Alhamisi, 6 Novemba 2025

Msifungiwe nira pamoja na wasioamini


2Wakorintho 6:14-18. “Msifungiwe nira pamoja na wasioamini, kwa jinsi isivyo sawasawa; kwa maana pana urafiki gani kati ya haki na uasi? Tena pana shirika gani kati ya nuru na giza? Tena pana ulinganifu gani kati ya Kristo na Beliari? Au yeye aaminiye ana sehemu gani pamoja na yeye asiyeamini? Tena pana mapatano gani kati ya hekalu la Mungu na sanamu? Kwa maana sisi tu hekalu la Mungu aliye hai; kama Mungu alivyosema, ya kwamba, Nitakaa ndani yao, na kati yao nitatembea, nami nitakuwa Mungu wao, nao watakuwa watu wangu. Kwa hiyo, Tokeni kati yao, Mkatengwe nao, asema Bwana, Msiguse kitu kilicho kichafu, Nami nitawakaribisha.Nitakuwa Baba kwenu, Nanyi mtakuwa kwangu wanangu wa kiume na wa kike,”




Utangulizi:

Mojawapo ya fundisho muhimu sana katika maisha ya Ukristo ni pamoja na fundisho hili Msifungiwe nira pamoja na wasioamini! Fundisho hili kimsingi linawaonya wakristo kutokuwa na ushirika wa karibu sana na mtu asiyeamini, uhusiano huu ni ule unaoweza kuathiri uhusiano wetu tulio nao na Mungu, hii ikiwa na maana ya ushirikiano wa kibiashara, kindoa, uchumba na urafiki wa karibu wenye ushawishi mkubwa wa kimaadili na kimwenendo! Pamoja na maswala ya kiibada au maswala ya kiroho. Kimsingi kuna aina ya maisha ambayo wakristo tunapaswa kuyaishi katika mazingira ya maisha yetu ambayo yatasababisha uhusiano wetu na Mungu kuwa wa karibu na wa kudumu.

2Wakorintho 6:17-18 “Kwa hiyo, Tokeni kati yao, Mkatengwe nao, asema Bwana, Msiguse kitu kilicho kichafu, Nami nitawakaribisha. Nitakuwa Baba kwenu, Nanyi mtakuwa kwangu wanangu wa kiume na wa kike,”

Leo tutachukua muda kujifunza somo hili la msingi na la muhimu sana katika maisha ya wokovu Msifungiwe nira pamoja na wasioamini kwa kuzingatia vipengele vikuu muhimu vitatu vifuatavyo:-


·         Maana ya kufungiwa Nira.

·         Madhara ya kufungiwa Nira na wasioamini.

·         Faida za kutokufungiwa Nira na wasioamini.


Maana ya kufungiwa Nira

2Wakorintho 6:14-15 “Msifungiwe nira pamoja na wasioamini, kwa jinsi isivyo sawasawa; kwa maana pana urafiki gani kati ya haki na uasi? Tena pana shirika gani kati ya nuru na giza? Tena pana ulinganifu gani kati ya Kristo na Beliari? Au yeye aaminiye ana sehemu gani pamoja na yeye asiyeamini?

Ni muhimu kuwa na ufahamu wa kutosha kuhusiana na somo hili, ili hatimaye tuweze kuyatumia maandiko haya kwa faida ya ufalme wa Mungu bila kuathiri uwepo wetu katika jamii, jambo la msingi na la muhimu kwanza ni kuhakikisha ya kuwa tunakuwa na ufahamu wa maana ya neno “Nira”, Neno Nira katika Lugha ya Kiebrania linasomeka kama neno “Motah” na katika lugha ya kiyunani linasomeka kama neno “Zygos” yote yakiwa na maana ya kifaa cha mbao au cha chuma kinachofungwa au kuwekwa juu ya shingo za wanyama wawili wanaofanana wa kazi ili waweze kufanya kazi kwa pamoja aidha ya kulima au kuvuta mzigo, kwa kiingereza “Yoke”, lakini katika maana ya kiroho neno hili linamaanisha kufanya agano, au kuingia mkataba wa ushirika wa karibu sana na mtu, nchi, biashara au ndoa, au patano au agano kwa hiyo kufungiwa nira ni uhusiano wa karibu sana na mtu mwingine ili kushirikiana katika maswala nyeti na ya ndani kiimani, kimaisha, kindoa, kibiashara au ushirika wa kiroho au udhamini, au kupana mikono, au kuambatana, au kutoa udhamini wa kisheria mahakamani. Ushirika wa aina hii kimaandiko umekatazwa na tunaonywa kujihadhari nao kwa gharama yoyote ile kwa faida yetu! Na kwa faida ya ushirika wetu na Mungu.

Agizo la kutokufungiwa nira katika andiko hili maana yake ni maneno ya fumbo “metaphor” lenye kumaanisha kuwa mtu anayemuamini Mungu ni tofauti na mtu asiyemuamini Mungu na kwa sababu hiyo hawawezi kutekeleza lengo moja lenye kumuhusisha Mungu kwa pamoja, Mtu alieyemuamini Mungu ni kama na mnyama kazi aliyefundishwa kufanya kazi, na yule asiyeamini ni kama mnyama asiyefundishwa kufanya kazi kwa hiyo lengo la kuifanya kazi iliyokusudiwa haiwezi kutimia au kufikia malengo ni sawa na kuvalishwa Nira kwa wanyama wa aina mbili tofauti jambo ambalo linaweza kusababisha maumivu kwa mmoja kwa sababu hawalingani uwezo na hawafanani  na nguvu zao pia haziko sawa! Au umri wa wanyama kazi hao au vimo vyao vinatofautiana sana! Na hivyo kum-athiri mwingine

Walawi 19:19 “Mtazishika amri zangu. Usiwaache wanyama wako wa mfugo wakazaana kwa namna mbalimbali; usipande shamba lako mbegu za namna mbili pamoja; wala usivae mwilini mwako nguo ya namna mbili zilizochanganywa pamoja.”

Kumbukumbu 22:9-10 “Usipande shamba lako la mizabibu aina mbili za mbegu; yasije yakaondolewa matunda yote, mbegu ulizopanda na maongeo ya mizabibu yako. Usilime kwa ng'ombe na punda wakikokota jembe pamoja.”

Zaburi 1:1-3 “Heri mtu yule asiyekwenda Katika shauri la wasio haki; Wala hakusimama katika njia ya wakosaji; Wala hakuketi barazani pa wenye mizaha. Bali sheria ya Bwana ndiyo impendezayo, Na sheria yake huitafakari mchana na usiku. Naye atakuwa kama mti uliopandwa Kandokando ya vijito vya maji, Uzaao matunda yake kwa majira yake, Wala jani lake halinyauki; Na kila alitendalo litafanikiwa.”

Watu walioamini ni aina nyingine ya mbegu na haiwezi kuchanganywa na watu wasioamini, ambao ni mbegu nyingine, watu wa Mungu hawawezi kuwa na ushirika wa karibu au wa kiagano au wa kiibada au wa kindoa na watu wasioamini, kuwaunganisha hivyo ni sawa na kuweka wanyamakazi Punda na Ng’ombe ambao kimsingi hawafanani wala hawalingani na hawawezi kufanya kazi moja kwa pamoja,  na sio haki kuwafunganisha pamoja, watu waaminio wana sheria na wasioamini hawana sheria, waaminio wanaishi kwa maelekezo ya Mungu wasioamini wanaishi watakavyo, walioamini wanajifunza na kufundishwa namna na jinsi ya kutembea na Mungu wasioamini ni tofauti wanafuata kawaida ya ulimwengu huu kwa hiyo hakuna ulinganifu wa kimzani kati ya mtu aliyemuamini Mungu na yule asiyeamini. Mmoja ni hekalu la Mungu mwingine ni hekalu la sanamu, hii ni lugha ya hali ya juu na ya ndani yenye kusisitiza utofauti ulioko kati ya mtu aliyeokoka na mtu asiyeokoka, aaminiye na asiyeamini, lugha zinazotumika kuelezea ushirika huu katika kiingreza “Be ye not unequally yoked together with unbelievers” kisha kuna maneno fellowship, communion, concord, part, agreement. kwa hiyo kuna maneno unequally, fellowship, communion, concord, part, agreement ambayo katika kiyunani yanasomeka kama Heterozugeo, (Associate), Motechē (Participation or intercourse), sumphonēsis (Concord, Harmony, a state of agreement), Meris (Share, Patakers), sugkatathesis – soong-kat-ath’-es-is (in company) kwa hiyo ukiyaangalia maneno hayo yote yanayotumika katika kifungu hiki cha 2Wakorintho 6:14-18 yanamaanisha kuwa hatupaswi kamwe kuambatana, kushirikiana, kuingiliana, kukubaliana nao, kushirikisha, kufanya urafiki, kufanya kazi moja, kuchanganyika nao katika jambo moja mfano kama vyombo vya muziki vinapopigwa gitaa, ngoma, na kinanda, kisha vikatoa mziki wa aina moja, “a simultaneous cccurence of two or more musical tones that produce an impression of agreeableness or resolution on a listener” kwa hiyo wakristo wanapofanya ushirika wa aina hii unaokatazwa na maandiko yanatufundisha kuwa kitakachotokea kitaalamu kinaitwa “DISCORD” – “a lack of agreement or harmony as between persons, things or ideas, active quarrelling or conflict resulting from discord among person or function” “harsh or unpleasant sound” hali itakayozalishwa itakuwa ni kelele za kutokukubaliana, kutokufikia muafaka, kupingana kimawazo na kimtazamo, kutokea kwa migogoro na ugomvi, kukosekana kwa amani na utulivu, kukosekana kwa utaratibu na ustaarabu, ugomvi endelevu, chuki na sauti zisizopendeza,  kwa sababu hiyo uwepo wa Mungu hauwezi kuwepo mahali pa namna hiyo  ni mpaka mtu wa Mungu ajiondoe kwenye patano la aina hiyo.

Nira huwaunganisha wanyama wawili wa aina moja na kuwafanya wafanye kazi moja wanyama hao ni kama ng’ombe kwa ng’ombe na punda kwa punda, Wanyama hao wanapokuwa hawafanani kuna uwezekano mkubwa wa kuumizana  na kumuathiri mmoja kwani wanaweza kuwa na tofauti ya nguvu na kimo, (horse power) Nguvu ya punda na ng’ombe zinatofautiana, aidha hata kiumri wakati mwingine wanatakiwa kufanana kama, hawafanani kunakuweko uwezekano mkubwa wa kuifanya kazi isiwe na ufanisi au kazi inakuwa ngumu sana na kusababisha maumivu na makwazo kwa kila mmoja. Lakini mbaya zaidi ni kuondoa uwepo wa Mungu, kwa hiyo agizo la Msifungiwe nira na wasioamini lina faida kubwa sana kwa Mkristo, mtu wa Mungu, kuliko tunavyoweza kufikiri.  Kwa hiyo hata mtu aliyeokoka akishiriki mapenzi na mtu asiyeokoka ni sawa na kuchukua viungo vya Kristo na kuvifanya vya kahaba

1Wakorintho 6:15-17 “Je! Hamjui ya kuwa miili yenu ni viungo vya Kristo? Basi nivitwae viungo vya Kristo na kuvifanya viungo vya kahaba? Hasha! Au hamjui ya kuwa yeye aliyeungwa na kahaba ni mwili mmoja naye? Maana asema, Wale wawili watakuwa mwili mmoja.  Lakini yeye aliyeungwa na Bwana ni roho moja naye.”   

Amosi 3:3 “Je! Watu wawili waweza kutembea pamoja, wasipokuwa wamepatana?

Neno la Mungu hapo linaonya kutokuingia katika ushirika wa karibu au uhusiano wa ndani sana na kujifunga na watu mnaotofautiana kiimani au hata kimafundisho, kimsingi tunaonywa kutokuchukuliana na wasioamini katika imani kwani imani yao na uadilifu wao na akili zao ni tofauti na kwa sababu hiyo upande mmoja unaweza kusababishiwa makwazo, majuto, maumivu na machungu na kuondoa ufanisi katika utii na uchaji wa Mungu. Hii haimaanishi kutokuweko kabisa duniani, au kutokushirikiana na watu wa dunia hii katika kuleta maendeleo, hapana bali neno la Mungu hapa linatoa tahadhari ya kutokujifunga kiagano, kipatano na kirafiki, na ushawishi na walimwengu kwani kimsingi badala ya wewe kuwavuta na kuwashawishi wewe mtu wa Mungu ndiye unayeweza kuathiriwa. “Believers should not be in close partnership with non- believers” Waamini hawapaswi kuwa na ushirika wa karibu na wasioamini. Ili kuwaepushia na madhara yanayoweza kuumiza mioyo yao na kupoteza ushirika na uwepo wa Mungu.

Madhara ya kufungiwa Nira na wasioamini.

Biblia iko makini sana na ushirikiano wa kiroho na muungano wa kiroho na agano la kiroho kati ya watu waaminio na wasioamini, kwa sababu Mungu anajua wazi kuwa kuna madhara makubwa sana katika muungano huo na shughuli zake haziwezi kwenda kwa ufanisi unaohitajika, ili Mungu atembee katikati yetu kwa uhuru na Baraka, Kimsingi hakuna kitu kinaweza kumzuia Mungu kutekeleza kutimiza kusudi, lake hata hivyo kwa kanuni ya neno lake Mungu ni kwamba kutofungiwa nira kuna:-

a.       Kuepusha migogoro ya kimaadili na kiimani – Watu wasioamini hawana Msingi wa Neno la Mungu, sawa na mnyama asiyefunzwa au kuandaliwa kama mnyama kazi na hivyo mtazamo wao kuhusu Ndoa, Biashara au maisha ya kiroho unapingana na ule msimamo wa maelekezo ya neno la Mungu, kwa sababu hiyo neno la Mungu linaagiza kwa ukali kuacha mahusiano nao, kwa maana nyingine kufanya maamuzi magumu ya kujiepusha nao (kuua, au kukata). Kuvunja na kuharibu kabisa mahusiano na wale wanaoweza kukukosesha.

