Jumapili, 7 Septemba 2025

Chembe ya ngano isipoanguka!


Yoahana 12:23-25 “Naye Yesu akawajibu, akasema, Saa imefika atukuzwe Mwana wa Adamu. Amin, amin, nawaambia, Chembe ya ngano isipoanguka katika nchi, ikafa, hukaa hali iyo hiyo peke yake; bali ikifa, hutoa mazao mengi. Yeye aipendaye nafsi yake ataiangamiza; naye aichukiaye nafsi yake katika ulimwengu huu ataisalimisha hata uzima wa milele.”



Utangulizi:

Leo tunachukua muda kiasi kutafakari maneno ya Bwana wetu Yesu Kristo aliyoyasema karibu na mwishoni kabisa mwa huduma yake Duniani, Yesu alikuwa ametembelewa na kundi kubwa la jamii ya watu wasiokuwa wayahudi, yaani Wayunani ambao kimsingi nao walikuwa na kiu na hamu na shauku ya kupata huduma ya Bwana wetu Yesu Kristo, Yesu anaiona shauku yao kama hitaji kubwa sana la kiroho kwa jamii ya watu wote duniani kama watu wanaomuhitaji Mungu na Mwokozi katika maisha yao, Hata hivyo kuhudumia jamii ya watu wote duniani kwa vyovyote vile kungemlazimu kutimiza mapenzi ya Mungu ya kufa msalabani ili aweze kuwa fidia ya wengi kama yanenavyo maandiko:-

Yohana 3:16 “Kwa maana jinsi hii Mungu aliupenda ulimwengu, hata akamtoa Mwanawe pekee, ili kila mtu amwaminiye asipotee, bali awe na uzima wa milele.”

Luka 2:34-35 “Simeoni akawabariki, akamwambia Mariamu mama yake, Tazama, huyu amewekwa kwa kuanguka na kuinuka wengi walio katika Israeli, na kuwa ishara itakayonenewa. Nawe mwenyewe, upanga utaingia moyoni mwako, ili yafunuliwe mawazo ya mioyo mingi.”

Akifafanua juu ya mauti yake huku akiunganisha na mafundisho yahusuyo kujikana nafsi, Yesu anatumia mfano wa wakulima wa ngano ili kufafanua kanuni ya kiroho ya kuleta mafanikio na kuzaa matunda mengi inavyogharimu maisha ya waanzilishi ili kuleta uzima kwa wengi au kwa ulimwengu na ndipo anapotumia mfano wa Chembe ya ngano (Yaani mbegu ya ngano) kwamba ili iweze kutoa mazao mengi ni lazima ife na kuzikwa na inapoota yaani kufufuka inasababisha mazao mengi sana.

Tutajifunza ujumbe huu Chembe ya ngano isipoanguka kwa kuzingatia vipengele vitatu vifuatavyo;-


·         Maana ya kuanguka kwa chembe ya ngano.

·         Chembe ya ngano isipoanguka!.

·         Faida za kuanguka kwa chembe ya ngano.


Maana ya kuanguka kwa chembe ya ngano.

Ni muhimu kufahamu kuwa Pamoja na ukulima wa zabibu, ufugaji wa wanyama wa aina mbalimbali,kama kondoo, mbuzi na ng’ombe, watu wa mashariki ya kati hususani Israel na baadhi ya waarabu ni watumiaji wazuri sana wa ngano kwaajili ya chakula na hasa mikate, sasa ili Yesu aweze kueleweka vizuri katika jamii yake alitumia mifano ya vitu vya karibu na vilivyozoeleka katika jamii yake ili aweze kuwasilisha ujumbe wa kiroho wenye maana inayoeleweka kwa watu wake, Yesu hapa anatumia mfano wa chembe ya ngano (yaani mbegu ya ngano) ambayo ili iweze kuzaa matunda mengi zaidi hutupwa au kuzikwa shambani na kisha inakufa katika udongo au ardhini na inapofufuka/kuota kama mmea na kuzaa inazalisha matunda au mbegu nyingine bora zaidi hii ndio kanuni ya kilimo.

Yohana 12:24 “Amin, amin, nawaambia, Chembe ya ngano isipoanguka katika nchi, ikafa, hukaa hali iyo hiyo peke yake; bali ikifa, hutoa mazao mengi.”

·         Chembe ya ngano kwa kiyunani (Greek) inaitwa “ho kokkos tou sitou” kwa kiingereza “a grainof wheat”  ikimaanisha mbegu ya ngano

·         Kuanguka  kwa kiyunani (Greek) linatumika neno Piptō linalomaanisha kuanguka chini kwa hiyari, au kuangushwa kwa kusudi au kupanda

·         Kufa  kwa kiyunani (Greek) linatumika neno apothnēskō linalomaanisha kufa kimwili au kufa kwa hiyari yaani kwa kiingereza “Self- denial” “Self-sacrificial” kujitoa dhabihu, kujikana au kujikataa au kujitoa sadaka.

Waebrania katika mtazamo wao kuhusu mbegu siku zote waliamini ndani ya mbegu kua kuna UZIMA, URITHI, na KIZAZI, walikuwa wanatambua kuwa uhai hauwezi kuendelea bila ya kuwako kwa mbegu, lakini ili mbegu iweze kuendeleza uhai na uzima na urithi na kizazi ni lazima mbegu hiyo itolewe kutoka kwenye kuhifadhiwa na itupwe katika moyo wa ardhi, kisha ife na izikwe na kuchipuka ndipo iweze kuendeleza kizazi kwa hiyo mbegu katika mukthadha wa wayahudi inaitwa ZERA ikimaanisha UZAO 

Mwanzo 22:12-18 “Malaika wa BWANA akamwita Ibrahimu mara ya pili kutoka mbinguni akasema, Nimeapa kwa nafsi yangu asema BWANA, kwa kuwa umetenda neno hili, wala hukunizuilia mwanao, mwanao wa pekee, katika kubariki nitakubariki, na katika kuzidisha nitauzidisha uzao wako kama nyota za mbinguni, na kama mchanga ulioko pwani; na uzao wako utamiliki mlango wa adui zao; na katika uzao wako mataifa yote ya dunia watajibarikia; kwa sababu umetii sauti yangu.”

Yesu alikuwa anatambua kwamba ni lazima ajidhabihu yeye mwenyewe kwaajili ya kuufikia ulimwengu, alifahamu wazi kuwa yeye hakuja kwaajili ya wayahudi pekee, bali alikuja kwaajili ya ulimwengu mzima, alifahamu kuwa anahitajika sio na wayunani pekee bali na ulimwengu mzima na kwa sababu hiyo, kujidhabihu kwaajili ya ulimwengu mzima kungerahisisha ukombozi utakaozaa matunda kwa Mungu wetu yaliyo mengi, Lakini wakati huo huo Yesu aliwataka wanafunzi wake wote ikiwa ni pamoja na wewe na mimi kuwa na ufahamu ya kuwa maisha ya uanzilishi wa kitu chchote yanahusisha kujitoa na kujidhabihu na matunda yake yangelikuja kuonekana mbeleni!, Yeye kama Uzao wa Ibrahimu ilikuwa ni lazima ajitoe sadaka yeye mwenyewe kwa hiyari ili mataifa yote waweze kubarikiwa

Tito 2:11-14 “Maana neema ya Mungu iwaokoayo wanadamu wote imefunuliwa; nayo yatufundisha kukataa ubaya na tamaa za kidunia; tupate kuishi kwa kiasi, na haki, na utauwa, katika ulimwengu huu wa sasa; tukilitazamia tumaini lenye baraka na mafunuo ya utukufu wa Kristo Yesu, Mungu mkuu na Mwokozi wetu; ambaye alijitoa nafsi yake kwa ajili yetu, ili atukomboe na maasi yote, na kujisafishia watu wawe milki yake mwenyewe, wale walio na juhudi katika matendo mema.”

Waefeso 5:1-2 “Hivyo mfuateni Mungu, kama watoto wanaopendwa; mkaenende katika upendo, kama Kristo naye alivyowapenda ninyi tena akajitoa kwa ajili yetu, sadaka na dhabihu kwa Mungu, kuwa harufu ya manukato.”

Maandiko hayo yanadhihirisha wazi kuwa kusulubiwa kwa Yesu Kristo halikuwa tukio la kupangwa na wazee na wakuu wa makuhani, lakini lilikuwa ni tukio la Yesu Kristo mwenyewe kujidhabihu na kukubali kufa na kufufuka kutoka kwa wafu ili atukomboe wanadamu, Yeye alikuwa  ni chembe ya ngano ambayo ilikuwa lazima ianguke ili kusababisha mazao mengi sana duniani.                      

Chembe ya ngano isipoanguka!.

Yoahana 12:23-25 “Naye Yesu akawajibu, akasema, Saa imefika atukuzwe Mwana wa Adamu. Amin, amin, nawaambia, Chembe ya ngano isipoanguka katika nchi, ikafa, hukaa hali iyo hiyo peke yake; bali ikifa, hutoa mazao mengi. Yeye aipendaye nafsi yake ataiangamiza; naye aichukiaye nafsi yake katika ulimwengu huu ataisalimisha hata uzima wa milele.”

Yesu anatumia msemo huu  wa chembe yaani mbegu ya ngano kama mfano (Metaphor)  kuonyesha kuwa mbegu ili iweze kuleta mavuno mengi sana ni lazima ianguke, izikwe ardhini kisha inapochipuka yaani kuota na kustawi inaleta mavuno makubwa sana, kanuni hii ni kanuni ya kilimo lakini ni kanuni ya kiroho na kanuni ya kawaida katika maisha.

Yesu anaonyesha kuwa wakati mwingine ili mtu aweze kuzaa matunda, hakuna budi watu wajikane nafsi na kujidhabihu kama yeye, lakini sio hivyo tu kuishi maisha ya kumfuata Yesu na kumpendeza vile vile kunahitaji kujikana nafsi, Ni lazima ujikane ili uweze kuishi maisha matakatifu nay a mfano, bila kujikana ni ngumu kuona mazao

Luka 9:22-25 “akisema, Imempasa Mwana wa Adamu kupata mateso mengi, na kukataliwa na wazee na wakuu wa makuhani na waandishi, na kuuawa na siku ya tatu kufufuka. Akawaambia wote, Mtu ye yote akitaka kunifuata, na ajikane mwenyewe, ajitwike msalaba wake kila siku, anifuate. Kwa kuwa mtu atakaye kuiponya nafsi yake ataiangamiza, na mtu atakayeiangamiza nafsi yake kwa ajili yangu ndiye atakayeisalimisha. Kwa kuwa yamfaa nini mtu kuupata ulimwengu wote, kama akijiangamiza, au kujipoteza mwenyewe?

Chembe ya ngano isipoanguka hakuna lolote linaloweza kutokea, watu wasipojidhabihu na kujioa hakuwezi kutokea mabadiliko yoyote chanya katika jamii, mambo mengi tunayoyaona duniani na kuyafurahia wakati mwingine yamegharimu maisha ya watu wengine lakini wengi wanafaidika leo kutokana na kuumia kwa watu wengine, hususani waanzilishi wa mambo, Imani, mataifa, ustawi, uanzishwaji wa taasisi yoyote ile, upatikanaji wa Amani na kadhalika, huwa haviwezi kupata usitawi bila watu kujikana, kujiyoa na kujidhabihu, maisha ya kujitoa kwaajili ya jamii yanaweza kuumiza wachache lakini yakanufaisha wengi, Leo hii tunaushangilia wokovu na kujivunia lakini yaligharimu maisha ya Mwana wa Mungu, Yesu Kristo aligharimika pale msalabani na kwa kupigwa kwake tumepona

Marie Curie ambaye ni mgunduzi wa tiba ya kutumia mionzi (Radiation in Medicine) alifariki dunia tarehe 04 Julai 1934 huko ufaransa akiwa na miaka 66, Mwanamke huyu aliyekuwa mwanasayansi alihatarisha maisha yake hata kufa baada ya kuathiriwa na mionzi hiyo alipokuwa anafanya kazi za kitafiti na matumizi ya tiba ya mionzi ya (radium and Plonium) ambayo leo imekuwa msaada mkubwa sana katika tiba ya kiuchunguzi ya mionzi kama X-Rays

Katika maisha wakati mwingine mambo hayawezi kutokea mpaka watu wengine wamesimama kidete na kuhatarisha maisha yao au hata kufa kwaajili ya kusababisha mabadiliko yatokee, Mahatma Gandhi alijitoa maisha yake kusababisha nchi ya India kupata uhuru wake  kutoka kwa waingereza akianzisha harakati za kuandamana bila kufanya ghasia, akivumilia vifungo mbalimbali na hata wakati mwingine aliacha kula yaani akifunga na kujinyima ili haki za kibinadamu zipatikane  katika India inayofurahia matunda ya uhuru huo leo.

