kwa roho yako yote, na kwa
akili zako zote, na kwa nguvu zako zote. Na ya pili ndiyo hii, Mpende jirani
yako kama nafsi yako. Hakuna amri nyingine iliyo kuu kuliko hizi.”
1Yohana 2:9-11 “Yeye
asemaye kwamba yumo nuruni, naye amchukia ndugu yake, yumo gizani hata sasa.
Yeye ampendaye ndugu yake, akaa katika nuru, wala ndani yake hamna kikwazo.
Bali yeye amchukiaye ndugu yake, yu katika giza, tena anakwenda katika giza,
wala hajui aendako, kwa sababu giza imempofusha macho.”
Wekeza katika
ujenzi wa uhusiano mzuri kwa familia ndugu, jamaa na marafiki na katika jamii,
tengeneza mtandao mwema wa uhusiano mzuri, tia moyo watu, furahisha watu, jenga
jamii, onyesha kujihusisha. Salimia majirani, jichanganye katika jamii,
jihusishe katika harusi zao, kama una nafasi na katika misiba yao nafasi
ikiruhusu, sema na watu vizuri, cheka na watu vizuri hata wasipokutendea mema
usijali wewe tenda, cheka na wanaocheka na lia na wanaolia, usiwe na maadui,
uwe rafiki wa kila mtu na wa kila rika!
3.
Jaa
shukurani – iweni watu wa shukurani, shukuru kwa kila jambo liwe kubwa au
dogo na lolote lile ambalo ulimwengu unatoa
1Thesalonike 5:18 “shukuruni
kwa kila jambo; maana hayo ni mapenzi ya Mungu kwenu katika Kristo Yesu.”
Zaburi 106:1, “Haleluya.
Mshukuruni Bwana kwa kuwa ni mwema, Kwa maana fadhili zake ni za milele.”
Zaburi 100:4 “Ingieni
malangoni mwake kwa kushukuru; Nyuani mwake kwa kusifu; Mshukuruni, lihimidini
jina lake;”
Wakolosai 3:15 “Na
amani ya Kristo iamue mioyoni mwenu; ndiyo mliyoitiwa katika mwili mmoja; tena
iweni watu wa shukrani.”
4.
Tia
moyo ustawi – wakati wote hakikisha kuwa ustawi unakuwa, yaani wakati wote
ongeza maarifa, ongeza ujuzi na mbinu mbalimbali za kuhakikisha unakua katika
kutafuta mbinu za kujiongeza kiimani, kiuchumi na kimaisha !
Luka 2:40-52 “Yule
mtoto akakua, akaongezeka nguvu, amejaa hekima, na neema ya Mungu ilikuwa juu
yake. Basi, wazee wake huenda Yerusalemu kila mwaka, wakati wa sikukuu ya
Pasaka.Na alipopata umri wake miaka kumi na miwili, walipanda kama ilivyokuwa
desturi ya sikukuu; na walipokwisha kuzitimiza siku, wakati wa kurudi kwao,
yule mtoto Yesu alibaki nyuma huko Yerusalemu, na wazee wake walikuwa hawana
habari. Nao wakadhani ya kuwa yumo katika msafara; wakaenenda mwendo wa kutwa,
wakawa wakimtafuta katika jamaa zao na wenzao; na walipomkosa, wakarejea
Yerusalemu, huku wakimtafuta. Ikawa baada ya siku tatu wakamwona hekaluni,
ameketi katikati ya waalimu, akiwasikiliza na kuwauliza maswali. Nao wote
waliomsikia walistaajabia fahamu zake na majibu yake. Na walipomwona
walishangaa, na mama yake akamwambia, Mwanangu, mbona umetutenda hivi? Tazama,
baba yako na mimi tulikuwa tukikutafuta kwa huzuni. Akawaambia, Kwani
kunitafuta? Hamkujua ya kuwa imenipasa kuwamo katika nyumba ya Baba yangu? Nao
hawakuelewa na neno hilo alilowaambia. Akashuka pamoja nao mpaka Nazareti, naye
alikuwa akiwatii; na mamaye aliyaweka hayo yote moyoni mwake. Naye Yesu akazidi
kuendelea katika hekima na kimo, akimpendeza Mungu na wanadamu.”