 

Kumbukumbu 13:6-10 “Atakapokushawishi kwa siri ndugu yako, mwana wa mamaako, au mwana wako, au binti yako, au mke wa kifuani mwako, au rafiki yako aliye kama moyo wako, akikuambia, Twende tukaabudu miungu mingine usiyoijua wewe wala baba zako; katika miungu ya mataifa yaliyo kando-kando yenu karibu nawe au mbali nawe, tokea ncha moja ya dunia hata ncha ya pili ya dunia; usimkubalie wala usimsikize; wala jicho lako lisimwonee huruma, wala usimwache, wala usimfiche; mwue kweli; mkono wako na uwe wa kwanza juu yake katika kumwua, na baadaye mikono ya watu wote. Nawe mtupie mawe hata afe; kwa kuwa alitaka kukupotoa na Bwana, Mungu wako aliyekutoa katika nchi ya Misri, katika nyumba ya utumwa.”

 

Mathayo 18:8-9 “Basi mkono wako au mguu wako ukikukosesha, ukate ukautupe mbali nawe; ni afadhali kuingia katika uzima hali umepungukiwa na mkono au mguu, kuliko kuwa na mikono miwili au miguu miwili, na kutupwa katika moto wa milele. Na jicho lako likikukosesha, ling'oe, ukalitupe mbali nawe; ni afadhali kuingia katika uzima una chongo, kuliko kuwa na macho mawili, na kutupwa katika jehanum ya moto.”

                 

Maandiko yanatumia lugha ya mkazo au mkuzo kitaalamu inaitwa “Hyperbole” kufundisha au kusisitiza msimamo mkali (Radical Action) kuhusiana na maisha ya dhambi na madhara yake, kwa hiyo katika maandiko hayo juu, maana yake sio katika uhalisia wa lugha iliyotumika lakini ni kuchukua hatua madhubuti au kufanya maamuzi magumu ya mabadiliko ya kitabia au kijamaa au kirafiki na watu wanaokukosesha au wenye kukupa ushawishi kuelekea katika maisha ya dhambi, ni afadhali kuua urafiki huo au ni afadhali urafiki huo ufe kuliko kuwa na mtu au watu au ushirika unaokufanya uende motoni, kwa hiyo Musa anaposema ndugu yako akikushawishi muue, na Yesu anaposema mkono wako au mguu wako ukikukosesha uukate wote wanaanisha kufanya maamuzi magumu kwaajili ya uzima wa milele kuliko kuchukuliana (Compromising) ambako kutakusababishia uende jehanamu ya moto kwa hiyo fundisho la kutokufungiwa nira hali kadhalika ni mkazo wa kufanya maamuzi magumu kujiondoa au kujitoa katika ushirika unaotushawishi kuishi maisha ya dhambi na yenye tofauti za kimtazamo na kiitikadi. Nuru na giza, au haki na uasi. Kwa hiyo neno la Mungu linatutaka tuache uhusiano unaotupelekea kumkosea Mungu au kujitia unajisi.

 

Waebrania 12:3-4 “Maana mtafakarini sana yeye aliyeyastahimili mapingamizi makuu namna hii ya watendao dhambi juu ya nafsi zao, msije mkachoka, mkizimia mioyoni mwenu. Hamjafanya vita hata kumwagika damu, mkishindana na dhambi;”

 

b.      Huduma na maisha ya Imani hudhoofika – Kufungiwa nira na wasioamini kunasababisha mtu akosane na Mungu na Mungu asitembee pamoja naye, Huduma ya mtu aliyefungiwa nira na wasioamini hudhoofika na kumfanya mtu kudhoofika kiimani na kihuduma na kuwa mbali na Mungu, au badala ya kumtumikia Mungu kwa furaha na moyo mweupe unaishi maisha ya maumivu mengi, kurudi nyuma kukwazwa, kudhoofishwa, kuchukizwa, kukosa amani na kukata tamaa badala ya kutiwa moyo, kuambatana na kushikamana na watu wa Mungu kunaleta uchochezi mkubwa wa kusonga mbele katika maisha ya wokovu na ustawi badala ya kudhoofika na kusinyaa au kupoa. Jambo hili linapunguza uwepo wa Mungu katika maisha yetu, Mfalme Suleimani aliyekuwa anampenda Mungu kiasi cha kutokewa na Mungu mara mbili katika maisha yake na kupewa akili na hekima nyingi kuliko mtu yeyote kbla yake au baada yake alipoa sana kiroho kiasi cha kuabudu miungu mingine kutokana na kushikamana na wake zake na kuwasikiliza na kuwatii ili kuwapendeza na wakamfanya apoe kiroho na kuabudu miungu mingine jambo ambalo lilimuhuzunisha sana Mungu!.

 

2Wakorintho 6:17-18.“Kwa hiyo, Tokeni kati yao, Mkatengwe nao, asema Bwana, Msiguse kitu kilicho kichafu, Nami nitawakaribisha. Nitakuwa Baba kwenu, Nanyi mtakuwa kwangu wanangu wa kiume na wa kike,”

 

1Wafalme 11:1-4 “Mfalme Sulemani akawapenda wanawake wengi wageni, pamoja na binti yake Farao, wanawake wa Wamoabi, na wa Waamoni, na wa Waedomi, na wa Wasidoni, na wa Wahiti, na wa mataifa Bwana aliyowaambia wana wa Israeli, Msiingie kwao, wala wasiingie kwenu; kwa kuwa hakika wataigeuza mioyo yenu kuifuata miungu yao. Sulemani akaambatana nao kwa kuwapenda. Akawa na wake mia saba binti za kifalme, na masuria mia tatu; nao wakeze wakamgeuza moyo. Maana ikawa, Sulemani alipokuwa mzee, wake zake wakamgeuza moyo wake, afuate miungu mingine, wala moyo wake haukuwa mkamilifu kwa Bwana, Mungu wake, kama moyo wa Daudi baba yake.”

 

c.       Kufanyika mtego na mjeledi kwa watu wa Mungu - Mungu aliwaonya Israel kuwa endapo wataungana na wenyeji na kuoana na watu hawa wasiomcha Mungu watu hao watakuwa mtego kwao, watakuwa kwazo na mtego na mzigo mzito shingoni mwao, lakini pia watakuwa mjeledi yaani watasababisha maumivu makali katika maisha yao watakuwa miiba, na Mungu hatawaondoa, itakuwa kama adhabu ya ukaidi kinyume na agizo la Mungu. Kwa ujumla kumpenda Mungu kunaenda sambamba na kujitenga na uovu na watu waovu

 

Yoshua 23:11-13 “Jihadharini nafsi zenu, basi, ili mmpende Bwana, Mungu wenu. Lakini mkirudi nyuma kwa njia yo yote na kushikamana na mabaki ya mataifa, yaani, mataifa haya yaliyobaki kati yenu, na kuoana nao, na kuingia kwao, nao kuingia kwenu; jueni hakika ya kuwa Bwana, Mungu wenu, hatawafukuza tena mataifa haya mbele ya macho yenu, bali watakuwa mtego kwenu na tanzi, na mjeledi mbavuni mwenu, na miiba machoni mwenu, hata mtakapoangamia na kutoka katika nchi hii njema, ambayo Bwana, Mungu wenu, amewapa ninyi.”       

 

Kumbukumbu 7:1-6 “Bwana, Mungu wako, atakapokutia katika nchi uendayo kuimiliki, atakapoyang'oa mataifa mengi watoke mbele yako, Mhiti, na Mgirgashi, na Mwamori, na Mkanaani, na Mperizi, na Mhivi, na Myebusi, mataifa saba makubwa yenye nguvu kukupita wewe; wakati Bwana, Mungu wako, atakapowatoa mbele yako, nawe utawapiga; wakati huo ndipo uwaondoe kabisa; usifanye agano nao, wala kuwahurumia; wala usioane nao; binti yako usimpe mwanawe mume, wala usimtwalie mwanao mume binti yake. Kwa kuwa atamkengeusha mwanao mume asinifuate, ili wapate kuabudu miungu mingine; ndipo itakapowaka hasira ya Bwana juu yenu, naye atakuangamiza upesi. Lakini watendeni hivi; zivunjeni madhabahu zao zibomosheni nguzo zao, yakateni maashera yao, ziteketezeni kwa moto sanamu zao za kuchonga. Kwa maana wewe u taifa takatifu kwa Bwana, Mungu wako; Bwana Mungu wako, amekuchagua kuwa watu wake hasa, zaidi ya mataifa yote walioko juu ya uso wa nchi.”

 

Ezra 9:10-12. “Na sasa, Ee Mungu wetu, tuseme nini baada ya hayo? Maana tumeziacha amri zako, ulizoziamuru kwa midomo ya watumishi wako, manabii, ukisema, Nchi ile, mnayoiendea ili kuimiliki, ni nchi ya uchafu, kwa sababu ya uchafu wa watu wa nchi zile, kwa ajili ya machukizo yao, yaliyoijaza tangu upande huu mpaka upande huu, kwa uchafu wao. Basi, msiwape wana wao binti zenu, wala msitwae binti zao kuwa wake za wana wenu, wala msiwatakie amani wala kufanikiwa milele; ili mpate kuwa hodari, na kula wema wa nchi hiyo, na kuwaachia watoto wenu iwe urithi wa milele.”

               

Nehemia 13:23-26 “Tena siku zizo hizo nikawaona wale Wayahudi waliokuwa wameoa wanawake wa Ashdodi, na Amoni, na Moabu; na watoto wao wakanena nusu kwa lugha ya Ashdodi, wala hawakuweza kunena kwa Kiyahudi, bali kwa lugha ya watu hao mojawapo. Nikagombana nao, nikawalaani, nikawapiga baadhi yao, na kuwang'oa nywele zao; nikawaapisha kwa Mungu, nikasema, Msiwaoze wana wao binti zenu, wala msiwatwae binti zao ili waolewe na wana wenu, wala na ninyi wenyewe. Je! Sulemani, mwana wa Daudi, hakufanya dhambi kwa kutenda hayo? Lakini katika mataifa mengi hapakuwa na mfalme mwingine mfano wake. Tena alipendwa na Mungu wake, naye Mungu akamfanya mfalme juu ya Israeli; walakini wanawake wageni walimkosesha hata yeye.”

 

Vifungu hivi vyote vinatukumbusha wazi kuwa watu wa Mungu ni tofauti na watu wa dunia hii, watu wa Mungu wana utamaduni wao, utamaduni wao ni neno la Mungu, mtu wa dunia hii anaweza kujiunga na utamaduni huo kwa kuokoka, au kwa kuona na kuvutiwa na maisha yetu ambayo ni nuru ndani ya Kristo, kwa kweli jaribio lolote la kuwaoa au kuoana nao na kutarajia mabadiliko kutoka kwao ambayo hayatokani na Mungu kunaweza kuwa mtego kwetu na kwa watoto wetu, Musa aliliona hilo na Nehemia na Ezra pia walilikemea na Paulo anatukumbusha juu ya maamuzi haya Nehemia anawakumbusha Israel kuwa huwezi kutumia Hekima, kwani hata mtu mwenye Hekima aliyependwa na Mungu yaani Suleimani alibadilishwa moyo kwa mtego huu, Mungu anamtarajia mtu wake kuwa tofauti na watu wa dunia hii, na kutokuishi sawa na watu wa dunia hii wasiojali sheria na maadili ya kiungu ambayo ni Muhimu kwa uwepo wa Mungu, hii haina maana ya kuwa Mungu ni mbaguzi la hasha hata kidogo, lakini Mungu anataka kupitia sisi watu wa mataifa yote wageuzwe moyo na kumuelekea Mungu aliye hai na wa kweli.

 

Mathayo 5:14-16 “Ninyi ni nuru ya ulimwengu. Mji hauwezi kusitirika ukiwa juu ya mlima. Wala watu hawawashi taa na kuiweka chini ya pishi, bali juu ya kiango; nayo yawaangaza wote waliomo nyumbani. Vivyo hivyo nuru yenu na iangaze mbele ya watu, wapate kuyaona matendo yenu mema, wamtukuze Baba yenu aliye mbinguni.”                

 

d.      Kuzuia ukuaji wako wa kiroho – Kufungiwa nira pamoja na wasioamini hukufunga wewe katika hali yako ya kiroho na kuzuia ukuaji wako wa kiroho, Mtu aaminiye anapounganishwa na asiyeamini ushawishi wake wa kiroho unaathiriwa na kukengeushwa kwa ujumla kunakuwa na ugumu mkubwa kuishi maisha ya kumuheshimu Mungu, Mtu aliyeokoka anamwamini Kristo, Mtu asiyeokoka anamwamini Beliari, ubaradhuli, Mtu aliyeamini ni Hekalu la Mungu, mtu asiyeamini ni Sanamu, Mtu aliyeamini ni Nuru, mtu asiyeamini ni Giza, hawa ni wanyama wasiofanana hawawezi kwenda pamoja maumivu makali sana yatatokea, watu wengi waliokiuka kanuni hii wameumia sana, hakuwezi kuwako mafanikio ya kiroho na mafanikio ya kihuduma kwa watu ambao wamefungiwa Nira na wasioamini hakuna patano! Hapo wala hakuna shirika!