Wakristo, na watumishi wa Mungu katika mazingira mbalimbali, tunapaswa kuelewa Yesu alikuwa anamaanisha kwamba bila wengine kujitoa muhanga, maisha yao, fedha zao, starehe zao, mifungo yao, kesha zao, maisha ya familia zao, haki, na injili haiwezi kuwafikia watu wa Mungu, umasikini hauwezi kuondoka, unyonge hauwezi kuisha, ukandamizwaji hauwezi kukomeshwa, udhalimu hauwezi kutokomea, maovu yataendelea kuongezeka, amani haiwezi kupatikana, ubaguzi hauwezi kuisha, upendeleo hauwezi kuisha, haki haiwezi kupatikana, na uhuru wa kweli hauwezi kupatikana bila baadhi ya watu kujitoa dhabihu yaani  Chembe ya ngano isipoanguka! Inabakia ile ile!

Faida za kuanguka kwa chembe ya ngano.

Kuanguka kwa chembe ya ngano ni kujitoa au kujidhabihu kwaajili ya Mungu, Neno la Mungu linatueleza kuwa kujitoa ndio dhabihu iliyo hai, takatifu na ya kupendeza, kama mtu anataka kumpendeza Mungu basi ni lazima akubali kujitoa, au kujidhabihu, Kwa nini Mungu alipendezwa na Yesu Kristo hata kujivunia kuwa huyu ndiye mwanangu mpendwa ninayependezwa naye? Sababu kubwa ni kuwa Yesu alijitoa yeye mwenyewe

Warumi 12:1 “Basi, ndugu zangu, nawasihi, kwa huruma zake Mungu, itoeni miili yenu iwe dhabihu iliyo hai, takatifu, ya kumpendeza Mungu, ndiyo ibada yenu yenye maana.”

Wafilipi 2:6-11 “ambaye yeye mwanzo alikuwa yuna namna ya Mungu, naye hakuona kule kuwa sawa na Mungu kuwa ni kitu cha kushikamana nacho; bali alijifanya kuwa hana utukufu, akatwaa namna ya mtumwa, akawa ana mfano wa wanadamu; tena, alipoonekana ana umbo kama mwanadamu, alijinyenyekeza akawa mtii hata mauti, naam, mauti ya msalaba. Kwa hiyo tena Mungu alimwadhimisha mno, akamkirimia Jina lile lipitalo kila jina; ili kwa jina la Yesu kila goti lipigwe, la vitu vya mbinguni, na vya duniani, na vya chini ya nchi; na kila ulimi ukiri ya kuwa YESU KRISTO NI BWANA, kwa utukufu wa Mungu Baba.”

Mwanafunzi wa kweli wa Yesu Kristo ni yule anayejitoa, unapodai kuwa unamfuata Yesu lakini hujitoi maana yake ni sawa na kuwa hauufuati mfano wake, Yeye mwenyewe anamkana kila mtu anayedai kuwa anamfuata yeye lakini hataki kuteseka kwaajili ya Kristo! Kimsingi huwezi kuwa mwanafunzi wa Yesu kama hutaki kugharimika na kumfuata

Luka 14:27 “Mtu ye yote asiyeuchukua msalaba wake na kuja nyuma yangu, hawezi kuwa mwanafunzi wangu.”

Kila anayejikana kwaajili ya Yesu Kristo na jamii nafsi yake haitapotea kwani atalipwa uzima wa milele, tunapojitoa na kujidhabihu hata kufa kwaajili ya wengine/kifo au mauti yako inayotokana na kujidhabihu haiwi mwisho badala yake unakuwa mwanzo wa uzima na maisha mapya yenye Baraka nyingi na yenye kukuzalia matunda

Isaya 53:5-11 “Bali alijeruhiwa kwa makosa yetu, Alichubuliwa kwa maovu yetu; Adhabu ya amani yetu ilikuwa juu yake, Na kwa kupigwa kwake sisi tumepona. Sisi sote kama kondoo tumepotea; Kila mmoja wetu amegeukia njia yake mwenyewe; Na Bwana ameweka juu yake Maovu yetu sisi sote. Alionewa, lakini alinyenyekea, Wala hakufunua kinywa chake; Kama mwana-kondoo apelekwaye machinjoni, Na kama vile kondoo anyamazavyo Mbele yao wakatao manyoya yake; Naam, hakufunua kinywa chake. Kwa kuonewa na kuhukumiwa aliondolewa; Na maisha yake ni nani atakayeisimulia? Maana amekatiliwa mbali na nchi ya walio hai; Alipigwa kwa sababu ya makosa ya watu wangu. Wakamfanyia kaburi pamoja na wabaya; Na pamoja na matajiri katika kufa kwake; Ingawa hakutenda jeuri, Wala hapakuwa na hila kinywani mwake. Lakini Bwana aliridhika kumchubua; Amemhuzunisha; Utakapofanya nafsi yake kuwa dhabihu kwa dhambi, Ataona uzao wake, ataishi siku nyingi, Na mapenzi ya Bwana yatafanikiwa mkononi mwake; Ataona mazao ya taabu ya nafsi yake, na kuridhika. Kwa maarifa yake mtumishi wangu mwenye haki Atawafanya wengi kuwa wenye haki; Naye atayachukua maovu yao.”     

Yoahana 12:25-26 “Yeye aipendaye nafsi yake ataiangamiza; naye aichukiaye nafsi yake katika ulimwengu huu ataisalimisha hata uzima wa milele. Mtu akinitumikia, na anifuate; nami nilipo, ndipo na mtumishi wangu atakapokuwapo. Tena mtu akinitumikia, Baba atamheshimu.”

Hitimisho.

Kuishi maisha matakatifu kunahitaji kujikana, kuishi kwaajili ya Kristo kunahitaji kujikana, kuwatumikia watu kunahitaji kujikana, kuanzisha kazi mpya kunahitaji kujikana, kufanya umisheni kunahitaji kujikana, kumtumikia Mungu kunahitaji kujikana, kufanya uinjilisti kunahitaji kujikana, kuimba kwaya kunahitaji kujikana, kuomba kunahitaji kujikana, kukesha kunahitaji kujikana, kila kitu duniani na mafanikio yoyote yale duniani hayawezi kuja kama hatuna kujikana, kuleta maendeleo kunahitaji kujikana, bila kujikana katika jambo lolote lile hakuwezi kuwako na matunda yanayokusudiwa, mwanafunzi ili afaulu mitihani yake anahitaji kujikana, kusoma kunahitaji kujikana, biashara inahitaji kujikana, kilimo kinahitaji kujikana maendeleo yoyote yake yanahitaji kujikana hali kadhalika maisha ya kiroho yanahitaji kujikana hii ndio kanuni ya mafanikio, ni lazima chembe ya ngano ianguke, isipoanguka inabakia ile ile, lakini ikifa ikizikwa inatoa mazao mengi sana hii ni kanuni ya wokovu, ni kanuni ya kiroho na ni kanuni ya maisha,  na ni kanuni ya kuleta mafanikio makubwa duniani chembe ya ngano isipoanguka ikafa, hukaa hali iyo hiyo peke yake; bali ikifa, hutoa mazao mengi, Ni dua yangu na maombi yangu wasomaji wangu na wasilikizaji wangu tujitoe kwaajili ya kazi ya Mungu kabla ya kuangalia faida zetu binafsi.               

1Wakorintho 15:36-38 “Ewe mpumbavu! Uipandayo haihuiki, isipokufa; nayo uipandayo, huupandi mwili ule utakaokuwa, ila chembe tupu, ikiwa ni ya ngano au nyingineyo; lakini Mungu huipa mwili kama apendavyo, na kila mbegu mwili wake.”

Na. Rev. Innocent Samuel Kamote.

Mkuu wa wajenzi mwenye hekima.

+255718990796

Jumapili, 31 Agosti 2025

Tazama nimekupa mlango uliofunguliwa!


Ufunuo 3:7-8 “Na kwa malaika wa kanisa lililoko Filadelfia andika; Haya ndiyo anenayo yeye aliye mtakatifu, aliye wa kweli, aliye na ufunguo wa Daudi, yeye mwenye kufungua wala hapana afungaye, naye afunga wala hapana afunguaye. Nayajua matendo yako. Tazama, nimekupa mlango uliofunguliwa mbele yako, ambao hapana awezaye kuufunga, kwa kuwa unazo nguvu kidogo, nawe umelitunza neno langu, wala hukulikana jina langu.”



Utangulizi:

Ni muhimu kufahamu kuwa katika maisha yetu kama wanadamu ziko nyakati ambazo tunaweza kujikuta katika dimbwi la mawazo na hali ya kutokufahamu kutokana na mambo kadhaa katika maisha yetu kutokuenenda kama tunavyotaka au kufikiri,  na mara nyingine tumejikuta hatuelewi au kuwa kama watu waendao gizani kwa kupapasa kwa sababu tu ya kutokuyajua mapenzi ya Mungu katika maisha yetu, tunaweza kudhani kuwa labda tuko katika maisha yaliyopoteza mwelekeo, au yaliyopoteza tumaini, na kukosa msaada ya kiungu au hata wa kibinadamu wakati mwingine unaweza kuwaza hata kufikiri kuwa labda una laana, au kuna mtu amekuroga kwa sababu tu huoni mwelekeo wa hatima ile unayoitamani katika maisha yako huu ni ule wakati ambapo tumekwama na kila mlango wa mpenyo tuliojaribu katika maisha yetu unaonekana kama umefungwa au umepata kile ambacho hakilingani na akili yako au mtazamo wako au kile ulichokitarajia! Mlango umefungwa! Unaweza kufikiria kuwa umekataliwa kila mahali na ukadhania kuwa hustahili na ni kama Mungu hausiki na maisha yako tena lakini Mungu anajua uliposimama na ameahidi kufanya kitu kwako!

Isaya 22:19-22 “Nami nitakusukuma na kukutoa katika mahali pako, naye atakushusha utoke hapa usimamapo. Na itakuwa katika siku ile nitamwita mtumishi wangu Eliakimu, mwana wa Hilkia; nami nitamvika vazi lako, nitamtia nguvu kwa mshipi wako, nami nitamkabidhi yeye mamlaka yako; naye atakuwa baba kwa wenyeji wa Yerusalemu, na kwa nyumba ya Yuda. Na ufunguo wa nyumba ya Daudi nitauweka begani mwake; yeye atafungua wala hapana atakayefunga; naye atafunga wala hapana atakayefungua.”

Leo tutachukua muda kutafakari mambo haya yanayotokeza katika maisha yetu kwa kuliangalia neno la Mungu linasema nini pale tunapohisi kuwa labda mlango huu umefunga, labda jaribu hili halitatoka, na pale unapohisi umekwama, leo tutajikumbusha kuwa neno la Mungu linaonyesha wazi kuwa hakuna mwanadamu anaweza kukufunga wala mchawi anayeweza kuzuia Baraka zako kwa sababu tunaye Mungu mwenye mamlaka ya kufunga na kufungua milango na hakuna mtu anayeweza kufunga alichokifungulia wala hakuna anayeweza kufungua alichokifunga, Yeye ndiye anayesema leo Tazama nimekupa mlango uliofunguliwa! Na tutajifunza somo hili kwa kuzingatia vipengele vitatu vifuatavyo:-


·         Maana ya mlango uliofunguliwa.