1Nyakati 4:9-10 “Naye
Yabesi alikuwa mwenye heshima kuliko nduguze; na mamaye akamwita jina lake
Yabesi, akisema, Ni kwa sababu nalimzaa kwa huzuni. Huyo Yabesi akamlingana
Mungu wa Israeli, akisema, Lau kwamba ungenibarikia kweli kweli, na
kunizidishia hozi yangu, na mkono wako ungekuwa pamoja nami, nawe ungenilinda
na uovu, ili usiwe kwa huzuni yangu! Naye Mungu akamjalia hayo aliyoyaomba.”
5.
Ni
heri kutoa kuliko kupokea – hakikisha ya kuwa unajitoa kwaajili ya wengine,
fanikisha maisha ya wengine, furahia mafanikio ya wengine, rudisha katika jamii,
Kwa matendo ya ukarimu, na utu wema, weka misingi ya kudumu kuwa mwema katika
jamii yako kwa kadiri Mungu alivyokubariki utakumbukwa Daima na Mungu na watu
pia.
Matendo 20:34-35 “Ninyi
wenyewe mnajua ya kuwa mikono yangu hii imetumika kwa mahitaji yangu na ya wale
waliokuwa pamoja nami. Katika mambo yote nimewaonyesha ya kuwa kwa kushika kazi
hivi imewapasa kuwasaidia wanyonge, na kuyakumbuka maneno ya Bwana Yesu, jinsi
alivyosema mwenyewe, Ni heri kutoa kuliko kupokea.”
Matendo 9:36-41 “Na
mwanafunzi mmoja alikuwako Yafa, jina lake Tabitha, tafsiri yake ni Dorkasi
(yaani paa); mwanamke huyu alikuwa amejaa matendo mema na sadaka alizozitoa.
Ikawa siku zile akaugua, akafa; hata walipokwisha kumwosha, wakamweka orofani.
Na kwa kuwa mji wa Lida ulikuwa karibu na Yafa, nao wanafunzi wamesikia ya
kwamba Petro yuko huko, wakatuma watu wawili kwake, kumsihi na kusema, Usikawie
kuja kwetu. Petro akaondoka akafuatana nao. Alipofika, wakampeleka juu orofani
wajane wote wakasimama karibu naye, wakilia na kumwonyesha zile kanzu na nguo
alizozishona Dorkasi wakati ule alipokuwa pamoja nao. Petro akawatoa nje wote,
akapiga magoti, akaomba, kisha akaelekea yule maiti, akanena, Tabitha, ondoka.
Naye akafumbua macho yake, na alipomwona Petro akajiinua, akaketi. Akampa
mkono, akamwinua; hata akiisha kuwaita wale watakatifu na wajane akamweka mbele
yao, hali yu hai.”
Matendo 10:1-8 “Palikuwa
na mtu Kaisaria, jina lake Kornelio, akida wa kikosi kilichoitwa Kiitalia, mtu
mtauwa, mchaji wa Mungu, yeye na nyumba yake yote, naye alikuwa akiwapa watu
sadaka nyingi, na kumwomba Mungu daima. Akaona katika maono waziwazi, kama saa
tisa ya mchana, malaika wa Mungu, akimjia na kumwambia, Kornelio! Akamtazama
sana, akaogopa akasema, Kuna nini, Bwana? Akamwambia, Sala zako na sadaka zako
zimefika juu na kuwa ukumbusho mbele za Mungu. Sasa basi, peleka watu Yafa,
ukamwite Simoni, aitwaye Petro. Yeye ni mgeni wa mtu mmoja, jina lake Simoni,
mtengenezaji wa ngozi, ambaye nyumba yake iko pwani, atakuambia yakupasayo
kutenda. Na yule malaika aliyesema naye akiisha kuondoka, Kornelio akawaita
wawili katika watumishi wake wa nyumbani, na askari mmoja, mtu mtauwa katika
wale waliomhudumia daima; na alipokwisha kuwaeleza mambo yote akawatuma kwenda
Yafa.”
6.
Yafikirie
yaliyo juu
Ni muhimu
kufikiria kuhusu mambo yajayo, yanayohusiana na uzima wa milele, hata kama
tutakuwa tumebarikiwa kwa kiasi gani tukiwa hapa duniani hii isiwe sababu ya
kupoteza urafiki wetu na Mungu, Mafanikio yasikutoe katika kufikiri kuhusu
Mungu na maswala ya milele!, Mche Mungu, fanya kila kitu huku ukijali sana
maswala ya maisha ya milele usiyapuuzikie, watu wenye akili ni wale wanaomcha
Mungu!