 

2Wakorintho 6:14-16 “Msifungiwe nira pamoja na wasioamini, kwa jinsi isivyo sawasawa; kwa maana pana urafiki gani kati ya haki na uasi? Tena pana shirika gani kati ya nuru na giza? Tena pana ulinganifu gani kati ya Kristo na Beliari? Au yeye aaminiye ana sehemu gani pamoja na yeye asiyeamini? Tena pana mapatano gani kati ya hekalu la Mungu na sanamu? Kwa maana sisi tu hekalu la Mungu aliye hai; kama Mungu alivyosema, ya kwamba, Nitakaa ndani yao, na kati yao nitatembea, nami nitakuwa Mungu wao, nao watakuwa watu wangu.”

                               

e.      Kuharibika kwa tabia njema – 1Wakorintho 13:33-34 “Msidanganyike; Mazungumzo mabaya huharibu tabia njema. Tumieni akili kama ipasavyo, wala msitende dhambi; kwa maana wengine hawamjui Mungu. Ninanena hayo niwafedheheshe.”

 

Kanuni ya kutokufungiwa nira na wasioamini pia inakwenda kugusa urafiki wa karibu, kuingia katika kufanya biashara au kuingia katika agano au kumdhamini mtu muovu waamini wanaaswa na maandiko kujihadhari kwani inaweza kukuweka matatani katika maswala ya imani yako kinyume na wasioamini, Neno mazungumzo mabaya katika Biblia ya kiingereza yanasomeka “Bad Company” neno la kiyunani linalotumika hapo ni “Homilia” ambalo ni sawa na neno la kiingereza “Companionship” au “intercourse” hii ikiwa na maana ya ushirika wa karibu na mtu muovu au watu waovu unamchango mkubwa sana katika kuharibu tabia njema, kwa hiyo waaminio hawapaswi kamwe kuwa na ukaribu wa kina na watu wenye ushawishi wa kutenda uovu, au wenye tabia mbaya ondoa watu wote wenye kusudi tofauti na lako kwa Mungu. 

 

Mithali 1:10-16 “Mwanangu, wenye dhambi wakikushawishi, Wewe usikubali. Wakisema, Haya! Njoo pamoja nasi, Na tuvizie ili kumwaga damu; Tumwotee asiye na hatia, bila sababu; Tuwameze hai kama kuzimu, Na wazima, kama wao washukao shimoni. Tutapata mali yote ya thamani, Tutazijaza nyumba zetu mateka.Wewe utashirikiana nasi; Tutakuwa na vitu vyote shirika. Mwanangu, usiende njiani pamoja nao; Uzuie mguu wako usiende katika mapito yao.”

 

f.        Kulinda utamaduni wa kikanisa – Kanisa ni chombo chenye utamaduni wake, tabia na maisha na mwenendo wetu ni tofauti na watu wa dunia hii, kufungiwa nira na wasioamini kunauwa utamaduni wa kanisa na kulifanya kanisa kupoteza ushawishi wake duniani, unaposoma yale yaliyomkuta Nehemia utagundua kuwa Mungu alikuwa na Mpango wa kulitunza Taifa la Israel ili liweze kuwa taifa la mfano na liwe Baraka kwa ulimwengu, kusudi hilo hilo limeletwa kwa kanisa, Kanisa leo limekuwa na utamaduni mchanganyiko kama ilivyokuwa kwa Israel, tabia nyingi sana zisizo za kiadilifu zimeingia makanisani, kuna kanisa moja katika mji fulani nilifika na kukuta hakuna mikesha huko, na kiongozi wa mahali hapo akaniambia anaogopa kufanya mikesha kwa sababu mikesha hiyo inatumiwa na vijana kufanya uovu, mikesha ni njia ya kanisa kupata muda mrefu wa kuomba pamoja lakini kama kanisa linafikia hatua ya kuogopa kukesha kwa sababu ya uasherati basi hakuna tofauti na wale wanaokwenda kukesha katika disco na ngoma utamaduni wa kumtafuta Bwana umetoweka, utamaduni wa kumcha Mungu na kuutafuta uso wake kwa bidi umetoweka na tabia za ajabu zimaingia, lugha na mwenendo umeathiriwa na mchanganyiko mkubwa wa kitabia umeingilia kati.  

 

Nehemia 13:23-25 “Tena siku zizo hizo nikawaona wale Wayahudi waliokuwa wameoa wanawake wa Ashdodi, na Amoni, na Moabu; na watoto wao wakanena nusu kwa lugha ya Ashdodi, wala hawakuweza kunena kwa Kiyahudi, bali kwa lugha ya watu hao mojawapo. Nikagombana nao, nikawalaani, nikawapiga baadhi yao, na kuwang'oa nywele zao; nikawaapisha kwa Mungu, nikasema, Msiwaoze wana wao binti zenu, wala msiwatwae binti zao ili waolewe na wana wenu, wala na ninyi wenyewe.”

 

1Petro 2:9-10 “Bali ninyi ni mzao mteule, ukuhani wa kifalme, taifa takatifu, watu wa milki ya Mungu, mpate kuzitangaza fadhili zake yeye aliyewaita mtoke gizani mkaingie katika nuru yake ya ajabu; ninyi mliokuwa kwanza si taifa, bali sasa ni taifa la Mungu; mliokuwa hamkupata rehema, bali sasa mmepata rehema.”

 

Warumi 12:2 “Wala msiifuatishe namna ya dunia hii; bali mgeuzwe kwa kufanywa upya nia zenu, mpate kujua hakika mapenzi ya Mungu yaliyo mema, ya kumpendeza, na ukamilifu.”

 

Kanisa ni taifa ni mzao mteule ni ukuhani wa kifalme, ni taifa takatifu, ni wtu wa miliki ya Mungu, Mungu amelitenga kanisa na dunia kwa sababu hiyo ni lazima kanisa likae katika utamaduni wake, kufungiwa nira na wasioamini kutalifanya kanisa kupoteza utaifa wake na utamaduni wake kwa hiyo badala ya waamini kuchukuliwa na tamaduni za ulimwengu huu, maandiko yanasisitiza kutokuenenda kwa viwango vya watu wa dunia hii, kwa hiyo ni lazima tujitoe kwa ukamilifu kwa Mungu  na kuyatoa maisha yetu kwake na kujihadhari sana na kujaribu kufuata tamaduni za ulimwengu huu, Mungu anataka iwe hivyo kwa wake zetu, waume zetu na watoto tutakaowazaa baadae wote waifuate njia ya Mungu na neno lake, sasa tukikubali kufungiwa nira tutapoteza hilo utamaduni wa kibiblia na wa kikanisa ambao Mungu ametuandaa sisi kuwa watu wa tofauti. Kumbuka wakati Israel waliposhuka Misri, Mungu aliugusa moyo wa Farao kuwapa nchi ya Gosheni, ili wasichangamane na Wamisri, kwani tamaduni zao zilikuwa tofauti na wamsiri hawachangamani na wafugaji jambo hili lilisaidia katiia kuwafanya Israel kuwa taifa la kipekee waliokuwa na kuongezeka katika inchi ya Misri, na kuwa na utamaduni wao na bila ya kupoteza utaifa wao na upekee wao kama Waebrania.

 

Mwanzo 46:31-34 “Yusufu akawaambia ndugu zake na watu wa nyumbani mwa baba yake, Nitapanda mimi nimpashe Farao habari; nitamwambia, Ndugu zangu, na watu wa nyumbani mwa baba yangu, waliokuwa katika nchi ya Kanaani, wamenijia. Na watu hao ni wachungaji, maana wamekuwa watu wa kuchunga wanyama, nao wameleta kondoo zao, na ng'ombe zao, na yote waliyo nayo. Itakuwa Farao atakapowaita, na kuwauliza, Kazi yenu ni nini? Semeni, Watumwa wako tumekuwa wachunga wanyama tangu ujana wetu, na hata leo, sisi, na baba zetu; mpate kukaa katika nchi ya Gosheni; maana kila mchunga wanyama ni chukizo kwa Wamisri.”

Faida za kutokufungiwa Nira na wasioamini

Paulo anapotukumbusha au kuwakumbusha Wakorintho kutokufungiwa Nira na wasioamini alikuwa anataka watu wa Mungu wawe na uhuru wa kumtumikia Mungu kwa ukamilifu, kujiwekea mipaka ya utakatifu, kuwa na amani ya moyo, kukua kwa haraka kiroho na kuepusha mivutano isiyo na ulazima, na zaidi sana kuruhusu uwepo wa Mungu katika maisha yetu, haya ni maswala ya msingi sana kama tulivyojifunza ya kuwa kuna madhara ya kufungiwa nira na wasioamini, Lakini kuna faida kubwa za kutokufungiwa nira na wasioamini. Moja ikiwa pamoja na kufurahia uwepo wa Mungu hususani katika ndoa zetu, urafiki wa karibu, ushirika wa kibiashara na ufikiaji wa malengi ya kiungu.

1Wakorintho 7:35 “Nasema hayo niwafaidie, si kwamba niwategee tanzi, bali kwa ajili ya vile vipendezavyo, tena mpate kumhudumia Bwana pasipo kuvutwa na mambo mengine.”

Kuoa au kuolewa au kufanya agano na kuwa na ushirika wa karibu au kupatana yaani kufungiwa nira kwa kuwa na mahusiano ya karibu na mtu asiyemjua Mungu au kupata mafundisho ya kutosha kuhusu huduma ya Mungu kunatengeneza mazingira ya mgawanyiko na migogoro inayoathiri utumishi wako kwa Mungu, muelekeo wako kwa Mungu unaathiriwa na mtu asiyemjua Mungu, kama mtu anataka kumtumikia Mungu kwa uhuru ni vema ukajitoa katika nira hiyo na kama umeshaingia ni ngumu kujitoa utalibeba, lakini kama hujaingia chukua tahadhari za kibiblia

2Wakorintho 6:17-18 “Kwa hiyo, Tokeni kati yao, Mkatengwe nao, asema Bwana, Msiguse kitu kilicho kichafu, Nami nitawakaribisha.Nitakuwa Baba kwenu, Nanyi mtakuwa kwangu wanangu wa kiume na wa kike,”

Kanisa limeitwa au lina wito wa kuishi maisha matakatifu, maandiko yanakiri kwamba pasipo utakatifu haiwezekani kumuona Mungu, maisha ya Utakatifu yanahusisha kutengwa na kujitenga, Kwamba Mungu anakutenga wewe na mimi kwa kazi maalumu, sisi nasi tunawajibu wa kujitenga na dunia kwa sababu Mungu aliyetuita ni Mtakatifu kwa hiyo wito wa kutokufungiwa nira na wasioamini unamuita kila mmoja wetu kuishi maisha Matakatifu.

1Petro 1:15-16 “bali kama yeye aliyewaita alivyo mtakatifu, ninyi nanyi iweni watakatifu katika mwenendo wenu wote; kwa maana imeandikwa, Mtakuwa watakatifu kwa kuwa mimi ni mtakatifu.”

Waebrania 12:14Tafuteni kwa bidii kuwa na amani na watu wote, na huo utakatifu, ambao hapana mtu atakayemwona Bwana asipokuwa nao;”

Kufukia malengo ya kiroho kwa Amani – Kimsingi watu wanapokuwa wamefungiwa nira maana yake wanatengeneza mwelekeo mmoja na kwa sababu hiyo lengo lao la kimwili na kiroho linakuwa moja kwa msingi huo inakuwa rahisi kwao kutimiza makusudi yao kwa Amani na utulivu na hivyo lengo lao linakuwa rahisi na lenye kuzaa matunda, sawa na ng’ombe ambao wamefunzwa kulima maana yake wote wataifanya kazi ya kulima au kusukuma mkokoteni wa kizigo kwa ufanisi kwa sababu wote wana mafunzo yanayolingana, lakini wanyama kazi hao wanapokuwa hawana ulinganifu mambo huharibika mwenendo hauwezi kuwa sawa na kunatokea maumivu makali, kuumizana na kukwazana na kusababisha kutokufikiwa kwa malengo yanayokusudiwa, Nilielezewa na Marabi wa Kiyahudi kuhusu habari za Iditi  “Idit”  kwa mujibu wa maelezo yao katika vitabu vya masimulizi ya kiyahudi kiitwacho Midrash Aggadah, Idit lilikuwa jina la mke wa Lutu, Biblia hailelezi mengi kuhusu mke wa Lutu na wala haitaji jina lake, Lakini Marabi wa kiyahudi wanaeleza ya kuwa mwanamke huyu hakuwa mkarimu kwa wageni tofauti na ilivyokuwa na mumewe, Marabi wanasema mwanamke huyu alikuwa na tabia sawa na watu wengi walioishi Sodoma, ni wazi kuwa huenda Lutu alimpata mwanamke huyu katika miji hii, Mwanamke huyu hakuwa mwema na inaelezwa kuwa hata malaika wale wagani walipowatembelea ni Mumewe ndiye aliyeonekana kuwachangamkia, mke wa Lutu yaani Idit alitoka nje na kweneda kuomba chumvi kwa wanawake wa Sodoma, sio kuwa hakuwa na chumvi nyumbani kwake lakini alikuwa anataka watu wa mji ule wajue kuwa nymkbani kwake kuna wageni na kuwa aliandaa chumvi ya kuwatosha wao tu lakini kwa kuwa wamekuja wageni aliamua kutoka kuomba chumvi, kwa kusudi la kuwasengneya wageni na mumewe kuwa amepokea wageni, hata pamoja na ukarimu wa malaika ambao walimuokoa nayeye na kuwaonya wasitazame nyuma yeye aligeuka nyuma na akahukumiwa kuwa nguzo ya chumvi, hii ndio sababu iliyopelekea yeye kuachwa, Tabia ya mke wa Lutu inaweza kuonekana katika nyumba nyingi leo ambapo mwanaume anaweza kuwa mkarimu lakini mkewe akawa mchoyo au mwanamke anaweza kuwa mkarimu na mcheshi lakini mumewe akawa tofauti, mkali na hacheki na yeyote, wakati kanisa litakaponyakuliwa watu wengi wataachwa katika mtindo kama huu mmoja atwaliwa mmoja aachwa hii ni kwa sababu ya watu wengi kufungiwa nira katika ndoa moja na asiyeamini, au mtu mwenye tabia mbaya, kwa hiyo swala la kuhukumiwa kwa mke wa Lutu haikuwa swala la kugeuka nyuma pekee, lakini alikuwa ni mtu mwenye kudharau maagizo ya Mungu na kuyapuuzia wakati mumewe na watoto walikuwa waelekevu waliotii walichofundishwa

Mwanzo 19:25-26 “Akaangusha miji hiyo na Bonde lote, na wote waliokaa katika miji hiyo, na yote yaliyomea katika nchi ile. Lakini mkewe Lutu akatazama nyuma yake, akawa nguzi ya chumvi

Ni mpango wa Mungu kutuokoa wote pamoja na familia zetu, lakini tunapofunguwa nira na wasioamini tunaweza kujiletea maumivu sisi wenyewe, nadhani mojawapo ya maumivu yaliyomkuta Lutu sio kupoteza kila kitu lakini alimpoteza me wake mpendwa ambaye alimvumilia ijapo kuwa alikuwa na tabia mbaya ambazo malaika hawakuzivumilia, Malengo ya kuokolewa kwa familia yake hayakuweza kutimia.