·         Tazama nimekupa mlango uliofunguliwa.

·         Na huyu ndiye mwenye mamlaka ya milango yote.   

      

Maana ya mlango uliofunguliwa.

Kwa kawaida neno mlango uliofunguliwa  katika maandiko una maana pana sana neno uliofunguliwa katika lugha ya kiebrania linatumika neno “Pāthah”  na neno lingine la kiebrania ni “Gālāh” kwa kiyunani “AnoigōKwa hiyo neno Mlango uliofunguliwa kwa kiyunani linasomeka “Anoigō thura” neno hili lilitumika kumaanisha kupata mpenyo, kufunguliwa macho, kufunguliwa kinywa, kufunguliwa masikio, kufunguliwa mlango, kupewa macho ya kuona, kufunguliwa mbingu, kuwekewa wazi, kupata nafasi, kutoka, na kupata muelekeo, kwa sababu hiyo Mlango katika lugha ya kiroho unawakilisha Nafasi maalumu anayoitoa Mungu kwa mwanadamu kwaajili ya huduma, kusonga mbele, kutoka katika changamoto inayokukabili katika maisha kwa msaada wa Mungu  na anayesababisha milango hiyo ifunguke ni Mungu mwenyewe na hufanya hivyo kwa watu wake ambao pia ni kondoo wa malisho yake! Yesu alikwisha kutangaza kuwa yeye ndio mlango wa kondoo, awaye yote ambaye anataka upenvyo wa aina yoyote katika maisha yake hawezi kutoka bila kupitia Yesu!

Yohana 10:7-10 “Basi Yesu aliwaambia tena, Amin, amin, nawaambieni, Mimi ndimi mlango wa kondoo. Wote walionitangulia ni wevi na wanyang'anyi; lakini kondoo hawakuwasikia. Mimi ndimi mlango; mtu akiingia kwa mimi, ataokoka; ataingia na kutoka, naye atapata malisho. Mwivi haji ila aibe na kuchinja na kuharibu; mimi nalikuja ili wawe na uzima, kisha wawe nao tele.”

Kwa msingi huu katika maisha yetu tunapoona kuwa kuna mambo hayaendi katika maisha yetu ya kila siku hatupaswi kuzimia moyo kwa sababu uko mlango uliofunguliwa kwaajili yetu na yuko mwenye mamlaka ya kufunga na kufungua, hakuna mtu awaye yote anayeweza kuzuia usiolewe, hakuna mtu anayeweza kuzuia usifanikiwe, hakuna mtu anayeweza kuzuia usizae, hakuna mtu anayeweza kuzuia usipate kazi, hakuna mtu anayeweza kuzuia usifanikiwe, hakuna mtu anayeweza kuzuia usipone,  hakuna mtu anayeweza kuzuia usijenge hakuna mtu anayeweza kuzuia usiendelee mbele, hakuna anayeweza kuzuia usifaulu! Mungu wetu sio binadamu, hakuna mnyanyasaji asiyekuwa na mwisho, hakuna adui asiyekuwa na mwisho, hakuna hali ngumu isiyokuwa na mwisho kwa sababu uko mlango uliofunguliwa kwaajili yako, Mungu amekupa mlango uliofunguliwa wengine wanaweza kuona giza lakini sivyo itakavyokuwa kwako wewe na mimi wewe na mimi neno la Mungu linatuambia kuwa tunao mlango ulio wazi nguvu ya mafanikio iko kwetu na Mungu anayeweza kutufanikisha yuko kwetu na yeye ndio mlango wenyewe!

Tazama nimekupa mlango uliofunguliwa

Ni muhimu kuelewa kuwa wakati tunapopitia changamoto na majaribu mbalimbali moja ya kazi kubwa anayoifanya Shetani au adui ni kutufanya tusione njia, yaani ni kutupofusha tusipate ufunuo wa mapenzi na makusudi ya Mungu na hii ndio inayotufanya tufadhaike na kuvunjika moyo au kukata tamaa kwa sababu ya hali unayoipita kwa wakati ule, lakini Neno la Mungu linasema kuwa kwa kila jaribu uko mlango wa kutokea, na Mungu amekupa mlango uliofunguliwa!

2Wakorintho 4:3-4 “Lakini ikiwa injili yetu imesitirika, imesitirika kwa hao wanaopotea; ambao ndani yao mungu wa dunia hii amepofusha fikira zao wasioamini, isiwazukie nuru ya injili ya utukufu wake Kristo aliye sura yake Mungu.”

1Wakorintho 10:13 “Jaribu halikuwapata ninyi, isipokuwa lililo kawaida ya wanadamu; ila Mungu ni mwaminifu; ambaye hatawaacha mjaribiwe kupita mwezavyo; lakini pamoja na lile jaribu atafanya na mlango wa kutokea, ili mweze kustahimili.”    

Ufunuo 3:7-8 “Na kwa malaika wa kanisa lililoko Filadelfia andika; Haya ndiyo anenayo yeye aliye mtakatifu, aliye wa kweli, aliye na ufunguo wa Daudi, yeye mwenye kufungua wala hapana afungaye, naye afunga wala hapana afunguaye. Nayajua matendo yako. Tazama, nimekupa mlango uliofunguliwa mbele yako, ambao hapana awezaye kuufunga, kwa kuwa unazo nguvu kidogo, nawe umelitunza neno langu, wala hukulikana jina langu.”

Mungu ametupa mlango uliofunguliwa, hakuna mtu wa Mungu ambaye anaweza kukwama milele, Mungu anapofunga mlango mmoja huwa anafungua mlango mwingine, kila mwanadamu anayejitahidi kukuzibia ataula wa chuya kwa uvivu wa kuchambua, hajui nguvu na uweza wa Mungu wetu sisi tunao ufunguo wa Daudi, kila mahali palipofungwa tutatoboa tu, ni lazima ufahamu ya kuwa wakati mwingine unapoona mambo yanakwama sio lazima iwe umerogwa wewe haurogeki sio lazima uwe una laana wewe haulaniki, lakini wakati mwingine ni sauti ya Mungu inafunga mlango mmoja ili kufungua mwingine, na ukisikiliza katika ulimwengu wa roho kwa makini mlango uko wazi kwako na kwaajili yako!

Matendo 16:6-10 “Wakapita katika nchi ya Frigia na Galatia, wakikatazwa na Roho Mtakatifu, wasilihubiri lile neno katika Asia. Walipofika kukabili Misia wakajaribu kuenda Bithinia, lakini Roho wa Yesu hakuwapa ruhusa, wakapita Misia wakatelemkia Troa. Paulo akatokewa na maono usiku; alimwona mtu wa Makedonia amesimama, akimsihi, na kumwambia, Vuka, uje Makedonia utusaidie. Basi alipokwisha kuyaona yale maono, mara tukataka kutoka kwenda Makedonia, kwa kuwa tuliona hakika ya kwamba Mungu ametuita tuwahubiri Habari Njema.”

-          Walimfanyia fitini Yusufu, walimtupa shimoni, walimuuza utumwani Misri, walimfitini tena na alitupwa gerezani, badala ya mema ilionekana kana kwamba mambo yanamuendea vibaya lakini katika mpango wa Mungu, Mungu alikuwa anatengeneza mlango uliofunguliwa wa kumuweka Yusufu katika ufalme

 

Mwanzo 41:40-44 “Basi wewe utakuwa juu ya nyumba yangu, na kwa neno lako watu wangu watatawaliwa. Katika kiti cha enzi tu nitakuwa mkuu kuliko wewe. Farao akamwambia Yusufu, Tazama, nimekuweka juu ya nchi yote ya Misri. Farao akavua pete yake ya muhuri mkononi mwake, akaitia mkononi mwa Yusufu; akamvika mavazi ya kitani nzuri, na kumtia mkufu wa dhahabu shingoni mwake. Akampandisha katika gari lake la pili alilokuwa nalo. Na watu wakapiga kelele mbele yake, Pigeni magoti. Hivyo akamweka juu ya nchi yote ya Misri. Farao akamwambia Yusufu, Mimi ni Farao, na bila amri yako, mtu asiinue mkono wala mguu katika nchi yote ya Misri.”

 

-          Walimdharau Daudi na kufikiri ya kuwa hafai kabisa kuwa miongoni mwa watoto anayeweza kuwa mfalme na kupakwa mafuta, alipigwa vita kila mahali, hakukubaliwa na baba wala hakukubaliwa na kaka zake, na mfalme aliyekuwepo madarakani alimkataa na kutaka kumuua, alimwinda katika mapango na kujaribu kwa kila jinsi na kila namna kumzuia asiwe mfalme, njia ilionekana kuwa ngumu milango ilionekana kufunga lakini Mungu alikuwa na sababu, hatimaye Yeye akawa ndiye mtu sahihi aliyeupendeza Moyo wa Mungu na aliyewaongoza Israel kwa ukamilifu wa moyo, Mungu alimpa Daudi mlango uliofunguliwa!

 

Zaburi 78:70-72 “Akamchagua Daudi, mtumishi wake, Akamwondoa katika mazizi ya kondoo. Nyuma ya kondoo wanyonyeshao alimwondoa, Awachunge Yakobo watu wake, na Israeli urithi wake. Akawalisha kwa ukamilifu wa moyo wake, Na kuwaongoza kwa busara ya mikono yake.”

 

-          Walimfukuza Hajiri na Ishamel na kuwatupilia jangwani, waliishiwa na mkate na waliishiwa na maji na hatari ya kifo ilikuwa ikiwakabili, Hajiri alilia na Ishamel alilia Lakini Mungu ni Mungu ambaye hakuwa na upendeleo aliwafungulia mlango wa uhai hata walipokuwa wametaka tamaa jangwani Mungu alijidhihirisha kuwa ni Mungu mwenye kujali ni Mungu mwenye upendo, ni Mungu asiye na upendeleo, Ni Mungu anayebariki na ni Mungu mwenye kukuza sana aliahidi kumfanya Ishamel kuwa Taifa kubwa hakuna upendeleo kwa Mungu!

 

Mwanzo 21:10-21 “Kwa hiyo akamwambia Ibrahimu, Mfukuze mjakazi huyu na mwanawe, maana mwana wa mjakazi hatarithi pamoja na mwanangu, Isaka. Na neno hilo lilikuwa baya sana machoni pa Ibrahimu, kwa ajili ya mwanawe. Mungu akamwambia Ibrahimu, Neno hili lisiwe baya machoni pako, kwa ajili ya huyo mwana, na huyo mjakazi wako. Kila akuambialo Sara, sikiza sauti yake, kwa maana katika Isaka uzao wako utaitwa. Naye mwana wa mjakazi nitamfanya kuwa taifa, maana huyu naye ni uzao wako. Ibrahimu akaamka asubuhi na mapema akatwaa mkate na kiriba cha maji, akampa Hajiri akimtwika begani pake, na kijana, akamruhusu; naye akatoka, akapotea katika jangwa la Beer-sheba. Yale maji yakaisha katika kiriba, akamlaza kijana chini ya kijiti kimoja. Akaenda akakaa akimkabili, mbali naye kadiri ya mtupo wa mshale; maana alisema, Nisimwone kijana akifa; naye akakaa akimkabili, akapaza sauti yake, akalia. Mungu akasikia sauti ya kijana. Malaika wa Mungu akamwita Hajiri kutoka mbinguni, akamwambia, Una nini, Hajiri? Usiogope, maana Mungu amesikia sauti ya kijana huko aliko. Ondoka, ukamwinue kijana, ukamshike mkononi mwako, kwa kuwa nitamfanya kuwa taifa kubwa. Mungu akamfumbua macho, naye akaona kisima cha maji; akaenda akakijaza kiriba maji, akamnywesha kijana. Mungu akawa pamoja na huyo kijana, naye akakua, akakaa katika jangwa, akawa mpiga upinde. Akakaa katika jangwa la Parani; mama yake akamtwalia mke katika nchi ya Misri.”