Mwanzo 13:2 “Naye
Abramu alikuwa ni tajiri sana kwa mifugo, kwa fedha, na kwa dhahabu.”
Waebrania 11:10 “Maana
alikuwa akiutazamia mji wenye misingi, ambao mwenye kuubuni na kuujenga ni
Mungu.”
Wakolosai 3:1-4 1. “Basi mkiwa mmefufuliwa pamoja na Kristo, yatafuteni yaliyo juu Kristo
aliko, ameketi mkono wa kuume wa Mungu. Yafikirini yaliyo juu, siyo yaliyo
katika nchi. Kwa maana mlikufa, na uhai wenu umefichwa pamoja na Kristo katika
Mungu. Kristo atakapofunuliwa, aliye uhai wetu, ndipo na ninyi mtafunuliwa
pamoja naye katika utukufu.”
Yakobo 4:13-16 “Haya
basi, ninyi msemao, Leo au kesho tutaingia katika mji fulani na kukaa humo
mwaka mzima, na kufanya biashara na kupata faida; walakini hamjui
yatakayokuwako kesho. Uzima wenu ni nini? Maana ninyi ni mvuke uonekanao kwa
kitambo, kisha hutoweka. Badala ya kusema, Bwana akipenda, tutakuwa hai na
kufanya hivi au hivi. Lakini sasa mwajisifu katika majivuno yenu; kujisifu kote
kwa namna hii ni kubaya.”
Luka 12:16-21 “Akawaambia
mithali, akisema, Shamba la mtu mmoja tajiri lilikuwa limezaa sana; akaanza
kuwaza moyoni mwake, akisema, Nifanyeje? Maana sina pa kuyaweka akiba mavuno
yangu. Akasema, Nitafanya hivi; nitazivunja ghala zangu, nijenge nyingine kubwa
zaidi, na humo nitaweka nafaka yangu yote na vitu vyangu. Kisha, nitajiambia,
Ee nafsi yangu, una vitu vyema vingi ulivyojiwekea akiba kwa miaka mingi;
pumzika basi, ule, unywe, ufurahi. Lakini Mungu akamwambia, Mpumbavu wewe,
usiku huu wa leo wanataka roho yako! Na vitu ulivyojiwekea tayari vitakuwa vya
nani? Ndivyo alivyo mtu ajiwekeaye nafsi yake akiba, asijitajirishe kwa Mungu.”
7.
Tunza
afya yako - Ni muhimu sana pia kuhakikisha unatunza afya yako, Afya ya
mwili akili na roho yako, hatuwezi kufurahia maisha yote ya kimwili na kiroho
kama hatutatunza afya zetu, hili ni jambo la muhimu sana !
3Yohana 1:2 “Maana
nalifÄrahi mno walipokuja ndugu na kuishuhudia kweli yako, kama uendavyo katika
kweli.”
1Wakorintho 6:19-20 “Au hamjui ya kuwa mwili wenu ni hekalu la Roho Mtakatifu
aliye ndani yenu, mliyepewa na Mungu? Wala ninyi si mali yenu wenyewe; maana
mlinunuliwa kwa thamani. Sasa basi, mtukuzeni Mungu katika miili yenu.”
8.
Ishi
kwa kiasi - Maisha yanahitaji
uwiano, yaani kiasi, jaribu kuweka kila kitu katika kiasi ridhika, Neno kiasi katika maandiko ya kiingereza ni Soberly au Modarate na katika kiyunani ni Sophronos ambalo
maana yake ni Self possessed/Self
control yaani kujidhibiti, au kujikana nafsi kwa hiyo ni muhimu kuwa na
kiasi ni muhimu kujidhibiti, usipitilize mipaka katika kila jambo ulifanyalo
Tito 2:11-12 “Maana
neema ya Mungu iwaokoayo wanadamu wote imefunuliwa; nayo yatufundisha kukataa
ubaya na tamaa za kidunia; tupate kuishi kwa kiasi, na haki, na utauwa, katika
ulimwengu huu wa sasa;”
Hitimisho:
Tukijikita
katika mambo hayo hapo juu tutajikuta tunaishi katika utoshelevu, unaotengeneza
maana kamili ya maisha bila kujali urefu au ufupi wa maisha yenyewe!
Na. Rev. Innocent Samuel Kamote
Mkuu wa wajenzi mwenye Hekima!