Kupoteza furaha na utulivu wa kifamilia. – Pamoja na Baraka zote walizokuwa nazo Isaka na Rebeka tunataarifiwa katika maandiko kuwa maisha yao yalitiwa uchungu na kuhuzunishwa sana na wake wa Esau, Esau wakato wote alionyesha kuvutiwa sana na maswala ya dunia kuliko mambo ya Mungu kwa hiyo bila kujali wala kuchukua ushauri wa wazazi alioa wanawake wawili wa Kihiti, hawa walikuwa waabudu miungu, kwa sababu hiyo moyo wa Isaka na rebeka haukuweza kufurahia na wanawake hao pia waliondoa utulivu wa kifamilia katika maisha yao

Mwanzo 26:34-35 “Esau alipokuwa mwenye miaka arobaini, akamwoa Yudith, binti Beeri, mhiti na Basemathi, binti Eloni Mhiti, Roho zao Isaka na rebeka zikajaa uchungu kwaajili yao

Isaka na Rebeka walikumbuka jinsi Mungu alivyohusika katika upatikanaji wa mke wa Isaka Abrahamu alimuagiza mtumishi wake na mtumishi huyu aliomba na kuweka nadhiri, Mungu alihusika moja kwa moja katika upatikanaji wa Rebeka lakini sio ilivyokuwa kwa kijana wao yeye alijiolea tu sijui kama Isaka na Rebeka walihudhuria harusi hii, lakini ilitengeneza mgogoro na kuondoa furaha na utulivu wa kifamilia Biblia ya kiingereza inasema “Esau marriages with unbeliever wives made life bitter for Isaac and Rebekah” Isaka na Rebeka hawakuwa wabaguzi wa rangi, wala hawakuwa na nia ya kumkataza Esau kuoa mke zaidi ya mmoja kwa sababu yakobo pia alioa zaidi, lakini changamoto hapa ilikuwa tamaduni tofauti, na wakaanani walikuwa waovu na wasiomcha Mungu hivyo swala la kiroho kwao ndilo lilipewa kipaumbele

Kuweka usalama wa maisha ya kiroho – Watu wa Mungu wanapoharibu nira yao na Mungu na kujiunga na wale wasiompenda Mungu kimsingi wanaharibu usalama wao na kwa sababu hiyo wanakaribisha mashambulizi makubwa ya aina mbalimbali katika maisha yao ya kiroho, hakuna jambo tunaloweza kulifanya ili tumpendeze Mungu kila kitu kwa Mungu tunakipata kwa neema ya Mungu lakini hata hivyo naada ya kuokolewa neno la Mungu linatutaka tutembee katika utii wetu kwa Mungu ili adui aweze kutukimbia, Mungu kamwe hawezi kuubariki uhusiano ambao unakwenda kinyume na mapenzi yake, kufungiwa nira na wasioamini kunatunyima watu wa Mungu kuzifikia usalama unaokusudiwa na Mungu kwa sababu upande mmoja utakuwa unaharibu na upande mwingine utakuwa unajaribu kutengeneza, ulinzi wa kiungu unaharibiwa pale mtu wa Mungu anapojiungamanisha na mahusiano ambayo kimsingi ni machukizo kwa Mungu

Yeremia 5:3-6 “Ee Bwana, macho yako je! Hayaangalii uaminifu? Umewapiga, lakini hawakuhuzunika; umewakomesha, lakini wamekataa kurudiwa wamefanya nyuso zao kuwa ngumu kuliko mwamba wamekataa kurudi. Ndipo nikasema, Hakika, hawa ni maskini; ni wajinga hawa; maana hawaijui njia ya Bwana, wala hukumu ya Mungu wao; nitawaendea watu wakubwa, nami nitasema nao; kwa maana hao wanaijua njia ya Bwana, na hukumu ya Mungu wao. Bali hawa kwa nia moja wameivunja nira, na kuvikata vifungo. Basi, kwa hiyo, simba atokaye mwituni atawaua, mbwa-mwitu wa jioni atawateka, chui ataivizia miji yao, kila mtu atokaye humo atararuliwa vipande vipande; kwa sababu makosa yao ni mengi, na kurudi nyuma kwao kumezidi.”         

Kwaajili ya kuepusha migogoro na migongano – Mkristo kuoa au kuolewa na mtu asiyeamini ni nira inayoweza kusababisha migongano ya kiimani, kiibada, kimaadili na kimaamuzi katika familia, Aidha kushirikiana kibiashara na mtu asiyeamini kunaweza kuleta maamuzi yanayopingana na kanuni za kiroho, rushwa, wizi,  udanganyifu, tamaa, kujitafutia na ushawishi wa tabia mbaya, Ushirika wa kiroho au kujiunga ma makundi yenye mafundisho potofu ni hatari kwa mustakabali wa kiimani ni kwaajili ya haya Neno la Mungu linatuagiza kuacha kufungiwa nira na wasioamini, aidha ukiacha ukweli kuwa ni hatari kwa imani, inaharibu baraka za Mungu, inaharibu hatima ya mtu, inaharibu uhuru wa mtu kuabudu na kumtumikia Mungu inaathiri uwepo wa Mungu na uhusiano wetu, Nira na wanaoamini inakuhakikishia usafi wa kiibada na kiimani na usalama, Kujifungia nira na wasioamini kunatuletea uchafu wa kiroho na kiimani kwa hiyo ni muhimu kujiepusha na ndoa za kisheria na wasioamini, kujiepusha na mikataba au mapatano yatakayokulazimu kufanya dhambi, kujiepusha na kumuwekea dhamana mtu ambaye haamini asije akakuliza na kukuweka matatani, ili uwe safi chagua marafiki na watu wa karibu ambao wanakuleta karibu na Mungu na sio vinginevyo, chagua watu ambao mna kusudi moja lenye kuwiana na ufalme wa Mungu.

Kumbuka kuwa fundisho hili halihusiani na kujiepusha kabisa na watu wa dunia hii, kwani kwa sehemu sisi ni sehemu ya jamii, lakini fundisho hili lina mkazo katika watu tunaowaleta karibu, wenye ushawishi, kikazi, kimkataba, kiagano, kiimani, kindoa na urafiki, hao ni lazima wawe watu wa Imani moja na wewe na wengine tunaishi nao katika hali ya kawaida kwa sababu ingelitulazimu kuhama ulimwenguni

Yohana 17:14-16 “Mimi nimewapa neno lako; na ulimwengu umewachukia; kwa kuwa wao si wa ulimwengu, kama mimi nisivyo wa ulimwengu. Mimi siombi kwamba uwatoe katika ulimwengu; bali uwalinde na yule mwovu.Wao si wa ulimwengu, kama mimi nisivyo wa ulimwengu.”

Hitimisho:

Mji wa Korintho ulikuwa ni kitovu kikubwa sana cha utamaduni wa Kigiriki, Uchumi na ibada za kipagani, sawa tu na dunia tuliyo nay oleo, na Wakristo wa Korintho walikuwa wameokolewa kutoka katika mazingira ya kuabudiwa kwa miungu mingi kama Aphrodite na zeuz, tamaduni mchanganyiko na biashara lakini pia ulikuwa mji mchafu kingono na ndoa zisizokuwa na uadilifu, mahusiano ya kijamii yalikuwa na machanganyiko wa kitamaduni ambazo kimsingi haikuwa zinajali lolote kuhusu Mungu, Kwaajili ya kuwalinda watu hususani Wakristo ili wasirudi nyuma. Paulo anakataza waamini kujiungamanisha katika fungano la ukaribu sana na watu wa Dunia ile, Paulo alikuwa akionyesha wazi kuwa watu waliookolewa wana nguvu tofauti, hatua tofauti, mwenendo tofauti, hisia tofauti, malengo tofauti na mazigo tofauti kwa hiyo Paulo anatumia fundisho lile lile la kiyahudi katika Torati akiwataka wakorintho wasijunganishe katika uhusiano wa karibu na amaagano na ushirika wa maisha na urafiki na watu waovu baada ya wao kuokolewa, huu ulikuwa ni wito wa kuishi maisha matakatifu lakini pia wa kujilinda kwa mujibu wa tamaduni na maisha ya Ukristo, Paulo alitaka watu wakuze uhusiano wao na Kristo maana yake kujitoa katika nira ya Kristo kwa hiyo wakristo wanaonywa kuhusu ndoa, biashara na urafiki wa karibu  na watu wanaoweza kuleta ushawishi wa uharibifu wa uadilifu katika maisha yao hii itaweka sawa ushirika wa kimaadili, kutiana moyo katika ukuaji wa kiroho, Kuimarisha na kuifanya kazi ya Mungu kwa Amani na Kukaribisha uwepo wa Mungu na Baraka zake katika maisha yake kwa hiyo ingawa wito huu u naonekana kuwa mkali lakini ni wenye manufaa makubwa kwa mustakabali wa furaha ya kweli katika maisha ya Ukristo;

 

Mathayo 11:28-29 “Njoni kwangu,ninyo nyote msumbukao na wenye kuelemewa na mizigo nami nitawapumzisha.Jitieni nira yangu mjifunze kwangu; kwa kuwa mimi ni mpole na mnyenyekevu wa moyo nanyi mtapata raha nafsini mwenu; kwa maana nira yangu ni laini na Mzigo wangu ni mwepesi.”    

Na Rev. Innocent Samuel Kamote

Mkuu wa wajenzi mwenye Hekima

Jumapili, 19 Oktoba 2025

Na tazama, pazia la hekalu likapasuka!


Mathayo 27:50-54 “Naye Yesu akiisha kupaza sauti tena kwa nguvu, akaitoa roho yake. Na tazama, pazia la hekalu likapasuka vipande viwili toka juu hata chini; nchi ikatetemeka; miamba ikapasuka; makaburi yakafunuka; ikainuka miili mingi ya watakatifu waliolala; nao wakiisha kutoka makaburini mwao, baada ya kufufuka kwake, wakauingia mji mtakatifu, wakawatokea wengi. Basi yule akida, na hao waliokuwa pamoja naye wakimlinda Yesu, walipoliona tetemeko la nchi na mambo yaliyofanyika, wakaogopa sana, wakisema, Hakika huyu alikuwa Mwana wa Mungu.”




Utangulizi:

Mojawapo ya matukio makubwa ya kutisha na kushangaza yaliyoambatana na kifo cha Bwana wetu Yesu Kristo pale Msalabani ni pamoja na tukio la kupasuka kwa pazia la hekalu, tukio hili lina tupa ishara madhubuti juu ya umuhimu wa kifo cha Yesu Kristo na nguvu ya upatanisho iliyofanywa na kifo chake kwa wanadamu wote wakiwemo Wayahudi pia, Njia ya kuufikia uwepo wa Mungu ilikuwa sio rahisi wakati wa agano la kale na ni watu wachache sana waliokuwa na ruhusa ya kuukaribia uwepo wa Mungu. Pazia kubwa zito lilitenganisha mahali patakatifu sana palipokuwa na kiti cha rehema na uwepo wa watu wa kawaida hivyo kuwanyima watu fursa ya kukutana na Mungu bila mtu wa kuingilia kati. Pazia hili lilitengenezwa kwa maelekezo ya Mungu kwa Musa, likizuia eneo la Sanduku.

Kutoka 26:30-33 “Nawe utaisimamisha hiyo maskani sawasawa na mfano wake ulioonyeshwa mlimani. Nawe fanya pazia la nyuzi za rangi ya samawi, na za rangi ya zambarau, na za rangi nyekundu, na nguo za kitani nzuri zenye kusokotwa, litafumwa na kutiwa makerubi, kazi ya fundi stadi; kisha litungike katika nguzo nne za mti wa mshita zilizofunikwa dhahabu, vifungo vyake vitakuwa vya dhahabu, katika matako ya fedha manne. Nawe tungika lile pazia chini ya vile vifungo, nawe lete lile sanduku la ushuhuda na kulitia humo nyuma ya pazia; na lile pazia litawagawanyia kati ya patakatifu, na mahali patakatifu sana.”