Ndugu yangu Mungu ametupa mlango uliofunguka, haijalishi sasa unapitia hali ya namna gani, au umesimama katika hali inayoonekana kuwa ni ngumu na kama kila kitu hakionekani kuwa sawasawa huna sababu ya kulalamika wala kunung’unika  Mungu anaweza kukufungulia mlango wa afya yako, masomo yako, visa yako, safari yako, biashara zako, cheo chako, mshahara wako kuongezeka, mapato yako kuchanua, kilimo na biashara kufanikiwa, walikuwa wakifukia visima vya Isaka lakini aliendelea kuchimba vingine hakuna mtu anaweza kukufungia mlango, njia za Mungu sio kama njia za wanadamu wala mawazo yake sio kama mawazo yetu yeye huweza kufanya njia pasipo na njia leo Mungu amenituma nikukumbushe ya kuwa uko mlango uliofunguliwa kwaajili yako, ndoa yako njema inakuhusu, mchumba anakuja na yule aliyeondoka haikuwa mpango wa Mungu Mungu atakufungulia mlango mwingine, kazi iliyopotea haikuwa mahali pako sahihi Mungu amekupa mlango ulio wazi Mungu amekupa mlango uliofunguliwa na hakuna awezaye kuufunga. 

Na huyu ndiye mwenye mamlaka ya milango yote

Ufunuo 3:7 “Na kwa malaika wa kanisa lililoko Filadelfia andika; Haya ndiyo anenayo yeye aliye mtakatifu, aliye wa kweli, aliye na ufunguo wa Daudi, yeye mwenye kufungua wala hapana afungaye, naye afunga wala hapana afunguaye.”

Yesu Kristo ndiye aliyejitangaza ya kuwa anao ufunguo na kuwa mwenye kufunga ni yeye na mwenye kufungua ni yeye na akifunga hapana afunguae na akifungua hakuna awezaye kufunga, huna sababu ya kulalamika wala kulia unapoona mambo hayaendi, Yesu anabatiza kwa Roho Mtakatifu, Yesu anamwaga neema juu ya neema, Yesu ndiye anayebariki, Yesu ndiye anayefungua kurasa mpya wakati nyingine inapofunga yeye anayo mamlaka yote, Yesu sio tu anafungua milango yote lakini pia anazo funguo za mauti na kuzimu hakuna wa kukupeleka kaburini bila ruhusa yake na uwezo wake, watu wanaweza kukuona umekwama lakini Yesu anakuona unaelekea anakotaka uko mlango na unaweza kuwekwa wazi kwako katika ndoa yako, katika maisha yako, katika magonjwa yako, katika familia yako, katika uponyaji wako, acha kuangalia milango iliyofungwa mwangalie mwenye funguo mwangalie Yesu ambaye yeye ana mamlaka na wokovu wako, na uponyaji wako na mafanikio yako ukimwangalia yeye kutoboa utatoboa katika jina la Yesu Kristo mwana wa Mungu aliye hai kataa kuona giza, kataa mahangaiko mwombe Bwana akufungulie mlango, Mwambie nipe kuona Malango uliofunguliwa nionapo giza naye amekupa mlango uliofunguliwa tayari!

Ufunuo 1:17-18 “Nami nilipomwona, nalianguka miguuni pake kama mtu aliyekufa. Akaweka mkono wake wa kuume juu yangu, akisema, Usiogope, Mimi ni wa kwanza na wa mwisho, na aliye hai; nami nalikuwa nimekufa, na tazama, ni hai hata milele na milele. Nami ninazo funguo za mauti, na za kuzimu.”     

 

Na Rev. Innocent Samuel Kamote

 

Mkuu wa wajenzi mwenye Hekima!

Jumapili, 24 Agosti 2025

Basi sasa unipe mlima huu!


Yoshua 14:12-13Basi sasa unipe mlima huu, ambao Bwana alinena habari zake siku hiyo; kwani wewe ulisikia siku hiyo jinsi Waanaki walivyokuwa huko, na miji ilivyokuwa mikubwa yenye boma; yumkini yeye Bwana atakuwa pamoja nami, nami nitawafukuza watoke nje, kama Bwana alivyonena. Yoshua akambarikia, akampa Kalebu, huyo mwana wa Yefune, Hebroni kuwa urithi wake.”



Utangulizi:

Leo tutakuwa na muda wa kutafakari sehemu mojawapo muhimu ya kitabu cha Yoshua katika kifungu cha Yoshua 14:6-13, ambapo kimsingi tunaweza kupata mafundisho ya kushangaza sana tunayoyapata kutoka kwa Kalebu mmoja wa wapelelezi 12 waliotumwa na Musa kuichunguza nchi ya Kanaani. Ni jambo la kushangaza kwamba Mungu hakuwa amemsahahu mtu huyu sawasawa na ahadi yake aliyompatia kwa kinywa cha Musa mtumishi wake, kimsingi wakati mwingi sana ulikuwa umepita na sasa Kalebu ana miaka 85 lakini bado anaonyesha imani thabiti kwa Mungu, uvumilivu na ukakamavu na kama mtu mwenye subira kubwa na tumaini la maisha asiyekata tamaa, ambapo licha ya muda mrefu kuwa umepita anaikumbushia ile ahadi, huku akiwa tayari kuipambania haki yake aliyoahidiwa na Mungu, baada ya watu wengine wote kuogopa kuingia katika nchi ya Mkanaani na kupambana na majitu yaliyokuwa yanaimiliki nchi hiyo na Mungu akamuahidi Kalebu na Yoshua.

Hesabu 14:28-31 “Waambieni, Kama niishivyo, asema Bwana, hakika yangu kama ninyi mlivyonena masikioni mwangu, ndivyo nitakavyowafanyia ninyi; mizoga yenu itaanguka katika jangwa hili, na wote waliohesabiwa miongoni mwenu, kama jumla ya hesabu yenu, tangu waliopata umri wa miaka ishirini na zaidi, hao walioninung'unikia, hakika yangu hamtaingia ninyi katika nchi, ambayo niliinua mkono wangu ya kwamba nitawaketisha humo, isipokuwa Kalebu mwana wa Yefune, na Yoshua mwana wa Nuni. Lakini Watoto wenu, ambao mlisema watakuwa mateka, ndio nitakaowaleta na kuwatia ndani, nao wataijua nchi ninyi mliyoikataa.”

Tutajifunza ujumbe huu muhimu “Basi sasa unipe mlima huu” kwa kuzingatia vipengele vitatu vifuatavyo:-

·         Sababu za ahadi ya Mungu kwa Kalebu na Yoshua.

·         Basi sasa unipe mlima huu.

·         Mambo ya kujifunza kutoka kwa Kalebu.


Sababu za ahadi ya Mungu kwa Kalebu na Yoshua.

Ni muhimu kufahamu kwanza ni kwanini Mungu aliwapenda na kuwaahidi Kalebu na Yoshua kwamba watairithi nchi ya Kanaani tofauti na wenzao miongoni mwa wapelelezi 12 waliotumwa na Musa kuipeleleza nchi ya Kanaani, ili tuweze kujifunza kutoka kwake na kuwa na moyo kama wa Kalebu na Yoshua hatimaye nasi tuweze kuzifurahia Baraka za Mungu. Kalebu na Yoshua walikuwa ni askari waaminifu na watiifu kwa Mungu, wote walikuwa wametokea Misri katika nchi ya utumwa wakiwa vijana wadogo, na walipata bahati ya kuchaguliwa miongoni mwa wapelelezi 12 waliotumwa kuipeleleza nchi ya Kanaani zoezi la upelelezi lilichukua siku 40, waliporejea walitoa taarifa kwa Musa nao walikiri kuwa inchi ile kweli ilikuwa ni nchi njema na ni kweli ilikuwa ni nchi ya maziwa na asali, na miji yake ilikuwa ni mikubwa na yenye ngome na watu wake walikuwa hodari lakini pia waliwaona wana wa Anaki, aidha pia walifanikiwa kuja na vishada vikubwa vya zabibu kutoka nchi ya Mkanaani.

Hesabu 13:27-28 “Wakaenda wakafika kwa Musa, na kwa Haruni, na kwa mkutano wote wa wana wa Israeli, katika jangwa la Parani, huko Kadeshi; wakawaletea habari, wao na mkutano wote, wakawaonyesha matunda ya nchi. Wakamwambia wakasema, Tulifika nchi ile uliyotutuma, na hakika yake, ni nchi yenye wingi wa maziwa na asali, na haya ndiyo matunda yake. Lakini watu wanaokaa katika nchi ile ni hodari, na miji yao ina maboma, nayo ni makubwa sana; na pamoja na hayo tuliwaona wana wa Anaki huko. Amaleki anakaa katika nchi ya Negebu; na Mhiti, na Myebusi, na Mwamori wanakaa katika milima, na Mkanaani anakaa karibu na bahari; na kando ya ukingo wa Yordani.”                

Hata hivyo katika namna ya kushangaza sana taarifa hii iliwatisha baadhi ya wana wa Israel wasiokuwa thabiti katika imani, kwani wao badala ya kuona fursa waliogopa na kufadhaika sana  na kwa mawazo yao walikimbilia kunung’unika na kulalamika badala ya kumuamini Mungu kwamba anaweza kuwarithisha nchi ile kama alivyowaahidi, wapelelezi wengine 10, walikazia kuwa haiwezekani kuirithi inchi ile kwa sababu zao za mitazamo ya kibinadamu, Lakini Kalebu na Yoshua wao walikuwa na mtazamo tofauti kwani walirarua nguo zao na kuwatia moyo watu Kuwa hawapaswi kuogopa kwani Mungu ni mwaminifu na angewapa nchi ile na watu wale walikuwa ni kama chakula kwao.

Hesabu 13:31-33 “Kalebu akawatuliza watu mbele ya Musa, akasema, Na tupande mara, tukaitamalaki; maana twaweza kushinda bila shaka. Bali wale watu waliopanda pamoja naye wakasema, Hatuwezi kupanda tupigane na watu hawa; kwa maana wana nguvu kuliko sisi. Wakawaletea wana wa Israeli habari mbaya ya ile nchi waliyoipeleleza, wakasema, Ile nchi tuliyopita kati yake ili kuipeleleza, ni nchi inayowala watu wanaoikaa; na watu wote tuliowaona ndani yake ni watu warefu mno. Kisha, huko tuliwaona Wanefili, wana wa Anaki, waliotoka kwa hao Wanefili; tukajiona nafsi zetu kuwa kama mapanzi; nao ndivyo walivyotuona sisi.”                

Hesabu 14:6-9 “Na Yoshua mwana wa Nuni, na Kalebu mwana wa Yefune, waliokuwa miongoni mwao walioipeleleza nchi, wakararua nguo zao; wakanena na mkutano wote wa wana wa Israeli wakasema, Nchi ile tuliyopita kati yake ili kuipeleleza, ni nchi njema mno ya ajabu. Ikiwa Bwana anatufurahia, atatuingiza katika nchi hii atupe iwe yetu, nayo ni nchi yenye wingi wa maziwa na asali. Lakini msimwasi Bwana, wala msiwaogope wale wenyeji wa nchi, maana wao ni chakula kwetu; uvuli uliokuwa juu yao umeondolewa, naye Bwana yu pamoja nasi; msiwaogope.”

Kutokana na ujasiri wa Kalebu mwana wa Yefune na Yoshua mwana wa Nuni ambao walionyesha ujasiri mkubwa uliochangiwa na uaminifu wao na imani yao kwa Mungu, Mungu aliapa kuwaangamiza wengine waliolalamika na kunung’unika lakini aliahidi kuwa sivyo itakavyokuwa kwa Kalebu na Yoshua kwa kuwa wao walikuwa na kitu cha ziada na cha tofauti na hivi ndo walivyokua:-

-          Alimfuata Bwana kwa moyo wake wote – Hesabu 14:23-24 “hakika yangu hawataiona hiyo nchi niliyowaapia baba zao, wala katika hao wote walionidharau hapana atakayeiona; lakini mtumishi wangu Kalebu, kwa kuwa alikuwa na roho nyingine ndani yake, naye AMENIANDAMA KWA MOYO WOTE, nitamleta yeye mpaka nchi hiyo aliyoingia; na uzao wake wataimiliki.”

 

Neno ameniandama kwa moyo wote katika maandiko ya kiebrania linasomeka kama ‘achr Rûach ambalo kwa kiingereza ni wind by resemblance yaani amekuwa na roho ya kufanana nami au punzi inayonifanania, maana yake Kalebu alikuwa anaona mambo sawasawa na jinsi Mungu anavyoona, wakati watu wengine wote wanaona mambo hayawezekani Kalebu na Yoshua wao walikuwa wanaona mbona inawezekana, Mungu alimuahidi Kalebu inchi ile kuwa atairithi yeye na watoto wake kwa sababu aliona kama Mungu anavyoona, aliona yasiyowezekana kibinadamu yanawezekana kwa Mungu, alikuwa na mtazamo wa yanayowezekana  wakati wanadamu wakiona yasiyowezekana.

               

-          Walimfuata Bwana kwa kila neno – Kumbukumbu 1:34-36 “Bwana akaisikia sauti ya maneno yenu, akaghadhibika, akaapa, akasema, Hakika yangu hapana mmoja miongoni mwa watu hawa wa kizazi hiki kibaya atakayeiona nchi hiyo nzuri, niliyowaapia baba zenu kuwapa,isipokuwa Kalebu mwana wa Yefune, huyo ataiona; nami nitampa yeye na watoto wake nchi hiyo aliyoikanyaga; KWA KUWA AMEMFUATA BWANA KWA KILA NENO.”

 

Neno amemfuata Bwana kwa kila neno kwenye lugha ya kiebrania linatumika neno Mâlmâlâ ‘Achar ambalo katika kiingereza ni neno Wholly Conjugation au Wholly Conjugate ambalo kwa Kiswahili ni kuenda Sambamba, kufuata barabara, au kufanya au kuungana kwa hiyo sifa nyingine aliyokuwa nayo Kalebu ni kuwa aliungana na Mungu katika neno lake lote, kile kilichozungumzwa na Mungu yeye aliungana nacho kama kilivyosemwa, hakuwa kinyume na neno, alilifuata, alilitenda aliungana nalo na kwa sababu hiyo Mungu anaapa kuwa atairithi nchi. 

 

-          Alimwandama bwana kwa utimilifu – Yoshua 14:13-14 “Yoshua akambarikia, akampa Kalebu, huyo mwana wa Yefune, Hebroni kuwa urithi wake. Kwa hiyo Hebroni ukawa urithi wa Kalebu, mwana wa Yefune, Mkenizi, hata leo; kwa sababu ALIMWANDAMA BWANA, MUNGU WA ISRAELI, KWA UTIMILIFU.”

 

Neno alimuandama kwa utumilifu katika maandiko ya kuiebrania linasomeaka kama Mâlmâlâ kusomeka linasomeka maw-lay kwa kiingereza ni neno concecrate ambalo maana yake kwa utakatifu, kwa unyoofu, kwa kujiweka wakfu, kwa njia tofauti na wengine yaani wakati wengine wanaasi wanazungumza kinyume na ahadi ya Mungu Kalebu yeye alifanya kwa unyoofu kwa utakatifu, kwaajili ya hili Mungu alimpa ahadi, Kalebu hafuati mkumbo             

 

-          Walikuwa na roho nyingine – Hesabu 14:22-24 “kwa sababu watu hawa wote, ambao wameuona utukufu wangu na ishara zangu, nilizozitenda huko Misri, na huko jangwani, pamoja na haya wamenijaribu mara hizi kumi, wala hawakuisikiza sauti yangu; hakika yangu hawataiona hiyo nchi niliyowaapia baba zao, wala katika hao wote walionidharau hapana atakayeiona; lakini mtumishi wangu Kalebu, KWA KUWA ALIKUWA NA ROHO NYINGINE ndani yake, naye ameniandama kwa moyo wote, nitamleta yeye mpaka nchi hiyo aliyoingia; na uzao wake wataimiliki.”

 

Neno alikuwa na roho nyingine katika maandiko ya kiebrania linasomeka kama Achr rûach ambayo kwa kiingereza “Strange Spirit”, roho nyingine, yaani tofauti na wengine ambao walikuwa na roho ya hofu, roho ya woga, yeye alikuwa na Roho Nyingine roho ambayo sio ya kibinadamu, Roho kama ya Mungu, ukiwa na roho nyingine tofauti na wanadamu wa kawaida wewe unakuwa na mtazamo mwingine, mtazamo wa tofauti, unaona kwa jinsi nyingine na kutazama mambo kwa jicho lingine, jicho la kigeni.

Basi sasa unipe mlima huu

Kalebu huyu ambaye hakuwa mtu wa kawaida na alikuwa na kitu cha ziada, akiwa na roho ya kufanana na Mungu, akiwa na moyo wa unyoofu, akiwa anaungana na neno la Mungu, akiwa na roho nyingine tofauti na wayahudi wengine yeye sasa anaidai nchi ya Kanaani aliyoahidiwa na Mungu na anamkumbusha Yoshua kwamba sasa ni wakati wa kupewa urithi wake, na kwa vile Yoshua alikuwepo anamkumbusha yale yote Mungu aliyokuwa ameahidi kwa kinywa cha mtumishi wake Musa, mbele ya Yoshua walipokuwa pamoja naye ni miaka 45 imepita sasa ahadi ilitolewa alipokuwa na miaka 40 sasa anakumbushia kile alichoahidiwa na Mungu, na hataki bure anasema yuko tayari kupigana kwaajili ya ardhi ile tena pale pale wanapoishi majitu yaani wana wa Anaki hili ni jambo la kushangaza sana

Yoshua 14:6-13 Wakati huo wana wa Yuda walimkaribia Yoshua hapo Gilgali; na Kalebu, mwana wa Yefune, huyo Mkenizi, akamwambia, Wewe wajua hilo neno Bwana alilomwambia Musa, huyo mtu wa Mungu, katika habari zangu, na katika habari zako wewe, tulipokuwa katika Kadesh-barnea. Mimi nilikuwa mtu wa miaka arobaini umri wangu, hapo Musa mtumishi wa Bwana aliponituma niende kutoka Kadesh-barnea ili kuipeleleza hiyo nchi; nami nilimletea habari tena, kama ilivyokuwa ndani ya moyo wangu. Lakini wale ndugu zangu waliokwea kwenda pamoja nami waliiyeyusha mioyo ya watu; ila mimi nilimfuata Bwana, Mungu wangu, kwa utimilifu. Kisha Musa akaniapia siku hiyo, akasema, Hakika hiyo nchi ambayo miguu yako imekanyaga itakuwa ni urithi kwako wewe, na kwa watoto wako milele, kwa sababu wewe umemfuata Bwana, Mungu wako, kwa utimilifu. Sasa basi, angalia, yeye Bwana ameniweka hai, kama alivyosema, miaka hii arobaini na mitano, tangu wakati huo Bwana alipomwambia Musa neno hilo, wakati Israeli waliokuwa wakienenda barani; na sasa tazama, hivi leo nimepata miaka themanini na mitano umri wangu. Hata sasa mimi nina nguvu zangu hivi leo kama nilivyokuwa siku hiyo Musa aliyonituma; kama nguvu zangu zilivyokuwa wakati huo, na nguvu zangu ndivyo zilivyo sasa, kwa vita na kwa kutoka nje na kuingia ndani. Basi sasa unipe mlima huu, ambao Bwana alinena habari zake siku hiyo; kwani wewe ulisikia siku hiyo jinsi Waanaki walivyokuwa huko, na miji ilivyokuwa mikubwa yenye boma; yumkini yeye Bwana atakuwa pamoja nami, nami nitawafukuza watoke nje, kama Bwana alivyonena. Yoshua akambarikia, akampa Kalebu, huyo mwana wa Yefune, Hebroni kuwa urithi wake.Kwa hiyo Hebroni ukawa urithi wa Kalebu, mwana wa Yefune, Mkenizi, hata leo; kwa sababu alimwandama Bwana, Mungu wa Israeli, kwa utimilifu. Basi jina la Hebroni hapo kwanza uliitwa Kiriath-arba; huyo Arba alikuwa ni mtu mkubwa kupita wenziwe wote katika hao Waanaki. Hiyo nchi nayo ikatulia, vita vikakoma.”

Miaka mingi imepita lakini Kalebu bado yuko vile vile hakuna kuchuja, nguvu zake ziko vile vile na anataka ardhi na kama ilivyo kawaida ya wanadamu wengi sio rahisi sana kuona faida za kukaa mlimani, tunapenda nchi tambarare iliyonyooka, watu wengi hawapendi milima, na zaidi ya yote mlima huu ulikuwa unamilikiwa na majitu makubwa wana wa Anaki, katika namna ya kushangaza sana Kalebu yeye anautaka mlima huo na yuko tayari kuupigania imani yake haijapoa miaka 45 imepita yeye yuko vile vile, moyo wake uko vile vile anamuamini Mungu vile vile akiwa na nguvu zile zile, akiwa na ujasiri ule ule hajachoka katika mapambano hii inatufundisha kitu kikubwa sana.

Hebroni ilikuwa ni safu ya milima katika milima ya uyahudi kusini mwa Yudea,  ambako ni ukanda wa Magharibi leo, mji wa Hebroni ni moja ya mji unaoheshimika sana na wayahudi kama moja ya miji mitakatifu walikozikwa wazee wetu Ibrahim, Isaka na Yakobo katika pango la Makpela  kwa hiyo ni eneo zuri kihistoria, wakati wa Yoshua sasa eneo hilo lilikaliwa na majitu, lakini Kalebu alikuwa anaiona fursa katika mlima aliouomba kuliko nchi tambarare, kiusalama na kiulinzi yeye angeishi juu na kama askari angeweza kuwaona adui kwa mbali na kuwa salama, chini ya milima kulikua na bonde zuri ambalo lingeweza kufaa kwa kilimo na mifugo na juu ya mlima makazi salama, sasa Kalebu anataka hilo, Kalebu mtazamo wake ni wa tofauti, ni kama ana moyo wa kufanya mambo kwa njia tofauti, ni kama mtu anayesema wakati watu wanaogopa kuendesha ndege mimi nitaendesha, ni kama mtu anayesema wakati watu wanaogopa hisabati mimi ninapenda hisabati, ni kama mtu anayesema wakati watu wanaogopa masomo ya sayansi mimi nitachukua sayansi, Moyo wa Kalebu ni moyo usioogopa mambo magumu, unaona fursa katika mambo yasiyowezekana hauchagui mambo mepesi, unachagua mambo magumu, unaona fursa katika mambo magumu, unawaza na kuyataja yanayoonekana hayawezekani kuwa yanawezekana “BASI SASA UNIPE MLIMA HUU” haijalishi umri umekwenda kiasi gani anataka MLIMA HUU ni mzee lakini bado anawaza na kufikiri akiona maono kama kijana tu, hasemi umri wangu umeenda, hasemi nguvu zangu zimeisha, ametunza Imani yake na uwepo wake vilevile, Kalebu hapoi wala haboi, mtazamo wake kuhusu Mungu uko vilevile wakati makanisa mengi yanapoa yanapofikia umri wa miaka 40, wakati wakristo wengi wanapoa wanapokaa sana katika wokovu, Kalebu hapoi, Kalebu bado anaona maono, Kalebu bado ana ndoto Kalebu bado anamuamini Mungu, haoni kuwa Mungu amechelewa, wala hana muda wa kumlaumu Mungu, anakumbushia haki zake, yuko tayari kwa mapambano, Kalebu hachoki mikesha, Kalebu hachoki kufunga, Kalebu hachoki kuomba, Kalebu hachoki mikutano ya injili, Kalebu hachoki kuhubiri vijijini, Kalebu  hachoki kufungua makanisa, Kalebu hachoki kusoma, Kalebu hachoki kujitoa, Kalebu hachoki kuishi maisha matakatifu, Kalebu hachoki kulifuata neno, Kalebu hachoki kuwa na roho ile ile ya Mungu, Kalebu hachoki kunena kwa lugha, Kalebu ana ujasiri ule ule wa kuhubiri sokoni, Kalebu, ana moto uleule aliokuwa nao jangwani, Kalebu hachoki kuvumilia, Kalebu hachoki kusubiria, Kalebu hachoki majaribu Kalebu hataki kuweka silaha chini Kalebu Kalebu Kalebu una miaka 85 sasa umezeeka, nguvu zako zimeisha, umestaafu sasa Kalebu si utulie, Kalebu si nikutafutie eneo tambarare, Kalebu si ukae karibu na mimi? Kalebu anasema BASI SASA UNIPE MLIMA HUU Mungu wangu ni moyo wa namna gani huu Kalebu? Umepigana vita vingi Kalebu, ukae chini utulie ule mema ya nchi inatosha sasa Kalebu, Kalebu “BASI SASA UNIPE MLIMA HUU” kuna waanaki huko Kalebu, Kalebu nitawafukuza huko, Bwana atakuwa pamoja nami, nguvu zangu hazijapungua niko vilevile kama hapo Musa aliponiapia “BASI SASA UNIPE MLIMA HUU” “shakarabashata skarabatulabosolitasaka Kalebu sotoribakarashika sata rakata risatika yekresatabsoliboso rokosotoka sebetaolasiotifaBASI SASA UNIPE MLIMA HUU neno la Mungu linasema “KWA HIYO HEBRONI UKAWA URITHI WA KALEBU, MWANA WA YEFUNE, MKENIZI, HATA LEO

Mambo ya kujifunza kutoka kwa Kalebu.