Leo tutachukua muda kiasi kujifunza umuhimu wa pazia hili kupasuka wakati wa kifo cha Yesu Kristo na maana yake kubwa sana kwetu ambayo kimsingi inatupa tiketi ya kuuendea uwepo wa Mungu na kuufurahia ushirika na Mungu bila kupata madhara ya aina yoyote na bila ya kupitia kwa mtu yeyote, tutajifunza somo hili, Na tazama, Pazia la hekalu likapasuka kwa kuzingatia vipengele vikuu vitatu vifuatavyo:-


·         Kazi ya Pazia la hekalu.

·         Na tazama pazia la hekalu likapasuka.

·         Faida za kupasuka kwa pazia la hekalu.


Kazi ya pazia la Hekalu!

Pazia la Hekalu ilikuwa ni nguo maalumu iliyotengenezwa kwa nyuzi za kitani zilizofumwa kwa ustadi kwa rangi mchangayiko wa aina tatu, rangi ya samawi, yaani mbingu, rangi ya zambarau na nyekundu, Pazia hili lilikuwa na ukubwa kwa maana ya urefu wa futi sitini (Sawa na mita 18) na upana wa futi 30 (sawa na mita 9) na unene wake ulikuwa kati ya inchi 4 mpaka sita yaani kati ya sentimita 10-15. Aidha lilifumwa pia likiwa na picha ya makerubi mfano wa ulinzi kwaajili ya patakatifu pa patakatifu, Pazia hili lilikuwa na kazi ya kupafunika au kutenganisha mahali patakatifu na patakatifu sana. Pazia hili lilitengenezwa kwa ustadi kufuata maelekezo yaliyotolewa na Mungu.

Kutoka 36:35-38 “Kisha akafanya hilo pazia la nyuzi za rangi ya samawi, na za rangi ya zambarau, na nyekundu, na kitani nzuri zilizosokotwa; akatia na makerubi kazi ya fundi stadi, ndivyo alivyofanya. Naye akafanya kwa ajili yake nguzo nne za mti wa mshita, akazifunika dhahabu; na kulabu zake zilikuwa za dhahabu; naye akasubu kwa ajili yake matako manne ya fedha. Kisha akafanya pazia la sitara kwa ajili ya mlango wa Hema, la nguo ya rangi ya samawi, na ya rangi ya zambarau, na nyekundu, na nguo ya kitani nzuri ya kusokotwa, kazi ya mwenye kutia taraza, na nguzo zake tano pamoja na kulabu zake; naye akavifunika dhahabu vichwa vyake na vifungo vyake; na matako yake matano yalikuwa ya shaba.”

Kazi kubwa ya Pazia hili ilikuwa ni kutenganisha mahali patakatifu na patakatifu sana, hekalu lilikuwa na sehemu kubwa tatu, Patakatifu sana au patakatifu pa patakatifu mahali ambapo lilikaa sanduku la agano la Bwana, na patakatifu mahali ambapo palikuwa na madhabahu ya dhahabu ya kufukizia uvumba, taa ya vinara saba na meza ya mikate ya wonyesho, eneo hili kuhani aliingia kwaajili ya kufukiza uvumba, kila siku na kisha eneo la tatu ulikuwa ni uwa wa kawaida ambapo Wayahudi walikaa, na Mataifa wasio Wayahudi walikaa mbali zaidi katika uwa wa wamataifa. Pazia lilitenganisha mahali lilipokuwepo sanduku la agano ambalo juu yake kulikuwa na kiti cha rehema,  mahali hapa kuhani mkuu aliingia mara moja tu kwa mwaka kufanya upatanisho kwa watu na Mungu, siku ya upatanisho tena akiwa amejitakasa kweli kweli (siku saba maalumu kabla ya kuingia katika ibada hiyo), Pazia hili ni alama ikiwa na fundisho kuwa Mungu ni MTAKATIFU SANA na sio rahisi mwanadamu wa kawaida kumsogelea bila kupata madhara, Pazia hili zito lilikuwa ni katazo kuwa huwezi kuufikia uwepo wa Mungu wala kuona ukawa salama, Kuhani mkuu mwenyewe aliingia hapa mara moja kwa mwaka wala si pasipo damu tena siku ya upatanisho (Yom Kippur) kutoa dhabihu ya dhambi kwaajili yake, familia yake na watu wa taifa zima! Kinyume chake kifo kingehusika.

Kutoka 30:10 “Naye Haruni atafanya upatanisho juu ya pembe zake mara moja kila mwaka; kwa damu ya ile sadaka ya dhambi ya kufanya upatanisho, mara moja kila mwaka ataifanyia upatanisho, katika vizazi vyenu vyote; ni takatifu sana kwa BWANA.”

Waebrania 9:1-9 “Basi hata agano la kwanza lilikuwa na kawaida za ibada, na patakatifu pake, pa kidunia. Maana hema ilitengenezwa, ile ya kwanza, mlimokuwa na kinara cha taa, na meza, na mikate ya Wonyesho; ndipo palipoitwa, Patakatifu. Na nyuma ya pazia la pili, ile hema iitwayo Patakatifu pa patakatifu, yenye chetezo cha dhahabu, na sanduku la agano lililofunikwa kwa dhahabu pande zote, mlimokuwa na kopo la dhahabu lenye ile mana, na ile fimbo ya Haruni iliyochipuka, na vile vibao vya agano; na juu yake makerubi ya utukufu, yakikitia kivuli kiti cha rehema; basi hatuna nafasi sasa ya kueleza habari za vitu hivi kimoja kimoja. Basi, vitu hivi vikiisha kutengenezwa hivyo, makuhani huingia katika hema hiyo ya kwanza daima, wakiyatimiza mambo ya ibada. Lakini katika hema hiyo ya pili kuhani mkuu huingia peke yake, mara moja kila mwaka; wala si pasipo damu, atoayo kwa ajili ya nafsi yake na kwa dhambi za kutokujua za hao watu. Roho Mtakatifu akionyesha neno hili, ya kwamba njia ya kupaingia patakatifu ilikuwa haijadhihirishwa bado, hapo hema ya kwanza ilipokuwa ingali ikisimama; ambayo ndiyo mfano wa wakati huu uliopo sasa; wakati huo sadaka na dhabihu zinatolewa, zisizoweza kwa jinsi ya dhambi kumkamilisha mtu aabuduye,”

Kwa sababu hii watu wa kawaida hawakuweza kabisa kupakaribia mahali hapa, kwani hata kuhani alivalishwa kengele (njuga) maalumu kiunoni na mguuni na kufungwa kamba maalumu ili kama atapigwa na Mungu na kufa wamvute nje, watu wengine wote, wangekuwa nje mbali wakiwa wametengwa mbali na mahali hapo patakatifu sana kwaajili ya dhambi na matakwa ya kisheria, hivyo pazia lilikuwa linawakilisha ugumu wa kuufikia uwepo wa Mungu, Pazia lilikuwa linawakumbusha wakati wote kuwa Mungu ni MTAKATIFU SANA na sisi wengine wote hatustahili, dhambi ilikuwa imetufarakanisha mbali na Mungu na hakuna jitihada yoyote ya kibinadamu inayoweza kutuunganisha, utaratibu wote huu ulikuwa pia unafundisha ya kwamba tunahitaji mtu wa kutupatanisha na Mungu, hakuna mwanadamu yeyote aliruhusiwa kupita kwenye pazia hili, maovu ya mwanadamu yalimfarikisha na Mungu.

Isaya 59:1-2 “Tazama, mkono wa Bwana haukupunguka, hata usiweze kuokoa wala sikio lake si zito, hata lisiweze kusikia; lakini maovu yenu yamewafarikisha ninyi na Mungu wenu, na dhambi zenu zimeuficha uso wake msiuone, hata hataki kusikia.”             

 

Na tazama pazia la hekalu likapasuka.

Katika namna ya kushangaza sana na isiyoweza kubuniwa kibinadamu Neno la Mungu katika agano jipya linatufahamisha katika injili zifafanazo zote kuwa pazia hili lililokuwa na unene wa nchi 4-6 hivi kwa njia ya muujiza mkubwa usiokuwa wa kibinadamu mara Yesu alipokata roho na kufa msalabani pazia hili la hekalu lilipasuka katikati vipande viwili kutoka juu hata chini! Muujiza huu usiokuwa wa kawaida ulirekodiwa katika injili zote tatu zifananazo.

Mathayo 27:50-51. “Naye Yesu akiisha kupaza sauti tena kwa nguvu, akaitoa roho yake. Na tazama, pazia la hekalu likapasuka vipande viwili toka juu hata chini; nchi ikatetemeka; miamba ikapasuka;”

Marko 15:37-38 “Naye Yesu akatoa sauti kuu, akakata roho. Pazia la hekalu likapasuka vipande viwili toka juu hata chini.”

Luka 23:44-45 “Hapo ilikuwa yapata saa sita, kukawa giza juu ya nchi yote hata saa kenda, jua limepungua nuru yake; pazia la hekalu likapasuka katikati.”

Kwa nini tukio hili linakuwa la muhimu kiasi hiki mpaka kila mtume anarekodi habari hii, kwa ujumla hili sio jambo dogo, lina kitu cha muhimu cha kutufundisha, Mwandishi wa kitabu cha Waebrania anaeleza kwamba sababu kubwa ni kuwa Yesu Kristo mwana wa Mungu alifanyika Mwana kondoo mkamilifu, aliyejitoa mwenyewe kama sadaka ya kudumu ya milele na kwa damu yake kuwa mpatanishi kati ya Mungu na wanadamu, Mwandishi anafafanua kuwa lile pazia linawakilisha mwili wa Yesu Kristo, kwa hiyo wakati mwili ule unasulubiwa kwa ajili ya dhambi zetu, Kristo anafanyika kuwa mpatanishi kati ya Mungu na wanadamu na hivyo hatuhitaji tena kuhani wa kuingia katika kiti cha rehema kwaajili yetu, na ukuta uliotutenganisha na Mungu umebomolewa, kusulubiwa kwa Yesu Kristo kumeleta uponyaji mkubwa sana kwetu wa kimwili na kiroho, na hatuhitaji tena mtu awaye yote ajifanye “dalali” wa kiroho, au ajifanye kuwa yeye  anaweza kutupatanisha na Mungu ni ukweli ulio wazi kuwa mpatanishi ni mmoja tu. Yesu Kristo!

Waebrania 10:19-21 “Basi, ndugu, kwa kuwa tuna ujasiri wa kupaingia patakatifu kwa damu ya Yesu, njia ile aliyotuanzia iliyo mpya, iliyo hai, ipitayo katika pazia, yaani, mwili wake; na kuwa na kuhani mkuu juu ya nyumba ya Mungu;”

Isaya 53:2-5 “Maana alikua mbele zake kama mche mwororo, Na kama mzizi katika nchi kavu; Yeye hana umbo wala uzuri; Na tumwonapo hana uzuri hata tumtamani. Alidharauliwa na kukataliwa na watu; Mtu wa huzuni nyingi, ajuaye sikitiko; Na kama mtu ambaye watu humficha nyuso zao, Alidharauliwa wala hatukumhesabu kuwa kitu. Hakika ameyachukua masikitiko yetu, Amejitwika huzuni zetu; Lakini tulimdhania ya kuwa amepigwa, Amepigwa na Mungu, na kuteswa. Bali alijeruhiwa kwa makosa yetu, Alichubuliwa kwa maovu yetu; Adhabu ya amani yetu ilikuwa juu yake, Na kwa kupigwa kwake sisi tumepona.”

1Timotheo 2:5-6 “Kwa sababu Mungu ni mmoja, na mpatanishi kati ya Mungu na wanadamu ni mmoja, Mwanadamu Kristo Yesu; ambaye alijitoa mwenyewe kuwa ukombozi kwa ajili ya wote, utakaoshuhudiwa kwa majira yake.

Waebrania 4:14-16 “Basi, iwapo tunaye kuhani mkuu aliyeingia katika mbingu, Yesu, Mwana wa Mungu, na tuyashike sana maungamo yetu. Kwa kuwa hamna kuhani mkuu asiyeweza kuchukuana nasi katika mambo yetu ya udhaifu; bali yeye alijaribiwa sawasawa na sisi katika mambo yote, bila kufanya dhambi. Basi na tukikaribie kiti cha neema kwa ujasiri, ili tupewe rehema, na kupata neema ya kutusaidia wakati wa mahitaji.”            

1Petro 2:9-10 “Bali ninyi ni mzao mteule, ukuhani wa kifalme, taifa takatifu, watu wa milki ya Mungu, mpate kuzitangaza fadhili zake yeye aliyewaita mtoke gizani mkaingie katika nuru yake ya ajabu; ninyi mliokuwa kwanza si taifa, bali sasa ni taifa la Mungu; mliokuwa hamkupata rehema, bali sasa mmepata rehema.”

1Wakorintho 6:19 “Au hamjui ya kuwa mwili wenu ni hekalu la Roho Mtakatifu aliye ndani yenu, mliyepewa na Mungu? Wala ninyi si mali yenu wenyewe;”      

 

Faida za kupasuka kwa pazia la hekalu

Kupasuka kwa Pazia la hekalu kunatupa faida lukuki ambazo muda usingeliweza kutosha kuelezea yote lakini njia ya kumuendea Mungu na kufanya ushirika naye leo imekuwa wazi kwa kila aaminiye, kutoka kokote kule duniani!