-          Ni lazima tuwe na Imani thabiti kwa ahadi za Mungu  -  Kalebu alikuwa ni mtu wa imani na hakuwahi kuchoka katika kumuamini Mungu ni miaka 45 imepita tangu alipokuja kuichunguza na kuipeleleza nchi na hata ingawaje wapelelezi wengine walileta habari chochezi kinyume na imani Kalebu tangu wakati ule aliamini kuwa Mungu hawezi kuwaangusha anakumbuka ahadi za Mungu na hakua na lawama kuwa Mungu amechelewa  au amekawia anaendelea kuipigania haki yake sawa na jinsi na namna ile ile aliyokuwa nayo awali.

 

Yoshua 14:9-12 “Kisha Musa akaniapia siku hiyo, akasema, Hakika hiyo nchi ambayo miguu yako imekanyaga itakuwa ni urithi kwako wewe, na kwa watoto wako milele, kwa sababu wewe umemfuata Bwana, Mungu wako, kwa utimilifu. Sasa basi, angalia, yeye Bwana ameniweka hai, kama alivyosema, miaka hii arobaini na mitano, tangu wakati huo Bwana alipomwambia Musa neno hilo, wakati Israeli waliokuwa wakienenda barani; na sasa tazama, hivi leo nimepata miaka themanini na mitano umri wangu. Hata sasa mimi nina nguvu zangu hivi leo kama nilivyokuwa siku hiyo Musa aliyonituma; kama nguvu zangu zilivyokuwa wakati huo, na nguvu zangu ndivyo zilivyo sasa, kwa vita na kwa kutoka nje na kuingia ndani. Basi sasa unipe mlima huu, ambao Bwana alinena habari zake siku hiyo; kwani wewe ulisikia siku hiyo jinsi Waanaki walivyokuwa huko, na miji ilivyokuwa mikubwa yenye boma; yumkini yeye Bwana atakuwa pamoja nami, nami nitawafukuza watoke nje, kama Bwana alivyonena.”                

 

Kalebu ni moja ya mashujaa wa Imani aliyeweza kusubiria ahadi ya Mungu kwa muda mrefu bila kukata tamaa, wakati Ibrahimu alimsubiri Isaka kwa miaka kama 25 hivi, na Daudi alisubiria ufalme kwa miaka kama 20, Yakobo alivumilia kwa mjomba wake kwa miaka 20 lakini Kalebu alivumilia kwa zaidi ya miaka 45 je wewe ni mvumilivu kwa kiasi gani?

 

-          Kuwa tayari kukabiliana na changamoto – Kalebu alikuwa na ujasiri wa hali ya juu, hakuiomba Hebroni hivi hivi tu, Hebroni ulikuwa ni mlima na sio tambarare na zaidi ya yote ulikuwa unamilikiwa na wana wa Anaki ambao kimsingi walikuwa ni majitu, wale wale walioogopewa na wengine Yeye Kalebu hakuogopa alikuwa tayari kukabiliana na hali hiyo huku akimtegemea Mungu kwamba angekuwa pamoja naye akiamini kuwa atawafukuza.

 

Yoshua 14:12 “Basi sasa unipe mlima huu, ambao Bwana alinena habari zake siku hiyo; kwani wewe ulisikia siku hiyo jinsi Waanaki walivyokuwa huko, na miji ilivyokuwa mikubwa yenye boma; yumkini yeye Bwana atakuwa pamoja nami, nami nitawafukuza watoke nje, kama Bwana alivyonena.”

 

-          Hakuogopa umri wake – Kalebu alikuwa mvumilivu sana na alikuwa na nguvu amefikisha miaka 85 lakini anajisikia ndani yuko vile vile na uwezo ule ule wa kukabiliana na changamoto zile zile alikuwa ni mbobezi katika maswala ya vita na jeshi, jangwa lilikuwa limemuimarisha na kumfanya kuwa mtu mgumu, umri kwake haukuwa kikwazo cha kuzirithi ahadi za Mungu na kuzipambania aliendelea kuwa na maono na imani na matumaini.

 

Yoshua 14:11 “Hata sasa mimi nina nguvu zangu hivi leo kama nilivyokuwa siku hiyo Musa aliyonituma; kama nguvu zangu zilivyokuwa wakati huo, na nguvu zangu ndivyo zilivyo sasa, kwa vita na kwa kutoka nje na kuingia ndani.”

 

-          Aliendelea kuwa mwainifu siku zote – Kwa kweli maneno ya Kalebu yanaonyesha kuwa alikuwa mwaminifu na aliendelea kuwa vile vile mpaka mwisho, uaminifu wake kwa Mungu tangu ujana wake  mpaka wakati huu anaonekana kuwa alikuwa mtu asiyekata tamaa, shujaa na mtu aliyeendelea kumtegemea Mungu huku akikumbuka ahadi zake na haki yake aliudai mlima huo kwa sababu alikuwa na uhakika na Mungu wake kuwa hatomwangusha

 

Yoshua 14:7-8 “Mimi nilikuwa mtu wa miaka arobaini umri wangu, hapo Musa mtumishi wa Bwana aliponituma niende kutoka Kadesh-barnea ili kuipeleleza hiyo nchi; nami nilimletea habari tena, kama ilivyokuwa ndani ya moyo wangu. Lakini wale ndugu zangu waliokwea kwenda pamoja nami waliiyeyusha mioyo ya watu; ila mimi nilimfuata Bwana, Mungu wangu, kwa utimilifu.”   

       

Hitimisho:

Kalebu anampa somo kila mmoja wetu kuhusu imani, uvumilivu, subira, ujasiri, na uaminifu kwa Mungu, alikuwa ni mtu asiyeogopa changamoto wala mtu wa kukata tamaa, hakukuwa na hata tone la hofu maishani mwake kauli yake BASI SASA UNIPE MLIMA HUU iwe changamoto kwetu kwamba tuteendelea kumuamini Mungu sio kwa mambo mepesi tu bali hata kwa mambo magumu, na tutaendelea kuwa wavumilivu bila kujali muda, na tutaendelea katika imani bila kupoa, na tutaendelea kuwa na ujasiri wa kukabiliana na magumu bila kujali umri na kuwa tayari kumtumikia Mungu mpaka siku zetu za mwisho!

 

Rev. Innocent Samuel Kamote

Mkuu wa wajenzi mwenye Hekima!

Jumapili, 17 Agosti 2025

Yeye ajaye kutoka juu, huyo yu juu ya yote!


Yohana 3:30-31 “Basi hii furaha yangu imetimia. Yeye hana budi kuzidi, bali mimi kupungua. Yeye ajaye kutoka juu, huyo yu juu ya yote. Yeye aliye wa dunia, asili yake ni ya dunia, naye anena mambo ya duniani. Yeye ajaye kutoka mbinguni yu juu ya yote.”




Utangulizi:

Moja ya watu waliokuwa na uwezo mkubwa sana wa kumuelezea vizuri Yesu Kristo na kumtambulisha kwa watu ni pamoja na Yohana Mbatizaji, huyu ni moja ya manabii waliopata neema ya ajabu sana ya sio tu kutabiri kuhusu ujio wa Maisihi, lakini kuonyesha moja kwa moja mubashara kuhusu Yesu Kristo, Mjadala kuhusu Yesu ulikuja baada  ya watu kumuhoji kuhusu habari za Yesu ambaye watu wengi walikuwa wameanza kumuendea, huku wengine wakiendelea kuonyesha heshima kubwa kwa Yohana Mbatizaji wakifikiri kwa kuwa alitokea nyikani na alikuwa kama Eliya kimtazamo na kimuonekano kwamba huenda ndiye angefaa kuwa masihi, Hata hivyo yeye aliendelea kuwasisitizia kuwa huyo anayefanya wanafunzi wengi ndiye masihi na yeye hana budi kupungua ili huyo aweze kuzidi

Yohana 3:26-31 “Wakamwendea Yohana, wakamwambia, Rabi, yeye aliyekuwa pamoja nawe ng'ambo ya Yordani, yeye uliyemshuhudia, tazama, huyo anabatiza na watu wote wanamwendea. Yohana akajibu, akasema, Hawezi mtu kupokea neno lo lote isipokuwa amepewa kutoka mbinguni. Ninyi wenyewe mwanishuhudia ya kwamba nalisema, Mimi siye Kristo, bali nimetumwa mbele yake. Aliye naye bibi arusi ndiye bwana arusi; lakini rafiki yake bwana arusi, yeye anayesimama na kumsikia, aifurahia sana sauti yake bwana arusi. Basi hii furaha yangu imetimia. Yeye hana budi kuzidi, bali mimi kupungua. Yeye ajaye kutoka juu, huyo yu juu ya yote. Yeye aliye wa dunia, asili yake ni ya dunia, naye anena mambo ya duniani. Yeye ajaye kutoka mbinguni yu juu ya yote.”

Yohana anamuelezea Yesu kwa ufunuo mkubwa ambao sio rahisi mwanadamu wa kawaida kuwa nao, Yeye anamuelezea Yesu kama Yeye ajaye kutoka juu, ana anamfunua hivyo kwa umati mkubwa wa watu akimaanisha kuwa Yesu sio nabii wa kawaida wala Mwalimu wa kawaida wa duniani bali huyu ashuka kutoka mbinguni, Yohana alikuwa akiuthibitishia ulimwengu kuwa Yesu ana mamlaka kubwa sana kuliko hata yeye mwenyewe, Yesu ana asili ya uungu na sio ya kibinadamu tu, Kila Mwalimu wa kweli wa neno la Mungu ni lazima awe na uhakika wa Yesu ni nani na awe anajua kumuelezea vizuri, na kutokujaribu kuchukua nafasi yake na kumleta Yesu mzima mzima kwa jamii ili jamii imkubali na kupata masaada kutoka kwake, leo tutachukua muda kuijadili kauli hii ya Yohana Mbatizaji Yeye ajaye kutoka juu! kwa kuzingatia vipengele vitatu vifuatavyo:-


·         Asili ya Yesu Kristo.

·         Yeye ajaye kutoka juu.

·         Yeye ajaye kutoka juu, huyo yu juu ya yote!


Asiili ya Yesu Kristo!

Yohana ni moja ya manabii wa ajabu sana na wa tofauti mno, Kabla ya wanafunzi wa Yesu kutuelezea kwa kina kuwa Yesu Kristo ni nani Yohana mbatizaji ni mtu wa kwanza kutuelezea ukuu wa Yesu Kristo Yeye anamuelezea Yesu kama ambaye asili yake si ya dunia kama alivyo Yohana na manabii wengine na sisi, Yesu anaelezewa na Yohana Mbatizaji kama ambaye asili yake ni ya mbinguni yaani Yeye ajaye kutoka juu!

Yohana 3:31 “Yeye ajaye kutoka juu, huyo yu juu ya yote. Yeye aliye wa dunia, asili yake ni ya dunia, naye anena mambo ya duniani. Yeye ajaye kutoka mbinguni yu juu ya yote.”

Yohana anatufunulia hapa kwamba Yesu amekuja kutoka mbinguni na hivyo asili yake sio ya dunia, ukweli huu unakubalina na mafundisho ya kibiblia na maneno ya Bwana mwenyewe kwamba Yeye amekuwepo kabla hata ya Ibrahimu baba wa Imani ya kiyahudi hajakuwepo, Yeye Ibrahimu asijakuwako mimi niko (“Before Abraham was born I am!”) yaani kabla Ibrahimu hajazaliwa mimi niko alisema Yesu Kristo mwenyewe.

Yohana 8:56-58 “Ibrahimu, baba yenu, alishangilia kwa vile atakavyoiona siku yangu; naye akaiona, akafurahi. Basi Wayahudi wakamwambia, Wewe hujapata bado miaka hamsini, nawe umemwona Ibrahimu? Yesu akawaambia, Amin, amin, nawaambia, Yeye Ibrahimu asijakuwako, mimi niko.”

Neno la Mungu vilevile linathibitisha ya kuwa Yesu Kristo kabla ya kuvaa mwili wa kibinadamu alikuweko tangu milele kama neno la Mungu na alihusika katika kuumba ulimwengu na hapa Duniani alijifunua kwetu kwa utukufu kama wa mwana pekee wa Mungu.

Yohana 1:1-3,1 4 “Hapo mwanzo kulikuwako Neno, naye Neno alikuwako kwa Mungu, naye Neno alikuwa Mungu. Huyo mwanzo alikuwako kwa Mungu.Vyote vilifanyika kwa huyo; wala pasipo yeye hakikufanyika cho chote kilichofanyika. 14 Naye Neno alifanyika mwili, akakaa kwetu; nasi tukauona utukufu wake, utukufu kama wa Mwana pekee atokaye kwa Baba; amejaa neema na kweli.”

Kwa msingi huo neno la Mungu linabainisha wazi kuwa Yesu Kristo hakuwa mwanadamu wa kawaida, mamlaka yake na uwezo wake ulikuwa uko juu ya kawaida ya kibinadamu kama anavyoeleza Nabii Yohana mbatizaji, ufahamu huu kwa kweli sio ufahamu wa kawaida ni lazima uwe umefunuliwa na Roho Mtakatifu kumfahamu na kumtambua Yesu kuwa ni mtu wa namna gani, mapema kabla ya kuzaliwa kwake nabii Mika aliyeishi karibu wakati sawa na nabii Isaya alieleza mpaka mahali atakapozaliwa Masihi na kuutaja mji atakaozaliwa kuwa ni Bethelehemu, lakini kama haitoshi alieleza kuwa mtu huyu asiyekuwa wa kawaida asili yake imekuwepo tokea enzi na enzi.

Mika 5:2 “Bali wewe, Bethlehemu Efrata, uliye mdogo kuwa miongoni mwa elfu za Yuda; kutoka kwako wewe atanitokea mmoja atakayekuwa mtawala katika Israeli; ambaye matokeo yake yamekuwa tangu zamani za kale, tangu milele.”

Nabii Isaya akitabiri kuhusu kuja kwa masihi Yaani Bwana Yesu yeye naye alitabiri na kuonyesha kuwa Yesu atakuwa mfalme wa ajabu na baba wa milele, na Mungu mwenye nguvu, kwa ujumla maandiko yanamuelezea Yesu kwa namna pana zaidi kuliko watu wengine wanavyoweza kufikiri au kukosoa kwa kukosa maarifa Isaya anasema:-

Isaya 9:6-7 “Maana kwa ajili yetu mtoto amezaliwa, Tumepewa mtoto mwanamume; Na uweza wa kifalme utakuwa begani mwake; Naye ataitwa Jina Lake, Mshauri wa ajabu, Mungu mwenye nguvu, Baba wa milele, Mfalme wa amani. Maongeo ya enzi yake na amani Hayatakuwa na mwisho kamwe, Katika kiti cha enzi cha Daudi na ufalme wake; Kuuthibitisha na kuutegemeza Kwa hukumu na kwa haki, Tangu sasa na hata milele. Wivu wa Bwana wa majeshi ndio utakaotenda hayo.”

Kwa msingi huo sio kuwa wakristo wanamkuza tu Yesu Kristo na wengine wanadhani kuwa tunakufuru, lakini ni ukweli ulio wazi manabii walimfunua Yesu Kristo kwetu pamoja na mitume wake ambao kwaasili ni wayahudi wanatuwekea wazi kuwa Yesu Kristo asili yake ni Mbinguni na kuwa alikuwako huko toka milele na sio hivyo tu tunaelezwa kuwa alikuwa Mungu na kwa kuja kwake duniani ililikuwa swala la unyenyekevu mkubwa na kujidhili au kujishusha kwa namna isiyoweza kufananishwa au labda kuwa sawa na mtumwa ingawa yeye alijijua kuwa hakuwa mtu wa kawaida, Paulo mtume analiweka hilo sawa katika waraka wake kwa Wafilipi ona:-

Wafilipi 2:5-8 “Iweni na nia iyo hiyo ndani yenu ambayo ilikuwamo pia ndani ya Kristo Yesu; ambaye yeye mwanzo alikuwa yuna namna ya Mungu, naye hakuona kule kuwa sawa na Mungu kuwa ni kitu cha kushikamana nacho; bali alijifanya kuwa hana utukufu, akatwaa namna ya mtumwa, akawa ana mfano wa wanadamu; tena, alipoonekana ana umbo kama mwanadamu, alijinyenyekeza akawa mtii hata mauti, naam, mauti ya msalaba.”

Kwa sababu hiyo Yohana alimtambua Yesu kuwa alikuwa mwanadamu wa viwango vingine, mwanadamu asiyekuwa wa kawaida alisema huyu ni mkuu mno akionyesha ukuu wa Yesu Kriso katika kiwango ambacho yeye mwenyewe alisema hastahili hata kulegeza gidamu za viatu vyake:-

Luka 3:16-17 “Yohana alijibu akawaambia wote, Kweli mimi nawabatiza kwa maji; lakini yuaja mtu mwenye nguvu kuliko mimi, ambaye mimi sistahili kuilegeza gidamu ya viatu vyake; yeye atawabatiza kwa Roho Mtakatifu na kwa moto; ambaye pepeo lake li mkononi mwake, naye atausafisha sana uwanda wake, na kuikusanya ngano ghalani mwake, bali makapi atayateketeza kwa moto usiozimika.”  

Yohana anatusaidia wanazuoni kutokumchukulia Yesu Kristo kama mtu wa kawaida au kama manabii wengine, Yesu Kristo hafananishwi wala kulinganishwa na kitu chochote, kujishusha kwake na unyenyekevu wake wa kukubali kudhalilishwa msalabani kusiwanye wanadamu wawe na nafasi ya kumdhalilisha na kumkufuru badala yake wanapaswa kuogopa na kumchukulia kwa heshima kubwa kwani ni zawadi ya kipekee ambayo Mungu amewapa wanadamu ili tuweze kuokolewa Yesu yeye asili yake ni juu, yaani yeye ametokea Mbinguni ambako alikuweko tangu mwanzo, Yeye yuko juu y asana kuliko ufalme wowote, mamlaka yoyote, usultani wowote, enzi yoyote, na jina lolote litajwalo ulimwenguni humu na vitu vyote viliumbwa kwa njia yake na kwaajili yake

Waefeso 1:17-21 “Mungu wa Bwana wetu Yesu Kristo, Baba wa utukufu, awape ninyi roho ya hekima na ya ufunuo katika kumjua yeye; macho ya mioyo yenu yatiwe nuru, mjue tumaini la mwito wake jinsi lilivyo; na utajiri wa utukufu wa urithi wake katika watakatifu jinsi ulivyo; na ubora wa ukuu wa uweza wake ndani yetu tuaminio jinsi ulivyo; kwa kadiri ya utendaji wa nguvu za uweza wake; aliotenda katika Kristo alipomfufua katika wafu, akamweka mkono wake wa kuume katika ulimwengu wa roho; juu sana kuliko ufalme wote, na mamlaka, na nguvu, na usultani, na kila jina litajwalo, wala si ulimwenguni humu tu, bali katika ule ujao pia;”             

Wakolosai 1:16-19 “Kwa kuwa katika yeye vitu vyote viliumbwa, vilivyo mbinguni na vilivyo juu ya nchi, vinavyoonekana na visivyoonekana; ikiwa ni vitu vya enzi, au usultani, au enzi, au mamlaka; vitu vyote viliumbwa kwa njia yake, na kwa ajili yake. Naye amekuwako kabla ya vitu vyote, na vitu vyote hushikana katika yeye. Naye ndiye kichwa cha mwili, yaani, cha kanisa; naye ni mwanzo, ni mzaliwa wa kwanza katika wafu, ili kwamba awe mtangulizi katika yote. Kwa kuwa katika yeye ilipendeza utimilifu wote ukae;”

Kwa msingi huu kwa uchunguzi wa kimaandiko utakubaliana nami kwamba Yesu, Yu Juu ya yote kama yanenavyo maandiko!

Yeye ajaye kutoka juu

Wako watu katika nyakati za leo hususani watu wanaoendesha mijadala ya kidini ambao humchukulia Yesu kwa mchezo mchezo na wala hawataki kumuelezea Yesu Katika namna ambayo maandiko humuelezea, mijadala ya aina hii, Nabii Yohana mbatizaji aliizima kabisa kwani wanazuoni wa wakati huo walitaka kumlinganisha Yeye (Yohana mbatizaji) au nabii (Yahaya bin Zekaria) na Masihi Bwana Yesu, wao walimtazama kwa mtazamo wa nje tu na kuona kama Nabii Yohana alionekana wa maana sana labda huenda hata kuliko Yesu, kwa sababu yeye alitokea Porini/Nyikani/jangwani na alivaa nguo za ngozi na singa za ngamia akila nzige na asali, akijiepusha na maisha ya kawaida ya mitaani akiishi nyikani, kujidhabihu kwake kulionekana kimtazamo kuwa alikuwa nabii kweli kweli na  maarufu sana labda huenda kuliko hata Masihi, Yesu alivyokuja na mtindo wake wa maisha pengine pia na kuonekana kwake kama kijana mdogo wa miaka 30 hivi, Yohana alitahadharisha kuwa Yesu sio wa kulinganishwa naye kumlinganisha yeye Yesu ni sawa tu na msimamizi wa harusi na Bwana harusi mwenyewe, aliwathibitishia kuwa maagizo yote anayoyatoa Yesu ni muhimu akasikilizwa kwa kuwa Yeye ni wa mbinguni na Yohana ni wa duniani, Yesu ni wa mbinguni anatoka juu na yuko juu ya manabii wengine wote ambao asili yao ni ya dunia na wananena mambo ya duniani Lakini sivyo ilivyo kwa Yesu Kristo ambaye asili yake ni juu na ananena maswala kutoka mbinguni!.