-          Tunaweza kumuendea Mungu kwa maombi na kuzungumza naye moja kwa moja bila dalali huku tukiwa na uhakika kuwa Mungu anatusikia  Wafilipi 4:6-7 “Msijisumbue kwa neno lo lote; bali katika kila neno kwa kusali na kuomba, pamoja na kushukuru, haja zenu na zijulikane na Mungu. Na amani ya Mungu, ipitayo akili zote, itawahifadhi mioyo yenu na nia zenu katika Kristo Yesu.”

 

-          Tunaweza kumuendea kwa ibada na kumuabudu kwa kumsifu na kumshukuru tukiwa na uhakika kuwa yeye ni Bwana Mungu wetu kwani tuna uwezo wa kuingia malangoni mwake Zaburi 100:4-5 “Ingieni malangoni mwake kwa kushukuru; Nyuani mwake kwa kusifu; Mshukuruni, lihimidini jina lake; Kwa kuwa Bwana ndiye mwema; Rehema zake ni za milele; Na uaminifu wake vizazi na vizazi.”

 

-          Tunaweza kulifurahia neno lake ambalo kimsingi zamani ni makuhani pekee ndio waliokuwa na uwezo wa kulisoma na kulifafanua kwa watu, Neno la Mungu sasa ni kwaajili ya kila mtu na linaeleweka kwa kila amtafutaye Mungu

 

2Timotheo 3:16-17 “Kila andiko, lenye pumzi ya Mungu, lafaa kwa mafundisho, na kwa kuwaonya watu makosa yao, na kwa kuwaongoza, na kwa kuwaadibisha katika haki; ili mtu wa Mungu awe kamili, amekamilishwa apate kutenda kila tendo jema.”

 

-          Tunaweza kuufurahia uwepo wa Mungu pamoja na wengine kwani kila tunapokutana na kukusanyika kwa jina lake yeye naye anaungana nasi na kuwa kati kati yetu.

 

Mathayo 18:18-20 “Amin, nawaambieni, yo yote mtakayoyafunga duniani yatakuwa yamefungwa mbinguni; na yo yote mtakayoyafungua duniani yatakuwa yamefunguliwa mbinguni. Tena nawaambia, ya kwamba wawili wenu watakapopatana duniani katika jambo lo lote watakaloliomba, watafanyiwa na Baba yangu aliye mbinguni. Kwa kuwa walipo wawili watatu wamekusanyika kwa jina langu, nami nipo papo hapo katikati yao.”

 

-          Tunaweza kuziungama dhambi zetu wenyewe moja kwa moja na Mungu akatusamehe bila kupitia kwa kuhani wa kibinadamu kama ilivyo katika baadhi ya dini ambapo makuhani hutaka kuwatawala wanadamu na kuwanyanyasa kisaikolojia kwa sababu wanataka kusikiliza dhambi zao, au wanafanya kazi ya upelelezi

 

1Yohana 1:8-9 “Tukisema kwamba hatuna dhambi, twajidanganya wenyewe, wala kweli haimo mwetu. Tukiziungama dhambi zetu, Yeye ni mwaminifu na wa haki hata atuondolee dhambi zetu, na kutusafisha na udhalimu wote.”            

 

Kupasuka kwa pazia la hekalu ni tukio la kusangaza sana na si la kihistoria tu bali ni kazi kubwa ya Mungu yenye kumaanisha kuwa Mungu anatoa mwaliko kwa kila mmoja kuukaribia uwepo wake haijalishi umetoka katika historia gani,  na wa kabila gani, Mungu sasa haishi nyuma ya pazia wala hafikiwi kupitia mtu, kuhani au dalali, lakini kupitia Bwana wetu Yesu Kristo mlango ulio wazi umefunguliwa kwa jamii nzima ya aina binadamu duniani kuwa huru na kuufikia uwepo wa Mungu, hakuna wa kujidai katikati yetu badala yake tunasaidiana na kujengana huku tukitiana moyo kwamba leo uiamini kazi  yake Bwana aliyoifanya msalabani kwamba imefungua njia kwaajili yako na yangu na Wayahudi wote duniani kokote waliko kwamba Mungu yuko tayari kukutana na kila mtu anayemjia katika jina la Yesu Kristo Mwana wa Mungu aliye hai Amen

               

Na. Rev. Innocent Samuel Kamote

 

Mkuu wa wajenzi mwenye Hekima!

Jumapili, 12 Oktoba 2025

Maumivu yako, maumivu yake!


Isaya 63:7-9 “Nitautaja wema wa Bwana, sifa za Bwana kwa yote aliyotukirimia Bwana; na wingi wa wema wake kwa nyumba ya Israeli, aliowakirimia kwa rehema zake, na kwa wingi wa wema wake. Maana alisema, Hakika ndio watu wangu hawa, wana wasio na hila; akawa Mwokozi wao.Katika mateso yao yote yeye aliteswa, na malaika wa uso wake akawaokoa; kwa mapenzi yake, na huruma zake, aliwakomboa mwenyewe; akawainua, akawachukua siku zote za kale.”

Utangulizi:

Tuwapo duniani wanadamu wote tunakutana na maumivu ya aina mbalimbali katika maisha, maumivu haya yanaweza yasilingane lakini kila mmoja anaweza kuhisi maumivu kwa jinsi yake, ziko nyakati maisha yanakuwa magumu, ziko nyakati tunaumia moyo, ziko nyakati tunalia machozi, ziko nyakati matumaini yanavunjika, ziko nyakati roho zinauma, kwa ujumla kunakuwa na maswali mengi sana hususani wakati tunapopitia maumivu haya, moyoni unaweza kuhisi kuwa labda Muumba naye angehisi maumivu haya, tunajiuliza anasikia na anaumia kama ninavyoumia? Mungu wetu anajali kweli? Neno la Mungu linaonyesha ya kuwa Mungu sio tu kuwa anayaona mateso yetu lakini pia anaumia pamoja nasi kama baba anavyowahurumia watoto wake ndivyo Mungu wetu anavyotuhurumia Maumivu yako ni maumivu yake!

Zaburi 103:11-14 “Maana mbingu zilivyoinuka juu ya nchi, Kadiri ile ile rehema zake ni kuu kwa wamchao. Kama mashariki ilivyo mbali na magharibi, Ndivyo alivyoweka dhambi zetu mbali nasi. Kama vile baba awahurumiavyo watoto wake, Ndivyo Bwana anavyowahurumia wamchao. Kwa maana Yeye anatujua umbo letu, Na kukumbuka ya kuwa sisi tu mavumbi.”

Mungu anatupenda mno, anaweza kuyatumia maumivu yetu kutimiza makusudi yake fulani fulani katika maisha yetu, lakini hata hivyo yeye hafurahii maumivu yetu na anapatwa na uchungu ule ule unaotupata sisi wakati wa maumivu yetu, anashiriki machozi yetu na anakaa nasi wakati wa mambo magumu na kutukomboa kuhakikisha usalama wetu na furaha yetu inakuwa kamilifu, Leo basi tutachukua muda kujifunza somo hili “Maumivu yako maumivu yake” kwa kuzingatia yafuatayo:-

·         Maana ya maumivu yako maumivu yake.

·         Mifano ya watu ambao Mungu alioshughulika na maumivu yao.

·         Maumivu yako maumivu yake.


Maana ya maumivu yako maumivu yake.

Usemi maumivu yako maumivu yake unatokana na maelezo ya unabii wa Isaya katika mstari wetu wa msingi tuliousoma ambao unaashiria kuwa, Mungu anaguswa sana na maumivu yetu, na ya kuwa anateseka pamoja na wanadamu wanaoteseka anasikia uchungu kama wanavyosikia uchungu, anahisi maumivu kama wanavyohisi maumivu, anaumia pale watoto wake wanapoumia, na Analia pale watoto wake wanapolia hii ndio maana kubwa tunayoipata katika mstari wa Msingi kutoka ktk

Isaya 63:9 “Katika mateso yao yote yeye aliteswa, na malaika wa uso wake akawaokoa; kwa mapenzi yake, na huruma zake, aliwakomboa mwenyewe; akawainua, akawachukua siku zote za kale.”

Neno katika mateso yao yote yeye aliteswa, Neno aliteswa katika lugha ya Kiebrania linasomeka kama “tsar tsar” ambalo katika kiingereza ni sawa na neno “Affliction” kwa hiyo katika kiingereza maneno Katika mateso yao yote yeye aliteswa yanasomeka “in all their affliction he was afflicted” neno hili ni sawa na kusema “Maadui zao wakawa maadui zake” au “Maumivu yao yakawa maumivu yake” au “Maumivu yako maumivu yake” au “Katika taabu zao alitaabika”hii maana yake ni kuwa Mungu anajua maumivu yako, anashiriki taabu zako na mashinikizo yako, anasikia uchungu wako kama mtu awaye yote mwenye huruma anavyohisi uchungu wa maumivu yako, wakati wote kama baba zetu wa duniani wanaposikia uchungu kwa habari ya maumivu ya watoto wao, Mungu wetu wa Mbinguni ambaye ni Baba anaguswa zaidi na maumivu yetu kuliko wanadamu ambao ni waovu, maandiko yanaonyesha ya kuwa Mungu ni Baba anayejali watoto wake kuliko, zaidi ya baba zetu wa duniani, ikiwa wao wanaumia kwaajili yetu, Mungu yeye Maumivu yako, ni maumivu yake!

Luka 11:11-13 “Maana ni yupi kwenu aliye baba, ambaye mwanawe akimwomba mkate, atampa jiwe au samaki, badala ya samaki atampa nyoka? Au akimwomba yai, atampa nge? Basi, ikiwa ninyi mlio waovu mnajua kuwapa watoto wenu vipawa vyema, je! Baba aliye mbinguni hatazidi sana kuwapa Roho Mtakatifu hao wamwombao?       

Mifano ya watu ambao Mungu alioshughulika na maumivu yao.

Biblia imejaa mifano mingi inayoonyesha jinsi ambavyo Mungu hakuwahi kuvumilia maumivu ya watu wake kwa sababu zozote zile, aliyajua maumivu, hofu na changamoto walizokuwa wanazipitia watu wake, alifahamu mashinikizo yao katika maisha na katika hekima yake na huruma zake aliweza kuwajali na kushughulikia kwa haraka, changamoto hizo kabla hawajamezwa kwa huzuni.

1.       Hajiri – Aliteswa na Sara Bibi yake kiutawala alimuamuru Abrahamu kumtupa na kumfukuzilia mbali majazi huko jangwani, Hajiri alikimbilia jangwani akiwa na mwanae ambaye alikuwa anakaribia kufa kwa kiu ya maji, walianza kulia katika jangwa, alimweka mtoto chini na kukimbilia mbali ili asimuone mtoto akifa, akalia kwa uchungu Mungu aliguswa na mateso na kilio cha mtoto na mama yake na akaleta ufumbuzi katika maisha yao

Mwanzo 21:14-19 “Ibrahimu akaamka asubuhi na mapema akatwaa mkate na kiriba cha maji, akampa Hajiri akimtwika begani pake, na kijana, akamruhusu; naye akatoka, akapotea katika jangwa la Beer-sheba. Yale maji yakaisha katika kiriba, akamlaza kijana chini ya kijiti kimoja.  Akaenda akakaa akimkabili, mbali naye kadiri ya mtupo wa mshale; maana alisema, Nisimwone kijana akifa; naye akakaa akimkabili, akapaza sauti yake, akalia. Mungu akasikia sauti ya kijana. Malaika wa Mungu akamwita Hajiri kutoka mbinguni, akamwambia, Una nini, Hajiri? Usiogope, maana Mungu amesikia sauti ya kijana huko aliko. Ondoka, ukamwinue kijana, ukamshike mkononi mwako, kwa kuwa nitamfanya kuwa taifa kubwa. Mungu akamfumbua macho, naye akaona kisima cha maji; akaenda akakijaza kiriba maji, akamnywesha kijana.”

2.       Israel Utumwani – Wote tunafahamu kuwa Israel walipata mikandamizo mingi na kuonewa na wasimamizi wao huko jangwani, hali ilikuwa mbaya kiasi ambacho Mungu alilazimika kuingilia kati kwaajili ya wokovu, ni ukweli ulio wazi kuwa Maumivu yao yalikuwa magumu na waliugua na kuumwa na shinikizo lile la utumwa usio wa kiungwana Maumivu yao yakawa  maumivu yake Mungu ambaye kimsingi aliguswa na kushuka akipanga wokovu wao

Kutoka 3:7-10 “BWANA akasema, Hakika nimeyaona mateso ya watu wangu walioko Misri, nami nimekisikia kilio chao kwa sababu ya wasimamizi wao; maana nayajua maumivu yao; nami nimeshuka ili niwaokoe na mikono ya Wamisri, niwapandishe kutoka nchi ile, hata nchi njema, kisha pana; nchi ijaayo maziwa na asali; hata mahali pa Mkanaani, na Mhiti, na Mwamori, na Mperizi, na Mhivi, na Myebusi. Basi, tazama, kilio cha wana wa Israeli kimenifikilia; tena nimeyaona hayo mateso ambayo Wamisri wanawatesa. Haya, basi, nitakutuma sasa kwa Farao, ili upate kuwatoa watu wangu, hao wana wa Israeli, katika Misri.”

3.       Mjane – Huyu mwanamke huko katika mji wa Naini alikuwa mjane, lakini licha ya kuwa mjane alikuwa na mwane mmoja kijana wa pekee, Neno la Mungu halisemi kulikuwa na mazingira gani kijana huyu alikufa na watu wa mji walitoka kwenda mazikoni, Yesu alipomuona mama huyu alimuhurumia maumivu yake yakawa maumivu ya Kristo, na akisukumwa na upendo wake na maumivu ya huruma zake Yesu alimfufua kijana yule mara!