Yohana 3:25-31 “Basi palitokea mashindano ya wanafunzi wa Yohana na Myahudi mmoja juu ya utakaso.Wakamwendea Yohana, wakamwambia, Rabi, yeye aliyekuwa pamoja nawe ng'ambo ya Yordani, yeye uliyemshuhudia, tazama, huyo anabatiza na watu wote wanamwendea. Yohana akajibu, akasema, Hawezi mtu kupokea neno lo lote isipokuwa amepewa kutoka mbinguni. Ninyi wenyewe mwanishuhudia ya kwamba nalisema, Mimi siye Kristo, bali nimetumwa mbele yake. Aliye naye bibi arusi ndiye bwana arusi; lakini rafiki yake bwana arusi, yeye anayesimama na kumsikia, aifurahia sana sauti yake bwana arusi. Basi hii furaha yangu imetimia. Yeye hana budi kuzidi, bali mimi kupungua. Yeye ajaye kutoka juu, huyo yu juu ya yote. Yeye aliye wa dunia, asili yake ni ya dunia, naye anena mambo ya duniani. Yeye ajaye kutoka mbinguni yu juu ya yote.”                 

Yohana alikuwa akiwahakikishia watu kuwa mamlaka ya Yesu sio ya kawaida  na kuwa iko juu kwa namna ambayo haiwezi kulinganishwa na mamlaka nyingine yoyote, alisema tena sifa za Yesu zinapaswa kuzidi na za kwake yaani Yohana mbatizaji zinapaswa kupungua, Yesu ni mwenye mamlaka na nguvu na hekina na akili na ujuzi na maarifa na ufahamu kuliko mtu mwingine yeyote, hakuna mamlaka, wala serikali,  wala usultani wala uongozi, wala bosi wala mwenye mamlaka wala mwenye serikali inayoweza kuzidi mamlaka aliyonayo Yesu Kristo, Yesu mwenyewe anathibitisha kuwa ameshuka kutoka mbinguni na anatakeleleza mapenzi ya baba yake wa mbinguni:-

Yohana 6:32-38 “Yesu akawaambia, Amin, amin, nawaambieni, Siye Musa aliyewapa chakula kile cha mbinguni, bali Baba yangu anawapa ninyi chakula cha kweli kitokacho mbinguni. Kwa maana chakula cha Mungu ni kile kishukacho kutoka mbinguni na kuupa ulimwengu uzima. Basi wakamwambia, Bwana, sikuzote utupe chakula hiki. Yesu akawaambia, Mimi ndimi chakula cha uzima; yeye ajaye kwangu hataona njaa kabisa, naye aniaminiye hataona kiu kamwe. Lakini naliwaambia ya kwamba mmeniona wala hamwamini. Wote anipao Baba watakuja kwangu; wala ye yote ajaye kwangu sitamtupa nje kamwe. Kwa kuwa mimi sikushuka kutoka mbinguni ili niyafanye mapenzi yangu, bali mapenzi yake aliyenipeleka.”

Yesu anadhihirisha wazi katika neno lake ya kuwa kama ile mana ilivyoshuka kutoka mbinguni na kuwapa uzima wa muda baba za wayahudi huko jangwani ambao kimsingi walikufa, yeye alikuwa anamaanisha kuwa ile mana ilikuwa ni ishara ya kuwa baba anawapa chakula kishukacho kutoka mbinguni na kuwa kama wakimuamini hawataona njaa tena na ya kuwa hawatakufa bali watakuwa na uzima wa milele wakati watu waliona kuwa yeye ni mwana wa seremala tu na wakidhani kuwa masihi atashuka moja kwa moja kwa jinsi ya kuonekana kimwili kama atakavyokuja mara ya pili duniani, Lakini masihi alikuja bila wao kuelewa. Ujio wa Yesu Kristo kutoka juu mbinguni una faida kubwa sana katika maisha ya wanadamu wote kama tutatambua kuwa Yesu yuko juu ya yote na kumuamini kuna faida lukuki ambazo tutafaidika kwa imani hii, Neno ajaye kutoka juu katika kiyunani linasomeka “Erchomai anōthen esti epanō ambapo maneno mawili “Anōthen na epanaō” yana maana “From the beginning he is over on” yaani mwenye mamlaka au mwenye cheo cha juu cha kijeshi tangu mwanzo, hii inazungumzia kuwa katika mamlaka za kijeshi Yesu ni jemadari tangu mwanzo na ni jemadari aliyeko juu ya mambo yote ya mbinguni na duniani, anaweza kukupigania vita ya aina yoyote ile, na anaweza kuagiza au kuamuru majeshi ya malaika kama amiri jeshi mkuu.         

Yeye ajaye kutoka juu, huyo yu juu ya yote!

Yohana sio tu katika majibu yake anataka kuonyesha kuwa Yesu asili yake sio ya dunia na kuwa Yesu asili yake ni kutoka juu, lakini pia anakazia kuwa yuko juu ya yote, Yohana anapotuelezea kuwa Yesu yuko juu ya yote anafunua faida kubwa zenye maana pana sana kwa kila mwamini ulimwenguni, hii inaonyesha kuwa Yesu ana mamlaka yote mbinguni na duniani, ana heshima ya kipekee na nafasi ya kwanza katika kila jambo, Yesu kuwa juu ya yote ina maana gani na faida gani hasa

-          Ana mamlaka yote mbinguni na Duniani – Mathayo 28:18 “Yesu akaja kwao, akasema nao, akawaambia, Nimepewa mamlaka yote mbinguni na duniani.” maana yake Serikali yake iko juu ya serikali zote, dola yake iko juu ya dola zote, mamlaka ya  kimwili na kiroho iko na yeye, kama ni kukata rufaa unakata kwake, kama ni hospitali ya rufaa yeye ndio hospitali ya mwisho, kama umeonewa yeye ndiye yuko juu ya wale waliokuonea ana mamlaka yote kama kuna watu wanajitukuza na kujiiinua juu yako basi kumbuka ya kuwa Yeye ana mamlaka kubwa kuliko hiyo yu juu ya yote, chochote kinachojiinua dhidi yako kikumbushwe kuwa Yuko aliye juu zaidi yake

 

-          Jina lake lina nguvu kuliko majina yote – Wafilipi 2:9-11 “Kwa hiyo tena Mungu alimwadhimisha mno, akamkirimia Jina lile lipitalo kila jina; ili kwa jina la Yesu kila goti lipigwe, la vitu vya mbinguni, na vya duniani, na vya chini ya nchi; na kila ulimi ukiri ya kuwa YESU KRISTO NI BWANA, kwa utukufu wa Mungu Baba.”

 

-          Hukumu yote ya wanadamu imewekwa chini yake – Matendo 17:31 “Kwa maana ameweka siku atakayowahukumu walimwengu kwa haki, kwa mtu yule aliyemchagua; naye amewapa watu wote uthabiti wa mambo haya kwa kumfufua katika wafu.”

 

Yohana 5:22-23 “Tena Baba hamhukumu mtu ye yote, bali amempa Mwana hukumu yote; ili watu wote wamheshimu Mwana kama vile wanavyomheshimu Baba. Asiyemheshimu Mwana hamheshimu Baba aliyempeleka.”   

 

-          Sisi tu warithi pamoja naye – Warumi 8:16-17 “Roho mwenyewe hushuhudia pamoja na roho zetu, ya kuwa sisi tu watoto wa Mungu; na kama tu watoto, basi, tu warithi; warithi wa Mungu, warithio pamoja na Kristo; naam, tukiteswa pamoja naye ili tupate na kutukuzwa pamoja naye.”

 

-          Yeye ndiye anayehusika na ufufuo – Yoahan 11:25 “Yesu akamwambia, Mimi ndimi huo ufufuo, na uzima. Yeye aniaminiye mimi, ajapokufa, atakuwa anaishi;”

 

-          Akifunga hakuna afunguaye, akifungua hakuna afungaye – Ufunuo 3:7-8 “Na kwa malaika wa kanisa lililoko Filadelfia andika; Haya ndiyo anenayo yeye aliye mtakatifu, aliye wa kweli, aliye na ufunguo wa Daudi, yeye mwenye kufungua wala hapana afungaye, naye afunga wala hapana afunguaye. Nayajua matendo yako. Tazama, nimekupa mlango uliofunguliwa mbele yako, ambao hapana awezaye kuufunga, kwa kuwa unazo nguvu kidogo, nawe umelitunza neno langu, wala hukulikana jina langu.”

 

-          Yeye ndiye mwanzo na mwisho Alfa na Omega – Ufunuo 1:8 “Mimi ni Alfa na Omega, mwanzo na mwisho, asema Bwana Mungu, aliyeko na aliyekuwako na atakayekuja, Mwenyezi.”

 

-          Ana mamlaka ya kusamehe dhambi – Marko 2:5-10 “Naye Yesu, alipoiona imani yao, akamwambia yule mwenye kupooza, Mwanangu, umesamehewa dhambi zako. Na baadhi ya waandishi walikuwako huko, wameketi, wakifikiri mioyoni mwao, Mbona huyu anasema hivi? Anakufuru. Ni nani awezaye kusamehe dhambi isipokuwa mmoja, ndiye Mungu? Mara Yesu akafahamu rohoni mwake kwamba wanafikiri hivyo nafsini mwao, akawaambia, Mbona mnafikiri hivi mioyoni mwenu? Vyepesi ni vipi, kumwambia mwenye kupooza, Umesamehewa dhambi zako, au kusema, Ondoka, ujitwike godoro lako, uende? Lakini mpate kujua ya kwamba Mwana wa Adamu anayo amri duniani ya kusamehe dhambi, (hapo amwambia yule mwenye kupooza)        

 

-          Ana mamlaka dhidi ya shetani - Wakolosai 2:14-15 “akiisha kuifuta ile hati iliyoandikwa ya kutushitaki kwa hukumu zake, iliyokuwa na uadui kwetu; akaiondoa isiwepo tena, akaigongomea msalabani; akiisha kuzivua enzi na mamlaka, na kuzifanya kuwa mkogo kwa ujasiri, akizishangilia katika msalaba huo.”

 

Yesu Kristo kuwa juu ya yote maana yake ana mamlaka ya kila kitu mbinguni na duniani na kuwa kila kitu kiko chini yake, yeye ni chanzo cha wokovu wetu wa mwili nafsi na roho, ni kiboko ya mahitaji yetu yote na ni mwenye nguvu dhidi ya adui zetu wote chochote kinachojiinua juu yako kikumbushe tu kuwa Yeye ajaye kutoka juu yu juu ya yote, mashetani, mapepo, wenye mamlaka wenye uwezo, wanajimu na wachawi, wasihiri, wapiga ramli, waganga wa kienyeji, waonevu,  magonjwa na mateso ya aina mbalimbali yakumbushwe tu kuwa Yeye ajaye kutoka juu  huyo yu juu ya yote, dhuruba yoyote ikikusumbua, mateso yoyote yakikusumbua, magonjwa yoyote yakikusumbua, majungu yoyote yakikusumbua, mtu yeyote akikusumbua, mwenye mamlaka yeyote akizingua, changamoto zozote zikikusumbua unapaswa kuzikumbusha tu kuwa AJAYE KUTOKA JUU HUYO YU JUU YA YOTE, Kristo Yesu sio wa kulinganishwa na nabii yeyote, wala mtume yeyote wa dini yeyote wala mwanafalsafa yeyoye, wala mwasiasa yeyote, wala msanii yeyote, wala kiongozi yeyote, watambulishe na kuwajulisha kuwa ajaye kutoka juu huyu yu juu ya yote, kama liko jambo linajitukuza juu yako, linaonekana kuwa gumu kwa sababu yoyote,  lina jina la kutisha, linakuogopesha, linakunyima usingizi, linakudhoofisha, iwe ni ndoa, watoto, kazini, biasharani, mdeni na kadhalika wote washitakie kwa Huyu mwamba aliye juu ya yote, aliye juu ya majeshi yote anayeweza kukushindia vita yoyote ambaye asili yake sio ya dunia huyu amekuja kutoka juu ana mamlaka yote kwa faida ya mahitaji yetu yu juu ya yote! Yesu kuwa juu ya yote maana yeke tunaweza kuliitia jina lake kwa changamoto zozote zile maana yeye yuko juu ya hizo, haupaswi kuogopa, haupaswi kulia, haupaswi kuhuzunika, haupaswi kusikitika tunaye aliye juu ya yote!

 

Na. Rev. Innocent Samuel Kamote

Mkuu wa wajenzi mwenye hekima!

0718990796