Luka 7:11-15 “Baadaye kidogo alikwenda mpaka mji mmoja uitwao Naini, na wanafunzi wake walifuatana naye pamoja na mkutano mkubwa. Na alipolikaribia lango la mji, hapo palikuwa na maiti anachukuliwa nje, ni mwana pekee wa mamaye ambaye ni mjane, na watu wa mjini wengi walikuwa pamoja naye. Bwana alipomwona alimwonea huruma, akamwambia, Usilie. Akakaribia, akaligusa jeneza; wale waliokuwa wakilichukua wakasimama. Akasema, Kijana, nakuambia, Inuka. Yule maiti akainuka, akaketi, akaanza kusema. Akampa mama yake.”

4.       Lazaro – Alikuwa rafiki wa Yesu Kristo pamoja na dada zake Martha na Mariamu, Lazaro aliugua na baadaye akafa, Yesu alihudhuria msiba huu akiwa Mungu katika mwili aliguswa sana na maumivu ya dada zake Lazaro, ambao walilia wakiwa wamekata tamaa ya uhai, wakitarajia kuwa uwezekano wa kufufuka kwa Lazaro ni labda katika siku ya mwisho lakini akisukumwa na huruma maumivu yao yakawa maumivu yake Yesu akafanya tukio akamfufua

Yohana 11: 32-35 “Basi Mariamu alipofika pale alipokuwapo Yesu, na kumwona, alianguka miguuni pake, akamwambia, Bwana, kama ungalikuwapo hapa, ndugu yangu hangalikufa. Basi Yesu alipomwona analia, na wale Wayahudi waliofuatana naye wanalia, aliugua rohoni, akafadhaika roho yake, akasema, Mmemweka wapi? Wakamwambia, Bwana, njoo utazame. Yesu akalia machozi.”

Yohana 11:43-44 “Naye akiisha kusema hayo, akalia kwa sauti kuu, Lazaro, njoo huku nje. Akatoka nje yule aliyekufa, amefungwa sanda miguuni na mikononi, na uso wake amefungwa leso. Naye Yesu akawaambia, Mfungueni, mkamwache aende zake.”

Maumivu yako maumivu yake.

Tunajifunza kupitia neno la Mungu la msingi na mifano iliyopo katika maandiko ya kwamba Mungu wetu huwa anajishughulisha sana na mambo yetu na kwa sababu hiyo pia ni muhimu kufahamu kuwa maumivu yetu ni maumivu yake, kwa sababu hiyo hatakuacha ujaribiwe kupita uwezavyo, yuko tayari kabisa kutoa mapumziko kwa wote wanaaonewa na kukandamizwa na Shetani kwa sababu zozote zile. Usifikri hata kidogo kuwa tuna Mungu asiyejali, Maumivu yako ni maumivu yake!

1Petro 5:6-7 “Basi nyenyekeeni chini ya mkono wa Mungu ulio hodari, ili awakweze kwa wakati wake; huku mkimtwika yeye fadhaa zenu zote, kwa maana yeye hujishughulisha sana kwa mambo yenu.”

Mathayo 11:28 “Njoni kwangu, ninyi nyote msumbukao na wenye kulemewa na mizigo, nami nitawapumzisha.”

Mathayo 8:16-17 “Hata kulipokuwa jioni, wakamletea wengi wenye pepo; akawatoa pepo kwa neno lake, akawaponya wote waliokuwa hawawezi, ili litimie lile neno lililonenwa na nabii Isaya, akisema, Mwenyewe aliutwaa udhaifu wetu, Na kuyachukua magonjwa yetu.”            

Ni muhimu kwa sababu hiyo kukumbuka kuwa maumivu yako ni maumivu yake, Maumivu yako si dalili ya kuwa Mungu amekutupa bali ni njia ya kuthibitisha ya kuwa yuko pamoja nawe na anakujali sana, wakati wewe unalia kumbuka Mungu analia pamoja nawe, Mungu anayabeba maumivu yako kuliko yanavyobebwa na mwanasaikolojia yeyote yule, na sio hivyo tu yeye atakupa nguvu na kukuwezesha kwa msaada wa Roho wake Mtakatifu, kilio chako wakati wowote kinaweza kugeuka kuwa mbegu ya furaha na mafanikio yako, uchungu wako unatambuliwa na Mungu kwa hiyo kama alivyosema katika mateso yako yote yeye anateseka pamoja nawe kwa hiyo leo ishi ukifahamu ya kwamba maumivu yako ni maumivu yake, ole wake anayekuumiza anamuumiza Mungu, ole wake anayekulaani anamlaani Mungu, ole wake anayekugusa anamgusa Mungu.

Zekaria 2:8-10 “Kwa maana Bwana wa majeshi asema hivi, Ili nitafute utukufu amenituma kwa mataifa wale waliowateka ninyi; maana yeye awagusaye ninyi aigusa mboni ya jicho lake. Kwa maana, tazama, nitatikisa mkono wangu juu yao, nao watakuwa mateka ya hao waliowatumikia; nanyi mtajua ya kuwa Bwana wa majeshi amenituma. Imba, ufurahi, Ee binti Sayuni; maana, tazama, ninakuja, nami nitakaa kati yako, asema Bwana.”

Na. Rev. Innocent Samuel Kamote

Mkuu wa wajenzi mwenye Hekima!

Jumapili, 5 Oktoba 2025

Namjua anayeishika kesho!


Mathayo 6:31-34 “Msisumbuke, basi, mkisema, Tule nini? Au Tunywe nini? Au Tuvae nini? Kwa maana hayo yote Mataifa huyatafuta; kwa sababu Baba yenu wa mbinguni anajua ya kuwa mnahitaji hayo yote. Bali utafuteni kwanza ufalme wake, na haki yake; na hayo yote mtazidishiwa. Basi msisumbukie ya kesho; kwa kuwa kesho itajisumbukia yenyewe. Yatosha kwa siku maovu yake.”



Utangulizi:

Mojawapo ya tatizo kubwa la kiroho na kisaokolojia linalowakumba wanadamu ni pamoja na tatizo la kuogopa kesho au wakati ujao, tatizo la kuhofia kuhusu kesho au wakati ujao kisakolojia linaitwa “Chronophobia” au “time anxiety”  hofu ya wakati hususani wakati ujao ambayo kitaalamu inafafanuliwa kama “a type of anxiety that involves  worrying about tomorrow or future”  yaani ni aina ya msongo wa mawazo unaohusisha kuogopa au hofu kuhusu kesho au wakati ujao,  Neno Chronophobia ni muunganiko wa maneno mawili ya kiyunani “Chronos” yaani muda na “phobos” yaani hofu kwa hiyo wanadamu wengi wanasumbuliwa na hofu kubwa sana kuhusu itakuwaje kesho, katika Afrika wanawake wengi huongoza kwa hofu hii na ndio maana wengi huogopa kufiwa na waume zao na utawasikia wakisema kuna leo na kesho hali itakuwaje? Na wakati mwingine watu huogopa kuwa huenda kuna jambo baya litawatokea na watu wengi wanaogopa magumu, wengine huogopa muda kwa kufungwa gerezani, masikini huogopa kwamba kesho itakuwaje, matajiri huogopa kufilisika, wenye vyeo huogopa kuviachia, wafanya biashara huogopa hasara, Wengine huogopa muda kwa kufikiri kuwa wamekawia katika maisha, Tatizo la hofu linaweza kuwako katika pembe nyingi,  Ingawa tatizo hili linaweza kuwa la kawaida lakini kuna wanadamu wengine tatizo hili huwa kubwa zaidi kwao na linaweza kufikia hatua likaathiri Imani yao na ni kwa sababu hii Neno la Mungu linamtaka kila mmoja wetu kutokuogopa kuhusu kesho au wakati ujao na badala yake kumtegemea Mungu.

Mathayo 6:34 “Basi msisumbukie ya kesho; kwa kuwa kesho itajisumbukia yenyewe. Yatosha kwa siku maovu yake.”

Kwa nini neno la Mungu linatuonya kutokuogopa kesho? Hii ni kwa sababu Mungu ndiye anayeishika kesho, kesho yako na wakati wako ujao uko mikononi mwa Mungu na ukilitambua hilo huwezi kuogopa lolote, Kwa msingi huu basi leo tutachukua muda kujifunza kwa kina na mapana na marefu juu ya somo hili “Namjua anayeishika kesho” kwa kuzingatia vipengele vitatu vifuatavyo:-


·         Hofu ya wanadamu kuhusu kesho.

·         Neno la Mungu linasemaje kuhusu kesho.

·         Namjua anayeishika kesho.


Hofu ya wanadamu kuhusu kesho.

Mathayo 6:25-34 “Kwa sababu hiyo nawaambieni, Msisumbukie maisha yenu, mle nini au mnywe nini; wala miili yenu, mvae nini. Maisha je! Si zaidi ya chakula, na mwili zaidi ya mavazi? Waangalieni ndege wa angani, ya kwamba hawapandi, wala hawavuni, wala hawakusanyi ghalani; na Baba yenu wa mbinguni huwalisha hao. Ninyi je! Si bora kupita hao? Ni yupi kwenu ambaye akijisumbua aweza kujiongeza kimo chake hata mkono mmoja? Na mavazi, ya nini kuyasumbukia? Fikirini maua ya mashamba, jinsi yameavyo; hayafanyi kazi, wala hayasokoti nami nawaambia, ya kwamba hata Sulemani katika fahari yake yote hakuvikwa vizuri kama mojawapo la hayo. Basi, ikiwa Mungu huyavika hivi majani ya kondeni, yaliyopo leo, na kesho hutupwa kalibuni, je! Hatazidi sana kuwavika ninyi, enyi wa imani haba? Msisumbuke, basi, mkisema, Tule nini? Au Tunywe nini? Au Tuvae nini? Kwa maana hayo yote Mataifa huyatafuta; kwa sababu Baba yenu wa mbinguni anajua ya kuwa mnahitaji hayo yote. Bali utafuteni kwanza ufalme wake, na haki yake; na hayo yote mtazidishiwa. Basi msisumbukie ya kesho; kwa kuwa kesho itajisumbukia yenyewe. Yatosha kwa siku maovu yake.”

Katika hutuba yake ya mlimani Mwalimu wetu mkuu na mwokozi wa maisha yetu Yesu Kristo hakuacha kuzungumzia swala zima la hofu ya wanadamu kuhusu kesho, wanadamu wengi masikini kwa matajiri wote wanakabiliwa na hofu kuwa itakuwaje kesho au maisha ya baadaye, hofu hii inaweza ikawa sio tu kwa mahitaji ya kawaida nitakula nini na nitavaa nini, lakini inaweza kuwa zaidi ya hapo, itakuwaje nikifiwa na mume, itakuwaje nikifukuzwa kazi, itakuwaje nikifilisika, itakuwaje nikidaiwa kodi, itakuwaje nikiachwa! Itakuwaje nikiugua? Itakuwaje nikishindwa uchaguzi, itakuwaje nikifeli, nini kitatokea, itakuwaje uchumi ukiyumba? Na kadhalika hofu hii ni tatizo kubwa la kiroho na kisaikolojia na Mungu analijua vema, anajua kuwa hofu hizi zinaweza kumpelekea mtu akakosa Amani, akapoteza usingizi, na hatimaye akapoteza Imani na matumaini na Ndio maana Yesu aliwafundisha wanafunzi wake kwamba hawapaswi kuogopa kuhusu kesho kwa sababu Baba wa mbinguni anajua mahitaji yetu na ndiye anayeishika kesho!.

Neno la Mungu linasemaje kuhusu kesho.

Neno la Mungu linatufundisha ya kuwa ni Mungu ndiye mwenye uwezo wa kudhibiti kesho ya kila mmoja wetu, na hakuna mwanadamu ambaye anaweza kujisumbua kuhusu kesho yake na akafanikiwa bila neema na kibali cha Mungu, hofu yako wasiwasi wako na hata maandalizi yako hayawezi kukuhakikishia kesho iliyo salama na kamili bila Mungu, kwa sababu kesho haiko katika mikono ya mwanadamu bali iko katika mikono ya Mungu mwenyewe, wako watu ambao walijisumbua sana kuhusu kesho na neno la Mungu likawatumia kama mifano ya kutuonya kuwa huwezi kufanya kitu kuhusu kesho na ukajithibitishia usalama bila ya Mungu! Kesho iko kwenye mapenzi ya Mungu! Mungu ndiye anayeishika kesho ili mwanadamu asiwe na kiburi, Tancredo Neves alikuwa mgombea urais wa Brazili mwaka 1985 wakati wa kampeni zake alisema nikipata kura 500,000 tu kutoka kwenye chama changu hakutakuwa na wa kuzuia nisiwe Rais hata Mungu hataweza kunizuia, Kwa kweli alipata kura hizo na akashinda uchaguzi, lakini aliugua ghafla na utumbo ulijikunja akafariki siku moja kabla ya kuapishwa kuwa raisi Tarehe 21/4/1985. Lazima kila mmoja kwa unyenyekevu akubali kuwa kesho iko mikononi mwa Mungu na sio mikononi mwa mwanadamu.

Yakobo 4:13-15 “Haya basi, ninyi msemao, Leo au kesho tutaingia katika mji fulani na kukaa humo mwaka mzima, na kufanya biashara na kupata faida; walakini hamjui yatakayokuwako kesho. Uzima wenu ni nini? Maana ninyi ni mvuke uonekanao kwa kitambo, kisha hutoweka. Badala ya kusema, Bwana akipenda, tutakuwa hai na kufanya hivi au hivi.”

Luka 12:15-20 “Akawaambia, Angalieni, jilindeni na choyo, maana uzima wa mtu haumo katika wingi wa vitu vyake alivyo navyo. Akawaambia mithali, akisema, Shamba la mtu mmoja tajiri lilikuwa limezaa sana; akaanza kuwaza moyoni mwake, akisema, Nifanyeje? Maana sina pa kuyaweka akiba mavuno yangu. Akasema, Nitafanya hivi; nitazivunja ghala zangu, nijenge nyingine kubwa zaidi, na humo nitaweka nafaka yangu yote na vitu vyangu. Kisha, nitajiambia, Ee nafsi yangu, una vitu vyema vingi ulivyojiwekea akiba kwa miaka mingi; pumzika basi, ule, unywe, ufurahi. Lakini Mungu akamwambia, Mpumbavu wewe, usiku huu wa leo wanataka roho yako! Na vitu ulivyojiwekea tayari vitakuwa vya nani?               

Maandiko yanatuonya wazi kuwa hakuna mwanadamu anayeweza kudai kwa sababu zozote zile kwamba anaweza kuwa na uhakika wa kesho, na hata hivyo hatupaswi kuiogopa kesho pia, lakini kesho iko katika mikono ya Mungu na kwa sababu hiyo neno la Mungu linatuonya kuiacha hofu ya kesho katika mikono ya Mungu, badala yake tunatiwa moyo kumuamini Mungu na kumtegemea yeye kwaajili ya mahitaji yetu ikiwepo kesho yetu,  Neno la Mungu halitutii moyo kuogopa kuhusu kesho kwaajili ya mahitaji yetu, wala halituhakikishii kuwa tunaweza kutengeneza usalama wetu wa kesho kwa kujilimbikizia ua kujiwekea akiba au kwa kutafuta sana kunakoambatana na hofu ya kesho na pia hakuna mwanadamu awaye yote wa ngazi yoyote ile anayeweza kujithibitishia kuwa na kesho iliyo njema nje ya uweza na mamlaka ya Mungu Mwenyewe. Kwa sababu hiyo hatupaswi kujivuna au kujisifia lolote kuhusu kesho!

Mithali 27:1-2 “Usijisifu kwa ajili ya kesho; Kwa maana hujui yatakayozaliwa na siku moja. Mwingine na akusifu wala si kinywa chako mwenyewe; Mtu mgeni wala si midomo yako wewe.”

Neno la Mungu linaonyesha wazi kuwa mwenye kesho ni Mungu tu, siku moja tu inaweza kuzaa jambo na likabadilisha kila kitu katika maisha yetu, kwa sababu hiyo hatuna budi kuishi kwa unyenyekevu na kwa kumtegemea Mungu pake yake, hatupaswi kuiogopa kesho kama tunamwamini Mungu na wala hatupaswi kujihami kuhusu kesho kama iko mikononi mwa Mungu hii maana yake ni nini? Maana yake ni kuwa Mungu ndiye anayeishika kesho na ukimjua yeye hutaweza kuishi maisha ya hofu ya aina yoyote ile, ukiwa na uhakika kuwa kesho yako iko kwake!

Namjua anayeishika kesho.

Ni muhimu kufahamu kuwa hakuna hofu wala woga utakaokutawala endapo tu utagundua kuwa ni Mungu ndiye anayeishikilia kesho yako, Mungu anaweza kubadilisha mambo kwa usiku mmoja tu, ukitambua kuwa ni Mungu ndiye anayeishikilia kesho yako hakuna mwanadamu atakayekutisha wala kukutetemesha kuhusu yajayo, kesho yako haiko katika mikono ya wanadamu, iko katika mikono ya Mungu, ukimjua yeye anayeshika kesho hautaogopa mabadiliko ya aina yoyote ile, utamtegemea yeye ambaye ni ngome iliyo imara  naye hatakuangusha, Mwandishi wa Zaburi hakuwahi kuogopa mabadiliko yoyote yale kwa sababu alikuwa anamjua Mungu na kutambua ya kuwa ndiye anayeshikilia kila kitu kwa hiyo lolote litokee haliwezi kututisha kwa sababu yeye Mungu ndiye mwenye kesho yake!

Zaburi 46:1-7 “Mungu kwetu sisi ni kimbilio na nguvu, Msaada utakaoonekana tele wakati wa mateso. Kwa hiyo hatutaogopa ijapobadilika nchi, Ijapotetemeka milima moyoni mwa bahari. Maji yake yajapovuma na kuumuka, Ijapopepesuka milima kwa kiburi chake. Kuna mto, vijito vyake vyaufurahisha mji wa Mungu, Patakatifu pa maskani zake Aliye juu. Mungu yu katikati yake hautatetemeshwa; Mungu atausaidia asubuhi na mapema. Mataifa yalighadhibika, falme zikataharuki; Alitoa sauti yake, nchi ikayeyuka. Bwana wa majeshi yu pamoja nasi, Mungu wa Yakobo ni ngome yetu.”

Mungu wetu ni Mungu asiyebadilika, Yeye ni Yeye yule jana leo na hata milele, Yu hai, na bado anaendelea kubarikia watu wake, anaendelea kulinda watu wake, anakomboa watu wake, bado ni mtawala wa mbingu na nchi majira na nyakati, ziko mkononi mwake, hajawahi kupoteza nguvu zake wala uwezo wake Yeye bado ni Bwana Mungu aliyeziumba mbingu na nchi na bahari na vyote vilivyomo, Ndiye aliyeigawa bahari ya Shamu, akamzika Farao na majeshi yake, akawalisha watu wake kwa mana, akawanywesha maji kutoka katika mwamba, akawapigania dhidi ya adui zao, akatimiza ahadi zake kwa kuwapa nchi ya Mkanaani, nguvu zake hazijawahi kupungua, alimfufua Lazaro, alimtoa Petro na Paulo na Sila gerezani, hakuna nguvu inaweza kupingana naye, Yeye ndiye anayeishika kesho, kesho yako haiko kwa waganga wa kienyeji, kesho yako haiko kwa bosi wako, kesho yako haiko kwa wenye mamlaka au cheo, kesho yako haiko kwa wachawi, kesho yako haiko kwa wapiga ramli kesho yako inashikwa na Mungu aliye hai, muumba wa mbingu na nchi, uaminifu wake unazidi kizazi hata kizazi na yeye anatuwazia mema na yeye habadiliki ni Yeye Yule jana leo na hata milele, Hakuna mtu anayeweza kuichafua kesho yako, hakuna mtu anaweza kuizibia kesho yako, kesho yako iko katika mikono ya Mungu, ukimjua anayeishika kesho yako hutaogopa, hakuna wa kukurudisha nyuma, tunaweza tusijue lolote kuhusu kesho, lakini tunaweza kumjua anayeishika kesho! Naye ni mwenye nguvu!

Kama Mungu ndiye anayeishika kesho yako maana yake unaweza kumuamini yeye kuhusu kesho yako na kutokuogopa wakati ujao ukijua ya kuwa anatuwazia mema na ana mpango mzuri kwaajili yako:-

Yeremia 29:11 “Maana nayajua mawazo ninayowawazia ninyi, asema Bwana, ni mawazo ya amani wala si ya mabaya, kuwapa ninyi tumaini siku zenu za mwisho.”

Kama Mungu ndiye anayeishika kesho yako maana yake hupawi kuogopa endapo unazingirwa na maadui pande zote na wanakukusudia mabaya hawawezi kutimiza mpango wao kwa sababu mpango wao sio mkuu kama wa yule anayeishika kesho:-

Zaburi 31:13-15 “Maana nimesikia masingizio ya wengi; Hofu ziko pande zote. Waliposhauriana juu yangu, Walifanya hila wauondoe uhai wangu. Lakini mimi nakutumaini Wewe, Bwana, Nimesema, Wewe ndiwe Mungu wangu. Nyakati zangu zimo mikononi mwako; Uniponye na adui zangu, nao wanaonifuatia.”

Kama Mungu ndiye anayeishika kesho yako maana yake ni yeye anayeweza kukulinda kwa nguvu zake na mkono wake kiasi kwamba hutakuwa na lolote la kuogopa, hutaogopa wachawi, hutaogopa Shetani, hutaogopa, laana, hutaogopa wanaoukutishia maisha Imani na tumaini litakuwa kubwa kwa Bwana Mungu wako na hutaogopa vita wala majeshi makubwa ya adui yajapojipanga kupigana nawe kwa sababu yuko anayeishika kesho yako!

Zaburi 27:1-5 “Bwana ni nuru yangu na wokovu wangu, Nimwogope nani? Bwana ni ngome ya uzima wangu, Nimhofu nani? Watenda mabaya waliponikaribia, Wanile nyama yangu, Watesi wangu na adui zangu, Walijikwaa wakaanguka. Jeshi lijapojipanga kupigana nami, Moyo wangu hautaogopa. Vita vijaponitokea, Hata hapo nitatumaini. Neno Moja nimelitaka kwa Bwana, Nalo ndilo nitakalolitafuta, Nikae nyumbani mwa Bwana Siku zote za maisha yangu, Niutazame uzuri wa Bwana, Na kutafakari hekaluni mwake. Mradi atanisitiri bandani mwake siku ya mabaya, Atanisitiri katika sitara ya hema yake, Na kuniinua juu ya mwamba.”

Kama Mungu ndiye anayeishika kesho yetu tunajengewa uhakika na matumaini ya kuwa anajishughulisha sana na mambo yetu, atakutana na mahiaji yetu, na tutaishi kwa kujiamini bila kuogopa tukijua ya kua kesho ni ya Baba mwenye upendo na rehema ataishughulikia, sina ada italipwa, sina chakula nitakula, sina nguo nitavaa, sina raha nitapewa, nina mizigo itapumzishwa, nina madeni yatalipwa, sioni njia ataniongoza, naona giza atakuwa nuru!

Kumbukumbu 8:11-16 “Jihadhari, usije ukamsahau Bwana, Mungu wako, kwa kutozishika amri zake, na hukumu zake, na sheria zake, ninazokuamuru leo. Angalia, utakapokuwa umekula na kushiba, na kujenga nyumba nzuri na kukaa ndani yake; na makundi yako ya ng'ombe na kondoo yatakapoongezeka, na fedha yako na dhahabu yako itakapoongezeka, na kila kitu ulicho nacho kitakapoongezeka; basi hapo moyo wako usiinuke, ukamsahau Bwana, Mungu wako, aliyekutoa katika nchi ya Misri, katika nyumba ya utumwa; aliyekuongoza katika jangwa lile kubwa lenye kitisho, lenye nyoka za moto na nge, nchi ya kiu isiyokuwa na maji; aliyekutolea maji katika mwamba mgumu, aliyekulisha jangwani kwa mana, wasiyoijua baba zako; apate kukutweza, apate kukujaribu, ili kukutendea mema mwisho wako.”

Kama Mungu ndiye anayeishika kesho yako, maana yake ni kuwa haitakuja utishike na kuweweseka kwa sababu yeye yuko siku zote, alikuwako tangu mwanzo, habadiliki, hageuki wala hana kigeugeu, wala kwake hakuna kubadilika badilika Yeye ni Yeye yule jana leo na hata milele  Waebrania 13:8 “Yesu Kristo ni yeye yule, jana na leo na hata milele.”

Yakobo 1:17 “Kila kutoa kuliko kwema, na kila kitolewacho kilicho kamili, hutoka juu, hushuka kwa Baba wa mianga; kwake hakuna kubadilika, wala kivuli cha kugeuka-geuka.”

Kama Mungu ndiye anayeishika kesho yetu basi ni wazi kuwa hakuna jambo lolote lile linaloweza kututenga na upendo wake, hakuna wa kutuhukumu, hakuna wa kututishia maisha, hakuna wa kututishia kuhusu kesho, hakuna wa kutupunguzia kitu, hakuna wa kutupokonya ushindi, hakuna wa kututisha kwa maana kesho iko mikononi mwake

Warumi 8:31-39 “Basi, tuseme nini juu ya hayo? Mungu akiwapo upande wetu, ni nani aliye juu yetu? Yeye asiyemwachilia Mwana wake mwenyewe, bali alimtoa kwa ajili yetu sisi sote, atakosaje kutukirimia na mambo yote pamoja naye? Ni nani atakayewashitaki wateule wa Mungu? Mungu ndiye mwenye kuwahesabia haki. Ni nani atakayewahukumia adhabu? Kristo Yesu ndiye aliyekufa; naam, na zaidi ya hayo, amefufuka katika wafu, naye yuko mkono wa kuume wa Mungu; tena ndiye anayetuombea. Ni nani atakayetutenga na upendo wa Kristo? Je! Ni dhiki au shida, au adha, au njaa, au uchi, au hatari, au upanga? Kama ilivyoandikwa, ya kwamba, Kwa ajili yako tunauawa mchana kutwa, Tumehesabiwa kuwa kama kondoo wa kuchinjwa. Lakini katika mambo hayo yote tunashinda, na zaidi ya kushinda, kwa yeye aliyetupenda. Kwa maana nimekwisha kujua hakika ya kwamba, wala mauti, wala uzima, wala malaika, wala wenye mamlaka, wala yaliyopo, wala yatakayokuwapo, wala wenye uwezo, wala yaliyo juu, wala yaliyo chini, wala kiumbe kinginecho chote hakitaweza kututenga na upendo wa Mungu ulio katika Kristo Yesu Bwana wetu.”

Na. Rev. Innocent Samuel Kamote

Mkuu wa wajenzi mwenye Hekima!